Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Ni Wangu! - Sehemu ya 69. - Naomi Simulizi

Ni Wangu! - Sehemu ya 69.

“Sasa ujue kuanzia sasahivi mimi ndio daktari wa Nanaa. Kama unataka atoke hapo kitandani na awe mzima, mimi ndio nitamuhudumia. Toa maagizo kwa madaktari wote na yeye mwenyewe Nanaa, kuwa kila kitu ni mpaka mimi niidhinishe. Na Nanaa hatatoka hapo kitandani mpaka mimi nimruhusu.” “Nanaa huwa hapendi kukaa hospitalini.” Geb akaongeza kwa jeuri lakini akionekana ameishiwa nguvu. “Kwa hiyo unataka historia ya alipojifungua Magesa ijirudie?” Lubuva akamuuliza kwa ukali. Geb Kimya.

Lubuva alionekana anataarifa zote za Nanaa, tena vizuri tu.  “Ndio nakuagiza Geb. Hakikisha Nanaa anakubali matibabu yangu yote na kufuata masharti yangu yote ili apone. Ukishindwa hapo ujue unaendelea kumuua Nanaa kwa mikono yako wewe mwenyewe.” “Acha kunitisha na kuniwekea hukumu.” “Nakwambia ukweli Geb. Na ni kweli wewe na mimi hatufanani. Mimi nilimkimbia ‘girlfriend’ tu. Wini. Tena nilimuacha mikononi kwa mwanaume mwingine aliyemchagua yeye mwenyewe Wini. Lakini wewe ulifanya unyama wakupitiliza. Ulimuacha  mwanamke ambaye kisheria tayari alikuwa mkeo.”

“Mbaya zaidi ulimuacha mgonjwa na kumpokonya watoto aliozaa kwa kuyatoa maisha yake na bado alikuwa mgonjwa. Angefanyiwa hivyo Oliva ungefurahi au ungeona sawa baada ya kupewa sababu ya kitoto kabisa kama hii uliyonipa mimi. Eti ‘Nanaa alinidanganya’! Ndio unafikiri hiyo sababu yako inahalalisha uharibifu uliofanya kwenye maisha yake? Amefanyiwa upasuaji wa kichwa na moyo wake ni mkubwa kwa sababu yako WEWE Geb. ‘So, stop whining like a little girl, and grow up already’.” Lubuva akaongea kwa jeuri ile Geb aliyoisikia kutoka kwa yule nesi, kisha akatoka akiwa amemwambia aache kujilalamisha kama mtoto mdogo wa kike, akue. 

~~~~~~~~~~~~~~~~

Kama aliyefika nje ya mlango na kukumbuka kitu akarudi. “Kwanza sikukuona hapa hospitalini juzi nzima. Unawezaje kulala nyumbani wakati yeye yupo hapa?” “Naomba acha kunichanganya zaidi ya hivi nilivyo dokta Lubuva. Mimi nilipatwa na matatizo sababu ya kuamka asubuhi ili kuwahi hapa. Nilichukua taksii ili iniwahishe hapa. Njiani nikagundua sina pesa yakulipia taksii. Nikamuomba dereva asimame kwenye ATM. Nimetoa pesa kwenye mashine, wakati nageuka, nikapokea ngumi ya jichoni. Sijakaa sawa, nikaanza kupigwa. Kuja kuzinduka nipo hospitalini. Sijui ilikuaje. James ndiye aliyekuja kunihamisha kutoka hospitali ya Mwananyamala, akanipeleka hospitali ya kulipia ambapo nilipewa matibabu ya haraka na kuweza kurudi tena hapa. Mimi sio kama wewe. Siwezi kumtelekeza Nanaa.” “Sema ‘siwezi kumtelekeza TENA’’.” Lubuva akamsahihisha na yeye kama vile Geb alivyomfanyia hapo awali. Geb kimya akabaki akimtizama kwa hasira. Kwa mara ya kwanza maishani Geb akawa amepata kiboko yake aliyemudu kiburi chake.

“Nitarudi tena baadaye. Na umtoe Jimmy kule ulipomuacha kama mtoto yatima, wakati anapo nyumbani kwao. Pale watoto ni wengi na ni sehemu ya kupita tu watoto baada ya kuzaliwa. Sio sehemu au kituo cha kulelea watoto. Mpeleke kwa ndugu zake nyumbani, awe anakuja hapa kusalimia kama kina Liv. Kama mnalemewa kuwatunza watoto wote, mseme mtafutiwe msaada.” Lubuva aliongea kwa jeuri, kisha akatoka na kumuacha Geb haamini kama mambo yamembadilikia. Baba wa Nanaa amekuja juu.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Alikaa pale akiwaza. Usingizi wote ulipaa. Akavuta kiti karibu na Nanaa, akabaki akimwangalia. Kweli alifanana na baba yake. Lakini baba yake alionekana na nywele laini. Nanaa alijaliwa kipilipili, tena kipilipili kikali. Nywele kavu, zilizokuwa zikijifinyanga. Geb akacheka. “Unacheka nini?” Nanaa alifungua macho na kukuta akicheka. “Nakucheka wewe.” “Sijui wananipa nini! Nikilala nakuwa kama mfu! Najikuta napotea kabisa.” “Nina hamu na wewe Nanaa!” “Basi zungumza nao kesho wanitoe, turudi nyumbani.” Geb akakumbuka maneno hayo hayo alimshawishi nayo baada ya kujifungua Magesa, na yeye akamshawishi daktari mpaka wakamruhusu kutoka hospitalini.

“Naomba safari hii tufuate ushauri wa daktari Nanaa. Tena dokta Lubuva.” Nanaa akakunja uso. “Anaonekana ni dakatri anayejua anachokifanya. Tuweke pembeni tofauti zetu na yeye, ili.. ” Geb akatumia muda wakutosha hapo kuhakikisha Nanaa anakubali kama alivyopewa mkwara na baba yake, dokta Lubuva. “Basi hatutakaa tukatoka hapa.” “Naomba safari hii uwe mvumilivu. Hata ikichukua muda mrefu, sawa tu, ilimradi upone. Sitaki kurudia kosa.” Nanaa akakunja uso.

“Kosa gani tena!?” “Mimi ndiye niliyekusababishia kuwa hapa. Nilikutoa hospitalini ukiwa mgonjwa, na sikukupa dawa ulizotakiwa kutumia.” Nanaa akavuta pumzi na kunyamaza. Inamaana na yeye amekubaliana na hilo!? Geb naye akawaza.  “Naomba tuvumilie na tupokee matibabu yote.” “Hata ikichukua mwezi?” “Hata mwaka. Naomba safari hii sisi tuwe wapokea maagizo tu.” Nanaa akafikiria. 

“Na Jimmy?” Nanaa akauliza baada ya ukimya. “Nafikiria arudi nyumbani.” Nanaa akabaki ameduwaa. “Ni kwa nia nzuri. Pale sio sehemu sahihi ya yeye kuwepo kwa muda mrefu. Tunakuwa kama tunamtenga na ndugu zake.” Machozi yakaanza kumtoka Nanaa. “Hakuna mtu atakayekupokonya tena watoto Nanaa. Ni wako. Na wewe utakuwa na amri nao. Muda na wakati wowote utakao wahitaji hapa, wataletwa. Sitaki Jimmy akae pale kama yatima. Anatakiwa kuwa na ndugu zake. Au unafikiriaje?” “Naogopa Geb. Hakika naogopa sana. Sitaki alikopitia Magesa ndipo apite Jimmy.” “Nakuhakikishia mbele za Mungu wangu, Nanaa, hakutakuja kutokea mtu yeyote akakupokonya tena watoto. Kwanza wote tumeonywa na Mungu. Hakuna hata atakayethubutu tena. Nakuahidi. Sawa?” “Sawa.” “Usilie sasa.”

“Nahisi nimepatwa hofu Geb. Na kwa Magesa ilikuwa hivi hivi. Tulianza vizuri, kwa ahadi nzuri, nikaishia kuwa na kama majipu ya maziwa!” “Huna haja yakuogopa. Naomba uniamini kuwa nimebadilika. Nimebadilika Nanaa.” “Na mimi nimekuona umebadilika Geb.” Geb akasimama, akamfuta machozi na kuanza kumbusu.

Baba yake Nanaa akarudi tena ndio akawakuta wanapeana mabusu. Geb akamwachia Nanaa, Nanaa akaanza kucheka. “Unacheka nini?” Dokta Lubuva akamuuliza taratibu. “Nimefurahi kukuona. Niseme kukuona tena.” “Naweza kukupima?” “Unanipima mara ngapi!? Wewe sio nesi. Kwa nini unafanya kazi za manesi?” “Nanaa!” Geb akamwita kama kumkumbusha mazungumzo yao. “Sawa.” Nanaa akakubali bila kubisha tena. Lubuva akasogea.  “Geb ameniambia niwe mvumilivu hapa, nisikatae matibabu yako wewe. Chochote utakachoniambia nikubali bila kufanya ubishi. Wewe unaonekana unajua jinsi yakunisaidia.” Lubuva kimya. Akajua ujumbe wake ulifika na Geb ametekeleza maagizo yake.

“Sasa sijui kama tutaweza kumudu garama zako!? Eti Geb? Si umesikia kuwa ni daktari bingwa wa kimataifa!” “Nataka kukupima pressure.” “Kwa hiyo ndio unaniambia ninyamaze?” “Ndiyo.” Nanaa akacheka taratibu akionekana na usingizi. “Mimi nimefurahi sana. Nani alijua Nanaa anaweza kuwa na baba ambaye ni daktari bingwa!? Hakika hata mimi ungeniambia masaa machache yaliyopita, nisingesadiki.” Nanaa akaendelea huku akimwangalia.

“Natamani ungenirithisha nywele zako. Muulize Geb, nina kipilipili kikali kweli! Nikianza kuchana nywele mpaka vyanuo vinavunjika.” Nanaa aliendelea kufanya mzaha. “Naona wewe nywele zako zipo kama za kiarabu!” Nanaa aliongea huku anamtizama kichwani. “Sasa hivi nilivyo, nafanana na nani?” “Bibi yako.” Lubuva akajibu nakumfanya Nanaa acheke tena. “Ila nywele hizo ni za mama yako.” Hapo mpaka Geb  akacheka. 

“Naomba uvute kiti hapa, tuanze kuzungumza.” “Naomba leo upumzike. Baada ya siku mbili, unaweza kuwa na akili iliyotulia na kuelewa. Bado unahitajika kupumzika. Ona unavyosinzia!” “Wewe uongee, mimi nitakuwa nakusikiliza tu.” Geb akamsogelea. “Naomba umpime kwanza pressure ili tujue ikoje. Ni sawa Nanaa?” Nanaa akanyamaza. Lubuva akampima.

“Siyo mbaya.” “Mbona sasa uso wako hauendani na unachoongea?” Nanaa akamuuliza. Lubuva akasita. Hata Geb alijua kuna kitu anaficha. “Wewe tuambie tu ukweli. Sisi tumeshasikia habari nyingi na mbaya juu ya huu mwili wangu kuliko hiyo ya pressure kuwa juu. Usiogope.” Nanaa akaweka msisitizo. “Kesho nitakuwa na conference call na madaktari wote wa mambo ya moyo, tushauriane. Najua watapata tu ufumbuzi.  Ila kwa sasa naomba upumzike Nanaa.” “Huyo bibi yangu ninayefanana naye, yupo hai?” “Yupo hai.” Lubuva akajibu. “Na babu?” “Wote wapo hai.” Lubuva akajibu.

“Umesikia mambo hayo Geb? Nimelala yatima, nimeamka na ukoo! Lazima nipone ili nikawaone.” “Ukiruhusu, wanaweza kuja kukuona.” “Acha mchezo!?” Nanaa akamfanya Lubuva acheke kidogo na kutingisha kichwa. “Wewe walete woote waje wanione. Nani hataki ndugu?” “Basi ulale upumzike. Hiyo pressure ikiwa sawa, nitawaleta wakusalimie.” Nanaa akacheka kama anayefikiria. “Subiri kwanza nizungumze na mume wangu. Unajua kama nimeolewa?” Nanaa akaanza kusinzia. Aliuliza huku anafunga macho.

“Nafahamu.” “Basi subiri nizungumze kwanza na Geb, ndio nitakwambia lini uwalete.” “Sawa, hamna haraka.” “Ila nataka kumjua mama yangu zaidi. Alikuwa ni mtu wa namna gani!?” “Kaa ule kwanza kabla hujarudi kulala tena. Kesho nitakueleza vizuri juu ya mama yako.” Nanaa akabaki amefunga macho. “Naweza kukusaidia kula.” Lubuva aliongeza. Wakamuona Nanaa anacheka. Akafungua macho.

“Inamaana unilishe!?” “Kama hutajali.” Akacheka na kufunga macho. “Namtaka Geb ndio anilishe. Nasikia njaa ila nahisi usingizi unanilemea.” “Basi usirudi kulala ili akulishe.” Nanaa akafungua macho na kumtizama Dokta Lubuva.

“Unaondoka?”  Nanaa akamuliza. “Ulitaka nibaki au niondoke?” Lubuva naye akarudisha swali. “Kaa kidogo na Geb. Usimwache peke yake muda mrefu. Anaingiwa hofu na hivi ninavyoumwa. Mwambie utanisaidia, nitapona na kila kitu kitakuwa sawa.” Nanaa alimalizia hivyo, nakurudi kulala.

Geb alizidi kuingiwa hofu. “Ni kweli unafikiri atakuja kupona na kurudia hali yake kama zamani? Ni kama mikono yake haina nguvu!” Geb akauliza akionyesha hofu yake. “Nikwambie tu ukweli Geb, hali ya Nanaa sio nzuri. Anatumia dawa za hali ya juu. Nampa dawa ambazo nimeletewa kutoka Ujerumani. Daktari huyo wa mambo ya moyo aliyenitumia amesema kama zisipoweza kushusha hiyo pressure kwa masaa 24, anatakiwa kufanyiwa upasuaji wa moyo.” “Tena!?” “Kumbuka huo moyo ameanza kuutibu kwa muda mrefu sasa. Amefuata masharti yote aliyotakiwa kufuata, akatumia na dawa pia. Nimemtumia huyo daktari matokeo yote ya vipimo vyake vya pressure. Tokea ni mjamzito mpaka sasa. Na ndio maana unaniona kila wakati ninampima mimi mwenyewe, ni kwa kuwa huyo daktari huko Ujerumani anafuatilia hayo matokeo. Kwa dawa na mapumziko yote haya kushindwa kushusha hiyo pressure, inamaana kinachofuata ni upasuji ambao wanaweza kuweka kifaa kitakachokuwa na uwezo wa kurekebisha mapigo yake ya moyo na usambazwaji wa damu kwenye moyo.” “Mungu wangu nisaidie.” Lubuva alimsikia Geb akiomba kwa hofu. 

~~~~~~~~~~~~~~~~

 “Unajua kuomba?” Geb akamuuliza Lubuva. “Unamaanisha kumuomba Mungu, yaani kusali!?” Geb akabaki akimtizama. “Mimi ni mkristo, lakini maswala ya kusali Sali huwa….” Lubuva akakwama. “Labda tugawane. Wewe Sali, mimi niwe upande wa matibabu.” Geb akabaki akimkodolea macho. “Wewe huwezi kumtibu kama mimi na mimi siwezi kuwa nasali muda wote kama wewe! Mbona ni rahisi tu. Tugawane na tusiingiliane.” Wakaanza tena.

“Kwa hiyo wewe huwa huombi!?” “Kwa nini!?” Lubuva akamuuliza kama anamshangaa. “Huzungumzi na Mungu!?” “Kwa nini?” Lubuva akaendelea kuhoji. “Kwa hiyo hata kanisani huendi?” “Kufanya nini na wakati Mungu amenipa kazi ya kutibu watu? Sasa bora lipi, kufanya kazi aliyonipa au kurudi tena kuanza kumuomba vitu ambavyo tayari ameshanipa au hata sihitaji!? Sina sababu ya kuomba chochote kwa kuwa kila ninachotaka ananipa! Sipotezi tena muda.” Geb akamgeukia vizuri.

“Nini!?” Lubuva akamuuliza. “Wewe omba sasa hivi kwa kuwa hujui chakufanya hapa kwa Nanaa, unataka Mungu akufanyie kitu. Mimi najua kitu ninachotakiwa kufanya na ninafanya. Kama wote tukianza kupiga magoti hapa tunaomba muda wote, nani atamtibu Nanaa!?” Geb akabaki akimshangaa. “Kwa nini unanishangaa kama hunielewi wakati nakwambia kitu cha kawaida kabisa!?” “Kama unajua kitu chakufanya kwa nini Nanaa yupo hapo kitandani mpaka leo?” Geb akamuuliza.

“Si ni mgonjwa!” “Sasa wewe unayejua kitu chakufanya, kwa nini hufanyi ili tutoke hapa?” “Yupo kwenye matibabu. Ndio maana nakwambia tunafanya kwa hatua. Kama dawa zimeshindikana, ndio unafuata upasuaji! Mbona wewe unaomba tokea majuzi hajapona na unaendelea kuomba? Kwa nini na mimi nisiamini kuwa tuendelee na matibabu atakuja tu kupona?” Geb akatingisha kichwa.

“Nini!?” Lubuva akamuuliza tena. “Sasa kwa kuwa unanihitaji hapa ili kumfanya Nanaa akubali matibabu kutoka kwako, na wewe utafanya nitakachokwambia.” Geb naye akambadilikia. “Nisipokubali?” Lubuva akamuuliza. “Unamaa kama ambavyo hukukubali mimba ya  Wini, ukamkimbia na kumtelekeza bila hata kujali maendeleo yake?”  Geb naye akamuuliza swali la kumuumiza.

“Sasa ukiendeleza hiyo tabia yako yakutokukubali mambo ya msingi na muhimu, nakuhakikishia hutamgusa tena Nanaa. Nitamtoa hapa, na kumpeleka ninapotaka mimi. Nitatafuta daktari mwingine. Nitampa historia ya Nanaa yote na vipimo vyake vyote. Nitamwambia kile ulichoniambia wewe juu ya upasuaji na maendeleo yake mpaka sasa. Nitamwambia aniandikie barua ya kumpeleka Nanaa Ujerumani. Mimi mwenyewe na huyo daktari ndio tutampeleka huko nchini Ujerumani akafanyiwe huo upasuaji wa kurekebishwa moyo wake, bila wewe. Tena nakuhakikishia atafanyiwa upasuaji na huyo daktari wako bingwa unayewasiliana naye.” Geb aliongea kwa jeuri bila haraka.

“Huwezi kufanya hivyo!” Lubuva akashangaa. “Try me! I dare you Lubuva, try me!” Geb alijibu kwa kitisho na jeuri akimwambia amjaribu, aone. Lubuva akabaki akimshangaa. “Kama huamini, nipe masaa 24, nitakuwa nimeshapata jina kamili la huyo daktari huko Ujerumani, namba yake ya simu na mazungumzo yenu yote yaliyokuwa yakiendelea kati yenu. Tokea unaanza kuwasiliana naye juu ya Nanaa mpaka leo.” Geb aliendelea kwa jeuri.

“Wakati wewe unasomea kupasua vichwa vya binadamu, mimi nilikuwa nikisomea kupasua kompyuta. Kutafuta habari zilizozikwa kwa siri na watu, nakuzifanya zisomeke hata na mtu asiyejua kusoma. So, try me.” Bado Geb alitaka amjaribu. Lubuva alibaki akimtizama Geb asiamini.  “Huwezi kuja leo kwenye maisha ya Nanaa na kuanza kuweka utaratibu wako wewe. Nanaa ni mke wangu mimi. Na ananisikiliza mimi kuliko mtu mwingine yeyote. Nikimwambia asubiri mahusiano na wewe, ujue atasubiri mpaka mimi nitakapomwambia. Kama huniamini, nijaribu uone.” “Mimi sijui kuomba kwa kuwa huwa sioni sababu ya kuomba.” Lubuva akakubali yaishe.

Wanaume hao wawili walikutana wote wajuaji. Wote wamesoma zaidi ya shahada mbili. Wataalamu kwenye fani zao. Na pesa ipo. Wajeuri wakupitiliza. Wote wanataka kuonyesha umuhimu wao kwa Nanaa. Sasa nani zaidi? Ndio wanatunishiana vifua.

“Anza kwa kufunga macho, mimi niombe.” “Huwezi kulazimishia mimi kuomba Geb! Hayo ni maisha yangu mimi na makubaliano yangu na Mungu wangu.” Geb akaweka mikono kifuani kama anayemsubiria. “Fine! Ngoja tupoteze muda hapa wote tukiomba, badala yakufanyia kazi majibu ya maombi yako.” Lubuva akafunga macho. Geb akaanza kwa kutubu kwa ajili yake yeye Lubuva anayehusika na kutibu mwili wa Nanaa. Akatubu na kumtakasa. Akamuombea akili tulivu ili aweze kumsikia Roho wa Mungu anapompa maelezo ya jinsi ya kumtibu mkewe. Akamuombea watu sahihi wakusimama naye kipindi hicho anachohitaji watu wakumsaidia Nanaa.”

“Akamsihi Mungu akumbuke rehema juu yake. Watu wote aliowasaidia, akumbuke kujitoa kwake na yeye amjibu wakati huo anapohitaji msaada kwa binti yake, Nanaa. Akaombea dawa anazotumia Nanaa, zikakubalike mwilini kwa Nanaa ili apone kwa haraka bila upasuaji mwingine. Akamalizia kwa kumbariki dokta Lubuva. Kwa muda anaotumia pale na kupoteza mamilioni ya pesa kwa kumuhudumia Nanaa. Geb akamsihi Mungu asimsahau Lubuva, aendelee kumbariki mpaka yeye mwenyewe ajue kama ni Mungu ndiye amembariki. Akamuombea mkewe na watoto wake wote. “Ameen!” Geb akamaliza.

Lubuva akaanza kucheka. “Nini?” Geb akamuuliza. “Nashukuru kwa maombi mazuri.” Geb akacheka. “Kweli. Sikejeli. Nimejisikia vizuri.” “Karibu.” Geb akajibu na tabasamu usoni, akamgeukia Nanaa. “Atapona tu. Amini.” Lubuva akajaribu kumtuliza. “Nashukuru. Wewe nenda tu kapumzike. Nitakuwa naye. Kukiwa na kitu cha kukutaka ushauri, nitakupigia.” “Sawa.” “Ila nina wasiwasi sana na kula yake. Hali chakula vizuri nahisi ndio maana anakuwa dhaifu. Hataweza kunyonyesha akiwa kwenye hali hiyo.” “Dawa ndizo zinamlevya. Hawezi kuishiwa nguvu kwa sababu ya hizo dripu alizowekewa. Halafu nashauri kunyonyesha isiwe kipaumbele kwa sasa. Mwache kabisa atulie. Maadamu mtoto ni mzima na hajakataa maziwa anayopewa, msubiri kwa sasa.” “Sawa.” Geb akakubali. 

