Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 1 - SEHEMU YA 43. - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 1 - SEHEMU YA 43.

Bale akatoka pale chumbani alipokuwa amelala kwa haraka akimfuata huku akimuita. Nyumba nzima alikuwa peke yake. Akawahi mlangoni, akakuta milango yote imefungwa. “Acha uhuni Malon!” Akaongea akimsaka mpaka chini ya uvungu. Alimtafuta mpaka panakaribia kupambazuka, hapakuwa na mtu ndani. Akatoka kumuuliza mlinzi kama alimuona mtu akiingia hapo. Mlinzi akakataa. Akaona avute kidogo kujituliza. Alfajiri hiyo ya jumapili, Bale alivuta bangi mpaka ikamkolea. “Kwani mimi nimemuuza Naya wapi? Si nimemrudisha kwa mumewe!” Bale akawa anajizungumzisha peke yake. Akatoka kuzungukia biashara zake akashindwa kurudi nyumbani kabisa, akabaki mtaani akimangamanga asijue atulie vipi.

Kwa Jema.

Siku ya Jumapili.

Aliamka amejawa furaha huyo, kama aliyetunikiwa ulimwengu. Maandalizi ya kwenda kanisani na kukutana na James yakaanza. Nguo zikawa si nzuri tena. Jema mjua mavazi asubuhi hiyo akawa hana nguo. Ikawa hivyohivyo kwa James. Alibadilisha mashati na suruali karibu kugairi kwenda kanisani. Kila nguo ikaonekana haitamuakilisha vizuri. Gafla viatu vyake vyote vikawa navyo ni kama Geb amevitia sumu. “Hata hivi havitaniwakilisha vizuri.” Alijisemea James akiwa amevaa shati jingine na viatu. Swala la suruali ndilo aliamua kuachana nalo kabisa, aliona vinamchanganya zaidi. Akabaki amevaa shati na viatu akihangaika, na kuchelewa miahadi na mwanamke aliambiwa ni mwiko.

Saa tatu na dakika 45 alikuwa ameshafika sehemu ya kuegesha magari akimsubiria Jema waingie wote kanisani. Nne kamili Jema akawa anavuta gari yake na yeye sehemu ya kuegesha. Akampigia simu James. “Nipo tu ndani ya gari nakusubiri wewe.” “Si ulisema nisiwe nakimbilia vitasa?” Wakaanza kucheka. “Nakuja mama.” James akatoka garini akafuata maelekezo mpaka akamfikia.

Akamfungulia mlango. “Yaani kwa kukuangalia tu hapo ulipokaa, umependeza sana.” “Na wewe umependeza sanaaaa. Halafu unanukia vizuri!” “Huko kupendeza sanaaaa! Kunaanza kunitia wasiwasi. Watafikiri nimevunja kabati.” “Kumbe hujavunja?” “Msema ukweli mpenzi wa Mungu. Nimevunja.” Jema alicheka sana.

“Ila umependeza sana James. Umebadilika sana usoni, ukavutia.” James akacheka. “Hizi sifa zinavyorudiwa! Basi Jema. Sitoi tena ndevu. Zitabaki hivihivi.” Jema akazidi kucheka na kushuka garini. “Nimeshajua kama ni zawadi ya viatu, viwe vya juu. Au nimekosea? Maana sijawahi kukuona na viati vya chini hata mara moja!” “Hapo umepatia. Na ninapenda viatu kuliko chochote. Ni kama ndio udhaifu wangu. Huwa naanza kununua viatu kwanza, ndipo linakuja swala la nguo.” “Pochi?” “Nakuwa nimeshaishiwa pesa, nabaki kurudia rudia pochi.” James alicheka sana. “Nguvu yangu ndogo.” “Itabidi tuongeze. Twende kanisani kisha uniambie ni nini kingine unapenda mbali na viatu.” “Kuwa na wewe hapa.” “Hicho umeshapata. Nataka kujua ambacho huna au unacho lakini ungetamani kuwa nacho zaidi.” “Wewe.” Jema akajibu kwa haraka, James akamwangalia na kucheka taratibu. “Mbona sasa hujibu!?” “Tukitoka kanisani. Twende kwanza tukamuabudu Mungu.” Wakaingia ibadani.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ibada ikaisha muda mzuri tu na ilikuwa nzuri sana. Wote wakapapenda hapo. “Sasa sisi huwa kila jumapili, tunakutana kwa kina Magesa kwa chakula cha mchana. Imekua kama desturi yetu kwa familia, kuwa angalau kwa juma tunakutana mara moja.” “Hiyo ni nzuri sana. Basi acha mimi nikuage, nisikucheleweshe.” “Sikuwa nimemaliza Jema!” Jema akacheka lakini alishakuwa amenyongea baada ya kusikia hivyo. Akajua James ndio anamuaga.

“Samahani sikusikiliza mpaka mwisho.” Akaongea akishindwa hata kumwangalia, na cheko lote likamuisha. “Hamna neno. Lakini nimewaambia mimi nitakwenda jioni, ili kama unanafasi twende sehemu tukae wote. Utakapokuwa tayari kwenda nyumbani, ndio na mimi niwapitie kuwasalimia.” “Mimi nipo tu James. Usiharibu ratiba zako kwa sababu yangu. Nenda tu. Sisi tunaweza kupanga kukutana hata wakati mwingine. Familia kwanza.” Akamalizia Jema akiweka msisitizo ambao wazi alionekana hakuwa tayari kuachana naye kwa wakati huo.

“Wewe unaratiba gani baada ya hapa?” “Naona nitarudi tu nyumbani kupumzika.” “Ni sawa tukienda sehemu tukakaa kidogo?” “Mimi ningependa James, lakini sikutaka kukufunga.” “Hamna neno. Basi twende sehemu tule, halafu tutafute sehemu ya kukaa kidogo. Unahamu ya kula nini?” “Kuku wa Makange. Nafahamu wanapotengeneza ila sio kwenye hoteli kubwa kama ile uliyonipeleka jana. Si pahadhi.” “Twende hukohuko kwenye nyama vumbi. Mimi sina shida.” Hilo nalo likamfurahisha James, kwamba Jema si wa mahoteli makubwa kila wakati kama Geb alivyomwambia. Kwamba hata kwenye nyama choma za mtaani anaweza kumpeleka! Pengo la Nanaa likaanza kuzibwa taratibu.

Wakatoka hapo mpaka Brekipointi kila mtu na gari yake. Jema akashuka garini na kumsubiria James mpaka akafika hapo, hapakuwa mbali na kanisani. James akaegesha na kuteremka garini, Jema akamsogelea. Ila akamuona kama amepoa zaidi, asielewe ni nini. Furaha aliyokuwa nayo ikawa imebadilika kabisa. Akaona ampe muda, asimkere kwa maswali. Wakaongozana mpaka sehemu ya kula.

Wakatafuta meza yao sehemu nzuri, wakakaa. Muhudumu akafika kwa haraka tu. Wakashangazwa maana watu walikuwa wengi kuashiria walishatoka ibadani wapo hapo kwa mlo. James akabaki akimwangalia Jema, alionekana yupo pale lakini hayupo. Akaweka mkono mezani akiwa ameufungua huku akimwangalia Jema aliyekuwa amepotelea mawazoni akiangalia sehemu ya barabarani kwani ilikuwa nje tu, hata hakuona mkono wa James.

Muhudumu alipoleta vinywaji na kuwakaribisha ndipo akaona mkono wa James pale mezani akiashiria aweke na wake pale. Jema akajishauri, James akijua amemuelewa. Akaweka kiganja chake taratibu juu ya kiganja chake akabaki akiangalia ile mikono yao, James akafunga vizuri na kuuminya taratibu, Jema akacheka taratibu na kumwangalia. “Mbona upo mbali, unaniacha hapa mwenyewe?” “Nipo.” “Mwili ndio, ila mawazo hayapo na mimi. Unawaza nini?” Akacheka kama anayesita.

