Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Ni wangu! – Sehemu ya 59. - Naomi Simulizi

Ni wangu! – Sehemu ya 59.

Geb alibaki kimya akimwangalia Nanaa na mwanae pale walipokuwa wamesimama. Hamu ya kuingia ndani bado ipo au ndio atagairi? Ndio swali alilokuwa akijiuliza hata Geb. “Pole sana Liv. Pole mama.” Nanaa akaongea naye kwa sauti ya upole. Liv akaweka kamdomo kadeko kama anayetaka kulia. “Paliuma?” Liv akatingisha kichwa kukubali. “Pole.” Liv akamsogelea mama yake akamkumbatia. “Sasa nisikilize Liv. Unamuona dad?” Liv akatingisha kichwa. “Na aunt Grace si unampenda?” Liv akatingisha kichwa kukubali. “Si dad ni dad mzuri?”  Nanaa akaendelea kumuuliza. Liv akacheka. “Nampenda dad.” Liv akaongea huku kidole kipo mdomoni. “Unajua kwa nini ni dad mzuri?” “Anampenda Liv.” Liv akajibu nakumfanya Nanaa acheke.

“Sawa sawa. Basi ujue bibi ndiye alimfundisha. Bibi akimpenda mtu, anamfundisha huyo mtu mpaka awe mzuri. Si unamuona aunt Grace alivyo aunt mzuri?” Liv akacheka. “Kwa kuwa bibi alimchapa mpaka akawa aunt mzuri. Bibi alikuchapa kwa sababu anakupenda. Anataka kukufundisha uwe mtoto mzuri kama aunt Grace. Si unapenda kuwa kama aunt?” “Nampenda aunt.” “Basi ukiwa karibu na bibi, atakufundisha uwe kama aunt. Lakini uwe unafanya kila anachokwambia ili asikuchape. Kwa kuwa ukiwa humsikilizi, bibi lazima atakuchapa tu. Na atamchapa na dad na mimi, kwa kuwa hatukufundishi vizuri. Wewe unataka bibi amchape dad wako na mama yako?” Liv akatingisha kichwa kukataa. 

“Basi. Akikwambia kitu tena, uwe unamsikiliza na kufanya kwa haraka ili aendelee kukufundisha bila kukuchapa kwa kuwa hatakubali uwe mtoto mbaya. Usipofanya kwa haraka anachokuwa akikwambia ujue unakuwa mtoto mbaya na atakuchapa tu. Tena huwa wakati mwingine anatumia fimbo kabisa kukuchapia ili uwe mtoto mzuri anayekupenda sana. Si unajua bibi anakupenda sana?” Liv akakubali. “Alikuwa anakuogesha. Anakununulia nguo nzuri. Unaona hereni nilizokuvalisha leo?” Liv akakubali. “Bibi alikununulia sababu anakupenda sanaaa.” Liv akakubali.

“Kwa hiyo ukimuona unamkumbatia na kumbusu.” Liv akakubali. “Utamwambia nini?” “Nakupenda bibi.” “Eheee! Atafurahi sana, halafu atakuwa anaendelea kukupenda na wewe.” Geb akavuta pumzi kwa nguvu. Liv akaonekana kuelewa akaongoza njia kuingia ndani, mama yake akamfuata nyuma.  

“Bonyeza kengele mlangoni, sisi tunakuja, Liv.” Geb akamvuta Nanaa nje. “Nakushukuru Nanaa. Lakini nilishazungumza na mama juu ya hilo, akaomba msamaha.” “We Geb! Mama anaomba msamaha wakumchapa Liv!?” Nanaa akashituka sana. “Mimi namfahamu mama yako. Anawapenda sana hawa watoto. Hakuna jinsi eti kuwa alimchapa kwa kuwa anamchukia. Ni vile mwanao anatabia na kichwa kama chako.” Geb akacheka. “Nanaa umenitukana.” “Kweli tena. KaLiv kanachapika. Kana msimamo kweli. Mtu mwenye mambo yake mengi ni ngumu kukavumilia. Na wakati mwingine inabidi kukasaidia.” “Anaakili sana.” Baba yake akasifia. “Ni kweli anaakili. Lakini bila kujenga tabia njema, hatakuwa dada mzuri.” Geb akamtizama. “Kweli mwenzangu umekua! Naona umekuwa na akili za kimama kweli!” Nanaa akacheka. 

“Twende ndani basi. Au wewe utangulie kwanza halafu uje uniite.” “Acha hizo Nanaa. Twende.” Wakaingia. Liv alishakuwa amepakatwa na bibi yake. “Na mimi nakupenda bibi.” Walimsikia Liv akimwambia bibi yake kwa upendo wakati wanaingi. Mama G alikuwa akilia. Nanaa akamuhurumia sana. Alikuwa amenyongea. Wazi alionekana mpweke. Akashindwa hata chakuongea naye. “Mwenzenu njaa inauma, naomba nijikaribishe jikoni.” Nanaa akapitiliza jikoni bila hata salamu kwa mama G, aliyekuwa akilia. 

“Usilie mama bwana! Kila kitu kitakuwa sawa. Watoto wamekuja kukuona. Pata muda nao. Sio na wewe unalia tena.” Mama G akafuta machozi nakubaki kimya. Akamweka Magesa chini. “Vipi, umekula?”  Nanaa akamsikia Geb akizungumza na mama yake. “Midomo imekukauka! Nikuletee maji?” Kimya. “Juisi?” Geb aliendelea kumuuliza mama yake. “Acha kulia mama bwana! Njoo hapa.” Nanaa hakujua kinachoendelea hapo sebuleni. Lakini alijikuta machozi na yeye yakimtoka huko jikoni.

~~~~~~~~~~~~~~~

Ni nyumba ile ile iliyokuwa imejaa furaha, amani na vicheko vya kila wakati. Walikuwa wamejaa humo ndani, mpaka wengine walikuwa hawajui wanaishije mle ndani. Mpaka Liz naye alikuwa akija kulala pale, lakini gafla mama G akabakia peke yake. Bila hata mtoto, wote wakimkimbia kama mchawi. Alilia huyo mama kama aliyefiwa. Mwili ule aliokuwa amejipunguza kwa ajili ya ugonjwa wa magoti, uliisha wote. Na kwa kuwa alikuwa sio mrefu sana, alibaki kama kitoto.   

~~~~~~~~~~~~~~~

Nanaa alibandika chai huku anapika kile alichokikuta kwenye friji. Chai ilipoiva, akaenda kuvuta stuli pale pembeni ya mama G, akamuwekea ile chai ya rangi yenye sukari nyingi kidogo. Ni kweli alionekana hakuwa akila. “Liv, mchukue Magesa mkacheze mbali na hapa. Nimemuwekea bibi chai ya moto sana, sitaki mtoto aungue.” “Twende.” Liv akaanza kumuita kaka yake. “Kunywa hiyo chai mama. Itakusaidia. Unaonekana umekaukiwa.” Geb akamsogezea karibu. Nanaa akarudi kupika jikoni. 

Baada ya muda Geb akaingia na kile kikombe.  “Nakushukuru Nanaa.  Naona  ameinywa yote.” “Chakula kitakuwa tayari muda si mrefu.” Geb akabaki amesimama pale. “Vipi?” Nanaa akamuuliza. “Hamna kitu. Nimesimama tu ili tuwe wote hapa.” “Nenda kakae na mama. Mimi nitakuja muda sio mrefu.” “Una uhakika?” “Nipo sawa Geb. Nenda tu. Nitakuja sasa hivi.” Geb akatoka. 

Nanaa akaendelea kupika kama kawaida yake. Haraka haraka huku akimsikia Geb ambaye si mzungumzaji akijaribu kuongea na mama yake. Mwishowe wakanyamaza kimya. Akajua Geb ameshaishiwa maneno. Ni tv pekee ndiyo iliyokuwa ikizungumza. Akaona Magesa anaingia huku anatambaa. Akacheka. “Liv amekufukuza?” Magesa akacheka. “Wewe unashuguli nyingi kwa wakati mmoja. Mwenzio hawezi mambo mengi kwa wakati mmoja, anaona unamchanganya. Muone. Njaa inauma?” Nanaa akaendelea kuzungumza na mwanae. Akamkatia kipande cha nyanya. “Usijichafue sasa. Kaa hapo ule, halafu nikimaliza kupanga chakula mezani nitakulisha. Sawa baba yangu?” Magesa alishakipokea kile kipande cha nyanya nakuanza kukishambulia.  

“Mbona anashambulia kwa nguvu hivyo wakati ametoka kula, au hakumaliza?” Geb akaingia nakumkuta mwanae amekaa chini kabisa amejaa nyanya kila mahali. “Alimaliza bakuli lote lile. Nikamuongezea na chupa nzima yamaziwa.” Wakacheka. “Ngoja niandae meza. Mwangalie hapo chini.” “Nikusaidie nini?” Geb akauliza. “Labda kumlisha huyo. Kwa kula hivyo, ujue njaa tayari.” Geb akambeba na kumtoa pale chini sakafuni. “Twende ukale.”  Geb  alikuwa  akizungumza  na  Magesa. 

“Muulize mama kama umpelekee chakula pale pale alipokaa au atakuja kula mezani.” Nanaa akamwambia Geb. “Lakini ngoja. Namuona amechoka sana. Mpelekee pale pale.” Geb akanyamaza. “Basi nitampelekea mwenyewe.” “Afadhali. Maana hapo nishachanganyikiwa, sijui nipakue nini niache nini na kwa kaisi gani.” Nanaa akacheka. “Wewe na mwanao Liv, mpo sawa sawa! Mkisikia chakula mnachanganyikiwa.” Nanaa akatoka. 

Alimpakulia mama G chakula, akaenda kumuwekea. “Liv! Njoo uombee chakula cha bibi ale.” Tayari ilishakuwa saa 11 jioni wakati Nanaa ameweka chakula mezani. Liv akaanza kucheka. “Utakula na bibi?” Liv akakataa. “Lazima ule Liv.” “Mwache nitamlisha baadaye. Huyo hawezi kula sasa hivi. Na hivi alikula mchana na asubuhi, hapo mpaka saa mbili.” Baba yake akamtetea. “Ngoja mimi na mwanangu Magesa tuendelee kula. Eti baba?” Magesa akacheka. Liv akaombea chakula cha bibi yake, Nanaa akarudi mezani walipokuwa Geb na Magesa. 

“Njoo ule mwanangu hata kidogo.” Nanaa akazidi kumbembeleza Liv. Liv akawa anakuja kula kijiko kimoja, anakwenda kucheza. Alikula mpaka Nanaa akaridhika ameshiba. “Ana maringo huyo! Mpaka umbembeleze ndio ale!” Liv alishaondoka baada ya mama yake kumuosha mdomo. Nanaa akaanza kula sasa. Alikula kama mwanae Magesa. “Hapa nataka nitafute mahali, nilale. Nimeshiba siwezi kuhema.” Geb alimwangalia huku akicheka. “Si ungekula kidogo, halafu na baadaye ule tena kidogo?” “Na baadaye pia nitakula.” Geb akatingisha kichwa. 

          “Ngoja nikajilaze kidogo.” Nanaa akasimama akataka kutoa vyombo. “Acha tu, mimi nitatoa. Nenda kapumzike.” “Mungu akubariki. Acha nikajilaze, maana hapa nimelevya na shibe.” Geb alikuwa anacheka. “Wewe nicheke kadiri ya uwezo wako. Lakini mwenzio nimeshiba.” “Umenisahau Nanaa.” “Sithubutu na siwezi mpenzi wangu. Cha kwako kipo kwenye poti ile ya chuma, uji nimekuwekea kwenye chupa. Lakini najua sasa hivi huwezi kula. Kwenye saa kumi na mbili na nusu, ukisikia njaa, ujue uji wako upo kwenye chupa. Cha usiku pia kipo.” Nanaa akamalizia huku akiingia chumba alichokuwa akilala hapo zamani kabla hawajahamia nyumba mpya kuishi kama mume na mke. “Asante.” Geb akamalizia kwa kushukuru wakati mlango unafungwa. 

~~~~~~~~~~~~~~~

Hakuwa amezungumza chochote na mama G, akaelekea moja kwa moja jikoni. Akahakikisha kila mtu amekula, ndipo akaenda kulala. Nyumba hiyo hakuwa amelala tokea Liv ni mchanga. Usiku mmoja kabla haijamlazimu kulala hotelini baada ya muda aliopangiwa kurudi nyumbani na Geb, kumkuta barabarani, ndio siku hiyo anarudi. Tena alirudi chumbani kwake, kule alikokaribishwa tokea anaingia nyumba hiyo. Akalala kama aliyekufa kwa kushiba.  

~~~~~~~~~~~~~~~

“Nanaa! Nanaa!” Geb akamwamsha. “Bwana umenitoa kwenye ndoto ya chakula.” Geb alicheka mpaka machozi. “Umeniharibia mtoto wewe! Umeacha chakula mezani, unakuja kukiota na hapa chumbani!” Nanaa akacheka. “Vipi?” “Watoto wanasinzia. Twende wakalale?” “Wapi tena?” “Si kule kwenye apartment?” Geb akauliza. 

Nanaa akafikiria kidogo. Akaangalia kulia na kushoto. “Nilishajisahau. Nimelala hata sijui nilipo. Lakini Geb, hatuwezi kumuacha mama hivi. Siwezi. Naona sitaweza hata kupata usingizi.” Geb hakuamini. “Ndiye mama tunayemtegemea mimi na wewe. Wote hatuna baba. Kajifamilia kenyewe kadogo sana! Hatuwezi kutengana tena. Kama hatajali kuishi na mimi na hii hali yangu, nashauri tubaki naye tu.” Geb akakaa nakujiegemeza.

Mpaka akasikia machozi yanamtoka. Nanaa akakaa. “Silazimishii Geb. Kama unaona nitamkera hapa, basi tuondoke tu. Mimi wala sitajali.” “Hapana Nanaa. Unajua vile Mungu anavyojibu zaidi ya tuombavyo!?” Nanaa akambusu begani, akawa ameshamuelewa Geb. “Naona Mungu ananijibu zaidi ya nilivyoomba. Siamini! Nakushukuru sana Mungu wangu. Na asante mpenzi wangu. Asante sana. 

Naamini mama atapata nafasi ya kukuomba msamaha. Mpe muda. Sasa hivi amechoka sana. Nahisi alikuwa kwenye mfungo.” “Tafadhali Geb! Sipo hapa kwa kuombwa msamaha na mama. Hata mimi nina sehemu ya kumuomba msamaha. Naomba  tumuache kabisa atulie.” “Nashukuru Nanaa. Basi ngoja nikalaze watoto, niende nikafuate mizigo.” “Nishapunguza usingizi, ngoja nikusaidie swala la watoto.” “Wote wanarembua.” Nanaa akacheka, nakutoka pale. “Wote watalala na bibi yao au tuwahamishie chumba kingine?” Nanaa akauliza, wakiwa wanasogelea alipokuwa amekaa mama G na wajukuu zake. 

          “Eti mama?” Nanaa akamuuliza mama G. Bibi yao alikuwa amejiinamia tu. Magesa alikuwa amejilaza kwenye kochi. “Hamuondoki?” Mama G, akauliza kwa upole. “Naona ndio tumefika. Simuoni muondokaji hapa. Eti Liv?” Liv akamwangalia mama yake nakurudisha macho kwenye tv. Geb alishawaogesha wote na kuwabadili nguo. Kwa hiyo wote walikuwa kwenye nguo zakulalia. “Njoo baba  yangu.  Dad  amekupa  maziwa?” “Amekunywa huyo. Usimpe tena.” Geb akamuwahi. “Na ningempa tena, angekunywa.” Wakacheka.

Nanaa akakaa, Magesa akatambaa mpaka kwa mama yake, akambusu na kumkumbatia. “Una usingizi?” Magesa akamwangalia mama yake kwa macho yaliyojaa usingizi. Nanaa akaendelea kumkuna taratibu mgongoni. Magesa akatulia kabisa akiashiria kufurahia anachofanyiwa na mama yake. Nanaa alimbusu mara kadhaa huku akiendelea kumpapasa. “Nakupenda Magesa mwanangu.” Nanaa alisikika kwa sauti ya chini kama akimbembeleza mwanae. Magesa akajiweka sawa, akapotelea usingizini.

 “Mchukue huyu, naona alikuwa anasubiri nimshike tu alale.” “Anashuguli nyingi huyo! Lazima achoke. Ameshazunguka nyumba nzima. Kila mahali yeye yupo!” Nanaa akacheka huku anamwangalia. “Mchukue huyu, nipe Liv wangu. Naona ametulia kama hayupo!” “Usingizi tu. Hapo anategea kama na yeye utamshika.” Bado mama G, hakuwa ametoa jibu. Walikuwa wakisubiria jibu ili wajue inakuaje. Kama wanaondoka, au wanakaribishwa hapo. 

“Njoo mama. Njoo kipenzi changu.” Liv akajivuta. “Mlishaomba na dad?” Liv akatingisha kichwa kukubali. “Ulimuombea mama?” Nanaa akaendelea kumuhoji taratibu. “Nimemuombea mama na Magesa.” “Asante mwanangu.” Akambusu na kuendelea kumpapasa. “Nampenda mama.” Liv akasikika akiongea na yeye kwa sauti iliyojaa usingizi. “Hata mimi nampenda Liv.” Liv akajisogeza zaidi karibu na mama yake. Akambusu na kufunga macho hapo hapo. 

“Naona wote walikuwa wamechoka.” Nanaa alinong’ona. Geb akabakia amembeba Magesa, Nanaa amempakata  Liv. Hawajui chakufanya. Nanaa akamwangalia Geb. Geb akajua ni nini anaulizwa na Nanaa. Lakini na yeye hakuwa na jibu. Mama G, alikuwa ameinama tu, huku ameshika shavu. 

“Mimi naona tumuache mama akapumzike Geb. Tutarudi wakati mwingine.” Nanaa akavunja ukimya. “Mimi nipo sawa tu. Nimekuwa nikilala humu ndani peke yangu! Naona hata usingizi umeniisha.” Mama G akamuwahi Nanaa.  “Nitashukuru kama mtaniachia nilale nao kidogo. Hamu iniishe. Nilikuwa na hamu nao sana.” Mama G aliongea kinyonge.  

“Basi ngoja tukawalaze. Kesho Geb atawatayarishia chumba chao ili kiwe tayari kwa wakati wowote watakapotaka kukitumia.” Geb akashukuru Mungu tena moyoni. “Usisimame naye huyo. Subiri nakuja kumchukua.” Geb akaenda kumlaza Magesa, kisha akaja kumchukua Liv. “Basi mimi ngoja nikaoge. Kwani utachelewa kurudi?” Nanaa naye akasimama na kumfuata nyuma. “Nimeshamtuma Jeri aende kuanza kukusanya vitu kule. Aviweke pamoja. Nikifika kule nikulipia tu, na kurudi. Sitakawia.” “Basi nakusubiria. Sina nguo za kulalia. Nataka kitenge na.. na..”  Nanaa akabaki akifikiria. “Nataka kila kitu. Itabidi nikusubiri tu au twende wote ili nikakusaidie?” “Hamna sababu. Nitakuwa na Jeri. Nitarudi baada ya muda mfupi sana.” Walikuwa wakizungumza kwenye korido.  Mama G akiwasikiliza. 

“Asante.” Geb akanong’ona. Nanaa akatoa tabasamu. “Naenda kujilaza wakati nasubiri taulo nikaoge.” “Nisubiri ili upate mtu wakuongea naye wakati ukioga.” “Basi nakusubiri.” Geb akaondoka pale. Nanaa akarudi chumbani.  

~~~~~~~~~~~~~~~

Geb akatoka pale akapita sebuleni ili atoke nje kabisa akafuate mizigo kwenye apartment. Akamkuta mama yake bado amekaa pale ameinama.“Nenda kalale mama. Usikae tena hapo. Umeshakula, umeshiba, sasa kajipumzishe.” Nanaa alimsikia Geb akizungumza na mama yake. “Unataka kitu chochote?” “Hapana.” “Basi nenda kajilaze kidogo. Nikirudi nitakuja kukuangalia.” “Sawa. Grace amekutafuta?” Nanaa akajiweka sawa. 

“Ilibidi kumtafuta.” “Ulimpata? Yupo salama?” Mama G alisikika ana wasiwasi kidogo. “Kuna kitu kinaendelea kwa Grace.” “Nini tena!?” Geb akafikiria. “Unamkumbuka Grace yule wa zamani? Grace ambaye..” Geb akasita. “Sijui nikwambie nini? Lakini kuna linalo endelea. Sio bure.” “Acha kunitisha bwana!” “Hapana. Sio kwa ubaya. Amechangamka. Anasikika anafuraha. Amenipa ushauri zaidi ya dakika kumi tena akiwa amejawa na tumaini. Grace aliyeondoka hapa siku nane au 9 zilizopita, sie huyu niliyezungumza naye jana.” “Afadhali. Maana yule akiwa kwenye shida au raha utajua tu hata kwenye simu.” “Mmmh! Grace yupo kwenye raha ile anayopenda yeye. Subiri, tutajua tu muda si mrefu. Si unajua hajiwezi akipata jambo lake?” Mama G akacheka kidogo. 

“Tutamsikia hivi karibuni. Amechangamka! ‘She is full of herself’. Kule kukatishwa tamaa, kutukanwa, kukandamizwa, huwezi kupasikia kwenye sauti yake. Anasikika mwenye amani. Namwambia rudi tu, mbona kama umeshapumzika? Anacheka, huku anakataa kurudi. Ila ameniahidi kama Nanaa akikubali nimuoe, atarudi kipindi tupo honeymoon, ili anisaidie mambo ya ofisini mpaka nitakaporudi, ndipo na yeye atarudi tena mapumzikoni.” Nanaa akakaa kwa mshituko. 

“Afadhali. Sasa na wewe umefikia wapi?” Geb akanyamaza kwa muda. “Sijui mama. Nikuendelea kumuomba Mungu.” “Mungu atakusaidia mwanangu.” “Sijui mama. Nahisi kama Danny ameharibu zaidi. Amemjaza maneno machafu sana Nanaa. Hata kama alitaka kukubali, kuna kusita kutakapojitokeza tena. Amemtisha na mambo ya ushirikina na maneno mengi.” “Basi asingekuwa hapa.” Geb akamtizama mama yake. Walikuwa wakizungumza kwa sauti ya chini, lakini Nanaa akajisogeza mlangoni kusikiliza. 

“Namfahamu Nanaa. Kama maneno ya Danny yangemwingia kwa ubaya, asingekuwepo hapa.” “Eti mama!?” “Mwenzio ni mwepesi sana wakuingiwa na huruma yule. Namfahamu Nanaa. Lakini Geb, hakika Mungu amenilipa. Amenilipa bila kunibakiza. Alihakikisha nalipa ubaya niliomtendea huyu mtoto. Mpaka naogopa! Ni rahisi sana kumtendea ubaya mtu aliyekutenda mabaya, lakini si kwa mtu mwema. Mungu hakuachi. Anakupatiliza. Nimegeuka kicheko na dharau mbele za watu wote! Kama vile nilivyomfukuza huyu mtoto, Mungu naye amehakikisha, amemruhusu shetani anifukuzishe mbele za macho ya watu wote! Nilimtenga huyu mtoto na wanae, nami Mungu alihakikisha ananitenga na kila mwanadamu aliyekwisha wahi kuniita mama.” Geb akanyamaza. 

“Wote walinirudi vibaya sana. Mpaka vijana wangu wa dukani wamenikimbia! Nimeletewa funguo na mlinzi wa pale dukani. Wote wamemuaga kuwa hawatarudi tena pale. Wote! Hata Side yule kijana niliyeanza naye ile biashara amenikimbia. Tokea juzi, hapokei simu zangu kabisa. Ikabidi kumuuliza yule mlinzi tena kujua upande wa Side ambaye tumekuwa naye karibu. Nimeishia kuumia zaidi. Maneno machafu yote niliyomtamkia huyu mtoto, Mungu alihakikisha anayarudisha kwangu yakiwa machungu mno.”  Geb alibaki kimya.  

“Kama Nanaa akikataa kuolewa na wewe, ni kwa sababu yangu Geb. Nahisi hajui hata ataishije tena na mimi. Lakini huyu mtoto anaupendo sana. Hakustahili tuliyomfanyia. Hasa mimi. Tena kipindi cha shida yake mbaya! Aibu! Kudhalilishwa! Akilia usiku kucha bila msaada, na bado tuliweza kumuacha sakafuni! Hakika Mungu amenilipa. Amehakikisha nimepita kule alikopitishwa huyu mtoto. Mungu amenionyesha kwa vitendo mkono wake juu ya huyu mtoto. Mpaka nimemuogopa!” Mama G aliongea taratibu. 

“Wote tumepitishwa hapo mama. Wote tuliokuwepo siku ile, nakushindwa kumsaidia Nanaa, Mungu ametuonjesha alichokipata Nanaa. Hakuna kati yetu aliyebaki kama alivyo. Nikiangalia ni kama usiku ule, ilimwagwa roho mbaya sana ya uharibifu. Hakuna kati yetu aliyeweza kusimama katika lile jaribu. Hakuna. Na madhara yake yametoka nje. Ulimwengu unayaona kwa macho.” Geb akaguna. 

“Badala yakumchukia Danny, gafla nimeingiwa na huruma juu yake. Maneno anayozungumza! Yanafanana na ukweli kabisa. Ni kama amevalishwa roho ya ajabu. Tofauti na yeye. Au tuseme imeendana na yeye. Shetani ametumia ukorofi wake, kumuangamiza yeye mwenyewe. Ameweka uongo kidogo tu. Sasa kwa kuwa amejawa na hasira na kiburi, anateseka sana. Ni kama anayetafuta wafuasi kwa anachokiamini. Nilienda siku chache zilizopita kwenda kutizama watoto na kuzungumza naye juu ya hatima yake na Grace!” “Haiwezekanai Geb!” Mama G akashangaa.   

“Grace ni jukumu langu mama. Watoto wao ndio wataishia kuteseka baadaye. Hata kama sasa hivi Danny anawafurahisha, wote tunajua ni kwa muda tu ili kuthibitishia ulimwengu yupo sawa. Lakini mama, Danny anahali mbaya. Nilikuwa nikimtizama vile anavyotukana, ni kama amechanganyikiwa. Anapigana vita kubwa, kwa watu watatu tu! Mimi, wewe na Grace. Anahaha kukusanya jeshi kubwa liwe upande wake.” “Na amefanikiwa.” Mama G akaongeza. 

“Halafu ili iweje? Tuseme amefanikiwa kugeuza watu wote. Halafu itakuaje mama? Hakuna hata kimoja tulichokipata hapa kutoka kwa mganga. Ni mkono wa Mungu juu yetu. Atashindana na mkono wa Mungu mpaka lini? Hujamsikia vile alivyokuwa akimwaminisha Nanaa. Yaani hata mimi kama ningekuwa upande wa pili, ningeamini tu. Halafu jiulize mwisho wake nini?” Geb alikuwa akizungumza kwa taratibu. 

“Nilimkumbusha Danny kuwa asisahau amezaa na Grace watoto watatu. Hakuna faida yeyote watoto wake watapata katika huu ugomvi. Na hakuna mwanamke yeyote atapenda wale watoto kama Grace mwenyewe.” “Akasemaje?” Mama G akauliza. “Wewe unamjua Danny, mama. Alijitahidi kuwa mtulivu ili ahakikishe ananifikishia ujumbe, lakini pia nilimtisha. Nilimwambia ni lazima atulie anisikilize, lasivyo zile pesa anazotangaza kuwa nimepata kwa uchawi, ataona zitakavyoweza kumuingiza matatizoni.”  Mama G akacheka. “Geb!” “Hakika niliamua kumtenda ukorofi sana ili anisikilize.”

 “Ungefanyaje?” “Kwanza unajua nina hisa kwenye kampuni anayofanyia kazi?” “Sijui!” “Basi yeye na James wanajua kama nilinunua hisa pale. Nyingi tu.” “Hongera.” Geb akacheka. “Najua moja ya masharti wanayotakiwa kuwa nayo pale kama wafanyakazi, hasa wa ngazi ya juu, ni kuwa waadilifu. Nikamwambia last time I checked, yeye sio mwadilifu kwa kuwa ametenganisha watoto wadogo na mama yao, tena anaishi na mwanamke wake humo humo ndani ya nyumba wanayoishi familia yake. Akataka kujidai kuwa mkorofi. Nikamkumbusha kuwa nilimlisha na kumlaza nyumbani kwangu wakati yeye anasoma. Wakati yeye anapata elimu shuleni, mimi nilikuwa nikitengeneza mtandao hapa mjini. Tena kwa maombi yakufunga. Nikamwambia kitendo cha kuthubutu kunyanyuka pale tulipokuwa tumekaa kabla yangu, atakijutia daima. Nikamwambia akae chini anisikilize, anijibu, ndipo nitakapomruhusu aondoke. La sivyo hatakaa akasahau jina la Magesa hapa duniani. Nilimwakikishia kutumia kila shilingi niliyonayo kumuweka magotini.” “Geb!” Mama yake alishangaa. 

“Ilikuwa lazima kumfanyia hivyo ili anisikilize.”   “Namjua Danny. Huwa hawezi kusikiliza mtu.” “Basi siku ile alikaa chini. Japo alijibu kwa kiburi, lakini nilipata majibu yangu yote.” “Nini?” “Mama! Ujue Nanaa ananisubiri nirudi?” “Jeri ataleta bwana. Hebu nisimulie kidogo ili nijue naombea nini.” “Kwa kifupi ile ndoa imeshaisha. Danny ameshaandika makaratasi ya talaka, anataka Grace aweke saini yake, wajue mwafaka wa ile nyumba tu. Ila hamtaki tena Grace. Ameapa kwa mbingu na nchi kuwa hamtaki tena Grace.” “Na watoto?” Mama yake akauliza.  “Amesema watapanga na Grace. Hawezi kuzungumzia hilo na mimi. Tena hapo ni baada yakumtisha na kumwambia akileta mchezo, nitahakikisha Grace anabaki na watoto kwa kuwa sheria inamruhusu mtoto kukaa na mama yake mpaka atakapofikisha miaka 7. Labda kama mama huyo hana uwezo wa kiafya au kiakili. Akasema uchawi je?” “Danny!” Mama G akasikitika sana. 

“Nikamwambia  namkaribisha  mahakamani. Tukashindanie hiyo kesi ya uchawi, ndipo atakapojua kama nina uchawi wa namna gani. Atajua nani atakuwa wa mwisho kusimama pale mahakamani. Na nikamwambia mpaka mahakama inamalizana na yeye pale mahakamani, atahamishiwa hospitali ya vichaa. Na nikamwakikishia, nitahakikisha mpaka daktari anakuja kumruhusu atoke hospitali ya vichaa Mirembe, ni pale Fili anaoa. Nikamwambia kama haamini, anijaribu aone.” Mama G akasikika akicheka. 

“Kweli ulimuamulia.” “Ameniudhi sana Danny. Kwanza ukumbuke alivyomsumbua Grace kwenye maisha yake yote. Kila siku fujo zisizokuwa na maana. Tena akisimama kwa jina la wivu. Muongo mkubwa. Wala hakuwahi kumpenda Grace. Danny ni mtu anayependa kutawala mama. Atawale kila kitu. Watu wajue anamiliki kitu cha thamani, ili kujionyesha yeye ni mkuu. Alipoona tunazidi kufanikiwa zaidi yake na Grace anaonyesha kumpita kwa kipato japo yeye analipwa kwa dola, ndipo akaanza fujo. Ubaya ni vile Grace alivyoweza kuwa mvumilivu kwake na bado kumnyenyekea. Ametafuta sababu ndio amepata. Anajidai Grace hafai. Nilimuuliza kwa hasira wakati namnyamazisha. Nilimuuliza kama Grace hakuwa akifaa na anakasoro anazozitangaza leo kwa watu, angekuwa akimfungia chumbani masaa kwa masaa?” “Geb wewe!?” “Kweli mama. Huko ni kunidhalilisha mimi. Hata Nanaa naye alimwambia hivyo hivyo. Alimwambia ni kama kumtukana na yeye.” “Kweli kabisa.” Mama G akaongeza. 

“Sasa nikamwambia nikimsikia anatamka tena mbele yangu kasoro za Grace, ajue atajuta.” “Sasa umemwambia Grace kama talaka inamsubiri?” “Hapana mama. Nimemkuta na furaha sana. Sikutaka kumtibua. Nimemuacha apumzike kidogo. Danny amemtesa tokea hajamuoa. Siwezi kuendelea kuruhusu amtese mpaka sasa.” “Sasa umemwambiaje Danny?” Mama yake akaendelea kudodosa. 

“Tumekubaliana amwachie zile karatasi mwanasheria. Halafu mwanasheria ndio atawasiliana nao wote wawili. Nimemwambia asimtafute Grace. Yupo mapumzikoni. Akirudi, atasaini hizo karatasi.” “Ulimwambia hata Grace naye hamtaki?” “Mjinga sana Danny. Sikutaka kupoteza naye muda zaidi. Nikaondoka. Ujue hapo nilimkuta yupo na wapambe wake wananisubiri!” “Nani?” “Gozi na Zinda. Nikawaomba watupishe. Na wamefurahia sana kuwa eti Nanaa ameniacha. Niliwasikia wakizungumza wakati mimi nazungumza na Danny kwenye sebule ile yao kubwa, wao wamehamia kwenye ile sebule nyingine ndogo iliyojaa vitu vya watoto. Najua walikuwa wakitaka nisikie kwa kuwa hawakutaka kwenda nje, wakahamia pale na kuzungumza kwa sauti tu huku wanacheka.” “Walikuwa wakisemaje?” Mama G akauliza. 

“Eti walikuwa wanacheka huku wakimsifia Danny kuwa yeye ni mwanaume. Haogopeshwi wala hafungwi na pesa. Zinda akawa anacheka anasema kuwa pesa yangu yenyewe haina nguvu kwa kuwa nimeshindwa kummiliki Nanaa. Akasema eti Malii ambaye hana kitu, amefanikiwa kunishinda kilaini, bila jasho. Gozi akadakia akisisitiza jinsi pesa ya uchawi isivyo na nguvu. Zinda akasema ndio maana hata shujaa Danny, mtoto wa kanisani anatutoa jasho!” “Lakini Geb, namlilia Mungu rehema. Hata wao nawaombea rehema. Namwambia Mungu asiwahesabie hatia. Ni uongo tu wa ibilisi.” Nanaa aliendelea kusikiliza.

“Hakuna sehemu ambayo shetani anafurahia kama kukiwa na machafuko kama haya. Ndipo kwenye kiti chake cha enzi. Lazima sisi tunaojua huu ukweli tusimame.” “Sasa mbona kama unajua hilo mbona unazidi kunyong’onyea?” “Geb! Hao watu wa nje mimi hawaniumizi kama nyinyi wanangu. Wewe unanijua mimi. Siogopi mtu hata kidogo. Nilishapambana kipindi cha Magesa, siogopeshwi na maneno ya hao vijana wenzako waliokubali kutumiwa na ibilisi sababu ya wivu! Shetani anaangalia nani amtumie vipi kutokana na kile kilichojaza moyo. Ametumia udhaifu wao wa wivu kwenu, kuwatesa wenyewe wakidhani wananitesa mimi. Danny mwenyewe najua pia alijawa wivu juu yenu. Si rahisi Geb. Si rahisi hata kidogo, kuwaona hivyo mlivyo sasahivi wakati mlikuwa wote pamoja! Mmefanya kila kitu pamoja! Leo wanakuja kukukopa wewe! Umewazidi sana wenzio. Hata jina walilokupa la Milionea, mimi nilijua limejawa wivu tu.”

“Hata mimi nilijua ni kejeli tu.” “Basi. Sasa wakakutafuta kila mahali. Danny naye akahangaika humu ndani, akakuta tumetulia tuli. Amefanya fujo zake zote, tokea anatufahamu mpaka anazaa na Grace watoto hao watatu. Ametutafuta sababu, ameshindwa kutupata. Yeye mwenyewe haelewi tuliwezaje kuishi naye!” “Si ulimsikia alivyokuwa akisema tena kwa kurudia rudia akikushukuru kwa kumpenda na kumvumilia, kwa vile alivyo mkorofi kuliko sisi watoto uliotuzaa?” “Eheee! Sasa ameshindwa kujua ni upendo mkubwa wa namna gani huo. Imebidi afikiri tunampendea uchawi tu. Hamna jinsi nyingine yakueleza jinsi tulivyo mvumilia.” “Na aibu huko mbele ya watu. Anajua wazi hata rafiki zake wanajua jinsi tulivyombeba kabla na baada ya kumuoa Grace. Sasa atajisafisha vipi kuwa yeye hana fadhila, nikusema sio kwamba tulimsaidia kwa upendo, ni kwakuwa tulikuwa tukinufaika naye.” Geb akaongeza. 

“Umeona sasa? Kumbe umelifikiria hilo? Ni kujisafisha tu kwa kutupaka sisi matope. Hilo mimi wala halinisumbui. Huwa ukweli wakati wote utakuja kujitenga na uongo. Iwe leo au kesho, sijali. Wao watakuja kupata majibu yao. Ndio maana huko mimi sihangaiki nako. Ila kipigo ambacho sitaweza kusimama, na shetani anajua ni kuwapoteza wanangu. Grace ambaye ndio rafiki yangu wakaribu sana, mimi ndiye msiri wake, hazungumzi na mimi tena! Japokuwa najua wewe unashindwa kuniacha, lakini sio kama zamani Geb. Nilikupokonya mwanamke aliyekupenda kwa dhati. Tena mlikuwa mmebakisha siku chache sana mfunge ndoa. Katikati ya amani na furaha. Akiwa ndio ametuongezea Magesa kwa mateso makali. Nikamkatili vibaya sana. Kwa kosa gani?” Mama G akauliza. 

          “Ni ubinafsi tu. Ni vile Mungu alikujalia hekima, umeweza kumrudisha Nanaa. Lakini niangalie uharibifu wote niliofanya.” “Sasa si tumerudi?” Geb akauliza. “Lakini haitakuwa kama zamani Geb. Watu wanasamehe, lakini kunauharibifu unafanyika, huwezi kurekebisha.” “Acha kukata tamaa bwana. Nakuaminia. Ukiamua kujenga wewe, hushindwi.” “Mmmh! Hata hivyo nimeshukuru kwa kuamua kurudi kuishi na mimi tena. Siamini Geb. Nasema ni Mungu. Kwa mabaya niliyomtendea huyu mtoto, ni Mungu tu.” 

“Basi kapumzike. Nishakupa habari njema za Grace. Mpe muda tu, atajirudi. Unamjua Grace. Haya, Nanaa amekurudishia wajukuu zako wote. Tena amezungumza vizuri sana na Liv.” “Nilimsikia. Si unajua nilisikia geti likifunguliwa, nikasimama kuja kukupokea. Nilikuwa pale barazani nikikuangalia ukishuka na familia yako mnakuja. Sikuamini Geb. Haya, gafla namsikia na Liv naye ananisemea kwa mama yake! Mimi nilijua Nanaa angekasirika kama wewe na kuamua kuondoka. Lakini nikashangaa jinsi alivyomuweka sawa. Amekuja hapa kweli akanipa busu na kuniambia ananipenda sana.” Wote wakacheka. “Na chakula ameniombea!” “Sasa? Huna haja yakusononeka tena. Mungu anaturudisha kwako. Mimi na Nanaa tupo hapa na wewe. Nanaa naona hataki tena kuondoka hapa. Sasa  unachotaka tena nini?” “Ni kweli Geb. Natakiwa kushukuru.” Geb akatoka. 

Nanaa Na Mama G.

Nanaa akajirudisha kitandani baada yakusikiliza kila kitu. Baada ya muda akasikia hodi mlangoni. Akajua ni mama G. Akakaa. “Karibu mama.” Akaingia. “Naomba nikae hapo kwenye kochi.”  “Nilikuwa nimekukasirikia.” Nanaa akaanza. “Uliniumiza mama. Ukaniadhibu kuliko kosa langu!” Nanaa akaanza kulia. “Geb ameniambia sababu ya kunitenga na watoto wangu. Lakini ungeniambia mimi mwenyewe kuliko ulivyonifanyia.” Nanaa hakujua hasira ilipomtoka.

“Ulinitukana na kusema nampendea Geb pesa zake. Lakini sio kweli mama. Nilimpenda Geb kabla hata sikujua kama anapesa. Hata wewe mwenyewe kuna kipindi ulikiri simpendei Geb pesa. Lakini ukaja kunigeuka. Halafu ukamtafutia msichana mwingine! Umeniumiza sana mama. Sana. Lakini nimesamehe. Yote nimesamehe.” Nanaa akaendelea kulia. Ni kama alijawa na jazba iliyomfanya aongee bila kufikiria.

Mama G alikuwa kimya akisikiliza shutuma zake pale kwenye kochi. “Nanaa mwanangu, wala sio wewe peke yako uliyenikasirikia. Hata Mungu wako alinikasirikia na kuniacha yanipate yale yote niliyotaka yakupate wewe.” Mama G akaongea kwa upole. “Grace alinipigia simu. Akaniambia neno gumu kweli. Akasema hivi, ‘kaburi ulilomchimbia Nanaa, nimetumbukia mimi’. Wala hakukosea. Nimevunja ndoa ya mwanangu mimi mwenyewe kwa mikono yangu.” “Hapana mama. Danny ni muongo. Wala asidanganye. Alitafuta tu sababu. Yaani msiba wangu mimi aufanyie matanga yeye! Muongo kabisa.” Nanaa akaingilia. 

“Lakini Nanaa, hata nikikataa, Danny anaoa mwanamke niliyemleta mimi! Nimehusika kumletea mke Danny. Niambie wale watoto watatu watakuja kukua wajue hilo! Wanakuwa mbali na mama yao au baba yao, kisa bibi alileta mwanamke mwingine!” “Hiyo watakulaumu mama. Wala si uongo. Kama ambavyo Magesa na Liv ambavyo wangekulaumu.” Nanaa akazidi kumuumiza. 

Mama G akanyamaza. Nanaa akazidi kumuhurumia. Akajua anazidi kumuumiza. “Ila mimi nimekusamehe. Kwanza nilikuwa na hamu na wewe!” Mama G akacheka kinyonge. “Hujabadilika Nanaa!” “Nimekata nywele mwenzio.” Wakacheka tena kidogo. “Nashukuru umerudi Nanaa. Niliipata habari yangu hapa! Sina hamu.” Nanaa akacheka sana. “Nani alikukomesha zaidi? Danny?” “Umbea hujaacha wewe mtoto!” Nanaa akacheka sana. 

“Bwana nisimulie mama. Atakuwa ni Danny tu. Maana amejawa jazba!” “Sara pia alinikomesha.” Nanaa alicheka sana. “Nanaa kwa kupenda stori! Sasa hapo unacheka nini?” “Niambie stori za Sara. Maana nimezipata nusu nusu kutoka kwa Jeri. Maana Jeri alikuwa akiniambia kuwa yeye ndio amegeuka kuwa dereva wake. Anampeleka kwa mashoga zake na sehemu zote anazozitaka Sara. Sasa akawa ananipa stori zote. Mazungumzo yake na mashoga zake. Mambo anayozungumza kwenye simu na wakikutana na hao mashoga zake. Jeri anasema akaujua mji na mitaa yake. Mpaka maduka ya kienyeji alikuwa akimpeleka kwenda kununua Shabuu!” Wawili hao wakaanza kusimuliana stori tokea walipoachana. Nanaa alikuwa anacheka sana.  

“Na alikukomesha.” “Sio kidogo! Alikuwa akinitoa pesa kama ATM! Hana analofanya.” “Sasa subiri akale dola za Danny.” “Hawana muda mrefu. Mimi namfahamu Sara na Danny. Ni kama ukutanishe moto na petrol. Vitakuja kulipuka muda si mrefu.” Stori zikanoga. 

Vicheko vikaendelea humo chumbani. Geb akaingia akashangaa. Nanaa alikuwa akicheka mpaka machozi. Yeye kajilaza kwenye kitanda, mama yake kwenye kochi. Wanacheka. Wanabadilishana maneno huku wakicheka sana. Geb akabaki amesimama mlango. Nanaa akakaa. “Pole.” “Nimekuta Jeri ameshakusanya kila kitu. Kwanza hapakuwa na vitu vingi. Vipi nyinyi?” “Mimi naenda kulala.” Mama G akasimama. “Usiku mwema.” “Na wewe mama.” Nanaa akajibu, akatoka. 

~~~~~~~~~~~~~~~

“Sasa unashangaa nini?” Nanaa akauliza huku anacheka. “Kweli umeamua kujenga mama.” “Nilikuwa na hamu na mama bwana. Ujue mama ndio alikuwa rafiki yangu wakaribu sana?” “Alikuwa au ni rafiki yako?” “Vyote bwana. Sitaki kuendelea kumpa shetani nafasi. Ashaharibu vyakutosha. Atoke na atuache kwa amani.” “Now you are talking!” Geb akasifia. 

          “Sasa mbona uko huku tena sio kile chumba kingine kikubwa?” “Kile ulichokuwa ukilala na Liz? Akuu!” Nanaa akakataa. “Nilibadili kila kitu.” Geb akatetea. “Kumbuka Nanaa. Nilibadili kitanda, mashuka, kila kitu.” “Lakini ndio chumba ulichokuwa ukilala na Liz. Mimi sikitaki. Nitalala hapahapa. Najihisi kama mimi nakula makombo yake! Akuuu! Wewe nenda kalale huko.” “Usinifukuze bwana Nanaa! Nionyeshe hata kama unanihitaji basi!” “Samahani mpenzi wangu. Haya njoo tulale hapa.” “Hayo ndio maneno. Ngoja niingize vitu vyako. Jeri ameacha kila kitu barazani. Sikutaka aingize, aamshe watoto.” Geb akatoka. 

Nanaa akajitahidi kumsaidia kupanga vitu vyao pale ndani. “Ona vilivyotoshea. Tunatosha kabisa hapa. Halafu kile chumba chako ukapange vitanda vya watoto.” “Naona tukifanye cha wageni tu. Lakini Liv anahitaji chumba chake. Hawezi kuendelea kulala na Magesa anayeamka usiku kula. Anamsumbua mwenzie.” Nanaa akanyamaza. Akajua wazi ile nyumba haina vyumba vyakutosha kuwa wao wapate chumba chao, Liv chake, Magesa chake, Mama yao na pia wapate cha wageni! Ni nyumba iliyokuwa na vyumba vinne tu. Kwa maana nyingine warudi kwenye nyumba kubwa.  Nanaa hakuwa tayari.

“Nitaanza kumlisha chakula kizito usiku, ili alale mpaka asubuhi.” “Atazidi kuwa mzito Nanaa. Kumbuka tulivyoambiwa tulipompeleka kliniki. Ameshazidi uzito. Ni heri tuendelee kumlisha vyakula vyepesi usiku, tusimwaribu mwili.” “Mimi sipo tayari kurudi kwenye ile nyumba nyingine Geb.” “Hamna haraka. Nitamtayarishia Liv kile chumba walichokuwa wakilala kina Grace. Atakuwa sawa tu. Na Magesa anaweza kulala na mama au tukamuweka hicho chumba cha wageni.” Nanaa akanyamaza.   

Ukweli Wa Yote.

Maisha ya amani na utulivu yakaanza hapo ndani. Kama kawaida ya Nanaa na mama G, kuamka asubuhi na kukutana jikoni kucheka. “Sasa hapa ni kupendeza na kwenda mbele!” Mama G akacheka. “Kweli mama. Yale aliyokusudia shetani kutuangamiza, yageuke kuwa baraka.” “Sasa mbona humtaki mwanangu?” Nanaa akanyamaza. 

 “Eti Nanaa? Au ni kwa vile nilivyokwambia unampendea pesa?” “Ndiyo.” Mama G akaanza kucheka. “Usicheke bwana mama! Mwenzio nalia.” “Sasa na wewe Nanaa, jambo haliishi? Kwa hiyo unataka kunithibitishia kuwa humpendei pesa kwa kumkataa mziwanda wangu?” “Sasa je? Kila mtu anasema nampendea pesa wakati mimi wala sijui Geb anakiasi gani cha pesa huko benki. Sijui chochote juu yake,  zaidi ya kumjua Geb mwanaume niliyempenda basi! Hata mkiniambia leo Geb amefilisika, mimi sitajua na wala haitanithiri kwa kuwa mimi sijui anamiliki nini. Watu wananionea tu.” Mama G akazidi kucheka. 

“Heri nimuache na pesa zake.” Nanaa akafuta machozi. “Ngoja Sara arudi.” “Bwana mama!” “Si umesema humtaki wewe? Sasa ngoja Sara akusikie.” “Namtaka bwana.” “Kwa hiyo?” “Mimi nasita mama. Watu wengi wanamwangalia sana Geb. Kila mtu anataka kujua huyo atakayeolewa na Geb ni nani. Kuna siku tulienda naye kwenye kikao cha harusi cha Zena. Yaani mama, mpaka ikabidi tuondoke. Kumbe Yasini ambaye ni mume wa Zena sasa hivi, anafahamiana na Geb. Ndiye anaye hizinisha malipo ya Geb huko Geb anapopeleka mazao yake, halafu yule Jeff, kumbe anafanya kazi benki. Sasa sijui anajua Geb anakiasi gani cha pesa huko benki! Yaani mama, mpaka ikakera. Wamechanganyikiwa, hamna hata anayeweza kuzungumza tena. Kila mtu amechanganyikiwa kisa Geb Magesa yupo hapo! Hata marafiki zangu walishindwa kuniongelesha. Tukaona tuondoke tu.” Nanaa akaendelea.

“Haya juzi napo nilikuwa na Jeri sehemu, akanitambulisha kwa mtu kuwa mimi ni mama watoto wake Magesa, nikaona vile yule baba alivyobadilika gafla baada ya ule utambulisho, nakuanza kunitetemekea. Nitapoteza marafiki halafu watu wanaanza kunitizama mimi kama doli la Geb! Akuu!” “Wewe olewa mtulie na mwenzio. Umri unazidi kwenda. Halafu unazidi kumtesa mwanangu. Mnalala naye halafu hapati kitu!” “Mama wewe! Umejuaje?” Nanaa akashituka sana mpaka akamgeukia mama G. 

          “Mimi mtu mzima Nanaa. Na hiyo kitu ni muhimu si kwako tu, hata kwake. Mnatesana bure wakati wote mnahitajiana. Olewa mfunge hilo swala.” Nanaa akanyamaza. “Unanielewa Nanaa?” Kimya. “Kwanza hizo sababu zote ulizonipa hazina hata uzito. Wewe niambie ukweli kinachokufanya usite tena kuolewa na mwenzio ni nini. Wakati mmehangaika miaka na miaka!” Kimya. Akamuona Nanaa anaanza kufuta machozi.

“Ni nini?” “Naogopa mama. Naogopa sana. Ujue tangia wakati ule naogopa hata kujishika huko? Sijui hata kunafananaje tena. Ni aibu hata kwenda kwa daktari. Najua natisha sana huko chini. Nimeshindwa hata kujisafisha! Lakini siwezi kujisaidia.” Nanaa akaendelea kulia.  

“Mimi naelewa Nanaa. Najua kabisa. Lakini lazima ukubali kupona katika hilo eneo. La sivyo utafungua milango mingi sana. Mshinde shetani. Shinda hofu. Jua unaolewa na mwanaume unayempenda na aliyekukubali hivyo ulivyo. Huna chakuficha. Na ujue kukubali kwako kutulia kwenye ndoa kutawanufaisha sana wanao. Unawapa wanao maisha ambayo hata pesa haiwezi kuwapa. Umeona jinsi wanao walivyo changamka? Unataka kufungua mlango wa kuwatesa bure wanao. Funga huo mlango, ijulikane Geb ni mumeo na baba wa watoto wako. Basi. Hakuna atakayeweza tena kukugusa. Kwa kuwa utakuwa na mamlaka kama Geb. Sio hivyo upo nusu nusu.” Nanaa akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha. Akanyamaza huku akifuta machozi. 

~~~~~~~~~~~~~~~

Usiku wakati anajiandaa kwenda kuoga wakati watoto wake wamelala, Geb akamuita. “Njoo kwanza kabla hujaenda kuoga.” Nanaa akakunja uso. “Usiogope. Siwezi kufanya kitu ambacho hutataka Nanaa. Naomba niamini.” Nanaa akasogea pale kitandani. “Lini unaenda tena kumuona daktari?” “Kesho kutwa.” Nanaa akajibu akiwa na wasiwasi. “Basi naomba leo nikusafishe.” Nanaa akaanza kulia. Ni kweli hakuwa amejisafisha zaidi ya miezi sita. Akajua Geb alisikia mazungumzo yake na mama yake. 

“Hapana Geb. Nitamuomba dada Fifi anisafishe. Najua nitakuwa natisha.” “Uliniahidi nini?” Kimya. “Eti Nanaa? Sio wewe ulisema tunarudi kuaminiana tena? Mbona tunaenda mbele na kurudi nyuma?” “Basi labda nikaoge kwanza, nitakuwa nanuka san..” “Nanaa! Ni mimi Geb. Njoo hapa.” Geb alipiga kitanda, akatengeneza mto vizuri. “Njoo ulale hapa.” Nanaa alikuwa na taulo tu, alikuwa tayari kwenda kuoga. Akajilaza taratibu.  

Geb akaanza kumsafisha kwa kuanza kulainisha msitu aliokutana nao huko chini na shaving cream. Ni kweli alionekana hakuwa amejisafisha muda mrefu. Geb aliendelea taratibu bila haraka wala kinyaa. Nanaa alijua hadha anayokutana nayo huko chini. Lakini akaamua ananyamaze na kutulia tu. “Nakuumiza? Naweza kuongeza shaving cream.” Geb akauliza. “Hapana. Nipo tu sawa.” Geb akaendelea kumsafisha. Alipomaliza kutoa nywele zote, akaenda kuchukua kitaulo kidogo na maji ya vuguvugu bafuni. Akaendelea kumsafisha kila mahali taratibu mpaka akamaliza. 

“Naona sasa hivi hata tukienda kliniki daktari hatanishangaa.” Geb aliongea huku akimfuta vizuri. Nanaa akacheka kidogo huku akijifuta machozi. “Sasa hivi, ruksa kuoga.” “Asante. Nakushukuru.” “Karibu.” Akaelekea bafuni kuoga na kumuacha Geb akisafisha pale. 

Alibadili mashuka wakati Nanaa akioga, alipomaliza kuoga na yeye Geb akaingia kuoga. Alitoka na kumkuta Nanaa amejilaza kitandani na yeye akaenda kujilaza karibu ili abembelezwe kama wanae.  “Nilimsikia mama akisema usuke? Unataka kusuka lini?” “Unapenda nisuke?” Nanaa akauliza. “Unapendeza zaidi ukisuka.” Nanaa akacheka kidogo. “Kwani ile ofa ya kunioa bado ipo?” “Ukikubali hata kesho, tunabariki ndoa yetu.” “Kweli?” Nanaa akamchungulia vizuri usoni kama anayetaka kupata uhakika.

“Sasa tunasubiri nini Nanaa? Mpaka Liv anaongea, Magesa anakaribia kutembea, na mdogo wao anakuja, sisi bado hatujakamilisha hilo jambo! Mwenzio sina kipingamizi.” Nanaa akafikiria kidogo. “Lakini bado mwenzio natamani kuvaa shela.” “Hilo halina tatizo. Unataka nini tena?” “Wewe uwepo.” Geb akacheka.  “Hayo umepata. Tena Grace ameniambia ukikubali tu nimwambie arudi kukusaidia kuandaa hiyo harusi.” Nanaa akafurahi sana. “Basi mwambie Grace bibi harusi yupo tayari kwa ndoa. Kesho nampigia msusi wangu simu aje anisuke vidogo vidogo. Nikichoka, atakuja kunimalizia kesho kutwa baada ya kliniki.” Nanaa akakaa. 

“Nataka gauni refuuuuuu!” Gafla Nanaa akaanza kuchangamka. Geb akawa anacheka. “Nataka..” Akamuona amekwama. “Nini tena?” “Sijawasiliana na kaka James tokea siku ile!” “Tutamfuata kwake na watoto.” “Kweli!?” “Naona hiyo ndio itakua heshima. Ngoja kwanza twende kliniki hiyo siku ya jumanne. Tuzungumze na daktari tujue afya yako. Akisema wewe na mtoto mpo sawa, nafikiria jumamosi ijayo tufunge ndoa.” Nanaa akaanza kucheka. “Siamini Geb!” “Kwa hiyo umekubaliana na siku ya jumamosi?” “Ni sawa. Wapi sasa?” Nanaa akauliza. Geb akafikiria kidogo. 

“Nafikiria harusi ndogo tu. Sitaki watu wengi kwa sababu za kiusalama. Ni familia yetu tu, James na mchungaji basi.” “Sawa. Lakini nani atatusimamia? Au nimuombe Zena?” “HAPANA!” Geb alikataa kwa nguvu mpaka Nanaa akashituka.  

“Geb!” “Simtaki Zena. Sitaki aje awe kwenye maisha yetu tena. Sio rafiki mzuri kwako. Yupo kushindana na wewe tu. Naomba unielewe Nanaa. Simtaki Zena awe kwenye maisha yako.” “Basi Geb. Naona safari hii badala ya kumblock tu, nitamtumia ujumbe wa kumwambia rasmi nasitisha mawasiliano naye. Asinitafute tena. Nitakuwa muwazi kwake. Hata hivyo wote tumeona madhara ya marafiki waliojaa hila mioyoni mwao huku wakituchekea. Inatosha.” “Kabisa. Na kama utafanya hivyo itakuwa vizuri. Umemvumilia vyakutosha. Nataka tuanze upya na watu watakao tupenda na kutukubali kwa vile Mungu alivyotubariki. Sio kuonea aibu baraka zetu! Hapana Nanaa. Hata mimi nimevumilia vyakutosha. Mtu hawezi kuniona ninapesa na kunifurahia, inamaana huyo sio mtu wa hatima yangu. Akae pembeni. Sitajifanya mjinga tena. Sina sababu. Utajiri sio adhabu hata kidogo! Lazima wajue na wakae pembeni. Zena ni mmoja wa marafiki tutakao watoa kwenye maisha yetu.” “Nimeelewa Geb. Nitazungumza naye. Nakuahidi hutamsikia tena.” “Asante.” Nanaa akamuona ameridhika.  

“Nitamuomba Grace anisimamie.” Geb akamgeukia vizuri kama haamini. “Wewe hujui jinsi Grace anavyonifaa. Huwa anazungumza na mimi vizuri sana tena bila kunificha. Akiwa msimamizi wangu ndio itakuwa vizuri zaidi.” “Na kashfa zote hizo ulizopewa, bado unamtaka Grace!?” “Danny mwendawazimu yule. Achana naye.” Nanaa akapuuza. “Samahani kusema hivi Geb. Lakini nahisi Danny alikuwa ni kama akitafuta tu sababu. Ameishi na sisi wote muda wote,  hapajawahi hata kuonekana dawa ya kienyeji, ya miti shamba humu ndani. Kwanza hata shetani mwenyewe huwa hatajwi sana hapa kwenu.” Geb akacheka. 

“Kweli Geb. Wewe msikilize mama yako kwa makini. Utagundua jina la shetani kulitaja ni mara chache sana. Ungekaa na mama yake James ndio ungeelewa ninachozungumzia. Shetani amepewa nafasi kuliko Yesu. Kila neno ni shetani. Hana jambo linalotokea kwake ikawa si shetani. Sasa eti leo uishi na wachawi, usijue! Hakuna mtu aliyelogwa akasema nimelogwa. Muongo tu. Na anatumia ukorofi wake vizuri tu. Ni kama alimpendea Grace pesa. Sasa amefanikiwa ndio anatoa makucha yake.” Geb akanyamaza kidogo.  

“Yeye si anasema alilogwa ndio maana akawa kama mjinga kumng’ang’ania Grace? Tumeishi nao wote hapa. Alivyokuwa akimfungia mkewe ndani huko siku nzima, tena kwa kumg’ang’ania yeye mwenyewe, kama angekuwa na kasoro anazozisambasa sasa hivi, si tungezijua tokea zamani! Kwanza tendo la ndoa kwao ingekuwa shida. Yaani ingekuwa mara moja moja kwa sababu kuacha kabisa angesema alishindwa kwa kuwa amelogwa. Au angesema Grace alikuwa akimlazimishia. Lakini kutwa alikuwa anamfungia Grace humo ndani. Grace alikuwa hawezi hata kuzungumza na mama humu ndani, sababu ya kumng’ang’ania kama hatosheki na huyo Grace! Mnafiki tu na muongo. Acha na Danny.”  

“Kazua uongo na bahati nzuri kakutana na marafiki zenu wanaokuonea wivu au wanaowaonea wivu. Wanaona mlikuwa wote kwenye shida, sasa hivi mmewapita. Ndio wanatafuta sababu. Kwanza mimi sijaona hata wakulogwa pale kwenye kundi lenu.” Geb akacheka. “Kweli tena Geb. Nani alogwe pale. Zinda?” Nanaa akauliza. “Ili mtu achukue nyota ya ulevi na umalaya kama Malii? Haya, Danny?” Nanaa akauliza tena. 

“Tena yeye ndio anyamaze kabisa. Wanaume waliologwa na wake zao wanakuwa kama Danny!?” Nanaa akaendelea. “Mwanaume aliyelogwa wewe ukimuona utamjua tu. Hawi mkorofi. Mpole na anakubali kila kitu. Danny alikuwa amejaa humu ndani utafikiri yeye ndio mwenye nyumba! Akianza kukoroma humu ndani mpaka wale waliokuwa wakija kusafisha nyumba walikuwa wakimuogopa, wakawa wakijua Danny ndio Magesa! Amejaa kuanzia getini mpaka ndani! Anasema amelogwa! Muongo tu.” Nanaa akakasirika kabisa. 

Kisha akamgeukia Geb. “Kwanza naomba uniambie ukweli Geb. Maana nasikia tu kwa watu.” “Unasikia nini?” Geb akauliza. “Kuwa wewe ni milionea.” “Wewe utawaweza watu Nanaa? Uzushi tu.” “Hapana Geb. Watu wanakuogopa. Namaanisha wanao kufahamu wewe. Wanaofahamu mali zako, wanakutetemekea. Unakumbuka jinsi Yasini na Jeff walivyo changanyikiwa baada ya kukuona siku ile tulipoenda kwenye kikao cha harusi? Kila mtu alikuwa akinong’ona kwamba wewe ndio Magesa! Haya, juzi nilipokwambia namtaka Jeri aje anipeleke sehemu. Ili nimwendeshe huku ananiangalia. Kuna sehemu tulienda, akanitambulisha kama mama watoto wako, na tulikuwa na kina Liv na Magesa. Yule baba akachanganyikiwa mpaka akawa mjinga na kunikera zaidi. Nikamwambia Jeri tuondoke tu pale.” Geb akawa kama anayefikiria. 

“Labda uniulize swali jingine. Lakini mimi sidhani kama ni milionea. Bado nina ndoto kubwa sana ambazo bado sijatimiza. Natamani kipindi mimi na wewe tunafikia uzeeni, pesa itutumikie sisi. Tuwe tumewekeza kiasi kwamba Magesa na ndugu zake wakikua, wanachagua kitu chakufanya kwenye miradi yetu. Wao na familia zao wawe na urithi wakutosha. Sasa ukiniita mimi ni milionea wakati tuna miradi tu hapa Dar. Tena sio Dar yote, sijioni kama mimi ni milionea, Nanaa.” Geb akafikiria kidogo. 

“Bado naona nina kazi kubwa yakufanya kuliko nilipo. Kuna kipindi, tena sio mbali, nilitaka kufikiria kuwa nimeshafanya kazi kubwa yakutosha, lakini nikakaa ofisini kwangu nikajiuliza maswali magumu. Tena niliyaandika chini. Nilijiuliza kutokana na nchi yetu ilipo, inapokwenda na tulipotoka.” “Ulijiuliza maswali gani?” Nanaa akataka kujua. 

Geb  akacheka. “Usicheke  bwana!” “Hapana. Nimefurahi umeniuliza. Ila moja ya swali nililojiuliza ni hili, kwa teknolojia inavyokwenda kwa haraka. Uchumi unavyobadilika mchana na usiku. Je kwa jinsi nilivyowekeza mimi, nitakuwa na uwezo wakusimama kwenye soko kwa muda gani? Unakumbuka stori ya baba yangu na ufugaji aliokuwa anafanya?” “Nakumbuka.” Nanaa akajibu. 

“Lakini aliniambia anguko lake lilifika pale walipokuja kuanzisha kiwanda cha kisasa, lakini walifanya biashara kama yake. Kwa hiyo wakachukua masoko yake yote, biashara yake ikaporomoka. Sasa mimi sitaki nifike huko. Pesa yote niliyonayo benki au popote kule, nimejiambia sio yangu. Lazima kuzidi kuwekeza zaidi na zaidi. Kujipanua. Kutafuta kitu cha kudumu ambacho hakitaondoka sokoni. Kuwe kuna ukame au kuna neema.” “Kama chakula?” Nanaa akauliza. “Ewaaa! Sawa sawa. Ndio maana sitakaa kuacha biashara ya chakula. Tajiri na masikini, mgonjwa na mzima wote watataka kula. Ndio maana nimewekeza sana kwenye hiyo biashara. Na ninajitahidi kufikia watu wote. Tukitoka kwenye honeymoon kabla hujajifungua, nitakutembeza uone nilichofanya, ninachofikiria kufanya ili na wewe unishauri.” “Sasa mimi nitakushauri nini Geb!” Nanaa akajidharau. 

“Usijidharau hata kidogo. Na usinione hivi mimi. Hata Jeri huwa nakaa chini na kumsikiliza. Wakati mwingine huwa namchukua kwenye gari yangu tunakwenda naye safari ya mbali kidogo, ili kujua kinachoendelea mtaani kwa watu wa kiwango cha chini, kawaida na vijana. Uhitaji wao ni nini. Na mimi naingia wapi hapo? Kwa hiyo akiwa haendeshi, mimi namwendesha, huwa anakuwa na wasiwasi sana. Na hapo anaongea sana.” Nanaa akacheka.  

“Na Jeri alivyo mpole!” “Na ananiogopa sana. Kwa hiyo huwa anaongea kupita kiasi ili tu kujituliza.” “Geb wewe!” “Mjini hapa Nanaa. Lazima kuishi na watu kwa akili. Kwa hiyo anapata muda wakupanda gari yangu na kuendeshwa na mimi. Wakati mwingine huwa nampeleka kupata chakula. Huku na mimi napata yanayoendelea kila mahali mpaka kwa wafanyakazi wengine. Kila mtu anajua nampenda sana Jeri. Lakini hawajui vile ninavyonufaika naye.” “Na yeye ananufaika.” “Sio kama mimi. Yeye analisha familia yake tu. Lakini mimi ananisaidia katika maeneo mengi sana. Si kwenye biashara zangu tu, mpaka nyumbani. Ni mtu ambaye sina wasiwasi akiwa na pesa yangu au kitu changu cha thamani. Naweza kumtuma anipelekee Liv wangu popote, na nikawa na uhakika Liv atafikishwa salama. Lakini sithubu kufanya hivyo kwa mtu yeyote yule. Hata Zinda siwezi kumuachia Liv.” Nanaa akashangaa sana. 

“Kwa hiyo, fikiria maswali yote unayotaka kuniuliza, tukiwa honeymoon utapata muda wakunifahamu zaidi.” “Honeymoon itakuwa wapi?” “Hatuwezi kwenda mbali sababu ya afya yako na watoto. Ukijifungua ndipo tutaweza kusafiri, lakini sasa hivi naona tutulie tu.” Nanaa alijawa na furaha sana.   

“Safari hii lazima tuoane Geb.” “Nimemuomba sana Mungu hiko kipengele tukikamilishe. Unajua nilijua ni rahisi sana! Nikajua ni mipango tu. Na nikajua kama mipango yangu mingine inavyofanikiwa, ndivyo na hilo litakavyofanikiwa kwa haraka. Lakini daah! Kila tukipanga hiki, kinatokea kitu. Safari hii nimemuomba Mungu aingilie kati. Naamini atatusaidia.” Nanaa akambusu shavuni. Geb akacheka. 

“Eti umezidiwa sana?” Nanaa akauliza kwa aibu huku akicheka. Geb akaelewa. “Naweza kusubiri mpaka jumamosi tukifunga ndoa. Usijali.” Nanaa akamwangalia kwa kumuhurumia. “Pole.” Geb akacheka. “Naomba kesho upokee simu ya Grace. Nitamwambia akupigie ili mpange zaidi.” “Sawa.” Akambusu.  

~~~~~~~~~~~~~~~~

Simu ya Nanaa ikaingia ujumbe. “Nani tena?” Geb akauliza kama wamesumbuliwa. Nanaa akasoma. “Msusi. Nilimuomba aje na watu wanne ili nisikae chini muda mrefu, halafu nikamuuliza kama anaweza kupata aina za nywele ninazotaka. Ndio amenijibu.” “Anasemaje?” “Amepata watu na nywele atazifuata asubuhi kabla ya kuja hapa. Ila anasema itanigarimu sana.” “Naomba usuke Nanaa.  Tena wakiwa wengi ndio vizuri ili usikae sana na waondoke kabla sijarudi kutoka kazini. Nisingependa niwakute hapa.” Nanaa akacheka. “Basi ngoja nimwambie sawa.” Nanaa akajibu. 

“Nimemsisitiza wawahi asubuhi sana. Nimemwambia akiona wamechelewa kuja, basi. Tutapanga wakati mwingine.” “Lakini Nanaa, nataka kukushukuru?” “Nini tena?” Nanaa akaweka simu chini na kumgeukia. “Kuweza kuweka pembeni yale yote tuliyokutendea na kuirudisha hii nyumba kwenye hali hii!” Geb akajiweka sawa. “Sio jengo.” Nanaa akacheka. 

 “Namaanisha hivi ilivyojaa amani na utulivu! Hata mama ameanza kutulia sasa hivi. Nimerudisha mapenzi na Liv wangu. Nakwenda kazini, najua narudi nyumbani kwa Nanaa na wanangu. Naamshwa na vicheko. Sina hofu yakutoka chumbani labda nitakutana na sura za matatizo. Kila mtu anacheka! Nakushukuru sana mpenzi wangu. Najua sio rahisi, lakini umeweza kunipa ‘home’. Sehemu ninayokimbilia kupumzika baada ya mihangaika na kelele za hili jiji.” “Asante kushukuru Geb.” Nanaa akajisikia vizuri kutambuliwa juhudi zake. Ni kweli alisamehe kwa ajili ya Geb. 

“Na mimi nakushukuru kunirudia Geb. Asante. Umesimama na mimi kipindi ambacho hakika nilikuwa nakuhitaji. Unakumbuka siku umekuja kuniona pale hospitalini?” Nanaa akaanza kulia. “Najiona nilichelewa.” “Hata kidogo Geb. Ulikuja kwa wakati sahihi. Nilikuwa nimekata tamaa. Kifo pekee ndio nilikuwa natamani. Nilijawa aibu ya mtoto ambaye sio wako. Nilijichukia na kujionea kinyaa mimi mwenyewe. Kitendo cha kushika huko chini kwangu, nilikuwa nakichukia nilikuwa najiambia ni kama nashika mauchafu gani sijui! Nilijichukia mimi mwenyewe hata mtoto mwenyewe. Nikajiambia labda nimpe jina la Jimmy, pengine nitampenda kama kaka, lakini wapi. Mandoto mabaya yakutaka kubakwa kila siku usiku ndiyo yalikuwa yakinipandisha presha.”

Lakini sasa hivi mpaka presha imerudi kuwa yakawaida. Mzima, mpaka yule daktari wa moyo alikuwa akinishangaa juzi ijumaa, nilipoenda na mama. Napata muda na Jimmy wangu. Naona hata nikimwambia kitu ananisikiliza. Akikaa upande nikiumia, namuomba ahame, anahama. Naomba naye. Tunazungumza wote wanne. Liv pia anambusu. Kaka mkubwa naye anambusu. Japo kwa kupaka mate.” Wakacheka.

“Nakushukuru kwa kuja kutuokoa mimi na Jimmy. Asante.” Geb akambusu tumboni. “Na furaha itaongezeka jumamosi zaidi kwenye fungate yetu. Nina hamu na wewe Nanaa! Mpaka huwa nikikungalia naumia.” “Pole Geb.” “Tena safari hii hakuna mtoto anayenyonya! Nitafaidi peke yangu kwa kipindi cha kama mwezi na siku kadhaa.” Nanaa akacheka sana. “Ninavyokupigia mahesabu! Naona hii week itaenda taratibu sana.” “Mungu atatusaidia Geb.” Wakalala.  

Grace Kwa Nanaa Tena.

           Wakati wanamsuka, simu ya Nanaa ikaanza kuita. “Naomba hiyo simu Liv mwanangu. Atakuwa dad huyo!” “Na mimi mama.” Liv akataka na yeye aongee na baba yake. “Haya. Ongea wewe kwanza na dad, halafu ukimaliza ndio unipe na mimi.” Liv alipoangalia simu ya mama yake, akampa mama yake bila kupokea. “Sio dad!” Picha ya Geb huwa inaonekana wakati akipigiwa na Geb. Hata Liv alikuwa akijua hilo. Nanaa akaangalia, akaona namba ngeni.  

Akapokea. “Niambie bibi harusi wangu.” “Grace!!” Nanaa akashituka na kuanza kushangilia. Grace akawa anacheka. “Naolewa mwenzio!” “Nimesikia. Geb amefurahi huyo. Anacheka muda wote.” “Mbona hapa kaondoka kimya kimya.” “Alikuwa ana play cool tu kwako. Hana lolote! Nimeongea naye zaidi ya lisaa. Mipango mingiii. Mwishowe nimemwambia aniachie mimi kila kitu.” “Kweli!?” Nanaa alikuwa haamini. 

Hapa nishawapatia sehemu ya kufunga ndoa yenu, sehemu ya  honeymoon kwa kuwa amekataa msisafiri mbali. Na hataki muwe mbali na watoto. Msimamizi wake yeye wa harusi, maana amesema wewe umenichagua mimi.” Nanaa akacheka. 

“Asante kama umekubali.” Nanaa akajua Grace amekubali. “Karibu. Mimi mwenyewe nimefurahi kuona bado unaniamini. Kwa hiyo kila kitu kipo tayari. Mtakuwa na harusi nzuri sana. Nikikata tu simu naanza mipango. Jumanne ameniambia mnaenda kumuona dokta. Akinipigia simu kuniambia kila kitu kipo sawa, nitakuja jumanne hiyo hiyo na ndege ya usiku. Ili jumatano tukatafute gauni. Alhamisi tunaondoka wote kasoro Geb.” “Tunaenda wapi tena!?” Nanaa akauliza na wasiwasi. 

“Kwa sasa nipo Arusha. Nipo kwenye hoteli nzuri sana. Naona hapa patawafaa. Nimeshauliza nafasi. Kama tunaweza kupata sehemu ya kufanyia hiyo ibada fupi na sehemu ya chakula, wameniambia ipo sehemu. Wanampishi mzuri sana. Kilichobaki ni wapambaji tu. Nitaenda kuonana nao leoleo. Ili tuzungumze nao. Kwani una aina fulani ya mapambo unataka?” “Sina hata ninachojua. Wewe nichagulie tu?” Grace akacheka. 

“Sawa. Je rangi? Kuna rangi unataka kwa ajili ya harusi yako?” “Napenda nyekundu. Ila kama itasumbua basi.” “Wewe! Hiyo ni siku yako. Chochote unachotaka, lazima tutatafuta mpaka tupate.” Nanaa akacheka kwa furaha. “Keki je? Unapenda keki gani?” Nanaa akaanza kufikiria. “Labda nikuulize hivi, huwa unapenda kula keki ya namna gani?” Grace akaendelea kuhoji taratibu. 

Take your time. Fikiria tu. Mimi naandika kila kitu. Geb ameniambia niweke kila kitu unachotaka wewe. Hapa nimeandika kila kitu. Nakuuliza moja baada ya kingine. Ukiona ni swali unalotaka kufikiria, niambie niruke, nikuulize kitu kingine.” Tayari machozi yalishaanza kumtoka.

“Nilijua tu. Kwanza naona umechelewa sana kuanza kulia. Basi tena hapo maandalizi hayo yatamshinda mwenzio.” Kumbe mama G, alikuwa amekaa nyuma ya Nanaa muda wote akisikiliza. “Bwana mama!” Nanaa  akafuta machozi. “Sasa hapo badala yakuongea haraka, useme unachotaka, mwenzio akaanze kuwaandalia, unalia tena!” “Nafikiria.” Nanaa akajibu. “Mmmh!” Mama G akaguna. Wote wakacheka mpaka wasusi. 

“Kafurahi mama. Ndoa ngumu mama yangu!” Mmoja wa wasusi aliongeza. Kwani ilimlazimu Nanaa kuweka sauti ya juu, speaker, ili aweze kusikia. Alishindwa kuweka masikioni sababu ya kusukwa. “Basi mwenzio anakusubiri.” Nanaa akacheka. “Napenda keki ya Vanilla. Wanaweza kuchanganya na chocolate kidogo. Muundo wowote ule.” “Sawa. Nitawaambia watengeneze mchanganyiko. Vanilla na chocolate.” Grace akajibu wazi akisikika anaandika. 

“Unapenda kuwe na maua gani mbali na roses?” “Hayo hayo.” Nanaa akajibu. Grace akacheka. “Unataka yachanganywe na rangi gani?” “Sijui ila mekundu ndio yawe mengi.” Grace akaandika. “Nimekupata. Kwa hiyo nimwambie achanganye na yeyote, ila mekundu yawe mengi?” “Ila zisiwe rangi nyingi. Nyekundu labda na pinki au nyingine. Mbili tu.” Nanaa akaongeza. “Hayo ndio maneno. Sio kusema yeyote.”“Mama!” “Ndiyo. Maana unaolewa mara moja tu.” Nanaa akacheka. 

“Eti Grace?” Nanaa akaita. “Nipo. Naandika tu hapa. Niambie?” “Nilionaga kwenye movie, watu wanafungia harusi nje. Nikapenda. Kwani itakuwa gali?” Kila mtu alicheka. Mpaka Grace. “Nanaaaa!” Mama G alizidi kucheka. “Bwana usinicheke mama!” “Mwanangu unataka  harusi ya kizungu?” Bado mama G alikuwa akicheka sana. “Kwani ni garama? Kama garama basi.” “Wewe unaolewa na Geb Magesa. Usiogope garama. Amenituma niandike kila kitu unachotaka bila kujali garama.” “Basi hapo tena ataanza kulia.” Mama G akapokea. “Bwana mama!” Nanaa akalalamika na kweli alishaanza kulia. Tayari machozi yalishafika mashavuni.  

“Niambie bibi harusi wangu? Kwahiyo Unataka harusi hiyo ifungwe nje, bustanini au pembeni ya pool?” Grace akauliza. “Pembeni ya pool si wanangu watatumbukia kwenye maji!” Wakacheka sana.

“Kama hapo ndio unapataka, watatafutwa watu wa kuwaangalia.” “Roho yangu haitatulia bwana. Magesa wangu anazunguka kila mahali siku hizi. Nitakuwa roho juu juu wala sitaweza kumsikia mtu.” Nanaa akasisitiza. “Wala usijali. Wana bustani pia nzuri. Wanaweza kuitengeneza na kupapamba, pakapendeza tu. Naamini utafurahia.” “Asante Grace.” “Karibu. Nini tena unataka?” Nanaa akabaki kama anayefikiria. “Naona ni hivyo hivyo. Sina kingine. Ila nakushukuru sana, tena sana. Asante kwa kutoa muda wako na kutusaidia. Nakushukuru.” “Karibu. Na mimi nimefurahi kuniamini na kupata kitu chakunifanya niwekeze mawazo yangu yote huko.” Grace akajibu. 

“Nina ombi la mwisho Nanaa.” Grace akaongeza. “Karibu.” “Jumanne usiku nitakuja hapo na mgeni wangu. Lakini sitalala hapo nyumbani.” “Mmmh!” Mama G kaguna. “Huyo ni mama ameguna?” Nanaa akacheka. “Sasa mama unaguna nini? Kwani wewe umeshajua mgeni wa namna gani?” “Nakujua sana wewe Grace. Ukiongea tu bila hata kuiona hiyo sura yako, nakuwa najua kila kitu.” “Mwaya Nanaa, naomba ututayarishie chakula. Hasa ndizi. Nimemsifia kuwa unajua kupika ndizi kuliko Yusuf mpishi wao, hajaamini. Sasa nataka aje kula ndizi uliyopika wewe.” Nanaa akacheka.

“Hilo tu, usijali. Kingine nini unataka?” Nanaa akauliza. “Huyo haambiwi hivyo. Shauri yako! Utajuta kuuliza.” Mama G akaingilia. Nanaa akacheka.  “Usimsikilize mama. Wala sina mahitaji makubwa. Ila tu naomba tuwakute watoto. Maana nilimringishia kuwa tuna watoto wazuri sana na watulivu. Sasa nataka awakute.” “Wewe usichelewe kufika hapa. Watoto wakiwa na usingizi, mimi nawalaza.” “Mama naye!” “Kinachokushinda kuja mchana ni nini mpaka uje usiku!?” “Watu wana kazi mama!” “Basi mtaona watoto kesho yake.” “Mama!” “Mama nini? Wewe shika yako. Achana na wajukuu zangu.” “Sasa chakula?” “Hayo zungumza na Nanaa. Hapo siingilii.” Mama G alirudi kushika usukani kwa wajukuu zake. Majukumu ya watoto alisaidia kwa asilimia kubwa sana. Hapo ndipo Nanaa alipoona upendo wa huyo mama kwa wajukuu zake. Alifanya bila unafiki. 

“Nanaa mwaya tutaongea ukiwa peke yako. Ila nikikumbuka kitu chochote nitakupigia ili nikuulize. Nataka upate harusi nzuri utakayokumbuka milele.” “Asante Grace. Kuhusu chakula usiwe na wasiwasi utakuta vitu vizuri vitupu.” “Nakushukuru mwaya wifi yangu.” Nanaa alizidi kufurahi kutambuliwa. 

“Gauni na viatu ni mpaka nije huko kesho. Jumatano tutakwenda wote kutafuta.” “Hamna shida. Uwe na siku njema.” Wakakata simu. Nanaa akaanza kushangilia. “Si ulikuwa unajidai hutaki kuolewa wewe?” Mama G akamuuliza. “Acha kukumbuka mambo ya kale bwana!” Nanaa akaendelea kushangilia. “Gafla!” Mama G akashangaa, kwa kumchokoza Nanaa. “Mama naye! Mambo hayaishi moyoni!?” Nanaa aliendelea kufurahia. “Kwanza humu ndani fujo zitaanza.” Mama G alikuwa akicheka sana. “Fujo gani tena?” “Nawaza vile kina mama Magesa tutakavyokuwa wengi humu ndani!” Mama G alicheka mpaka machozi. “Ila itabidi uniachie kwa muda mpaka nizoee bwana!” Mama G alizidi kucheka.  

“Nanaa unaakili za kitoto wewe!” “Nakaribia kuwa mke wa mtu mama. Naomba uongeze heshima bwana!” Wale wasusi walikuwa wanacheka huku wakimsubiria Nanaa akae waendelee kumsuka. “Liv!” Nanaa akamwita mwanae aliyekuwa akicheka vile mama yake anavyocheka na kufurahia. “Nampenda mama.” Liv aliongea huku akicheka. “Hata dad anampenda mama.” Nanaa akajibu na kufanya wazidi kucheka. 

“Yaani Geb angekuona leo hapa, asingeamini.” “Wewe acha kabisa mama. Kuzalishwa watoto wawili na bado niolewe! Si mchezo.” “Ndio ukae, umalizwe kusukwa kabla hajarudi humu ndani.” Nanaa akakumbuka akarudi kukaa. 

Jumanne.

Siku ya jumanne ambayo Nanaa alitakiwa kwenda kumuona daktari wa watoto, Geb hakwenda kazini. Kulikuwa na umuhimu wa yeye kuwepo ili aulize maswali yote kujiridhisha. Ndiye mtu ambaye angeweza kuidhinisha kama Nanaa anaweza kusafiri au la. Kutoa tathimini kamili ya afya ya mtoto na Nanaa. Mama G alibaki na watoto nyumbani, Geb akatoka na Nanaa. 

          Walikaa kwenye foleni wakisubiria zamu yao ifike wamuone daktari wa wanawake. Nanaa alikuwa ameshafanyiwa vipimo vya awali. Uzito ulikuwa mzuri, mkojo msafi. Wakampongeza kwa kunywa maji mengi. Pressure ndiyo ilikuwa juu kidogo. “Sidhani kama atasema ni sawa kusafiri. Mimi namjua huyu dokta. Muoga kuliko mimi mwenyewe.” Nanaa alianza kutoa tahadhari. “Huwa anakwambia ukweli, Nanaa. Kwa faida yako na mtoto.” “Basi tujiandae kuambiwa tusubiri mpaka nijifungue. Mimi namfahamu dokta Lyamu. Nimeanza nae tokea Liv mpaka leo kwa Jimmy. Kila kitu yeye ni tahadhari! Ukimsikiliza yeye hatutakaa kufunga ndoa.” Geb akanyamaza. 

Akamuona amekosa  raha.  Akamvuta mkono. “Jumamosi ni lazima tutabariki ndoa yetu. Usiwe na wasiwasi. Iwe hapa au Arusha, lakini lazima tutakamilisha. Usiogope.” Nanaa akavuta pumzi na kujiegemeza pembeni. “Unawaza nini sasa?” “Hii Presha! Kwa nini ipo juu wakati nimekuwa na wakati mzuri? Hamna hata jambo baya nililowaza!” “Kumbuka sasa hivi kuna tatizo la moyo pia, Nanaa. Daktari ametuambia hiyo yenyewe inaleta pressure. Bado mtoto mwenyewe anazidi kukua. Yote hayo yanaongeza pressure.” Nanaa akafikiria. 

“Nimechoka Geb. Nafikiri huyu mtoto awe wa mwisho. Nifunge kabisa kizazi. Wanatosha. Au wewe unataka zaidi?” “Hata kama ningekuwa nataka zaidi isingekuwa kwa mateso kayo unayopitia. Nashukuru kwa kuwa wewe mwenyewe umeona hivyo. Watoto watatu wanatutosha kabisa.” Nanaa akalifurahia hilo.  

“Nakushukuru Geb. Asante kwa kuwa na mimi kila ninapokuwa mgonjwa.” Geb akacheka kidogo. “Karibu.” Geb akajibu huku akionekana amekumbuka kitu. “Unacheka nini?” “Grace huwa ananiambia kuwa kwa sababu siwezi kulala bila wewe pale kitandani, ndio maana huwa inanilazimu kuja kulala na wewe hospitalini. Kwa maana nyingine ananisema kuwa nakuwa hospitalini na wewe kwa sababu yangu sio yako.” Nanaa akacheka. 

“Anakuchokoza tu. Tena leo usiku anakuja na mgeni wake. Unajua?” “Ameniambia kuwa umemkubalia kuwatayarishia chakula cha usiku.” “Atakuwa amepata mchumba?” “Sijui Nanaa. Tumsubiri tuone. Ila kwa furaha aliyonayo Grace, lazima awe amepata faraja. Aliondoka akiwa ameumizwa sana.” “Utafanyaje?” Nanaa akazidi kumuuliza. 

“Nimezungumza naye swala la talaka. Ameomba kesho nimsindikize kwa mwanasheria. Ameomba niwepo wakati wanakamilisha mambo yao.” “Kwani Danny atakuwepo?” “Lazima awepo. Wana watoto na ile nyumba yao. Grace inamuuma sana ile nyumba. Anasema amewekeza pesa nyingi sana na muda wake mwenyewe. Hawezi kumuachia Sara aishi pale bure. Anataka kumlipa Danny pesa aliyowekeza pale. Amwachie nyumba.” “Danny akikataa?” Nanaa akauliza. 

“Basi waandikishane kwamba ni nyumba yao wote wawili. Ikitokea wanakufa, wapewe watoto wao.” Nanaa akafikiria. “Sasa kwa sasa hivi wataifanyaje?” Nanaa akaendelea kuhoji. “Grace amesema inategemea watakavyoamua kwenye swala la watoto. Atakayekuwa na watoto kwa muda mrefu, ndiye atakayeishi pale. Lakini anahisi hata iweje, Danny hawezi kuishi bila wale watoto. Ndio ndugu zake wa pekee.” “Kwa hiyo Danny ndiye ataishi pale?” “Itabidi.” Geb akajibu.“Na Grace?” Nanaa akahoji. “Grace hawezi kukosa pakuishi. Hilo haliwezi kuwa tatizo hata kidogo. Ninachomfikiria ni watoto wake tu.” Nanaa akanyamaza akiwaza.

“Wakati wote kwenye kutengana, ni rahisi sana kwa wazazi. Kama sasa hivi Danny anaye Sara, ambaye anamfariji kwa namna yake. Grace naye hivyo hivyo. Watoto je? Wao ndio wanabakishwa bila faraja ila mateso na kumbukumbu mbaya. Maneno mabaya wanayojazwa na upande wa mama au baba. Ugomvi ulikuwa ukitokea mbele yao wakiona. Baba na mama wanapata faraja, lakini sio wao. Mara nyingi huwa tunasahau sana upande wao. Hatukumbuki madhara tunayokuwa tunayasababisha kwao. Tunaendelea na maisha yetu, kana kwamba hakuna kitu kimetokea kwao.” Geb aliongea kwa kina huku akifikiria.  

“Nawafikiria wale watoto, nakuwahurumia sana. Niliona vile watoto wangu walivyoteseka. Najua kwa namna moja au nyingine, hata wa Danny wanapitia au watapitia hapo. Hakuna mtu anayeweza kulea watoto vizuri kama mama yao mzazi.” Nanaa akabaki kama anayewaza. Zamu yao yakuingia kumuona dokta ikafika. 

~~~~~~~~~~~~~~

Daktari akajaribu kuzungumza nao kwa mapana na umuhimu wa kuwa makini kipindi hicho mtoto anapoendelea kukua, kama wanamuhitaji huyo mtoto. Geb akapata nafasi yakuuliza maswali mengi ili kujua waamue nini. “Kama mtatumia usafiri wa ndege, haitakuwa na shida sana. Lakini sishauri safari ndefu. Inaweza kusababisha kutoka kwa mtoto, au kuanza kutokwa na maji ya uchungu kama ilivyokuwa kwa Magesa.” Daktari aliendelea.  

“Najua mambo ya harusi Geb na Nanaa. Yana mambo mengi sana hasa kwa hii mnayotaka kuifanya ndani ya juma hili. Shuguli nyingi kwa wakati mmoja, pia hazitafaa kwa hali ya Nanaa.” “Nitahakikisha maandalizi yote hayatamuhusu yeye. Yeye atakuwa na kazi ya kuwepo tu siku ile ya sherehe. Muda wote atakuwa kwenye mapumziko. Vitu vyote visivyo vya muhimu havitakuwepo, na nitahakikisha huduma zote muhimu atakazohitaji siku ile ya harusi zinamfuata chumbani. Hapatakuwa na shuguli zozote na baada ya harusi tutakuwa hapo hapo hotelini.” Kidogo daktari akaridhika. 

“Naomba na wewe uhudhurie. Sio kama daktari lakini mtu ambaye umehusika sana kwenye maisha yangu. Tokea mimba ya Liv, mpaka sasa umekuwa na mimi bila kuchoka. Umekuwa zaidi ya daktari kwetu. Naomba usiache kufika. Hata ukitaka tiketi ya kwenda na kurudi siku hiyo hiyo, Geb amesema atahakikisha unapata. Ataandaa utaratibu wakupokelewa uwanja wa ndege na kurudishwa. Huna haja yakulala.” Nanaa akaongeza. Yule daktari akacheka. “Nitazungumza na mke wangu, halafu nitawajulisha kabla ya alhamisi. Inaweza kuwa sehemu ya mapumziko yetu pia na angalau nitajiridhisha kuwa upo salama.” Wakazungumza kidogo, wakatoka. 

~~~~~~~~~~~~~~

Walitoka hapo wakiwa wameridhika. Geb akampigia simu Grace nakumwambia aendelee na maandalizi kwani harusi ipo. Wakapita sokoni kununua vitu baadhi kwa maandalizi ya ujio wa Grace na mgeni usiku huo. Wakarudi nyumbani. Walimuelezea kila kitu mama yao. “Hilo halina shida. Hata kesho huna haja yakuzunguka madukani. Unaweza kuwepo kwenye gari au ukabaki hapa. Mimi na Grace tukakuletea aina ya magauni utakayokuwa umetuelekeza unayataka.” “Hiyo iyakuwa rahisi mama. Ili asizunguke sana.” Geb akaongeza. 

          “Na pia humu ndani itabidi aache kabisa kujishugulisha na shuguli za watoto. Atulie kabisa. Kutaliwa kitakachowezekana. Kitafanywa kitakachowezekana. Ilimradi watoto wawe sawa, mengine tutavumiliana.” “Nashukuru mama. Angalau nisogeze siku. Sitaki kuja kuhamishiwa tena hospitalini.” Nanaa akaongeza. “Ila utulie Nanaa. Jitahidi kutulia. Acha kuhangaika na shuguli za humu ndani. Hata kama ukiona kitu hakijafanywa, vumilia mwanangu.” “Nitafungia macho kila kitu, ilimradi Geb wangu apate tu chakula.” “Ndio hayo ninayosema.” Mama G akaanza.  

“Nikumpikia tu Geb, mama.” “Wewe nimekwambia niachie mwenyewe. Hata kama chakula kitachelewa, atakunywa maziwa. Mwishowe mtahamia tena hospitalini. Maana nyinyi mmoja akilazwa hospitalini, wote mnahamia huko huko. Mnaacha watoto wanahangaika hapa au wanazungushwa kwenye gari kama makodakta.” Nanaa na Geb wakacheka. 

“Msicheke. Naomba tulia Nanaa. Mtapoteza huyo mtoto.” “Nitapumzika mama.” “Hata hivyo nitazungumza na Jeri kama anaweza kutupa mkewe atusaidie kwa kipindi hiki.” “Na kweli Geb. Mke wa Jeri alikuwa akinisaidia sana pale kwenye apartment siku alizokuwa akija. Halafu msafi na anaupendo na watoto.” Nanaa akaongeza. “Basi nitazungumza na Jeri.” Nanaa akatulia kidogo. 

“Nini tena?” Geb akauliza baada yakumuona anafikiria. “Nilazima niende kwa kaka leo. Siwezi kufunga ndoa bila yeye kuwepo.” Nanaa akaongeza. “Tutakwenda jioni kabla ya kina Grace kufika. Nilishamtumia ujumbe kumwambia ninashida yakumuona. Amesema jioni atakuwepo nyumbani.” “Nashukuru Geb. Nilijua umesahau.” “Siwezi.” Mipango ikaendelea hapo. Wakajikuta wageni walio nao wakuhudhuria harusi ni wachache sana. Daktari anayemtibu Nanaa na mkewe. James na dada Fifi. Hao ndio watu wa Nanaa. Kwa Geb ilikuwa ni mama yake na Grace. Mbali na watoto wao na mgeni wa Grace ambaye ndio atakuwa msimamizi wa Geb. Lakini wakakubaliana ibaki hivyo hivyo. Wasikaribishe mtu mwingine. 

Nanaa kwa Kaka

Ilipofika saa kumi na 11 jioni Geb, Nanaa na watoto wao walitoka kwenda kwa James. Nanaa hakuamini baada ya kumuona kaka yake. Alikuwa amebadilika sana. Na James naye alishituka sana alipomuona Nanaa kwenye hali ile. Mjamzito! Nanaa akajua. Bado walikuwa wamesimama mlangoni wakishangaana baada ya James kuwafungulia mlango. Geb alifika pale, akiwa amembeba Magesa. Nanaa amemshika Liv mkono. “Karibuni ndani.” Wakaingia. 

“Unaumwa?” Nanaa akauliza. “Hapana. Mambo mengi tu. Karibuni.” James akajibu na kukaa. “Hamna kitu chochote chakuwakaribisha humu ndani. Mimi mwenyewe ndio nimeingia muda si mrefu.” Nanaa akamuhurumia sana kaka yake. “Pole kaka. Unaonekana umechoka!” James akacheka kidogo. 

“Vipi na nyinyi? Naona watoto wanazidi kukua!” “Tunamshukuru Mungu wanaendelea vizuri.” Nanaa akajibu. “Ila huyu kaka anaonekana atampita sasa hivi dada yake.” James akaongeza. “Mwenzie anapenda kula. Liv mvivu sana wakula. Halafu nahisi Magesa amechukua urefu wa baba yake. Nguo akivaa week hii, hawezi kurudia tena week ijayo. Zinambana. Muone na kitambi chake. Njoo.” Magesa akacheka akatoka kwa baba yake akamwendea mama yake. Wakiwa wamekaa pale pale kwenye kochi.  

“Mpenda kucheka kama wewe.” James akaongeza. Wote wakacheka. “Eti Magesa. Dimpozi kama za mama? Muone.” Nanaa akambusu. Muda wote Geb alikuwa kimya tu msikilizaji. “Mnaendeleaje lakini?” James akauliza. “Tunataka kubariki ndoa siku ya jumamosi. Itakuwa Arusha.” Hapo Geb akaongea. “Jumamosi hii!?” James akastuka kidogo. “Ndiyo kaka.” Nanaa akajibu. 

“Mbona tukiza?” James akauliza. “Mimi ndiye nilikuwa sipo tayari. Nilipokuwa tayari ndio Geb akaona hamna kusubiri tena. Tufunge tu kabla mtoto hajazaliwa.” James akanyamaza kidogo kama mwenye swali lakini anashindwa aulize nini. Alianza swali mara kadhaa, akasita.  

“Mtoto.. Hiyo mimba..” Akanyamaza. Nanaa akainama akimchezea mtoto wake. Alijua swali alilotaka kuuliza lakini alijua hajui aulizaje. James akavuta pumzi kwa nguvu, akanyamaza. Geb aliyeweza kumwangalia alimuona amebadilika rangi akawa mwekundu mpaka macho. “Yale matatizo yalinisababishia ujauzito. Nilipata mimba. Ni mtoto wa kiume. Anaitwa Jimmy James au JJ kwa ufupi.” Nanaa akaongeza huku machozi yakimtoka. James akasimama, na kuondoka pale. Baada ya kama dakika 18 hivi, akarudi akiwa amebadilisha mpaka nguo. Wazi alionekana ameoga kabisa. 

“Mngependa nikawaletee kinywaji chochote dukani?” James akauliza. “Hapana kaka. Nataka tuwahi kurudi nyumbani mapema. Saa mbili usiku natarajia wageni.”  “Unaishi wapi?” James akauliza. “Naishi na Geb, nyumbani kwake na mama yake.” Lile jibu halikumfurahisha Geb. Lakini akanyamaza. “Mbona Danny aliniambia hauishi pale?” “Baada ya yale matatizo niliondoka kaka. Lakini Geb akanitafuta. Alinipata nikiwa na mimba ya miezi 5 tayari, ndio akanirudisha nyumbani.” James akanyamaza kidogo kama anayefikiria. 

“Kwa hiyo sasa hivi una miezi 7 na siku kadhaa?”  Nanaa akajua kaka yake amepiga mahesabu. “Ndiyo. Leo tulikuwa kliniki.” “Mtoto anaendeleaje?” James aliendelea kuuliza. “Anaendelea vizuri.” Nanaa akajibu. “Na wewe mwenyewe unaendeleaje?” “Naendelea vizuri.” Nanaa akajibu kwa kifupi tu. James akamwangalia. “Naendelea vizuri kabisa. Sasa hivi nipo sawa.” Nanaa akasisitiza. Hakuna aliyejua kama Nanaa ni mjamzito. Hakuwa ameonana si rafiki wa kaka zake tu, hata kaka yake mwenyewe hakuwa ameonana naye tokea siku ya tukio. 

“Umemwambia?” Lilikuwa swali fupi ambalo James aliuliza, lakini Nanaa na Geb walielewa. “Hapana kaka. Nimekusudia nisimwambie kama nimebeba mtoto wake. Nitamlea tu mwenyewe labda mpaka baadaye sana mtoto mwenyewe akitaka kujua. Ila tumekusudia kuwalea pamoja.” “Watoto wa Geb wanajulikana Nanana. Waangalie hivyo walivyo hapo. Wapo kama mapacha! Utaficha hiyo siri mpaka lini?” James akauliza. Nanaa akanyamaza na kuinama. 

“Kila kitu kitajijibu kadiri tunavyokwenda James. Sasa hivi tunaweza tukawa hatuna majibu yote. Lakini namwamini Mungu kutupa majibu kadiri siku zinavyokwenda.” Geb akaingilia kati. “Hata hivyo Nanaa alishaandika kila kitu anachojua kitafaa kujibu maswali yote ya Jimmy pindi atakapokuwa na maswali. Kwa hiyo naamini kwa sasa tupo sawa.” Geb akasisitiza. James akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu.  

“Nakushukuru Geb. Asante. Nilitaka kusikia kutoka kwako mwenyewe ndio maana ilinibidi kuendelea kudadisi zaidi. Nitajitahidi kuwepo Arusha siku hiyo ya jumamosi.” “Kutakuwa na sehemu ya kulala, kama ungependa kulala na tunaandaa usafiri wa ndege wakuwaleta huko. Hatutakuwa wengi.” Geb akamuelezea idadi ya watu na jinsi harusi itakavyokuwa.  

“Nafikiri mimi nitaendesha ili nipate usafiri wa kunipeleka Moshi, nikamuone Mzee. Na kama harusi haitachelewa kuisha, nafikiria kwenda kulala nyumbani kwa Mzee pia. Kwa hiyo sitahitaji usafiri wa ndege wala sehemu ya kulala. Nitaua ndege wawili kwa jiwe moja. Ili Jumatatu niwepo kazini.” James akajibu. “Unaweza kuwa na nafasi ya mtu mmoja kwenye gari?” Nanaa akamuuliza kaka yake. “Nani? Maana siku hizi sipendi mazoea na watu.”  “Kuna huyu dada anaitwa Fifi, alinisaidia sana kipindi nilipotoka kwa Geb. Mpaka sasa amekuwa kama dada yangu. Ningetamani na yeye awepo kwenye harusi. Sasa kwa kuwa mimi naondoka alhamisi, na yeye anashuguli zake, nafikiri kwa kuwa wewe unaenda na kugeuza, ungemfaa.” “Hamna shida Nanaa. Tutaweka utaratibu mzuri tu ili na yeye ahudhurie. Mwache James aendelee na ratiba zake. Lakini tunakushukuru sana James. Asante. Tunategemea kukuona siku ya harusi.” Geb akaongeza. “Siwezi kukosa. Tuombe uzima.” Wakaaga na kutoka. 

~~~~~~~~~~~~~~

Nanaa amekubali yaishe. Amerudi kujenga ‘home’ kama alivyoombwa na Geb. Amejenga kwa garama kubwa sana, KUSAMEHE. Amefanikiwa kurudisha Amani, urafiki ambao hata mama G hakutegemea kama ungerudi, Nanaa amerudisha bila kinyongo. Geb amempokea kama alivyo yeye na mtoto wake. Tena bado akimtamkia anautamani mwili ule ule ulioubaka Malii.

Michakato ya harusi imeanza upyaaa. Tena wakiwa wamekusudia kuwepo na watu wanaoweza kuwapokea na baraka zao.

v Je, safari hii watafanikiwa?

Grace anarudi jijini na mwanaume wa ndoto zake ili kukamilisha talaka anayotaka kupewa kwa aibu. Amechafuliwa vilivyo.

v Nini kitatokea kati yao? Grace & Man, Danny & Sara. Watoto nao?

v Je, kuonana ana kwa ana kwa Grace na Danny kutawakumbusha jukumu la uzazi, nakuamua kuacha penzi jipya ili warudi kulea watoto wao? Au Danny amelevya zaidi na penzi la Sara kama Grace kwa Man!

J.5 ndio hatima ya misukosuko ya ndoa hiyo waliyoombea kwa kufunga.

Usipitwe Yatakayojiri Kwa Mwanasheria. 

 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment