Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 2. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 2 - SEHEMU YA 2.

Akampigia simu mama Jema. “Samahani mama yangu nakusumbua lakini nilitaka kujua umefikia wapi?” James akaenda kwenye point moja kwa moja baada ya kujitambulisha na salamu kwa mama Jema. “Wala usijali. Hivi hapa nilitaka kuzungumza na Jema. Bibi yake amefurahi sana. Ila kwani wewe James, huna washenga?” Hapo James akatulia kidogo na kukumbuka mshenga angekuwa Joshua na Geb, ndio hao ametoka kuvunja undugu. Akapoa kidogo. “Maana kungekuwa na washenga, ungeanza kutuma kwanza posa. Ndipo wapewe taratibu za mahari. Ndipo tarehe ipangwe kisha, mje kutoa mahari. Ije sendoff, mambo ya kitchen party. Maana mama zake huyo Jema naona wote wanaitaka hiyo harusi, naona na mipango ishaanza. Ndipo sasa harusi yenyewe.” James akachoka kabisa.

“Nisaidie mama yangu. Huo mlolongo ni mrefu mno. Mimi sitaki makuu. Kuna aina ya harusi aliyokuwa akiiwaza Jema. Anasema alikuwa akiiwaza tokea mtoto. Hiyo ndiyo naona ni ya msingi na pengine aina hiyo ya gauni ndio nitaruhusu inicheleweshe, ila hivyo vitu vingine naomba unisaidie tufupishe mama yangu.” “Kama nini James mwanangu?” “Nisaidie tuvuke vyote, twende kwenye mahari moja kwa moja. Wakati tukisubiri gauni la Jema, mnaweza kumfanyia mambo yote. Gauni likiwa tayari tu, tunafunga ndoa.” Mama Jema akacheka.

“Kwani huyo Jema anataka gauni gani?” James akacheka. “Naomba umuulize yeye mwenyewe, ila nafikiri inabidi kutengenezwa. Anasema alikuwa nalo akilini tokea mtoto mdogo, akitamani siku akiolewa ndio avae hilo. Na mimi nilipata hiyo bahati ya kulijua kutoka kwenye mazungumzo yake tu. Sijamwambia kwamba nitahangaika mpaka alipate maana ni kama amekata tamaa ya kulipata, ila hapa kazini kuna mama ameniambia anamfahamu mtu anayetengeneza magauni mazuri sana ya harusi, anauhakika akikutana na Jema mwenyewe akamuelekeza, ataweza kumtengenezea japo inaweza kuchukua muda. Kwa hiyo nataka jumamosi akitoka kazini, nimkutanishe na huyo fundi.” “James unampenda Jema!” Ikabidi tu mama mtu aseme akisikika kufurahia.

“Sana mama. Ni msichana aliyetulia, halafu nimejikuta anavigezo vyote vya ninayetaka awe mke wangu. Si mgomvi kabisa, kitu kinachonifanya niwe na uhakika wa pumziko hapa duniani.” “Basi kumbe umemjua. Jema hapendi ugomvi na ndicho kilichomtoa hata hapa nyumbani. Kelele zangu na Jelini zilimshinda kabisa. Hawezi ugomvi mpaka utamuhurumia.” “Nimemgundua. Nisaidie mimi ndio nimuoe mama yangu. Sitaki kuja kuzidiwa mahesabu.” Mama Jema alicheka sana.

“Hawakawii!” “Hapa mjini hakuna waoaji wa hivyo James mwanangu. Wachezeaji watupu. Ndio maana unamuona mpaka leo huyo Jema yupo. Ila usiwe na wasiwasi. Acha nizungumze na bibi yake pamoja na mama zake, niwaambie hivyo.” “Asante mama yangu.” Akakata simu na kubaki akifikiria.

Mama ni Mama.

Akajua kwa hakika alimpunja mama yake mengi sana tokea anakua. Ndoto za mtoto wa kiume alizokuwa nazo akiwa anamtafuta James, zilikuja kuisha pale James alipoweka msimamo kwa Nanaa. Kukaanza kuvutana kati yao. Akajiona anajukumu katika hili, kumtaarifu kuwa amepata mchumba. Akaamua kumpigia simu mama yake. “Shikamoo mama.” “Marahaba. Vipi huko?” “Nimepata mchumba naoa.” James akaongea hivyo moja kwa moja. Akamsikia mama yake akicheka. “Unacheka nini sasa?” Akamuuliza mama yake na yeye akicheka. “Nimefurahi. Mlete basi nimsalimie.” “Ili uanze kumkagua?” “Kwani namuoa mimi? Hata akiwa chongo, ni wako. Tutapapasana hivyohivyo.” James akacheka sana. “Huna neno?” “Hata nikiwa nalo, ni wako. Unaishi naye wewe. Mimi nataka kumuona tu mkwe wangu, tufahamiane, basi.” “Kama ndio hivyo basi nitamleta.” “Lini? Maana si unishitukize, nishindwe hata kumpikia!” James akashangaa sana.

“Sasa mbona hata huulizi kabila!?” “Litanisaidia nini wewe? Niambe lini unamleta.” Ikawa tofauti na alivyotarajia. Ikamshusha kabisa James aliyekuwa amejiandaa vita kwa upande wa mama yake. “Wewe ndio upo busy mama. Niambie wewe.” “Mbele ya mkwe. Hata ukitaka leo, nitawahi nyumbani nipaweke sawa, nipike, aje ajue nyumbani.” James alifurahi sana. “Nashukuru mama yangu. Basi naomba iwe kesho ili leo nimuandae.” “Sasa sio upotee James, bwana! Maana umeshaniamsha morari!” “Kweli mama?” “Sana James! Dada zako wote hakuna aliyeolewa. Wewe naye muendeleza ukoo ukawa kimya! Wewe unafikiri najisikiaje? Angalau na mimi nitaonekana nina uzazi jamani! Sio uzazi wangu unaishia kwenu tu. Kama mwenye laana!” “Basi nitamleta mama yangu. Hapo umenipa moyo. Kesho.” Mpaka James akamshangaa jinsi mama yake alivyofurahi na kujutia kumuogopesha Jema juu ya mama yake.

Wema Hauozi.

James akabaki akiwaza lakini na tumaini jipya. Danny akamfuata. “Kwema kaka?” “Kwema Danny. Nataka kuoa.” Danny akacheka sana. Alikuja kuulizia aliyoyaona alipowaona kina Magesa, hakutarajia kusikia maswala ya James kuoa. “Jamesss!” “Nimepata msicha aisee!” “Hongera sana. Lini?” “Hata pete bado sijamvalisha. Na sijui namvalishia wapi?” “Pete yenyewe unayo?” “Sina aisee.” “Twende tukaisake.” “Acha masihara Danny! Kwamba kweli unanisindikiza?!” “Wewe! Huna utakaloniomba nikasema hapana James.” Danny akacheka na kutingisha kichwa.

“Labda iwe roho yangu, napo ni kwakuwa sina jinsi ya kukupa. Ila wewe! Hata ukiomba mshahara wangu wa mwezi mzima. Wote, nakupa.” James alicheka sana. “Sikutanii James. Ulinitizama nikiwa sitizamiki kwa dhambi chafu, mbaya ambayo nilisababisha mwenyewe kwa ujinga wangu. Najua hata malaika mbinguni walishindwa kuniangalia ila wewe.” “Acha hizo Danny!” “Ooh! Najua nilichokifanya James. Najua. Niliua watoto wangu vibaya sana. Ni kama niliua wote. Nasikia Fili hanitaki kabisa. Ni kama siku ile nilipoua wadogo zake, ni kama nilimuua na yeye. Niliua ndoa yangu mimi mwenyewe. Nikiwa kwenye ile hali, sijui pakwenda maana hata wauguzi wenyewe walikuwa wakiingia pale si kunisaidia ila kuniona kiumbe kikatili, kibaya kilichokuwa kikisemwa mitandaoni. Lakini James, hata mimi ulinishangaza aisee! Mimi mwenyewe sikujua uliwezaje!” Danny akatingisha kichwa kwa masikitiko.

“Miezi miwili upo na mimi hospitalini bila kuchoka. Ukiniosha kama mtoto mdogo na kuhakikisha nakula! Bila kulalamika wala kunisimanga! Umenitunzia kazi yangu hapa, ukiandika barua kila mahali ukihakikisha sifukuzwi kazi! Nimetoka hospitalini bado ukahakikisha sikosi mazoezini ili kuweza kurudi kutembea tena! Haya, nimekuja kugundulika nimeathirika, pia hujawahi hata kuniangalia tofauti ila kuuliza dawa sahihi kwangu na kuhakikisha nakula vizuri! Upo na mimi nikiwa nimepoteza kila mtu! Hakika twende tukatafute pete na wewe uoe.” James akacheka sana. “Unalipa fadhila” “Wala sitaweza.” Wakatoka wakicheka.

Chanda Chema, Huvikwa Pete.

“Nipe basi wazo jinsi ya kumsuprise. Maana yupo busy mno na kazi.” Wakaendelea kuongea wakiwa njiani wakienda kutafuta pete. “Cha kwanza jua ni nini anapenda. Maeneo yepi yanamfurahisha.” James akatulia akifikiria. “Aisee muda mwingi anakua kazini.” “Kanisani je?” “Ndio tumeanza kwenda naye kanisa jipya. Sina ninayemfahamu huko.” “Duuuh! Hapo sasa kazi ipo.” “Kwani nikimvalisha kazini kwao sio sawa?” Danny akatulia akifikiria.

“Wewe unayafahamu mazingira ya kazini kwao?” James akatulia akitafakari. Hakutaka kumuhusisha Kumu. Lakini akawa hana namna. “Yupo mtu anayeweza kunisaidia kuandaa mazingira. Japo ni bosi wake, na yeye anamuogopa sana.” “Mbona humtaji jina huyo msichana mwenyewe?” James akacheka.

“Ni nani?” “Nahisi na wewe utakuwa unamfahamu.” Danny akatulia akijaribu kufikiria katika watu anaowafahamu yeye pamoja na James, halafu aolewe na James! Akafika mwisho. “Acha kunipa wakati mgumu bwana. Niambie ni nani?” “Unamkumbuka yule msichana wa Coca, yule aliyekuwa..” “Jema!?” James akadakia kwa mshituko. “Wewe umemfahamia wapi Jema!?” Danny akacheka sana.

“Kasa alikuwa akimmezea mate kuliko nitakavyokwambia. Kuna kipindi Jema alikuwa akishugulikia mambo ya kampuni yao, akitaka aunganishwe na mtu wa Utawala anayekusika na jengo zima, ili azungumze nao waje wafanye biashara hapa. Akakutana na Lela, naye Lela akamuelekeza kwako, ndio Kasa akamlalamikia Lela eti kwa nini hakumuelekeza kwake, yeye anamtaka. Ndio Lela akamwambia hata angemleta kwake, Jema sio type yake.” “Haiwezekani! Hamjui Kasa nini?” “Alimfanyia kusudi ili kumkera tu. Anasemaga Kasa anaringa sana. Si unajua ile sema yake. Yupo hapa kazini, lakini si kwa shida kama sisi wengine. Kwao mamilionea. Sasa hicho kinamkera sana Lela. Halafu anamsema Kasa anajidai matawi ya juu sana. Kwahiyo alimfanyia kusudi, kumdharaulisha tu. Sasa bwana Kasa amemmaindi Lela vibaya sana. Hataki hata kumuongelesha, akipita hamsalimii.”

“Sasa siku moja mimi nikamuona Kasa anagawa vinywaji pale mbele kwa wale wasichana wa pale mapokezi wote kasoro kwa Lela. Nikamuuliza kulikoni?” James akacheka akitingisha kichwa. “Kasa! Sasa akakwambia nini?” “Si ndio akanisimulia kisa kizima. Mimi nikawa nacheka tu. Ndio na Lela si unajua anavyopenda kunitania mimi mkwewe? Akaniita na kunisimulia kuwa amemkomoa makusudi. Na ashamwambia na Jema kuwa Kasa tapeli, asiwahi kumsikiliza.” “Haiwezekani!” “Nakwambia wanabifu la waziwazi. Na mpaka leo namaanisha leo hii, Kasa amemnunia Lela sababu ya Jema. Kumbe ndio unataka kumuoa!? Sasa amekubali?” “Acha maswali ya ajabu. Ningeenda vipi kutafuta pete kama hajakubali?” Danny akacheka sana. “Mpigie huyo bosi wake basi kuweka mazingira.” Danny akaweka ushawishi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

James akafikiria na kuamua kumpigia Kumu. Akapokea kwa haraka tu. “Umepotelea wapi wewe?” “Nipo. Vipi Naya?” “Namshukuru Mungu anaendelea vizuri aisee. Kwema?” “Leo nataka kumchumbia Jema.” Kumu hakutegemea. “Upo Kumu?” “Subiri kwanza James, wewe ndiye uliyekuwa ukileta maua na zawadi kwa Jema?” “Sijui kama kuna mwingine, ila na mimi nimekuwa nikileta.” Joshua akajikuta akicheka. “Nimekukubali James.” “Kwa nini kaka?” “Aisee mimi mpaka nikawa najiambia, huyu mtu amekusudia kwelikweli. Ila kwa kuwa ni wewe, furaha yangu imeongezeka. Jema is like a little sis God gave to me. Anastahili mwanaume kama wewe. Na hongera sana.” “Nashukuru Joshua. Sasa nataka kumchumbia leo. Itawezekana au anamajukumu mazito?” Akaomba kiustarabu.

“Kwa Jema! Aisee kila kitu kitasimama kwa muda ili kufanikisha hili. Wewe niambie tu ni saa ngapi unataka kuja, ili nikutayarishie mazingira mazuri.” “Aisee nakushukuru Kumu.” “Lazima aisee. Unakumbuka jinsi alivyojitoa kwangu na Naya?” James akacheka tu. “Aisee sina jinsi ya kumlipa ila kwa njia hii. Unaye mpiga picha sasa?” “Sijafikiria umbali huo.” “Basi acha nimpange jamaa aliyenisaidia kwenye shuguli zangu zote. Amenitengenezea kumbukumbu nzuri sana. Utamkuta akikusubiria hapa.” Wawili hao wakapanga mipango vizuri, James hakutegemea uungwaji mkono wa kiasi hicho. Juhudi ya Jema kazini, na kujinyenyekeza kwa bosi wake, siku hiyo ikamlipa. “Aisee nakushukuru Kumu.” “Kwa Jema, wewe tamka tu kaka, mimi nitakimbia.” Wakacheka na kuagana Joshua asiamini kama ni James kwa Jema!

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

James alikwenda kulekule alikonunua Joshua pete ya Naya. “Hapa ni garama kaka!” Danny akamtahadharisha. “Kwa Jema, acha nitoe tu.” Danny alicheka sana. “James umependa!” “Aisee nimependa. Nampenda Jema. Sana. Ni watofauti na vile anavyoonekana. Amebeba unyenyekevu fulani hivi! Aisee namtaka yule mtoto kwa garama yeyote ile. Halafu hana makuu!” “Mbona lakini anaonekana viwango vizito sana!?” “Na mimi nilishangaa sana baada ya kumfahamu. Unaweza kumuonea kirahisi sana. Ule ujasiri wake nimegundua ni kwa vile huyu Kumu, bosi wake, alivyo muamini sana na kumuonyesha anaweza, ndio ikamfungua na kumpa ujasiri wa kufanya kama vile anavyoonekana kwetu. Lakini ukiwa mpuuzi tu, unaweza kumdhulumu kirahisi sana. Ana moyo mnyenyekevu na anaimani kubwa sana. Nampenda Jema, aisee. Acha nimuoe roho yangu itulie.” Danny akamsikiliza, wakashuka garini lakini Danny akawa kama amepotelea mawazoni.

James alimuona ila akamuacha tu. Akajua lazima atakuwa na majuto makubwa sana. Danny anaishi sasahivi kama mseja tu, tena ameathirika. Wakati alishamiliki mke wa maana na watoto watatu! Akaweka heshima kwenye jamii kama mwanaume mwenye familia bora! Amebakiwa na kumbukumbu mbaya za vifo vya wanae. Ila anajua kama sasahivi Grace ni kama alilipwa na Mungu. Amerudisha idadi ya watoto watatu vilevile, akaongezewa na wakike. Akatulia kimya.

James alishawahi kumuuliza Jema anavaa pete kwa saizi gani, Jema akamjibu. Lakini jinsi alivyomuuliza na kumjibu, hakujua James alikuwa na maana yake, maana aliichomekea tu katikati ya stori. Basi siku hiyo akakutana na aina za pete nzuri hata Danny mwenyewe akazikubali. Akalipia ndipo akampigia simu Joshua. Wakapanga tena vizuri, na Joshua naye akamwambia anajipanga kumfanyia Jema surprise nzuri.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakakata simu Joshua akatumia watu wote wa kitengo chake kasoro Jema kuwa wanataka kumfanyia Jema surprise, baada ya dakika 45, kila mtu atoke ofisini wawepo eneo la nje tu, lakini wajibaraguze, asijue. Akawaambia na watu wengine wa vitengo vingine ila sababu hakutoa akijua wapo wasio na kifua wanaweza kuharibu kwa kumwambia Jema mwenyewe. Kwa hiyo akabakiwa na sababu yeye mwenyewe. Ila wengine wakishangaa na kuulizana Kumu anataka kumfanyia Jema surprise gani! Ikabakia kila mtu anahamu yakuona hiyo surprise.

Muda ulipofika, James akawasili na kuandikisha jina getini akisema ni mgeni wa Joshua Kumu, na Kumu akaruhusu aingie. Akampigia simu Jema na kumwambia wotoke waende kitengo cha Uzalishaji, kuna mambo anataka kuweka sawa. Haraka sana Jema akachukua Tablet yake na kutoka kwa kasi kama kawaida yake na kiatu chake cha juu. Kumu ametangulia mbele  yeye anafuata nyuma kwa haraka asimchelewe. Wakatoka mpaka nje ya jengo la kitengo cha Masoko sehemu ambayo aliomba James apelekwe. Walipofika, Kumu akajidai amepokea simu, anazungumza. Ikabidi Jema kumpita ili kumpa faragha kwenye mazungumzo yake.

Mara akamuona James. Kitu kikaruka moyoni kwa Jema na kushindwa kujizuia. Akaruka kwa furaha na kumkimbilia akiwa amesahau kuwa, bosi wake yupo nyuma yake.  Kumu! “James!” Akamkumbatia kwa furaha zote. “Unafanya nini huku!? Au umemfuata Kumu?” “Nimekufuata wewe.” Jema akakunja uso akicheka. “Mwenzio nina kazi, James. Nipo katikati ya…” Akashangaa James anapiga goti, akawa hajaelewa kabisa. Maana mawazo ya Jema hayakuwa kwenye kuchumbiwa kwa kuvishwa pete, ila kulipiwa mahari. Hicho kipengele cha kuvalishwa pete, akawa kama amekisahau kabisa.

“We James!?” Akatoa pete akiwa amepiga goti kwa mguu mmoja, mbele yake. “Nimekuja kukuchumbia Jema. Nataka kukuoa, uwe mke wangu!” Jema alishangaa sana mpaka akajifunika uso na tablet aliyokuwa ameishika. Kumu akaikimbilia na kuichukua, akicheka. Jema akashangaa sana huku machozi yakimtoka. “Kubali Jema wangu tuoane.” “Mimi nakupenda James!” James akamvuta mkono na kumvalisha pete. Jema akashangaa watu wanapiga makofi. Akamwangalia James na Kumu huku bado machozi yakimtoka, James akamalizia kumvalisha pete.

“Umeipenda?” “Mimi sikutegemea James! Asante.” James akamvuta, akamkumbatia na kupata busu palepale juani, watu wakazidi kupiga makofi na miluzi. Na James hakumuachia akabaki akinyonya midomo yake watu wakizidi kushangilia. “Naye James hana kiasi bwana! Mpaka tujute!” Danny akafanya James na Jema kuachiana na kuanza kucheka. “Nimefurahi sana.” Jema akaongeza asiamini. “Tuone Jema.” Kumu akamsogelea, Jema akampa mkono. Joshua akacheka na kutingisha kichwa. “Vipi?” “Heshima yako.” Wakazidi kucheka ndipo watu wengine wakampongeza na kuondoka taratibu maana Kumu alikuwa hapo, na ni muda wa kazi.

“Mimi nilijua tunakwenda Uzalishaji!” “Hapa ndio Uzalishaji kwenyewe. Vipi Jema wewe! Au uzalishaji ni lazima uwe wa vinywaji tu?” Wakazidi kucheka. “Nimefurahi sana. Hata sijui niseme nini! Natamani..” “Kurukaruka?” Kumu akamuuliza, Jema akajifunika kwa aibu. “Ukimletea zawadi huyu, mimi na Fina tunakoma. Anajifungia ofisini kwake halafu anaanza kurukaruka kwa shangwe.” Joshua akaongeza. “Mimi sikujua  kama napiga kelele.” Wakazidi kucheka. “Hongereni sana.” “Tunashukuru aisee.” “Sasa kusherehekea ni wapi?” Hapo James akakwama.

“Aisee sina mipango endelevu. Yaani nilikuwa napanga nikienda. Nimekaa ofisini, nikammisi Jema wangu, nikasema bora nimvalishe pete tu. Danny akanikuta nawaza, nikamwambia wazo langu, na yeye akaniambia tutoke tukasake pete. Ndipo na wewe ukanifanikishia hapa. Acha mengine niwaze taratibu.” “Basi acha mimi niwaandalie chakula cha jioni, niwakaribishe kwangu.” James akaonekana kusita. Joshua asielewe.

“Tunaweza kuzungumza pembeni kidogo?” Joshua akakubali. Wakajitenga wao wawili tu. “Nashukuru sana Kumu, lakini najua aina ya watu unaowafikiria kwenye hicho chakula utakachokiandaa, kwa sasa nimeamua kumuweka Jema mbali nao kidogo.” “Hakika sijaelewa James.” “Kama utaniruhusu nisiende kwa undani, nitashukuru. Ila kwa sasa sitaki Jema awe karibu na kina Magesa. Nilimpeleka nyumbani kwao jana, haikuishia vizuri. Sitaki kumchanganya Jema sasahivi.” “Japokuwa sijaelewa, lakini pia tunaweza kukuandalia chakula wewe na Jema tu. Mkaja kula pamoja na mke wangu. Tukawa wanne tu. Hatuna sababu ya kualika watu wengine.” “Ni sawa tukimkaribisha Danny, mama Jema pamoja na mdogo wake?” “Bila shaka. Nipe idadi tu, kisha niweke mazingira mazuri nyumbani.”

“Haitakuwa usumbufu kwa Naya?” “Naona kama itamsaidia kupata kitu chakufanya mbali na kujifikiria yeye mwenyewe.” “Nashukuru kaka. Basi acha nizungumze na mama Jema nione kama atakubali kuja. Ila nikuombe jambo gumu kidogo.” “Karibu.” “Naomba na Jema naye apate nafasi kama uliyompa Naya. Aandae nyumbani kwangu.” Hapo Joshua akasita. “Tafadhali Kumu.” “Basi nitakuja na Naya mimi mwenyewe. Huyo bado simuamini na mtu aisee. Nalinda kama mboni ya jicho langu. Mimi na Jema leo tutafunga ofisi mapema. Nitakwenda kumchukua Naya na kuja naye kwako. Ila mpishi nitamwambia akimaliza tu kupika, alete chakula nyumbani kwako. Nafikiri tunazo sahani nyingi tu, tunaweza kumpa azilete pamoja na chakula na kuandaa mazingira mazuri.” “Hapo utakuwa umenisaidia sana.” Wakazungumza kidogo, Kumu yeye akarudi ofisini.

“Acha nirudi ndani James. Tuongee kwenye simu. Mimi ndio nashika ratiba yake yote. Hana anachokifanya bila mimi.” James akambusu. Jema akacheka. “Sasa leo bosi wako amesema atakuruhusu mapema ili ukawaandalie wageni wetu chakula. Waje washukuru Mungu pamoja na sisi kwa hatua yetu ya kwanza kwenye maisha.” Mpaka hapo akawa amemchanganya Jema. “Tunaandaa tafrija fupi nyumbani kwetu Salasala. Mimi nitaalika watu, nitazungumza na mama Jema. Nakumuomba yeye na mama James ili waje waungane nasi. Nitawaambia ni gafla, lakini hatukuwa na jinsi. Itakuwa vizuri pia wapafahamu nyumbani.” Jema alifurahi sana.

“Uwahi mama, ili kupokea wageni na kuwakarimu.” Jema akazidi kucheka na machozi. “Acha kulia sasa. Njoo.” Danny akawapisha. Akamshika mkono na kumsogeza kivulini. “Umeelewa lakini?” “Nahisi.” James akacheka. “Kumu atakuruhusu mapema. Kimbia nyumbani kwako. Chukua nguo, funguo hizi hapa za kwetu Salasala.” Jema akawa kama haamini. Akakabidhiwa fungua aliyokuwa amepewa Nanaa na kupokonywa asubuhi hiyo. Akabaki akiiangalia na kucheka huku akifuta machozi.

“Mpishi ataleta vyakula na sahani. Msaidiane jinsi ya kuandaa. Kumu atakuja na Naya kukusaidia baadaye. Na watu wote nitawaambia wafike nyumbani saa moja usiku. Si umeelewa.” “Nimefurahi James! Hujui tu.” James akamsogelea zaidi na kupata busu la muda tu kisha akamuachia. “Wahi kazini tusiharibu na usilie bwana. Mimi nilitaka ufurahi.” “Nimefurahi James, siamini! Sikutegemea kuvalishwa pete kwa namna hii! Sikutegemea hata kidogo. Bado siamini!” James akacheka. “Acha nikatulie na kuangalia pete yangu vizuri. Nzuri sana. Kuliko hata ya Naya!” James akazidi kucheka na kufurahia furaha aliyoiweka kwa Jema. “Nakupenda Jema.” Jema akambusu kidogo. “Asante James. Asante kwa kila kitu. Na sitachelewa. Nitajitahidi kuwaandalia wageni wetu vizuri.” “Hayo ndio maneno. Kuna mtu unataka kumkaribisha kwenye hiyo tafrija ili tuweke idadi ya kutosha ya chakula?” “Sasahivi akili imevurugika, sijui tena. Acha nikatulie nitakujulisha. Lakini kwa hapa kazini sina ushoga na mtu wakusema kumkaribisha nyumbani. Labda ndugu.” “Haya nenda usichelewe. Tuwe na kiasi.” Jema akarudi ofisini kwa haraka. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Zungu la nguvu!” Fina akamtania mara alipoingia. “Nimefurahi Fina! Sikutegemea! Wewe ulijuaje?” Fina akamvutia ofisini kwake na kufunga mlango. “Nini?” “Bosi wako huyo. Kumu ndio kaandaa watu wote waje washuhudie ukivalishwa pete.” “Haiwezekani Fina!” “Kweli. Nafikiri walipanga na huyo mzungu wako.” “Fina mimi napendwa!” Fina alicheka mpaka akakaa kwenye kiti. “Unapendwa?” “Sana. Hivi hapa na funguo za nyumba nimepewa. Nimeambiwa nikaandalie wageni wetu, kwetu.” “Jema huyo!” “Napendwa mwenzio. Na nina kwangu na mpenzi wangu!” “Hongera.” “Asante dada. Nimefurahi sana.” Simu ya mezani kwa Fina ikaanza kuita. “Kumu huyo.” Akatoka mbio.

Kisha akasikia anaitwa. Akatoka kuelekea ofisini kwa Kumu. “Nashukuru bosi wangu. Asante Kumu.” “Hongera sana Jema. Sasa kabla hujaanza kunichanganyia ratiba kwa furaha, naona leo uchukue off. Nenda kajiandae na tafrija jioni.” “Na wewe?! Bado mapema sana, acha nifanye kazi hata angalau ifike mchana, nisogeze kazi usilemewe!” Jema hakuamini, akaanza kubabaika yeye mwenyewe. “Nitumie ratiba yangu yote. Na majukumu yako, mimi nitafanya.” Jema akajishangaa anaanza kulia mbele ya Kumu.

“Sasa unalia nini?” “Mimi sikutegemea!” “Wewe ulinibeba sana miezi michache iliyopita, Jema. Ni hivyo huelewi tu. Nilihitaji mtu kama wewe, na wewe ukakubali Mungu kukutumia kwenye kipindi nilichohitaji sana msaada. Sina jinsi ya kukulipa ila kukusaidia katika hili. Nilimwambia hata James, wewe umekuwa kama mdogo wangu, niliyepewa na Mungu.” Jema hakutegemea kusikia hivyo kutoka kwa mtu kama Kumu kumwambia hivyo. “Nenda kajiandae na siku yako. Ni muhimu sana, najua utahitaji.” “Nashukuru. Nimefurahi sana.” Kumu akacheka na kurudisha macho kwenye kompyuta yake bila ya kujibu. Jema akatoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Hatimaye Jema Naye Amechumbiwa kwa Staili ambayo hakutegemea!

Mambo yanaendelea.

Nini kitaendelea mbeleni?


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment