Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Ni Wangu! - Sehemu Ya 66. - Naomi Simulizi

Ni Wangu! - Sehemu Ya 66.

Nanaa akaona atoe maelezo, kwani kila mtu alikuwa kimya sana. “Samahanini jamani. Najua wote hamjaelewa. Hasa Geb, mpenzi wangu.” Geb akamtizama kidogo na kuendelea kuendesha. “Kuna dada mmoja. Mtu mzima kidogo. Anaitwa Mama Mazigo au dada Mazigo, kila mtu pale kliniki alimwita vile anavyopenda yeye, na yeye hakuwa na shida. Na yeye tulikuwa naye kliniki. Sema tumeachana naye kwa kuwa tumebadilishiwa siku za kwenda kliniki. Lakini mwanzoni kabisa mara ya kwanza kukutana naye, nikamjua ni mwanasheria. Ni machachari sana. Au mzungumzaji sana. Akawa akisimulia kuwa yeye anatetea haki za wanawake. Ameshafanya kazi mpaka UN. Mimi nikapata moyo wakuzungumza naye.”

“Siku hiyo tulipotoka kliniki, nikazungumza naye kwa muda mrefu. Nilimueleza mkasa wangu mzima juu ya Malii. Nikamuuliza mtu kama mimi anaweza kunisaidiaje? Wakati huo sikuwa na pesa zakuanza kulipia wanasheria, lakini roho yangu ilikuwa ikiniuma sana. Nilijiambia hata kama sina mtu wakunitetea, basi angalau nijitetee mwenyewe.” Ikaanza kuwagusa.

“Akaniuliza kama hilo tukio liliripotiwa? Nikamueleza kuwa watu wote siku ile walinikimbia na ni kama waliona nastahili. Nikamwambia kwa kifupi hakuna hata anayejali kile nilichofanyiwa, niliachwa peke yangu. Hakuna hata anayejali nilipo. Ila nikamwambia yule dada, najihisi kuwa sikutendewa sahihi. Yule dada akaumia sana. Akaniambia nisiwe na wasiwasi, atanisaidia. Lakini tatizo likawa mashahidi sasa. Tukio lenyewe likawa halikuwahi kuripotiwa. Kwa kiyo akasema ugumu utakuwa ni maneno kati yangu mimi na Malii. Maana yule dada Mazigo alikwenda mpaka kwenye ofisi ya kampuni ya walinzi wale wa Geb.” Geb akashangaa.

“Alikwenda kuulizia tarehe hiyo kama kuna tukio lolote liliripotiwa. Yule mwenye kampuni ni kama alimfukuza yule dada. Na kumwambia ule ni uzushi tu. Lakini yule dada hakukubali. Akatafuta mmoja wa walinzi waliokuwepo siku ile. Akampata. Tena alikuwa na yeye ameacha kazi hapo. Akamfuata yule mlinzi mpaka kwake. Akaambiwa ametoka, yupo kazini. Yule dada akamtafuta yule mlinzi mpaka akampata. Uzuri alikuwa ni yule mlinzi aliyekuwa amekuja kule chumbani siku ile niliyokuwa nimebakwa. Alinifungua na kunifunika. Kwa hiyo alijua kweli nilibakwa, na akamwambia dada Mazigo alishindwa kuripoti kihalali japo walimwambia mwenye kampuni tukio zima. Ila wenye nyumba wenyewe waliomba hilo tukio lisiripotiwe kabisa kwa kuwa waliondoka na ndugu yao. Yaani waliondoka na Danny, na wakasema wakitoa taarifa polisi, Danny atauwawa. Yule dada akamuuliza yule mlinzi sasa kwa nini wasiripoti hilo tukio baada ya Danny kurudi? Ndio yule mlinzi akamwambia yule dada kuwa, wenye nyumba walihama pale, wakaniacha mimi mle ndani peke yangu. Kwa hiyo yule mlinzi akawa ni kama ameongea kabisa kama mimi. Yule dada akazidi kupata ushahidi.” Nanaa akaendelea.

“Alinitafuta tena, akasema kwa sasa tunaweza kufungua kesi, lakini tunahitaji ukiri wa mtu aliyeshuhudia lile tukio. Ndio nikamwambia kwa wakati ule sikuwa na mtu ambaye anaweza kunisimamia au kunitetea, nimebaki peke yangu. Yule dada akahangaika ili kama Malii anaweza kukamatwa, akamatwe. Lakini hatukujua pa kumpata Malii. Nilimpelekea jumbe zote alizokuwa akinitumia Malii, akaziprint kabisa. Lakini kutokana na zile jumbe za Malii, tukajua kwa hakika hayupo hapa nchini.” Nanaa akendelea.

“Basi, tukawa kama tumepata ushahidi wa kiasi. Maana Malii alituma jumbe za kuniomba msamaha kwa kitendo alichonifanyia. Lakini nayo yule dada mwanasheria akasema anao uwezo wa kukataa. Maana siku hizi watu wanacheza na mitandao. Anaweza kusema sio yeye. Na akatoa uthibitisho wa tiketi ya siku alipoondoka nchini, na kuwa hakuwepo nchini. Akaunti ya Whatsapp anayotumia ni ya namba ya kitanzania. Anaweza kusema ni mtu mwingine alikuwa akiitumia wakati yeye hayupo nchini. Akaniambia nisikate tamaa. Atatunza ule ushahidi. Lakini itasaidia kama nikipata rafiki yake hata mmoja ambaye atakiri.” “Oooh! Ndio maana ulikuwa ukimuuliza vile Gozi?” Grace akauliza.

“Yale ni maswali aliyokuwa amenifundisha dada Mazigo. Vitu vya msingi. Kutaka kujua kama pia wanawasiliana. Inamaana watajua kuwa Gozi anajua alipo. Wakimkamata Gozi, ndio watakuwa wamempata Malii. Amesema watambana mpaka ataje alipo.” “Pole sana Nanaa.” Man aliyekuwa amekaa kiti cha nyuma yake akampa pole. “Asante Man. Naomba Mungu hiyo jioni waje.” “Utamfanyaje sasa?” Man akauliza. “Sasa hivi nampigia simu huyo dada. Namwambia huo ujio wa Gozi. Najua atataka kuja na polisi ili wamkamate.” “Sasa Gozi hatakimbia akiona polisi?”  Man akauliza. “Hawezi. Huyu dada anaonekana ni mzoefu sana. Kwa jinsi nilivyomuona na jinsi anavyozungumza, anaonekana matukio kama haya anauzoefu nayo.”

“Sasa si atakuwa anakudai pesa nyingi sana?” “Sijawahi kumpa hata shilingi. Anasema kunakuwa na pesa maalumu zinatengwa kwa ajili ya kutetea wanawake. Zinatolewa na umoja wa mataifa. Wanaangalia na uwezo wa mtu. Kuna wanaochangia kidogo, na wengine bure. Sasa wakati ule mimi nilianza naye nikiwa sijui hata kesho yangu itakuaje. Ndio maana alikuwa akihangaika ili amkamate Malii, na nilipwe fidia, japo hilo halikuwa lengo langu. Lakini niliamua nijitetee mwenyewe.” Nanaa aliongea kinyonge, asijue hukumu wanayoipata Geb na Grace.

“Pole sana Nanaa. Mungu atakulipia.” “Lakini Man, usifikiri mimi ni mtu wakulipiza kisasi. Lakini siku ile niliumia sana. Niliona nimeadhibiwa kupita kiasi. Niliachwa nikiwa navuja damu, peke yangu! Siku ile nilipoteza kila kitu, Man. Kila kitu. Nilibaki peke yangu kama nilivyoletwa hapa duniani. Malii alinipokonya kila kitu changu, zaidi utu wangu. Mbaya zaidi alinifanyia ule ukatili mbele ya kaka yangu, ambaye ni kama baba yangu! Niliumia mno. Amenisababishia maradhi ya kudumu. Sijui kama nina siku ngapi zakuishi hapa duniani. Kila siku naiishi kama sitaiona kesho. Madaktari hawana uhakika na maisha yangu siku ya kujifungua kwangu. Siwezi kuzaa kwa kawaida sababu ya matatizo ya moyo yaliyonianza baada ya Malii kunitenda. Sijui kama nitatoka chumba cha upasuaji au la.” Nanaa aliongea kwa upole.

“Nilikata tamaa kabisa ya hiyo kesi. Kwanza nilikuwa nikiipigania mimi peke yangu. Tena nikiwa ndio ninasumbuliwa na pressure. Mara nianguke kwenye daladala, mara nilazwe. Nikamwambia yule dada tuache tu kwa kuwa kwanza sina uwezo wakupata ushahidi mwingine, na sipo tayari kuiona sura ya Malii. Nikamwambia nahisi siku nitakayomuona tena, itakuwa kifo changu. Tukapotezana na yule dada. Lakini siku chache kabla ya harusi, alinipigia simu kunijulia tu hali. Nikamuelezea nilipo. Akaniambia kama naweza tena kupata ushahidi tunaweza kufufua ile kesi. Nikawambia sidhani, kwa kuwa kwanza hamna hata mtu anayefikiria kumshitaki Malii. Nikamwambia na mimi nahofia kuanzisha mazungumzo kama yale wakati ndio nimepata neema yakurudishwa kwa wanangu na ahadi ya ndoa. Nikamwambia naona tuache tu. Lakini akasisitiza, ikitokea napata mwaya, hata kidogo tu, nitumie.” Nanaa akaendelea.

“Leo nilipomuona Gozi, nilianza kutetemeka kwa hofu. Lakini nikajiambia moyoni inawezekana ndio Mungu ananitetea. Ndio nikatumia ule mwanya vizuri. Nimerikodi kila kitu. Nataka kumtumia yule dada haya mazungumzo yote. Najua akiwa karibu na yupo sawa kiafya atakuja na polisi. Akishindwa, mimi mwenyewe naenda mpaka kituo cha polisi. Uzuri yule dada alinitengenezea faili lenye kila kitu. Kesi aliyofungua na ule ushahidi wote. Alitoa kopi na kuniwekea. Akasema chochote kitakachompata yeye, au nikibadili mawazo hapo badaye naweza kutumia hilo faili. Yaani hapa tukifika tu nyumbani, nikihakikisha mmekula na kushiba, mimi nitatoka. Nitahakikisha Gozi anakamatwa leo, na nitendewe haki yangu kabla sijaenda kujifungua. Hata nikifa huko chumba cha kujifungulia, basi. Lakini na yeye Malii awe amelipa ubaya alionitendea.” Nanaa akawa amemaliza. 

“Pole sana Nanaa. Mungu atakutetea. Ukihitaji msaada wowote hata mimi naweza kukusaidia. Nafahamiana na watu wanaojua mambo ya sheria.” “Asante Man. Basi nitalikumbuka hilo. Kama huyu dada hataweza, nitakuomba msaada. Maana na  yeye alishika mimba zile za utuuzimani. Alikuwa na wasiwasi sana ndio maana alianza kliniki mapema. Hakuwahi kushika mimba. Ndio mtoto wake wa kwanza, na yeye alikuwa anasema umri umekwenda. Kwa hiyo akishindwa, basi nitakutafuta. Asante.” “Karibu na wakati wowote.” Wakatulia.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Grace na Geb wakabaki kimyaa. Ni kweli hawakuwa hata na wazo la kushitaki. Geb hakujua kama Nanaa ana mzigo mkubwa hivyo. Hakujua hata kama anafaili la Malii. Hakujua kama ni aibu mbele ya Man kwa ukweli aliousema Nanaa pale. Ni kama alifungua mabaya yote. Grace yeye alijichukia kuokoa uhai wa Danny siku ile na kumuacha Nanaa.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

          “Kweli mama hakukosea.” Grace alisikika kwa majuto. “Unajua mama huwa anasema Mungu wa Nanaa huwa anapigana na watesi wake na huwa anamtetea tu?” Man alimgeukia Grace na kumsikiliza. “Mimi ndiye niliyemuonya yule mlinzi hata asiwaambie wenzake. Nikamwambia atoke kimya kimya na aendelee na shuguli zake na ajifanye kana kwamba hakuna kilichotokea. Ili tu kumuokoa Danny.” Grace akacheka. “Lakini malipo yake, wala hayakusubiri. Yule mwanaume alishindwa hata kusema asante! Yaani kuanzia usiku ule, naona mpaka leo, Mungu ananichapa kwa hilo.” Grace aliongea kwa uchungu sana. Nanaa akashindwa hata aseme nini. “Ni kama niliokoa maisha ya Danny usiku ule ili kuja kuwaua wanangu!” Kimya. Hata Nanaa hakujua aseme nini.

“Hakika nimejawa na majuto ambayo hakuna jinsi naweza kueleza mtu akanielewa. Danny hakuwahi kuwa mnafiki kwangu. Hata kabla hajanioa hakuweza kujificha. Sina hata sababu ya kulaumu kama wanawake wengine, eti kusema alinidanganya akaja kubadilika baada ya kunioa! Hata kidogo. Hakuwahi hata kujifanya watofauti kwangu. Danny huyu wa leo, ndiye Danny niliyeingia naye kanisani na kukubali awe mume wangu. Najiuliza hivi kwa nini nilifunga macho yangu nikaolewa naye, mimi sijui! Kwa nini nilikubali kuuwa utu wangu kwa kiasi kile kwa Danny, sielewi! Ni kweli tulimuacha Nanaa akilia peke yake. Tena akilia kwa uchungu sana. Sikuweza hata kusogelea alipokuwepo.” “Wakati mwingine jambo linapotokea kuna kupaniki, Grace. Usijilaumu sana.” Man alijaribu kumfariji.

“Na kesho yake? Kesho kutwa yake je!?” Geb akauliza. “Tulifanya kosa Man. Wala hakuna haja yakujitetea. Hakika tulikosa. Wote. Haswa mimi. Hakina Mungu aturehemu. Asiendelee kutupatiliza. Namsihi hasira yake ikome juu yetu. Atusamehe tu.” Geb akaendelea. “Na sijui niseme nini! Ni kama sisi wote tuliokuwepo siku ile na kushuhudia ule ubaya, hatujawahi kubaki tulivyo. Kila mtu alilipwa kwa wakati wake. Na Mungu alihakikisha ametulipa na kusikia ule uchungu. Hakika Mungu atusamehe.” Nanaa alibaki kimya kabisa. Alionekana anatuma jumbe zake.

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Walirudi nyumbani. Nanaa akasaidia kupangwa kwa chakula mezani. Wakati wapo mezani wanakula, simu ya Nanaa ikaanza kuita. Akaingalia, wakamuona ananyanyuka kwenda kuzungumza nje. Akarudi, akatulia tu mezani bila kuongea chochote. Watoto wake walikuwa wamelala. Tumbo hilo lilishakuwa kubwa kama anayetaka kujifungua. Geb akamuona mikono inaanza kutetemeka taratibu. Akajua tayari pressure imepanda. Akamtizama, lakini yeye mwenyewe alikuwa ametulia tu.

“Nikuongezee juisi?” Nanaa akamuuliza. “Naona inatosha. Asante.” “Umeshiba?” Nanaa akauliza tena.

Fili alifika hapo akiwa amelala. Walienda kumlaza. Hapo mezani alikuwa mama G, Man, Grace, Geb, na Nanaa. Mke wa Jeri anayemsaidia Nanaa maswala ya watoto alishaondoka mara baada ya wao kuingia. Msichana wa kazi wa Grace alirudi kwao mara baada ya kuzika. Kulikuwa na utulivu wa namna yake hapo mezani. Mama G hakushangaa. Bado kila mtu alikuwa kwenye maombolezo.

“Naona inatosha. Ulikumbuka kumeza dawa?” Geb akamuuliza. Nanaa akafikiria kidogo. “Nilikunywa asubuhi kabla ya kwenda hospitalini.” Alijibu na kusimama akitoa vyombo. Geb akaona na yeye asaidie. Akamfuata jikoni. “Pressure imepanda Nanaa.” Nanaa akajiangalia mikono. “Naomba twende ukapumzike.” “Natoka mara moja. Naenda kukutana na yule dada. Yupo ofisini, kisha nitarudi kupumzika. Usiwe na wasiwasi. Mimi nitakuwa sawa tu.” “Twende wote.” “Geb!” Nanaa akashangaa. “Naomba wewe acha tu. Kaa hapa na wageni. Grace anakuhitaji sana sasa hivi. Mimi nitarudi baada ya muda mfupi sana. Naenda kuwekana sawa na huyo dada, kisha nitarudi.” Geb akabaki kimya, akabaki akimtizama.

“Nitachukua taksii hapo nje, itanifikisha tu. Sitaki ujiingize kwenye mambo ambayo hayana umuhimu Geb. Naomba pumzika tu, mimi nitashugulikia hilo. Kwanza Liv atafurahi akiamka na kukukuta wewe.” Nanaa akataka kutoka. “Nanaa! Kwa kutofuatilia hili jambo haimaanishi sijali.” “Najua mpenzi wangu. Naelewa kabisa. Wala usijisikie vibaya.” “Najisikia vibaya. Na wewe kukataa kuongozana na mimi sasa hivi ndio najihisi ni kama umenisusia.” “Geb!” “Sasa ni nini kama sio hivyo?” Geb akauliza.

“Nilikwambia nilikosa Nanaa. Tokea hili jambo limetokea nilikosea jinsi ya kukusaidia. Sasa hivi nataka kusaidia. Naomba usiendelee kunisukumia mbali.” “Sikutaka kukuingiza huko. Kwanza ni kama jambo lenyewe linaishia. Najiona ni kama nakaribia kupata haki yangu.” Nanaa alisikika akicheka taratibu, lakini cheko iliyojaa simanzi.

“Wewe tulia hapa nyumbani. Nitakuja kukwambia yale tuliyozungumza na huyo dada.” “Naomba twende wote ili na mimi niweze kuzungumza naye. Naweza kuwa msaada.” “Unauhakika?” Nanaa akauliza. “Si mlikuwa mkitafuta shahidi aliyeshuhudia hilo tukio, mimi nilikuwepo Nanaa. Naweza kuwa shahidi wako.” “Hata mimi Nanaa.” Alimsikia Grace naye akiongeza. Nanaa akaanza kulia. “Kuna nini?” Mama G akauli na kusimama kumfuta Nanaa na Geb jikoni.

“Huyu pressure imeshapanda.” Mama G akaingia na kushika mikono ya Nanaa. “Geb, kalete mashine ya kumpimia na wewe njoo ukae hapa. Halafu uniambie kinachopandisha pressure wakati tuliagana asubuhi ukiwa mzima.” Wakakaa. Nanaa akamsimulia kwa kifupi. “Sasa Nanaa mwanangu, kesi yenyewe hujaanza, pressure ishapanda! Utakamata walifu wewe?” Nanaa akaanza kucheka huku analia.

“Muulize Grace jinsi nilivyomrikodi Gozi. Kama polisi! Mimi nipo sawa kabisa na leo nitawakamata tu.”  “Sasa pressure kwa nini ipo juu?” “Hasira mama.” Nanaa akajibu. “Hasira hizi kwa Malii au Geb?” Mama G, alimjua Nanaa. Akainama na kuanza kulia kwa uchungu sana. “Mimi nakujua sana Nanaa. Najua moyo wako. Hasira hizi ni za Geb tu wala sio mtu mwingine. Bado unamlaumu Geb.” “Aliniacha mama. Heri kila mtu angeniacha lakini sio Geb.” “Na nilikwambia nini? Eti Nanaa? Sasa hivi hapo unazidi kuteseka kwa ajili ya hilo. Samehe mama. Samehe hilo liishie Nanaa.” Geb akarudi na mashine. Akamvuta mkono, akaanza kumpika.

“Inabidi twende hospitalini Nanaa.” “Mimi siendi mpaka nimkamate Gozi.” Nanaa alijibu huku akilia. “Basi utakufa kabla hata huyo Gozi hujamkamata!”“Bwana usiseme hivyo mama! Ujue mimi nimemkasirikia Geb.” Man akacheka kidogo. Wote walikuwa wamesogea hapo jikoni. “Basi utakufa huku hujamkamata Gozi na umemkasirikia Geb.” Mama G, akaongeza. “Twende tukazungumze Nanaa.” Geb akamshika mkono. Akakataa. “Mimi naona heri tu uende. Hiyo hali yako ilivyo, hakika nenda tu. Presure ipo juu, hupo kwenye nafasi ya kuadhibu mbaya wako hata mmoja.” Nanaa akacheka huku analia. Akasimama. 

“Sasa kwa nini uliniacha Geb?” Nanaa aliendelea kulia huku anatoka pale jikoni, Geb anamfuata nyuma. “Uliniacha wakati mimi nakulilia! Tena uliniacha sakafuni! Mimi bado nimeumia. Kila saa nasahau halafu nakuja kukumbuka tena. Mimi nisingekufanyia hivyo.” Walimsikia akiongea huku anapandisha ngazi, Geb nyuma. “Utaanguka Nanaa. Naomba utulie kwanza. Halafu acha kulia.” Walisikia wakiongea huku wanapandisha ngazi.

“Mmmh!” Grace akaguna. “Asipojifungua huyu leo, ni bahati.” “Mama!” Grace akashangaa. “Mimi nipo hapa. Kwanza ameshachoka. Na hayo aliyoyaanzisha ndio kabisa.” “Lakini hao, wanawezana wao wenyewe. Labda atatulia.” Wakahamia kwenye makochi. 

~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

Baada kama lisaa Geb akashuka. “Amelala.” Geb aliongea wakati anatafuta sehemu ya kukaa. “Na hiyo pressure?” “Nimeongea na daktari wake. Alitaka nimpeleke sasa hivi. Lakini amezungumza na Nanaa mwenyewe, akamuomba twende baadaye. Kwa hiyo ameniambia nimpe dawa ya usingizi, alale kabisa. Mpaka nitakapompeleka akamuone.” “Sasa na hiyo kesi yake?” Grace akauliza.

“Nimezungumza na huyo dada aliyekuwa akiifuatilia hiyo kesi. Tumekubaliana aje na askari kanzu, watakaokuwa nje tu. Hawataingia ndani mpaka kina Gozi waingie humu ndani. Huyo dada na yeye atakuwepo hapa kabla kina Gozi hawajafika. Atauliza maswali ya kutosha ndipo wamkamate Gozi. Watambana mpaka wataje Malii alipo.” “Afadhali umsaidie apumzike. Lakini ujue huyo hana siku nyingi. Nanaa atajifungua.” “Acha kuniogopesha mama, bwana!” “Ndio nataka ujiandae.” Geb akapooza.

“Umenisikia Geb? Tumbo lake limeshuka sana. Inamaana mtoto yupo tayari kutoka. Au yupo kwenye njia ya uzazi. Wakati analia pale, lilishaanza kukakamaa. Limeanza kuwa gumu na kuachia. Dalili za kuanza ule uchungu.” “Mbona daktari alivyomuuliza kama anasikia dalili zozote za uchungu, alikataa! Na ndio maana ameniambia nimpe dawa ya usingizi tu alale.” “Ni mawili, hajui au anajikaza mpaka akamilishe mambo yake.” “Basi namrudisha hospitalini sasa hivi. Hawezi kuanzwa na uchungu mbali na madaktari.” “Mwache alale kwanza. Muache ashuhudie Gozi amekamatwa, ndipo umwambie swala la kumpeleka hospitalini. Bila hivyo ataona umempuuza.” Geb akanyamaza.

“Usiogope Geb. Atakuwa sawa tu.” Grace alijaribu kumtuliza kaka yake. “Hakika Mungu anitetee katika hili. Ampitishe Nanaa kwenye hili pia. Asinipokonye. Nahisi nitachanganyikiwa kabisa.” “Wewe umeona Mungu wake anavyompigania. Atatoka tu, wala huyo sio wakufa leo.” Mama yake aliweka msisitizo. Geb akasimama. “Sasa unaenda wapi?” Grace akamuuliza. “Naenda kuomba. Nashauri na nyinyi mkapumzike mpaka jioni.” “Unamaana tuondoke?” “Mnataka kufanya nini sasa hivi? Mmelala hospitalini usiku kucha. Nashauri mkapumzike hotelini au muingie kwenye chumba chochote hapo mlale.” Geb akaondoka. Grace na Man wakaangaliana.

“Unafikiri ni sawa tukiondoka?” “Huna utakachokifanya hapa. Kapumzike tu. Chochote kikitokea tutawajulisha.” “Nimezungumza na yule msichana wangu wa kazi, aliyekuwa akiwalea kina Fillius, amesema atarudi jumamosi. Atakusaidia.” Grace akaongea kinyonge. “Sasa hapo si ulitakiwa kufurahia kwa kuwa tumepata msaada?” “Nawakumbuka wanangu mama. Nawakumbuka sana. Yaani nakaa wakati mwingine najiambia labda nitawaona wanaingia au labda nitaona zile fujo zao! Siamini kama ndio wameenda na sitawaona tena! Naumia sana mama yangu.” “Naelewa Grace. Pole mama.” Man alimsugua mgongoni taratibu.

“Jipe muda. Hiyo hali itapungua tu.” “Kweli mama?” “Kabisa. Bado mapema sana. Kama alivyokwambia Geb, hata katika hilo, tafuta faraja.” “Sioni mama.” “Kwa sababu umeumia. Jipe muda. Kubali tukusaidie Fili, pata muda mwingi wa kupumzika. Usingizi ukiisha, tafuta kazi yakufanya. Itakusaidia. Usikubali mawazo yako yawe hayana kitu chakufikiria. Utakaa hapo muda mrefu sana.” “Unafikiri nirudi kazini?” “Zungumza na mwenzio. Kazi pia itakusaidia. Lakini usijipe muda mwingi wa upweke.” “Namuhurumia Man. Namsumbua kweli!” “Naelewa Grace. Mimi nipo sawa tu. Pole.” Akambusu kichwani. “Kweli naona tukapumzike.” Grace akasimama.

“Kikitokea chochote mtujulishe.” “Mimi nakufahamu Grace. Hiyo sentensi ushairudia zaidi ya mara tatu. Unawasiwasi na Geb.” Grace akacheka. “Nyinyi  kapumzikeni kule nje kwenye chumba cha wageni. Hamna atakayewasumbua huko. Huyu baba mzazi akimka huko hafiki. Atazunguka huku huku. Usingizi ukiwaisha mje hapa. Usiku ndio mkalale hotelini.” Grace akamwangalia Man. “Wewe ulitakaje?” Man akamuuliza. “Natamani kuwepo mpaka nijue Nanaa ataamkaje. Sitaki tuondoke halafu..” Grace akanyamaza. “Sawa, twende.” “Asante Man, najua unanivumilia sana. Nitakuwa sawa tu.” Man akambusu na kumshika mkono. Wakaondoka.

Usiku wa Heka heka

Mpaka inafika saa moja kasoro usiku, James hakuwa amepokea simu yeyote kutoka kwa Gozi. Akaamua kwenda yeye mwenyewe nyumbani kwao. Man alikuwa akicheza na watoto hapo sebuleni wakati Grace na mama yake wakiwa jikoni. Nanaa aliamka. Geb akampima pressure, ilikuwa imeshuka kwa kiasi. Akampeleka bafuni kuoga, wakatoka.“Bado unanipenda?” “Nakupenda Geb, ndio maana unaniumiza.” Geb akamvuta karibu. “Nifanyeje ili unisamehe kabisa?” Nanaa akacheka. “Nimekusamehe lakini kila nikikumbuka nakuwa naumia.” Geb akambusu.

“Nilikosa Nanaa.” “Kweli ulikosa Geb. Lakini yaishe.” Geb akambusu tena. Nimemuomba Mungu anipe miaka mingi ili nilipize mabaya niliyokutendea.” “Utafanyaje?” Nanaa akauliza huku akicheka. “Nitakupenda mpaka ushangae.” Nanaa alicheka sana. “Unanitia hamu yakuishi.” “Ndio usife. Tutamkamata Malii, atalipa kwa ubaya aliokutendea. Halafu sisi tuendelee kuishi.” “Sawa.” Wakaanza kupeana mabusu. Wakasikia mlango unagongwa taratibu.  “Nani?” Geb akauliza, wakamsikia Liv akicheka kwa kisauti kidogo. “Ni nani huyo anagonga?” Geb hakufungua akabaki akimuuliza. “Liv wa Geb, binti Magesa!” Liv alijibu na kufanya kila mtu acheke mpaka bibi yake aliyekuwa jikoni na kina Grace.

Geb na Nanaa walifungua mlango kwa pamoja huku wanacheka. Walimkuta amesimama nje ya mlango anacheka na kidole chake kimoja mdomoni. Alijibu vizuri na kwa ufasaha. Geb alifurahi sana. Akambeba na kumfanyia kitu Liv anapenda. Akamuweka kifuani kwa muda huku akigugumia, na kuanza kumbusu. Liv alikuwa akicheka kwa sauti nzuri na kufanya kila mtu acheke. “Nampenda dad!” “Na mimi nampenda sana Liv, binti Magesa.” Geb alimjibu binti yake nakumfanya azidi kufurahia. Alitingisha kimguu chake kimoja akiwa bado amebebwa na baba yake.

Geb akambusu tena. “Anko amekuja.” “Asante kwa taarifa Liv. Ujue wewe ni mtoto mzuri sana?” Geb akawa anamuongelesha Liv, akacheka. “Twende Nanaa.” Wakashuka huku Geb akiongea na mwanae. “Mbona umechoka hivyo!?” James akamuuliza Nanaa. “Geb huyo ndio amenipa madawa ya usingizi. Hata hivyo siku zimesogea kaka yangu. Nipo mwishoni. Nahisi kulemewa!” Akakaa. “Shikamoo kaka.” “Marahaba.” “Kina Gozi wako wapi?” “Hawajanipigia ndio maana imenibidi nije tu.”  Mlinzi akapiga simu, Geb akapokea. Akawaambia mama anamgeni. “Nani?” Geb akauliza na kuweka spika ili kila mtu asikie. “Amejitambulisha kama mama Mazigo.” “Ni yule dada mwanasheria.” Nanaa akaongeza kama anayemwambia Geb. “Mfungulie.” Geb akamwamuru mlinzi.

 Yule dada akaingia. Ni kweli alikuwa dada mtu mzima kidogo na ni mjamzito. Nanaa akamtambulisha kwa kila mtu, akakaa. “Tuhamie mezani. Mimi njaa inauma.” Nanaa akatoa wazo. “Ni sawa. Lakini naomba kwanza tujue watakaa wapi ili nitafute sehemu nzuri nitakayo kaa mimi ili niweze kuwachukua video na nitegeshe hii recoder yangu. Nataka nipate mazungumzo yote vizuri ili kusiwepo na kurukana hapo baadaye.” Yule dada mwanasheria, Nanaa aliyemwita dada Mazigo, alionekana yupo kikazi.

“Kama unavyopaona hapa dada yangu. Wewe chagua tu. Utakapotaka wakae, ndipo watakaa hapo.” Nanaa akajibu. Mazigo akaangalia vizuri. Akajaribu kuangalia kwa camera ya kupitia simu yake akiwa pale mezani, akapata sehemu atakayowapata vizuri. Akawachagulia sehemu ya kukaa. Wakakubaliana watakapoingia wakae huo upande wa sebuleni. Akategesha na hiyo kinasa sauti chake.

Ndipo wakahamia mezani kwa chakula. Nyumba hiyo huwezi kuingia bila kula. Marafiki zao wote walipajua nyumbani kwa mama G. Lazima kuliwe. Huwezi ukaondoka hapo bila kupewa chakula. Wakakutana na Nanaa mpenda kula! Hapo huwezi kupata aibu. Anakukaribisha chakula wakati na yeye amejaza sahani akisifia chakula chake na umuhimu wa kula. Alijulikana mpenda kula. Wakaanza kula. Kulikuwa na ukimya kidogo. Grace alishamsaidia mama yake kumlisha Magesa, kwahiyo alikuwa akizunguka tu hapo wakati Geb akimlisha Liv. Fili alikuwa amekaa kwenye kochi ametulia tu.

Grace akatoka mezani akamfuata. “Vipi Fili?” Fili akanyamaza. “Unasikia maumivu?” Grace akamuuliza taratibu. Fili akakataa. “Unataka kula?” Akakataa. “Njoo basi nikupakate.” Akahamia mapajani kwa mama yake. “Nakupenda Fili.” Grace alisikika akiongea taratibu. Fili akajisogeza kifuani kwa mama yake akajilaza.

Za Mwizi Ni 40.

    Baada ya muda kidogo mlinzi tena akapiga simu. Grace aliyekuwa karibu na simu akapokea kwa kubonyeza spika. “Ongea, wenye nyumba wanakusikia.” Grace alimwambia mlinzi. “Mama!” Mlinzi akaita. “Wewe ongea. Wanakusikiliza usiwe na wasiwasi.” Grace akasisitiza. “Kuna wageni hapa. Lakini wawili wapo kwenye ile orodha ya watu ambao hawaruhusiwi kuingia hapa. Gozi na Zinda.” Geb akasimama. Akasogelea simu. “Na wengine ni kina nani!?” “Wamejitambulisha kama familia ya Malii.” Mlinzi alijibu, moyo wa Nanaa ukashituka sana. Geb akamwangalia Nanaa. “Subiri kwanza. Nitakupigia kukupa maelekezo.” Geb akamjibu mlinzi na kukata simu. 

“Waruhusu waingie tu Geb.” “Unauhakika Nanaa?” Akatulia kidogo. Geb akabaki akimtizama. “Unaweza kufanya mambo yote ukiwa umeshajifungua.” “Acha tu nimalizane nao Geb.” “Huwezi kumalizana nao hao Nanaa. Ujue ndio watakuwepo kwenye maisha yako daima.” Mama G akaongeza. “Waache waingie ili tuwasikie.” Nanaa akasisitiza. “Subiri kwanza Nanaa. Tunaweza kuuwa ndege wawili kwa jiwe moja. Kwani kuna wenye ‘restraining oder’ hapo?” Geb akasimulia kwa ufupi ni kwa nini aliwatafutia rafiki zake hiyo ‘restraining order’. “Safi sana. Na wao wanajua kama wamezuiliwa kufika hapa?” Mazigo akauliza.

“Ndiyo. Niliwatolea nakala yao. Nikawapelekea mbele ya mwanasheria wa mwenzao. Na nilimpigia simu yule mwanasheria kuhakikisha aliwasomea na kuwaelewesha, akasema alifanya hivyo.” Geb akamjibu Mazigo. “Safi sana. Sasa wewe waruhusu waingie, lakini naomba na mimi nipate nakala ya hiyo ‘restraining order’ .” “Bila shaka.” Geb akajibu. Akapiga tena simu getini kwa mlinzi. “Waruhusu waingie, lakini waache magari yao nje. Wasiingie na chochote humu ndani. Sitaki pochi, wallet hata simu. Kila kitu waache kwenye gari lao. Sitaki mitandio humu ndani na kama wamevaa makoti au sweta, tafadhali wakaguliwe vizuri. Wakikubali hayo masharti, basi wafungulie geti dogo.” “Sawa.” Mlinzi akajibu, Geb akaelekea chumbani kwake kufuata moja ya nakala za hiyo retraining order’ ili amkabidhi Mazigo. 

Baada ya muda mfupi tu, akarudi nayo. Akamkabidhi, akarudi kwenda kuendelea kumlisha Liv. Mazigo naye akajirudisha sehemu yake. Ukimya ukatanda. Nanaa akatoka pale kwenye meza ya chakula na sahani yake ya chakula, akaenda kukaa kwenye makochi. Akaendelea kula taratibu.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Kengele ya mlango ikasikika. Mazigo akasimama kwa haraka, akaenda kuwasha ile rekodi aliyokuwa ametegesha chini ya kimeza kidogo, sehemu aliyojua atawapata sauti zao vizuri. Ndipo akarudi kukaa kama anayekula. Geb akaenda kufungua mlango. Alitangulia baba yake Malii, akaja mdogo wake, mama yake mzazi, mjomba wake Malii, Gozi na Zinda. Mama G hata hakusalimia. Geb akawakaribisha wakae. Nanaa akawa kimya akiwatizama.

“Hujambo mama?” Baba yake Malii akamsalimia Nanaa. “Shikamoo.” Nanaa akasalimia. “Marahaba. Tumekuja kukusalimia.” Nanaa akabaki akimtizama. “Tunataka kujua wewe na mjukuu mnaendeleaje?” “Ni nani aliyewaambia yupo mjukuu wenu hapa?” Nanaa akauliza, wakaangaliana kidogo. Wakababaika. “Wanajua kila kitu Nanaa.” Gozi akadakia. “Wanajua kila kitu!?” Nanaa akamuuliza Gozi. “Acha kuwazungusha wazazi Nanaa. Wana haki na huyo mtoto. Ni damu yao.” “Nyinyi ndio mmenifuata nyumbani kwangu, kwa mume wangu. Mnaniambia mmekuja kuniangalia mimi na mjukuu wenu. Nawauliza swali, mnababaika. Gozi umejibu wanajua kila kitu. Nakuuliza ni nini wanachojua ambacho sisi hapa tunatakiwa tukifahamu, unaniambia nawazungusha. Sidhani kama nyinyi wote mlikuja hapa mkitaka tuzungushane. Zungumzeni kitu kinachoeleweka, ili tusipotezeane muda.” “Kufupisha habari ndefu, kwani hiyo mimba Nanaa ni ya nani?” Zinda akauliza. “Wewe unauliza kama nani?” Nanaa akamuuliza swali. Kimya.

“Labda mimi ambaye ni baba yake Malii niulize hiyo mimba uliyonayo ni ya nani?” “Kwa hiyo wewe mzee unachofanya nikuzunguka kwenye majumba ya watu, unauliza wake za watu mimba ni za nani!?” Nanaa akamuuliza yule Mzee. “Yaani nyinyi mmekuja hapa kuniuliza mimi mke wa mtu kuwa mimba niliyonayo ni ya nani!? Kweli!?” Nanaa akauliza.

“Mama Magesa wewe tunaheshimiana sana. Haya mambo yanaweza kuwa yalitokea katika ubaya lakini Mungu amekumbuka ukoo wetu. Ametupa mjukuu. Hiyo ni damu yetu.” Mama G akasimama akamsogelea mama yake Malii. “Umesema mimi na nyinyi tunaheshimiana?” Mama G akauliza. Kabla hajajibu akaendelea. “Heshima hiyo ni ipi? Mnakuja kwenye majumba ya watu. Mnauliza mke wa mtu. Moja kwa moja! Hamjamtaka mumewe au mama yake. Mnaulizia mjukuu mliyeletewa habari ambazo hata nyinyi mmeshindwa kumjibu Nanaa mwenyewe. Heshima yenu nyinyi iko wapi? Mamlaka hiyo yakumfuata mke wa mtu, usiku, mnaulizia mjukuu wenu! Mjukuu huyo wakichaga, katikati ya kina Magesa! Kweli? Nashauri mjipange vizuri.” Mama G alikuwa amesimama.

“Labda mimi nizungumze jamani. Ili tusiwachanganye hawa wazee ambao wamefika leo. Wametoka Kilimanjaro, wamechoka.” Gozi akaingilia. Mama G akakaa. “Mimi nilikuwepo kwenye siku ya tukio.” “Sikiliza Gozi. Kama unataka tukusikilize, ongea mambo kwa wazi. Acha kufumba.” Nanaa alimkata. “Naona kuna wageni.” “Acha kutufanya sisi ni watoto wadogo. Umeshatangaza kwa kila mtu. Ni nani hapa ambaye hutaki ajue? Wewe ongea mambo kiuwazi, yaishe.” Nanaa akasisitiza.

“Sawa. Mimi nia yangu ni nzuri tu. Malii ni rafiki yangu. Siwezi kumkana hapa. Na nitasimama naye hata kama wengine hawanielewi.” Wote wakanyamaza. “Sasa ni hivi. Siku Malii alipokuja hapa na kumbaka Nanaa, mimi pia nilikuwepo. Siku aliyombaka karibia wengi wetu hapa tulikuwepo. Nanaa alikuwa akitokea hospitalini, na baada ya kubakwa, kesho yake hawa watu wote walihama hapa, wakamuacha Nanaa hapa peke yake, ndio Nanaa akaamua kuondoka. Alipofikisha mimba kubwa kabisa, ndipo wakarudiana na Geb, na kuamua kuona kabisa. Malii anamtaka mtoto wake. Huyo mtoto ni wa Malii. Kwa kuwa baada ya kumbaka, Geb alimuacha Nanaa. Hakuna muujiza kuwa huyo mtoto ni wa Geb. Malii anasema ameshamuomba Nanaa msamaha, amemtaka amfuate wakaendelee na maisha yao, lakini anasema anashangaa Nanaa hamjibu lolote na anaona kabisa anasoma jumbe zake. Halafu akashangaa anaolewa na Geb, na kunyamaza na mtoto wake! Malii anasema hataki damu yake ipotee.” Gozi aliongea kwa kujiamini.

“Kwa nini asije Malii mwenyewe, akutume wewe?” Nanaa akauliza akiwa ametulia tu. “Malii yupo mbali. Nje ya nchi. Ndio ametuma wazazi wamsaidie kuweka sawa mambo ili kuhakikisha mtoto wake hapotei.” “Naomba niwaulize swali nyinyi wazazi wa Malii. Gozi naomba usijibu.” “Sawa.” Gozi akajibu. “Nyinyi kama nyinyi wazazi, habari kuwa nina mtoto wa Malii, amewapa Malii mwenyewe?” Nanaa akauliza. “Hapana. Malii yupo mbali. Rafiki yake huyu, ndiye aliyetupigia simu na kutueleza habari za mjukuu wetu.” Akajibu baba yake Malii. “Kwa hiyo mpo hapa kwa ajili ya maneno ya Gozi tu? Yaani amewaambia kuwa Malii, alibaka mwanamke, akampa ujauzito, njooni mdai damu yenu, ndio mkaja?” Nanaa akahoji.

          Walibabaika sana wakizungumza hili na lile. “Kama nimewasikiliza vizuri na kama nimewaelewa vizuri majibu yenu, ni kwamba, mpo hapa kwa ajili ya maneno ya Gozi, na hamjui mahali alipo Malii?” “Sio kwamba ni maneno tu Nanaa, acha kusumbua wazazi. Mimi nilikuwepo siku Malii anakubaka, na mimi mwenyewe nimewasiliana na Malii, Malii ndiye amenituma niwaombe wazazi wake waje kudai mtoto wao.” Gozi akaweka msisitizo na kuendelea kuongea kwa kujiamini kama anayetaka kumbana  Nanaa kwenye kona. Aliongea bila aibu wala huruma kwa Nanaa aliyebakwa mbele yake na alimsikia akilia.

“Dada Mazigo umesikia, kila kitu?” “Yaani nakushukuru sana Nanaa. Nimepata kila kitu na nimechukua video nzuri tu. Nimeshawatumia ujumbe waje.” Mazigo akajibu. Wageni wao wakawa hawajaelewa. Kidogo, kengele ya mlango ikasikika tena. Geb akasimama kufungua.

“Sasa mimi ni mwanasheria ambaye ninasimamia kesi ya Nanaa. Tunakushukuru Gozi kwa kuwa shahidi wetu wa hiari wa tukio lililompata Nanaa. Tulikuwa tukitafuta ushahidi tu wa mtu wakaribu sana na Malii, kama wewe. Ambaye atakuwa tayari kuthibitisha unyama wa Malii, aliomfanyia Nanaa.” Mazigo, akasimama. “Sasa kwa kuwa umekiri wewe mwenyewe kuwa ulikuwepo siku ya tukio. Mnawasiliana na Malii, na unajua alipo, basi, naomba utujulishe alipo.” Gozi akashituka sana. Na wale askari kanzu watano walikuwa wamesimama pale.

“Hao ni askari kanzu. Kitu cha kwanza kilichowaleta hapa na watakachokihitaji kutoka kwako Gozi, nikujua alipo Malii. Ukishataja alipo, ndipo tutajua chakufanya kuanzia hapo. Lakini ukikataa, ujue unalo kosa la kusaidiana na muhalifu. Tuanzie hapo kwanza.” “Lakini hivyo mnavyofanya sio vizuri Mama Magesa. Sisi tumekuja kwa amani tu, tukidai haki yetu.” “Tafadhali mama Malii! Mmetuanza wenyewe. Hata hivyo mlisema mmekuja kukutana na Nanaa, sio mimi. Kama ungekuwa ukitambua mahusiano yetu tokea zamani, ungeanza kunitafuta mimi, tukazungumza. Mmekuja kuharibu amani ya nyumbani kwangu. Mmekutana na mkono wa Mungu aliye hai.” Mama G alijibu na kumgeukia Zinda.

Kwa Zinda!

Tayari wote walikuwa wakitetemeka kama waliopigwa shoti ya umeme.  “Zinda! Unakumbuka mara ya mwisho ulipokuwepo humu ndani? Ulikuja kuomba msamaha kwa mabaya uliyomtendea Nanaa. Na ukamuombea msamaha Mira kwa uchawi aliomfanyia Nanaa. Nanaa akaponywa na Mungu hospitalini, yale mauchawi yote, yakamrudia Mira. Wewe mwenyewe ulikuja kukiri humu ndani. Unakumbuka maneno niliyokuonya lakini?” Kimya.

“Nakukumbusha, ili ukatafakari ukiwa jela.” “Kwani mimi nimefanyaje?” Zinda akauliza. “Hukujua kama ulipewa ‘restraining order’ ya kutokufika humu ndani?” Mazigo akamuuliza. “Mwanasheria wenu hakuwasomea madhara yatokanayo na kukiuka yale masharti?” Mazigo akamuuliza. “Sasa utakwenda kujibu tuhuma zako mbele ya vyombo vya sheria. Mama endelea.” Mazigo alimpisha mama G.

“Nilikuonya Zinda. Na nikakwambia ukawaambie wenzako, kuwa wasicheze na Nanaa. Mungu wake huwa anampigania, mpaka sisi wenyewe tunaogopa. Huna baya utakalomfanyia huyu mtoto, Mungu wake asishuke yeye mwenyewe kupigana na watesi wake. Hakuna mtu hata mmoja hapa aliyehusika na kukamatwa kwenu. Kwanza ndio leo sisi wote ndio tumejua kama Nanaa aliwafungulia mashitaka. Alikata tamaa kwa kuwa hakuwa na ushahidi wa kutosha. Akaamua kunyamaza, yaishe hivi hivi. Lakini ona Mungu wake alivyoshuka kupambana nanyi! Kwanza amemtafutia mwanasheria wa kimataifa. Amesimama na hii kesi, mpaka sisi tunashangaa. Maana na sisi wenyewe ndio tumemuona leo, usiku huu. Hata hatukuwa tukimfahamu.” Mama G akaendelea.

“Pili, mmejileta nyinyi wenyewe. Tena mkijua wazi mlikataliwa kufika hapa sababu yakutaka kunidhuru mimi. Leo mkajitia ujasiri katika upumbavu wenu, mkarudi tena hapa ili kuharibu amani ya nyumbani kwangu. Umekutana na Mungu aliye hai. Mmetoa ushahidi wote bila hata kuficha. Mmeyasema wenyewe tena bila hata kulazimishwa wala hakuna aliye tumia nguvu. Huyo ndiye Mungu wa Nanaa na Mungu tunayemtumikia. Nilikwambia Zinda, hukunisikiliza. Ona jinsi Mungu alivyowatia mikononi mwake! Na hatatulia mpaka mabaya yote mliyomtendea Nanaa, myalipe na ulimwengu ushuhudie. Mlifanya hila zenu kwa siri. Mmeenda kuongeza nguvu, kwa kuwaleta wazazi wake Malii, mkijua leo mtampata Geb, kwa kumchukua mtoto wa Nanaa, lakini ona mlipo.” “Sio walipo sasa hivi mama Magesa. Watakapoendelea kuwepo kuanzia sasa hivi.” Mazigo akaongeza.

          “Acheni kucheza na nguvu za Mungu nyinyi watoto. Aliyebarikiwa na Mungu mwenyewe, amebarikiwa tu. Mnaona wivu wenu dhidi ya Geb pale unapowapeleka? Niliwaambia sisi huwa tunaomba tu. Magoti ndio silaha yetu. Acheni kushindana na Mungu aliye hai! Hamtaweza.” Zinda kimya kama aliyemwagiwa maji.  “Sasa nyinyi wawili mmevunja sheria. Mlitakiwa msifike hapa na mnajua hilo. Mlipewa onyo tu, baada yakumfanyia fujo mama Magesa. Sasa mtashitakiwa kwa hilo. Wote nyinyi mmevunja sheria, tena kwa makusudi.” “Mpo chini ya ulinzi.”  Wawili wa wale askari kanzu wakawakamata na kuweka pingu.

“Mimi naweza kuwatajia mahali alipo Malii.” Gozi akajitetea. “Hilo sina shaka nalo. Mpaka leo papambazuke, utakuwa umetoa habari zote za Malii.” Mazigo alijibu kwa kujiamini. “Kwanza una makosa mengi sana bwana Gozi. Umekiuka masharti ya kufika hapa, na una wasiliana kwa siri na muhalifu anayetafutwa. Inamaana unamficha. Utakaa ndani mpaka tutakapo mkamata Malii, na wewe utakapojibu shitaka lako la kuvuka mipaka.” Mmoja wa askari kanzu akamjibu huku akitaka kumsukumia Gozi nje.

James Na Yeye Na Ushahidi Wake.

James akasimama kwa haraka. “Naomba usubiri kwanza.” Yule askari akasimama. James akamsogelea Gozi. “Naomba uone hii?” James akamuonyesha Gozi simu yake. Gozi akawa kama anasoma, kisha akamwangalia James kwa mshangao. “Usishangae Gozi. Nilikaa bila kula wala kunywa, baada ya Malii kumbaka dada yangu. Nilikuwa najiuliza ni kwa vipi Malii alijua kama wageni wameondoka na ule ndio ulikuwa wakati muafaka wa yeye kuleta majambazi wake na kumkatili dada yangu? Kwanza ilikuwa siku ya sherehe, halafu akapatia muda. Akaweza kuwalevya walinzi wote bila shida! Nilijiuliza sana.” James akaendelea.

“Ndipo Mungu akaanza kunifungua macho. Mtu mbaya na mnafiki aliyekuwepo siku ile, na kubaki mpaka mwisho ulikuwa wewe peke yako. Nikaanza kutafuta mazungumzo yako kwenye simu. Ndipo nikagundua mawasiliano yaliyokuwa yakiendelea kati yako na Malii. Ulikuwa ukimwambia kila kitu kinachoendelea hapa. Nani bado yupo, na nani anatakiwa aondoke. Tena akasisitiza akinitaka mimi nibaki ili mniumize. Danny maneno mengi, mlimtaka na yeye abaki ili aje kusimulia wengine, kilichompata dada yangu.”

“Mlipanga unyama wenu vizuri sana. Mkatumia wema wangu kwenu vizuri sana. Ukawa na kazi yakutuzubaisha mimi na Danny pale ili tubakie mpaka mwisho, ili tushuhudie Malii akifanya unyama wake kwa Geb, kupitia mdogo wangu! Umenishangaza na kuniumiza sana Gozi. Ukijua ukweli juu ya Malii kwa Geb, unashirikiana naye kumuadhibu Geb kupitia Nanaa mtoto yatima, aliyeishi maisha machungu sana, na nyinyi mnajua! Hakika Mungu akulipe ipasavyo Gozi. Akuadhibu na wewe paume kabisa. Mungu ajilipie kisasi kwako.” James aliongea kwa kusikitika mpaka machozi yalimtoka.

“Nitahakikisha huu ushahidi nao utakufunga Gozi. Hata kama utamtaja Malii alipo, lakini utakuwa naye jela. Hakika utalipa. Ulishiriki kikamilifu kwenye kumfanyia dada yangu unyama. Alikuwa akilia usiku kucha, kumbe wewe unapongezana na Malii! Hakika mtalipa. Namshukuru Mungu kwa kuwakamata leo.” James akajifuta machozi. “James. Na mimi naomba nitolee nakala ya hayo mazungumzo yao ili niwe nayo. Mbona hii kesi inazidi kunoga!” Mazigo alionekana kufurahia. “Nitakutumia kwa fax kesho.” James akajibu.

          “Basi Gozi ndio ona dunia kwa mara ya mwisho hivi. Wewe hutakaa ukatoka leo wala kesho huko jela. Hakika utalipa. Naomba ondokeni nao.” Gozi na Malii wakatolewa na pingu wasiamini kilichowapata. Walikuja kwa ujasiri, wameondoka pale na pingu. Nanaa alikuwa akifuta tu machozi. Ile familia ya Malii hawakuwa wakiamini. Walipotaka kuwatetea, wakaambiwa na wao wanaweza kuwekwa ndani kwa kuzuia upelelezi, wakanyamaza. 

Kwa Wazazi wa Malii.

Walipotolewa tu, baba yake Malii akaanza tena. “Lakini sisi bado tunaulizia swala la mtoto.” “Hakika hatutakubali damu yetu ipotee hivi hivi tu. Ni haki yetu.” Mama Malii naye akaongeza msisitizo. “Naombeni niwaelezee kitu kwa kifupi tu ili tuachane kwa amani.” Nanaa akajifuta machozi. Sauti ilisikika ya uchungu.  “Dada Mazigo naomba usiondoke.” “Siwezi maana hapa nina kifungu cha sheria nataka niwape hao wazazi wake Malii. Nisipofanya hivyo naweza nisilale usiku.” Nanaa akacheka kidogo, alimfahamu huyo dada alivyo machachari.

“Haya dada yangu. Subiri kidogo tu ili niwaelezee hawa wazazi wa Malii, waelewe. Maana wanaonekana wamesikia upande wa Gozi tu.” Yule dada akakaa kwenye kochi. “Sasa ni hivi.” Nanaa akawageukia wazazi wa Malii. “Ni kweli Malii aliingia hapa na majambazi aliokuwa amewalipa kumsindikiza kuja kunifanyia ubaya mimi. Nikiwa nimetoka hospitalini kujifungua yule mtoto wangu pale. Akanibaka siku kama kumi na mbili au 13 baada ya kujifungua. Maana ilinilazimu kuwepo hospitali kwa matibabu baada ya kujifungua.”

“Siku narudi kutoka hospitalini, kulifanyika sherehe ya kunikaribisha nyumbani, na ilikuwa pia ni sherehe ya birthday ya watoto wangu hao wawili. Wote walizaliwa siku moja. Walialikwa marafiki na familia zao. Walikuwepo watu wengi tu na watoto wao. Gozi aliyewaletea habari ndiye aliyehusika kumtaarifu Malii muda wakuja kunibaka kama mlivyosikia. Alikuja na majambazi ambao walifanya fujo. Lakini huko sitakwenda kwa kuwa wahusika waliamua kulinyamazia hilo. Mimi naomba niongelee ya kwangu.” Nanaa akaendelea

          “Sasa baada ya miezi miwili, nikajigundua ni mjamzito. Inawezekana kabisa huyu mtoto niliyebeba ni wa Malii. Lakini kisheria, hata kama Malii hakuwa amenibaka. Naruhusiwa kukaa na huyu mtoto mpaka afikishe miaka..” “Sasa na wewe Nanaa hilo ndilo nilikuwa nataka kusema bwana! Mbona kuninyima usingizi?” Nanaa akaanza kucheka.

“Haya dada yangu.” Mazigo akasimama. “Kisheria kama wazazi wametengana, na wana watoto. Mama anatakiwa kukaa na mtoto mpaka afikishe miaka saba. Endapo mama huyo hana uwezo, ndipo mwanaume au baba wa mtoto anatakiwa kutoa pesa za matumizi. Baba ataruhusiwa kumchukua mtoto huyo akiwa chini ya miaka 7, kama tu mama huyo anamatatizo ya akili. Hana uwezo wa kumtunza mtoto, labda ni Malaya, mlevi, anahatarisha maisha ya mtoto ndipo baba anaruhusiwa kumchukua mtoto wake.” “Sisi hatutaki kumchukua mtoto ila ni kuwa tu na mahusiano.” “Nisikilize mama. Huko nitafika, usiniharakishe.” Mazigo akawa mkali kidogo.

“Malii amefanya kosa la kubaka na kukimbia. Amevamia nyumba ya watu akiwa na watu wenye silaha. Endapo atakamatwa, ataishia jela. Hatakaa akatoka mpaka kifo chake. Na ninaomba mumfikishie Malii ujumbe kuwa, tutamkamata tu. Mwambieni Nanaa anasimamiwa kesi yake na mwanasheria aliyefanya kazi na UN. Bado ninao watu nafahamiana nao nje na ndani ya nchi. Nishakamata wanaume wenye makosa kama ya Malii wengi sana. Tena waliokuwa  wamekimbilia nchi za nje, wakajidai kuomba uraia huko. Niliwakamata na kuwarudisha kwenye nchi zao kujibu shutuma zao. Kwa hiyo mwambieni Malii, MIMI, nitamkamata tu. Hakuna umbali atakaokimbia, vyombo vya usalama visimfikie. Dunia imekuwa ndogo sana. Nina wahakikishia, hata siku saba hazitaisha, Malii atakuwa hapa nchini. Si mmemsikia rafiki yake huyu Gozi, yupo tayari kusema alipo? Sasa hapo hajaenda kuminywa. Atataja mpaka nyumba anayoishi. Kesho kutwa, nitaenda kumpokea Malii hapo uwanja wa ndege na pingu mkononi.” Mazigo aliongea kwa kujiamini.

“Kuhusu swala lenu nyinyi na mahusiano ya mtoto. Kwanza nitaenda kuwafungulia mashitaka kwa kuhatarisha maisha ya huyu mtoto ambaye hajazaliwa.” “Kivipi!?” Mdogo wake Malii akauliza kwa mshangao. “Mmeleta watu hatarishi karibu ya mama mjamzito. Mmekuja na Gozi ambaye kwanza mbali ya kuwa alishuhudia kitendo cha abakwaji na hatotoa taarifa polisi, amehusika katika tukio moja kwa moja. Hana tofauti na kijana wenu huyo Malii. Ameshiriki au amesaidia kosa la jinai kwa asilimia 100. Bila yeye, Malii asingefanikiwa. Pia anayo barua yakuzuiliwa kufika mita mia moja hapo getini. Lakini nyinyi mmevunja sheria kwa kumleta hapa.” “Sasa sisi tungejuaje?” Mdogo wake Malii akauliza tena.

“Swali zuri sana ambalo najua mngeuliza hata mahakamani. Lakini Mzee hapo amekiri kuwa Gozi alimpigia simu na kumueleza kila kitu. Kwa hiyo anajua wazi kuwa Gozi alikuwepo akishuhudia kijana wake akifanya uhalifu. Na anajua Gozi ni rafiki ya muhalifu, na ndiye anayetoa habari hapa na kupeleka kwao na kwa huyo muhalifu. Kwa hiyo kwanza mpo hapa mkiwa tayari mnajua kuwa Gozi anakosa la kushiriki kwenye uhalifu kwa asilimia zote. Kama nilivyosema hapo awali. Alishiriki kukamilisha uhalifu na anamficha muhalifu. Na nyinyi mnajua hilo na mmelifumbia macho. Badala ya kwenda kituo cha polisi, mmemfuata mama mjamzito, kwenye familia yake, na kumnyanyasa. Huo ni unyanyasaji na ukandamizaji wa mwanamke. Mkitetewa sana pale mahakamani, mkapona, basi, nitahakikisha na nyinyi mnapewa ‘restraining oder’. Mkae mbali kabisa na huyo mtoto, ili msihatarishe maisha yake na mama yake zaidi. Mnaswali la nyongeza hapa au kituo cha polisi?” Mazigo aliuliza huku akiwatizama kila mmoja.

“Mimi naona tuyaache haya mambo kama yalivyo mume wangu. Kwanza hatujui lolote.” “Haya, mlango ule pale.” Mazigo akawaonyeshea kidole mlangoni, wakanyanyuka wote kwa pamoja. “Na msifikiri hatuta waripoti!? Nimewapiga picha kadhaa, na kuwachukua video mkiwa mmekaa hapa na wahalifu wenu na maelezo yenu yote. Kwa hiyo hamtatakiwa kumsogolea kabisa Nanaa wala mtoto. Msije sahau hilo yakawapata yaliyompata Zinda na Gozi usiku huu. Haya wazee wangu, usiku mwema.” Wakatoka. 

Bado Ni Usiku Wa Hekaheka.

Nanaa akamgeukia Mazigo. “Dada Mazigo, naomba nikushukuru kwa kusimama na mimi. Najua bila wewe nisingeweza kufanikiwa.” Nanaa alishukuru huku akisikika akitetemeka midomo, akisindikizwa na machozi. Geb akajua mambo yameshaharibika. Wengine walijua ni sababu ya kilio cha kuguswa na Mazigo kukamata watesi wake, lakini sio Geb. Alimfahamu Nanaa, hata kwa kusikia sauti yake tu bila kuiona sura yake. Alijua kilichopo nyuma ya kila kilio cha Nanaa. Kama ni majonzi au furaha. Ugonjwa au uzima. Geb alimjua Nanaa.

Akamfuta Liv kwa haraka, akamtoa pale kwenye kiti. “Asante Nanaa mdogo wangu. Basi tutawasiliana. Sasa hivi huna haja ya kulia. Shukuru ukijua haki itatendeka. Malii tutampata tu.” Wakapeana mikono. Nanaa akasimama kumsindikiza. Mazigo akatoka Nanaa akamsindikiza mpaka nje. Alipoondoka ndipo Nanaa akarudi ndani, na Geb naye ndio alikuwa akimfuata nyuma. Aliingia akakutana na Geb mlangoni. Alikuwa akisugua tumbo.

“Vipi?” Geb akamuuliza wakiwa wamesimama karibu na hapo sebuleni. “Sasa hivi tunaenda hospitalini Nanaa. Pressure ipo juu sana. Na unaonekana..” Akaona Nanaa anajiangalia, na yeye akaona maji yanachuruzika. Akamwangalia Geb. “Chupa imepasuka!” Bila kuongeza neno, Geb akamnyanyua pale, akambeba. Man akanyanyuka kwa haraka akaenda kufungua mlango wazi zaidi ili Geb na Nanaa waweze kupita. “Naomba funguo za gari.” Grace akamuonyesha Man funguo zilipo, Man akatoka kwa haraka kuwafuata.

“Sasa wewe baki na watoto, ngoja mimi niwafuate na begi la Nanaa. James mwambie Geb anisubiri, nakuja na begi lake.” James alikuwa ndio anakimbilia nje. Baada ya nusu saa, Grace akajikuta amebaki pale na watoto wote wakimwangalia yeye. Akaanza kucheka, maana Magesa alikuwa akiwasindikiza kila mmoja wao kwa macho. Alimuona vile baba yake akikimbia na mama yake, akafuata Man, akaja James na wa mwisho bibi mtu. Magesa akarudisha macho kwa shangazi yake. “Mimi siondoki  Magesa, baba yangu. Njoo.” Magesa akaanza kucheka huku akitambaa akimfuata shangazi yake. Grace aliyekuwa amempakata Fili, akamnyanyua kwa mkono mmoja. “Vipi?” Grace akambusu. Akaamua kuwawashia tv ili waangalie kitu wanachokipenda. Akawaweka wote kwenye kochi wakatulia kimya. Yeye akaendelea na usafi wa pale Nanaa alipomwaga maji ya uchungu.

Mwili Ni Udongo.

Walikuja kugundua wote wamepanda kwenye gari ya Geb. Hata James, aliacha gari yake nyumbani kwa Geb kwa kupaniki. Nanaa hakutakiwa apatwe na uchungu ili asizae kwa kawaida. Alitakiwa kuzaa kwa upasuji. Alibakisha siku chache tu, mtoto akaomae vizuri ili akatolewe. Lakini sababu ya hekaheka za Nanaa mwenyewe, na afya yake, chupa ilipasuka majuma machache kabla. Wakiwa njiani Geb   akampigia     simu Lyamu daktari anayemshugulikia.

Akamwambia kwa wakati ule yupo hospitali ya taifa ya Muhimbili waende hapo yeye ataanza kutafuta kitanda, sehemu ya kulipia. Alimuuliza baadhi ya maswali, yule daktari akamwambia lazima na daktari wa moyo awepo. Akamwambia wafike moja kwa moja mapokezi, watawakuta hapo wakiwasuburia.

Geb akaendelea kukanyaga mafuta kuelekea huko. “Vipi?” Walimsikia Geb akimuuliza.  “Sasa hivi naona maumivu ndio yanachanganya.”  “Kwa nini unafanya hivyo Nanaa? Inamaana uliazwa na uchungu muda mrefu!?” Kimya. “Kwa nini uliamua kunificha? Kwa nini unafanya hivyo wakati unajua madhara yake!?” Geb alisikika akilalamika kwa kuumia.  “Nilijua nikikwambia utakataa kile kikao, Geb. Nilianza kusikia maumivu tokea mchana, nikapuuza nikijua ni kawaida tu. Kwanza siku tuliambiwa bado kidogo. Kwa hiyo nikapuuzia, nikasema nitakwambia baada ya kukamilisha mambo ya kina Gozi. Naomba usikasirike Geb. Shukuru Mungu pamoja na mimi.” “Sasa hiyo itanisaidia nini mimi kama ukipata madhara? Umekaa na uchugu zaidi ya masaa 6, Nanaa! Kwa nini unafanya hivyo? Kwa nini hunifikirii mimi na watoto?” Geb aliendelea kulalamika.

Akamuona Nanaa anahangaika pale kwenye kiti. Kanyamaza. “Vipi?” “Nasikia maumivu makali Geb. Nahisi mtoto anatoka.” “Mungu wangu!” Alisika mama G. “Pole Nanaa. Naomba usipaniki wala usisukume. Tumekaribia kufika. Naomba jikaze.” Geb alizidi kukanyaga mafuta, akampigia tena simu Lyamu kwa kutumia spika ya gari. “Mtoto anatoka!” Geb aliongea mara baada ya yule daktari kupokea. “Mmefikia wapi?” “Kwenye mataa ya Fire, ndio nakata kona.” “Naomba atulie. Laza kiti chake kabisa. Mwambie aheme tu. Asisukume. Sisi tupo hapa tunawasubiria.” “Umesikia Nanaa?” Geb akamuuliza. “Nanaa?” Daktari akaita. “Nipo nakusikiliza. Nimeshalaza kiti.” “Tulia kabisa na usisukume hata iweje. Nataka nikusikie unavuta hewa safi na kushusha taratibu. Naomba tuanze.” Nanaa akawa anamfuatisha yule daktari jinsi ya kuhema mpaka wakafika.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Wakafika mapokezi wakakuta madaktari watatu na wauguzi wakimsubiria Nanaa, alipokelewa na kuwekwa kwenye kitanda. Yule daktari alianza kuwaambia wale wauguzi wakimbilie chumba cha upasuji wamwandae Nanaa, wao wapo nyuma yao. “Naomba mumsaidie tafadhali.” “Wote tupo hapa kwa ajili yake. Tutafanya kila tuwezalo ili wote watoke salama. Lakini kama nilivyokwambia Geb, hukutakiwa kumsubirisha mpaka afikie hatua hii. Ulitakiwa umelete pale tu ulipoona pressure imepanda na ameanzwa na uchungu. Tulizungumza hilo na leo nilipozungumza na nyinyi kwenye simu mkaniambia hamna uchungu ni pressure tu. Nikataka kuwaona, ukijua ubishi wa Nanaa, na wewe ukakubali kusubiria mpaka hali imekuwa mbaya!” Geb kimya.

Nanaa alimbembeleza kwa machozi asimpeleke hospitalini mpaka ahakikishe kina Gozi wamekamatwa. Geb kwa kumuhurumia na hukumu ambayo tayari ilikuwa ikimsumbua moyoni, akamkumbalia Nanaa, nakusahau masharti yote ya daktari. Nanaa alitumia hukumu ya Geb vizuri sana. Akajilalamisha mpaka Geb akamkubalia kusubiri swala la hospitalini. Akampa dawa ya usingizi, akalala.

          “Kwa vile alivyo, sitaki kukukatisha tamaa, lakini hali sio nzuri Geb. Kwa kumwangalia tu, pressure ipo juu sana. Hakuna jinsi akasukuma mtoto na yeye akatoka salama. Iwe muujiza kweli” “Nawaombea mfanikiwe.” Walikuwa wakitembea kwa haraka huku wakielekea chumba cha upasuaji. “Sisi tupo nyuma yenu kwa maombi, baba. Tunawaombea.” Mama G akaongeza. “Ni kweli tunahitaji maombi.” Wale madaktari wakaingia chumba cha upasuji, wakawaacha Mama G, Geb, James na Man pale nje wakisubiri. Geb hakukaa. Akatafuta sehemu akapiga magoti. Walimsikia akiomba. Mama yake akamwangalia. Akavuta benchi akaenda kukaa pembeni yake na yeye akaanza kuomba. Geb alikuwa akiomba bila kunyamaza.

~~~~~~~~~~~~~~~~~

Nanaa amefanikisha kukamatwa kwa wahalifu wake na wakina Magesa. Ameua ndege wawili kwa jiwe moja. Bado Malii, lakini kutokana na mtetezi wake, amemuahidi Nanaa kuwa Malii atakamatwa tu.

Sasa hivi yupo hospitalini kutetea uhai wake. Kufa na kupona. Ahadi ya kupendwa mpaka ashangae ipo, ni yeye kutoka tu pale hospitalini. Mtoto awe wa Malii au Geb, amepata dhamana ya kumlea bila shida wala kuingiliwa ila mapenzi mazito.

 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment