Alikuta
vijana wawili na msichana mmoja. Grace akasalimia kwa kuwapungia mkono kwa
chini, kwani mziki ulikuwa ukitumbuiza. Akakaa kwenye kiti kilichokuwa
hakijakaliwa na mtu. Wakawa wametimia wanne. Wasichana wawili na vijana wawili.
Kulikuwa na vinywaji mezani. Wakamwambia ajichukulie chochote. Grace akasogeza
chupa ya maji, lakini hakuifungua. Akabaki akiangaza macho, mziki ukiendelea.
Baada
ya muda mfupi, MC akasimama. Akaongea maneno mengi, lakini akasema
atamkaribisha mmoja wa wamiliki wa hoteli hiyo kuja kuwakaribisha ramsi, na
kufungua shuguli nzima. Grace akajiweka sawa, akiwa na shauku tu hiyo fashion
show ianze, basi. Akashangaa kuona Man ndio anasimama pale. Grace akabaki
ametoa macho. Wale waliokuwa wamekaa nao pale mezani wakaanza kunong’ona. Grace
akawasikia. “Huyo ndio Manase. Ndiye mtoto wake kubwa.” “Hapana bwana! Wanae
kaka yao, wa yule mwanamke wa kwanza aliyefariki kabla ya mama yao hawa.”
“Lakini nasikia huyu ndiye Mzee anamtumia zaidi.” Mwingine akadakia kwa sauti
ya chini wakati Man akiongea. “Basi akifa Mzee, kijana ameula.” Mwenzie
akaongeza. “Halafu bado mdogo tu. Sidhani kama hata ameoa!” “Nasikia anamke.”
Grace akaendelea kusikiliza.
Man
akasalimia. Alitoa salamu kutoka kwa baba yake, ambaye alisema bado ni mgonjwa
ila angetamani kuwepo hapo. Akashukuru waandaaji wa tamasha hilo kwa kuchagua
pale kuwa ukumbi wao wa shuguli kwa mwaka huo tena. “Tunashukuru, na Mzee
ametuma shukurani zake za dhati kwa kuendelea kupafanya hapa kuwa uwanja wa
nyumbani. Japokuwa hayupo hapa, lakini amenituma kuwaambia anawaombea mzidi
kufanikiwa.” Man akaendelea na kukaribisha wageni wote ambao wamehudhuria
tamasha hilo kwa mara ya kwanza na wenyeji. Kisha akaruhusu sherehe ziendelee
kwa amani. Akashuka jukwaani. Grace akainama.
Mambo
yakaanza kushika kasi mle ndani. Grace akawa anafurahia na kupiga makofi. Hata
akasahau alipo. Alikuwa akicheka kila wengine walipokuwa wakishangilia.
Kulikuwa na wachekeshaji. Kila waliposimama, Grace alikuwa akicheka mpaka
machozi. MC ndio alikuwa akimfurahisha zaidi Grace. Kila aliposimama kutangaza,
Grace aliburudika. Hata hakujua kama masaa yalishakwenda wapo siku ya pili.
Ilipokuwa
ikikaribia kuisha, aliokuwa amekaa nao kwenye meza, walimwambia wanakwenda
mziki, club. Kama angependa waongozane. Grace akakataa. Akasema anakwenda
kupumzika bila hata kujua muda. Alipoona ushawishi unazidi, akaona aondoke
kabla shuguli haijaisha kabisa, ili pia
asipate shida yakutoka pale ukumbini kwa fujo na kelele za wahudhuriaji wenzake
na pia ingekuwa njia ya kuwakimbia wale watu pale mezani, kirahisi.Akaaga kwa
kupunga mkono tena, akasimama na kuanza kutafuta njia kutoka nje.
Alipofika
nje ya mlango wa ukumbi, akamkuta Man amesimama na warembo kama watatu. Grace
akageuza shingo upande mwingine
kama hajawaona. Lakini kulikuwa na mwanga mkali wa taa. Hakuna
jinsi unaweza ukasema hujamuona mwenzio wakati ilikuwa nje ya ukumbi na watu
wengi wapo ndani. Ni wao tu walio kuwepo pale nje. Kwa hiyo hata wale wasichana
waliokuwa wamesimama na Man wakicheka, walimuona Grace akitoka. Hakusimama wala
hakuwasalimia, akaendelea kutembea kutafuta lifti yakumpandisha juu gorofani,
kilipokuwepo chumba chake.
~~~~~~~~~~~~~~
Man
ni moja ya wanaume wa ndoto za Grace. Umbile kama baba yake. Lakini Man alikuwa
mweupe. “Mmasai gani mweupe hivi!?”
Grace akajiuliza wakati akisogelea lifti. Maana alishasikia jina la mmiliki wa
pale ni Mmasai. “Ndio maana warembo
wanamsonga. Sababu ya uzuri huo na vijipesa.” Grace aliendelea kuwaza
wakati amesimama mbele ya mlango wa lifti.
~~~~~~~~~~~~~~
Akageuka
akakuta bado Man anamwangalia. Halafu kwa haraka sana akajifunika uso kwa
viganja vyake vyote viwili kama
mtoto mdogo. Wale
warembo waliokuwa wamemzunguka
Man, wazi walijua Man anamtizama Grace. Grace alipomuona amefanya kama mtoto,
akacheka na kugeuza shingo kuangalia lifti. Lifti ikafunguka, Grace akapanda na
kuondoka.
~~~~~~~~~~~~~~
Alipofika
tu chumbani, simu ikaanza kuita. Akaangalia saa, ilikuwa saa nane na nusu
usiku. Kwamba kumeshakuwa siku ya jumapili. Akasogelea ilipo ile simu ya
mezani, akaipokea akiwa na mshangao ni nani anampigia simu muda ule! “Samahani. Mimi ni muhudumu wa hapa mapokezi. Chakula chako kitaletwa
baada ya muda mfupi sana kuanzia sasa.” “Mimi sijaagiza chakula! Utakuwa
umekosea chumba.” “Hapana dada Grace. Ni chakula chako.” Yule muhudumu akasisitiza kwa kumtaja jina kabisa.
“Lakini mimi sijaagiza chakula, na nisingependa kula chakula kizito
mida hii!” Yule muhudumu akatulia.
Grace
akasikia minong’ono upande wa pili. Akajua anapokea maagizo kutoka kwa mtu. “Ni nani kama sio Man!” Grace akawaza
huku akisubiria kusikia huo ujumbe. “Hakitakuwa
chakula kizito. Ni chepesi tu, kitakachokufanya ulale vizuri.” Yule muhudumu akarudisha ujumbe. Grace akacheka. “Mwambie asante.” Grace akarudisha ujumbe na kukata simu.
Kadiri
alivyokuwa akisubiria, ndivyo njaa ilivyoanza kumuuma. Akatamani walete hicho
chakula mapema zaidi. Na kweli hawakuchelewa. Baada ya muda, mlango ukagongwa.
Aliletewa supu nzuri sana. Iliwekwa pronds, minofu mizuri ya samaki na mboga
zilizokuwa zimekatwa vizuri. Vililetwa kwenye kigari alichokuwa akisukuma yule
muhudumu. Kulikuwa na bakuli jingine lililokuwa limepangwa matunda kwa ustadi.
Grace mwenyewe alivutiwa. “Nashukuru sana.” Akashukuru na kumpa pesa kidogo,
kama kumtip.
~~~~~~~~~~~~~~
Sababu
ya kushiba vizuri, Grace alilala karibia siku nzima ya jumapili. Aliamka
mchana, akaoga na kuamua kutoka kwenye baraza lililokuwepo upande wa makochi.
Alipotoka na kuchungulia chini, akakutana na pool tatu kubwa, zote zimejaa watu
wakiogelea. Kila mtu alionekana anafurahia kuwepo pale. Pool iliyoonekana fupi,
ilikuwa na watoto tu wakiogelea. Grace akabaki akiangalia kwa chini. Akagundua
wengi wao wana ngozi nyeupe. Yaani wazungu. “Wanaonekana
wanatengeneza sana pesa hapa.” Akawaza.
Akaona
asiendelee kukaa peke yake mle ndani. Ndicho kitu alichokuwa akikifanya kwa
uaminifu na Danny alihakikisha anamudu kumfungia. Akatoka akiwa amevaa gauni
lake jepesi kama shumizi, akaachia nywele zake zilizokuwa nyingi kama za kaka
yake. Wakamrithisha Liv na Magesa. Hakuwa akiweka dawa ya aina yeyote ile.
Lakini hakuacha kuzipiga pasi. Kwa hiyo mara nyingi ungekuta nywele zake nzito
zimenyooka mpaka mgongoni. Ungeweza kusema ameshonea wiving. Lakini nyusi
nyingi alizonazo na baby hair kuzunguka kichwa chake, ndizo zitakujulisha kuwa
zile nywele ni zake. Alivaa sendozi nzuri sana kama vimalapa, ukaongezeka
umaridadi wa kucha zilikuwa zimepelekwa saluni. Zikatendewa haki. Alipendeza
kuanzia kucha za miguu mpaka mikono. Akashuka.
Moja
kwa moja akaenda kule alikoona watu wakiogelea. Akatafuta sehemu akakaa, chini
ya mwamvuli. Muhudumu akamsogelea. “Kuna supu nilikula au kunywa jana usiku,
sijui jina lake! Lakini natamani kama ningeipata tena.” Muhudumu akacheka. “Ilikuwa
na nini?” Grace akamuelezea. “Basi usijali. Nitaenda kuwaelekeza jikoni,
nitakuletea. Vipi juu ya kinywaji?” “Naomba juisi ya embe tafadhali. Walinipa
jana, nikaipenda sana.” “Umeshakunywa juisi ya mapera?” Muhudumu akamuuliza na
tabasamu.
“Hapana.”
“Naomba nikuletee. Usipoipenda, nitakuletea ya embe. Ni nzuri pia. Leo nataka
ubadilishe.” Grace akacheka. “Nakushukuru. Basi naisubiria kwa hamu.” Yule
muhudumu akaondoka. Alikuwa mgeni kabisa kwa Grace. Lakini akashangaa vile wote
walivyo wakarimu. Akajua wamiliki wa hapo, wamewekeza vizuri kwa wafanyakazi
wao.
Man kwa Grace.
Baada ya muda mfupi akamuona Man anakuja na kigari
cha chakula na juisi, kama muhudumu. Grace akacheka. “Wewe ni mtundu sana, Man!”
Man akaanza kupanga vitu pale mezani. “Karibu sana.” Grace akaendelea kucheka. “Asante.”
Grace akashukuru huku akicheka. “Ungependa kitu kingine chochote?” Man akauliza
huku akionekana yupo kikazi zaidi. “Hapana. Asante.” “Basi kule jikoni
wameniambia nisubirie vyombo.” Man akaongeza. “Yaani usubiria hapa hapa wakati
nakula!?” Grace akauliza na mshangao huku akicheka. “Mimi mwenyewe nilishangaa!”
Man akaongeza. “Karibu ukae.” “Daah! Afadhali.” Man akavuta kiti kwa haraka na
kukaa mbele yake.
Akabaki
akimtizama. Grace alijua wazi macho yake huchanganya wengi. Hata Man,
alionekana kuzubaishwa. “Asante kwa supu ya jana usiku.” Grace akavunja ukimya
wakati anajisogezea juisi. “Naona umeipenda.” “Ni nzuri.” Grace akasifia. “Hata
mimi huwa naipenda.” “Mbona sasa ya kwako siioni?” “Nilikuwa sina uhakika kama
nitaruhusiwa kukaa hapa au la.” Grace akacheka tena. “Si naruhusiwa na mimi
kuagiza kinywaji?” Man akauliza. “Karibu.” “Asante.” Akamuita muhudumu kwa
ishara ya mkono. Akaja kwa haraka. Na yeye akaomba juisi ya mapera. “Wewe ndio
ulinipendekezea juisi ya pera?” Grace akauliza baada ya kuona na yeye ameagiza ‘guava juisi’. Man akacheka
ishara ya kukubali.
“Umependa?”
Akamuuliza. “Ni nzuri sana. Mna
wapishi wazuri na wahudumu wazuri sana.” “Asante. Lakini huyu mpishi ni mgeni.
Kila anayekula chakula chake anasifia. Anafanya vizuri sana.” Man na yeye
akasifia.
Juisi yake ikaletwa. “Ni kesho ndio unakwenda mbugani?” Man akauliza. “Sijui Beka atanipangia vipi! Ameniambia kesho atakuwepo kazini.” “Kuna gari inaondoka asubuhi na washindi wa mashindano yale ya jana usiku. Wamepewa zawadi ya kwenda kutembelea mbuga za wanyama. Watashukia kwenye moja ya hoteli zetu. Tumewapa punguzo.” Grace akabaki kimya tu. “Na mimi nitakuwa nao.” Man akaongeza. “Nyinyi nendeni pamoja tu. Acha mimi nimsubirie Beka.” “Kwa nini?” Grace akabaki kimya.
“Eti
Grace?” “Wewe nenda ukapate wakati mzuri na warembo wako. Watafurahia ukiwa nao
wewe bila mmama kama mimi kuwepo katikati yenu. Wataona nawawekea usiku
bure. Nyinyi nendeni tu.” Man akabaki akimtizama. “Kweli tena. Nyinyi nendeni
tu. Mungu awasaidie muwe na wakati mzuri.” “Naona umeamua kugoma kabisa kuwepo
kila sehemu ambayo mimi nipo.” Man alilalamika kidogo.
“Hapana
bwana! Mbona tumekaa hapa pamoja? Sina shida yeyote ile na wewe. Ila ukweli
nipo hapa kupumzika Man. Nataka utulivu wa akili kwa asilimia zote. Kusafiri na
watoto kama wale! Tena walioshinda wasichana wenzao! Sitaweza hiyo
shangwe huko njiani. Na mimi huwa kelele nyingi sana huwa siwezi. Nakuwa
napatwa maumivu ya kichwa. Sasa naweza kufika mgonjwa hata kilichonipeleka kule
nisikifurahie. Nashukuru kwa mwaliko, lakini hapana.” Ongea yenyewe
ilikubaliana na anachozungumza.
Grace
alijaliwa sauti tulivu. Na yeye mwenyewe pia alionekana ametulia sana. Hata
kama unamatatizo yako, ile hali ya kuwa karibu naye, unahisi kutulia. Man
alikuwa ametulia tu akimwangalia. “Grace akiamua kukukatalia jambo! Hakubakizi
na hoja! Haya mama. Nimeelewa.” Grace hakuongeza, akatabasamu na kuinamia
chakula chake.
“Unampango
wakukaa huko siku ngapi?” Man akaona aulize tena wasifunge mazungumzo maana kwa
Grace alionekana ni kama amemaliza. “Inategemea.” Grace akajibu na pia hapo
akawa amemaliza. “Na nini?” “Na mazingira nitakayo yakuta huko.” Grace akajibu
tena. “Naomba jitahidi kuongeza maelezo zaidi Grace! Unajibu kwa kifupi sana na
kuniacha na maswali mengi.” Grace akacheka. “Mbona nimejieleza sana!?
Nimekwambia inategemea na mazingira nitakayoyakuta huko, Man.” Tayari alisikika
kuchoka.
“Ndio
sijaelewa unamaanisha nini, Grace. Ukisema mazingira, unamaanisha nini.” Grace
akavuta pumzi, akafikiria kidogo. Akaanza tena. “Labda niseme hivi, nipo kwenye
mapumziko ya mwili na akili. Nahitaji kulala sehemu nzuri ambayo sitakuwa
nikiogopa usiku wala mchana, nakufanya akili yangu isitulie. Nataka nikimaliza
siku zangu za likizo, niwe nimepumzika kiukweli. Sijui umenielewa?” “Nimeelewa.
Kwani ni vitu gani unatarajia kwenye mapumziko yako?” “Utulivu Man. Nimekuja
huku, nitakwenda na huko mbuga za wanyama. Kisha nitazunguka mikoa mingine au
sehemu nyingine ili tu kufanya kitu cha tofauti mbali na kile nilichokuwa
nikifanya huko Dar.” Grace akaongeza.
“Kama
nimeelewa vizuri, ni kwamba hukuwa na utulivu huko ulikotoka. Si ndio?” Grace
akatingisha kichwa huku ameinama. Man akamuona amebadilika mpaka sura. Hata ule
uso uliokuwa na tabasamu ukapotea. Akajua kuna kinacho msibu. “Leo
wamekuongezea pronds kwenye hiyo supu. Sijui umegundua?” Akabadili mazungumzo,
Grace akajua. Akacheka kidogo. “Nimeona. Nashukuru.” Akajibu kwa kifupi akabaki
akikoroga ile supu huku akifikiria. “Kule mbugani utapafurahia Grace. Hakuna
kelele. Kuna utulivu wa aina yake.” “Wewe utakaa huko siku ngapi?” “Bado
sijajua. Inategemea na hali nitakayoikuta kule.” Man akaendelea.
“Kama ulivyosikia. Sasa hivi baba ni mgonjwa.
Mama ambaye walikuwa wakisaidiana hii biashara yao, ndiye anayemuuguza.
Wameniachia jukumu ya hizi hoteli za huku, halafu kaka yupo kwenye biashara zao
nyingine. Imebidi wote tuingilie kati kusaidia ili baba na mama watulie,
wafikirie swala la matibabu tu. Kwa hiyo kila kitu kinachoendelea hapa na kule
kwenye hoteli ya mbugani, ni mimi. Na kuendesha kitu cha mtu mwingine ni kazi
sana. Hasa kama mwenye nacho yupo na anakusimamia mgongoni. Ni ngumu sana.” Man
aliongeza.
“Kwa
hiyo mambo yangu mengi yanategemea na vile nitakavyotumwa.” “Pole kwa kuuguza
na hongera kwa majukumu.” “Asante kwa pole ya ugonjwa, lakini hongera ya
majukumu, sijui. Silali mchana wala usiku kwa hofu yakuharibu.” “Basi pole. Ila
utahitaji kupumzika Man. Yapo madhara yakutunza stress kwa muda mrefu. Mwili na
akili vinahitaji kupumzika mara moja moja.” “Basi na mimi nitachukua ushauri.
Nahisi nakaribia kulemewa.” “Pole.” Wakatulia.
Kulikuwa
na utulivu wa namna yake wakati wakiendelea kula na kunywa mpaka Grace alipoaga
nakumwambia anataka akapumzike. “Kwa hiyo umekataa kuongozana na sisi kesho?”
“Hapana kwakweli. Wewe enjoy na vijana wenzio. Kama nitarudi hapa na kufanikiwa
kukuona kabla sijaondoka hapa mjini Arusha, itakuwa vizuri. Tusipoonana tena,
basi ujue nilifurahia kila kitu. Asante.” Man akabaki akimtizama. Grace akatoa
tabasamu. “Uwe na usiku mwema Man.” “Asante.” Grace akaondoka kurudi chumbani
kwake.
~~~~~~~~~~~~~~~
Alirudi
kukaa pale pale alipokuwa amekaa mwanzo akiangalia watu wakiogelea kwa chini
mpaka giza likaingia, na baridi ya mji wa Arusha ikamuingiza ndani. Akawasha
tv, kuangalia kulikoni. Alipokutana na taarifa ya habari akaona azime tu,
hakutaka kujua kinachoendelea huko duniani. “Nipo hapa kwa ajili yangu.” Akazima na kuweka rimoti pembeni. Kwa
hakika hakujua kitu cha kufanya na maisha yake.
Alishalala
karibia siku nzima, hakuwa na usingizi. Kilichomtoa kwa haraka pale kwa Man, ni
kama maneno ya Geb yalitaka kutimia. Kadiri walivyokuwa wakizungumza na Man,
alizidi kuvutiwa naye. Umbile, sura, mipango yake na vile alivyokuwa
akimtizama, akaona asiibue kitu kingine. “Hata
hivyo Man bado ni kijana sana. Sitaki kuanza kumfikiria tofauti wakati mimi sio
msichana kama hao wanaomzunguka.” Grace akawaza.
Simu
ya mezani ikaita. “Hallow!” Grace akaitika
kwa sauti tulivu. “Nimekusumbua?” Akasikia sauti ya Man upande wa pili. “Hapana. Nipo tu nimekaa hata sijui nifanye nini na maisha yangu.”
“Kwani huwa unapenda kufanya nini?” “Huwezi amini, nimesahau Man. Niko kama
mjinga au mtu niliyeshuka ulimwengu mwingine kabisa! Hata sijui huwa watu wa
umri wangu wanatakiwa wafanye nini au wapende nini?” Man akacheka kidogo.
“Lazima kuna
kitu unapenda bwana. Jaribu kufikiria kidogo.” “Muda wote tangia nimefika hapa
ndio nilikuwa nikijifikiria. Hata pale uliponiona nakwenda kwenye fashion show,
ni wazo la Beka. Nilikuwa hata sijui nini natakiwa kufanya.” Grace akakaa. “Nimekuwa busy
sana na mambo ya familia. Nikaacha kujifikiria mimi mwenyewe kwa muda mrefu
sana. Sasa, sasa hivi mambo yamenibadilikia. Nimepokonywa majukumu yote, hata
sijui tena kitu chakufanya. Namsubiri tena Beka, anitafutie usafiri kesho.
Niende huko bunga za wanyama. Nikiona hamna chakufanya. Nahama mkoa.” “Kabla
hujafikiria kutukimbia, niruhusu nikupeleke ukaangalie cinema.” Grace akacheka.
“Kwa nini
unanicheka?” “Hapana Man. Naomba wewe endelea tu na mipango yako. Sitaki ukwame
kwenye mambo yangu. Nitakuwa sawa tu. Kwanza nahisi nitarudi kulala.” “Umelala karibia siku nzima
Grace. Bado unataka kuendelea kulala tu! Utakuwa hujitendei haki na hayo
mapumziko unayoyatafuta hutapata.”
Grace akaona anapoint.
“Basi
nielekeze huko kwenye cinema, niende tu mimi mwenyewe. Nitatafuta taksii.” “Kwa
nini unakuwa mzito kupokea chochote kutoka kwangu?” Grace akanyamaza. “Eti Grace?” “Sikufahamu Man. Halafu nipo kwenye matatizo makubwa sana
kwenye maisha yangu. Nipo kwenye kujaribu kutulia ili niweze kufanya maamuzi
sahihi ambayo sitakuja kujutia baadaye.” “Kwa hiyo unahofia kuwa naweza
nikakufanya ukashindwa kufikiria?” Man
akauliza, Grace akanyamaza.
“Kwa kuwa tokea nimekuona mara ya
kwanza umejaribu kunifukuzia mbali sana.” “Sio kukufukuza Man. Nimejaribu
kujibu maswali ya baadaye, mwanzoni. Wakati mwingine muonekana huwa unadanganya.
Nikaona nikupunguzie haso za baadaye. Usije kudhani mimi ni kama wanawake
wengine ambao ungependa kuwa nao karibu au ambao unajitahidi kuwaonyesha upendo
kama ulivyosema kwenye ndege.” Man akaishiwa
nguvu.
“Oooh! Kumbe
ndio maana unanikwepa!? Unajua mimi ni kama wachezeaji wengine tu? Kwa hiyo
unajua ndio kawaida yangu kwamba kila dada ninayemuona kwenye ndege huwa
natafuta kuwa naye karibu, ili niweze kulala naye?” “Sijasema hivyo Man!” Grace akajaribu kujitetea. “Ndivyo ulivyomaanisha. Naomba nikuulize swali Grace.”
“Karibu.” Grace alisikika kutulia wala
hajapaniki.
“Unajua
kulikuwa na abiria wangapi pale kwenye ndege?” “Hata sikuwa nimezingatia hilo!”
“Walikuwa wengi pamoja na watalii. Huwa vitu kama hivyo huwa sipuuzii kwa kuwa
nakuwa nipo kazini. Huwa najiuliza kwa siku Arusha huwa inapokea wageni wa
ngapi ambao watataka sehemu ya kulala? Na kwa nini isiwe moja ya nyumba za Mzee
Ole? Kwa hiyo nakuwa makini na kila kitu ili kujua nini chakuboresha na nini
kusaidia ili niweze kupata wateja wengi kila siku wanaoshuka kwenye ndege.” Man akaendelea.
“Taksii
uliyopanda wewe kukuleta hapa, baada ya kukataa lifti yangu, ni moja ya taksii
nilizoziweka pale uwanja wa ndege ili kutafuta abiria kama wewe ambao
wanatafuta sehemu ya kulala. Ndio maana uliponikatalia mimi tu, moja ya vijana
wangu au wetu walikuchukua na kukuleta hapa. Kama alifanya kama
nilivyowafundisha, alianza kukusifia hii hoteli na kukwambia vile wateja
wengine wanavyopafurahia. Si ndio?”
Grace akakumbuka.
“Basi. Huwa
kila nikisafiri, ninapokuwa narudi hapa Arusha, nakuwa nimeshajua kwenye ndege
hiyo niliyopanda nilazima nipate wateja wakulala hapa. Nawatumia ujumbe
madereva taksii wangu wote na kuwaambia wakae tayari au wasogee karibu na
uwanja wa ndege, kuna wateja kadhaa. Wengine wanaweza hata kuingia ndani na
flyer za hoteli kutafuta wateja ndani ya uwanja wa ndege. Wakitoa punguzo la
bei ya usafiri, au kuwabeba bure kabisa. Inategemea nipo kwenye msimu gani hapa
hotelini. Kama nataka wateja wengi au nimejaza.”
Grace akashangaa sana.
“Sasa huwa
unajuaje kama ni wageni na hawana sehemu yakufikia?” Grace akahoji.
“Kuku mgeni hakosi kamba mguuni,
Grace. Halafu nilisomea mambo ya saikolojia na Mungu alinisaidia kipaji cha
ucheshi. Hainisumbui kuwa karibu na watu na kujua wanahitaji nini na kujitoa
kusaidia. Nilisumbuka sana kipindi cha mwanzoni baba aliponiachia hii kazi.
Nikagundua kuna siku vyumba vinakuwa havina watu kabisa wakati hili ni jiji la
utalii. Nikajua kuna shida tu. Maana hoteli yenyewe haipo pabaya. Sasa ni kwa
nini tusipate wateja? Ndio nikajitupia kwenye kuwekeza. Imechukua muda na
inanichukulia muda mwingi lakini hatimaye naona kuna matunda mazuri.” “Unaakili
sana Man. Hongera.” Grace akasifia.
“Kwa hiyo
Grace, ucheshi wangu na ukarimu kwa watu wengine haimaanishi nilazima niishie
kulala nao. Au ni kwa kuwa nawataka kimapenzi. Hapana.” “Sikusema hivyo Man!” Grace aliendelea kusisitiza. “Lakini ulimaanisha hivyo, Grace. Usikatae. Mungu hakunijalia nguvu
hizo. Nakutana na mabinti wengi sana. Na nina wafanyakazi warembo kama kina
Beka. Shuguli zangu zinanikutanisha na watu wengi tofauti tofauti wenye sifa
mbali mbali. Kama nikijaribu kulala hata na mmoja wao, najua nitaharibu sana.
Sitaweza kufikia malengo.” Grace
akanyamaza.
“Kwa hiyo
Grace, huwa pia sina mtindo wakupigia simu wateja nakutaka niende nao Cinema.
Ukipata muda kidogo na Beka, jaribu kumdodosa juu yangu. Wengi wanahisi mimi
ninatatizo. Lakini ni maamuzi tu.” “Samahani Man. Nahisi ni kwasababu ya mambo mengi kichwani au hapa
ninapopitia sasa hivi ndio maana nakuwa si muungwana. Naomba unisamehe tu.”
“Apology accepted.” Wakacheka na kutulia kidogo.
Grace
hakujua aongee nini tena. “Huwa unaondoka hapa
saa ngapi?” Grace akaona atupie swali. “Kwenda wapi?” Man akauliza. “Namanisha kurudi nyumbani kwa familia kutoka hapa kazini.” “Hilo swali
naweza kukujibu wakati tukielekea kwenye ukumbi wa Cinema?” Grace akasita
kidogo. Akatulia kwa muda. Man akajua anafikiria. “Unataka nikuache ufikiri na hilo?” Grace akacheka. “Sawa.” “Sawa tunakwenda au sawa nikuache ufikirie kama unataka kwenda cinema
na mimi?” Akamsikia Grace anacheka kidogo. “Sawa tutaongozana. Lakini nitahitaji muda wakujiandaa kidogo.” “Hamna
shida. Unafikiri kama baada ya muda gani?”
Grace akabaki akifikiria. “Ili unikute
nikikusubiri hapo nje. Nisikuweke sana.” “Sitachukua muda mrefu. Kama nusu saa
tu nitakuwa nimeshuka.” “Basi utanikuta mapokezi nikikusubiri.” Wakakata simu.
Grace akavuta pumzi kwa nguvu. Akajikuta amehamasika kweli.
~~~~~~~~~~~~~~~
Man & Grace.
Grace
akatoka kuelekea ilipokuwa lifti. Akapanda ili imshushe gorofa ya chini kabisa walipokubaliana
wakutane na Man. Ilimteremsha mpaka chini, akamkuta Man anasubiria nje ya
lifti. Akacheka. “Umejuaje kama ndio
nashuka?” “Uliniambia baada ya nusu saa. Ilipotimu na mimi nikajisogeza hapa. Umependeza
sana Grace.” Ni kweli alipendeza. “Asante. Hata wewe Umependeza.”
“Asante.” Grace alijuwa wazi na yeye alioga na kubadili. Kwanza hakuwa amevaa
vile walipoachana na alinukia so fresh. Kuashiria
alitoa jasho la siku nzima.
Wakaongozana
mpaka kwenye gari. Hapo njiani wakielekea kwenye gari, Man alishasalimiana na
watu kadhaa na kuweka utani wa hapa na pale. Kuanzia wahudumu wa hiyo hoteli
mpaka wageni wao, hakukosa neno lakuzungumza nao, nakuwafanya wacheke. Grace
alitembea pembeni yake kimya akimsikiliza na kumwangalia anavyowatania. Ndipo
wakafanikiwa kufika kwenye gari. “Wewe ni mtundu sana Man.” Man akacheka. “Ndio
wanaoniweka mjini hao! Lazima kuwapa muda. Samahani lakini.” Grace akacheka. “Hamna
neno. Na mimi najifunza.” Akamfungulia mlango.
Baada
ya wote kufunga mkanda, wakaondoka. Baada ya muda mfupi tu wa kuwa hapo
barabarani, akamwambia wamefika. “Kumbe sio mbali!?” Grace akauliza. “Ni kwa kuwa pia mida hii
hamna foleni.” Akatafuta sehemu ya kuegesha gari yake, akafungua mkanda na
kumgeukia Grace. “Naomba nikwambie kitu na nikujibu swali lako kabla
hatujashuka.” “Karibu.” Grace akamgeukia baada ya yeye pia kufungua mkanda.
Man Afunguka Kwa Grace.
Man akaanza. “Kwa nini upo hapa na mimi au kwa nini
nimekualika uje na mimi hapa? Tena baada ya kukwambia huwa si kawaida yangu.”
Grace akacheka kidogo. “Najua hilo swali lilipita kichwani mwako. Naomba niwe
mkweli, lakini usinielewe vinginevyo wala usinifikirie nina nia nyingine.”
Grace akabaki kimya akimsikiliza. “Una utulivu fulani hivi! Yaani ukizungumza
au mtu yeyote anayebahatika kuwa karibu yako, anapata hiyo hali. Unajisikia
utulivu wakutoka ndani. Kama kupumzika fulani hivi! Sijui nimejieleza vizuri?”
Grace akacheka sana.
“Usinicheke
bwana! Sasa kwa kuwa nimekuwa busy kwa takribani miaka miwili mfululizo. Kazi
na kufikiria kufanya nini huku tukimuuguza Mzee tu, nilitamani kupumzika hata
kwenda mahali. Nikajaribu kufanya kama wewe, sikupata pumziko. Nikajikuta
naamka asubuhi yake na kurudi kazini. Nilipokufuata kwenye ndege, ni kwa kuwa
kwanza kabisa nilivutiwa na rangi yako ya mwili halafu ukawa upo wakisasa.
Nikajiambia labda wewe ni mwana mitindo hivi au mambo fulani ya hali ya wenye
pesa au wanaoishi na pesa. Nikajua nitapata mteja. Kumbuka ulikuwa umevaa
miwani kama ya jua. Sikuwa nimekuona hayo macho yako.” Grace akatingisha kichwa
huku anacheka.
“Nilihamia
pale ili tu kukuchokoza na kukukaribisha hotelini kwetu. Nikijua ukifika hapa,
utavutiwa na kuniletea wateja wengi zaidi. Lakini tokea nimekaa pale, mpaka leo
muda mfupi tuliokuwa tumekaa pale nje, nilijisikia kupumzika sana. Ile hali ya
utulivu iliyonifanya nisafiri, ili kuitafuta, niliipata kwa kukaa tu na
kuzungumza na wewe. Nikajiambia sio mbaya nikuombe tutoke tukaangalie movie
pamoja. Wewe utapata pumziko la akili kwa kuangalia movie, na mimi kwa kuwa
karibu yako. Unafikiri nimekosea?” Grace akacheka na kutingisha kichwa
akiashiria hajakosea.
“Nakushukuru.
Sasa kujibu swali lako. Na mimi ni baba wa mtoto mmoja wakiume. Nilioa miaka
kama kumi iliyopita. Ndoa yangu iliisha baada ya miaka minne, migumu sana ya
hiyo ndoa. Yote hiyo miaka minne, nilibaki na huyo mwenzangu, nikifikiria
tungeweza kunusuru ile ndoa ili tulee mtoto na pengine kuongeza mtoto mwingine
hasa wa kike. Kwa kuwa tayari tulikuwa na wakiume. Lakini ilishindikana.
Hatukuwa tukionyesha mfano mzuri mbele ya huyo mtoto. Ugomvi wa mara kwa mara.
Matusi mabaya. Kwa kifupi hapakuwahi kuwa na amani humo ndani. Naona mwenzangu
alinivumilia mpaka akafika mwisho. Akaamua kunitaliki.” Man akaendelea.
“Kabla
ya yote hayo, au tuseme kilichokuwa kikinibakiza pia kwa miaka yote hiyo ya
shida zikiwa zinaendelea ndani ya hiyo ndoa, mojawapo ilikuwa swala la mtoto.
Nani anabaki na mtoto endapo tunatengana! Ikawa kikwazo kwangu. Nilijua
tukiachana tu ndio nitapoteza mtoto. Nikajua hata tukipelekana mahakamani,
siwezi kushinda. Kwa kuwa mwenzangu alikuwa nchini kwao, rangi kama wao,
alikuwa na kazi nzuri inayomuingizia kipato kuliko mimi, nikajua wazi mahakama
itampa dhamana yakubaki na mtoto. Mimi ndio nitakuwa nimepoteza mwanangu.
Ikabidi kuendelea kuwa mpole mpaka akachoka yeye.”
“Mbaya
zaidi yule dada alikuwa mwanasheria. Alikuwa na pesa, na ni kama nilikuwa
nikiishi nyumbani kwake japo tulifunga ndoa. Baada ya yote, alihakikisha
ananiharibia kiasi ya kwamba siwezi kurudi tena pale nchini. Hapa
ninapozungumza na wewe huu ni zaidi ya mwaka wa 8 sijamuona mtoto wangu wala
sijui anaendeleaje.” “Pole Man. Pole sana.” Grace akamuhurumia.
“Ni habari
ambayo siizungumzi mara nyingi kwa kuwa inaniuma sana. Ni mtoto ambaye nilimlea
mimi mwenyewe tokea mama yake anamzaa mpaka napokonywa. Alikuwa hajui maisha
mengine bila mimi. Mama yake alikuwa na kazi nyingi sana. Kama nilivyokwambia
alikuwa mwanasheria. Kipato chake kilikuwa kikubwa kuliko mimi. Tukashauriana
mimi ndio niache kazi nibaki nyumbani kulea mtoto.” “Ulikuwa ukifanya kazi
gani?” Grace alitupia swali, Man akacheka.
“Mbona
unacheka mwenyewe?” “Katika mambo niliyoyafanya ya ajabu hapa duniani, jingine
ni hilo. Nilifaulu vizuri hapa kidato cha sita. Katika muda ambao nasubiri
kwenda kusoma mambo ya udaktari katika chuo kikuu cha Muhimbili, nikapata
mtalii mmoja, aliyekuwa amefikia hapa hotelini kwa baba. Akaniambia nikienda
huko nchini kwao, watanisaidia kusoma kwa kuwa nilifaulu vizuri na ninaonekana
nina akili.” Man akaendelea. “Kufupisha stori, nikafika huko, nikakutana na
kundi la vijana wa huku. Wakaniambia mwili wangu unauzika kule kwa kufanya
matangazo.” Wakacheka.
“Usicheke
sasa. Ukumbuke hapo nilikuwa na kibali cha shule. Wakaniunganisha na kampuni
moja ambayo ikanikubali urefu na umbile. Wakanipa kazi yakutangaza bidhaa zao.
Wakati mwingine wakipata tenda yakutangaza nguo za kiume, basi mimi ujue
nitashinda. Napata kazi. Iwe saa, pafyume, viatu na mambo mengine mengi, mimi
nikawa nikiwafanyia kazi ya kuwatangazia. Kufunga na kufungua Manesa nikawa
Celebrity. Pesa inaingia vizuri. Nipo kwenye mabango ya hapo nchini.” “Nchi
gani sasa, mbona hutaji?” Man akacheka.
“Subiri
sasa. Kule kwa wale wazungu waliokuwa wamenileta pale nchini, nikahama. Shule
nikaanza kuona inanipotezea muda. Kwani si nasoma ili nipate pesa? Sasa kipaji
na mwili wakuniingizia pesa ninavyo. Shida iko wapi? Kwa nini nitupe mapesa
yote hayo kulipa ada shuleni wakati naweza kuwekeza hata kwenye biashara nikaendelea
kupata pesa? Maisha yakaendelea. Naishi vizuri, Man nikawa gumza la watoto
wenye ngozi nyeusi huko mitaa ya weupe. Huwezi kuniona hovyo hovyo. Na hivi
Mungu alinijalia sio mlevi, basi hata club huwezi kunikuta. Maisha yakaenda
mpaka mwaka wa pili. Kumbuka wa kwanza ilikuwa kazi na shule. Mwaka wa pili
nikanogewa, nikaacha shule. Ikawa kazi tu.” Man akaendelea.
“Pia
kumbuka kilichokuwa kikiniweka kihalali pale nchini ni shule. Sasa shule
ilipoisha, au nilipositisha kusoma, moja kwa moja na vibali vya kuishi hapo
nchini vikaisha. Si unatujua sisi ngozi yetu tunavyopendana? Wakawapigia simu
ofisi za uhamiaji kuwataarifu kuwa nafanya kazi kwenye kampuni fulani wakati
nipo pale nchini isivyo halali. Sina vibali.” “Haiwezekani Man!” Grace
akashangaa.
“Acha
utani na wana wa Bin-adam! Si nikaanza kufuatiliwa sasa? Ile kampuni ikaanza
kuingizwa kwenye matatizo. Wakanitafutia mwanasheria mdada wakunisaidia. Hapo
bado haikuwa kesi. Ila tu kujihami au kujiweka sawa ili kampuni
itakaposhitakiwa, isiingie matatizoni. Basi, nikapewa huyo mwanasheria
msichana. Akashauri kwa wakati ule niache kabisa kazi. Na njia pekee na nzuri
kwa haraka ni nioe raia wa pale. Ndipo itanirahisishia. Sitaweza kukamatwa.
Swala likawa wakumuoa ni nani? Kumbe yule dada tayari alishanipigia mahesabu,
mimi sina habari. Alikuwa mtu mzima kidogo na alikuwa na maisha fulani hivi.
Yaani mazuri kwa pale nchini. Kwa hiyo hata sikuwa nikimfikiria kama anaweza
kunitaka mtu kama mimi.” Man akaendelea.
“Kwanza
sikuwa na taaluma yeyote kama yeye. Halafu tulipishana kama miaka 6 hivi. Kwa
hiyo sikuwa hata na wazo. Akawa ananiita huku au kule tuzungumzie swala langu
la uhamiaji. Huku na kule akanialika nyumbani kwake kwa chakula cha usiku.
Nikaenda. Tukapata chakula. Yeye akanywa wine, anavyosema alilewa. Akaniambia
yote yaliyokuwepo moyoni na kunitaka kimapenzi. Mimi nikamchangamkia usiku huo,
nikaondoka.” Grace akamuona amebadilika sura.
“Nilijuta
Grace. Ndio ilikuwa mwanzo wa matatizo yangu. Siku inayofuata yule dada
akanipigia simu nakuniambia kwa nini nililala naye wakati yeye alikuwa amelewa?
Nikajaribu kumkumbusha kuwa yeye ndiye aliyeniomba, tena aliniambia alikuwa
akinitamani muda mrefu. Imekuwa akinionyesha ishara zote, mimi sielewi.
Nikamkumbusha yote hayo, akasema hakumbuki. Kitu anachokumbuka alikunywa sana,
mimi nili ‘take advantage’ ya ulevi wake.” “Haaa!” Grace akashangaa.
“Yeye
ni mwanasheria. Nina kesi tayari uhamiaji. Dada ananililia kwenye simu ni kama
nimembaka. Akanionyesha video aliyotoa kwenye kamera ya ulinzi hapo nyumbani
kwake. ‘CCTV’. Kuanzia naingia nyumbani kwake, mpaka tunafanya mapenzi hapo
kwenye kochi. Ikabidi kumuomba msamaha ili yaishe, lakini nilijua wazi
alinitega. Niliumia sana. Yule dada akasema amesamehe, lakini zile zilikuwa
siku zake mbaya. Heri ningevaa kondom. Haya. Hilo nalo likawa kosa la pili.
Ikabidi kusubiria kama ameshika mimba.” “Pole Man.” Grace akazidi kumuhurumia.
“Hatujakaa
sawa, akanipigia kuwa ameshika mimba. Lazima nimuoe ili jamii isimuelewe
vibaya. Ametoka kwenye familia yenye maadili, hawezi kuonekana ana mtoto bila
ndoa. Hapo ananiambia tuoane kwa haraka kabla watu hawajajua kama ni mjamzito.
Na ujue hapo tena anaongea na mkosaji, sio mpenzi wake. Kwa hiyo ni lazima
kumuoa kwa kuwa mimi nimemsababishia. Sawa. Ikabidi kukubali, ili nalo hilo liishe.
Kwa upande mwingine nikajiambia nitaua ndege wawili kwa jiwe moja. Ikitokea
uhamiaji wananifuatilia, nitakuwa nimeshakuwa mume wa yule dada ambaye ni raia.
Tena nikajiambia nitaanza kufuatilia swala la uraia mapema sana. Halafu
nitakuwa pia karibu na mtoto wangu.” Man akaendelea.
“Familia
yake wakagaramia harusi. Ndoa ikafungwa. Huku nyumbani sikutaka hata wajue. Kwa
kuwa ukumbuke hapo nilikuwa nimetumwa kuja kusoma si kuanzisha familia. Maisha
yakaanza. Lakini Grace, kitu chochote kilichoanza kwa hila huwa hakidumu.
Kitashamiri kwa muda tu, lakini mwisho wake lazima kitaharibika sababu ya
misingi mibovu. Hasa kwenye swala la mapenzi.” Grace akakumbuka mwanzo wake na
Danny. Man akamuona ameinama anafikiria. Akatulia kidogo.
“Basi.
Migogoro ikaanza. Kwa kuwa mimi sikuwa na kazi, akataka nibaki tu nyumbani
nilee mtoto. Lakini ukumbuke bado nilikuwa na kinyongo naye. Nilijua wazi
alinitega, akijua hali yangu kwa wakati ule. Halafu sikuwa tayari kuoa. Kwa
kifupi hakuwa mwanamke ambaye hata ningemfikiria kuoa. Sikuwahi kutamani kuoa
mwanamke mweupe. Hata siku moja. Nilikuwa nikifikiria kuja kuoa nyumbani. Tena
baadaye. Kwa hiyo niliingia kwenye ndoa ambayo sikuwa na furaha nayo. Mimi ni
mwanaume wa kimasai, wakujua maadili ya kimasai. Kuja kuishi na mwanamke ambaye
yeye ndio anaongoza mambo! Hapo napo ilitusumbua sana. Mpaka ikafika mahali
sasa ananitishia, ndipo ikabidi kuwa mpole.” “Anakutishia nini tena?” Grace
akauliza.
“Kumbuka
bado alikuwa na ile video ya siku ya kwanza kufanya naye mapenzi! Pili alijua
kesi yangu ile yakufanya kazi pale nchini kwao kwa muda wa mwaka mmoja, bila
vibali. Na yeye alikuwa mwanasheria. Mbona niligeuzwa yaya? Nilimtumikia vile
anavyotaka yeye. Ungenikuta wakati ule ungesema mimi ni mfanyakazi aliyeniajiri
kazi ya yule mtoto. Nilimfanyia kila kitu anachotaka yeye. Nilimlea mtoto vile
alivyotaka yeye. Uzuri yule mtoto alizaliwa tukiwa tunafanana naye sana. Hilo
likanipa moyo. Lakini Grace, nilijuta kuzaliwa mwanaume.” “Kwa nini
hukutoroka?” Grace akauliza.
“Kumbe
sikukwambia?” Man akauliza. “Nini tena?” “Alinipokonya hati yangu yakusafiria.
Akaificha. Nilikuwa siwezi kutoka kwenda popote bila ile hati. Na nisingeweza
kuondoka pia bila mtoto wangu. Kwa kuwa nilishamjua ni mtu wa namna gani,
sikutaka kumuachia mwanangu. Kufupisha stori, nyumba haikuwa na amani kabisa.
Ugomvi kila kukicha. Unaweza kufikiri wanaishi maadui humo ndani. Akagoma
kabisa kunishugulikia kubadili uraia. Akawa akinikumbusha kuwa nipo pale nchini
isivyohalali. Ule nao ukawa wimbo ulionifanya kutulia kila anaponiona
nimekasirika, akiwa yeye ameniudhi au anataka nimfanyie kitu.” Man akaendelea.
“Mtoto
alipofikisha miaka 4, hapo ndipo nilipojua rangi zote. Akanibadilikia haswa.
Akawa anatafuta sababu za kuniacha sasa. Hapo na mimi nikawa nimeshamjulia.
Namkwepa sababu ya mtoto ameshapata uelewa. Sitaki atuone vile tunavyogombana.
Nikishajua anataka kugombana, nanyamaza kabisa. Akija usiku amelewa, nalala
kwenye makochi. Hali ya ugomvi ikawa haipati kwa kuwa mimi nanyamaza. Mtoto
akawa anamkwepa sasa. Kwa kuwa yeye ndio alikuwa mkali na mtoto anamuona.
Akimshika mtoto, analia mpaka anatapika. Akitaka kwenda na mtoto mahali, mtoto
hataki. Analia kama vile anashikwa na mwizi. Ukumbuke mimi ndio nilikuwa
nikimlea yule mtoto masaa 24. Kwanza wala hakutaka kunyonyesha ili asiharibu
matiti yake.” “Jamani!” Grace akashangaa sana. Man akacheka.
“Sasa
mapenzi aliyokuwa akiyajua Liam, ni ya baba tu.” “Mtoto alikuwa akiitwa Liam?”
Grace akauliza. “Samahani sikukwambia. Ni Liam. Tena jina alimpa yeye mwenyewe.
Basi, alipoona mambo yanazidi kuwa mabaya, akaenda kunifungulia kesi.”
“Haiwezekani! Nini tena?” Grace akazidi kushangazwa.
“Mambo
yote. Kesi ile yakufanya kazi bila kibali, akaifungulia mashitaka. Akaongeza
kesi ya kumbaka akiwa amelewa. Akasema nilifanya hivyo ili nimpe mimba, ili
nimuoe, anisaidie uraia. Alitengeneza ile kesi, wakanifunga jela bila shida.”
“Man! Pole sana.” Grace akamuhurumia.
“Ila
alitumia akili. Alimwanzisha mtoto shule. Alipoona mtoto ameanza kuzoea shule.
Anatoka asubuhi anarudi jioni, ndipo akanihamishia mimi jela. Akadanganya kuwa
huwa nampiga sababu ya hasira yakukataa kunibadilishia uraia. Siku hiyo
nimetoka kumpeleka mtoto shule, nipo tu nyumbani, nashangaa nafuatwa na polisi.
Nauliza ni nini? Hapo ndipo nilipochoka. Kumbe mke wangu alikwenda polisi. Amevimba
jicho, anasema nilimpiga asubuhi hiyo nje ya nyumba wakati anaenda kazini. Na
ile nchi bwana, huwezi kucheza na mwanamke, mbaya zaidi, yeye mweupe mimi
mweusi. Nilicheza ngoma za kwetu.” “Pole sana.” Grace akamuhurumia zaidi.
“Kumbuka
hapo nipo ugenini. Wazazi hawajui kama nimeoa wala nina mtoto. Sina kazi.” “Ile
familia iliyokuwa imekupeleka pale nchini?” Grace akauliza. “Nilihama mji
kabisa. Si nilipata kazi? Kwa hiyo nikawaaga na kuwaambia nahama mji kwa kuwa
nimepata kazi na nitasoma. Hawakuwa ndugu Grace. Kila mtu yupo busy na maisha
yake, nani anifuatilie? Na sikuwa nimewasiliana nao zaidi ya miaka 5 mpaka
nawekwa jela. Usiombe ukawa mweusi, kosa lakunyanyasa mwanamke mweupe,
ukafungwa jela ya ughaibuni! Grace, niliteswa huko jela! Usitake kujua zaidi.”
“Pole.” Grace aliweza kuhisi.
“Kama
wakati ule ungeniambia nitakuwa hapa sasa hivi, nisingekubali. Hakuna mateso na
manyanyaso unayoweza kufikiria ambayo sikupitia. Tena kwa shida sana. Sina
wakunitetea, sina pesa. Hakuna mtu aliyekuwa akija kunitembelea jela, nilikuwa
mimi tu. Miaka mitatu ikaisha. Kesi yangu imetupwa mbali. Hakuna
wakunisikiliza. Ni kama nilirushwa shimoni. Nateseka. Mwaka wa nne, nikawa
nimeshakuwa mwenyeji pale. Nimezoeana na kila mtu hata watesi wangu nikawa
najua wanachotaka. Hapo ndipo nilipoweza kupata nafasi yakumpigia simu Mzee
Ole, nakumwambia nilipo maana hata wao walishaingiwa na wasiwasi.” Man
akaendelea.
“Baada
ya siku kama 10 hivi. Nikasikia nina mgeni. Nikahisi mzee Ole ameshatua nchini.
Kumbe kweli. Alikuja na mama, na mwanasheria. Hapo kesi yangu ikawa sasa
imehamishiwa ikawa si ya mtu binafsi tena. Nchi yatanzania inataka haki
itendeke. Ilikuwa kesi kubwa sana. Hapo Mzee alikuwa akimwaga pesa kulia na
kushoto. Uzuri hapa nchini alikuwa akifahamiana sana na viongozi wengi wa
serikali. Vikao vingi vya kimataifa vilikuwa vikifanyika kwenye moja ya hoteli
zake. Kama sio hapa Arusha, basi jijini. Kwa hiyo Mzee alikuwa akifahamika
sana. Kufupisha habari, kama baada ya miezi 6, nikaachiwa huru.” “Afadhali.”
Grace akapumua.
“Afadhali
kwa kuwa nilitoka jela. Lakini ukumbuke hapo ndio ukweli wote ulijulikana kwa
wazazi. Wakajua miaka yote ile nipo pale, nilikuwa sijasoma. Sina elimu yeyote
zaidi ya elimu ya mwaka mmoja niliosoma nilipofika pale nchini. Na nilikuwa
nikiwadanganya nipo shule. Haya, mtoto nilipokonywa, kwa sababu kwanza nilikuwa
mtuhumiwa. Nisingeweza kabisa kuruhusiwa kuwa na yule mtoto. Pili sikuwa raia
wa pale. Nilipewa masaa 12, niwe nimetoka hapo nchini. Ndio nikarudi sasa hapa
nchini nikiwa nimechanganyikiwa, nipo kama mgonjwa.” “Pole.”
“Ilinichukua tena karibia mwaka
kuja kurudi kujijua mimi ni nani, ila sijui chakufanya. Nishapoteza miaka zaidi
ya 10. Akili haiwezi tena kurudi kuwa
mwanafunzi. Wala siwezi tena kuwa kama watu wengine. Mawazo yapo kwa Liam.
Mtoto niliyemuacha shuleni, tukiwa na mipango ya nini chakufanya jioni yake
akitoka shule. Mimi ndiye nilikuwa rafiki yake mkuu. Kuoga, kula na kucheza ni
mimi. Nilikuwa kama nimechanganyikiwa sababu yakumuwaza na kumuhurumia yule
mtoto. Sina picha yake, sina kumbukumbu yeyote niliyochukua kati yangu mimi na
yeye.” “Kwa nini ulivyotoka jela, kabla ya kurudi huku hukuomba kwenda
kumuaga?” Man akacheka.
“Mama yake alilijua hilo. Kwa hiyo moja ya masharti niliyokuwa nimepewa, nikuwa mbali au nisisogee karibu na yule mtoto!” “Jamani!” Grace akashangaa. “Ukumbuke nilishitakiwa kwa makosa makubwa sana Grace. Yaani kutoka pale ilikuwa ni Mungu tu. Nakwambia nilirudi hapa nimechanganyikiwa. Mzee anahasira na mimi, haniamini tena. Wadogo zangu wote wakawa wamesoma. Wanakazi zao na makwao. Mimi nimerudi kuwa tegemezi kwa asilimia zote. Halafu mimi ndio kaka mkubwa kwa mama. Baba alikuwa na mtoto mwingine wa kiume alizaa na mama mwingine aliyefariki. Lakini alikuwa na maisha yake na anajitegemea. Hawakuwa karibu sana na baba, japo alilelewa na mama.” Grace akakumbuka mazungumzo ya wale watu aliokuwa amekaa nao meza moja, siku ya fashion show.
“Basi ikabidi mama kuanza kunijenga upya. Akawa karibu na mimi. Yeye ndiye mtu wa pekee mbali na wewe niliyeweza kumuelezea haya yote. Yaani tokea kipindi kile, sikuweza kumwambia mtu chochote, mpaka leo kwako.” Grace akainama kama anayefikiria. “Nikaanza kuingia kwenye miradi ya baba. Hatukukaa sawa, na yeye akaanza kuugua. Ndio ikabidi kunikabidhi kwa lazima. Lakini akiwa hana imani na mimi kabisa. Kumbuka nilishamdanganya, na nikawa nikiendelea kumdanganya kwa muda mrefu tu. Kwa hiyo akabaki akiniambia kama sio kufungwa jela, asingejua ukweli. Ambayo ni kweli. Lakini nikakusudia moyoni, kumwakikishia nimejuta kwa nilichofanya, na nimekusudia kubadilika.” “Nikaingia kazini sasa. Uelewa wa kule nilikoishi ughaibuni ukanisaidia. Nikaanza kutafuta sababu zinazomfanya asiingize pesa kwenye hii hoteli ya hapa. Nikahamia kuishi hapa hotelini. Ili kuchunguza kinachoendelea ili niweze kurekebisha. Nikagundua natakiwa kubadili mambo mengi sana. Kuanzia wahudumu, mpishi na jinsi yakujitangaza. Tokea wakati ule mpaka sasa, naishi pale hotelini. Maisha yangu ni kazi tu. Nawaza ni nini chakufanya kuboresha. Namshukuru Mungu nimeweza kurudisha heshima nyumbani. Nimeweza kumpanulia baba biashara mpaka nikaingia naye ubia. Sasa hivi ni nusu kwa nusu. Namiliki naye. Tumeweza kuongeza hoteli mbugani. Nimefungua kampuni ya utalii, ambayo ipo pale pale hotelini kwa nyuma. Nimewekeza kwenye magari ya utalii, zikiwemo hizo taksii ambazo zinanisaidia kusaka wateja. Na mengineyo. Ndio nipo hapa na wewe.” Grace akatabasamu.
“Pole
na hongera.” “Kwa mara ya kwanza tokea nirudi nchini leo ndio nimepata amani
yakutoka na mwanamke. Yaani sio kikazi.” “Kwa nini?” Grace aliuliza taratibu. “Nilikinahiwa
mno. Unakumbuka nilikwambia nilijuta kuzaliwa mwanaume?” Grace akatingisha
kichwa. “Unakumbuka nilikwambia sikutaka kuoa mwanamke mweupe?” Grace
akatingisha kichwa kukubali. “Si mweupe tu kuwa mzungu, ila hata mweupe wa
rangi.” “Kwa nini!? Wanawake weupe walikufanya nini?” Grace akauliza kwa
mshangao.
“Mama
yangu na dada zangu ni weupe haswa.” “Hata wewe ni mweupe Man.” Grace
akaongeza, wakacheka. “Basi. Ndio hivyo. Kasoro Mzee tu ndio mweusi. Kwa hiyo
kila mwanamke mweupe ninayekuwa namuona, namuona kama mama yangu au dada zangu.
Siwezi kulala nao au kuwa nao kwenye mahusiano ya kimapenzi.” Grace alicheka
sana. “Najua utanishangaa. Lakini hata mimi sielewi ni kwa nini hiyo kitu
imeniingia hivyo. Sielewi. Ila ujue kwa
muda wote huo niliokuwa na yule mwanamke, nilikuwa kwenye mateso. Neno mapenzi,
likapoteza maana kabisa. Alinipitisha mahali nikayachukia mapenzi na matendo
yake yote. Nilirudi nchini nikawa nimekinahiwa. Hata watu wanaponisema sasa
hivi kuwa ninatatizo ndio maana nakimbia wanawake warembo napenda kuwa karibu
na wanaume, huwa sipingi. Nanyamaza kabisa na wala huwa sikanushi. Naona
garama ya hizo shutuma, ni ndogo sana kuliko kuwahakikishia mimi ni mwanaume na
wala sipo ule upande wa pili.” Grace akainama. Akiwa ameelewa kuwa yeye sio
shoga.
“Wewe
ndio mwanamke wa kwanza wananiona ninatoka naye leo jioni. Kwanza huwa sitoki.
Kama nipo hapa Arusha, wakati wote nakuwa nazunguka pale hotelini. Kila mahali
kuhakikisha kila kitu kipo sawa. Nimewafanya wawe karibu na mimi ili waweze
kuniambia matatizo yao na ya pale kazini. Lakini sio kunizoea sana. Nimeweka
pia mipaka, ili kutunza heshima yangu. Sijui kama unanielewa?” “Pole kwa
matatizo yote.” Grace akaongea taratibu.
“Ndio
maana umenifanya niongee ambayo hata sikutakiwa kuzungumza!” Grace akacheka
tena. “Kweli Grace. Nimekufahamu kwa kukuona jana tu! Lakini tayari nimefunguka
kwako kama nimekufahamu miaka 10 iliyopita!” Grace aliendelea kucheka. “Nimefurahi
umeniamini.” “Sio kukuamini tu. Umetulia sana Grace. Unaweza kumfanya mtu
ajisikie vizuri na kuwa yupo salama.” “Sio wote Man. Labda wewe tu.”
“Unajua Grace, nimekuja kujifunza kitu kimoja. Hata Mzee alishaniambia sana.
Nimeamini.” “Nini?” Grace akauliza.
“Wakati
mwingine huwa hatuoni thamani ya kitu pale tunapokuwa nacho. Mpaka kikiwa kwa
mwingine ndipo mtu anapoanza kushituka. Mwanadamu ameumbiwa kuzoelea mambo. Na
mbaya zaidi, huwa tunapitiliza. Inafika mahali mpaka tunapuuza. Tunatoa
thamani ya kile kitu, tunaanza kutumia kwa matumizi mabaya. Ndivyo tulivyo.”
Grace akainama kwa muda. Man akamuona anavuta pumzi na kugeukia dirishani.
Akaangalia
saa. Grace akamsikia akicheka. “Unajua sasa hivi ni saa ngapi?” Grace
akaangalia na yeye saa ya gari. Akacheka. “Hata kwenye Cinema watakuwa
wamefunga. Ona tumebakia sisi wenyewe tu hapa. Hamna gari jingine! Utajuta
kukubali kuja na mimi.” Grace akacheka. “Hapana. Nimefurahia tumepata muda
mtulivu. Tumeweza kuzungumza. Nilikuwa sijui nifanye nini peke yangu pale chumbani.
Nilifurahi uliponialika kuja hapa. Haijalishi ni nini tumefanya. Ila ujue
nimefurahi kukufahamu Man.” Man akabaki akimwangalia.
Grace
alikuwa amepooza zaidi ya alivyo. “Njaa inakuuma?” Man akauliza. “Ningependa
kula, lakini muda umekwenda sana. Sidhani kama tunaweza kupata sehemu ambayo
bado wanauza chakula.” “Ngoja nimpigie Yusuf simu.” “Yusuf ni nani?” “Mpishi wa
pale hotelini. Wakati mwingine anakuwa jikoni mpaka sasa hivi.” Man akapiga.
Grace
akamsikia akitaniana naye kidogo, wakaagana. “Amekubali kututayarishia chakula.
Turudi. Najua utapenda chakula chake. Sijui anaweka nini bwana! Sijawahi
kuchoka chakula anachopika.” Grace akacheka. “Au wewe umechoka chakula cha
pale?” Man akamuuliza baada ya kumuona amecheka tu. “Hapana. Kwanza mimi huwa
sichagui vyakula. Napenda kula. Kwa hiyo nakula kila kitu.” Man akacheka.
Wakatoa gari.
~~~~~~~~~~~~~~~~
“Nilikwambia
asante kwa kunitoa pale chumbani?” Grace akauliza. Man akacheka. “Uliniambia.
Japo sijajua ni kwa nini unakosa kitu chakufanya Grace. Wewe sio Mzee kama
unavyonitangazia. Japokuwa hata Mzee Ole sasa hivi Mungu akimjalia afya njema,
nakupata uhuru ulionao, nina uhakika hatakosa chakufanya.” Grace akacheka
kidogo, akafikiria.
“Nahisi
ni kwa kuwa nimekuwa nikiishi kwa muda mrefu kwa ajili ya mtu au watu. Kuambiwa
kitu cha kufanya kila wakati. Au jinsi gani yakuvaa, nani uzungumze naye. Wapi
pakwenda. Au wapi uwe na kwa wakati gani. Mpaka nimepoteza identity yangu. Unakuwa umefunikwa kwa muda mrefu, kiasi ya
kwamba ukiachiwa huru, unakuwa hujijui tena wewe ni nani, wala hujui tena
ufanye nini juu ya maisha yako.” Grace akaongea kwa upole na majonzi. “Mbona
nakuelewa kile unachozungumza! Nilikwambia nilirudi hapa nchini nikiwa kwenye
hali hiyo. Nimechanganyikiwa haswa. Mimi nilifika mahali mpaka nilishapoteza
hata kujijua mimi niwa jinsia gani.” Grace akamwangalia.
“Kweli
Grace. Acha niwe mkeweli kwako. Niliishi maisha mabaya sana, yamateso
yakupindukia huko jela. Na hivi nilipewa sura kama mtoto wa kike, nilijuta. Ilikuwa
mbaya.” “Pole sana Man. Pole.” Grace alielewa anachozungumzia.
“Matibabu ya kiroho na kimwili
ndiyo yamenifikisha leo hapa na wewe. Na kuweza kuibua hisia ambazo maisha
yalikusudia kuyaficha. Ni Mungu mwenyewe Grace, ndiye atendaye sasa hivi kazi
ndani yangu. Wala si kwa uwezo. Mpaka mimi mwenyewe nimeshangaa. Sikujua kama
ningejihisi hivi, wala ningeweza hata kuwa hapa na wewe na nikaweza kuzungumza
hivi.” Grace akainama.
“Tafadhali
usinielewe vibaya. Sina nia mbaya. Ila naeleza kule nilikotoka na hapa nilipo.
Ni muujiza. Kwa hiyo ninachotaka kukwambia Grace, jipe muda. Kila kitu kitakuwa
sawa. Mungu atakusaidia tu. Japokuwa sijui ni nini unapitia, ila sidhani kama
ni mbaya kama kule nilikopitishwa mimi. Sasa kama mimi Mungu alinitendea,
hatashindwa kwako. Jipe muda tu. Na pole.” Grace akatoa tabasamu na kuvuta
pumzi kwa nguvu na kuzishusha zote kwa pamoja. Akishiria kupata aghueni. “Asante
Man. Nashukuru.” Wakatulia.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Haikuchukua
muda mrefu kurudi hapo hotelini. Walifika, mtu akaja kuchukua gari ya Man. Na
yeye alivaa sare kama za vijana waliokuwa wakihudumia ndani. Ndipo Grace akajua
pale pia kuna huduma ya ‘Valet’.
Walipokuwa wakiingia tu mlangoni, mlinzi akamwambia Man, anatafutwa sana. “Mbona
unanitisha tena?” “Wewe ingia ndani ukajionee mwenyewe.” Wakaingia. Walikuta
watoto wawili wakiume wakikimbia humo ndani kama wamechanganyikiwa. Man
akasimama nakuanza kucheka. Walipanda hapa na kushuka. Man akaanza na yeye
kuwakimbiza mpaka akamkamata mtoto wa kwanza, akaendelea kukimbia na yule
aliyemkamata mara ya kwanza mpaka akafanikiwa kumkamata na wa pili. “Njooni
kwanza mnisalimie.” Man alikuwa akihema huku amewashikilia kwa nguvu. “Mimi
nahisi baba yao kawapa pombe hawa watoto. Sio bure.” Mrembo mmoja aliongea huku
akisimama, kumsogelea Man.
“Hivi
nyinyi watoto wa Malisa, mnajua sasa hivi ni saa ngapi?” “Shikamoo anko.” Wote
wakasalimia kwa pamoja. “Baba yenu yuko wapi?” Man akawauliza. “Yule pale
kalala na gazeti usoni.” Man akacheka. “Sasa mbona hamjaenda kupumzika?” Man
akauliza huku akimwangalia mama yao. “Hamna chumba. Na tumeambiwa kwa mara ya
kwanza anko ametoka na mdada mrembo. Nikaona hata nisipige simu kukusumbua.
Tuwe tu wapole.” Man akacheka. Grace alisikia na yeye akacheka. Man akamgeukia.
“Grace! Huyu ni mdogo wangu
anayenifuatia. Anaitwa Malisa. Hawa ni watoto wake.” “Na yule
anayekoroma pale, ni mume wangu.” Grace akacheka huku akimgeukia mume wa
Malisa. Grace akampa mkono Malisa. Alionekana mtundu kama kaka yake. “Nimefurahi
kukufahamu Malisa.” “Hata mimi Grace.” Malisa akajibu.
“Mmekula
sasa?” Man akauliza. “Yusuf katutenda vyema. Hapa tupo sawa. Tunachotaka ni
sehemu ya kulala tu. Niingize hii kelele kwenye hata chumba kimoja tu, hapa
patulie. Wageni wote wanatushangaa sisi!” “Sasa mbona mmekuja usiku?” “Shuguli
zisizoisha za yule bwana!” Malisa akamnyoshea kidole mumewe. “Si umeona
alivyochoka? Tangia asubuhi yupo ofisini. Hata kanisani hakwenda. Nimeenda mimi
na chekechea yangu tu.” “Basi nisubirini.” Man akasogea mapokezi akiwa ameshika
wale watoto. Grace akawafuata.
Akaulizia
vyumba, kweli akaambiwa vimeisha. Kimebaki kimoja tu. Sio suit. Na kitanda
chake sio kikubwa sana. “Naweza kuwapisha chumbani kwangu.” Grace aliongea kwa
upole. Man akamgeukia kwa kumshangaa. “Unasema!?” Grace akacheka. “Naweza
kubadilishana nao chumba. Mimi nikahamia kwenye hicho chumba kidogo, wao
wakachukua kile changu. Ni kikubwa sana. Nina uhakika watatoshea na watoto kwa
usiku huu.” “Una uhakika Grace!?” Man hakuamini. “Kabisa. Kwanza unakumbuka
kuwa kesho nitaondoka? Kwa hiyo ni usiku wa leo tu. Hamna shida.” “Mteja ni
mfalme.” Man akasisitiza. “Ufamle wangu haubadiliki kwa kuhama chumba bwana!
Wewe wahamishie pale kwangu.” “Kwa kweli wala sitajivunga. Naona hiyo ndio
suluhisho pekee.” Malisa akaongeza, Grace akacheka kidogo.
“Nipeni
funguo ya hicho chumba kingine, nikahamishe vitu vyangu.” Grace alizungumza na
muhudumu. “Basi tangulia wakati natafuta mtu wa kukusaidia kuhama.” Grace
akataka kuondoka. “Grace!” Man na Malisa wakaita kwa pamoja. Grace akageuka
akawa hajui amwangalie nani. “Asante.” Man akashukuru. “Mimi nilitaka kusema
wewe ni mrembo. Mzuri kila kitu. Mpaka sauti. Kuanzia kesho naanza kuongea kama
wewe.” Malisa alimfanya Grace na Man, wacheke sana. “Na asante yakutupisha chumba.”
Malisa akaongeza. “Asante na asante kushukuru.” Grace akaondoka taratibu
akielekea ilipo lifti.
“Naona
Man mambo umeyaanzisha pazuri! Nishampiga picha zakutosha, kesho namrushia mama
Ole, kumtoa wasiwasi.” Grace alimsikia Malisa akiongea na kaka yake. “Acha
umbea Mali. Futa bwana.” “Kwa hiyo unasikia raha hivi mama anavyohangaika na
wewe?” “Sasa mimi nimekwambia kama huyu ni mtu wangu? Acha bwana. Futa hizo
picha.” Man aliendelea kusisitiza, Grace akiwasikiliza hapo nje ya lifti “Mimi
sijasema ni mtu wako. Ila tu nitamwambia kuwa umetoka na mwanamke mrembo.”
“Acha bwana Mali!” Grace akasikia kama na wao wanakimbizana pale pale karibu ya
mapokezi. Malisa akaanza kupiga kelele akiashiria anakaribia kutaka kukamatwa. “Ujue
wote tunaonekana watoto kama hao wanao? Nipe simu yako nifute.” “Sitaki.
Kwanza nishatuma wakati nakimbia hapa.” “Ujue unaakili za kitoto sana Malisa?”
Akamsikia Malisa akicheka. Grace akaingia kwenye lifti mara baada ya mlango
kufunguka, akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~
Ni
kweli Malisa alikuwa mweupe kama alivyosimuliwa na kaka yake. Mcheshi kama kaka
yake, mtundu kama wanae. Grace alipanda huku akicheka yeye mwenyewe.
Alifurahishwa na muda alioupata na Man. Hakujua aongelee nini kwa wakati ule.
Lakini gafla akajihisi amepata umuhimu. Baada ya muda wa miezi sita na siku
kadhaa akiwa anamlilia Danny, huku Danny akimuonyesha si kitu. Anafaidi penzi
la Sara chumba cha pili. Akisifia maumbile ya Sara hata mbele yake. Kuwa ni
mweupe, mwepesi kubeba popote. Hali makapi usiku kucha. Sasa hivi anapata penzi
laini. Gafla anampata Man anayesema anapata utulivu akiwa naye! Malisa
amemsifia kila kitu! Siku hiyo ikawa inaisha vizuri kwa Grace. Alijawa furaha.
Akapata mwenzie aliyepita kwenye magumu ya ndoa. Man anaonekana kuvutiwa na
rangi yake pia. Grace akafarijika sana. “Kumbe
weusi wangu unalipa!” Grace akawaza.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akaja mtu wa kumuhamishia mizigo yake, na mwingine wakusafisha tena kile chumba anachotoka Grace. Akapelekwa kwenye chumba kingine. Grace akashangaa. Kwani bado kilikuwa chumba kizuri tu. Akapanga vitu vyake. Akasahau hata mambo ya chakula. Akaingia kuoga, akavaa nguo zake za kulalia, akapanda kitandani tayari kwa kulala, amalize siku. Hata hivyo alijua wakati huo Man atakuwa busy na wageni wake. Hawezi tena kukumbuka chakula. Akajiweka sawa pale kitandani ili alale.
Mapya Na Mageni.
Mara
akasikia hodi mlangoni. Akatoka kitandani akaelekea mlangoni. “Nani?” Akauliza.
“Man!” Grace akababaika kidogo. “Naomba usubiri kidogo.” Akakimbia kujifunika
shuka. Akatoa nywele kwenye kofia nakujitengeneza kidogo, ndipo akafungua. “Samahani
nilikuwa nimeshapanda kitandani.” “Ulisahau kula?” Man akauliza huku akiingiza
kigari kilichokuwa kimebeba chakula. “Nilijua muda umekwenda, halafu umepata
wageni. Nikajua itakuwa tena ngumu kukumbuka.” “Gafla nikusahau! Hapana bwana.
Kwanza Malisa na familia yake sio wageni hapa. Walichokosa ni chumba tu. Lakini
kama wangepata chumba, usingewaona leo, mpaka kesho. Na Malisa hapendi kulala
sehemu nyingine ila hapa. Kwa kuwa amewazoea karibia watu wote hapa. Akitaka
kutoka na mumewe au kwenda kwenye shuguli zake, anajua ana watu wakuwaachia
wale wanae. Ni watundu kupitiliza. Kila anapokwenda lazima awe nao.” Grace
akacheka.
“Karibu
ukae. Lakini kitandani kwa kuwa hapa hamna makochi.” “Daah! Samahani bwana.”
“Wala usijali. Mimi nipo sawa tu. Vyumba kama vile vipo kila mahali. Naweza
kulalia popote, lakini wakati mtulivu ndio ninahitaji.” Man akaenda kukaa. “Sasa
unapata huo wakati mtulivu?” Grace akacheka. “Mpaka sasa, siwezi kulalamika.
Tumekuwa na wakati mzuri.” “Wakusikiliza matatizo yangu tu?” Man akauliza.
“Sio
kwa upande huo.” “Upi sasa?” “Nimefurahi umenitoa. Umeniamini. Sijui niseme
tumetengeneza urafiki? Au ni mapema sana?” Man akacheka bila kujibu huku
akimwangalia. “Haya, umenifariji na hata sasa hivi inakwenda saa 7 ya usiku,
bado umenikumbuka, ukaja hapa. Nimefurahi.” Man akacheka tena. “Kwa hiyo
najisikia vizuri.” “Karibu. Lakini kabla ya kukiona chakula. Nataka ubashiri
kwa kukionja bila kukiona. Na ili usichungulie, nakufunga kitambaa machoni.
Kila kijiko kitakachoingia mdomoni kwako, uniambie nimekulisha nini.” Grace
akacheka sana.
“Mbona
kama nimeshajua?” “Usidanganyike na harufu. Sio vyote vinanukia samaki ni samaki.”
Grace akaendelea kucheka. “Wewe si umesema unapenda kula? Basi hautakuwa
mtihani mgumu.” “Sawa.” Man akamfunga moja ya napkin zilizokuwa zimeletwa na
chakula. Wakakaa pale pale kitandani wamegeukiana. Grace amefungwa macho,
wanacheka sana.
Man
akamlisha mara ya kwanza. “Viazi vilivyopondwa.” Grace akasema. “Huwa mtihani
unaanza na maswali rahisi, usibweteke.” Grace akacheka. “Ila nimeonja na supu
ya ya.. Hebu nipe supu peke yake.” Man akacheka. Akamuwekea supu mdomoni. “Mbona
nilipata kama harufu ya samaki lakini mchuzi sio wasamaki?” “Unapata ladha
gani?” Man akamuuliza. “Kamaaaa..” Grace akabaki akifikiria. “Ni kama ladha ya
mboga za majani, sijui!” Man akacheka. “Ngoja nikulishe tena.” “Sasa hivi
umenipa samaki wa kuchoma.” Akawa amepatia. “Na sasa hivi?” Man akampa tena.
Grace akatafuna huku akisikilizia ladha. “Ile ile supu. Mimi nasema ni ya mboga
mboga.” “Mboga gani?” “Mchanganyiko.”
Man akacheka sana. “Acha ujanja Grace.” “Nimepatia bwana!” “Hapana. Lazima
useme ni mboga gani.” Wakaendelea kucheka huku akimlisha Grace mpaka mwisho.
“Umeshiba?”
Man akamuuliza wakati anamfuta mdomo baada ya kumfungua. “Nimeshiba sana. Umenilisha
kama mtoto! Ninauhakika hujashiba.” “Unafikiri kwa nini nilikufunga macho?”
Grace akacheka sana. “Hiyo ilikuwa janja ya kula zaidi yako. Wewe nakupa
kimoja, mimi viwili.” Grace akaendelea kucheka. “Nimefurahia sana Man. Asante
kuwa na mimi hapa.” “Umeangalia saa lakini? Unaweza kujuta.” Grace akacheka.
“Sijali.
Ila ujue nilihitaji kucheka hivi. Nimelia kwa zaidi ya miezi sita
mfululizo bila faraja yeyote. Nilikuwa nimechoka sana, karibia kuchanganyikiwa,
ndio maana nikaona heri nitoke pale. Sikujua kama nitakuja kucheka tena hivi.”
“Pole. Naamini utakuja kupata amani yakuja kunisimulia siku moja. Ili na mimi
nijue kulikoni. Lakini naomba kesho tuongozane huko mbugani.” “Ningependa Man.
Lakini nitashindwa kelele. Nimetoka kwenye kelele nyingi, natafuta utulivu.
Naomba nyinyi tangulieni tu. Naweza kukukuta huko, au nikirudi nitakutafuta ili
nikuage kabla sijaondoka.” “Umeshajua ukitoka hapa unakwenda wapi?” Grace
akafikiria kidogo.
“Sijui
Man. Lakini sio nyumbani kwangu. Najiona bado sipo tayari kukabiliana na
yanayoendelea. Kwa kifupi mume wangu anaishi na mwanamke mwingine mle mle
ndani. Mtoto mdogo tu. Yaani kasichana walichokutana nacho humo humo ndani
akiwa ameleta watoto wa mdogo wangu au kaka yangu, kuja kututembelea. Sasa heri
ingekuwa wanaishi humo ndani kwa heshima. Lakini ni fujo kunifanyia makusudi.”
“Grace! Kwa heshima ndio inakuaje? Kuishi na mwanamke mwingine ndani ya nyumba
moja na mkeo wa ndoa! Ndio mnaishije kwa heshima? Labda leo unifundishe.” Man
hakuwa ameelewa.
“Hata
sijui Man! Mimi sielewi. Lakini ni msichana mwenye akili za kitoto. Kelele za
kitoto kama vile visichana nilivyokuona navyo jana. Kelele. Bado hawajajua
shida za maisha, kwa hiyo wanachojua ni kutumia tu na kushindana. Mimi sio
mtoto Man. Nimehangaika na Danny kupita nitakavyo kwambia. Mungu wangu anajua.” Grace akaanza kulia.
“Nimehangaika sana na Danny. Hakuna jinsi nikakueleza ukaelewa. Nimehangaika
naye tukiwa hatuna kitu. Anaishi kwetu. Nikikwambia kwetu sio nyumba. Ni chumba
kimoja. Tunaishi humo na mama yetu, na kaka yangu. Lakini tukavumiliana mpaka
leo analipwa kwa dola, ndio ananigeuka! Ananitukana kama hanifahamu! Anamsifia
huyu binti kana kwamba angepewa nafasi yangu yule binti, angeweza kusimama naye
wakati ule, wakati mimi najua Sara yupo naye sasa hivi sababu ya pesa tu.
Ananidhalilisha mbele yake, na mbele ya wafanyakazi.” Grace aliendelea kulia huku akiongea taratibu, kwa
upole.
“Gafla vile vitu alivyokuwa akivipenda na kunigombania mbele ya watu,
vimekuwa kero kwake! Danny sasa hivi anasema hajui hata alinipendea nini na
weusi huu. Mnene. Yaani kasoro ambazo sina jinsi yakujibadilisha. Nimeomba,
Man! Huwezi kuelewa. Nimefunga na kuomba bila kuchoka nikimsihi Mungu
anirehemu. Anisaidie abadili ile hali. Au basi anisaidie niweze kumudu kubaki
pale kwa ajili ya watoto wetu, lakini nimeshindwa Man. Watoto amewageuza, sijui
amefanyaje! Hawana hata mpango na mimi.”
Grace akamsimulia Man kuanzia mwanzo wake na Danny, mpaka alipo pale.
Man
aliumia sana. “Pole sana Grace.” Akaenda kujiegemeza kwenye kitanda. Akamvuta
mpaka karibu yake. Grace akapandisha miguu yake yote miwili. Akamfunika vizuri.
Akamkumbatia huku akimsugua mgongoni kama kumtuliza. Akiwa amelala pale kifuani
akilia. Akajisikia kutulia. Akazungusha mikono kifuani kwake. Wakabaki wamelala
huku wamekumbatiana. Man aliendelea kumbusu kichwani huku akichezea nywele zake.
“Nasikia
usingizi, Man.” Grace alinyanyua uso akakuta akimwangalia. Akambusu kwenye
kipanda uso. “Asante na samahani. Nilikuwa nina uchungu ambao sikujua kama
nikizungumza hapa naweza kupitiliza. Samahani sana. Sikukusudia ku..” Man akacheka na kumbusu tena.
“It’s okay. Unataka nikuache ulale?” Man akauliza swali la mtego. Grace
akababaika sana. “Najua na wewe umechoka. Nenda kapumzike tu.” “Hata hapa
nimepumzika.” “Unauhakika sikuumizi? Au nijilaze kwenye mto ili ulale hapo
vizuri?” “Hapana. Nipo sawa tu. Wewe lala.” Grace akambusu pale kifuani.
Akajiweka sawa. Man alimchezea nywele taratibu kama anayembembeleza, mpaka
akalala kama Geb na mwanae Magesa wakichezewa nywele na Nanaa.
Asubuhi Ya Kwanza Kuamka Mikononi
Mwa Man!
Waliamshwa
na simu ya mezani. Man akanyosha mkono na kuivuta. “Gari ipo tayari. Watu wote wamepanda. Unasubiriwa wewe tu.” Man akabaki akifikiria. Ndio alikuwa anatoka
usingizini. Bado amemkumbatia Grace. Hata hakujua kama palikucha saa ngapi! “Niwaambie wasubirie kama dakika ngapi?”
Sauti ya kike upande wa pili ilisikika ikiuliza. Grace akajua kwa hiyo watu
wote wamejua kama Man amelala hapo chumbani kwake. “Waambie watangulie. Nitawafuata baadaye. Nitampa maagizo yote,
Sedekia. Atawapokea wakifika kule.” “Sawa. Nitamwambia kiongozi wao.” “Asante.” Man akakata simu.
Grace
akajinyanyua na kuondoka pale. “Samahani nimekuchelewesha kuamka.” Man akatoa
tabasamu. Bado alikuwa amevaa nguo zake vile vile. Grace akaelekea chooni
kusafisha kinywa. Tayari ilikuwa imeshafika saa 5 asubuhi. “Hata hivyo
tulichelewa kulala.” Akamsikia Man akijibu. Grace akatoka akiwa ameshajisafisha
na uso. “Jiandae tukapate kifungua kinywa.” Grace akabaki kimya kama anayefikiria.
“Grace?” “Sidhani kama ni sawa Man.” “Nini tena!?” “Kila mtu anajua sasa hivi
umelala hapa. Un..” “Unahofia nakuharibia reputation
yako? Nakuharibia sifa njema na hutaki watu wajue kama tuko hapa pamoja?”
Tayari Man alishaonekana kukwazika.
“Hapana
Man. Nazungumzia kwa ajili yako wewe mwenyewe.” “Mbona kama na wewe
unanitafutia sababu zisizoisha Grace?” “Hapana Man. Ni kwa ajili yako
mwenyewe.” “Leo ni ipi tena? Maana jana ulikuwa ukiongelea swala kuwa
mimi ni mdogo sana kwako. Wewe ni mama mtu mzima. Umenisikiliza muda mrefu
sana. Ukagundua mimi sio mtoto kama ulivyodhani. Nimeshaishi maisha zaidi yako.
Sasa sasa hivi ni nini tena?” Grace akanyamaza kama anayefikiria.
“Au
umeamka asubuhi hii umepata muda wakufikiria ukaona unikimbie kwa ukweli
mzito nilio kwambia jana?” “Man!” Grace akastuka. “Au labda niliharakisha sana
kuwa muwazi kwako? Nilitakiwa nianze kwa kukudanganya?” Man alikua akizungumza
taratibu tu. “Hapana Man! Nia yangu ilikuwa nzuri. Sijali maisha yako ya nyuma.
Kwanza nimefurahi sana umeweza kuwa muwazi kwangu.” “Sasa tatizo ni lipi?” Man
akauliza.
“Wadhifa
ulio nao hapa! Halafu watu wanakuheshimu sana. Hujawahi kuharibu hata mara
moja. Halafu eti leo ujulikane upo huku chumbani na mimi! Watu hawajui kile
kinachoendelea kati yetu. Lakini kwa wewe kuwepo humu ndani na mimi, tena mimi
najulikana kama mke wa mtu. Mama! Sio msichana. Wapo wasichana najua
wanakuwinda mchana na usiku. Lazima watatafuta kunijua ili kukusambazia wewe
sifa mbaya.” “Unamaanisha wewe?” Man akauliza.
“Man!
Mimi sina chakupoteza tena. Grace aliyehapa mbele yako ni rejected. Used. Sikrepa nisie na thamani.”
Grace akaanza kulia. “Kama
nikudhalilishwa, mimi nimeshadhalilika sana. Mume wangu ni muongeaji sana.
Hafanyi uovu wake kwa kujificha. Anafanya wazi ili kuniumiza mimi, Geb na mama.
Simu yangu ilikuwa imejaa pole kutoka kwa marafiki, kwa kutendwa na Danny. Ndio
maana nimeicha. Picha za Danny na Sara wakiwa na watoto wangu, zilikuwa
zikisambwaza kwa kuchekwa. Wengine walinitumia kwa kujidai wamekosea namba.
Kumbe wananicheka tu, huku wakiniambia Danny amechoshwa na weusi wangu au
amekinahiwa na umbile langu. Sina chakupoteza Man. Sina sifa nzuri yakutunza.
Ndio maana nipo hapa ili angalau kunusuru nafsi yangu. Sitaki nije kukuharibia
na wewe wakati nitakuja kuondoka hapa hivi karibuni.” Man akamkumbatia tena.
“Unacho
chakupoteza Grace. Ni heri upoteze kila kitu, lakini sio nafsi yako mwenyewe.
Acha watu wakutamke vibaya, lakini sio wewe mwenyewe. Wewe sio rejected wala
used. Labda kwenye ulimwengu wao waliozoea kutumia watu vibaya. Lakini sio
katika ulimwengu nilioapa kuja kuishi mimi, Grace. Nilitumiwa kwa kadiri ya
watu walivyopenda. Na nikaapa sitafanya hivyo kwa mwanadamu mwingine yeyote.
Hata awe duni vipi. Ndio maana naheshimu kila mtu kwa heshima iliyo sawa.
Usitegemee nikampa mheshimiwa fulani heshima zaidi ya mfagizi wangu wa hapa
hotelini ambaye ananisaidia kwa maisha yangu ya kila siku! Hapana. Wote
nitawaheshimu kwa heshima ileile. Naomba kuwa huru na mimi. Nakuahidi
sitakutumia kwa faida zangu binafsi. Chochote utakachoona kitakuharibia wewe,
niambie nini chakufanya, nitafanya.” “Na wewe?” Grace akauliza huku akifuta
machozi, mikononi kwa Man.
“Mimi sina chakutunza wala kupoteza, kwa
kuwa sina. Wala sijawahi kumdanganya mtoto wa mtu hapa Tanzania. Kwa hiyo mimi
nipo huru kuonekana na wewe muda na mahali popote. Hamna anayenidai au
atakayenilaumu. Maneno ya uzushi nilishazoea. Huwa wanadamu hawabadiliki. Hata
umpeleke wapi? Yuko hivyo hivyo. Unakumbuka nilikwambia waliwapigia simu watu
wa uhamiaji kuwaambia nafanya kazi bila kibali?” Grace akatingisha kichwa
kukubali.
“Hawakuwa
wazungu walionishitaki Grace. Ni watanzania wenzangu. Kwa hiyo huwa wananisema
tu. Tokea enzi hizo mpaka hivi leo. Kama sio niko na wewe basi watasema mimi ni
shoga. Wakajaribu mpaka kuuliza vijana wanao nifanyia kazi kama nilishawahi
kuwatongoza. Tena wakitaka wanitege, kwa ahadi za pesa nyingi tu. Lakini
waliokuwa waaminifu kwangu walirudi kuniambia.
Waliopenda pesa wakapokea hizo
pesa, nakubaki wakinitega bila
mafanikio. Kwa hiyo usiogope kuwa na mimi. Unanielewa?” Grace akaridhika,
lakini akabaki na swali moja.
“Kwa
hiyo wewe huna shida kujulikana upo na mtu kama mimi?” “Kama wewe ambaye
ukoje?” “Ni mama mimi, Man! Sio binti. Sasa leo uje uonekana unazurula na mama
mwenye watoto watatu!?” “Unakumbuka nilikwambia na mimi nilioa na nilipata
mtoto mmoja?” Kimya. “Nilioa mwanamke ambaye hakuwahi kuwa na watoto, lakini
sikuwahi kulala usingizi kama niliolala jana usiku.” Grace akacheka kwa aibu.
Man alilala na suruali yake lakini alisema alilala vizuri.
“Na
wewe sio mwanamke wa kwanza kuja hapa au kukutana na mimi. Nimekutana na wengi
na nimezungukwa na wengi. Lakini mimi ndiye ninayejua nini nataka, na ninapata
wapi.” Man akasisitiza. “Nimeridhika.” “Basi jiandae tukapate kifungua kinywa,
tuanze safari ya kwenda mbugani. Tutakuwa mimi, wewe na dereva tu.” “Okay. Kwa
hiyo nitakukuta sehemu yakulia chakula?” “Nitakusubiria pale chini.” Grace
alijawa furaha, akambusu shavuni na kurudi bafuni.
~~~~~~~~~~~~~~~
Alimkuta
Man akiongea na simu nje ya lifti. Akamshika mkono kumuongoza sehemu ya kula
huku akizungumza na simu. Lakini akamgeukia Grace. “Umependeza sana.” “Asante.”
Grace akajibu kwa sauti ya chini. “Huyo ni
Grace?” Akasikia sauti ya mwanamke inauliza kwenye simu. “Ndiyo mama jamani! Kwani huwezi kunyamaza!? Mzee Ole amekuharibu wewe.
Hukuwa hivyo.” Akamsikia akicheka. “Basi niwaache. Muwe na wakati mzuri.” Wakaagana. Man akarudisha simu
mfukoni.
“Man!
Umeshamwambia mama yako!?” “Malisa huyo! Yaani imenibidi kutoa maelezo
yakutosha ili kusafisha hali ya hewa. Ametuma picha zako kwenye kundi la
familia. Nimeamka nimekuta kila mtu ameongea lake. Hata wale ambao huwa hawachangii
kitu kwenye hilo kundi, wameandika, wanakuulizia. Ndio nikaona nianze kujieleza
kwa mama kwanza kabla hajamwambia Mzee, kumbe na hapo nimechelewa.” “Uwii! Sasa
umewaambia nini?” Man akacheka.
“Mbona
unawasiwasi sasa?” “Niambie tu Man. Sitaki wakuelewe vibaya. Au wakafikiria
kitu ambacho hakipo.” “Kaa chini tule kwanza.” Man alikuwa akicheka. “Acha
kupaniki Grace. Nimewaelewesha.” “Nini?” Mara Malisa akasogea. “Naomba uondoke,
Mali. Nenda kakae na wanao meza nyingine.” “Sijakufuata wewe hapa. Mimi
nimemfuata Grace.” Malisa akavuta kiti. “Umekuwa gumza kwenye familia ya Ole, Grace.
Baba ameomba upelekwe nyumbani.” “Hivi wewe vipi Mali jamani!? Unamuogopesha
Grace bwana! Ondoka.” “Usiogope. Mimi ndio kipenzi cha Mzee Ole. Nimemwambia
kama Man hatakupeleka, mimi mwenyewe nitakupeleka wewe na wanao, ili baba
akakuone.” Grace alizidi kuingiwa hofu.
“Mpaka
watoto wangu!” Grace akashangaa sana. “Man amesema una watoto watatu. Au
ametudanganya?” Grace akamgeukia Man
huku anatetemeka. Man akamuona. “Naomba ondoka Mali. Kweli tena. Sijui baba
huwa anakupendea nini! Hukui, mmbea, huwezi kutunza jambo moyoni! Wewe mtu
gani?” “Mimi nitacheza na watoto wa Aunt Grace.” “Ona wanao wako kama wewe!
Nendeni bwana.” Malisa akawa anacheka.
“Kama
unataka niondoke niwaache, nipige picha mimi na
Grace. Tena tukiwa tumesimama.”
“Hapana Malisa.” “Haya watoto wa Ole, vuteni vitu tuanze kula tena.” Malisa aliwaambia wanae. “Acha fujo Malisa.”
“Hata mimi nimempenda Grace. Nataka muda naye.” “Si uende kwa mumeo?” “Hayupo,
ana kikao mjini. Kaniachia chekechea yake.” Man akabaki akimtizama Malisa. “Eti Grace, hutaki kupiga picha na mimi?” “Na mimi
mama.” “Hata mimi nataka kupigwa picha.”
Wale watoto wote wawili wakataka picha na Grace. “Huko ndiko kuharibiana
picha sasa. Mtanijazia picha bwana! Nitawapiga ya kwenu na anko. Tufanye girls
picha yao, na ‘real Men’ picha yao.” “Yay….” Wale watoto wakafurahia.
“Namuhurumia
sana mumeo. Kapata hasara ya mke na watoto pia.” Malisa alikuwa akicheka sana. “Bwana
lakini Grace wewe ni mzuri bwana! Mpaka raha kukuangalia. Halafu hivi Man
alikwambia huwa anapenda wasichana weusi?” “Grace! Naomba upige nae picha
aondoke na wanae. Tafadhali. Hatutakaa tukala hapa.” Grace akasimama huku akicheka.
“Niguse basi hata kidogo! Watu wajue mimi ndio nimekufahamu wa kwanza kabla ya
wao. Halafu wajue pia tuna mahusiano kidogo.” Malisa alimfanya Grace acheke
mpaka ainame.
“Mzee
Ole anahasara. Hapo!” “Nataka sifa mjini. Niwekee mkono begani.” Grace
akasimama, akamuwekea Malisa mkono begani. “Sasa hayo ndiyo mambo. Anko fanya
vitu vyako.” Man akawapiga picha. “Mbona nashukuru! Nimepata nyingine yakutuma.
Ujio wangu umeleta maana zaidi.” “Naomba uondoke Melisa. Uliniahidi utaondoka baada ya picha. Nenda.”
“Mbona sisi hatujapiga picha ya Men, mama!?” “Hamsahau!? Haya kila mmoja ambusu
anko. Moja, Mbili, tatu… Haya twendeni mkaogelee wakati mama anatuma ujumbe.”
“Angalia watoto Mali.” “Hamna mzamaji hapo. Wewe usiwe na wasiwasi.” Malisa
akajibu huku macho kwenye simu.
“Nyinyi
hamuendi mbugani?” Grace akauliza. “Na hawa!?” Malisa akauliza akiwaangalia
wanae. “Ndiyo. Na watoto.” Grace akajibu na cheko. “Si thubutu. Mzee Ole
alishatupeleka wakati watoto, naona inatosha. Hawa viumbe ukiwapeleka huko ndio
mwanzo wakunirudisha tena leba.” Grace hakuwa ameelewa. “Nimefunga biashara ya
kuzaa Grace. Sitaki na wala sina mpango wakuzaa tena. Sasa hawa ukiwapeleka
kule, ujue umepelekea simba kitoweo.” Grace akacheka sana. “Kwanza hawajui
kutembea. Wanaruka kila mahali. Sasa wakiliwa hata mmoja, itabidi kuzaa tena
mwingine, kufidia idadi. Halafu utashangaa hata ukirudia, unapata sampuli hii
hii. Watoto wasioweza kukaa chini. Nimefunga huo mkataba. Acha tu wakue.
Wakishaoa, nikihakikisha wapo chini ya uangalizi wa wake zao, mimi ndio
nitaenda huko mbugani na Ole wangu. Sio sasa hivi. Nisimpe shetani nafasi.”
Malisa akamaliza.
Akarudisha
macho kwenye simu yake. “Sasa Grace wewe kuwa na wakati mzuri huko mbugani.
Ngoja mimi nipeleke Masai wangu kwenye maji.” “Asante Malisa.” “Karibu.
Nitatafuta namba yako ya simu, tupange mipango yakwenda kumtembelea Mzee Ole.
Sio Ole wangu! Ole baba.” Malisa akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Man!
Ni nini?” “Nisikilize Grace. Asubuhi Malisa na wanae walinitafuta mpaka
chumbani kwangu. Malisa alitaka kuniachia watoto, aende na mumewe. Akanikosa.
Akaulizia mapokezi, wakamwambia sijaonekana tokea jana usiku waliponiona napita
na chakula kuelekea chumbani kwako. Moja kwa moja Malisa akajua nimelala
chumbani kwako. Acha aanze kubebea bango! Kama nilivyokwambia, niliamka
nikakuta tunazungumziwa kwenye kundi. Ikabidi kumpigia mama simu ili kumuweka sawa.
Mama akaanza kuniuliza wewe uliamkaje. Nikawambia asimsikilize Malisa.
Anakuza mambo.” Man akaendelea.
“Akaniambia
unaonekana ni msichana mzuri na umetulia. Kwa nini natafuta sababu? Ndio
ikabidi kumwambia ukweli juu yako. Kwamba tumekutana hata masaa 72, hayajaisha.
Bado upo kwenye ndoa takatifu na umezaa na huyo mwanaume watoto watatu. Na
usiku huo sio kwamba nililala na wewe kama Malisa anavyosema, nilipitiwa tu na
usingizi. Kumbe baba alikuwa akisikiliza. Akadakia akasema mimi ni masai.
Natembea na kisu kikali. Lazima nile nyama. Nisimwaibishe na nisirudie
tena kusema nililala na mwanamke, nikapitiwa na usingizi. Nikujidhalilisha.”
Grace akacheka mpaka akajifunika uso.
“Subiri
kwanza umsikie Mzee Ole. Naona amepona. Si kwa ushauri ule!” “Akasemaje tena?”
“Akasema nichangamke. Niache sababu za kitoto. Nisijilize kama mtoto wa kike. Nikazane
kuongeza mtoto wangu wa nne.” “Mungu wangu Man!” “Hivyo unavyomuona Malisa,
ndivyo baba yake alivyo. Na ni mrafiki mno. Halafu akasoma sana bila shida,
akaolewa na Mmasai mwenzie baba. Yaani kama ukoo mmoja. Basi nakwambia Malisa
ndio mfano wa kuigwa kwenye familia. Kana kazi nzuri na kasomi kweli! Usimuone
akijitoa akili kwako. Ana masekretari wawili hapo ofisini kwake.” Grace akabaki
akicheka nakufikiria.
“Malisa
amekuza haya mambo sana!” “Sana. Na hakuna jinsi nikaelezea watu wakanielewa
tena. Kila nikijibu swali hapo kwenye kundi la familia, na yeye anaongeza
maneno yake hapo chini. Nimeamua kuacha tu. Ametangaza tunaenda kupumzika mbuga
za wanyama. Nikakanusha. Nikawaambia kuwa, wewe ulikuwa na safari zako na mimi
naenda kikazi. Hamna anayetaka kunielewa. Kila mtu anashangilia. Nauliza
wanashangilia nini, wanasema wanashangilia safari yangu ya kikazi. Kama sio
uongo ni nini, wakati mimi kwenda mbugani ni kitu cha kawaida sana.”
Wakaendelea kuzungumza huku wakicheka.
~~~~~~~~~~~~~~~
Mambo
yameanza kwa Man & Grace. Ameamka mikononi mwake. Amejibiwa maswali yote yaliyokuwa yakimtia
wasiwasi kuonekana naye hadharani. Sasa yupo huru kuendelea kuonekana naye
popote.
v Upande wa kina Man, familia
inaonekana kumpokea vizuri sana bila shida. Yale mabaya aliyokuwa anamsema nayo
Danny, huku kwa wamasai, wanasifia. Gafla Grace aliyetua jijini Arusha akiwa na kilio
moyoni, amebadilika sio huyu. Grace ni Celebrity kwenye familia hiyo ya
‘Masai’, wasomi na walio endelea. Watoto watatu si tatizo kwao. Wanaelekea
mbugani.
Je,
aliyotabiri Geb yanatimia?
Usikose uhondo wa Mbugani?
Endelea Fuatilia yanayoendelea kujiri kwenye maisha ya Grace, Man, Nanaa &
Geb pamoja na mama yao.
Danny na Sara, Je?
0 Comments:
Post a Comment