Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 1 - SEHEMU YA 42. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 1 - SEHEMU YA 42.

“Vilishindikana kusubiri!?” “Tapeli tu yule, wala mama hakukosea. Hapakuwa na kusubiri kokote. Alikuwa akiendelea na uchafu wake kama kawaida ila huku kwangu akijifanya ni mcha Mungu. Ila huyu binti ameniambia atamuoa. Ni mwanamke wakuwekwa ndani, anatambua mamlaka za kimungu.” James akabakia kimya kwa muda halafu akauliza.

“Hayo anakwambia wewe akikiri kosa?” “Anasema kosa ni kuendelea kunivumilia kwa muda mrefu mpaka kumfanya akamkosea Mungu wake.” “Kwamba wewe ndio kosa?” “Naona umenielewa.” “Na mlikokuwa mkijenga?” “Stori ilibadilika. Pakageuka kwake. Yeye ndio aliyenunua kiwanja na kusimamia ujenzi wakati mimi nikihangaika na wanaume za watu, yeye alikuwa halali. Anasema amejenga kwake na watoto wake, mimi nilishindwa kusimama naye kujenga nyumba.”

“Pesa uliyowekeza?” “Ameniuliza bila aibu, ni hela gani nilimpa?” “Jema!” “Nikimwambia nililia mpaka nikakaukiwa, amini nililia James. Hapa nilipo nakatwa mshahara kwa asilimia zaidi ya 70. Na yeye ndiye aliyenifundisha kukopa benki tofauti tofauti. Nimemjengea kwake, mimi naishi kwenye kile kinyumba chakupanga pale.” “Lakini ni pazuri.” “Ila si kwangu James.” “Ni kweli.”

“Na mbaya zaidi sina hela zakusema nianze tena ujenzi. Itachukua zaidi ya miaka hata 8 kuja kumaliza deni na kuanza tena. Halafu Temu ni muongeaji kwelikweli. Huko kote tunapojulikana mimi na yeye kama tulikuwa wachumba, ametangulia kunichafua hata kama kungekuwa na mchumba mwingine wa kuoa atagairi tu.” “Kumbe bado nia ya kuolewa ipo?” “Jana umenijenga James. Umenitoa chini sana, ni hivyo hujui tu. Leo nimeamka na nguvu mpya.” “Afadhali na pole sana.” Wakatulia kila mmoja akaendelea kunywa kinywaji chake mpaka chakula kilipoletwa.

“Hujaniambia juu yako James. Wewe ni kwa nini hujaoa mpaka sasa?” “Wala sina stori ndefu. Sijawahi kuumizwa na mwanamke kwa kuwa sikufungua huo mlango. Si kwa woga ila sikuwa tayari sababu ya kwanza Nanaa. Sikutaka kujichanganya. Nikajikuta nakwama kwenye mambo mengi kwa kuwa kama ungeniambia wakati ule yule Nanaa niliyekuwa nikimlea, ndiye angekuwa huyu! Pengine nisingeamini, na kama ningeamini basi pengine ningebweteka kwake. Kwahiyo sikutaka kujichanganya kabisa. Sikutaka kufikishwa mahali nichague kati yake na mapenzi.”

“Hilo moja. Pili nilikuwa na malengo yangu kwenye maisha, niliona nisubiri mpaka nikamilishe. Ila Geb na Joshua wao wananiambia ni sababu tu, sikupata mtu aliyenivutia.” “Ambayo ni kweli?” “Nahisi pana ukweli. Ila japokuwa nimezungukwa na wasanii wengi wa mapenzi, lakini pia nina uhakika wa upendo au mapenzi ya dhati yasiyochanganywa na pesa au usanii. Kwa kuwa katika hao wengi matapeli, ninao wachache wamelithibitisha hilo na kunifanya nisiharakishe mpaka na mimi nipate mtu wangu.” Jema akatulia kabisa na kuendelea kula taratibu.

“Unaonaje chakula chao?” James akauliza kwa kujali. “Kizuri sana. Na wewe je?” “Na mimi nimekipenda.” Wakaendelea kula. “Wewe huwa unapika?” James akacheka huku akijaribu kujifikiria. “Nafikiri naweza kupika mtu akala, japo sina muda na si kitu nafurahia kufanya. Akinisahau Nanaa, ujue ndio basi tena.” “Kwamba anakupikia kila siku!?” “Nafikiri anapika kingi. Anajaza kwenye makontena. Anakuja kuniwekea kwenye friji. Akihisi kimeisha, analeta kingine au sijui mwenyewe huwa anafanyaje! Sijui huwa anapita kwangu kukagua au la! Ila anajitahidi kwakweli. Na nisipokuta chakula najiona ni bora  kulala tu kuliko kuanza kupika.” Jema akacheka akifikiria, akaona aulize zaidi.

“Na unapenda vyakula gani?” “Sijapata muda wa kujichunguza na kujua nini napenda zaidi. Ila Nanaa anapenda sana nyama choma! Basi amenifanya na mimi niwe mpenzi. Ukitaka afurahi mpeleke kwenye nyama choma.” Jema akacheka. “Sasa amenilemaza, najikuta ni kitu nakuwa na hamu nacho. Geb mumewe siwezi kumpeleka huko mara kwa mara. Ukiwaita yeye na Kumu wanabaki kuwa watizamaji na maswali yanayokera mpaka hufaidi nyama yenyewe!” “Maswali gani?” Jema akauliza akicheka. “Usafi wake. Kama imeandaliwa kwa usafi na kama kweli ni fresh sio ngombe au mbuzi kibudu/mzoga, mpaka nikaona niwe nawaacha tu nakwenda na Nanaa.” “Yeye hana shida?” “Yule chochote kinachoitwa chakula, hata uweke kwenye jani la mgomba, atakula bila wazo la pili.” Jema alicheka mpaka machozi.

“Yaani ungemleta hapa. Angesifia hiki chakula kuanzia kijiko cha kwanza mpaka anamaliza.” “Nanaa huyo!” “Marafiki wa karibu sana na chakula. Hawajawahi kugombana.” “Labda akiwa mgonjwa.” “Tena iwe tumbo. Lakini sijui homa tu, kichwa! Mwenyewe anakwambia haviingiliani.” Jema alicheka sana. “Sasa mbona hana mwili mkubwa.” “Mama mkwe wake alipata matatizo ya magoti. Kupunguza mwili kulimsaidia sana. Sasa imebidi wajiandikishe gym na wanamashine za mazoezi pale kwao. Ndio pona ya dada yangu yule. Ila si kujinyima chakula. Hapo ni kumnyanyasa.” Jema alicheka sana.

Wakapata wakati mzuri wakufahamiana taratibu, James akitupia maswali hapa na pale kujaribu kumfahamu. “Na baba mzazi?” Jema akacheka kwa masikitiko. “Sijui hata ni nani na mama mwenyewe alituzaa kila mtoto na baba yake. Ukimuuliza anakwambia ni katika kuchanganyachanganya huko ndio ametupata sisi wawili.” James akashangaa sana. “Sijaelewa!” “Na mimi ndio hivyohivyo. Ingekuwa maisha yanakupa nafasi ya kuja kukutana na mama yangu mzazi mimi, ndio ungeelewa ninachozungumzia. Kile anachokifikiria kichwani huwa hawezi kukiacha moyoni. Atakisema tu.” “Kama kumwambia Temu ni tapeli?” “Ewaaa! Sasa usimkute amekasirika au usimuulize swali linalomkumbusha machungu yake. Utajuta kuuliza. Kwa hiyo kwa kifupi mimi na mdogo wangu hatuna taarifa za baba zetu. Akiwa ametulia atakwambia alibakwa. Mdogo wangu huwa anamuuliza mara zote mbili? Anakwambia mimba haiitaji kitanda kutungwa. Ashamaliza. Akiwa amekasirika atakujibu majibu mabaya, kisha atakwambia nenda kaulize Ustawi wa Jamii.” James akacheka taratibu.

“Bibi mwenyewe anasema anahisi alidondoka alipokuwa mdogo akagonga kichwa.” Ilibidi James acheke. “Huna mfano wa mama yangu.” “Lakini nyinyi aliwalea.” “Kwakweli siwezi kulalamika. Na ni kwa kadiri ya uwezo wake. Hilo nitamtetea. Sema mimi mwenyewe nilitamani maisha ya kujitegemea mapema sana. Kwahiyo nilipomaliza tu chuo, mama mwenyewe ndiye aliyenitafutia kazi pale Coca. Alifanyaga kazi pale zamani, akawa anafahamiana na watu pale. Kwahiyo baada ya kupata mshahara wangu wa kwanza, mama mwenyewe akanisaidia kutafuta pakuishi. Akanisaidia kuhama, nikaanza kujitegemea.” “Kumbe anajali hivyo!” “Sana. Yaani hata sasahivi nikimpigia simu, nikamuomba aje popote, nikamwambia nina shida naye, hatauliza mara mbili, ataacha kila kitu na kuja kunisikiliza. Anatujali sana, ila mimi mwenyewe napenda kujitegemea.” James akarudishwa kwa mama yake yeye mwenyewe. Vituko vyake na maisha yake mjini kama hana mume! Akapoa kabisa.

“Kwa hiyo uliajiriwa moja kwa moja kwenye kitengo cha Masoko?” “Ndiyo, lakini nilifanya pale kwenye ile kampuni wala hakuna aliyekuwa akinijali mpaka alipokuja Kumu. Na shule yangu ndogo, akataka nifanye naye kazi kwa karibu. Niliogopa James! Ukumbuke ni Kumu, halafu mimi sijasoma! Nikasahau maombi yote niliyokuwa nikimsihi Mungu aniinue kwa kidogo nilicho nacho.” “Ulitaka nini?” “Sikuwa nikijua kwa hakika kwa kuwa sikuwa nimesoma sana. Ila niliona ufanywaji kazi pale, nikawaona hao walio soma na kazi zao, hakika nilijua na mimi nitaweza tu. Tena nikawa najiaminisha eti naweza kufanya vizuri zaidi yao.” Wote wakacheka.

“Basi nikawa sina uwezo wa kurudi shule ila kufunga na kuomba nikimsihi Mungu atumie kidogo nilicho nacho kuniketisha na wakuu. Sasa eti Kumu kuja kuniambia nifanye naye kazi, nikaingiwa hofu sana. Kwanza nilishakuwa nimesahau hayo maombi, kwa kuwa ni kama nilikaa muda mrefu bila kujibiwa. Mpaka akaja Kumu sasa. Alipoona nimeingiwa hofu, ndipo akaniambia yeye hataki mtu mwenye vyeti vikubwa, ila anataka kufanya kazi na mtu mwenye tabia kama zangu. Ilichukua muda mfupi sana kumuelewa na kuanza kufanya naye kazi. Na pesa ninayolipwa pale, kwa mtu mwenye shule yangu, hakuna sehemu wanaweza kunilipa hivyo.” “Ila imeongezeka ujuzi.” “Kwa sasa ndiyo. Ila namuombea sana Kumu asije kuondoka pale. Naweza sema ndio kama nguzo yangu pale. Anatetea sana maslahi yangu.”

“Kwa hiyo kujibu swali lako, sijui baba yangu ni nani, wala kabila yake. Ila mama yeye ni mtu wa Kilimanjaro.” James alifurahi sana. Kabila ya mama yake vikaendana. James mtoto wa kwanza. Alitamani kuoa mwanamke ambaye haitakuwa shida kumtambulisha hata kwa bibi yake. Akajiambia atasimamia hapohapo, ataachana na maswala ya baba na hatajali tena ni Kilimanjaro ipi huyo mama yake anatokea. “Ibakie tu Kilimanjaro.” Akawaza James nafsini mwake.

“Nikwambie ukweli James?” Akamtoa mawazoni. “Hilo lakutojua baba yangu, lilichangia sana kutulia kwangu na kutamani sana ndoa. Kuwapa watoto wangu familia na baba wakueleweka. Najihisi kama kuna kitu au upendo fulani nimenyimwa au kupunjwa hapa duniani, kupitia baba. Ndio maana najitetea hata kwa Temu, nilibaki kama mjinga akininyanyasa huku tukiwa na picha ya kuwa ni couple ya wacha Mungu, nikijua nitabahatika ndoa. Nikajifunga kwake nikimvumilia, na kumuamini Mungu pengine atakuja kumbadilisha, nikijua nahangaika kwa ajili ya watoto wangu, lakini imekua tofuati. Aliponitenda nilimlaumu sana Mungu kwa sababu kuna wakati nilikuwa mpaka nafunga na kuomba kwa jili yake kwamba Mungu abadili moyo wake. Huku nikijaribu kumpa kila pesa anayotaka! Lakini haikusaidia. Nilimlaumu sana Mungu na kumwambia kwa hasira kuwa hathamini kujitunza kwangu.”

“Inawezekana Mungu ndio amekujibu Jema.” Jema akakunja uso. “Kutendwa kikatili kiasi hicho!?” “Wewe ulikuwa mwaminifu kwa Mungu. Si ndiyo?” “Kabisa James!” “Na ukamuomba?” “Ndiyo. Tena kwa uwaminifu kabisa, nikijikinga na kila vishawishi, jamani!” “Ulikuwa na jinsi yako ya Mungu atakavyokujibu. Lakini majibu ya Mungu aisee ni ya ajabu sana Jema. Mimi si mcha Mungu sana. Lakini kwa kukaa na Geb pamoja na Kumu, nimekuja kujifunza mambo mengi sana juu ya Mungu. Tunavyofikiri sisi sivyo anavyofikiri yeye. Njia zake sio zetu kabisa. Wakati wewe unafikiri hajakujibu, kumbe ndio amejibu kwa kukuonyesha kwa wazi kabisa yeye ni mtu wa namna gani. Akamshupaza shingo yake kabisa asije hata kukuomba msamaha ukamsamehe, ili tu kumtoa kwako. Maana kwa jinsi nilivyokusikia ni kama aliyaendesha mahusiano yenu kibabe.” Jema kimya.

“Nina uhakika angerudi kukuomba msamaha na kukwambia ilikuwa bahati mbaya, pengine ungemsamehe. Sasa fikiria ungekuja kuolewa na mwanaume wa namna hiyo. Anayekunyanyasa vibaya hivyo. Ndio mpaka kifo chake! Inamaana hata hao watoto wenu wangezaliwa wakawakuta kwenye hiyo hali. Wewe huoni hiyo garama ya deni la pesa alilokuachia ni dogo sana kulinganisha na mateso ya maisha yako mpaka kufa?” “Lakini kweli!” “Mshukuru Mungu.” “Ndio maana neno la Mungu linasema tushukuru kwa kila jambo!” Jema akawa kama amekumbuka mwenyewe.

“Ukute Mungu alikuwa akiniepusha naye!” Akaendelea kuwaza kwa sauti. “Pengine Mungu wangu alinihurumia!” “Na ndipo linapokuja swala la kutokata tamaa. Mimi nilimwambia mama G, kama Kumu na yeye ameoa, basi na mimi nitaoa tu.” Wakacheka. “Maana mama G alikuwa akitusema sana mimi na Joshua. Anasema tunazidi kuzeeka. Joshua akanitia moyo akaniambia, upo upendo wa kweli, niwe mwaminifu kwa Mungu, Mungu si mwanadamu hata aseme uongo, atanipa haja ya moyo wangu. Ndio na wewe nakwambia hivyohivyo. Endelea kumtumainia Mungu. Subiri bila kukata tamaa. Atakujibu tu.” “Nakushukuru James.”  James akacheka.

“Kweli umenituliza. Nilikuwa nikijiuliza kweli uaminifu wangu kwa huyu Mungu ni bure tu!” “Hata kidogo. Inaweza kuchukua muda, na inaweza isiwe kama tulivyotaka wewe. Kuwa itokee kilaini tu. Ila Mungu anajua walio wake. Jicho lake lipo kwao, hajawahi kuwaacha.” “Sasa mbona unasema humjui sana Mungu lakini unahekima ya kimungu hivyo!?” James alicheka sana.

“Kina Kumu wameniathiri sana. Ndio watu wangu wa karibu. Naweza nikashindwa kwenda kanisani, lakini huwa jumapili baada ya ibada lazima tukutane kwa kina Magesa. Hapo tutashinda tukizungumza mpaka usiku. Na mama G ni mcha Mungu sana. Kwa hiyo wameathiri hata mtizamo wangu mkubwa kwa Mungu.” Wakaendelea kuzungumza mpaka wakaona watoke hapo.

Kukawa na kitu kingine kimejengeka kati yao, lakini kama kila mtu akaona achukulie taratibu au kuwindana. Wakapata utulivu moyoni. James akiwa amemfahamu Jema kwa asilimia kubwa iliyojibu maswali mengi sana mpaka ambayo hakujua jinsi ya kumuuliza, Jema akawa ameyajibu.

“Sasa na kusimama nako ndio inakuaje?” Jema akauliza. “Usubiri Jema! Nakuja kukusaidia kusimama.” Jema alicheka sana. “Ningeshavuta kiti mimi!” “Acha haraka. Hiyo kazi yangu.” Wakazidi kucheka. James alishapitishwa shule na Geb, akawa anajua nini chakufanya. Wapi asimame ili kuvuta kiti wakati akisimama. Akafanya kama mtaalamu, Jema akicheka sana. “Mwenzio sijazoea.” “Taratibu tu, utazoea. Ukiwa na mimi uache kukimbilia vitasa vya mlango.” Jema alicheka sana mpaka akainama James akimwangalia. “James wewe mtundu kuliko unavyoonekana!” “Mimi nakwambia ukweli.” “Haya, basi.” Wakatoka hapo ndani hotelini.

“James!” Jema akamuita kabla hajafungua mlango. “Nashukuru kwa usiku mzuri sana. Nilihitaji kila kitu. Chakula kizuri, mazungumzo yote. Nahisi Mungu amenijibu kilio changu, maombi yangu mbele zake kwa kupitia wewe usiku wa leo. Asante kwa muda wako pia. Nashukuru kuwa na mimi usiku wa leo.” “Na mimi nikisema kama ulivyosema nitakuwa nikiiga?” Jema alicheka sana.

“James!” “Ni hivyo uliniwahi tu. Na mimi nimekuwa na wakati mzuri Jema. Asante kukubali kutoka na mimi baada ya kushindikana mara ya kwanza.” “Sema baada ya kunikatalia mara ya kwanza.” “Hapana Jema. Sikukataa ila nilikuwa na miahadi niliyokuwa nikikumbushwa na Nanaa karibu siku nzima. Kuna game huwa watoto wake wanapenda kucheza, zaidi Magesa.” “Yule mwimbaji?” “Ewaa! Huyohuyo. Sasa huwa inachezwa na watu wawili. Akicheza na baba yao, huwa anawafunga, basi Magesa huwa anaishia kulia.” “Hataki kufungwa?” Jema akauliza akicheka.

“Kabisa. Sasa na yeye Geb anamkaba mtoto, hampi mwanya wakufunga hata mara moja. Na Nanaa hapendi vile mwanae akilia, na Geb hataki kumuachia anasema anamfundisha kupapanda na changamoto za maisha.” “Ambayo ni kweli.” “Akikusikia Nanaa mtakosana sana. Mimi napendwa pale kwao kwakuwa huwa namuachia anifunge.” Wakazidi kucheka.

“Kwahiyo ile miahadi uliyosema, kumbe ni ya kwenda kufungwa?” “Naona umeelewa. Nilikuwa nakumbushwa siku nzima, maana asubuhi yake baba yao huwa haendi kazini, ila mama yao anakwenda. Nasikia wakaamkia game. Geb akamfunga Magesa. Mama yake anasema akapokea simu kutoka kwa mwanae akilia, anasema yeye anampenda sana. Yeye anaona amtume dereva ampeleke tu ofisini akafanye naye kazi. Anamtaka yeye. Nanaa anasema akafikiria kwa haraka, akajua Geb kashamfunga. Ndio nikapigiwa simu nikiombwa niende, akanifunge, ili alale vizuri.” “Sasa kwa nini Nanaa yeye hachezi nao?” “Hajui. Na Magesa anaakili sana. Ushindi wake anataka aupate kwa mjuaji. Yaani akijua unajua halafu akakufunga ndio raha yake. Sasa baba yao nasikia amepigwa marufu kwa muda. Nanaa hataki acheze naye mpaka mwanae ajue sana. Ambayo najua haitakaa ikatokea maana na yeye Geb anaongeza ujuzi ili asije wahi kufungwa na Magesa.” Jema alicheka sana lakini angalau akaridhika kuwa sio kwamba alikuwa akikataliwa tu. Kweli alikuwa na miahadi.

Safari ya kurudi kwa Jema ikaanza. Pakazuka ukimya. James akashindwa aendeleze vipi mazungumzo yanayowahusu wao wawili. Akaona asije akaharibu, akatulia. Jema akajivuta nyuma vizuri, akajiegemeza kichwa, macho nje ya dirisha, kimya. James akamrushia macho mara kadhaa akamuona ametulia tu.

“Upo wapi tena?” Akageuka na kucheka. “Nipo?” “Wapi?” “Nawaza. Ila si kwa vibaya kama zamani.” “Nini?” “Pakuanzia kwenye maisha.” “Hutakiwi kuanza, ila kuendelea.” “Unakumbuka nilivyokwambia nimeharibu kwa madeni ambayo ni kama namlipia Temu na familia yake? Hiyo inaniuma James! Inaniuma sana.” “Mimi naona ni garama ndogo sana yakulipa kwa uhuru wako. Hebu fikiria Jema, lipi bora? Kulipa hilo deni huku ukinyanyasika, huna raha au kulilipa ukiwa na akili iliyotulia?” “Ni bora kulilipa nikiwa nimetulia nipo huru, lakini James, bado ni deni ambalo natakiwa kulilipa huku maisha yaendelee. Ningekuwa na muda ningesema hata nitafute kijibiashara nifanye niwe naingiza pesa sehemu mbili. Halafu sitaki niishi nyumba zakupanga daima na sitaki kurudi kuishi kwa mama kwa kushindwa kumudu maisha! Kwahiyo nashukuru kwa nafasi ingine ya uhuru, ila inabidi kujipanga na hili nilikabili.” “Hilo ndilo la muhimu.” James akaongeza na kuendelea.

“Mimi nina imani na wewe Jema. Kwa vile nilivyoambiwa na Joshua, naamini hutakwama hata katika hili. Jipe tu muda utaona mambo yanaanza kukaa sawa. Ile pesa uliyokuwa ukiigawa kwake, itaanza kutulia mfukoni.” “Ni kweli.” Akaafiki na kutulia. Mpaka wakafika nyumbani kwake.

“Nikikukaribisha ndani utakaribia?” “Naomba iwe wakati mwingine Jema.” “Sawa, kama kutakuwa na wakati mwingine.” “Naamini tutakuwa na wakati mwingine. Au unafikiri leo ndio iwe mwisho?” Jema akatulia kama anayefikiria. “Vipi? Hutaki tena?” “Sijui James! Acha wakati uje ujibu hili.” James akabaki amepoa kama aliyemwagiwa maji. “Kwamba hataki kuja kutoka tena na mimi! Nimekosea wapi!?” James akawaza. “Usiku mwema James. Na asante kwa kila kitu. Mungu anajua ni kiasi gani nilihitaji usiku kama huu ulionipa.” “Asante Jema. Usiku mwema.” Akashuka garini baada ya James kumfungulia mlango. Akamsindikiza mpaka mlangoni. Jema akacheka. “Kwamba huondoki mpaka niingie ndani?” “Na ufunge mlango kabisa, nijiridhishe upo ndani salama.” Jema akacheka kujaliwa. “Asante kujali James.” “Karibu.” Akangoja mpaka alipoingia ndani kabisa na kujifungia mlango ndipo akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jema alitamani kumtumia ujumbe lakini akaogopa hajui aseme nini. Wazo likamjia. Akampigia na James naye akapokea kwa haraka sana. “Nakusindikiza.” James akacheka kwa furaha maana aliondoka pale kwa masikitiko akijua ni kama Jema amehitimisha. “Nakushukuru. Nilifikiri ungetaka kulala!” “Nitalala tu. Hata hivyo kesho naenda ibada ya saa nne, kwa hiyo nitakuwa na muda wa kutosha tu wa kulala. Halafu sitaki ujikute peke yako huko barabarani ukirudi nyumbani. Au ni usumbufu?” “Hata kidogo japo sirudi nyumbani kwanza. Kuna mahali napitia.” “Basi nikuache nisiingilie.” “Hapana. Na mimi nataka unisindikize. Ni mambo yangu ya kibiashara.” James akaendelea.

“Kuna mzigo umeingia ndio nakwenda kuangalia. Ni kama biashara mpya nimeanza nafikiri hata mwaka haujaisha, sitaki kiharibike kitu.” “Hongera japo sijajua ni biashara gani.” Ikawa kama anayetaka kujua zaidi. “Nilifungua duka la Spare Parts. Naingiza nchini zaidi vifaa vya Toyota ambavyo ni uhitaji mkubwa hapa nchini na Nissani ambavyo ni hadimu.” “Unaonaje?” “Aisee siyo mbaya kabisa. Nilianza kama kujaribu tu. Lakini inalipa aisee, ndio maana sitaki kitu kiharibike. Nipo nayo makini sana.” “Hongera James.” “Asante.” “Basi ukifika uniambie ili nikate nikuache ufanye kazi.” “Sitasindikizwa nyumbani?” Jema alicheka sana.

“Au usindikizwaji huu ni wa masharti? Mara moja, basi. Nitakapoishia ni hapohapo!” “Ukinipa ruhusa nitakusindikiza popote uendapo.” “Basi ujiandae kukesha maana nikitoka hapo, nakwenda na Kariakoo.” “James! Usiku huu?” “Mjini pesa hailali Jema.” “Lakini kweli! Mpaka umenitamanisha! Kwa kazi nzuri uliyonayo ungeweza kubweteka!” “Kazi hii ya ofisini ni ya watu. Hii ya pili ni yangu. Hata nikikosana na Mwajiri, akataka niondoke kazini, siyumbi kiuchumi.” Akazidi kumvutia Jema.

“Ni kweli kabisa. Sasa na Kariakoo nako ni nini?” “Ndipo lipo duka kubwa la vifaa vya magari. Huku nawasogezea huduma matajiri wangu kama mafundi wa wakina Kumu na Magesa.” Jema akacheka lakini akizidi kushangazwa na James. “Nishasema hongera nyingi sana, utanichoka.” James akazidi kucheka. Wakaendelea kuongea.“Acha mimi ndio nikupigie nisikumalizie pesa yako.” “Asante.” James akampigia yeye. Maongezi yakaendelea. Akamsindikiza mpaka saa sita na nusu usiku.

“Hujachoka tu?” “Bado. Nafurahia mwenzio.” “Sasa unafurahia nini? Kukesha na mimi?” “Nafurahia kampani yako. Mwenzio nilikuwa nakesha kwa mawazo, bora hivi nakesha nikicheka na kuzungumza vitu vya maana vya maendeleo.” “Basi kama ndio hivyo tuendelee. Ila baada ya muda mfupi sana nitakuwa nimefika na wewe upumzike ulale. Usikeshe tena. Au bado unawasiwasi?” James akauliza akisikika kujali.

“Wasiwasi hapana James. Ila natakiwa kujipanga ili kurudia kwenye mstari na kujijenga kwa upya.” “Nakuelewa. Na najua utaweza tu. Panga matofali yako taratibu ukiwa na msingi mzuri, utafanikiwa tu. Na usijali tena maneno ya watu.” “Ila kanisa nitahama. Pale pameshachafuka, kutanipotezea utulivu.” “Sio kwa kukimbia Jema!” “Hivi nilikwambia kama Temu ni yule mzungumzaji tena wa jazba?” “Uliniambia.”

“Sasa ametangulia yeye kujisafisha kwa kunichafua mimi. James, pale sitapata utulivu. Japokuwa alinikuta pale kanisani, acha tu nimpishe. Makanisa ni mengi sina sababu ya kujitesa.” “Umeshajua sasa pakwenda kuabudu?” “Naenda kujaribisha kanisa moja hivi, lipo pale Victoria. Wanapasifia ni pazuri.” “Basi naomba na kesho tuongozane wote.” Jema alishituka moyoni akabaki kimya kwa muda. James akaangalia simu yake aliyokuwa ameweka kiti cha pembeni akizungumza kwa kutumia bluetooth. Akakuta bado yupo hajakata.

“Jema?” “Kweli James?” “Kama ni sawa kwako. Ila ningekuwa mimi ningekubali tu.” Jema akaanza kucheka. “Angalau huwi mgeni peke yako.” “Mwenzio nimefurahi mpaka nahisi machozi kunitoka. Sitaanza kwa uchungu nikiwa mpweke.” “Umeona mambo hayo. Wewe kila ukitaka kuanza kitu, nipigie nikusindikize huko mwanzo unakoanzia.” Jema alicheka sana. “Hutachoka?” “Nyumba ni msingi, mama. Sasa nina shida gani kuwepo kwenye vitu muhimu kama hivyo? Yaani wewe ukiwa unafanikiwa mbeleni, unakuwa na kazi yakunikumbuka tu mimi niliyeanza msingi na wewe.” Jema akazidi kucheka kwa furaha.

“Naamisha Jema.” Hapo Jema akatulia. “Sitaki unisahau Jema. Na sitaki unisahau kwa ubaya. Ila mema. Siahidi kuwa mkamilifu kama Mungu, lakini sikusudii kukusababishia maumivu.” Ikamgusa sana Jema. Japo James hakuongea kwa wazi, lakini ikamfariji. “Kwa umbali gani James? Nisije weka tumaini nikajiona sipo peke yangu tena kumbe sivyo.” Jema akauliza kwa sauti ya upole. “Umbali wowote utakao niruhusu wewe.” Jema akatulia kabisa. “Upo Jema?” “Labda niulize tena. Kwa muda gani? Kwamba hii ofa ipo mpaka lini? Inaku expire?” “Utakavyoamua wewe.” “James!?” Jema akashangaa sana.

“Mimi nakwambia ukweli Jema. Na nilishakwambia sikuwahi kumfungulia mwanamke mlango. Nilikuwa na sababu zangu. Lakini wewe umekua wakwanza. Na mimi najijua si muongo. Siwezi na kesho nikamwambia tena mwengine hayahaya niliyokwambia wewe. Kwanza sijajaliwa huo uwezo. Ndio maana nilipokuwa nikimlea Nanaa, kama unakumbuka nilikwambia wazi sikutaka kujichanganya.” “Kwahiyo sasahivi unajiona upo tayari kwa jukumu jingine?” “Kwako, ndiyo. Kwa kuwa nimekusoma na kusikia sifa zako, naona hutakuwa jukumu ila kampani yakunifikisha mbali zaidi au mtu wa kuwa naye nisiwe mpweke tena.” Akaongea kama anayejua anachozungumza. Hajakurupuka. Anamaanisha kwake. Jema akatulia kabisa kusikiliza.

“Mfano hiki ulichokifanya usiku huu. Kwako kinaweza kisilete maana, lakini ndicho nilichokuwa nikikitamani. Binafsi sikutegemea kama ungeweza kuwa na mimi usiku wote huu ukinisubiria kwenye simu. Na usifikiri nategemea ufanye hivi kila siku! Hapana, kwa kuwa na mimi sitakuruhusu. Nitataka ulale ili uamke na nguvu yakufanya kazi vizuri. Sikuwa hata na mpango wa kusema haya sasahivi, lakini umenifanya niseme, Jema. Na sitaki kuchelewa nikaja kujuta. Kama utaona nitaweza kuanza na wewe huko unakoanza, tafadhali anza na mimi na nakukaribisha pia uendelee na mimi kama hivi leo kwenye usiku huu.” “Nashukuru James. Asante sana.”

“Kwamba upo tayari?” Akauliza kutaka na yeye uhakika. “Sina sababu ya kujichelewesha zaidi, James. Na siwezi kukataa hiyo bahati! Isingekuwa wewe pengine na leo ningekesha kwa mawazo nikijua Mungu amenisahau. Sina bahati. Nina mkosi kama wa mama zangu, nakushindwa tena kula. Wewe umekua msaada Mungu alionitumia. Wala sitafikiria mara mbili. Wewe ukiwa na nafasi nitashukuru ukinisindikiza popote utakapoweza, na kama unaniruhusu kuomba ushauri, basi naomba nitumie hekima yako kuanza upya. Ulipomfikisha Nanaa sio pabaya. Na mimi naomba unishike mkono.”

“Sasa hapo unakaribia kuharibu tena!” “Kwa nini tena!?” Jema akawa hajaelewa kabisa. “Nanaa nilimfikisha kwa Geb, unataka na wewe…” Jema alicheka sana. “Yaani niishie kuitwa shemeji kila siku!?” Jema alicheka mpaka machozi. “Unataka kuninyima nini tena Jema, mama?” Jema alicheka, hakutarajia. “Mimi sijakupatia mwenzako.” “Na ibaki hivyohivyo.” “Asipatikane mwingine?” “Hapana. Sitaki.” “Basi hakuna kupatikana mwingine.” “Hapo sawa.” “Umefurahi sasa?” “Nani asiyependwa kusindikizwa maishani?” “Hakuna.” Jema akajibu akicheka.

Hakujua kama James ni mzungumzaji hivyo. Akawa naye kwenye simu mpaka alipofika na yeye kwake. “Sasa ulale Jema. Kesho kanisani. Nakushukuru saaaana kuwa na mimi safarini.” “Karibu na asante kwa wakati mzuri.” “Ni hivyo itakuwa ni kama nakuigilizia. Basi bwana.” “Lakini kama si kuigilizia?” Jema akauliza akicheka. “Na mimi ningesema asante kwa wakati mzuri.” “Kweli huko ni kuigilizia.” “Kama si kuigilizia?” “Ningesema karibu.” Wakacheka na kuagana wote wakiwa na furaha sana.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

James akakutana na Jema mbaye hata hakumtegemea! Ile furaha Kumu aliyosema alikuwa akiipata kuwa na Naya masikioni, usiku wote, wote wawili usiku huo wakaelewa ni nini Kumu alikuwa akimaanisha. Ile kuwa pamoja ikawatoa upweke na kujengwa ahadi ambazo kwa mara ya kwanza hisia zilizokuwa zikitembea usiku huo, zikamfanya James kwa mara ya kwanza kutoa ahadi kwa Jema aliyekuwa akimlilia Mungu na kusubiri kwa uaminifu. Jema ambaye alishamparamia Joshua akidhani ni wake, kumbe sio. Alipompiga stop, Jema hakuwa na makuu. Akashukuru Mungu na kujiweka pembeni akimtumikia huyo Joshua hata alipokuwa akimtuma kwa Naya. Alifanya bila kinyongo akimwambia Mungu anawekeza kwake, asiwahi kusahau kuja kumlipa kabla ya kufa kwake. Leo anafurahishwa na James! Mkaka anayependa maendeleo! Alifurahi Jema, akabaki akimshukuru Mungu na kufurahia kusubiri kwake.

Kwa Bale.

Wakati usiku huo ukiendelea kwa furaha pande hii, huku kwa Bale aliyekuwa amefanikiwa sana kwa mali zake na za Malon, ambazo hazikuwa na maswali na yeyote kwani hakuna aliyekuwa akijua Malon anamiliki nini na kipo wapi. Akajikusanyia mpaka akaridhika na nyumba ya Kunduchi akajimilikisha. Akaunti zikawa zinasoma vizuri sana. Akiwa amelala akasikia kwa wazi kabisa. “Nikiwa nipo hai au nimekufa, usiwahi kuuza binti yangu!” Bale alishituka sana. Ilikuwa sauti ya baba yake masikioni kwake ila kwa wazi kabisa mpaka akatoka usingizini.

Alipofungua macho, akamuona Malon anatoka hapo chumbani kwake. Bale alishituka zaidi mpaka akaruka kitandani. Aliyemuongelesha ni baba yake. Aliyemuona akitoka hapo chumbani ni Malon.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Mziki Ndio Kwanzaaaa Unaanza. Usipitwe.


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment