Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 1 - SEHEMU YA 47. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 1 - SEHEMU YA 47.

 Ila akatumia akili ya haraka ili kumjibu. “Kama unamvyomjua baba yenu. Hakuwa mzungumzaji ila ninachojua kwa kila mmoja wetu, au wale ninao fahamiana nao mimi kwa karibu, kila mmoja alizungumza naye la kwake kwa vile walivyofahamiana. Sasahivi ni kama kila mmoja wetu anakumbuka lake kwa jinsi alivyofahamiana na baba yenu. Kabla ya kifo chake, akiwa kwenye hali mbaya sana, ilibidi sisi tufuatwe kwa kuwa ni kama alikuwa akimsubiria Naya amuage. Hakukata roho mpaka tulipofika pale, Naya alizimia kwa mara ya kwanza alipomuona. Baba yenu aliungua vibaya sana, Bale. Alikuwa akitisha mno. Anyways.” Joshua akaendelea.

“Japokuwa Naya alitolewa pale kwenda kupata huduma ya kwanza, ikawa ni kama bado anasubiria mpaka kuna nesi mmoja akasema nilazima kumruhusu ndipo ataondoka. Nakumbuka Naya mwenyewe alipozinduka aliomba arudishwe kwa baba yake. Sijui ni nini Naya alikumbuka au alijua, lakini ni kama yule mzee alikuwa akisubiri ukiri wa kila mmoja wetu pale.” “Kwani hakuwa akizungumza?” Ikabidi Bale kuuliza.

“Bale, baba yenu aliungua vibaya sana. Alichoweza kufanya ni kuangalia na kuhema tu. Kama si kuambiwa kama ni yeye ndio amelala pale, usingeliweza kumtambua. Alibadilika akawa kiumbe kinachotisha mno. Anyways, Naya akazungumza naye na kumwambia anakumbuka wosia wote aliokwisha kumuachia, na akamuahidi atafanyia kazi. Akanitizama na mimi. Nikamwiga Naya. Nikamwambia ya kwangu, alipomalizia mama G kutokana waliyokuwa wakizungumza naye na kumwambia wote tunakumbuka kila kitu na tutafanyia kazi, asiwe na wasiwasi juu ya Naya, hatabaki peke yake akamuahidi atamtunza kama mtoto wake, akamruhusu apumzike ndio baba yenu akafunga macho na ikawa amemaliza mwendo.”

“Ninachotaka kukwambia ni hiki, wosia aliomuachia Naya, Mimi, Geb, Nanaa na mama G ni tofauti kwa vile walivyojisogeza kwake. Yaani sisi baada ya pale ndipo tulikuwa tukikumbuka moja baada ya jingine, na havikuwa vikifanana. Kwa hiyo hata wewe tulia, utakumbuka tu alichotaka kukuacha nacho. Mimi si mtu sahihi wakujibu hilo.” Bale akatulia. Lakini akahisi ana kitu anashindwa kumwambia.

“Pengine uwe na swali jingine.” “Je, juu ya nyumba?” “Unamanisha kiwanja cha Kiluvya? Maana nyumba ndio ile mlichoma wewe na Malon.” Hapo Joshua akamuweka sawa. “Ndio hapohapo. Kwani alisema hata kusijengwe!?” Hapo akawa amemchanganya Joshua. “Nina mambo mengi sana Bale, na hapa nawahi kazini. Utarahisisha haya mazungumzo kama utakuwa muwazi zaidi.” “Ni vile ambavyo nilitaka kupatengeneza pale.” “Unamaanisha kujenga?” “Ndiyo.” Bale akajibu na kuendelea.

“Maana nilianza na mafundi tu wakaiwada, wakashindwa. Nikatafuta kampuni kabisa. Huyo mwenye kampuni anasema wajenzi wake wamemwambia eti ardhi imekataa kujengwa. Wewe umeshasikia kitu kama hicho?” “Kuwa mkweli tu kwako Bale, sijawahi kukutana na mazingira kama yako.” “Unamaanisha nini?” Bale akauliza kwa ukali kidogo.

“Mimi sijui nafsini kwako unajiambia nini na kujiaminisha nini. Lakini kwa kule ulikopitisha familia yako, namaanisha mbali na mama yako, unahitajika rehema Bale. Mungu angilie kati. Unavilio vya watoto wa bibi yako wote.” “Nitakwenda kuzu…” “Hawawataki Bale. Na walizungumza kwa wazi kabisa kuwa baba yenu anamkosi ulioambukiza watoto wake. Yaani nyinyi. Wanasema ndio maana kila anayejaribu kuwa karibu naye yeye au nyinyi, anakufa.”

“Wanasema alianza dada yao, yaani mama yenu. Wanalalamika wanasema na mama yao alipomsogelea tu, ili kuishi naye amsaidie baba yenu, akafa kifo kibaya sana ambacho si cha kawaida. Na pia wanalalamikia kifo cha Luka, mtoto mdogo asiye na hatia. Wanasema alikuwa mtoto mwenye maisha yake mazuri, lakini kila kitu kiliharibika pale tu aliposogezwa na kwenu, ambako alikuwepo baba yenu. Wanawaogopa, hawawataki. Na wamesema upande wa kwao chochote kikitokea, nimkataze hata Naya kwenda. Hawataki msaada wowote kutoka kwenu.” “Sasa hapo kosa la baba ni lipi!?” Bale akauliza kwa mshangao. Joshua hata hakumjibu.

“Mimi nilitaka tu kupaendeleza nyumbani.” “Nashauri utulie ukumbuke chochote alichozungumza baba yako na wewe Bale. Hata kipindi kile mlichokuwa mkibishana naye sana kwenye maamuzi yako. Kumbuka tu. Ukiweza hata uandike. Mimi nimegundua kuwa Naya alikuwa akiandika sana kila anachoambiwa na baba yake. Hata sasa nafikiri japokuwa hakumbuki kabisa, ila akilini mwake kunarudia wosia wa baba yake. Nimesoma kitabu chake cha siri, nimegundua huwa wosia wa baba yenu unamrudia na anaandika. Ni kama mwanzoni hakujua ni nani alizungumza naye au nini anakumbuka kila siku, lakini anaonekana alirudia diary yake ya nyuma, akalinganisha matukio ndio amejua ni baba Naya. Nashauri na wewe utulie, ukumbuke.” “Mimi kila kitu kinachohusu yeye kwangu ni lawama tu.” Akalalamika.

“Basi katika hizo lawama zake, japokuwa hukuwa ukimsikiliza, jaribu kukumbuka alichokuwa akisema, utagundua ndio wosia wako. Kama utaniruhusu naweza kukukumbusha kitu.” “Juu ya nini!?” Bale akauliza kwa mshangao kidogo. “Unakumbuka siku ambayo ulisema umeamua kuondoka kumfuata Malon?” Kimya. “Uligomba sana siku ile ukimlaumu sana baba yako, na Naya kuwa alianzisha mapenzi mapema na bado baba yako alimuunga mkono, nia yako ni maendeleo ila hakuna anayekuunga mkono na..” “Nakumbu..” Bale akamkatisha kama ambaye asiyetaka kukumbushwa maneno yake mwenyewe.

“Hapana Bale, ninachotaka kukwambia wewe HUKIKUMBUKI na ndio maana unakumbana na ugumu huko kwenye ujenzi unaotaka kuuendeleza pale kwa siri bila ruhusa ya Naya.” “Pia kuendeleza pia natakiwa kuomba ruhusa!?” “Unapaendeleza kwani ni kwako?” Joshua na yeye akamuuliza kwa ukali kidogo. Bale akashangaa sana.

“Unashangaa nini Bale na kila kitu uliambiwa mpaka na yule mwanasheria!? Na mbali ya hapo, si ulikuwepo siku baba yako akitamka wazi kabisa mbele za watu siku ile pale nyumbani kwetu, Goba, kuwa Kiluvya ni pa Naya! Na alisema wazi kabisa hata alimuomba mama yenu ambaye wewe unamuamini sana. Au naye mama yako utasema hana akili ya kufikiria? Maana alikubali.” Kimya.

“Baba yako alitamka Bale, na akaacha mpaka kwa mwanasheria! Sasa wewe unatoka vipi kwenda kuendeleza kwa mtu bila adhini yake?” “Sasa Naya si hakumbuki!” “Haraka hiyo ni ya nini Bale!?” Joshua akauliza kwa ukali kabisa akisikika kuumia. “Haraka hizo kwenye mambo yako ni lini utajifunza kusubiri? Unataka nini kitokee ili uwelewe kuna wakati mwingine japokuwa tunakuwa na tamaa ya mambo fulanifulani, lakini Mungu anaposema subiri, SU-BI-RI.” Hapo hata Joshua akabadilisha sauti ikawa ya ukali.

“Wewe unajua Naya atapona lini?” Bale naye akamuuliza. “Mimi sijui! Ila wewe uliyemsababishia hivyo mke wangu ulitakiwa uulizie hali yake sio kwenda kinyumenyume kuanza kujimilikisha mali yake.” Joshua akambadilikia. “Nia ilikuwa nzuri Joshua.” Bale akashuka. “Nia yako nzuri ni ipi Bale? Ipi na katika nini?” Kimya.

“Kitu nilichotaka kukumbusha kabla sijakuaga maana nakaribia kuingia ofisini, n..” “Si ulishasema..” “Tafadhali sikiliza Bale. Usiwe mwepesi wa kuzungumza na ndio maana unapishana na jumbe zako, kwakuwa kila mtu anapojaribu kuzungumza na wewe, tayari wewe umeshakuwa na jibu la kumjibu. Ndio maana umekosa hekima za baba yako.” “Acha kuniambia hivyo Joshua.” “Bale! Unakataa nini wewe? Utajichelewesha mpaka lini? Labda nikuulize. Ni kwa nini tunazungumza asubuhi hii?” Kimya. “Ni kwasababu HUJUI baba yako alichokuwa akikisema japo mimi nakumbuka!” Kimya. Bale alishakuwa amekasirika anatamani kukata simu na Joshua alijua akaamua aachane naye.

“Uwe na siku njema, Bale.” “Sasa mbona hutaki kuniambia!?” “Hujataka kunisikiliza na mimi sitawahi kubishana na wewe Bale. Mimi ni mkubwa sana kwako. Na nina majukumu mengi sana yakufanya. Sina muda wa kujibishana na wewe. Uwe na siku njema.” “Nakusikiliza.” Bale akasikika ametulia.

“Siku uliyoaga kuwa unaondoka unamfuata Malon. Baba yako alikwambia hivi, ‘utakapofanikiwa huko, usijekurudi kujenga kwangu’. Unakumbuka jinsi ulivyomjia juu baba yako mpaka ukaanza kumuanika Naya huku ukimfoka baba yako kuwa mbona pesa za Naya ambazo hazikuwa hata zikijulikana zinapotoka zilikuwa zikipokelewa pale nyumbani, kwa nini wewe mtoto wakiume ukataliwe? Unakumbuka baba yako alikwambia uende ukajenge kwako sio kwake?” Hapo Bale alipoa kabisa.

“Mungu amekufikisha kwenye amri moja tu yenye ahadi Bale. ‘Waheshimu baba na mama yako, upate miaka mingi na heri duniani.’ Kwa vyovyote ulivyokuwa ukimchukulia baba yako, lakini ujue kabisa, Mungu alikuweka kwa aina ile ya baba si kwingineko. Yeye Mungu alijua aina hiyo ya Bale, inamuhitaji baba kama baba Naya wala si mzee mwingine. Ukachezea hiyo nafasi kwa fujo nyingi mpaka kumuua baba yako mzazi ukiona hana akili ya kufikiria. Lakini Bale, natamani ungesoma diary ya dada yako pengine ungemfahamu baba uliyempuuza wewe, lakini akamfaa sana dada yako. Ukimsoma baba Naya aliyeandikwa na Naya, unaweza ukadhani si baba aliyekuwa akiishi na wewe ukimfoka hata mbele za wageni kama mimi.” Bale kimya.

“Ninakukumbusha hili tena, pengine tu utaelewa hilo wanalokwambia hao wajenzi. Adamu alipomkosa Mungu pale bustanini, unakumbuka laana yake? Tena Mungu mwenyewe alimwambia hivi, ‘Kwa sababu umemsikiliza mke wako na ukala kutoka kwenye mti niliokuamuru Msile tunda lake’ Yaani Mungu anamwambia kabisa, kwa sababu alimsikiliza Hawa, akatenda dhambi. Unakumbuka laana yake?” Kimya. “Acha nikukumbushe maneno ya Mungu wala si yangu. Alimwambia hivi, ‘Aridhi imelaaniwa kwa sababu yako,…. Na kuendela, nafikiri unakumbuka.” Kimya.

“Kukuleta karibu kabisa na ninachotaka kukwambia ni juu ya Kaini alipomuua ndugu yake, yale maneno Mungu aliyomwambia. Unakumbuka?” Bale akaanza kulia kwa uchungu sana. Maana alikumbuka kwa wazi kabisa. Bale mtoto wa kanisani, amekua kanisani, hata kama hatatendea neno kazi, lakini analijua neno la Mungu kwa hakika. Naye Joshua akaendelea kumwambia. “Sikwambii hivi kama kukuhukumu. Nakuelekeza njia pengine itakusaidia kufika unakotaka kwenda, kama utataka. Kaini aliambiwa hivi na Mungu, ‘Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako, kwa mkono wako. Utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake. Utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani.’ Nafikiri unakumbuka Bale. Na pengine ndicho unachokumbana nacho. Kama upo na swali jingine karibu. Vinginevyo nikutakie siku njema.” Joshua akasikia simu imekatwa. Ila akaridhika kwamba angalau amefika kwenye machozi, inamaana moyo uliopondeka bado upo.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ni nini Kitaendelea?

Usikose muendelezo kujua Penzi Jipya la J&J. Joshua&Naya? 

Bale! 

Nanaa dada mpendwa, wifi wa Jema!?

Usipitwe.

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment