Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 4. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 4.

Baada ya watu kula na kumshukuru Mungu, wakabaki marafiki wa James wakaribu wakisema wanaanza kikao cha kwanza. Hapohapo wakaanza kutoa pleges/ahadi. Jema akashangazwa na ule utayari wa marafiki wa James. “Kama bado James hujachagua mwenyekiti, mimi nitakuwa mwenyekiti.” Mpaka James akacheka na kutingisha kichwa. “Basi bwana Geb.” Mama G akaanza kupiga tena vigelegele. “Na kama utaona sawa, naona mimi nitamsaidia Geb.” Kumu akajiongeza.  “Kwanza wewe Geb nani alikwambia kama leo sisi tunakutana hapa?” “Mimi.” Kumu akadakia kwa haraka. James hakuamini. Akamtizama na kutingisha kichwa. Mama G vigelegele. Akacheka. Usiku huo mambo yakaenda kwa haraka na kifupi, wafanyakazi wenzake James nao wakaondoka na kuwaacha kina Kumu, Geb, mama G, James, Jema na Naya.

“Huwezi kutugawa James. Hiyo tumekataa. Tutabebana hivyohivyo na Jema ajifunze kutuvumilia.” “Nashukuru Joshua mwanangu.” “Kabisa. Familia nyingi zina matatizo, sidhani kama yetu yamezidi kipimo. Hapana James. Sisi tumekataa.” “Basi Joshua. Basi.” Ikabidi James apoe lakini Jema hakujua kinachoendelea. “Naona mpaka sasa mambo yamekwenda vizuri. Leo najua Jema atakuwa amechoka. Lakini tungependa kujua mnataka ukumbi gani. Hilo tu. Halafu mambo ya wasimamizi, mavazi yake bibi harusi na wasimamizi wao, mapambo ni…” “Mimi, Nanaa na Grace.” Akadakia mama G.

“Labda mngemuacha kwanza Nanaa.” “Hataachwa mtu James. Nanaa ni mdogo wako, kama mtoto. Mtoto akinyea mkono haukati. Na Jema ampokee wifi yake hivyohivyo. Kitakachoongezeka hapa ni mama James. Kwa hakika mama yako amefurahi James.” “Sana. Nimemuona eti hata bia amekataa ili asiharibu!” “Basi huyo tutamuingiza kwenye kundi letu. Na mama Jema ili afurahie harusi ya mwanae, na watu wetu wengine tutakao wachagua. Tutapanga mpaka mambo ya kitchen Party. Si sawa Jema mwanangu?” James akamwangalia. “Sawa mama. Mimi nashukuru kwa kutaka kunisaidia. Lakini nilikuwa na ombi.” Akaongea Jema akimtizama James.

Maneno Yakitamkwa Yametakwa, Harudi.

“Sema tu usiwe na wasiwasi.” James akamtia moyo. “Nashukuru kwa kusimama na sisi. Ila naomba kwa upande wangu. Nikimaanisha mambo ya kitchen party, saluni, mavazi na wasimamizi wetu wote mpaka watoto, nishugulikie mimi nikimaanisha upande wa kina mama zangu. Kwanza itanirahisishia mimi binafsi kufanya kwa haraka kama James anavyotaka tufunge ndoa kwa haraka. Na pia nitakuwa huru nao kwa kuwa wananifahamu na wameshanizoea vile nilivyo. Kingine mama zangu wamekuwa wakitamani kushiriki kwa karibu sana. Yaani ni kama wameshajipanga kwa hili japo tumewashirikisha kwa muda mfupi.” Wakajua Jema ameshajenga ukuta kwao. Yaliyotamkwa na Nanaa nyumbani kwake, yameshamtenga nao. Hawahesabu tena kama wapo pamoja.

“Kwa kufupisha tu, naomba tugawane. Nyinyi niwaachie mambo yote ya harusi mkisaidiana na James. Nikimaanisha mbakiwe na shuguli ya siku ile ya harusi tu. Ila kitchen Party, sendoff na hao wasimamizi wetu wote, mimi nifanye na kina mama zangu. Na kwakuwa leo nimefanya kazi na hawa mawifi zangu wawili, Vai na Viola, tukisaidiwa na Naya. Nimeona tumekwenda kwa kasi nzuri tu bila shida. Kila kitu tumefanya kwa haraka bila kuchelewa. Tena tulikuwa tukicheka hapo jikoni na Naya, imekua kila ninachokifikiria, na yeye ndio alikuwa akikifikiria kukifanya, na kina Viola wakatusaidia kwa haraka. Basi naomba Viola na Vai wasaidie upande wangu. Najua ni ndugu wa James, walitakiwa wawe upande wa harusi, lakini naona watanisaidia kwenda kwa kasi yangu. Wawe kama ndio watakao wawakilisha kwenye maandalizi ya upande wetu. Kuwapa taarifa ya kitakachokuwa kikiendelea.” Kina Viola ndio wamesimama naye! Ikawa ngeni kabisa kwao na kuwauma kuona wamekosa hiyo nafasi ya kuendesha mambo kama walivyozoea. Jema amechagua watu duni. Kina Viola wasio na kitu, hawajasoma, wasichana wa mtaani tu huwezi kuwafananisha na upande wa Nanaa hata kidogo! Ikawa kama wamefikishiwa ujumbe.

“Kukiwa na kualikwa kwenye kitchen Party, watawasiliana na nyinyi kupata idadi yenu ambao pengine mngependa kuhudhuria kwenye hiyo kitchen Party na Sendoff na kuwawakilisha kwenye kamati za upande wetu. Na mama James amemuomba mama rasmi kusaidia kwa karibu. Kwa hiyo naamini hakutakuwa na pengo, na mambo yote yatakwenda kwa haraka na urahisi tukiwa tumegawana. Viola na Vai wakiongozwa na mama James, watawawakilisha kwetu wakati na nyinyi mkiendelea na James ili kuwa ukurasa mmoja.” Pakazuka ukimya hapo, maana ni kama wakina Magesa wamepigwa STOP.

Lakini wakakumbuka pia jeshi la ndugu waliokuwepo usiku huo, wakapoa. Jema si yatima kama Naya au vile walivyojiwa na Danny kwenye maisha yao. Analo jeshi lake, na wamejipanga. Mama zake wakubwa na wadogo ni wachaga wa mjini. Wamama wa nguvu na walionekana wanaelewa mambo, sio wazubaifu. Hawataendesha mambo kama walivyozoea wakigawana majukumu. Mama G akapoa kabisa. Na kwa aina ya ndugu zake, ndipo wakaamini Jema alikwenda kwao si kwa shida ila kuomba mahusiano ambayo aliyakosa kwao, sasa amejitenga na mali zao pia.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakamuona Naya anamnong’oneza kitu mumewe kisha wakamuona Joshua anakataa. “Ni nini?” James akauliza. “Anataka kusaidia upande wa bibi harusi. Awe na Jema. Lakini hapana. Nitashindwa kufanya kazi ya kumsaidia Mwenyekiti, na mimi nitajikuta kwenye kamati ya Kitchen Party bure.” Wakaanza kucheka. “Kweli! Acheni tu.” Joshua akaweka msisitizo. “Ila leo nimefanya naye kazi kwa wepesi kweli! Amekua msaada sana. Naya anaakili ya kufikiria na kutenda kwa haraka. Meza ya chakula ameandaa yeye mwenyewe akipanga na kuweka napkins kama vile mlivyoona.” “Tatizo wala si yeye. Ni mimi. Siwezi nikamuacha mahali ambako macho yangu hayamuoni. Asee nitashindwa kufikiria. Niombe kitu kingine Jema, lakini si huyu. Tafadhali.”

“Unajua sijawahi kukuangusha Kumu.” Jema akaendelea kumuombea Naya. “Jema wewe unataka kuniua kwa pressure.” “Itamsaidia na yeye. Nakuahidi akihitajika popote, atakuwa na mimi na jicho langu haliondoki kwake mpaka nakukabidhisha mkononi mwako. Halafu sio kila sehemu atatakiwa kuja. Mambo mengine nitakuwa nikiwasiliana naye kwa simu tu.” Joshua akafikiria, akakumbuka maneno yanayofanana na hayo, alipewa na Nanaa, akaishia mikononi kwa Malon. Wakamuona kama anayefikiria kisha akatingisha kichwa kukataa mawazoni. “Aisee hapana. Labda siku zenu za vikao vyenu msipange siku moja na vikao vyetu vya harusi. Kama nyinyi mnafanya jumapili, sisi iwe jumamosi. Ikitokea ni siku moja, iwe mida tofauti ili niweze kuhudhuria naye. Utanisamehe Jema. Huyu natunza kama mboni ya jicho langu.” “Sawa. Basi siku zitapishana. Usijali.” Jema akamtuliza.