“Si unajua unaweza kuzungumza na mimi chochote kama vile ulivyozungumza na mimi jana au kabla?” “Sipendi kuonekana kama wale wanawake needy.” James akatulia tu akimsikiliza akiwa amemuelewa. “Yaani over attach kwako ukaniona mzigo. Nakuganda na kukufanya ushindwe kufanya mambo yako au ukashindwa kuwa na watu wako wa muhimu. Sitaki kukuingilia na ratiba zako za kifamilia. Tafadhali usijisikie nilazima kuwa hapa. Mimi naweza kuagiza chakula nikala hapa au nikakibeba nikaenda kula nyumbani. Wewe ukaendelea na ratiba za familia.” Jema akahitimisha James akimsikiliza tu.

Kwanza James alikuwa amependeza na kujipangilia. Hapo alipokuwa amekaa amekaa vizuri kama mwanaume anayejitambua. Msafi anavutia. Jema akajiona kama kipanzi kwake. Kama asiyemstahili huyo James. Uzuri wa James ni kama ulipitiliza sana kwa viwango vya Jema ambaye kwanza hawakuendana rangi na James. James alikuwa mweupe wa kupitiliza kama mdogo wake Nanaa na watoto anao zaa Nanaa. Na hivyo alivyotengeneza nywele na kulambishwa, akawa kama chotara. Akaongeza utulivu wa pesa aliyo nayo, na elimu ya wanaume wote wawili mfano wake wa mapenzi. Geb na Joshua. Jinsi wanavyofanyia wanawake zao, James alikuwa ameiva ila tu hakuwa tayari kwa mwanamke. Jinsi alivyojibeba hapo kwa Jema, akabaki akimbambaisha Jema. Kwanza ile hali yakumshika mkono kwa namna ile, ilishamsisimua vilivyo.

“Unakumbuka mimi ndiye niliyekuomba tuje wote hapa?” Kidogo Jema akapoa, na kuinama James akiwa bado amemshika mkono. Akamvuta kidogo kama akimuita. “Jema! Mimi nataka kuwa hapa na wewe na wala si kwingineko. Najiona nipo sehemu sahihi na mtu sahihi, labda uniambie vinginevyo.” “Mimi nipo, ila sitaki kukuvurugia mipango yako.” “Ushajiuliza pengine ndio unaitengeneza?” “Sijui Jamesi!” “Basi naomba uwe na amani. Huniharibii chochote. Sawa?” “Sawa.” “Basi karibu kinywaji.” Akamuachia mkono wakanza kunywa, walishaagiza na chakula. Wakaletewa. Pakawa na utulivu fulani hivi wakila.

“Umependa nyama yao?” Jema akauliza kwa kujali. “Hapa pia ni viwanja vyetu na Nanaa. Tukimuongeza Geb, anabakia mtizamaji akiwa ameonywa na mkewe asiongee chochote, atulie akinywa maji mpaka tumalize. Kwa hiyo huwa napenda nyama yao sana tu.” Jema akacheka. “Sikujua.” “Sasa kuna sehemu nyingine hiyo, chini ya hapa kidogo. Kimara huko. Wanachoma nyama, hatari. Huko ndiko tunapapenda zaidi.” Jema akaendelea kula na tabasamu usoni kama anayejaribu kufikiria.

“Uliniambia ukitoka hapa unarudi nyumbani. Tunaweza kwenda mahali?” “Wapi?” “Nanaa anavyosema eti ni sehemu yake alipagundua yeye. Anaita ni Pa-siri. Lakini nikagundua na Geb naye aliambiwa hivyohivyo na Joshua naye alishaelekezwa.” “Kwa hiyo si siri tena?” Jema akauliza akicheka. “Sidhani. Ila kweli ni patulivu. Twende tukakae hapo kidogo ndipo nikuache ukapumzike. Au tena mimi ndio nageuka kuwa Needy?” “Hapana bwana James! Mimi nisiye na mipango ndio sitaki kuwa Needy.” “Huwa unakwenda kumtembelea mama?” “Inategemea nipo kwenye hali gani. Kama kipindi hiki nilikuwa nikimkwepa.” “Sababu ya Temu?” “Aisee nimekukubali James! Unaakili ya kufikiria na kuunganisha matukio.” Wakacheka.

“Namuogopa. Namkwepa. Sitaki arudie kuniambia, aliniambia, sikumsikiliza. Yeye anawajua watoto wa mjini kwa kuwaangalia. Wanaume hawana maana. Wana mwanzo mwisho hawana. Hakuna waoaji. Wachezeaji watupu. Walioko kwenye ndoa, wanataka wasio kwenye ndoa. Najitafutia matatizo na lazima nije kumkumbuka. Na mengine mengi.” “Daah! Mpaka hapo tu yameshakuwa mengi sana.” “Basi ndio ujue ndio maana namkimbia. Ila pia na yeye nilimkopa pesa nyingi sana sababu ya huo ujenzi.” “Jema!” “Ilikuwa shuguli James! Siwezi kuhema Temu akitaka pesa. Nilikopa kila mahali. Sasa najua mama atataka kujua hiyo nyumba ilipofikia.” “Na huna pakuonyesha!” “Ewaa! Ndio maana najificha kwake. Ila anatujali sana. Hilo si tatizo kwake. Anaweza hata akanisamehe hiyo pesa. Anatupenda sana. Asiponisikia hata siku tatu atapiga au kutuma ujumbe kujua kama nipo salama.” James akanyamaza mpaka wakamaliza kula. Akamwambia amfuate kwa nyuma mpaka hiyo sehemu waliyotambulishwa na Nanaa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ilikuwa upande wa baharini. Jema akacheka maana walikuta watu wengine. “Usiwe na haraka sasa. Sehemu yenyewe bado.” Akamuona James anavua viatu na soksi. “Haiwezekani!” Jema akashangaa. “Nakuahidi utafurahia hii baridi yake. Vua tu, utajisikia kupumzika. Kwa huko tuendako kuna kukanyaga na maji kidogo, utaharibu viatu vyako.” Aliposikia hivyo, Jema mpenda viatu, akavua kwa haraka sana na kushika mkononi. Wakaanza kutembea upande wa bahari wakiifuata hiyo sehemu. Kweli wakakuta kama kijipango kwa ndani.

“James!” “Si nilikwambia! Sasa tukae hapo ndani kidogo.” Wakaingia hapo, Jema akatafuta sehemu akakaa wakiangalia maji kwa mbele kidogo tu maana ni kama maji yalizunguka hapo, mtu anaweza asitake kukanyaga maji kuingia huko ndani. Kwa nje hakuonekana kama kuna kapango kwa ndani. Kwa haraka usingependa kufika huko.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

{Nanaa alipagundua kwenye Simulizi ya Ni Wangu! Akiwa rafiki na kina Zena. Akataka kumpelekea Geb kwa mara ya kwanza, lakini Liz aliyekuwa mpenzi wa Geb kwa wakati ule, naye akafika nyumbani kwa Geb na kumchukua Geb wakiwa wanajiandaa kutoka na Nanaa. Nanaa akaachwa, Liz mwenye kisu kikali akaondoka na Geb. Akabaki ameumia sana.}

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

James akaenda kukaa pembeni yake. Wakatulia. Kimya, bado Jema yule wa asubuhi kabla ya kupewa taarifa za James kuwepo nyumbani kwa kina Magesa kila jumapili, hakuwa amerudi. Alipoa. James akamuona ni kama anasubiria muda, akijua baada ya muda mfupi sana, James ataondoka tu. Akamsukuma kidogo kwa bega. Jema akacheka na kumwangalia, macho yakagongana. “Mimi nataka uwe needy kwangu.” Jema akacheka taratibu na kuinama. “Umenisikia?” Jema akamwangalia. “Sitaki unichoke.” “Kwako sitachoka. Nigande utakavyo, na ukiona kitu hujakipenda, au unataka kifanyike tofauti na ninavyokwambia, nakupa ruksa yakutoa mapendekezo. Tutajadiliana. Na mimi naomba ruhusa ya kuwa huru kutoa mapendekezo kwako. Halafu tufikie maamuzi pamoja. Usikae ukinyongea kwa maamuzi ya upande mmoja, yaani yangu tu. Ukafikiri ndio nakuwa nimechora mstari. Mimi si mbishi sana japo ninakuwa na msimamo kwenye mambo fulani fulani. Hayo huwa najitahidi kusimamia bila kukubali kubadilika.” “Mambo gani?” Jema akauliza akitamani kujua.

“Nitakwambia wakati mwingine. Ila nataka kujua kama umeelewa hili.” “Nimeelewa. Na samahani James. Nilikuwa nimejiandaa kuwa na wewe leo siku nzima ndio maana niliishiwa nguvu uliponiambia huwa unaratiba ya jumapili. Nafikiri nilipanga nikidhania upo kama mimi tu. Huna mambo yakufanya siku za jumapili.” “Usijali. Kuanzia leo tuwe tunazungumza.” “Hapana. Usibadili ratiba zako kwa sababu yangu. Nitaliheshimu hilo. Na nitaacha kupanga mambo ya mbele kichwani mwangu nikikujumuisha na wewe.” “Hapo tena umeshaharibu.” Jema akaanza kucheka.

“Mimi nakusaidia James!” “Kwamba hujaelewa swala la kutaka WEWE uwe needy kwangu?” Jema alicheka sana. “Basi nitakuwa nikikushirikisha.” “Na niwepo kwenye hiyo mipango.” “Sasa huoni kama nitakuvurugia ratiba zako?” “Ndio alamu yakunitaka nianze kujipanga upya. Itabidi tutengeneze ratiba mpya.” “Nanaa na wengine waliopo kwenye maisha yako hawatanichukia?” “Itabidi waelewe tu. Ilimradi kusiwe na kubadilikana Jema. Sipendi drama za kijinga za mapenzi, kwa kuwa nishaona watu waliotilia umaanani kwenye mahusiano, na wakafanikiwa, naomba na kwetu iwe hivyo.” Ikamgusa sana Jema mpaka akatulia kwa muda.

Ilikuwa sentensi iliyojaa maana kubwa, na James akaiongea kama Jema alishafahamu wapo kwenye mahusiano. “Umenielewa Jema?” “Hapana. Kwamba unaanzisha mahusiano ya kimapenzi na mimi?” Hapo James akagundua ameongea lililokuwa likiendelea moyoni mwake. Akalitamka bila kufikiria. Akajilaumu amefanya haraka sana. Akatulia kabisa. Akahisi ameropoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Hakuwa hata amemtongoza! Akapoa kabisa na kukumbuka ushauri wa Geb. Asiropoke na awe makini na maneno yake. Jema akamuona amepoa haswa. Moyoni kwa James alishampitisha Jema. Jema kumganda kuanzia usiku uliopita. Wakati mzuri waliokuwa nao mpaka kulala usiku mwingi, kukamfanya James ajisikie wameshakuwa kwenye hiyo hali kwa muda mrefu na wameshakuwa kitu kimoja kwani kwa muda mfupi sana walishaendana kwenye mengi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Jema akatulia kabisa kumpa nafasi atafakari. Hata yeye hakutaka kucheza tena. Na hakutaka kupoteza muda akijipa tumaini ambalo halipo. Akatulia na kupotelea mawazoni. Wote kimya. Baada ya muda James akamsukuma tena taratibu kama kumtingisha. “Upo?” “Nipo.” James akabaki akimwangalia. Akacheka na kujiinamia. Akaokota jiwe dogo pembeni akaanza kuchora mchangani.

“Unakumbuka siku ya harusi ya Kumu?” Jema akamwangalia na kukunja uso kama ambaye anataka kujua anatakiwa akumbuke nini. “Nilikukuta sehemu peke yako kama uliyekuwa umejificha, umeshika simu ikawa kama umetoka kulia.” Jema akakumbuka. Akacheka taratibu na kuinama tena. “Nikakuuliza upo sawa! Ukafikiria kwa haraka na kunipa jibu la haraka kuwa katika vitoweo vya pale, ulipenda sana Crub. Ukaniambia hujawahi kula Crub waliotengenezwa vizuri kama wale. Ukaniambia unanishauri na mimi nikale, nisipitwe. Ukaondoka na kuniacha palepale nimesimama.” Jema akabaki kimya.

“Najua umekumbuka. Kwanza nataka kujua ulikuwa ukilia nini ndipo niendelee na ninachotaka kukwambia.”  Akamuona anajifuta machozi. “Ilikuwa ni nini Jema? Niambie tu.” “Nilikuwa nimetoka kuzungumza na Temu. Akanitukana sana. Ikaniuma sana, na ni kama sikujua chakufanya tena James. Kama na mimi kuomba, niliomba sana. Kama ni uaminifu kwa Mungu niliweka kwa asilimia zote. Nikabaki nikimsikiliza Temu jinsi anavyoweza kunitukana kirahisi tu bila hata huruma, nikiwa sijakosa! Sikuweza hata kumjibu, mpaka akamaliza na kunikatia simu. Nikabaki kumuuliza Mungu ni kipi cha tofauti mtu kama Naya amefanya mbele zake yeye Mungu, tofauti na mimi?” “Pole sana Jema. Kwa nini!?” Jema akajifuta machozi.

“Swali langu lipo na sehemu mbili. Japo moja ni kama nimeshapata jibu. Juu ya Naya. Ila ya pili ni kwa nini Temu akutukane siku kama ile!?” “Kwa upande wa Naya, ni vile Joshua alivyoweka uthamani kwake. James, Joshua anajua kumuenzi yule msichana! Sijawahi ona mimi hapa duniani. Na si kwa kujitahidi. Mimi nimefanya kazi na Joshua kwa karibu sana, nimemuona jinsi anavyokuwa linapofika swala la Naya. Anampenda kuliko nafsi yake. Na japokuwa Joshua Kumu yupo busy. Nikisema busy, amini yule mtu yupo busy. Lakini James, wakati wote anafikiria jinsi gani ya kumfurahisha Naya, lakini mimi natukanwa kama mpuuzi tu! Niliumia sana.

“Naomba usilie Jema. Na Temu?” “Temu ni mengi, lakini pia alikuwa akinitukana na kuniambia siku ile ndio siku nzuri kwangu, nipo huru. Najiuza mbele ya wasomi na wenye pesa nikijionyesha kama mwanamke,…” Jema akajaribu kufikiria neno sahihi. “Sijui niwekeje hili neno aliloniambia! Mpaka naona aibu.” James akamuona anatingisha kichwa kwa masikitiko. “Acha tu.” “Tafadhali niambie. Usinifiche tena. Maana nilikaa nikijiuliza na kuumia sana. Maana ulikuwa umependeza. Halafu ulijitoa Jema! Mpaka ukatushangaza.” Jema akacheka tu na kujifuta machozi.

“Kweli! Ulikuwa busy sana siku ile ukashindwa hata kukaa!” “Wewe ulijuaje?” “Kwa sababu nilikuwa nikikufuatilia!” Jema akamwangalia na kuinama kuendelea kuchora. “Baada ya harusi tulibaki mimi, Kumu, familia ya Geb. Mama yake na Nana. Pamoja na baba yake Nanaa, tukiweka tathimini ya mwisho na kutaka majina ya waliohusika kufanikisha shuguli nzima siku ile tutume kadi za shukurani na zawadi kidogo. Geb akauliza wewe ulikuwa kamati gani? Ndipo Kumu akasema hakutaka kukupa kazi maalumu akitaka macho yako yawe kila mahali ndipo akasema ile sifa yako na nyingine. Kuwa, ‘Jema hawezi kukubali jambo limuharibikie mbele ya macho yake’. Na ndipo aliposema, ‘ni wale wanawake ambao ukiwapa mahindi kwa ajili ya chakula, ujue utakuja kukutana na shamba la kuvuna’. Ndio maana alikutaka wewe uwepo pale uangalie kila kitu akiwa na uhakika hapata haribika jambo hata moja. Na wote pale tukaafikiana ni kweli ulifanya zaidi ya kawaida. Kumu akasema yeye hashangai, ndio maana yeye asipokuwepo sehemu anayotakiwa kuwepo, hana wasiwasi kama wewe upo.” Jema akacheka taratibu.

“Lakini ukumbuke hapo sisi tulishafahamiana ila kikazi. Na wakati wote ulijibeba kwangu kikazi tu. Kama nilivyokwambia, hata salamu yako kwangu ilikuwa ikionyesha ni kiungo cha mazungumzo ya muhimu. Unakuwa ukija ofisini kwangu upo na muda mfupi na agenda nzito uliyoambiwa na yule sekretari mimi naweza kukusaidia kwa kuwa nafahamiana na wale wahusika wa pale kwa karibu.” Jema akacheka.

“Yeye ndiye aliyeniibia siri kuwa nikitaka chochote kwa wale watu wa Utawala, nikwambie wewe. Nikamuuliza mbona wewe upo kwenye mambo ya simu huusiki na maswala ya Utawala? Akasema anauhakika na anachoniambia, nije kwako, utanisaidia. Ndipo nikaja kujitambulisha kwako. Nikashangaa mmeishia kuwa karibu na Kumu, mimi nikawekwa pembeni!” James akacheka sana.

“Halafu bwana sijui ilikuaje na Kumu! Na yeye tukajishangaa kama tumeshakuwa ndugu! Kuja kukutana na Geb na Nanaa, akataka nimtambulishe kwao, ndipo undugu ukanoga. Akafanyika mmoja wa familia. Tukajikuta ni ndugu tunaoendana kwenye mengi. Ila ni nini nataka kukwambia?” Jema akatulia kumsikiliza.

“Sijakurupuka kwako, ila sikujua ni jinsi gani ya kukufikia. Nilishavutiwa na wewe mwenyewe. Nikaja kuzisikia sifa zako. Nikajiambia mbona huyu ni kama ananihusu! Ila nikaja kusikia tena upo kwenye mahusiano yanayotarajiwa kuwa ndoa. Basi nikapoa. Ndio maana uliponikaribisha chakula, nikawa kama nimekwama tena. Nikijiuliza huyu mchumba wa mtu tena vipi! Halafu Jema ninayemfahamu mimi si nje ya kazi! Halafu tena ikawa natakiwa nikacheze game kwa kina Magesa, ndipo ikabidi nitulie nikusome vizuri kujua ukaribisho ule ulikuwa upi. Ulipokataa kwa maneno lakini moyo wako ukazungumza kingine kama leo pale kanisani.” Jema alicheka mpaka akainama kujificha.

“Mimi nilikuwa namaanisha James.” “Ila moyo wako ulizungumza vingine nikazidi kuvutiwa na kukupenda zaidi.” Hapo Jema akaacha kucheka kabisa. Akabaki kimya ameinama kisha akamwangalia. “Sijakurupuka Jema. Pata muda na wewe unichunguze ujue kama na mimi ni mtu unaweza kuja kuishi naye. Ukipata jibu, basi tuendelee kuanzia hapo. Ila kwa sasa naomba tuwe wote kwenye mahusiano. Na kujibu swali la kwanza ambalo uliliuliza, naomba yawe ya kimapenzi. Kwamba kusiwe na mchumba Temu tena.” Jema akacheka.

“Yaani huyo samehe. Na pesa ulizompa iwe ndio sahau ili tuweze kuendelea mimi na wewe tu. Au sina vigezo vya kuwa mume? Maana mimi nilikuwa nikikufuatilia kwa sababu niliona unavyo vigezo vya mke wangu.” Jema kimya. “Eti Jema?” “Nikwambie ukweli James?” “Hilo nitalifurahia sana. Kusiwe na usiri, vificho na kudanganyana kati yetu.” “Sawa. Ila nataka ujue huwa napata amani na utulivu sana nikiwa na wewe ndio maana natamani kuwa karibu yako tu. Natulia mpaka nafsini mwangu. Nakuona una hekima yakunifaa mimi.” James akacheka taratibu.

“Kweli.” “Basi tujipe muda tuone hizi hisia zitatupeleka kwenye hatua ipi ya maisha. Ni sawa?” “Sawa. Mimi nitatulia James. Nishang’atwa na nyoka! Sitaki tena.” “Kumbe bora alipita Temu hapo ili kukushikisha adabu!” Jema alicheka sana. Angalau wakafunguka na kufurahia mwanzo wao mpya. Walishitukia giza linawafuata hapo. Ikabidi kuondoka baada ya kupiga picha nyingi sana siku hiyo.

Kwa Bale.

Usiku wakati amerudi nyumbani anaingia ndani, akamuona tena Malon ni kama anatoka chumba anacholala yeye, akielekea kilichokuwa chumba chake. Bale alishituka sana ila akajikaza na kukimbilia kwenye hicho chumba alichomuona akiingia. Akakuta hata mlango umefungwa, tena alifunga yeye mwenyewe Bale. Akaanza kusukumana na mlango akisema Malon amemfungia kwa ndani. Hata akili yakusema atumie funguo afungue hakuipata. Akasukumana na mlango akipiga mateke mpaka mlinzi akaingia akidhani kuna tatizo. “Kuna nini bosi?” “Hataki kufungua mlango.” Mlinzi akasogea. “Nani?” “Wewe saidia, acha kuuliza ujinga.” Basi mlinzi naye akaongeza nguvu mpaka wakafanikiwa kuvunja mlango. Akakimbilia mpaka humo ndani chooni na bafuni, hapakuwa na mtu. Mlinzi akashangaa sana. Akahisi amezidisha bangi maana alivuta sana siku hiyo.

“Hakika nimemuona ameingia humu ndani.” “Nashauri upate muda wa usingizi bosi. Kukiwa na tatizo nitarudi.” Akatoka na kumuacha Bale na sintofahamu kubwa sana. “Huwezi kunivizia na kuniua mimi.” Akaongea kibabe akimwambia Malon endapo amejificha mahali. Alipojaribu kusogea, kumbe ameumiza mguu. Akajikaza  na kujivuta mpaka sebuleni. Bangi ikamsaidia kulala vizuri.

“Usijekuwa unatoka kutafuta ulichokiacha ndani ambacho wenzako wanakililia na kukihangaikia huko nje unakokimbilia.” Bale alishituka sana kwani kwa hakika alimsikia baba yake akiongea masikioni kwake tena kwa sauti iliyoweza kusikika kwa wazi kabisa. Akakaa akihema kwani ndio alikuwa amepitiwa na usingizi mzito, kwa kutolala usiku uliopita. Akakumbuka kuambiwa maneno kama yale. Kumbukumbu ikakataa kumkumbusha msemaji kwa hakika. “Haya maneneno aliniambia Naya, au baba!?” Akabaki akijiuliza kwa sauti, akihema kwa nguvu.

Akataka atoke hapo aende kunywa maji. Akagundua mguu unamaumivu makali sana, na ni kama umejaa. Akajishika akajisikia maumivu. Akachechemea mpaka alipoweza kupata ganja, akapuliza hapo usiku kuchwa akishindwa kulala kwa hofu. Akamkumbuka mama yake. Bale akaanza kulia peke yake. Akatamani kama mama yake angekua hai. Akakaa hapo kochini akishindwa hata kusogea. Alipotaka kwenda chooni ikabidi kutambaa kwa magoti kwani mguu ulikataa kabisa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Malon mtoto wa Mjini. Kweli alikufa au yu hai anacheza na akili za Bale tu.

Au

Bangi inasaidia dhamira kutengeneza uhalisia kwa Bale?

Inaendelea….

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment