“Msiondoke
bila kula James!” Mama G akamuwahi. “Kama ni chakula tu, tumepita magenge kibao
huko barabarani mpaka kufika hapa. Kilichotuleta hapa, ni hiki alichokatazwa
Jema. Kufahamiana kwa karibu, kwa kuwa namuoa Jema. Tena namuoa siku za
karibuni sana. Sasa kwa kuwa nilijua nyinyi wote mnamfahamu, ilikuwa ni kiasi
cha kuendelea tu kujenga ukaribu zaidi, sikuwa na shaka. Sasa kusikia tena
mnataka tuanze mwanzo! Tena taratibu! HAPANA kwakweli. Nyinyi anzeni kwa
taratibu hizo zenu mpya lakini si kwa Jema huyu, na si kwa kumfoka
kama mtoto mdogo.” Hapo James akabadili gia.
“Mnamfoka
mpenzi wangu mbele za watoto halafu eti mnatudanganyishia chakula! Kweli jamani
au mmemdharau mpenzi wangu?” “Acha hasira James!” “Ingekuwa ni wewe mkeo
amefanyiwa hivyo, ungemrudisha sebuleni, asubiri chakula? Eti Geb? Kwa njaa
gani jamani ambayo mnatuona nayo?” Kimya. “Acha sisi tukaendelee na ya
kwetu.” James akamchukulia pochi yake. “Twende zetu Jema wangu.” Akamshika
mkono. Wakatoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Samahani
James. Nia ilikuwa nikusaidia tu. Nilijiona nimebaki pale sebuleni peke yangu.
Sikutaka kutayarishiwa pale kama mgeni rasmi, wakati tulishakutana nao kwa Kumu
zaidi ya mara moja. Tena tukafahamiana na kufanya nao kazi pamoja, kwa karibu
sana mpaka mwisho wa harusi ya Kumu. Nikajua tumeshafahamiana. Leo nikaona
nisaidie nisijifanye mgeni. Sikukusudia kuharibu, tafadhali nisamehe. Sio
kiherehere wala ujasiri wa kupitiliza kwenye nyumba za watu.”
Akakumbuka hayo maneno yatamuuma zaidi kwa kuwa ndiyo aliyoachwa nayo na Temu.
“Usingefanya hivyo ndio ningekushangaa.”
Wakamsikia James akimjibu. “Mimi ndiye nimekosea kukuelekeza tokea mwanzo. Ila
ni kwa vile nilivyomfahamu huyu mama na wanae. Alitupokea tukiwa vijana wadogo
hatuna kitu wala yeye hana kitu ila upendo tu kwetu. Akiwa na chumba kimoja
alitufungulia milango ya nyumbani kwake, pakawa kwetu bila kujali kabila wala
haiba zetu. Nilipokwambia huyu mama ni kama mama yangu wa pili, sikukudanganya
Jema.” Wakamsikia akimtuliza kwa Upendo.
“Kuna kipindi
niliugua, akaniuguza kama vile mimi ni huyo Geb mwanae. Nikiwa na gumu lakutaka
ushauri, ni mtu wangu wa karibu na haachi kuniombea mimi kama mwanae wakumzaa.
Nilikwambia nakuamini naye kuliko hata mama yangu mzazi, ni kweli. Kwa sababu
ya vile nilivyoishi naye mimi. Kwa hakika kosa ni langu Jema. Mimi ndio
unisamehe, nilikosea mpenzi wangu, na naomba usilie.” “Najihisi
nimeharibu sana. Hakika sikukusudia.” “Nakuhakikishia
hujaharibu, Jema. Ingia kwenye gari, tusisimame juani. Panda twende.” Wakasikia
kilio cha Jema kidogo, kisha mlango ukafunguliwa na kufungwa.
Nyongo, Mkalia Ini.
Baada ya
muda James akarudi. “Nanaa!” Wakamsikia akimuita bila kuwaongelesha wale
waliokuwepo pale sebuleni. Nanaa akatoka, alikuwa jikoni, Geb na mama yake
sebuleni, kimya. “Isiwahi kutokea tena katika maisha yako, ukampazia
sauti Jema. Iwe mwanzo na mwisho. Huruhusiwi kumfoka Jema. Leo naishia
hapa kwakuwa imetokea nyumbani kwenu, ila nitajitahidi kumuweka mbali na
nyinyi ili hiki kilichotokea leo, kisiwahi kurudiwa hata kwa kusimuliwa.
Iwe mwanzo na mwisho wako.”
“Kwa
vyovyote ulivyomuona na kumfikiria, mpe heshima kama unayowapa watu wengine
baki. Huko itakapotokea unakutana naye, akatenda jambo ambalo hujapenda, ondoka
hiyo sehemu, au zungumza naye kwa heshima. Umenielewa?” “Ndiyo na …” “Na
ingetokea kwa mtu mwingine, ningeelewa. Ila WEWE!” James akamkatisha akimshangaa
sana. “Hakika SIKUTEGEMEA Nanaa! Watu hubadilika, lakini isingekuwa WEWE!” James
akaondoka kwa hasira. Geb na mama yake kimya. Kimeumana ndugu.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Huku kwa
Jema akawa kama amepata mshituko. Alichokitarajia kwa hamasa, hakijawa hata
nusu yake! Nanaa aliyemuona nyumbani kwa Kumu siye aliyekutana naye kwenye jumba
lake. Alimshusha, mpaka Jema akajiona ni mdogo asiyefaa. Akatulia kwenye
gari mpaka akahisi baridi, kwa mshituko. James akarudi garini. “Unataka kwenda
kula wapi?” “Naomba nirudishe tu kwangu James.” “Hapana.
Hatuwezi kufanya hivyo Jema! Leo ni Nanaa. Kesho ukienda kukutana na mama yangu
ikawa mbaya zaidi ya hivi ndio tunaahirisha ndoa?!” “Mimi
hata sijui tena! Tutakuwa na ndoa ya namna gani ndugu zako hawanipendi?” “Ulitaka
tukishaona ukakae pale kwao?” “Hapana James!”
“Niambie
tu kama umepalinganisha kule kwangu na kwao, kisha ukapapenda kwao, ukawa
umeshapigia mahesabu ya kwenda kuishi pale.” “Hapana James. Mimi
sijapadharau kwako. Ila hata tufanyaje, hawa ni ndugu zako.” “Utaolewa
na mimi, na nishakupeleka ambako utaishi na mimi. Hakuna wakukubugudhi.” “Wakati
yeye ndio anajua kula yako! Anaingia mpaka kwenye mafriji yako na kukupangia
ule nini!” James akatulia kidogo. Alishasahau hilo.
“Sitaki
kuwa kwenye maisha ya misukosuko James.” “Nilikwambia sasahivi ndio
tunajenga msingi wetu. Kila kitu kitakavyokwenda kuanzia sasa ni vile
tutakavyokubaliana mimi na wewe.” Hapo Jema akatulia. “Umenielewa? Inamaana
kuanzia sasa, hawezi tena kufanya kile alichokuwa akikifanya kabla
sijakutambulisha kwao. Mimi nachukulia ndio nimeshakutambulisha, na wenyewe
lazima kuelewa kuwa sipo tena peke yangu. Niambie kitu kingine.” Jema akatulia.
“Naomba
tukale sehemu kwanza ndipo nikurudishe nyumbani.” “Kama unaweza kusubiri,
naweza kupika tukala.” James akacheka. “Umeona mambo hayo! Acha kupaniki bwana!
Ujue watoto watakuwa wakikuangalia sana wewe?” “Sikutegemea James! Nanaa
niliyekuwa nimekutana naye kwa Kumu hakuwa hivi. Alikuwa mcheshi mno. Imekua ni
kama amenipiga kibao cha usoni, tena hadharani!” “Pole. Ila sasahivi
tuendelee na yetu. Hakuna tena kuangalia watu. Sisi tu.” Safari ya nyumbani kwa
Jema ikaanza. Haikuwa mbali. Alipangisha Sinza, karibu na Makaburini.
Akafungua
mlango wakaingia. “Karibu.” “Acha kunyongea bwana Jema!” “Nimeumia James.
Nimeumia sana. Ila nashukuru kusimama na mimi pale mbele yao. Ingekuwa
mbaya zaidi kama ndio ningetakiwa kurudi kukaa pale na watoto wakiendelea
kunihoji!” “Naomba tupange mipango yetu. Njoo ukae hapa.” Jema akaenda kukaa
hapo ila mbali kabisa. James akamsogelea. “Utaishi na mimi Jema. Naomba uwe na
amani. Hilo limeshatokea, lisituibie muda wetu. Niambie nifanye nini ili utulie
na kurudisha mawazo yako kwangu.” Wakabembelezana hapo, akapata mabusu
yakutosha, akaanza upishi.
Kwa Magesa.
Huku kwa
kina Magesa kukapoa. Nanaa akajua wazi ameharibu kupitiliza. Angalau mama G
akajipongeza safari hii yeye hajaharibu. Nanaa alishinda huko jikoni na
kushindwa kutoka mpaka akamaliza kila kitu, akaweka mezani akataka kukimbilia
chumbani, mama G akamuwahi. “Usiende kujificha, njoo hapa.” “Mimi naenda
kuoga.” “Mpaka tuzungumze.” Mumewe akabaki akimwangalia. Akajishauri na kurudi
kukaa.
“Wewe
umeruhusu hasira ya muda mrefu imekukosanisha na kaka yako. Unakumbuka sababu
aliyotupa James ya kusubiri kuoa?” Nanaa kimya, ameinama anasugua mikono. “Kaka
yako alisema hakutaka ajichanganye. Hakutaka kufika kwenye mahusiano ambayo
yatampasa kuchagua kati yako na huyo mpenzi, endapo mpenzi akatokea kukuchukia wewe.
James anakupenda kiasi ya kwamba aliweka maisha yake pembeni, ili akufikishe
wewe mbali. Alikosana na wazazi wake, na kupoteza furaha ya mzaliwa
wa kwanza, kwa ajili yako Nanaa. James hajui mambo nusunusu.” “Nimekosa
mama. Hata sijui ilikuaje nikamlipukia vile! Kaka amenichukia.” Nanaa
akaanza kulia.
“Basi na
sisi kwetu alikuwa hivyohivyo lilipokuwa likifika swala lako. Ni vile tulikuwa
hatukwambii. Siku ile Marangu ilikuwa karibu ampige Liz, ndio akashikwa.
Ilikuwa ugomvi, James hashikiki akikutetea wewe. Sasa na wewe ukaenda kuharibu
kulekule ulikomuona miaka yote akisimamia. James ni wale watu ambao hawajui
kuyumba akiamua kufanya jambo au akiwa na kitu chake mkononi.” “Naenda
kumuomba msamaha.” “Sio leo.” Akadakia Geb kwa haraka sana. “Sawasawa Geb. Leo ndio
utaharibu zaidi, maana sasahivi yupo kwenye kutengeneza kwa Jema. Kupiga
sasahivi ni kumuingilia. Na utamtibua zaidi.” Nanaa kimya.
“Sisi wote
tunajua ni hasira tu, maana hata wewe siku ya kwanza umekuja kwetu, ulifikia
jikoni, ukiwa umepita sebuleni. Au umesahau?” Mama G akamuuliza kwa kituo.
Nanaa asijue ndio anakumbushwa alikotoka au la! Akashindwa kujibu. “Sikumbuki
kukaribishwa kwako jikoni ila uliingia na kuanza kusaidia kazi. Na sisi sote
tukaona ni jambo Jema tu. Si ni kweli Nanaa mwanangu?” Akamng’ata na kumpuliza.
Nanaa akashindwa hata kujibu akabaki akilia. Mama G akaona anyamaze akijua
ujumbe wake umefika.
Maji Yameshamwagika, Hayazoleki Tena.
Jumatatu.
Siku ya
jumatatu asubuhi, James akaitwa kuwa anawageni. Akahisi ni kina nani ila
akaamua tu kwenda. Ni kweli akawa amepatia. Akakutana na Geb, mama G pamoja na
Nanaa. “Naomba tuzungumze James mwanangu.” “Nashukuru sana mmekuja ili
tuzungumze bila wasiotufahamu sisi. Watoto na Jema. Njooni hapa kwenye chumba
cha mkutano. Hakuna mtu.” Wakamfuata. James akawapisha mlangoni ili waingie,
Danny naye akawa anapita. Wakatizamana lakini ni kama aliyejionya, Danny
hakuwasemesha. Na kweli hali yake ni kama ilianza kurudia kuwa ya kawaida. Ule
udhaifu wa maradhi haukuonekana tena.
Wakaingia
wote ndipo James akafunga mlango. Akakaa mbele yao kama kuwaambia
anawasikiliza. “Nimekuja kuomba msamaha, kaka. Nilikosa.” “Hapana hukukosa
Nanaa. Hapo unataka kunifanya mimi mjinga. Labda nianze kukumbusha
unazungumza na mimi, nipo kwenye maisha yako tokea unazaliwa, na nipo kwenye
maisha ya kina Magesa kabla yako.” James akaanza taratibu bila jazba.
“Ninachotaka
kukwambia ni kwamba, SISI tunafahamiana, kwa undani sana. Nimekuona
jinsi unavyokarimu wageni uliochagua wewe. Tuanze kwa upande wa Kumu.”
Wote kimya. “Nilikuwepo na kukuona jinsi ulivyompokea Naya alipoletwa
kwenu na Kumu. Ulimfungulia milango yote bila hata yeye mwenyewe Naya kuomba,
tena alikuwa akikukatalia zaidi ya mara moja, na hukuwahi kuchoka
kumfungulia milango hata ya nyumbani kwako. Tuje kwa Man, mume wa Grace.” Wote
wakashituka kidogo.
“Unamkarimu
yule jamaa, kwa kutetemeka. Nilikuwepo nyumbani kwako mara ya kwanza wakati
dada yake Man, Malisa, alipokuja na yeye pale kwenu, kukutana nao, kina Man na
Grace walipokuwa wamekuja hapa Dar. Bila hodi wala ruhusa, kama wewe umesahau, acha
nikukumbushe. Yule dada alienda mpaka jikoni akiwa ametuacha sisi wote
sebuleni, akaongea kwa sauti akisema, amekimbilia jikoni kama anayepafahamu
vile, akiwa anataka glasi ya pili apunguze juisi ya mtoto wake alipewa nyingi
ataishia kuchezea tu. Unakumbuka Nanaa au umesahau?” Kimya.
“Ulikimbilia
jikoni kwenda kumsaidia kupata glasi huku ukicheka na kumwambia haina shida,
anakaribishwa, ajisikie yupo nyumbani.” Wote kimya. “Nikurudishe kwa ndugu
uliowapata juzi upande wa baba yako mzazi. Hao ndio hawana
mipaka. Wanaingia pale kokote, na kufanya chochote ukiwa huna neno nao. Siku ya
kwanza alipofika mke wa baba yako hapa nchini, ukumbuke na mimi nilikuwepo
Nanaa. Yule mama alisimama akiwa anataka kuongeza nafikiri juisi hiyohiyo.
Alisimama na kuelekea jikoni, ndipo akakuita. Sikumbuki kukusikia ukimkaripia
kuwa anakiherehere. Ujasiri wa kuzunguka kwenye nyumba yako anaupata
wapi! Na wala sikumbuki ukiwakaripia hao wote kuwa wamekaribishwa sebuleni,
wanataka kufika mpaka chumbani!” Hapo James alishabadilika kuwa mwekundu, kilio
cha Nanaa kilisikika. Geb na mama yake kimya.
“Anakuja
Jema. Mtu anayenihusu mimi. Nikisema mimi, namaanisha MIMI. Eti leo ndio
unamkaripia kwa kutaka kusaidia! Halafu si kwa neno moja useme uliropoka!
Unamuhoji mfululizo mkisaidiana na mwanao! Ukionyesha wazi ulikusudia, uliendelea
kumfoka mpaka nikashindwa kuvumilia, ikabidi kuja kumuokoa na kinywa chako.”
James akaendelea.
“Mbaya
zaidi, Jema si mgeni kwako! Anakufahamu kwa kukuona unapokuwa na wengine! Labda
mimi nikuulize, ungefanya hivyohivyo kwa mtu aliyeletwa na baba yako
mzazi, au Kumu au Man?” “Nimekosa kaka.” “Huo ni unafiki na sitakuruhusu
unidanganye ili kujisafisha dhamira yako. Wewe umechagua aina ya watu wa
kuwapokea kwenye maisha yako. Watu wenye hadhi fulani ndio unawatetemekea
na kuwakubali. Jema amekuwa tatizo kwa kuwa ameletwa na mtu kama mimi
na si Kumu, wala Man au baba yako.” James akaendelea.
“Nimejuta
kujipa nafasi kwako ambayo nilidhani ninayo kumbe sina! Nikamuaminisha
Jema jambo ambalo halipo! Sasa hivi mimi ndiye nalipa garama. Umeyapa mahusiano
yangu na Jema picha ambayo sikuitegemea! Msingi niliokuwa nimejenga naye
mwanzo, inabidi nianze upya kwa kumjenga yeye kama Jema. Kwa kuwa ameshakuona
ukiwa na Naya pamoja na Kumu. Jinsi ulivyo au unavyokuwa ukiwa katikati yao
ukiwatetemekea. Inabidi kuanza upya kumueleza mimi si Kumu na yeye hatakaa
kuja kuwa Naya. Hilo naweza nikafaulu kulijenga kwa upya, ila kigumu ambacho
kinaniuma ni, maneno yakitoka au kutamkwa, huwezi kuyarudisha.
Hakuna jinsi nikamjenga sasa hivi nikikanusha maneno yako uliyomtukania
ila kumjenga juu matusi yako kwake.”
“Mbaya
zaidi, umetonesha donda ambalo nilikuwa nikilitibu kwa muda wote
niliowaomba mnipe ili kuweka msingi. Nilikwambia wewe na mumeo. Tena
nilikwambia wazi kabisa, nivumilie kwakuwa kujenga msingi ni kazi. Jema ametoka
kwa mwanaume aliyekuwa akimpa maneno makali na matusi yanayofanana
kabisa na uliyomwambia jana!” “Pole sana James mwanangu.” James akacheka
akitingisha kichwa.
“Yaani ni
kama shetani alitumia kinywa chako wewe mtoto, kumtesa mpenzi wangu!
Maneno yaleyale aliyokuwa akiambiwa na mimi kumjenga, eti na wewe
unakuja kuyarudia vilevile! Tena kwa kiumbe kama Jema! Hakika Mungu afanye
jambo. Umefuta tumaini zima nililokuwa nimempa Jema, mpaka ananiuliza pengine
yule mnyanyasaji wake hakuwa akikosea, kweli yeye ni tatizo kama ulivyomsema
jana!” “James mwanangu, naomba usamehe tu.” “Nikishatamka nimesamehe,
inamsaidia nini Jema ambaye mmeharibu moyo wake? Au mpo hapa kurudisha amani na
furaha ya Nanaa tu kisha muondoke, niwaonyeshe kila kitu ni sawa?” Akawatizama
wote kwa zamu.
“Halafu
nikishatamka hapa msamaha. Nikawaambia yamekwisha, mnataka iweje kwa Jema?” “Na
yeye tutamuomba msamaha.” Akadakia mama G. “Utamwambia nini? Tafadhali naomba
kusikia. Maana neno samahani tu, halitoshi kufuta ulichomwambia jana. Huku
ukimfoka mbele ya watoto wenu. Na kumwambia eti uliropoka, ulikosea si
kweli. Utakuwa ukimdanganya na sitakuruhusu. Maana mtu huwezi kuropoka
mazungunzo mazima au kukosea kwa kumsema kwa kumuhoji kwa muda mrefu vile.
Utamwambia nini kufuta ubaya wote ule?” James akamuuliza akiwa anamtizama.
“Jamani,
kwa vyovyote mtakavyoniona nipo. Au vyovyote vile ulivyonipima wewe Nanaa,
ukinilinganisha na kina Man, au Joshua, vyovyote vile, lakini Jema amenipokea
kwa upendo mkubwa sana na ananiheshimu. Na kwa vyovyote mlivyomuona Jema. Mkampima
kwa vipimo vyenu mkimlinganisha na kina Naya, Malisa, Grace na wengine wote,
vyovyote vile mnavyomuona, lakini kwangu Jema amebeba sifa zote za kuwa mke
wangu mimi na nimeridhika naye. Na ndio maana wakati wewe ukimfoka, hata mumeo
na mama G hapa walinyamaza kimya, lakini mimi nilishindwa. Siwezi
nikaona anateseka kwa namna yeyote ile, nikanyamaza. Siwezi na
sitaruhusu labda iwe nje ya uwezo wangu.”
“Na ndio
maana hata kwako wewe Nanaa, nilikubali kutoa kafara upendo wa wazazi wangu
kwangu kama mzaliwa wa kwanza na furaha ambayo mama yangu alikuwa akiitafuta
mpaka kunipata ili tu kukulinda wewe. Unajua ni kiasi gani nilijitoa kwako
nikihakikisha upo salama, kwa vile nilivyo wezeshwa na Mungu. Sasa kwa kipimo
hichohicho nitamlinda Jema.” Nanaa akazidi kulia akishindwa hata kumwangalia
mtu.
“Sasa
basi. Kwa kuwa sasahivi Mungu amekuweka kwenye daraja jingine ambalo
mimi binafsi silijui. Maana lile nililokufahamu nalo, ndilo nililomwambia Jema
na kumtambulisha kwako na ndio maana nilimleta kwenu. Huyu Nanaa mpya, mwenye
kufanikiwa sana. Ambaye Mungu amekupa na baba yako mzazi na ndugu zako
wote. Watoto wazuri na jamii unayojitengenezea wewe kwa kuchagua kwako, umeweka
wazi mimi na Jema hatufiti kwenye hiyo jamii yako.”
“Jema
hana familia kama yako. Hana baba. Narudia tena, kwa namna yeyote ile
unayoniona na kunilinganisha na vipimo vyako, mimi ni majibu ya Jema kutoka kwa
Mungu. Nimekusudia kumpa nafasi kama wewe uliyopewa na Geb, kujenga jamii yake
itakayomkubali na kutupokea sisi kama tulivyo. TENA, nataka aijenge
jamii na familia yangu akiwa ametulia kabisa kama wewe nilivyokutoa kwenye
kelele za Moshi, nikakuleta hapa Dar, nikakuwekea mazingira tulivu, nikipambana
mchana na usiku mpaka ukafanikiwa, ndivyo nakusudia kufanya na kwa Jema. Ila
zaidi kwake kwa sababu atakuwa mama wa watoto wangu.”
“Nataka
ajenge akiwa ametulia, bila kujishuku, au mtu wakumshika mikono. Sasa basi.
Tafadhali naomba unisikilize Nanaa, maana katika hili ndio sitakusamehe
kabisa.” Nanaa akazidi kulia. “Na naomba wote mnisikilize ili atakapotulia na
kujaribu kukiuka, mumkumbushe, maana katika hili sitatoa mwanya wa
kukosea tena kama jana. Na Nanaa ananijua, ninapolinda, sina undugu. Nakua
mwaminifu kwa nguvu zangu zote na akili zangu zote. Ninaposhindwa au kupelea ni
ubinadamu tu. Mama yangu atalithibitisha hili kwa vile nilivyokuwa linapofika
swala la Nanaa.” “Hata sisi ni mashahidi James mwanangu, ulifanya kwa kadiri ya
uwezo wako.”
“Nashukuru
kukumbuka mama, tafadhali usisahahu kumkumbusha na Nanaa. Huruhusiwi
kufika nyumbani kwangu.” “James, unazidisha!” Geb akashituka sana. “Unaongea
nini Geb wewe!?” Akamuuliza kwa hasira kabisa. “Si wewe uliniambia wanawake
wanapenda kulindwa na wanataka mwanaume ambaye anamsimamo si myumbaji?
Kwamba James aliyekutana naye leo ndiye huyohuyo akutane naye kesho! Au hukuwa
ukimaanisha?” Kimya.
“Unataka
niwe najenga huku halafu nyinyi mnabomoa!? Mimi namwambia nakukutanisha na
familia yangu. Nanaa ni mtu mwema sana, anaupendo na kila mtu, halafu anakuja
kwenu inakuwa tofauti. Halafu napata kazi yakuanza kurekebisha kwa shida maana
huwezi hata kukanusha aliyokutana nayo kwenu, maana inakuwa kama ulimdanganya.
Ulichosema na ulichokutana nacho ni tofauti! Hujui hata ukisema utetee unatetea
nini maana hata huyo Nanaa niliyedhani namfahamu siye Nanaa huyu aliyekuwa na
baba daktari bingwa ulimwenguni. Mume milionea na mama aina yako
wewe mama G! Nanaa huyu mpya ameketisha na wakuu, si ninayemfahamu mimi!
Unatetea nini kama si kuanza tena upya!?”
“Umebomoa
msingi na picha nzima ya mahusiano yangu na Jema. Ni vile ananipenda, inakua
rahisi kupokea picha hii mpya na kuanza kujenga upya na kumbadilishia kibao.
Kumwambia Mungu anamtaka yeye ndio aanze kujenga kwake sio kulilia kujiingiza
kwenye majumba ya watu yenye misingi yake. Jana umeanzisha jambo jingine jipya kabisa!
Lakini nashukuru Mungu naanzisha na Jema mwenye moyo wa utayari. Sasa siwezi
kuanza kila siku wewe ukiwa katikati yangu ukibomoa. Sitakuruhusu Nanaa. Sijui
kama unanielewa?” Kimya akilia.
“Nitajitahidi
sehemu nitakazojua nyinyi mpo, kumuweka mbali kabisa ili asije kuwa kwanzo
kwenu nyinyi, na wewe fanya juhudi za makusudi kukaa mbali na Jema. Kama kuna
chochote nimeacha kwenu, tupeni. Na chochote ulichoacha kwangu, sitarudisha
kwenu. Kwanza nyinyi mnahela nyingi. Wala hamtapata shida kununua vingine. Kwa
kusema hivi, tafadhali usilete tena chakula kwangu. Iwe kwa kutuma dereva au
wewe mwenyewe kuja. Maana kwangu kutakuwa kwa Jema. Mkifika kwangu mnaweza kukutana
naye na kumvuruga akili bure. Haya, naomba funguo zangu za nyumba.” Nanaa
akazidi kulia.
“Geb,
mkeo anazo funguo zangu za nyumba, tafadhali nisaidie kubania pesa maana nataka
kufunga ndoa ya ndoto za Jema. Sitaki kutumia pesa chache nilizo nazo kubadili
vitasa vya nyumba. Naomba funguo zangu.” Akawa anamwangalia Geb akimaanisha
kama hawatampa funguo zake za nyumba, anakwenda kubadili vitasa. Geb akachukua
pochi ya mkewe akatoa funguo za James na kumkabidhi.
“Hili ni
kwa wote, kwa mara ya kwanza tokea chuoni, nitabadili namba ya simu ili
kuwasaidia nyinyi wote. Msinitafute kwa la kheri wala la shari. Hata mkisikia
nipo hospitalini, tafadhalini msije kushawishika mkaja.” “James mwanangu
umekasirika na unafika mbali.” “Sasa mkifika nilipo mimi si mtakutana na Jema
yuleyule mliyeshindwa kumpokea jana nyumbani kwenu!?” Akamuuliza mama G
akimshangaa.
“Si mimi
jana nilimleta kwenu na mkashindwa kumpokea? Au wewe hukusikia wakati akifokwa
na Nanaa?” Kimya. “Japokuwa jumba lenu ni kubwa, lakini wala Nanaa hakufanya kwa
unafiki. Alipaza sauti yake kwa juu kabisa mpaka mwanae akatoka chumba cha
michezo na kufuata kujua kulikoni. Akawa akimuhoji Jema na nyinyi wote mkiwa
kimya mkimsikiliza anavyomsulubisha Jema kama anayestahili! Sasa mnataka
kumfuata tena ili iweje!?” Kimya.
“Msitufanye
sisi ni wajinga jamani! Pole ya hospitalini si dawa au uzima. Wewe mama ni
muombaji. Ukisikia nipo kwenye shida, tafadhali niombee tu, ila mkae mbali na
mimi pamoja na Jema. Na mimi sitawabugudhi, kwanza hakuna mnachohitaji kwangu
tena. Mimi sina mamilioni ya pesa wala si daktari bingwa. Sina hadhi ya kina
Kumu wala kina Man. Kunifuata popote ni uchokozi na sitaruhusu. Naachana na
nyinyi kwa amani kabisa. Hata Ibrahimu na Lutu japokuwa walikuwa ndugu,
wakatembea kwa muda mrefu pamoja, lakini ilifika sehemu walishindwa kuendelea
kuwa pamoja kwa vile Mungu alivyowajalia kwa vingi. Ilibidi watengane tu. Sisi
si wa kwanza. Mungu ametujalia vingi, naona imeshindikana kuwa pamoja. Kwa hiyo
mimi kama Ibrahimu, nimempa nafasi Nanaa ya kuchagua kwanza. Amewachagua nyinyi
na uzuri wenu wote na watu wenu, acha mimi na Jema wangu tukaanzishe
kwetu.”
“Na
mtanisamehe, mimi si mnafiki. Sitawadanganya. Na siwezi mambo nusunusu. Nanaa
kila la kheri kwenye jamii yako, tafadhali mwache Jema akajijenge kwake.
Sikudai kwa chochote na narudia tena, kama unanidai itabidi usamehe tu
au utamdai Geb kwa chochote unachonidai. Atakulipa. Yeye sina shaka
naye. Najua huwa habadiliki. Geb aliyenisaidia kuniandikia darasani akiwa hana
kitu, ili nije kukuona nyumbani, amekua Geb yuleyule hata alipokuwa milionea aliyenisaidia
kunilipia mahari yako, mama yangu aliyonidai, na kubaki akinitizama mimi
kama James. Haya, kwaherini. Acheni mimi nikawajibike. Mimi sio kama nyinyi.
Nalipwa na mwajiri.” James akasimama.
“Mkimaliza
hapa, mnaweza kutoka. Ila nashauri msichukue muda mrefu zaidi, hiki ni chumba
cha mkutano, kinatumiwa na watu tofautitofauti.” Akatoka na kuwaacha wamekaa
hapo. “Nashauri mama urudi na Nanaa nyumbani akapumzike, mimi niwahi kazini.
Nitajitahidi kuwahi kutoka jioni.” “Twende Nanaa, mwanangu.” Mama G akamshika
mkono kumsaidia kusimama, wakatoka hapo Nanaa akilia kama amefiwa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
‘Tafadhali
naomba namba ya simu na ruhusa ya kuwasiliana na mama.’ Ujumbe
ukaingia kwenye simu ya Jema. Jema akakunja uso na kumpigia. “Upo mzima
mpenzi wangu?” “Nipo.” “Mbona sasa umenyongea?” “Hapana. Nipo na mambo mengi
kidogo.” James akatulia. “James?” “Mimi nilijua ukinisikia ndio ungefurahi!”
“Nimefurahi James. Sema bado nipo kama….” “Unanifanya nikose raha Jema. Kweli
Nanaa ndio anatupa hatima ya mahusiano yetu?” “Hata iweje James, Nanaa ni ndugu
ambaye ulisema ni kama mtoto wako. Siwezi kukwepa ukweli kuwa yupo kwenye
maisha yetu. Imenivuruga James. Nimekaa leo naanza kurudia kote nilikopita na
Temu na jinsi nilivyotenda.”
“Sio jana
tulikubaliana tuyaache hayo?” “Mimi ni binadamu James. Aliyozungumza jana ni
kama malalamishi ya Temu tu. Lazima akili itanirudisha huko.” “Sasa labda iwe
unataka kurudiana na Temu. Ila mimi namtaka Jema huyohuyo wanayemsema.”
“James!” “Sasa wewe unafikiri ni kwa nini wewe na sio wasichana wengine
waliokuwa wakinizunguka miaka yote?” “Mimi sijui James!” “Kwa kuwa hawakuwa na
sifa zako Jema. Au wewe unafikiri ni kwa nini nakutaka wewe?” James
akamuuliza.
Jema
akatulia akijitafakari. Maana kwa ukweli hata yeye alijijua sio kwamba alikuwa
na sifa kama za malaika au umbile la kushitua mtu au kumfanya mwanaume kugeuka
mara mbilimbili. Hakuwa na vya ajabu mwilini mwake. Akajirudi. “Jema?”
“Sijui James!” Hapo akapoa. “Basi ndio ujue. Nilivutiwa na hizo sifa
zinazowashinda wengine. Hizo ndizo zilizonivutia na kunifanya sasa kuanza
kukuangalia vizuri na kugundua uzuri wako.” Jema akaanza kucheka.
“Acha
kunidanganya bwana James!” “Kwamba wewe hujui kuwa una macho ya rangi ya
udongo. Ugoro fulani hivi?” Jema akazidi kucheka. “Rangi yako
wewe huoni kama nzuri?” “Hapo unanidanganya kabisa James. Mimi mweusi.” “Kwa
hiyo? Kwamba ukiwa mweusi ndio nini? Kwanza hiyo rangi yako inafanya mpaka meno
yako yanakuwa meupee! Jema wangu laini, nikikushika tu mimi hali mbaya.” Jema
alicheka sana mpaka akajisahau.
“Mimi
nataka ucheke hivyo sio unalilia sifa za watu ambao sio waume zako. Haya,
naomba ruhusa yakuzungumza na mama Jema.” “Sasa unataka nini?” “Nimuulizie
maswala yangu yakuoa. Naona wewe utanichelewesha. Nimekupa dhamana yakujenga
kwetu, mwenzangu naona upo unalilia waume za watu na…” “Bwana mimi simlilii
Temu.” “Unamlilia sana tu ndio maana nimekupigia tu, ukaanza kumtaja. Mimi nisingekuwa
nakutajia tajia wapenzi zangu wa zamani.” “Basi James, naomba nisamehe. Natoka
huko. Naanza kuwaza yetu.” “Wewe nipe namba ya simu ya mama Jema, bwana.
Utanichelewesha.” “Unataka kuoa mwenyewe!” Jema akamtania. “Tena kwa
haraka! Unanipasha tu joto, nakunitesa bure. Bora nioe ili ukinipasha joto,
namaliza kabisa.” Jema alicheka kwa mshituko na kukata simu. James akacheka akiwa
ametegemea.
Mara
namba ya simu ikaingia, na jina la mama Jema. Akamrudishia ujumbe wa kushukuru.
‘Asante.’
‘Uache matusi James.’ Jema akamrudishia huo ujumbe. James akacheka sana. ‘Hayaitwi
matusi.’ ‘Wala sikuulizi yanaitwa nini.’ James akacheka sana baada
ya kupata huo ujumbe. ‘Kweli hutaki kujua?’ ‘Hakika sitaki.’ Jema akajibu. ‘Ujue
ukibadili mawazo baadaye na kutaka kujua, naweza kugairi.’ ‘Sitakulaumu.’ Jema
alijibu vile nakumfanya James acheke sana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Shilingi imempindukia Nanaa. Ilikuwa kwake, akitetewa, Sasa anaonja
upande wa wengine.
James amekusudia kuoa kwelikweli. Nini Kitaendelea?
0 Comments:
Post a Comment