“Kwa hiyo mzee utakuwa ukienda kwenye vikao vya Kitchen party pia!?” Swali la James likafanya waanze kucheka. “Ninapokwambia natunza kama mboni ya jicho, jua sina mipaka James. Nitahakikisha nakaa sehemu ambayo namuona wakati wote.” “Asante Joshua. Mimi nitakuwa muangalifu naye. Nakuahidi.” “Nashukuru Jema. Ila tafadhali tuwasiliane. Kila unapomtaka tu, niambie nijipange.” “Sawa.” Hilo likakaa sawa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Na mimi niwe kama Jema. Kuna jambo inabidi kuliweka wazi mapema. Bado nina mahusiano ya karibu sana na Danny. Na kama mlivyoona hapa, na leo alikuwepo.” Kimya kwa muda, mama G akamwangalia Geb. Wamebanwa kila kona. Jema ni kama amejitoa kwenye umoja wao, wa wakina mama Magesa. Na James naye anakuja na Danny ambaye hawakutaka hata waje wajikute chumba kimoja kama mama G alivyomwambia siku wakiagana kwenye talaka yake na Grace! Leo James anamrudisha kwao! Pagumu!

“Ulitaka tufanyaje?” Geb akatumia akili na hekima akauliza. “Na yeye atakuwepo kwenye kamati.” James akaongea akiwatizama. “Ulitaka afanye nini?” Geb akauliza tena. “Chochote kile ila nilitaka mjue atashiriki.” “Nafikiri uamuzi ni wako James. Sisi tupo kukusaidia kwa vyovyote utakavyotaka. Hata kama umeshapanga timu yako, ukitupa sisi nafasi zingine, haitatusumbua kabisa, ilimradi kufanikisha tu hilo.” “Sina hata  kamati. Sasa wote hawa waliotoa ahadi, watu wa Danny wakaribu sana. Nashauri tumpe yeye uweka hazina, kesho pombe zikiwa zimewaisha kichwani, watuambie haya mamilioni ya pesa waliyokuwa wakitamka hapa ni wao au pombe.” Wakacheka.

“Lakini kweli. Maana wote waliondoka hapa wamelewa! Tunaweza sema tunapesa nyingi kumbe pombe ndio ilikuwa ikitoa ahadi.” “Basi acheni Danny awafuatilie. Atawapanga hata wao ili mpate watu wakuwasaidia kwenye kamati.” Kukawa kama hakuna tena chakuongeza. Maharusi hao ni kama walikuwa na misimamo yao na watu wao. Wakawa wastaarabu wakitaka kufuata matakwa yao. Wakaona waagane tu wasubiri siku ya kikao cha kwanza wakiwepo watu wengine, ambacho James aliwaambia atawajulisha baada ya kulipa mahari.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakati wanawasindikiza, Jema akamuita Naya kwa kumgusa maana alikuwa akitembea nyuma ya mumewe kidogo. Akageuka. “Nashukuru kunisaidia.” “Nimefurahia! Wewe ni mtu mzuri Jema. Nimefurahi umeniamini na wageni.” Jema akacheka. “Sijui kama unajua hili Naya, wewe unaakili sana ya kubuni vitu. Kuna mfumo ulibuni pale kazini kiasi ya kwamba umesaidai kuziba pengo la mtu aliyekuwa ameondoka. Anaitwa Njama. Mumeo alituambia ni wewe ndio ulibuni, akatengeneza vizuri tu akisaidiwa na watu wa IT. Natumia bila shida. Sipigizani kelele na watu, na kazi siku hizi zinakwenda zaidi ya zamani.” Naya akacheka. “Aliniambia Joshua. Ila na wewe umeniamini Jema. Asante. Nimefurahi kufanya kazi. Mwenzio sifanyi kazi yeyote. Nakaa tu nyumbani. Kwa hiyo leo nimefurahia.” Kumbe Joshua alikuwa akiwasikiliza. Akageuka. “Asante sana Jema. Ni kweli alihitaji hiki alichofanya.” Joshua akaongeza.

“Hata kwenye mambo yako ya maandalizi, ukimuhitaji tuwasiliane tu. Nitakuwa nikimleta, na mimi pia itanisaidia kuanza kumpa vitu vingine vya kufanya.” “Basi nitakuwa nikikwambia Kumu. Ili ajikute na vitu vingi vyakufanya.” Mama G na Geb wao wakawa wakitembea kimya kimya kurudi kwenye gari. Kila mmoja akiwaza lake. James kimya. Akiwajua hiyo familia na ugumu wanaokutana nao kwa wakati huo. Danny anarudi kwenye maisha yao bila kupenda na hawawezi kumkwepa tena, na Jema ameshajitoa kwao! Ikawa ngeni. Walishazoea kuvuta watu karibu na watu kuwakimbilia, lakini safari hii ikawa tofauti. Akawaacha tu. Wakaaga na kuondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakajikuta wamebaki wawili. “Nimefurahi James, nimefurahi sana. Asante kwa heshima uliyonipa hata mbele ya familia yangu. Mama zangu wote wanakusifia sana. Wanasema umewapokea na wao vizuri na umewaheshimu.” “Nimeona jinsi mama yako mkubwa alivyokuwa akizungumza na mimi. Amesema wanaandaa mazingira jumamosi nikalipe mahari, kunipunguzia mlolongo. Na bibi atakuwepo. Amesema wataandaa tafrija nzuri tu hapo kwa mama Jema, naweza kualika watu wangu wa karibu, ili tupate muda kama huu.” “Wamefurahi sana.”

“Nina surprise nyingine.” Jema akacheka. “Nini tena?” “Unakumbuka gauni ulisema ulikuwa mpaka ukiliota umevaa kwenye harusi yako?” Jema akabaki ametoa macho. “Tunaweza kulipata.” “James! Sikujua kama ulikuwa ukinisikiliza na kutilia maanani!” “Nisipokusikiliza wewe, nimsikilize nani?” Jema alifurahi sana. “Kuna mama anashona, lakini ameniambia kwake itachukua muda mrefu sababu ya nilivyomuelekeza, ila anayo sehemu, sio hapa lakini. China. Anasema ukizungumza naye, atawasiliana nao na kuwatumia vipimo vyako, watatoa gauni kama hilo, hivyohivyo.” Jema akafurahi sana. Usiku huo kwao ukaisha ukiwa na furaha ya namna yake.

Kisa Kimempata Kasa.

Lakini ikawa kinyume na Kasa. Wote waliondoka pale wakiwa na furaha lakini si Kasa. Alihisi kudhalilika vibaya sana. Akaapa ni lazima afanye kitu. Alipoingia tu garini akampigia simu kijana wanayemtumia sana kwenye familia yao. Hata baba yake, mzee Kasa mwenyewe alimpenda sababu alikuwa mwepesi na mtekelezaji wa kila jambo bila vipingamizi. Walimtumia mchana na usiku. “Niambie bosi.” Akaanza Zilo. “Kuna mtoto anaitwa Jelini. Najua kwa hakika anaishi Tegeta Mwisho. Sasa nataka unitafutie habari zake kamili.” “Anafanya kazi au biashara wapi?” “Na usinicheleweshe.” Simu ikakatwa. Zilo akatingisha kichwa.

“Pesa mwanaharamu! Yaani unaweza kuta mwanaume mwezio anakutumikisha bila heshima hivihivi!” Akalalamika kwa wenzie kijiweni. “Nani? Kasa nini?” “Kumbe mwingine nani? Bora baba yake anaadabu na utu, kuliko yeye. Naona kapata demu, anataka habari zake.” “Tuchangamkie mwana. Si unajua anavyojuaga kulipa?” “Kesho.” “Acha masihara Zilo! Hela ya leo unataka ilale?” “Sasa usiku huu utapata wapi habari…” “Twende kwa masela wa Tegeta. Kama mwingi wa habari, usiku huu huu tutapata habari zake, tulipwe.” Zilo akabaki akijishauri. “Wewe unashida ya hela, huna?” “Twende.” Zilo akatoka na rafiki yake wa karibu mpaka Tegeta Mwisho na kuanza kumuulizia Jelini.

Kabla ya kupambazuka, Kasa akawa na habari kamili za Jelini. Baa anayoweza kupatikanika bila kukosa, kila siku. Akazitunza hizo habari, ikabaki kazi ya kujipanga maana baa anayoshinda Jelini haiendani na hadhi ya Kasa kabisa. Kwanza si mkaa baa. Ila kwa kulipa kisasi, alijiambia lazima ajipange.

Mahari.

Maandalizi ya kupokelewa mahari yakaanza kwa James, na Jema kutolewa mahari. Nyumbani kwao pakaanza kuandaliwa, na bibi yake akakusudia kufika mjini kupokea mahari ya Jema. James alipotumiwa orodha ya vitu vinavyohitajika, akamwambia baba yake, na yeye akaja mjini kwa ajili ya hilo. Hata James aliona jinsi baba yake alivyofurahi. Alifika Dar na ndugu zake wengine wawili, na wote wakafikia hapo nyumbani kwa James wala si kwa mama James. Kwa hiyo James akawa na baba zake watatu hapo nyumbani, tayari kwa kwenda kulipa mahari. Viola akawa anafika hapo yeye na mdogo wake kumsaidia kupikia baba zao na usafi. James akashangazwa na hao dada zake waliokuwa wameshindika, ila akajiambia pengine wamekua, utoto umewaisha. Au wamekutana na uhalisia wa maisha. Akawa na kazi ya kuwasaidia nauli kila siku akienda kazini anaacha nyumbani pesa ya matumizi na nauli yao ili wakija waikute.

Mama G alipotaka kusaidia, James akamwambia mama yake amechangamkia hivyo vitu vya mahari, amebakiza vichache alivyochukua Danny. Akapoa na kumwambia hata Grace. “Basi mama. Mimi nashauri tufanye kama alivyosema Geb. Tushiriki vile tutakavyo pewa nafasi.” “Bado utakuja?” “Lazima mama. James tumetoka naye mbali hata kabla ya Nanaa. Ila tutakuja siku yenyewe ya shuguli, hiyo jumamosi asubuhi. Nitakuja na Man tu, tunaacha watoto. Jumapili asubuhi tunageuza.” Grace alishajua kuwa Danny angekuwepo na anashiriki kwa karibu sana. Man mumewe akamwambia asiwe na wasiwasi angekuwepo naye wakati wote.

Ndugu wa mama Jema wakaanza kutayarisha mazingira ya nyumbani kwake kupokea wageni na sherehe ya siku hiyo. Mama Jema alijenga Tegeta Mwisho miaka mingi sana watu wakipakwepa. Yeye akanunua eneo kubwa tu. Kwa kuwa hakuwa na pesa akajenga nyumba ya kawaida sana. Vyumba vitatu tu. Choo kimoja ndani. Hapohapo na bafu. Akatulia na hao binti zake wawili mpaka Jema alipoondoka. Nje ya nyumba akawa akilima tu vitu mbalimbali ila migomba ndio ikawa mingi. Mbele ya nyumba akapanda maua yake ya kawaida tu, nyuma ndio hiyo bustani au shamba. Kukawa shamrashamra kila ndugu macho na masikio kwa mama Jema wakichangishana kumsaidia kufanikisha shuguli nzima. Jema akawa ameleta kitu cha tofauti kwao, ndoa!

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakati James anajipanga kuoa akisaidiwa na marafiki zake wakaribu, Kasa yeye alikuwa akijipanga jinsi ya kumpata Jelini. Kwanza alijua ni mropokaji, hakutaka amfuate kwa gafla aingie aibu tena. Hapo akabaki akiwaza. Kasa anapenda kuabudiwa na kujulikana kuwa yeye ni bora kuliko mtu mwingine. Akampigia tena Zilo. “Huko baa, anakuwa na wanaume au?” “Tulivyosikia huko baa wanakundi lao wanakunywa pamoja. Mchanganyiko wa wanaume na wanawake ambao ni wao wawili. Yeye na msichana mwengine ambaye ni rafiki yake sana wa karibu na ndiye anayeonekana anayo hela ya kumnunulia pombe kila siku. Kwa hiyo huwa anakuwa naye hapo kila siku jioni baada ya kazi.” “Kwa hiyo kwenye hilo kundi hana mwanaume?” “Labda niulize zaidi.” Simu ikakatwa. Zilo akajua ndio ametumwa tena.

Akakimbilia tena Tegeta, ila safari hii akaamua kuuliza ila pia kujithibitishia. Zilo akakusanya habari zote. Saa usiku, Kasa akapigiwa. “Sasa safari hii nimekwenda umbali mrefu zaidi. Nipo hapa baa. Na imebidi mpaka kuzungumza na muhudumu ambaye anawahudumia wao. Inavyoonekana hili kundi ni la watu tofautitofauti. Wote, kasoro Jelini wanafanya kazi hizi za maofisini. Jioni baada ya kazi huwa wanakutana hapo kunywa mpaka usiku mwingi tu. Msichana niliyekwambia ni rafiki wa Jelini, kwa kumuangalia yeye anaonekana mkubwa kwa Jelini. Maana nimemsikia akimuita ‘dada Doro’, na ndiye nasikia kampani ya Jelini. Na hata Jelini ndiko anapokwenda kulala huko kwake.” “Kwa hiyo hapo hana mwanaume?” “Kwa pale baa nasikia yeye anamfuataga Doro, ili apate bia za bure na hataki kufanya kazi.” “Nani?” Kasa akauliza. “Huyo Jelini. Hana kazi wala biashara yakumuingizia kipato.” Akajibu Zilo na kumfanya Kasa afikirie sasa, kwa uzuri na unadhifu ule, nani anamtunza!

“Ila nilikwenda umbali mrefu kidogo bosi wangu, japo hujanituma.” “Nini?” “Kutafuta habari za Doro na kujua pakumpata endapo ungetaka kumfikia yeye kwanza.” Ni hivyo tu ni Kasa alishindwa kumsifia kwamba amefanya jambo zuri. Lakini hata yeye alimkubali Zilo. “Kwamba?” Akauliza Kasa kwa jeuri.

“Doro nasikia yeye ndio anafanya kazi hizi za waliosoma maana nasikia anayopesa haswa. Hakuna anayejua ni kwanini, lakini ni dada mzuri tu ila kila siku lazima awe baa ndio maana alipenda kampani ya Jelini ambaye hana kazi na anamsindikiza popote anapotaka yeye Doro. Nasikia Doro amejijenga vizuri sana, anaishi Kunduchi. Na hata leo ameondoka na Jelini. Hata usafiri wake wenyewe ni wa ukweli.” “Anafanya kazi wapi?” Akamtajia. Simu ikakatwa. Ila kwa pesa aliyotumiwa baada ya kukatiwa simu akajua Kasa amefurahi sana. Asijue jinsi alivyomfanikishia Kasa. Akawa ameshajua pakuanzia. Kwa Doro.

Atafutaye Hachoki.

Kesho yake mida ya chakula cha mchana Kasa akawa amewasili ofisini kwa Doro. Baada tu ya salamu, Kasa akaanza kwa ujasiri kwani alishamuona Doro amechanganywa naye. “Unakitu ambacho nahitaji msaada wako kukipata.” Doro akafurahi sana akijua ni mapenzi tu kwani hata yeye alikuwa akilipa. “Hata hunifahamu!” Akaongea kwa pozi akicheka kike. “Taka cha uvunguni shuruti ainame, si ndivyo?” Doro akacheka. “Nakufahamu sana Doro. Nafahamu mpaka unapoishi. Ulichonacho ambacho nakihitaji kwa pesa yeyote ile ni Jelini.” Doro alishangaa sana na kuishiwa nguvu kabisa.

“Jelini!?” “Ndiyo. Na najua jana aliondoka na wewe pale baa mkielekea nyumbani kwako Kunduchi.” Ikabidi Doro ajiweke sawa akiwa na mshangao mkubwa sana usoni. Kasa akacheka. “Si nilikwambia unacho kitu ninachokitaka? Kwa hiyo macho yangu yapo kwake.” “Na nimemuacha amelala. Mvivu hataki kazi. Yeye kula kulala tu.” Akaanza Doro kwa jazba. “Basi, nisaidie mazingira ya kumpata.” Wivu ukazidi kumkaba Doro na kumshangaza asichoelewa nini! Kwamba hajamsikia au!?

“Wewe humfahamu Jelini. Uzuri ule unawachanganya wengi, lakini wakishamfahamu Jelini mwenyewe wanakimbia, ndio maana unamuona kakwama kwangu. Wanaume wote wanajaribu na kujiachia. Sasa wewe unaonekana ni kaka uliyetulia, unajielewa, ndio nakuokoa. Usijipotezee muda na yule mtoto. Hamuendani kabisa.”

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Huyo ndiye anayesemekana rafiki wa karibu sana wa Jelini. Maneno yake kwa Kasa aliyeonekana na nia naye ndiyo hayo.

Nini kitaendelea kwa Kasa aliyekusudia kumpata Jelini na Doro ndiye aliyebakia kama njia ya kumfikia?

Hatimaye Danny na Grace, wanandoa walioanza tokea Chuo, wakiwa wamebeba historia ngumu kwenye mahusiano yao, watakutanishwa na shuguli ya James.

Itakuje?

Usipitwe.




CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment