~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
James
aliambiwa kuchelewa iwe mwiko. Ilipofika saa 12 kamili jioni hiyo akawa ameshaegesha
nje ya nyumba aliyokuwa akiishi Jema. “Sikutegemea kama utafika kwa urahisi
hivi!” “Kwako hapapotezi. Rahisi kama ulivyonielekeza kwa ujumbe. Umependeza
sana Jema.” “Nilikuwa najishuku! Sijui nitokaje.” “Umependeza sana.” “Wewe
umebadilika sana James. Tokea tukutane kwenye harusi ya Joshua na nilipokuona
majuzi! Hakika ningekukuta sehemu nyingine nisingekutambua.” “Nimebadika vibaya
au vizuri?” “Vizuri sana. Na leo zaidi. Umependeza na unanukia vizuri sana.”
Ushauri wa Geb ukaanza kulipa. “Asante. Twende basi. Au bado?” “Nipo tayari.”
Wakatoka.
James
akawa muungwana kama alivyofundishwa na Geb. Akamfungulia mlango na kumfungia.
Jema akawa wakucheka moyoni haamini. Hakutaka hata kuuliza wanapokwenda ila
kufurahia tu. “Gari yako safi!” “Siitumii mara kwa mara, natumia ya ofisi ndio
maana unaiona hivyo.” “Ila na wewe unaonekana mtunzaji.” James akacheka na
kushukuru kwa sifa. Kimya mpaka sehemu aliyochagua James.
“Hukuniambia
una hamu ya kula nini. Na mimi nilitaka leo ule maana umeniambia haukuwa ukila
vizuri. Kwa hiyo nimepachagua hapa makusudi kwa kuwa wanavyakula vingi, na hata
kama hamna, wanatoa nafasi ya kutaja unachotaka, wanakupikia.” Jema akacheka
kwa furaha. “Nashukuru kujali James. Asante.” “Basi twende tukapate muda wa
chakula.” Wakati James anataka kwenda kumfungulia mlango, Jema akawa
ameshashuka.
“Nikusaidie
kubeba pochi?” Jema alicheka mpaka akainama. “James!” “Mimi nimeuliza tu.” “Ni
ya urembo!” “Kwa hiyo?” “Sasa si ndio viendane na nguo!” “Mimi sina shida hata
yakubeba karibu na nguo yako ili bado umachi, upendeze.” “Hii pochi ni ya kike
James!” “Na wewe mwenye nayo si utakuwa ukitembea pembeni yake?” Jema akazidi
kucheka. “Bwana James acha bwana!” “Ni katika kutaka kusaidia tu. Ila kama
unapenda kubeba kipochi chako mwenyewe, basi twende.” Wakaingia wakicheka.
James
alikuwa akikumbuka kila kitu. Akamvutia kiti, akakaa. “Asante James. Ndio upo gentleman
hivyo!” “Ni vile uliharakisha kushuka garini. Lakini pia ningekufungulia na mlango.”
Jema alicheka sana. “Nilikuja kukumbuka wakati nishashuka, nafunga mlango.
Nikajiambia ni ushamba tu.” “Basi ukiwa na mimi usijali maswala ya mlango.”
“Ndio itakuwa kazi yako?” “Bila shida.” “Inamaana safari kama hizi niendelee kuzitegemea?”
“Sana tu.” Jema akamwangalia kama ambaye hana uhakika.
“Ahadi
hii ni wewe wa kwanza kukupa, na sina mpango wa kumpa mwingine. Nanaa
yeye hajawahi pewa hii ahadi ila kwake nawajibika.” “Kivipi?” “Nanaa ni kama
mtoto wangu. Nimemlea tangia anatolewa hospitalini, baada ya mama yake kufariki
akiwa anajifungua yeye. Acha tuagize kinywaji kwanza.” Wakaagiza na mpaka
vyakula.
“James!
Ukisema kumlea unamaanisha nini?” “Kama mama. Yaani mimi ndiye nimemsafisha
mpaka kitovu cha uchanga na kikakatika mikononi mwangu. Kumlisha na kumuogesha.
Nimemtunza mpaka kumfikisha kwa Geb.” Akamsimulia kwa kifupi na kumfanya Jema
avutiwe zaidi. “Ndio maana upo hivyo James!” “Nikoje?” James akamuuliza
akicheka. “Una upendo fulani hivi! Ambao na mimi jana nikaona upande wako
mwingine. Unajua kumtuliza mtu kwa namna fulani hivi. Unabembeleza.” James
alicheka sana.
“Kweli
James. Jana nilishindwa kuelewa aina ya ule upendo, lakini sasahivi ndio
nimekuelewa kwa nini upo hivyo. Nilikuwa na hali mbaya! Chakula kilikuwa
hakipiti kooni na nilikuwa nikilala kwa dawa za usingizi.” “Haiwezekani Jema!
Ndio ilikuwa mbaya hivyo!” “Acha James. Nimelizwa mpaka machozi yamekauka.
Natamani kulia sina machozi. Halafu sasa sina wa kumlilia. Mama niliye naye
alishanionya sana, ila sikumsikiliza. Aibu, sina pakuficha uso, ila
kazini. Ndio maana Kumu alipotingwa na majukumu yakifamilia, nilishukuru sana.
Nikafanya hata ambayo hajanituma! Ilimradi tu kupoteza mawazo.” “Pole sana.
Ilikuaje?”
Historia Ya Jema.
“Sisi
tumezaliwa watoto wakike wawili tu. Mama hakuolewa, alituzaa kila mmoja na baba
yake. Akatulea yeye mwenyewe. Au tuseme anatulea mpaka sasa, maana mdogo wangu
yeye bado yupo kwa mama na bado anamtunza. Mwenzangu alikataa mambo ya shule
mapema tu na akazaa. Mtoto wake wa kiume ndio kama mtoto wa mama. Mama anamlea
na kumsomesha.” “Kwamba ndio mkubwa kiasi hicho!?” “Mama anasema anahisi
alipovunja tu ungo akashika na mimba. Hata yeye mwenyewe ni mdogo tu. Wala si
mkubwa. Anyway, mama yangu ni mkristo jina. Hana mambo ya kanisani,
anasema ni utapeli.” Jema akaendelea, James akisikiliza kwa makini akijua
katika hiyo historia, yatajibiwa mengi. Akaongeza umakini.
“Mimi niliokoka
nikiwa sekondari. Kidato cha 3 mwishoni naingia cha nne. Mama akalipinga
sana hilo. Akawa ananiambia nakaribisha ujinga kwa wakati ule ninaohitajika
sana shuleni, nitaishia kujichanganya na kuharibu maisha yangu. Wakati huo
angalau mimi ndiye aliyekuwa akinitegemea kwenye mambo ya shule, tuseme
nilikuwa nikijitahidi shuleni kuliko mdogo wangu. Ubaya ulikuja nilipomaliza
kidato cha nne, nikafeli. Mama aliumia sana. Akalalamikia wokovu
ndio umeniponza. Maana matokeo mengine yote ya nyuma nilikuwa nikifanya vizuri
tu mpaka hayo ya mwisho yaliyochanganyikana na wokovu ndipo nikafeli. Mahusiano
yetu yakabadilika kabisa. Sio marafiki tena kama zamani. Akawa akichukia nikiwa
naenda kanisani. Nilikaa nyumbani zaidi ya mwaka, ananiambia hawezi kunisomesha
tena kama bado naendelea na mambo ya wokovu.”
“Lakini
sijui ilikuaje James! Nilikutana na Yesu kwa kipekee, nilikuwa siwezi
kuacha. Nilikuwa nimefika sehemu ni bora kukosa kila kitu nibakie na Mungu
wangu tu. Na ukumbuke injili ya wakati ule tuliyokuwa tukihubiriwa ilikuwa
tofauti na hii ya sasahivi.” James akacheka. “Ya sasahivi ikoje?”
“Imechanganywa kiasi ya kwamba haimpi mtu pumziko ila inakuwa kama
mwanadamu ameongezewa vita na shetani. Anahubiriwa aokoke, akishakubali
kumpa Yesu maisha, kisha inakuwa kama yale Yesu aliyokuwa akiwaambia wataalamu
wa sheria ambao ni kama hawa wanaojiita watumishi wa Mungu wanao aminiwa
sana na kizazi hiki.” James akawa bado anataka ufafanuzi zaidi.
“Kitabu
cha bibilia, Luka 11 pale. Kuanzia mstari wa 46, Yesu alikuwa akiwaambia
wataalamu wa sheria kuwa, ‘Ole wenu, kwa sababu mnawatwika watu mizigo
mizito ambayo hawawezi kubeba, wala ninyi wenyewe hamwinui hata kidole kimoja
kuwasaidia.’ Mstari wa 52 anaendelea kusema hivi, ‘Ole wenu
ninyi wataalamu wa sheria, kwa sababu mmeuondoa ufunguo wa maarifa. Ninyi
wenyewe hamkuingia kwenye ufalume, na wale waliokuwa wanaingia mkawazuia.’ James
akaanza kucheka akawa ameelewa.
“Kweli
James. Sasahivi kila mtu anatumia vibaya bibilia kujipatia wateja.
Wanaona wakisema kazi aliyofanya Yesu pale msalabani tu inatosha,
inamaana hawatapata watu wakuwategemea wao. Wanatafuta kufanya watu
mateka ili kuwa na wateja wengi watakao jinufaisha nao. Kujipatia wateja
wakudumu wakitumia bibilia lakini maneno yao. Sisi tulikuwa tukihubiriwa wakati
ule, ukiokoka unawekwa huru kwelikweli. Nikutembea kutokana na
kanuni za kibibilia tu, na hapo utakuwa salama. Kama, asiyefanya kazi,”
“Asile.” Akamalizia James.
“Ewaaa!
Sasa siku hizi hawa wahubiri badala ya kufundisha watu kweli, na kanuni
za kibiashara, kuwa kutofanikiwa mara ya kwanza na ya pili ni jambo la kawaida.
Angalia makosa, rekebisha. Hawataki kuwaambia hivyo watu, wanawafunga na
kuwaambia ni laana. Labda ya ukoo, au mambo waliyofanya nyuma na
mambo yanayofanana na hayo. Basi mtu anakazana kwenye kuomba. Kufuta laana za
ukoo, kutubu na mengine mengi wakijitakasa mpaka vitomvu! Lakini huyu mtu aliye
kwama kwenye biashara, hatafundishwa kanuni za waliofanikiwa kwenye
biashara, au kwenye ajira, ufugaji, ndoa na mengine yanayofanana na hayo ila kuongezewa
kifungo. Watamwambia afunge na kuomba. Atoe laana za ukoo. Ajitakase.
Ajiunganishe na madhabahu fulani na mazinga ombwe mengi tu, wakihangaikia mafanikio
haya ya mwilini wanayoita ni BARAKA.”
“Siku
hizi mtu akitafuta mafanikio kwenye chochote kile na kukwama kidogo tu, bila
kujali ukiukwaji wa kanuni kwenye njia nzima alizotumia mpaka kukwama kufikia
yale mafanikio, basi wanapunguza nguvu ya Msalaba kabisa. Wanawatafutia matatizo
yanayosikika ni ya kiroho kabisa, kuwafanya wawe nao makanisani au kwenye simu kuwaombea.
Huyu mtu anakua na kazi ya kuomba huku akipingana na kanuni alizoweka
Mungu mwenyewe na wakihangaika kufanya alichokifanya Yesu msalabani. Uhuru
tuliotangaziwa kupewa baada ya kumpokea Yesu, wao wanaweka pembeni na kuanza
kupigana na shetani kwa maneno mengi wakiutafuta uhuru huohuo.” James akacheka
sana.
“Inauma!
Acha tu James. Huyu mtu ambaye ameshaokolewa, amewekwa huru,
badala afundishe kuishi maisha ya ushindi ndani ya Yesu,
anafundishwa jinsi shetani alivyo na nguvu. Na anaweza kuwashinda wakati wowote
kama hawajapigana naye vita yakutosha. Unajiuliza hizi injili wanatoa wapi,
mbona hata Yesu mwenyewe hakuhubiri hivyo! Hizo laana, mtu aliyeokolewa,
na bibilia inatamka wazi kabisa, unakua kiumbe kipya, hizo
laana wanazowaanzishia hawa walioitwa ni warithi pamoja na Kristo
wamezitoa wapi? Unajiuliza, hivi kazi nzima ya msalaba, mateso yote aliyopitia
Yesu ilikuwa ni nini? Yesu aliposema IMEKWISHA, alimaanisha nini kilikwisha, na
nini kilibakia? Bibilia inaposema mtaijua kweli nayo itawaweka huru!
Mbona hawa watu hawawekwi huru? Mbona hata hawaitafuti kuijua hiyo kweli
yenyewe ila kutafuta kazi za shetani mchana na usiku?”
“Tunarudi
kulekule mtume Paulo alipowakemea Wagalati mpaka akawaita wapumbavu.
Ilikuwa ni kama hivi injili hii ya sasa. Paulo alipita akawahubiria injili
nzuri tu. Wakaamini. Paulo akaondoka, wakaja wahubiri wengine waliowaambia kama
hivi watu wanavyoambiwa sasahivi. Kuokoka tu haitoshi.
Mnatakiwa kufanya hivi na vile. Washirika walewale walioamini injili ya uhuru,
ya mtume Paulo, wakaja tena wakaamini injili hii ya kujishugulisha kama hii ya
sasa. Wakafuta yote waliyohubiriwa na Paulo, wakaanza kufanya kama watu
wa leo wanavyofanya. Kuombea mambo ya mwilini kabisa. Kujiunganisha na
madhabahu. Kupanda mbegu. Kujipaka mafuta na mambo mengiiii kama ushirikina tu ila unafanywa kanisani!” James
akacheka sana.
“Hakika
siongezi James. Kasome kitabu cha Wagalatia. Alichokikemea Paulo, ndicho
kinachoendelea sasahivi kanisani. Badala mshirika awekwe huru, ndio wamejawa na
vita na shetani mchana na usiku. Sikiliza maombi yao. Ni vita na shetani,
wakijikomboa katika kila eneo la maisha yao ambayo Yesu alishalipia garama,
mpaka unawahurumia. Wanaishi kwa hofu kuliko mlevi anayekesha baa. Unaweza
kumwambia mlevi atoke baa arudi kwake usiku akitembea, akarudi kwa amani kabisa
akipiga miluzi kuliko mshirika aliyeokolewa. Wamejawa na hofu. Shetani
yupo midomoni mwao kuliko Mungu. Wanajua nguvu za shetani kuliko
uwezo na mamlaka ya Mungu kwao. Roho mtakatifu tuliyeachiwa sisi
atusaidie, hawana habari naye, wapo kwenye vita na shetani wakijikomboa
mchana na usiku. Hakika inaniuma.” “Mbona na mimi nayaona sana tu. Najua
unachozungumzia.” James akaongeza akicheka.
“Anyway.
Binafsi nilikutana na wokovu ule wa kina Paulo na Yesu. Hakika nilitulia kabisa
nyumbani nikiwa na pumziko nafsini mwangu. Nikijua nimekua kiumbe kipya.
Nikaamini andiko linalosema nimehamishwa kutoka kwenye ufalme wa giza, na
kuhamishwa katika ufalme wa mwana wa pendo lake. Nimesamehewa dhambi.
Sina laana na mikosi yangu yote imabadilishwa kwa kazi ya msalaba. James,
nilikuwa na amani na utulivu wa hali ya juu. Sina hofu nikijua uhai wangu
umefichwa ndani ya Yesu. Si mimi tena ninayeishi, ila Kristo
ndani yangu. Namtegemea Mungu tu. Vita zangu zote nikamuacha Yeye.
Namtii mama kwa kila kitu. Nafanya kazi pale ndani bila hata kutumwa, ila
kanisani sikuacha kwenda. Naomba hapo ndani, asubuhi na jioni. Nikipata tu
kinafasi, napiga kabisa magoti, naomba kuwa na ushirika na Mungu wangu. Basi
mama akinikuta hivyo anazidi kukasirika. Tukaendelea hivyo, huku akinihakikishia
hatanisomesha. Nikatulia tu. Maisha yakaendelea.”
“Nakumbuka
dada yake alikuja kumwambia ni bora vile naenda kanisani kuliko ningekuwa
nakimbilia kwa wanaume kama mdogo wangu. Akamsema wee, ndio ikawa kama mama
amefunguliwa macho. Akaniambia hana pesa ya kunirudisha shule hizi za
sekondari. Ila anaweza kuhangaika anipeleke nikafanye kozi fupi itakayonipatia
ajira. Tukaanza kufikiria kitu gani chakufanya. Ndio nikasomea mambo ya Masoko
kwa Mwaka mmoja tu.
“Sasa katika
huko kutafuta ushirika na Mungu, kumjua zaidi, ndipo nikajiingiza kwenye kanisa
nililolipenda kwa sababu ya neno. Kama nilivyokwambia, kwetu tulikuwa wakristo
jina.” “Kwamba mama hakuwa akienda kanisani?” “Si krismasi wala pasaka. Labda
kwenye harusi alizoalikwa na misiba ya watu.” James akacheka. “Kwenye hilo
kanisa ndipo nilipokutana na Temu. Na yeye alihamia kwenye hilo kanisa. Hapo nishamaliza
chuo huo mwaka mmoja, mama amenitafutia kazi pale Coca. Akanifuata na kutangaza
nia. Kwamba anataka kuja kunioa.”
“Anyway,
nilisikia watu wakisema upande wa wakina mama wanamkosi huwa hawaolewi.
Ndio maana bibi aliachika, mama na dada zake hawajaolewa. Sasa mimi
nilimuombaga Mungu nikamwambia anisaidie nije kupata mwanaume mcha
Mungu, tuone nije niwe na familia. Isiwe kama kina mama. Maana
kwao kuna waliosoma na wenye hali nzuri tu kama kina mama yangu. Nikimaanisha
wanaoweza kuyamudu maisha yao, ila wote hawajawahi kuolewa. Alipokuja Temu,
nikafurahia sana na kujua Mungu amenipa haja ya moyo wangu.”
“Nikaingia
na moyo wangu wote. Tukaanzana na Temu.
Ila nafikiri niliharibu tokea mwanzo wetu.” “Kwa nini?” “Nilikuwa muwazi sana
kwake, na yeye hakuwa mwanaume au niseme mwanadamu mwema. Alitumia
niliyomwambia vibaya.” “Ulimwambia nini?” James akaendelea kudodosa akinywa
kinywaji chake taratibu. “Nilimwambia, kuna makosa yametendwa kwenye familia
yetu, sitaki kurudia kosa. Kwamba namlilia Mungu anipe mwanaume
atakayenioa. Na ambaye atanisubiri mpaka ndoa. Kwa kuwa sitaki kuja kuzaa nje
ya ndoa. Basi Temu akaanza kama mcha Mungu haswa na yeye akasema anataka
kusubiri mpaka ndoa. Nikampeleka mpaka kwa mama. Mama alipomuona tu, akamwambia
wewe ni mlokole tapeli.” “Kwamba alimwambia mwenyewe!?” James akahisi
hajamuelewa.
“Hivi,
usoni kwake. Nikiwa nimempeleka kumtambulisha kwake. Nilichukia James, ikawa
chanzo cha ugomvi wangu tena na mama. Nikaacha hata kumtembelea. Ila akawa
akinipigia simu kunijulia hali na kunihimiza kazi, ‘si kubweteka hapa mjini.
Wanaume hawana pesa, matapeli tu, hawajui kuhonga, maneno mengi tu ya bure. Wanaume
suruali,’. Na mambo mengi tu anayosema anayoyajua kwa wanaume wa mjini.” James
akacheka.
“Wewe
acha aisee. Nina mama na nusu. Lakini ukweli ni muhangaikaji, anayependa
kujishugulisha si kukaa tu bure. Na akiamua kufanya jambo, hata kazi ya mtu,
hutakuwa na pakumlaumu. Anafanya kwa nguvu zake zote na akili zake zote.”
“Ndiko ulikorithi?” Jema akacheka. “Labda, ila naona yeye amezidi. Basi uchumba
ukaendelea na Temu kila anayetufahamu anajua tumechumbiana. Akashauri tununue
kiwanja. Wazo si baya. Ila sasa yeye hana kazi ya kueleweka. Pesa hana, kiwanja
alichoniambia amepata kipo maeneo mazuri kweli, bei kubwa. Nikakopa benki kwa
mshahara wangu. Tukanunua. Ikaanza kazi ya ujenzi.” Akamuona anacheka na
kutingisha kichwa.
“Nini?”
“Hivi unajua nilijimaliza haswa! Isingekuwa safari anazonipa Kumu, ningekuwa
mtu wa kuishiwa hata sina mafuta ya gari. Lakini nikajikaza. Bwana Temu ni
mkali. Simu zake na jumbe hataki zisubiri.” “Ndio maana ulinishangaa mimi!”
“Bwana anaweza akaanza kugomba, na hapo unasubiriwa na Kumu, yeye anagomba
hujajibu au kupokea simu kwa wakati.” “Na anakuwa na dharula?” “Dharula yake pesa.
Kila ukigeuka pesa ya ujenzi. Nikawa nikiishi kwa wasiwasi, na katumaini
kidogo kuwa najenga kwetu. Watoto wetu watapata kwao. Tukaendelea
hivyohivyo huku nikimtetea kuwa ukali ule ni kuchoka na ujenzi.” “Kwamba
alibadilika?” James akauliza.
“Hapana
James. Ni kule kujifariji tu maana nilifika mahali ilibidi kuepukana na uhalisia.
Nilijiona nimefika naye mbali, siwezi kurudi nyuma.” “Kifedha?” “Aisee sijui
James! Inawezekana, ila pia nafikiri aligundua madhaifu yangu, akajua kunibana
kwenye kona nikawa kama siwezi kutoka tena kwa hofu. Nikajikuta sina kimbilio,
yeye ndio amebeba majibu ya maombi yangu.” “Baba wa familia?” “Ndio ilikuwa
shauku yangu James. Pia nilishajiapa hata kwa mama, mimi nilazima
nitaolewa tu. Sasa ile hofu ya kuja kuachika, nafikiri ilinisumbua. Basi na
yeye sijui alishaona sina pakwenda!”
“Jamani
alikuwa mkali kwangu na mbaya zaidi hapendi ninachokifanya, anasema kazi ya
kitumwa nalipwa kidogo hata pesa haionekaniki. Gafla ikawa ni kama mimi sina
mchango mkubwa kwenye hiyo nyumba, anahangaika yeye peke yake! Hakuna utulivu,
mkali kweli akinisimanga kwa hili na lile hata mambo madogo kama kuchelewa
kupokea simu. Kwamba namuabudu sana Kumu, siwezi kumkatalia jambo.” “Jamani!
Hajui kwamba unawajibika kwake kama kiongozi wako!?” “Huna utakalomwambia,
akaelewa.”
“Haya,
tukaja swala alilonimaliza nalo kabisa kuwa mimi siwezi kuwa mwanamke wa
kuja kuwekwa ndani!” “Kivipi!?” “Sijui James! Ila anasema haiba yangu ipo kama
mama yangu, siwezi nikaweza kuwa mke wa mtu na kumtambua mume kama kichwa cha
familia. Mara awe kama ananisifia huku akinisanifu kuwa mimi ni jasiri kama
simba. Kwamba tukiwa ndani ya nyumba, tukiingiliwa au kukiwa na matatizo ya
kifamilia, eti basi mimi ndio nitakuwa nikikimbilia hilo tatizo, bila kupitia
kwa mume wangu!” James akashangaa sana.
“Mara
aseme eti mimi nina mtindo wakumfanya mtu ajisikie dhaifu kwa kuwa kila tatizo
nalifanya sio tatizo hata kama mwenzangu akisema ni tatizo kubwa, eti mimi napuuza
na kufanya aonekane dhaifu!” “Basi acha nikwambie kitu kingine anachokusifia
Kumu na kunifanya kunivuta kwako. Ni hicho anacholalamikia huyo mchumba
wako.” “Kitu gani!?” “Kumu anasema ni kiasi cha kukupa tu tatizo, wewe
unatafuta ufumbuzi na huna tabia ya kutolea sababu jambo wala kulalamika.
Utapambana nalo mpaka unafanikisha. Anakusifia kuwa, eti wewe ni wale wanawake
unaoweza kuwapa mahindi kwa chakula, lakini ukarudi na kuvuna shamba
zima.” Mpaka Jema akajisikia machozi kutoka.
“Kweli!?” “Kabisa.
Nisingekudanganya na ndio maana ikabidi kuanza kukuangalia kwa makini. Joshua
anajivunia sana wewe. Anasema katika wafanyakazi bora, wewe upo. Na usidharau
kazi yako Jema. Unafanikisha mambo makubwa sana, ni hivyo tu Joshua hawezi
kukwambia mara kwa mara usije bweteka. Na ndio maana nakwambia usijibadilishe
hata kidogo ila kujiongeza. Sasa mchumba anaendeleaje!?” “Acha kunisanifu
bwana!” James akacheka sana.
“Tena!
Mimi namuulizia mchumba Temu.” “Mchumba amempa mimba msichana mwingine.”
James akatoa macho na kicheko kikakoma.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Itaendelea..
0 Comments:
Post a Comment