Hatimaye Na Kwa James Nako Kunaliwa.
Jema
aliwahi nyumbani kwa James akidhani itabidi kusafisha kwanza, akakuta ni kama
kuna mtu ametoka kusafisha hapo. Ikawa kupanga tu. Dereva wa Kumu akaleta
vyombo. “Naamini sijakosea nyumba. Nimeelekezwa mpaka hapo getini. Nimeleta
vyombo na vitambaa vya kujifutia.” “Karibu na asante sana. Wakasaidiana
kuingiza ndani, ndipo dereva akaondoka. Jema akaanza kupanga taratibu. James
naye akafika. “Naomba kazi.” Jema akacheka. “Njoo kwanza unikiss mpaka nitulie.
Bado siamini.” Akasikia sauti ya Jema upande wa jikoni. Akamfuata. Wakaanza
kupeana midomo bila kutosheka.
“Umenifuta
machozi James. Asante.” James akacheka akiwa bado amemkumbatia. “Pete nzuri, na
ya hadhi. Umenifanyia surprise nzuri, mpaka naona raha na fahari pale
ofisini. Halafu wewe mzuri.” James alicheka
mpaka akamuachia na kuinama. “Kweli tena. Mwenzio najivunia uzuri wako.
Nimefurahi. Halafu napenda unavyoniletea vitu pale kazini, sasahivi na mimi
najulikana nina mpenzi anayenijali. Asante James.” “Karibu Jema. Furaha yangu
ni kukuona unafuraha. Ila nina zawadi ingine.” “Bwana acha mimi nikupe yangu
kwanza. Utanizidi sana.” “Sio mashindano, mama!” “Sawa, lakini acha na mimi
nikupe. Nimetoka kukununulia ndio nikaja hapa.” Akaenda kwenye pochi yake
akamtolea cheni nzuri sana ya dhahabu ya kiume na kidani kimeandikwa J&J.
“Kabla
hujanivalisha acha nione kwanza. Nzuri sana!” “Kweli umeipenda?” “Kwa sababu
imetoka kwako na ina jina lako pia. Kithibitisho kuwa ndio umenikabidhi Jema
wangu?” “Mpaka kifo changu. Mimi nitakuwa na wewe tu.” Yakaanza mabusu mengine
bila papara. Ndipo Jema akamvalisha. “Na hivi wewe mweupe, ndio imekupendeza
zaidi.” “Nakwambia ninavyosifiwa! James anapendwa rangi yake!” “Sana! Natakaga
unishike tu, nikusikie mwilini mwangu.” James akamshika tena na kumbusu tena na
tena. Ndipo akamuachia.
“Naona
mama James amekua tofauti na nilivyotegemea!” “Amekuaje tena!?” Kidogo
akaingiwa na wasiwasi. “Acha nisiongee sana, tuje tumuone. Nisije nikazungumza
kwa haraka, yakawa kama jana.” Jema akapoa. “Hawatakuja hapa.” Jema akawa kama
hajaelewa. “Nanaa hatakuwepo hapa. Kwa hiyo usiwe na wasiwasi.” “Kwa nini
sasa?” “Hapa ni kwako Jema. Sitaki mtu akunyime raha.” Jema hakutegemea. Ni
Nanaa ambaye sifa zake zilikuwa zikiimbwa na huyo James kila siku! Akatamani
aongee kitu, akaona ayaache kama yalivyo.
“Naona
nimeletewa vyombo vingi! Kwani tunategemea wageni wangapi? Na watakaa wapi?”
“Mama Jema ameniambia yeye watu wake watakaa hata jikoni au hata nje hawana
neno. Na watakula hata kwa kuonja, nisiwe na wasiwasi.” Jema akafurahi sana.
Japokuwa hapakuwa kama nyumbani kwa Kumu, lakini bado nyumba ilikuwa mpya
kabisa na ni ya kisasa. Kutoka kutapeliwa nyumba mpaka kukabidhiwa funguo za
nyumba! Huna utakalomwambia Jema akaelewa mbali na anachoambiwa na James.
Kumbuka Shuka, Kumekucha.
Maandalizi
yakaendelea, Danny naye akaleta vinywaji vingi sana mpaka pombe, kisha
akaondoka na ahadi ya kurudi usiku. Ndio akili ikamrudia Jema kuwa anaolewa na
James ambaye hajawahi kumsikia kama ameokoka japo anampeleka kwenye makanisa ya
walokole. “Njoo kwanza James. Hivi harusi yetu itakuwa na pombe?” “Wewe kwa
nini hujaniuliza kama mimi nakunywa au sinywi?” Hapo Jema akapoa kidogo.
Akamtizama kwa wasiwasi ila akaona aulize tu. “Kwani wewe unakunywa?” “Mbona
sasa umekosa raha?” “Mimi siwezi kuolewa na mlevi James. Siwezi na
nilijiambia sitafanya hivyo.” James akaweka mikono mfukoni. “Mimi huwa nakunywa
ila si mlevi.” Akamjibu akimtizama machoni. “Mmmh!” Jema akaishia kuguna.
“Inamaana
gani?” “Hapo tena nimekwama James.” “Kwa nini?” “Sasa tutakuwa na maisha gani
hayo? Mimi sitaki pombe.” Jema akaongea akilalamika. “Tokea tumeanzana
mimi na wewe umeshaniona nikiwa nimelewa?” Jema kimya, macho chini. “Mimi sina
tatizo na pombe. Unywaji wa chupa mbili kwangu si tatizo.” Jema akabaki
ameinama ametulia kama anayefikiria.
“Unakumbuka
maneno uliyotoka kuniambia sasahivi wakati unanipa hii cheni?” “Nakumbuka.”
“Kwa hiyo tafrija ya usiku ipo au nianze kupigia watu simu kuwaambia wasije,
bibi harusi amegairi kwa sababu amegundua mimi sina tatizo na pombe ndio
hanitaki tena?” “Mimi sijasema hivyo. Ila nafikiria tu.” “Unafikiria nini?”
“Sasa kwa nini unywe!?” “Mimi sina ugomvi na pombe na wala
hazijawahi kunifanya kitu kibaya kilichonifanya nijutie kunywa. Sasa tatizo
lipo wapi?” Jema akakwama.
“Kwani
wewe unashida gani na pombe?” Jema akaitizama ile pete na kuishika kama aivue.
James kimya akimtizama. “Mimi siwezi pombe. Na sitaki pombe.” “Hilo
nimelisikia. Kwa hiyo?” “Naomba muda James. Ni uamuzi ambao natakiwa kufikiria
na kukubaliana nao kwamba nitaishi nao mpaka kufa.” “Kwa hiyo ukishakubaliana
nao. Na mimi nikagundua kuna kitu kwako ambacho sikikutegemea kwa
atakaye kuwa mke wangu, naomba muda wa kukufikiria?” Kimya.
“Eti
Jema? Pengine hapo tunakuwa tumeshaoana. Tuna mtoto mmoja tayari, au umjamzito. Halafu nagundua kuna jambo
ambalo WEWE unalo, na sikuwahi kutaka kutoka kwa atakayekuwa mke wangu, nakuacha
kwa muda ili nifikirie kwanza ndipo nijue kama nakurudia wewe au naoa
tena mwanamke mwingine?” Hapo Jema akaanza kupoa. “Sio wewe niliyekuomba
unichunguze udhaifu wangu wowote utakao kutana nao, unibebe
hivyohivyo ukijua mimi ni wako?” Kimya.
“Ukafanya
nikakuamini! Nimekupa moyo wangu, unakuja kuniadhibu leo hadharani!?” “Sijasema
nakuacha James! Nikufikiria tu.” “Kwa hiyo hawa wageni leo natakiwa kuwapigia
simu na kuwaambia mchumba ameomba muda wakunifikiria, akimaliza
tutawajulisha?” “Naomba usiwe unalewa James. Mimi pombe sipendi.” “Sawa.” James
akakubali haraka bila shida mpaka akamshangaza Jema. “Sawa nini sasa!?”
“Nisilewe. Au?” “Na ujitahidi kuacha. Mimi nakuombea uache.” “Sawa.” James
akakubali tena.
“Sasa kwa
nini unakubali kila kitu!?” “Ulitaka sasa nifanyaje na mimi leo ndio
nimekamatwa na ‘udhaifu’? Si ndio nakubali kila kitu.” “Si kwa vibaya.”
James akabaki akimtizama, Jema akaanza kujisikia kusutwa. “Zile sifa zote
zimefutwa kabisa?” “Mimi nakupenda James.” “Ila unataka kwenda kunifikiria
kwanza?” Kimya. “Ila ujue mimi sitakufanyia hivyo Jema. Nikikutana na
kitu ambacho sikukitarajia kwako, sitakukimbia. Nitazungumza na wewe
kama ni kitu cha kurekebisha, urekebishe na kama ni cha kukuombea, nitakuombea
lakini si kukukimbia. Sitafanya hivyo.” “Nakupenda James. Mimi
nisingekukimbia.” Jema akabadili gia. Lakini akawa ameshachelewa. James
alimuona vile alivyotaka hata kuvua pete. “Ndicho ulichotaka kufanya Jema!
Umenifanya nijisikie sipo salama kwako.” Yale maneno yakamuuma sana Jema
akajikuta anaanza kulia.
“Na kwa
taarifa yako tu, mimi nilishaacha pombe, ndio maana hujawahi kupata harufu ya
pombe mdomoni kwangu hata mara moja. Niliacha nafikiri ni miaka miwili imepita
sasa. Ila Danny amekaribisha wafanyakazi wenzetu ambao wao wanakunywa.
Aliponiomba kama alete pombe hapa, nikamwambia sioni kama ni tatizo. Kwa hiyo
usinikimbie sababu ya hilo.” “Mimi nisingekukimbia James, ila niliona ni
tatizo.” James akanyamaza.
“Nisamehe
James. Nitajifunza mpenzi wangu. Na kuanzia sasahivi nakuhakikishia nitakuwa na
wewe hata iweje.” Kimya. “Usinichukie James.” “Sijakuchukia ila
nimeingiwa hofu.” “Tafadhali usiogope tena James. Mimi ni wako. Niambie udhaifu
mwingine wowote, uone. Sitakimbia tena.” “Basi Jema. Leo nataka
ufurahi. Naomba acha kulia.” Jema akaelekea chooni na kujifungia mlango. James
akamsikia akiendelea kulia. James akasogelea mlango akakuta umefungwa kabisa na
funguo ndani.
“Mama
mwenye nyumba wangu! Wageni watakuja wanakutana na mama mwenye nyumba macho
mekundu, hakuna chakula.” Jema akaosha uso na kutoka. “Mimi nimejisikia
vibaya.” Akajilalamisha. “Ujisikie vibaya hivyohivyo.” “Sasa mbona hata hayaishi!?”
“Ubakiwe nalo rohoni kabisa, ili siku nyingine ukumbuke Jema. Tunasafari ndefu
sana mimi na wewe. Hujui ninakuaje ninapokasirika au kuchoka! Hujui nalalaje!
Naweza nikawa mbaya kwako kwa namna nyingine na pombe sinywi!”
“Nitakuombea mpenzi wangu. Ila mimi nikilala sikoromi. Na si kisirani hata
nikichoka.” “Basi mimi nikilala nakoroma sana.” “Basi acha nikakufikirie kwanza.”
Jema akamchokoza. “Ujue Jema usianze utani wakati hata hapajapoa! Umetoka
sasahivi kuonyesha unanikimbia halafu unanifanyia utani!”
“Mimi
naanza kujiona sipo salama na wewe James.” Akarudia maneno ya James
mwenyewe na kuendelea. “Jambo haliishi jamani! Sasa najiuliza nikiwa nakosea huko
kwenye ndoa, na pengine nimeshakuzalia mtoto mmoja, au ni mjamzito, nani
atanisitiri” James akashangaa sana. “Jema! Yaani hapahapa unanigeuzia kibao?”
Jema akaanza kucheka. “Mimi na wewe mpaka kifo James bwana! Tutabebana wala usihofu.”
“Muone!” Jema akacheka na kukimbilia jikoni.
Tumaini Jipya.
Ilipofika
jioni, kwenye saa kumi na mbili, mama James na binti zake wakawa wa kwanza
kufika hapo. Mpaka Jema akashangaa James alimaanisha nini juu ya mama yake.
Mama James akawa mwema kwa Jema kuliko mama G alivyofanya walipokwenda kwake. Akamfurahia
Jema kwelikweli na kuwapongeza sana yeye na James mpaka James mwenyewe
akashangaa. Wadogo zake walikuja wasafi na watulivu. Wakaonekana kumpenda Jema
na kutaka ukaribu naye. Heshima ya hali ya juu kwake. “Sisi tumewahi ili
kukusaidia wifi yetu. Tuelekeze kitu chochote chakufanya, tutafanya tu. Mama
hataki uchoke.” Jema akacheka. “Nashukuru mama yangu. Basi wewe kaa hapo
uzungumze na James, wakati sisi tukirekebisha mambo. Nakuletea kinywaji
sasahivi.” “Iwe maji tu. Tena mpe huyo Vai alete.” “Sawa mama yangu.” Jema na
wifi zake wakaongozana jikoni. James akawa anasikia vicheko tu huko kwa Jema na
wadogo zake, mpaka akashangazwa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Giza
lilikuwa limeshaingia nje wakati Joshua na Naya nao walipoingia. Wakamuona
Joshua akimnong’oneza kitu. Halafu akatulia. “Hujambo Naya?” Akamwangalia
Joshua. Jema naye akatoka kusalimia baada ya kumsikia James akisalimiana na Joshua
kisha Naya ambaye akaonekana hajui ajibu nini. “Usimpe shikamoo. Msalimie tu
kawaida ila mama yeye msalimie.” Akamuona ameshakosa raha kama aliyekwisha
changanyikiwa na mengi wakati ni salamu tu. “Unataka kunisaidia huku jikoni au
mezani?” Jema akamuwahi. Akamwangalia Joshua. “Wewe unataka nini? Maana huyu ni
Jema.” “Kama kumbukumbu inanijia Joshua! Ila haijakaa vizuri.” “Nisikilize
Naya. Hilo ni jambo zuri. Na uache woga. Fanya kile watakachokuelekeza.”
“Nikikosea?” Akawa kama aliyeingiwa na
wasiwasi tena.
“Tutakuwa
wote. Usihofu. Twende.” Jema alishaambiwa habari zake na Kumu mwenyewe ila
akaomba asije akatangaza kazini. Jema naye akawa muaminifu kwenye hilo. Akimsaidia
kazi Kumu ili awe na mkewe bila hata kuropoka kwa Fina. Kwa hiyo kazini kwao
hakuna aliyejua kinachoendelea kwa mke wa Kumu ila Jema tu. “Utakuwa na mimi
Naya. Na nitakuelekeza vizuri tu, wala usitie shaka.” Jema akazungumza naye kwa
utulivu, ili atulie. Akamgeukia mumewe. “Usije kuniacha Joshua!” Akamsisitiza
mumewe. “Sithubutu. Nitahakikisha jicho na masikio yangu vipo kwako muda wote
na nitakuwa nakuja kukuangalia kila wakati. Naomba ukamsaidie Jema.” Akakubali.
“Ila
hakuna kitu chakufanya Joshua. Mwache akae na wewe tu hapa. Kina Viola wapo na
Jema kumsaidia.” James akamuhurumia vile alivyoondoka akiwa amejawa wasiwasi.
“Nataka achangamke kidogo. Si umeona kumtoa leo amesema ameanza kumkumbuka Jema?
Acha afanye kitu cha tofauti. Atakuwa sawa.” “Ila amependeza! Amebadilika sana.”
“Nashukuru Mungu asiee. Mungu amenirejeshea mke wangu.” Mama James alivyoona
Joshua anakaa na James hapo sebuleni, akaona ni bora kuwaacha. Akahamia jikoni
walipokuwa wanae na Jema pamoja na Naya.
Baada ya
muda Jema akamuachia kazi Naya. Ila akaenda kumwambia Joshua amemuacha peke
yake, yeye anakwenda kujitayarisha. “Atakua sawa. Mwache tu. Si mlango wa nyuma
umefungwa?” James akasimama kwenda kuhakikisha mlago wa jikoni, wakutoka nje kama
kweli umefungwa na funguo kabisa, yeye Jema akaenda kuoga chumbani kwa James.
Wakwe.
Baada ya
muda tena wakaja ndugu wa Jema. Jema aliposkia
kelele zao akamuita mama yake akiwa mlangoni chumbani kwa James. Mama yake akamfuata
akasimama nje ya mlango. “Mmekuja na Jelini?” “Alivyoniambia yeye, atakuja.
Sasa sijui. Maana ilibidi kumtumia ujumbe na kumwambia. Ndio akarudisha majibu
hayo.” “Sasa asije akaja hapa usiku mwingi na amelewa.” Mama yake akabaki
akimwangalia kama vile anamwambia unauliza makofi polisi! Jema akaona ajiachie
tu. Akarudi chumbani, kaka yake akarudi kwa ndugu zake na kina mama James.
Wakashangaa
Naya amechangamka ndiye anayekaribisha wageni wakati Jema akijiandaa chumbani.
Joshua akafurahi kumuona vile. Akabaki akimsindikiza kwa macho kila anapokwenda
na anachofanya. James alimuona vile anavyomtizama mkewe kila wakati. “Kwa nini
unawasiwasi naye?” “Aisee sitaki kutendeke kosa tena. Anatakiwa kuchukuliwa
taratibu sana na simuamini naye na mtu yeyote yule. Naona watu wakimuona
amesimama vile, wanaona yupo sawa. Rahisi kumsahau. Na akiingiwa na hofu tu,
ndipo utagundua hayupo sawa. Kwa hiyo sitaki kufanya kosa. Jicho langu lipo
kwake masaa 24. Hata wafanyakazi pale nyumbani sitaki wakutane naye ili asiogope.”
“Joshua!” “Hakika katika hilo sizembei. Na ukimuona akiwa ameingiwa na hofu,
ndipo utaelewa ni nini nazungumzia James. Bado. Yaani leo nimemtoa makusudi nikijua
mimi mwenyewe nitakuwepo.” “Na yeye anakuangalia kila wakati kuhakikisha bado upo!”
“Nikiondoka tu hapa bila yeye kujua nilipo, utamuhurumia na kujua bado
anahitaji msaada.”
“Jana
usiku nilitoka kwenda kwenye gari, kuna karatasi niliziacha huko. Nikakutana
nazo, nikakaa kwenye gari nikaanza kuzisoma na kujisahau. Na mbaya zaidi nilisahau
kumuaga. Nikafunga milango na simu nikaacha ofisini. Nilirudi akiwa na hali
mbaya sana mpaka nikamuhurumia. Aliingiwa na hofu ya ajabu sana.”
Kina Magesa.
Wakashangaa
Geb na mama G wanaingia. James hakuamini. “Haiwezekani!” “Mimi nihangaike
kufunga na kuomba. Upate mke ndio unifukuze! Hakika hii harusi hainipiti. Wewe
utajuana na mdogo wako.” Mama G akapiga vigelegele, ndipo wangine wakapokea.
Gafla pakachangamka kwelikweli. Mama G akajaa hapo kama hawakufukuzwa asubuhi
yake. Geb akakaa kwenye kochi bila ya kukaribishwa. James akamtizama na
kutingisha kichwa. “Hongera James.” “Hivi wewe ninapokwambiaga jambo huwa
unanisikia lakini?” Geb akabaki akimtizama. “Geb?” “Nakusikia James, ila naamua
kutofanya kama unavyotaka.” Mpaka Joshua akacheka.
“Basi
bwana.” “Umenyanyua mikono?” Joshua akamuuliza akicheka. “Yaani asubuhi ya leo,
nimempiga marufuku kukanyaga hapa, yeye na mkewe. Nikisema asubuhi, namaanisha
ya leo. Akaonekana ameelewa! Nashangaa yupo hapa!” “Mambo ya familia ni
magumu James. Itabidi Jema ajifunze tu na kutuvumilia. Wewe sitakupoteza.”
Geb akajibu na kutulia.
Shuguli Watu.
Mara
ikaingia kelele ya Danny na wafanyakazi wengine. “Hawa wamenichelewesha.
Wameagiza nyama na vinywaji, mimi ndio nikabaki na kazi ya kuvifuata.” “Leo
tunakesha. James anaoa!” “Kesho kazini jamani.” James akawatahadharisha
akiwapokea. “Wewe tuwekee sisi viti nje, tuanze kunywa.” Wakasaidiana na Danny
na wadogo zake, wakawatolea viti nje. Wakaa wao tu. Ikawa ni kundi la wafanyakazi
wenzake James, Wakaanza kunywa na kelele nyingi. Wakibishana mambo hata yasiyo
maana. Kukawa na shamrashamra ikasaidia kutokuwa karibu kwa Danny na kina
Magesa. Danny akabaki na wafanyakazi wenzao muda wote huko nje, Geb kimya
kwenye kochi akiangalia tu. Mama G akawa na wakina mama upande mwingine.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Jema akatoka chumbani akiwa amependeza haswa.
Zikazidi shangwe. Akamuona mama G na kuingiwa hofu. Wakasalimiana vizuri tu,
lakini ukweli Jema alijitahidi kumkwepa hata yeye alijua. Kila alipojaribu
kumsogelea akaongeza shuguli akimpa tabasamu huku akimuonyesha ana hili na lile
lakufanya akihudumia wageni.
Baada ya
kuona kama wote walio waalika wamefika, James akaomba patulie na watu wote wakusanyike
sebuleni amtambulishe mchumba wake. Watu wakapiga vigelegele wakisogea.
“Nilishamchumbia asubuhi, kazini kwao. Naona baadhi ya picha nimeshatumiwa
wakati nikimchumbia asubuhi. Zitaanza kurushwa hapa sebuleni kwenye luninga.
Atakayependa kuona, karibu hapa sebuleni. Ila sasahivi nataka tu mumtambue. Na
mimi naoa jamani. Aliyekuwa akisubiriwa ni Jema. Ameshakubali, naoa.”
Vigelegele vikawa vingi. Mama G amechangamka kwelikweli, mwanae anamtizama tu,
kimya. Utambulisho ukaendelea hapo.
James akamtambulisha
mama yake kwa furaha zote na dada zake. Kisha
akamkaribisha Jema atambulishe ndugu zake na yeye akampa nafasi mama
yake mkubwa atambulishe wote waliokuja naye. Akafurahia hiyo heshima. “Mama
amefurahi sana. Ni hivi imekua gafla tu, ila anasema leo na yeye angekuwepo.”
Mama yake mkubwa akaongea hapo, akimuwakilisha bibi yake Jema pia. Ila ni kweli
mama James alikuwa amefurahi haswa. Kila mtu alimuona jinsi alivyokuwa mwema.
Akamletea Jema vitenge kama zawadi.
Jelini.
Jema
akawakaribisha chakula kwa kukiombea. Wakati kila mtu anasahani yake wakila,
Jelini akaingia. Jema akamtizama tu. “Sasa unakasirika nini wakati hata
sijachelewa!” “Umechelewa sana.” “Usafiri wa shida dada yangu. Nikisema
mnichangie na mimi ninunue gari, mnaanza…” “Usianze Jelini. Salimia bwana! Wewe
ukoje?” “Mamkubwa naye! Basi shikamoo.” “Wewe kwa nini mambo yako ya usiku
usiku?” “Basi ninunulie gari mama yangu mkubwa.” “Haya nenda.” Akaanza kucheka.
“Mimi nahama ukoo. Naenda kutafuta koo tajiri. Ukoo mzima mnashindwa kumnunulia
mtu mmoja gari!” Jema akabaki akimtizama.
“Nimepita
kwa haraka, lakini kule nje nimeona kama kuna bia za kumwaga! Acha nikachukue
ndio nije kushushia na chakula.” Mama yake hakumuongelesha kabisa, akabaki akimtizama
tu. Akaenda hatua chache mbele kisha akarudi. “Ila bwana Jema umependeza halafu
umeuchinja dada yangu. Pazuri hapa! Bonge la jumba! Hongera.” “Asante.” “Na
mimi natafuta mwanaume mwenye hela kama shem, anioe.” Ndugu zake wote wakaanza
kucheka kwa sauti. “Tatizo lenu nyinyi dharau. Na kwa taarifa yenu naweza sana
kuwa mke wa mtu na nikatulia.” James akasikia sauti yake maana
alipitia mlango wa jikoni. Akaamua kwenda kumsalimia.
“Hujambo
Jelini?” “Sijambo shemeji wangu wa nguvu. Hongera, nyumba yako nzuri kama wewe
mwenyewe.” Jema akashituka sana. “Mama!” “Sasa mimi hapa nimefanyaje!? Si
nimemsifia tu!” “Wewe nenda kafuate bia nje.” Mama yake mkubwa akamfukuza. “Eti
shem naweza kwenda?” “Kuwa tu huru. Ila nilitaka kukutambulisha.” “Umeona mambo
hayo? Twende mwaya shemeji yangu. Huwezi jua, harusi ijayo inaweza kuwa yangu!”
Ndugu zake wote wakaguna, wengine wasiomjua wakacheka. “Watu hawana imani
jamani! Jema dada yangu ataniombea.” “Utapata wa kanisani.” Mama yake mkubwa
alimfanya Jelini acheke mpaka akakaa chini sakafuni. Wote wakaanza kucheka.
“Basi
Jema dada yangu. Yale maombi sitaki tena. Acha nitatafuta mwenyewe.”
Mpaka Jema na James wakacheka. “Jelini!” “Wee mamkubwa, sasa hivi nipate
mlokole mimi si msala huo! Nafanyaje naye mimi.” “Wewe si unataka ndoa?”
Mama yake akamuuliza. “Siyo kihivyo mama na wewe! Kwamba iwe adhabu! Usiombe
mwaya Jema. Tuache nitatafuta wakufanana na mimi.” Wakazidi kucheka.
“Si ndio
hivyo ilivyoandikwa kwenye vitabu vya Mungu?” “Ni bibilia Jelini.” “Hukohuko.
Nitapata wakufanana na mimi. Twende mwaya shem ukanitambulishe kwa sampuli za
wanaume kama wewe.” “Wakoje?” “Shem kasoma na anahela.” “Sasa uwe na kiasi
kuanzia maneno na vitendo.” “Basi twende wote Jema. Maana wewe huniamini.”
“Tunakujua wewe.” “Utakuwa sawa tu, twende.” “Afadhali wewe una imani na mimi, shem.”
Akanyanyuka kutoka hapo sakafuni alipokuwa amekaa.
“Umependeza
mwanangu Jelini!” “Lakini kawaida yangu mimi. Ushanikuta nipo hovyo?” “Hata
siku moja.” “Biashara matangazo, mamkubwa.” “Sasa na wewe unaendeleao
kumuongelesha huyo ujue unamfanya
asimame hapo aendelee kuongea, na kunyamaza huyu hawezi. Mnayemchosha ni
James.” “Bora mama.” Jema akadakia. James na Jelini wakaondoka hapo. “Ana moyo
wa ajabu huyu!” Mama yake mkubwa akaongeza. “Anaweza kukufanya ukasirike, halafu
yeye hasira yake sekunde. Kashamaliza na kashakusamehe na kukutaka ushoga
hapohapo.” Jema akaongeza.
Wakamsikia
akisalimia huko sebuleni kwa heshima. “Kama mtu vile!” Wote wakacheka
wakimsikiliza. “Ndiyo, mimi mdogo wake. Sema mimi sijulikani sana sababu kwetu
mimi ndio mpole sana.” Ndugu zake walicheka mpaka James. Ilibidi Jema
aende huko sebuleni. Akamkuta ametulia kama siye yeye. “Nashukuru kuwafahamu,
ila kuna sehemu shemeji ananipeleka. Acha mimi niwaache.” James akawa hajaelewa
wanakwenda wapi.
Akamvuta
pembeni. “Twende ukanitambulishe kule nje kwenye bia za bure. Ili niwe huru
kuchukua wasije sema mimi mwizi.” James akatoka naye akicheka. Jema akamuita.
Akarudi akichungulia mlangoni. “Na urudi hapa Jelini.” “Raha ya pombe ni unywe
na wanywaji.” “Usinitanie Jeline! Angalia maneno yako huko na vitendo.” “Jema
naye! Mbona hapo sebuleni nimekutana na wasomi sana, na wanaonekana wanamahela
lakini nimekua mstaarabu?” “Basi na huko nje ikawe hivyohivyo na urudi hapa.”
“Havina hata raha!” Akaondoka akilalamika. “Na Jema angalau anamuwezea. Atarudi
tu.” “Akirudi James hapa bila yeye, namfuata.” Wakacheka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Walipowakaribia tu, Kasa akaanza. “Mtoto
mzuri huyo! James umemtoa wapi?” “Mdogo wake Jema.” “Acha masihara! Kabisa?”
“Sasa wewe huamini nini?” Jelini akaanza. “Mimi hapa, mdogo wake Jema. Basi,
tushamaliza utambulisho.” “Sasa hutaki kufahamiana?” Kasa akaendelea. “Akuu!
Mimi sitaki kufahamiana na wewe. Labda yule pale.” Akamnyooshea kidole, Colins,
mmoja wao. Wote wakamgeukia. Colins alikuwa ameinamia simu yake akamtizama
Jelini. “Huyo hapo akitaka tufahamiane, ndio nakubali. Ila wewe sitaki.”
Mpaka James akapoa. Kasa! Anavyopenda sifa! Leo umkatae mbele za watu!
Ila
akajikaza na kuuliza. “Kwani mimi nina nini?” “Yule pale anaonekana akikufahamu
anakuwa anakupenda. Halafu anakuheshimu na kukupenda. Anakutunzia heshima
halafu mzuri. Wewe msumbufu halafu sikutaki tu kukufahamu.” “Mimi sina kitu.
Kasa ndio anaweza kukutunza mtoto mzuri kama wewe.” “Akuu mimi sitaki kutunzwa.
Na uache kujiliza shida. Mimi mpaka nitajuta bwana! Utakua sio mchumba wangu
tena.” Vikaanza vicheko vile Jelini alivyokuwa akiongea. Lakini kila mtu alijua
Kasa amekasirika sana.
“Basi
shem nisaidie kubeba tuondoke. Jema atanifuata mwenzio, halafu aanze
kunigombesha. Si unamjua mkeo?” James akacheka akitingisha kichwa. “Hawa rafiki
zangu wote hawa. Tunafanya nao kazi.” “Sio wewe niliyekwambia nitafutie mchumba
ukasema wote wameoa!? Mbona sasa yule pale hajaoa?” “James anatubania!” “James
hataki na sisi tuoe!” Kila mtu akamlalamikia kivyake.
“Twende
shem. Jema atakuja sasahivi halafu atataka niondoke nikalale nyumbani wakati
mimi ndio kumekucha.” “Jelini mtoto mzuri njoo unywe hapa na sisi.” “Akuu! Jema
mimi kanikataza. Labda huyu hapa ndio…” “Anaitwa Colins.” Danny akamsaidia kwa haraka.
Acha Jelini aanze kucheka. Akacheka mpaka na wao wakaanza kucheka. “Bwana
mchumba wangu mimi anajina zuri! Colins! Sasa hilo nitalitengeneza vizuri
zaidi.” Wote wakazidi kucheka na Colins naye akawa anacheka tu. “Hutamuita
Colins?” Mmoja wao akaendelea kumchokoza. “Akuu! Kwanza hata wewe unalitamka
vibaya!” “Wewe ungeitaje?” Acha aanze kucheka tena. Na wenyewe wakawa wanacheka
kama yeye.
“Jelini?”
Akashituka sana baada ya kusikia sauti ya Jema akimuita. Wakamuona cheko yote
imeisha. “Si nilikwambia shem mimi? Ona Jema huyo! Basi zungumza naye
asinirudishe nyumbani!” “Basi ndio ukaitike. Mimi nitakujia na vinywaji.” “Moyo
wangu ushakosa raha! Nishaanza kuona dalili za kufukuzwa hapa wakati
mimi sijafanya kosa! Naonewa tu.” Wakamsikia akilalamika huku akiondoka.
Huku nyuma
wanaume wote wanatoa macho. “Acheni bwana! Huyu mtoto mdogo sana jamani.”
“James naye! Mgumu hata kwa shemeji yake!” “Kwani si tunaangalia tu!” Wanamjibu
hivyo James lakini bado macho kwa Jelini. “Muulize shem kama mimi nimeongea
jambo baya pale zaidi ya salamu! Utanionea bure masikini wa Mungu mimi!”
Wakamsikia akijitetea hata kabla hajaulizwa. “Haya, nenda kakae pembeni ya mama
yako mzazi. Nisikuone ukinyanyuka mpaka mnaondoka.” “Sasa Jema hapo unakasirika
nini jamani!? Na ujue nimekuletea zawadi ya hongera.” “Muongo.” “Tatizo lako
wewe huniamini. Sasa unafikiri…” Wakapotelea ndani.
“Daah!
Pombe yote imeisha!” “Bwana mtoto mtamu huyu! Sema kampenda Colins. Mimi
ningempa hata gari!” “Mimi roho yangu kabisa aishike mkononi.” Kila mtu akaanza
kutaja lake lakini Jelini kamchagua Colins. Wakaanza kumtania Colins anabahati
ya mtende. Kapendwa na Jelini halafu wala hakuwa akiongea. Jelini kafanya
kumteua yeye. “Sikuwaambia mimi kama Colins ana kimzizi?” Wakazidi kumtania.
Zile sifa zikazidi kumuumiza Kasa. James akachukua chupa baadhi za bia,
akaona awaache wenyewe, akijua hawatamudu hiyo hasira ya Kasa hapo baadaye
pombe zikiwaisha. Colins alikuwa kama Kasa na baadhi ya wengine. Wao hawakuwa
wakinywa pombe, stori tu, ila Kasa akijigamba kwa hili na lile wengine wakinywa
na kumsikiliza Kasa mpaka Jelini alipokuja na kumkata kauli.
Alimshushua
mbele za wanaume wenzake alipokuwa akijingamba kwao kujionyesha yeye bora!
Kasa! Eti hamtaki Kasa ambaye anajiona bora kuliko mwanaume yeyote yule kwenye
ile kampuni nzima! Ikamuuma vibaya sana. Jelini akawa ameiba furaha yake yote
usiku huo. Ila ukweli Kasa alitokea kwenye familia ya kitajiri sana hapo
nchini. Baba yake ni wale walioweza kushika pesa, na pesa ikatulia mfukoni mwao
miaka na miaka hata kabla kina Colins hawajaja duniani.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Nini Kitaendelea? Usikose muendelezo.
Kikaoni! Kasa! Jelini! Colins! Na maandalizi ya harusi.
0 Comments:
Post a Comment