Grace
alifungua macho pale kwenye kochi. Ilikuwa asubuhi. Alilala baada ya kuchomwa
sindano iliyomsaidia kupata usingizi mzito. Chumba kilikuwa kimya. Ni mashine
za Fili tu ndizo zilizokuwa zikisikika akiwa usingizini. Akamwangalia Man.
Alikuwa amelala kwenye kiti. Akaumia sana moyoni. “Man hastahili haya yote. Alitakiwa kuwa sehemu nzuri amepumzika sasa
hivi na mkewe, kama sio kunioa mimi, mama mwenye watoto na historia mbaya ya
ndoa.” Grace akawaza. “Wanangu!”
Machozi ya uchungu yakaanza kumtoka kila alipokumbuka wanae. Kumbukumbu ya
mwisho ya wale watoto wake, ni vile walivyokuwa wakimlilia aende nao. Yalipita
mawazo kadhaa kichwani mwake. Akijilaumu kwa kila hatua aliyowahi kuchukua
kwenye maisha yake.
Akatoka
pale kwenye kochi alipokuwa amelala, akaelekea bafuni kuoga. Man alipomsikia
bafuni akamfuata. “Vipi? Unajisikiaje?” Grace akafunga maji kwenye sinki la
kupigia mswaki. “Najisikia vizuri,
lakini nahisi nahitaji muda Man.”
“Unamaanisha nini?” Man akauliza. Grace akajifuta machozi. “Kwa sasa siwezi kuwa mke mzuri kwako. Nimechanganyikiwa.
Nina maumivu na majuto ambayo sijui nitafanya nini na sijui nitapona lini.
Naomba unipe muda.” “Unamaanisha nini?” Bado Man
alirudia swali lake.
“Nashauri wewe uondoke Man. Rudi kwenye biashara zako. Au niseme rudi
kwenye maisha yako kama kawaida. Nitakapokuwa sawa, nitakutafuta.” Man alijirudisha nyuma akaegemea kwenye ukuta
akabaki akimtizama Grace. “Sio
kwa nia mbaya Man. Ni kwa ajili yako. Hii ndoa inakuwa kama inamkosi! Tumeoana
tu nimeingia na misiba! Ndio maana nilikuwa nikisita tokea mwanzoni nikikwambia
mimi sio msichana Man. Ona nilipokufikisha!”
“Naomba usiongeze neno jingine Grace. Najua umeumia. Lakini naomba usiongeze
neno jingine. Tafadhali sana.” Grace akakaa chini kabisa sakafuni nakuzidi
kulia.
Man
alimchukua kutoka pale sakafuni, akamtoa nguo na kumwingiza bafuni. Grace
akaoga akiwa analia kwa uchungu sana, mpaka akamaliza. Alitoka na kukuta taulo
likimsubiri mkononi kwa Man. Akajikausha na kuvaa, akabaki kama ameduaa.
“Twende ukapumzike.” Wakatoka pale bafuni, wakarudi chumbani alipokuwa amelazwa
Fili. Grace akarudi kujilaza kwenye kochi, lakini akageukia ukutani akawa
amempa mgongo Man. Akamfunika, nakubaki akimsugua mgongoni mpaka Grace akalala
tena.
Baada
ya muda nesi akaingia kusamfisha Fili na kumpa dawa. Grace akaamka. Akauliza
kama angetaka msaada, lakini yule nesi alimwambia anamfanyia kitu kidogo tu.
Man alivuta kiti pembeni ya Fili, kama aliyelevya na madawa, Fili akarudi
kulala. Man akabaki akiwaza.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ilipofika
kwenye saa 3 asubuhi mama G akaingia akiwa na Liv. Man akasalimia. Grace
alibaki amelala vile vile amegeukia ukutani. “Pole baba na matatizo.” “Asante
mama. Vipi na wewe umeamkaje?” Man akamuuliza. “Naona nimeamka vizuri.”
“Namuomba Liv nimsalimie.” Liv aliposikia jina lake likitajwa akajificha nyuma
ya bibi yake. “Nenda bwana kasalimie. Ni nini Liv?” Bibi yake alimchungulia
pale alipojificha. “Nenda kamsalimie anko.” Liv akacheka na kidole chake mdomoni.
Bibi yake akajua ndio amekataa.
“Umependeza
Liv!” Man akamsifia. Liv akamchungulia. “Nywele za Liv nzuri! Sijui nani
amemtengeneza?” “Bibi.” Liv akajibu huku anachungulia. “Jamani bibi ni mjuzi!
Umemuona Fili?” Man akamuuliza. “Nampenda Fili.” Liv akaongeza. “Njoo basi
umsalimie.” Akaingia Nanaa na Geb akiwa
amembeba Magesa. Wakasalimiana. Geb akaenda kukaa kwenye kochi alilokuwa
amejilaza Grace. Akamuweka Magesa juu yake. Magesa akaanza kuruka ruka pale
alipokaa juu ya anti yake. Grace akamgeukia. Alijawa cheko, Grace akatabasamu.
“Kila
wakati wewe ni kucheka tu!” Grace akamshika vizuri. “Muone!” Magesa alikuwa
anaruka ruka pale mwilini kwa shangazi yake alipokuwa amekaa, huku akiongea
anayoelewa yeye na cheko juu. Grace akabaki akimwangalia huku akicheka. Huwezi
kumshika huyo mtoto usiburudike moyoni.
“Wewe amani yako huwa inakutoshea mwenyewe! Muone!” Grace alimwambia Magesa
nakumfanya azidi kucheka.
Oliva
yeye akajivuta taratibu mpaka kwa mama yake. “Namtaka Fili.” Akaongea kwa
upole. Lakini kama Fili alisikia kutoka usingizini akafungua macho. “Liv!”
Alifurahi sana. “Njoo uone. Naumwa mwenzio.” Geb akaenda kumnyanyua Liv mpaka
pale karibu ya Fili. “Nimeumia mkono. Halafu wamenitoboa hapa.” Liv akainama.
Baba yake akajua anataka kumbusu Fili. Akamsogeza akambusu kichwani. “Na hapa
mkononi Liv.” Liv akajisogeza kwa nguvu kama kufikia ule mkono alioonyeshwa na
Fili. Geb akamsogeza. Liv akabusu mkono. “Pole Fili.” Liv aliongea kwa upendo.
Wote wakabaki kimya wakiwasikiliza.
“Nampenda
Fili.” “Na mimi nakupenda Liv. Lakini unajua dad wangu alinipiga tena?” Fili
akamuuliza Liv. Kila mtu kimya. “Nampenda Fili.” Liv aliongea tena kwa upole.
Akainama tena akambusu. “Mbusu dad.” Akamgeukia baba yake, akitaka na yeye
ambusu Fili. Geb akambusu na yeye Fili. “Aahahaa!”
Liv akamkatalia baba yake, kama aliyekosea alichotaka afanye kwa Fili. Geb
akawa hajaelewa kitu Liv anataka tena. “Hapa dad.” Liv akamuonyeshea baba yake
kifuani. “Mwenzio anataka umuweke Fili kifuani kama unavyomfanyia yeye.” Nanaa
akaingilia. “Aaaahaa!” Geb akaelewa. “Sasa kwa nini wewe usimfanyie? Fili
atafurahi sana kama wewe ukimfanyia.” Geb alimwambia Liv. Liv akacheka na
kidole chake kimoja akakiingiza mdomoni. Akambusu dad wake. Akataka amshushe,
amuweke hapo kitandani.
“Sasa
hapo taratibu we Geb na mwanao. Msimtoneshe Fili.” “Liv ni mstaarabu bwana! Eti
mama? Utamuumiza Fili?” Geb akamuuliza. Liv akatingisha kichwa kukataa. “Haya.
Taratibu usichomoe waya hata mmoja.” Geb akaendelea kumtahadharisha Liv. Kweli
Liv alikuwa mstaarabu. Walimtoa viatu. Wakamuweka pale kitandani. Akatembea
taratibu huku baba yake amemshika mkono asianguke pale kitandani. Alitembea kwa
tahadhari mpaka pale alipokuwa amekaa Fili. Baba yake akamwachia huku
akimwangalia. Akamkumbatia Fili, zaidi kichwa chake sio kifua ambako alitobolewa.
Wakamsikia
Liv akifanya kama baba yake. “Mmmmmmh!”
Kisha akaanza kumbusu kila mahali usoni. Kila mtu alicheka. Alifanya kama
anavyofanyiwa yeye na baba yeke. Geb alimtizama mwanae asiamini. Alifanya bila
kukosea. Kisha akakaa pembeni ya Fili. “Nampenda Fili.” Akamshika mkono. “Na
mimi nakupenda Liv.” Walimsikia Grace akilia.
Tayari
akili ya Magesa ikaruka. Akaanza kuruka ruka macho yapo kitandani alipokuwa
amekaa Fili na Liv. Mikono hewani ili atolewe pale kwa shangazi yake, apelekwe
na yeye pale kitandani. “Huyo ataharibu bwana! Una nini Magesa wewe? Wewe mbusu
tu anti hapo.” Magesa alizidi kurukaruka akiashiria achukuliwe na baba yake.
Mikono yote juu anaita kwa vidole. Geb akacheka na kwenda kumchukua. “Naomba
usije kumuweka pale kitandani Geb. Tafadhali sana. Huyo atang’oa kila kitu
pale. Mashine zote zitatupwa na atawavuruga wenzake.” “Nitamshika.” “Na umshike
kweli. Unamjua alivyo na manguvu. Akimshika tu Fili, atamvuta mpaka amtoe waya
zote mwilini. Naomba yeye ambusu ukiwa umembeba. Hakuna kukumbatia.” Nanaa
alizidi kutoa maelekezo juu ya mwanae Mgesa. Kidogo watu wakacheka.
“Umemsikia
mama yako? Wewe huruhusiwi kukaa kitandani. Unabusu tu na kuondoka. Sawa?”
Magesa akaanza kucheka huku akimwangalia Fili. Geb akamwinamisha, akambusu. Kisha
akafungua mikono ili amkumbatie na yeye kama Liv. “Hapana Geb. Huyo mpeleke
akamkumbatie anko Man.” Mpaka Grace akacheka. “Njoo Magesa.” Hakuwa na makuu.
Akakubali kwa haraka. Akanyoosha mikono kule kwa Man. Man akampokea. Cheko na
mate juu. “Uzuri mwenyewe hana shida.” Mama G akamsifia. Kweli akamkumbatia
Man, na kumbusu. Akamuachia mate shavuni. “Pole mwaya Man. Chukua kitambaa hiki
ujifute. Yuko kwenye kuota meno. Basi kila mtu anamlowesha mate yake.” Man
akacheka. “Hamna shida. Mwache tu tupakane hayo mate. Ndio nafurahi.” Man
alijibu huku akimwangalia Magesa akimchekea.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mara
James akaingia. Nanaa akasimama. “Shikamoo kaka!” “Marahaba. Vipi wewe?”
“Hatujambo. Mbona huna raha?” Nanaa akamuuliza kaka yake. James akafikiria
kidogo. Akanyamaza kisha akauliza. “Vipi Fili?” Akasogelea kitandani. “Naona
Liv anauguza.” Liv akacheka, kidole mdomoni. “Shikamoo anko.” Fili akasalimia.
“Unajisikiaje?” James akamuuliza. “Nimefurahi Liv amekuja kunisalimia.”
“Nakwambia aliyeingia hapa ni Liv peke yake!” Bibi yake akanong’ona. “Wewe
umemkumbatia na kumbusu?” Nanaa akamuuliza mama G. Akaguna. “Maana mwenzio
tangia ameingia hapa anaimba ‘nampenda Fili’. Mabusu mpaka ya kichwani! Huwezi kujilinganisha
naye.” Wote wakacheka.
“Vipi
Grace?” “Nipo James.” “Pole mama. Pole sana.” “Asante.” Grace akajibu kwa
upole. Geb akaenda kukaa pembeni yake, akabaki akimtizama. “Umekula?” “Sisikii njaa.” Grace akamjibu kaka yake na machozi. “Lazima ule G.
Kula kama dawa.” Wakamuona anamtengeneza nywele. Anazitoa usoni na kuziweka
nyuma ya masikio na nyingine anazirudisha nyuma taratibu. Akamfuta dada yake
machozi. Man alirushia macho, akamwinamia Magesa akaendelea kucheza naye. Nanaa
na mama G, wakaangaliana, wakanyamaza. “Nikumiminie uji kidogo?” “Uji kama
mzazi!? Au uji wa Nanaa?” “Ukikataa kuunywa mimi nitaunywa.” Nanaa alijibu wote
wakacheka. “Kwanza nashauri nyinyi wawili mkapate kifungua kinywa, mlale
kidogo, ndio mrudi. Mimi na mama ndio tumefika hapa.” Nanaa akaongeza.
“Kweli
mtabaki?” Grace akauliza. “Tumekuja tukiwa tumejiandaa na chakula mpaka cha
mchana. Nyinyi nendeni mkapumzike. Mrudi hata jioni. Mlezi yule pale kitandani.
Huyo baba mzazi tumekuja na walker yake. Atatembea hapa mpaka achoke. Nyinyi
nendeni tu.” Mama G akaweka msisitizo. “Kapumzikeni Man. Mtarudi baadaye. Mama
na Nanaa watakuwepo hapa, na mimi nitarudi baadaye. Naenda kuchungulia tu hapo
kazini, nitarudi. Nashauri mkapumzike.” Geb akaweka msisitizo. Man akamtizama
Grace. “Twende.” Grace akaongea kwa upole.
Akasimama
na kwenda kumbusu Fili. “Unataka nikuletee nini?” Fili akafikiria, akamwambia
mama yake hataki kitu. “Basi nitakuona baadaye. Nakupenda sana Fili.” “Mimi
najua mama. Nilimwambia hata Sara. Ila yeye ndio alikuwa akibisha.” “Nimefurahi
kama unajua hilo Fili. Nimefurahi sana.” Fili akacheka. Grace akambusu tena
mwanae na kumuaga kwa ahadi ya kurudi baadaye ili awe naye usiku huo pia. Fili
akaridhika. Ndio Grace akapata Amani ya kuondoka.
Wakati wanataka kutoka ndio wapo
mlangoni, akaingia mama Ole, Malisa, wadogo zake wawili Man na mke wa kaka yao.
Ikabidi Grace arudi ndani. Man akawaambia Grace anatakiwa kwenda kupumzika.
Wakasalimiana na kumpa pole Fili, wakaelewa hawatakiwi kukaa hapo muda mrefu.
Wakatoka na Grace na Man huku wakizungumza.
James Na Yaliyojiri!
James
alikuwa ameinama. “Umetokea kazini?” Nanaa akamstua kaka yake. “Daah!
Sijakwenda. Yaani hapa umenikumbusha. Ngoja niende. Nahisi nimekuwa kama
nimepatwa na mshituko fulani hivi. Nashindwa kufikiria. Sijui chakufanya! Akili
inazidi kuchanganyikiwa.” Geb akamuweka Magesa kwenye walker yake tayari kwa
kuondoka. “Mama!” James akaita akiwa kama anawaza. “Vipi James mwanangu?”
Walijua lazima James awepo kwenye mshituko. Ndiye aliyewazoa watoto wa Danny na
Grace na kuwaweka kwenye mfuko.
Akarudi
kukaa. “Namfikiria Danny, bila kupata majibu. Nimemuuliza maswali ambayo hata
sikumpa muda wa kuyajibu, lakini ni kama nimepata majibu kwa sehemu.” “Kwani
umeonana naye!?” Nanaa akauliza swali la kwanza. “Ndio nimetokea huko.”
“Unaposema ulimuuliza maswali na umepata majibu, unamaanisha nini?” Mama G
akauliza taratibu. “Upo mchezo mchafu sana umechezwa mama. Najua Danny
amewaudhi sana. Lakini kuna jambo kubwa sana linaendelea. Na tusipokuwa makini,
hakuna kati yetu atakaye simama au kusalia.” James akaanza kusimulia kuanzia
alivyoingia yeye, na mazungumzo yake na Danny. “Amebaki kama amepigwa ganzi.”
James akamalizia kipengele cha kwanza na kwenda cha pili.
“Hivi
tunavyozungumza, Sara amelala kitandani kwa Zinda.” James akaendelea “Sikuamini
aliposema amelala na Sara. Tena kwa kumwambia mwenzie hajaona chochote kwa huyo
Sara!” “Kaka wewe!” “Mbele yetu. Tena akamwambia amemfukuza kwake, hataki
mikosi. Tena wanasaidiana na Gozi kumcheka mwenzao. Sijui mwisho wa Danny
utakuaje. Hakika namfikiria simpatii jibu. Alichoweza kufanya asubuhi hii niku freez
akaunti zake zote, kwa kuwa siku ya ajali, Sara alitoroka na wallet yake. Tokea
siku ya ajali mpaka jana usiku, Danny ameambiwa na watu wa benki, Sara alikuwa
na kazi ya kuzunguka kwenye ATMs kutoa pesa.” “Sasa ataamini niliyomwambia juu
ya Sara. Nilimwambia mimi Danny kuwa Sara sio muhuni, ni Malaya asiyeona shida
kuvulia wanaume hata watatu nguo kwa siku moja. Akabisha. Atamfilisi.” Nanaa
akaongeza.
“Ila
naona amemuwahi. Bado salio lake ni zuri tu. Na mshahara bado utaendelea
kuingia. Hayupo pabaya kifedha.” James akaongeza. Mama G alikuwa amenyamaza
kimya. Geb hakuweka hata neno.
“Ameulizia
hali ya Fili, nikamwambia ukweli wote. Jinsi mwanae anavyosimulia kisa chote.
Na nikamwambia aombe Mungu Grace asimshitaki. Hatakaa akamuona tena huyu
mtoto.” “Akasemaje?” “Sio alichosema yeye, ni alichosema Zinda na mama yake
ndio kinachonichanganya mimi hata Danny mwenyewe.” Geb na mama yake wakakaa
sawa. James akajua wanataka kusikia.
“Niliposema
mchezo mchafu msifikiri nazungumzia mambo ya Sara! Hata kidogo. Mchezo mchafu
waliocheza Zinda na mama yake.” James akasimulia tena mazungumzo ya mama Zinda,
Zinda na Danny. Kila mtu akaingiwa hofu. “Yule mama bado anamlalamikia Nanaa!”
“Kaka wewe!? Mimi!?” “Unajulikana huko Tabora. Na kosa ni la Danny. Kuwa
alimpokonya Zinda mchumba kwa kutulaghai mimi na wewe kisha akakuozesha kwa
Geb. Yule mama bado ana kinyongo.” “Kwa hiyo walimpokea Danny ili
kumuangamiza!!” “Sawa sawa Nanaa. Wewe umewaza sawa.” “Shetani ametumia vizuri
sana hasira za Danny.” Mama G akawaza kwa sauti.
“Hivi
unajua mama yake Zinda alirudia kumwambia Danny yale maneno ya kuwa
alilaaniwa!” “Haiwezekani James!” “Kweli mama. Na amemwambia mizimu ya kwao
imemkataa. Hawamtaki arudi tena kwao. Amebakizwa ili kulipa ubaya aliomfanyia
Zinda. Bahati zake zote alizozichukua kwa Zinda ndio zinarudi sasa kwa Zinda na
kumuacha yeye mtupu kama alivyotakiwa awe. Lakini mama na Geb, naombeni
mnisikilize kwa makini sana, tusaidiane hili jambo. Maana sisi wote hapa majina
yetu na maisha yetu yapo huko Tabora. Tunajulikana.” Kila mtu akatulia.
“Kuna
jambo yule mama alitaka kumalizia, Zinda akamkata kwa haraka kama kuficha
asiendelee kuzungumza. Lakini kwa mazungumzo yao ya awali, imenifanya nifikirie
sana. Binafsi nimeingiwa hofu. Hawa kina Zinda walipompokea Danny. Au tuseme
Danny aliporudi kwao akiwa na hasira juu yenu, cha kwanza walichohakikisha ni
kumfanya kuwa mateka wao. Mimi nilivyofikiria. Wakamuaminisha kuwa mmemloga.
Danny alisimulia mbele ya Zinda kuwa hata mama yake Zinda alimwambia kuwa
mganga wao amemthibitishia nyinyi mmemloga. Sasa sikiliza walichoanza kumfanyia
Danny.” James akaendelea.
“Wakamwambia
inabidi kutakaswa na kukombolewa na nyinyi. Ndio safari za Tabora zikaanza.
Kumbe anaenda kuaguliwa kwa mganga wao. Danny anasema alikwenda mara tatu yeye
na watoto wakisindikizwa na Zinda. Mara ya tatu ndipo akaambiwa akatafute
kondoo, mbuzi na jogoo mwekundu. Vyote hivyo vilikuwa vyakutakaswa yeye na
watoto. Zinda ndiye aliyemsaidia kuvipata kivyo vitu. Yeye na watoto wakaenda
kufanyiwa walichofanyiwa. Sasa safari hii ya nne, ndio walikuwa waende
wakapatanishwe na ukoo wa kina Zinda. Si ndio Danny amepata ajali.
Kilichomshangaza Danny ni kuwa, safari zote alikuwa akienda na Zinda. Ila
safari hii walimwambia Zinda hatakwenda ni yeye na familia yake tu. Ndio mama
Zinda akataka kuropoka kitu, Zinda akamkata. Ila kabla ya kumkata ndio akasema
yale maneno kuwa mizimu imemkataa Danny kwa kuwa anamkosi mkali. Imemzuia hata
asifike kwao.” Wasikilizaji wote walikuwa wameduaa. James akawaangalia mmoja
baada ya mwingine.
“Danny
akamuuliza Zinda kama ni wao wamehusika na ajali yake. Zinda akambadilikia
vibaya sana. Amemgeuzia maneno yote. Yaani Zinda amemgeuka mwenzie, hutakaa
ukaamini kama ni wao.” James akatulia kidogo. “Sasa nisikilizeni. Hawa watu
niwashirikina sana. Kumbukeni mambo ya Mira. Na Mira naye ametoka sehemu moja
na Zinda. Kwa kusikiliza tu, bila hata kutaka ufunuo, hawa watu walimtega
Danny. Waliwapeleka watoto wote na Danny kwa mganga wao, Danny akijua anatakaswa,
kumbe wanamuangamiza. Yule mama anaonekana anahasira sana na Danny.”
“Hakika
anasikika anahasira ambazo hawezi kuzificha. Ametaja mambo ambayo
yametushangaza mimi na Danny. Anasema mpaka kazi ya Danny ilitakiwa iwe ya
Zinda! Sasa kivipi, hakuna anayejua.” Kumbukumbu zikamjia Geb kwa haraka.
“James wewe umesahau. Unakumbuka siku moja tulikuwa wote tumekaa, ukaja ukasema
kuna nafasi ya kazi ofisini kwenu. Ukasema wanatafuta mtu. Ulipotaja sifa zake,
Zinda akasema yeye anaweza kuomba hiyo nafasi. Akakuomba umuunganishie.
Ukakubali. Lakini Danny akasema kwa kuwa yeye hana kazi, na Zinda anayo kazi
tayari, kwa nini usimuunganishie yeye. Jamaa wote wakakubaliana na wazo la
Danny. Tena nakumbuka bila hata kuwekana sawa na Zinda, wewe ukahamisha
mazungumzo yote ya ile kazi kwa Danny. Pale pale mkapanga mambo yenu juu ya ile
kazi. Ukampa njia ya kuipata ile kazi. Yaani sasa hivi ndio nakumbuka vizuri
zaidi. Zinda aliondoka pale wakati wewe na Danny mkiendelea kuzungumza.” Geb
alimfanya James akumbuke kila kitu. “Mungu
wangu!” James akahamaki.
“Inamaana
Zinda amekiweka hicho kitu moyoni mpaka leo!!?” James akauliza akiwa kwenye
mshangao mkubwa sana. “Si ndio maana mama yake amekisema tena leo? Inamaana
wanayo orodha ya makosa yetu wote sisi.
Sasa hutuwezi kujua waliwafanyia nini! Umbali gani walikwenda au
watakwenda kulipiza kisasi! Na kwa nani! Na kama bado wataendelea kufanya! Fili
yupo hapa hospitalini, lakini tukumbuke na yeye alifanyiwa kile walichofanyiwa
wadogo zake. Sisi tuanze kumwita Mungu wetu sasa hivi. Geb, tuombe kabla
hujaondoka.” Mama G akachangamkia eneo lake la kujidai.
“Tuweke
kikomo kwenye ajali zote na tumkomboe Fili na mama yake. Tokea
jana Grace ameanza kutokwa damu isiyo yakawaida! Tuvunje madhabahu zote
zilizoshikilia majina yetu sisi wote hapa na kizazi chetu. Hata wewe James.
Lazima kutubu na ujiweke kwa Bwana. Hakuna aliye salama kati yetu. Hawa
watu wanaonekana wamebeba visasi na wamekusudia kutuangamiza. Lakini kama Mungu
wetu aishivyo, watapigana na Mungu. Tumwiteni Mungu wetu, akaingilie
kati. Hata wakituita tena huko kwenye madhabahu zao, wakakutane na simba wa
kabila la Yuda. Yesu mwana wa Mungu. Hatutamlipa mtu kisasi. Acha Bwana
ashugulike nao.” Hapo wakawa wamemchokoza mama G.
Akasimama
akiwa amejawa nguvu ya ajabu. Maombi yakaanza pale ndani. Waliomba kwa nguvu ya
ajabu huku watoto wao wakiwatizama. Magesa alitulia kimya akiangalia bila hata
kuongea. Chumba kilijaa utisho wa ajabu. Walivunja na kung’oa bila kuchoka.
Mara Fili akaanza kutapika, mpaka nesi ikabidi aingie.
Alitapika
vitu vyeusi vitupu huku amejinyoosha kitandani kama nyoka. Alipoanza kutambaa
kama nyoka, wakajua ni pepo. Mama G akamsogelea maana nesi alikimbia kwa hofu.
Fili ni kama alikuwa akijitonesha kile kidonda. Akageuza jicho kama anayetaka
kukata roho. James alimtoa kwa haraka Liv pale kitandani. Mama G na Geb
wakakemea bila yakuogopa.
Nanaa
akashangaa Geb ameweka mkono juu ya Fili, akaamuru kwa kifupi tu, “Nyamaza na
mumtoke Fili kwa haraka.” Hapo hapo Fili akajinyonga na kutulia. Wote wakaduaa
na kumshangaa Geb. Geb alikuwa amejawa nguvu za Mungu. Tokea wanaanza maombi
alikuwa akiomba kwa roho. Pakatulia
kidogo. Geb akamnyanyua Fili akaenda naye bafuni. Alikuwa amejawa matapishi
kila mahali. Na alikuwa amejitoa kila kitu mwilini mwake. Mashine zote zilikuwa
zimetolewa. “Unajisikiaje?” Walimsikia Geb akimuuliza huko bafuni. Nanaa aliita manesi kwa kubonyeza kengele.
Wakaja kusafisha na kuleta nguo safi za Fili. Wakamrudisha Fili kitandani.
Ndipo
maombi ya shukurani na kuomba ulinzi juu yao yakaanza. Mama G alimuomba Geb ahitimishe
kwa maombi. Geb alitaka washikane wote mikono. Walitengeneza duara. Wakashikana
mpaka na watoto na Fili pale kitandani. Geb akaanza kuomba na kumwambia Mungu
anamshika Grace na Man mikono katika ulimwengu wa roho. Akakemea kutokwa kwa
damu kwa Grace na kuruhusu mzunguko sahihi ulioamriwa na Mungu. Wakafunga roho
za mauti. Ndipo wakamaliza hayo maombi. Kila mtu alisema amepata amani. Geb na
James walitoka kwenda kazini na kuwaacha hapo mama G na Nanaa, wakiwa na
watoto.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
“Umeona
jinsi Geb alivyoamuru yale mapepo!?” Nanaa akamuuliza mama G. “Mimi mwenyewe
nilishangaa.” “Ujue nilikuwa nataka kukimbia kama yule nesi!” Wakaanza kucheka.
“Ni vile kaka James alisema na Fili alifanyiwa kama wadogo zake, nikajua na
yeye anakufa. Sasa hofu ikaniingia, nikasema mimi sitaki kushuhudia.” “Mimi
nilijua ni mapepo tu, ndio maana nikamsogelea.” “Nilikuona mwenyewe mama. Kama
sio wewe!” Mama G akaanza kucheka. “Kumbe mwenyewe una maeneo yako yakujidai?”
“Huwa shetani ananikera sana, Nanaa. Mpuuzi wa mwisho. Siwezagi kumvumilia
mimi.” “Mama huyo! Kwengine huwa unaganda.” Mama G alicheka sana.
“Acha
uchokozi Nanaa.” “Lakini umenitia ujasiri. Nifundishe mama. Mimi sijui hata
kukemea pepo.” Wakaendelea kuzungumza. Wakakumbushana Vile Geb alivyotumika
kwenye uponyaji wa Nanaa alipoharibiwa miguu. “Lada Mungu ndio amempa huduma ya
uponyaji.” “Labda. Lakini ujue Geb anaomba mama, mpaka mimi nashangaa. Kila
siku saa 11, utamkuta amepiga magoti kule kwenye ile sebule ya pale chumbani
kwetu, anaomba. Halafu taratibu. Na anaomba muda mrefu mpaka nashangaa.
Namuuliza unaomba nini? Anacheka, anasema mara nyingi anakuwa anaomba kwa
roho.” Nanaa na mama G walishinda hapo hospitalini wakiongea hili na lile.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Ilipofika
jioni Man na Grace waliingia hapo chumbani. Grace alionekana akiwa ametulia.
Alimwambia mama yake alilala vizuri. Na damu ilikata. Wakaangaliana na Nanaa.
“Mbona mnaangaliana?” Grace akauliza. “Naomba tukazungumze kidogo hapo nje.”
Grace na Man wakamfuata mama G. Wakatafuta
mahali wakakaa. “Kuna nini?” Grace akauliza. “Unakumbuka siku ya kwanza Zinda
kujirudi kwa Danny akitaka Danny amsamehe?” Grace akatulia.
“Tulikuwa
nyumbani kwa Geb na Nanaa.” “Siku ile James alipowaleta ndugu zake?” “Ewaaa!
Sasa si unakumbuka yale majibu ya Danny kuwa yeye mwenyewe ndio atamtafuta
Zinda. Zinda asiende kwake.” “Nakumbuka.” Grace akaitikia. “Sasa inavyoonekana,
shetani ametumia hasira ya Danny vizuri sana. Kwanza walianza kwa kumwaminisha
tunamloga. Akaingiwa hofu na sisi. Najua kusudi zima, ni kumtenga na sisi
ambako alikuwa akifunikwa kwa maombi.” “Mama, mimi sitaki kumsikia kabisa huyo
mtu.” Grace akataka kuondoka.
“Nisikilize
Grace. Tena nataka unisikilize vizuri sana. Kwa kuwa hasira na ukorofi wa Danny
ndizo zimetufikisha hapa tulipo. Wametumia udhaifu wake vizuri sana, sasa hivi
wamemuacha anateseka peke yake hospitalini wakimcheka waziwazi. Kama
wanaofurahia yaliyompata. Na ninakuhakikishia Grace, ukiruhusu hasira zikuweke
mbali na Mungu, hata Fili utampoteza.” Grace akarudi kukaa.
Mama
G, alipomuona Grace ametulia akaendelea. “James alikuja na taarifa
zilizotupelekea kuingia kwenye maombi. Alikwenda kumuona Danny, huko ndiko
alikokutana na kina Zinda. Akayasikia mazungumzo yote kati ya Zinda, mama yake
na Danny.” Mama G akamtizama Grace, alikuwa ameinama tu. Mama yake akaendelea.
“Kwa mazungumzo yote yalivyokuwa yakiendelea, hakika wale watu wamebeba mambo
mengi sana mioyoni mwao na wamekusudia kulipa kisasi vibaya sana. Wameanza kwa
Danny.” Grace akanyanyua macho kumtizama mama yake.
“Sasa
turudi tokea mwanzo. Kipindi kile cha machafuko ya kuingiliwa na Malii, Danny
akakasirika, nasikia alimtafuta Zinda akitaka au akimtambua kama ndio ndugu wa
kweli. Nasikia kitu cha kwanza Zinda alichokifanya nikumrudisha Danny kwao.
Lakini mama yake Zinda akamwakikishia kuwa ni kweli tumemloga, na kumchukulia
bahati zake. Lazima yeye na watoto wake wapelekwe kwa mganga ili wamzindike au
wamwague, vitu kama hivyo ili sisi tusimguse tena.” Man alikuwa kimya
akisikiliza.
“Ndipo
safari za Tabora zikaanza sasa. Danny, Sara na watoto, wakisindikizwa na Zinda,
ili kwenda kuaguliwa na kuingizwa kwenye ukoo wa kina Zinda. Walipelekwa huko
mara tatu. Wakafanyiwa dawa za kienyeji kwa huyo mganga. Sasa safari ya mwisho
ambayo Danny alipelekwa na watoto, wanasema walifanyiwa utakaso, sijui! Lakini alipeleka
kondoo, mbuzi na jogoo mwekundu kwa huyo mganga. Sasa unajua hayo ya kumwaga
damu ni kama unaingizwa kwenye maagano fulani. Danny ameingizwa kwenye maagano
ambayo yeye mwenyewe hayajui!” “Mara
zote hizo inamaana alikuwa akienda na wanangu!?”
Grace aliuliza huku akilia.
“Sio
kwenda tu, kwenda kuaguliwa nao huko kwa mganga. Sasa safari hii walimwambia aende yeye na watoto tu, bila
Zinda ili akaunganishwe na ukoo wao. Nasikia ndio ilikuwa yakafanyike mambo ya
matambiko. Kufanya kafara na mengineyo. Sasa bila kujijua, Danny ametoa watoto
kafara. Hawa watu walikuwa wakimchezea tu Danny na kumloga yeye mwenyewe bila
kujua.” Grace akazidi kulia kwa uchungu sana.
“James
anasema wamezungumza mambo mengi sana. Wakimlaumu Danny kuwa alikuwa akimfanyia
Zinda kama kumdhulumu haki yake. Kuwa amempokonya hata mchumba wake. Ambaye ni
Nanaa, akampa Geb.” “Mpaka leo
wanamlilia Nanaa!?” Grace akauliza. “Bado wana uchungu
naye. Wakajidai wamesamehe, yameisha, kumbe bado. Kuna maswala ya kazi. Si
unakumbuka ile kazi aliyonayo Danny ni James alimuunganisha?” “Nakumbuka. Tena tukamshukuru sana Mungu.
Ulikuwa ukifunga na kuomba kwa ajili ya Danny apate kazi baada ya kumaliza
chuo.” Grace akajibu huku akifuta
machozi yaliyokuwa yakitoka kama mvua. “Ewaaa! Kumbe unakumbuka Grace?”
“Siwezi kusahau mama. Niliteseka na yule mtu, hakika sikujua kama
mwisho wetu utakuwa mbaya hivi! Nakumbuka kila kitu mama yangu. Siwezi kusahau
yale maisha ya wasiwasi niliyopita na Danny. Wewe na Geb mkitulisha kama watoto
wa ndege! Hatukuwahi kupumzika na Danny. Mwanzo wetu mpaka leo hii bado
ananiliza Danny! Amekuwa ni mwiba ambao sijui utanitoka lini! Unaniuma vibaya
sana.” Grace aliendelea kulia. Man
akamsogeza karibu. “Pole Grace. Pole sana.” Man alijaribu kumtuliza.
“Ehe
mama!” Man akataka mama G aendelee. “Basi, nasikia baada ya James kuwatangazia
marafiki kuwa kuna kazi, Zinda yeye ndio aliomba wakwanza. Lakini Geb
alivyotusimulia ni kama wakashauriana aunganishwe Danny kwa kuwa wakati ule
Danny hakuwa na kazi, na Zinda alikuwa nayo.” Grace akatulia kama anayevuta
kumbukumbu. “Ni mambo mengi sana. Lakini kwa kifupi, wamebeba mambo mengi sana
ambayo wamekusudia kulipa kisasi. Na wamemwambia mizimu ndio imemzuia kufika
nyumbani kwao, kwa kuwa anamkosi mkali sana. Hawamtaki tena, na wamembakisha
Danny ili kulipa ubaya wote waliomtendea Zinda. Sasa swali likawa kwa…” “Mwanangu
Fili? Mungu wangu mama! Watammaliza mwanangu.” Grace akahamaki. Alimkata mama yake kwa haraka
sana akiwa amepaniki.
“Subiri
sasa. Tunaye simba wa kabila la Yuda, Grace. Usije sahau hata siku moja.
Kumepigwa maombi ya nguvu hapa, hujawahi kuona Grace. Hatujawahi kuomba kama
leo. Tulitubu kwa kumlilia Mungu akumbuke rehema kwenye maagano aliyoingia
Danny. Tulivunja kila madhabahu iliyoshikilia majina yetu wote. Geb alijawa nguvu
za Mungu mpaka mapepo lakamlipuka Fili.” “Mama!” “Alianza kutambaa kama nyoka. Ametapika vitu
vyeusi sana. Akajichomoa kila kitu. Nesi mwenyewe alikimbia. Alikuwa amegeuza
jicho kama anakata roho. Unamjua Geb hapendi kesi wala maneno mengi. Akaliamuru
hilo pepo sijui mapepo, linyamaze na kumtoka Fili kwa haraka. Hapo hapo Fili
akawekwa huru. Walikusudia kummaliza yule mtoto pia. Lini, hatujui. Lakini
tumeomba Grace. Tumemlilia Mungu akukomboe wewe na uzao wako. Geb akaamuru hiyo
hedhi iliyokuwa imeanza gafla, ikome na urejeshewe mzunguko wako kama kawaida.”
“Basi ndio maana nikashangaa
nimeamka mchana, hamna kitu. Damu imekauka na wakati ilikuwa ikimwagika isivyo
kawaida ya siku zangu!” “Basi mshukuru Mungu.
Amekukomboa.” Mama G akamgeukia Man.
“Man
mwanangu. Najua umeingia kwenye ndoa ukakutana na misiba. Mimi sijui kiwango
chako cha imani, na wala sijui ni umbali gani upo tayari kwenda na Grace.
Lakini sisi wakati wote imani yetu ipo kwa Yesu. Hatujawahi kutishwa na
shetani. Ameshatupitisha kwenye magumu mengi sana. Lakini hatuna nia wala
hatuna mpango wakumuacha huyu Yesu. Ndio kimbilio letu pekee. Sina baba wala
mama. Sisi na watoto wetu ndio ukoo umekamilika. Wakati wote Mungu amekuwa
kimbilio letu. Nilimwambia Geb, na wewe nakushauri. Kama umekusudia kuwa na
familia. Iwe Grace au mwanamke mwingine yeyote yule, magoti ndio itakuwa silaha
pekee itakayokusaidia kushinda na kuweka ulinzi
kwa familia yako. Nikisema magoti, namaanisha piga goti haswa mbele za
Mungu, mwambie unamwitaji akupe uongozi kwenye familia yako.”
“Awe
mlinzi wako, ndipo utaishi kwa uhuru. Kwa kuwa shetani yupo na amepewa mamlaka
yake na anatawala kwenye hii dunia. Nguvu zake sisi tumeziona sio kusimuliwa.
Tumemuona akifanya kazi. Lakini Mungu ametutetea. Sisi wenyewe kwa maombi yetu.
Hatujui kukimbilia kwa mchungaji wala kwa jirani, maana mambo mengine ni magumu
hata kusikika kwa watu. Tunaishia kung’ang’ana na Mungu mpaka anatujibu.” Mama
G akaendelea.
“Sina
mpango wakumpokea tena Danny kwenye maisha yetu. Na nitahakikisha hatakuwa karibu
na Fili. Sio leo wala kesho, hatarudi kwenye maisha yetu. Atabakia kuwa baba
yake Fili kwa kuwa alitoka kwetu akiwa na akili zake timamu. Na alikataa kabisa
kubadilika. Swala la hasira na kiburi nilishazungumza naye zaidi ya Grace
ambavyo anaweza kujua. Nilishamshawishi tuombe maalumu kwa ajili ya hilo ili
kama ni roho chafu zimtoke, lakini alisuasua. Hakuonyesha kutaka kubadilika.
Nilikwambia kuwa Danny hakuwa mkwe tu, nilimuhesabu kama mtoto wangu. Kwa hiyo
wakati mwingine nilimchukulia kama Geb na kumvumilia hata pale nilipomuona
anamuonea na kumdhalilisha Grace. Ukimya huo na uvumilivu kwa Danny, ndio
umeniletea makaburi mawili ya wajukuu ambao hata sijafaidi nao! Hakika hatarudi
tena kwetu. Namuombea bila unafiki kuwa yaliyompata, yamsogeze karibu na Mungu,
lakini si sisi.”
“Alimruhusu
shetani amchezee yeye mwenyewe akiwa ameonja vipawa na karama za Mungu.
Alituona kule tulikopitishwa na shetani na Mungu akitupigania, lakini akaamua
kutoka kwa Mungu. Sasa sijui amefika umbali gani na shetani! Sijui amemkubalia
kumtumikia kwa umbali gani! Siwezi kumruhusu tena Danny kuwa na familia yangu.
Ila nawashauri wewe na Grace, mumpokee Yesu kwa upya. Shetani hachoki kujaribu.
Fili tumemuombea na amewekwa huru. Yale aliyopanga shetani juu yake, wala
hayatatimia. Pateni muda, mfikirie juu ya maisha yenu, lakini Yesu awe ndio
msingi wenu.” Wakati wanamalizia, Geb naye akawa ndio anaingia hapo
hospitalini.
Aliwaona
wamekaa hapo, akasogea. Akamkuta dada yake ameinama pembeni ya mumewe analia.
Akamsogelea. “Njoo G.” Akamshika mkono akasimama. Geb akamkumbatia. “Jipe muda.
Nakuamini. Naamini ile nguvu ndani yako. Naamini ule uwezo Mungu alio kujalia.
Kila kitu kitakuwa sawa. Nakuombea sana. Namuomba Roho mtakatifu awe msaada
wako sasa hivi. Jaribu kutulia ili uweze kumsikia. Sisi wote tupo kwa ajili
yako.” “Sijui hata kama
naweza kuomba Geb. Mungu amenichukulia watoto wawili kwa pamoja! Tena kwa kifo
kibaya cha maumivu makali sana. Hakika nimeumia. Najiuliza ni kipi
kibaya hicho, nilichomtendea Mungu, mpaka kuniadhibu mimi kwa kiasi hicho!?
Hakika Mungu amenitenda Geb. Nimeumia vibaya sana. Nafsi yangu imejeruhiwa
vibaya sana. Sijui hata namsikiaje tena huyo Roho mtakatifu.”
“Mbaya zaidi nimechanganyikiwa Geb. Sijui chakufanya tena. Nilikuwa ni
kama nimeshapa dira. Najua kila kitu. Kipi kinaanza, kipi kinafuata, lakini
sasa hivi, sijui tena. Nimekosa hamu ya kila kitu. Ni kama gafla nimehamishwa
kutoka sayari hii, nikapelekwa sayari nyingine. Nikiwa peke yangu na natakiwa
niishi. Sijui chakufanya Geb. Nina majuto ambayo sijui kama yatakuja kuisha
maishani.” Grace aliongea kwa uchungu sana,
akilia. “Nashauri pata muda wakutosha na Man. Na naomba pia umsikilize. Sasa
hivi wewe upo kwenye maumivu. Ni ngumu kutuliza mawazo. Huwezi kuwaza vizuri.”
Hapo kidogo Man akafarijika.
“Niangalie
G.” Grace akamtizama kaka yake. “Ujue siku nzima ya leo nilikuwa nikimuuliza
Mungu, kwa nini uolewe tu na matatizo yaanze! Yaani hata fungate hujafurahia!
Kwa nini anakuwa anamwingiza mtu kama Man kwenye matatizo ambayo hakustahili!
Tuwe tu wawazi mama na Grace, hakuna mtu, au hata mimi nisingependa kuinginia
kwenye ndoa ya namna hii. Nikasimama upande wa Man, nikamuuliza Mungu.
Nikamlilia Mungu kwa ajili ya Grace. Ni kweli G, hastahili kupita hapa
anapopita. Wote tunajua jinsi Grace alivyomwema. Amebeba wale watoto kwa shida
sana. Maumivu na mateso. Hata kuzaa, amezaa kwa shida sana. Leo wameondoka
wakiwa hata hajafaidi au hajawafurahia watoto wake! Nilifika ofisini nikajikuta
nikipiga magoti pembeni ya meza yangu na kumlilia Mungu.” Geb akaendelea.
“Mimi
sijui ni kwa nini iwe ni Man. Sijui kwa kuwa Mungu hakunijibu hilo. Lakini
labda Mungu ameona kuwa ipo nguvu ndani ya Man, ya kukubeba sasa hivi katika
hili. Inawezekana pengine ni kule alikopitishwa Man, kwenye maisha yake, ndio
Mungu ameona yeye pekee ndiye anayeweza kukubeba kipindi hichi kigumu. Sijui
Grace! Maana hawa watoto Mungu angeweza kuwachukua siku nyingine yeyote, lakini
akaamua kuwachukua siku Man ameapa atasimama na wewe!” Geb akamtizama Man.
“Naomba
unielewe vizuri Man. Tunampenda sana Grace.” “Hilo najua.” Man akajibu. “Hapana
Man, hufahamu. Huyu Grace kwangu ni mkubwa, lakini kwangu na mama, ni kama
unavyomuona Liv, yule binti yangu. Ndivyo alivyo Grace kwetu. Ndivyo
tunavyomtizama. Hajawahi kukua kwetu na hatujawahi kumuona yupo tayari kuondoka
kwenye maisha yetu. Hata leo ukiona kina hichi cha maji kwako ni kirefu
sana, tutafurahi sana ukituachia Grace. Tutakupa baraka zote na tutakuaga kwa
amani kabisa. Hata ukisema unaondoka kwa muda, ili ukapate muda wakufikiria
ndipo urudi, basi pia tutaagana kwa amani tu, na bado tukabakia ndugu.” “Grace
ni mke wangu, Geb.” Man aliongea bila paniki.
“Unaweza
usielewe, au ukadhani nimechanganyikiwa. Lakini namuhitaji Grace sasa hivi,
kuliko pengine wewe na yeye mwenyewe Grace angeweza kufikiria. Ukiniuliza kwa
nini, mimi sijui! Lakini namuhitaji Grace. Mungu amenipa mimi. Kama ilivyo
kwako, hata mimi sijui ni kwa nini Mungu amenipa Grace, na amenipa sasa hivi.
Msinielewe vibaya jamani. Ila naomba niwe muwazi tu. Muda mfupi uliopita mama
alisema Danny hatakuwepo kwenye maisha yenu, wala hataruhusu awe karibu na
nyinyi au Fili, kwangu ni habari njema.” Kidogo wakacheka.
“Kweli.
Binafsi nitapata muda wa kujenga familia yangu mimi na Grace tukiwa tumetulia
kabisa. Hapatakuwa na vurugu. Tukitulia, tutakuwa tumetulia. Nimetoka
kuzungumza na Grace leo, juu ya Fili. Ni kama Mungu ametupa sasa jukumu kamili
na kutufungua macho kwenye maisha. Ana uwezo wa kutupa na kutupokonya wakati
wowote. Fili amerudishwa kwetu kwa upendo tu. Hatuwezi kupuuza hilo. Nimepewa
Grace kwa sababu maalumu. Hata mimi sijui iwe kwa nini Grace. Mungu
amenifungamanisha na Grace, siwezi hata kuhema. Sijui kwa nini iwe yeye, tena
kwa miaka yote hiyo! Sijui. Ila nampenda sana Grace. Sijuti kumuoa. Nipo hapa
leo sio kwa sababu najitahidi au najificha kwa jamii kuwa itanionaje, ni kwa
kuwa nataka kuwa karibu naye. Mimi namtaka Grace na kila kitu chake cha
nyuma, nimempokea, ni wangu. Nashukuru Geb kwa kumwambia anisikilize. Maana
ameshaanza kunifukuza.” Geb akamwangalia Grace.
“G!”
“Naona namwingiza matatizoni Geb.
Nimemkuta na maisha yake mazuri. Anaendelea na biashara zake. Ona sasa hivi.
Ameingia tu kwenye ndoa, tayari mikosi.”
“Nisikilize G, Mungu alijua kama unamuhitaji Man, ndio maana akamleta kwako.
Mimi nimeishi maisha ya Man, naelewa anachojisikia. Na wewe ni shahidi. Maisha
ya kutafuta pesa peke yake, na kuzungukwa na watu wanaokutazama wewe kama ATM,
yanachosha Grace. Yupo hapa na wewe kwa kuwa anakuhitaji. Mpe nafasi ya kuwa
mume muone mtafika wapi.” “Maisha
ya Man hayapo hapa Dar, Geb. Sasa hivi nawahitaji wewe na mama. Unajua kipindi
hichi ni lazima niwe na mama. Nitakufa bila wewe wala mama. Na ninajua mama
hawezi kukuacha wewe. Naondokaje au naishije mbali na nyinyi?” Grace aliongea yaliyopo moyoni, hata Man
akashangaa.
“Umemwambia
hayo Man?” Geb akamuuliza. Grae akatingisha kichwa kukataa. “Inamaana hilo
jambo la wapi mtaishi, bado hamjazungumzia!?” “Ndio ilikuwa nikamuulize kwenye fungate, maana mimi nilimuona ni kama
ameshajua tutahamia Arusha. Na ilikuwa rahisi wakati ule kabla sijapoteza
watoto. Hata mimi nikajiambia akinitaka nihamie Arusha, nitahama tu. Lakini
naona ugumu kuacha makaburi ya wanangu. Naona ni kama nazidi kuwatelekeza.” Geb akavuta pumzi na kuzishusha taratibu. Akamvuta
karibu Grace na kumkumbatia tena. Man alibaki kama amepigwa shoti ya umeme,
mama G alijua wazi hilo ni tatizo. Ila alipoona Grace anakubali kufunga ndoa,
akajua amekuza binti, amekubali kufunga ndoa na Man ili ahamie Arusha.
“Nikuulize
swali G?” Grace akakubali kwa kutingisha kichwa. “Kuwa tu muwazi. Wewe utakuwa
na amani kuishi na mimi na mama hapa Dar, halafu umuache mumeo Arusha peke
yake?” Grace akanyamaza. “Eti G?” “Nitafanyaje Geb?” Grace akauliza.
“Sijui. Lakini mimi nisingekubali kuishi mbali na Nanaa. Kwanza sivyo ndoa
inavyotakiwa kuwa G. Utafungua milango mingi sana kwa shetani, tena bila
sababu. Arusha ni karibu sana na Dar. Hata masaa mawili hayaishi kufika Arusha.
Mimi na mama tupo na wewe hasa kipindi hiki kigumu. Na hata mama unajua hawezi
kukuacha katika kipindi hiki kigumu. Kwa nini usisubiri Fili akaruhusiwa hapa
hospitalini. Apone kabisa, ndipo mjipange na Man? Popote utakapokwenda, mama
atakuwa na wewe. Safari hii nakuachia mama.” Grace akacheka.
“Kweli?” Grace akauliza huku akikausha
machozi. “Kama Man atakukubalia lakini. Mimi nitakuachia mama, mpaka aone upo
sawa, ndipo atarudi nyumbani. Ila bado nafikiri mnahitaji mapumziko yenu nyinyi
wawili.” “Na Fili?” Grace akauliza. “Naona Liv anamuuguza vizuri.” Geb alijibu
nakufanya wacheke. “Na alivyokazana. Kila mtu akiingia mpaka manesi anawaambia,
‘nampenda Fili’. Na kidole chake kile mdomoni, na tabasamu usoni.”
Mama G akafanya wacheke tena. “Na mabusu ya kila saa.” Grace akaongeza. “Fili
halalamiki tena. Akilalamika tu, busu.” Geb akaongeza nakufanya wacheke
zaidi.
“Sasa
ndio nilikuwa natoa wazo, kama mtakubali lakini. Sasa hivi mtuachie Fili kwa
muda. Mpaka atakaporudia hali yake ya kawaida. Mnaweza kurudi mapumzikoni kama
mlivyopanga. Najua mkitulia, mtapata muda wakupanga mambo yenu vizuri. Mkirudi
mtatuambia vile mlivyokubaliana. Sisi tuko na wewe G. Chochote utakachotaka,
tutakusaidia. Usiogope. Muda na wakati wowote utakao nihitaji mimi nipo, na
wewe unajua. Sawa?” Hapo kidogo Grace akapata nafuu.
“Na
ninaomba niongezee kwenye swala la makaburi Grace. Naomba yale makaburi
ya watoto yasikufunge. Sisi tunajua Fillius na Fillan walipo.” Grace akaanza
kulia. “Tutayatunza kama kumbukumbu yetu sisi. Lakini sio kwa sababu eti kwa
kuwa wapo pale. Mimi naishi na nyinyi, lakini kaburi la baba yenu lipo
Kinondoni. Tumejengea vizuri. Na tukienda, tunaenda kuangalia na kusafisha, sio
kwa kuwa yupo pale. Ni kumbukumbu yetu tu. Sijui kama unanielewa?” Grace
akatingisha kichwa.
“Muda
ukifika, tutajengea yale makaburi vizuri, na tutayatunza daima. Ila usifungwe
na yale makaburi. Huko nako utafungua milango mingi sana. Hutakaa utoke hapo.
Utachukua muda mrefu sana hapo, ukilinda yale makaburi. Lazima maisha yaendelee.”
Mama G, huwa ni muwazi sana kwa wanae. “Umemuelewa mama?” Grace akatingisha
kichwa huku akilia. “Pole sana G. Pole sana. Mungu atakuvusha hapo.” “Hakika nimeumia Geb. Nimeumia sana. Ila
nashukuru kwa kuwa na mimi sasa hivi. Angalau mmenisaidia kimawazo. Wasiwasi
umepungua. Ni kweli nilishaanza kuona uzito wakuondoka na kuacha yale
makaburi.”
“Nataka
wasiwasi uishe G. Nataka utulie kabisa. Najua sasa hivi unauchungu wa watoto,
lakini usisahau faraja Mungu aliyokutumia. Usisahau pole ya Mungu kwako,
ukazidi kuteseka ukifikiri Mungu amekuacha. Man, ndio pole yako kutoka
kwa Mungu kwa sasa. Ndio faraja pekee Mungu aliyokutumia, kukufariji
katika kipindi hiki. Usije ukasahau hilo na kuendelea kuumia. Huwezi
kubadilisha ya nyuma, lakini unao uwezo wa kutengeneza mbele. Pokea baraka za
sasa, omboleza ukipokea upendo wa watu unao kuzunguka. Hata katika hili, Mungu
atakupitisha tu.” Geb akaendelea taratibu.
“Yale
aliyokusudia kukuangamiza nayo shetani, Mungu atakutumia kicheko siku moja.
Sijui ni kwa nini imetokea, lakini mimi na wewe tumepita kugumu sana. Na bado
Mungu akatuonyesha yupo na sisi.” Geb aliongea na dada yake kwa upole.
“Si kwambii kuwa pengo la Fillius
na Fillan kama litakuja kuzibika, lakini kwani hivi leo mimi na wewe tulijua
tutafika hapa siku ile tunamzika baba?”
Grace akaanza kulia tena na kutingisha kichwa. “Tuliumia sana. Nakumbuka
uliumia sana G. Ukawa unasema unahisi na wewe utakufa. Lakini leo tumesimama
hapa. Pengo la baba halikuwahi kuzibwa, lakini Mungu hakuwahi kutuacha. Hata
sasa Mungu atakusaidia tu. Na hapa pia atakutumia faraja, na utavuka tu.” Grace
akatingisha kichwa kukubali. Geb akambusu kichwani.
“Asante Geb.” Grace akashukuru. “Asante hii ni
ya kukupa mama?” Grace akacheka huku anafuta machozi. “Ulijuaje?” Grace akauliza. “Man mwanangu, pole.” “Pole
na wewe mama.” “Naona pole yangu iwe kubwa. Maana umesikia hapa wanavyonigawa
bila hata kuulizwa!” Wote wakacheka.
“Yaani
wanafanya maisha yangu kama yao vile! Vile wanavyotaka wao wawili ndivyo hivyo
hivyo mimi natakiwa nikubali tu.” “Hata kwetu utakuwa na wakati mzuri mama.”
Man akaongeza. “Nashukuru mwanangu. Akitulia tu huyo. Akili zake zikiwa sawa,
tutakuachia moja kwa moja.” Man akacheka. “Wala hamna shida. Muda na wakati
wowote, sisi pia tunakuhitaji. Tena ndio vizuri na mimi nitapata nafasi
yakumjua Mungu kwa karibu na…” Wakamuona Nanaa anatoka na Magesa. Magesa
alikuwa kwenye walker yake anatembea kama anakimbia. Wakacheka.
“Vipi?”
Geb akamuuliza. “Nimemletea bibi yake. Wala sikujua kama na wewe upo!”
“Amefanyaje tena?” Geb akamkimbilia na kukanyaga ile walker ya Magesa ili
asimame. Akaanza kucheka. “Fujo! Fundi wa zile mashine za mle ndani, ni yeye.
Daktari, ni yeye. Nesi ni yeye. Kila kitu! Anataka kuchomoa zile nyaya pale na
kumvuta Fili pale kitandani. Sasa sijui anataka akakae pale kitandani kama Liv?
Mate tu!” Wote walikuwa wakicheka. “Eti Magesa?” Geb akamtoa pale kwenye Walker
ili ambusu. “Hashikiki mkononi, anataka kufanya kila kitu!” Nanaa akaongeza.
“Mimi naona mbaki naye tu hapa hapa nje, mimi nirudi ndani kwa Fili na Liv.
Nimemuachia nesi mara moja.” “Na mimi nakuja sasa hivi.” “Sawa.” Nanaa alimjibu
Geb nakurudi ndani.
Grace
akaguna. “Hivi Nanaa ataweza kukaa mbali na mama kweli?” “Jasho litamtoka.” Mama G akajibu nakucheka
huku akimfikiria Nanaa. “Lakini hana shida. Nanaa ni muelewa sana. Ilimradi
ajue ni kwa faida yako, hatakuwa na shida.” Wakazungumza kidogo, Geb akaingia
ndani.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Baada
ya siku tatu Fili akaruhusiwa akiwa ananafuu kubwa sana. Geb akaenda kulipia
kila kitu, wakakusanya vitu. Wakatoka. Walikuwa Geb, Nanaa, Grace, na Man. Mama
G alibaki nyumbani akiandaa chakula, kwa kuwa alijua wataruhusiwa siku hiyo.
Hasidi Haachi Asili.
Wakati
wanatoka kwenye hilo jengo, wakamkuta
Gozi na Zinda wamesimama kama wanawasubiria. “Habari zenu?” Wakasalimia, lakini
wote walinyamaza. Geb alikuwa amembeba Fili. “Nina shida ya kuongea na Nanaa.”
Gozi akaanza. “Nakusikiliza.” “Tunaweza kuzungumza pembeni?” “Unamaana mbali na
mume wangu?” Nanaa akauliza. “Nimetumwa kwako. Ni ujumbe wako wewe peke yako.
Nafikiri ingekuwa vizuri tuzungumze pembeni.” “Huyo aliyekutuma hajui kama
nimeolewa?” Nanaa akauliza. Gozi akamwangalia Zinda.
“Msitupotezee muda. Huyu ni Geb,
mume wangu. Huyu ni Grace na mume wake. Grace wifi yangu lakini pia ndio
waliotusimamia harusi. Hakuna utakachoongea hapa kikawa cha hatari wao kusikia.
Ukitaka kuongea, ongea. Kama huwezi, utupishe sisi tuendelee na mambo mengine.”
“Ni Malii!” Gozi akaongeza. “Subiri kwanza. Kabla hujaanza kuongea.” Nanaa
akachukua simu yake kwenye pochi. Akabonyeza vitu kadhaa.
Kisha
akamgeukia Gozi. “Ehe! Nakusikiliza.” Nanaa akamtizama. “Nimetumwa kwako na
Malii, ndio nilikuwa nataka tuzungumze pembeni.” “Wewe unawasiliana na Malii?”
Nanaa akamuuliza, Geb asielewe ni nini anafanya. “Ndiyo. Na ndio amenituma
kwako tuzungumze. Njoo basi pembeni.” “Nisikilize Gozi. Wakati Malii ananibaka,
wewe ulikuwepo na wote hawa walikuwepo, kasoro huyu mume wa Grace na huyo Zinda
hapo. Lakini wote uliwafikishia ujumbe wa kubakwa kwangu. Hakuna asiyejua kama
nilibakwa na Malii. Si ni kweli?” “Ndiyo, lakini..” “Lakini nini cha ajabu?
Kilichobadilika ni kwamba sasa hivi nimeolewa. Kwani hujamwambia hilo Malii?
Maana kazi yako kubwa hapa mjini ni kuhamisha maneno kutoka nyumba moja hadi
nyingine. Kutoka kwenye uhusiano huu kwenda kwenye uhusiano ule. Kutoka kwa
huyu kwenda kwa huyu. Kwa hiyo kwa uhakika hata hili la kuolewa na Geb, ninajua
umemwambia.” “Lakini yeye anataka mtoto wake.” Kila mtu akashituka, lakini si
Nanaa.
“Kwa
hiyo pia ulimwambia kuwa umenipima na umekuta nina mimba yake?” “Sikiliza
Nanaa. Kila mtu anajua baada tu ya kubwakwa, wakina Magesa walikufukuza. Kwa
hiyo sio siri kuwa huyo mtoto sio wa Geb. Acha kumnyima Malii haki yake ya kuwa
baba.” “Kwa hiyo wewe sasa hivi ndio unayegombania haki za Malii?” Nanaa
akahoji.
“Hata
kama jamaa amekosea, lakini anahaki ya mtoto wake.” “Hayo unaongea wewe au
Malii mwenyewe?” “Anasema ameona umesoma jumbe zake. Alikuomba msamaha, lakini
hujibu. Anachoshangaaa umeamua kwenda kumuuza mtoto wake kwa Geb.” “Kwa nini
asinifuate yeye mwenyewe tuzungumze?” Kimya. “Wewe si umemuhakikishia mtoto ni
wake? Sasa kwa nini asije mwenyewe kumdai mtoto wake kutoka kwangu na Geb?”
“Yeye anakutambua wewe, hamtambui Geb.” “Basi. Kwa kuwa sasa hivi tumetoka hapa hospitalini. Kila mtu
amechoka, naomba jioni uje nyumbani tuzungumze vizuri.” Geb alishituka sana.
Akamtizama Nanaa.
“Jamaa
ametuwekea ‘restraining order’.
Hataki tufike karibu na kwake. Si umeona hata jinsi alivyokuangalia?” “Si
umesema unataarifa kuwa nimeolewa na Geb?” Nanaa akamuuliza. Kimya. “Unajua
kama na mimi sasa hivi ninaitwa Nanaa Magesa?” Kimya. “Kwa kifupi tu, pale kwa
Geb pia ni kwangu. Yaani nina amri yakualika mtu yeyote ninayemtaka mimi. Kama
umetumwa habari za mtoto wa Malii, njoo nyumbani kwangu. Nitakujibu maswali
yote uliyotumwa.” “Unauhakika sitaingia matatizoni?” Gozi akauliza. “Mjumbe
anauwawa?” Nanaa akamuuliza.
“Nataka
tu uhakika wa usalama wangu.”“Basi kwa usalama wako, kamuombe kaka James, uje
naye. Utapita pale getini bila shida.” “Sidhani kama James atakubali.” Gozi
akajibu. “Mimi nitazungumza naye hawezi kukukatalia. Wewe niambie muda utakao
taka kuja jioni ili tuwekane sawa tukiwa tumetulia, tuache kuviziana
barabarani.” “Kama kwenye saa moja hivi.” “Sawa.” Nanaa akajibu. “Twendeni.”
Nanaa akarudisha simu yake kwenye pochi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
Geb
alikuwa ameumia sana. Alinyamaza kimya, mpaka Grace alijua kama kaka yake
aliumia. Hakuna aliyekuwa amemuongelesha mwenzake. Wote waliingia kwenye gari.
Nanaa akatoa simu akampigia simu James. Akamuelezea kila kitu. “Naomba atakapokuomba uwalete nyumbani, usikatae kaka yangu. Tafadhali
sana.” “Umezungumza na Geb? Sitaki matatizo Nanaa. Hawa watu ni washirikina na
waharibifu sana. Hakuna sehemu wanayoingia wakaacha salama.” “Ndio nataka
kuweka kikomo kaka. Hata mimi nimechoka.” “Kikomo na kina Gozi?” James akauliza. “Wewe walete au
mlete hiyo jioni. Utaelewa tu.” James
akanyamaza. “Kaka!” “Sawa Nanaa. Lakini
nasita sana.” “Usiwe na wasiwasi kaka yangu. Naomba uwalete tu.” Wakaagana.
~~~~~~~~~~~~~~~~~
v
Grace bado yupo kwenye
maombolezo. Ndio wameruhusiwa na mtoto akiwa salama kiroho na kimwili. Ushauri
ni warudi kwenye fungate, ili kupumzika. Ni kama ameshapata suluhu kubwa sana
juu ya hatima yake na Man. Kazi kwake yeye.
-
Ni ipi Hukumu ya Danny kutoka kwa
Grace?
v Malii anataka mtoto wake!
Isivyo kawaida, Nanaa anaalika
adui wakubwa sana wa Magesa nyumbani kwao! Zinda ndiye anayesadikika kuua
watoto wa Grace na Danny. Leo Nanaa anawakaribisha bila hata kuuliza! Kumsogeza
tena karibu na Fili waliyemtoa mapepo si jambo hata mmoja wao analotamani!
Imemuuma sana Geb na kushangaza kila aliyesikia. James, Grace na Man.
-
Je, yale aliyosema Man yanatimia
kwa Geb? Kuchuma mali kwa miaka yooote
hiyo, leo Nanaa ameolewa hata mwezi haujaisha, anatangazia adui wa Magesa na
yeye ni mmiliki mwenza wa Geb!
-
Nini nia ya Nanaa? Amesema ndio anataka kuweka kikomo.
-
Kwa nani?
-
Je, ndio Nanaa naye anafungua
makucha yake? ‘Jino
kwa Jino!’ Kwa nani?
Endelea kusoma…..
0 Comments:
Post a Comment