“Bila kukubaliana, kama
unavyomjua Nanaa, akaanza kusukuma. Ikabidi tumsaidie kumpokea mtoto. Amezaa
mtoto wa kiume. Mzima kabisa na ana nguvu. Nimeacha anamaliziwa kusafishwa ili
atolewe. Mtamuona.” “Vipi Nanaa mwenyewe?” Geb akauliza kwa wasiwasi.
Akanyamaza kidogo, wote wakapatwa na wasiwasi. “Hali sio nzuri Geb. Acha
nikwambie tu ukweli. Baada tu ya kujifungua, Nanaa alipoteza fahamu. Ni kama
amepata stroke au heart attack. Sasa kama nilivyokuwa nimekwambia au kama
mlivyoambiwa na daktari wake, yapo madhara mengi ambayo kwa sasa ni ngumu
kusema. Inawezekana tayari ile mirija ya kupeleka damu kwenye ubongo
imeshapasuka. Hofu ni kutengenezwa clots, zitakazozuia usambazwaji wa damu.
Hiyo itamuondoa kwa haraka sana.” Daktari akaendelea.
“Pili ipo hatari ya ‘Dementia’.
Kama atafanikiwa kuamka, hatujui kama atarudi kuwa kwenye hali yake ya zamani.
Anaweza asiwe na kumbukumbu kabisa. Na hatujui hali hiyo itachukua muda gani.”
“Hiyo ya kuzinduka?” James akauliza. “Ndiyo. Lakini yupo kwenye vipimo kadhaa
hapo ndani. Na wale madaktari mliowaona nipo nao, mmoja ni daktari wake wa
mambo ya moyo. Ameshampigia simu ‘Neurologist’ anakuja yupo njiani. Kwa kifupi
yupo kwenye mikono mizuri au atakuwa kwenye mikono mizuri sana. Huyo
Neurologist anayekuja ni daktari wakimataifa. Ni dakatri bingwa. Ninaujasiri wa
kusema ni daktari bingwa duniani. Wanahangaika kufanya kila wawezalo kumuokoa.
Ikiwezekana au wakiona ni muhimu, wanaweza kumfanyia upasuaji. Ni hilo nilitaka
kuwataarifu ili mjue kinachoendelea ndani.” “Naomba msimkatie tamaa tafadhali.
Waambie vile Nanaa alivyo mpambanaji. Sio dhaifu kama anavyoonekana, wafanye
kila wawezalo. Wasimkatie tamaa hata kidogo.” Geb aliongeza. “Tutafanya kila
liwezekanalo Geb. Hata mimi Nanaa ananihusu sasa hivi.” Yule Daktari akamjibu
Geb. “Asante.” Lyamu akarudi ndani, Geb akapiga magoti tena palepale.
Nanaa Atoa
Maajabu Ya Kushangaza Kila Mtu.
Baada ya
muda mfupi kupita, nesi akatoka na mtoto. James akasogea yeye wa kwanza kumpokea.
“Jimmy!” James aliongea huku
akimsogelea. “Heee!” James akasikika
akishangaa nakufanya Geb anyanyue kichwa. “Nini James?” Mama G aliyekuwa nyuma
yake akaongeza mwendo kumfikia. James akabaki ametoa macho. Man naye akasogea.
Mama G akabaki ameduwaa. Geb akabaki akiwatizama. “Mungu wangu!” Mama G alisikika. “Ni nini mama?” Geb akauliza. Mama
G akamchukua yule mtoto kutoka kwa James akaenda kumpelekea Geb pale alipokuwa
amepiga magoti, akamchungulia. “Mungu Wangu!” Machozi yalianza kumtoka Geb.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Kumbukumbu zilimrudisha siku
ile yakutoka hospitalini baada ya kujifungua Magesa, alipomfuata Nanaa bafuni
siku aliyokuwa ameruhusiwa kurudi nyumbani. Penzi alilopewa pale bafuni.
Akakumbuka ni kama Nanaa alimuonjesha tu. Bado hakukata kiu yake. Akaamua
wakachukue chumba hotelini, kabla hawajafika nyumbani. Geb akakumbuka vile
alivyokuwa na uchu na Nanaa. Aliwekwa mapumzikoni pale hospitalini. Hawakuwa
wamefanya mapenzi kwa muda mrefu. Wakafika hotelini, Geb akajishindia magoli ya
nguvu. Alifanya mapenzi na Nanaa kama hatakuja kufanya naye mapenzi tena
maishani.
Kwanza nesi aliyemshona Nanaa,
baada ya kujifungua, ni kweli alimrudisha kama binti mdogo. Akahudumiwa mpaka
akapona. Wametoka hospitalini siku hiyo, Nanaa akiwa na joto la kupevusha yai.
Geb alipoingia humo ndani, hakuwa akitaka kutoka. Alifanya mapenzi kwa kuridhika,
akaishia kulala. Waliamka jioni na kukimbilia nyumbani, ili Nanaa akanyonyeshe.
Na ndio usiku huo nao Malii akambaka Nanaa, zikiwa mbegu za Geb zilishawahi
ndani na mbegu ya Jimmy ikawa imeshapitishwa na Mungu.
Jimmy mikononi kwa baba yake.
“Jamani mwanangu!” Geb
alisikika na kumchukua Jimmy kutoka
mikononi mwa mama yake. “Kumbe muda wote Nanaa anateseka na uchungu wa
kubeba mtoto akidhani ni wa Malii, kumbe mjukuu wangu ametulia kimya! Atakuwa
aliteseka sana kihisia.” Mama G naye alijibu kwa mshangao. Geb alimkumbatia
yule mtoto na kumbusu.
“Nakupenda Jimmy! Umekuja sehemu sahihi, kwa muda sahihi na kwa watu sahihi. Wewe ni
zaidi ya Duma, mnyama anayekimbia sana hapa ulimwenguni. Zaidi ya simba, mfamle
wa jangwa. Katika maelfu wote ya siku uliotungwa mimba, wewe ukashinda na
kuweza kukaa kwenye tumbo la mama yako. Hakuna gumu la ulimwengu huu
utakaloshindwa. Hakuna hila wala mtego wa muovu utakao wekwa juu yako
ukafanikiwa Jimmy. Umebarikiwa mwanangu. Kwa baraka zote za duniani na mbinguni.
Utaishi ukayashuhudie makuu ya Mungu.” Geb aliendelea kumuombea
mwanae na kumbariki akiwa bado amepiga magoti mpaka akamaliza.
“Naomba umchukue mama.” Geb akamrudisha
kwa mama yake, yeye akarudi kuomba. Walimsikia akinza kushukuru, mwishowe akarudi
kumuombea Nanaa. Geb alikuwa akilia akimuomba Mungu amrudishie Nanaa, walee hao
watoto. “Nanaa mwenyewe ameweza hata kumuona mtoto wake?” Mama G akamuuliza
yule nesi. “Hapana mama. Alipoteza fahamu mara tu baada ya kutoa mtoto.” “Mungu
amsadie Nanaa. Aje aone hiki alichokuwa amebeba.” Mama G aliongea huku macho
yapo kwa mjukuu wake.
Man akampigia simu Grace. “Weka video umuone mtoto.” Man
alisikika akiongea na Grace. Grace akaanza kushangilia akimshukuru Mungu. “Sasa
hapo hajaona kama ni pacha mwenzie Magesa. Akiona hiyo sura, ndio atashangaa
zaidi.” Man akamsogelea mama G, akamuonyeshea yule mtoto. Mara wakasikia kelele
zimekoma. “We Man! Huyo
mtoto ujue ni wa Geb! Amefanana macho na sisi, halafu ni kama kopy ya Magesa!
Magesa alizaliwa hivyo hivyo na manywele kama ya baba yake. Nipe mama.” Grace
alikuwa kwenye mshituko. Alicha kupiga kelele. “Nakusikia Grace.” “Geb yuko wapi?” Grace
akauliza. “Anaomba.” “Amejua
kama Nanaa alikuwa amebeba mtoto wake?” “Amejua. Lakini sasa hivi akili ziko
kwa Nanaa. Hali sio nzuri Grace.” Wakamuelezea kwa kifupi hali
ya Nanaa. “Na mimi naingia
kwenye maombi. Naamini Mungu atatenda. Nipe Geb.” Wakampa Geb simu.
“Hongera na pole Geb.” “Hali ya Nanaa sio nzuri G.” Geb
akajibu. “Unakumbuka jinsi
Nanaa anavyokuaga kwenye hali mbaya na bado anapona?” “Safari hii ni tofauti G.
Nanaa amepoteza fahamu na nilishaambiwa madhara yake.” “Nisikilize Geb, tunaye
Mungu wa yasiyowezekana na wanadamu. Mungu wa miujiza. Kama aliponya
miguu ya Nanaa, tena madaktari wakiwa hawajui jinsi yakumsaidia, atashindwa
vipi kumtoa kwenye hiyo hali arudi kunyonyesha mtoto wake?” Kimya.
“Naomba ondoa hofu na uendelee kuomba na mimi nakuombea.
Lakini si kwa hofu ila ukijua nguvu ya Mungu na mkono wake juu ya Nanaa. Hakuna
linalotokea sasa hivi eti limemshangaza Mungu. Amini na jua kwa wakati
wake atatenda. Sawa?” “Asante.” Man akachukua simu. Geb akaendelea kuomba.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Nanaa aliacha hukumu kwa kina
Magesa, kila mmoja alianza kujutia lake kwa wakati wake. Walimtelekeza kwa muda
mrefu baada ya kubakwa, akiwa amebeba damu yao. Aliporudi pia walimshangaa
kumuona ni mjamzito, wasijue kuwa amebeba mtoto wa Geb. Hata yeye mwenyewe
alirudi akitangaza kupata mimba baada ya kubakwa. Kila mtu alijua ni mtoto wa
Malii. Mungu alifunga kumbukumbu zao kabisa na kusahau mapenzi waliyofanya siku
ile baada yakutoka hospitalini kama yaliweza kumpatia ujauzito. Hata mama G
alisahau kama wapenzi hao kabla ya kurudi nyumbani, walikuwa hotelini.
Kumbukumbu ilibakia moja tu, yakubakwa kwa Nanaa. Kufunga na kufungua wote
walisahau uzuri na wema wa Nanaa, na kumtelekeza.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
James akamchukua tena Jimmy
kutoka kwa mama G, akabaki akimtizama. Nesi akaomba amrudishe kwenye chumba cha
watoto, aendelee kuhudumiwa. Nesi akaondoka na Jimmy, wakabaki kila mmoja
akiwaza lake. Ilisikika sauti ya Geb tu akiomba taratibu. Bado alikuwa amepiga
magoti amegeukia ukuta, mwisho kabisa. Alijitenga na kila mtu.
Baada ya muda daktari akarudi tena.
Alikwenda moja kwa moja alipokuwepo Geb. Akamwita. “Vipi Nanaa?” “Wamegundua
kuna damu inayovujia upande mmoja wa ubongo. Kwa hiyo anaandaliwa kufanyiwa
upasuaji wa kichwa ili kusaidia kusimamisha uvujaji huo na kuondoa damu
iliyokwisha mwagika.” “Mungu wangu nisaidie!” Geb
alisikika na kuweka mikono kichwani. “Lakini haya yote tulishazungumza kabla,
Geb. Yule daktari wa mambo ya moyo alizungumza na nyinyi wote wawili. Tena kwa
undani. Aliwapa madhara ya Nanaa kuendelea kubeba ile mimba. Unakumbuka?”
Daktari alijaribu kumkumbusha Geb asijue anaongea na kichwa kisichosahau.
“Nani atamfanyia huo upasuaji?”
Geb akauliza. “Huyu daktari aliyeingia hapa muda mfupi uliopita, ni daktari
bingwa wa mambo ya ‘neuro’. Ni mzuri sana kwenye upasuaji na ni rafiki wa karibu
sana wa huyu daktari aliyekuwa akimsaidia Nanaa, kwenye mambo ya moyo. Nimeacha
wakizungumza. Naamini watafanya kitu kizuri. Tuendelee kuomba.” “Naomba na wewe
usiondoke.” “Kazi yangu humo ndani imeesha. Mimi ilikuwa ni mambo ya uzazi tu.
Nimeshamuhudumia kwa upande huo, hakuna tatizo. Lazima niwapishe ili kuwapa
nafasi ya kumuhudumia. Hata hivyo wamenifukuza kwa kuwa wanajua mahusiano yangu
na Nanaa. Wanaona nitawazuia kufikiria na kufanya kazi yao vizuri. Sitaondoka
kabisa. Naenda kumuangalia mtoto. Nataka kuhakikisha hamna tatizo lolote kwa
Jimmy ndipo nitarudi. Nanaa amelipa garama kubwa sana kwa huyu mtoto. Sitaki
chochote kitokee. Nimeshampigia simu dakatri wa watoto, amekubali kuja kumuona
sasa hivi. Nataka anikute pale.” “Nashukuru sana.” Lyamu akaondoka. Hata yeye
alionekana yupo kwenye wasiwasi. Kwa muonekano ule, hata James alijua mambo sio
mazuri.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya masaa matatu kuanzia
yule daktari azungumze nao, Nanaa akatolewa pale akiwa anapelekwa ICU. Bado
hakuwa na fahamu. Daktari alizungumza na Geb. Akamwambia kile walichomfanyia
Nanaa. Na kumwambia wasubirie azinduke ndipo wataweza kujua kwa hakika madhara
yatakayopatikana na ile stoke na upasuaji.
“Naweza kwenda
kuwa naye?” “Haiwezekani Geb! Nanaa anakwenda ICU. Atakuwa kwenye
mashine muda wote mpaka azinduke. Haruhusiwi mtu yeyote kuingia humo, isipokuwa
wauguzi tu.” “Haiwezekani!” Geb alihisi wanataka kumnyima
pumzi. Aondoke na kumuacha Nanaa hapo hospitalini, aliona atachanganyikiwa.
“Huna utakachoweza kufanya kwa sasa. Nashauri mrudi nyumbani mje kumwangalia
tena kesho. Kama kuna mabadiliko yeyote tutawajulisha.” “Mungu wangu nisaidie!” Geb aliweka mikono kichwani.
“Inamaana atakuwa hapo peke
yake!?” Geb akauliza tena. “Mimi mwenyewe nahisi nitakuwa naye usiku huu ili
kuhakikisha chochote hakitokei. Wapo manesi watakao kuwa wakimwangalia muda
wote. Usiwe na wasiwasi. Yupo kwenye mikono mizuri.” Akaongeza huyo daktari bingwa
aliyejitambulisha kwa jina la Lubuva ambaye amemfanyia huo upasuaji. “Naomba basi
nione hata atakapokuwepo.” Wakaongozana mpaka huko ICU. Walisubiri mpaka
alipowekwa kila kitu. Nanaa alijawa mashine kila mahali. “Naomba unihurumie Mungu wangu! Usinipokonye Nanaa wangu.” Kila
wakati Geb alisikika akiongea hivyo. Waliweza kumchungulia Nanaa pale alipokuwa
amelazwa. Wasiamini kuwa ni Nanaa yule yule aliyekuwa akiendesha kesi masaa
machache yaliyopita pale nyumbani, na ndiye huyu amejawa mashine kila mahali,
hajitambui.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Usiku huo Geb alishindwa
kuondoka kabisa. Alibaki akiomba. Ilibidi James abaki naye. Alikuwa amepiga
magoti usiku kucha akiomba. Palipo pambazuka, Grace akaja. Akamtoa kichwa pale
alipokuwa amekiinamisha kwenye benchi, akakiweka mapajani kwake. Geb akaanza
kulia. Huku amemuegemea dada yake. “Naomba usikate tamaa Geb.” Akaendelea kumsugua
taratibu mgongoni. “Vipi James?” Akamuuliza. “Hamna mabadiliko, Grace. Nesi
aliyetoka hapo sasa hivi anasema yupo vile vile.” James alijibu kwa upole.
Ilikuwa tayari ni saa 12 asubuhi.
“Twende tukamuone mtoto.” Grace
alimuongelesha kaka yake. “Siwezi G.”
“Lazima Geb. Sasa Nanaa akiamka sasa hivi akikuuliza habari za mtoto utamjibu
nini!?” Geb akabaki akifikiria. “Lazima umuonyeshe umethamini kazi ngumu
aliyofanya. Yeye anapambana na afya yake, wewe unaangalia watoto huku
ukimuombea.” “Maisha yangu yatakuaje bila Nanaa, G? Hawa watoto wote
nitafanyaje nao?” “Nisikilize Geb. Hizo ni kauli za mtu anayekubali kushindwa.
Wewe ni mpambanaji. Nakujua Geb. Usikubali hofu ikutawale. Ukishindwa kusimama
kwenye nafasi yako kumdai mkeo, unafikiri nani atafanya? Lazima akimka akute
unafanyia kazi kile alichokilipia garama! Unafikiri atafurahi eti aamke akute
huna habari na watoto!? Hapana Geb, lazima umuunge mkono mwenzio.” Geb akakaa.
“Sasa natakiwa kufanya nini?”
Geb akauliza. “Twende tukaangalie mtoto anaendeleaje. Amelishwa nini, amelala
salama. Amewekwa mahali pasafi. Hayo yote unatakiwa kuwa na majibu yake wewe
mwenyewe. Ili endapo Nanaa anaamka, wewe ndio unatoa hiyo ripoti. Sio mtu
mwingine.” Grace akampandisha morari. “Basi twende.” Akasimama. “Nashauri James
na wewe ukapumzike, unaweza kurudi baadaye. Chochote kitakachotokea,
nitakujulisha.” James akaomba waongozane ili na yeye akaone mtoto.
Hiyo siku ikaisha, Geb akiwa
busy. Kwa Nanaa, na kwa mtoto. Grace akaondoka, akaja mama yake. Mchezo ukawa
huo huo. Anatembea kutoka alipo mtoto wake, akimuona, anarudi ICU kwa Nanaa.
Atamchungulia na kuanza kuomba. Hakula wala kunywa. Grace akarudi jioni akiwa
amemuachia watoto wote Man. Walikaa hapo akitaka kila mtu aombe. Waliomba mpaka
wakachoka. Giza likaingia, mbu wakazidi.
“Sasa kitakachofuata ni Nanaa
kutoka hospitalini, na wewe unalazwa kwa malaria.” Grace alianza baada ya mama
yake kumtaka warudi nyumbani akapumzike na Geb kukataa. “Itakuaje akiamka
halafu anikose?” “Sasa kwa hali hiyo unafikiri hata akiamka sasa hivi
utafanyaje Geb? Hata mswaki hujapiga. Unanuka jasho na ndevu pia hujanyoa.
Yaani wewe mwenyewe ni mgonjwa kuliko hata huyo Nanaa mwenyewe. Badala ya
kukuona na kufurahi, anaweza kuzidiwa kabisa.” “Usiseme hivyo G!” “Muulize mama
kama hunuki Geb. Siku nzima unazunguka juani. Joto kali. Unakaa nje tu. Hata
kwa mwanao hivyo ulivyo sio sawa kumshika. Utaendaje kumpa maziwa ukiwa mchafu
hivyo!? Nenda kaoge vizuri, lala, kesho ukija unakuwa na uwezo wa kumshika
mwanao na mnaomba. Liv anawatafuta nyumba nzima. Hakuoni wewe wala mama yake.
Unafikiri ndicho kitu Nanaa atataka ufanye?” Geb akakubali kuondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ukaanza huo utaratibu.
Anakwenda kulala nyumbani. Asubuhi ya saa 12 anakuwa ameshawasili hospitalini.
Anakwenda kumwangalia Nanaa, kisha anawahi kumlisha Jimmy. Akishakunywa maziwa
anayokuwa amewekewa na nesi, anamuacha na kurudi kwa Nanaa. Atakaa hapo
akiomba, siku nzima. Siku ya pili ikaisha. Nanaa hakujigeuza wala kusogeza hata
mkono. Siku ya tatu ndipo Geb akazidi kujaribiwa. Mpaka inafika usiku, hali ya
Nanaa ilikuwa vile vile. Daktari aliyemfanyia upasuaji alimwambia mara nyingi
huwa hazizidi siku tatu mmgonjwa aliyefanyiwa aina ile ya upasuaji
anakuwa amezinduka. Sasa siku ya tatu ikawa imeisha.
Geb alishaomba maombi yote.
Alishalia mpaka kichwa kilikuwa kikimuuma karibu kupasuka. Hakuwa akila wala
kunywa. Anashinda kwenye joto kali. Anatoa jasho jingi. Anatembea kuanzia
asubuhi mpaka usiku. Kutoka ICU mpaka kwa watoto. Jua lake, joto lake. Mawazo
na hofu vilimjaa japo alikuwa akiomba.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Siku ya 4 ilibidi Man aondoke
arudi Arusha kuendelea na kazi. Harusi ilifana, lakini hapakuwa na mapumziko
yeyote. Ni kama alijikuta anajiingiza kwenye matatizo zaidi. Aliondoka jijini
akiwa na baraka zote za mama mkwe wake na mkewe. Wote waliona ni heri yeye
arudi kazini kuliko wote waharibikiwe. Geb hakuwa akienda kazini. Maisha
yalikuwa hospitalini. Ikabidi Grace awe anakwenda yeye kazini. Habari za
kuomboleza zikawekwa pembeni. Msiba wa watoto wake ukaanza kusahauliwa
kulinganisha na hali ya Nanaa na wasiwasi wanaongezewa na Geb.
Mama G yeye ndio ilibidi awe
anabaki na watoto na kuangalia mambo ya nyumbani. Akishawaweka sawa watoto, mke
wa Jeri akiwa anakuja kusaidia kazi, ndipo mama G, anakwenda hospitalini kuwa
na Geb kidogo, nakurudi nyumbani. Yeye hakuwa akiweza kuzunguka pale
hospitalini kama Geb. Joto lilikuwa likimshinda. Akishamuona mtoto, na kupata
kijimwanya chakumchungulia Nanaa pale alipolazwa, anarudi nyumbani kwa watoto.
Geb
Matatizoni Zaidi.
Siku ya nne Geb alimka saa 10
asubuhi. Hata yeye ilimsumbua kutoka kitandani. Mwili ulikuwa dhaifu sana.
Alijua wazi asingeweza kuendesha. Akapiga simu getini kuomba mlinzi
akamchukulie taksii ili awahi hospitalini. Mlinzi akafanya kama alivyoagizwa.
Geb akaondoka asubuhi hiyo na mapema. Mama yake alipoamka, akaona magari yote
yapo nje, akamshukuru Mungu akijua siku hiyo Geb ameamua kupumzika. Akaadhimia
kumuacha angalau mpaka hata saa nne ndipo amuamshe. Hakuwa akila wala kulala
vizuri. Alifika nyumbani usiku na kuondoka asubuhi sana.
Saa nne ikafika, kimya. Saa
tano, kimya. Mama G hakumuona akitoka chumbani, asijue Geb alishatoka pale
nyumbani muda mrefu. Grace naye alishatoka kwenda kazini tokea saa mbili
asubuhi. Mambo yalikuwa mengi kazini, Geb alimpa maelekezo mengi usiku
uliopita. Kwa hiyo hata mama yake alijua siku hiyo Grace naye hatakuwepo
nyumbani siku nzima. Ilipofika mchana wa saa sita na nusu, ikabidi kwenda
kugonga. Ndipo alipogundua Geb hakuwepo chumbani kama alivyodhania. Akapiga
simu getini, mlinzi aliyeingia saa mbili asubuhi hakuwa na taarifa na
kilichotokea. Yeye alipewa taarifa za usiku. Kuwa walilala salama, hapakuwa na
wizi wowote wala hatari yeyote, siku yake ya kazi ikaanza.
Wasiwasi ukamwingia mama G.
Akampigia simu Grace. Alimueleza kuwa magari yote ya Geb yapo hapo nyumbani,
lakini Geb mwenyewe hayupo na mlinzi aliyekuwepo hapo hajamuona akitoka. Mbaya
zaidi, simu yake haipo hewani. Ikabidi Grace aende akamtizame hospitalini.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Geb alikataa huyo mtoto
asirudishwe nyumbani, amsubirie mama yake ili watoke nae. Kila mama yake
alivyomshauri, wamchukue Jimmy, awe nyumbani, Geb alikataa katakata. Alikuwa
akisema huko ndiko kumnyang’anya Nanaa mtoto. Wakaona wamuache tu. Alikuwa
akiamka asubuhi, anakwenda kumlisha huyo mtoto. Anakaa naye mpaka muda ukiisha,
anamuacha na kwenda kwa Nanaa. Kila baada ya masaa matatu alitakiwa kurudi na
kumnyonyesha maziwa ya chupa. Kwa hiyo alikuwa akirudi kwa mtoto, kisha anaenda
kukaa nje ya ICU akiomba.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Grace alijua ratiba yake ya hapo hospitalini.
Akajua muda huo atakuwa anampa Jimmy maziwa. Akaanzia kwa mtoto, manesi
waliokuwepo zamu walimwambia siku hiyo hawakumuona Geb. Geb alishafahamika na
kila muuguzi pale kwenye upande wa watoto. Kwani kwa wakati ule yeye ndio
alikuwa baba pekee aliyekuwa akienda kumuhudumia kichanga chake. Wengine wote
walikuwa ni kina mama. Kina baba walikuja kuchungulia watoto wao na kuondoka.
Geb alikuwa akikaa hapo na wakati mwingine alisaidia kubadili diaper. Na kwa
kuwa walijua anakuwa maeneo ya hapo hospitalini, kila Jimmy anapoanza kulia,
aliomba awe anaitwa. Kwa hiyo alikuwepo hapo muda mrefu na mtoto wake.
Wasiwasi ulimuingia pale
alipoambiwa pia kule kwa Nanaa hawakumuona. Akampigia simu mama yake na
kumueleza. James naye akafika hapo hospitalini alipokuwepo Grace. Bado simu ya
Geb haikuwa ikipatikanika. Mama G ikabidi apige simu kwenye kampuni ya ulinzi
akimtafuta mlinzi aliyekuwepo hapo usiku uliopita. Walikuwa wawili. Mmoja ndiye
akasema alimtuma akalete taksii. Hakutaka iingie ndani. Geb mwenyewe alitoka
mpaka nje ya geti, kuifuata hiyo taksii, wakaondoka bila yule mlinzi kujua
alielekea wapi. Alipoulizwa kama anamfahamu huyo dereva taksii, yule mlinzi
alisema ni taksii aliyoisimamisha barabarani. Alibahatika wakati alipofika tu
barabarani na yenyewe ndio ilikuwa ikipita.
Wanasema mkubwa hapotei. Lakini
mpaka inafika saa 12 jioni, hakuna aliyejua Geb alipo. James akatoa taarifa
kituo cha polisi. Heka heka za kumsaka Geb zikaanza. Kwa hali yake ilivyokuwa,
mama G akamwambia James aanze kumtafuta kwenye wodi za wanaume. Inawezekana
alianguka, nakupoteza fahamu. Pengine mtu alimuokota na kumpeleka hapo
mapokezi. James alizunguka kitanda kimoja hadi kingine. Geb hakuwepo wodini.
Akakaza moyo kwenda chumba chakuwekea maiti. Geb hakuwepo huko pia. Kazi
yakumsaka Geb ikaendelea. Hakuna aliyemkumbuka Nanaa siku hiyo wala Jimmy. Hiyo
siku ya 4 ikapita.
Nanaa!
Kumbe Nanaa alizinduka tokea
saa 4 asubuhi ya siku hiyo ya 4. Sababu ya kupoteza fahamu kwa muda mrefu,
madakatri wakawa na wao na shuguli ya kuhakikisha ana ‘stabilize’, harudi kwenye ‘shock’ tena. Mpaka inafika jioni,
daktari Lubuva, ambaye alikuwa amehusika na upasuji wake, akajiridhisha kuwa
baadhi ya mashine kama za kumsaidia kuhema, zinaweza kutolewa tu. Alizinduka
akiwa ameathirika ‘speech’ tu.
Zungumza yake ndio ilibadilika. Aliongea kwa shida kama mtoto anayejifunza
kuongea. Daktari alimtaka arudi kupumzika. Hata hivyo hakuongea sana zaidi
alimuulizia tu Geb mara kadhaa, nakurudi kulala.
Kesho yake asubuhi, Nanaa
alimka mapema tu, akabaki pale kitandani akiwa bado na baadhi ya mashine,
lakini akili zake zikiwa zimemrudia vizuri tu. Alikaa pale akishangaa jinsi
alivyotelekezwa. Hakumuona mtu hata mmoja akija kumtembelea pale hospitalini.
Wakati madaktari wanapita round hapo ICU, daktari aliyekuwa akimshugulikia
tokea mwanzo, Lubuva, akashauriana na madaktari wengine, wakaonelewa Nanaa
atolewe ICU, apelekwe kwenye chumba cha kawaida tu kwani hakuwa na sababu
yakuendelea kuwepo ICU.
Nanaa alionekana kupona kwa haraka hata pressure yake ilikuwa sio mbaya. Akahamishiwa kwenye chumba chake hapo hapo hospitali ya taifa ya Muhimbili, sio wodini. Kwani tokea mwanzo Nanaa alipata huduma za kulipia kwenye hospitali hiyo ya Taifa. Hata chumba chenyewe cha ICU walilazwa wawili tu.
Mpaka anahamishwa kwenye hicho
chumba, hiyo siku ya tano, hakuwa amemuona ndugu hata mmoja. Hofu ikaanza
kumwingia. Akahisi ametelekezwa. Manesi wote na madaktari wote aliokuwa
akikutana nao pale walikuwa wageni kwake. Hakujua amuulize nani na bado alikuwa
dhaifu. “Geb yuko wapi?” Ndilo swali
lililomuumiza kila mtu.
Siku
ya tano.
Siku hiyo ya tano tokea Nanaa
alazwe na ya pili tokea Geb apotee, James alimkia hospitali ya Mwananyamala.
Akiwa na ripoti yake ya polisi. Akaomba waanzie chumba cha maiti. Akamtafuta
Geb bila mafanikio yeyote. Hizo zikawa habari njema. Akaona akamtafute wodini
pia. Akaenda kuanza kumsaka. James ndiye aliyekuwa mtu sahihi kumsaka Geb,
kwani mama G alijua haitamsumbua kumtambua hata kama akimkuta akiwa amevimba
uso kupitiliza au hata kama akiwa amekatwa kichwa. Alijua James atamtambua hata
kwa kumuangalia mikono au miguu yake. Geb alikuwa naye pamoja. Hata akiwa
ameinama, akaona nyayo tu. Haikuwa shida kwa James kumtambua Geb, Danny, Zinda
au hata kina Gozi. Walijuana vizuri sana.
Akiwa amekata tamaa kabisa,
James alimkuta Geb amelala kitanda cha mwisho kabisa, amefunga macho,
akilalamika sana maumivu. Asijue ni ya kichwa au mwili mzima. Maana usoni
upande wa kushoto, jicho lilivimba na kuvilia damu. Kama aliyekuwa amepigwa
vibaya sana. Wauguzi walimwambia alishapewa dawa ya kupunguza maumivu,
anasubiriwa mtu wakumpeleka kwenye X-ray.
James hakutaka kupoteza muda,
alimtoa hospitalini hapo kwa gari ya wagonjwa, akimuhamishia hospitali ya
kulipia huku akipiga simu nyumbani kwao kueleza kila kitu. “Anaonekana
alivamiwa na majambazi.” James alieleza, lakini Geb hakuwa akiongea zaidi ya
kugugumia maumivu na kuonekana dhaifu sana. Alifikishwa hospitalini hapo na
kupewa huduma ya kwanza kwa haraka.
Mama yake alifika kwa haraka na
kueleza pia hakuwa amekula kwa siku zaidi ya nne. Walimuwekea dripu ya sukari,
wakaifungulia iende kwa haraka. Zilipoisha mbili, huku akiwa amechomwa sindano
ya kupunguza maumivu, ndipo Geb aliweza kulala. Alifanyiwa huduma za
harakaharaka, akapigwa xray. Hapakuwa na kitu chochote kilichoonekana kina
tatizo mwilini mwake isipokuwa hilo jicho. Akapewa kitanda kama kupumzishwa
wakati anawekewa dripu zakuongeza nguvu na daktari alimwambia mama yake
watamlaza ili kuendelea kufanyiwa vipimo vingine.
Kwa uchovu, njaa, hofu, baada
yakupata zile dripu za haraka, dawa ya maumivu, Geb alilala kuanzia ile asubuhi
alipofikishwa hospitalini hapo na baada ya vipimo, mpaka saa 11 jioni ndipo
akashituka kutoka usingizini.
Aliposhtuka tu, “Nanaa!” James,
mama G, na Grace wakaangaliana. Geb akajua hakuna anayejua habari za Nanaa,
akachomoa zile dripu. “Naomba utulie Geb. Unataka kuniua wewe!” Mama G
akaanza kulia. “Naomba Grace ulipie hapa, James nipeleke Muhimbili.” Hapo Geb
anazungumza akiwa mlangoni anaeleka bafuni. Alishachukua kibegi kilichokuwa
hapo. Alijua kina nguo zake. Mama yake alimletea. Akaoga kwa haraka na kubadili
nguo, akatoka bafuni.
“Mama, naomba uniletee uji kule
Muhimbili.” Geb akatoka, James akamfuata nyuma kwa haraka. Grace na mama yake
wakabaki wamekaa hapo kwenye makochi ndani ya chumba alichokuwa amelazwa Geb,
wasiamini. Geb huyu aliyekuwa amelala hapo wakidhani amezidiwa sana, ndiye huyu
anatoa maagizo. Kwa kutaka uji, ndio alikuwa akimtuliza mama yake na kumwambia
anaendelea vizuri.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Walifika ICU kule alipokuwa
amelazwa Nanaa, wakachungulia, kitanda kitupu. Nusu Geb aanguke chini kabisa sakafuni
akijua alishakufa, mwili wake ukatolewa pale. Lakini James akamdaka. Sura ya
James ilishabadilika nakuwa nyekundu kwa uchungu na yeye akijua amepoteza dada
ambaye ni kama mtoto wake. Ikabidi warudi kuzungumza na wauguzi. Palikuwa kimya
sana. Wakaambiwa Nanaa alitolewa hapo, amehamishiwa kwenye chumba cha kawaida.
Ni habari ambazo Geb
hakutegemea kuzipata. Walitoka hapo kwa haraka, kuelekea kwenye hicho chumba.
Walimkuta Nanaa amelala. Hakuwa na mashine nyingi, lakini bado alikuwa na
mashine baadhi. Alikuwa akihema mwenyewe na dripu mkononi.
Nanaa alimshwa na kilio cha Geb
shingoni kwake. Akahisi anaota, lakini bado alimsikia akilia. Akageuka
taratibu, akamuona Geb amejificha hapo kwenye shingo yake akilia. “Geb!”
Akamuwekea mkono kichwani. Alilia mtoto huyo wa kiume, huku James amesimama
pembeni akiwatizama. Akatulia, lakini akabaki ameegemea pale pale. “Nianga-lie
ba-si.” Nanaa akajaribu kumgusa kichwani. Kimya. “P-ol-e Ge--b.” Nanaa
alijaribu kumtuliza. Aliambiwa alilala hapo hospitalini kwa siku 4. Hakuwa
amemuona yeyote yule hata huyo Geb. “Sasa
alikuwa wapi tokea jana nazinduka!?” Nanaa akajiuliza huku akimtizama pale
alipojilaza.
Akajisogeza taratibu mpaka
akaweza kumgeukia, akafanikiwa kumbusu kichwani. Mashine zikaanza kupiga
kelele, zikamshitua mpaka Geb. Nesi akaingia. Nanaa alikuwa amechomoa ile
iliyokuwa kwenye kidole. “Vipi!?” Geb akasimama kwa haraka. “Imetoka tu kwenye
kidole, lakini kila kitu kipo sawa.” Nesi akajibu huku akirekebisha.
“Pressure?” Geb na James wakajikuta wanauliza kwa pamoja. “Ndio tulikuwa
tukiingalia tokea alivyohamishiwa huku. Naona ipo vizuri tu, haitaji tena
mashine. Nafikiri dokta Lubuva akirudi tena baadaye, anaweza akaruhusu mashine
nyingine hizi zilizobakia zitolewe. Ni kama kwa sasa hazina kazi kubwa.” Nesi
alijibu.
“Daktari atarudi tena mida hii!?”
James aliuliza huku akiangalia saa yake. “Ni kama huwa analala naye tu hapa.”
Geb na James wakamtizama yule dada kama kushangaa. “Analala humu ndani na
Nanaa!?” James akauliza kwa mshangao. Yule nesi akacheka. “Sisi wenyewe
tunasema Nanaa ana bahati ya mtende. Ni yule daktari aliyemfanyia upasuaji wa
kichwa. Anasifika sana hapa. Tuseme hapa nchini. Ndiye daktari mdogo, mwenye
akili na utaalamu mkubwa sana wa mambo ya ubongo. Ana miaka michache sana tokea
arudi hapa nchini kutoka masomoni na huko alikokuwa akifanya kazi. Sasa sijui
ni ujana au kulevya na sifa, huwa ni mkorofi sana. Salamu yenyewe huwa
inamshinda kwa wenzake. Yaani kumuona analala hapa kwa Nanaa, sisi wenyewe
hatuamini. Anajiamini sana. Hapa wote wanamwita mungu mtu. Hajawahi kuua
mgonjwa hata mmoja kwenye upasuaji wake, tokea afike hapa. Huwa watu wanamuhesabia
na kumngojelea hiyo siku atakapotoa maiti huko chumba cha upasuaji.”
“Hata aletewe mgonjwa mwenye
tatizo kubwa vipi, akimshika yeye, na akasema atamtibu, basi ujue huyo atapona
tu. Ndio maana wanamwita yeye ni mungu mtu. Tunasemaga huwa ana kazi ya kuumba upya huko kwenye
chumba cha upasuaji. Na akishamtoa mgonjwa huko, wenzake ndio watamuhudumia
huyo mgonjwa huko wodini mpaka aruhusiwe. Yeye kupita huko kwenye mawodi, ni
mara moja moja sana. Huwa anaona wale wagonjwa wenye matatizo makubwa. Labda
wenye vimbe kubwa sana za kichwani. Ambao mpaka madaktari wote wamekata tamaa,
hizo ndizo kesi zake dokta Lubuva.”
“Sasa kitendo cha kulala kwenye
chumba cha Nanaa na kumuhudumia yeye mwenyewe, ameshangaza mpaka madaktari
wengine. Akitoka hapa kwenye chumba cha Nanaa, ujue hata masaa 6 hayaishi,
atarudi tena. Na atataka kumuhudumia yeye mwenyewe. Haruhusu hata mumpe dawa ya
maumivu bila yeye mwenyewe kusema. Mngemkuta hapa. Mmepishana naye kidogo tu,
na amesema atarudi tena.” James na Geb wakaangaliana. Lakini wote wakajua
sababu ya maombi.
Yule nesi akamgeukia Nanaa.
“Kuna kitu chochote utahitaji?” “Na-omba m-aa-ji ya ku-ny-wa.” Nanaa alitaka
maji ya kunywa. “Mbona anaongea hivyo?” Geb akalalamika. “Daktari atakuja
kuzungumza na nyinyi. Usiwe na wasiwasi.” Nesi alijibu na kutoka kwenda
kumletea maji. Nanaa alibaki akimwangalia Geb. Alimuona vile jicho lilivyo
vimba na kuvilia damu. Akanyoosha mkono ili amshike.
“P-ol-e.” Nanaa akaongea kwa
shida. “Unajisikiaje?” Geb akamuuliza. “Nimefurahi kukuona. Nilikusubiria tokea
jana nilipozinduka.” “Ulizinduka jana!?” James akauliza kwa mshangao. Nanaa
akatingisha kichwa taratibu machozi yakimtoka. Akamuona na Geb machozi
yakimtoka. “Njoo.” Nanaa akamuita taratibu. Wakati
Geb anataka kuinama ili amfikie pale kitandani, nesi naye akawa amerudi na
maji. Akanyanyua kitanda ili awe kama amekaa, akataka kumywesha, lakini Geb
akampokea. Akamnywesha yeye. “Asante. Nasikia koo lina kereketa.” Nanaa
alilalamika. “Itaisha tu. Ni sababu ya ule mrija uliokuwa umepitishwa kooni.
Itaisha tu.” Yule nesi akamuweka sawa, akatoka.
“Pole sana Nanaa.” James
akamsogelea. “Asante. Lakini nilikuwa na wasiwasi. Nilijua
mmenisahau kaka.” Nanaa akaanza kulia. “Hapana. Geb alipatwa matatizo. Hivyo
unavyomuona na yeye ametoka hospitalini. Alikuwa amelazwa, wala hajaruhusiwa,
ametoroka tu. Fahamu zilipomrudia tu, akaoga na kuja hapa.” Nanaa akashangaa.
Akamgeukia Geb.
“Nilikuwa nimechanganyikiwa
Nanaa, unisamehe mdogo wangu. Nilimtafuta huyo tokea jana asubuhi tulikuwa
hatumuoni. Nikajua ukiamka ndio mtu wa kwanza utakayemuulizia. Nimemtafuta
mpaka kwenye vyumba vya maiti! Huko kwenye wodi za wanaume ndio usiseme! Mpaka
wote nahisi wamenifahamu. Nilikuwa nafunua wagonjwa mpaka waliozidiwa. Yaani
ndio leo asubuhi nikaenda kumkuta wodini Mwananyamala, analalamika maumivu.
Ndio nikamuhamishia hospitali ya Agakhani. Asubuhi ile ile walimfanyia vipimo
karibia vyote kuangalia ndani kwenye huo mwili. Maana kwa nilivyomkuta,
nikahisi alivamiwa na majambazi wakampiga. Lakini walikuta kila kitu kipo
sawa.” Nanaa akarudisha macho kwa Geb.
“Hajala wala kulala tokea
umelazwa hapa. Kwa mara ya kwanza leo ndio amelala kule hospitalini. Tena kwa
masaa hata nane hayajafika. Alikuwa anashinda amepiga magoti pale nje ya ICU
kuanzia asubuhi mpaka usiku.” Nanaa akashangaa sana, machozi yakaanza kumtoka.
Geb akasimama na kutoka. “Haiwezekani kaka!” “Kweli.
Hajaongea kitu zaidi ya kukuulizia wewe pale alipotoka tu usingizini. Lakini
tunahisi alivamiwa na majambazi wakati anakuja huku au atakuwa amejeruhiwa na
huyo dereva taksii aliyekuwa anamleta huku, na kumpokonya kila kitu. Alikuwa
anatafutwa tokea jana. Mama yake alikuwa akilia kama amechinjwa. Hapo amewaacha
Grace na mama yake Agakhani kwenye chumba alichokuwa amelazwa, yeye akaja
huku.” “Jamani
Geb!” Nanaa akazidi kulia.
“Sasa usilie, usije ukapandisha
tena pressure.” James akajaribu kumtuliza. Nanaa akajifuta machozi. “Ila Nanaa,
Geb anakupenda sana. Anakuthamini na anakuhitaji kwenye maisha yake. Sijawahi
ona! Nilikuwa nikishinda naye hapa, mimi mwenyewe nilikuwa nashindwa kuhimili,
naondoka. Joto, njaa, na kiu! Nilikuwa namletea hata maji, hataki kunywa.
Aliomba bila kuchoka.” Nanaa alibaki na mshangao.
Jimmy Mikononi Mwa Mama Yake.
Baada ya muda Geb alirudi akiwa
ameshika mtoto. Nanaa alitoa macho. “Huyo ni Jimmy?” Akanyanyua mikono ili
ampokee. “Hawakuwa wameniletea mwanangu! Walisema
nisubiri mpaka nipate nguvu.” Nanaa akafuta machozi. Geb akamsogeza mpaka
pale kwa Nanaa. Nusura Nanaa amtupe baada ya kuiona sura yake. Geb akamdaka kwa
haraka. “Mungu wangu!” Nanaa akashangaa. Macho aliyatoa, akaweka mkono mdomoni. “Ni
mtoto wangu Nanaa. Jimmy ni Magesa bila ubishi.” Bado Nanaa hakuwa akiamini.
Jimmy alikuwa ameshikwa na baba yake. “Sasa nimemtoa kule wakiwa bado hawajampa
maziwa. Njaa inamuuma. Walikuwa wakiniambia, ukizinduka, unaweza kuwa unamuweka
kwenye chuchu avute. Maziwa yatakuja kutoka.” Bado Nanaa hakuwa akiamini.
Alilia Nanaa bila hata kumshika huyo mtoto. Nesi aliingia na kumwambia wapo
kwenye kubembeleza afya yake ili pressure isije kupanda tena. Anatakiwa atulie
kabisa.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Nanaa alikumbuka shida na
wasiwasi aliokuwa amebeba akidhani Jimmy ni mtoto wa Malii. Akakumbuka jinsi
alivyokuwa amemchukia huyo mtoto na kukasirikia hiyo mimba. Nanaa alilia
akimuhurumia huyo mtoto jinsi alivyokuwa akimnyanyasa huko tumboni. Kila
alipokuwa akijigeuza, alikuwa akilia kwa hasira. Ni kama aliyekuwa akimkumbusha
siku Malii alivyombaka. Alitamka wazi hamtaki. Akakumbuka mazungumzo yake na
Geb, akimtuliza na kumwambia Jimmy ni baraka. Wala Mungu hakukosea kumpa
yeye. Akakumbuka vile Geb alivyokuwa akizungumza na Jimmy huko tumboni mpaka
akaweza na yeye kuzungumza naye. Nanaa alijisikia vibaya sana na kumuhurumia
mwanae.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Namuomba Geb.” Nanaa akajaribu kutulia.
Akampokea. “Mungu anisamehe na wewe unisamehe Jimmy.
Sikukutendea haki mwanangu.” Nanaa alianza kulia tena. “Naomba utulie
Nanaa. Nakuhitaji turudi nyumbani.” Geb alijaribu kumtuliza. Simu ya James
ikaanza kuita. Alikuwa Grace na mama yake. Akatoka kuwaelekeza walipo, na wao
walikuwa wamefika hapo ICU na kumkosa Nanaa. Walipoenda kule kwa watoto,
hawakumkuta Jimmy. Nesi waliyemkuta zamu aliwaambia baba yake alimchukua. Ndipo
wakampigia James kwa kuwa Geb hakuwa na simu.
“Walikuwa wakimlisha nini siku
zote hizo?” Nanaa akauliza huku akimwangalia kwa makini. “Maziwa ya kopo.
Nilikuwa nikienda kumlisha mimi mwenyewe.” “Asante Geb.” Wote walikuwa
hawaamini. “Mjaribishe kumnyonyesha.” Geb akajaribu kumuwekea mto na kumpanga
Jimmy ili anyonye. Akamshikia mtoto na kumuwekea chuchu. Jimmy akaanza kuvuta
kama aliyekuwa amefundishwa kitu chakufanya. Akaona machozi yanamtoka Nanaa.
“Pole na hongera mke wangu.” Geb akambusu kwenye kipanda uso. “Nimefurahi, sijui nieleze nini kwa Mungu akaelewa ninavyomshukuru!” “Mimi
nahisi ni zaidi yako Nanaa. Mungu amenipa watoto watatu na amenirudishia wewe!
Hakika siamini.” “Pole Geb. Pole kwa matatizo.” “Wewe
ndio zaidi Nanaa. Niliingiwa na hofu ya ajabu. Sijui kwa nini. Nilijua safari
hii ndio utaniacha moja kwa moja.” Nanaa akamuhurumia.
Mama G, Grace na James
wakaingia. Nanaa akaanza kulia. Grace akamsogelea, Geb akamfunika Nanaa kifuani
kama kumsitiri ziwa alilokuwa akinyonyesha. Grace akamkumbatia. “Pole Nanaa.
Pole sana.” Mama G naye akasogea. “Pole sana Nanaa. Pole mama.” “Asanteni. Wanangu hawajambo?” “Inabidi ujitahidi hapo utoke.
Mama mzazi ana kazi yakuwatafuta kuanzia asubuhi mpaka usiku anapokwenda
kulala.” “Jamani Liv wangu. Labda kesho wataniruhusu.
Wasiponiruhusu naomba mniletee.” “Sasa
na hizo gozi kichwani! Si ataogopa?” Mama G akauliza huku akimwangalia Geb.
“Leo nitazungumza na huyo daktari aliyemfanyia upasuaji. Nimsikilize
anasemaje.” “Giza limeshaingia. Sasa hivi labda unaweza kumpata daktari wa zamu
tu, huyo daktari aliyemfanyia operation ni mpaka kesho tena. Nashauri mpate
ushauri wa daktari kwanza kabla hatujaanza kuleta watoto.” “Wamesema atarudi.”
Geb akamjibu mama yake. Alionekana kushangaa kidogo, akatizama saa yake
kuangalia muda.
“Umemuona Jimmy?” Nanaa
akamuuliza mama G. “Huyo mtoto katufunga mdomo na kututoa macho watu wote!
Mungu ni waajabu Nanaa! Amekusitiri mwanangu. Mpaka leo mimi siamini!” “Hata
mimi mama. Na hivi walishaanza kumdai wakidhani alikuwa wa Malii, ni vile Geb
alinituliza siku ile nilivyokwenda naye chumbani kabla ya kile kikao. Nilikuwa
namlilia na kumwambia Geb, namshangaa Mungu ni kwa nini aruhusu mimi kubeba
mtoto wa Malii na si yule aliyekuwa mkewe. Naye Geb bila kujua akawa
ananituliza akaniambia Mungu anajua kuwa tunamuhitaji huyu mtoto. Akawa
ananibembeleza nitulie na tumpokee kama zawadi tu. Sasa nikawa najiuliza hivi
huyu Geb amesahau kama jioni hiyo tunakuja kudaiwa huyo mtoto! Lakini nikamuona
mwenzangu ametulia. Akanibembeleza mpaka nikalala. Sikujua kama ni mtoto wetu!”
“Hakika hapa itabidi kutoa shukurani kubwa sana.” Wakabaki wameduaa.
Mlio wa Jimmy akivuta ziwa la
mama yake ndio ulisikika. “Hapati kitu huyo ndio maana anavuta kwa nguvu na
unasikia hizo kelele. Nimemtuma Jeri alete uji. Daktari akikubali, itabidi
uanze kula, maziwa yatoke.” Mama G alivunja ukimya.
“Itabidi Grace urudi ukanifungashie nguo zangu, halafu umpe Jeri aniletee huku hospitalini.” Kila mtu akamwangalia Geb. “Nini?” Akamuuliza mama yake. “Wewe si uliambiwa huwezi kulala hapa?” “Ni wakati ule yupo ICU, sasa hivi naweza. Siwezi kuondoka hapa bila Nanaa. Na nikiona wananikatalia, nahama hospitali. Namuhamishia Nanaa hospitali..” “Watakayokuruhusu na wewe kulala?” Mama yake akamalizia kwa kumuuliza swali. “We Geb?” “Nimesema sirudi nyumbani bilaNanaa, mama. Kokote alipo na mimi nitakuwepo.” “Na watoto?” “Waleteni kesho!” Geb akajibu.
“Kwa nini usirudi usiku wa leo,
ukawaona watoto na kuagana nao vizuri halafu kesho ndio ukaja hapa moja kwa
moja?” Geb alimtizama mama yake kwa jicho la huo ndio uamuzi wangu sibadiliki. Mama
yake akaelewa. “Sawa baba. Basi acha tumsubiri huyo daktari tujue kama
mtaendelea kuwa hapa au mnahama hospitali nyingine. Ili tujue pakuwapata hiyo
kesho tunapoanza kazi ya kusafirisha watoto.” Geb akarudisha macho kwa Nanaa na
mtoto aliyekuwa amefunikwa.
“Naona kweli hashibi. Ngoja
nimrudishe kule ili nikampe maziwa.” “Lakini bado nina hamu naye Geb!” Nanaa
alilalamika kama asiyetaka Jimmy aondolewe pale. “Acha mimi niende nikalete
hayo maziwa ili umpe mwenyewe. Akilala ndio tumrudishe kule ili na wewe
upumzike.” “Nitashukuru Grace. Naomba niulizie kama naweza kulala naye.” “Kazi
imeanza.” Mama G akaongea nakumfanya Nanaa acheke kidogo. “Wewe mwenyewe
umejawa mashine, ongea yenyewe ya shida na bado unataka ulezi! Utaweza kachanga
sasa hivi wakati wamekupasua kichwa juzi tu hapa!? Nipeni mimi huyo mtoto
nitamrudisha kesho.” “HAPANA.” Geb alishitua kila mtu mpaka Nanaa mwenyewe.
“Nimesema Jimmy atatoka hapa hospitalini siku mama yake atakapotoka. Anabaki hapahapa.
Daktari wake akipita nitamuuliza kama ni sawa Jimmy kuhamia hapa. Mimi mwenyewe
nitamtunza Jimmy na Nanaa.” “Sawa baba.” Mama G akakubali kwa haraka. Grace
akatoka kwenda kufuata maziwa. Nanaa alifurahi sana moyoni. Akamshukuru Mungu
wake.
Nanaa na
Dokta Lubuva.
Nanaa alibaki akimtizama yule
daktari. “Sura yako sio ngeni.” Aliongea taratibu huku akiendelea kumtizama
yule docta kwa makini kama anayevuta kumbukumbu. Ndiye aliyemfanyia upasuaji wa
kichwa. Alirudi hapo chumbani kwa Nanaa, usiku huo na dokta Lyamu pamoja na
nesi wa zamu. Wakina mama G na James walishaondoka baada yakujua kuwa Nanaa na
Geb watakuwepo hapo hospitalini mpaka Nanaa atolewe. Jeri alishaleta nguo za
Geb na uji.
Aliridhika kujua Geb atakuwepo
hapo pamoja naye. Alirudi kulala kwa haraka wala hakuongea sana kama kawaida
yake. Hata wakati kina mama G wakiondoka alikuwa alisharudi kulala. Lubuva
ndiye aliyemuamsha kutoka usingizini wakati akimpima pressure. Akaendelea
kuangalia mambo kadhaa mwilini mwa Nanaa huku Nanaa naye akimtizama kwa makini
kama anayejaribu kuvuta kumbukumbu ya wapi alimuona. Alimmulika na tochi ndogo
machoni na kutaka afuate ule mwanga. Akamuhoji maswali machache na kumtaka
Nanaa ayajibu. “Una watoto wangapi?” Dokta Lubuva akarudia tena swali, kwani
Nanaa hakuwa amejibu.
“Nikumbushe kwanza ni wapi
tulionana.” Ikabidi Geb asogee pale kitandani. Kwa sababu Nanaa hakuwa akijibu
maswali aliyokuwa akiulizwa na yule daktari na yule daktari alionyesha kukwepa
lile swali la Nanaa. “Nanaa! Labda kwa kuwa ndiye aliyekufanyia upasuaji na
ndiye aliyekuwa akikuhudumia tokea uzinduke.” Geb aliingilia. “Hapana. Ni zaidi
ya hivyo.” Nanaa alijibu kwa uhakika huku macho yake yakiwa kwa Lubuva. “Anza
kwa kujibu maswali madogo madogo ili na mimi nijue hali ya ubongo wako baada ya
upasuaji. Hasa sehemu ya kumbukumbu.” Yule daktari akaongeza. Nanaa
akamwangalia tena na kufunga macho. Kila mtu aliyekuwepo hapo akashangaa.
Geb akamgusa. “Nanaa!”
“Nimechoka Geb. Hayo ni maswali wananiuliza tokea nazinduka. Nakumbuka kila
kitu.” “Naomba basi ujibu tena.” “Nakumbuka mpaka na maswali yake ambayo pia
sasa hivi hajauliza. Nimechoka Geb.” “Nanaa!” Geb akaendelea kumsihi. “Nina
watoto watatu. Liv, Magesa na Jimmy. Mume wangu ni Geb Magesa. Mimi ni mtoto wa Wini niliyekataliwa na baba yangu mzazi.
Nimelelewa na kaka James. Daktari wangu ni Lyamu. Na sasa hivi nina usingizi
nataka kulala.” Nanaa akavuta pumzi kwa nguvu, kisha akatulia. Wakajua analala.
“Atakuwa amechoka. Tumemfanya aongee sana jioni hii.” Geb akamtetea na kumfunika baada ya kumbusu. “Kwani kuna kitu kingine ulitaka kumuuliza? Naona kama amejieleza kwa mapana sana!” Geb akamgeukia Lubuva. “Hapana. Nafuatilia tu maendeleo yake. Kutaka kujua baada ya ule upasuaji kama ubongo wake umerudi kwenye hali ya kawaida na hapotezi kumbukumbu.” “Unaonaje sasa?” “Naona kila kitu kinafanya kazi sawasawa. Ila pia nilitaka kujua kama ana maumivu.” Lubuva akajibu. “Kwa jinsi nilivyozungumza naye, anaonekana anakumbuka kila kitu. Hana tatizo kwenye kumbukumbu ila kuzungumza tu.” Geb akajibu.
“Na kingine pia chakuongezea
hapo, ujue Nanaa sio mlalamishi. Halafu hospitalini ni sehemu ya mwisho
atakayokubali kukaa kwa siku nyingi akiwa na akili zake timamu. Maswali ya
unajisikiaje, ujue jibu utakalopewa ni moja tu, ‘nzuri’, ili mruhusu atoke. Na usipomruhusu, kama anaweza kutembea,
ujue utakutana naye mlangoni akiondoka, na hatarudi mpaka azidiwe karibu ya
kufa.” Dokta Lyamu aliweka msisitizo, wakacheka kidogo.
“Sikutanii Lubuva. Huyo ndio
Nanaa. Labda awepo Geb ndio mnaweza kuelewana naye. Anachagua aina yake ya
matibabu na muda wake yeye.” Lyamu akasisitiza. “Tutaendelea hivyo hivyo.”
Dokta Lubuva akajibu huku akicheka na kumtizama Nanaa kwa makini sana. “Nawashukuruni
sana kumsaidia.” Geb akashukuru. “Tupo pamoja. Haina shida.” Geb hakuyaamini
maneno ya yule nesi aliyosema juu ya huyo dokta Lubuva. Alikuwa mnyenyekevu
sana hapo kwao.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Naomba kuuliza kabla hamjaondoka.” “Juu ya
nini?” Dokta Lubuva akamuuliza. “Ni juu ya chakula cha Nanaa na kunyonyesha.
Nanaa hapendi watoto wake wale kitu kingine zaidi ya maziwa yake. Swala la
kujua mtoto wake anakunywa maziwa ya kopo, linamnyima raha na hilo tu linaweza
kumfanya asitulie.” “Kabla Lyamu
hajajibu, mimi niongezee kwenye swala la chakula. Najua alibadilishiwa vyakula
au alipewa masharti juu ya vyakula anavyotakiwa kula, sababu ya pressure yake
kuwa juu au kupanda. Hata sasa inabidi kuendelea hivyo hivyo. Anaweza kula,
lakini mzingatie chumvi na mafuta. Vyakula mnavyojua vitamsumbua kupata choo,
msimpe kwa sasa. Vyakula vinavyopikwa na mafuta mengi kama chips na nyama za
kukaanga, vinatakiwa kusubiri mpaka apone na kurudia hali yake ya kawaida. Tena
kwa kula mara moja moja kwa hamu, sio yakawa ndio maisha yake ya kila siku. Nafikiri
nyinyi mnaelewa mambo ya afya.”
“Kwa upande wa dawa, hakuna
dawa kali anazopewa sasa hivi zakumfanya ashindwe kunyonyesha au kuathiri
maziwa ya mtoto. Aanze tu taratibu mpaka maziwa yatakapotoka. Lakini lazima
ujue Nanaa anahitajika mapumziko Geb. Najua mngetamani kumuona anafanya mambo
fulani fulani, lakini mjue ni mgonjwa. Amefanyiwa upasuaji mkubwa sana na bado
tatizo la kupanuka kwa moyo halijatibiwa, anahitajika mapumziko.” Lubuva akahitimisha.
“Naona Lubuva amejibu kila kitu, sina pakuongeza labda kuangalia tu tumbo
lake.” Lyamu akafanya wacheke kidogo. Akajisogeza pale alipokuwa amelala Nanaa,
nakuanza kuminya tumbo lake.
“Naona kila kitu kipo vizuri.”
“Nawashukuru wote. Najua hizo zitakuwa habari njema kwa Nanaa.” Geb akashukuru
tena na kuongeza mbele ya madaktari hao bingwa wanaosifika hapo hospitalini
kwenye fani zao. Ni kweli Nanaa alikuwa kwenye mikono mizuri. Hawakuruhusiwa
kulala na mtoto kwa usiku huo, ili Nanaa apate masaa mengi yakulala bila
kuamka. Lakini Geb alikuwepo hapo.
Nanaa Na Dr.Lubuva Tena.
Alfajiri sana Lubuva akarudi
tena. Akavuta mkono wa Nanaa taratibu ili kumpima pressure. Nanaa akafungua
macho. Akamwangalia kwa makini. “Nimekumbuka wapi nilikuona.” Nanaa aliongea
taratibu. “Wapi?” Dokta Lubuva akauliza huku akiendelea kumpika. “Naomba shika
mkono wangu kwa nguvu zako zote.” Alimtaka Nanaa amminye mkono wake kwa kutumia
mkono wake wakulia na kushoto. “Nilikuwa benki. Sikuwa na kalamu. Ukaja kwa
nyuma yangu ukanipa kalamu kama uliyejua nina shida ya kalamu, kisha ukaondoka
bila kuchukua kalamu yako.” Nanaa akamkumbusha. Kisha akaminya mkono wake.
“Naomba unishike tena na mkono
wako wakushoto. Kwa nguvu zako zote.” Lubuva aliendelea bila kuongeza kwa kile
alichozungumza Nanaa. Geb alikuwa akiwasikiliza. “Siku nyingine tulikutana
super market nikiwa na mama pamoja na watoto wangu. Uka…” Nanaa akakunja uso na
kumtizama kwa makini kama aliyeshituka kwa kukumbuka jambo. Lubuva akaendelea
bila ya kuongeza neno kwenye hizo kumbukumbu za Nanaa. “Unaonekana unae…” “Wewe
unanifahamu mimi!?” Nanaa akamkata yule dokta kwa kumuuliza swali.
Geb akasimama na kuwasogelea pale
kitandani. “Nanaa!” Geb akamwita taratibu. Lakini bado macho ya Nanaa yalikuwa
kwa dokta Lubuva. “Uliomba kumsalimia Liv, mtoto wangu yule mkubwa. Ukampa na
mkono na kujaribu kuzungumza naye. Ulimuuliza maswali kadhaa, akakujibu na
kukushangaza. Ukatuambia hukutegemea kwa mtoto wa umri wake kuwa na uwezo
mkubwa vile wakuelewa swali na kujibu kifasaha kwa kiasi kile. Nimekukumbuka
kwa kuwa ulishangaa sana na kumpongeza. Ulitaka kumpa zawadi. Ukamwambia
achague kitu chochote pale ili umnunulie, Liv akakataa. Ukaondoka. Tena
uliondoka bila kuwa na kitu chochote mkononi.” Nanaa akaendelea kukumbuka
taratibu.
“Unanifahamu?” Nanaa akauliza
tena. “Naomba utulie akupime, Nanaa. Mpe nafasi akuhudumie. Inawezekana
ilitokea tu.” Geb alijaribu kumtuliza. Nanaa akafunga macho. “Vipi
unavyomuona?” Geb akamuuliza dokta Lubuva. “Anahitaji tu kupumzika. Lakini
nikimwangalia ni kama kila kitu kipo sawa.” “Lini mtaniruhusu?” Nanaa akauliza
akiwa amefunga macho. “Ukiendelea hivyo, baada ya siku mbili tutakuruhusu.
Tutaanza kukupunguzia dawa ili kupunguza huo usingizi, urudie hali yako ya
kawaida.” Dokta Lubuva alimjibu huku akimwangalia. “Utarudi tena baadaye?”
Nanaa akamuuliza huku akisinzia. “Ndiyo.” Akarudi kulala.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Dokta Lubuva ni nani?” Hilo
swali likaanza kumsumbua na Geb. Nanaa hakupata tatizo la kumbukumbu mara baada
ya upasuaji. Hata wenyewe wamekiri hivyo. Amekuwa akikumbuka na kumkumbusha
Lubuva, naye hakukubali wala kukanusha. “Anamfuatilia
Nanaa?” Geb akaendelea kuwaza pale alipokuwa amekaa peke yake. “Kwa wema au ubaya?” Wasiwasi ukaanza
kumwingia Geb. “Kama ingekuwa ni kwa ubaya,
asingehangaika naye hivi. Au alimuona Nanaa huku hospitalini akija kwa matibabu
au kliniki, akampenda mke wangu!” Wivu ukaanza. “Kwa nini ajitoe hivi mpaka ashangaze watu!? Ipo namna tu.” Geb
alianza kumtilia mashaka. Ni kweli Lubuva hakukanusha chochote alichoongea
Nanaa. “Lubuva ni nani?” Swali hilo
likaanza kumuumiza kichwa Geb.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Lubuva ni nani? Nanaa anaonekana kumkumbuka, lakini
Lubuva hatoi maelezo yakutosha.
Bado Nanaa yupo hospitalini baada ya
upasuji mkubwa wa kichwa. Nini kitaendelea?
0 Comments:
Post a Comment