Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Mapenzi & Pesa! - PART 1 - SEHEMU YA 39 - Naomi Simulizi

Mapenzi & Pesa! - PART 1 - SEHEMU YA 39

 Kikomo.

KISASI KWA MALON.

Bale alitoka pale, akarudi Kunduchi nyumbani kwa Malon, akaambiwa ameingia hapo muda si mrefu. Akazidi kuumia kwamba ni kweli ametoka jela. Akaingia ndani bila kutaka fujo naye. Akamkuta ametoka kuoga. Wakazungumza maswala ya biashara tu. Wala hakumzungumzia Naya kabisa, ndipo Bale akajua bado anamipango na Naya, hataki amuingilie tena. Na yeye hakumtaja kabisa dada yake. Akampa majukumu yakufanya hapo Dar, Bale akatoka hapo, akamuacha akipumzika. Mipango yakumtoa Dar, na kumfanya Malon arudi Mbeya ikaanza.

Akazungumza na Mbaki aondoke pale anapoachwa kama mlinzi wa mali yote kwenye mji wa Malon huko Mbeya kwa kumwambia Malon kuwa amepatwa nadharula, lazima aondoke ili Malon mwenyewe arudi. Bale akamlipa pesa nzuri sana, akijua Malon hamuamini mtu yeyote na pale isipokuwa Mbaki tu, kwa hiyo lazima atarudi kwa haraka sana. Na kweli. Wakati anarudi nyumbani Kunduchi, Malon akawa anamuga kuwa lazima arudi Mbeya kwa haraka, Mbaki amepatwa dharula. Hilo likamfurahisha Bale.

Malon anatoka tu Dar, Bale naye akamfuata nyuma baada ya kama masaa mawili tu akihofia asije akamchelewa, akaweka mambo sawa huko Mbeya kwa haraka, na kurudi tena Dar kwa Naya. Bale aliendesha mpaka alipofika Mbeya mjini. Akanunua petroli nyingi, madumu mengi yakutosha, ndipo safari ya kuelekea kwenye mji wa Malon ikaanza tena akiwa ameshajipanga vizuri tu.

Mida anafika kwenye mji wa Malon, alijua kwa hakika Malon atakuwa na yeye amefika na amelala kwa uchovu wa rumande. Hakutaka hata papambazuke. Gari aliyokuja nayo mida hiyo, ambayo nayo ni ya Malon aliyokuwa akitumia Bale kwa shuguli zake binafsi na anazotumwa na Malon akaegesha mbali kidogo ili Malon asimsikie akija hapo na pia kumsaidia kukimbia baada ya kufanya yake.

 Akaenda moja kwa moja mpaka sehemu lilipo ghala lake. Sasa kwa kuwa mbwa walishamjua Bale, na akawa amewaletea nyama aliyokwisha tia sumu, walipomuona, hawakupiga kelele kabisa wakati anaingia hapo. Akawapa ile nyama yenye sumu, wakafa wakati akibebelea madumu ya petrol na kumwaga kuzunguka ghala nzima la Malon. Kisha kuzunguka kijijumba chote alicholala Malon na mlangoni pia.

Akafunga komeo taratibu analopenda sana kutumia Malon kila anapotoka hapo na kuweka na kufuli ili mtu asiingie kwenye hicho chumba chake endapo hayupo. Akiwa ndani kufuli huwa nalo ndani. Sasa Bale akalirudishia hilo komeo na kufuli ambalo alishanunua wakati akinunua hiyo petroli. Tena akarudiarudia kumwaga petroli nyingi kuzunguka hiyo nyumba mpaka akaridhika.

Wakati Malon yupo kwenye usingizi mzito, uchovu wakulala rumande na kuendesha safari ndefu, Dar mpaka Mbeya bila kupumzika, akasikia mtu anamgongea dirishani. “Malon! Malon!” Bale akawa anamuita. “Nini?” Malon akaitika akisikika alikuwa usingizini. “Usiku huu wa leo, nakulipiza kwa kumuua baba yangu kikatili. Ulichomfanyia Zayon kiumbe asiye na hatia, bibi na Luka. Usiku wa leo, utaonja kile walichoonja wao. Nakwambia, ili wakati ukiteketea hapo ndani kwa moto, jua Bale AMEKULIPIZA.” “Unaongea nini wewe!?” “Na bila wewe kuondoka hapa duniani, Naya na mimi wote tutakuwa watumwa wako milele.” Bale akaendelea.

“Sasa, sasahivi nasimama nafasi ya baba, kumtetea Naya. Hii dunia itakuwa salama sana bila wewe Malon.” “Acha upuuzi  wewe.” “Kama unafikiri ni upuuzi vuta harufu uniambie kama hupati harufu ya petroli! Eneo lako zima, mpaka ndani ya dirisha hapo ulipo nimemwagia petroli. Nikitupia njiti moja tu ya kiberiti, wewe na mali zako zote ni jivu. Angalia mafuta hapo dirishani.” Malon akakurupuka kwa haraka na kusogelea dirishani akagusa kwa kidole, pamoja na harufu, ndipo akajua Bale hatanii. Akakimbilia mlangoni. Ukakataa kufunguka. Akajua Bale amemfungia kwa nje.

“Naweza kukufungulia endapo utaniambia ukweli ni kwa nini Naya amegeuka kuwa tahira. Asiye na kumbukumbu.” “Nifungulie nikwambie.” “Unanipotezea muda Malon na ujue unawajibika na kilio cha mama yako. Wewe unafikiri kutokuwepo kwa Mbaki leo ni bahati mbaya? Nilimtoa hapa kusudi ili nikuweke shule wewe uliyekimbia shule na kudharau waliosoma.” Malon akarudi tena kusukuma malango kwa nguvu tena na tena mpaka akachoka.

“Kama umemaliza naomba tuendelee. Na safari hii nakupa dakika moja tu Malon. Niambie ukweli lasivyo nawasha moto.” “Sawa. Naya alianguka akagongesha kichwa kwa nguvu, mpaka anakuja kuamka akawa hajitambui tena.” “Hapo nimeshaelewa kuwa ulimgongesha dada yangu kichwa kwa nguvu. Haya, dawa gani ulimpa? Na usiniambie ni za usingizi maana amepimwa, akaonekana ni madawa ya kulevya ila hayajulikani ni yapi.” “Nilikuwa nikichanganya tatu ili kuingia mwilini mwake na kuzoea damu yake kwa haraka.” Akamtajia. Bale akaumia sana.

“Aisee wewe ni mshenzi Malon! Na ni kina nani uliwatumia kuua familia yangu?” Akiwa amejawa hofu kubwa, akitambua umbali aliopo na walipokuwepo wanakijiji ambao wanaweza kumuokoa, Malon akawataja mpaka sehemu anayoweza kuwapata. “Nirushie simu zako zote nje kwa kupitia dirishani ili kuwatafuta. Nikiwapigia kwa simu yako, watapokea kwa haraka.” Malon akiwa amepaniki akijua na bangi za Bale zimeshawaka kichwani, hatashindwa kumchoma kweli endapo akikaidi, akatoa simu zote huku akikwepa yale mafuta pale dirishani.

“Sasa leo hukumu yako ya hapa duniani imefika. Leo nakuhukumu, sitakusamahe. Naanza kukuchoma moto wewe ndio ghala na shamba lako. Sitaondoka hapa mpaka nihakikishe umeteketea Malon. Nitashibisha masikio yangu kwa kilio chako ndipo niridhike, mshenzi wewe. Teketea ukijua Naya yupo kwa Joshua na ametulia, na mimi nakwenda kuchukua pesa zako zote.” Akawasha moto dirishani na mlangoni kwake. Malon akaanza kupiga kelele kwa hofu akimsihi Bale amsaidie na kumsamehe.

Bale hakumjibu kitu akawahi kuwasha na kule galani kisha akatupia moto mwingine shambani kwake kwa haraka ili wanakijiji ambao ni kweli walikuwa wakiishi mbali sana na eneo alilonunua Malon wasije wakaja kumuokoa. Ila alifarijika kadiri alipokuwa akimsikia Malon akiteketea kwa uchungu sana. Wakati huo alishakuwa amerudisha yale madumu ya mafuta yote kwenye gari. Akakumbuka maneno ya Nanaa kwamba wamejua kwao kumechomwa moto kwa makusudi sababu ya ushahidi wa chupa iliyookotwa yenye petroli. Bale hakutaka ushahidi. Akamsikia Malon akipiga kelele kwa maumivu makali sana kama anayeteketea. Akajua hata wanakijiji wakitokea wakati huo wakazima moto, hatapona. Akaridhika hivyo na kuondoka hapo kwa haraka sana. Usiku huohuo akaondoka mjini Mbeya kurudi Dar.  

Huko Jijini.

Bale alirudi Dar, palepale nyumbani kwa Malon, Kunduchi, akalala kama hakuna alilofanya. Alipoamka, akampigia simu Joshua na kumwambia anajua jinsi ya kuwapata moja kwa moja waliochoma familia yake. Akampa wazo arudi kwa anayehusika na kesi yao, atafute wale walinzi wa usiku ule, kisha wahojiwe. Akamuahidi kumfanikishia kukamatwa kwa watuhumiwa wenyewe pindi atakapopata ukiri kutoka kwa walinzi walio linda nyumbani kwao usiku ule palipoungua moto na kusababisha kifo cha ndugu zake Kiluvya.

Wakati Joshua anafufua kesi ya kina baba Naya akiwa na ujasiri wote kwa kuwa safari hii ana ushahidi wa kutosha, huku Bale akawa anajinufaisha. Kwa kuwa alimjua Malon  ni mtu wa peke yake. Hakuna hata ndugu au rafiki anayejua mali zake au hakuwahi kumkaribisha yeyote kujua mambo yake zaidi mali. Hata nyumbani kwao hakuna hata mmoja aliyemjua Malon na anachomiliki kwa hakika isipokuwa kuwapa tu msaada. Alijua hata wakifanikiwa kujua Malon amekufa, haitakuwa kwa haraka labda yeye ndio awapelekee taarifa za kifo chake kwa kuwa alikuwa na simu za Malon, alijua akitaka, anaweza kupata namba za wazazi wake kupitia simu hizo. Hakufahamiana na wazazi wa Malon na hakupajua kwao Morogoro. Naya ambaye anamfahamu mpaka kwao, ndiye amemgeuza tahira. Bale akajiambia hata kama wakijua Malon amekufa, hakuna anayejua mali zake. Kwahiyo zimeshakuwa zake.

Bale akaanza kujichotea pesa za Malon akiwa amelala nyumbani kwa Malon. Akajihamishia pesa yote mpaka akaridhika. Akachukua namba za simu za muhimu alizojua sitamsaidia kwa kuendeleza baadhi ya biashara za Malon, kisha akazitupa zile simu chooni kabisa kupoteza ushahidi. Akahamia kuhamisha pesa za Malon benki kwa haraka kabla benki hawajapata taarifa za kifo chake na kufunga hizo akaunti. Na kwa kuwa akaunti yake ya biashara na yeye Bale alikuwa akijua ilipo kwa kuwa alikuwa akienda kumuwekea pesa huko na alikuwa akimtuma hata kuchukua, Malon alishamtambulisha hata kwa wahudumu wa benki ili awe anahudumiwa kwa haraka. Bale akaanza yake mapema siku hiyo bila hofu ya kukamatwa.

Kwa Joshua.

Wale walinzi wakafikishwa kituo cha polisi, mahojiano yakaanza upya. Ikajulikana kumbe yuleyule aliyepiga simu kwa Magesa kutoa taarifa kuwa Kiluvya kumeteketea moto ndiye aliyefanya mipango na Malon, hata walipoingia kulala, yeye ndiye aliyempigia simu Malon kama alivyomuomba. Akawaambia baba Naya alishaingia ndani, na amefunga mlango. Akakiri hajui ni kwa nini alitaka hiyo taarifa ila kwa kuambiwa na kuthibitishiwa na Malon mwenyewe, alijua Malon ni kama mtoto wa pale.

Alipoambiwa ilikuwa ni njama ya kuwachoma moto, yule mlinzi akaonekana kwa hakika hakuwa akijua hilo. “Hakuniambia ni kwa nini anataka nimwambie pale mzee atakapoingia na kufunga mlango. Sikujua kama atafanya ukatili kwa mzee mwema kama yule!” Mlinzi akakiri kwa uchungu akiwa ameshapigwa na kuteswa sana. Ndipo Joshua akampigia simu Bale kumwambia pale polisi walipofikia, na yeye akamwambia afike kwenye baa fulani maeneo ya Mbezi ya Kibamba. Akiwa na askari kanzu. 

“Sasa nyinyi muwahi kabla yangu. Mkae kwenye meza, mimi nikifika tu nitawapigia wafike pale. Nikiwaona nitajitahidi tukae kwenye meza karibu na nyinyi ili msikie mazungumzo yetu, na mimi nitawarikodi wakati nikifanya nao mazungumzo. Nitawadanganya kuwa nimepata kazi ingine kama ile waliyomfanyia Malon, na nitawadanganya kwamba mimi nitawalipa zaidi. Wakishakiri tu kuhusika, ndipo hao askari wasogee mezani kwetu wawakamate.” Bale akaongea na Joshua akisikika amejipanga vizuri.

“Sawa Bale. Lakini kabla hatujaagana, maana najua tunaweza tusizungumze tena. Naomba nikwambie kitu na nikushauri. Nisikilize tu, huna haja yakutendea kazi ninachotaka kukwambia ila naomba unisikilize. Cha kwanza, sina haja ya kuchukua kiwanja chenu Kiluvya, wala Naya hana shida nacho. Kwa msaada wa GM tunavyo viwanja vingi sana tu na vyote nimeviendeleza. Lakini sitakupa kiwanja cha Kiluvya, kwa sababu ni kitu alichotaka baba yenu. Ila GM anaweza kukusaidia kupata kiwanja kizuri na sehemu nzuri tu.” “Sina shida.” Akajibu Bale kwa jeuri.

“Sawa. Kingine na cha mwisho, ulipofika sasa hivi hujachelewa kurudi. Umebaki wewe tu kama ndugu yake Naya. Na anakuhitaji.” “Ananihitaji vipi na hanijui?” “Naya atakuja kupona. Na akipona atahitaji kukuona Bale. Viko vituo vingi tu vinaweza kukusaidia kutoa hiyo sumu ya madawa mwilini mwako na kuacha akili yako ikaweza kufanya kazi vizuri.” “Kwamba unafikiri mimi sina akili?” Bale akauliza kwa ukali.

“Unajua simaanishi hivyo Bale. Lakini kumbuka maisha na maamuzi ya Malon. Kuna umbali amefika Malon, anafanya mambo si ya kawaida lakini ni kwa sababu ya kutumia bangi kwa muda mrefu mpaka kumuharibu akili. Tafadhali usiruhusu ufike huko Bale. Unayo maisha marefu sana mbeleni.” “Cha kwanza Malon si tatizo tena. Nilikwambia nitamdhibiti, ujue nimemdhibiti milele.” Joshua akashituka sana.

“Umefanya nini Bale!?” Joshua akamuuliza kwa tahadhari. “Alicho mfanya baba yangu, Zayoni, bibi na Luka ndicho na mimi nilichomfanya.” Joshua akahisi mwili kuishiwa nguvu. “Hakuna wakumsogelea tena Naya. Lakini nataka kumalizana na watuhumiwa hao wa mwisho ambao wao naacha vyombo vya sheria viwashugulikie. Nikiona hawawafanyi kitu, nitawahukumu mimi mwenyewe. Sasa na wewe usichelewe pale baa na hao askari kanzu. Na leo nakwenda kumalizia deni la Magesa. Nataka na wewe ujue kuwa baba hatakuwa akidaiwa tena, kachukue hati kwa Magesa, muhifadhie Naya.” Simu ikakatwa. Joshua akabaki akiangalia simu yake akimtafakari shemeji aliyebakishiwa naye hapa duniani.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Joshua akampigia simu Geb. Akamsimulia kila kitu alichozungumza na Bale. “Daah! Hivi utafanyaje Joshua?” “Aisee sijui! Lakini kwani wewe umesikia taarifa zozote juu ya moto ulioteketeza huko Mbeya?” “Bado.” Wakatulia kwenye simu wanaume hao hawajui waseme nini. “Daah!” Akasikika Joshua. “Lakini kwa upande fulani yupo sahihi.” “Juu ya nini?” “Utapumzika. Angalau utakuwa na uhakika kuwa Naya yupo salama.” “Japokuwa hatujathibitisha, ila njia aliyotumia si sahihi! Kuua si kitu kirahisi. Hatabakia salama. Itamsumbua tu.” “Na kweli. Si unakumbuka hata na kauli ya Mbabe?” “Bora kufuatwa na pesa kuliko damu ya mtu?” Akauliza Joshua. “Sawasawa.” “Ndio ninachokwambia GM, hawezi kubakia salama hata iweje. Itamsumbua tu. Lakini sina chakufanya. Anaonekana amekusudia kabisa kuniweka mbali na maisha yake. Na mimi nitamuacha kabisa.” Nanaa akaingia ofisini kwa mume wake akajua anazungumza na Joshua.

“Joshua?” “Nipo.” “Tafadhali naomba zungumza na mke wangu.” Joshua akawa ameshaelewa, akasita akiwa ameelewa nia yake. Akabaki kimya. “Msikilize tu tafadhali. Amekua akitafuta jinsi ya kukufikia, naona inamuathiri na kumnyima raha. Nakukabidhi.” Nanaa akachukua simu. “Umenichukia sana Joshua?” Nanaa akauliza kwa upole. “Hapana Nanaa, ila niliingiwa hofu.” “Nikiomba tena msamaha itasaidia?” “Sisi ni ndugu Nanaa. Hilo haliwezi kubadilika, ila naomba kwa sasa nimfungie tu Naya. Tafadhali sana. Na mama nitamwambia. Mpaka angalau aweze kujitambua. Bado hayupo tayari kukabiliana na mambo haya yanayoonekana ni madogo madogo tu kwa wengine. Kwake bado kabisa. Ukikaa naye na ukawa huna kitu kingine cha kufanya ukaweka mawazo yake kwake tu, utagundua bado. Anahitaji muda. Acha nimsaidie kwa namna hiyo.”

“Nimekuelewa Joshua. Na tunaomba msamaha kwa kuzembea. Ila ujue tunawapenda. Mtakapokuwa tayari na sisi, mjue milango ipo wazi muda na wakati wowote. Na mtakapo tuhitaji wakati wowote, tafadhali msisite.” “Hilo najua. Na hata usingesema sasahivi, bado najua nyinyi ni ndugu zetu wa kwanza na wakaribu. Na nilipanga kukutafuta kukuomba unisaidie mtu wa kumtengeneza nywele, lakini iwe nyumbani. Hataki kutoka kabisa.” Hilo kidogo likamfurahisha Nanaa.

“Ninao wasusi wanaokuja nyumbani kwa ajili ya kumsuka binti Magesa. Anampenda kwa kuwa anasema hamvuti nywele. Naona huyo atamfaa na yeye Naya. Basi mkiwa tayari mniambie aletwe.” “Hapo utakuwa umenisaidia sana. Nakushukuru sanaaa.” Kidogo wakacheka ndipo wakaagana. Na kumrudisha kwa Geb.

“Nashukuru Joshua. Na kama alivyosema Nanaa. Utusamehe sana. Kilikuwa kitendo cha muda mfupi!” “Usijali GM. Malon alikuwa hatua moja mbele. Hata walinzi hapa kwangu nilibadilisha. Tafadhali mwambie na mama asijilaumu.” “Kama utaweza, atajisikia vizuri kusikia kutoka kwako mwenyewe.” “Basi nitampigia. Acha nikamtendee haki baba Naya. Sijui kwa nini Geb, moyo wangu hautatulia mpaka nihakikishe haki kwa yule mzee imetendeka. Walimtenda vibaya pasipo sababu bwana!” “Ni kweli. Wamemwaga damu za watu wasio na hatia! Mungu aingilie kati.” Wakazungumza kidogo na kuagana.

 Bale.

Kweli Bale akafanikisha kumalizia deni la kina Magesa lote hata kabla ya kwenda kukamata hao vijana walioshirikiana na Malon kufanya uhalifu nyumbani kwao. Akaondoka ofisini kwa kina Magesa bila nyongeza wala kuulizia hati. Na wenyewe wakamuacha kabisa, wala hawakumuongelesha. Akatoka hapo akielekea kukamata waliohusika na kifo cha familia yake.

Na Joshua naye hakuzembea. Alihakikisha anapata hao askari kanzu na kwenda nao walipokubaliana na Bale na wakafanya kama alivyosema Bale. Walipokiri tu kuwa walipokea malipo mazuri kutoka kwa Malon na wanaweza kumfanyia kazi nzuri zaidi endapo atawalipa vizuri, ndipo wakatiwa nguvuni.

Kazini.

Huku kazini sababu ya mambo ya kifamilia, hata utendaji kazi wake Joshua ulibadilika sana. Jema ndiye akawa mtu wa kumsaidia Joshua kupita anavyotakiwa, akiendesha mambo kama Joshua mwenyewe. Kila wakati alikuwa akijiuliza kama Joshua mwenyewe angekuwepo, angefanya nini au angechukua hatua gani. Akafanyika kama malaika aliyetumwa na Mungu kwa wakati huo ili kumsaidia, mpaka akamshangaza Joshua mwenyewe. Bado pengo la Njama halikuwa limezibwa, kwa hiyo alifanya kazi zao zote bila kuchoka wala kulalamika, hilo nalo likamgusa Joshua zaidi.

Mkataba wa Coca na kwenye jengo wanalofanyia kazi kina James uliisha, walitakiwa kusaini tena. Hilo Jema akalikumbuka. Akachapisha mkataba mpya lakini unaofanana na wa kwanza. Akampa mwanasheria wa kampuni yao. Akaupitia kama mwanzoni na kuusaini. Jema akampa dereva aupeleke kwenye ofisi husika kwenye hilo jengo. Sekretari akawa akifahamiana na Jema. Alishampigia simu na kumuomba apokee. Kwa hiyo alishajua dereva anapeleka hizo nyaraka. Alipofikisha akapokea na kupeleka kwa muhusika.

Mida ya saa kumi kama na nusu jioni Jema akiwa busy sana, akapokea ujumbe kuwa ipo tayari. Akajua kumtuma dereva kwenda kufuata, itakuwa si sawa maana ndio karibu na mida yake ya kutoka. Akamtumia ujumbe James. ‘Samahani bosi, inawezekana ni matumizi mabaya ya namba yako binafsi, lakini nimebanwa sana, na mkataba wetu upo tayari hapo kwenye ofisi za hilo jengo. Niombe kama utakuwa na muda unichukulie halafu nitakuja kuupitia hapo ofisini kwako.’ Hapohapo akajibu. ‘Sawa.’ Mpaka akamshangaza Jema. “Kwamba alikuwa na simu mkononi!” Jema akajiuliza na kushangazwa. Ila akapata aghueni maana alijua angechanganya ratiba na hilo lisingemfurahisha Kumu.

‘Nashukuru Bosi. Nitajitahidi kabla ya saa 12 niwe nimefika hapo, ili nisikuweke sana.’ ‘Haina shida.’ James akarudisha huo ujumbe kwa haraka. Jema akacheka na kurudisha simu mezani akimtafakari James na kupotelea mawazoni.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Alipomalizana na shuguli za kiofisi na kumtumia Joshua ripoti ya siku na kupata ujumbe wa ‘You are the BEST.’ Akajua amemfurahisha. Akatoka kwa haraka kwenda ofisini kwa James, hakuwa amemuona kwa muda mrefu tokea kwenye harusi ya Naya na Joshua. James alibadilika haswa. Alifuga ndevu na Geb ndiye aliyemwambia. “Acha kuweka muonekano kama kina Magesa bwana! Au unataka kuwa na baby face mpaka uzeeni? Nobody will take you serious.” “Unamaanisha wanawake?” “Namaanisha acha kunyoa ndefu zote. Weka sura ya kiume.” Geb akamalizia hivyo. James akacheka na kuondoka. Ila kikamuingia na kuanza kutengeneza ndevu mpaka zikapata muonekano wakueleweka ndipo akapeleka saluni na kuchongwa vizuri. Kweli akapendeza.

Sasa siku hiyo Jema kumuona, akababaika mpaka akamshangaza James asielewe anababaishwa na nini, asikumbuke jinsi alivyojibadilisha. “Haina shida kabisa. Tena ameniletea hapahapa wala sikuifuata. Kwa hiyo haikuwa usumbufu hata kidogo. Karibu, muda na wakati wowote.” “Umekula?” Hilo swali likamfanya James atulie na kubaki akimwangalia. Nakuzidi kumbabaisha Jema. Akaanza kujitetea. “Ni kama malipizi tu na shukurani kwa ulichonifanyia. Nikutoe kwa chakula cha jioni. Kama ungependa lakini.” “Nashukuru lakini kuna mahali nakwenda baada ya hapa.” Jema akajisikia vibaya, ujasiri wote ukamuisha na uchangamfu usoni ukapotea.

Akahisi amejitongozesha kwa James na amemdharau. “Sikuwa na nia mbaya. Ingekuwa ni chakula tu. Kwa kuwa na mimi mwenyewe sijala kwa muda mrefu, nikajua isingekuwa tatizo kwenda kula pamoja. Lakini si kwa nia mbaya. Na unisamehe kama nimevuka mpaka.” “Haina shida kabisa. Ila ni vile nina miahadi sehemu.” Jema akaangalia ile bahasha mkononi. Akatoa tabasamu la kunyongonyea. “Nashukuru James, na jioni njema.” Akatoka bila hata kusubiri nyongeza na wala hakumwangalia tena. James akatafakari na kuangalia saa, akatoka kuwahi kwa kina Magesa ndiko alikokuwa na miahadi.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Alipofika na kukuta gari ya Geb nje akamtumia ujumbe. ‘Toka nje bila ya kumwambia mtu. Kuna kitu nataka nikuulize.’ Geb akasoma ujumbe. Akasubiria kidogo na kutoka. “Vipi?” James akasita kidogo. “Nini wewe? Kwanza shuka kwenye gari watoto wote wanakusubiria wewe ili wakufunge ndipo wakalale.” “Subiri kwanza Geb.” Geb akatulia akimtizama. Akashuka garini. Na kubaki amesimama.

“Wewe vipi!?” “Mbona huna subira Geb bwana?” “Umenitoa katikati ya game, James. Na nilikuwa nakaribia kumshinda tena Magesa.” “Acha kushindana na mtoto Geb! Wewe unajisikia raha akilia?” “Wewe cheza nao unavyojisikia, na mimi nacheza nao ninavyojisikia. Siwezi kumuachia anifunge eti sababu ni mtoto! Sitakuwa nao huko duniani wakati wakikumbana na changamoto.” “Hata mara moja moja tu bwana?” “Basi ndio maana wanakusubiria wewe huko ndani. Wewe nenda kawaachie wakufunge. Mimi nacheza kwa haki. Wajifunze kukabiliana na changamoto.” James akacheka na kutingisha kichwa kwa masikitiko.

Kila Magesa akicheza na baba yake, lazima ataishia kulia tu. Maana Geb anahakikisha anamfunga. Ila walimpenda James alikuwa akiwaachia wamfunge. Basi Nanaa akiona wanae wanalia na Geb anazidi kuwafunga, anamtoa Geb kwenye mchezo na kumuomba kaka yake aje acheze nao ilimradi wamfunge, zaidi Magesa afurahie.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

“Inaweza kuwa si kitu.” Akaanza James akijihami. “Lakini unachukuliaje mtu akikuambia mtoke naye kwa chakula cha jioni?” “Inategemea na mazingira.” “Acha bwana kunijibu kama unaongea na mtu mwenye kichwa kama chako.” Geb akaanza kucheka. “Labda uongeze maelezo.” “Labda tuache tu.” Geb akatulia akijua yeye mwenyewe hawezi kuacha. Kuna linalomsumbua. Akaenda hatua chache kama anayeingia ndani, lakini akarudi palepale akakuta Geb amesimama palepale kama aliyejua atarudi tu.

“Kwa mfano ukamkatalia halafu akaonekana ameumia kidogo?” “Nisikilize James. Mimi na wewe tunajua kabisa huyo sio mwanamke wa kwanza kukukaribisha chakula…” “Ni..” “Subiri James. Kwa mara ya kwanza unaonekana umepata mtu anayeanza kuleta maana kwako ndio maana upo kama ulivyo.” “Mimi..” “Subiri kwanza James!” “Sasa unacheka nini Geb?” “Nimefurahi hatimaye na wewe unapita tulikopita na sisi. Maana ulikuwa ukiishi kama huna hisia bwana! Halafu wenzako tukaonekana kama wanaume dhaifu!” “Mimi sijasema nina hisia kwake.” James akabisha.

“Hivyo ulivyo. Maswali uliyo nayo juu ya mlichozungumza na kutoridhika juu ya hali uliyomuacha nayo, hizo ndizo hisia zenyewe kwa kuwa hujawahi kujali unavyojibu wengine ila yeye.” James akarudi na kuegemea kwenye gari akabaki kama anayefikiria. “Sasa usipoteze muda James. Hicho unachojisikia, kitafutie majibu ya haraka bila kusuasua.” “Umesikia maelezo yangu lakini?” “Nayakumbuka na ndio maana nakwambia usipoteze muda.” “Nafanyaje sasa wakati nishakuwa kama nimeharibu tokea mwanzo? Anahisi nimemkatalia! Halafu yule ni msomi na anajielewa.” “Nani?” “Nice try. But NOPE.” Geb alicheka sana kwani alimuuliza kwa haraka ili kumjua huyo msichna aliyemudu kumchanganya James, Mgumu. James akamshitukia.

“Sawa. Lakini ndio anza kwa kujirudi.” “Nimwambiaje tena!?” “Unataka nikusaidie kukutongozea?” “Acha hizo Geb! Wewe unaakili ya kufikiria. Na nishakwambia tatizo lilipo.” Geb akazidi kucheka akimwangalia James ambaye hakuwahi kuwa hata na dalili ya mwanamke. “Unanisaidia au?” “Kwa mfano nikikukatalia, utafanyaje?” James akacheka akitingisha kichwa.

“Ukiwa unatoka hapa, mtumie ujumbe wa kuonyesha ulijali ila kweli hukuweza kwenda kula naye.” “Acha kunipa mambo nusunusu Geb!” “Kwahiyo unataka nikuandikie na ujumbe wenyewe!?” “Kwani utapungua wapi?” “HAPANA James! Mimi mume wa mtu, siwezi kuweka moyo wangu kwa mwanamke mwingine. Maana hapo atakuwa akisoma moyo wangu sio wako. Nishakwambia chakufanya, fikiria mwenyewe na andika maneno yako.” “Lakini kweli.” Akabaki akifikiria.

And stop smelling cheap.” “Acha dharau Geb! Hii pafyumu nimenunua agali.” “Gali kiasi gani James?” “Hela nyingi lakini si kama pafyumu zako na Joshua. Hapo hapana.” “Sasa umeelewa ninachokwambia? You smell very cheap, na haivutii. Huna majukumu James, kwa nini usijigaramie? Mbona wakati ulipokuwa ukimlea Nanaa ulikuwa ukitumia pesa kwake, kwa nini unajionea ubahili  wewe mwenyewe mtafutaji? Ni wakati wakujigaramia na wewe James. Maisha ni hayahaya. Na ipo siri kubwa sana kwenye harufu. Mimi wakati mwingine mke wangu ananitaka sababu ya kupata tu harufu yangu. Na wakati mwingine hata katikati ya siku sihitaji kuoga kupata penzi. Akipata harufu yangu tu, ananing’ang’…” “Acha bwana Geb!” Geb akacheka sana.

“Nilisahau baba mkwe wangu. Ila..” “Basi bwana. Nitanunua hiyo pafyumu. Acha kunitukana.” Geb akazidi kucheka kila akimtafakari James na hisia mpya. “Kama nakuhisi unachocheka sasa hivi ni zaidi ya pafyumu!” Geb akazidi kucheka. “Acha kunicheka Geb!” “Acha nifurahie kupatwa kwa James.” James akaondoka na kuingia ndani.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

 Magesa alimfunga anko wake mpaka akafurahi. Vilisikika vicheko vyake tu humo ndani. “Na hakuna kucheza na mwanangu tena leo. Acha mwanangu akalale na furaha.” Nanaa akamkoromea mumewe kwa sauti ya chini. Geb akacheka akitingisha kichwa. “Mimi leo mbaya!” “Ndiyo. Wewe unashindana na mtoto kama mtumzima bwana! Na usiseme unamfundisha maisha.” “Sawa mama. Ila najua mtarudi tu kwangu. Kwani James anakuja kucheza naye kila siku?” “Wewe leo muache mwanangu.” “Lakini ujue unamlea sivyo huyo. Si kila changamoto atakuwa akishinda kwa urahisi.” “Wewe muache kwa leo akalale na furaha. Mengine kesho.” Nanaa akaondoka mama G hana mbavu.

“Atakufuata yeye mwenyewe.” “Lakini si umesikia maonyo ya mama yake?” “Ndiye huyohuyo atarudi kukuomba ukacheze naye.” “Na ajue nitamfunga tu mwanae. Sitamuachia kama hivyo James.” Geb na mama yake wakazidi kucheka wakiwateta Nanaa na mwanae.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Ø Kwa Mara ya Kwanza JAMES kujali hisia ngeni. Hatua gani atachukua.

Ø Bale amelala masikini, ameamka tajiri wa kupindukia.

Ø Sababu ya USIRI wa Malon kwenye anayomiliki, Bale amejishindia mali zake kilaini. Hana wakumuuliza. Hata wakijua kama Malon amefariki, hakuna ajuaye alikuwa na MALI gani, wapi na kwa kiasi gani.

Malon alilala akiwa na mipango mingi, hakujua masaa machache mbeleni, hakuijua kesho yake, kama wengi wetu tunavyoepuka ukweli wa KIFO.

ILA Mfamle Daudi aliomba hivi Zaburi 90:12

{‘Tufundishe kuzihesabu siku zetu vizuri, ili tujipatie moyo wa Hekima’}


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment