Taratibu
akatoka hapo kitandani kwani tumbo lilizidi kumuuma na hali ya kutapika
ikamjia. Akatoka hapo kwa kunyata na kwenda kwenye chumba cha chini chenye vitu
vyake. Akakimbilia chooni akakuta ameloa damu, na kuanza kutapika huku akizuia
sauti kama mtu asimsikie. Alitapika Naya mpaka panapambazuka asijue afanye
nini. Akakaa sakafuni chooni kichwa amening’iniza chooni. Akatapika mpaka akabakiwa
kutapika tu mate.
Joshua
anaamka asubuhi, mke hayupo kitandani. Akashituka na kwenda choo cha chumbani,
hakuwepo. Akashuka sebuleni. Hakuwepo. Akafikiri atakuwa kwenye meza ya kulia
ya jikoni akila kwa sababu alilala bila kula chakula cha usiku. Hakuwepo. Akili
ikamjia kwenda kwenye chumba alichoanza kukizoea. Chumbani hakuwepo. Pakawa
kimya sana. Akabaki hapo chumbani akitafakari alipo. Akarudi chumbani kufuata
simu yake kuangalia kama kuna mlango ulifunguliwa huku amejawa hofu yakupita
kiasi. Simu ikaonyesha hakuna mlango uliofunguliwa, kidogo akatulia na kujaribu
kufikiria anapoweza kuwepo.
Akarudi
kwenye chumba ambacho alidhani angekuwepo, lakini safari hii akaamua kwenda
kumuangalia na chooni. Akamkuta amepitiwa usingizi ila amening’iniza kichwa
chooni. Damu mpaka sakafuni. Akamuhurumia. “Naya!” Akashituka sana. “Samahani
kama nimekuamsha.” “Vipi?” “Safi tu, sikutaka kukuamsha.” “Unatapika?” “Nipo
sawa. Sikutaka kukuamsha.” Joshua akaumia, akajua amembadilikia, ameanza
kumficha.
“Naya,
naomba usinifiche. Niambie ukweli tafadhali. Usiogope.” “Naogopa
Joshua. Sikumbuki kitu. Na nasema ukweli, sidanganyi. Sikumbuki. Kila
nikijitahidi sikumbuki.” Naya akalia akijitetea. “Najua hunidanganyi Naya. Naomba utulie
mke wangu. Na samahani kwa kukufanya ujisikie unatakiwa kukumbuka. Haikuwa nia
yangu kukuogopesha ila nilitaka kukufurahisha zaidi. Pengine nilitumia sauti ya
msisitizo mpenzi wangu, ila sikuwa na nia ya kukushutumu.” Bado akaonekana kama
haelewi tena, kichwa kimevurugika tayari.
“Na
sikukusudia kukuamsha, ndio maana nilitoka. Sijui nifanye nini! Nakosea kila
wakati! Ni kama akili yangu inashindwa kujua nini chakufanya kwa wakati.”
“Nisikilize Naya. Tafadhali tulia uniangalie.” Akarudi kuanza kutapika tena.
Joshua akamshikilia mbavu, hakuna kitu kikawa kinatoka. “Naomba usimame hapo,
utoke ukaoge ili uvae pedi.” “Acha mimi nibaki tu chumba hichi ili ukilala
nisikuamshe. Nataka kubaki hapa. Peke yangu ili nitulie. Nahisi sielewi tena.
Kichwa kinazunguka.” “Basi tulia, acha nikuletee vitu vya kujisitiri.” Akataka kutoka.
“Hapana.
Acha tu.” Joshua akarudi.
“Sasa
utajisaidiaje, Naya?” “Nataka kutulia, nifikirie mimi mwenyewe nijue nini natakiwa
kufanya. Usinisaidie kitu. Niache tu.” Akazidi kulia tena
akionekana maumivu yamemzidia. Kisha akainamia tena choo. “Hakuna kitu kinatoka
mpenzi wangu. Naomba utulie na ndipo utaweza kufikiria.” Akaendelea kulia,
Joshua akatoka kwenda kumletea chupi na pedi nyingi tu. Akarudi akamkuta
akioga. Kisha akaanza kutapika tena. Joshua akataka kuingia amsaidie, lakini
akaona amuache. Analia huku akitapika halafu akioga. Joshua akabaki
akimwangalia mpaka akamaliza. Akamkabidhi taulo. Akajikausha huku upande
mwingine akipaka damu hilo taulo. Joshua akajua ni kweli ameshituka, damu
zilikuwa zikitoka nyingi sana.
“Naya!
Huwa tumbo kama hilo lilipokuwa likiuma na kupatwa hiyo hali, kuna dawa ulikuwa
ukinywa inakusaidia sana.” “Sikumbuki.” “Mimi nakumbuka na
nafikiri ninazo, nikuletee?” “Nielekeze nikachukue mwenyewe. Sitaki
kukusumbua zaidi.” “Hunisumbui hata kidogo. Nisubiri narudi sasahivi.” Joshua
akatoka hapo akikimbia mpaka anapoweka dawa kwenye kabati ndogo. Akarudi na
soda ya Sprite. Hapo kunywa napo ikawa shuguli. “Nitatapika zaidi. Siwezi
kuweka kitu mdomoni.” Baada ya kumbembeleza kwa muda mrefu akakubali kunywa hizo dawa
na hiyo soda. Akakataa kurudi chumbani kwao. “Hapana. Kule
nitakusumbua.” “Hutanisumbua Naya!” Akazidi kulia, Joshua akaona amuache tu
hapo. Alipotulia na kupanda kitandani, ndipo akatoka kwenda kujiandaa kwenda
kazini.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Joshua
alitoka hapo hajui hatima yake na Naya. Naya huyu amerudia hali kama
amechanganyikiwa, mtiririko wa mawazo yake ni vile anavyochagua yeye, halafu
akawa na msimamo na anachokitaka sio rahisi kama mwanzo aliporudi na kumuuguza
kirahisi. Amesimamia kukumbuka. Hataki kuwa tegemezi. “Amehama na chumba!”
Joshua akawaza na kuamua kujisalimisha kwa Mungu wake.
Penzi Kikohozi.
‘Acha
kumnyima raha na kumtia wasiwasi mke wangu. Mpigie simu.’ Ujumbe
wa Geb ukaingia kwenye simu ya James, ndipo akakumbuka. Hapohapo kabla hajasahu
tena akampigia simu. “Kwema kaka!?” Nanaa akauliza kwa kulalamika kidogo. “Kwema,
unisamehe nilitingwa.” Nanaa hakuridhika. “Kiasi chakushindwa hata
kunijulia hali hata kwa ujumbe tu!? Ni nini kinaendelea kaka? Au nini
nimekuudhi!? Kama nimekosa tafadhali uniambie tu nirekebishe. Wewe..” “Nanaa!
Ni habari njema tu nitakuja tuzungumze.” “Umepata mchumba?” Nanaa
akauliza swali la moja kwa moja.
“Ndiyo.” Nanaa
hakutegemea. Akabaki kimya kabisa, James asielewe kama ndio amefurahi au bado
anahasira ya kutorudishiwa simu. “Nanaa?” “Hongera kaka.
Lakini usingeacha kuwasiliana. Niliingiwa na wasiwasi!” “Unisamehe. Nilikuwa
kwenye kuweka sawa mambo, ndio maana niliona nikutafute nikiwa nimetulia.”
“Sawa. Uwe na siku njema.” “Usikasirike sasa! Mimi nilijua ungenifurahia!”
“Nimeumia kuona unanitenga kaka!” “Pole mdogo wangu. Nisamehe. Ila mwanzo ni
mgumu. Nipo kwenye kuweka msingi. Nivumilie tena kidogo tu, mambo yakikaa sawa,
nitakutafuta na nikutambulishe. Ni sawa?” “Sawa. Kila la kheri.” James
alijua wazi hajaridhika, na yeye hakuwa na muda wa zaidi, alikuwa akichat na
Jema. Akamuaga kwa ahadi ya kuja
kumpigia tena baadaye. Akakata.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ilipofika
mchana Joshua akajaribu kumpigia mkewe bila mafanikio na mpaka anatoka kazini
hakuwa amemsikia. Akaona amuache. Ila akawahi kutoka kidogo ili kumuwahi.
Akafika nyumbani akamkuta amelala, hajanywa hata chai. Akaenda kukaa pembeni
yake. Akashituka. “Joshua!” “Vipi tumbo na hali ya kutapika?” Akatulia kama
anayejaribu kufikiria.
“Najisikia
vizuri. Lakini nina swali.” “Uliza tu.” “Eti Zayoni ni nani na yuko wapi?”
Joshua akashituka sana, hakutegemea. “Alikuwa mdogo wako.” Naya akawa
hajaelewa. “Mlizaliwa watatu. Wewe ndio dada mkubwa, halafu Bale na wa mwisho
ni Zayoni. Unakumbuka nilikwambia sisi ni yatima?” “Nakumbuka. Kwamba sina
ndugu hata mmoja aliyebakia hapa duniani?! Kwamba kama vile wewe ulivyokuwa
ukienda kwa kina Magesa, mimi sina mtu hata mmoja kweli!?” Hilo swali likazidi
kumtia wasiwasi Joshua.
“Naomba
upone kabisa, nitakusimulia juu ya ndugu zako Naya. Nakuomba isiwe sasahivi.”
Akamuona machozi yakimtoka ila hakuongea tena. “Ni kwa faida yako. Sitaki
kukuchanganya. Ni sawa?” “Nitasubiri japo nilitamani sana kujua. Nimekuwa na maswali
yasiyo na majibu, yanaanza kunisumbua.” Akaongea hivyo na
kujirudisha kulala vizuri. Joshua hakutaka kuongeza chochote kwenye hilo kwani
kwanza ni kama hawapo kwenye maelewano na anaumwa. Msisitizo wake ni hataki
amsumbue. Hakujua kama anauliza kwa nia ya kwenda kwa ndugu zake na kurudi, au
la! Akasimamia alichosema, atasubiri. Akakaa hapo kimya kwa muda.
“Naya?” Akajigeuza
na kumwangalia. “Nikuletee supu? Niliomba upikiwe.” Akakataa kwa kutingisha
kichwa. “Umekula kitu chochote?” “Tumbo limejaa mpaka
linakuwa kama lina vichomi. Siwezi kunywa hata juisi. Ila nakunywa maji.” “Pole
Naya.” “Asante. Naomba kurudi kulala.” Joshua akatulia kidogo
akijua ndio anamfukuza.
Akatumia
akili kwa haraka kabla hajapotelea usingizini. “Leo tunalala huku?” “Hapana.
Ila mimi nataka kulala hapa ili iwe rahisi kutumia choo. Nisikusumbue.”
“Unakumbuka nilikwambia hunisumbui!” Akanyamaza akamuona machozi yakimtoka.
“Siwezi kulala bila wewe Naya. Usipolala na mimi ndio nitasumbuka. Naomba nije
tulale wote.” Akanyamaza hakujibu.
Joshua
akaenda kupiga magoti pembeni ya kitanda mbele ya uso wake. “Nakupenda Naya. Na
maisha yangu yanakuwa magumu kama sipo na wewe. Kila kitu unachoona nafanya,
hata kwa kukosea, ujue nafanya kwa ajili yako mpenzi wangu. Naomba unisamehe na
univumilie.” Akamuona anatingisha kichwa kukubali. “Asante. Basi naomba turudi
kitandani kwetu. Na uwe huru kutumia choo muda na wakati wowote ule, hutanisumbua.”
“Hapa nilipo
nimechafuka mpaka nimechafua magodoro. Nataka kujaribu kusafisha tena, ndipo
nikimaliza nije.” “Unajua kwa nini mchana nilikuwa nikikupigia sana?” “Sijui
simu
![]() |
“Nenda
ukaoge, mimi nitabadilisha hapa, ukimaliza nitakupa pullups ili uvae,
ulale vizuri.” “Acha tu nitasafisha mimi mwenyewe. Wewe nenda ukapumzike. Najua
umechoka na kazi.” “Sijachoka Naya. Naomba niruhusu niwe na wewe.” Akakaa. “Ni
sawa?” “Nikikwambia nimechafua, ujue nimechafua mpaka godoro. Mchana
ilibidi nilifute na taulo la maji. Hapa nimelalia taulo. Ndio maana naona
nisafishe kila kitu.” Wakavutana hapo, Joshua akibembeleza mpaka akakubaliwa. Naya
akatoka hapo kitandani, Joshua akabaki amehamaki. Ni kama kulichinjwa mbuzi.
Akajua hilo godoro halitafaa tena na ndio maana alikuwa akikataa kurudi
chumbani akihofia kuchafua na huko nako. Lilijaa damu na bichi kuashiria
alishaliosha na kubakia bichi. Inamaana siku nzima alikuwa amelalia maji.
Akamuhurumia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Alichokifanya
nikukusanya yale matandiko yote na kwenda kuyaweka kwenye mashine yakufulia.
Akayaona yale maua pale chumbani wakati akifuta damu sakafuni, yakamtia hasira
kabisa. Akaanza kuyakatakata kwa hasira na kwenda kuyatupa. “Haya ndiyo
yameniponza.” Akalaumu maua. Akafanya kila kitu kwa haraka kisha akamfuata
chumbani. Akamkuta akilia peke yake upande wa bafuni, damu zinachuruzika mpaka
kwenye nyayo. “Niambie nikusaidie nini.” “Sijui natakiwa kufanya
nini!” “Tuanze kwa kuoga kwanza, uvae nguo za kulalia na pullups.
Nitakupa tena dawa, utajisikia vizuri.” Akamshika mkono mpaka bafuni. Akaamua
kuoga naye kabisa. Wakaoga, Joshua akawahi kutoka yeye. Akamtafutia taulo jeusi
kabisa ili asichanganyikiwe tena pindi atakapoona damu. Akahangaika naye mpaka
akamuweka kitandani. Na yeye akafanya yake na kupanda kitandani. Akawa
amegeukia kwengine amejifunika. “Umeshalala?” Akamjaribisha. Kimya.
“Umenichukia?” Kimya.
Akakumbuka
heating pad, akamzungushia chini ya tumbo, akaanza kumsugua
kiuno taratibu. “Asante, najisikia vizuri.” Akashukuru akiwa amelala vilevile
amempa mgongo wala asigeuke. “Basi jaribu kulala. Ila nataka usisahau kuwa nakuhitaji
Naya. Humu ndani maisha si sawa bila wewe mpenzi wangu. Nakupenda, na ujue sitabaki
sawa bila wewe. Usinichukie.” Hakumjibu lakini akajua amemsikia. Baada ya muda
akamsikia akihema kama aliyelala.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Usiku
hakuamka hata mara moja, ila alfajiri na mapema Joshua yeye akaamka na kwenda
kuabudu. Akaimba akipiga kinanda kwa sauti ya chini mpaka akamaliza.
Alipojisikia anataka kuomba, akapiga magoti sakafuni kabisa, akawa kama
amesujudu akaanza kuomba akajisikia kulia mbele za Mungu. Akamimina moyo wake
mbele za Mungu, na kupotelea kwenye maombi. Akiwa anakaribia kumalizia
akamuhisi Naya pembeni yake, anapenyeza mkono amshike kama alivyozoea kuomba
naye akimshika mkono. Alifurahi Joshua, karibu ahitimishe kwa kusema Amen.
Lakini akapiga magoti vizuri, akamvuta mikono yote miwili akaanza kuomba kwa
sauti akiomba naye. Hakuomba muda mrefu ila alitubu kibinafsi, kisha akamuombea
afya nje, amani kutoka ndani ya moyo wake na utulivu wa fikra. Akamuombea kwa
upendo mpaka akamaliza. Akatamka baraka, umoja na upendo juu yao. Ndipo
akahitimisha. “Amen.” Na yeye akajibu. “Amen.” Akamwangalia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Pole
Naya wangu.” “Sasahivi najisikia vizuri. Sina maumivu ila usingizi.” “Nilijua
ungelala vizuri. Nilikupa dawa za usingizi pia.” “Ndio maana nilipitiwa,
sikukusikia wakati ukiabudu. Ungeniamsha!” “Nimekuombea.” Akatabasamu na kusimama.
“Asante, lakini uwe unaniamsha niwe naomba mwenyewe. Baba Naya aliniambia
sitakuwa salama mbali na magotini. Mungu peke yake ndiye atanifanya nibaki
salama.” Joshua alishituka, ila akaogopa kumuuliza. “Na mimi pia aliniambia.
Nakumbuka nilishabahatika kuingia naye kwenye maombi ya kufunga na kuomba kama
mara mbili hivi. Baba yako alimpenda sana Mungu, Naya. Na wewe. Alikupenda
sana.” Akatulia kama anayejaribu kukumbuka kitu.
“Twende
tukaoge.” “Njaa inaniuma Joshua!” “Kwa kuwa jana hukula. Unajisikije sasahivi?”
“Kidogo hofu imepungua. Niliingiwa na hofu kubwa, nikapaniki sana. Ila
nimemuomba Mungu awe ananiambia kitu natakiwa kufanya ili nisiwe
nakuudhi.” Joshua akazidi kuumia. “Akili yangu nahisi haina uwezo wa kufikiria
kwa haraka. Kile nafikiria mimi ni kizuri kumbe si..” “Hapana Naya. Mimi ndiye
niliyekosea mpenzi wangu. Amini akili yako haina tatizo na wala usijitilie
shaka.” “Usiniambie hivyo kunifariji. Acha Mungu anisaidie tu.” “Hakika hapana.
Mimi nilikosea. Hapakuwa na ulazima wa yale maua kwa wakati mzuri kama ule.
Maua yangesubiri lakini si sisi. Wewe ndio ulikuwa ukifikiria vizuri zaidi
yangu. Nilikosa.” Naya akatulia.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Njoo
ukae hapa kidogo nikwambie kitu.” Wakatoka sakafuni na kuhamia kochini.
“Unaakili sana Naya. Sana. Mungu alikujalia kipaji cha ubunifu. Si kwenye
mavazi tu. Hata tulipokuwa tukifanya wote kazi. Kwenye idara uliyokuwa ukifanya
wewe kazi, ilikuwa ikinisumbua sana. Ulikuja wewe kwa muda mfupi sana, ukabuni
kitu ambacho mimi nimeiga kutoka kwako ndio natumia mpaka sasa.” “Kweli
Joshua?” “Kabisa. Sasahivi napata matokeo mazuri sana kutoka kwa watu wa chini
yangu kutokana na wazo lako ambalo nililichukua, nikawapelekea watu wa IT
nikawaambia walitengeze, likawekwa kwenye kompyuta kitaalamu. Imekua msaada
sana mpaka kampuni nzima imeiga. Na sikutaka kuwa mwizi, walipokuwa
wakinipongeza, niliwaambia wazi nililitoa kwako.”
“Sasa na
hicho kipaji naona kipo mpaka nyumbani. Ulibuni usiku mzuri sana kwetu, mimi ndiye
niliyeharibu. Nimejuta sana, na nimemsihi mungu anisamehe, akusaidie ujasiri wa
kutengeneza kitu kingine kwa ajili yetu, na naahidi kukusikiliza. Sitakukatili
kama jana. Naomba usinichukie.” “Nakupenda Joshua. Siwezi kukuchukia.”
“Sasa kwa nini ulianza kuulizia pakwenda?” “Si kwa kukuacha, ila angalau kwenda
kujiuguza kwa muda. Nilikuwa sijui kitu chakufanya nikaona nakuharibia vitu
vyako.” Joshua akashangaa sana.
“Unamaanisha
nini kusema unaniharibia vitu?! Si nilikwambia hapa ni kwetu?” “Kwenye ndoa,
ndiyo. Lakini sasa hivi najua hapa ni kwako Joshua. Kuna diary yangu
niliandika mambo mengi kipindi cha karibu na ndoa. Najua kwetu kulikuwa
Kiluvya, hapa na kila kitu nilikukuta navyo. Mara ya kwanza nilipokugundua wewe
ni nani na unavyomiliki, nilipaniki. Si ndiyo?” Joshua akatulia. “Niambie
ukweli ili nisichanganyikiwe zaidi.” “Ni kweli Naya. Lakini naomba usipaite kwangu!
Inaniuma na ninaona juhudi zangu ni bure kabisa. Nataka upaite kwetu na watoto
Mungu atakao tujalia.”
“Na pia
nimegundua ulisema hutaki tuwe na watoto mpaka baada ya miaka miwili ya ndoa.
Si ndivyo?” “Naya!” “Ndivyo nilivyokuwa nimeandika siku na tarehe uliyokuwa
umeniambia, sasa labda uniambie vinginevyo.” “Ni kweli.” Ikabidi kujisalimisha.
“Kwahiyo sikuwa nikikukimbia, ila nilitaka kwenda kujiuguza mpaka nipone ili
kukupumzisha.” “Kwahiyo na mimi nikiugua kwa muda mrefu utaondoka?” “Hapana
Joshua! Najua unamajukumu mazito kazini. Sitaki ukwame kwenye kuniuguza kila
mara. Halafu sikujua kama kuna dawa huwa natumia na kunifanya nijisikie hivi.
Nilikata tamaa.”
“Nakutaka
wewe ukiwa mzima, na mgonjwa. Wewe ni mimi. Ukiugua wewe, ujue na mimi naugua
sema maumivu unakuwa nayo wewe. Tutakuja kuzungumza zaidi juu ya familia. Ila
nenda ukale wakati mimi naoga kwa
haraka. Na naomba leo uwe na simu mpenzi wangu. Itanifanya nitulie
kazini. Nipo kwenye kipindi kigumu huko, nahitajika sana.” “Hata sijui simu ipo
wapi! Nitaitafuta.” “Niliipata. Na niliiweka kwenye umeme. Ipo chumbani juu ya
meza.”
Akamsogelea
zaidi. “Na nikirudi naomba unikumbushe ahadi zako zote ulizonipa, Naya.”
Naya akaanza kucheka. “Usicheke bwana! Nahisi kuna kubadilikiwa.” “Mimi
sikumbuki.” Naya akajibu akicheka. “Basi kazi yako ya leo. Huko ulikokuwa
ukisoma mambo yako ya nyuma uliyoandika, basi leo ukasome zile ahadi zako zote
ulizonipa. Ili tubakie ukurasa mmoja.” Naya akazidi kucheka. Akambusu juu ya
mdomo, na kukimbilia juu chumbani, Naya akaelekea jikoni akilalamika. “Mimi
nilidhani ananisogelea anibusu vizuri! Joshua naye!” Akajilalamisha Naya.
Kisicho Riziki, Hakiliki.
Akiwa
njiani simu ya Bale ikaingia. Akashangaa sana, ila akapokea. “Ni asubuhi
sana Bale! Kwema?” “Kwamba nakusumbua?” Joshua akatulia, hakumjibu
maana aliuliza kwa jazba. “Kama unaona huna muda wa kupokea simu zangu,
useme, nisikutafute.” Joshua hakujibu. “Maana unakua kama unaona nakubugudhi! Muda gani
ulitaka kupigiwa simu?” Kimya. “Niambie sasa?” “Utakaponiona napokea simu yako. Muda na wakati
wowote ule ujue nipo tayari kukusikiliza.” Akamjibu Joshua kwa
utulivu tu. “Sasa mbona ni kama unalalamikia muda?” “Niliingiwa tu na wasiwasi
juu yako Bale! Sikutegemea simu yako alfajiri hii. Nikusaidie nini?” Joshua
akaamua kujishusha amtulize kwani kadiri alivyoongea alihisi hasira inampanda.
Kimya.
“Bale?” Joshua
akamuita taratibu tu. “Kwani wewe baba alikuachia wosia gani?” Hilo
swali likawa pana sana, Joshua akawa hajui amjibu nini! Na kwa nini ampigie
simu mida hiyo kuuliza swali kama hilo!
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
0 Comments:
Post a Comment