Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 1 - SEHEMU YA 48. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 1 - SEHEMU YA 48.

Penzi kwa James likakolea. Hakuwa akikimbuka chochote wala yeyote isipokuwa Jema, kazi na biashara zake. Muda wake waziada, wote, alimpa Jema. Kama si kuonana basi Jema yupo kwenye simu, sikioni kwa James, kama Kumu na Naya walivyokuwa wakifanya. Wawili hao wakaiga hivyohivyo. Usingekuta akituma jumbe kwengine popote hata wa salamu kwa yeyote isipokuwa kwa Jema. Akijitahidi sana kama si simu za kikazi na biashara zake ambazo lazima kupokea, wengine wote ujue watarudishiwa ujumbe kuwa, ‘Samahani, nitakupigia baadaye’. Ujue ndio hatarudisha hiyo simu.

Akawa mtu wa kumtia moyo Jema na kujitahidi kuwa kile alichomsikia Jema akitamani. Kile alichokuwa akilalamikia juu ya Temu, ndio akawa James. Akaziba hayo mapengo kwa haraka sana. Akawa mwanaume wa ndoto za Jema. Jema akawa kama mkimbiaji aliye kwenye mchuano na mshangiliaji wa uhakika pembeni yake. Akiheshimiwa akiwa na majukumu ya kazini na James akionyesha akithamini anachokifanya sio kumbughudhi na kumuingilia ratiba zake. Ila alikuwa akimwambia kila akipata mwanya hata wa kunywa maji tu, basi amtumie hata ujumbe amjulishe kama yupo salama au kumpigia simu kwa kifupi tu ili amsikie sauti yake. Naye Jema akawa akifanya hivyo. Wakati mwingine alimpigia James, akipokea tu anamwambia, “Mwenzio bado nakupenda sanaaaaaa.” Na simu kukatwa. Basi James atacheka lakini akifurahia kumsikia.

Ikawa hivyohivyo kwa James. Upweke ukatoweka kwa James aliyekuwa akihangaika mjini peke yake, zaidi usiku ambao Kumu na Geb wapo makwao na wapenzi wao. Akawa na mtu anayemsifia na kujali choka yake, kula na mapumziko yake huku akithamini majukumu yake yote zaidi akili kubwa kwenye biashara zake. Ungejua wote wapo kwenye kujaliwa. Walifanya kazi kwa morari na ujasiri wote wakijua yupo mtu anayethamini wanachokifanya. Ujasiri kwa Jema ukawa mara dufu. Ukimkuta kazini ungepende kumuona. Kujiamini kukarudi, akili ikatulia kazini.

 Wakatengeneza utaratibu wao siku za weekend. Jumamosi chakula cha usiku wanakuwa pamoja hata kwa muda mfupi tu. Watapeana mabusu hapo, kisha kuachana, James kwenda kwenye biashara zake, Jema maandalizi ya juma zima. Ila jumapili wanakwenda kanisani pamoja, chakula cha mchana, baada ya hapo ndio utamsahau James. Kimya na Jema wake wakibembelezana sehemu. Hapo hata umtumie ujumbe, au umpigie simu, ujue hutampata James siku za jumapili.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jema alijawa furaha, Mungu wake amemjibu, lakini ikawa tofauti kwa Nanaa. Akaona huyo mwanamke aliyempata anamfunga kaka yake kiasi chakushindwa kumpa mwanya na ndugu zake! Hana utu wa kumkumbusha hata ndugu zake! Nanaa akazidi kuumia kuona ameporwa kaka. “Hata kama ni mapenzi jamani, ndio anashindwa hata kujulia hali watoto ambao wameshamzoea! Watoto wanamuulizia bila jibu la maana.” Akalalamika Nanaa akiwa na mama G pamoja na Geb. “Yupo kwenye kuweka msingi. Mpe muda mama. Akiweka mambo sawa, atakutafuta tu.” Mama G akajaribu kumtuliza. “Na si ndivyo hata wewe ulivyoniambia alikwambia?” Geb akauliza taratibu asije akamtibua pakalalika vibaya maana alishajua hali ya mkewe si nzuri.

“Sasa ndio toka wakati ule na wewe Geb!? Wewe unajua msingi unajengwa kwa muda gani?” “Hatujui Nanaa, ni wao wanaojua.” “Basi inamaana huyo mwanamke hatakaa akamuachia kaka! Itakua ni kujengwa kwa msingi daima!” Mama G akaanza kucheka. “Wifiii! Ushaanza kulia wivu?” “Sio hivyo mama. Mbona hata Joshua alivyoanzana na Naya hakupotea? Yeye huyo mwanamke wake hajui kama kaka anayo familia inayomtegemea? Hashangai mwenzie hatafuti ndugu, anamkaba tu! Maana kaka hakuwa hivyo. Kaka alikuwa mtu wa familia. Ananijali mimi na watoto niliozaa. Leo kaka anashindwa hata kujulia hali wanangu kweli!” “Nanaa, unajipandisha pressure. Naomba utulie.” Geb akaongea vizuri lakini akabadilikiwa.

“Kwa hiyo unaona mimi nalalamika ujinga?” Geb akatulia akajua mambo yameshambadilikia. “Na usininyamazie.” Akatishwa. “Mimi nataka utulie mpenzi wangu.” “Basi ndio urudi kucheza na mwanangu na usimfunge.” “Nanaa!” “Kama huyawezi ndio mlete sasa kaka James hapa. Maana mimi naongea, unaona si jambo la maana. Sasa si umeona pengo lake halilizibiki?” “Nashauri Magesa ajifunze kucheza na ashinde kwa haki si kuachi..” “Umeona sasa nilichokuwa nikizingumza?” Nanaa akauliza kwa ukali.

“Wewe tulia. Kesho huyu atacheza naye, na atatulia afungwe.” “Mama! Hivyo si sawa!” “Basi kamlete hapa kaka. Maana ndiye mtu anayeweza kucheza na watoto.” Nanaa akaendelea kwa jazba. “Kwa hiyo mimi ndio nimekuwa siwezi kucheza na watoto?” “Ndiyo.” Geb akacheka akitingisha kichwa. “Wewe Nanaa, naomba tulia bwana. Huyu kesho atacheza naye na atafungwa.” Mama G akaweka msisitizo. “Sasa sio niwe kazini nipate simu za vilio!” Akamtisha mumewe. “Mimi si nimekwambia kesho mumeo atafungwa?” Mama G naye akamjia juu. Nanaa akatulia. “Nimekwambia atafungwa, tulia.” Nanaa akanyanyuka hapo kwa hasira na kuondoka.

“Huu usiku ushaniharibikia!” Geb akalalamika, mama yake akaanza kucheka. “Sasa mimi kosa langu ni kutaka haki jamani!?” “Wala si wewe. Huyo wifi kashachukiwa, ndio na wewe umeingia humohumo.” “Sasa kwa nini asimkasirikie kaka yake anatukasirikia sisi!?” “Hathubutu. Anavyomwamini, na kumpenda James! Ni mkamilifu kama Mungu, ila watu ndio mnamsababishia.” Geb akatingisha kichwa kwa masikitiko.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Kuliko kufungwa na mwanae, Geb akawafikiria hao wanawake wawili hapo ndani, akaona awazidi mahesabu. Akafikiria jinsi ya kufanya. Asiache kutomtii mama yake, na kumzidi mkewe zaidi mpaka yeye ashinde. Akapata jibu. Isivyo kawaida yake, siku hiyo ya jumamosi ambayo huwa hafanyi kazi, asubuhi na mapema akaondoka hapo nyumbani mapema sana. Usiku alinyimwa na asubuhi kavukavu. Njiani akajaribu kumpigia James bila mafanikio. Akaamua amuache. Akaenda kujificha kwenye kazi, sehemu nyingine kabisa ambayo mkewe hafiki huko. Kwenye magala yake. Kimya.

Nanaa anataka kutoka kwenda kazini asubuhi ya saa mbili na nusu, mama G anamwambia Geb alishatoka, ila amesema hatachelewa kurudi. “Amekula?” Mama G hakujibu akabaki akimtizama. Nanaa akapata jibu, akaamua kumpigia. Akapokea. “Kwema?” Geb akamuuliza. “Sasa mbona umeondoka bila kula?” Nanaa akauliza. “Sikutaka.” Geb akamjibu na kubaki kimya. Akajua anamfanyia kusudi.

“Naweza kukuletea chakula huko uliko.” Nanaa akajirudi kidogo. “Sidhani kama kuna umuhimu. Acha nimtafute James ambaye ndiye naona ni wa muhimu hapo ndani. Nikifanikiwa kumpata, basi nije naye, pengine na mimi nitaonekana wa thamani.” “Sasa nani amekwambia wewe si wa thamani?” “Wewe. Na naomba kukuaga Nanaa nipo na kazi. Uwe na siku njema.” “Sawa.” Nanaa akakata simu kwa hasira.

Penzi Njatanjata.

Baada ya mawasiliano ya takribani majuma mawili mfululizo ya bila kuonana sababu ya ubusy wa James, jumamosi hiyo Jema na James walipanga walazimishie muda wao. Wakapanga wakitoka kazini, waelekee bichi ya Kigamboni, iwe kama pikiniki yao. James akawa busy kumaliza siku ya kazi na biashara ili Jema akitoka, asiwe na chakumchelewesha, kwa hiyo tokea alipozungumza na mpenzi wake akiwa kitandani asubuhi hiyo, simu ya mawasiliano ya kawaida, ikawekwa pembeni, ikabaki kufanya kazi simu ya kazini na biashara. Wapenzi hao akili ikawekwa kazini tu, basi. Jema naye akafanya majukumu yake kwa makini ili kumridhisha Kumu, bosi wake, atoke mapema. Kumu alipotoka tu mida ya saa tano na nusu akiwahi nyumbani, Jema akajua kila kitu kipo sawa, na yeye yupo huru. Akatoka bila kuchelewa kuwahi kwake kwa matayarisho ya siku hiyo na James.

Majira ya saa saba wakawa wapo kwenye gari ya James wakielekea Kigamboni wote wapo tayari kwa mapumziko. “Ulifanikiwa kumaliza mambo yote?” Jema akauliza akijali. “Nimejaribu. Nimeona nisikuchelewe, mengine nitamalizia usiku. Sikutaka kukuchelewa.” “Ningesubiri tu James!” “Nilivyokuwa na hamu ya kukuweka mikononi! Mimi mwenyewe nilikuwa nataka kukuwahi.” “Hata mimi nimekua na hamu na wewe James!” “Sasa huofii utaolewa na mwanaume ambaye yupo busy sana.” “Ikiwa ni wewe, sitakuwa na shida, ilimradi mwisho wa siku unarudi kwangu, sina wasiwasi.” James akacheka. “Basi wewe utanifaa. Wakatulia mpaka Kigamboni.

Wakafika kwenye hiyo hoteli, wakaagiza chakula na kuhamia kwenda kula ukingoni mwa bahari. Nia wawe wao wawili tu bila kelele na macho ya watu kwao. Walipojikuta peke yao, chakula kikawekwa pembeni, yakaanza mabusu. “Nivumilie mpenzi wangu na endelea kuniombea. Biashara zikikaa sawa, tutakuwa tukipata muda mwingi na sitaacha kuongozana na wewe kanisani. Haya majuma mawili yalikuwa na mambo mengi.” “Endelea kunishika hivyohivyo. Usiniachie.” James akacheka na kurudi kumvutia kwake karibu. Jema alikuwa amekaa juu ya kibambaza kama cha ukuta kilichotenganisha bahari na eneo la juu ya hiyo hoteli, James akasimama katikati ya mapaja yake, kiss zikaendelea kwa muda mrefu tu wakiwa wamekumbatiana kwa nguvu na kuvutana kama wasije wakaachiana wakaanguka gorofani.

Jema akashitukia James anarudi nyuma kwa haraka na kumuachia. “Naomba tule, Jema.” Jema kumtizama, Mzee amesimama kama atoboe jinsi. Akacheka na kuvuta sahani yake. “Nitarudi muda si mrefu.” Jema akahisi anatoka pale ili atulie. Akamuacha. Baada ya muda akarudi akionekana ameosha mpaka na uso.

“Ni lini unakwenda kunitambulisha kwa mama?” James akamuuliza akikaa. “Nipe muda James.” James akashangaa sana. “Ni kwa nini tena!?” Jema akamuonyesha ujumbe wakutoka kwa mama yake aliomtumia usiku uliopita. ‘Nimekwama Jema mwanangu. Nisaidie pesa kidogo.’  James akasoma. “Sasa kwa mama ujue sio kwamba ananiomba mimi pesa kama msaada, ni anakumbushia deni lake. Anataka hata nimpunguzie kidogo. Sasa Kumu ana safari ya Afrika Kusini, amekuwa akiisogeza mbele, nahisi ni mambo ya kifamilia. Akiwa tayari tu, nikilipwa, napunguza deni, hapo nitakuwa na ujasiri wa kukupeleka.”

“Kwa hiyo msiposafiri na Kumu, mimi nijue ndio sipelekwi kwenu!?” Jema alicheka sana. “Wewe umefikiria mbali sana. Sasa nashauri tuombe.” “Hakika siombi usafiri, ila sasahivi nataka unipeleke kwa mama yako.” Jema akazidi kucheka. “Kweli Jema. Mimi nataka kukuoa bwana. Nahisi kama unanichelewesha!” “Mimi mwenyewe nataka kuolewa na wewe, James. Vuta subira, nitengeneze makosa yangu.” James akaanza kula, bila kujibu.

“Au basi acha nimkope Fina. Yeye huwa haishiwagi. Nitamtumia ujumbe leo usiku, akinitumia pesa, namlipa mama, jumapili ijayo nakupeleka kwa mama Jema. Usikasirike mpenzi wangu. Kwani ndoa ulitaka iwe lini bwana harusi wangu?” “Acha mzaha Jema.” Jema akazidi kucheka. “Hali mbaya.” James akalalamika. “Basi acha niweke utaratibu jumapili tukamuone mama Jema. Mimi mwenyewe nakutaka James. Wala sijivungi kwako.” Hapo kidogo akamuona ametulia. “Tuone, tupumzike. Si umesema leo upo tayari kwenda kupaona nyumbani?” “Mwenzio nilijua umegairi!” “Hapana. Kwanza hakuna chakula, nilijua wote tungetaka kula. Halafu nilitaka kukutoa kwanza upumzike sehemu nzuri kama hii, ndio twende nyumbani. Siwezi kusahau. Mwenzio nishajua wewe ni mke wangu, sina ninaloficha kwako.” “Nashukuru James.”

“Na deni la mama acha mimi nililipe.” “Hapana James. Hatutajenga wote huko kwa Temu.” “Ulitaka ujenge na nani?” “Ni ujinga wangu mimi mwenyewe, acha tu nilipe deni ya ujinga wangu.” “Usijali.” James aliongea tu hivyo na kunyamaza akiendelea kula. Jema naye akaona anyamaze.

Aluta Kontinua.

Huku kwa Nanaa akarudi nyumbani mida ya saa 8, mumewe hajarudi. Akamkuta mama G ametulia na wajukuu zake sebuleni pamoja na msichana wao wa kazi, kila mtu anafanya lake hapo sebuleni zaidi macho kwenye luninga. “Yaani Geb hajarudi tu mpaka sasahivi!?” “Kwani nyinyi hamuwasiliani?” Mama G akamuuliza kama kumsuta. “Basi atakuwa amenikasirikia. Sasa anakasirika nini wakati mimi nili…” Akatoa simu ili ampigie, mama G kimya. “Wewe umekasirikiwa na dad?” Magesa akamuuliza mama yake. Mama G akamtizama tena Nanaa. “Mimi sijui!” “Umefanya nini mami?” Magesa akaendelea kumuhoji mama yake kwa upendo tu, mama G akabaki akimtizama kama anayemwambia ‘jibu sasa’. Akababaika bila kujua ajibu nini ndipo akafanya na wengine wote mpaka hao wanae wakimya, kumtizama.

Wote macho kwake. “Mimi sijafanya kitu. Itakuwa ni majukumu tu.” Akajirudi taratibu kama anayekwepa lawama. “Majukumu hayo ya jumamosi! Yameanza lini?” Mama G akamuuliza kwa kumsuta. “Sasa mama wewe unafikirije?” “Mie huyu!?” Mama G akamuuliza kwa kumshangaa. “Maana mimi nadhani ni majukumu tu.” “Ndio maana na chakula hajala?” Mama G akaendelea kumkaba kwa maswali ya kumsuta. “Dad hajala chakula?” Magesa akamuuliza tena mama yake, Nanaa akaona aondoke akampigie simu huko chumbani kwao.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Akampigia, Geb naye akapokea. “Mbona hurudi nyumbani?” “Kuna anayenihitaji huko?” Geb akamuuliza taratibu tu. “Si sisi!” “Sisi ndio kina nani? Maana ubaba umenishinda. Anayeweza majukumu yangu ya ubaba vizuri na kusifiwa, tena anayehitajika hapo ni James. Na kulithibitisha hilo hata majukumu yangu ya umume naona pia umeamua kunipokonya ramsi.” Geb akatumia akili kumzidi mahesabu makusudi tu. Gafla yeye ndio akanunua ugomvi na kuukuza. “Nilikuwa nimechoka, ila sasahivi nipo fiti. Njoo tuoge mpenzi wangu, halafu ule.” Geb kimya.

“Sasa umezira nini Geb?” “Mimi sitaki kuoga.” Nanaa akaanza kucheka, alimjua Geb. “Vyote unavyotaka nitakupa.” “Sasa sio nije hapo, uanze shuguli nyingi wewe na wanao, halafu mimi niwekwe pembeni.” “Tutawatoka kiakili. Safari hii mimi ndio natangulia chumbani, halafu wewe ndio ufuate.” “Kama ndio hivyo sawa. Maana nikitangulia mimi naishia kukusubiria chumbani, halafu huji.” “Sawa. Na leo nakupa ya kweli mpaka uchoke wewe.” “Kama ndio hivyo nafunga ofisi sasahivi nakuja. Ila si ni mpaka nije na James ili anisaidie majukumu yangu ya ubaba?” “Geb naye!?” Nanaa akajibaraguza.

“Maana naona unapenda vile alivyokulea wewe, ndio alee na wanangu pia. Acha tu nisubirie hapahapa kama atarudisha simu yangu, nimlete.” “Asiporudisha sasa?” “Nitahamia hotelini nikisubiria.” “Acha hizo Geb!” “Nakaaje na watoto ambao siwezi kuwalea? Njia alizonifundisha baba yangu mimi, nakutaka na Magesa apitie, naona wewe umezikataa. Mimi nakua sina haki ya kulea watoto wangu mwenyewe ambao Mungu amenipa kuwa warithi wetu wa wakina MAGESA, ila James.” Akazidi kumuwekea ngumu.

“Basi kuanzia sasahivi sikuingilii tena. Fanya vile unavyotaka na wanao. Mimi nitamfundisha mwanangu kucheza mpaka siku moja aje akufunge kihalali.” “Na hayo uyakumbuke Nanaa. Mimi mambo ya vigeugeu siwezi.” “Wewe rudi nyumbani, utanikuta chumbani na lingerie. Tena rangi yako unayopenda. Unashika utakavyo. Ziwa mdomoni mwanzo mwisho. Staili zako tupu leo.” “Hapa jamaa ameshasimama.” “Ndio uwahi sasa. Achana na mambo ya kaka.” “Nakuja kwa kasi.” Nanaa akatoka kwa shangwe.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Wala mume wangu hajakasirika. Anakuja.” Akajiongelesha kwa sauti akishuka ngazi. “Kuna aliloahidiwa ndio maana anarudi.” Mama G alimfanya Nanaa acheke mpaka akakimbilia jikoni. “Ulikoroge mwenyewe, halafu utake tulinywe nyumba nzima!” “Wala sio mimi.” Akakana akicheka.

James & Jema

Walitoka huko ufukweni mpaka nyumbani kwa James. “MmmH! Umejijenga James! Sasa hapa unaishi na nani?” “Peke yangu.” “Familia yako? Nikimaanisha, wazazi na ndugu mbali ya Nanaa.” Akamuona kama anayefikiria. Anajishauri aongee nini juu ya wazi wake, mwishoe akajibu. “Mama yangu mzazi na wadogo zangu hao wawili wanaishi hapa Dar, lakini hatupo kwenye mahusiano mazuri. Baba yupo, anaishi Moshi.” Jema akatamani kuuliza lakini hakujua aulize vipi, akaona anyamaze. “Njoo uangalie na vyumbani. Kwengine hakuna hata vitanda. Nimehamia si muda mrefu sana. Niliijenga taratibu sana tokea nipo chuo, nafikiri.” “Hongera sana James.” Wakaanza kuzunguka.

“Nikuombe kitu Jema?” “Nini?” “Kina Magesa wamekuwa wakinitaka sana niende kwao. Pale ni kama nyumbani. Tafadhali kesho baada ya ibada naomba tuongozane wote.” “James! Si umealikwa wewe?!” “Ile ni familia ambayo natamani mje kuwa nao karibu. Nanaa na mama G ni watu wazuri sana. Amepungua Grace tu pacha mwenzie Geb, tulisoma wote, yeye amehamia Arusha. Ameolewa huko. Naye ni mtu natamani uwe naye karibu. Na usiogope. Kwa kina Magesa milango huwa ni wazi wakati wote. Unakumbuka nilikwambia hata Kumu nilimtambulisha kwao?” “Nakumbua.” Jema akakubali.

“Basi na Naya naye amekuwa kama mmoja wa familia yao. Ni watu wanaopenda sana watu. Utawapenda tu.” James akauza sera mpaka Jema akahamasika kwelikweli na shauku ya kuwe kesho ikaongezeka. Wakahamia kwenye kochi. Mabusu tena yakaanza. Jema akajisogeza karibu mpaka James akapata joto lake la mwili. Ile hali ya kuguswa na matiti ya Jema, ikamfanya James ajilaze zaidi kwake mpaka wakajikuta wamelala kochini. James juu ya Jema hapo kochini mikono ikiendelea kumkamata kwa nguvu. Wakaanza kung’ang’aniana, hali mbaya.

James katikati ya mapaja ya Jema aliyekuwa amevaa kigauni tu. Ilikuwa ni kiasi cha kukinyanyua tu, na kuingia maana Jema alisikika yupo tayari kabisa. Kama kitu kikapita akilini kwa James akasimama kwa haraka. “Samahani Jema. Samahani sana.” “Usiondoke James jamani!” “Hapana. Utakuja kunichukia maisha yako yote. Hapana Jema.” Jema akaumia sana na kukaa akiwa anajirudishia nguo yake vizuri, kisha akainama.

“Tafadhali usinikasirikie Jema. Umejitunza maisha yako yote, ukitaka mumeo ndio awe mtu wa kwanza. Umeepuka majaribu yote mpaka leo. Hii hali unayojisikia sasahivi, itaisha baada ya muda mfupi sana wa kutimiza hiyo tamaa. Hutajisamehe na utanichukia sana baada ya kufanya mapenzi hapa na mimi. Utajilaumu kuona umeshindwa kumaliza mwendo. Niamini utajichukia Jema. Tafadhali tuvumilie ili kujitunza kwetu kusiwe bure. Tumekula ng’ombe mzima, tumebakisha mkia. Wewe utakuwa mke wangu, sitaki kuweka kumbukumbu mbaya kwako ila nzuri. Huu ni msingi wetu mimi na wewe, tusiweke msingi dhaifu utakao kuja kutuvunjia nyumba yetu baadaye. Naomba kubaliana na mimi.” Jema akasimama na kuvuta pumzi kwa nguvu akijiweka sawa.

“Usikasirike Jema.” “Nimejichukia James!” “Sasa baada ya kufanya mapenzi leo, ndio ungejichukia zaidi. Samahani nakiri nimevuka mipaka. Matiti yako yamenisisimua kupita kiasi. Na najua ni kwa sababu sijawahi kumshika mwanamke hivyo. Tafadhali nisamehe.” “Ila nakushukuru James. Na nimeamini wewe ni mwanaume aisee. Asante.” James akaelekea kwenye choo cha hapo karibu na sebuleni. “Chukua chochote kitakachokufaa huko kwenye friji. Nitatoka sasahivi, acha nijiweke sawa.”

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jema akamtumia ujumbe mama yake. Akashangaa anapiga. “Jema, mama?” “Mbona hujalala mpaka sasahivi!?” “Sasahivi saa mbili Jema mama. Mbona umenitupa? Au ni ile hela?” “Hapana mama. Yule mwanaume alinitapeli, nikawa nakuonea aibu.” “Pole. Na nyumba?” Jema akaumia sana lile swali maana mama yake alilirusha mapema sana kabla hata yakwenda mbali ya mazungumzo. “Amenitapeli mama yangu.” “Usilie sasa. Pole.” Jema akajaribu kutulia. “Ila nimepata mwanaume mwingine. Huyu atanioa mama. Si tapeli.” “Ulivyokazana na hao wanaume! Hujakata tamaa tu! Mjini hakuna waoaji, Jema mwanangu.” “Huyu ananipenda kiukweli mama. Si tapeli.” James akawa anamsikiliza akiwa chooni.

“Mlete basi.” “Lini?” Akajifuta machozi na kuuliza. “Hata leo. Mimi nipo tu nyumbani. Nilikuwa sijisikii vizuri, leo nimeshinda tu nyumbani.” “Pole mama. Nini tena?” “Vijihoma tu. Mlete basi nimuone.” “Nimemwambia mpaka week ijayo. Halafu sio wale wanaume wakuyumbishwa mama. Sitaki anione sina msimamo, nabadilika badilika tu. Acha nije naye jumamosi, ila mimi nakuja leo kukuona. Nikuletee nini?” “Chochote nitashukuru.” “Umekula sasa?” “Tushakula.” “Basi nitakuja muda si mrefu. Napitia kuku wa kuchoma, nikuletee.” “Usisahau basi na ndizi.” Jema akacheka. “Na fanta ya kaka.” “Sawa mama. Acha basi nimuage. Nitoke.” “Kwani upo kwake?” “Leo ndio amenileta kupaona.” “Kumbe mpo serious!?” Mama yake akashangaa ila kwa furaha.

“Mungu amenifuta machozi mama yangu. Naona amenipa haja ya moyo wangu. Huyu anaeleweka. Na wala haniombi hela.” Wakacheka. “Ananijali sana. Ananitumia zawadi kila siku kazini. Maua, matunda na chokleti.” “Unastahili Jema mwanangu. Wewe sio kama sisi. Umetulia mama. Unastahili mwanaume anayekujali.” “Nashukuru mama yangu kama na wewe umeona hivyo.” “Mbona najua! Ndio maana ulipomleta yule muhuni hapa, nilishindwa kujizuia.” Wakaanza kucheka tena. “Basi kwa huyu naomba uwe na stara mama jamani!” “Nikimuona ni wa kusitiri nitamsitiri. Kama ni tapeli…” “Usimwambie. Mwache tu.” Wakacheka. Jema alikuwa akiongea sauti ya chini asisikike. Hata cheka yake ikawa ya sauti ya chini tu. Akakata na kutulia akimsubiria mwenyeji wake.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

James akatoka. “Naomba nikuage, nikamuone mama.” “Kwema?” “Naona anadeka tu, maana sijamuona muda. Acha nikamnunulie kuku wa kuchoma. Anataka na ndizi pamoja na soda ya mjukuu wake.” “Na mdogo wako?” “Jumamosi hii, mida hii, huwezi kukumkuta nyumbani hata iweje.” “Jema! Sasa anakuwa anakwenda wapi?” “Sijui James. Mimi huwa naangalia yangu, basi. Hutamuweza kwa hoja, wala ushauri. Acha niende.” “Itakua vibaya nikikusindikiza?” Jema hakuamini.

“Usiku huu! Si uliniambia una…” “Twende, usijali. Acha nikakutane na mzaa chema wangu. Pengine mimi nitapendwa.” Jema akaanza kucheka. “Au unafikiri hatanipenda?” “Ndio twende tukajionee. Ila ujue nimefurahi sana.” “Basi tulipe kwanza deni. Tukienda huko hatudaiwi.” Hapohapo akamtumia Jema hiyo pesa yote, Jema naye akamlipa mama yake yote asiamini. “Naomba hata kukubusu shavuni James. Umenitua mzigo ambao sikuwa nikijua chakufanya.” James mwenyewe akamsogolea. Akamshika vizuri kiunoni, akampa busu la mdomo kwa kutulia tu.

“Nakupenda Jema. Na wewe ni wangu, sipo kukuchezea. Mungu akijalia, utakuwa mama watoto wangu. Nimeona makosa yanayotendeka kwenye ndoa, na naona waliokusudia kutokosea jinsi wanavyofanya. Nataka mwanamke atakayelea watoto wangu awe kama wewe muombaji. Anayemjua Mungu na kutambua nafasi yake. Ninapoweza kusaidia, nakusudia kufanya kwa uwezo wangu wote ili wewe utulie. Sitaki kuzembea. Na usiogope kuomba.” “Kabla sijaomba naona unatimiza James. Nakushukuru.” “Basi pale ambapo unaona natakiwa kufanya, na nimejisahau, niambie tu, usisite.” “Na wewe iwe hivyohivyo.” Wakasindikiza hayo makubaliano kwa mabusu lakini si kwa kushikana kwa kung’ang’aniana tena. Kiasi tu tena kama James akikwepa joto lake la mwili. Asijijaribu. Wakatoka.

Mama Jema.

Mama Jema alifurahi kumuona James, mpaka wakamuona jinsi anavyobabaika. “Sasa sijui niwapikie nini!? Sitaki muondoke bila kula kitu.” “Mama! Kaa bwana chini uzungumze na sisi! Tutaondoka hapa muda si mrefu.” “Hata hivyo tumeshakula mama. Usihangaike. Tumekuja kukuona tu.” “Kweli?” “Kabisa mama. Usihangaike. Wote tumeshiba mpaka tumeacha chakula. Nyinyi kuleni tu hicho tulichowaletea.” “Kama ndio hivyo afadhali.” Akakaa.

“Kwa hiyo wewe James umetokea wapi?” James akajieleza kwa kifupi ila kifasaha. “Oooh! Kwa hiyo mama yupo hapahapa mjini?” “Ndiyo.” “Mnaishi naye?” “Hapana. Anaishi na wadogo zangu hao wakike wawili.” “Hapo nimeelewa kabisa. Karibu sana.” “Nataka kumuoa Jema, mama.” Jema akashangaa sana. “Acha nichangamke Jema. Bahati haziji mara mbili.” Wakacheka. “Ulitaka iwe lini?” “Hata kesho.” Mama Jema akaonekana kufurahi zaidi!

“Si utatuma washenga? Au unataka iweje?” “Kabisa. Nikipata baraka zako, na siku, watakuja.” “Acha na mimi nikaulizie. Huku kwetu hakuna mambo ya harusi. Ila najua bibi yake huyu atataka kuwepo. Anampenda sana Jema. Wajina wake.” “Yeye yuko wapi?” “Migombani. Maisha ya mjini hayataki kabisa. Ila ukimwambia Jema anaolewa, hiyo sababu itamtoa migombani lakini si vinginevyo.” Wakacheka.

Mara akaingia mdogo wake Jema.  Jelini. Tofauti kabisa na Jema. Mzuri sana, umbo la kipekee kabisa na watu wa nyumbani kwao. Umbile lakumfanya yeyote umtizame mara mbilimbili ili kuona vile alivyoumbwa kwa ustadi wa namna yake. Si mwembaba. Alikuwa na mwili, mrefu hata kwa Jema. Kwa hakika alikuwa mzuri haswa. Hafanani hata na mama yao. Na yeye ana rangi nyeupe lakini si sana kama kina James , ila rangi nzuri hata kuitizama kwenye huo mwili wake. Msafi na amevaa vizuri.

“Mambo!” “Safi tu. Hujambo?” James akaitika na swali la salamu. “Mimi nipo poa.” Akajibu hivyo na kumgeukia Jema. “Sasa unaniangalia nini na wewe Jema? Mjini hakuna maswala ya shikamoo.” “Mimi sijasema kitu.” “Kwani mimi sikujui wewe? Na mimi umeniletea chakula?” “Una mambo mengi wewe! Hata hujatulia na kuniulizia hali yangu, unadai chakula.” “Nikimsikia mama yupo kimya najua wewe mzima. Maana tatizo la Jema ni la familia nzima!” “Maneno mengii! Kuku umebakishiwa.” Akaanza kucheka.

“Sasa huyu mgeni naye anaitwa nani?” “Ungetulia, ungetambulishwa.” “Jema mkoloni! Mambo yake ya mipangooo! Mpaka utambulisho! Mlokole mwenzio nini?” “Anaitwa James, mchumba wangu.” Akaanza kucheka. Akacheka na kucheka tena. “Sasa unacheka nini?” “Mama, umekazana! Si umeambiwa wewe wanaume wa kuoa mjini hawapo. Sasa lile janaume ulilolileta hapa liliishia wapi?” “Nenda kale muache mwenzio.” “Acha niongee na dada yangu bwana! Maana Jema kwa ndoa! Sasa yule imeshindikana, umeleta mwingine wa kizungu!”

“Nampenda Jema. Na mimi nitamuoa. Sitamtapeli.” Hapo mdogo mtu akaguswa na kumgeukia vizuri James. “Makubwa! Huna mdogo wako wakizungu na mimi akanioa?” “Mama, naomba zungumza na Jelini, tafadhali.” “Sasa mimi kosa langu lipi!? Si na mimi nataka kuolewa!” “Ndoa yataka utulivu.” “Kwani mimi ndio nimesema sitatulia? Sijapata wakunituliza, ndio namsaka. Sasa mnataka nitulie aje anifuate humu ndani!? Nyinyi watu vipi?” “Huyawezi wewe.” Mama yake akapinga. “Ni kwa kuwa sijapata mwanaume wakutulia. Ningempata ningetulia tu.” Akamgeukia James tena.

“Sasa shem? Huna mdogo wako mwingine? Na mimi pia nataka mzungu, napenda sana wanaume weupe, ili tukichanganya, tunazaa wazungu wa hapahapa Bongo. Halafu sasa, nikiolewa kwenu, ndio undugu unakua..” “Twende mwaya James.” Jema akasimama. “Sasa Jema unakasirika nini?!” “James ana mambo mengine ya kufanya. Na hana mdogo wa kiume. Kwao mtoto wa kiume ni yeye peke yake. Halafu sio mzungu. James ni mchaga.” “Acha masihara Jema! Kwamba hajachanganyia hata kidogo! Maana na sisi mama yetu mchaga, ila baba zetu ndio majanga.” Akaanza kucheka yeye mwenywe. “Hakuna mwenye baba humu ndani. Ila mchaga huyu na wenzie tunaowafahamu  sisi, wote weusi kama Jema. Nitafutie basi mchumba shem. Hata mimi nimeokoka kama Jema.” James akacheka na kusimama.

“Mimi nipo serious. Huna hata rafiki ambaye hajaoa?” “Rafiki zangu na watu wangu wote wakaribu wameoa.” “Waw! Kasoro wewe tu?” “Mimi tu ndiye niliyekuwa nimebakia.” “Kwa nini sasa?” “Kwa sababu nilikuwa nikimsubiria Jema.” Ikamgusa mpaka Jema. “Ni wakati ule Jema alipokuwa na yule tapeli wake? Maana mama alimfukuza hapa mchana kweupe. Alimwambia hivi usoni, wewe tapeli. Na kumbe kweli tapeli. Lakini wewe unaonekana una hela halafu umetulia. Sijakuona kwenye viwanja vyangu!” “Hivi wewe Jelini kichwa chako kinafanyaga kazi kweli wewe!” James akacheka tu. “Kwani hapa nimeongea baya gani jamani au kunitafutia tu sababu ili leo nisikuombe hela?” Jema akachukua pochi yake.

“Acha sisi tuwaache mpumzike mama. Jema atakaponipa tarehe, basi nitatuma watu, ili tukamilishe hili kwa haraka.” Mama Jema na yeye akasimama. “Nitajitahidi kukusanya taarifa kwa haraka. Nashukuru kwa kunilipa deni langu.” “Mama wewe! Sasa unajuaje kama ni yeye wala si mimi!?” James akacheka. “Mimi na wewe tunajuana hali zetu, Jema mwanangu. Ukope hata mwaka haujaisha, utapeliwe na bado uwe na pesa ya kulipa deni lote! Uwezo huo uupate wapi?” “Hakika siamini!” “Si ubishe tu useme si yeye aliyenilipa.” Jema akaanza kucheka.

“Huyu mwanaume anaonekana ana hela. Nipeni basi na mimi kidogo nianze biashara.” “Twende mwaya James.” Jema akamvuta mkono James ili watoke. “Nikikaa tu hivihivi, mnanisema. Nikitaka kufanya biashara pia hamniungi mkono! Sasa mnataka nifanye nini?” Akalalamika. Jema akarudi akiwa amemuacha James mlangoni. “Ni mara ngapi nimekupa pesa ya mtaji?” “Sasa tokea miaka ile!? Jema naye?” “Hata miezi sita haijaisha.” Mama yao akadakia. “Asante mama. Ukipewa pesa unanywea pombe na kuvaa.” “Sasa hivi nimeacha.” “Hapa niliposimama tu, nasikia harufu ya bia.” “Nimekunywa moja tu, tena nimepewa hapo baa.” “Si kwakuwa huna hela!  Ungekua na hela, leo ungekesha baa mpaka uimalize. Na kama ulivyosema, nilitapeliwa. Kwa hiyo sina hela.” “Sasa kwani nakuomba wewe? Si namuomba shemeji yangu?” Akaongea bila aibu. “Shemeji yako katoka kumlipa mama yako mzazi pesa niliyokopa.” “Unamzuia tu. Kwani wewe unajua salio lake? Unajuaje kama anayo pesa ingine je?”

“Twende James.” “Usiku mwema jamani.” “Asante baba. Nashukuru. Na nyinyi pia.” Wakawa wanatoka. “Jema anajishaua tu. Mwanaume wake anazo pesa sana! Kwani sijaona gari yake hapo nje! Anazibania pesa kama zake!” Wakamsikia akilalamika ndani. “Na umbakishie mama chakula, Jelini. Nimemletea yeye.” “Sili chote jamani! Sijui mimi mnanionaje humu ndani! Na nitaondoka.” Akamjibu kwa sauti. “Bora.” Jema naye akamjibu kwa sauti. “Au labda kweli amebadilika.” James akamuuliza Jema wakiwa wanaelekea kwenye gari wasijue mama Jema yupo nyuma yao.

“Hana lolote. Wewe wala asikusumbue kichwa. Huyo sisi tunamjua. Hivi ndio amerudi jana. Aliondoka hapa siku tatu, sijui alipo, sijui kama yupo hai au kafa. Kaniweka roho juu juu, amerudi jana. Nikisema jana, namaanisha jana. Na hivi tokea ameondoka saa kumi jioni, ndio anarudi sasahivi, na sijui kama ni mlalaji. Hajui mtoto wake anakula nini wala anasoma wapi. Ukimpa pesa huyo, ujue umekwenda kunywesha wanaume wenzio usiowajua huko baa. Jitunzie pesa yako, James mwanangu. Angalia yako, huyo ni wangu na Jema. Tunavutana naye hivyohivyo siku zinasogea.” Mama Jema akamueleza bila kumficha.

“Labda shule.” “Huna darasa la kumuweka huyo ukamfundisha kitu, kichwa chake kikaelewa. Amejawa wanaume na starehe tupu. Nimemfunga kizazi ili ashie na huyu mmoja.” “Mama jamani!” “Bora umwambie mwenzio aelewe unakotoka. Huyu mtoto ni janga, huna utakaloweza kumsaidia. Acha dunia imfunze. Kila siku namwambia wenzie wanafanya umalaya, na akili kichwani. Yeye hana akili ya kesho. Kazi yake matumizi. Anaiga ya tembo, atayaweza wapi? Mimi nimejenga hapa kwangu. Hata kama pabaya, lakini sidaiwi na mtu. Sasa yeye ukimwambia anakwambia mbona hata wewe hukuolewa, na una watoto wawili!” James akashangaa sana, ila akakumbuka ya dada zake na mama yake.

“Mama wewe jamani! Acha kumwambia James mambo mazito hivyo!” “Kwahiyo wewe ulimwambia James niliolewa ndio baba yako akafa au?” “Mambo mengine ni ya ndani sana bwana mama! Utamkimbiza.” “Huyu muoji tu na wewe, acha kupaniki.” “Ndio atachoka hata kabla hajanioa!” “Mimi si nilikwambia nawajua wanaume wa mjini? Huyu si mkimbiaji. Mwanaume wa familia. Kwa hiyo James mwanangu, huyo hana msaada. Kazi yake kujitengeneza, na kutoka. Akirudi amelewa kama hivyo, hata mfuko wa chips yai mkononi hakumbuki.” James akabaki hajui aseme nini.

“Wewe mwenyewe ukikaa vibaya atakutongoza.” James alishituka sana. “Hilo mama hakutanii.” Jema akaweka msisitizo. “Sasa wewe mchekee kama hajakuvulia nguo akuonyeshe hilo umbo lake linalomvuruga kichwa.” “Acha kumtisha bwana!” “Bora kumwambia ukweli, ajue. Haya usiku mwema. Ngoja mimi nikaangalie chakula kama nimebakishiwa.” Mama Jema akarudi ndani. Jema akamwangalia James na kuanza kumcheka. “Bado unataka ndoa?” “Daah! Sijui hawa watoto wanakosewa wapi aisee! Ninao dada zangu sampuli hiyohiyo. Twende Jema.” Wakaondoka hapo.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Angalau na James naye akapata nguvu yakumsimulia juu ya familia yake. “Huyo mkubwa, anayenifuata, naye amezaa kama hivi huyu Jelini wenu. Hataki shule kabisa. Na mdogo wake naye yupo hivyohivyo.” “Wanafanya nini sasa?” “Nimeacha kuwafuatilia aisee. Wananiumiza tu. Nimeona bora kuwaacha na mama yao.” “Huwa unakwenda kuwatembelea?” “Najitahidi kupiga simu kwa mama kuwajulia hali, basi. Hata hivyo ni kama wananiogopa sana. Wasichana wazuri tu ambao wangeweza kujiendeleza na kuwa msaada kwenye jamii, lakini waoga wakuthubutu. Wavivu. Wanataka kila kitu kiwafuate walipo.” “Basi ndio Jelini. Anataka nyinyi ndio muhangaike, mumpe kila anachokitaka. Na hatosheki, hana aibu wala huruma.” Wakaendelea kufahamiana huku akimrudisha Jema nyumbani kwake.

Wifi.

Jumapili kwa kuwa walikuwa na miahadi ya kwenda kwa kina Magesa, James akawa dereva wa Jema. Akamfuata tena kwenda kanisani. Baada ya ibada ndipo safari ya Tabata ikaanza. “Eti ni kama naogopa!” “Ingekuwa nakupeleka kwa mama yangu mzazi, hapo sawa. Lakini kwa mama G, huyo sina wasiwasi naye kabisa. Ni mama mzuri mno. Naweza sema ni kama mama wa pili kwetu. Mwema mno.” Sifa za mama G zikamwagwa nyingi mno. “Geb ndio mbali na salamu, wewe anaweza asikuongeleshe kabisa. Ni mkimya sana.”  Akamsimulia historia yao na kina Magesa mpaka wanafika nyumbani kwa kina Magesa.

Ikawa kama wenye nyumba nao wameingia muda si mrefu kutoka kanisani. Wakakutana hapo sebuleni. Wakawa kama wamepigwa na bumbuwazi. Hawakutegemea mchumba anayemuendesha mbio James ni Jema! James akacheka na ili kuwatoa kwenye ile hali ikabidi kuwatambulisha kwao ramsi kama mke mtarajiwa, na si Jema msadizi wa Joshua. “Kwa nini hukuniambia James bwana mimi nijiandae vizuri?” “Hayo ndio nilikuwa siyataki. Tulitaka muda na nyinyi. Jema awafahamu vizuri zaidi kiundugu sio vile mlivyokutana kwa kina Kumu.” Nanaa yeye akapitiliza chumbani kubadili nguo za kanisani bila hata kuchangia neno wala kutoa pongezi kwa kaka yake. James yeye akaendelea na mama G, Jema pembeni yake kimya akaanzwa na wasiwasi maana Nanaa huyu siye aliyemuona kwa Kumu akiwa na Naya. Ila akajituliza kuona muendelezo.

“Unataka kucheza game?”  Magesa akafurahi sana kuona anko wake yupo hapo. Wakahamia chumba cha pili, mama G akamuaga Jema kwamba na yeye anakwenda kubadili nguo ila angerudi muda mfupi tu, asingechelewa. Jema akajikuta sebuleni peke yake maana na Geb naye ni kama alimfuata mkewe mara baada ya kuondoka. Msichana wa kazi naye alikuwa jikoni. Kimya.

 Baada ya muda Nanaa akashuka kama anayeelekea jikoni, wala hakumsemesha Jema. Jema akasimama kama anayemfuata. “Vipi!?” Nanaa akamuuliza kama anayemshangaa. Kidogo Jema akaingiwa na wasiwasi. “Nilifikiri unaelekea jikoni na mimi nikasaidie kidogo.” “Wewe huna cha mgeni siku ya kwanza!?” Jema akashituka sana maana Nanaa alimuuliza kwa jazba mpaka akashindwa kujibu. “Yaani wewe unakuja nyumbani kwa watu siku ya kwanza tu, unataka kufika kila mahali! Unataka kutawala kila kitu!?” Magesa akawa ameshafika baada ya kumsikia mama yake akigomba. “Wewe umekaribishwa sebuleni, unataka kwenda mpaka vyumbani! Ujasiri huo unapata wapi?” “Wewe unataka kwenda chumbani kwa mama yangu?” Magesa akamuuliza Jema. “Haraka hiyo na ujasiri huo ugenini, kwenye majumba ya watu, unatoa wapi!?”

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Alichokuwa akikiepuka James tokea zamani akimlea Nanaa na kushindwa kuwa kwenye mahusiano, akihofia mapenzi yasije yakamfikisha sehemu na kumtaka kuchagua kati ya mpenzi na Nanaa, ndio kimempata. Ila imekuwa tofauti. Nanaa ndiye amebadilisha shilingi. Kwa kumjia juu wifie kwa jazba.

Ø  Nini Kitaendelea hapo?

Ø  James ametahadharishwa kwa Jelini huku akitaka kuoa kwao. Inamaana ukaribu kwao utaongezeka na Jelini ameshajua James anayo pesa, anayembania ni dada yake. Nini kitaendelea?

Ø  Na Bale naye?

Usikose Muendelezo.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment