“Umeniombea?”
Geb akacheka. “Sana tu.” “Asante.” Nanaa akajiweka kitandani. “Kwanza
nakushukuru kwa kuturuhusu tupikie hapa.” “Karibu. Ila hukuwa na sababu ya
kushukuru. Wote tunaishi hapa. Kuwa huru kufanya chochote unachotaka.” “Lakini
siwezi kuepuka ukweli kwamba wewe ndio unapamiliki Geb. Ni kwako.” “Kwetu.” Geb
akarekebisha, Nanaa akacheka. Geb akaweka kidole kwenye dimpozi zake.
Kweli
alimkumbusha Nanaa mbali sana. Tokea enzi wanaanza mapenzi, Geb alipenda
kufanya hivyo. Nanaa akainama kama anayefikiria. Geb akamvuta mkono. Nanaa
akatoa kicheko cha kinyonge. “Dada Fifi amekuja. Tunaanza kupika. Ila
tutajitahidi tusiwasumbue.” “Usiwe na wasiwasi. Unataka msaada wowote?”
“Hapana. Tutakuwa sawa tu. Japo nafikiria vitu tulivyonavyo na gari ya dada
Fifi! Nahisi itakuwa ndogo. Itabidi tufanye safari mbili au tatu. Nitaangalia.
Ila itabidi kuwahi kuondoka ili nihakikishe vitu vyote vinafika ukumbini kwa
wakati.” Nanaa akawa kama anayeweka mipango akifikiria kidogo.
“Ngoja
nikaanze kazi. Wewe pumzika tu. Najua mida ya kaka ndio hii. Akiamka nitampa tu
uji wake.” “Wewe hiyo kazi ya watoto niachie mimi leo. Nataka na Liv akimka,
niende nao ofisini kidogo. Lakini tutarudi mapema tu kabla hujaondoka. Au
niseme nikuombe usiondoke kabla sijarudi.” “Sawa. Nitakusubiri. Nikuletee kitu
chakula?” “Nitakula jioni. Asante.” Nanaa akajua na hiyo siku pia amefunga. Akamuhurumia. Akambusu shavuni, akasimama. “Asante Nanaa.”
Geb akashukuru. “Kwa nini!?” Nanaa akauliza. “Kunibusu. Nimefurahi sana.” Nanaa
akacheka kama asiyesadiki.
“Kweli.
Nimefurahi.” “Karibu. Basi ngoja nikaanze kazi. Wewe pumzika.” Akatoka asiamini
kama bado Geb anafurahia busu lake. Hasa baada ya kubakwa na isitoshe amebeba
mtoto wa Malii! Hapo napo akawa amemtumia ujumbe mwingine uliomfanya Nanaa
aanze kufikiria tofauti.
~~~~~~~~~~~~~~~
Liv
alivyoamka tu, Geb akamtayarisha na yeye baada ya kula, wakatoka nakumuacha
Nanaa akiendelea na mapishi. Akaanza kuchukia kujaza nyumba yote na harufu ya
maandazi, vitumbua, chapati, bajia na sambusa. “Inabidi siku nyingine tusipikie
hapa dada.” “Ila Nanaa, mimi naomba utafute watu watakao kusaidia. Hii biashara
mwenzio siiwezi. Nimeshaichukia.” “Dada Fifi!” “Kweli tena. Wewe uliniambia
nitafute pesa. Nitatafuta kwa njia nyingine sio kwa kupika vitumbua bwana! Wale
wapangaji nimewaambia wanipe kodi ya hata miezi sita. Wamekubali. Wameniambia
week ijayo watanipa. Mimi naanza kufuga kuku. Mtindo wa kuamka asubuhi na
kusambaza maandazi, huo sio wito wangu.” Nanaa akanyamaza akaendelea kupika.
Mwishowe
akaona ampigie simu Geb. “Vipi?” “Naomba unishauri. Nataka
kumuomba Jeri anitafutie mabinti wawili. Wazuri, wepesi kufundishika na
waaminifu. Dada Fifi kasema leo ndio mwisho. Anaanza kujiandaa na biashara yake
nyingine. Ni kama alikuwa akinisaidia tu. Halafu ngoja kwanza Geb.” Nanaa akamgeukia Fifi akiwa amekumbuka kitu.
“Wewe
dada Fifi, hao kuku unaanza kufuga wapi?” Nanaa akauliza. “Wakati najipanga,
naanza na vifaranga pale ulipopakimbia wewe.” “Dada Fifi wewe jamani!! Sasa
mizigo yangu utaweka wapi? Halafu nikirudi mimi nitalala wapi?” “Acha
kunidanganya Nanaa. Pale hutarudi tena. Labda huyo mwanangu. Naye nitaishi naye
pale kwangu. Mimi na yeye tutatoshea tu. Kwanza pale nilipo mimi sasa hivi ni
pakubwa tu. Chumba kizima na sebule! Kweli mimi na Jimmy wangu hapatatutosha?”
“Kweli dada Fifi unakichukua chumba changu!? Usifanye hivyo bwana!” Geb alikuwa
akiwasikiliza.
“Nakwambia
najua wewe sio mtu wakurudi. Wamekuganda hawa kina Magesa, huwezi kurudi pale.
Mimi nayajua mapenzi kwa…” “Kwa kupendwa.” Nanaa akarudia usemi anaoupenda
Fifi. Wote wakacheka. “Sasa je! Nayajua mapenzi kwa kupendwa Nanaa. Si kusimuliwa
wala kuyasoma mahali. Na pia nayajua sehemu mapenzi yalipo. Hata kama mtu
akijidai kushupaza shingo vipi! Penzi kama lipo lipo tu. Wewe hutarudi pale.
Labda mwanao, tena ukifa.” “Kwanza nimegairi kufa.” Fifi akacheka sana.
Mpaka akakaa.
“Umeona
dunia ilivyo tamu mdogo wangu? Sasa wewe jitangulize kaburini.” Nanaa na Fifi
wakawa wamejisahau. Wanaongea nakucheka huku Geb akiwasikiliza. “Lakini wewe
sio mtu mzuri dada Fifi bwana! Hutabiriki.” “Acha nitengeneze pesa mdogo wangu.
Tena niitengeneze kwa raha. Mimi nilishakwambia kupika sipendi. Halafu leo
uniamshe asubuhi kwa ajili ya kupika! Unanitesa bure! Wewe kusanya huku, mimi
kule. Tukizichanganya tutakuwa mbali. Au unasemaje?” “Ngoja niongee na Geb
wangu nione atanishauri nini.” Fifi akacheka sana.
“Yamekua
hayo!” “Kumbe. Wewe upo kama kinyonga bwana. Ngoja nimpigie Geb.” Nanaa
akachukua tena simu, akataka kupiga lakini akagundua bado Geb yupo hewani. “Geb!!” Akaita kwa kushituka. “Nipo.”
“Nilijua umekata!” “Uliniambia nisubiri mara moja, Nanaa.” Nanaa
akaacheka. “Samahani.” “Hamna shida. Niko na
Jeri hapa. Nitazungumza naye kama anaweza kukutafutia watu wa kukusaidia kazi.”
“Nitashukuru.” Wakaagana.
~~~~~~~~~~~~~~~
Ilipofika
saa 9 na nusu jioni, Nanaa na Fifi wakawa wamemaliza kupika kila kitu. Wakaamua
waoge ndipo waanze safari. Alipomaliza kuoga akiwa chumbani kwa watoto,
akampigia simu Geb. “Mmepotelea wapi wewe na wanao?”
“Njoo hapa sehemu tunayoegeshea magari.” “Nimemaliza kupika Geb. Nataka kuanza
kujaribu kupanga vitu kwenye gari ya dada Fifi nione kama tutahitaji kurudi au
inatosha ili nisicheleweshe chakula cha kwenye sherehe.” Nanaa alionyesha hataki kwenda.
“Sitakuchelewesha
mpenzi wangu. Njoo.” Kwa kuitwa mpenzi na Geb, akaona
ni heri aende tu. Akacheka. “Nakuja basi.” Akatoka. “Geb ananiita hapo nje. Twende tutoke na
baadhi ya vitu.” Wakatoka. Tumbo la Nanaa lilikuwa kubwa. Na maradhi aliyokuwa
nayo, nikweli alikuwa amechoka. Alijikaza kufanya hiyo kazi lakini wazi
alionekana amelemewa. Zaidi siku hiyo ambayo alisimama siku nzima akipika.
Walitoka
kuelekea sehemu ya kuegesha magari. Geb alipomuona tu amebeba vitu
akamkimbilia. “Nimekwambia usibebe vitu vizito Nanaa!” “Ningefanyaje?
Nitajipanga taratibu.” Geb
akampokea. “Nimerudi na Jeri na mabinti wawili ili wakusaidie. Nimeleta na hii
gari. Liangalie na wewe kama itakufaa utumie kubebea vitu vyako.” Nanaa alibaki
kama ameduaa. “Hivi umesikia chochote ulichoambiwa?” Fifi akamsukuma kidogo.
“Nahisi
nimeshituka. Sikutegemea kupata msaada wa namna hiyo. Nashukuru Geb.” “Angalia
kwanza kama itakufaa.” “Hata kama gari haitafaa, lakini kile kitendo cha
kunifikiria tu, ndio nakushukuru.” Jeri na wale wasichana wawili walikuwa
wamesimama upande wa pili, waliposikia Geb na Nanaa wakizungumza wakazunguka.
“Hee!
Wana mpaka eproni na kofia kama wapishi!” Fifi akafurahi sana. “Mbona tutaenda
kuweka heshima huko! Hata mimi nimefurahi.” Wakasogelea lile gari. Ubavuni
ilikuwa imeandikwa Magesa Co. Anuani chini yake. Akajua ni gari yake Geb.
“Naona hili kubwa. Halafu safi!” Nanaa akasifia. “Ndio kazi niliyokuwa nayo
leo, mama. Nimeisafisha vizuri sana. Hata mkuu ameikubali.” Jeri akajisifia. Kabla
hajamjibu Jeri wale mabinti wakamsogelea Nanaa. “Shikamoo.” Nanaa akacheka
nafsi mwake. Wale wasichana walionekana wakubwa kuliko yeye. “Wewe dada Fifi,
unasalimiwa!” Akamrushia mpira Fifi huku akijua wazi ni yeye. “Wala
hawanisalimii mimi.” “Ni wewe.” “Umejuaje? Mbona walikutizama wewe wakati
wakisalimia na si mimi?” “Wewe ungeitika tu dada! Wewe ndio mkubwa.” “Ukubwa wa
umri na pesa ni tofauti. Si uliniambia heshima haiombwi?” “Basi dada yangu.
Tuyafanye mafupi.” Wale wasichana walicheka tu. Kwa kuwa Geb alikuwepo, Jeri akajibaraguza,
akaondoka pale. Geb alitulia kimya.
Akamsogelea
Geb. “Nakushukuru mpenzi wangu. Asante.” Akajikuta ameongea neno ambalo hata
yeye hakutarajia. Akamshika mkono. “Mungu akubariki katika hili.” Geb
alitabasamu huku akimtizama. Alijua anatamani amkumbatie, lakini akamuona
anasita, akaona amuache tu. “Asante.” Akarudia tena. “Karibu. Nimefurahi kama
litawafaa. Sasa uwaelekeza hao wawili kitu chakufanya. Na Jeri naye atakuwepo.
Ataendesha hili gari, mpaka huko.” “Asante. Nakushukuru.” Bado alibaki
akishukuru kama anayetaka kutimiza kitu baada ya ile shukurani lakini anasita.
Akamsikia Fifi anazungumza kwa sauti ya chini. “Umeniita dada?” “Nilikuwa
najiambia tu mwenyewe.” Nanaa akacheka. Alimjua Fifi ni mtundu.
“Unajiambia
nini?” “Nilikuwa najiambia mpaka tuje tuondoke hapa, tufike huko, sherehe
itakuwa imeisha.” Nanaa akacheka. “Yaani wewe! Si nilikuwa nashukuru?” “Sawa!” Itika ile, ikabidi tu Nanaa acheke zaidi.
Akamuachia Geb mkono, akashukuru tena. “Asante.” Fifi akaanza kucheka.
“Naombeni
na mimi nipokelewe hii mizigo, jamani!” Fifi aliongea huku anamcheka Nanaa.
Jeri akarudi kwa haraka. Maana alisogea zaidi kama kumpa nafasi Geb na Nanaa.
Nanaa akaondoka na wale wasichana kurudi ndani. Akawaonyesha vitu vyote
alivyotayarisha. Nguvu ilimjaa kwa upya. Akawa amechangamka kama sio mjamzito
mwenye tatizo la moyo. Wakamsaidia kupanga vitu vyake ndani ya hiyo gari. Jeri
na wale wasichana wakaondoka kutangulia ukumbini. Fifi na Nanaa wakafuata
nyuma. Walimuacha Geb na watoto walio lala. Njia nzima Nanaa na Fifi walikuwa
wakiongea na kucheka.
~~~~~~~~~~~~~~~
Walifika
ukumbini, Jeri akiwa na maagizo ya kunyanyua vitu vyote vizito. Kabla ya muda
wakula haujafika, Nanaa na timu yake wakawa wameshamaliza kupanga kila kitu, na
panavutia. Watu walipenda upangwaji wa chakula. Usafi ulioonyeshwa kwenye vile
vyakula, na mwisho ladha. Akajitengenezea baadhi ya marafiki/wateja, siku hiyo
ikaisha ikiwa imejaa matumaini.
~~~~~~~~~~~~~~~
Wakati
Jeri anapandisha vyombo kwenye gari, huku wale wasichana wakimalizia kusafisha
pale, Fifi ndiye aliyekuwa akisubiria amaliziwe kulipwa pesa yake iliyokuwa
imebaki kwa ajili ya shuguli nzima,
Nanaa akaanza kusikia vichomi. Akajiweka kwenye kiti wakati anasubiria
wote wamalize. Fifi alimuahidi angemrudisha. Alikaa mwisho kabisa wakati
sherehe ikiendelea. ‘Vipi?’ Ujumbe ukaingia
kutoka kwa Geb. ‘Nimechoka. Nipo hoi!’ ‘Pole.
Unafanya nini sasa hivi?’ ‘Nimekaa tu. Jeri na wale wasichana wamenisaidia
sana, nakushukuru. Sasa hivi Jeri ananisaidia kupandisha vitu kwenye gari na
wale wasichana wanasafisha. Ni kama tumeshamaliza. Tukilipwa tu, tunaondoka.
Dada Fifi amekubali kunirudisha.’ Nanaa akajibu. ‘Nipo hapa nje, nakusubiri.’
Nanaa hakuamini. Akasimama kwa haraka na kutoka hapo ukumbini.
Alimkuta
Geb na watoto wake kwenye gari wanamsubiri. Watoto wapo kiti cha nyuma
wakiangalia cartoons kwa kupitia screen ndogo zilizoning’inia nyuma ya viti vya
mbele vya hiyo gari. Wametulia kimya. Nanaa akasogea mpaka kwenye dirisha la
Geb. “Mama!” Liv akamuwahi. “Hey baby!” Nanaa akawa hajui asimame pale mbele
hapo kwa Geb au arudi kwa Liv aliyekuwa akimchangamkia.
“Usinge
hangaika Geb! Dada Fifi angenirudisha tu.” “Tulipitiwa na usingizi. Tumeamka
muda sio mrefu. Nikawalisha hawa, ndio nikaona nikufuate. Pole na uchovu.”
“Asante. Naona sababu ya kusimama sana, kiuno kinauma, vichomi ndio vimeanza
kuwa vikali. Nimekataa oda zote za kusambaza ofisini week nzima.” Nanaa
akafikiria.
“Eti
nilikuwa nikifikiria. Sijui ni sawa?” “Nini?” Geb akauliza. Nanaa akafikiria
tena kidogo. “Kwa sasa hivi na hii hali yangu jinsi nilivyo na watoto, labda
niwe nafanya kwenye masherehe tu. Nisisambaze maofisini kila siku asubuhi.
Nitashindwa kufanya vyote na afya yangu bado haijakaa sawa. Nisije nikapoteza
mtoto au kujidhuru mimi mwenyewe zaidi. Sijisikii vizuri. Au unanishaurije?”
“Kwangu ingekuwa furaha Nanaa. Kazi yakupika kila siku na kusambaza sio kitu kidogo,
halafu bado na watoto wanakutegemea wewe! Ikiwa mara moja moja, ni afadhali.
Lakini sio kila siku.” Akatulia kidogo.
“Nimegawa namba yangu kwa watu baadhi.
Wameniahidi tenda. Nitasubiri nione.” “Panda kwenye gari basi upumzike.
Nitamwambia Jeri kuwa upo hapa.” “Afadhali.” Nanaa akapanda. Geb akamuona
anatetemeka mikono. “Umekumbuka kunywa dawa leo?” Nanaa akabaki akifikiria.
“Hujanywa. Na nafikiri presha imepanda Nanaa. Turudi nyumbani. Fifi
atakuchukulia pesa. Nitamwambia Jeri kuwa tumeondoka.” “Na wale wasichana
wanalipwa kiasi gani?” “Jeri ameshamalizana nao. Mwambie Fifi asiwalipe tena.” Akajua yeye ndiye aliyempa Jeri pesa
zakuwalipa wale wasichana waliomsaidia kazi. “Asante Geb.” “Karibu.”
Wakaondoka. Ikabidi njiani ampigie simu Fifi kumtaarifu kila kitu.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akashusha
watoto, na kuwaweka chini pale sebuleni. Akaenda bafuni alipokuwa Nanaa.
“Nikusaidie nini?” Bafu lilikuwa dogo si kubwa kama la chumbani kwa Geb, kwa
hiyo alikuwa akimuona pale bafuni akioga. “Nipo tu sawa. Nataka nimalize hapa,
nijilaze kabisa.” “Utataka nikupishe pale kitandani?” Nanaa akanyamaza kidogo.
“Nakushukuru kwa kunifuata Geb. Kweli nilikuwa nimechoka.” “Nilihisi tu utakuwa
umechoka. Ulisimama siku nzima ukipika!” Nanaa akacheka kidogo. “Nimefurahi
kuweza kunifikiria.” Geb akatoa tabasamu tu.
Akamsaidia
kukausha miguu wakatoka. “Najisikia vizuri. Natamani kutokee godoro kubwa hapa
sebuleni, nijilaze hapo wakati wanangu wanacheza hapa hapa nikiwaangalia.” Geb
akaenda kufuata godoro la kitandani kwake. Akalitoa. Nanaa akaanza kucheka.
“Litakuangusha hilo godoro!” “Si unataka kulala hapa sebuleni na wanao? Basi
acha mimi nitimize shauku yako.” Geb akaliweka chini lile godoro na
kulitandika. Nanaa na wanae wakapanda. Magesa alikuwa amemshika mama yake huku
akiruka ruka. “Anamwaga ute huyo! Muone. Anakazi yakucheka tu.” Nanaa akamfuta
mwanae na kumtekenya zaidi. Magesa akawa anacheka sana. Wakajilaza pale wote
mpaka Geb. Nanaa akapitiwa na usingizi muda uleule.
Kinachoendelea Ndani Ya Nanaa.
Mtoto
akawa anacheza tumboni huku akiota ndoto mbaya. Geb akamuona anahangaika. “Nanaa,
vipi?” Nanaa akashituka, akafungua macho na kugeuka. “Geb!” Aliita
kwa mshangao. Alikuwa amelala nyuma yake. Karibu sana. Watoto wamezagaa kila
mahali. “Mbona machozi tena?” Geb akamfuta. Nanaa akavuta pumzi huku amejishika
tumbo.
“Nilikuwa usingizini naota ndoto mbaya. Lakini Jimmy naye huwa anacheza
sana asubuhi. Wakati mwingine anakuwa upande mmoja. Naumia.” “Sasa hivi una maumivu?” “Upande huu.” Nanaa
akaendelea kusugua taratibu. “Sijui
huyu mtoto nimuite wa bahati mbaya! Wakati mwingine huwa hata sielewi Geb!
Nilikuwa nikiweza kuzungumza na watoto wangu wote wakati wapo tumboni. Lakini
nashindwa kitu cha kumwambia Jimmy.Nakuwa..” Nanaa
akashindwa kuendelea kuzungumza, akaendelea kulia.
“Naweza
kumshika?” Geb akauliza kwa upole. Nanaa akatingisha kichwa kukubali. Geb
akaweka mkono. Akampapasa kwa muda kama kumtuliza yule mtoto, kisha akabusu
tumbo la Nanaa. Akateremka mpaka chini alipokuwa ametuna yule mtoto, akaanza
kuzungumza naye. “Umebarikiwa Jimmy. Mungu
alikuweka hapa kwa wakati na muda alioona unafaa. Upo sehemu sahihi na kwa mama
sahihi anayekupenda kuliko nafsi yake. Mungu amekuweka hapo na baraka zote
anazojua utahitaji hapa duniani. Wote tunakusubiri kwa hamu.” Machozi
yalikuwa yakiendelea kumtoka Nanaa wakati Geb akizungumza na Jimmy.
“Yupo dada
mkubwa Liv na Magesa. Wote watakupa wakati mzuri. Tutakupenda na ninakuombea.
Unisikilize Jimmy, huu ni muda wa mke wangu kulala. Sio wa wewe kucheza.” Nanaa akacheka. “Sasa hivi
kila mtu amelala, na wewe unatakiwa ulale. Ndugu zako wakiamka na wewe
tutakuamsha ucheze. Mwache mama alale. Umesikia?”
Geb akambusu. Kweli Jimmy alikuwa anacheza. Geb akaendelea kumsugua huku
akizungumza naye mpaka akatulia. “Amekusikia!” Wakacheka. Geb akambusu, na kurudi
kulala pembeni yake.
“Tumekupokonya
godoro, ikakulazimu ulale chini na sisi?” “Nimependa kulala hapa. Ona wanao.”
Wakacheka. “Magesa anakaribia kuanguka.” “Mwache tu. Hata hivyo muda wake
wakula umefika.” “Mbona na wewe ulikuwa hujalala?” “Niliamka kuomba. Nimemaliza
nikakuona unahangaika. Ulikuwa ukiota nini?” Nanaa akanyamaza. “Niambie tu.”
Akamuona anaanza kulia. “Ni ndoto mbaya?” Nanaa akatingisha kichwa kukubali. “Nakuwa napata ndoto mbaya ya kile
alichokuwa akinifanyia Malii. Sasa wakati mwingine nakuwa naota sura za wanaume
tofauti tofauti. Nakuwa napambana sana kujiokoa.”
Geb akamuhurumia. “Pole sana Nanaa. Pole mpenzi wangu na samahani nilishindwa
kukusaidia.” Nanaa alilia na kulia. Alilia kwa uchungu sana, Geb akamkumbatia
akawa anaendelea kumbembeleza. Alilia kwa kwikwi, mpaka akajihisi uchungu
umeisha, ndipo akatulia.
“Nilijua ungekuja hata kunisaidia kuoga!”
Nanaa akalalamika. “Lakini ulinikimbia
wakati nakuhitaji sana Geb. Uliniacha usiku kucha peke yangu, nikilia kwa
uchungu na maumivu.” Nanaa aliendelea kulalamika.
“Nilikosa Nanaa. Naomba nisamehe. Hakuna muda unapita, sijajutia. Ni kweli
nilishindwa kusimama upande wako. Lakini sasa hivi nipo na wewe. Natubu
nimekosa, Nanaa. Nisamehe.” Akaendelea kumbembeleza mpaka akatulia.
“Umenisamehe?”
Geb akamuuliza huku akimbusu kichwani. Nanaa akatingisha kichwa kukubali.
“Na mimi naomba unisamehe Geb. Sikukwambia kila kitu kilichotokea siku ile
tulipokuwa na Malii, kwa kuwa niliogopa. Sikujua ungefanyaje kama ungejua
Malii alishaniona nikiwa uchi. Maana ulipiga teke kiti ulichokalia mara
nilipokwambia tulikiss. Hofu ya kuniacha iliniingia. Lakini najua nilikosa. Ni
heri ningekwambia tu ukweli. Naomba unisamehe.” “Nimekusamehe Nanaa. Naomba
Mungu atusaidie yaishe kabisa. Uwe ukurasa tutakaoweza kuufunga kabisa.
Unafikiri utaweza?” “Sijui Geb. Kama ulivyosema ni kwa rehema za Mungu.
Niliumizwa sana. Nahitaji muda.” “Naelewa. Na mimi nitaendelea kukuombea.”
Wakatulia.
Geb
akambusu tena na tena pale kichwani alipokuwa amemuegemea, wakiwa bado wamelala
pale pale chini kwenye godoro. Wakati Nanaa anataka kurudisha busu, Magesa
akaamka na kukaa kwa haraka. Alipowaona tu akaanza kucheka. “Yaani huyu! Amani
yake huwa inamtosha yeye mwenyewe. Njoo.” Geb akamuita. Akaanza kutambaa
kuwafuata huku akivuta mashuka.
“Taratibu
usimwamshe Liv.” Magesa akamwangalia Liv kwa muda, akaendelea na safari ya
kwenda kwa wazazi wake. “Kumbe anaelewa!?” Nanaa akashangaa. “Sana tu. Na Liv
anampenda kweli. Si unamuona vile alivyolala pale kama amekufa? Hata ukimumsha
hataki kuamka, basi ngoja Magesa alie. Hata dakika haiishi, na yeye ataamka.
Hata kama ni usiku, akimsikia tu mdogo wake analia hata chumbani kwangu,
atanifuata. Hatakuongelesha, lakini atakuja kumwangalia mdogo wake. Huwa pia
anamuongelesha.” “Jamani Liv wangu! Kumbe ninaye wakunilelea watoto!” Geb
akacheka.
“Muone. Umenikatili busu langu ambalo nilikuwa nalisubiria kwa hamu kweli! Usinichekee.” Magesa alimshika mama yake akasimama huku akimchungulia baba yake na cheko juu. Nanaa alicheka sana. “Geb wewe! Haya hilo.” Nanaa akambusu shavuni. “Wala halikuwa la shavuni. Mimi nililiona sana wakati linakuja.” Geb alilalamika na kumfanya Nanaa na mwanae wazidi kucheka.
~~~~~~~~~~~~
Amani
na utulivu kati yao vikarejeshwa. Japo haikuwa kama zamani, lakini kulikuwa na
utulivu wa aina yake. Nanaa alitaka kukaa karibu na Geb wakati wote. Japo
amuegemee tu. Kama si wakiwa wamekaa, ampandishie miguu, basi walale kwenye
godoro, awe nyuma yake amsikie akihema mgongoni kwake. Na Geb alijua kama
anaanza kufunguka kwa kujisogeza karibu. Akaamua kumchukulia taratibu sana si
kwa pupa huku akikazana na maombi.
~~~~~~~~~~~~
Siku
hiyo ya jumapili hawakwenda kanisani, walibaki tu nyumbani. Ila Geb akataka
kuzungumza naye juu ya ndoto anazoota. “Zinaweza kuwa zipo sababu nyingi
zinazokufanya uendelee kuota ndoto mbaya, lakini moja wapo kubwa ni kwa kuwa
bado hujasamehe Nanaa.” Walianza kuzungumza mara baada ya chakula cha mchana
wakati watoto wanapata usingizi wa mchana. “Nina maumivu ambayo sijui nifanyaje
Geb. Nimemuachia Mungu.” Nanaa alianza kwa upole.
“Sijihesabii
haki, lakini nahisi niliadhibiwa na kila mtu zaidi ya kosa langu. Niliadhibiwa
kikatili, kama niliyekuwa nikitafutiwa sababu ya kukomolewa! Ni kama niliyekuwa
nikitafutiwa sababu ya wapi nikosee, nitendwe mabaya. Nashindwa kuamini kwamba
kwa kusema uongo tu, au kutokuwa muwazi, ndio watu waliosema wananipenda, gafla
kugeuka kuwa kama wanyama wakatili kwangu! Hapana Geb. Sidhani hata kama
kulishawahi kuwa na upendo kwangu. Nashindwa kuamini.” Nanaa akaendelea.
“Hujui
ni kwa kiasi gani hata huyo Malii alivyokuwa akinisumbua kunibembeleza na
kunishawishi kuwa ananipenda kwa dhati. Alikuwa akinisumbua mchana na usiku
mpaka nikamtishia kuwa nitakwambia kama asipoacha kunisumbua. Kidogo akatulia.
Ili kuepusha ushahidi, akawa anatafuta jinsi ya kuonana hata na wewe ukiwepo
ili azungumze na mimi. Safari za nyumbani pia akaongeza ili tu anione. Akawa
kama amepagawa! Vyote hivyo alikuwa akiniambia ni kwa vile ananipenda sana. Na
hapo nikamuonya.”
“Siku
moja wakati akiongea maneno yake bila yeye mwenyewe kujua, nikamrikodi.
Alipomaliza kuongea, nikamwambia nimemrikodi. Tena alikuwa kama anakuvizia.
Nafikiri alikuwa akikupigia kwanza simu. Akijua hampo nyumbani, au siku za kazi
ambazo anajua hata mama hayupo nyumbani, alikuwa akija. Siku hiyo nilipomrikodi
ilikuwa siku ya kazi, mchana. Nyinyi wote hamkuwepo. Nilikuwa na Liv tu.
Nilipomaliza kumrikodi, nikamsikilizisha mazungumzo yake yote. Nikamwambia
akiendelea kuja pale nyumbani na kutafuta kuzungumza na mimi, nikamwambia
nitakwambia wewe au mama na nitawasikilizisha hayo mazungumzo yake yote. Malii
alisikitika sana. Nakwambia kweli Geb, Malii alilia. Tena hapo nilikuwa
tayari ni mjamzito wa Magesa. Analia anasema ananipenda kwa dhati. Nikimkubali
tunaweza kukimbia naye hata nje ya nchi, tukaanze naye maisha mapya. Mimi
nikamwambia Malii, ile hali aliyonayo wakati ule sio kawaida. Amepagawa mapepo.
Akasema si mapepo ni penzi la dhati kwangu. Nikamwambia haiwezekani aendelee
kunifikiria mimi wakati mimi nilikuwa na mtoto wako na tayari nina mimba
nyingine. Yeye anaye mkewe nyumbani. Dada mzuri tu aliyetulia. Kwa nini
asitulie na mkewe? Nikamshauri akaombewe na asirudi tena pale, lasivyo
nitakwambia.”
“Hapo
tena akatulia kwa muda. Akaacha kuja nyumbani muda ambao anaojua nyinyi hampo
nyumbani. Sasa niambie ukweli Geb, hata kama kweli Malii anasema nilikosea
kumvulia nguo na kuacha kulala naye, kama kweli ananipenda kama alivyokuwa
akiniambia, ndio angeniadhibu mbele za watu!? Mtu unayempenda huwezi kumfanyia
vile.” “Alikuwa akinikomoa mimi zaidi.” Geb akaongea kwa upole.
“Na
yeye ameniambia hivyo hivyo.” “Kwani mliendelea kuwasiliana!?” Geb akashituka
sana. “Alikuwa akinitumia jumbe za kuomba msamaha mchana na usiku kwa kutumia Whatsapp kwa namba yake au tuseme kwa account yake ya zamani. Anasema angetafuta njia nyingine
ya kukuadhibu lakini sio kunitendea mimi alichonitendea. Anaomba msamaha, na
kuniambia anajutia. Alidhani ingemsaidia kupata furaha, lakini eti baada ya
bangi kumuisha, ndipo akili zikamrudia, akajutia. Nimsamehe.” “Kwa hiyo ulikuwa
ukisoma jumbe zake?” Geb akauliza kwa kuumia.
“Mwanzoni
sikuwa nikisoma kabisa. Nilipogundua kama nina mimba yake, na nimepatwa
matatizo ya moyo. Pengine naweza nisiishi baada ya kujifungua, ndipo ikabidi
nirudi kusoma zile jumbe. Zilikuwa zaidi ya jumbe 1000. Ikabidi nizipitie tu.
Nikajiambia hata nifanye nini, sitaweza kumkwepa tena.” “Kwa hiyo anajua kama
na yeye ana mtoto wake kwake?” Geb akauliza akisikika kuumia zaidi.
“Hapana Geb! Hatakaa akajua leo
wala kesho. Labda hapo baadaye, mtoto wake aje amtafute yeye mwenyewe. Lakini
sitamwambia kwa haraka. Nimemwambia na kumwandikia hata dada Fifi. Ikitokea
ninakufa na sitakuwepo, Jimmy aje aambiwe baba yake alipo. Kama akizidiwa na
ulezi kabla Jimmy hajaweza kujitegemea mwenyewe, basi amtafute Malii huko
alipokimbilia mpaka ampate. Nikamwandikia mawasiliano yake yeye na ya wazazi wake Malii. Ili awatafute kama
Malii hatamjibu kwa haraka au kama hatakuwa akipatikanika tena.”
“Maana aliniambia yupo kwenye hiyo nchi
akinisubiri kwa muda. Kama sitamjibu kwa miezi sita, atajua nimekataa, yeye
atahama tena na kwenda kuanza maisha nchi nyingine ambayo anajua, maisha sio
magumu kama hapo alipo sasa lakini anasema hapo alipo au alipokuwepo sasa hivi,
panafaa kwa kuanzisha familia. Au kwa maisha ya familia.” “Subiri kwanza
Nanaa.” Geb akataka atulie. “Malii hayupo hapa nchini?” “Aliniambia alitoroka
siku ileile usiku. Kumbe alikuwa ameuza vitu vyake vyote baada ya kumtaliki mkewe,
akawalipa wale vijana na kukata tiketi ya kumtoa hapa nchini usiku ule. Ndio
maana alikuwa akirudiarudia kuwa atachelewa. Kumbe alikuwa anawahi ndege.”
Nanaa akaendelea kufunguka.
“Sasa
sijui alikuja kuambiwa na nani kuwa uliniacha kesho yake baada ya kunibaka,
napo hapo akapata chakuzungumza. Akaniambia anajuta hata kwa nini aliniacha.
Angejua angebaki ili pengine ningepata mtu wakuwa naye kipindi hicho kigumu.
Akazidi kusisitiza kuwa ni kweli hunipendi. Ni heri tu niamini kuwa ulikuwa
ukinitumia tu. Na kwa kuwa wakati huo ulishapata jinsia ya mtoto wote uliokuwa
ukiwataka hapa duniani, ndio maana umeniacha. Umeona nitakuwa tu mzigo, sina
matumizi mengine tena kwako. Ndio maana uliwachukua watoto na kuniacha peke
yangu. Akaniambia anitumie nauli nimfuate tukaanze naye maisha. Na ahadi nyingi
tu. Lakini sikuwahi kumjibu. Na hayo yote nilikuja kuyasoma nilipojua nina
mimba yake.”
“Nili
m’block’ kwa muda ili niweze kutulia. Kwa hiyo kwa sasa sipati jumbe zake tena.
Lakini nafikiria nitakuja kumfungulia siku za kujifungua zitakapofika ili
nimkabidhi dada Fifi simu yangu awe na uwezo wa kuwasiliana naye, kama ikitokea
sitatoka chumba cha kujifungulia. Na nilishamwambia dada Fifi kila kitu.
Ikitokea hata naanguka leo na kufa halafu Jimmy akapona, basi afungue hiyo akaunti
na kuwasiliana naye Malii kama atataka. Asipotaka basi Jimmy atakuwa ndio
zawadi yake.” Nanaa akafikiria.
“Najua
Jimmy atakuja kujua jinsi mimba yake ilivyoshikwa. Hata akimkasirikia baba
yake, ni baba yake tu. Kwa hiyo sikufuta jumbe hata moja katika zile jumbe
alizonitumia Malii, ili Jimmy aje aweze kusoma upande wa pili wa baba yake.
Labda yeye ataweza kumsamehe, maisha yake yakaendelea. Ninachotaka ni mwanangu
aje kuwa na maisha mazuri sio kama mimi.” Nanaa akatulia kidogo kama
anayefikiria.
“Lakini
hebu niambie Geb. Katika yote hayo, sawa nimekosa. Nimetamkiwa upendo wa kila
namna. Kweli ndio nitendwe nilivyotendwa!? Mpaka neno upendo limepoteza maana
kwangu. Sielewi tena mtu anaposema anakupenda ndio nini! Ni neno la wakati tu
ili kufurahishana au labda hata mimi mwenyewe sijalielewa lina maana gani!”
Tayari Geb alijua maneno yalizagaa. Kila mtu anajua kilichoendelea na
kinachoendelea kwenye maisha yake.
“Malii
alijua udhaifu wangu na ratiba zangu, ndio akaamua kutumia vizuri. Tamaa yake
juu yako iliongezwa kwa kuwa mimi nilikuwa na wewe. Malii hajawahi kukupenda.
Lakini wakati wote alipenda kile ninachokipenda mimi. Nilikwambia vile
anavyohangaika kushindana na mimi tokea tupo sekondari. Tena sio kwamba atataka
anifikie, atataka kunishusha ili achukue vyangu. Nakumbuka kumsikia hata James
akimuonya wakati tupo sekondari. Alikuwa akiumia vile nilivyokuwa nikipata
alama za 100 hata kama anayenifuata amepata 20. Malii akadhani huwa
naangalizia. Naiba mitihani halafu nawaficha. Siwapi na wao. Akaanza kusambaza
huo uongo. James akamwambia siibii, ila huwa sisahu. Malii hakuamini. Akaenda
mpaka kunisemea kwa walimu. Nikawa nawekwa kiti cha mbele kabisa kila siku za
mitihani. Na bado nikawa napata 100 wala sio 99. Hapakuwa na jinsi walimu
wangeweza kunifelisha.” Geb akaendelea.
“Akaendelea
hivyo hivyo mpaka chuoni. Akiona wasichana wanakuja kuomba msaada niwafundishe,
basi atajitahidi kulala nao. Na atahakikisha kundi letu lote wanajua. Mimi
nilijua kama anashindana na mimi. Ni Frida tu ambaye alimshindwa wakati tupo
naye chuoni. Kwa kuwa Frida alikuwa mweusi au maji ya kunde sijui, lakini
alimshindwa akasema sio type yake. Ikaendelea mpaka kwenye uchumi na kila
mahali.” Geb akaendelea.
“Malii
hakuwa hata na mpango na wewe. Kuja tu kukuona na kujua naweza kukupata, ndipo
akaanza fujo. Siwezi kumsema vibaya kwa kuwa na yeye utazaa naye kama mimi, ni
baba yake Jimmy ambaye nipo naye sasa hivi. Na ninajua atafurahia sana akijua
kama na yeye anazaa na wewe kama mimi.” Nanaa akaanza kulia.
“Kwa nini Mungu ameruhusu haya yote kwenye maisha yangu? Kwa nini huyu
mtoto asizaliwe na mke wa Malii iwe mimi? Kwa nini mimi!?” Nanaa akaendelea kulalamika na kulia sana. “Sijui nafanya nini! Sijui kwa nini mimi!
Lakini sio kitu nataka kinitokee kwenye maisha yangu. Na ninasikitika pengine
Jimmy anajua. Lakini sio kitu nilikuwa nataka. Mungu anisamehe kwa kweli.
Lakini sio na Malii. Sikutaka huyu mtoto. Na sijui naishije naye huyu mtoto!
Sitaweza ni heri kufa tu.” Akasimama na
kuondoka pale huku analia.
Aliingia
chumbani kwa wanae, akaenda kupiga magoti kitandani na kuendelea kulia sana
huku ameinamisha uso kwenye godoro. Geb akamfuata. Akaenda kupiga magoti
pembeni yake akamuwekea mkono akaanza kumsugua mgongoni. “Naomba niangalie Nanaa.” Nanaa akamgeukia. “Naomba
turudi sebuleni tukamalizie mazungumzo yetu.” Nanaa akakubali. Wakatoka tena.
Bado
alikuwa akilia. “Najua ni ngumu sana kuniamini tena. Kwa kuwa si Malii tu
aliyekuumiza, mimi nimekuumiza zaidi ya Malii. Ila nipo hapa na wewe. Naahidi
kusimama na wewe wakati wote. Sasa hivi ukiwa mjamzito, siku unayojifungua, na
wakati unamlea Jimmy. Malii anajua na najua amekwambia kuwa huwa
sipiti kule alikopita yeye.” Nanaa akatingisha kichwa kukubali kuwa alishamwambia.
“Lakini safari hii amekosea. Ni wewe Nanaa. Wewe ni mke wangu mimi. Hata
kama nimeshindwa kuishi chochote nilichowahi kukuahidi tokea nakufahamu, basi
safari hii niamini. Nipo hapa, sina ninapokwenda. Nitakuwa na
wewe.” Machozi na kamasi vilikuwa vikimtoka. Geb akamfuta.
“Jimmy
hajaletwa kwenye maisha yetu ili akutese. Yeye sio adhabu. Hiyo ni baraka. Kwa
sasa utashindwa kujua lakini jipe muda. Naomba kwanza tumpokee na kumkaribisha
kwenye maisha yetu. Itakuaje baadaye, hata mimi sijui. Lakini ninachojua ni
kuwa hata katika hili, Mungu atatupitisha tu.” “Sidhani Geb. Haitakuwa kama zamani.” “Niangalie
Nanaa. Niangalie tu.” Nanaa akanyanyua uso na kumtizama huku akilia.
“Niambie
ni mangapi magumu tumepitia mimi na wewe na bado tupo pamoja mpaka sasa na
Mungu akatubariki watoto!?” Nanaa akaendelea kulia. “Naomba kwa mara ya kwanza nikwambie ukweli
Geb. Ila usinishangae.” “Niambie tu.” “Lakini usinielewe vibaya. Ni kitu
nimekibeba sina pakusemea.” “Mimi
nitakusikiliza.” “Mimi simtaki
kabisa huyu mtoto, Geb. Simtaki Jimmy. Wakati mwingine akicheza huwa nalia si
kwa maumivu, ila hasira niliyobeba kwa baba yake. Namchukia sana. Na ninajua
hata yeye pengine anajua huyu mtoto. Lakini mimi simtaki. Naona ni kama
kitu kilichokuja kunitenga na wanangu. Ataniua nisindwe kuwa na Liv na Magesa.
Hakika mimi huyu mtoto simtaki Geb.” Geb
akamuhurumia sana. “Najua ni vibaya.
Lakini angalau umejua kilichopo moyoni mwangu.”
“Pole Nanaa. Pole sana. Naomba utulie tuzungumze.” Geb alijaribu kutulia sana
usoni ili Nanaa apate faraja.
“Unakumbuka
ule ugonjwa wa miguu?” Nanaa akatingisha kichwa. “Unaweza kulinganisha na
Jimmy?” “Hapana!” “Unakumbuka Mungu alivyotutembelea kwa namna ya
ajabu pale hospitalini?” “Nakumbuka.” “Basi naomba ukumbuke kuwa, Mungu tunayemuamini
huwa hashindwi na kitu. Jimmy si tatizo, na wala hatakuwa tatizo. Tutakuwa naye
kama mtoto ambaye Mungu ametupa dhamana naye. Kwamba ameangalia hapa duniani ni
nani mwenye uwezo wa kumlea Jimmy, akatuchagua sisi. Yaani naomba uone hivi,
kuwa Mungu ametuamini, ndio maana akatukabidhi Jimmy. Hatakuwa jaribu
kwetu. Na utaona yale shetani aliyokusudia kuwa mabaya kwetu, vile Mungu
atakavyoyageuza kuwa mema.” Geb akaendelea.
“Cha
msingi naomba unipe nafasi na mimi. Nipe nafasi tafadhali. Tutembee
pamoja. Tuzungumze kama tulivyo zungumza leo. Ukawa huru kuzungumza kila kitu
bila kificho. Ndio napenda iwe hivyo. Tuzungumze kila kitu. Narudia tena. Hata
kama kitakuwa kibaya, unajua kitaniumiza, tafadhali nishirikishe tu.
Nakuahidi hakutakuwa na siri kati yetu. Niulize chochote unachotaka kujua,
nitakujibu. Ila yale ambayo najua yatakuumiza kwa sasa, naweza nisikwambie
mpaka utakapopona kabisa na daktari akanihakikishia utaweza kubeba mambo
mazito. Ila sitakudanganya.” “Kwa
hiyo bado unanichukulia kama mpenzi wako?” Geb
akacheka.
“Nakupenda
Nanaa. Nakupenda sana. Wewe ni wangu. Na ukitulia tu, nataka tukapeleke ndoa
yetu kanisani.” “Kabla
sijajifungua!?” “Ukiwa tu tayari, wewe niambie.”
Geb akamsogelea. Akashika mkono wake na kuubusu. Akabaki akimwangalia kama
anayesubiria jibu. “Naomba nipe muda
tena kidogo Geb. Angalau akili itulie. Sitaki tubariki ndoa yetu nikiwa na hii
hali moyoni.” “Bado unapata muda wa peke yako
nakuomba?” “Najitahidi.” Nanaa akaongea kama hana uhakika.
“Maombi
pekee ndiyo yatakutoa hapo.” Akabusu tena mkono wa Nanaa, aliokuwa bado
ameushikilia. “Asante Geb. Nakushukuru.” Geb akatabasamu huku akimwangalia kwa
uchu kama anayetamani jambo litokee pale. Nanaa alijua, akainama. “Unakumbuka
nilizungumza na wewe juu ya kusamehe?” Nanaa akakubali. “Basi muombe Mungu
akupe hiyo rehema. Wakati mwingine usisikilize sana hisia. Huwa zinachelewa
kuendana na jambo jema. Fanya tu. Chukua hatua ya kwanza ya kusamehe,
utashangaa hisia nazo zinakufuata nyuma.” “Basi niombee.” Geb akacheka.
“Kabla
ya kukuombea, nataka kwa mara ya kwanza, mshike Jimmy.” Nanaa akaanza kulia
tena. “Mshike tu. Mtamkie jambo jema. Zungumza naye. Jitambulishe wewe ni nani
kwake. Ukiweza, muombe msamaha kwa chochote kibaya ulichowahi kumtamkia.
Mwambie vile inavyokugarimu yeye kuwepo humo ndani, ili ajue unalipa garama
kubwa kwa upendo ulio nao kwake. Mtambulishe kwa Liv na Magesa. Hakikisha
wanapata muda naye kama ulivyokuwa ukimfanyia Liv kwa Magesa. Ruhusu watu
wengine wawe na ushirika naye. Usimuone kama ni jukumu lako peke yako. Acha na
sisi tuwe karibu naye. Halafu mkiwa peke yenu, pata muda naye. Utashangaa kitu
kipya kitajengeka kati yenu.”
“Sasa wewe nitakutambulishaje kwake?” Nanaa
akauliza. “Vyovyote vile utakavyotaka wewe.” “Wewe hutakuwa na tatizo?” “Hata
kidogo. Magesa na Liv hawakuchagua mimi niwe baba yao. Wamejikuta tu. Ndivyo
ilivyokuwa kwa Jimmy.
Hakuchagua.” “Ni kweli Geb. Namwadhibu mwanangu bure.
Asije kuwa kama mimi akajihisi ni mtu wa kukataliwa. Maana na mimi
sikuchagua kuzaliwa na wazazi wangu.”
“Basi unao muda wakutengeneza.” “Nashukuru Geb.” “Basi naomba uzungumza na Jimmy
ndipo nikuombee.” Nanaa akafanya kama alivyoelekezwa na Geb, huku akilia kwa
uchungu sana. Alitubu hata mbele za Mungu. Alipomaliza, Geb akamshika mikono
yake yote miwili, akamuombea. Akashangaa mpaka wanamaliza, kuna kitu kipya
kimejengeka. Si kwa Jimmy tu, hata vile alivyojisikia kwa Geb. Akawa kama
ametua mzigo.
Kwa Grace!
Wakati mambo ya Nanaa na Geb yanaendelea vizuri, kwa
Grace bado kulikuwa kunawaka moto. Alishafunga na kuomba lakini mambo yalikuwa
vile vile. Danny akawa kama amepagawa. Hasikii wala haoni. Grace alishatumia
maandiko yote aliyoyajua kuyakiri ili kunusuru ndoa yake, lakini wapi. Akabaki
kuwa mke mwema wa kupika na kupakua. Kusubiria Danny arudi usiku. Akaishia
kuumia kila mara alipokuwa akimuona anarudi nyumbani usiku akiwa na Sara.
Akaamua kuacha kumsubiri. Akajitahidi kuwepo nyumbani muda watoto
wanaporudishwa. Anawahudumia, akishawaweka kitandani anarudi chumbani
kuomba.
Danny
alishahama hata chumba. Akamuachia Grace chumba. Hakutaka kujua yanayoendelea
usiku lakini Sara aliyasimulia yote kwa msichana wa kazi wa Grace. Danny
anapokuwa akiondoka na watoto, Grace naye kwenda kazini, basi Sara hubaki hapo
ndani akitawala kwa uhuru wote yeye kama mama mwenye nyumba. Majigambo na
kujisifia mbele ya huyo msichana wa kazi, tena kwa kusudi tu ili kumfikishia
Grace ujumbe. Kwani Grace alikuwa akishaingia ndani kwake usiku, hatatoka mpaka
asubuhi anaposaidiana na msichana wa kazi kutayarisha watoto wake ili waondoke
na baba yao kupelekwa shule. Sara akaona Grace anapitwa na starehe anazopewa na
Danny. Akahakikisha ujumbe unamfikia hata kama hataki kushuhudia.
Kwa
asili Grace alikuwa mkimya sana. Mpaka afungue mdomo wake, ujue ni muhimu. Sasa
hicho kilizidi kumkera Sara aliyekuwa akipenda kuongea. Danny akiwepo, Sara
alijitahidi asizungumze ya ndani. Lakini akijua Grace yupo hapo ndani hata kwa
dakika kumi kabla muda wake wakutoka kwenda kazini haujafika, Danny akiondoka
na wanae, basi Sara alitumia huo muda vizuri sana kumkera Grace. Kama
hatajiongelesha koridoni akiwa anapita, au sebuleni akiwa ndio amehamia hapo
kujilaza. Akisema anapumzisha kiuno sababu ya shuguli ya usiku, basi atahakikisha
kokote alipokuwa Grace, anapata ujumbe wa kile anachotendewa na Danny usiku
huko chumbani. Starehe zote za kitandani, ndio zitasemwa hapo. Pesa anazopewa,
aina ya nywele zilizopo kichwani mwake na zitakazowekwa tena, na kutoa ratiba
yake ya siku nzima. Labda atakwenda huku au kule, ilimradi tu ni kero. Grace
alikuwa kimya. Hakuwahi kumjibu wala kumsemesha.
~~~~~~~~~~~~
Ilikuwa
siku ya ijumaa, Grace akampigia simu Geb. “Naomba
tukutane kwa chakula cha usiku. Tutakuwa na mama. Nataka kuzungumza na nyinyi.” Geb akatulia kidogo. Alikuwa ndio
amefika tu nyumbani anataka kupata muda na Nanaa, na watoto wake. “Geb!” “Wapi na saa ngapi?” “Kama unaona ni usumbufu, basi.” Akamsikia ni kama amekasirika. “Nitakuja G. Samahani. Ndio nimeingia tu nyumbani sasa hivi. Hata
sija…” Geb akaona abadilishe. “Niambie nije wapi na saa ngapi.” “Kama unataka muda na familia yako,
basi Geb. Sitaki kuendelea kuharib..” “Grace! Mimi nimekwambia nitakuja.
Niambie unataka kuniona hapo saa ngapi na wapi.” Grace akamuelekeza. Wakakata
simu.
Geb
akamwangalia Nanaa na wanae. Wote walikuwa wapo tayari wakimsubiria arudi
nyumbani watoke. Geb aliwapigia simu akiwa njiani, akamwambia Nanaa awaandae
watoto anakuja kuwachukua awapeleke kula na kucheza. Lilikuwa juma zito kidogo
kwa Geb. Alikuwa akitoka asubuhi na kurudi jioni giza likiwa limeshaingia.
Ilipofika ijumaa, ndipo akaona akatumie jioni hiyo na familia yake. “Samahani
Nanaa.” “Wala usijali. Sisi tupo tu sawa. Tulikuwa tukicheza hapa karibia siku
nzima. Tutatoka wakati mwingine.” Geb akajiweka kwenye kochi. “Lakini kula kwanza kabla hujaondoka. Maana
hujui ni saa ngapi utarudi na kama utapenda chakula cha huko au la.”
“Nashukuru.” Nanaa akamuwekea chakula akala. Akacheza kidogo na watoto wake,
akaingia kuoga na kutoka.
Mchuma Janga!
Alifika
pale walipokubaliana kukutana na Grace pamoja na mama yao, akawakuta
wameshaagiza vinywaji wanakunywa. Akaangalia saa. “Hujachelewa. Sisi ndio
tuliwahi.” Grace akamuwahi kaka yake. “Kwema?” Geb alikuwa na haki yakuuliza
kwa kuwa Grace alikuwa naye kazini. Hapakuwa na mazungumzo yeyote yale ya
haraka. “Sijui Geb! Ila nilitaka niwashirikishe jambo. Utakula kitu chochote?”
“Hapana. Nimeshakula nyumbani. Nipo sawa tu. Labda maji.” Geb akajibu.
“Nanaa
na watoto hawajambo?” Mama yake akauliza. “Namshukuru Mungu wanaendelea
vizuri.” Geb akamjibu mama yake. Muhudumu akaja, wakaagiza. Geb akabaki
akimtizama Grace. “Mbona unaniangalia hivyo!?” Grace akamuuliza kaka yake.
“Umebadilika sana, lakini ukapendeza.” Grace akacheka. “Hata mimi nimemwambia
amerudi kuwa msichana mdogooo.” Mama yake akaongeza. “Nimepitia magumu mengi.
Mwili wote wa umama umeisha. Mpaka tumbo!” “Umesema umepita?” Geb akauliza.
“Ndio
maana nimewaita hapa.” Grace akajiweka sawa. “Kwa ufupi tu, naona ndoa yangu
imeisha kabisa. Nafikiri nyinyi mmekuwa mashahidi vile nilivyomlilia Mungu kwa
ajili ya Danny. Lakini naona amekusudia kuachana na mimi. Mbaya zaidi, naona
yeye na Sara, wamekusudia kuniumiza kwa kuwa Danny anajua udhaifu wangu. Hakika
anautumia vizuri sana.” Grace akaendelea kuongea, Geb akimsikiliza kwa makini.
“Nipo
kwenye wakati ambao, nikiendelea kuwepo pale ndani nikiwa kwenye hali hii, kama
sitachanganyikiwa, basi naweza mimi mwenyewe kumuandikia Danny talaka. Kwa kuwa
hisia zangu zimekinahiwa kabisa. Kila sehemu ya mwili wangu imemchukia Danny
kitu ambacho sikutegemea kama kinaweza kunipata. Nimeanza hata kujuta ni kipi nilichokiona
kwake mpaka akanioa. Nimefika mahali hata sitamani tena kumuona. Yaani
najiuliza hata akirudi kuniomba msamaha na kutaka turudiane kama nilivyokuwa
nikimuomba Mungu, najiona sitakubali kabisa. Kwa ufupi, na mimi nimefika sehemu
ambayo naogopa hata kukiri, lakini ukweli simtaki tena Danny.” Grace
akaendelea.
“Nikikaa
mimi mwenyewe, najikuta namkosoa kila kitu chake.” “Hudhani nikuchoka?” Geb
akauliza taratibu. “Nahisi hivyo. Nahisi nafsi yangu imechoka kiasi kwamba sasa
hivi naongozwa vibaya sana nahisia kitu ambacho nakumbuka hata wewe Geb
nilishakwambia kuwa mahusiano hayaongozwi na hisia. Kwa kuwa inaweza kufika
siku unaamka, hutaki hata kumuona mwenzio. Lakini inabidi tu. Sasa sijui kama
hivyo ndivyo nilivyokuwa nikiishi na Danny nikawa najibidisha tu! Sijui! Lakini
sasa haya mambo anayonifanyia ndiyo yametibua, sijui Geb. Ila nakwambia ukweli,
simtaki tena.” Grace akasisitza.
“Hii
yakunikuta siku hizi nimeshafika kazini, sio kwamba nimeongeza juhudi kazini!
Ni kwa kuwa nawakwepa. Sitaki hata kumuona sura yake. Najitahidi kutoka asubuhi
na mapema kabla hawajaamka, na nikirudi, nahakikisha wamelala, au hata nikikuta
gari yake nje, basi nipite mlango wa jikoni, niingie chumbani kwangu nilale?”
“Na watoto!?” Geb akauliza kwa mshangao.
“Ndio
kinachoniogopesha Geb. Sijali tena.” “Hapana Grace. Lazima kuna tatizo.” “Si
ndio maana nimewaita! Hakika kuna tatizo. Mwenyewe anajitahidi sana kutoka nao
na kuwapa vitu vizuri ili wasiwe na muda na mimi. Ukiwakuta wakicheza video
game na wanae, hata ukiingia, watoto hawataki hata kugeuza shingo kukusalimia.
Nyumba imegeuka kama sehemu yakucheza watoto. Kuna michezo ambayo hata mimi
mwenyewe sijawahi kuiona. Basi utasikia wakishangilia yeye na wanae, usiku
kucha. Vimejaa vicheko. Kwa kifupi, amefanikiwa kutengeneza kambi yake kwenye
ile nyumba. Hawajui naingia saa ngapi wala natoka saa ngapi. Hakuna hata mtoto
anayeniulizia. Hata kutaka kuja chumbani kwangu kunisalimia, hawataki.
Watacheza na baba yao hapo sebuleni na Sara akiwepo hapo na vinguo vyake vya
nusu uchi. Basi hata umtume msichana wa kazi akuitie watoto waje wakusalimie
chumbani, hawataki. Michezo imekolea. Danny anazungumza na msichana wa
kazi tu. Na ndiye anayempa maelekezo yote juu ya watoto.” Grace akacheka kwa
kuguna.
“Siku
10 zilizopita, nafikiri Danny alichukua likizo. Nimerudi kutoka kazini,
sijawakuta hapo nyumbani. Nimekaa mpaka kesho yake, hawajarudi. Nikamuuliza
msichana wa kazi, akaniambia Danny alimwambia aandae vitu vya watoto wote,
anasafari ya siku 7. Kwa hiyo amesafiri. Mimi nikacheka tu. Ndio wamerudi juzi.
Wapo tu hapo ndani. Mama!” Grace akamgeukia mama yake.
“Natamani
wasafiri tena. Ilikuwa bado kidogo nimwambie Danny kama hana pesa naweza
kumuongezea ili waondoke tu hapo ndani kuwe na amani. Lakini maneno yakakwama.
Nikimuona, hasira inapanda! Sitamani hata kuhisi kama yupo chumba cha pili.”
Kimya. Mama G akavuta pumzi kwa nguvu.
Geb
alitamani kumwambia waombe, lakini akajua Grace ameshaomba na walishaomba
pamoja mara nyingi tu. “Sasa unataka kufanya nini?” Geb akarusha swali.
“Nashukuru umeniuliza. Naomba nipe siku 30 za likizo. Nitoke kabisa hapa mjini,
nisafiri nikasafishe akili zangu. Mbali na maneno ya kashfa ya Sara anayejisifia
kuwa Danny anamtendea haki huko kitandani. Mbali na Danny anayenitukana kwa
wazi tena wakati mwingine hata mbele ya yule msichana wangu wa kazi. Na mbali
ya wale watoto, pengine itawasaidia kupatwa na hamu na mimi. Wakanikumbuka mama
yao, wakataka hata kuiona sura yangu tena. Humuwezi amini hata Fili hataki
kukaa na mimi hata kwa dakika moja! Fili aliyekuwa anapenda nimkumbatie, siye
huyu. Watoto wote wananifanya kama mimi ndiye mgeni pale, halafu Danny na Sara
ndio wazazi wao. Naumia kuliko nitakavyosema hapa.” Kila mtu kimya.
Grace
akaendelea. “Kwa aliponifikisha Danny nakujisikia hivi ninavyojisikia sasa
hivi, ipo sehemu ndani yangu inaniambia niliharakisha sana kuolewa na Danny.
Nimepita naye kwenye magumu mengi sana. Yeye ndio amekuwa mwanaume wangu wa
kwanza. Na tukahangaika sana. Kuanzia tunampata Fili mpaka wadogo zake, akili
na mawazo yangu yote vilikuwa kwao tu. Ni kama sehemu ya maisha yangu imekuwa
wao tu. Danny na watoto wake. Ni kama nimefika mahali ‘I CAN NOT TAKE IT
ANYMORE’. Kutoka kwake na wanae. Naona wananilipa visivyo na mbaya zaidi, nafsi
imechoka. Halafu sioni sababu tena. Kwa hakika nahitaji mapumziko. Mbali kabisa
na yeye Danny. Labda nikirudi, nitajisikia tofauti.” Grace akawa amemaliza.
“Likizo
haina shida. Lakini naomba ujue nitakuhitaji kipindi Nanaa anajifungua.
Nitataka kuwa naye karibu.” “Amebakisha muda gani kujifungua?” Mama yake
akauliza. “Itakuwa miezi miwili kasoro au niseme mwezi mmoja na siku chache.”
“Mbona huko nitakuwa nimesharudi! Sitakawia kurudi. Ni likizo yangu ya mwaka.”
“Hauna siku zilizobaki za likizo Grace. Ulimaliza siku zako zote.” Geb
akamgeuka dada yake.
“Basi
nakopa za mwakani.” Geb akamtizama. Alimjua Grace kwa kukopa likizo. “Mambo
yalikizo yaache tu Grace. Umeshachukua siku zaidi ya unazotakiwa kuchukua za
mapumziko kwa mwaka. Wewe kama unataka mapumziko, mimi naelewa. Lakini naomba
nikutahadharishe Grace. Na nakuomba usinichukie. Nisikilize tu kama mimi ninavyokuwa
nikikusikiliza ukinishauri.” “Niambie tu. Nakusikiliza.” Geb akamtizama kama
kutaka uhakika.
“Wewe
niambie chochote.” “Mimi nitakwambia Grace, kwa kuwa umekuwa msaada wangu
mkubwa. Nipo hapa nilipo sababu yako. Wewe hujui tu. Lakini umehusika sana
kwenye maendeleo yangu ya uchumi, mahusiano na kila mahali. Unajua udhaifu
wangu, na kila ninapokosea, japokuwa unadhani huwa sikusikilizi, lakini huwa
nakusikiliza sana. Na wakati mwingine huwa nachukia naona unakuwa umechelewa
kuzungumza na mimi, mpaka naingia kwenye matatizo.” Grace akacheka.
“Sasa
leo naomba na mimi unisikilize tu. Na usiniingilie. Niache nimalize na usianze
kulia.” “Bwana wewe ongea.” “Tokea wewe unakua, ndoto zako na usemi wako
ulikuwa ukitaka kuolewa na mwanaume kama baba. Wakati wote ulisema utaolewa na
mwanaume mwenye umbile kama baba. Kuanzia urefu na haiba yake, vile vile kama
baba. Ukasema awe kama vile baba alivyokuwa akikubembeleza kila wakati.
Anakuweka mikononi kila unapokuwa naye. Awe muhangaikaji. Yaani mfanyabiashara.
Mwenye pesa nyingi na akupende wewe tu. Mama unakumbuka?” Mama yake akaguna tu
bila ya kujibu kitu kama anayejua anapoelekea Geb.
“Mliponiambia
umeamua kuolewa na Danny. Mwanaume ambaye hana sifa hata moja ya mwanaume
ambaye ulikuwa ukiimba unamtaka, nilishangaa sana. Muulize mama kama
sikumuuliza kama kweli unauhakika na unachotaka kufanya. Nilimwambia mama
nataka kuzungumza na wewe, mama akanikataza. Akasema nikuache tu kwa
kuwa wewe mwenyewe ndio umeamua na ulimfuata Danny mpaka Tabora.” Geb
akaendelea.
“Nikamwambia
mama, upo confused. Ulikuwa umechanganyikiwa kwa wakati ule. Sio
akili zako. Sio kweli kama unampenda Danny kwa dhati ni kwa kuwa alikuganda
sana, na maisha yenu yote wewe na Danny amekuwa kama amekufunika shuka. Hujui
mapenzi yakoje. Danny alikukaba kila kona. Nikamwambia mama, sijui kama
anakumbuka. Nikamwambia kabisa mama, siku Danny atakapompa mwanya Grace.
Akamuacha apumue hata dakika moja, Grace atajua kama aina ya wanaume kama Danny
sio chaguo lake. Na hapo atakuwa amechelewa. Nilimwambia mama maneno kama hayo
hayo uliyotuambia hapa sasa hivi, vile unavyojisikia sasa hivi kila ukimuona
Danny. Mama unakumbuka?” Mama G akanyamaza.
“Nilikutahadharisha
mama. Na nikakwambia haya yanayotokea sasa, ni lazima yatakuja kutokea tu. Uliolewa
na Danny kwa kuwa aliacha kukufanyia aliyokuwa akikufanyia kwa wakati ule, na
akaondoka. Alikubali kuolewa na Danny huku akifungia macho mapungufu mengi sana
ya Danny, kwa kuwa tu, alikuwa akikusindikiza bafuni. Sasa, sasahivi hayafanyi
hayo yote tena, huoni umuhimu wa Danny tena.” “Lakini…” “Subiri kwanza Grace. Nimekuomba
usiniingilie.” Geb akataka kumaliza.
“Unakumbuka
mazungumzo yetu ya mwisho niliporudi nchini, kabla hujaolewa na Danny, juu ya
Danny mwenyewe?” Grace akanyamaza huku akilia. “Ulimsema vibaya sana Danny.
Ukaniapia humpendi kabisa. Hutaki hata kumuona. Kama hivi unavyosema sasa hivi,
ndivyo ulivyokuwa ukimsema Danny. Tena ukaniambia huwezi hata kumfikiria eti
anaamka pembeni yako. Hana sifa hata moja yakuwa mumeo. Tukazungumza siku ile
mpaka usiku. Nimeondoka, hata miezi miwili haijaisha, mama ananiambia unaolewa
na Danny! Hakika nilishituka sana. Sikuamini. Kwa kifupi tu Grace, hukuwahi
kumpenda Danny.” Mama yake akamwangalia Geb.
“Utanisamehe
mama. Lakini lazima niseme ukweli. Hizi zote sasa hivi ni sababu zilizochipua
ukweli uliopo ndani yako Grace.” “Danny ndio amechangia.” “Nisikilize
Grace. Nyinyi mlijua kilichotokea kati yangu na Nanaa. Alibakwa wote
tukimsikiliza. Ana mimba ya Malii. Yaani amebeba mtoto wa Malii. Lakini
mama na Grace, garama ya kuishi bila Nanaa, ni kubwa
kuliko kusamehe na kumpokea vile alivyo. Maisha yalinipa nafasi yakuchagua
mwanamke mwingine. Na nilikuwa naweza kufanya hivyo. Nyinyi ni mashahidi,
lakini sijaona mwanamke ambaye anaweza kuchukua nafasi ya Nanaa kwenye maisha
yangu. Ndio maana nilikuwa nakonda. Ni kwa kuwa nilikuwa na hasira, lakini bado
namtaka Nanaa.” Geb akaendelea.
“Nimekuja
kugundua nampenda yule binti, kwa kila namna. Hakuna kosa au kitu atanifanyia
nisitake kuwa naye. Nalala usingizi, nikijua yupo na mimi na mimi ndiye
nammiliki. Kwamba ni wangu. Malii alimwambia kwa jinsi anavyonijua, sitamkubali
tena baada ya yeye kumbaka. Hakukosea. Kama angekuwa amembaka mwanamke
mwingine, hakika hiyo ndio ingekuwa sababu. Lakini ni Nanaa wangu. Ni
wangu mimi. Wala sitakaa nimwachie mtu mwingine. Hapo shetani ajue
ameshindwa. Akikubali tu, nitamkimbiza kanisani, nifunge mbingu na nchi, ili
Nanaa awe wangu wa maisha.” Geb aliongea kwa uhakika.
“Hapo
ndipo nilipoelewa mapenzi ni nini. Kabla ya Nanaa, sikuwa najua. Unaweza ukawa
umekasirika. Au umemkasirikia mtu, lakini bado ukamuhitaji.” “Hunitendei haki Geb. Wewe hujaona vile
nilivyohangaika na Danny? Yeye ndio amenikataa.” “Naomba
usilie Grace. Nitashindwa kuzungumza.” “Kwa nini unashindwa kunielewa?” “Nakuelewa.
Na ndio maana nataka kukusaidia. Naomba unyamaze G.” Mama yao alikuwa kimya
ameinama chini, kashika shavu kama linataka kumwagika.
“Chukua
likizo ya hizo siku 30. Nenda kapumzike. Safisha mawazo, lakini ujue wazi huo
ndio ukweli utakao kutana nao hata baada ya hizo siku 30.” “Sasa nifanyaje?” Grace akauliza. “Hilo ndio swali la msingi
namuhimu. Sasa hivi umerudisha umbile na sura ya kisichana. Haitakuchukua hata
siku hizo 30, kupata mwaume wa ndoto zako. Shetani hasinzii wala halali kwa
kuwa anajua haja zako, atakutega tu. 1koritho 10: 13 inaeleza juu ya majaribu
tunayoyapata kuwa yapo ndani ya uwezo wetu. Kuwa tunaweza kuyashinda. Na Mungu
atakupa mlango wakutokea.” Grace akanyamaza.
“Kuachana
na Danny isiwe ni suluhisho lako la
kwanza. Ila kupumzika na kurudi ukiwa na nguvu mpya iwe ndio nia ya sasa. Mungu
anaweza kukurejeshea yale yote shetani aliyokupokonya. Kama ulivyonituma
nikamwambie Nanaa, na wewe pia pokea hayo maneno yakinabii. Omba rehema kwa
Mungu. Msihi aumbe moyo safi ndani yako. Moyo uliojaa upendo. Akujalie
kumtizama Danny kwa namna ya tofauti. Inawezekana Grace. Utaweza na utafanikiwa
kwa kuwa sasa hivi unaanzisha mahusiano yako kwenye madhabahu ya bwana.
Ukifanikiwa hapo. Haitakuwa kama zamani. Upendo Mungu atupao, sio ulimwengu
unaweza kutupa. Utakuwa mkubwa na wa ajabu. Utarudishiwa ndoa yako ukiwa na
upendo wa tofauti.” Grace akanyamaza.
“Wewe
Grace!?” Mama yake akashangaa Grace hajibu ameinama kama anayefikiria.
“Nimeshaomba sana mama. Nimechoka.” “Grace wewe! Kwa hiyo unataka kumuacha
kabisa Danny?” Kimya. “Lakini hivyo sivyo tulivyozungumza Grace. Ulisema
unasafiri kidogo, utarudi kwa wanao na mumeo.” “Bibilia yenyewe imeruhusu
kuachana kwa kosa la uzinzi!” Grace alimjibu mama yake. “Grace wewe umeingiwa na roho nyingine.” Mama
yake akasisitiza. Geb alikuwa kimya kabisa akiwasikiliza.
“Mimi sijaingiliwa na roho yeyote kwa kuwa
nilikuwa kwenye maombi. Ukute Mungu ndio amenifungua macho. Simtaki
Danny, mama. Simtaki tena. Nimevumilia nimechoka. Analala na Sara humo humo
ndani! Sara ananiringishia mambo yao wanayofanya usiku kwenye mapenzi! Siwezi
kumruhusu anishike tena. Nimeingiwa kinyaa mimi. Wewe unafikiri hata
tukirudiana ndio nitasahau kama alilala na mwanamke mwingine humo humo ndani ya
nyumba ambayo anajua na mimi nilijenga kwa jasho langu? Nawezaje kurudiana naye
nikijua anafanya kwa makusudi, tena wala sio mara moja! Au sio kwamba ni bahati mbaya!
Anaishi na Sara huku akinitukana mbele ya Sara na mfanyakazi wangu! Kwamba
alikuwa anakula makapi usiku kucha, sasa hivi Sara anamlisha penzi kwa mrija.
Anakula vitu laini kwa mtoto laini!” “Haiwezekani Grace!” Mama G alianza kutokwa na machozi. Grace
hakukusudia kuyasema yote, lakini akajikuta anayaongea tu mbele ya kaka yake.
“Kweli mama. Unafikiri ni kwa nini nakwambia nitachanganyikiwa?
Ninatukanwa matusi ya nguoni tena waziwazi. Nenda kazungumze na msichana wangu
wa kazi. Ni vile yule dada alitokea kunipenda tu. Lakini mama, mimi
nimeshindwa. Sijawahi kudhalilika maishani kama hivi. Najiuliza ni mpaka lini? Na
kwa nini!? Au kwa Lipi jamani!?” Grace
aliendelea kuongea kwa uchungu sana huku akilia.
“Mwili huu nimejisitiri hapa kwenu tu. Lakini nikiingia tu pale ndani
ya ile nyumba, ni kama nipo uchi kwa vile ninavyochambuliwa huu mwili kwa
matusi. Sina thamani.” “Na watoto?” “Ndio hicho kinachoniogopesha mama. Sasa
hivi wanatukana kwa lugha ya mafumbo. Ila mnajua vile Fili alivyo na akili.
Nahofia ataanza kuelewa, na yeye ashindwe kuniheshimu. Naumia sana. Hakika
ningevumilia, na wewe Geb unakumbuka nilikwambia namuombea Danny. Lakini sina
hata pakuombea tena. Unafuatwa na matusi kuanzia asubuhi mnaamka, Sara
akimsifia hapo koridoni mapenzi waliyofanya asubuhi hiyo, au anatoka huku
akitangaza dada akae na watoto kwa muda, wao wanaingia kuoga. Usiku napo
mtaagwa kwa sauti. Kuwa wanaenda kuanzisha safari ya mapenzi. Kweli jamani!
Mlitaka nifanye nini zaidi?” Kimya. Kila mtu
kikawa kimemuingia moyoni. Hasira wote zikawapanda.
“Unataka
kuondoka lini?” Geb akamuuliza. “Kesho.” “Unataka nikutafutie tiketi ya
wapi?” Geb akamuuliza. “Nataka kwenda
kwanza Arusha. Halafu baada ya hapo nitajua. Lakini nitaacha simu.” “Una watoto wadogo wewe. Wakipatwa na tatizo?” “Naona mama wewe hujanielewa. Nakwambia
Danny amefanikiwa kutoa nafasi yangu pale ndani, hata wanae wamejua kama sina
matumizi kwao. Sina chakufanya kwa wale watoto na wale watoto hawana habari na
mimi. Sijui uzima wao wala ugonjwa. Danny anazungumza kila kitu cha wale watoto
na yule msichana wa kazi. Yaani mimi najua maendelea ya wanangu kwa kupitia
yule msichana wa kazi.”
“Na ili kujua maendeleo ya huko wanakoshinda shuleni, ilinibidi mimi
mwenyewe kwenda kuonana na walimu wao. Nako huko Danny amemwaga sumu kali, ni
vile mwenye ile shule naye ni mama na tulifahamiana tokea Fili anaanza kusoma
pale. Tunaheshimiana sana. Walimu waliponizuilia, ndipo ikabidi kumtafuta sasa
yeye mwenyewe yule mama mwenye shule. Nikamueleza kwa ufupi pale tulipo na
Danny, ndipo akazungumza na wale walimu wa wakina Fillius. Hapo ndio nikaweza
kupewa maendeleo yao. Hasa Fillius na Fillan. Ndio hao nilikuwa na wasiwasi nao
kwa kuwa bado ni wadogo. Kwenda asubuhi na kurudi jioni! Nikaona wanateswa tu.
Ndio nikaambiwa wanapata muda wa kulala mchana. Nikazunguka kwenye hiyo shule,
na sehemu wanazokuwa wao kwa siku nzima. Nipazuri kwa kweli. Nikaridhika,
lakini sio wale watoto wenyewe. Hawanitaki mama. Huna utakalowauliza wakakujibu
kwa muda mrefu. Wanakujibu kama wanaharaka na Danny naye akijua umewaita tu, na
yeye atawaita hapo hapo. Sina raha mama. Acha niondoke. Labda hata wanangu
wanaweza kunikumbuka tena. Sasa hivi hata wao wamechanganyikiwa.” “Naomba unyamaze Grace. Usilie. Pole.” Geb
alimtuliza dada yake. “Kunywa maji kidogo.” Geb alitaka Grace atulie kabisa.
Alishaumia na kumuhurumia sana. “Pole.” Akarudia. Grace akanywa maji,
akatuliwa. Mama yao akabaki kimya.
Grace
ni mkimya. Hawakujua hayo yote yaliyokuwa yakiendelea kwenye maisha yake. “Kuna
kitu kingine unataka?” Geb akauliza. “Hapana. Pesa ninazo.” “Safari njema. Ila
nitataka kujua kama ulifika salama. Na kila baada ya siku tatu unijulishe kama
upo salama. Sawa?” “Sawa. Kwa hiyo natakiwa kukupigia simu mara 7 katika hiyo
likizo?” “Naona tumeelewana. Nisipokusikia baada ya siku 3, ujue nitaanza
kukutafuta. Kwa hiyo nilazima unitafute, Grace.” “Sawa.” Geb akasimama.
“Utatumiwa
tiketi yako muda si mrefu.” Akamgeukia mama yake. “Usiku mwema mama.” Mama G
akabaki kimya akifuta machozi. Alilizwa na mengi. Sara alikwenda kumtafuta yeye
mwenyewe. Hakutumwa na mtu. Alitaka awe mke wa Geb, leo amekuwa mke wa mkwewe!
Yule mama alijawa na majuto, asijue safari hii anamwita Mungu au Baba wa Yatima
yupi wakati alimtenda yatima mwenzake ubaya wa namna ile. Hata Nanaa naye
anatetewa na huyohuyo Baba wa yatima, Mungu anayemwitaga mama G. Halafu
mchafuaji ni Danny, na yeye ni Yatima. Mtoto aliyempokea kama mwanae! Akabaki
kulia, hata kuomba anashindwa. Geb akaenda alipokuwa amekaa, akambusu kichwani.
“Uwe na usiku mwema mama.” “Na
wewe. Nisalimie Nanaa na watoto.” “Asante.”
Geb akaondoka na kumuacha mama yake akiendelea kufuta machozi, akijua
anachojisikia huko moyoni. Hata hilo la Grace kuolewa na Danny pia alimuonya
mama yake. Geb alimjua Danny kwa kuishi naye miaka 7, tena chumba kimoja,
darasa moja.
Kwa Nanaa.
Geb
alirudi nyumbani akamkuta Nanaa amejilaza kwenye kochi peke yake, godoro lipo
chumbani. “Vipi? Mbona godoro umetoa tena? Hatulali hapa?” “Nimeona kama watoto
wanaanza kuzoea kulala hapa na mimi, Geb. Hata mchana wanataka nilale nao.
Naona ni kitu ambacho kitaanza kuwasumbua kipindi nitakachokuwa hospitalini na
mdogo wao. Ule utaratibu uliokuwa umewazoeza ni mzuri. Kila mtoto alale
kitandani kwake. Au nimekosea?” Geb akatulia. “Lakini wapo tu sawa. Niliwatoa
kwenda kucheza hapo kwenye mabembea. Wamecheza mpaka wamechoka. Nimerudi
nikawaogesha, wamekula ndio wamelala. Tena umewachelewa kidogo tu.” Nanaa
akaendelea kujieleza bila kujua kinachomfanya Geb anyong’onyee vile.
“Lakini
kama unaona ni sawa tuendelee kulala nao, basi. Tukatoe tena godoro, tuwalete
tulale tu hapa. Lakini nilikuwa nakuhurumia wewe kipindi ambacho mimi nitakuwa
hospitalini. Wakati umebaki nao hapa peke yako, utateseka.” “Kama hiyo ndio
itanisaidia kulala karibu na wewe, sitajali kunyanyua godoro na kulirudisha
hapa.” Nanaa akashangaa. Akakaa. Geb aliongea kwa kunyong’onyea.
“Naona
tunarudi tena nyuma Nanaa! Mimi na wewe nilifikiri tunasogea mbele, lakini
naona tunarudi mwanzo kabisa! Unarudi kulala kwenye kochi, mimi narudi kulala
chumbani peke yangu!” “Sikujua kama, kama…” Nanaa akasita asijue amalizie vipi
sentensi yake. “Kama nataka kulala na wewe au kama nafurahia kulala pembeni
yako? Unataka nifanye nini Nanaa? Niambie.” Nanaa akanyanyuka, “Mimi natangulia
chumbani.” Geb akabaki hana chakusema tena. Nanaa akaenda chumbani kwa Geb,
akapanda kitandani.
Geb
akamfuata. “Sasa unalala hapa kwa kuwa unapenda au unaona nimekulazimisha?”
“Naomba uje tuzungumze ukiwa umelala hapa, Geb. Najua umechoka. Week hii nzima
umekuwa busy. Njoo hapa ulale. Nitakubembeleza utalala kama Magesa.” Geb
akacheka, akavua nguo haraka akapanda kitandani.
“Habari
za huko ulikotoka?” Nanaa akaanza kumuhoji taratibu wakati akimchezea nywele.
“Sijui Nanaa. Ila ujue nimefurahi umelala hapa na mimi.” “Nakusikia unavyoongea
kwa kugugumia raha.” Geb akacheka. “Na ushikwaji huo sijaupata tokea nakutoa
hospitalini baada ya kujifungua Magesa. Nishaanza kusinzia.” “Wewe lala tu.”
Nanaa akajua hataki kuzungumzia habari za huko alikotoka, akaona amuache tu.
Alimchezea nywele huku akimpapasa taratibu mpaka akalala. Akamcheka na
kumfunika vizuri, ndipo na yeye akalala.
Grace safarini
Grace
aliondoka na ndege ya asubuhi ya saa 4, kuelekea jijini Arusha. Alipendeza,
ungependa kumwangalia dada huyo. Kama angekwambia ana watoto watatu
usingesadiki. Alikuwa akivutia. Alikumbushia enzi za usichana wake.
Akajitengeneza na kuvaa nguo aliyopenda yeye. Hapakuwa na Danny wakumrudisha
wala mtu wakumuuliza. Kwa hiyo alivaa alichopenda, na akapendeza. Geb alimtuma
Jeri akamchukue kumpeleka uwanja wa ndege.
Aliingia
kwenye ndege, akakaa kiti cha dirishani. Geb alimpatia kiti kule First class,
kwa matajiri. Grace akajiweka sawa. Hakuwa na simu wala kitu chakufikiria ila
kule aendako tu. Akaja mtu kukaa pembeni yake akiwa anazungumza na simu. Grace
hata hakujisumbua kumtizama. Akageukia vizuri dirishani, akaendelea kuwaza
maisha yake. Matangazo yakaendelea, akajua wanakaribia kuondoka. Akahakikisha
amefunga mkanda vizuri. Akatulia.
Wakati
ndege ipo angani akahisi mtu anamgusa. Akageuka. “Karibu usome gazeti.” Grace
akatizama lile gazeti, akapokea bila hata kumwangalia usoni. “Asante.” “Huwa
pia wananiita Man.” Ikabidi Grace amwangalie na tabasamu. “Nimejitahidi
kukohoa, kuhangaika hapa kwenye kiti, lakini wapi! Imebidi nimuombe jirani gazeti
nikupe ili uniangalie. Pia naona umepokea bila kuniangalia!” Grace akacheka.
“Naitwa Grace.” “Daah! Afadhali. Mpende jirani yako kama nafsi yako. Huwezi jua
litakalo tupata huko angani. Ni bora kufahamiana mapema.” “Kwa hiyo kila
unayesafiri naye huwa unajitahidi kumpenda?” “Kwa kweli najitahidi. Katika hilo
huwa najisifu.” Grace akacheka na kugeukia gazeti.
Pakatulia
kidogo. “Mimi naenda Arusha.” Grace akamgeukia akiwa ametulia. “Nimesema mimi
naenda Arusha.” Man akarudia, Grace akacheka. “Sawa.” Grace akajibu na kugeukia
gazeti. “Eti mimi nilijua na wewe utaniambia wapi unakoelekea.” “Mimi nilijua
umenipa gazeti nisome.” Grace akajibu. “Hapana. Nilitaka tu uniangalie.” Grace
akacheka. “Na mimi naelekea Arusha kwa mapumziko.” “Daah! Heri yako wewe.” “Kwa
nini unasema hivyo?” Ikabidi Grace amuulize tu. “Mimi natafuta hayo mapumziko,
huu ni mwaka wa pili, sijayapata.” “Wakati mwingine unalazimishia.” “Eti eeh!”
Man akawa kama anafikiria.
Grace
alishamuona ni mtundu. Akacheka. “Hapa nafikiria jinsi yakulazimishia. Lakini
najua nitaweza tu. Unajua nilikuona ukiingia humu ndani ya ndege. Kiti changu
kilikuwa kile pale. Nikamlazimishia yule jamaa, tubadilishane viti. Alitaka
kukataa, nikamlazimishia mpaka amekubali. Sasa nimekuja tena hapa, nikaona
huniangalii! Nikajiambia juhudi zote zile, halafu hata nisiione sura kwa
karibu, heri nimuombe jirani gazeti.” Grace alizidi kucheka.
“Naitwa
Grace. Nimeolewa na nina watoto watatu.” “Woooh! Wooh! Taratibu Grace. Acha
kunifukuza kwa nguvu hivyo! Mbona mimi nimesema ni salamu tu! Naona umeamua
kunifukuza kabisa!” “Hapana. Huo ndio ukweli.” “Lakini sijaona pete hapo
kidoleni!” “Si hii..” Grace akaangalia kidoleni akagundua hana pete. Man
akamtizama kama kumsuta. “Kweli tena. Sio kwamba nakufukuza. Nina watoto
watatu. Ngoja nikuonyeshe picha zao kwenye simu yangu.” Akafungua pochi,
akakumbuka hata simu aliacha. Man akapandisha nyusi juu.
“Naona
nimesahau na simu.” Man akajidai anacheka kwa kukohoa. “Bwana wewe ni mtundu
Man. Ila ujue sijakudanganya.” “Labda niulize Grace. Kusudi la ule utambulisho
mzito vile ni nini?” Grace akaingiwa na aibu mpaka akajikuta anavua miwani
aliyokuwa amevaa kwa ajili ya jua na mwanga. Amekuwa mama kwa muda mrefu sana.
Hajui kujitenga na wanae. Akainama kama
anayefikiria huku akichezea ile miwani. “Niliona nikwambie tu usije kufikiria
umekaa hapa na msichana, kumbe ni mama.” Grace aliongea kwa upole huku
akimtizama Man. Na sauti yake na macho, ungependa tu kumsikiliza. “Ila sikuwa
na nia mbaya.” Aliongeza kwa upole baada ya kumuona Man amebaki ameduaa
akimwangalia. “Nimefurahi kukufahamu, Grace.” Man akapunguza uchokozi, akaongea
na yeye kiustarabu. Grace akatoa tabasamu na kugeukia dirishani. Kimya.
Wakatulia
kabisa kwa muda mpaka wakawa wamekaribia kufika. Man akamgusa tena. “Nafikiri
hiki kikaratasi ni chako.” Man akamkabidhi, Grace akakipokea na kukifungua. ‘Samahani. Sikukusudia kukuudhi.’
Grace alikutana na huo ujumbe kwenye hicho kikaratasi. Akajua kinatoka kwa Man.
Akamwangalia akakuta na yeye anamwangalia. “It’s okay.” Grace alijibu kwa sauti
ya chini. “Thanks.” Man naye akajibu taratibu huku akimwangalia. Grace
akarudisha macho dirishani mpaka wanafika hakumwangalia tena.
“Ningekuwa
sijaharibu, ningekukaribisha jijini. Lakini najua hutakubali tena. Basi naomba
nikutakie mapumziko mema.” Man aliongea kabla hajashuka. Grace alitabasamu tu,
akarudisha macho kwenye pochi yake. Akaingiza baadhi ya vitu vyake kwenye pochi
huku Man akimwangalia. Alipoona Grace hata hamgeukii tena, akasimama na kutoka.
Baadaye Grace na yeye akashuka taratibu bila haraka huku akifikiria chakufanya
jijini hapo.
Akachukua
sanduku lake kubwa na dogo, pamoja na begi jingine alilokuwa ameweka kwenye
ndege. Yote yalikuwa yakifanana. Akayaweka pamoja ili kupata urahisi
wakuyasukuma. Akayaburuza mpaka nje.
Akaangalia kulia na kushota akitaka taksii, imsogelee. Lakini ikamsogelea kwa
haraka gari ambayo wazi haikuonekana kama ni taksii.
Alikuwa
tena Man. Akashusha kioo. “Naweza kukusogeza.” “Hapana. Asante. Nitachukua tu
taksii.” Grace alikataa bila hata kufikiria. Man akafikiria kidogo, akaondoa
gari. Alipoondoka tu Man, taksii ikamsogelea. Grace akapanda. “Mimi ni mgeni
hapa Arusha. Unafahamu hoteli yeyote nzuri.” “Usiwe na wasiwasi dada. Hapa
umefika. Nitakupeleka kwenye hoteli ambayo huwa pia wanatoa huduma za utalii.
Ni pazuri sana.” Grace akashukuru. Akatulia ndani ya hiyo taksii akimsikiliza
huyo dereva taksii akisifia hiyo hoteli na huduma zake. Kadiri yule dereva
alivyokuwa akiongea akisifia huduma ya hiyo hoteli, Grace alikuwa akijiambia
kama ni kweli, basi ataua ndege wengi kwa jiwe moja. Akajua mapumziko yake
yatafanikiwa.
~~~~~~~~~~~~~~
Dereva
alimpeleka mpaka kwenye hiyo hoteli. Akamshusha. Kwa nje tu, Grace akakubali
kuwa ameletwa sehemu ya hadhi yake. Alipokelewa mizigo yake na mtu aliyekuwa hapo
mlangoni na sare nzuri sana. Akashukuru, akakaribishwa ndani mpaka mapokezi.
Kitu alichotaka ni chumba ambacho kitakuwa gorofa ya mwisho kabisa. Ambako
hatamsikia mtu ila yeye mwenyewe. Muhudumu akacheka, na kurudisha macho kwenye
kompyuta iliyokuwepo mbele yake.
Kwa
ukarimu ule aliokuwa akifanyiwa na kutetemekewa kama mfalme, Grace alijua wazi
pesa ya kutosha itamtoka. Lakini alikusudia kwa mara ya kwanza maishani, afaidi
jasho lake yeye mwenyewe. Akabebewa tena mizogo yake mpaka chumbani. Chumba
kilikuwa full suit. Madhari ya pale ndani tu, yakafanya moyo wa Grace
usuuzike.
Muhudumu
yule yule aliyekuwa amevaa sare za hapo hotelini, ambaye alimbebea mizigo yake
tokea anafika hotelini hapo, aliingiza ile mizigo mpaka ndani na kuuliza kama
angetaka kitu chochote. Lakini Grace akakataa. Alimpa pesa kidogo. Kama tip,
akafunga mlango. Hakuwa na simu ya mkononi. Ikabidi atumie simu ya mezani
kumtaarifu Geb kuwa amefika salama kama alivyomuahidi. “Nimefika salama.” Grace akaongea tu mara baada ya Geb kupokea simu
yake. “Mapumziko mema.” Geb akakata simu.
~~~~~~~~~~~~~~
Akaanza
kuwaza sasa. Likizo ile ya siku 30, ataifanyia nini? Tokea yupo chuo mwaka wa
pili, maisha yake yote yalijawa Danny tu. Ni kweli alimganda kila mahali. Na
baada tu yakufunga ndoa, Grace akashika mimba. Akamzaa Fili. Maisha yake yakawa
Danny na Fili. Baadaye wakaja mapacha. Grace hakuwa akijua maisha yake binafsi
bila watoto au Danny. Hajui anatakiwa kufanya nini juu yake binafsi akiwa hana
mtu mwingine wakumfikiria. Swali la nini afanye, likawa mtihani. Afanye starehe
gani ambayo itatunza hadhi yake? Kukaa tu pale chumbani, akajua ndio maisha
aliyokuwa akiishi muda wote huo kabla hajapanda ndege yakumtoa jijini Dar.
“Lazima kufanya kitu cha tofauti.” Grace akaazimia moyoni. “Lakini nini?” Huo ukazidi kuwa mtihani. “Nioge na kubadili nguo, nikakae sehemu wanayouza vinywaji.”
Hakuwahi kunywa pombe, wala hajui ladha yake. Akajua soda tu itamchosha kukaa.
“Sasa kwani mimi huwa napenda nini?” Grace akajiuliza kwa sauti. Tayari
alishasahau hobies zake. Akaoga na kubadilisha nguo, akatoka kwenda
mapokezi.
“Samahani!”
Alimkuta mrembo yuleyule aliyempa chumba, pale mapokezi. “Umebadili na kuzidi
kupendeza!” Grace akacheka. “Asante. Lakini naomba msaada wako.” “Karibu!” Yule
mrembo akamtolea tabasamu. Grace akajisikia huru kuuliza. “Kwanza asante kwa
kunichagulia chumba kizuri. Nimekipenda.” Yule mrembo akacheka. “Nilijua tu
utaridhika. Nikusaidie nini tena?” Akamuuliza Grace.
“Hivi hapa mjini Arusha kuna vivutio gani? Kitu gani kizuri kinaweza kunifaa?” Yule dada akacheka. “Kwani wewe unapenda nini?” Grace akafikiria kidogo. “Nataka kufanya kitu cha tofauti. Wewe nitajie tu vitu vyote, nitachagua.” “Okay. Kama unapenda kutoka usiku, kuna kumbi nyingi tu za starehe. Hata hapa huwa wanakuwa na ‘Live band’. Kila jumamosi usiku huwa wanapiga mziki. Na leo kuna fashion show hapa. Japokuwa nimesikia kuwa tiketi zimeuzwa zote, lakini naweza kukutafutia ticket, uingie tu uone kinachoendelea. Huwa inakua nzuri sana. Kunakuwa na mambo mengi, huwezi kuchoka.” Grace akaona hamna chakupoteza. Kwanza itakuwa ni hapo hapo hotelini.
“Lakini
pia huwa tunakuwa na magari ya Safari. Yanapeleka watalii mbuga za wanyama.
Unaweza ukapenda kwenda na huko.” “Kumbe afadhali nimekuuliza. Nilisahau tu, lakini
hata yule dereva taksii aliniambia. Afadhali umenikumbusha.” Wakacheka. “Naona
vitu vyote nitafurahia sana tu. Huwa nasikia Tanzania kuna simba, tembo na
wanyama wengine. Lakini sijawahi kuwaona kwa macho. Ni heri na mimi niende
nikashuhudie kwa macho.” “Sawa. Ungependa kwenda lini?” “Kwa kuwa leo nitakuwa
huko kwenye fashion show, najua naweza nikachoka. Kesho nitataka kupumzika.
Jumatatu naona itakuwa siku nzuri.” “Ungependa nikutafutie hoteli kabisa?”
“Mbona hiyo ingenisaidia zaidi! Kama sio usumbufu, nitafutie kila kitu, ili
nisisumbuke.” “Hii hoteli ina tawi huko huko mbugani. Kwa hiyo itakupa huduma
ya gari na hoteli pia.” “Usisahau chumba kizuri.” Wakacheka.
“Basi
wewe jiandae, saa 12 jioni kuwa tayari. Tiketi yako itakufuata huko huko
chumbani.” “Asante. Swali la mwisho. Lakini usinichoke.” “Wala usijali. Nipo
kukusaidia dada yangu.” “Haya. Vipi chakula? Mnakuwa na vyakula vizuri?” “Kwa
swala la chakula, hapa umefika. Tunaye mpishi mzuri sana. Utapenda vyakula
vyake. Nenda kajaribu tu.” “Sawa. Tutaonana baadaye. Unaitwa nani tena?” “Beka.
Wengi wananijua kwa jina la Beka, lakini ni Rebeka.” “Nashukuru Beka. Baadaye
basi. Natumaini nitakuona tena.” “Jumatatu nitakuwa hapa. Kesho napumzika.”
Wakazungumza kidogo, akamuelekeza ilipo sehemu ya kulia chakula. Grace
akaelekea kule.
~~~~~~~~~~~~~~
Grace
aliingia pale mgahawani, akakuta wamekaa watu wengine. Akatafuta meza ya peke
yake, akakaa. Muhudumu akamfuata kwa haraka. Mpaka Grace akashangaa. Wala
hakusubiri sana na wakati walikuwepo wateja wengine. Akavutiwa na huduma za
pale. Akaagiza juisi ya maembe. Wakati anasubiria juisi iletwe, akavutiwa na
ule mgahawa, akaamua kuangaza macho.
Alipogeuka
ili kuangalia kona ya upande wa kulia kwake, macho yake yakagongana na Man.
Grace akashituka sana. Akarudisha macho mezani kwake. Man alikuwa amekaa kwenye
meza moja na mwanamke aliyeonekana nadhifu sana. Jinsi alivyovaa, alionekana
mdogo kwa umri wake. Hakuwa na mwili mkubwa. Na vijana wengine wawili. Wazi
walionekana wapo kwenye mazungumzo ya kikazi.
Grace
akafikiria kwa haraka, akaona aondoke pale. Akasimama. “Grace!” Man akasimama
na yeye kwa haraka akamfuata. “Huna sababu yakuondoka hapa kwa ajili yangu.
Nakuahidi sitakusumbua. Kaa tu ule.” “Hapana. Mimi nilikuja tu kupaangalia.
Napita.” Grace akajitetea kwa sauti ya chini. “Wewe sio muongo Grace. Tafadhali
usianze kwangu. Nakuahidi wala hutahisi uwepo wangu. Wewe kaa tu. Furahia
chakula na kinywaji ulichoagiza. Sitakughasi.” Grace akawa amekamatwa.
“Please.” Man akamsihi. Bila kujibu, Grace akageuka na kurudi kukaa. Man
akaondoka.
Hakujua
kikao cha Man na wenzake kiliisha saa ngapi! Au kama walihamisha kikao au la.
Lakini alipomaliza kinywaji chake, akitaka kuondoka, akagundua hawapo. Ndipo
alipopata nguvu yakuagiza chakula. Alipenda kila kitu. Akakubaliana na Beka
kuwa wanampishi mzuri. Akaamua kurudi chumbani kwake.
“Man anafanya nini hapa? Kwa nini tuna..” Grace akanyamaza. Akaamua kujipumzisha mpaka jioni
ili aende kwenye fashion show. Akapitiwa na usingizi. Akalala kama mfu. Uchovu
wa miaka yote, mbali na kero za Danny na Sara. Kuwaza wanachofanya chumba cha
pili, kelele za watoto, hata hakugeuka, akalala mpaka saa 11 jioni.
Alipoamka
tu, akakuta tiketi yake chini ya mlango. Akajua muhudumu ndio ameweka pale. “Mbona hawajanidai pesa?” Grace
akajiuliza. “Labda wataniwekea kwenye
bili yangu yote!” Grace akaendelea kujiandaa. Akatoa viatu virefu.
Akajicheka kwanza. Hakuwa amevaa viatu virefu kwa muda mrefu sana. Kwanza
alikuja kunenepa sana. Mwili ukawa unamlemea. Akaanza kuumia kila akivaa viatu
virefu. Akaamua kuacha kuvaa viatu virefu. Akaja kuzaa watoto. Unaenda wapi
ukiwa umevaa viatu virefu na watoto watundu kama wa Danny? Grace akahamia
kwenye viatu vya chini kwa miaka mingi tu.
Akajaribu
kutembea navyo pale chumbani. Akaona bado anakumbuka kutembelea viatu virefu.
Akavaa gauni ambalo ni refu lakini halina mikono wala mikanda. Linaishia
kifuani. Na umbile la Grace, hutakaa ukaacha kumwangalia. Lilikuwa jeupe lenye
pindo nyeusi zilizopita kifuani na kwenye V iliyoanguka chini ya kiuno nyuma.
Akavaa na viatu vyenye nyeupe na nyeusi, tena mchongoko mbele. Akavaa na hereni
ndeni kama cheni. Zilishuka mpaka mabegani. Hata Danny angemuona asingeamini
kama ni Grace, mkewe. Rangi yake nyeusi, ikapendeza kwenye lile gauni jeupe.
Akajipulizia pafyum.
“Sijui nimezidisha?” Grace akajiuliza wakati anageuka kwenye kioo. “Wasije wakasema nimepania bure!” Grace
akacheka. “Lakini si wamesema ni Fashion
show? Nipo sawa bwana!” Grace akatoka.
~~~~~~~~~~~~~~
Akatembea
kwa kunyata mpaka kwenye lifti iliyomshusha mpaka chini. Akatoka kwenye lifti.
Akatembea kwa mwendo wa taratibu ili asianguke. Aliona vile watu walivyokuwa
wakimwangalia. Akacheka moyoni. Akajua hakika amependeza. Akaendelea kusogelea sehemu
ya mapokezi ili kumtafuta Beka amshukuru. Alimuona kwa mbali kijana ambaye kwa
mgongoni tu, alionekana mrefu vyakutosha. Alivaa nadhifu. Suti nyeusi iliyokuwa
imemkaa vizuri sana. Alikuwa amesimama pale mapokezi, na kuegemea pale
akionekana amezama kwenye kitu alichokuwa akifanya. Moja kwa moja Grace akajua
atakuwa na yeye anaelekea kwenye hiyo tamasha.
Bado
Grace alikuwa akitembea taratibu kusogelea mapokezi, na yule kijana alionekana
amezama kufanya hicho alichokiinamia, hakugeuka. Grace alikuwa akimuona kwa
nyuma tu. Alifika mpaka pale mapokezi, akagundua mrembo aliyekuwepo pale si
Beka japo sare zao za kazi zilifanana. “Samahani. Namuulizia Beka.” Grace
akaongea na huyo mrembo aliyemkuta pale mapokezi na yeye alimpokea kwa tabasamu
zuri. “Beka ametoka saa 10. Hatakuwepo hapa mpaka siku ya jumatatu. Ataingia
tena asubuhi. Lakini hata mimi naweza kukusaidia. Karibu.” Grace ni kama
akaishiwa nguvu.
“Asante.
Lakini nilitaka kumshukuru na kumpa zawadi kidogo. Amenisaidia sana tokea
nafika hapa. Ila kwa kuwa nitakuwepo mimi mwenyewe mpaka hiyo jumatatu,
nitamkabidhi tu yeye mwenyewe. Asante.” “Karibu. Ila Umependeza sana. Utafikiri
na wewe upo kwenye fashion show!” Grace akacheka. “Asante. Ni Beka huyo ndio
amenishauri niende.” Akagundua yule kijana aliyekuwa ameinama pale kaunta,
pembeni yake, anamwangalia muda wote na kumsikiliza. Akaona na yeye amgeukie.
“Man!” Grace
akashituka sana. Akajikuta anaita jina lake taratibu kwa mshangao. Man
akamgeukia vizuri kama na yeye ameduaa akimshangaa yeye. Wakaangaliana kidogo
wote wasijue waseme nini, Grace akaamua kuondoka. Kabla hajapiga hatua nyingi
akasikia “Waw!” Man ameshangaa kwa
sauti. Hakugeuka. Grace akaendelea kutembea kuelekea ulipo ukumbi. Moyoni
akacheka. Akajua hata Man amevutiwa. “Kumbe
bado sijazeeka!” Grace akajisifia mawazoni, akacheka.
~~~~~~~~~~~~~~
Haya tena, mambo yameanza
kuchanganya kwa mapacha wa Mama G.
-
Geb anaanza kupokelewa na Nanaa
mwenye mimba ya Malii.
-
Grace kaondoka nyumbani, kwa
kuchoshwa na familia yake, ametua jijini Arusha, na Man naye yupo.
Mama G amebakishwa peke yake
akilia. Anamwita Mungu yupi? Ameshaanza kuvuna alichopanda.
-
Hata Magesa ambaye ni kama mtoto
wake, anamkataa. Liv ambaye ndiye wajina wake pia hamtaki.
-
Amevunja ndoa ya mwanae bila kutarajia. Aliyokusudia kumfanyia Nanaa, yanamrudi
yeye mwenyewe kwa mwanae Grace.
Mpaka lini, kwa umbali gani? Hakuna ajuaye. Lakini amebaki na kilio cha Grace
akiwasimulia yanayoendelea kwenye
maisha yake.
-
Udhalilishwaji wa hali ya juu
anaopitia kwa wakati ule.
-
Watoto wake aliokuwa
akiwahangaikia pia hawana muda naye! Ilibaki ikimuumiza sana si mama G tu, hata
Geb pacha mwenzie.
Geb anaumizwa zaidi kuona
anayofanyiwa na Danny sasa hivi, hasa baada ya kumvumilia Danny mpaka hapo
alipofikia.
Usikose kujua kitakachoendelea
kati ya Grace & Man.
-
Man ni nani? Kwa nini na yeye
yupo pale hotelini? Aliyosema Geb yanatimia kwa dada yake?
-
Geb & Nanaa! Geb amemwambia
Nanaa akimkubali tu, atamkimbiza kanisani haraka sana.
§ Na mtoto wa Malii!?
-
Itakuaje kwa Nanaa ambaye ni
mgonjwa na bado amebeba mambo mengi sana moyoni? Amekiri kuwa mambo
yamebadilika sio kama zamani kukubali kila kitu kwa haraka. Ameomba apewe muda.
Wa nini? Kwa nini?
-
Mama G!?
o INAENDELEA…
0 Comments:
Post a Comment