Geb
alikuwa amemuweka Magesa begani, Liv amemlalia mama yake. Wote wamevaa nguo zao
zakulalia tayari kwa kwenda kulala baada ya salamu na anti yao. Geb akasimama
kwenda kufungua mlango na kuwakaribisha. Walimsikia Geb akisalimiana nao hapo
nje. Grace akatoa utambulisho. “Geb, huyu ni Manase au Man kama wengi
walivyozoea kumwita. Na Man, huyu ni Geb. Magesa mkubwa na huyu ndio Magesa
Jr.” Wakasikia wakisalimiana. Mwishowe wakaingia ndani.
Alipomuona
tu Man, mama G akainama na kuguna huku anatingisha kichwa. Grace akaanza
kucheka. “Sasa mama unaguna nini jamani!?” “Mie huyu? Akuu! Nasafisha koo.
Karibuni.” Kila alipokuwa akiwatizama vile walivyosimama pamoja, tabasamu
lilimjaa mama G. Man alikuwa na umbile na muonekano kama ndoto za Grace. Aina
ya mwanaume aliyekuwa akimwambia mama yake ataolewa naye.
“Karibu baba.” Mama G akampa
mkono akiwa amekaa. “Asante mama. Shikamoo.” “Marahaba. Poleni na safari.”
“Asante. Lakini safari yenyewe ilikuwa fupi. Hatujachoka.” “Afadhali.
Karibuni.” Mama G akarudia. “Asante.” Man akajibu kwa heshima zake zote. “Na
huyu ndio mama mwenye nyumba wetu. Mke ya Geb! Mama Magesa mwenyewe.” Grace
akaendeleza utambulisho. “Nanaa?” Man akauliza. “Haswaa!” Wakacheka. “Karibu
Man.” Wakapeana mikono lakini Nanaa alikuwa amejiegemeza kwenye kochi. “Ningesimama. Lakini unaliona lile jicho la
mama pale? Basi kunyanyuka hapa labda kwenda msalani tu, si vinginevyo.” Nanaa
aliongeza. Wakacheka kidogo. “Grace aliniambia unatakiwa mapumziko. Usiwe na
wasiwasi, hata kule Arusha, tutahakikisha unapata mapumziko yakutosha tu.” Man
akaongeza. “Asante. Karibuni sana. Nimefurahi kukuona Grace. Nilikuwa na hamu
na wewe?” “Hata mimi Nanaa. Naamini
ulipata salamu zangu zote.” “Geb alizifikisha.” Grace akainama na kumkumbatia.
“Geb
ameniambia presha ipo juu kidogo.” “Ndivyo tulivyoambiwa. Lakini wala sijisikii
vibaya! Ila tumeona tufuate tu kile wanachotuambia ili tusogeze siku.” “Pole
sana.” “Asante. Umependeza sana Grace. Unaonekana unafuraha tofauti na
nilivyokuona mara ya mwisho!” “Namshukuru Mungu. Ni neema tu Nanaa. Najua wewe
unajua.” Nanaa akacheka, Liv akambusu mama yake pale alipokuwa
amemuegemea.
“Umemsahau mama mzazi! Ndio
anakukumbusha hivyo.” Mama G akaongeza. “Nampenda mama.” “Hata mimi nampenda
Liv. Umemuona aunt?” Liv akacheka huku akitingisha kimguu chake. “Anasubiri
busu lake hivyo!” Nanaa akaongea naye kwa upendo. Liv akasimama pale kwenye
kochi. Grace akamkumbatia na kumbusu. “Ngoja nikubebe kabisa. Nilikuwa na hamu
na wewe Liv!” “Nampenda aunt.” Liv akaongea kwa kudeka. “Na mimi nampenda Liv
wangu.” Akamkumbatia. “Msalimie anko.” Liv akamchungulia Man, akarudisha kichwa
kwa aunt yake kwa haraka. Wakacheka.
“Kwa
maringo huyo! Msalimie anko bwana.” Mama yake akasisitiza, lakini Liv akagoma.
“Mpaka amzoee.” Grace akamtetea. “Karibuni jamani. Twendeni moja kwa moja
mezani. Wote hatujala tulikuwa tunawasubiri nyinyi.” “Poleni. Nilijua mkila tu
mtapata usingizi na mimi nilitaka kuwaona.” “Hamna shida.” Nanaa akaongeza.
“Ngoja nikawalaze hawa. Kesho mtapata nao muda vizuri. Sasa hivi watakuwa
wamechoka. Wamekuwa na siku ndefu. Tuliwapeleka kwa James pia.” Geb akaaga.
“James anaendeleaje?” Grace akauliza.
“Anaendelea vizuri. Amesema atakuwepo kwenye harusi yetu.” “Afadhali.” Grace
aliitika.
“Naomba
kumsalimia Magesa. Kama yeye atakubali.” Man alimuwahi Geb. “Man anapenda sana
watoto. Yeye ndiye aliyeomba kuona watoto.” Grace akaongeza. Geb akamsogezea
Magesa. Akambeba. Alikuwa ameshasinzia. “Kaka
Mkubwa huyo!” Man akasifia. “Mwili ndio mkubwa kuliko umri.” Geb aliongeza.
“Halafu wanafanana sana.” Man akaongeza. Liv alikuwa akichungulia tu. “Kesho
utacheza na anko?” Grace akamuuliza Liv. Akacheka tu bila kukubali au kukataa.
“Eti Liv? Tutacheza wote?” Man akauliza, Liv akajificha kwa aunt yake.
Walimuona
Man akimbusu Magesa kwa upendo mara kadhaa. “Na mimi nina mtoto mmoja wakiume.
Nilimlea tokea siku anazaliwa. Mimi mwenyewe. Alikuwa na rangi kama huyu, ila
hakuwa mkubwa hivi.” Man aliongea huku akimsugua Magesa mgongoni taratibu na
kwa upendo. “Napenda sana watoto.” “Sasa hivi ana umri gani?” Nanaa akauliza.
“Atakuwa amekuwa kijana mkubwa sasa. Mama yake alimchukua. Sijamuona zaidi ya
miaka 8 sasa.” Man aliongea huku akimtizama kwa upendo na kumpapasa mgongoni
Magesa. “Watoto wanasiri kubwa sana. Labda ndio maana Yesu alisema kama
tusipokuwa kama watoto, hatuwezi kurithi ufalme wa Mungu.” Man aliongeza taratibu
huku akiendelea kumpapasa Magesa na kumtizama.
“Hongereni
kwa watoto wazuri.” Man akaongeza kisha akacheka. “Grace aliponiambia mnawatoto
watulivu, nikapata shauku yakuwaona. Nilikuwa na hamu yakubeba mtoto hivi.
Yaani nimshike mkononi halafu atulie kama huyu au kama hivyo Liv. Maana ukoo
wetu una watoto hao! Huwezi kuwagusa.” Grace akacheka. Akakumbuka watoto wa
Malisa. “Yaani kama ungeingia hapa, ndio ikawa ndio kwao, na wao wapo ndani,
vile umegonga kengele, unafunguliwa mlango na wao wanakusukuma hapo hapo
mlangoni. Wanashindana kutoka hapo mlangoni na wewe mgeni umesimama hapo hapo,
ili wawahi nje wakaruke ruke. Kama hujakaa sawa hapo mlangoni, umesimama
kihasara halafu hufahamu kama kuna watoto wa namna ile pale, unaweza kuanguka
hata ndani hujaingia! Hawana mchana, wala usiku wale watoto!” Wote
wakacheka.
“Huwa
tunamuuliza mama yao anachowalisha wale watoto, hamna anayeamini. Watoto wako
kama vipepeo!” Wakazidi kucheka. “Ni hali ya utoto tu.” Nanaa akatetea. “Mmh!
Muulize Grace kama wale watoto ni wakawaida. Anawajua. Wakiwepo mahali, huitaji
kuuliza. Mpaka hamu ya kuwashika inakuja na inaisha, hujawaweka mkononi!
Angalau hawa wanashikika. Kesho lazima kulazimishia undugu. Eti Liv?” Man
alizunguka akaenda kumchungulia. Liv akacheka.
“Unaonekana
wewe ni mtoto mzuri sana, Liv. Unanywele nzuri kama za aunt. Nani amekusuka?”
“Mama.” Liv akajibu huku akijishika kichwani. “Jamani mama anajua kusuka!” Liv
akatingisha kichwa. “Nampenda mama.” Liv akaongeza kwa upole. “Hata mimi
nampenda Liv.” Man akaigiza. Liv akacheka huku anatingisha kimguu chake, kidole
kimoja tayari mdomoni. “Hapo mtapatana. Anavyopenda kupendwa huyo!” Bibi yake
akaongeza. “Umbebe kama hivyo halafu
umkumbatie na kumwambia maneno mazuri kwa sauti iliyotulia, hapo mtaelewana.”
Bibi yake akaongeza, wakacheka.
“Basi
kesho tutacheza wote. Sawa Liv?” Liv akatingisha kichwa kukubali. Man
akafurahia sana. “Kwani wewe unajua
kucheka mpira?” Man akamuuliza. Liv akatingisha kichwa akikubali huku anacheka,
kidole chake kimoja bado kilikuwa mdomoni. “Nacheza na dad wangu!” Liv
akaongeza kwa sauti ya kitoto na upole. “Basi utanifundisha na mimi.” Liv
akatingisha kichwa kukubali. “Asante sana Liv. Basi nitakuja kesho
unifundishe.” Liv akakubali huku anacheka. “Umekazana mpaka umekubaliwa!” Grace
akamtania. “Si mchezo. Na ameniongelesha bwana!” Man akajibu. Wakacheka kidogo.
“Nakushukuru sana Geb. Asante.” Akamrudisha Magesa kwa baba yake, wakaenda
kuwekwa kitandani, Grace akisaidiana na kaka yake. Waliongozana Grace akiwa
amembeba Liv, Geb amembeba Magesa.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Geb
na Grace wakarudi baada ya kulaza watoto, wakahamia mezani. Baada ya kuombea
chakula, Nanaa akawakaribisha. “Jamani naomba nishukuru kwa kunikaribisha
nyumbani kwenu.” Man akaanza kabla ya kula. “Karibu.” Geb akajibu. Wakajua Geb
ataendelea lakini akawa ndio amemaliza. “Anzeni wageni kupakuwa.” Nanaa
akasogeza vyakula upande wao. “Nikupakulie nini?” Man akamuuliza Grace. “Kila kitu. Zaidi ndizi. Napenda ndizi
anazopika Nanaa.” Man akacheka kidogo.
“Haya
mama. Nitazila na mimi.” “Ndio utaamini hata
Yusufu haoni ndani.” “Naona hata harufu inavutia.” Man alishachukua
sahani akampakulia Grace na kumuwekea mbele yake. Nanaa akamkonyeza mama G.
Mama G akatulia tu anajiangalizia. “Kina vutia kwa macho na kinaonekana ni
kitamu sana!” Man akaendelea kusifia. Hakuna ugumu kama kufika ukweni. Tena
ikawa ni nyumbani kwa kina Geb! Wazito kuongea. Wasikilizaji tu.
“Kwa
hiyo Man wewe unaishi Arusha?” Ikabidi Nanaa aulize. “Ndiyo. Nipo hapo Arusha
kwa sasa.” “Ooh! Vipi Arusha? Unapaonaje kulinganisha na Dar? Au kwa nini
Arusha?” Nanaa akaendelea. Wakacheka. “Nanaa kwa kupenda stori!” Grace
akacheka. “Mimi heri niulize tu. Maana namjua mpenzi wangu. Hataongea hata neno
moja. Mpaka Man anaondoka humu ndani, tutakuwa hatujamjua.” “Basi hapo
mtakutana na Man. Anapenda stori huyo!” Wakacheka. “Hamna shida.” Man
akaongeza.
