“Sasa sio
unipe pafyumu ya kulingana na mshahara wangu halafu ikiisha nabakia..” “Acha
kujiliza James! Tumia pafyumu kila siku tena nzuri, sio zile unatumia halafu
ukitoka chumbani na yenyewe unaiacha hapohapo! Unatoka hunukii kitu!” “Sawa
Geb. Lakini nafanyaje kama hajanijibu?” “James wewe umepaniki na utaharibu.”
“Kwa nini tena?”
“Wanawake
hawapendi wanaume wasiokuwa na msimamo. Mbambaishaji na asiyejielewa na hili
hata Joshua tulikuwa tukizungumza naye na wewe ulikuwepo. Wanawake wanataka
uhakika wa usalama wao. James waliyekutana naye leo ofisini, ndiye huyohuyo
akutane naye kesho, hutatumia nguvu nyingi kumpata.” “Wewe niambie nifanye nini
kuanzia sasa.” “Wewe unataka kwenda umbali gani?” Geb akamuuliza.
“Acha
nikwambie ukweli Geb. Kuna vitu vilinivutia kwake tokea mwanzo. Ila nikaambiwa
na mtu wake wa karibu kuwa tokea anamfahamu alisikia anamchumba waliyekuwa
wakikaribia kufunga ndoa. Ila akashangaa siku zinaenda, kimya. Nikaona
nimuache tu. Sasa alipokuja leo na kuniomba nitoke naye kwa chakula, japokuwa
mwenyewe alisema ilikuwa ni kutoka yakawaida tu, lakini kuna jinsi
alikuwa kabla, nikahisi labda kutomjibu ndiyo au hapana tokea
mwanzo nilimuogopesha ndipo akajirudi kwa haraka akajitete ni ukaribisho wa kikazi.
Ila ukweli nataka kupata naye muda ili nimfahamu zaidi na kujibu swali kama
bado anaye mtu au la.”
“Basi
nenda umbali mrefu kidogo ila si kwa haraka usije kumuogopesha.” “Huu ndio
ujumbe nimemtumia, hajanijibu.” Akamuonyesha. “Inawezekana ameona au hajaona.
Na kama ameona, pengine anajiuliza maana yake. Ni mtoto wa kike, hataki
kuharakisha na kuharibu. Lazima kuonyesha unamaanisha huo ujumbe.
Usitume wa pili kwa haraka usije ukaonekana huna mipaka na upo desparate.
Tulia mpaka kesho uone atakujibu nini.” “Asante kwa pafyumu.” “Na acha kufunga
vifungo vya shati mpaka juu kama Jimmy anavyofungwa na mama yake akijitetea
anaogopa baridi kwa mwanae kumbe ni wewe ndio umemuharibu mke wangu. Unataka
kufunga tai?” “Geb umeniamulia!” “Muonekano una matter James. Mwanamke
anapenda mwanaume ambaye hatamuonea aibu mbele za wenzake. Fungua hivyo vifungo
viwili vya juu.” “Geb! Kifua kitaonekana!” “Unakificha kwani una matiti? Hata
cheni yako haionekaniki!” Geb mwenyewe akamfungua. “Geb!” “Na usifunge James.
Tafadhali uwe unajiwakilisha vizuri. Usiku mwema. Naenda kulaza wanangu.” Geb
akamuacha. Akaondoka akitamani kutuma ujumbe wa pili akakumbuka ushauri wa Geb.
Akatulia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kesho
yake mida ya saa nne asubuhi akapata majibu. ‘Nashukuru kwa kila kitu.’ James
akasoma akajua amejibu kwa jumla sana na ni kweli anamtega. ‘Ulipenda
ulichokula?’ James akaongeza hilo swali msisitizo wa kujali. ‘Niliamua
kwenda kulala tu. Hata hivyo muda ulikuwa umekwenda.’ ‘Basi wakati mwingine
itabidi tuwahi.’ Jema akarudia huo ujumbe mara kadhaa kama ambaye hajaelewa. James
akaelewa. Akaamua kuongeza ujumbe mwingine. ‘Huwa unapendelea vyakula vya
aina gani?’ ‘Si mchaguzi sana. Ni kama nikipata utulivu naweza kula kitu
chochote.’ ‘Utulivu wa ndani!?’ James akaongeza swali kuonyesha anazingatia na kuelewa
anachomwambia. ‘Naona umenielewa.’ James akacheka akiendelea kusoma.
‘Basi
tuanze kwa kuandaa mazingira matulivu ya nje kwanza ili tukapate chakula
pamoja.’ ‘Tafadhali usijisikie deni kwa kukuomba jana. Nakiri nilivuka mipaka,
ila sikuwa na nia mbaya.’ ‘Hakuna nia mbaya kwenye chakula. Na kama isingekuwa
miahadi ambayo nilishaiweka tokea mwanzo, ningependa kwenda kula na wewe.’
‘Kweli?!’ ‘Nisingekutafuta tena, Jema.’ Ikamgusa sana moyo wake
akatulia.
‘Najua huwa
unakuwa na majukumu mengi. Sitaki kukupotezea muda. Lakini jumamosi zako
zinakuaje? Tunaweza fanya jioni tu baada ya majukumu yote kuisha. Tukapata
sehemu nzuri, tukaenda kula.’ Akafurahi sana kusikia hivyo. ‘Sawa. Na asante.’ James
akashindwa kuelewa shukurani hiyo ni ya nini. ‘Japo sijaelewa shukurani ni
ya nini, ni sawa nikipiga simu ijumaa jioni.’ ‘Ni sawa kabisa. Na asante.’ James
akacheka.
Ujumbe mwingine
tena ukaingia kwenye simu ya James. ‘Asante kwa muda wako
sasahivi na asante kwa utayari wa kukutana jumamosi kwa chakula.’ Ikawa kama anamjibu
shukurani ni ya nini. ‘Karibu na mimi sikushukuru kwa
ukaribisho wa jana. Samahani na asante.’ ‘Haina shida na karibu.’ James akawa hajui azungumze nini tena, akaona awe na
kiasi. ‘Kazi njema Jema.’ ‘Na wewe. Uwe na siku
njema na mkono wa Mungu usiondoke juu yako.’
Hilo likamfanya James atulie atafakari kidogo ila akajibu. ‘Amina na kwako pia.’ ‘Amina.’ Ikawa mwisho wa kuchat japo wakafurahia huo mtiririko wa maongezi yao.
Jema
akajifikiria vile atakavyokuwa na James. Mawazo yakamfikisha mpaka aina ya
watoto atakao kuwa nao. Akawafananisha na watoto wa Nanaa. Alifika mbali akiwa
ameshakuwa mke wa James mpaka akajishitukia. Akaogopa na kusimama kwa haraka. “Nawaza
nini hiki! Ndio maana naishia kuumizwa.” Akatoka kabisa hapo ofisini kwake
akijionya asije fika mbali ambako atajiumiza yeye mwenyewe endapo James hakuwa
na nia ya kwenda umbali huo.
Ijumaa.
Aliisubiria
hiyo simu ya James mpaka akahisi amesahau. Mpaka anarudi nyumbani kwake usiku,
kimya. James hakuwa hata ametuma ujumbe. Ikamuuma sana. Akashindwa hata kuweka maji
mdomoni kwa wasiwasi na maumivu ya moyo. Akiwa anajiandaa kulala, ujumbe
ukaingia. ‘Samahani sijui nimechelewa sana? Naweza kupiga au tuzungumze kesho
mida mizuri kidogo?’ ‘Haina shida.’ Hilo jibu likamfanya James
ashindwe kuelewa. Aliuliza maswali mawili, amejibiwa hivyo! Asijue huo ujumbe
wake jinsi ulivyoeleweka kwa maumivu na kuzidi kumnyong’onyesha Jema aliyedhani
siku ya jumamosi ndiyo yakutoka, anasikia ndio siku ya kupigiwa simu! Akajihisi
ni mkosi. Uchungu ukamzidia moyoni. Akajisikia kuumia sana. “Kweli
sisi tuna mkosi wakutokuolewa!” Akasalimu amri kwa machozi
hapo kitandani akiwa peke yake.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akapiga
picha yale mazungumzo yake na Jema nakumrushia Geb. ‘Nifanye
nini?’ Akamtumia na hilo swali. ‘Ni usiku sana James! Nipo na
mke wangu.’ Geb akamjibu hivyo akilalamika kusumbuliwa. ‘Unazidi
kupoteza muda, Geb. Maneno yote hayo, ungeshanishauri chakufanya.’ ‘Mpigie. Na
USIKU MWEMA.’ James akacheka akijua ndio anaambiwa asimtafute tena.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kwa
haraka sana akampigia simu Jema. “Pole na majukumu.” Jema
alianza mara alipopokea. “Asante. Pole na wewe.” “Asante.” Kimya. “Upo Jema?”
“Nipo.” “Bado unadhani kesho tunaweza kutoka?” “Nilijua umeahirisha James!” James akashangaa kidogo. “Ni nini
kimekupelekea kufikiri hivyo!?” “Uliposema unipigie kesho.” “Hapana. Labda
nilishindwa kuiweka vizuri. Nilimaanisha kukupigia kesho mapema kabla ya
miahadi yetu jioni. Mimi bado naisubiria kwa hamu.” Hapo
akamgusa Jema, na kusahau yote. Akacheka. “Na mimi pia.” “Basi
tujiandae kwa chakula cha kesho. Vipi lakini siku yako.” “Namshukuru Mungu
amenipa uwezo wakukamilisha majukumu yangu yote.” “Unaifurahia kazi yako?”
“Sana James, japo inaniponza.” “Tena!?” “Acha tu.” “Itabidi kesho tupate muda
tuzungumze vizuri unieleze ni kivipi.”
“Nitakuchosha
bure. Niambie na wewe siku yako iliendaje?” “Hutanichosha bwana.” “Utanikimbia
James. Tuyaache tu.” “Sio kirahisi hivyo. Siku yangu haikuwa mbaya. Na mimi
nashukuru Mungu nimeimaliza vizuri.” “Umekula sasa?” “Nimechoka, hata kula
sitaki. Nataka kulala tu mpaka kesho. Sitaki kupika.” “Sasa si unalala na
njaa!?” “Mchana Nanaa alimtuma dereva kuniletea chakula kazini. Kilikuwa kingi.
Nipo sawa. Na wewe umekula?” “Nilipata kifungua kinywa asubuhi, mchana nikakosa
muda, usiku hamu yakula haikuwepo, nikaamua kulala tu.”
“Kwanini
hamu ya kula imepotea tena? Au hukupata unachopenda?” “Kuna hali napitia
nafikiri hiyo ndiyo inanifanya napoteza hamu ya kula.” “Nilikuona umepungua
sana, nikafikiri ni kusudi!” Jema akacheka tu. “Pole sana. Na
hilo nitataka kujua.” “Pengine umeshasikia.” “Linalokuhusu wewe, hapana.
Ningeshakutafuta kukupa pole.” “Sio kweli James. Tunaongea leo kwa sababu
nilikuomba msaada. Bila hivyo usingenitafuta.” “Hapana.” James akakanusha kwa haraka.
“Kwamba si kweli!?” “Kwamba
tunazungumza leo kwa sababu uliongeza kitu kingine mbali na kazi ndipo nikapata
ujasiri wa kuzungumza na wewe Jema. Wakati wote unaponijia ofisini kwangu, au
hata tunapokutana unakuwa umejibeba kikazi tu, na mazungumzo yako ni ya kikazi
tena kuashiria unaratiba ngumu kwa siku hiyo. Huna muda wa jingine.” “James!” Jema
akashangaa sana.
“Kabisa
Jema. Nakwambia vile ulivyojitambulisha kwangu. Na hata salamu yako inatoa ruhusa
ya jibu moja tu. ‘Salama au Nzuri’ basi. Kisha unaendelea na
kilichokuleta kwangu na ndio maana uliniona siku ile nilinyamaza kidogo kama
kukupa nafasi utafakati ulichozungumza ili upate nafasi yakurekebisha kabla
sijakujibu. Na kweli ukakanusha.” “Jinsi ulivyolipokea ndio iliniingizia hofu,
nikajua nimevuka mpaka. Lakini nilikuwa na nia ya kukukaribisha chakula.” “Na
jinsi ulivyokanusha ndipo nilipojua nia yako ya kweli na kukufahamu Jema wa
namna nyingine ambaye sikuwahi kumjua.” “Jema gani huyo?” Ikabidi
Jema aulize. “Ambaye ni mkarimu mwenye moyo mnyenyekevu si kama ambaye anaonekana
akiwa na majukumu ya Joshua.” Jema akaona hapohapo ajiridhishe kwa maoni ya
James pia.
“Eti
nikuulize swali?” “Juu ya Jema wa kwanza au wa pili?” “Wa kwanza.” “Karibu?”
“Eti huyu Jema wa kwanza anatisha kiasi kwamba hawezi kuwa mke wa mtu?” “Inategemea
na muoaji.” “James! Hilo jibu ni la jumla sana, bwana.” “Ni kweli Jema.
Inategemea na mtu. Nikwambie ukweli lakini usitishike.” “Niambie tu. Nahisi
moyo wangu umekufa ganzi James. Nimeumizwa sana, kiasi ya kwamba maumivu
mengine yanakuja juu ya yale makali yaliyotangulia, mpaka sioni kama kuna
jipya.” “Pole sana. Na yote haya yanatokana na…” “Huyo Jema unayemzungumzia
wewe.” “Huyu wa kwanza?” “Huyohuyo. Ameniponza na sijui chakufanya sasahivi
ambapo nahisi Kumu ananihitaji sana. Najihisi nikiyumba tu, nitamwaribia sana
na yeye.” Jema akasikika kama amekwama sehemu.
“Cha kwanza
labda nitengeneze kauli yangu. Binafsi sioni tatizo la Jema wa kwanza maana
ndiye aliyenivutia mpaka nikaweza kumfahamu Jema wa pili.” “Kweli James?!”
“Hakikaa. Napenda jinsi unavyojibeba Jema. Unajua ni nini unataka, na kukifanya
kwa nguvu zako zote na akili yako yote. Hujui jibu la hapana na hukubali
kukatishwa tamaa. Hilo umelithibitisha hapa mpaka ulinishangaza, na Kumu
nilimsimulia na akaniambia ndio maana bado hajakupatia mtu mwingine na akasema
unaweza wewe usijue, lakini unamrahisishia sana mambo yake. Hiyo ni siri
nakupa. Joshua anakuheshimu sana na anakutegemea. Hiyo ni siri ingine nakupa.”
“Nashukuru kwa kuniuza kwake.” James akacheka.
“Ila
sikudanganya. Nilipenda jinsi ulivyo handle hii ishu ya hapa mpaka
ukafanikiwa wakati wengi walikuja kutaka kufanya biasha hapa, walishindwa. Na
uadilifu wako kwenye mambo unayoaminiwa nayo. Nasemea kwa upande wangu, binasfi
nilivutiwa. Naomba nishauri kama naruhusiwa lakini?” “Nishauri tu. Sasahivi
sina chakupoteza.” “Unacho. Tena kikubwa sana. Huyu Jema ninayemzungumzia mimi
wapo aina yake wachache sana.” “Sio kwamba nimezidisha ujasiri?” Hapo
Jema akauliza kwa kupoa kidogo. “Kuzidisha sijui. Lakini
usipoteze ulichonacho kwa kushindwa kwa mtu mmoja au wawili kukuhimidi.
Sijui kama unanielewa?” “Nakusikiliza.” Jema alishachoshwa na shutuma,
akatamani kusikia na upande wa mtu kama James anayejua shule yakutosha ipo kichwani
kwake na amefanikiwa kwenye taaluma yake, kama bosi wake, huyo Kumu.
“Mimi
nimeishi na watu wengi, tena kwa karibu sana.” James
akaendelea. “Nikafanikiwa kumfahamu mwanadamu kwa kuishi naye. Tena mimi nilibarikiwa
kuishi na wenye haiba tofautitofauti. Ninaposema kwa karibu. Ni sana.
Nikimaanisha kukua nao pamoja kama watoto wa mama mmoja na kuwa pamoja kila
wakati na kila sehemu. Katika mambo mengi niliyojifunza kwa hawa wanadamu wenye
haiba tofautitofauti ni, usithubutu kubadilika kwa ajili yao hata siku
moja, kwa sababu na wao huwa wanabadilika. Sijui kama unanisikiliza?”
“Nakusikiliza
James.” “Huyo Jema mwingine wanayemtaka kutoka kwako sasahivi, utashangaa sana
utakapobadilika na kuwa kama watakavyo wao. Watamtaka tena Jema huyu wa
kwanza, wanayemsema abadilike. Bakia kama ulivyo. Ili watakapobadilika wao,
wakirudi wakutane na Jema huyu ambaye siye kinyonga.” “Naona Mungu alikutuma
kwangu James. Nilikuwa nashindwa hata kula, sijui chakufanya. Aibu tupu!” Jema
akapata tumaini akaanza kujisikia kufunguka kwa James aliyeonyesha angalau yeye
anamkubali jinsi alivyo.
“Japo
sijajua ni kwa upande upi ila na mimi marafiki walinipitisha hapo. Nikakonda
nikawa kama kijiti kwa msongo wa mawazo. Na mimi Mungu akanitumia Geb. Mpaka
leo nina uhakika hajui kama alinisaidia mimi. Ila alinipa somo lililonifunza
sana.” “Somo gani?” “Kuwa, wapo watu sahihi. Waaminifu. Wanaoweza
kusimama na mtu hata kipindi kibaya kisichoweza kutamkika. Namaanisha cha aibu
na fedheha. Na akanipa moyo kuwa, yapo mapenzi ya kweli.”
“Kweli James?” Hapo akamleta karibu kabisa Jema aliyekata tamaa haswa kwenye
mapenzi. “Ooh kabisa Jema! Mimi nimeshuhudia kwa mifano. Hata nikutane na
watu wenye mfano mbaya kwa kiasi gani kwenye mapenzi, NAJUA kwa hakika, mapenzi
ya kweli yapo hapahapa duniani. Na unaweza kupendwa wewe kama wewe. Ndio
maana katika hilo sina hofu kabisa.”
“Kumbe bora
tumezungumza! Hakika nilikata tamaa kabisa.” “Maadamu bado Mungu yupo na ndiye
mwenye enzi, marufuku kukata tamaa na kujibadilisha sababu ya mwanadamu.
Vile alivyokuumba Mungu ni kwa ajili ya mazingira anayotaka kukuweka hapa
duniani. Ukijibadilisha tu, ujue hutaweza kuyamudu mazingira yako. Na utafeli
vibaya sana. Acha nikuache ulale, tutazungumza vizuri kesho.” “Nakushukuru sana
James. Utanifanya nilale vizuri na niamke na ujasiri wangu. Asante.” “Karibu.
Usiku mwema.” Wakakata simu. Hapohapo Jema akalala, wakasahu hata kuweka
mipango ya kesho yake.
Jumamosi.
Waliamka
wakiwa wamejenga kitu cha tofauti ila kila mtu akaogopa kumtafuta mwenzie wa
kwanza. Wakabaki kujiwinda kila wakati macho kwenye simu wakivizia kama kuna
jumbe. Kwa kuwa Geb alizima simu ili alale alipowasha mida ya saa 4 akakuta
jumbe tatu kutoka kwa James. Mama yake akamuona anacheka. Akampigia. “Nyumba
inaungua James?” “Unakumbuka jinsi nilivyokufanikishia mpaka wewe ukaoa huku
mimi nikitukanwa?” Geb alicheka sana. “Unarudi kudai kulipwa
fadhila?” “Tafadhali usinizimie simu, Geb.” “James, unajua jumamosi huwa
sifanyi kazi, nakuwa nyumbani na watoto. Na ninachelewa kuamka.” “Mkeo
ameniambia amekuacha ukiwa umeshaamka.” “Kwamba umempigia mpaka Nanaa simu huko
kazini!?” Geb
akashangaa sana.
“Kumbe! Kwa
nini hupatikaniki Geb?” “Mambo yaliendaje jana?” “Acha kunicheka bwana!” Geb
akazidi kucheka. “Na kwa taarifa yako tu, yamekwenda vizuri sana. Leo nataka kumtoa
kwa chakula cha jioni.” “Wapi?” “Kuna sehemu wanachoma..” “Naomba uishie
hapohapo James!” Geb akamkata akiwa ameshituka sana. “Kwani vipi!?
Wanachoma mbuzi vizuri!” “Unataka kumpeleka viwanja unavyoendaga na Nanaa?” James
akanyamaza.
“Wewe vipi
James!?” “Nanaa anapasifia sana. Na anapapenda.” “Kuna sehemu kunakochomwa
nyama Nanaa asipapende?” Mpaka mama G akacheka huko jikoni. “Hata stendi ya mabasi
ukimpeleka Nanaa ukimwambia kunachomwa nyama vizuri, yeye na mwanae Magesa
wataenda kula bila kujali eneo ilimradi wafikie hiyo nyama.” “Lakini kweli
asiee! Sijafikiria vizuri. Huyu Nanaa ataniponza bwana!” “Acha kumsingizia mke
wangu. Wewe mwenyewe unashindwa kufikiria.” “Basi tuanze taratibu.”
“Nimpeleke
wapi? Na usisahau nilikwambia ni mtoto wa mjini na amesoma. Anauwezo halafu..” “Acha
kupaniki. Tuanzie kwenye swala la uvaaji wako kwanza wewe halafu utapata
picha.” “Usianze Geb.” “Ulitaka uvae nini sasa?” Akatulia. “First impression matters
a lot James. Usiende kutuabisha.” “Sasa nivae vipi?” “Casual simple, and
smart.” Akatulia. “Umenielewa lakini?” Kimya. “Kwani
wewe huwa hutuonagi tunavyotoka na mke wangu?” “Sijawahi kuzingatia! Inakuaje?”
“Kwanza jipange kiasi ya kwamba hata kama yeye atapendeza sana, hutamuangusha.
Na hata kama atavaa kawaida, bado hakutakuwa na utofauti. Nakutumia picha zangu
na Nanaa upate picha ya nini nazungumzia. Na huwa nikitoka na mke wangu
simpeleki kwenye nyama choma. Nampeleka kwenye sehemu wanazokula kwa kisu na uma.
Kwa hiyo andaa walet.” “Sawa.” Geb alicheka
sana. “Hakika James umekamatika! Umekubali kutoa
pesa kwa haraka hivyo!?” “Tuma picha Geb.”
James akamkatia simu akimuacha Geb akicheka sana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akaamua yeye
ndio aanze kumtumia ujumbe Jema. ‘Uliamka salama?’ Baada ya
kama lisaa ndio Jema akampigia. “Samahani James. Nimebanwa
hapa kazini nimeshindwa kushika simu. Niliiacha ofisini.” “Usijali kabisa.
Chapa kazi.” “Hujakasirika sasa?” “Nini kiniudhi!?” James akawa hajaelewa.
“Kwamba sijajibu ujumbe kwa wakati.” “Hapakuwa na
deadline ya majibu Jema! Acha wasiwasi. Umeshamaliza kazi lakini?” “Bado kikao
cha mwisho cha Kumu, ndipo nifunge siku.” “Basi usichelewe. Ila ukitulia naomba
nijulishe ungependa nije kukuchukua saa ngapi? Na unataka kwenda kula wapi au
unahamu yakula nini?” Jema akacheka.
“Kuja mpaka
kwangu si usumbufu? Au tukutane?” “Hiyo itakuwa siku nyingine tutakutana huko.
Leo nilikuomba mimi ndio nikutoe, kwa hiyo leo mimi ndio dereva wako.” Jema
alifurahi sana. “Mbona unacheka?” “Sikutegemea! Nimefurahi sana.” “Basi wahi kazi,
tutawasiliana ukipata nafasi.” “Asante James.” Jema alikata simu akiwa
haamini. James hana neno kusubirishwa majibu ya simu yake! Anakata simu ili
Jema arudi kufanya kazi! Jema akabaki ameshikilia simu haamini. James alifanya
kila kitu alichoshauriwa na Geb. Hata kwenda kumchukua nyumbani ni wazo la Geb.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Akafanya
shuguli zake ndipo na yeye akaenda saluni kutengenezwa kichwa. James mweupe
kama dada yake Nanaa. Damu ya upande wa mama zao. Akachongwa vizuri na
kulambishwa dawa kichwani. Nywele zikalala kama zakishombe. Wakamuwekea rangi
nyeusi kwenye sehemu ya ndevu/mustachi na kichwani. Alipendeza James, mpaka
mwenyewe akajikuta akicheka mbele ya kioo. Akasita kununua nguo mpya asije Jema
kumgundua. Akarudi kwake kuanza kutafuta nguo, akiangalia picha za Geb.
Akakwama kwenye viatu. Hakuwa na aina hiyo ya viatu.
Akampigia
Geb. “Nimekwama viatu.” “Bora umenipigia maana nilikuwa nikiwaza, naomba
Mungu usije ukatokea na zile raba zako.” “Zina nini?” “Wote tunajua
hazikuwakilishi vizuri ndio maana umenipigia.” James akapoa. “Basi
nielekeze huko unakonunua zako.” “Usilie bei.” Geb akamtahadharisha asijue James
alishayavulia maji nguo. “Wewe niambie.” “Kweli umepania mzee!” “Unanichelewesha Geb.”
Akamuelekeza wanapouza sneakers anazovaaga yeye na Joshua. James akakata simu
akaondoka kwenda kuzisaka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Usipitwe na Dinner ya James na Jema. Ipi Historia ya Jema naye. Mara
ya mwisho James alisikia anakaribia kuolewa. Kipi Kiliendelea kwake. Na yapi
yatajiri kwao?
Je, Hatimae James amepata?
Usikose
muendelezo.
0 Comments:
Post a Comment