“Namaanisha hata na yeye umwambie hivyo hivyo. Asione amefeli kutimiza jukumu fulani kwa Jimmy. Mkumbushe ameshamlipia garama kubwa sana. Amemzaa akiwa mzima kabisa. Mwambie sasa hivi afikirie jinsi ya kutoka hapo ili awe na watoto wake wote. Atamnyonyesha kwa kadiri ya uwezo wake kama atatulia na kupona.” “Sawa.” Lubuva akatoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Lubuva alirudi alfajiri akamkuta Geb akimnywesha uji. “Vipi?” “Njaa ilikuwa ikimuuma.Akaniamsha nipe uji.” “Afadhali.” Nanaa akafungua macho. “Vipi?” Lubuva akamsogelea. “Nahisi kuchoka tu. Lakini nipo sawa.” Nanaa akajibu. “Leo sitampa hizo dawa, ili tuone leo utashindaje.” “Na hiyo pressure!?” Geb akauliza kwa mshituko. “Ndio tumeona tuondoe ili tupate uhalisia halisi wa moyo wake bila dawa. Kama inakuwa juu zaidi ya hivyo, hatua nyingine ifuate kama tulivyozungumza jana.” “Hatua gani?” Nanaa akamuuliza Geb. “Nitakwambia kama pressure itaendelea kuwa juu. Kama itarudi kuwa kawaida hakutakuwa na haja tena.” Geb akajibu. Nanaa akamwangalia na kunyamaza. Akala mpaka akamaliza.

“Kwa nini uliondoka na kwa nini ulirudi?” Nanaa akauliza taratibu. “Niliondoka nikiwa sina uhakika kama wewe ni mtoto wangu. Nimerudi kwa kuwa niliambiwa Wini alifariki na ameacha mtoto wangu.” Lubuva akajibu. Nanaa akamtizama kwa muda kisha akavuta pumzi. “Kwa hiyo ni kweli kuwa mama yangu alikuwa muhuni sana?” “Hapana Nanaa! Kwa nini unakubali hivyo?” “Umesema uliondoka kwa kuwa hukuwa na uhakika kama mimi nilikuwa mtoto wako. Inamaana mlikuwa wanaume wengi kwenye maisha yake!” “Mimi ndiye nilikuwa mwanaume wake wa kwanza.” “Halafu!?” Nanaa akauliza.

“Alikuja kumpenda mwanaume mwingine. Nafikiri mimi sikuwa mwanaume wa ndoto zake.” “Sasa ikawaje aje akutaje kama wewe ndio mwenye mtoto kama alikuwa amepata mwanaume wa ndoto zake!? Kwa jinsi nilivyosimuliwa, ni wewe tu ndiye aliyekutaja kwa dada yake. Hakumpeleka kwengine isipokuwa nyumbani kwenu. Inamaana angekuwa amewachanganya wanaume wengi, angewataja wanaume wote. Lakini wanasema alimleta mama mkubwa, kwako tu. Na ulivyokataa, hakumtaja mwingine akaishia kulia tu, mpaka kifo chake.” Nanaa akaweka msisitizo.

“Sasa hivi ndio nimeelewa kwa nini alinitaja mimi.” “Unamaanisha nini?” Nanaa akaendelea kuhoji. “Nahisi nilipatwa na wivu. Hapo ndipo nilipokosea na kuharibu kila kitu. Mama yako hakuwa muhuni, ila mtoto. Mimi ndiye nilianza naye mapenzi. Nikamtambulisha kwa rafiki yangu..” Geb akageuza kiti kwa nguvu mpaka kikasugua sakafu, kisha akamgeukia Lubuva. Nanaa na Lubuva wakamtizama. Nanaa hakuelewa, lakini Lubuva akaelewa. Akapata ujumbe wake vizuri, akabadili alichotaka kuzungumza. 

“Samahani. Endelea dokta Lubuva.” Nanaa akarudisha macho kwa Lubuva. Na Geb naye akamkazia macho. “Ndio nilikuwa nasema, nahisi tatizo lilikuwa wivu. Nilipomtambulisha kwa rafiki yangu, wakaanza kuwa karibu. Ndipo nikaanza kupatwa wivu, nikahisi wana mahusino ya kimapenzi. Nikazungumza na Wini kumuomba apunguze huo ukaribu. Au niseme nilimuonya aache kabisa ukaribu na yule jamaa. Siku hiyo ya mazungumzo tulikuwa na Wini usiku wote. Sasa baada ya siku kadhaa, nikaambiwa Wini ameonekana tena na yule jamaa!”

“Basi hapo ndio nikakata mawasiliano nao wote wawili. Tena kwa kumuita yule rafiki yangu na kumuonya asinitafute tena na amwambie hivyohivyo Wini. Kwa hiyo nikapotezana nao wote wawili. Baadaye ndio Wini na dada yake wakanijia nyumbani. Wini akiwa analia anasema mimba ni yangu!” Lubuva akajieleza kwa tahadhari sana.

“Nilikosea Nanaa. Tokea mwanzo nilikosea. Kumbuka nilisikia tu kuwa Wini alionekanika na jamaa. Sikumuuliza. Pengine ningemuuliza, ningejua nini kilikuwa kikiendelea. Mimi nikakasirika tu na kuwapiga marufuku wasinitafute tena. Sijui kama unanielewa?” Nanaa akavuta pumzi kwa nguvu, hakujibu.

          “Wini aliletwa nyumbani na dada yake, sio kuniambia kuwa ana mimba yangu, hapana. Dada yake alinijia juu akaniambia anataka kunishitaki kwa kumpa mimba mtoto chini ya miaka 18, maana mimi hapo tayari nilikuwa nimeshatimiza miaka 18. Alituogopesha. Wakati huo baba ananiangalia. Ni mkuu wa mkoa, na amehangaika kunitafutia chuo, nina kila kitu mkononi, natakiwa tu kuondoka. Kwa ujinga na hofu, nikiwa nimemchukia Wini nikijua amenisaliti, njia pekee iliyokuwa rahisi, nikijua anadanganya mtoto sio wangu, pengine anataka tu pesa zangu, kwa kuwa mimi nilikuwa mtoto wa mkuu wa mkoa, na jamaa alikuwa mtu tu wakawada. Nikamkana. Nilitumia kila neno nililojua nitawaondoa pale na kwenye maisha yangu, ili niwe huru, niondoke nchini kwa haraka.” Wakamuona machozi yakimtoka Nanaa.

“Nilikosa Nanaa. Nilikosea tokea mwanzo. Natamani kama Wini angekuwepo nika..” “Ulishawahi hata kumpenda au alijirahisisha tu kwako ndipo ukawa ukilala naye kila unapohitaji?” Nanaa akauliza huku machozi yakimtoka. “Kwa sababu namfananisha na mimi. Na yeye baba yao aliwakimbia sababu walikuwa wakizaliwa watoto wa kike. Pengine alikuwa akitafuta kimbilio. Kutaka upendo wa mwaume, asijue anajiingiza matatizoni! Aliangukia kwenye mikono ya rafiki yako, kitu kilichokuudhi wewe na kumtupilia mbali. Akateseka peke yake mpaka kifo. Na mimi nimepitia hapo. Kuangukia kwenye mikono ya rafiki yake Geb. Yakanipata kama yaliyompata mama.” Hapo kidogo Nanaa akaweka usawa kati ya Geb na Lubuva. Lubuva akapata aghueni. Kabla hajatulia, Nanaa akaendelea.

“Lakini nikiwa kwenye hali ya kufa. Nimekata tamaa hospitalini, Geb alirudi kuniuguza. Alisimama na mimi mpaka sasa. Huyo Jimmy, ni juzi nilipojifungua ndipo wote tumejua ni mtoto wa Geb. Lakini kabla ya hapo, Geb alikubali kumpokea mtoto wa rafiki aliyemsaliti. Akakubali kunioa akijua au watu wakijua nimebeba mtoto asiye wake. Sijui kama unanielewa?” “Naelewa Nanaa.” Lubuva akajibu.

“Ninachojaribu kusema ni kuwa, hukuwa na mapenzi ya dhati kwa mama. Ulikuwa ukimchezea tu. Ndio maana alipokosa, au tatizo lilipotokea, uliweza kuondoka kwa urahisi. Wewe hudhani kama endapo ungekubali pale mbele ya watu, yaani usimkane. Ukazungumza neno lolote kama vile, labda huna uhakika na mimba aliyobeba, ila unaomba usubiri mpaka ajifungue ndipo mjue kama mtoto ni wako! Hudhani kuwa pengine asingekufa? Hata kama ungeondoka kwenda masomoni, pengine ungemuacha akiwa anaheshimika sio kunyanyaswa kama binti Malaya tu! Hudhani hivyo?” Nanaa aliuliza kwa uchungu sana, lakini taratibu. Alijaribu kushindana na machozi yake, lakini yakawa yakimlemea.

“Nilikosa Nanaa. Nilikosea tokea mwanzo. Nafikiri utoto ulichangia, sijui nilipatwa na nini! Ila nilimpenda Wini.” “Ulidhani kuwa ulimpenda. Upendo unajidhihirisha pale mtu anapokosa. Ndipo upendo sasa unapojionyesha. Kusitiri wingi wa dhambi, huhesabu, huvumilia na kadhalika. Sio wakati kila kitu kipo shwari. Hukuwahi kumpenda mama yangu.” Lubuva kimya. Nanaa akajifuta machozi.

“Ulimuacha akidhalilika na kuteswa. Pengine alikuwa akikulilia wewe. Kuna ahadi zozote ulizokwisha kumuahidi?” Nanaa akauliza. Lubuva akababaika sana. “Ndiyo au hapana?” “Nilijua angetulia na mimi mpaka tuje kuoana. Nilimuah…” “Kwa hiyo hakuwa ametulia!?” Nanaa akauliza kwa kushangaa. Geb akakaza macho. Napo hapo Lubuva akaanza kurudia hili na lile. “Kumbe ni alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na huyo rafiki yako na sio ukaribu tu!?” Lubuva akashikwa kwenye kutaka kuficha ukweli. “Alikuwa mtoto mdogo, Nanaa. Ni mimi ndiye niliyeshindwa kumlinda mpaka akaangukia kwenye mikono ya huyo rafiki yangu.” Nanaa alilia sana. Alilia kwa uchungu sana. “Naona inatosha kwa leo. Mtaendelea wakati mwingine. Kama hakuna dawa ya kumpa, naomba umwache apumzike.” Geb alimwambia Lubuva.

“Naomba nikwambie kitu nilichofikiria. Pengine kilichokuwa kikimfanya alie sana.” Nanaa akajifuta machozi akitaka kumsikiliza. “Mara ya mwisho nilipokuwa na mama yako, nilimbembeleza aniambie ukweli juu yake na yule jamaa. Kwa ahadi ya kuwa chochote atakachoniambia, mimi nitakipokea, na nitamsamehe hata kama alishalala naye. Akiwa na hofu, Wini alikiri. Nikamwambia kama ataachana na yule jamaa, tena kwa kumtamkia wazi, mimi na yeye tutaendelea na tutakuja kuona na kuwa na maisha ya pamoja. Akakiri na nikamthibitishia kuwa nimemsamehe, ndio tukatumia usiku huo pamoja.”

“Sasa nafikiri, pengine alirudi kwa yule jamaa labda kuvunja mahusiano akiwa tayari ameshika mimba bila yeye mwenyewe kujua. Akaachana na yule jamaa, halafu na mimi nikamtumia ujumbe kuwa sitaki tena kumuona. Pengine alijiona amekosa kote kote. Na mimi nilimkataa baada ya kumtumia usiku kucha. Sasa nashuku alipokuja kujigundua ni mjamzito wa mimba yangu na mimi nilimkana baada ya yote hayo, halafu alikuwa mtoto, ndio maana alikuwa akilia. Mimi ndiye nilikosea Nanaa. Nilikosea tokea mwanzo wa mahusiano. Nakiri mimi ndiye niliyesababisha kifo chake. Na upo sahihi, angalau ningekubali nilishakuwa na mahusiano naye ya kimapenzi, siku alipoletwa kwetu, na mbele ya kila mtu, pengine ingemsaidia. Lakini nilikosea Nanaa. Naomba unisamehe. Hakika unisamehe, nilikosa.” Akamuona Nanaa ametulia, akafunga macho bila kujibu kitu.

“Alikuwa na dimpozi kubwa kama hizo zako.” Nanaa akafungua macho, akatoa tabasamu. Lubuva akamsogelea karibu. “Meno yake ya hapa mbele yalikuwa yamepandana kidogo. Ni kama ncha ya jino moja ilipanda kidogo juu ya jingine. Ungependa kumwangalia akicheka. Hata kama unahasira, akicheka, lazima moyo wako ufarijike. Na alipenda kucheka. Hakuna kitu utazungumza, Wini asicheke. Hakuna tatizo kubwa kwake. Kila kitu ukimwambia kama tatizo, atakipunguza uzito wake, mpaka uone huna tatizo kabisa.” “Kama Nanaa.” Geb akaongeza, Nanaa akacheka.

“Alikuwa akipenda kula?” Nanaa akauliza. “Mmmh!” Lubuva akawa kama anavuta kumbukumbu, akacheka. “Alikuwa mwembamba. Hakuwa na mwili. Ila Wini alipenda kucheka.” Wakamuona Lubuva ameina kama anakumbuka kitu, akacheka. “Alikuwa na namna yake yakumfanya mtu ajisikie vizuri. Nafikiri ndio maana nilipenda kuwa naye karibu. Sikumbuki kucheka hivyo tena. Halafu…” Akataka kuzungumza kitu, akacheka na kunyamaza.

“Kwa hiyo hatujafanana hata kidogo!?” Nanaa akauliza. Lubuva akacheka. “Nimekwambia hizo nywele ni zake.” “Mama naye! Ndio nini sasa! Wenzake wanarithisha watoto wao vitu vizuri, yeye ananipa kipilipili hiki!” Wakacheka. “Na dimpozi hizo ni zake. Kwetu hakuna mwenye dimpozi.” Lubuva akaongeza, Nanaa akacheka, Geb akaweka kidole pale shavuni. Wote wakacheka. “Ila yeye kipilipili chake kilikuwa chekundu.” Lubuva alimfanya Nanaa na Geb wacheke sana. “Alikuwa anakata nywele chini sana. Hakuwa akithubutu kuacha nywele zake zikue. Alikuwa akisema akichana, nyumba nzima itajua yupo mahali anachana nywele zake.” Nanaa alizidi kucheka.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Mara akaingia mama G na Liv. Uso mwekundu na macho kama aliyekuwa akilia. “Mbona mama mzazi analia?” Nanaa akauliza. “Kwanza mbona hushangai tumekuja mapema? Sasa hivi huu sio muda wake wakuamka, lakini hakulala vizuri na asubuhi ameamka anakulilia.” Mama G akajibu. “Pole Liv mwanangu. Njoo.” Nanaa akamwita. Liv alikuwa anavuta pumzi kama anayetaka kulia. Geb akamvua viatu akampandisha pale kwa mama yake. “Nampenda Liv.” Nanaa akamkumbatia. Liv kimya.

“Labda aliogopa vile alivyokuona na hizo mashine, halafu hamkupata muda mrefu wa pamoja.” Mama G, akaongeza. “Usiwe na wasiwasi Liv. Mimi ni mzima. Jana nilikuwa tu na usingizi.” Kimya. “Liv!” Nanaa akamwita taratibu akiwa amemlalia. “Mwangalie mama basi!” Liv akamwangalia na kumbusu pale kifuani.

“Nampenda mama.” “Nampenda sana Liv. Umemuona dad?” Liv akamwangalia. “Nampenda Liv.” Geb akaongea naye kwa upole. “Nampenda dad.” “Naomba basi nikusalimie binti Magesa.” Liv akasimama na kwenda kwa baba yake.

Geb akamuweka kifuani. “Mmmmmmh!” Walimuona Geb akigugumia huku akifunga macho. Kisha akaanza kumbusu. Liv akaanza kucheka kama aliyekuwa akisubiria. “Nampenda dad.” “Nampenda sana Liv.” Akacheka na kidole chake mdomoni. Lubuva akamsogelea. “Liv!” Akamwita taratibu. Liv akamwangalia Lubuva, akajificha shingoni kwa baba yake. “Kuna kitu nimeficha kwenye moja ya mmkono wangu. Ni upi?” Akamuuliza Liv.

Liv akajitoa kwenye shingo ya baba yake. Akaangalia mikono ya Lubuva aliyokuwa amemnyooshea huku amefunga ngumi. Akaitizama kwa makini, kisha akamtizama na yeye. Akamtizama kidogo na kurudisha macho kwenye ile mikono. Kila mtu kimya akimtizama. “Ukipatia, nakupa kazi yakumpima mama yako pressure.” Liv akacheka, na kunyoosha kidole kwenye mkono wake wa kushoto. Lubuva akafungua. Alipatia. Wote wakacheka. “Liv wewe ni mtoto mwenye akili sana. Haya njoo tumpime mama pressure. Subiri kwanza nikuonyeshe.” Geb akamuweka pale kitandani.

“Unapenda kuja kuwa daktari?” Lubuva akamuuliza. “Kwa akili ulizo nazo wewe, unaweza kuja kuwa mtu yeyote yule na ukafanya vizuri sana.” Liv akacheka. “Haya, mimi namfunga mama mkono. Wewe unatakiwa ubonyeze hapa. Namba zikisha andikwa hapa, ndio tutajua pressure ya mama. Sawa?” Liv akatingisha kichwa kukubali. “Nampenda mama.” Lubuva akamwangalia. Liv kidole mdomoni, anacheka na dimpozi zake. Lubuva akacheka nakurudisha macho kwenye mashine. Liv akabonyeza kama alivyofundishwa. “Safi sana.” Lubuva akamsifia. 

Matokeo yalipotoka, Lubuva akazima bila kusema kitu. Nanaa akajua majibu sio mazuri. “Asante kunisaidia kumpima mama.” Liv akacheka. “Unataka nikupe kazi nyingine?” Liv akaitikia kwa kichwa. “Muwekee mama hiyo mashine ndogo ya kidoleni. Mvalishe kwenye kidole, halafu nakuletea plasta ili uifunge vizuri isitoke anapolala. Unafikiri utaweza?” Liv akatingisha kichwa kukubali huku anacheka. Kila mtu alikuwa akiwasikiliza na kuwaangalia. 

“Vipi pressure yake huyo?” Mama G akauliza. James naye akaingia. “Shikamoo kaka.” “Marahaba. Angalau leo unaongea. Ulinitia wasiwasi jana!” “Wamenipunguzia dawa. Angalau leo nimeweza hata kula vizuri.” “Vipi pressure?”James akauliza huku akimtizama Lubuva na Nanaa. “Nitatoa majibu kamili kesho. Naona tuendelee kuiangalia tu.” Lubuva akajibu kwa kifupi.

Wakati Liv na Lubuva wakiendelea kufanya wanachofanya Nanaa akamwangalia Geb kama anayemuuliza kitu. Geb akabaki kimya. “Unaweza kusema Pulse Oximeter?” Wakamsikia Lubuva akimuuliza Liv. Akacheka. “Jaribu tu. Ukishindwa nitarudia tena. Anza kwa kusema Pulse.” Lubuva alikuwa akizungumza na Liv taratibu huku akimfunga mama yake.  “Puz.” Liv akarudia. “Waw….” Lubuva akasifia japo hakuwa amepatia sana. “Sasa sema Oximeter. Taratibu tu. “O-xi-me-ter.” Liv akarudia. “Safi. Sasa rudia neno zima. Pulse Oximeter.” Liv akacheka, kisha akarudia.         Lubuva akampigia     makofi. Mpaka Geb akafurahi. Nanaa akacheka.

“Sasa unajua Pulse Oximiter ni   nini?” Lubuva akamuuliza. Liv akabaki akiangalia zile mashine. “Sema tu usiogope.” Akanyooshea mashine zilizokuwa zimesimamishwa pembeni. “Umepatia, ila hiyo unayofunga kwenye kidole cha mama, ndio Pulse Oximeter, inapeleka majibu ya mama, pale kwenye ile screen. Umeelewa?” Liv akatingisha kichwa kukubali. “Kwa hiyo ukiona zile mashine zote pale, usiogope wala usiwe na wasiwasi. Ujue hiyo Pulse Oximeter uliyoweka kwenye kidole inapelekea ujumbe pale kwenye zile  screen ili kujulisha watu wengine wanaokuja kumwangalia mama kuwa, mama yake Liv yupo salama, msiogope. Hata Liv mwenyewe amemuwekea mama yake, hajalia wala haiumi.” Liv akazidi kucheka.

“Si unaona sasa hivi hizo mashine haziogopeshi tena?” Liv akatingisha kichwa kukubaliana na dokta Lubuva. “Basi, mimi naomba nikushukuru kwa kunisaidia kumpima mama na kumuwekea hiyo ya kidoleni. Inaitwaje tena?” “Puz Oximta.” Kila mtu akapiga makofi kwa jinsi Liv alivyojibu. “Kweli wewe Liv ni mtoto mwenye akili. Sasa unajua kazi iliyobaki?” Liv akacheka. “Nikuendelea tu kusoma pale, na kumfanya mama apumzike. Unajua kumbembeleza alale?” Liv akacheka huku anatingisha kichwa kukubali. “Basi. Hakikisha ukilala, na yeye analala.” Liv akakubali.

Baba.

“Nitawaona baadaye.” Lubuva akaaga, ili atoke. “Naomba usiondoke, nikutambulishe kwanza.” Nanaa akamuwahi. Lubuva akabaki akimtizama Nanaa. Wote kimya. Wakamgeukia Nanaa. Gafla Nanaa akaishiwa maneno. Akawa hajui amtambulishaje. Wakamuona machozi yanatoka, akanyamaza. Mama G akamgeukia Geb. “Ni nini tena!?” Geb naye kimya. James akabaki na yeye haelewi. “Huna haraka Nanaa. Chukua muda wowote unaotaka.” Geb akasimama na kumsogelea. “Ni sawa?” Geb akamuuliza. Nanaa akatingisha kichwa kukubali. James akabaki kimya akimtizama dokta Lubuva na Nanaa.

Kisha akamuuliza. “Wewe ni nani?” James akauliza. Mikono mfukoni, amekunja uso kama aliyeanza kuhisi kitu. “Wewe ndiye uliyekana mimba ya mama mdogo Wini?” James akauliza swali la moja kwa moja. Mama G akatafuta sehemu akakaa. “Ndiyo. Mimi ndio baba yake Nanaa.” James akaanza kubadilika sura. Geb na Nanaa wakajua hasira zinapanda. Wakamuona anatoka bila kuongeza neno. Ukimya ukazuka. Kimya kikaongezeka. Hakuna aliyejua aongeze nini. “Nitawaona baadaye. Kwaheri Liv.” Lubuva akatoka na kuacha kimya. Hata mama G alishindwa chakuongea.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Siku hiyo Nanaa alishinda hapo hospitalini na Liv. Mama G aliondoka na Jimmy. Nanaa hakuwa na maziwa yakunyonyesha kwa hiyo mama G aliondoka na kwenda kumpa maziwa huko nyumbani. Jioni walirudisha watoto wote. Nanaa akaweza hata kuwashika. Magesa alionekana kufurahi sana kumuona mama yake. Japo fujo zilimzidi. “Jamani Magesa! Ninahamu na wewe lakini hushikiki mwanangu. Tulia basi!” Cheko lilimjaa, kuruka ruka ndio kukazidi. Kila mtu alikuwa anacheka. Kila wakati alitaka amshike Jimmy. Alirudishwa Jimmy akiwa ameshabadilika. Alivalishwa vizuri, akafanania kweli na kina Magesa. Nanaa akawa ameridhika.

“Hajasumbua?” Nanaa akauliza huku akimuweka sawa pale alipokuwa amempakata. “Naona huyu atakuwa kama baba yake. Mkimya kama Liv.” “Mama wewe! Sasa unataka kusema Magesa amefanana na wewe!?” Wote walizidi kucheka. “Mimi sijui! Ila ninachosema ni kuwa, Jimmy na Liv, ni wa kimya kama baba yao. Inawezekana wamerithi kwangu.” Mpaka Grace alicheka. “Mimi naomba tumsubiri kaka aje asema vile nilivyokuwa mpole kama Liv.” “Ila huwa anasimulia sana stori zako Nanaa.”

“Kuwa nilikuwa mpole kama Liv?” Nanaa alifanya wazidi kucheka. “Mimi siwaelewi jamani! Mbona sisikii jibu la ndiyo! Eti Magesa? Wewe umefanana na bibi?” Magesa akazidi kucheka huku anaruka. “Mwenyewe pia amekataa!” Mama G akajibu, Nanaa akacheka. Siku hiyo ikaisha vizuri.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Ilipofika saa 10 na nusu jioni, wote wakaondoka. Geb ndiye aliyetaka waondoke na watoto ili Nanaa apumzike. Walipotoka tu, Lubuva naye akaingia. “Kuna kitu nataka kuzungumza na nyinyi.” “Kuna nini?” Geb akauliza. “Leo nilikuwa na mazungumzo ya muda mrefu na hao madaktari juu ya vipimo vya Nanaa, wote wameshauri kuwa Nanaa afanyiwe upasuji kwa haraka. Hawezi kuendelea kuishi hivi akiwa ana pressure ya juu.” Nanaa kimya. “Mungu naomba unisaidie. Please!” Geb alisikika akizungumza na Mungu wake. Mikono akaiweka kichwani, wakamuona anatoka. Nanaa kimya.

           Baada ya muda akarudi. “Anafanyiwa wapi na lini?” “Yule daktari wa Ujerumani, ameniambia siku yeyote nitakayompeleka, atamuhudumia. Kwa swala la lini, ninataka kukusikia wewe ili nianze kutayarisha makaratasi yakusafiria.” Geb alionekana wazi zile sio taarifa alizotarajia kwa aina ya maombi aliyokuwa akimuombea Nanaa. Alijua Nanaa atapokea uponyaji wake. Kama sio muujiza wa moja kwa moja kutoka kwa Mungu, basi pengine Lubuva angekuja na dawa au aina nyingine ya matibabu ili kumsaidia Nanaa. Kusikia Nanaa anatakiwa kufanyiwa upasuaji, tena Ujerumani! Hazikuwa habari njema kwake. “Usiogope Geb.” Nanaa akamshika mkono. “Nitapona tu.” Geb kimya.

Lubuva akaanza kuwapa muongozo wa nini chakufanya. Akawaelewesha. Muda Nanaa anaotakiwa kutumia huko nchini Ujerumani kwa matibabu. Geb alibaki kimya. “Lakini siwezi kuondoka na wewe bila baraka za kaka. Hajarudi tena hapa. Lazima nizungumze naye kwanza. Na umueleze kwa kirefu na aelewe kwa nini ulimuacha mama. Mkipatana na kaka, ndio nitaweza kuwa karibu na wewe. Kaka James ndiye mama, baba na ndugu wa pekee niliyemfahamu maishani. Sina maisha mengine bila kaka.” “Naelewa. Nilikuwa nikifikiria nimtafute leo, tuzungumze naye.” “Hapo itakuwa sawa.” Wakakubaliana hivyo. Wakamuona Geb anatabasamu kama anayefikira kitu.

“Nini?” Lubuva alimuuliza. Geb akacheka  kidogo kama anayefikiria. “Sijui nikwambie ‘good luck!’ au ‘join the club’?” “Kwa nini?” Lubuva akauliza. “Nahisi ni kama unahitaji vyote.” Geb akaendelea na tabasamu usoni. “Kwa nini? Mbona unanitisha!?” “Nashauri ujiandae tu kwenye hicho kikao chako na James.” “Nitajitahidi kuwa muwazi.” “Na pia uwe na kiasi kwenye uwazi wako. Maana linapofika swala la Nanaa kwa James, kwanza ujue hana aibu wala hofu. Hana ndugu wala rafiki. Ni kaka kwa Nanaa kwa utaratibu huu uliowekwa hapa duniani.”

“Lakini kiukweli, ni kama mama aliyebeba mimba ya Nanaa. Inakuwa ni kama mama aliyepitia hatua zote za mimba. Kuanzia siku ya kwanza mpaka mwisho akazaa baada ya kupitia ule uchungu wa masaa mengi kabla ya kuingizwa kwenye chumba cha kujifungulia. Ndio James kwa Nanaa. Swala la kutokumuona hapa leo, usifikiri ametingwa na kazi. Huwa hakuna kitu kinasimama kati yake na Nanaa, wewe ndio utakuwa wa kwanza. Na hawezi kukubali kwa urahisi. Kwa hiyo nafikiri nikuambie, ‘Good luck as you join the club’! Maana mimi nilipita hapo ulipo. Tena kwa kuponea ngumi zake mara kadhaa.” Lubuva akatulia akitafakari huo ukaribisho anapojiunga chamani.

          “Hajui maisha mengine bila huyu Nanaa. Na ni kweli wewe na Wini, mlimpokonya utoto wake, ujana wake na ndoto zake zote. Mimi nakutana na James tukiwa watoto wadogo au vijana wadogo sana, kundi letu wote lilikuwa likifikiria kucheza mpira, na stori za starehe za maisha, lakini yeye James mazungumzo yake yalikuwa ni kama mama aliyetelekeza mtoto nyumbani. Atakwambia maswala ya poda, nepi, mafuta ya kupaka watoto, uji na mambo ya kunyonyesha. Nazungumzia James. Mtoto wa kiume wa pekee nyumbani kwao! Very smart darasani, lakini anashahada moja sababu ya Nanaa.”

“Wengi wetu, tuliokuwa darasa moja, wameendelea kusoma zaidi ya James, tena wakiwa hawana akili kama James, sababu ya Nanaa. Kwa hiyo ujiandae vizuri sana. Hata hii safari unayopanga kwenda na Nanaa, nashauri iwe ya kuomba ruhusa, sio kumtaarifu.” “Haiwezekanai! Nanaa ni mgonjwa, akikataa!? Hata kama kuna tofauti zetu, tuzimalize baada ya Nanaa kupona.” Lubuva akabisha. Geb akashangaa sana. “Unafikiri hapo alipo Nanaa ni mgonjwa wa kushitua mtu! Au unafikiri yupo kwenye hatari yakumpoteza!? Acha kabisa Lubuva! Tena usirudie kubisa.”  Geb akambadilikia kwa hasira.

“Ulikuwa wapi miaka yote hiyo!? Unajua kitovu cha Nanaa kilisafishwa na nani pale alipotolewa hospitalini baada ya Wini kufariki? Unajua Nanaa alinyonya wapi baada ya mama yake kufariki? Wakati mama yako anakuficha kama una mtoto, James aligombana na wazazi wake sababu ya kumlea Nanaa! Wewe unakiri unampenda sana mama yako, lakini ujue James amempoteza mama aliyekuwa akimpenda kama mtoto wa kwanza na wakiume pekee nyumbani kwao, sababu ya mtoto mliyemuacha wewe na Wini, na kwa sababu ya mtoto aliyekuficha mama yako unayempenda. Umepokonya mapenzi ya James kwa mama yake! Mmeua mahusiano ya James na mama yake, sababu ya kumtelekeza Nanaa! Mkamuacha hana wakumtetea ila James!”

“Hivi unanielewa nikikwambia au baba yake akikwambia umeua malengo na ndoto za James lakini? Wakati sisi tunasoma, James alikaa chini kama mama akimlea Nanaa. Wakati sisi tuna wanawake, James alishindwa kuwa hata na wazo la msichana yeyote ili asije akajisahau kwa Nanaa. James hajui starehe ya mwanamke sababu ya Nanaa! Wakati mimi na wewe tunazisaka pesa, na kumkimbia Nanaa, James hakuwahi kumtua chini. Amemtunza Nanaa kwa pesa ya matumizi aliyokuwa akipewa na wazazi wake. Alipofika chuo kikuu, akawa anamtunza kwa BUMU! Sijui kama unanielewa?” Geb akambadilikia kwa hasira sana.

“James anakuja shule hana hata shilingi sababu pesa alizopewa za matumizi, amemnunulia Nanaa vitu vya shule na vya kujikimu, pamoja na kumlipia ada. Nanaa anavunja ungo, dada au mama anayemshirikisha na kumuomba pedi ni James! Mimi nilikuwa nikimwandikia darasani na kuja kumfundisha kama mwalimu wake, kwa kuwa ilikuwa ikimlazimu James kutoroka au adanganye anaumwa, ili arudi nyumbani akamwangalie Nanaa na kukaa naye kidogo. Sijui kama unanielewa Lubuva!?” Geb akamuuliza kwa hasira.

“Ukifikiri wewe ndio una njia moja ya kumtibu Nanaa, wewe mwambie James kuwa umeshindwa kumtibu Nanaa umsikie. Kama unafikiri mimi ndio nakesha na Nanaa hapa hospitalini, basi jua James halali huko nyumbani. Anatafuta dawa na hospitali ya kumpeleka Nanaa. Kama huamini, subiri aje hapa, mwambie matibabu uliyompa Nanaa yameshindwa kumsaidia, halafu uone. Kila akija hapa, anasoma kile kijalida cha Nanaa. Anasoma dawa unazompa, na lazima azungumze na nesi. Hutamtisha James kwa kumwambia eti Nanaa hatapona bila wewe. Mpaka tunazungumza hivi, sitashangaa kama ameshaweka mpaka appointment ya daktari aliyempata yeye, nchi nyingine, aliyesikia ni bingwa. Na hatamuomba mtu pesa. Ni kwa pesa zake. Kwa hiyo, ujipange kweli unapozungumza na James.” Lubuva akabaki hoi.

“Na ujipange sawasawa. Maana linapofika swala la Nanaa kwa James, hatishwi na pesa wala wadhifa wa mtu. Na anapoona unasuasua au unashindwa kumsaidia Nanaa kwa haraka, anaweza kuja na kumbeba kumtoa alipolala Nanaa na kumpeleka anakojia wanaweza kumsaidia kwa haraka. Mbele yetu, katikati yetu tukimwangalia, anaweza kutoka naye mlangoni. Hawezi kusubiri linapofika swala la Nanaa. Wewe si unasema unaye daktari bingwa huko Ujerumani?” Lubuva kimya.

“Sasa ukamuulize yeye anao wangapi. Atakutajia madaktari bigwa wa dunia nzima, wale wenye uwezo wa kukabiliana na ugonjwa huo wa Nanaa. Na hakika atamchukua na kumpeleka akatibiwe. Alimtoa Nanaa kwenye kitanda chetu. Namaanisha changu mimi na Nanaa. Tukiwa ndio tunaamka, tupo na nguo za kulalia tu, aliingia. Akampita kila mtu aliyekuwa mlangoni na chumbani na kumbeba Nanaa kumkimbiza hospitalini na kutuacha tumeduaa.”

“Wakati wewe unajiuliza ni nini chakufanya na Nanaa, yeye anakuwa ameshajua. Na hata ukiwa naye huwezi kumdanganya. Muulize Nanaa. Na hajui unafiki, na ni ngumu kunyamaza akiona humtendei Nanaa anachojua anastahili. Ndio mtu wa kwanza na wa pekee unayehitaji baraka zake ili uwe karibu na Nanaa. Narudia tena, ni kama mama mzazi, kwa Nanaa. Nanaa ananyonyesha wanae kwa ziwa, James alimnyonyesha Nanaa kwa kidole chake hiki kidogo. Tokea siku anatolewa hospitalini mpaka mimi nampokea Nanaa, James ndiye anahusika na kula, kuvaa pamoja na furaha ya Nanaa. Na wala sio mama yake uliyemjengea nyumba kwa malipo aliyokutajia. Labda kumpa hifadhi.” Nanaa aliyekuwa akitokwa na machozi akashituka sana.

Mama James kwa Lubuva Pia!

Nanaa akajiweka sawa pale kitandani na kuuliza kwa mshangao. “Umemjengea mama mkubwa nyumba!?” Geb kimya. “Kwa nini!?” Nanaa akauliza tena kwa mshangao huku akimuangalia Lubuva. “Kwa malipo kama vile alivyolipishwa Geb. Lakini mimi ilikuwa zaidi na hakutaka kunipunguzia kwa kuwa nilimtelekeza Wini, nikamuachia yeye mzigo.” Nanaa alilia sana.

“Mlikutana wapi mpaka akulipishe?” “Mimi mwenyewe ndiye ilinibidi kumtafuta ili kujua ulipo. Ndiye aliyenielekeza kwako na kwa James.” Lubuva akajibu nakumfanya Nanaa kushindwa kuamini. “Mungu wangu! Kwa nini ananifanyia hivyo, kuniuza kwa kila anayemuahidi pesa bila kuniuliza mimi mwenyewe? Nakuwa sina uhuru na maisha yangu! Kwa nini na wewe ulimlipa sasa?” “Kwa sababu bila hivyo alisema asingeniambia ulipo, na akasema angenishitaki na kunitangaza katika kila chombo cha habari. Asimulie ubaya niliokuwa nimemfanyia mdogo wake akiwa mtoto mdogo mpaka kumsababishia kifo. Mara ya kwanza akataka pesa. Nikampa ile pesa, lakini akanibadilikia. Akaniambia ile ni pesa ya kunitajia tu jina lako. Akataka nimjengee nyumba hapa Dar ndipo aweze kunitajia ulipo wewe. Hapo alikuwa amekataa kabisa hata kuniambia ulipo wewe wala James. Na alinionya kabisa.” Luvuva akafikiria kidogo.

“Yule mama anaakili sana. Kwa kuwa alishajua najua jina la James na jina lake la ukoo, akajua sitapata shida kumpata James. Ndipo sasa akaja kwa vitisho vya kunishitaki endapo nitamtafuta James. Aliniambia mimi na Wini tulimwachia huo mzigo yeye, na nitachukua huo mzigo kutoka kwake pindi nitakapokamilisha malipo yake yaani hiyo nyumba. Kinyume na hayo masharti yake, atahakikisha naishia jela. Akanionya nisiwahi kumtafuta James wala kumshirikisha kwa lolote. Iwe mimi na yeye tu. Ndipo kazi ya ujenzi ikaanza. Hakuwa na makuu kwenye hiyo nyumba. Ila tu alitaka nyumba ya vyumba vinne. Nikaanza ujenzi, wakati nakaribia kumaliza, nikamfuata tena kumuomba anitajie hata ulipo. Nikamuahidi sitakufuata ila tu kukuona. Akasema nikirudi kwake na hati ya nyumba pamoja na funguo, atanitajia ulipo. Alikataa katakata.” Lubuva akaendelea.

“Basi, ikabidi kukazana na ujenzi mpaka nilipokamilisha ndipo nikamtafuta ili kwenda kujaza fomu za umiliki wa ile nyumba. Alipojaza kila kitu, ndipo nikamwambia kabla ya kukamilisha hatua ya mwisho, nilazima anipeleke unapoishi wewe.”

“Akanieleza jinsi ilivyo ngumu kuingia hapo nyumbani kwako. Kuna ulinzi mkali, akalalamika kuwa mlimdhalilisha sana alipokuja hapo kwenu akiwa na binti zake. Na malalamiko mengi tu ya jinsi Nanaa ulivyomuacha sebuleni katikati ya watu asio wajua, halafu akaenda kulala, wakati yeye hakukutelekeza hospitalini baada ya Wini kufariki. Hapo napo yalikuwa malalamishi ya karibia siku mbili. Kila nikimfuata, analalamikia hili na lile. Siku ya tatu ndio akakubali kunileta sasa mpaka kwenu lakini akanionyesha nyumba kwa nje, akasema yeye hataki kuingia tena ndani. Ndio safari za Tabata zikaanza sasa. Kukusubiria labda utakuja kutoka nikuone.” Lubuva akanyamaza kama anayefikiria. Akacheka huku akivuta mawazo.

“Siku nakuona pale dukani umekuja kuulizia dawa ya kukausha maziwa, sikutambulishwa na mtu. Lakini nilijua wewe ni mtoto wangu au wewe ndiye Nanaa na wala mama hakukosea kuwa wewe ni damu yetu. Nilimuona mama kuanzia kichwani mpaka miguuni.” Lubuva akafikiria kidogo.

“Baada ya hapo sasa ikabidi kuanza kukufuatilia kwa karibu. Nikawa siwezi kusubiri tena sababu tulikutana ukionekana ni mgonjwa na huna furaha kabisa. Siku nakuona umezidiwa na pressure upo kituo cha daladala, ukakataa kupanda taksii, nikaamua kukufuatilia na gari yangu. Sijui yule dereva wa daladala alifanya nini! Tukapotezana. Nikaja kuiona tena ile daladala tukiwa tumeshafika Ubungo. Nikasimama kwa haraka, nikatafuta sehemu ya kuegesha gari ili na mimi niingie mle ndani kama abiria. Nilipopanda ukawa haupo ndani ya ile gari ndio nikawa nimekupoteza kabisa. Nikawa sijui pakukupata.” “Nilizidiwa ndani ya daladala kabla hata hatujafika Ubungo. Ndio nikaona ni heri nishuke nichukue tu taksii inikimbize hospitalini.” Nanaa akajibu. 

          “Basi ndio sababu. Basi, nikaamua kurudi kukuulizia pale kwa wale walinzi wa nyumbani kwenu kwa kuwa niliingiwa hofu yakutaka kujua kama ulipata matibabu, lakini wale walinzi walinizungusha karibia kukata tamaa. Nikamfuatilia mmoja wao, baada ya kazi. Nikambembeleza sana na kumwambia sitamwambia mtu kama amenisaidia kujua ulipo na unaendeleaje.” Lubuva akanyamaza kidogo. Wakamuona amebadilika mpaka uso.

“Ndipo akanieleza mkasa mzima. Lakini akaniambia yeye hakuwepo usiku wa tukio hilo la Malii, lakini anajua kama mumewe na Nanaa alimkimbia na watoto wake. Watoto huwa wanaletwa hapo, lakini Nanaa haruhusiwi kuwashika. Hapo ndio nikajua chanzo cha ugonjwa wako. Haya, akasema kuwa uliondoka hapo, hujulikani ulipo, hiyo ni week ya pili sasa. Hakuna mwenye habari zako. Nikajua utakuwa umelazwa mahali. Nilichokosea, nilikuwa naulizia madaktari wa mambo ya moyo. Jamani nilihangaika kukaribia kuchanganyikiwa. Nikahisi labda siku ile ulipopanda daladala, ulianguka ukafa, ukaenda kutupwa kwenye vyumba vya maiti. Nikaanza kupita sasa kwenye nyumba za maiti. Sikufanikiwa.” Lubuva akaendelea na kushangaza wote wawili.

“Ikabidi niulizie madaktari wote sasa. Sifahamu jina la pili. Najua Nanaa tu. Baadaye ndipo Rweta akaniambia jina sio geni. Akaanza kunisaidia kutafuta kwenye orodha ya wagonjwa wake. Ndipo baadaye akaniuliza tena kama nafahamu jina Wini. Hapo ndipo nikajua amekupata. Ila akasema wewe ni mgonjwa wa Lyamu. Nikitaka habari zako zote, nimtafute Lyamu maana na yeye alikufahamu au ulipelekwa kwake na Lyamu. Yeye alikuwa nchini India, msaidizi wake ndio alimtumia jina la Nanaa Wini.”

“Haya, ndipo ikabidi sasa kufahamiana na Lyamu ili aweze kunipa habari zako. Lyamu ni mgumu! Hujawahi ona. Anamlinda Nanaa, kuliko utakavyojua. Ikabidi kumuomba tena Rweta anitambulishe rasmi kwa Lyamu. Baada ya mahangaiko, Lyamu ndipo akafunguka sasa. Akanieleza kwa kifupi juu ya afya ya Nanaa. Rweta naye akawa amerudi, nikamuomba tukutane ofisini kwa Rweta ili tuzungumze tujue chakufanya.”

“Tukafanikiwa kukutana ofisini kwa Rweta, Lyamu akiwepo na mafaili yako yote kuanzia mimba ya Oliva ukiwa chuoni mpaka wakati huo.” Nanaa akainama. “Nikaanza kupitia faili moja hadi jingine na dawa alizokwisha kupewa, na yule daktari wangu wa moyo wa Ujerumani alikuwa kwenye skype. Swali likawa, je dawa alizopewa mara ya mwisho na Rweta baada ya kujifungua Magesa, kama alizitumia na kushindwa kumsaidia? Maana yule daktari wa Ujerumani alisema zile dawa ulizokuwa umepewa na Rweta, ni nzuri sana. Zilitakiwa zikusaidie.”

“Haya, tukamtuma Lyamu aje azungumze na wewe, kwa kuwa Rweta alisema nyinyi wawili huwa mnaelewana. Lyamu kuja kukuuliza ukiwa wodini, ukaonekana hata hujui anazungumzia nini. Mungu bariki na wewe Geb ukapiga simu kumuulizia Nanaa. Lyamu akakuuliza swala la dawa, ukaonekana hukumpa. Ndipo sasa tukaelezwa wote kwa pamoja madhara yake, na yule dada, daktari wa kule Ujerumani, akashauri upewe dawa nyingine. Zilikuwa za garama kidogo. Tukasema ujaribishiwe ukiwa hospitalini, zikikukubali, basi ndipo uruhusiwe. Swala la garama Lyamu akasema tusiwe na wasiwasi. Maadamu Geb mwenyewe amerudi kwenye maisha ya Nanaa, mtamudu tu garama.” Lubuva akacheka kwa kusikitika.

          “Kama kuna kitu kibaya umerithi kutoka kwangu, ni ubishi na msimamo unapoamua jambo lako. Sijakaa sawa, napokea simu kutoka kwa Lyamu ananiambia muda ule tunazungumza, ulishajiruhusu pale hospitalini, upo sehemu ya kuchukulia dawa, unasubiri upewe dawa zako uondoke pale hospitalini. Umeamua kuondoka. Sikuamini. Nikamwambia akueleze madhara yote ya kuondoka bila matibabu. Akaniambia umemwambia aache woga.” Wote wakacheka. 

“Akaniambia kuja kukuona wewe tena, ni siku unayorudi mahututi. Ndipo nikamwambia hutakuwa tena na hiyo nafasi, lazima Rweta akupigie simu, akupe tarehe za kila wiki za kumuona yeye. Akwambie ni kliniki ya lazima, na iwe na punguzo ili isiwalemee. Kwa kuwa Rweta ni rafiki, akakubali kuwaona kwenye hospitali ya kulipia, kila wiki, na mimi nikawa nalipa nusu, nusu nyinyi. Lakini vipimo vikawa vinatumwa na kwa yule daktari Ujerumani ili washauriane na Rweta. Rweta akafurahia sana hiyo. Kwanza alijiongezea rafiki na ujuzi pia. Ukaribu kati yetu ukaongezeka.” Lubuva akaendelea.

“Sasa pressure ikawa inazidi kuwa juu. Wakaonelea wamtoe mtoto kwa kuwa amekomaa ili wewe utibiwe. Tulipomwambia hivyo Lyamu, akacheka sana. Akasema haitakaa ikatokea. Nikamuomba aje akujaribishe. Akasema kwake yeye hutakaa ukakubali, labda sisi wenyewe tuzungumze na wewe. Alipokuja kukwambia kuwa kuna daktari mwingine bingwa anataka kukuona au uende ukamuone, ndio ukampa ule ujumbe kuwa dokta Rweta aende yeye, akafundishwe na huyo mtaalamu ndio aje kukutibu wewe. Wewe hutaki kubadilisha madaktari.” Wakacheka tena.

“Lyamu akaona azungumze na wewe na Geb kuwapa madhara yote yakuendelea kubeba ile mimba. Ulichomjibu Lyamu, akasema umemtuma hata kwa Rweta kuwa, tuache uoga. Kama Mungu angetaka Jimmy akuzwe kwenye chupa, basi mimba yake ingeanzia kubebwa kwenye chupa. Lakini alitaka wewe uibebe, kwa hiyo Jimmy atakua hapo tumboni, hatatolewa, ila sisi ndio tutafute matibabu yakukufanya uishi wewe na mtoto. Mimi huwa najijua ni mbishi, lakini wewe umezidi, aisee! Tulikaa tunafikiria jinsi ya kukusaidia mpaka leo.” Mpaka Nanaa mwenyewe akacheka.

 “Mimi mimba zangu nazijua. Nikianza kusikiliza madaktari na sayansi zenu, nisingekuwa na mtoto hata mmoja. Halafu Lyamu ni muoga sana.” “Kwa kuwa hataki upatwe na madhara.” “Mimi nitakuwa sawa tu. Kwanza nataka kutoka hapa, nitembee kidogo. Najiona nimelala sana.” “Nanaa!!” Geb akastuka. “Lakini hilo ni wazo zuri. Anahitaji mazoezi. Nilijua tukimpunguzia dawa, usingizi utaisha, lakini upunguze shuguli. Kuwa na kiasi ili usije pandisha hiyo pressure zaidi.” “Sawa.” “Basi hiyo dripu ikiisha, nitamwambia nesi aje akutoe hapo kitandani. Utoke ukatembee.” Lubuva akatoka. Nesi alikuja kumtoa kila kitu, akahamia kwenye wheelchair, Geb akawa ndiye anamsukuma. Wakatoka pale chumbani kwenda nje kutembea kidogo. 

Kwa ajili ya kutembea kwa muda mrefu walipofika nje, huku Geb akimfuata nyuma bila wheelchair na kushinda siku nzima na wanae hapo hospitalini, Nanaa alipojiweka tu kitandani, akapotelea usingizini. Geb alikesha usiku huo akiomba. Alimlilia Mungu juu ya Nanaa, bila kuchoka. Alitubu kwa kumtelekeza Nanaa na kumfikisha hapo alipo. Geb aliomba usiku kucha.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Usubuhi na mapema James akawa mtu wa kwanza kufika hapo. “Na mimi ndio nimekutana naye hapa hospitalini kaka. Sikuwa hata nikimfahamu. Lakini alikuwa akinifuatilia mimi bila kujua nia yake. Ni juzi ndipo nilikumbuka sura yake na kumbana mpaka akaniambia. Unajua nisingeweza kukuficha kaka yangu.” Nanaa alijikuta akiongea mara baada ya kufungua macho na kumkuta kaka yake amesimama hapo akimtizama. “Sikulaumu. Kwanza anaonekana ni mtu mzuri. Acha kulia bwana.” “Umezungumza naye!?” Nanaa akauliza kwa mshangao. “Alinitafuta jana usiku. Tukapata muda wa maongezi. Anaonekana ni mtu mwenye nia nzuri na wewe. Tumpe nafasi tuone na yeye atafika wapi.” Nanaa hakuamini. Akajifuta machozi.

“Kwa hiyo mmekubaliana naye juu ya hayo matibabu ya huko Ujerumani?” Geb akauliza. “Nimemwambia ni mpaka nikusikie na wewe ndipo tushauriane. Jana siku nzima nilikuwa nina kazi ya kutafuta daktari atakayeweza kumsaidia Nanaa. Nilipiga simu Afrika ya kusini na India. Kote wanaonekana wanaweza kumuhudumia kwa haraka endapo nikijiandaa vizuri kifedha. Napo pia sio garama kubwa sana. Naona tumsikilize yeye, na mimi niwaambie pale nilipofika, ndipo tufanye maamuzi.” Geb alimjua James. Huwa hawezi kutulia linapofika swala la Nanaa.

Lubuva naye akaingia. Baada ya kusalimiana na wote, akamsogelea Nanaa pale kitandani. “Ulilala salama?” “Nimelala kama kachanga. Nimeamka nikala na kurudi kulala tena. Ndio nimeamka tena sasa hivi.” “Afadhali. Nataka kukupima pressure.” Nanaa akatoa mkono. “Lakini nimewakatalia mtindo wakuniogesha hapa kitandani na kunifanya nijisaidie kitandani kama mtoto mdogo. Sitaki tena catheter.” Lubuva akacheka.

“Waliniambia umekataa kurudishiwa catheter.” “Ila usifikiri mimi ni mkorofi. Naweza kujisaidia mwenyewe, sitaki wanifanye kama nipo mahututi au mtoto mchanga!” Lubuva akacheka tu na kumpima. Habari za ubishi wa Nanaa alishazisikia kabla hata hajaanza kumuhudumia. Hakuwa akishangaa. Hata hivyo alijua ni ubishi wa kurithi.

Wakamuona anarudia tena na tena. Wote wakaingiwa na wasiwasi, wakasogea. “Vipi tena!?” Geb akauliza. “Naona pressure yake imeshuka!” “Asante Mungu wangu!” Walimsikia Geb akishukuru huku Lubuva akirudia tena. “Mkono unauma.” Nanaa akalalamika. “Kwa nini umeamini kwa haraka majibu ya pressure kuwa juu, sikukuona ukirudia kupima mara mbili mbili, lakini tumepata majibu ya kuwa pressure ipo chini unashindwa kusadiki!? Acha kumuumiza mkono kwa kurudia kumpima tena na tena. Kuwa na imani Lubuva.” “Lazima kuhakikisha Geb. Kwa aina hii ya pressure, inamaana kuna dawa fulani inabidi nisimpe sasa hivi.” “Basi usimpe. Endapo ikipanda tena, ndipo umpe tena.” “Naona nifanye hivyo.” Wakamuona anacheka.

“Nini sasa?” Geb akamuuliza. “Nilikuwa na wasiwasi sana. Sikutaka mwanzo wangu na Nanaa uwe hospitalini.” “Ulitaka uwe wapi sasa?” Nanaa akauliza. “Kucheza na wajukuu zangu na mambo mengine. Umenizeesha wakati mimi nilikuwa najiona kijana kabisa!” Wakacheka. “Ni kweli umebadilisha mtazamo wangu kabisa Nanaa. Sikuwahi kujiona na kuyatazama maisha kama sasa. Ndoa zangu zote zimekuwa na matatizo sababu sikuwahi kutoa kipaumbele kwa familia au tuseme kwa mtu wa karibu yangu kama hivi hapa. Nilikuwa nikijiwekea ratiba zangu, sitaki zivunjwe. Nitazisimamia na kuhakikisha natimiza bila kukosea. Na mbaya zaidi kazi yangu inanihitaji sana. Hakuna siku ninakuwa nipo tu, au niseme nakuwa sina kitu chakufanya kuanzia asubuhi mpaka usiku. Kwa hiyo kama anavyosema Geb, Mungu asadie utoke hapo. Hata mimi naungana na Geb, Oliva, Magesa na Jimmy kukusubiria. Maisha yangu yote kwa sasa yamesimama, akili ipo hapa.” Ilimgusa kila mtu, zaidi Nanaa.

“Mungu atanisaidia nitapona tu, na tutapata tu huo muda. Naona na kaka amekukubali.” “Nanaa! Huna siri wewe!?” Wakacheka. “Hapana kaka, nilimwambia siwezi kuwa naye karibu kama wewe hutamkubali.” Wakacheka. “Ni kweli umejitoa dokta Lubuva. Binafsi nakushukuru sana. Asante.” Geb akampa mkono. Wakacheka kama waliokumbuka malumbano yao.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Kufumba na kufungua kengele masikioni mwa James zinaanza kulia. Nanaa si mzigo wake peke yake tena. Alishamkabidhi Geb, na sasa baba yake amerudi rasmi, amesimama na mwanae kwa hali na mali. Mchana na usiku yupo pale. Maisha yake yanatakiwa yaendelee au yaanze sasa!? Anajiuliza James. Wanaume hao wawili walioongezeka sio tu kama wanampenda Nanaa, bali pesa ipo na wote wanatamka kumuhitaji Nanaa. Kipi kinamzuia James? Lubuva hakuwa amewapita sana. Ni miaka michache tu. Lakini anao wajukuu kutoka kwa Nanaa, Geb anao watoto kutoka kwa huyo huyo Nanaa ambaye ni kazi ya mikono yake yeye mwenyewe James. Ni wakati wa James kuanza au kuendelea? Yapi yalikuwa malengo yake yaliyosimama sababu ya Nanaa? Nanaa ni jukumu la nani sasa hivi? Ataweza kuwaamini na kuwaachia Nanaa waliyekutana naye ukubwani? Wakamuona anavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu. Akaweka tabasamu usoni. 

Malii!

“Unacheka nini kaka?” “Nimekuletea habari njema. Nilikuwa nikisubiri wakati muafaka kukwambia.” “Nini!?” Nanaa akauliza tena. “Jana jioni, Malii ameingizwa nchini kutokea nchini Uingereza. Alikimbilia kwa binamu yake huko, akajificha. Wamemsaka mpaka wakamkamata.” “Kaka!” “Alinipigia simu yule mwanasheria wako, Mazigo, akaniambia kama nitataka niende nikamuone anavyoingizwa nchini.” “Ulikwenda?” Nanaa akauliza. “Kwa haraka sana. Yaani wote walinikuta nimeshafika pale uwanja wa ndege, na nilihakikisha Malii ananiona na ninampa ujumbe wake. Ametolewa uwanja wa ndege na pingu mkononi. Mazigo hakudanganya.” Nanaa akafurahi sana.

“Hongera kwa kujipigania Nanaa.” “Asante kaka. Nimefurahi mno. Nikitoka hapa nitamtafuta dada Mazigo.” “Nilishamwambia bado upo hospitalini, akuache kwanza. Akasema haina haraka, hata hivyo hukumu yake hawezi kutoka jela.” Hilo nalo likawa jambo jema zaidi.

~~~~~~~~~~~~~~~

Pressure ya Nanaa ikaendelea kujitengeneza kitu kilichowashangaza madaktari wote. Geb alimuomba Mungu akisema afanye kitu si kwa ajili yake tu, bali hata kwa hao madaktari bingwa, wauone mkono wa Mungu kwa waziwazi ili wajue kuwa yupo Mungu awezaye kutenda kwa ajabu. 

Baada ya siku mbili mbeleni, wazazi wa baba yake Lubuva na ndugu zake wengine walikuja kumtembelea Nanaa pale hospitalini. Kweli Nanaa alikuwa akifanana na upande wa baba yake. Nanaa alifurahi sana. Alishindwa hata kuweka kinyongo kwa kumkataa kwa mara ya pili tena, alipopelekwa kwao wakati ni mchanga, baada ya kifo cha mama yake.

Walijawa toba na kila wakati walieleza majuto yao. Babu yake ndio akaongea kama alivyosema Nanaa. Anatamani asingemkataa Wini moja kwa moja ila kuomba mtoto apimwe baada ya kuzaliwa. “Ni ubinafsi tu ndio uliniingia kupitia hofu ya vitisho vya dada yake Wini. Ambapo pia najiambia, ningeweza kuzungumza naye ili kumtuliza tu. Nilikosa Nanaa mjukuu wangu. Nisamehe mama.” “Hapa nimefurahi mpaka nimesamehe dhambi zenu wote.” Wakaendelea kucheka na kuzidi kufahamiana.

~~~~~~~~~~~~~~~

Baada ya siku 3 tena mbeleni, Nanaa alionyesha kupona kabisa. Yeye mwenyewe ndio alikuwa akihangaika na Jimmy pale wodini na wanae wengine hasa Magesa, Lubuva akaona amtoe. “Naona muondoke tu. Mmepageuza hapa kama shule ya chechea!” Nanaa akacheka sana. Alimkuta Mama G na watoto wote humo ndani mpaka Fili. Alikuta chumba hicho kimechangamka, Nanaa anakimbizana na Magesa akimzuia asiangushe mashine ambazo zilishazimwa muda mrefu, kwa kuwa Nanaa hakuwa akizihitaji tena. Amembeba Jimmy mkononi huku anakimbizana na Magesa mle ndani. Geb alikuwa amekwenda kazini akamuacha Nanaa wakati mama yake anaingia na watoto.

Alitoka hospitalini na kurudi nyumbani akiwa na familia ya upande wa baba yake. Walimtafutia wasichana wa kazi wawili waliokuwa msaada  kwa Nanaa. Upande wa swala la watoto mmoja wao akajitenga akiomba yeye aachiwe watoto tu, akisema anapenda sana watoto. Hiyo ikawa nafuu kwa wote kwani mama G na Fili walikuja kuhamia Arusha kuwa na Grace. Bibi yake Nanaa naye akawa bega kwa bega kwa Nanaa mpaka Nanaa akahisi ni dhamira ilikuwa ikimsumbua kwa kumkataa na kumficha kwa baba yake. Alikuwa akijitoa kupita kiasi.

Grace & Man!

Grace na Man walirudi kwenye fungate kwa muda wa siku 5, ndipo waliporudi kumchukua Fili na mama G, wakahamia Arusha. Mungu alimbariki Grace, akazaa mapacha wengine. Safari hii alizaa mtoto wa kike na wa kiume. Wakike ndiye aliyekuwa mdogo, tofauti na yeye na Geb. Walifanana na Man, kasoro tu macho ndio ungejua ni watoto wa Grace. 

Alifanikiwa kutengeneza ramani inayofanana kabisa na nyumba aliyojenga na Danny jijini Dar, lakini hii ilikuwa na mwanaume waliyependana na kuheshimiana, Man, huko jijini Arusha. Maisha yao yalijawa utulivu, kwani Grace naye aliingia kazini na kumpokea majukumu mumewe. Na huko nako akawa msaada mkubwa kwa Man kama kwenye kampuni ya kaka yake. Mama G alikuwa na kazi ya kulea vijukuu.

 Hakumtafuta tena Danny. Danny akajua hiyo ndio adhabu pekee anayopokea kutoka kwa Grace. Kumpokonya mtoto aliyekuwa amebaki, Fili.

Danny!

Hata hivyo na yeye Danny alijiona hawezi kuwa karibu tena na Fili. Kumbukumbu ya kumpiga kikatili wakati akimkumbusha kufunga watoto mkanda ilikuwa ikijirudia akilini na kwenye mitandao. Danny alichafuliwa na ushuhuda wa mtoto wake mwenyewe, akisimulia hatua kwa hatua kilichokuwa kikiendelea ndani ya gari mpaka mauti ya wadogo zake.

James ndiye aliyemuhudumia kuanzia yupo hospitalini, mpaka akatolewa akiwa anatumia magongo. Aliishi nyumbani kwa James mpaka alipopona kabisa ndipo akatafuta kwake. Alianza maisha akiwa hana mke, wala watoto kama kijana mdogo ambaye ndio amemaliza chuo, wakati umri ulishakuwa umekwenda. Hawakuwa na tofauti na James tena. 

Sara hakumtafuta tena na yeye hakutaka kumtafuta tena Sara. Sara alimuachia madonda ambayo hayakuwa yakitibika au kusahaulika kamwe. Alimlaumu kwa mengi, zaidi kusababisha kifo cha wanae. Na Sara naye aliogopa hata kukutana na rafiki za Danny au Grace, akijua atakuwa akitafutwa na vyombo vya usalama ili kujibu shutuma zilizokuwa zimeenea mitandaoni.Kusababisha ajali akiwa anapigana na Danny. 

Mwisho Wa Ubaya.

Ni kweli Malii alikamatwa na kurudishwa nchini akiwa na pingu kama    alivyoahidi dada Mazigo, mwanasheria. Alikaa muda mrefu sana jela kabla ya hukumu yake ya kifungo cha maisha kutajwa. Kwa ufupi maisha yake ndio yaliishia huko. Gozi naye alipewa miaka 35, ambayo ukichanganya na umri wake, angetoka akiwa mzee wakutosha tu. Maisha yasingekuwa na ladha tena. Ni kama naye alipewa kifungo cha maisha.

Safari hii uchawi wa Zinda haukumsaidia. Mwanasheria wa kina Magesa alisuka kesi yao vizuri sana. Na kwa kuwa walishasomewa madhara yatokanayo na kuvunja masharti yale, Zinda naye alipata miaka 6 jela. Hapo ndipo wote wakaelewa ile ‘restraining order’ ya kina Magesa haikuwa ikiongopa na Geb anamaanisha, hataki undugu tena na wao.

Mama James!

Maisha yake yaliendelea jijini Dar kama kawaida. Bar yake ilishamiri na kuweza kumuingizia pesa     ya kutosha. Alimuhakikishia James na baba yake anaweza kujitegemea na wala hakukosea kumuacha mumewe. Hakurudi tena kwa mumewe, akaendelea kuishi na binti zake jijini Dar, huku pesa ikiendelea kuingia bila shida. Zawadi ya kumpokea Wini akiwa amefukuzwa na kila mtu japo kwa manyanyaso ilikuwa nyumba ambayo aliendelea kuishi na binti zake. Napo pia akawekeza hapo. Akatengeneza fremu za maduka mbele ya nyumba hiyo, maisha yake yakawa yakusaka pesa tu.

Mahusiano yake na James hayakuwahi kupona. Bado James alimlaumu kumkimbia baba yake, tena akikumbatia dada zake bila kuwashauri vizuri. James ndiye aliyebaki na mahusiano na baba yake. Akimtunza na kumtembelea.

Nanaa & Geb

Maisha ya Nanaa na Geb, yalijawa baraka na amani. Kale kaukoo kadogo kalipanuka kakaongezwa nguvu na ukoo wa Warangi. Kina Lubuva. Walijaa kwenye maisha yao na wao wakilea wajukuu kwa bidiii zote. Nanaa alisaidia kurejesha ndoa ya baba yake huku akisaidiwa na Geb aliyekuwa karibu na ukajengeka urafiki na Lubuva. Wawili hao walijikuta wana mengi yakufanana na kuzungumza. Vijana waliofanikiwa kwenye fani zao. Pesa ipo na kiunganishi alikuwa Nanaa anayewahusu wote kwa karibu.

Geb alimuweka sawa Lubuva na kusisitiza umuhimu wa baada ya mahangaiko yoote ya siku nzima, lazima kuwe na sehemu anayorudi na kuitambua kama nyumbani na mtu wa kumkimbilia bila kificho, mke. Lubuva akajirudi kwa mkewe na kutengeneza.

Nanaa na Geb walisaidiana kufanya kazi kwa bidii. Ni kweli Nanaa alichukua nafasi ya Grace kikamilifu na kuwa msaada mkubwa kwa Geb. Baada ya Jimmy kufikisha miaka 3, Magesa 4 na dada yao Oliva miaka 6, ndipo Nanaa alipoanza kwenda kazini rasmi. Kabla ya hapo kazi nyingi alifanyia nyumbani akilea watoto na siku chache ndipo alipokuwa akienda kazini. 

Utaratibu wa kwenda kanisani kwenye familia hiyo ya Magesa, ukamuambukiza Lubuva. Na yeye akaanza kuongozana nao kwenda kanisani. Kitendo cha Nanaa kupona bila upasuaji, ukawa muujiza wakumtosha na kumuaminisha Lubuva juu ya uwepo na nguvu za Mungu. Baadaye Geb aligundua kipo kipawa cha uponyaji ndani yake. Japokuwa hakuwa akishinda kanisani, au kufungua kanisa, lakini Mungu alimtumia kwenye mazingira yake. Akabaki akimcha Mungu.

***************MWISHO************

 

 

 kwa simulizi nyingine nyingi na zijazo uwe unatembelea ukurasa wangu wa Facebook wa 

Naomi Simulizi.

(20+) Naomi Simulizi. | Dallas TX | Facebook


CONVERSATION

1 Comments:

  1. Mungu aendelee kukuza kipaji chako dada yangu..

    ReplyDelete