“Nisimulie mwaya Man.” “Basi hapa tutakesha. Hamalizi huyo maswali! Ukimwendekeza huyo, utajuta kuja usiku hapa.” Mama G akaongeza, wakacheka. Nanaa akacheka sana. “Nimeuliza maswali mawili tu jamani!” “Mengine yanakuja. Mimi nakujua wewe. Akijibu hilo, anajingine.” “Hamna shida mama. Ndio mwanzo wakufahamiana.” “Haya baba. Endelea.” Wakacheka.
“Wazazi
ndio walipata ufunuo wakuwekeza Arusha. Walikuwa na hoteli moja ambayo ndiyo
hapo mtakapofungia harusi. Baba alipougua ndipo akanikabidhi mimi. Na kwa
bahati nzuri na mimi ndio nilikuwa nimerudi nchini kutoka Sweeden ambako
nilikuwa nikiishi huko. Na ndiko nilioa na kupata huyo mtoto ambaye nilimwacha
kwa mama yake hukohuko Sweeden.” Man akaendelea.
“Kwa
haraka, Arusha haukuwa mji ambao ningefikiria kuishi kwa wakati ule, lakini
majukumu yakanifanya niwepo. Nilirudi nikiwa sina chakufanya. Kwa hiyo biashara
ya hoteli ndiyo ikawa nafasi pekee yakujishugulisha. Kwanza kusaidia wazazi,
pili hata mimi mwenyewe. Lakini kadiri siku zilivyokuwa zikizidi kwenda ndivyo
nilivyoona kuna nafasi ya kuwekeza zaidi hapo jijini. Nahisi nikanogewa.
Nimewekeza zaidi kwenye huo mji.” “Hongera. Kwa hiyo biashara kubwa hapo
unayofanya ni hoteli?” Nanaa akauliza na kufanya kila mtu acheke.
Man
akameza huku anacheka. “Chakula nikizuri sana.
Grace umeshinda. Kweli hii ndizi ina shahada zote. Asanteni jamani!” Man
alionekana mtu wa shukurani sana. “Karibu.” Nanaa akajibu. “Ni rudi kwenye
swali. Biashara hiyo ya baba, iliibua ideas
nyingi ambazo nimefanyia kazi baadhi na nyingine bado. Naendelea taratibu.
Niliweza kufungua hoteli nyingine mbugani. Ndiko tulikuwa huko na Grace mpaka
siku tatu zilizopita.” “Ni pazuri sana. Naamini siku moja na nyinyi mtakwenda
kupaona.” Grace akasifia, Man akacheka.
“Asante
Grace.” Man akamtizama kwa upendo kama kitu cha thamani na tabasamu usoni.
Nanaa akamkanyaga tena mama G, kama kumkonyeza. “Kwa hiyo Nanaa. Mbali na hizo
hoteli, nikafungua kampuni ya utalii hapo hapo Arusha na usafirishaji pia. Ili
kuhakikisha wageni wanaofika hapo kwa utalii, wanapata usafiri wa kuwapeleka
kwenye hoteli zetu na kuwatembeza hapo mjini.” “Waw! Hongera Man.” Nanaa
akasifia. Geb na mama yake kimya.
“Kwa
hiyo huko ndiko mlikokutana na Grace?” Nanaa akaongeza swali lililowafanya wote
wacheke mpaka Man. “Si nilikwambia? Hapo ndio ameanza huyo.” Mama G akaongeza.
Geb akacheka huku akimwangalia Nanaa. “Eti Geb? Hilo ni swali baya?” “Hapana
Nanaa. Unafanya vizuri kuuliza ili ujue.” Geb akaongeza. “Si umeona hata Geb
hana wasiwasi. Tuendelee mwaya Man.” “Naomba mimi nimjibie Man ili ale.” Grace
akaingilia. “Mimi naomba nimsubirie tu
Man, bwana! Wewe Grace mvivu wa kuongea. Utanijibu kwa kifupi sana.” Walicheka,
mpaka Grace akapaliwa. “Nanaa wewe!” “Kweli Grace. Usinielewe vibaya. Wewe upo
kama Geb. Mnajibu maswali tu, bila stori ya ziada.” “Sasa wewe ulitaka kujua
nini?” “Kila kitu.” Nanaa akajibu. “Nanaa wewe mtoto!” Mama G akaongea huku
anacheka.
“Haya
Nanaa. Mimi nilioa mwanamke wa ki Swedish. Huko huko Sweden. Ndoa iliisha miaka
6, kabla sijarudi nchini. Na niliishi kwenye ndoa ambayo nilitamani kuja kuoa
nyumbani. Lakini baada ya mikasa mingi sana ya huko ugaibuni, nikakinahiwa hata
ndoa. Kwa kujibu swali ambalo najua ungekuja kuuliza, nilioa na nina mtoto
mmoja. Kama nilivyokwisha kusema. Na ndoa ilidumu kwa miaka 4, ikaisha kwa
talaka.” Wakacheka.
“Nilirudi
nchini nikiwa na maumivu makali mno. Akili na mawazo yangu yote nikawekeza
kwenye biashara. Ndio maana umenisikia nina miradi mitatu ambayo ni kama yote
inalenga watalii tu. Sasa maisha yangu yalikuwa wazazi na kazi. Nikisema wazazi
ni huku Dar. Ilibidi baba kuhamia huku jijini kwa ajili ya kuwa karibu na
madaktari wake. Kwa hiyo nikiwa hapa Dar, ujue nipo kwenye kifamilia na
nikipanda tu ndege, akili inarudi kikazi.” Man akacheka.
“Nina
mtindo nikiwa kwenye ndege au hapo uwanja wa ndege kabla sijapanda ndege,
tukiwa kwenye kusubiria, huwa naangalia abiria kwa makini ili kupata wateja.
Endapo nikigugundua wewe ni kuku mgeni, basi nitajitahidi kukushawishi ushukue
kwenye hoteli zetu, kuhu nikikuuzia huduma zote nilizonazo.” Man akamwangalia
Grace akacheka tena kidogo. “Wewe ni mchokozi Man. Huna lolote.” Grace
akalalamika.
“Hapana
bwana.” Man akajitetea. “Haya basi. Nikamuona Grace. Kwanza nikavutiwa na rangi
yake. Nikataka kumsemesha, nikaona ukimya kama huu aliosema Nanaa. Nikaona
nitulie mpaka kwenye ndege. Wale wahudumu wa ndege nimezoeana nao sana.
Tulipangiwa viti mbali mbali, nikaomba nihamishiwe alipo kaa Grace. Nia ya
kwanza ilikuwa nimuuzie huduma zetu. Kwa kuwa nilimuona ananukia pesa. Nikajua atamudu
huduma zetu. Lakini nilipohamia kukaa naye pale. Nikasahau hata mambo ya
biashara. Nikawa kama nishachanganyikiwa. Kwanza alinipuuza. Nikahangaika wee
mpaka akanigeukia. Wewe fikiria mtu mmekaa naye kiti kimoja, anakujibu bila
kukuangalia! Nikajua nimepuuzwa. Nikahangaika wee, mpaka nikaazima gazeti la
jirani ili nimpe yeye ili tu anigeukie anitazame!” Watu wote wakacheka.
“Sasa
kule kuangaliwa ndiko kukanifanya nisahau sasa mambo ya biashara. Nikawa kama
nimepigwa na bumbuwazi. Sijui niseme nini! Sasa kabla hata…” Man akainama na
kuzidi kucheka. “Uchokozi tu umekujaa! Eti mimi nilimuwahi nikamwambia mimi
ni mke wa mtu na nina watoto watatu. Basi ndio mpaka leo hayaishi!” Man
aliendelea kucheka mpaka wote wakaanza kucheka. Alikuwa anacheka huku
anamwangalia Grace.
“Bwana
Grace alinipiga stop! Mpaka nikaishiwa nguvu.” Man alizidi kucheka mpaka
machozi. “Ukiangalia kidoleni hana pete! Akajishtukia.” “Waliniibia pete zangu,
cheni na hereni zangu zote za dhahabu pale nyumbani. Hata mama nilimwambia.”
“Sawa Grace, lakini sasa mimi wakati ule ningejuaje? Ungeniacha hata niongee
mpenzi wangu. Sio vile ulivyonishushua.” “Mimi nilikuwa nakutahadharisha
bwana.” “Sasa ikawaje?” Nanaa akauliza.
“Basi
hapo mmekutana na Man. Anapenda stori huyo! Na hamalizi jambo. Na anachekaga
mwenyewe kwenye stori zake, yaani mpaka wewe msikilizaji hata kama hukuwa na
mpango wakucheka utacheka tu.” Grace akaongeza. Wote wakacheka, maana kweli Man
alipenda kucheka.
“Basi
tena. Wewe si unajua vile Grace alivyo mtulivu. Kwanza kashaniwahi yeye mke wa
mtu. Nikamwangalia kidoleni makusudi, akajitetea ameacha pete yake nyumbani.
Ila ana watoto watatu wa kiume. Anazo picha zao. Haya tuone sasa hizo picha.
Akaingi mkobani. Akaanza kutafuta simu, akakumbuka na simu pia hana. Hapo ndio
nikamuona ameishiwa nguvu. Nikamuhurumia kweli! Maana alipooza mara mbili yake.
Lakini ndipo nikampenda Grace.” Grace akainama.
“Kwanza
nilifurahia kile kiwango cha uaminifu wake kwenye agano alilokuwa nalo na
mwenzie. Halafu hakujificha kwangu swala la watoto. Kile kiwango cha ukweli na
uwazi kwangu, ni kweli mama yangu, sijawahi kukipata kwa mwanamke yeyote tokea
nilipofika hapa Tanzania au hata kule nilipokuwa mpaka nikaoa. Kwanza nilioa
kwa kutegwa. Mwanamke niliyekuwa nimemuoa alinitega tena kwa kamera na
kuniambia lazima nimuoe ili asinishitaki. Nimekuwa nikikutana na wasichana
warembo tu, lakini tokea mwanzo wa hata salamu unahisi uongo mtupu.” Man
akaendelea.
“Sasa
kutokea pale, Grace akaamua kunikwepa. Lakini akajikuta amepanda taksi ya
kwenye kampuni yangu iliyomleta mpaka pale hotelini kwetu bila yeye mwenyewe
kujua. Kwa kuwa nilishaanza kuvutiwa naye, nikataka kuwa naye karibu tu. Ili
kufahamu aina hii ya wanawake kama bado wapo hapa duniani. Nakutaka kujua wapo
wapi ambako wenzetu wanafanikiwa kuwapata! Wanafanya nini na sisi tunakosea
wapi! Maana kwa majukumu niliyonayo ninakuwa nakutana na wanawake wa kila
namna. Washindanao urembo, mavazi, sijui nywele. Kila aina ya wanawake huwa
nakutana nao kwenye shugli zangu sababu hutumia huduma zetu zaidi kumbi ya pale
hotelini. Niliokutana nao haikuwa
kwa uwazi huo.”
Man akaendelea.
“Ndipo
nikaanza juhudi za kujisogeza sasa. Lakini Grace akawa ananikwepa kitu
kilichozidi kunishangaza. Huwa natafutwa kusalimiwa, lakini Grace akawa
ananikwepa! Akiniona sehemu hii hapa, anaondoka. Ndio shauku ikaongezeka kutaka
kumfahamu Grace. Naamini nimejibu swali lako.” “Haaah! Usinifanyike hivyo Man!”
Nanaa alilalamika kwa huzuni sana. Kila mtu alicheka tena. Man alikuwa akicheka
huku akimwangalia Nanaa. Alicheka na kucheka mpaka wote wakaanza kucheka
tena.
“Nimalizie
tu.” “Acha mwenzio akapumzike Nanaa.” Mama G akaingilia. “Kwani Man umechoka?”
“Nilikuwa nakuchokoza tu.” Man akajibu. “Afadhali. Ehe?” Wakacheka tena. “Basi.
Baada ya kuhangaika sana nikafanikiwa kukaa naye meza moja akiwa ametoka kukaa
nje siku hiyo jioni. Ndio ukawa mwanzo wetu. Lakini nikajikuta mimi ndio nina shida
na Grace kuliko hata yeye. Nilikuwa nimebeba mambo machungu moyoni ambayo ni
Grace pekee aliyaweza kuyabeba na bado akanitazama kama mwanaume.” Man akainama
na kufikiria kidogo.
“Unajua
Grace anautulivu fulani hivi, ambao unaambukiza mtu yeyote anayebahatika kuwa
naye karibu, nakukufanya ujisikie umetulia. Ndio kitu nilikuwa nikihitaji. Usiku
wa kwanza kuwa naye baada ya kumtoa ili tukaangalie sinema, nikajikuta
nimeishia naye kwenye gari, nikitua mizigo yangu moyoni.Unajua kama vile
wakatoliki wanavyoungama kwa padre?” “Mimi nilikuwa nasali huko.” “Basi wewe
utaelewa zaidi. Basi ndivyo ilivyokuwa kwangu usiku ule kwa Grace. Niliongea
machungu ambayo sikuwahi kumwambia mtu yeyote hapa duniani, kwa aibu na kuhofia
fedheha. Hata mama yangu kuna mambo sikuwa nimemsimulia, lakini nikajikuta
nayaongea kwa Grace mpaka nikapata aghueni moyoni.” Grace alikuwa ameinama huku
akimwangalia mara moja moja.
Man
akamvuta mkono. Akamshika. “Najua watu wanaweza kusema ni mapema sana. Au
nimemfahamu Grace kwa muda mfupi sana. Haifai kusema mambo fulani juu yake.
Lakini kama nilivyomwambia Mzee Ole, kwa mara ya kwanza maishani ninaujasiri
wakusema nimependa. Sijui Mungu atanipeleka wapi mimi na Grace, lakini am in love for sure. Sina shaka juu
ya hilo. Na sina hofu kuonekana na Grace popote. Kwanza amebeba sifa za
mwanamke wa ndoto zangu. Hata familia yangu walipomuona Grace kwa mara ya
kwanza tu, walijua ni kwa nini yeye. Kuanzia rangi yake, utulivu, werevu na ile
heshima kwangu. Vyote vimenivutia kwake.” Man aliongea bila hofu.
“Mama
na Geb! Sijawahi kufika nyumbani kwa mtu au kwenye familia ya mtu kukaa kwenye
meza hivi kwa ajili ya binti yao. Lakini kwa Grace imenibidi. Nampenda Grace.
Tulitumia siku tano mfululizo kufahamiana tu. Najua Grace alipotoka, alipo, ila
sijui Mungu atakapompeleka kuanzia sasa. Ila nimemuomba Mungu niwepo kwenye
maisha yake. Sio kwa ajili yake Grace tu, ni kwa ajili yangu pia. Najua inaweza
kuwa ni kama kwake sio wakati muafaka kufikiria vizuri. Kufanya maamuzi fulani
fulani kwa sasa. Lakini nilimuahidi kumpa muda wa kufikiria. Baada ya mambo
yake kesho kukamilika, mpaka atakapojiweka sawa. Nimemuahidi kumsubiri mpaka
atakapokuwa tayari. Hata kama akitaka nisiwe karibu kabisa ili nisimsumbue
kwenye kufikiria. Lakini nilitaka kuwa naye kesho. Angalau niwepo tu kama
itatokea atanihitaji mara baada ya kumalizana na mwanasheria au kwenye kipindi
hicho.”
“Pia
sitawazonga. Kwa kuwa ameniambia Geb atakuwa naye. Mimi naweza hata kusubiria
nje. Akitoka na kuniambia yupo sawa, nitaondoka kabisa kurudi Arusha. Nipo hapa
kwa ajili yake tu. Mambo yakiwa sawa, nitaondoka kurudi Arusha kuendelea na
mambo ya maandalizi ya harusi yenu. Na baada ya harusi hata kama sitamuona kwa
muda ili apate muda wakufikiria zaidi pia nimemwambia nitasubiri. Sitaki
mfikirie nitamshawishi vibaya katika kipindi hichi. Nampenda Grace na
nimekusudia kuwa naye.” Man akaendelea.
“Najua
na ninaelewa anakopita sasa hivi kwa kuwa na mimi nilipita hapo. Najua maumivu
ya kutalikiwa na hofu ya kupoteza watoto. Kwa kuwa na mimi nilishapita hapo.
Tena kwa machungu makubwa sana. Hakuna jinsi
yakumuelezea mtu mwingine akaelewa. Ila mimi niliyepita naelewa.”
Man akacheka kidogo. “Najua Danny ni mume wa Grace. Na amemuumiza sana. Lakini
hata Grace nilimwambia kama ikitokea kesho Danny anamuomba msamaha na kutaka
warudiane walee watoto, na yeye akaona ni sawa moyoni mwake, pia asisite
kumkubali. Japokuwa nitaumia kumkosa, lakini pia nitamuunga mkono katika hilo
ili watoto wao wasiteseke.” “Na kama ataachiwa watoto wote?” Nanaa
akauliza.
“Nitamlea
Fili na wadogo zake bila shida. Na hilo nimemwambia hata Grace. Nimemwambia umuhimu
wa mama kwa mtoto. Lakini kama ni mama anayetaka watoto wake. Wapo wanawake
hawapendi watoto, jamani! Mimi nimeona. Lakini kwa kuwa Grace anapenda wanae,
natamani awe karibu na watoto wake na mimi nitakuwepo kumsaidia. Tumezungumza
naye. Ataenda kuomba kama Danny anaweza kumkabidhi yeye watoto. Achague siku
gani anazotaka kuona watoto. Ataletewa watoto bila shida, ili Grace alee watoto
wake.” “Basi wewe una upendo wa kweli.” Grace akacheka nakuinama. Wengine wakanyamaza. Mama G akabaki anafikiria.
Geb ndio na yeye akabaki kimya.
“Geb
wewe jamani!” “Nimesikia Nanaa.” “Sema basi hata kitu mpenzi wangu!” Nanaa akaendelea. Geb akacheka kidogo.
Akavuta pumzi. “Labda mama yeye ndio aseme. Mimi nasikiliza tu.” “Mimi
nimesikiliza. Labda nianze kwa kukushukuru kwa kumshauri mwenzio vizuri. Ni
kweli hatujui kitakachotokea kesho. Kikubwa ni watoto ndio wanao tuweka macho
hapa. Lakini mali si tatizo hata kidogo. Hizo zinatafutwa. Ila watoto! Ndio
kilio changu. Kwa hiyo nikuwaombea tu.” Mama G akaendelea.
“Unajua
Manase mwanangu, hakuna mama aneyemuozesha binti yake akiwa amejipanga kuja
kuona talaka, ila wajukuu. Haya mambo yametokea na kutushtua wote. Yamekuja
kukiwa na amani. Hakuna hata aliyejua kutakuwa na machafuko kama haya. Najua
Grace atakuwa amekueleza, lakini Danny kwangu hakuwa mkwe tu. Alikuwa mtoto
kama Geb. Tena alikuwa karibu na mimi kuliko ambavyo ungeweza kudhani. Tulikuwa
marafiki mno. Grace hana tofauti na Geb. Wana ukimya wakuzaliwa na wala sijui
wamepata wapi! Lakini Danny ndio alikuwa rafiki yangu. Kinachotokea kesho si
kuvunjika tu kwa ndoa ya Grace rasmi, kwangu mimi ni kama msiba. Kuzika mtoto
wakumzaa. Ni mtoto yatima ambaye nilimchukua kwangu kama mtoto.” Mama G
aliongea kwa huzuni.
“Pole
sana mama. Poleni sana.” Man alitoa pole. “Nashukuru. Kwa hiyo naungana na wewe
Man. Najua alikotoka Grace, alipo, lakini sijui kesho yake. Anakopita sasa hivi
ni maumivu makubwa sana kwangu. Hasa nikijua vile alivyojitunza na
alivyohangaika na Danny huku wanaume wenye uwezo wakimsumbua, najuta sana.
Najuta kutoa baraka zangu kwao kwa wakati ule. Najuta, lakini hata sijui
ningefanyaje! Nilimpa baraka zangu wakati ule nikijua ndio mwanaume anayeweza
kuja kuzikana na Grace. Sikujali uwezo
wa kimali. Lakini ona yanayotokea sasa hivi! Nafikiria wajukuu zangu. Naumia
nakujilaumu sana, lakini basi, tumuachie tu Mungu. Najiambia kama mimi yatima,
ambaye nilitupwa tu. Sikujua hata wazazi wangu au ndugu zangu walipo, nimeweza
kufika hapa, basi, namsihi Mungu aliyetenda kwangu, akatende na kwa wajukuu
zangu pia. Awarehemu wajuu zangu. Na kwa kuwa sisi wote tupo hapa, na endapo
Mungu atatujalia maisha marefu, naamini tutasaidiana tu ili wakue vizuri.” Mama
G akamaliza.
Wakamgeukia
Geb. Japokuwa mama G, hakutoa jibu la moja kwa moja, lakini walitaka kumsikia
na Geb pia. “Labda kwa niaba yangu na Nanaa, tukushukuru kwa kumsaidia Grace
kutuandalia harusi yetu. Najua una mambo mengi sana muhimu yakufanya, lakini
umesimama na Grace kufanikisha hilo. Na asante kukubali kunisimamia kwenye
harusi. Najua ni gafla, lakini ilikuwa lazima nimuoe Nanaa jumamosi.” Geb
akaongea. Nanaa akamkodolea macho Geb kama anamshangaa. “Naendelea Nanaa.
Sijamaliza.” Wakacheka kidogo.
“Namfahamu
Grace mpaka wakati mwingine huwa naogopa. Najua anapokuwa na furaha au huzuni.
Hata tukiwa tunaongea kwenye simu, au hata kama akiwa anazungumza na mtu
mwingine chumba kingine mimi nikiwa napita nje, nikisikia mazungumzo yao tu,
najua Grace yupo kwenye hali gani. Thanks for making her happy.” Geb aliongea taratibu lakini kwa hisia. Grace
akafuta machozi.
“Sijui
mtafika wapi, lakini ninaweza kusema, Grace huyu wa sasa au ambaye nilikuwa
nikimsikia kwenye simu, sijamsikia kwa muda mrefu sana kitu ambacho kilikuwa
kikiniumiza na kushindwa kujua mwisho ni nini. Grace amerudisha furaha na
kujiamini ambako alikupoteza muda mrefu tu bila yeye mwenyewe kujua. Niliona
mabadiliko hayo muda mrefu sana, na nilikuwa nikisumbuka moyoni bila kujua
jinsi ya kumsaidia. Lakini kwa muda mfupi tokea atoke hapa na kuniambia amefika
salama, amebadilika sana. Binafsi nimeshukuru. Kwa Grace huyu wa sasa, sina
wasiwasi na maamuzi atakayoamua kesho. Kwa kuwa hajajawa hofu wala woga.
Ataamua kutokana na anachojisikia yeye. Na Grace ananijua, kwa maamuzi yeyote
yale, mimi huwa namwambia ukweli bila kumficha. Na ikifika kwenye kutakiwa nichague,
huwa yeye anakuwa wakwanza. Namtanguliza yeye tokea tupo wadogo. ” Geb
akaendelea.
“Kama
alivyosema mama. Pesa haijawahi kuwa kipaumbele kwetu. Tokea hatuna kitu mpaka
sasa hivi Mungu ametubariki. Pesa haijawahi kuwa kipaumbele, ila utu. Danny
tulimfungulia milango yote, lakini akaja kumuumiza sana Grace. Binafsi sijali
anachofanya kwangu na mama, lakini kwa Grace na watoto ndicho kinachoniumiza
sana. Kwa hiyo naomba usirudie kufanya alichofanya Danny. Kama kuna
upungufu wowote kwa Grace, hata ukawa mdogo vipi, lakini ukauona na kufikiri
utavumilia tu, tafadhali mwache Grace. Mwache mapema kabisa. Habari
zakuja kusema ulivumilia hili au lile hapo baadaye, hapana Man.
Nasisitiza, usije kumuumiza Grace. Acha mapema. Usiishi naye kama unamsaidia yaani
unamuhurumia kwa hapa alipo sasa au kwa kumvumilia. Nimeishi na binadamu wengi
sana, lakini Grace ni mwema. Ni mwema mno. Mwema wakutokujitahidi. Ndivyo Mungu
alivyomuumba. Anastahili mema.”
“Nampenda Grace, Geb. I handle her with care.” “Ni kweli.” Grace akamtetea Man. Wakacheka.
“Basi Mungu awasaidie.” Geb akawa amemaliza.
Wakaendelea kuzungumza hili
na lile. Mpaka Grace na Man wakaaga.
“Grace!” Mama yake akamuita pembeni, wajitenge na Geb na Man pale walipokuwa
wamesimama nje wakizungumzia mipango ya harusi. “Tumekuandalia chumba hapa.”
Mama yake akamchokoza tu. “Siwezi kumuacha Man peke yake mama. Amekuja hapa kwa
ajili yangu. Sioni kama ni sawa kumuacha hotelini peke yake.”
“Grace wewe mtoto wewe!” Grace
akaanza kucheka. “Kwanza sasa hivi siwezi
kulala bila Man. Ananichezea nywele mpaka nalala. Silali huku nalia. Hamna
wakunigombesha. Nasikilizwa mawazo yangu. Kwanza naulizwa nitoe mawazo yangu.
Hamna mapenzi ya kijeshi. Kuna kuaminiana. Wamenipokea kwao kama nilivyo mimi
na watoto wangu. Sijifichi kwa Man. Ananipenda. Akianza kunibusu, hamalizi
mama. Uthamani wangu umerudi. Nasifiwa rangi yangu ya mwili! Nina amani. Si
ndicho tulikuwa tukiomba hicho?” Mama G akanyamaza.
Man akarudi. Alikuwa akizungumza na Geb mbele kidogo. Walishamuacha Nanaa ndani
akiwa ametangulia kulala. Geb alitaka kujua zaidi mipango ya harusi hasa mambo
ya garama. Man alimuelezea kwa kifupi garama nzima za harusi na mipango yote.
Wakakubaliana jinsi yakulipana pindi Man atakapomtumia garama nzima. Geb
hakutaka vya bure. Man akamuheshimu kwa hilo. Wakazungumza wapi pakupata suti
zao za harusi ili zifanane na mipango mingine ndipo akarudi kwa Grace.
Hata
jinsi alivyomuangalia tu Grace, ungejua anampenda. Alisimama nyuma yake
akambusu kichwani, Grace akageuka. “Mmemaliza?” Grace akamuuliza. “Kwa leo
naona inatosha. Tuwahi ukapumzike kwa ajili ya kesho ili uamke una akili nzuri
na nguvu. Siku ya kesho itakuwa ndefu sana kwako, unahitaji kupumzika.” Man
alizungumza naye taratibu kwa sauti ya chini, Grace akiwa amemgeukia. “Okay.”
Grace akajibu na tabasamu. Geb na mama yake walibaki kimya wakisubiri.
Grace
akageuka. “Usiku mwema. Ngoja sisi tukapumzike.
Si wote mtakuja kesho?” Grace akauliza. “Lazima mama. Siwezi kukuacha
peke yako. Na ujue nakuombea pia.” “Asante mama yangu.” Grace
akamshukuru mama yake. Akashangaa machozi yanamtoka. Geb akabaki kimya. “Msiwe
na wasiwasi, Grace atakuwa sawa tu. Na kesho Mungu akipenda atakuja akiwa
ametulia. Usiku mwema.” Grace na Man wakaondoka.
Hatima Ya Grace & Danny.
Kikao kilikuwa saa tatu asubuhi. Geb na mama yake
walifika pale kwenye ofisi za mwanasheria Upanga, ambako walikuwa na jengo lao
la wanasheria wakashangaa marafiki zao karibia wote wapo pale. Geb akacheka na
kutingisha kichwa. “Mmmh! Watoto
wamenigeuka vibaya hawa! Siamini kama ni wao.” Mama G akaongea wakati Geb
akiegesha gari. “Ila naomba Mungu mtu asikuguse wala asikuongeleshe
vibaya.” “Hapana Geb. Acha tu.
Wanatafuta sababu.” Japokuwa walikuwa hawasikii maneno wanayozungumza, lakini
Danny muendesha kikao alionekana akikiendesha kwa ushabiki sana. Walikuwa
wakicheka na kushangilia.
“Inamaana wote wale
wameacha kwenda kazini leo, asubuhi hii, siku ya kazi, wapo hapa mida hii
kushuhudia kuachwa kwa Grace!” Mama G aliongea kwa kuumia sana. “Danny ame..”
“Mama! Naomba acha mazungumzo yatakayo kunyima raha. Naomba weka akili zako
sehemu unayojua itakufurahisha. Kujiumiza huko ndiko wanakokuta wao. Usiwape
nafasi hata kidogo.” Geb alimkatiza mama yake. Mama yake akanyamaza.
“Hivi
unajua yamebaki masaa mangapi nioe?” Geb akamfanya mama yake acheke. “Masaa au
siku!?” “Nimekuuliza masaa mama.” “Basi kazi ipo! Unahesabu masaa?” “Sasa je?
Namuoa Nanaa, mama. Mwanamke aliyenizalia watoto wazuri. Anajua kasoro zangu
zote, na bado amekubali nimuoe.” Mama G akamwangalia huku akicheka. “Hongera.”
“Na ninastahili hongera kweli kweli!” Geb akajisifia. Mama G akazidi kucheka.
Wakazungumza hili na lile huku wakicheka humo humo ndani ya gari wakisubiria
Grace afike.
Ilipofika
saa tatu kasorobo wakaona gari ya Grace inaingia. “Lazima kushuka mama. Sitaki
mtu msogelee Grace na kumbugudhi kwa chochote. Sitaki hata wamsalimie. Nataka
ile furaha aliyokuwa nayo jana ndio aingie nayo kwa mwanasheria ili awe
ametulia. Lasivyo ataishia kulia muda wote nakushindwa kuzungumza chochote.”
Wakashuka.
Man
ndiye aliyekuwa akiendesha gari ya Grace. Wakaegesha pembeni ya gari ya Geb
wakashuka. Walionekana walikuwa wakicheka. Angalau mama yake akatulia.
“Nakuombea Mungu ukue hata kidogo Man!”
Grace alisikika akiongea
wakati anafunga mlango. “Umependeza sana Grace.” Grace
akacheka na kujizungusha. “Asante mama yangu.” Wote wakawasogelea.
“Shikamoo
mama.” “Marahaba Man, mwanangu. Hata wewe Umependeza.” Wakacheka. “Asante.
Sijui mlipata kifungua kinywa? Sisi tulipitia kula kwanza, nahisi ndiko tuliko
chelewa.” “Wala hamjachelewa. Sisi ndio tumewahi. Geb alitaka Grace amkute
hapa. Lakini tulikula. Nanaa alituandalia kifungua kinywa, tumekula ndio
tukaja.” Mama G akajibu.
“Si
mlisema bibi harusi wangu anatakiwa apumzike!?” Grace akauliza huku akishangaa.
“Hawezi yule. Kwanza yeye mwenyewe na mwanae Magesa lazima waamke saa 12
asubuhi, wale kwanza ndio warudi kulala.” Wote wakacheka. “Huna utakachomwambia
Nanaa akaweza kukaa na njaa. Kama mwanae. Naye yuko hivyo hivyo. Basi akiwa anaamka
kula, ndio anapika hapo hapo. Basi na mimi naponea hapo hapo. Lakini tumemuacha
amerudi kulala, saa tatu hii mke wa Jeri ataenda kumsaidia mambo yote. Kwa hiyo
atapumzika tu.” “Afadhali.” Grace akajibu huku wanacheka.
“Hongera
kwa familia nzuri Geb.” Geb akacheka. “Asante. Namshukuru Mungu kwa kweli.”
“Sasa umeshaandika Vows?” Man akamuuliza Geb. Geb akafikiria kidogo. “Natakiwa
kuandika eeh!?” Geb akauliza. “Sijui utaonaje. Lakini kwa jinsi nilivyosikia
mlikotoka na Nanaa, anastahili kiapo kutoka kwako sio kile cha kila mtu
kilichotungwa na watu wengine. Binafsi nimejiapia, kama nitafanikiwa kufikisha
mwanamke ninayempenda kanisani, nitatoa vows/kiapo nilichokitengeneza mimi
mwenyewe. Kuoa mwanamke unayempenda na anayekupenda hapa duniani ni hadimu Geb.
Mimi nimetoka huko. Upo kwenye harusi, badala ya kuona mchungaji mbele yako,
unaona ni kama upo mbele ya hakimu anakuhukumu kifungo cha maisha!”
Wakacheka.
“Basi
na mimi nitapata muda wakuandaa kiapo changu kwa Nanaa. Nitasubiri mpaka
akiondoka kesho ndio nitaanza kuandika ili asije kukiona kabla ya siku.”
Wakacheka. “Na mimi nitamwambia Nanaa akundikie.” “Acha kuiba mawazo yangu
Grace!” Man alimwambia Grace, wakacheka kidogo. “Sasa unataka sisi upande wa
bibi harusi ndio tuonekane duni? Hapana. Na nitahakikisha vow ya Nanaa, inakuliza
Geb.” Grace akasifia. “Sasa sio uende ukamwandikie mwenzio!” “Hapana bwana Man!
Ila nitahakikisha namvuta hisia zote ndipo nimwambie aandike.” “Mama umekamia! Haaa!”
Grace akampiga ngumi. “Maana wazo ni langu, lakini naona mwenzangu umelichukua
na kulikuza! Itabidi na mimi nipitie vow ya Geb. Sio asimame pale na mstari
mmoja tu. Tukaingia aibu.” “Sasa huko ndio kujazana maneno yasiyo kweli.” Grace
akaongeza. Wakazidi kucheka. “Sasa inamaana wewe kumsaidia Nanaa ni sawa,
lakini mimi kumsaidia Geb sio sawa?” Man akauliza.
Upande Wa Pili, Maisha Yanaendelea.
Vikaendelea
vicheko na kutaniana kwa muda mrefu mpaka wakajisahau walipo. “Jioni Mzee Ole
ameniambia niende nikamsalimie na watoto.” Geb na mama yake wakamgeukia vizuri
Grace wakabaki wanamshangaa. “Sasa mbona mnanishangaa!? Anajua kama nimerudi
hapa Dar. Man alimwambia tutakuwa na mapumziko ya siku mbili, akaomba nifike
kwao nikamsalimie. Kwani mama ni vibaya?” Grace akauliza kwa upole. “Mmmmh!” Mama G akashindwa chakujibu pale
mbele ya Man.
“Ni
chakula cha jioni tu mama. Hamna kitu kikubwa sana.” Man akaongeza. “Wamekuwa
wakimsikia na kuziona tu picha za Grace. Baba na mama ndio wameomba kumuona.
Kama tukiweza kupata watoto, pia ingekuwa vizuri ili na wao wakamuone babu Ole.
Anaakili kama wajukuu zake! Kama wakimkuta leo ana hali nzuri, nina uhakika watafurahia
sana kuwa nae.” Man akaendelea kusisitiza. Mama G akanyamaza.
“Sasa
mama mbona hujibu jamani!?” “Sijui niseme nini Grace!” Mama G akajibu.
“Chochote kile.” Mama G akanyamaza. Wakamuona anafuta machozi nakuondoka pale.
Geb akataka kumfuata. “Naomba mimi nikazungumze naye, Geb. Wewe baki hapa na
Man.” “Mama ameingiwa na hofu G. Naomba umuelewe.” “Mimi najua Geb. Lakini…”
Grace akanyamaza akaanza kulia na yeye.
“Nisikilize G, mimi nipo hapa
tokea saa mbili na nusu, ili kuhakikisha unaingia kwa mwanasheria ukiwa
umetulia. Naomba nyamaza kabisa ili uweze kukamilisha jambo lililotuleta hapa.
Sitaki uingie kule ukiwa unalia, nakushindwa kuzungumza kabisa. Unanisikia?”
Grace akatingisha kichwa. Man akamvuta pembeni kidogo na kumkumbatia.
Alizungumza naye maneno machache sikuoni, Grace akafuta machozi na kwenda
alikokuwa mama yake nyuma ya gari ya Grace.
Man Kwa Geb.
Man
akanza “Nampenda Grace.” Kimya. Geb
akabaki akimtizama. “Si kwa kutaka kumpotezea muda au kwa kuja kumuumiza tena
baadaye. Nampenda dada yako, Geb.” Man akaendelea kujieleza. “Mimi ni mtu mzima
kwenu. Japokuwa naweza nikawa sijawapita sana, ila ni mtu mzima ninayejua
maisha ni nini na wanawake wakoje. Kwangu Grace sio mtu ninayetaka kupoteza
naye muda tu. Sina huo muda wakucheza na wanawake, na sio asili yangu. Nampenda Grace kwa hakika. Sijawahi kumpeleka
mwanamke nyumbani kwetu, Grace ndio mwanamke wangu wa kwanza, na ninaomba Mungu
asije kutokea mwingine.” “Na huyo uliyekuwa umemuoa Sweeden?” Geb
akauliza.
“Huyo
hata wazazi wangu hawamfahamu. Ni mwanamke ambaye..” Man akamuelezea Geb kwa
kifupi sana, lakini Geb akaelewa. “Pole kwa matatizo.” Geb akajikuta
akimuhurumia. “Asante. Kwa hiyo nilirudi hapa nyumbani kwanza nikijihami sana
na wanawake, pili nilikinahiwa Geb. Sikuwa na hamu na mapenzi kutokana na
mahusiano au ndoa niliyokuwa nayo. Ilikuwa ngumu kuliko ambavyo naweza
kukusimulia na ukaelewa. Heshima hamna. Alinitumikisha kama mbwa. Vile
anavyotaka yeye yule mwanamke, tena mbele ya mtoto wangu.” Man akaendelea.
“Nikikwambia
nipo kwenye hoteli ya baba yangu, ujue niliikuta ikitaka kufa. Nikazama humo
ndani kuifufua. Akili na mawazo yangu yote yalikuwa huko mpaka juzi
nilipokutana na Grace. Nilikuwa sina muda na kitu kingine ila miradi yangu tu.
Na nilipopatwa na hamu ya kuanzisha familia tena, nikajaribu sasa kuangalia
wanawake kama wake sio wateja. Napo ndio nikaona ni heri nirudi tu kazini.
Utapeli mwingi. Hakuna uhalisia wa chochote. Moyo ukaingiwa na hofu tena.
Nikajua historia itajirudia tu. Nitaangukia kule kule. Nikaachana kabisa na
wanawake.”
“Najua
wewe ni mfanyabiashara. Unajua jinsi pesa inavyotafutwa kwa shida. Halafu uje
ufike mahali, uishie sehemu ambayo aidha huwezi kuitumia kwa raha sababu ya
karaha ya mwanamke, au muishie kugawana na mwanamke mliyekutana naye mwaka
mmoja, mkafunga ndoa, halafu mahakama inaamuru mgawane sawa sawa! Usinifikiri
mimi ni mbinafsi, lakini hilo nalo likanifunga sana. Nikaona ni heri kuacha
kwanza.”
“Ninapokwambia
nampenda Grace, ni kwa kuwa nimeona uzee wangu na Grace. Simuoni Grace kama
mwanamke anayekidhi haja zangu leo, halafu kesho nakimbilia kitandani na
mwanamke mwingine. Kwanza mimi ni muoga. Kwangu Grace, ni Grace ya Rehema
kutoka kwa Mungu. Nasema Mungu amenirehemu na kunipa Rehema au Grace kama nyinyi
mnavyomwita kwa lugha ya kingereza.”
Man akaendelea.
“Si
kwamba nampenda Grace kwa uzuri kama wengi wanavyoniambia sasa hivi. Kwamba
nimechanganywa na urembo au umbile la Grace. Hapana. Ni zaidi ya muonekanano
wake. Dada yako ametulia Geb! Najua hilo unalijua. Lakini sijui niseme nini,
ila Grace ananifanya napumzika. Sina hofu. Kuna hali fulani ninaipata
ninapokuwa karibu na Grace. Sasa sijui ni ule utulivu wake au am in Love, sijui!
Ila ninachojua kwa hakika namuhitaji Grace. Swala la kwamba ninaharakisha
kusema hivyo wakati nimemfahamu siku chache hata mwezi haujaisha, hilo
sikubaliani nalo. Kwa kuwa mimi ndiye ninayejisikia. Nilikuwa natafuta kitu
nilichopata kwa Grace tu.” Geb akavuta pumzi na kuzishusha akimwangalia
mwanakaka huyo mtanashati. Mtoto wa mjini akitoa sera zake mbele yake. Ni kweli
Man alionyesha ipo
Neema ya pesa.
“Ninachoomba
Mungu, ni hiki anachokipitia Grace leo, kisije wahi kutokea tena maishani
mwake. Ni hilo tu Man. Kwa hiyo naomba kuwa mwangalifu sana. ‘She is very delicate’ kwa kuwa anajua
kupenda sana. Naomba usimfikishe mbali ambako unajua huna mpango naye wa muda
mrefu. Tafadhali sana Man.” Geb akasisitiza. “Nakuahidi Geb. Leo tumesimama
hapa kwa jambo lisilo heri, lakini nakuhakikishia, kama Mungu atatupa miaka
mingi zaidi, ujue utaendelea kuniona nimesimama pembeni ya Grace daima.
Nakuhakikishia Geb. Mimi sio tapeli. Na sina sababu ya kuwa hapa kama nina nia
yakumchezea Grace. Mbona nazungukwa na vitoto vidogo tu! Si ningeishia naye
hotelini na ndio ikawa basi? Lakini nipo hapa kwa sababu nimempenda Grace, na
ninataka kushuhudia akiwa huru. Wakati Danny anamtaliki leo, ni huzuni kwenu,
lakini kwangu ndio nimejibiwa maombi.” Wakacheka kidogo.
“Kweli
kabisa. Naogopa hata asibadili mawazo, japo ahadi ya kumuunga mkono endapo
atataka kurudiana na muweme ipo pale pale sababu ya watoto, lakini upande
mwingine naomba Mungu leo muujiza wangu ukamilike.” Geb na Man wakaendelea
kuzungumza taratibu wakisubiria muda.
Grace kwa mama yake.
Grace akaanza mara alipomsogelea mama yake.
“Nampenda Man, mama. Na yeye ananipenda.” Akaendelea. “Hajanilazimisha kumpenda. Amenipa uhuru wa
kumpenda na safari hii nimependa mama. Naomba Mungu asibadilike. Kama yupo hivi
alivyo kiukweli na asibadilike, basi ujue kufunga kwangu Mungu amekusikia. Kunikataa
Danny, sio fedheha. Man ndio mlango
wangu wakutokea mama yangu. Nimemwambia yote kuanzia mwanzo wangu mimi na Danny
mpaka hivi leo niliposimama naye hapa. Bado Man ananipenda na kuniheshimu.”
Grace akaendelea.
“Tulikuwa
naye huko mbugani. Akaniacha hapo siku moja ili nipate muda wangu peke yangu
wakufikiria. Akaniambia niwe huru kumuuliza yeyote na kama nikijisikia moyoni
sipotayari kuwa naye, basi niondoke. Alinitafutia hoteli nyingine jijini
Mwanza. Kwamba niende nikapumzike na huko. Akaniambia nipo huru kutorudi pale
mpaka nitakapokuwa tayari naye. Au hata kama sitakuwa tayari, basi. Yeye
anaelewa. Akaondoka na kuniacha pale.” “Nimepata muda wa kumuomba Mungu.
Nimetulia mama yangu. Naona Man ni mwanaume atakayenifaa. Ananiheshimu na
kuniamini.”
“Hamna
tena kutukanwa na kudhalilishwa mbele za watu. Najua hata nikiwa naye nitakuwa
na amani. Yale mambo ya ugomvi kila siku kama nimefumaniwa hayatakuwepo. Halafu
ananifanyia mambo ambayo hata sikuwahi kufanyiwa kwenye mapenzi. Nilikuwa
nasikia tu kama yapo. Danny alikuwa hajui na wala hakutaka kujifunza, alisema
ni uchafu.” “Grace wewe mtoto!!” Mama yake akashituka sana.
Grace
akacheka. “Kweli mama.” “Naomba unyamaze.” Grace akazidi kucheka. “Mwenzio siku
hizi nafurahia kweli mapenzi. Sichubuki tena. Yale mambo yakupaka mafuta kila
nikitaka kufanya mapenzi yameisha. Man anani…” Grace akaangalia kulia na
kushoto akamwinamia mama yake sikioni na kumnong’oneza. “Grace wewe mtoto!”
“Kweli mama.” “Haya naomba unyamaze. Nyamaza kabisa usiniambie uchafu wako.”
Grace akazidi kucheka. “
“He is a love machine’, mama. Ninafuraha.” “Mmmh!” Mama yake akaguna huku
akimwangalia kwa pembeni maana aligeuka baada ya Grace kumnong’oneza. “Sasa
unaguna nini?” “Nakuona ulivyo furahi!” Grace akazidi kucheka. “Sasa geuka
nikwambie kitu kingine.” “Usiniambie mambo yako machafu.” Grace akazidi
kucheka. “Sasa nitamwambia nani mama, wakati mwenzio sina rafiki halafu
nikiwaambia watu wengine wataniona mshamba.
Watanicheka. Watashangaa na uzee huu sijui mapenzi! Hata yeye mwenyewe
Man sijamwambia. Nikajidai najua.” “Wanaume wanajua sana kama mwanamke ni mgeni
kwenye jambo au la. Amekustahi tu mwenzio.” “Mama!” “Kumbe. Wewe niambie hicho
unachotaka kuniambia.” Grace akacheka.
“Nimejiambia
hivi, hata kama atakuja kubadilika baadaye, ni angalau huyu nitakuwa nimefaidi
kidogo mama yangu kuliko Danny.” Grace akatafuta uungwaji mkono. “Nisikilize tu
mama na uwe mkweli. Tokea naanzana na Danny imekuwa ni hekaheka mpaka leo. Sisi
ni shida tu. Kama sio shida ya kifedha, basi maisha yakijeshi tu. Hakuna
kuaminiana. Tulianzia chini mnoo. Mungu akatutokezea kwenye upande wa pesa,
ukaona jinsi alivyobadilika. Siwezi hata sema kama nimepumzika na Danny. Acha
nipumzike mama yangu. Hata kama ni kwa muda. Acha na mimi nile starehe kidogo.
Tafadhali mama yangu naomba niunge mkono.” Grace akambembeleza mama yake.
“Kwa
hiyo unaenda kwa wazazi wake?” Mama yake akamuuliza. “Acha niende mama.
Japokuwa naogopa, lakini acha niende kwa ajili ya Man. Anasema hajawahi peleka
mwanamke kwao. Kwake yeye hii ni heshima. Halafu wamenikubali japo mimi si
msichana. Wamenikubali mimi na makinda yangu yote! Watoto watatu mama! Wala si
mmoja. Wanawajua watoto wote na bado wanataka nifike kwao! Nishazungumza nao
kwenye simu. Mzee Ole anaonekana nimtundu kama Man au Malisa ambaye ni dada
yake Man, lakini mama yake ni mkimya kidogo. Lakini na yeye anaonekana
kunikubali. Kwanza hata hawajaonyesha tatizo kwanye swala la kwamba mimi
nilisha kwisha kuolewa. Tena Mzee Ole alikuwa akimtania Man kuwa anatakiwa
anizalishe harakaharaka ili Danny akijua
azire kabisa. Amwachie.” Mama yake akacheka kidogo.
“Kwa
hiyo utazaa tena?” “Mungu akinijalia mama, nitamzalia Man bila shida. Hata
akitaka watoto wawili, nitazaa tu.” “Grace wewe mtoto!?” “Kabisa mama. Nina shida
gani?” “Mmmh!” “Lakini nisifie basi mama! Najua unaogopa nisije kuingia tena
matatizoni. Lakini tuwe wawazi. Safari hii nimekuletea dume la ukweli. Au
unasemaje?” “Hapo sina ubishi. Na hakika mnapendezana. Wote warefu. Na nikijana
anayeonekana anabusara.” “Asante mama yangu. Namshukuru Mungu pia amejawa
upendo sana. Anajali mno.” “Anaonekana.” Mama G akajibu na kupotelea
mawazoni.
Kwa Danny Na Wapambe Wake.
Danny na marafiki zake bado walisikika
wakishangilia. Mara kwa mara vilisikika vicheko vya sauti ya juu huku
wakishangilia kishabiki. Geb alijua wazi wanataka kuwakera wao. Walitenganishwa
na magari. Kina Geb walisimama nyuma ya sehemu ya kuegeshea magari, japo
walionekana wakiingia na wao waliwaona walipokuwa wamesimama kama kundi wakati
ndio wanaingia sehemu ya kuegesha magari. Geb na Man wakawasogelea mama G na
Grace.
“Naona
muda umefika. Watu wameanza kuingia ndani.”Geb akaongea wakati wameshafika.
Grace akavuta pumzi.“Njoo.” Man akamuita. “Mimi nitakuwa hapa nje nakusubiri.” Akaongea
kwa sauti ya chini na kumbusu midomoni. “Naomba twende wote.” Wakamsikia Grace
akiongea taratibu. “Unauhakika?” Grace akatingisha kichwa kukubali. Man
akamgeukia Geb na mama yao. “Eti ni sawa na mimi nikaunga msafara?”
“Unamaanisha mpaka ndani kabisa kwenye chumba cha kusainishana!?” Geb akauliza
akimwangalia Grace. Grace akatingisha kichwa kwa wasiwasi. Geb akamwangalia
mama yake. “Naomba niwe muwazi kwako Man. Danny nikijana asiye na staha ya
maneno hasa sasa hivi akiwa na hasira na sisi, na akiwa na lengo la kutukomoa.
Ana maneno machafu na ya kukera sana. Sitaki upite huko. Kwa kuwa amekuwa
tatizo letu, tumelea huo uozo kwa muda mrefu sana, acha sisi tukamalizane naye,
uanze na sisi kukiwa kuna amani.” Kidogo wakaelewa mama yao anachomaanisha.
“Ni
kweli Man. Danny anaweza kuchafua hali ya hewa, ukatoka pale hata ukashindwa
kumtizama mama usoni. Sikuwa nimefikiria hilo.” Grace akaongeza. “Nimeelewa.
Basi ujue mimi nipo na kama utanihitaji jua nakusubiria nje ya chumba cha huo
mkutano.” Man akamshika mkono. “Naombeni tuombeni kwanza.” Mama G akatoa wazo
kabla hawajaondoka. “Hatuna kimbilio jingine isipokuwa Mungu.
Naomba tujitakase. Tuombe toba
kwa chochote kile au popote pale tulipokosa. Kisha tuombe rehema na hekima za
Mungu katika hili.” Wakashikana mikono, mama yao ndio akaanza kuomba. Aliomba huyo
mama kwa machozi, akimwita Mungu ajidhihirishe hata katika hilo. Akatubu na
kujinyenyekeza huku akiomba rehema. Akamaliza. “Amen.” Kila mmoja akaitikia.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Wakati
wanaingia mlangoni wakasikia minong’ono wakiwasema. “Wamekimbia nini?” Wakawa
wakicheka. Walipotokezea tu wote wakanyamaza. Man alikuwa mgeni kwao. Hakuna
hata aliyemsalimia mama G. “Habari zenu?” Man akasalimia, wachache wakajibu. Geb
akamsogelea secretary, akajitambulisha. “Nafikiri mnasubiriwa nyinyi tu.”
Akamjibu Geb. “Ni chumba kipi?” Yule dada akasimama ili kuwaelekeza. “Grace!”
Walipofika mbele kidogo Man akamvuta mkono.
Walikuwa
wamepita lile kundi la wale vijana. “Nitakuwa hapa kwenye hivi viti
nikikusubiri. Sawa?” Grace akainama, akaona anafuta machozi. Alishamuona
amebadilika baada yakuona lile kundi la wale vijana. “Niangalie Grace.” Man
akamshika kwenye shingo na mikono yake yote miwili. “Utakuwa sawa, usiwe na wasiwasi.
Na ukitoka, utanikuta hapahapa nikikusubiria.” Tayari machozi yalishafika
kidevuni. Man akamkumbatia huku akinyonya midomo yake mpaka akatulia. “Utakuwa
sawa?” “Nipo sawa.” Grace akajibu na kuanza kuondoka.
Man
akamkimbilia na kumvuta tena mkono. “Usisahau nakusubiria.” Grace akatingisha
kichwa kukubali. Man akambusu tena. “Nakupenda Grace.” Man akaongea taratibu
huku akimtizama. Grace akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu.
“Nisubiri. Usiondoke.” “Siwezi.” Man akajibu. Grace akajisogeza karibu naye, na
yeye akambusu kwa muda kidogo. “Nitakuwa sawa. Hata hili nitalimudu!” Grace
aliongea kwa ujasiri. Man akacheka. “Nakuaminia.” Wakacheka, Grace akaondoka.
Wapambe wa Danny waliona na kusikia kila kitu, wakanyamaza kimya. Grace
akaingia ndani.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Grace
aliingia akakuta upande wa kulia wa meza amekaa Danny na Zinda. Katikati ya ile
meza upande wa juu alikuwa amekaa kijana mtu mzima kidogo, ambaye baadaye
kidogo alikuja kujitambulisha ndio mwanasheria na mwanamke mwingine ambaye
alijitambulisha kama mtu anayehusika na Ustawi wa Jamii alikaa upande wa chini
wakiangaliana na yule mwanasheria. Geb na mama yake walikuwa wamekaa upande wa
kushoto, Geb alisimama akamvutia kiti dada yake alipoingia ili akae. Akakaa.
“Asante.” Grace akamshukuru. Wazi walionekana walikuwa wakimsubiria yeye.
Baada ya salamu, mwanasheria akaeleza
kilichowaleta pale. Kwamba Danny anataka Grace asaini hati ya talaka.
Grace akaomba zile karatasi, akamkabidhi Geb zile karatasi zote. Geb alianza
kusoma moja hadi nyingine huku akimpa kila aliyosoma yeye nakuridhika, asaini.
Kulikuwa na ukimya wa namna yake ndani ya kile chumba wakati Grace akisaini
talaka yake. Alikuwa ametulia tu, pembeni yake akiwa Geb akipitia zile karatasi
kwa makini kabla dada yake hajaweka saini yake. Walipomaliza, wakamkabidhi yule
mwanasheria. Akazipitia. Akaona zipo sawa.
“Limebaki
swala la watoto na mali.” Mwanasheria akaanza tena. “Ile nyumba nimewekeza pesa
nyingi sana. Siwezi kuhama pale. Uzuri kwamba nimetunza kumbukumbu za garama
zote.” Danny akadakia. Geb alishazungumza na Grace wakawa wameelewana. Grace
alibaki tu kimya. “Unasemaje Grace?” Mwanasheria akamuuliza. “Mimi nina
mapendekezo. Lakini naomba nitoe la kwanza.” Grace akaanza. “Karibu.” “Lengo la
kujenga ile nyumba, ilikuwa si kuiuza. Tulitaka watoto wetu wawe na kwao.
Akiishi baba yao na mimi, ita..” “Haitakaa ikatokea tena.” Danny akadakia.
“Naomba
tumpe nafasi Grace amalizie. Tafadhali Danny.” “Nataka kumfupishia maneno.
Asiwe amekuja akiwa amejiandaa na kilio akifikiri nitamrudia. Huo ni ukurasa
ambao nishafunga.” Grace akanyamaza. Geb na mama yake hata hawakuongea
neno. “Endelea Grace.” “Okay. Ndio nilikuwa nikisema, yeyote atakayeishi pale,
iwe ni baba yao au mimi, lakini tujue ni garama tuliwekeza pale. Iwe ya mali au
hali, ni kwaajili ya watoto. Binafsi nisingependa iuzwe.” “Kwa hiyo ulitaka na
wewe uje uishi pale? Maana mimi naoa?” Danny akakatisha tena.
“Hapana.”
Grace alijibu akiwa ametulia kabisa. Akili ikafanya kazi kwa haraka. “Kwa kuwa
wewe unakaribia kuanzisha familia, nafikiri ni busara ukaishi tu pale. Lakini
mimi nitachukua watoto.” “Ati nini!?” Danny akahamaki. “Naomba umuache amalize.
Au ndio umeshamaliza Grace?” Mwanasheria akauliza. “Hapana.” Grace akajibu
taratibu. “Afanye haraka. Watu tunashuguli zetu. Hata kama wanatuona hatuna
pesa, tunashuguli zakufanya hata sisi. Tuache dharau.” Hata yule mwanasheria
akapigwa na butwaa. Kimya.
“Anaweza
kuendelea?” Ikabidi yule mwanasheria
amuulize Danny. “Ndio maana yake!” “Karibu Grace.” “Nisingependa watoto wangu wakue bila baba yao. Lakini wale
watoto bado ni wadogo sana. Ningetamani kuwakuza mimi mwenyewe. Ni watoto
wadogo, halafu ni wakiume. Najua wanangu niwatundu sana. Hakuna..” “Sio..”
Danny akamkata Grace. “Nisikilize Danny. Wote tunashuguli zakufanya. Naomba
tuheshimiane. Unapozungumza wewe, watu wote wanakusikiliza. Kwa nini
anapozungumza mtu mwingine unashindwa kusikiliza? Anachozungumza Grace ni cha
msingi sana. Hapa tunaweka hisia zote pembeni tunataka kujua hatima ya watoto.
Na ndio maana kisheria nipo Hapa. Ukishindwa kutulia, utataka ifunguliwe kesi
ambayo nakuhakikishia, utakosa watoto na nyumba. Kwa kuwa kisheria watoto chini
ya miaka 7, wanatakiwa kuwa chini ya uangalizi wa mama yao, endapo mama yupo
hai. Na kwa kuwa wewe ndio humtaki Grace, kisheria unatakiwa utoke na mizigo
yako tu, umuachie Grace ile nyumba na bado uwe unampa pesa za matumizi kutokana
na mshahara wako. Sasa useme kama unataka tufike huko sasa hivi au
tunamsikiliza Grace.” Yule mwanamke wa Ustawi wa jamii, akamjia juu Danny.
Alionekana kukereka tayari. Kimya.
“Naomba
kukusikiliza Grace.” “Asante.” Grace akaendelea. “Nilitaka kulea watoto wangu
mimi mwenyewe kama nilivyotangulia kusema. Hakuna mwanamke ambaye anaweza kulea
wale watoto, akaweza kuishi nao kwa amani isipokuwa mimi mwenyewe ambaye
nimewazaa. Sidhani kama kuna mwanamke yeyote atakayefurahia kuingia kwenye ndoa
yenye watoto wadogo watatu. Tena ambao bado wanavaa diaper! Najua kulea jinsi
ilivyo kazi jamani.” Grace akaendelea.
“Naombeni
nilee watoto wangu mimi mwenyewe. Sihitaji hata shilingi ya Danny, na wala
sitataka ahame pale. Ila asije akawahi kupauza, au kuja kurithisha watoto wake
wengine. Ibakie nyumba ya wanangu tu. Na tukirudi kwenye swala la watoto,
nitahakikisha lazima wanamuona baba yao. Kwa kadiri ya nafasi ya Danny. Mimi
nitahakikisha wanamuona baba yao na wanamtambua Danny kama baba yao. Ni hilo
tu.” Grace akamaliza.
“Umesikia
Danny?” Yule mwanasheria akauliza. “Kwa hiyo sasa hivi naruhusiwa kuongea?
Maana nilijaribu kuzungumza, naona nikakatishwa.” Yule mama akaguna na
kutingisha kichwa. “Karibu.” Yule mwanasheria akaona aende kwenye pointi.
“Mpaka mwisho wa mwezi huu nina ratiba na watoto wangu. Nimeshaomba likizo
kazini, nataka kusafiri na wanangu. Kwa hiyo kama ni kwenda kwa mama yao, iwe
baada ya safari.” Danny akajibu kibabe.
“Ambayo
itakuwa tarehe ngapi?” Yule mwanasheria akauliza. “Nimesema nitamjulisha.”
Danny akajibu. “Hapana. Tumekubaliana leo ndio tuweke hitimisho la kila kitu.
Unaishi na watoto wadogo sana ambao kisheria huruhusiwi. Nilazima kuweka
mikakati yakueleweka.” Kimya.
“Naomba
niombe kitu kimoja.” Grace akaongea kwa upole. “Karibu Grace.” “Hii ilikuwa
nafasi yangu yakuzungumza. Mbona mnampendelea Grace? Au mmeshakula pesa yao?”
Danny akalipuka kama moto. “Nimekuuliza, ukakaa kimya
Danny.” “Kwani siruhusiwi
kufikiria? Mnataka nijibu kama mashine halafu mje mnigeuke? Nina haki
yakufikiria. Acheni dharau.” “Nisikilize Danny. Hii kampuni haiendeshwi kwa
rushwa, ila sheria. Ulikuja kwangu wewe mwenyewe. Hata hawa watu mimi sikuwa nikiwafahamu.
Grace ndio leo namuona hapa kwa mara ya kwanza. Punguza hasira, tumalize hiki
kikao.” Mwansheria akajibu.
Zinda
akamgusa. “Tulia Danny. Tulia tumalize.” “Sitaki kuonewa! Kama watu wanatumia
ushirikina hata humu ndani kupumbaza watu, ndio wajue uchawi wao hauwezi
kunipata mimi. Waliyonilisha nilishatapishwa. Tena nimewekewa ulinzi ambao
hawawezi tena kunigusa.” Danny akaendelea. Kimya. Hakuna aliyejibu.
Palipotulia,
Mwanasheria akamuuliza tena. “Umepata tarehe?” Danny akataja tarehe ambayo ni
mwezi mmoja kuanzia hapo. “Haiwezekani! Hao watoto ni wadogo sana Danny.
Hawawezi kuishi mwezi mmoja bila mama yao!?” “Muulizeni Grace kama mimi sikuwa
nikihusika kuwalea hao watoto. Tena ni kama niliwalea mwenyewe. Grace hana
uwezo wakulea watoto. Alikuwa akilia mara nyingi tu akitaka nirudi nyumbani kwa
kuwa watoto wamemzidia nguvu. Hawawezi wale watoto. Hata ushahidi wa jumbe
alizokuwa akinitumia nirudi nyumbani haraka, watoto wanamsumbua ninazo.” Grace
akaingiwa hofu.
“Kwa hiyo kwa akili zako wewe kama wanaweza kumliza
mama yao mzazi, unafikiri mama wa kambo atawaweza!? Nipe mimi huo
ushahidi nimpelekee jaji. Na kama unafikiri kwa aina hiyo ya watoto ni sawa
kulelewa na mama wa kambo, nitakutafuta baada ya miezi sita kama hujaniambia
mlishawazika kwa kufungiwa kwenye friji au oven au hata kupigwa mpaka kifo.
Tena kama unaenda kuoa kasichana, ujiandae Danny. Kwa hivyo ulivyo wewe
mwenyewe, na aina ya watoto mnaowazungumzia hapa, halafu unaanza ndoa mpya!
Utaishia jela wewe. Na utanikumbuka.” Yule mama wa Ustawi wa Jamii,
akamuhakikishia akisikika ameshakerwa na Danny.
“Naomba
nisikie ombi la Grace.” Yule mwanasheria akamgeukia Grace. “Sijawaona wanangu
kwa majuma zaidi ya matatu sasa. Nafikiri ni zaidi ya hata mwezi. Naomba leo
jioni nipewe.” “Hivyo sivyo tulivyokubaliana.” Danny akahamaki tena. “Nitawarudisha
jumatatu. Leo ni jumatano. Jumamosi ni harusi ya anko wao. Naomba na wao
wahudhurie.” “Hapana. Haiwezekani.
Tayari jumamosi ninasafiri nao.” Grace akaanza kulia.
“Usifanye hivyo Danny. Na mimi nina haki na hao watoto. Nimekuachia
siku zote hizo! Na nimekukubalia ukae nao mpaka huo muda uliosema. Unashindwa
kuniruhusu nikae na wanangu kwa siku tano tu!? Tena kwa kitu maalumu kama
hicho! Mimi sidhani kama unanitendea haki Danny.”
Grace akalalamika.
“Cha
kwanza sio kwamba wewe ndio umeniruhusu kukaa na wanangu. Hata mimi najua
sheria. Msinigeuze mjinga. Cha pili mnatabia yakufanya mipango yenu ndio muhimu
kuliko wengine sababu ya dharau tu. Sasa kama wewe unaona kuna umuhimu wa
harusi, basi ujue na mimi naenda kuwatambulisha wanangu upande wa baba yao.
Msifikiri mimi ni yatima nisie na watu. Hata mimi ninao watu. Kama mlikuwa
mkinichezea kwa uchawi ili nigombane na ndugu wanaonipenda na kunijali, basi
ujue nina safari yakuwapeleka watoto wangu Iringa, kuwaona watu walionilea mimi
na baadaye kwa familia yangu uliyonitoa
kwa madawa. Tabora kwa kina Zinda.” Ni Grace tu alisikika akilia.
Alilia
kwa uchungu. Wote walikuwa kimya. “Naomba sisi tuondoke.” Grace akataka
kutoka. “Subiri kwanza Grace.” Yule mama
akamzuia. “Hao ni watoto wako. Ni wadogo. Wanahitaji wewe
uwapiganie. Hakuna mwanaume anayejua uchungu wa uzazi ila wewe.
Usiondoke bila kujua hatima ya watoto wako. Ikishindikana hapa, tutakwenda
mahakamani. Hata Ustawi
wa Jamii utakutafutia mwanasheria. Usikubali
kirahisi.” Yule mama akawa mkakamavu.
“Naomba
kujua hao watoto wanaenda lini kwa mama yao, na watakuwa wakimuona baba yao
siku gani tena kwa masaa mangapi.” “Masaa!?” Danny akamuuliza yule mama wa Ustawi
wa Jamii, kwa ukali huku akishangaa. “Naongea na mwanasheria wako Danny. Mimi
siwezi kuzungumza na watu kama…” “Naomba turudi kwenye jambo la msingi.”
Mwanasheria akamkata yule mama akataka watulie.
“Kama
nimekuelewa vizuri Danny, safari yako ni ijumaa, sio leo usiku wala kesho. Ni
sawa?” “Ndiyo. Lakini leo jioni nina appointment yakuonana na dakatri wao
kuhakikisha wanachanjo zote. Ili nikisafiri nao wasiugue. Siku ya kesho
nitatumia kufanya nao shopping ndipo nisafiri siku ya ijumaa.” “Mmmh!” Yule mama
akaguna na kutingisha kichwa.
“Hata
kama hamniamini, mjue ndio hivyo. Walipokuwa wakiishi na watoto wangu sikwenda
mahakamani kuwakataza. Wamezaliwa kwao na kuwafanyia yote waliyoyataka. Sasa
safari hii ni zamu yakwenda kwa upande wa baba yao na wao wakawatizame hayo
waliyolishwa upande wa mama.” Danny akaongea kibabe.
“Naomba turudi kwenye pointi jamani.” Yule mwanasheria akaingilia tena.“Kwa hiyo mpaka hiyo tarahe mliyokubaliana, ndiyo Grace ataona watoto?” “Ndio maana yake.” Danny akajibu. “Umesikia Grace?” “Nimesikia.” Grace akajibu huku akifuta machozi. “Unafikiri ni lini utakuwa na uwezo wa kuwarudisha kwa baba yao?” “Inategemea.” Grace akajibu. “Ati nini?” Danny akasimama.
“Naomba
tumsikilize Grace. Kaa chini Danny.” “Asianze kubadilika eti kwa kuwa sasa hivi
wote mpo upande wake sababu ya machozi. Hiyo ndio silaha yake. Inategemea na
nini?” Danny akapayuka. “Unakaa chini tumalizie kikao, au tuandike kuwa
umeshindwa kumaliza kwa amani?” Yule mama akauliza. “Khaa chini Danny. Tumebakisha
pafupi sana.” Mwanasheria wake akamsihi, kisha akamgeukia Grace. Geb akampa
dada yake maji ya kunywa na tissue yakufutia machozi. Grace akanywa yale maji
huku akijifuta machozi mpaka akatulia.
“Eti
Grace, inategemeana na nini?” Grace akasafisha koo kidogo, kisha akaongea.
“Hawa watoto sijawaona. Mpaka wanakuja kwangu nitakuwa sijawaona zaidi ya miezi
miwili. Sijui watakuwa na hali gani. Sijui watahitaji nini! Nilazima na mimi
kuweka mazingira yakuwaweka sawa, ndipo nitakuwa na uwezo wakujua nawakutanisha
na baba yao lini. Siwezi kufanya watoto wangu wamange mange barabarani kama
adhabu. Jamani hawa watoto hawana kosa. Kama ni kosa ni langu mimi lakuendelea
kufuga uozo kwa muda mrefu.” “Uozo!?” Danny akauliza lakini Grace
akampuuza na kuendelea.
“Siwezi
kuadhibu wanangu kwa kuwazungusha hovyo. Lazima kujua maendeleao yao, ndipo
nitakupigia simu wewe, wewe utamjulisha Danny utaratibu kamili. Lakini
inategemea kama nilivyosema. Kama nikiwakuta na hali mbaya, hakika itamchukua
muda mrefu sana Danny kuja kukutana na hao watoto. Nitafika popote kukushitaki
Danny. Sitaogopa.” Grace akabadilika.
“Kwani nani amesema unaogopa? Si pesa ipo?” Danny akauliza kwa kashfa. “Sasa utaona vile pesa inavyofanya kazi na utajuta kuzaliwa masikini.” Yule mama akaanza kucheka. “Simba kajeruhiwa.” Yule mama akapiga meza huku akicheka.
“Hunitishi
Grace.” “Hakika utatishika Danny. Omba Mungu urudishe watoto wangu wakiwa
wazima. Wakija hata na michubuko, ujue ndio mwisho wako na wanangu.” “Hapo
ndipo utanijua.” “Hapana Danny. Hapo ndipo utanijua mimi ni nani. Nilivumilia
umaskini wako, matusi, ukorofi, dharau zako, na kuniendesha vile utakavyo wewe,
lakini sio watoto wangu.” Grace aliongea taratibu ila kwa ukali.
“Hakikisha unarudisha watoto wangu salama. Nimemaliza kuzungumza na wewe.”
“Unani..” “Nimekwambia nimemalizana na wewe Danny. Sina muda wakupoteza
kupigishana kelele na wewe. Unalilia nyumba, nimekupa wewe na mwanamke wako.
Mkae bure maskini nyinyi wa nafsi na akili. Unachotaka kingine tena
ni..”
“Sijalilia
nyumba. Nyumba ni…” “Nyumba nini Danny? Nyumba nini? Tafadhali acha kelele, na
ukue hata mara moja maishani mwako. Huna adabu kwa yeyote yule wala huna
shukurani. Kelele tu na matusi. Unalalamika kulogwa! Unalogwa kwa lipi maksini
wewe!?” Grace akapatwa jazba.
“Akuloge
nani Danny wewe hata kuvaa mimi ndio nimekufundisha? Unalogwa ili usaidiwe?”
“Ili mnitumie.” “Umetumiwa na nani wakati wewe ndio ulikuwa ukilishwa na
kulazwa bure?” “Si huku mnanufaika na mimi?” “Basi tutakuona sasa hivi kama utafanikiwa
halafu sisi tutakuwa maskini. Na nyumba nimekuachia ukae wewe na mkeo, bureee.
Wewe uliyelogwa. Acha ujinga wakudanganya watoto wangu.” “Kwani ni uongo kama
mliniibia nyota yangu? Mliniibia nyota yangu ili muitumie kujipatia mali.”
“Wewe
ni mshezi usie na shukurani tu Danny. Kwa nini hujiulizi kwa nini hiyo nyota
yako isikusaidie wewe mwenyewe ije isaidie wengine? Nimekuokota ukiwa unanuka mikojo
na chupi moja tena imechanika, leo unajidai tumenufaika na wewe!” Danny
akasimama kwa hasira na Geb akasimama kama mshale. “Usithubutu hata kumgusa
Danny.” “Utanifanya nini Geb? Utanifanya nini?” “Utakapomgusa Grace, ndipo utanijua
kwa hakika mimi ni nani. Na sikutanii.” Geb aliongea kijasiri.
“Mungu
akusaidie usimguse Grace. Nakuapia Danny. Utaona maisha yako machungu kuliko
sasa.” “Maisha yangu mimi sio machungu. Nyinyi ndio mliyafanya maisha yangu
machungu.” “Mnafiki mkubwa wewe. Ulikuwa unapewa mpaka nauli ya kupanda
daladala, halafu unasema umelogwa! Ulikuwa ukilishwa na kulazwa bure!
Unajitakasa kwa watu kwa kutupaka sisi matope! Wewe ni mshezi tu Danny. Sasa
subiri wewe na Sara mrudishe watoto wangu na tatizo, utajua nguvu ya pesa
na uchungu wa kusukuma watoto leba. Kuzaa bila ganzi. Hakika hutakaa ukasahau
jina la Magesa mpaka kifo chako.” Grace akachukua pochi yake. Wote watatu
walikuwa wamesimama.
“Twende
mama.” Grace akaongea huku anavuta kiti.
“Na swala la watoto?” “Nisikilize Danny. Utasikia kutoka kwa lawyer wangu.
Sizungumzi na watoto wadogo mimi. Halafu kuna kitu kinaitwa muda, masikini huwa
hamkitambui ndio maana mmeacha kazi zenu wote mmejazana hapa kuja kutushangaa
kina Magesa. Unanyamazishwa tokea mwanzo wa kikao mpaka mwisho hunyamazi,
umejawa jazba kama nini!” “U..” “Shashi Danny. ‘Shashi
please!’. Tushakusikiliza vya kutosha.
Tangia nakufahamu mpaka muda mfupi uliopita nilikuwa nasikiliza ujinga wako.
Mwanaume huna hoja, ni kelele tu. Huchoki!?” Grace akazungumza naye kwa
dharau akionyesha amechoka.
“Jamani
asanteni kwa muda wenu. Na samahanini sana. Lawyer wangu atawatafuta.”
Akimjulisha yule mwanasheria wa Danny. “Siwezi kuendelea kupoteza muda wangu
hapa. Nishapoteza mambo yangu mengi sana kwa ajili yake huyu. Siwezi kuendelea
kubishana naye. Inatosha. Twende mama
yangu.” Grace akatangulia kutoka, mama yake akafuata, akaja Geb.
Wachuma Janga.
Alipofika
mlangoni, akahakikisha mama yake na Grace wametoka, Geb akarudi. “Naomba
uwaambie wenzako na wake zao, siku nilipowakuta dukani kwa mama yangu wakifanya
fujo, iwe mwanzo na mwisho. Isikae ikarudia tena, Danny. Waambie wote
nimewaonya.” Geb akajiweka sawa. “Nimewafungulia mashitaka polisi. Masharti
yote mliyo andikiwa yapo hapa kwenye hili faili. Waambie ndugu, jamaa na wake
zenu wote, chochote kibaya kitakachompata mama yangu, Grace, Nanaa na watoto
wangu, wapo matatizoni. Majina ya wote waliomfanyia fujo mama, nimewapa polisi.
Wapo kwa kesi ya kumtishia mama yangu kifo.” Geb akaendelea.
“Wewe
si mume wa Grace tena, hukaribishwi tena nyumbani kwetu. Vivyo hivyo na
marafiki zako na wake zenu pia. Tumeagana hapa kwa amani. Waambie wahakikishe
wanakaa mbali na sisi kabisa.” Geb alikuwa amesimama katikati ya mlango. Waliokaa
nje wanasikia, na wandani wanasikia. Kimya kikatanda. Geb asiyemzungumzaji
akiongea, nilazima usikilize. Utisho wa pesa yake ulimuwakilisha vizuri sana.
Kwanza ni kama alikuwa akiwadai wote waliokuwepo pale. Ilikuwa lazima kumsikiliza.
“Hakuna
anayenidai. Na waambie ninaowadai wote ifikapo mwishoni mwa mwezi ujao, pesa
yangu yote, bila kukosekana hata shilingi, iwe imefika benki, ukiwepo na wewe
pia Danny. Majina yenu na kiwango cha pesa ninachowadai nimeorodhesha kwenye
faili nitakalomkabidhi mwanasheria wako. Ipo akaunti ambayo nitataka hiyo pesa
iwekwe. Nimewaandikia namba ya hiyo akaunti na jina lake. Ukishalipa, mtafute
tena huyu mwanasheria ili kumkabidhi hiyo slip itakayokuwa imegongwa muhuri wa
kupokelewa hiyo pesa benki. Huyu mwanasheria atamkabidhi mwanasheria wetu. Mtu asinitafute
tena, kwa sababu yeyote ile. Narudia tena, maelekezo yote ya malipo na kiasi
ninachowadai kipo humo kwenye faili nitakalomkabidhi mwanasheria wako Danny.
Kama umesahau ni kiasi gani ulinikopa, taja jina lako kwa huyu mwanasheria
kisha atawatajia kiwango unachodaiwa. Waambieni na wake zenu hivyo hivyo,
walipe pesa yote bila kupungua hata shilingi moja.” Geb akaendelea.
“Yapo
madhara yakutokulipa hiyo pesa yote kwa muda niliopanga mimi.
Yameorodheshwa hapohapo kwenye hilo faili. Nashauri wote msindoke kabla
hamjazungumza na huyu mwanasheria. Ipo tarehe uliyokopa na tarehe utakayotakiwa
kulipa, endapo kama yupo hata mmoja wenu atakayekuwa amesahau ni lini alikopa
basi jiridhishe kwa huyu Muheshimiwa hapa.” Geb akaendelea.
“Sitataka
kupokea simu kutoka kwenu au wake zenu TENA. Nalo hilo lipo kwenye hili faili.
Kusogea karibu na familia ya Magesa, kwa nia yeyote ile na kwa njia yeyote ile,
nikukiuka masharti haya. Nitamkabidhi mwanasheria wako hili faili zima.
Atawaeleza vizuri, nashauri muelewe ili kuepuka madhara yake.” Geb alitulia
kidogo akimtizama Danny.
“Danny!
Huruhusiwi hata kuleta watoto nyumbani kwangu. Kama alivyokwambia Grace,
utaratibu wa kukabidhiana watoto, utausikia kutoka kwa lawyer wetu. Narudia.
Huruhusiwi au hatutaki kuwaona tena kwenye maeneo yetu. Kuna umbali umewekwa
hapo, hakikisha unaelewa. Walinzi wangu wanayo picha yako na rafiki zako wote,
tena na wake zenu pia. Watakapowaona tu maeneo ya kwetu, ujue watakukamata.”
Kimya.
Geb
akamkabidhi yule mwanasheria faili alilokuwa ameshika muda wote. “Tafadhali
sana. Baada yakumsomea Danny mambo yaliyoandikwa hapo, na ukaridhika kuwa
ameelewa, hakikisha anaweka saini kukubali kuwa amesoma na kuelewa. Nitamtuma
mwanasheria wetu aje kutoa copy ili kusiwe na kugeukana baadaye. Na
atawasiliana na wewe juu ya slip za malipo yangu utakazokuwa umekabidhiwa.
Endapo hutapokea malipo yeyote yale, tafadhali usisite kuwasiliana naye. Yeye
atajua jinsi yakuwasiliana na waajiriwa wa wadaiwa wote walioorodheshwa hapo
ndani ili kupata hiyo pesa na malipo ya usumbufu. Naomba nikushukuru sana kwa
muda wako na niombe radhi kama kuna tulipoupoteza. Asante sana.” Geb akampa
mkono. Yule mama akaanza kucheka upyaa huku anagonga meza kishabiki. Geb
akatoka. Kila mtu kimya. Aliwapita wale marafiki zake, kama viti tu.
~~~~~~~~~~~~~~~~
“Bwana
pesa inajeuri mbaya! Imenyamazisha wanaume wote. Eti mtasikia kutoka kwa lawyer
wetu!” Yule mama akakusanya vitu vyake.
“Sasa subiri kusikia kutoka kwa lawyer wake. Maana ataanzia kutoka
kwangu, kujua nilikuonaje hapa kwenye mazungumzo ya awali. Kama unafaa kuwa na
watoto au la. Atafuata huyo mwanasheria wako uliyesema amepewa hongo. Hapo
ndipo utakapojua miezi tisa ya kubeba mtoto tumboni, na uchungu wa leba ni upi.
Heri umkimbilie myamalize humu ndani. Lasivyo anza kutafuta nyumba ya kupanga.”
“Haiwezekani!” Danny akabisha.
“Hakutanii
Danny. Nina uhakika hutaki haya mambo yaende mbali. Kwa nilivyokuona leo wewe!
Huna stamina yakusimama kwa jaji hata dakika moja. Una jazba. Na kisheria, kwa
kuwa wewe ndio umeomba talaka, ndio utatakiwa utoke pale ndani. Halafu pia,
wakati wote sheria inamwangalia mama na mtoto. Mna watoto wadogo sana. Hata
hiyo kukaa nao kwa mwezi mzima bila uangalizi wa mama yao, tena anayewalilia
watoto! Ni kosa jingine. Ndio maana watu huwa wanapenda kumaliza mambo wao
wenyewe.” Mwanasheria akagongelea msumari.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Bubu kasema. Grace amemjia juu
Danny. Geb amegeuka rafiki zake. Hataki tena urafiki wakushikana miguu. Anadai
pesa zake, hataki tena mahusiano na mtu. Madhara yote yapo kisheria na amemkabidhisha
mwanasheria wa Danny. Katika mashabiki wale wa Danny waliojaa dharau na nia
yakuwakomoa kina Magesa, nani wakufuata nani wa kupuuza. Kitakachowapata??
v Jazba ya Danny yaanza kumrudi yeye mwenyewe. Yupo hatarini kukosa
nyumba na watoto. Je, ataweza kujishusha na
kuzungumza na Grace aliyemwambia hataki kumsikia tena? Hatima ya watoto wao itakuaje?
v Marafiki waliokuwa wakimcheka Grace, wamenyamazishwa baada ya dume Man
kutoa mabusu ya nguvu mbele zao. Hakuna aliyewahi kumuona Man. Mgeni kwao. Man
naye hana kiasi kwenye kubusu. Kabusu
tena na tena bila haraka huku akimsisitiza Grace, yupo nje anasubiri. Kama
aliyekuwa akimuomba Grace asije badili mawazo.
Yapi yatajiri?
Usikose Muendelezo.
0 Comments:
Post a Comment