Danny akatoka kama mshale. “Grace!
Grace!” “Ameshatoka nje.” Wenzake wakamjibu wote wakionekana kuishiwa nguvu sio
kama walivyoingia kwa makeke wakisubiri kusulubishwa kwa kina Magesa. Danny
akatoka nje akimkimbilia Grace. Yule mama aliendelea kucheka huku anatoka pale
ofisini. Akawasogelea rafiki zake Danny. “Naomba kuuliza jamani.” Kimya. “Eti
hapo mlipokaa nyinyi, wangapi wenu wameoa na kuacha wake zao wakiwa na watoto
wadogo, au mmekuja kumshabikia mwenzenu akiharibu familia yake tu halafu nyinyi
jioni mnarudi kwa wake zenu na watoto?” Kimya.
“Eti
jamani?” Yule mama akasisitiza swali lake akiwatizama kwa zamu. “Lakini wale
walizidi ushirikina sista.” Gozi akajibu. “Nyinyi wake zenu wamewaambia
hawawalogi? Au labda niulize hivi. Bora vipi, vile alivyokuwa amelogwa akatulia
na kusaidiwa kufika hapo alipo. Akapewa maisha na watoto. Jioni anarudi
nyumbani kwa mwanamke aliyetulia kama Grace, au hivyo mnavyosema hajalogwa,
yupo kama kachanganyikiwa? Anajibu watu hovyo, hata mwanasheria aliyemtafuta
yeye mwenyewe pia amesahau kama yuko upande wake!”
“Hamumuurumii
mwenzenu? Leo akiwa na watoto watatu ndio akumbuke mke aliyemuoa siye!? Kwa
kuzungumza na Grace kwa dakika chache tu, utagundua ni mwanamke wakuoa na
kuweka ndani. Na ndio maana aliweza kumvumilia rafiki yenu muda wote huo. Kwa
shangwe zile mlizokuwa mkishangilia kabla hawajafika kina Grace hapa, nikajua
huyo Grace ni kituko. Grace mwenyewe kapoa kama maji ya mtungini! Neno moja
kulitoa kinywani mwake ni shida. Roho yake inaonekana safi mpaka usoni! Leo
mnamshangilia mwenzenu aache mke kama yule na watoto!? Ili aende wapi?” Yule
mama aliwakazia macho wakashindwa hata kujibu.
“Sasa
macho ya Mungu yapo juu yenu nyinyi wavunja amani kwenye majumba ya watu. Kila
shida watakayopata hao watoto wao, ni pigo kwa watoto wenu. Sasa endeleeni
kushabikia. Umati huo ni wa kwenye harusi tu, wakivunja ndoa, mnawaacha wenyewe
wawili. Tena mnakaa mbali kabisa. Nyinyi ndio mnakimbilia kujilaani!” Wakaanza
kutoka mmoja baada ya mwingine.
Akabaki
Zinda. Akamgeukia “Wewe ndio msimamizi wao wa harusi?” Kimya. “Umeoa?” Kimya. “Kwa
hiyo wewe ndio rafiki wa karibu? Umekuja kumuunga mkono mwenzio akijizika
mwenyewe? Umekuja kushabikia au?” Kimya. “Huogopi kushabikia kuvunjika kwa agano
la Mungu wewe!? Unajua Mungu alisemaje katika hili?” Kimya. “Alichokiunganisha
Mungu, mwanadamu asikitenganishe. Sasa naona wewe ndio umekuja kusimamia
kuvunjika kwa agano la Mungu. Subiri Ole yako inakuja. Utajibu mapigo ya Mungu.”
Kimya.
“Sasa
jua wazi leo ndio umeshuhudia kifo cha mwenzio. Amejizika hivi hivi ukiwa
unamshangilia. Hamuwezi kushindana na mama mwenye watoto wadogo, halafu anayo
pesa.” Yule mama akataka kuondoka, kisha akamgeukia Zinda aliyekuwa akitaka
kutoka nje. “Au shida yako na wewe ni hawa watu waachane?” Kimya. Yule mama
akacheka kwa kusikitika. “Kweli kikulacho ki nguoni mwako. Wewe haupo hapa
kumkomoa Grace kama Danny anavyofikiri. Upo hapa kuhakikisha unamtoa rafiki
yako kwenye neema! Umesimama naye kwa makini sana mpaka mwisho kuhakikisha habadili
mawazo. Umesimama naye bega kwa bega mpaka umehakikisha amemtaliki mkewe, ili
abakiwe hana kitu!” Yule mama akawa kama amegundua hila ya kweli ya Zinda.“Sasa,…” Zinda akatoka kwa
haraka asitake kumsikiliza zaidi huyo mama.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Grace
alitoka pale na hasira, wote wakimfuata nyuma, hakufika mbali akaangua kilio
kama amefiwa. Man akamuwahi. “Ni nini?” Grace aliendelea kulia kwa hasira sana.
Mama yake akasogea na Geb naye akaja. “Huna
haja yakulia Grace. Nitaenda kuzungumza na mtu sasa hivi, haya mambo yatakuwa
sawa.” “Nataka kuwaona
wanangu Geb. Ni haki yangu.” “Naelewa. Rudini
na mama nyumbani, ukapumzike. Nitakupigia simu baadaye kidogo.” Grace
akaendelea kulia.
“Naomba
unyamaze Grace. Unahitaji tu muda. Kila kitu kitakuwa sawa.” “Hapana Man. Sihitaji muda, nahitaji watoto
wangu. Sara ni mtoto wa juzi kabisa. Hawezi kunilelea wanangu. Mimi wale watoto
nawajua. Niwatundu sana. Na Danny anahasira sana. Watakuja kuwaua bure
wanangu.” “Zipo njia nzuri tu na sahihi
tunaweza kutumia ili kuwapata watoto. Kama nilivyokwambia ni haki yako. Mimi
nafahamiana na watu wengi sana ambao hawawezi hata kumaliza week moja watakuwa
wamekamilisha hili. Lakini watakuhitaji wewe Grace. Hivi ulivyo kwa sasa huwezi
kutetea watoto wako. Unatakiwa utulivu mkubwa sana. Unakumbuka?” Grace
akatingisha kichwa kukubali, nakujiegemeza kifuani kwa Man, akampitishia mikono
kwa juu na kubaki akimsugua mgongoni.
“Atakuwa
sawa tu Geb. Naomba tupate muda wakufikiria kwanza kabla ya kuchukua hatua
tukiwa hatujatulia.” Akambusu Grace kichwani pale alipokuwa amemuegemea na
kumuuliza taratibu. “Vipi lakini hatua ya kwanza, mmefikia wapi?” Grace
akanyanyua uso na tabasamu. “Tumeachana rasmi.” Grace akajibu. “Pole na
hongera.” Grace akacheka kwa deko. Man akaanza kumbusu pale pale huku
amemkumbatia. Mama G alishageuka pembeni. Geb alitoa simu yake nakuanza
kuperuzi.
“Unaweza
kumtuma mtu akaja kuchukua watoto.” Wote wakageuka. Man aliacha kumbusu Grace.
Alikuwa Danny. “Pale ni kwangu Danny. Sihitaji kutuma mtu kufuata wanangu.
Nitakuja kuwachukua mimi mwenyewe. Wewe niambie muda wa kuja kuwachukua.”
“Lakini lazima uwarudishe Grace. Nimeshakata tiketi za ndege kuondoka ijumaa
jioni kuelekea Mwanza, kisha Tabora.” Grace akanyamaza.
“Eti
babe?” Man akamuuliza kwa upendo na kumbusu kichwani kwani alikuwa amempa
mgongo wote wakimtazama Danny. Grace akaanza kulia tena kwa uchungu. “Huwezi jua jinsi nilivyohangaika na huyu
mwanaume Man. Ukiniambia malipo yake nikuwafanya wanangu wanatangatanga kama
upepo hivi! Hakika Mungu atakulipa Danny. Hatakuacha.” Grace akaendelea kulia. “Naomba unyamaze Grace.” Man
akajaribu kumtuliza. “Nilimuuliza kabisa
kabla sijabeba mimba ya hawa mapacha. Tena afadhali Fili alikuja bila taarifa.
Nikamuuliza kama anauhakika anataka watoto wengine. Akajibu ndiyo. Leo amegeuka
na matusi juu wakati yeye ndio aliwataka hao watoto! Leo wamezaliwa, anatesa
wanangu! Kila siku watoto wako barabarani wanasafirishwa huku na huko! Kila
weekend unasikia wanangu wapo Tabora! Na mazingira ya kule mimi nayajua Man. Ni
nini wanachotaka na hao watoto wangu!? Kwa nini usiwe unaenda wewe mwenyewe
angalau kuacha watoto wapumzike jamani!? Kimya.
“Mungu atakulipa Danny. Hakika utavuna unachopanda kwangu na wanangu,
tena bila hatia!” Danny kimya. “Nitakuja kuchukua wanangu jioni.” “Sawa.”
Wakashangaa Danny ametulia. “Na
kesho wakati narudisha watoto, ndio nitakuja kuchukua mizigo yangu yote. Kwa
hiyo naomba nisikute kuna chumba hata kimoja kimefungwa.” “Sawa.” Danny akakubali. Grace akakunja uso kama
anashangaa kulikoni.
“Mimi
naomba kukuaga rasmi Danny.” Mama G akajisogeza. “Lakini kwa hakika
nakuhurumia. Nakuhurumia kwa kuumia sana. Najiuliza, hivi baada ya hii hekaheka
yote hii kuisha. Grace akachukua watoto. Na..” “Grace hawezi kunipokonya
watoto.” “Usibishe Danny. Usibishe hata kidogo. Kwa kuwa haitakaa ikatokea
katika ulimwengu huu ambao MIMI, Oliva Magesa ninaishi, eti nikaruhusu wewe na
Sara mkalea watoto wa Grace! Naomba hapo usibishe. Kwa kuwa unajua
hutaweza kushindana na sisi ukashinda. Na ninakushauri usithubutu. Wewe
mwenyewe umeshindwa kuelewa nguvu inayofanya kazi kwetu. Umekaa na sisi umeona
vile tunavyopita kwenye moto, kisha tunatoka tukiwa tunang’aa. Usibishe hata
kidogo. Unaweza kuharibu zaidi.” Danny kimya. Mama G aliongea kwa kutulia
lakini kwa ukali. Rafiki zake nyuma wakisikiliza kwa kujiiba.
“Ila
ninachojiuliza, baada ya hii hekaheka yooote hapa. Wapambe wako wote wanakuacha
sasa baada ya kuridhika wewe kutengana na familia yako. Utafanyaje Danny!?
Usinijibu kwa haraka, kwa kuwa nakufahamu Danny. Nimeishi na wewe kama mtoto
wangu. Nalia kwa uchungu nikikuhurumia Danny. Nakuhurumia sijui mwisho wako
utakuwa upi! Kweli umeruhusi yaliyowapata wazazi wako yakupate na wewe!?” “Sara
ametulia.” “Nilikuomba usinijibu Danny. Ila unisikilize. Naomba kukupa ushauri
wa mwisho.” Danny kimya.
“Wewe ni yatima kama mimi tu. Tena yatima
ambaye huna hata ndugu mmoja au ukoo unao ufahamu. Walio upande wako sasa hivi,
hawajui umuhimu wa familia. Mimi naelewa ndio maana nilikubeba kwa kukuvumilia
sana kwa miaka yote hiyo. Kwa kuwa sasa hivi unataka kuanza upya, tulia, anza
vizuri mwanangu. Anza ukitaka historia ya baba yako usikurudie. Namfahamu Sara,
kwa kuishi naye nikiwa nimemchagua awe mke wa Geb. Kwa hiyo ujue sikuwa
nimemchukia. Nilimpenda sana tu. Namfahamu yeye, nakufahamu na wewe. Sasa ili kilichotokea
leo kati yako na Grace kisitokee tena kwako na Sara, tulia. Muombe Mungu
akusaidie Danny. Anza upya ukikusudia kujenga vizuri, sio kama ulivyoanza na
Grace. Ukiwa umejaa chuki, hasira, jazba, kutokujiamini, hali yakutaka
kutawala, kutaka wewe ujulikane na kuheshimiwa hata ambapo hukuwa unastahili
tena ukiwa huna chochote ila suruali uliyokuwa umevaa tu.” Hapo Danny pia
hakujibu. Geb alikuwa karibu sana na mama yake.
Madume
wawili, wanaojielewa kimaisha walikuwa upande
wake. Wamesimama kama
wanaume wanaojielewa. Wametulia. Kwa kuwaangalia tu, utajua pesa ipo na
wana uelewa wakutosha. Utamwambia nini mama G? Aliongea kwa kujiamini bila
hofu. Aibu waliodhani atapata mtoto wake Grace siku hiyo imewarudi wao
wenyewe! Wakawa wamepoa. Walimchambua Grace watakavyo.
Walitukana mwili wake, Danny akiwasaidia kumdhalilisha kwa undani sana kana
kwamba Grace alikuwa changudoa aliyelala naye siku moja tu na si mke!
Sasa ameshasaini talaka, mwanaume Man ameshikilia kiuno na mabusu ya kichwani
na shingoni kila wakati. Utamueleza nini mama G?
Man alionyesha wazi alishaonjeshwa anachokitukana Danny, na amekolezwa na Grace. Wakati mama G anaongea, Man alishamvuta Grace karibu kabisa. Grace akiwa amempa mgongo, Man aliegemeza uso wake pembeni ya shingo ya Grace na yeye akimsikiliza na kumtazama mama G na kina Danny. Mara kwa mara alirudia kubusu shingo ya Grace huku mikono imezunguka kiunoni kwa Grace aliyekuwa ameinama lakini akimsikiliza mama yake. Ni mama G tu ndiye aliyekuwa akiongea. Kwa ukorofi wake wa asili aliweza kuzungumza na Danny bila hofu.
“Nazungumza
na wewe leo, kwa kuwa sitarajii kupata muda na wewe tena. Nisingependa kuja
kukuona karibu na nyumbani kwetu. Sitaki hata baya litokee kwa wajukuu zangu
ili tusije pata sababu ya kuwepo chumba kimoja na kunitukana kama
ulivyonitukana leo. Leo ndio mwisho wako wakunitukana Danny. Wewe si mume wa
Grace tena, kwa hiyo kwa kuja kuinua kinywa chako na kunitukana tena. Kwa namna
yeyote ile, ninakuahidi nitakuadhibu vibaya sana. Hakika hutakaa ukanisahau
maishani mwako. Sikutishi, ila ninakuhakikishia nitakuadhibu vibaya sana.
Tunakuacha leo ramsi, tena kwa amani kabisa. Kwa hiyo huna sababu yakuendelea
kutufuata nyuma wala kututukana.” Danny na marafiki zake kimya.
“Naomba
Mungu, akuweke mbali kabisa na sisi ili uyaishi maisha unayofikiria sisi
tulikuzuia kuyaishi. Na ninakushauri pata muda wa kumsihi Mungu akusamehe kwa
mabaya yote uliyomtendea Grace. Umemtenda ubaya ambao hakustahili. Umemlipa
mwanangu adhabu ambayo hakika hastahili. Umemchafua sana moyo wake. Lakini
Danny, Mungu ni mwenye rehema. Naamini atamrejeshea Grace miaka yake yote
aliyopoteza kwako. Alikupenda na kukuheshimu hata pale ambako hukustahili.
Hakika pata muda umuombe Mungu msamaha. Mimi naelewa ninachozungumza Danny. Patana
na Mungu kwa haraka ndipo utakuwa salama. La sivyo, nakuhurumia.” Mama G
akaendelea.
“Cha mwisho, nasisitiza, kwa kuwa hujatoka
kwenye asili ya pesa, na huijui pesa, ndio umekutana nayo sasa hivi, kuwa
makini sana.” “Hapo unanitukana mama.” “Nakwambia ukweli. Wote sisi hapa mpaka
rafiki zako waliosimama na wewe sasa hivi wakikushangilia hapa, tunafahamiana
vizuri sana. Hakuna siri kati yetu. Hakuna hata mmoja wenu hapo ambaye
hajafanikisha jambo fulani kama hakupitia kwenye mfuko wa Magesa. Bisheni.”
Kimya.
“Kwa
hiyo nakusihi uwe makini na pesa ya ukubwani. Pesa inaleta baraka, na pia
huleta laana. Haina tabia yakuishi sehemu isiyo na amani. Huwa inakimbia na
kabla ya kukimbia huwa inamtindo wakuharibu kwanza. Itakuchafua halafu ndipo
ikimbie. Mungu awe nawe katika mwanzo wako.” Mama G akawa amemaliza. “Twendeni
wanangu.” Mama G akatangulia. Geb, Man akiwa amemshika mkono Grace wakamfuata
nyuma. Walipoondoka Man na Grace, ndipo na Geb akaondoka na mama yake.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Ilibidi
wote warudi nyumbani kwanza kama alivyoshauri Man. Wakaingia sebuleni wakakaa. “Umeridhika?”
Geb akamuuliza Grace. Grace akafikiria kidogo na kuanza kulia. Alilia sana.
Kila mtu akabaki kimya, Man alibaki akimsugua mgongoni. Mwishowe akamshika
mkono na kumtoa nje. Alilia Grace mpaka akakaa chini. Hakuna aliyejua anacholia.
Mama yake akabaki kimya. Kila mtu kimya.
“Naomba
mnisaidie maji ya kunywa.” Man akarudi ndani. Geb akaenda kuchukua na kurudi
nayo kwenye glasi. Baada ya muda wote wawili wakarudi ndani. Grace alikuwa
ametulia. “Geb! Naomba nikushukuru kusimama na mimi kuanzia mwanzo wa hii ndoa
yangu na Danny mpaka leo. Kunivumilia kwa kila namna. Kazini na kila mahali.
Anaweza Danny akashindwa kukushukuru, lakini naomba mimi nikushukuru. Asante
kwa kutubeba tokea tunaanza maisha mpaka leo bado nataka mnisaidie.” Grace
akaanza kulia tena.
“Naomba unyamaze Grace.” “Nina hasira sana Geb. Nina hasira siwezi
kujizuia. Nina hasira, sijui nifanye nini.” Geb
alijaribu kumtuliza dada yake. “Jipe muda.” Geb akaendelea. “Mpaka lini? Niambie Geb. Mimi nakuwa mtu
wakuanza kila siku! Hapa nafikiria pakuweka mizigo yangu mara baada ya kuchukua
kutoka kule anakoishi Danny na Sara, sina. Nafikiria pakulala na wanangu usiku
wa leo. Wawe na furaha, wacheze. Sina! Nimepoteza muda mwingi kujenga kwenye
mchanga. Mvua imenyesha kila kitu kimeparanganyika. Utafikiri mtoto
niliyemaliza shule jana!” Grace aliendelea kulalamika.
“Hamjui ni kiasi gani nilivyokuwa nimechoka nikidhani labda siku moja
nitapumzika. Pesa yangu yote ya akiba nilitoa nikawekeza kwenye ile nyumba.
Imejaa vitu vya mamilioni ya pesa zangu. Nina hasira yakushindwa kujisaidia.
Zaidi nikifikiria ni Danny, mtu ambaye hana hata shukurani na heshima ndio
anakwenda kuishi pale! Nimenunua kile kiwanja kwa pesa zangu mimi mwenyewe na
Geb. Tena Danny akiwa hana kazi, mimi namlisha. Amewekeza pesa kidogo tu,
tayari nyumba ndio yake anatangaza anataka kuoa aweke mkewe pale ndani! Naumia
sana. Nimepoteza muda na pesa zangu nyingi.”
Grace aliendelea kulia akilalamika.
“Zaidi yeye kuwa ndio mwanaume wangu wa…”
Grace akanyamaza na kuendelea kulia. “Nasikia hata kutapika. Nasikia hata kufa sijui!” “Nisikilize Grace. Kwanza tuongelee kitu cha
msingi kwanza. Ya Danny yameshaisha. Naomba tuanze taratibu tu.” “Sina muda Geb. Sina huo muda mimi.” “Hapana G. Sasa hivi unaanzia pazuri sio kama
zamani tukiwa hatuna pesa.” “Nianze
ujenzi upya!? Hapana Geb.” Grace akazidi
kulia.
“Niangalie G. Naomba tulia. Baada ya harusi tu, tutachukua siku 7. Mimi na wewe, tunatafuta nyumba popote unapotaka wewe.” “Ile nyumba nimeijenga kwa muundo wangu mimi Geb. Wewe unajua jinsi nilivyokuwa nikihangaika kuchora kila chumba na kupangilia kila kitu. Kila kitu pale ndani nilikaa chini na kufikiria ndio nikawapa mafundi. Sitaki majumba ambayo watu wanayajenga tu hata hawajui yana ukubwa gani! Sina muda huo Geb.” Grace aliendelea kulalamika.
“Basi
baada ya harusi, tutatafuta kiwanja. Kizuri unachopenda wewe. Halafu mimi
mwenyewe nitatafuta kampuni ya ujenzi. Wazuri. Tutawakabidhi ile ramani. Tena
kwa kuwa ulishakaa humo labda kuna kitu utataka kirekebishwe. Utarekebisha
kwenye michoro yako. Nitawapa. Nakuhakikishia Grace, ndani ya mwaka mmoja
unahamia kwako. Kwa sasa hivi kuna nyumba hiyo hapo pembeni ya huo ukuta.
Kubwa, tupu. Weka vitu vyako na wanao, muishi kwa kadiri ya unavyotaka wewe kwa
muda ambao unasubiri nyumba yako ijengwe.” Geb aliendelea.
“Siwezi kuishi hapo
na wakati najua
hapo ulipahangaikia kwa ajili ya Nanaa na wanae!” Grace akaendelea.
“Mimi nakaa hapa na mama. Huko sitaki kurudi.” Nanaa akawahi kwa
haraka. Grace kashangaa. “Kwa
nini?” Kimya. “Wewe Nanaa!? Kwa nini hutaki kuishi kwenye nyumba yako nzuri
unataka kuendelea kuishi hapa kwa kubanana na watoto?” Ikabidi Grace atulie,
amuhoji Nanaa vizuri. “Hapa hatubanani Grace. Tunatoshea tu.” Grace hakuwa
ameelewa.
“Mama wewe!” “Mimi nimefanyaje? Ni Nanaa
mwenyewe. Ukimwambia arudi kwake, pressure zinapanda, hatakula siku nzima hapa.
Atalia tu. Huna utakachomwambia akarudi pale. Wewe muache tu humu humu ndani
wabanane na wanae. Wewe nenda kakae pale kama alivyokwambia Geb. Na unyamaze
maisha yako yaendelee.” “Danny amenipotezea muda mwingi sana.” Grace akalalamika
tena. “Basi ujue anazidi kukupotezea muda.” Mama yake akamkatiza.
“Sikubali.”
Grace akakataa. “Wewe jana tuliongea vizuri hapa. Tumepanga mipango mizuri ya
leo na kesho. Na unajua kabisa kwenye swala la mipango wewe ndio tunakutegemea.
Sasa badala maisha yaendelee, unakuja hapa, unaanza kumlilia Danny.” “Aku mimi
simlilii Danny!” Grace akabisha. “Tokea uje hapa, jina ni hilo moja na nyumba.
Kwa nyumba gani bwana wakati sisi tumelala mpaka chini!? Unalilia baraka za
jana, unasahau yale Mungu ametutendea na anatutendea mpaka sasa? Angalia mambo
mazuri yanayotuzunguka na yanayokusubiri wewe uyafanyie kazi ili yatimie!” Mama
G akaendelea.
“Wewe
ndio umeshika mipango mizuri sana ya harusi ya mwezio. Harusi kesho kutwa,
Nanaa hana gauni anakutegemea wewe. Wote hapa sisi tunakutegemea wewe mtu wa
mipango. Usikubali Danny aendelee kukukandamiza. Ni juzi tu hapa tulikuwa
tunafurahia na Geb, kwamba Grace wa mipango amerudi. Ukawa kama Grace
tunayekujua wa miaka ile kabla ya Danny. Hata jambo liwe baya vipi, una uwezo
wa kulitengeneza mpaka linakuwa zuri. Mungu kakurudishia akili zako, leo
unakubali tena kuchanganywa na Danny!? Huko umeshatoka mama. Shukuru Mungu
umetoka salama, tena umezungukwa na watu wanao kupenda na kukutia moyo.” Mama G
akaendelea.
“Haki
haililiwi Grace. Kama ni haki yako ni yako tu. Itakujia. Mungu wako yupo.
Tumemwita kwenye magumu mangapi na akajidhihirisha
kwetu? Eti Grace?” “Mengi.” Grace akajibu. “Basi naomba utulie. Mimi najua
ulivyohangaika na Danny. Lakini leo ulimuweza vizuri sana pale mbele ya
mwanasheria wake, mpaka amejirudi. Sasa simama hivyo hivyo. Asikurudishe tena
chini. Panga mipango yako ukiwa umetulia. Ukiwa huna pressure. Geb amekupa mipango
mizuri kabisa. Wamekupa nyumba yao. Nenda kaishi hapo na wanao huku ukifikiria
chakufanya. Huyu Nanaa hapa ndio kafika. Jioni kachukue wanao. Wakafanye fujo
pale usiku kucha, asubuhi warudishe kwa baba yao. Tena kwa amani tu bila ugomvi
wala hasira. Shukuru Mungu. Jioni tuondoke zetu twende Arusha.” Mama G
akaendelea.
“Wewe
si ulitaka siku 30 za mapumziko?” Grace akanyamaza huku ametulia. “Basi ujue
Mungu ndio amekupa hizo siku 30. Kaanze upya. Ukiwa huru ukijua sasa huna
Danny, ila watoto watatu. Kapange mipango yako vizuri. Ukirudi hapa unanguvu na
akili safi. Na nina kuhakikishia Grace, anguko lako lipo kwenye kukaa chini na
kulia. Aliniambia baba yenu mimi wakati ananiacha. Wewe ukiona unadalili za
kukaa chini na kuanza kujuta mambo ya nyuma na kulia, basi ujue ndio unaharibikiwa
kabisa. Huna utakachoweza kubadilisha kwenye yaliyopita. Chukua mazuri,
mabaya yaache, endelea. Ndio siri iliyonifanya kuwafikisha nyinyi hapa.”
“Lasivyo
mngekuwa kama watoto wa kawaida tu, kama ningeamua kukaa chini nilie na
kujilaumu kwa maamuzi mabaya niliyofanya nyuma. Mimi sio mjinga. Najua wapi
nilikosa, wapi nirekebishe na garama ipi inabidi kulipa kwa maamuzi mabaya
niliyofanya nyuma. Sasa hivi unalipa garama kwa maamuzi mabaya uliyochukua
zamani. Danny yupo hivi hivi, hajawahi kubadilika tokea tunamfahamu mpaka leo.
Hakuwahi kuficha makucha yake, tuseme kwamba alikubadilikia! Wehu wake upo
hivyo hivyo, lakini ukakubali kuolewa naye. Garama ndio hiyo. Jifunze, endelea.
Tena endelea kwa makini ukijua una watoto watatu unaotakiwa kuwafikisha si
pazuri tu, pazuri sana. Basi.” Kila mtu akaelewa.
“Unanielewa
Grace?” “Nimeelewa mama.” Grace akajibu. “Haya, naomba ukaoge. Badili nguo
twende tukazunguke madukani mapema kisha ukachukue wanao. Harusi ya jumamosi
lazima ifungwe.” “Nguo zipo hotelini.” “Kwani wewe hutembei na nguo Grace
bwana? Utanicheleweshea mambo.” Nanaa akacheka. “Muone naye huyu! Wewe cheka tu
wakati huna gauni.” “Naenda kuoga na kubadili. Nakuja sasa hivi.” “Na nakuomba
urudi Grace.” “Narudi mama! Mbona huna imani na mimi!?” “Mimi nakujua wewe.
Rudi hapa mapema. Sitaki unikwamishe.” “Mama kwa mipango!” “Uliianza mwenyewe.
Na ujue mwenzio niliiandika chini yote. Na tutaitimiza tu.” Grace akacheka.
“Twende mwaya Man.” Kidogo kukatulia.
“Labda
mimi niwaage kabisa.” Man akasimama. “Ukiondoka ndio hutarudi tena?” Mama G
akauliza. “Najua Grace atahitaji muda na nyinyi na baadaye watoto. Nafikiria
kurudi Arusha, ili apate nafasi bila mimi kumbugudhi.” Grace akabaki amezubaa. “Man!”
Akamuita kwa upole. “Hapana babe. Ni sawa kabisa. Najua unahitaji muda na
watoto. Mimi nitakuwa Arusha nikikusubiri.” Grace akapooza sana. Man akamshika
mkono.
“Twende
uniambie vile unavyotaka Grace. Mimi nipo hapa kwa ajili yako. Lakini sitaki
nikuzuie kufanya mambo ya msingi.” “Unanikimbia?” Grace akaanza kulia. “No no
nonononooo! Mungu wangu nishahidi Grace.” Man akastuka sana. “Nafanya hivi kwa
ajili yako. Ukitaka nibaki, nitabaki. Hata ukitaka nikusindikize kutafuta gauni
la harusi la Nanaa, tutaenda wote. Naomba usilie Grace. Niliacha kila kitu, ili
niwe hapa na wewe. Ila nilijua unataka muda na watoto. Kama unaona ni sawa mimi
niwepo, basi twende tukaoge, tuje tuwachukue au tukutane kokote kule.
Tuzunguke, kisha tukachukue watoto, halafu jioni twende kwa Mzee Ole. Au
unasemaje?” Kila mtu alimuona vile Man alivyokuwa amepaniki kwa haraka kama
aliyekuwa akiogopa asiharibu.
“Twende.”
Grace akabaki ameinama. “Babe!” Man akaita. “Twende. Twende tukazungumze huku
tunaenda. Najua tutafikia muafaka tu.
Twende.” Akamshika mkono na kumvuta. Grace akasimama. Wakatoka. “Siwezi kukukimbia
Grace. Wewe unajua.” Wakamsikia Man akiendelea kujitete huko nje, kwa
kubembeleza. “Kweli?” Wakamsikia Grace akiuliza. “Naenda wapi?Au
nikimbilie wapi? Haya yote mimi niliyategemea. Ndio maana nilitaka kuwa hapa na
wewe. Hakuna talaka nzuri. Kila talaka inamadhara mpenzi wangu. Naelewa.”
Wakasikia milango ya gari inafunguliwa na kufungwa, gari ikaondoka. “Mmmh!”
Mama G akaguna.
Kwenye Shopping siku hiyo Ya Jumatano Ya
Talaka.
Walikutana
madukani. Grace alikuja amechangamka kama sio yeye! Man alikuwa pembeni yake. Geb alisisitiza Nanaa
asiwe anazunguka. Kwa hiyo alibaki naye kwenye gari. Ikitokea mama G, Grace na
Man wanapata nguo nzuri, wanamwita Nanaa, anaingia ndani kwenda kujaribu, Geb
na Man wanabaki kwenye gari. Walifanya hivyo kwa maduka mawili, wakati wanaenda
duka la tatu, Nanaa akiwa ameongozana na Grace na mama yao, wakakutana na
Gozi.
Gozi
alibaki ameduwaa. Kwa asili Gozi ni muongeaji na muhamisha maneno sana.
Alikuwepo asubuhi akishangilia talaka ya Grace. Ndiye aliyesambaza habari za
kubakwa kwa Nanaa. Ndiye aliyemwambia hata Malii kuwa Geb alimuacha Nanaa. Sasa
hawakujua anachoshangaa ni nini! Lakini tayari Nanaa alikosa raha. “Twendeni
wanangu.” Mama G akatangulia. Hakutaka hata wasalimiane. Wote walimuona jinsi
Nanaa alivyopooza. “Gauni hili zuri. Nimelipenda.” “Mbona sasa furaha yote
imeisha?” Grace akamuuliza. Nanaa akacheka. “Labda kuchoka.” Akajibu taratibu,
lakini wakajua liko jambo tu. Kwenye duka hilo hilo Nanaa alipata kila kitu
walichokuwa wamebakiza. Maana vingine Grace na mama yake walikuwa wakinunua
wakati Nanaa yupo kwenye gari.
“Basi
rudi ukapumzike kwenye gari wakati sisi tunasubiria hapa kwenye foleni ili
tulipie.” Grace alimgeukia, maana Nanaa alikuwa amezubaa akiangalia sehemu
moja. “Acha tu niwasubiri.” Nanaa alijibu na tabasamu la uongo. Bila kujua,
Grace akamtumia ujumbe Geb. Ndani ya dakika mbili Geb akawa amemsimamia nyuma
yake.
“Umepata
gauni unalopenda?” Nanaa akamgeukia Geb. “Nimelipenda.” Geb akabaki akimtizama
machoni. “Vipi?” Geb akamuuliza. Akamuona anaanza kulia. Akamshika mkono
wakatoka pale. “Gozi ameniona.” Geb akawa ameelewa. Akavuta pumzi kwa nguvu. Mama
yake akatoka. “Kuna nini?” “Mlikutana na Gozi?” Geb akauliza. “Tulimuacha hapo
akishangaa. Kwani vipi?” “Nanaa hakutaka Malii ajue kama ni mjamzito.” Geb
akajibu. “Na akijua Gozi, basi ujue ulimwengu mzima utajua.” Wote wakatulia kwa
muda.
“Nisikilize
Nanaa. Tusimpe shetani nafasi. Tufanye kama tulivyomwambia James. Kila
changamoto tutakabiliana nayo kwa wakati wake. Tusijibu changamoto za baadaye
sasa hivi. Kwa sasa hivi Jimmy ni mtoto wetu. Hata Malii akijua hana
atakachofanya.” “Sitaki kuiona sura
yake sasa hivi Geb. Bado sipo tayari kukutana naye. Na ninamjua akijua hivyo,
atapata sababu yakutaka kukutana na mimi.” “Tutashugulika
naye siku atakapokuja. Naomba usipaniki. Tulia kabisa.” “Mimi nakubaliana
na Geb. Kwanza Malii anakabiliwa na kosa la ubakaji. Hiyo ni fimbo ya kwanza
yakumchapia. Pili, tunaweza kumfanyia kama tulivyowafanyia wenzie mpaka
wakanyamaza.” “Mmewafanyiaje?” Nanaa akauliza.
“Geb
aliwafungulia mashitaka wale wote na wameambiwa chochote kitakacho tupata sisi
wote, ni jela. Mbona wamepoa! Wewe usipandishe pressure ukashindwa kuolewa.
Usikubali na wewe Malii akurudishe nyuma. Niliyomwambia Grace na wewe yazingatie.
Kila kosa lina garama zake. Usikubali Malii akupokonye na ndoa. Unanielewa?” “Nimeelewa mama. Nilishaingiwa na hofu.” “Hata kidogo. Sasa hivi tunasonga mbele kama
ulivyoniambia wewe. Tuendelee na mipango
yetu mpaka washangae. Kupaniki, kulalamika na hofu, ndiko kuanguka kwetu.
Tumesameheana, tuendeleeni kusonga mbele. Tena tunaendelea kwa kushikana
mikono. Akianguka mmoja, tunanyanyuana. Haya futa machozi, tujiandae kwa
harusi.” “Asante mama.” Nanaa akasikika ametulia. Wakarudi kwenye gari
walipowaacha Man na watoto.
“Wamekusumbua?” Nanaa
akauliza wakati wamefungua mlango wa gari. “Hata kidogo. Wako kama vile
mlivyowaacha. Mwanao haongei kama nyinyi hampo.” Nanaa akacheka. “Mama!” “Amemwimbia
anko Man wimbo wa Diego?” Liv akamwangalia na kucheka. “Utamwimbia baadaye?”
Akakubali kwa kichwa. “Basi nasubiri Liv. Sawa?” Man akamuuliza. Liv akacheka tu na kidole chake kimoja
mdomoni. “Vipi? Mmefanikiwa?” Man akauliza huku akimwangalia Grace. “Naona kila
kitu kipo.” “Afadhali. Lakini nina ombi moja.” Man akamgeukia Mama G na
Geb.
“Karibu.”
Geb akaitika. “Twendeni niwapeleke sehemu tupate chakula cha mchana. Binafsi
nina sababu ya kusherehekea.” Wote wakacheka. “Kweli Man umekusudia.” Nanaa
akadakia. “Bahati haziji mara mbili Nanaa.” “Mimi mwenyewe nakuunga mkono.
Twende tu tukasherehekee. Kwanza Grace wifi yangu anastahili kupumzika.” “Wewe
unakubali kwa haraka sababu ya chakula tu.” Mama G alifanya wacheke.“Asante
Man.” Grace alishukuru. Man akamgeukia Geb. “Sawa. Pia itatusaidia kuwa kwenye
ukurasa mmoja kwenye upande wa mambo ya harusi.” Wakaondoka.
Mchana Wa Siku Ya Jumatano Ya Talaka.
Walifika
kwenye mgahawa huo ikiwa imetimu saa saba na nusu mchana {7:30}. Kila mmoja wao
alikuwa na njaa. Wakaagiza vyakula. Kucheka kukakolea. Walikula na kunywa,
Nanaa na Man wakiwachekesha. Nanaa anauliza maswali, Man anajibu na kucheka
kwanza yeye mwenyewe huku akisimulia kwa tahadhari mbele za wakweze. Geb kama
baba yake Grace na mama G. Lakini wakawa na wakati mzuri sana. Hakutajwa Danny
hapo. Vilikuwa vimejaa vicheko tu.
Grace
na yeye alikuwa akicheka mpaka machozi. Kwa muda mfupi waliokuwa pamoja ni kama
Man alimjulia Grace vilivyo. Hakuacha kumsifia kwa hili au lile. Alimtizama na
kutaka kumsikia akizungumza kitu chochote tena kwa kirefu zaidi. Alimtaka asimulie labda kituko fulani
walichokiona wakiwa pamoja. Grace alipokuwa akifupisha, Man alimtaka arudie
kipengele hiki au kile, ilimradi tu kumfanya azungumze. Waliwasikiliza kwa muda
huo mfupi, lakini tayari walishakuwa wameandika historia nzito pamoja. Hapakuwa
na ubishi kama wawili hawa wanaendana au walikusudiwa.
Mama
yake alijiridhisha, hata Geb alikuwa akicheka, ishara kuwa amempokea au ametoa
baraka zake kwa Man. Man alikuwa na utundu wa maneno. Akichanganya na kicheko
chake chakutoka rohoni, nilazima utacheka tu. Akakutana na Nanaa ambaye kucheka
ndio kwao, basi ungependa kuwepo hapo. Na wala usingeamini kama ni hawa kina
Magesa waliokuwa kwa mwanasheria asubuhi ya siku hiyo marafiki wakiimba
wasulubishwe.
Saa 10 Jioni Ya Siku Hiyo Ya Jumatano Ya Talaka.
Waliwarudisha
nyumbani Nanaa, watoto na mama G. Grace, Man na Geb wakaenda kwenye nyumba ya
Geb. Wakazungumza kidogo huku wakizunguka humo ndani. Geb akawaachia funguo kwamba
wawe huru. Watakapochukua watoto, warudi hapo. “Nimemwambia Jeri atafute vijana
wawili, watakusaidia kuhama. Utawakuta wakikusubiria nyumbani kwako getini na
ile gari kubwa. Watakusaidia kubeba mizigo na kukuingizia hapa. Atakuletea
msichana wa kazi wa kukusaidia kwa usiku huu mpaka kesho utakapo warudisha
watoto. Nimemuomba alale hapa na nyinyi ili usihangaike na watoto.” Grace
akaanza kulia.
“Ni
kwa muda tu G. I promise. Utapata kwako soon. Na sitakubali uhamie sehemu
ambayo hutaipenda. Nakuahidi utapata kitu bora. Usilie.” Man alikuwa
akiwasikiliza. “Asante Geb.” “Basi mimi nawaacha. Muwe na wakati mzuri. Msalimie
wazazi.” “Nashukuru Geb. Watasikia.” Man akajibu na kumpa mkono. Geb akawaacha
hapo
Mama ni Mama Tu.
Walishahamishia mizigo yao hapo kwa
Geb. Waliitoa hotelini, wakahamishia hapo ndipo wakaenda nyumbani kwa Grace
kuchukua watoto na mizigo ya Grace. Hapakuwa mbali na pale anapoishi Geb. Hata
Man alielewa ni kwa nini Grace alililia ile nyumba. Haikuwa kubwa ya kutisha,
ila ilipangiliwa kwa ustadi sana. Kuanzia getini mpaka vyumbani. “Unauhakika
hii ramani yote imetoka kichwani kwako!?” Man aliuliza kwa mshangao. “Kila kitu
Man. Hakuna hata jani ambalo limeota hapo nje kwa bahati mbaya. Nimefikiria
ndipo likapandwa hapo. Nikikwambia nimetumia mamilioni ya pesa hapa, niamini
Man. Hamna kitu cha bei nafuu hapa. Hakuna. Nimemwaga pesa kwa ajili ya
wanangu. Wala si mimi na Danny. Kwa kuwa mara nyingi sisi wawili tulikuwa
kwenye wakati wa hekaheka. Hata kama ni mapenzi, sio kwa kubembelezwa. Ni fujo
tu.” Man aliendelea kuangaza macho kila mahali.
“Itabidi
na mimi unichoree. Nilifikiria kununua nyumba, lakini umenitia shauku ya kuwa
na kitu kizuri na chatofauti. Na Geb amesema kuna uwezekano ndani ya mwaka
mmoja nyumba inaweza kukamilika. Sioni sababu ya kutokujenga. Unafikiri
utanisaidia?” Grace aliendelea kukusanya vitu vyake. “Nitafanya Man. Tukiwa
mapumzikoni tutaanza taratibu kuhu ukiniambia ni vitu gani unataka.” “Naamini
tutakuwa na wakati mzuri Grace. Tulia tu. Tufanye
kwa hatua.” “Nakushukuru Man. Nakushukuru kusimama na mimi.” “Nakupenda Grace.
Nakupenda sana.” Grace akamsogelea nakuanza kumbusu mpaka Jeri alipogonga.
“Naona
dada ameshaandaa watoto wote wapo tayari. Kama kuna kitu chakusaidia niachie
nimalizie.” Grace hakumkuta Danny wala Sara. Alikuta watoto wake wote wamelala.
Akawaamsha. Isivyo kawaida au ambavyo hakutegemea akaona watoto wake
wamefurahia sana kumuona. Fili alitaka kuondoka na mama yake. “Utanichukua na
mimi?” Fili alimuuliza na kumliza mama yake. “Ngoja dada akakuogeshe kwanza
ndipo tuondoke.” Grace alizungumza naye kwa upole, akambusu.
Man
alishamsadia kuweka kila kitu kweye maboksi aliyokuwa ameleta Jeri. Wakawaacha
Jeri na wale vijana wakichukua mizigo ya Grace,
wao wakaondoka na watoto pamoja na msichana wao wa kazi. Alimwambia Jeri
hatahitaji tena msichana mwingine. Yule aliyenaye atamtosha. Kwanza amezoea
watoto na anamuheshimu sana Grace. Hakutaka mtu mgeni kwa usiku huo mmoja tu
ndio awahudumie. Jeri akaelewa. “Mbona watoto wenyewe wametulia Grace? Sio
watundu kama ulivyosema?” Man akauliza. “Mimi mwenyewe nimeshangaa. Labda
usingizi.” “Halafu wote wanamacho kama yenu!” Wakacheka.
Ukweni.
Grace
hakutegemea mapokezi makubwa aliyoyapata nyumbani kwa kina Man. Alikuta ndugu
zake Man wote wakimsubiria mpaka huyo kaka yake mkubwa na familia yake.
Walimfurahia na kumuonyesha upendo wa namna yake. Kwa kuwa kulikuwa na watoto
wadogo, michezo iliendelea huku wao wakifahamiana. Mama yake Man alikuwa
mtulivu, lakini sio Mzee Ole.
Vilijaa
vicheko na utani. Ndipo alipojua utundu wa Man aliiupata kwa baba yao. Wajukuu
walimfuata na kucheza naye kisha kuondoka. Ulikuwa ni usiku ambao Grace
aliufurahia sana. Picha nyingi zilipigwa. Watoto wote walionekana kuzoeana,
kasoro mke wa kaka yake Man alionekana kuwa mbali kidogo na wao. Grace aliliona
hilo lakini akanyamaza. Watoto walipoanza kulia, Malisa akasema ndio ishara
kuwa wamechoka. Yeye na mumewe wakaanza kuondoka na watoto wake. Man na Grace
nao wakaondoka na watoto wao.
~~~~~~~~~~~~~~~
Wakati
wapo njiani Fili akaanza. “Unaturudisha kwa dad?” “Hapana. Kwani unataka
kurudi?” “Nataka twende wote mama.” Grace akanyamaza kwa muda. Man akaona
anafuta machozi. “Labda kunakuwa na upweke dada. Siku hizi Sara hataki wawe
wanakimbizana mle ndani. Anasema hataki kelele.” Dada yao akadakia. “Ndio maana
wamepooza! Huwa anawachapa?” Grace akauliza. “Hapana. Ila baba yao ndio huwa
anawachapa wote hawa.” Grace akanyanyua simu nakumpigia Geb.
“G?” Geb akapokea. “Grace?” Geb akaita tena.
“Ni nini tena!?” “Nataka nyumba yangu. Sitaki Sara
akae pale. Nimebadili mawazo.” “Naomba usilie Grace.
Niambie kuna nini?” “Sara anakataza wanangu
wasikimbie ndani ya nyumba yangu! Yaani yeye anawapangia wanangu kitu
chakufanya nyumbani kwangu? Nataka nyumba yangu. Zungumza na mwanasheria wako,
mwambie nipo tayari kupigania haki yangu. Siogopi hata kwenda mahakamani.
Lakini Sara hataishi pale.” “Basi usilie. Hilo
tutalifanyia kazi. Wanaendeleaje lakini?” “Wamepooza
kweli, kama sio wao! Si unajua Danny anavyopenda kuchapa? Sasa nasikia
anawachapa mpaka hawa wadogo. Watoto wamepoa Geb, kama wagonjwa!” Geb akatulia kidogo. “Mwambie aniletee niwaone.” Akasikia
sauti ya mama yake. “Mama anaomba awasalimie.” “Ngoja
nizungumze na Man, nitakupigia.” Kidogo
Man akapumua. Alihisi amesahauliwa.
“Mama
anataka kuona watoto. Unafikiriaje? Twende leo au kesho?” Grace akauliza. “Unajua
Danny alikataa kabisa mama na Geb wasiwe karibu kabisa na wanangu?” “Kwa nini?”
Man akauliza. “Anasema tutawaloga kama yeye tulivyomloga.” Man akacheka sana. “Usicheke
bwana!” “Duniani kuna mambo! Yaani kuna vitu vingine unasikia unafikiri ni
utunzi tu.” “Mmmh!” Grace akafikiria.
“Lakini
Man, Danny amenichokoza. Sitakubali. Hakika nimeamua sikubali!” Man akanyamaza. “Unafikiriaje sasa?” “Juu ya
nini?” Man akauliza. “Kuwapeleka kwa bibi yao.” “Ni sawa tu. Twende.” Wakaenda
mpaka nyumbani kwa Geb.
Liv alifurahi sana kumuona
Fili. Mpaka kila mtu akashangaa. Aliruka ruka huku akiimba jina la Fili wakati
ndio alikuwa anasinzia wakati Grace anaingia na wanae. “Lakini hawana afya
mbaya.” Mama G aliongea huku akiwatizama kwa zamu. “Si kwa kuwa nimemuacha dada
yao? Yaani bila yeye naona hawa watoto wasingekuwa hivi.” Geb alikuwa kimya
akiangalia. Liv alianza kumbusu Fili. “Naona mama mzazi alikuwa na hamu kweli
na Fili.” Nanaa akachokoza. “Mimi nataka kukaa hapa na Liv, anko. Sitampa pipi.
Nitacheza naye tu. Simfundishi kuruka. Nitakua siongei sana.” “Njoo kwanza
Fili.” Geb akamvuta karibu.
“Nitatulia
anko.” “Nisikilize. Cha kwanza wewe ni mtoto mzuri sana. Hivyo ulivyo ndivyo
Mungu anataka uwe. Wewe umeshaona mtoto mdogo anayezungumza kifasaha na vizuri
kama wewe?” Fili akanyamaza. “Huyu
Danny sijui kafanyaje wanangu. Wote wamekuwa kama wajinga!” “Baba Fili hataki
kelele dada.” Msichana wa kazi akadakia. “Sasa mbona yeye anapiga kelele? Aache
kuniharibia watoto.” Grace alishakasirika.
“Naomba
mnisamehe jamani! Nashindwa kujizuia. Sijui ni kupaniki!” “Hakuna mtu
anayejiandaa kwenye tukio kama hili Grace. Mimi naomba nitoe hoja yangu.”
“Karibu Man.” Geb akamkaribisha, wote wakamgeukia. “Tulikuwa tuna mpango
wakusafiri na Grace kwa siku kadhaa. Lakini kwa hali jinsi ilivyo, najua Grace
hawezi kutulia. Au niseme hata mimi siwezi kutuliza mawazo wakati tunajua wazi
watoto wanamlilia Grace. Itakuwa tunajidanganya tu. Hatuwezi kuwa na mapumziko
wakati kuna vilio vya watoto.” Man akaendelea.
“Kwa
kuwa Danny amekusudia kusafiri nao weekend hii. Na Grace alishamkubalia. Basi,
baada ya harusi tu, sisi turudi hapa Dar, tushugulikie swala la watoto.” “Amesema anasafiri nao tena.” Grace akadakia. “Tutampelekea
watoto uwanja wa ndege hiyo siku anayotaka kusafiri nao tena, au popote
atakapotaka yeye. Sisi tutamwandalia kila kitu atakachohitaji cha hao watoto
huko safarini, tutampelekea. Akirudi nao tutakuja kuwachukua tena mpaka
mtakapoweka sawa mambo ya watoto. Hawa watoto bado ni wadogo sana na
wanamuhitaji Grace.” Kila mtu alishangaa hekima ya Man.
“Kabla
hamjanijibu kuhusu wazo la kwanza, naomba niende kwenye pendekezo la pili.”
“Lakini wewe Man kweli unaakili za kiutuuzima. Na ni kweli una upendo wa dhati.
Umebeba matatizo ya Grace kama yako! Binafsi nimeshakupenda gafla.” Mpaka Man
mwenyewe alicheka. “Nanaa huyu mtoto jamani!” “Kweli mama. Nani anataka kuanza
maisha mapya na mtu akiwa na watoto wa mtu!? Mimi naelewa mama. Najua hofu
aliyonayo Grace kwa kuwa nilikuwa hapo. Ni Geb tu ndiye ananiwezesha kuwa hapa.
Nilikuwa nalia na hili tumbo mchana na usiku. Hofu, na itakuaje ndio
vilikuwa vikinisumbua. Wawili ni wawili mama. Tena mmoja akawa na uwezo wa
kushika taa na kuongoza njia! Hakika safari inakuwa rahisi. Binafsi nakubaliana
na wazo la Man. Jamani Danny ni mkali nyinyi! Wote tulikuwa tukimuona
anavyomchapa Fili. Sasa leo awe kwenye hali ile, hawa watoto hawatakuwa
salama.”
“Lakini
si mnamjua jinsi Danny alivyo mbishi? Itachukua muda mrefu sana kufikia muafaka
wakati wanangu wanahangaika.” Grace alilalamika. “Nisikilize Grace. Hawa wanao
mpaka sasa hivi hapo walipo hawapo hatarini. Panga karata zako kwa makini sana
ili ukiweza kuwa nao, unakuwa nao moja kwa moja. Kama alivyosema Man, tupange
haya mambo kwa utulivu na kwa umakinifu. Hakuna jeuri mbele ya sheria. Na pesa
inaongea mahali popote. Harusi ikiisha tu, hata kama bado hawajarudi, tuanze
kufuatilia swala la watoto. Tutafanikiwa tu. Mungu yupo.” Mama yake akamtuliza
Grace, akatulia kidogo.
“Una
wazo gani la pili?” Grace akauliza kwa upole. Liv alishaondoka muda mrefu sana
na Fili wakaenda kucheza michezo yote Magesa aliyokuwa akimvurugia. Na nikweli
alifurahia. Mara kadhaa walimsikia akicheka huku akimfundisha Fili na Fili naye
akimwelekeza Liv. Waliwageukia na kuwatizama. Liv alikuwa anacheka sana. “Leo
dada kapata alichokuwa anakitaka. Liv sio wakucheka mida hii. Sasa hivi
angekuwa anajizungusha pale kwa mama yake au kifuani kwa baba yake. Kumuona amechangamka vile, ujue kafurahi
sana.” “Alikuwa anamuulizia kila siku.” Nanaa akamjibu mama G.
“Mungu
atasaidia tu.” “Mimi ndio kauli nilitamani kukusikia ukiiongea kwa muda mrefu
sana G. wewe mtu wa mipango, kwa nini unakatishwa tamaa bwana?” Geb alimuuliza.
“Wewe umeshajua sasa hivi ni nini unataka, ujue hapo umeshatatua matatizo kwa
asilimia 85. Kule kujua tu nini unataka, umeshatatua tatizo lako. Basi sasa
hivi tuanze kufikiria jinsi yakupata.” “Sawa.” Grace alijibu safari hii
akasikika ametulia.
“Karibu
Man kwa wazo la pili.” “Lakini msinielewe vibaya kwenye hili wazo la pili.” Man
akajaribu kuwatahadharisha. “Karibu tu.” “Okay. Nina taka kusema hivi, ipo
tofauti ya mtu aliyezaliwa kwenye pesa na ambaye amepata pesa ukubwani. Kuna
vile viwango vya pesa mtoto kama Liv ameshazoea kuvisikia tokea anazaliwa mpaka
anakuwa mkubwa. Akienda dukani anapomuona dad au mama ananunua vitu halafu
analipa bila shida. Anapomsikia bibi yake amemnunulia dhahabu. Yaani dhahabu
yeye ameivaa tokea ni mtoto. Hatasumbuliwa na viwango vikubwa vya pesa au
dhahabu anapokuwa mkubwa. Tofauti na mtoto aliyekuwa katika mazingira ambayo
anaona wazazi wanalalamikia mpaka bei ya chumvi.” Wakacheka kidogo.
“Zipo pesa ukimtajia mtu,
hata kama ni mkorofi kiasi gani, lazima anatulia na kufikiria mara mbili mbili.
Ni rahisi kwa mtu ambaye hajazoea kushika pesa nyingi kumpokonya kitu chake cha
thamani kwa pesa ndogo sana. Na kuna useme unasema, ‘everybody has price’. Hakuna mtu ambaye hanunuliki. Hata Danny ambaye
Grace anamuhofia na kusema ni mkorofi sana, anaweza kununulika tu tena bila
ugomvi. Kwa mfano. Grace ameniambia aliwekeza pesa nyingi pale kuliko Danny.
Tunaweza kukisia tu kutokana na mshahara wake, tukapata hicho kiwango. Halafu
tukakizidisha mara mbili. Unamfuata na pesa taslimu kwenye mkoba.” Wote
wakacheka.
“Mimi
sio tapeli jamani! Ni mfanyabiashara tu. Msinielewe vibaya.” Man alijitetea,
wakacheka zaidi. “Hakika Danny atakubali. Ninavyomjua yule.” Grace akadakia. “Si
umeona sasa?” “Lakini ili kuongeza nguvu, uende akiwa amekaa na Sara. Sara
anapenda sana pesa. Mimi nimeishi naye hapa, namfahamu linapokuja swala la
pesa, hajiwezi. Akikataa Danny, Sara atamuweka sawa mpaka akubali.” Grace
akaanza kucheka.
“Si
umeona mambo yanavyokwenda vizuri?” Geb akamuuliza Grace. “Sasa hivi
ninafuraha. Asante Man.” “Karibu. Ila mimi sio tapeli.” Wakazidi kucheka. “Hapana.
Hatukuelewi vibaya Man. Tunashukuru kwa mawazo. Nafikiria kufanyia kazi kesho
asubuhi tu, tukiamka. Nataka Grace aondoke hapa Dar akiwa ametulia. Kwa kuwa
ndege yenu yakuwapeleka Arusha ni ya jioni, asubuhi nitazungumza na yule
mwanasheria wetu. Amuombe mwanasheria wa Danny, tukutane kwa kikao cha dharula
na kifupi. Atamwambia nilazima Sara awepo kwa kuwa anahusika kwenye maisha ya
hao watoto. Tutakapokutana ndipo tutatoa mawazo yote mawili ya Man. Tuone
watasemaje. Na akikubali, tunasainishana kesho hiyo hiyo na kuacha hati ya
nyumba ikibadilishwa. Atoe jina lake kabisa kwenye hati ya nyumba. Ibaki kuwa
ya Grace tu. Yeye na Sara wakatafute sehemu nyingine yakuanza maisha. Tutaweka
wazi kuwa hatupo tayari Danny na Sara waanzishe familia nyingine pale ndani. Wanawajibika
kwa watoto wao, sio sisi.”
“Asante
Geb. Nakushukuru. Lakini itakuaje endepo atataka pesa kesho hiyo hiyo?” “Si ndivyo tulivyokubaliana tuwe na pesa yote
taslimu na alipwe papo hapo ili asije badili mawazo baadaye? Tusimpe hata muda
mrefu wakufikiria na tumjengee hoja ngumu sana ambazo hataweza kushinda hata
akitaka kupeleka kesi mahakamani.” Nanaa alibaki kimya. Ndipo alipoamini kuwa
ni kweli Geb anapesa na anampenda dada yake.
“Kwanza amekiuka masharti mengi sana ya
kampuni anayofanya kazi. Nayo hiyo nitazungumza na yule mwanasheria. Nimpe
nakala za sheria za kampuni yao ili kumtuliza kesho. Na nitamwambia akicheza,
atapoteza vyote. Kazi na familia.” Grace akatulia kabisa. “Leo naweza hata
kulala.” Grace akasikika ametulia kabisa. “Asante Man.” “Karibu.” Wakabaki
wakiangaliana. Wakacheka.
“Jamani
naomba mimi nikapumzike. Nimefurahi mmeweza kufikia muafaka. Tutaonana kesho.”
Nanaa akaaga akionyesha kutulia zaidi ya kawaida yake. “Asante Nanaa. Ulale
salama.” Grace akajibu. “Sasa yule dada mimi namuacha. Kumtoa pale ni
kumkatili.” “Kwanza hatakubali.” Bibi yake akaongeza. “Liv! Njoo mbusu mama.
Naondoka.” Akaja anakimbia. “Twende wote mama.” “Mimi naenda kulala.” Liv
alishabadilika. “Twende mama. Twende.”
“Liv! Mimi nakwenda kulala ndani chumbani, mwanangu. Siendi popote.” Nanaa
akamuhurumia. “Liv! Unataka kumsindikiza mama kulala?” Geb akaingilia.
Alishakuwa mwekundu. Akatingisha kichwa kukubali.
“Haya,
mshike mkono umpeleke chumbani.” Liv akafanya kama alivyoambiwa na baba yake. “Usilie
sasa. Twende. Fili twende mnisindikize kulala.” Fili aliyekuwa ameduwaa akimtizama
Liv, akafurahia mualiko. Wote wakaenda kupanda kitandani. Liv aligoma kutoka
pale kitandani. Geb aliingia nakukuta wote wamelala. Akacheka. Akamtoa Liv wa
kwanza na kumuweka kitandani kwake, ndipo akamchukua Fili. “Watakuwa wamechoka.
Nasisi tunaondoka. Man anatakiwa na yeye kupumzika.” Grace akasimama. Akaenda
kumuamsha dada. Alikuwa amelala na mapacha chumba alichokuwa akiishi Grace na
Danny. Wakaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Njoo
hapa.” Mama yake alimuita Geb baada ya kufunga milango yote na kujikuta
wamebaki wao wawili tu pale sebuleni. “Sasa hivi kuwa sana makini kwenye
mipango yako. Haupo tena peke yako upo na Nanaa. Anapokusikia ukitamka mipango
mikubwa hivyo na yeye hajashirikishwa, yeye kama binadamu ni lazima ataumia.
Halafu unakuwa ni kama unamtuma akafanye hivyo hivyo kwa kaka yake. Nilikwambia
Geb. Unaweza usione madhara yake sasa hivi, lakini Nanaa hatakuwa mjamzito
milele. Au hatakuwa anaishi humu ndani milele. Wewe mwenyewe uliona jinsi
ulivyochanganyikiwa wakati ule alipokuwa na mipango na kaka yake. Kuwa makini
sana.” Mama G akasimama na kuondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~
Geb
alielewa kila kitu. Ni Grace! Grace pacha mwenzie. Grace aliyehangaika naye
kwenye biashara ile mpaka sasa imekua! Grace ni jukumu alilokabidhiwa na baba
yake tokea mdogo! Haitaji kuomba ushauri akitaka kumsaidia. Kwa nini? Mbona ni
jambo la kueleweka tu! Geb aliwaza. Akili ikamkumbusha vile alivyochanganyikiwa
baada ya kujua James anataka kumsaidia Nanaa, kununua gari na kufanya naye
biashara. Taratibu akajirudi. Akakumbuka ule wivu aliojisikia na kuona James
anamwingilia kwenye mambo yake. Kweli akaona hamtendei haki Nanaa. Akanyanyuka
kwenda chumbani.
~~~~~~~~~~~~~~~
Alimkuta
Nanaa ndio anatoka chooni. “Vipi?” “Naona leo nimekuwa na siku ndefu.
Sijatuliza mawazo. Nimeshituka sasa hivi na kunywa dawa ya usingizi ili nilale
kabisa niweze kutulia. Na pressure nayo nimepima naona imepanda kidogo.”
Akapanda kitandani. “Lakini nitalala tu. Nimeshajisaidia kabisa, ili nikilala
nilale nisiamke tena.” Geb akakaa pembeni ya kitanda. “Nikuletee kitu chochote
cha kula?” “Hapana. Nipo tu sawa. Usiku mwema. Acha nipumzike tu.” Akajilaza.
Ni kweli Geb akamuona amekuwa mtulivu zaidi. Akajua aliyozungumza mama yake ni
kweli.
“Basi
na mimi ngoja nisafishe meno, nakuja tulale.” Geb akaenda maliwatoni, kurudi
Nanaa alishakuwa amelala. Akabaki akiwaza. Afanye nini! Amuombe ruhusa
yakumnunulia dada yake nyumba!? Yalikuwa ni maisha mageni ambayo hata hakuwahi
kufikiria kuja kuyaishi. Anatafuta pesa yake kwa shida sana. Halafu leo aje
aanze kuomba ruhusa jinsi ya kutumia!? Akakumbuka maneno ya Man ya asubuhi
hiyo. Juu ya kuhangaika maishani. Unafanikiwa. Unaoa mwanamke, unaishi naye
mwaka mmoja tu, anataka muachane halafu mahakama inaamuru mgawane mali! Geb
akabaki akifikiria.
Lakini
akajua kipimo hicho hicho anachompimia Nanaa, ipo siku na yeye atampimia na
hatakuwa na haki yakuuliza. Swali likawa je, yupo tayari kuishi kwenye nyumba
moja na famle mbili tofauti!? Nanaa ahangaike kivyake na watu wake, na amgawie
amtakae bila kumuuliza? Geb akabaki akijiuliza na kujijibu mpaka akapitiwa na
usingizi.
Alhamisi.
Nanaa aliamka asubuhi na kufuata ratiba yake kama
kawaida, akamlisha mtoto na yeye akala. Alipomlaza Magesa, akarudi chumbani kwao. Alimkuta Geb
ameamka, ila yupo tu kitandani. “Vipi?” “Narudi kulala tena. Najisikia
kuchoka!” Nanaa akajibu wakati anapanda kitandani. “Kuna maumivu yeyote?” Geb
akauliza. “Hata sijui!” Bado Geb aliona hana furaha. Akajilaza. “Nikuulize
kitu Nanaa?” “Mmh!” “Nimekuudhi?” “Kwa nini unafikiria
hivyo?” “Hapana. Nilitaka tu kujua. Maana usiku umelala bila kunisubiri.”
“Nafikiri nikuchoka tu. Halafu mambo mengi yanaendelea sasa hivi. Hamna
utulivu. Nawaza hili na lile. Kwa hiyo nafikiri akili imeanza kuchoka. Nalala
kwa haraka.” “Kama ningekuwa nimekuudhi, ungeniambia?” “Kama ni jambo la
kuzungumzika, ningekwambia tu ili tuwekane sawa.” Nanaa akajibu kwa jumla.
“Kwa
hiyo kuna mambo naweza kukuudhi na ukashindwa kuniambia kwa sababu
hayazungumkiki?” Nanaa akafikiria kidogo. “Sijui. Ila nitajua siku itakapotokea
na kushindwa kukwambia. Sasa hivi sijui. Ila mimi najua kuna mambo mengine
wakati mwingine hayana majibu ya papo hapo yanahitaji muda. Halafu Geb, mimi na
wewe tumetoka katika ulimwengu miwili tofauti. Kuna mambo hata kama utanioa,
huwezi kuyaelewa ila kaka James tu. Hivyo hivyo wewe. Kuna mambo utakuwa huru
kwa Grace na mama kuliko mimi. Kwa kuwa unajua watakuelewa kwa haraka na
kukushauri kwa haraka. Kwa hiyo kujibu swali lako nafikiri mimi na wewe tuna
mambo fulani fulani hata kama tunapendana, lakini hatuwezi kukaa chini pamoja
tukayazungumza. Na hatuwezi kuepuka hilo.” Kimya. Lakini yale maneno
yalimwingia Geb mpaka moyoni. Akapata ujumbe wake.
“Baadaye
nitatoka kwenda kufanya kile kikao kama tulivyozungumza jana.” “Ni vizuri.”
Nanaa akajibu kwa kifupi tu. Akajigeuza mara kadhaa. “Vipi?” “Nampanga Jimmy,
ili nilale.” Akatulia. “Nilikuwa nikifikiria kumsaidia Grace kununua ile
nyumba.” “Nilikusikia jana pale kwenye kikao. Hongereni sana. Naamini Mungu
atawasaidia kufanikisha.” Nanaa akajibu. Geb akabaki kimya. “Uji upo tayari
kama njaa ikianza. Nimekuwekea kwenye chupa na bakuli kubwa. Nataka nilale tena
kidogo.” “Umeangalia pressure?” “Sikutaka kujinyima raha. Ila nimekunywa dawa.
Nitakuwa sawa tu.” Nanaa akalala.
Kikao Cha Pili.
Kikao kilianza ila kama walivyopanga mwanzoni tu, wakafungua mkoba wenye pesa. Sara alikuwa kama amechanganyikiwa baada ya kuona mamilioni ya pesa, tena tasilimu, yamepangwa kwenye mkoba, halafu eti zikiwasubiria wao! Danny alipotaka kukataa, Sara akamshangaa sana. Geb akatumia akili ya haraka sana. Akawashauri wakapate muda nje ya hapo wakazungumze. Mpaka wanarudi ndani, Danny alitaka alipwe akaanze maisha yake sehemu nyingine. Mwanasheria wa Grace alimwambia ni heri akubali hiyo pesa kuliko wakifikishana mahakamani, atatakiwa kumwachia Grace nyumba na atatakiwa pia kumpa Grace pesa ya matumizi kila mwezi. Alipofikiria, na Sara alipoongeza nguvu na kuthibitishiwa na mwanasheria wake kuwa ni kweli, akaona heri achukue hiyo pesa akaanze kwake. Kwanza itakuwa mbali na kina Geb. Mpaka inafika saa tano asubuhi ya siku hiyo, nyumba ikawa kwa jina la ‘Grace Magesa’.
“Asante sana Geb. Nakushukuru sana kaka yangu.
Sijui niseme nini!” Grace alijikuta machozi
yakimtoka mara baada yakutoka kuandikishana na Danny. Alikubaliwa kuchukua
watoto wake mara baada ya kurudi safari na baba yao. Na nyumba ilishakuwa yake.
Hakuwa na jinsi yakumshukuru Geb kwa pesa yote aliyomlipia na kusimama na yeye mpaka
mwisho. “Cha kwanza ujue unastahili. Ile nyumba ni yako. Nilikuona jinsi
ulivyokuwa ukihangaika nayo. Cha pili, umesimama na mimi G, tokea naanza ile
biashara mpaka sasa. Hayo ndio matunda yake. Hongera.” Grace akabaki kama
akifikiria.
“Nini
tena?” “Naomba tukae sehemu tuzungumze.” Alikuwa Grace na Geb tu. Wakaenda
kukaa kwenye gari. “Nampenda Man.” Geb akacheka. “Nafikiria hata akitaka kuja
kunioa, sitafikiria mara mbili. Itakuaje?” “Kuhusu nini?” Geb akamuuliza akiwa
anajua kabisa ni nini anafikiria. “Maisha yetu sisi wawili.” Grace akaanza
kulia.
“Hatujawahi kutengana Geb.” “Na
wala hatutatengana.” “Man anaishi
Arusha. Amejijenga sana kule. Na wewe umejijenga sana huku. Siwezi kuishi mbali
na Man wala wewe. Nitafanyaje?” Geb
akacheka. “Naomba utulie G. Kuna mambo mengine hayana majibu kwa haraka. Lakini
mimi nataka kukuona unafuraha. Nataka kukuona upo kama ulivyokuja na Man. Full of yourself. Na kwa kuwa yeye ameweza kukufanya hivyo,
nakushauri usiachie hiyo nafasi endapo atakutaka kwa ndoa.” Grace akamwangalia.
“Na
kazini?” “Kumbuka na mimi naoa Grace. Mungu amenipa Nanaa. Anaakili na
anajituma. Akishajifungua, nitampa kazi zako. Atakuwa anazifanya nyumbani. Kwa
hiyo usiwe na wasiwasi. Mungu amenipa msaidizi. Na wewe ukawe msaidizi huko.”
Grace akacheka. “Hicho ndicho kilikuwa kinaniumiza kichwa.” Grace akafikiria
tena kidogo. “Ila umebadilika Geb! Umekuwa na akili za kiutuuzima kwa kweli. Mungu
akufanikishe kwenye ndoa yako.” “Amina. Usiache kuniombea.” “Siwezi Geb.”
Wakarudi nyumbani.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Naona
unacheka.” “Namshukuru Mungu mama. Amenitetea. Namshukuru na Geb. Amenirudishia
nyumba yangu na watoto. Wakirudi tu kutoka safari, wananipa watoto wangu.”
Nanaa alikuwa amejilaza kwenye kochi. Geb moyo ukampasuka baada ya dada yake
kusema anamshukuru kwa kumrudishia nyumba yake. Nanaa hakuwepo kwenye
picha. “Sara aliposikia mamilioni ya
pesa, Danny akataka kukataa. Naona akaenda kumpanga. Akarudi anataka pesa.
Halafu hapo wanasheria wote wakamuogopesha kuwa anaweza kukosa vyote. Geb
akamkabidhi ule mkoba wote wa zile pesa. Ungemuona Sara alivyofurahi!” “Mimi
namuhurumia sana Danny. Anajizika mwenyewe! Hana mshauri. Waliomzunguka wote
hawana akili.” “Na alivyomjuaji yule, atawapa wapambe wake zote, aanze upya.
Lakini haanihusu tena. Sasa hivi nipo huru mama. Ngoja niende zangu kwa Man,
nimemuachia watoto. Tutakuja baadaye tukisharudisha watoto kwa Danny, ndipo
tuje kujiandaa kwa safari.” Grace alikuwa amechangamka kweli.
“Vipi bibi
harusi wangu?” Nanaa akacheka. “Hongereni kwa kufanikisha kila
kitu.” “Mbona sasa hujachangamka wakati harusi kesho kutwa?” “Nasinzia hapa,
kama mlevi!” “Vipi pressure lakini?” Geb akauliza. “Mama amenipima, nashukuru
Mungu imeshuka. Tangia ulivyoondoka nilikuwa
nimelala, ndio nimeamka muda sio mrefu.” “Afadhali. Sikutaka usafiri
ikiwa ipo juu.” Wakatulia. “Sisi tupo tayari. Kila kitu kipo kwenye gari.
Nilikuwa naweka kimoja hadi kingine kuanzia asubuhi ili nisisahau. Sasa wewe
usitucheleweshe.” “Siwezi mama. Usiwe na wasiwasi.” Grace akatoka.
~~~~~~~~~~~~~~~
Baada
ya yakurudisha watoto na kuweka mambo yake sawa, Grace aliwapigia simu kina Geb
kuwataarifu wao wapo tayari, wakutane uwanja wa ndege. Geb aliwasindikiza
familia yake mpaka uwanja wa ndege. Nanaa alikuwa akiondoka na watoto wote,
pamoja na mama G. Alikaa kiti cha mbele akiwa ametulia kimya. Geb alikuwa
akizungumza na mama yake wakati Nanaa amevuta kiti nyuma, amejilaza. Dawa za
usingizi alizokunywa mchana wake zakusaidia kutulia ili pressure isipande
ilikuwa sababu tosha ya Nanaa muongeaji kuwa kimya. Man aliwaahidi watapata mtu
wa kuwasaidia kazi huko waendapo. Kwa hiyo wasihangaike swala la mfanyakazi.
Grace na Man walikuwa wakiendeshwa na Jeri ambaye alitakiwa kurudisha gari ya
Grace na kesho yake achukue gari hiyo yenye mizigo ya Nanaa na watoto wake,
awafuate Arusha.
~~~~~~~~~~~~~~~
v Ndoa ya Grace na Danny imeisha rasmi. Kwa
haraka kila mmoja kati yao amepata alichokuwa akitaka. Penzi na pesa. Danny anaye Sara. Grace anaye mwanaume wa nguvu, Man. Mwanaume wa ndoto zake. Kama mwanaume aliyekuwa akimtaka tokea utoto. Mungu ampe nini? Kaka yake amemnunulia
nyumba na watoto atapewa baada ya kurudi safari.
Furaha ya watoto wao je? Hatima yao?
v Nanaa amekubali kwa hakika wao ni wamapenzi tu. Hawezi kuingilia
mahusiano ya Geb na ndugu zake. Hata hivyo alimkuta yeye na dada yake
wakihangaika pamoja kuzisaka pesa. Anaanzia wapi? Kinachomchanganya na kumfanya
akose raha ni pale Geb anapomzuia na yeye kuwa na mahusiano na kaka yake.
Ni kwa nini? Kukubali
kuingia kwenye aina hiyo ya ndoa ni sawa? Itampa uhuru au ndio kifungo? Akakumbuka
ugomvi alioanzisha Geb juu yake na kaka yake. ‘Akinioa
je?’ Ndio swali
alilokuwa akijiuliza Nanaa akiwa njiani kuelekea uwanja wa ndege ili waende
Arusha kwenda kufunga pingu za maisha.
v “Kweli hizi
zinaweza kuwa pingu za maisha!” Nanaa akaendelea kuwaza.
Akajiangalia tumbo la mtoto aliyebeba. “Inamaana mimi na huyu mtoto wa Malii
tutaishi kwa kudra za Geb tu!? Hataniruhusu nijishugulishe wala kufanikiwa
wakati yeye na ndugu zake wanastawi!”
Nanaa aliendelea kuwaza wakati Geb akiendelea kukanyaga mafuta kuelekea
uwanja wa ndege.
Ni
Nini Kitaendelea? Usipitwe.
0 Comments:
Post a Comment