Liv alikuwa amepooza kwenye kiti, na ndio walikuwa wanakaribia kuondoka. “Liv!” Aliita taratibu. “Mama!” Liv akasimama kwa haraka. “Beba mama!” “Naomba umuweke hapa kifuani.” “Unauhakika Nanaa!? Unaonekana umechoka!” “Muweke tu nijisikie vizuri.” Geb akamnyanyua na kumuweka juu ya mama yake. “Nampenda mama.”Liv akambusu. Wakamuona machozi yanamtoka.
“Nakupenda Liv.
Nakupenda sana mwanangu na ninahamu na wewe!”
Nanaa alijibu kama anayesinzia. Liv akajilaza kwa mama yake. Hata mama G, Grace
na kaka yake hakuwasalimia. Ni kama hakuwaona.
Walishazoea Nanaa akilazwa ndio mtoa stori. Watacheka wakati wote. Lakini Nanaa wa safari hii hakuwa hata akiongea. Kidogo wakaingiwa na wasiwasi. Alikuja kuamka tena usiku. “Vipi?” Geb akasimama na kumbusu kichwani. “Najisikia vizuri.
Ninahamu na wewe Geb!” “Hata
mimi. Pona bwana tutoke hapa.” “Endelea kuniombea. Najisikia mwili mzito”
“Nakuombea sana.” Nanaa akatulia kama anawaza. “Vipi?” “Liv alikuja leo?”
“Tulishinda nao wote hapa.” “Na kaka zake!?” Nanaa akauliza. “Wote walikuwa
hapa. Mama, James, Grace, Liv, Magesa na Jimmy. Tulipewa Jimmy karibia siku
nzima. Magesa pia amembeba.” Nanaa akacheka. “Atamuangusha!” “Ungemuona
usingekubali. Alimbeba kwa nguvu zote. Amembusu weee, mpaka tukamchukua.”
“Atakuwa amempaka mwenzie mate!” “Kila mahali.” Nanaa akacheka.
“Na
Liv wangu!” Nanaa akauliza tena. “Si unajua alivyotulia. Nimemchukua video
wakati anambembeleza Jimmy. Alikaa pale kwenye kochi. Akataka tumuwekee.
Alikuwa anambembeleza bila hata ya Jimmy kulia. Magesa ndio aliwavuruga. Alikuwa
anamtaka Jimmy kila wakati.” “Jamani Magesa!” “Halafu sasa yeye hawezi kutulia.
Anataka akipewa, ashuke naye chini.” Wakazidi kucheka. “Naamini kesho nitakuwa
sawa niwaone. Nimepitwa.” “Nimekuchukulia video, uone fujo za kaka mkubwa.”
Wakati wanazungumza, dokta Lubuva akaingia.
Dokta Lubuva.
Lubuva
akamsogelea Nanaa pale kitandani. “Unajisikiaje?” “Una duka la madawa karibu na
maeneo ya Tabata Barakuda?” Nanaa akamuuliza bila yakujibu swali. Geb akabaki
kimya akisikiliza. “Hapana.” Lubuva akajibu kwa kifupi. Lakini Nanaa akabaki
akimtizama kama ambaye hajaridhika. “Unaishi maeneo ya huko?” Nanaa akauliza
tena. Kimya. Lubuva hakujibu, akabaki akimtizama. “Unajisikiaje?” Lubuva
akauliza tena huku akiendelea kumpima. “Kuna siku nilikwenda duka la madawa,
kuulizia dawa ya kuzuia maziwa yasitoke. Niliyemkuta akiuza akaniambia hamna
dawa. Nakukumbuka kabisa, ulikuwa umesimama pembeni ya lile duka ukiwa kama
unatumia simu yako, ukaongeza kuwa naweza kupata homa, ninywe dawa ya kupunguza
maumivu na kushusha homa kila baada ya masaa 6. Kisha ukasema kuna dawa ya
asili, niweke maganda ya kabichi mabichi, yaliyowekwa kwenye friji. Kisha
ukaendelea na kitu ulichokuwa ukifanya kwenye simu yako.” Nanaa akaendelea
taratibu.
“Nakumbuka
siku nyingine kama baada ya siku tatu tokea unipe ule ushauri, nilikuwa
nimezidiwa na pressure. Nakwenda hospitalini. Nilikuwa nimekaa kituo cha
daladala. Pale pale Tabata Barakuda. Ukaja ukakaa pembeni yangu. Nakumbuka
nilikuwa nimejiinamia tu. Daladala ilipokuja, ukanistua, na kunisaidia kupanda
kwenye daladala. Nilikuwa natetemeka sana nusura kuanguka. Tena nakumbuka
ulisisitiza nipande taksii, nikakukatalia. Najua unakumbuka. Na haupo hapa kwa
bahati mbaya. Wewe ni daktari wa upasuaji. Tena nimesikia wakikusema ni bingwa.
Kwa muonekano tu, hufananii kuwa ni mtu unayepanda daladala. Lazima una gari.
Hiyo ni moja. Pili, kwa hadhi yako wewe, huwezi kuwa unasimama kwenye maduka ya
madawa, tena Tabata, ukiwa unacheza na simu mchana, siku ya kazi au kuwa
unalala hapa na mimi na kunitembelea kila wakati. Lazima unanifuatilia mimi.”
Hapo Geb akakaa sawa.
“Nimejaribu
kukufikiria sana. Na kwa muonekano wako sasa hivi, baada ya kukwambia haya
yote, inamaana nimepatia. Sijakosea. Sasa kwa nini unanifuatilia?” Nanaa
akamuuliza taratibu huku akimtizama kwa makini. Kimya. “Wewe ni nani na kwa
nini unanifuatilia mimi? Unataka nini kwangu au kwa familia yangu?” “Ukipata
nafuu kabisa, tutapata muda wakuzungumza.” Lubuva akajibu. “Basi utajulishwa
nitakapopona ili uje kuzungumza na mimi. Lakini hapa sitaki kukuona tena na
wala usiniguse.” “Sina nia yakukudhuru Nanaa. Mimi ndiye niliyekufanyia
upasuaji. Nimekuwa…” “Ukilala na mimi tokea nitolewe chumba cha upasuaji?”
Nanaa akamuuliza. Lubuva kimya. “Najua.” Nanaa akaongeza. “Geb, mpigie simu
dokta Lyamu mwambie aje au anitafutie daktari mwingine. Naomba wewe uondoke.”
“Nanaa!” Lubuva akamwita akiwa ameishiwa nguvu.
“Hakika
sikutanii. Hutanigusa tena mpaka nikujue wewe ni nani.” “Huwezi kupata daktari
mzuri atakayeweza kukusaidia kama mimi.” “Ndivyo unavyojidanganya!?” Nanaa
akamuuliza. “Ungejua nusu tu ya historia yangu ya maisha, ungeelewa wala si kwa
nguvu zako ndio maana nipo hapa. Wewe si mungu mtu kama wanavyokuita.
Hata usingekuwepo hapa leo, na Mungu angekusudia nipone, angetumia hata nesi
kuniponya. Nishapitishwa kwenye maradhi ambayo hayakuwa na matibabu. Madaktari
walishindwa jinsi yakunitibu. Hivi unajua Mungu mwenyewe alituma malaika wake
kuja kunitibu? Mikono hiyo ya Geb ambayo haijui hata kushika sindano, Mungu
aliitumia kuniponya! Toka hapo mlangoni, halafu rudi hapa baada ya kesho kutwa
kama utanikuta hapa kitandani. Nenda.” “Nipe siku ya leo, halafu kesho
tuzungumze vizuri.” “Kwa nini?” Nanaa akamuuliza.
“Unahitaji
kupumzika.” “Hivi unajua kama nimelala hapa siku nzima? Hata wanangu
walipoletwa nilishindwa kukaa nao.” “Nafahamu Nanaa. Hakuna kinachoendelea hapa
kwako, mimi nisijue.” Nanaa akakunja uso. “Wewe
ni nani!?” Nanaa akazidi kuchanganyikiwa.
“Habari kamili za Wini nilikuja kuzipata hata miaka
minne haijaisha. Sikuw.. .” Nanaa akawa ameelewa kila kitu. Akajiweka sawa.
“Subiri kwanza. Naomba kukuuliza swali kabla hujaendelea sana. Samahani lakini,
nakukatiza kwenye maelezo yako. Najua unayo stori nzuri sana ambayo umeiandaa,
ungependa kuisema au ulitaka niisikie. Lakini kuna kitu kilikuwa kikinisumbua
tokea nakuwa, au tokea napata fahamu zangu, vile mama mkubwa alivyokuwa
akiniambia kila wakati kuwa mimi ni mzigo ambao hajui atautua lini. Nikawa
najiuliza, ilikuwaje mpaka mimba yangu ikashikwa? Nilipata majibu nusu nusu
kutoka kwa mama mkubwa lakini hayakuwa yakinitosheleza kwa kuwa alikuwa
akiongea kwa jazba akiwa ananitukana au akinilalamikia. Yaliniacha na shauku
yakutaka kujua zaidi. Aliniambia ulinikataa mimi na mama. Sasa nikawa
najiuliza, ni mazingira gani au ya namna gani mimba yangu ilishikwa?” Nanaa
akauliza.
“Labda
nikupe mfano. Na mimi nilifanya kama alivyofanya mama. Nilishika mimba zote nje
ya ndoa. Lakini tokea mtoto wa kwanza niliyemzaa, baba yake alipojua tu,
alikuwa akimng’ang’ania yule mtoto. Na usifikiri ni kwa huyo mtoto wa kwanza
tu, mpaka wa pili. Na usifikiri ni Geb mwenyewe, na mama yake hivyo hivyo. Wanang’ang’ania
wanangu kuliko nitakavyokueleza. Watoto wangu ni kama alumasi kwao.
Nilipokosana nao au nilipowakosea, walinipokonya watoto wangu. Kwa upande wangu
mimi walinitenda ubaya sana, lakini kwa upande wa watoto wangu, ni kwa ile
thamani waliyoona kwa wale watoto. Yule mama alikuwa halali mchana wala usiku
akilea watoto wangu mimi niliyewaudhi. Peke yake bila msaada wangu wala Geb
mwenyewe. Yule mama alikuwa akihangaika na watoto niliowazaa mimi! Tena akiwa
mgonjwa. Sijui kama unanielewa? Mimi nilikuwa mbaya sana kwao, lakini sio wale
watoto. Yaani mimi hata nikifa leo, sina hofu ya watoto wangu, najua upendo
unao wazunguka. Watoto wangu wanavalishwa vitu vya thamani kutoka kwa bibi yao
na shangazi yao. Sikumbuki mimi kutoa pesa yangu na kumnunulia Liv hata hereni.”
“Nguo
na viatu anavyoleta shangazi yao, huwa natamani angekuwa akinipa mimi hizo
pesa. Ni garama, na yule mtoto ni msafi kuanzia kichwa mpaka mguu. Kazi ya bibi
yake na shangazi yake. Hata nikiwepo mimi nyumbani, bibi yake huwa
anamuhudumia. Na yeye anajua Liv. Kuna vitu anajua hivi ni bibi ndio
ananifanyia wala si mtu mwingine. Ule ukaribu na mahusiano aliyonayo bibi yao
na wale watoto, au shangazi yao, ni ajabu sana. Na hawana unafiki wala kusema
wanajitahidi kumfurahisha hata Geb. Wanafanya kutoka moyoni. Kwamba wale ni
watoto wao. Sasa hicho kitu nacho kikazidi kunishangaza na kuzidi kuibua
maswali. Nikawa najiuliza, hivi
ilikuwaje mpaka mimba yangu ikashikwa? Au na mimi ni mmoja wa wale
watoto wanaoitwa ni wa bahati mbaya!? Yaani mwanamke anashika mimba inakuwa
kama amebeba mkosi! Linakuwa kama tatizo la kuhatarisha maisha ya mtu, hasa
mwanaume aliyempa mimba! Yaani kuna kuwa na mipango ya muhimu sana mbeleni,
halafu katikati ya starehe, mimba inatungwa, na inakuwa ni jambo baya sana la
kuharibu maisha au mipango ya watu!” Nanaa alibonyeza kitanda chake ili akae
vizuri.
“Naomba
utulie Nanaa. Bado hicho kichwa hakijapona vizuri.” Dokta Lubuva alijaribu
kumtuliza. “Halafu kweli tumefanana! Yaani sasa hivi nikikuangalia ndio naiona
sura yangu hapo kwako.” “Unatakiwa kuchukulia mwili wako taratibu. Upasuaji
uliofanyiwa ni mkubwa sana.” “Lakini binafsi nimefurahi kukuona. Muulize Geb.
Nilikuwa nataka kukutafuta ili nikuone tu sura yako. Ungeniambia tu mapema,
kuliko kunifuatilia nyuma kimya kimya.” Kimya.
“Halafu
wewe ni rafiki na dokta Rweta? Yule daktari wa mambo ya moyo au na pale
ulikwenda siku ile kwenye kliniki yake ili unione tena?” Nanaa akamuuliza.
“Yaani sasa hivi ndio nakukumbuka vizuri sana. Kuna siku tulikwenda kwake, na
wewe ulikuwepo ofisini kwa dokta Rweta. Nilikuwa na mama. Hukuzungumza neno
hata moja. Ulikuwa kimya kabisa kama unayesoma kijalida fulani hivi. Ila
alikutambulisha kama daktari mwenzake, tusiwe na wasiwasi na uwepo wako pale.
Tukazungumza naye, akanipa ushauri baada ya maswali mengiii. Mpaka nikamstukia
na yale maswali! Nikamuuliza mbona ananiuliza maswali kana kwamba ndio ananiona
kwa mara ya kwanza wakati mimi ni gonjwa wake wa kila siku? Unakumbuka?” Nanaa
akamuuliza Lubuva.
“Sisi
tukaondoka na kukuacha pale pale ofisini.” “Rweta ni rafiki yangu. Nilijua kuwa
yeye ndiye anayekutibu pia. Nikataka kujua historia yako kutoka kwako wewe
mwenyewe. Vile unavyojisikia baada ya kubadilishiwa dawa. Kama zinaendana na hali uliyokuwa nayo kwa wakati ule au la.
Ndio maana nilimpa yale maswali akuulize, ili
nikusikie wewe mwenyewe kwa wakati ule. Ili niweze kutafuta ushauri
zaidi kwa marafiki zangu niliokuwa nikifanya nao kazi zamani.” Dokta Lubuva
akajibu.
“Sasa
kwa nini hukutaka kuniuliza wewe mwenyewe?” Nanaa akauliza. “Ulikataa Nanaa.
Dokta Lyamu alipokwambia kuna daktari mwingine mzuri anaweza kukuona,
unakumbuka ulikataa ukasema hutaki kubadilisha madaktari? Tena Lyamu alikuja
kunijibu kuwa ulimwambia amwambie Rweta aje ajifunze kwa huyo daktari mwingine
mzuri, alafu yeye Rweta ndio akutibu wewe. Wewe hutaki kubadilishiwa
madaktari.” Hapo Nanaa akakumbuka na kunyamaza.
“Sasa
kwa nini hukujitambulisha muda wote huo? Au ulikuwa ukinichunguza kwanza ili
kujua kama nina shida kiasi gani? Kama nastahili kuwekwa karibu kwenye ufalme
wako au la! Nisije kukufilisi!?” “Hapana. Hata kidogo. Nili…” Akasita.
“Nakusikiliza.” Lubuva kimya. “Kama huna kitu cha kuniambia, mimi naomba
niulize swali jingine, japo nimejua unachagua kipi chakujibu na kipi uache.
Umeoa?” “Ndiyo. Na nina watoto wawili. Au una wadogo zako wawili wakike na
wakiume.” Nanaa akacheka taratibu huku akimtizama kwa makini.
“Sasa
mimi leo nimelala siku nzima. Naomba ukae hapo uanze kunisimulia stori zako
zoote na mimi nikuulize maswali juu ya mama yangu. Maana sikuwahi kupata mtu
anayemfahamu mama yangu vizuri na akawa tayari kunieleza juu yake. Si unajua
alikufa wakati anajifungua?” Nanaa akamuuliza.
“Nafahamu.”
“Ni kweli unafahamu kwa kuwa nililetwa kwenu mkanikataa.” “Nilikuwa
nimeshaondoka.” Nanaa akacheka. “Naomba basi ukae ili unipe stori ya upande
wako. Inayohuzunisha na kukuonyesha hukukosa. Wini ndiye aliyekosea.
Alishika mimba kizembe. Alikuletea taarifa ukiwa na malengo ambayo hayakuweza
kusubiri. Ulishakuwa na VISA tayari ya kwenda kusomea udaktari. Ulishitukizwa!
Mlikuwa watoto sana, mimba ikaingia kwa bahati mbaya! Wini alikuwa na wanaume
wengi! Au stori yako wewe haiendani na moja ya
hizo hapo?” Geb kimya.
“Basi
kama zinaendana na hizo, huna haja yakurudia. Naomba unisaidie kumfahamu mama
yangu. Ninakuwa nikimfikiria sana na wakati mwingine nakuwa nikimuhurumia.
Angalau wewe uliweza kunikana na kunikimbia, lakini yeye alionekana kushindwa
kunikimbia. Si unajua angeweza hata kutoa mimba? Angalau kuficha aibu na yeye
akajiweka huru kama wewe. Sasa huwa namfikiria sana. Kwa umri ule, akiwa na
shida, hana pakwenda, lakini alihangaika na mimi mpaka mauti. Natamani kusikia
upande wake mwingine mbali ya habari nilizozisikia kutoka kwa watu waliokuwa na
hasira naye.” Kimya.
“Usiniambie
kama hata humkumbuki!!” Nanaa akashituka sana. Akakunja uso. “Nakumbuka.” “Sasa
mbona hunijibu, umebaki tu kimya!? Unazo picha zake?” Kimya. “Kwani nyinyi
mlikuwa mkikutana wapi huko ambako mlikuwa hampigi hata picha!? Au hapakuwa na
mahusiano, ulipita tu ndio akashika mimba?” Kimya. Hasira zikampanda Nanaa, na
Geb akajua. Akamsogelea karibu. Maana alimpisha dokta Lubuva azungumze naye,
pale alipoingia.
“Labda
niulize hivi, wewe ulikuwa ndio mwanaume wake wa kwanza au ni kweli vile
ulivyosema wakati unamkataa kuwa alikuwa na wanaume wengine? Namaanisha sio
wewe uliyemtoa bikra yake, kwamba ulimkuta..…” “Nanaa! Hapo unavuka mipaka.
Naomba upumzike utaendelea wakati mwingine.” “Nataka kujua Geb. Mama alikufa akiwa mtoto mdogo sana. Na yeye
alimkataa akisema asipewe mzigo ambao sio wake. Mzigo huo ndio mimi.
Akidai hakuwa peke yake kwa mama. Ndio
nataka kujua kama ni kweli au la! Hanijibu kitu, anakuwa kimya. Sasa kwa nini
alinikataa na kwa nini amerudi nakunifuatilia kila mahali! Kwa nini yupo hapa?” Geb akamvuta mkono na kuushika.
“Leo
umeletewa watoto wote hapa, umeshindwa hata kuwatizama au hata kujua kama
walikuwa hapa. Jimmy ameshinda hapa, umeshindwa kunyonyesha kabisa. Mimi
nakufahamu linapofika swala la watoto wako, Nanaa. Kushindwa kuwa na watoto leo
siku tuliyoambiwa wanaweza kuletwa, ni kwa kuwa ni kweli hujisikii vizuri. Sasa
hivi haupo kwenye nafasi ya kupokea ukweli wowote wa nyuma. Tena uliokuumiza.
Nataka turudi nyumbani ukiwa umepona. Kwa kesi hiyo unayotaka kuianzisha hapo,
ni njia nzuri sana yakukupandisha pressure, na hapa hatutatoka leo wala kesho.
Tutaendelea kutesa watoto. Wote tunakusubiri wewe. Mimi, Liv, Magesa na Jimmy.
Wote sisi maisha yetu yamesimama tunakusubiri wewe. Kwa hiyo nakuomba sana
Nanaa, kipaumbele iwe ni kupona na kutoka hapo. Mengine yatafuata. Maadamu
umeshajua ni wapi pakupata majibu ya maswali yaliyokuwa yakikukera sana, naomba
uendelee kusubiri.” Wakamuona anabonyeza kitanda. Kikaanza kushuka upande wa
kichwa taratibu. Geb akamfunika, na kumbusu kichwani. “Asante.” Geb
akamshukuru.
“Nasikia usingizi. Nataka kulala.” “Unaweza
kujaribu kula tena kidogo?” Nanaa akafikiria kidogo. “Naona nilale kidogo, nimeshajitibua. Nina
hasira sana. Nimekasirika Geb. Naona nilale tu, ili pressure isipande zaidi.” “Pole. Ukitoka hapa utapata muda wakutosha wakuuliza
maswali yote. Lakini kwa sasa naomba lengo liwe ni kupona na kutoka hapa.
Sawa?” Nanaa akanyamaza. Akamuona
anavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu akafunga macho. Geb akaanza
kumpangusa machozi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Ni
kwa nini analala hivyo!?” Geb akamgeukia Lubuva aliyeshindwa kujibu maswali ya
Nanaa. “Madawa anayopewa yanachangia kumfanya alale.” “Madawa ya nini tena!?”
“Nanaa ni mgonjwa Geb. Kufanyiwa upasuaji wa kichwa sio kwamba ndio amepona.
Kumbuka bado moyo wake ni mkubwa. Hapo bado hajatibiwa hilo. Ametoka
kujifungua, amepoteza damu nyingi tu, na bado mwili haujarudia hali yake.
Kumbuka pia mimba yenyewe alibeba akiwa mgonjwa. Halafu kufunguliwa pia kichwa
kwenyewe anahitajika muda wakutosha kupona kabisa. Lazima awepo kwenye dawa
kutuliza maumivu, kufanya pressure iwe sawa na kurudisha huo mwili wake kwenye
hali ya kawaida. Anahitaji muda.” Geb akamtizama Nanaa.
“Lakini
baada ya hapa, unafikiri atapona kabisa?” “Nimekuona ukiomba sana Geb. Weka
imani yako kwa Mungu. Hata hivyo alivyo sasahivi, ujue ni muujiza. Kesi nyingi
kama za Nanaa, watu huishia kufa au hata wakiamka wanakuwa wamepoteza
kumbukumbu kabisa. Lakini unamuona jinsi anavyopona kwa haraka? Hata jinsi
anavyozungumza leo nitofauti na jana. Wengine inawalazimu kufanyiwa speech therapy ili kurudisha uwezo wao wakuzungumza tena. Kwa
hiyo anahitaji muda na kuruhusu ahudumiwe na watu wenye uwezo wakutibu tatizo
lake.” Geb akawa amemuelewa.
“Lakini
sidhani kama wewe ni mtu sahihi kwa sasa wakuendelea kumtibu Nanaa.” “Nafahamu.
Lakini nakuhakikishia Geb, utataka mimi ndio niwe karibu na Nanaa. Kila
utakayemuuliza, atakwambia hivyo hivyo. Mpigie simu dokta Lyamu na Rweta,
watakwambia mimi ni mtu sahihi ambaye unamuhitaji kwa Nanaa.” “Lakini ni kama
kazi yako iliisha! Wewe si ni daktari wa upasuaji tu? Naomba nitafutie daktari
unayefikiri ana uwezo wa kumtibu Nanaa, ila usiwe wewe. Utamfanya Nanaa
achelewe kutoka hapo kitandani. Anazidi kupandisha hasira. Atataka kujua ukweli
ambao najua kwa sasa hana uwezo wa kupokea ukweli wowote ule kutoka kwako,
atazidi kujiumiza tu. Na mimi najua hataweza kuendelea kunyamaza. Ni mambo yaliyokuwa
yakimuumiza sana. Ndio habari za kwanza kuniambia mimi siku ya kwanza kabisa napata
nafasi ya kukaa chini na Nanaa na kuzungumza naye.” Geb akaendelea.
“Nitakulipa
pesa yako yote ya matibabu uliomfanyia Nanaa. Hata sasa hivi unaweza kuniletea
bili nikulipe ili tu uondoke. Sitaki akiamka akukute wewe. Utazidi
kumchanganya. Tafadhali nitafutie dakatri mwingine. Yeyote na kwa bei yeyote
ile, ila sio wewe. Unaweza kuja kurudi wakati mwingine wowote, lakini
sio sasa hivi akiwa mgonjwa.” “Geb, najua na wewe umesikia upande mmoja wa
maisha ya Nanaa, na umenichukia sana na kuniona mimi ni mnyama. Lakini
nakuhakikishia mimi ni mtu sahihi kumtibu Nanaa. Nipo hapa kama ‘neurosurgeon’
lakini nina timu ya madaktari bingwa wa Ujerumani, wapo nyuma yangu, wapo na
mimi muda wote na wakati wowote nitakao wahitaji kwa ajili yakumtibu Nanaa.
Nipo nao kwenye simu mchana na usiku wakinishauri jinsi yakumtibu. Kila tatizo
alilonalo hapo Nanaa, nimetafuta daktari bingwa huko Ujerumani, ndio wana mtibu
hapa.” Lubuva akajibu na kuendelea.
“Na
naomba nikuhakikishie Geb, sina shida na pesa yako hata kidogo. Natengeneza
pesa nzuri sana. Kwa kuwepo kwangu mimi hapa hata nusu saa tu, ujue napoteza si
chini ya milioni ya kitanzania. Nalipwa kwa kazi ninazofanya kwenye
mahospitali. Tokea siku Rweta ananipigia simu na kuniambia Nanaa yupo chumba
cha upasuaji, amepoteza fahamu baada ya kujifungua, Lyamu akiwa hajui kama
alikuwa na uchungu siku nzima. Maana nilimuomba Lyamu amfuatilie kwa karibu
sana ili asishikwe na uchungu, maana aliniambia Nanaa mwenyewe amekataa kabisa
kumtoa mtoto ili awekwe kwenye chupa akue. Wakanipigia simu siku ile usiku,
nifike hapa kwa haraka, Nanaa ameletwa, amejifungua na kupoteza fahamu.
Nilipokuwa nikiwalaumu, waliniambia ni kama Nanaa mwenyewe alificha swala la
uchungu. Hata wewe alikuficha ukashitukia chupa imepasuka tu mkiwa nyumbani. Si
ndio hivyo?” Geb akakubali.
“Sasa
nakuhakikishia Geb, tokea siku ile mpaka leo nimesitisha safari zote za nje ya
nchi. Huwa nasafiri nchi mbali mbali hasa hapa barani Africa, kwenda kufanya
nilichomfanyia Nanaa, nakurudi hapa. Mimi mwenyewe najijua ni mzuri. Utaalamu
ninaotumia mimi, bado haujafika hapa Africa. Nimeufanyia kazi huko nilikokuwa
Ujerumani, kwa muda mrefu sana na kupewa ‘awards’ nyingi tu. Kwa
mweusi kupata award kwenye nchi kama
Ujerumani, utakubaliana na mimi kuwa ninajua ninachokifanya. Na ndio maana
wananiita mungu mtu. Sio mimi najiita hivyo. Ni kwa kuwa utaalamu
ninaotumia kwenye upasuaji wangu kwa wagonjwa, ilikuwa inawalazimu kusafirisha
wagonjwa wao nje ya nchi ili wakafanyiwe kile ninachowafanyia mimi kwa bei
nafuu.”
“Nimekuja
na vifaa vyangu na bado ninaingiza vifaa hapa nchini. Serikali imeniunga mkono,
inakubali na ninachofanya. Hata Afrika ya kusini wananitumia sana. Ninayo
kliniki na wagonjwa ninao wahudumia kama hapa. Kwa hiyo Geb, bado nasisitiza,
mimi ni daktari sahihi kwa Nanaa na wala pesa sio sababu inayonifanya niwe
hapa. Kwa mimi kuwepo hapa kwa Nanaa, ujue ninapoteza pesa nyingi sana zaidi ya
utakavyoweza kunilipa wewe.” Lubuva akaweka msisitizo.
“Weka
mbali tofauti zetu zote, mfanye Nanaa akubali mimi nimuhudumie. Dokta Lyamu
alishanieleza zaidi juu ya Nanaa. Amenihakikishia wewe ukiwepo, Nanaa atakubali
matibabu ya aina yeyote ile. Amefika hapo alipo, kwa kutopata matibabu sahihi
tokea mwanzo. Nakuhakikishia Geb, hutaki kunikwepa. Kama kweli unamtaka Nanaa
kwa kiasi nilichokuwa nikikuona ukipiga magoti pale nje ukiomba mchana na
usiku, nakuhakikishia mimi ni majibu yako kutoka kwa Mungu wako.
Usinifukuze. Sihitaji hata shilingi yako, ila kuwepo tu hapa.” Geb akavuta
pumzi kwa nguvu na kumtizama tena Nanaa.
Lubuva Afunguka Kwa Geb.
Geb
akamgeukia tena Lubuva aliyekuwa akiwatizama yeye na Nanaa. Ulikuwa wapi muda wote huo? Kwa nini
unajitokeza sasa hivi?” Geb akauliza kwa hasira na kulalamika kidogo. “Kwa nini
hukutokea kabla ya haya yote ili kuwekana sawa na Nanaa?” “Najua unafahamu kwa
kiasi watu waliomlea Nanaa.” Geb akanyamaza. “Kitendo tu chakujua mtoto aliyemwacha
Wini anaitwa Nanaa, imenigarimu kupita nitakavyokwambia. Haya, kujua napo alipo
pia imegarimu muda na pesa yakunifanya nijisikie nimelipa garama. Niliambiwa
nilazima kulipia pesa ya matunzo yake, mpaka maziwa aliyomnyonya mama
yake mkubwa pia niliambiwa nilipe ndipo niweze kujibiwa swali la kuwa yupo wapi
mtoto mwenyewe, aliyeachwa na marehemu Wini.”
“Mbona
na mimi nilishalipia hiyo na wakasema hawamdai tena Nanaa!?” Geb akashangaa sana.
“Najua. Na waliniambiwa kama na wewe ulilipa, tena mliomba mpunguziwe. Sasa akasema alikubali kupunguza kwako, kwa
kuwa wewe huusiki na Nanaa. Sasa hiyo garama yangu mimi kama baba yake!” Lubuva
alicheka kwa kusikitika.
“Nilipewa
orodha hiyo. Kuanzia siku namkana Wini mpaka siku Nanaa anahamia nyumbani kwako
wewe. Nilitakiwa kulipia kuanzia garama za usafiri aliotumia siku alipomleta
Wini akiwa mjamzito nikamkana mbele yake. Alipomleta tena Nanaa akiwa kichanga
pale nyumbani na kufukuzwa. Haya, fidia ya kutunzwa Wini mwenyewe akiwa
mjamzito wa mtoto wangu, mazishi yake Wini, ndipo ikaja sasa garama za Nanaa
mwenyewe. Matatizo aliyopitia huyo mama mwenyewe wakati anamlea Nanaa. Fidia za
biashara zake zilizokufa wakati akimlea Nanaa. Pesa aliyopoteza James kwa Nanaa
na si kwa mama yake na ndugu zake. Ada za shule, nguo, mpaka pesa ya chupi
alizonunuliwa Nanaa, nililipishwa ili tu kujua Nanaa alipo.” Geb hakubisha
katika hilo. Alimjua mama yake James.
“Tunapozungumza
hivi sasa hapa, ndoa yangu ipo matatizoni sababu ya mama yake mkubwa Nanaa.
Jumla ya hiyo pesa yote ilikuwa zaidi ya milioni 250. Akasema nimjengee nyumba
hapa Dar.” “Haiwezekani! Kwa nini usimtafute mumewe!?” Geb akauliza. “Nakwambia
nilianzia nyumbani kwao. Yule mzee hakuwa mnafiki. Alinieleza ukweli bila
kinificha. Akaniambia hakumtaka kabisa Wini. Alimfukuza pale tokea siku ya
kwanza amekwenda kuomba hifadhi. Lakini mkewe akamkubalia akae hapo mpaka
atakapojifungua, ndipo aondoke. Akaniambi hajawahi kujihusisha naye Wini, wala mtoto wake ambaye ndio Nanaa. Lakini
yule baba aliona shida kutaja jina la Nanaa mdomoni kwake. Akaniambia hajawahi
kujihusisha na hao watu wawili, Wini na mwanae, mpaka Mungu alipoamua kuwaondoa
hapo nyumbani kwake. Mama mtu kwa kifo, mwanae hajui habari zake. Akasema mkewe
alimkimbia yeye na binti zake wawili. Anasikia wapo wanaishi Dar, na wao ndio
wanataarifa kamili za mtoto wa Wini.”
“Hakukwambia
kuwa mwanae James ndiye aliyehusika na maisha ya Nanaa?” Geb akauliza.
“Aliniambia kwa hasira na kunitukana juu. Huku akinilaumu kuwa mimi nilikana
huyo mtoto ili maisha yangu yaendelee vizuri. Matokeo yake nimeharibu maisha ya
mtoto wake wa pekee wa wakiume, James. Yeye ndiye aliyebeba mzigo niliokuwa
nimekimbia! Maisha yake yameharibika sababu ya mtoto wa Wini. Tena akanionya
kwa vitisho vikali sana, nisiwahi kumtafuta tena James na nisithubutu
kumwingiza kwenye maisha yangu mimi na mtoto wangu.”
“Akanieleza
ugomvi mkubwa kati ya James na mama yake ni sababu ya mtoto tuliyemtelekeza sisi.
Akanilalamikia kuwa tokea huyo mtoto ameletwa kwenye hiyo nyumba kutoka huko
hospitalini alipokua ameachwa na Wini, imekuwa ni tatizo kubwa sana. Ni kama
mkosi uliingia kwenye nyumba yao.” Lubuva akaendelea. “Alilalamika akisema James alikuwa mtoto mzuri na mwenye malengo
makubwa sana maishani. Lakini ni kama yote yalikufa na Wini. Akaishia
kuhangaika na mtoto huyo tuliyemtelekeza. Amesahau malengo yake yote.”
“Alisema
mbaya zaidi mtoto aliyenaye James sasa hivi, anayemuhesabu ni mtoto wake ni
huyo wa Wini pekee. Hafikirii kuoa wala kuwa na watoto wake yeye mwenyewe.
Alinifukuza pale nyumbani kwake vibaya sana, na akanionya nisiwahi kurudi tena
pale. Nilimsihi angalau anipe namba ya simu ya mkewe. Tena kwa kumpigia magoti,
hapo alishanitoa ndani kwake. Ndipo akanitajia namba ya simu ya mkewe, tena
akiwa anafoka sana. Niliikariri na kuondoka pale. Nikarudi hotelini na kuanza kumtafuta mama
yake mkubwa.”
“Kwani
nyumbani kwenu nyinyi sio Moshi?” Geb akauliza tena. “Hapana. Kipindi nakutana
na Wini tulikuwa tumehamishiwa Moshi. Baba alikuwa amehamishiwa hapo kuwa mkuu
wa mkoa wa Kilimanjaro. Tukakaa hapo kama miaka mitatu na miezi kadhaa, akapata
uhamisho tena, tukaondoka hapo. Maisha yetu yalikuwa yakuhama hama. Kwa hiyo
Moshi nilikaa kwa muda mfupi tu. Na nilipotoka Moshi, wala sikuhama na familia,
niliacha ndio wanataka kuondoka hapo baada ya miezi michache, mimi nikaenda
kusomea mambo ya udaktari. Nilijua ningesomea udaktari tu na kurudi, lakini
nikapata bahati ya kulipiwa, nikaona niendelee kusoma tu. Nilikuwa mdogo, sina
majukumu au kizuizi chakunifanya nisisome.
Nikaendelea na shule tu. Walipoona nina uwezo mkubwa, wakanishauri
niingie kwenye mambo ya ubongo. Nikapata hospitali iliyokubali kunilipia ada,
kwa masharti yakuwa niwe nafanya kazi chini yao kwa miaka isiyopungua 10.”
“Basi,
pesa ikawa inaingia huku nasoma. Hata kuoa kwenyewe nimeoa miaka michache sana
iliyopita. Sikuwa na muda wakuanzisha familia. Hivi ninavyokwambia hata hao
watoto wawili nilio nao, ni wadogo sana. Nilijaribu kuoa kabla ya mke huyu wa
sasa, nikashindwa. Tukaishia kupeana talaka. Sikuwa na muda wa kitu kingine ila
kazi tu. Akili zangu zote zilikuwa kazini. Muda wa kufanya kazi kwenye hiyo
hospitali ulipoisha na nilipoona uhitaji huku nyumbani unakuwa mkubwa, ndipo
nikaamua kurudi nyumbani nikiwa sina hata wazo la Nanaa au tuseme Wini.”
“Unamaanisha nini?” Lubuva akafikiria kidogo.
Kilichotokea Kati Ya Lubuva Na Wini!
“Sikutaka
kumwambia Nanaa haya mambo kwa undani, ili isimuumize. Lakini acha nikusimulie
wewe. Nitatafuta hekima nyingine yakuzungumza naye. Ilikuwa hivi. Nilimpenda
Wini akiwa kweli binti mdogo. Hata mimi nilikuwa bado mdogo tu. Tukaanza
mahusiano. Ni kweli mimi ndiye nilikuwa mwanaume wake wa kwanza. Tukaendelea na
mahusiano kwa miezi kadhaa, nikamtambulisha kwa rafiki yangu. Wini akaonekana
kuvutiwa naye kuliko mimi. Nikaona mahusiano na yule jamaa yanazidi kuliko
mimi. Na yeye yule jamaa akaanza kama kuchanganywa na Wini.”
“Gafla
akasahau kuwa mimi ndiye mpenzi wake Wini, na mimi ndiye niliyemtambulisha kwa
Wini. Akaanza yeye kuwa akinipa salamu kutoka kwa Wini! Tena akawa mkali
kwangu. Wini akaanza kunikwepa, lakini nikawa nasikia anaonekana mtaani na yule
jamaa. Shule zikifungwa, anatoka kwao anakuja mjini kwa yule jamaa bila hata
kunitafuta mimi, au alikuwa akiomba ruhusa shuleni akidanganya hiki au kile
kuwa anarudi nyumbani kumbe anakuja kumfuata yule jamaa mjini.” Lubuva
akaendelea.
“Ile
kitu ikaniuma sana. Nikajiambia lazima nimtafute Wini, nizungumze naye. Kama
nikuachana, basi anitamkie yeye mwenyewe kama hanitaki tena, anamtaka yule
jamaa, Mchanga mwenzake.” “Kwani wewe ni kabila gani?” Geb akamuuliza.
“Mrangi.” Lubuva akajibu. “Oooh! Watu wa Kondoa?” Geb akauliza. “Hivyo
unavyomuona Nanaa, ndivyo alivyo mama yangu mzazi, ndio maana…” Lubuva akasita
kidogo. “Au subiri nimalizie kwanza. Twende kwa utaratibu.” Lubuva akaendelea.
“Shule
zilipofunga, nikajua yupo likizo, nikamtafuta Wini. Tukazungumza kwa muda
mrefu. Akakiri kuwa alikuwa na mahusiano na yule jamaa. Nikambembeleza sana
turudiane. Wini alikuwa ni msichana wa kawaida tu. Lakini…” Lubuva akasita tena
kidogo, akaona asimalizie alichotaka kukiongea. “Anyway, siku hiyo tukapatana.
Akaniahidi ataachana na yule jamaa, sisi tuendelee. Aliaga kwao anakuja mjini
kwa dada yake. Kwa hiyo tulikuwa na muda mrefu tu. Mambo mengine yakaendelea
kama unavyojua. Ni kweli tulipata wakati mzuri na ahadi ya kuanza upya ikawekwa
hapo. Sasa kilichoniumiza ni kuja kusikia kutoka kwa mdogo wangu, siku chache baadaye kuwa amemuona tena Wini na
yule jamaa, hapo hapo mjini! Hakika nilikasirika Geb. Sikutaka kumtafuta tena
Wini na sikutaka mawasiliano naye kabisa. Hata aliponitafuta, sikutaka
kuzungumza naye tena.” “Ulizungumza naye baada ya kuambiwa alikutwa na huyo
rafiki yako?” Geb akahoji. Lubuva akababaika sana akijitetea. Mwishoe akajikuta
anatulia mbele ya Geb aliyekuwa akimtazama na kumsikiliza kwa makini sana bila
kumwingilia.
“Labda
hapo ndipo nilipokosea. Sikumtafuta na hata aliponitafuta sikutaka kuzungumza
naye tena. Niliona amenidhalilisha. Kuniacha mimi na kutembea na rafiki yangu!
Wini alikuwa akifahamika mpaka na baba yangu mimi. Alijua nilikuwa nikimpenda
sana, lakini akanisaliti. Basi, nikamtumia ujumbe yule rafiki yangu aliyekuwa
amenipokonya Wini, nikamwambia nimemuachia kabisa Wini, ila sitataka kumuona
tena yeye wala Wini mwenyewe. Nikamuonya asije kurudi nyumbani kwetu na
amfikishie huo ujumbe Wini. Wale watu wote wawili wakapotea kwenye maisha
yangu. Ndipo baadaye sasa, miezi kadhaa ilishapita ndipo akaja Wini akiwa
mjamzito na dada yake, wanadai mimba ni yangu!”
“Naomba
tuwe wawazi Geb. Mimi nilikuwa nikijana tu. Ndio mambo yangu ya chuo
yamenikalia vizuri. Mpaka chuo ninachoenda kilikuwa kipo tayari. Visa na tiketi
ipo mkononi, halafu ni nje ya nchi! Ujerumani! Ada ipo inanisubiria mimi kwenda
tu kusoma ili ilipwe! Msichana mwenyewe alikuwa ni kama amemchagua jamaa!
Alishakiri kwangu walifanya mapenzi mara kadhaa, au walikuwa na mahusiano ya
kimapenzi. Nikamsamehe, tukalala siku hiyo moja, nikaambiwa ameonekana tena na
yule jamaa. Mbaya zaidi aliletwa Wini na dada yake, mama James! Kama unavyomjua
yule mama, halafu mbele ya Mzee Lubuva aliyekuwa amehangaika kweli kunipatia
hiyo nafasi ya kwenda nje kusoma! Alikuwa ameshatoa pesa zake nyingi tu ili
mimi niende chuo. Kweli Geb! Hata ingekuwa wewe umesimama kwenye nafasi yangu,
ungefanya kama mimi tu!” “Hapana Lubuva. Kama ingekuwa ni Nanaa huyu, mimi
nisingefanya kama wewe.” Geb alimkatalia bila kupepesa macho.
“Mimi
nina hasira sana, lakini huwa najirudi. Ni heri nife au nikose kila kitu kuliko
kumuachia mwanaume mwingine, Nanaa wangu. Mimi si mkamilifu zaidi yako, lakini
huwa najua ninachotaka maishani. Na nikikijua, huwa nahakikisha nakimiliki kwa
garama zozote zile.” Lubuva kimya. “Ikawaje?” Geb akataka aendelee. Lubuva
akavuta pumzi.
“Niliondoka
nchini. Na nilipofika Ujerumani, nilifanikiwa sana. Nikikwambia nilifanikiwa, nilifanikiwa
haswa mpaka mimi mwenyewe nilikuwa nashangaa. Nilikuwa ‘among of the best Neurosurgeons in Germany’. Nilisoma kwa kuteleza bila kusimama. Tena
nilikuwa nafaulu kwa nafasi za juu sana. Ndani ya miaka 15, nilikuwa
nimeshakuwa ‘Neurosurgeon’.
Tena mzuri. Sikuwa hata na wazo la mapenzi au Wini tena. Ila kazi tu. Nilikuwa
busy mnoo. Wazazi ndio walikuwa wakija kunitembelea, lakini sikuwa nikirudi
mara kwa mara.” Lubuva akaendelea.
“Mzee
alipostaafu, walikuja kuishi na mimi kule kwa muda fulani. Wakati huo nilikuwa
nimeoa mwanamke wa kule. Wakayaona yale maisha yangu. Kazi tu, sina muda na
familia. Wakaniambia lazima kubadilika. Nikajitahidi kupunguza kazi, ndipo
tukapata mtoto mmoja wa kiume, na yeye huyo aliyekuwa mke wangu, alikuwa
daktari. Nikajaribisha maisha ya familia, lakini baadaye tukaishia kuachana tu
na yule mwanamke. Nikarudi tena kazini kwa juhudi zote. Maana huyo mwanamke
aliondoka na mtoto. Lakini kwa makubaliano yakumuona kila ninapotaka. Hapo
hapakusumbua.”
“Nilikaa
muda mrefu kidogo bila kuoa tena. Kelele za mama zilipozidi, nikaamua kurudi
huku nyumbani na kuoa mtu wa hapa. Lakini napo ndoa yenyewe inasuasua. Ni kama
tumetengana. Nafikiri akili yangu ipo kwenye kazi zaidi sina muda na...” Akasita tena. “Turudi kwenye swala la Nanaa.”
Lubuva akabadili tena mazungumzo alionekana kutotaka kuzungumzia na Geb juu ya
maisha yake binafsi ila yanayomuhusu Nanaa na mama yake.
“Hakika
sikuwa na wazo la Wini tena. Nilijua maisha yake yanaendelea. Kwanza niliondoka
nikiwa nimeumia nakumuona ni mshenzi ambaye hakuwa hata akitumia kinga! Amekuwa
na mahusiano na jamaa mpaka kumpa mimba! Nilimsusa na kuendelea na maisha
yangu. Miaka michache iliyopita, mama aliugua sana.Wote tulijua atakufa. Mimi
nikarudi nchini kumuuguza. Na tangia natua uwanja wa ndege, mimi ndiye niliyekuwa
nikilala naye hospitalini.”
“Siku
moja usiku sana, nikiwa naye hapo hospitalini. Tulikuwa wawili tu, usiku wakati
anapewa dawa na muuguzi aliyekuwepo zamu, usingizi ulikuwa umemuishia, mimi
nasinzia kwenye kiti. Kwanza ukumbuke tulikuwa tunatofautiana masaa. Kule
tulikuwa masaa 7 mbele. Muda wakulala kule, huku mnaamka. Nikawa nimechoka
sababu ya mvurugiko wa masaa na mawazo. Kichwa nacho kikawa kinaniuma sababu ya
usingizi wa mang’amu ng’amu. Mawazo na hofu ya kumpoteza mama yangu ndio
ilikuwa inanichanganya zaidi. Nampenda sana mama yangu. Hofu yakufikiri kuwa
atakufa na mimi ni daktari nashindwa kumsaidia nayo ilinizidia, haya, huku nako
nikawa natakiwa kazini, vyote vilikuwa vikininyima utulivu.”
“Anyway,
nikiwa nimelala hapo kwenye kiti akasema, ‘Wini alijifungua. Mtoto
anafanana sana na mimi’. Sasa mimi nikahisi ni kama
sikuwa nimemsikia vizuri. Nikahisi amemtaja ndugu yetu mwingine. Nikaogopa
kumuuliza vizuri, asije akafikiri bado nina mawazo na Wini, kwa kuwa mama
alijua vile alivyokuwa ameniumiza Wini, tena baada ya kujua mimi ndiye nilikuwa
mwanaume wake wa kwanza na nilikuwa nikimpenda sana.” Lubuva akaendelea.
“Tuwe
wa kweli Geb, inauma kuachwa na mwanamke sababu ya mwanaume mwingine. Unahisi
watu wanakuona hufai au unakasoro. Pengine unatatizo kubwa. Halafu nikawa
nimeshaachana na mwanamke wa kwanza pia. Sikutaka kuendeleza yale mazungumzo.
Hasa na mama. Nikanyamaza tu. Lakini kile kitu kikaanza kunisumbua sana. Nikawa
sijui mtu wa kumuuliza.” “Yule rafiki yako uliyemwachia Wini?” “Sikuwa
nimemuachia. Nili..” Geb akamtizama kwa macho yakumsuta. Lubuva akajirudi.
“Alifariki
miaka mingi ilishapita.” Akajibu kwa utulivu kidogo. “Mama alipona. Akaruhusiwa
hospitalini, lakini hakurudia tena yale mazungumzo tukiwa pale hospitalini.
Tulitoka pale yeye akijua bado nimemkasirikia Wini ndio maana sikumfuatiliza
alichoniambia, kumbe mimi sikuwa nimemsikia vizuri na nilisita kumuuliza.”
“Nafikiri neno sahihi ni ‘hukutaka’
kumuuliza zaidi sio ‘kusita’.” Geb
akamsahihisha. “Sawa.” Lubuva akakubali kinyonge bila kubisha. “Ulirudia kosa
kama lile la kwanza.” Geb akaweka msisitizo. “Ha…” Lubuva akataka kubisha,
lakini akaona ajishushe tu.
“Nakubali
nilikosea tokea mwanzo, lakini na mimi ni binadamu Geb.” Geb akabaki akimtizama
kwa muda. “Lakini hata yeye Wini alikosea pia.” “Labda kama una mpango wakuua
uhusiano wako kabisa na Nanaa. Nafikiri unakumbuka maneno yake hapa kabla
hajalala. Kama unataka mahusiano naye, nashauri uubadilishe kabisa huo utetezi
wako.” “Wini mwenyewe…” Akanyamaza. “Sawa.” “Sawa!?” Geb akamuuliza akimshangaa
kidogo. “Nakubali kosa kuwa nilitanguliza hasira.” “Nakushindwa kujirudi.” Geb
akaweka msisitizo.
“Si
hivi nimejirudi!?” “Kwa Nanaa!?” Geb akamuuliza kwa kumshangaa zaidi. “Yaani
unajitetea kujirudi kwa Nanaa ambaye hata hukuwa ukimjua kama yupo!? Hapa
hujirudi Lubuva. Unachofanya hapa nikuomba, narudia tena na uelewe, WEWE NDIYE
UNAYEMUOMBA, Nanaa undugu. Alipofikia Nanaa sasa hivi, anaweza kuishi vizuri tu
bila wewe. Muda na wakati aliokuhitaji hukuwepo. Aliniambia tukutafute ili
akuone tu sura yako ajue unafananaje. Hakutaka hata umjue kama yupo. Kwa hiyo ‘put your facts
together’ na uelewe kabisa. Upo hapa kwa
hiari yako mwenyewe. Kujisafisha kwa kile ulichomtendea Wini sio Nanaa.” Geb
akambadilikia.
“Sitakuruhusu
uzidi kumtesa Nanaa. Kama hutaweza kujirudi kwa Nanaa, bila kumchafua mama
yeke, ondoka. Tena uondoke mapema sana. Na ninakuhakikishia Nanaa
atapona tu. Ondoka hata sasa hivi, uone kama Mungu hatamtoa Nanaa hapo
kitandani.” Geb akambadilikia Lubuva vibaya sana. Alimpa maneno kama ya Nanaa.
“Ulilala
na mtoto ambaye hata miaka 18 hakuwa amefikisha! Umeshindwa kumlinda na ulaghai
wa rafiki yako. Akamlaghai, akalala naye. Na wewe ukarudi tena kulala naye!
Anarudi akiwa ni mjamzito, ukamkana! Leo unasema Wini alikuwa na kosa!? Are you serious!?” Geb akamuuliza kwa hasira
kabisa. Kimya. “Ni vile hapakuwa na mtu wa kumtetea Wini kwa wakati ule. Wewe
na rafiki yako wote mlitakiwa mshitakiwe. Ungekuwa umemfanyia hivyo binti yangu
mimi, hakika ningekufunga.” Tayari Geb alishabadilika.
“Na ninakuonya
kabisa. Usiharibu sifa ya Wini kwa Nanaa. Ni jina analolithamini sana. Vyeti
vyake vyote vya shule na kuzaliwa, vimebeba hilo jina la Wini. Mimi mwenyewe
nimefanya kuongeza jina langu mbele ya jina la Wini. Anamuenzi huyo mwanamke
kuliko utavyofikiria. Hivi unajua kama tokea siku unamkataa Wini mpaka kifo
chake alikuwa akilia tu?” Geb akamuuliza. Kimya.
“Sasa
ujue ndio sura pekee na sifa alizoambiwa Nanaa juu ya mama yake kutoka kwa mtu
anayemuamini sana na kumuona kama baba yake, ambaye ni James. Alichomwambia juu
ya mama yake ni kuwa alikuwa akimuona mama yake akilia kwa uchungu sana, muda
wote mpaka anapelekwa hospitalini kujifungua, alikuwa akilia. Na hakutoka
chumba cha kujifungulia. Hizo ni hisia ambazo kwanza zinamtesa James
mwenyewe mpaka leo na Nanaa pia. James
akiota Wini analia, anasema ndio ujumbe anatumiwa kuwa Nanaa yupo matatizoni.
Hata kama ni usiku, James akimuota Wini analia, atamtafuta Nanaa alipo ili ajue
anaendeleaje. Na ukifikiria kwa makini, utagundua kuwa ni kweli Wini
alipokelewa na dada yake baada ya kufukuzwa nyumbani kwao, lakini utagundua ni
kama alitelekezwa na kila mtu kwenye maisha yake. Hakuna aliyemjali yeye kama
mtoto aliyekuwa mjamzito!”
“Alikufa
sababu ya kutotunzwa vizuri. Hakuna aliyejua kama anakwenda kliniki. Hakuna
aliyejua kama ana damu ya kutosha akiwa vile mjamzito. Hakuna anayejua kama
alipatwa na pressure kama hivi Nanaa au la! Watu wote walimtelekeza mtoto wa
chini ya miaka 18, aliyekuwa mjamzito. Mama yake Wini alishindwa kabisa
kumsamehe Wini, na wala hamtambui kabisa Nanaa. Mpaka leo amemkataa kabisa
Nanaa, kitu kinachomuuma sana Nanaa. Walimnyima hata kutumia jina la ukoo wao!
Ndio maana Nanaa aliishia kuitwa Nanaa Wini.” Geb akaendelea kwa jazba.
“Nanaa alikwambia jana kuwa alikataliwa na
baba yake. Tena mara mbili. Mama yake akiwa mjamzito, na aliporudishwa kwenu
mara baada ya mama yake kufariki. Alikwambia ulimkimbia yeye kama mzigo
ili maisha yako yaendelee. Huna jinsi yakujiweka wewe upande mzuri, halafu
kumuweka mama yake upande mbaya, ukawa na mahusiano mazuri na Nanaa.
Hata siku moja.” “Nimeelewa.” Lubuva akajibu kwa upole.
Geb
akamgusa Nanaa kichwani kama anayempima joto kwa kiganja chake. Akambusu na kukumbatia
mkono wake. Akainama na kuubusu mkono wa Nanaa. Lubuva akaona anafunga macho.
Hakujua kama anasali au la. Akaamua atulie kidogo. Alipoona kimya kinazidi
akaamua kuvunja ukimya.
“Nataka
kuwa na mahusiano na binti yangu.” Geb akamgeukia na kumtizama Lubuva.
“Nilifanya kosa mara ya kwanza, nikaondoka. Sasa hivi nataka kuwepo kwenye
maisha yake.” Lubuva akaweka msisitizo.
“Ni
nani sasa aliyekwambia tena kama yupo?” Geb akauliza. “Baada ya mama kupona,
nikatakiwa kurudi kazini. Tukiwa uwanja wa ndege, kabla sijapanda ndege, mama
akaniita pembeni. Akasema hata kama nilimkasirikia Wini, lakini siwezi kutupa
mtoto daima. Nikamwambia mtoto aliyekuwa amembeba Wini hakuwa wangu. Ndipo
akasema Wini alifariki wakati akijifungua. Nanaa akaletwa pale nyumbani mimi
nikiwa nimeshaondoka. Mama akasema japokuwa walimkataa Nanaa, lakini
yeye alijua ni damu yake kwa kuwa alifanana sana na yeye hapakuwa na jinsi
akawa mtoto wa yule jamaa. Kwanza jamaa mwenyewe alikuwa mweusi sana. Na
tulikuwa tukifahamu wazazi wake. Japokuwa Wini alikuwa mweupe, lakini anasema
Nanaa alibeba rangi ya weupe ya kwetu. Yeye mama anajua. Akasema hata sura
tulikuwa tukifanana. Sasa hapo ananiambia, ndio nilikuwa natakiwa niondoke.
Yaani ndio nipande ndege. Natakiwa kazini. Nikaondoka niki…” “Kosa la tatu
hilo!” Lubuva akanyamaza.
Geb
akasimama vizuri pale alipokuwa amemuinamia Nanaa. “Kwa nini upo hapa dokta
Lubuva!? Kwa nini sasa hivi!? Unaweza kuwa umekuja kummaliza mke wangu bila
hata wewe mwenyewe kujua.” “Geb! Sina nia..” “Subiri kwanza. Swala lakujulishwa
kuwa yupo Nanaa, ulilijua lini kwa hakika?” “Miaka kama 3 na miezi kadhaa
iliyopita.” Lubuva akajibu. “Ambapo Nanaa ndio alikuwa akitafuta pakwenda!
Anahitaji msaada. Ndicho kipindi alifukuzwa kwa James, akahamia nyumbani
kwangu.” “Najua. Ndio na wewe ukampa mimba!” “Acha kunibadilishia maneno. Mimi
nilimpenda Nanaa.”
“Kilichokushinda
kumuoa kwanza ndipo umzalishe ni nini kama sio kuona ni binti wa kuchezea tu,
asiye na mtetezi? Ulimpa pakuishi, ukamshikisha mimba na kumtelekeza.
Wangemfanyia hivyo Oliva, binti yako ingekuwa sawa?” Lubuva naye akambadilikia.
“Usijifananishe
na mimi, kwa Nanaa. Mimi nilijirudi.” “Mara ngapi umekuwa ukijirudi kwa Nanaa?
Hivi unajua leo yupo hapa kwa sababu yako wewe Geb?” Lubuva akamjia juu. “Siku
nampa ushauri wakunywa dawa za kupunguza maumivu ya matiti kuuma, wewe ulikuwa
umemkimbia na kumpokonya watoto wake. Nilimkuta tena kituo cha mabasi
anatetemeka kwa pressure kuwa juu, kwa sababu ulikimbia na dawa zake alizokuwa
amepewa hospitalini. Unafikiri na mimi sijui uliyomtendea Nanaa?” “Nanaa
alinidanganya ndio maana nilikasirika.” Lubuva na yeye akakunja mikono na
kuiweka kifuani, akamwangalia na jicho kama kumsuta Geb. Yapi na yepi! Alimsuta
Lubuva kwa Wini, na yeye kwa Nanaa!!! Lubuva akabaki akimtizama.
“Lakini
mimi nilijirudi mapema sana sio kama wewe.” “Ulijirudi ukiwa umeshamsababishia
madhara yakudumu! Akiwa ameshaharibika moyo! Yaani ameugua peke yake, ndio
unajirudi! Na wewe ulitumia ukiwa wake vizuri sana kumnyanyasa.
Ulishindwa kumlinda na rafiki yako mlaghai mpaka akamjeruhi!” Lubuva akambana
Geb kwa maneno yake yeye mwenyewe.
“Umemsababishia
maradhi ya kudumu. Na sasa ni lazima umfanye atulie hapo, mimi ndiye
nimuhudumie. Unanielewa Geb? Tafuta lugha yeyote yakuzungumza naye atakapoamka
hapo, mpaka akubali mimi ndio niwe daktari wake.” “Nikikataa wewe kuwa daktari
wake?” Geb akauliza kwa jeuri kama
akitaka kujua atamfanya nini sasa! Tayari alishakasirika.
“Unamaanisha
kama ulivyokataa kuweka hasira zako pembeni, na kumtelekeza baada yakumuombea
aruhusiwe hospitalini akiwa mgonjwa, ukamuahidi dokta Lyamu na Rweta kuwa
utakuwa ukimrudisha hospitalini kwa vipimo na kumpa dawa, halafu kesho yake
ukamkimbia na watoto wake pamoja na dawa ulizosisitizwa azitumie?” Na yeye Lubuva
akamuuliza akimtizama machoni.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Wamekutana mafahari wawili. Lubuva&Magesa. Wote
wajuaji. Itakuaje?
Nanaa aliyekuwa akitafuta Ukweli, ameupata, anashindwa
kuumudu. Itakuaje kwa
baba yake?
Usikose muendelezo.
0 Comments:
Post a Comment