Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Ni Wangu! - Sehemu ya 55. - Naomi Simulizi

Ni Wangu! - Sehemu ya 55.

 Geb akaendelea kuwaza wakati hajui aseme nini pale mbele ya Nanaa “Inawezekana ni kweli mimi ni mbinafsi?” Akajiuliza nafsini mwake. “Kweli inawezekana huwa sijui kusimama kipindi cha kujaribiwa kwangu. Sijawahi kusimama hata mara moja! Kwanza alipotukuta uchi mimi na Liz, Nanaa alikasirika sana. Badala yakumsaidia, nikakasirika na kumfukuza hata nyumbani.” Geb akakumbuka hiyo ni mara ya pili anampokonya mtoto. Mwanzoni alimpokonya Liv. Huyo mtoto akalia sana, kama hivi. Akaweza kurudi kwa mama yake.

Hilo nalo Nanaa akasamehe. Akaja kwa msichana wake wa zamani. Frida. Alimuacha Nanaa, akaishia kufugwa mpaka jela. Napo Nanaa akasamehe wakarudiana. Ikaja kesi ya Malii tena. Geb akakumbuka kila kitu taratibu. Mara zote aliishia kuharibu vibaya sana. Akaanza kujichukia nafsi yake, na kuchukia hasira kali alizonazo, zinazomfanya anashindwa kuzitawala. Zikipanda hasira anashindwa hata kufanya maamuzi sahihi.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Bado ninaamini Mungu atakusaidia utatoka salama Nanaa. Uje ulee watoto. Namuomba Mungu akusaidie. Nafikiria maisha ya watoto bila wewe! Haijalishi nani yupo na hao watoto. Haitakuwa kama ilivyo sasa hivi. Hii hali ya utulivu hapa. Haijawahi kutokea tokea tuondoke na watoto. Kwa muda wote huo sikuwahi kurudi nyumbani nikakuta wanangu wapo tu kama hivi walivyo sasa hivi. Najua ninachoongelea Nanaa. Nimeishi hapo. Hakuna anayeweza kutuliza hawa watoto kama wewe mwenyewe.” Geb akaendelea.

“Japokuwa Magesa anaumwa, hakuwa akikufahamu kama mama yake na tupo hospitalini, lakini upo utulivu mkubwa sana kwetu sisi wote watatu. Ulituona siku mbili tu zilizopita Nanaa, mimi na wanangu wote tulikuwa hoi! Katika ujinga na mapungufu yangu yote, na mimi najua umuhimu wako kwenye maisha yangu na wanangu. Naweza nikawa sijakwambia vyakutosha au sijawahi kukwambia. Labda kila neno linalotoka kwangu ni tatizo, lakini naomba uniamini katika hili Nanaa, unajua kuishi na kina Magesa wote. Una jinsi yako yakuleta utulivu fulani katikati yetu. Japokuwa tunakuwa na ukorofi wetu, mapungufu yetu, lakini unauwezo wa kuwa katikati yetu na kututuliza na kuweka amani.” Geb akaongeza.

“Kwa hiyo wakati ukimfikiria Jimmy, naomba utufikirie na sisi. Fikiria jinsi utakavyotuacha.” “Wewe unaye mwanamke Geb. Maisha yako yanaendelea, kamwe hayajawahi kusimama.” “Mwanamke gani huyo unayemzungumzia Nanaa!?” “Sara.” Nanaa alienda moja kwa moja kwenye pointi. Geb akameza mate. Nanaa akamuona vile alivyobabaika.

“Ni kweli Sara aliletwa nyumbani. Lakini Nanaa, sijawahi kupata hata dakika moja ya mazungumzo na yule binti. Na wala mama hakuwahi kuzungumza na mimi juu yake. Mimi nilijua ni binti aliyekuja pale kumsaidia mama swala la watoto, basi. Sikujua kama ameletwa kwa ajili yangu na wala hapakuwa na mazungumzo yanayohusu mimi na yule binti. Nilichokuwa nikijua au nikiambiwa juu yake ni pale nilipokuwa nikielezwa juu ya watoto. Labda naambiwa wametoka na Sara pamoja na Jeri, wamepelekwa labda kwa Grace au wanakutana na Danny sehemu ili wacheze na watoto wao. Nikaona anahusika na watoto wangu na wa Grace kwa karibu sana. Kuwapeleka sehemu kucheza na kuwazungusha. Ukaribu ukawa wake, mama na Danny sababu ya watoto. Na ndio kitu alikuwa akipenda kufanya Sara. Au ndio kitu niliona anafurahia kufanya. Atapenda kutayarishiwa watoto, nakuwapeleka sehemu za starehe. Lakini si vinginevyo. Sidhani hata kama anajua majina yao. Lakini Nanaa, nakuapia kwa Mungu wangu. Hata kama angependa watoto na watoto wangempenda, nisingemuoa yule binti wala sikuwa hata na mawazo yakutafuta mwanamke. Kwanza nilikuwa nimeumia moyoni.” Geb akaendelea.

“Swala la mapenzi nilikusudia kuachana nalo kabisa, nilee wanangu tu. Nimejiona hata mimi sistahili kuwa na mwanamke. Wewe ni shahidi. Nimeweza kufanikisha kila kitu kwenye maisha yangu, isipokuwa mapenzi. Nimeweza kupanga mambo makubwa na magumu, nayakafanikiwa. Lakini kila linapokuja swala la mahusiano! Nimekuwa nikifeli kwa asilimia zote. Nimeamua kuacha niangalie kile ninachoweza kufanya kwa wanangu tu. Basi.” Nanaa hakujibu kitu.

“Kwa hiyo Nanaa, kama sio wewe kulea hawa watoto, hakuna mwanamke mwingine atawalea. Nitabadili maisha yangu. Nitajitahidi mimi mwenyewe kulea wanangu. Kwa shida na raha. Watakuwa tu. Lakini nakuomba katika mipango unayomfikiria Jimmy na sisi utufikirie. Mimi na wanangu. Hata kama sio mimi, basi Liv na Magesa. Usikate tamaa nakufikiria kufa. Naomba tubaki kwenye maombi yakuomba Mungu akuongezee miaka. Uje ulee watoto wote watatu kwa pamoja.” Nanaa akamwangalia. “Naleaje watoto wako na wa Malii pamoja, Geb!?” Geb akatulia kidogo.

~~~~~~~~~~~~~~~

Ameshapitishwa kwenye kashi kashi za maisha. Akiwa na pesa zake na jumba au majumba ya fahari, lakini alikuwa hapati usingizi. Alikasirika mpaka hasira zikamuisha. Nyumba haikuwa na amani. Watoto wanalia mchana na usiku! Akasalimu amri. Muda mchache aliokuwa na Nanaa pale, aliweza kuwatuliza wanae na yeye.

Liv alisharudisha kicheko. Nywele alizokuwa hataki mtu aziguse, mama yake aliweza kumsuka vipande viwili kama minyoosho. Liv akawa amependeza, msafi na ameshiba vizuri. Japokuwa Geb alikuwa akilala hapo hospitalini, lakini alishapata utulivu wa namna yake. Kula vizuri, kulala, na akaweza hata kunyoa ndefu. Magesa hakuwa akilia tena. Garama ya kumpokea mtoto wa Malii ili aishi na Nanaa, ilikuwa ndogo sana kulinganisha na haso za maisha alizokuwa akizipata bila Nanaa.

~~~~~~~~~~~~~~~

Nanaa akajua amemkamata pabaya sana. Geb mtu wa hasira na kutunza mambo moyoni. Sio mwepesi kusamehe na kuacha mambo yapite tu hivi hivi. “Ilimradi awe anazaliwa na wewe, haitajalisha, Nanaa.” Nanaa Hakutegemea. Akabaki na mshangao. “Mungu akipenda, kesho tutaruhusiwa. Nataka kuchukua apartment tena. Pale pale kwenye ile sehemu tuliishi mimi, wewe na Liv kwa muda mpaka tukahamia pale kwenye ile nyumba tuliyoikimbia.” Nanaa akanyamaza.

“Na mimi nataka muda wakutosha na hawa watoto. Nakukaribisha. Kuwa huru kuja kuishi kwa kipindi chochote unachotaka. Hata kama ni miezi hii michache iliyobaki kabla hujaenda kujifungua. Njoo upate muda na watoto. Hakuna atakayekusumbua. Hakuna atakayekuingilia. Ni wewe na watoto tu.” Nanaa akavuta pumzi kwa nguvu. Akajigeuza upande mwingine. Akamvuta Liv karibu. Akambusu. “Nampenda mama.” Liv akaongea kwa sauti ya kitoto akiunganisha maneno. Lakini mama yake akaelewa. “Na mimi nampenda sana Liv.” Liv akafurahi sana akambusu tena mama yake.

~~~~~~~~~~~~~~~

Alimlisha Liv vizuri. Akampeleka bafuni kuoga ili alale. Wakati yupo bafuni, Geb akaingia na kiti. Kaa hapa wakati mimi namuogesha. Nanaaa akajikonyeza mwenyewe. Geb alikuwa akimjali mno, mpaka akashangaa na kucheka nafsi mwake. Akaanza kumuimbia Liv huku anaogeshwa na baba yake. Liv alikuwa akicheka mpaka Geb alikuwa akicheka. Aliimba kitoto, ungependa kumsikiliza. Tamaa yakuishi maisha marefu ili amuone binti yake akikua ikaanza kumwingia. Geb akamtoa bafuni, akamvalisha na kumuweka kitandani. Wakaomba naye, wakamwambia alale.

Nanaa akabaki akifikiria. “Unawaza nini?” Geb akavuta tena kiti karibu ya Nanaa. “Liv atakuwa dada mrembo!” Wakacheka. “Ameanza kuongeza uzito. Angalau kanatizamika.” “Ni Imani tu Geb. Siku tatu haziwezi zikaonyesha tofauti.” “Kweli Nanaa! Ndivyo ulivyomkuta huyu mtoto hivi? Kwanza alikuwa hata hacheki.” Nanaa akanyamaza.

Unauwezo wakuendelea kumfanya awe na furaha.” “Mambo yamebadilika Geb. Majukumu yameniongezekea. Sio kama zamani nakuwa na uwezo wakuamua kwa haraka. Sasa hivi inabidi kuwa makini zaidi ili nisiwaumize wanangu wote, zaidi Jimmy ambaye hana kimbilio ila mimi.” “Sasa ni nini unafikiria?” Nanaa akawaza kidogo.

“Sasa hivi nina biashara inayoweza kuniingizia vijipesa kidogo. Ninaweza kuweka juhudi kwa hii miezi michache iliyobaki. Nikakusanya pesa zakunitosha mimi na Jimmy kipindi cha uzazi, au kama sitakuwepo, basi dada Fifi na Jimmy. Kuishi na dada Fifi kutanisaidia kufanya naye hiyo biashara nakumuweka karibu zaidi na mimi pamoja na Jimmy. Kuliko eti leo niondoke kwenye maisha yake, nije kutokezea siku yakujifungua! Nimwachie tu mtoto! Hatapata uzito kama nikiishi naye pamoja. Akaweza kupata muda na mimi pamoja na Jimmy. Wakawa wanazungumza kama hivi hata kabla hajazaliwa. Sijui unanielewa Geb?” Geb akabaki kimya.

“Moyo wangu unatamani sana nije kuishi na nyinyi ili nipate muda na wanangu. Itakuwa faida kwao lakini hasara kwa mdogo wao, Jimmy. Wao wanalo kimbilio, wewe. Lakini sio Jimmy. Lazima kumfikiria ndio maana wakati ule nilipoona mnanikatalia watoto wangu, nikaona ni heri nife naye tu huyu. Hapakuwa na sababu yakuishi.” Geb akanyamaza.

~~~~~~~~~~~~~~~

 Kama ni ahadi alishaziongea zote kwa Nanaa. Kumfuta machozi, lakini akaishia kumuacha akilia. Kumpenda mpaka kifo. Lakini alimuacha akijua ni mgonjwa na wala hakuonyesha kujali. Akakumbuka alipomfungia nje pindi alipojifungua Liv. Tena akalazimishwa na mama yake amfungulie, akaingia akiwa amelowa damu.

          Alipomzalia mtoto wa pili, akabakwa ndani ya nyumba yake. Akiwa anajua alimtoa hospitalini akiwa bado mgonjwa. Daktari alimsisitizia lazima atumie dawa na arudi kumuona. Geb alikumbuka vile alivyomuacha akilia huku amempigia magoti sakafuni akimlilia asimuache, lakini aliondoka na kumuacha. Tena aliondoka huku akimshutumu kwa uongo. Akakumbuka maneno makali sana aliyomwambia. Zaidi hataki tena kuiona sura yake maishani. Akafunga misaada yote, na kumuacha peke yake kwenye jumba alilofanyiwa unyama mbaya. Tena watu wote waliokuwepo siku ile wakisikia na kujua anachofanyiwa bila hata kupewa pole na yeyote yule kati yao. Kana kwamba walikuwa wakishangilia asulubishwe. Ameyataka mwenyewe. Lipi amebakiza kwa Nanaa?

~~~~~~~~~~~~~~~

Nanaa akajinyanyua taratibu. “Nashauri leo ulale hapo kitandani Geb. Jipumzishe mgongo.” Geb akasimama. “Unakwenda wapi tena?” “Nataka nikatembee kidogo ndipo nirudi kulala. Najihisi kuchoka viungo. Pia nataka nizungumze na dada Fifi. Nataka kumtia moyo kwenye biashara yetu. Ni mwepesi sana kukata tamaa. Japo sipo naye kikazi, basi angalau kumtia moyo na kumsaidia kimawazo. Sasa hivi yupo peke yake. Anapika na kusambaza. Atakuwa anachoka na atakata tu tamaa. Sasa nikimpigia simu hapa ndani, tukaanza kuzungumza, tutaamsha watoto wote.”  Geb akatulia kidogo.

Nanaa akavuta simu yake. “Nilikuwa nina wazo Nanaa.” Nanaa akamgeukia. “Yeye awe anapika, halafu Jeri awasaidie kusambaza.” Nanaa akacheka kidogo. “Mbona unacheka?” “Mawazo yako ni mazuri sana Geb. Na yote yanaonyesha kutoa suluhu zuri sana, lakini huwa ni kwa muda mfupi sana. Nakushukuru sana. Lakini hapana. Nimeamua kuanza kujiwekea msingi wa maisha yangu. Nijijenge kuanzia chini. Ni kwa shida. Lakini naamini nitafika tu. Kama nisipojikaza sasa hivi nikaanza kitu chakueleweka na chakudumu, nitampa shida Jimmy na historia ya maisha yangu haitakaa ikabadilika. Itajirudia daima. Na sitakuwa na wakumlaumu.” Nanaa akaendelea.

“Nimekuwa nikiishi kwa kusaidiwa kana kwamba mimi ni mjinga, Geb!” “Usiseme hivyo Nanaa.” “Kweli tena Geb. Niambie ni muda gani umepita tokea nimalize chuo? Nina sababu gani ya msingi ambayo inanifanya niwe hivi nilivyo? Yaani hata kitanda changu cha kulalia mimi mwenyewe, sina! Yaani hapa unavyoniona, hata nguo au chupi ninazovaa ni zilezile ulizokuwa ukininunulia wewe. Sijawahi kutengeneza pesa yakununua hata kijiko changu!” Nanaa akajicheka.

“Niambie Geb, kama sio ulemavu wa akili ni nini? Sina tofauti yeyote na wewe au na watu wengine kama dada yako. Kwa nini mimi niwe hivi na wengine wawe na maendeleo? Hivi unajua wenzangu niliomaliza nao chuo walipo? Wengi wameolewa. Yaani wana waume zao. Wametulia makwao na watoto wao. Japo sio matajiri, lakini maisha ya familia yanaendelea. Niangalie mimi. Mpaka hivi sasa ndio nahangaika kuanza maisha na nina watoto. Sina rafiki wala familia. Yaani ndio nahangaika na dada Fifi, mtu niliyekutana naye hospitalini! Ndio amenipa mpaka mashuka yakujifunika. Niambie ukweli Geb, kama mimi sina tatizo ni nini?” Nanaa aliongea taratibu lakini kwa makini.

“Kama ningekuwa nimetulia na nipo makini. Kuanzia kwenye mipango yangu, nina uhakika wanangu wasingeteseka hivi. Nimeleta watoto duniani mimi kama mama nikiwa sijajipanga na wala sijielewi nataka nini. Nimekuwa nikijiegemeza kwa watu na kwenye mapenzi ambayo hayakuwahi kuwepo tokea mwanzo. Lakini nimekuwa kama mjinga kufungia macho hata yale Mungu aliyokuwa akinitumia ishara kunishitua na kunieleza sehemu ninazoegemea sio sahihi. Ni dhaifu sana.  Lakini nimekuwa nikishupaza shingo. Lakini sasa hivi ndio kama maisha na majanga yaliyonipata yamenifungua macho.” Geb kimya.

“Nimejiambia kila siku Mungu atakaponijalia kuamka au kunitoa kitandani, lazima nijikumbushe mimi ni nani. Nipo wapi! Na nani! Ninakwenda wapi! Najiambia mimi mwenyewe Nanaa, ndio ninauwezo wakubadili maisha yangu. Sio mtu mwingine. Hata kama Mungu anataka kunisaidia, hawezi mpaka mimi mwenyewe nitende kazi pamoja naye. Sitatoka hapa nilipo Geb, kama sitabadilika. Hii misaada ambayo unanipa leo, kesho ukikasirika unanipokonya au kuniacha, haitanipeleka kokote! Nawatesa tu wanangu na mimi mwenyewe.” Kama aliyemwagiwa maji, Geb akatulia kimya.

“Najua natakiwa kutafuta msambazaji. Naelewa sana. Lakini bado biashara haijakuwa. Lazima nilipe garama zote sasa hivi nikiwa mgonjwa na wanangu wakinihitaji kwa kuwa Mungu alinipa nafasi nyingi sana, nikachezea. Inanilazimu kulipa garana Geb. Nimekusudia sitarudi huko tena. Hata ikinilazimu mapumziko yangu yawe kwenye daladala nikiwa natoka sehemu moja kwenda nyingine. Iwe kusambaza maandazi au kuwaona wanangu. Nitafanya hivyo. Kwa kuwa nimeyataka mimi mwenyewe. Ila najua haitakuwa kwa muda mrefu sana. Nitatoka hapa, na wanangu watapumzika siku moja. Hata kama sasa hivi nitawapa lisaa limoja kila siku, lakini namuomba Mungu azidi kuyaongeza hayo masaa. Biashara ikue, niongeze wafanyakazi ili niweze kuwa na muda na watoto wangu.” Nanaa akaongeza.

“Kwa hiyo Geb, nakushukuru sana kwa kutaka kunisaidia. Lakini hapana. Ila naomba unisaidie kwa upande wa watoto tu. Nakusihi sana, niruhusu kuwa na wanangu pale nitakapoweza. Sitakusumbua uwalete au utume dereva. Nitawafuata popote walipo, kasoro nyumbani kwenu wewe na mama yako, hapo hapana ili nisizidi kuwakera. Kama siku nyingine utaniruhusu hata nilale nao kwangu, nitakushukuru sana. Ukitaka niwalee mimi, pia nitakushukuru mno. Ila tu, nitaomba unisaidie matumizi yao. Sitataka pesa yako hata shilingi. Hilo msiwe na wasiwasi nalo. Nitakuwa nikikuandikia mahitaji yao, au unaweza hata kumtuma Jeri awe analeta hivyo vitu nitakavyohitaji vya watoto ili kuhakikisha au muwe na amani na pesa yenu. Kwangu unakaribishwa muda na wakati wowote ule. Iwe mchana au usiku, njoo ili uje kuona wanao. Nakuachia wewe uamue Geb.” Nanaa akatoka. Usingizi wote ulimpaa Geb. Akabaki kimya pale chumbani na watoto wake akiwaza.

Maisha Baada Ya Kuruhusiwa Magesa Hospitalini.

Kesho yake Magesa akaruhusiwa kutoka. Geb alipoenda kulipia, Nanaa akakusanya vitu vyote akaviweka kwenye mifuko ila kwa kutenganisha. Vitu vya watoto wake, akaviweka sehemu moja, na vyake akaviweka kwengine. Geb akarudi. “Upo tayari?” Geb akauliza. “Naona nimewafungashia kila kitu chenu kipo tayari. Lakini naona kama mimi mtaniacha. Bado dada Fifi ana kazi kidogo. Amesema atakuja baada ya kama nusu saa. Nina mizigo mingi. Vyombo alivyokuwa akileta. Na jana alisahau kuchukua. Siwezi kupanda navyo kwenye daladala. Ngoja nikusindikize na watoto kwenye gari, nitarudi huku juu, kumsubiria. Nesi ameniambia hata nikitaka kulala, naweza kujipumzisha tu.” Nanaa akamalizia kwa kucheka.

“Kwa hiyo nitakuwa sawa tu. Twende nikusindikize kwenye gari. Nikusaidie kubeba watoto.” “Twende wote niwapeleke.” Nanaa akatulia kidogo. “Unamaanisha na watoto?” Nanaa akauliza akiwa hajamuelewa Geb. “Unafikiri nitafanyaje Nanaa? Magesa ameruhusiwa akiwa bado anatakiwa aendelee na matibabu. Namuona ameshaanza kukuzoea. Ukimshika wewe, anatulia kwa haraka. Siwezi tena kwenda kumuanzishia maisha mengine huku ni mgonjwa. Umeona kwa siku chache tu jinsi Liv alivyobadilika? Mtoto wangu amerudisha kicheko na anakula. Amerudi kuwa msafi, angalau anatizamika. Acha mimi ndio nilipe hiyo garama, kwa kuwa nimeyataka mimi mwenyewe. Twende tu. Nitakuachia watoto na nitasaidia kwa kadiri nitakavyowezeshwa na Mungu.” Nanaa akajawa furaha isiyo kifani.

“Nakushukuru sana Geb. Nakuahidi nitawalea watoto vizuri. Na kwangu utakuwa hujawapoteza wanao. Muda na wakati wowote, wewe njoo tu kuwaona. Hata ukitaka kuzungumza nao kwenye simu, piga muda na wakati wowote ule.” Geb hakujibu kitu katika lile.

“Ngoja nianze kuweka mizigo kwenye gari. Halafu nitakuja kukuchukua wewe na watoto. Ila Liv usimbembe. Nitakuja kumfunga kwenye gari yake, halafu nimsukume mwenyewe. Usiwabebe hao.” “Sawa.” Nanaa alitamani kuruka ruka kwa furaha. Lakini baada ya Geb kuondoka, akakumbuka chumba chake. Akakaa.

~~~~~~~~~~~~~~~

Anawaweka wapi wale watoto wa Geb, waliozoea kulala huku AC ikiwapuliza. Yeye anapepewa na feni na wakati mwingine anaongeza nguvu yakujipepea na karatasi usiku joto linapokuwa kali. Watoto waliozoea kulala kwa kujinafasi, tena kwenye vitanda vyao! Wasiwasi ukamwingia.

~~~~~~~~~~~~~~~

Geb akamkuta anatuma ujumbe. “Upo tayari?” Geb akamuuliza. “Nilikuwa namtumia ujumbe dada Fifi, asije tena hapa. Ila anipangie pale ndani. Nimemwambia nakwenda na watoto. Halafu nataka akaninunulie feni na kapeti ndogo. Nitandike pale chini ili kama Magesa akitaka kutambaa, asipate shida. Halafu..” Nanaa akaendelea kumueleza mipango mingi anayotaka kufanya. Geb alijua tu itamgarimu pesa. Lakini kwa kuwa alishakataliwa kutoa msaada. Akaamua anyamaze.

Akatafuta sehemu akakaa. Akabaki akimsikiliza. Nanaa alipoona hapati uungwaji mkono, akarudi kwenye simu yake na kuendelea kutuma ujumbe huku wazi akionekana ameshapaniki. Geb kimya. Akamaliza. “Nipo tayari. Tunaweza kwenda.” Geb akasimama. Kwa kuwa alishaingiza vitu vyote kwenye gari, akambeba Magesa mkono wa kushoto, Liv akawa anamsukuma kwenye kigari chake, mpaka kwenye gari.

Walipoingia tu kwenye gari, Fifi akapiga simu. “Hivi wewe Nanaa unajua hali yetu ya kiuchumi lakini?” Nanaa kimya. Akatamani kupunguza sauti ya simu Geb asisikie. “Nanaa!” “Nitakupa pesa dada. Wewe tumia ulizo nazo.” “Tulizungumza nini jana juu ya kupanua biashara? Jana tulipanga mambo mengi. Na yote ni mazuri. Ukasema tuache kutumia pesa kwa kujinunulia vitu ambavyo havitatuingizia faida. Ukanitajia pesa uliyonayo benki. Tukaweka mipango. Ukaniambia nikubali ile tenda kubwa ya jumamosi. Nimetoka sasa hivi kuzungumza na mama yake yule bibi harusi. Nimemwambia kama tulivyozungumza.  Kuwa tutaweza kuwalisha wote kwenye hiyo sherehe yao. Leo asubuhi unataka kapeti, sijui feni na mambo mengine. Huo uwezo tunautoa wapi, mdogo wangu?” Nanaa kimya.

“Tenda tushakubali. Tunatakiwa kuanza kununua vitu. Chupa zakuwekea chai zinahitajika tano. Haya, tukakubaliana tununue yale mabakuli makubwa ya chuma cha kuwaka yenye mifuniko yake ya kioo kwa ajili ya kuwekea vitafunio. Ili tukiyapanga mbele ya watu yaonekane masafi na yavutie. Haya, tukasema na miko mizuri yakupakulia. Wewe mwenyewe ukasema unataka ya chuma, ili iendane na sinia. Seti za vikombe, sahani na vijiko. Tumepanga vizuri. Tumeandika. Ukaniambia niwapigie, niwaambie tutawalisha kwenye kitchen party yao. Sasa mbona tena unageuka?” “Ninakuja na watoto dada.” Nanaa akaongea kwa upole.

“Wewe kwa sasa huna uwezo wa kulea hao watoto Nanaa! Nimekutana na wanao. Mazingira mliozalia hao watoto na maisha wanayoishi sasa hivi, hawatapaweza hapa uswahilini. Kuna mbu na nzi kila wakati! Joto kila wakati! Hamna nafuu mchana wala usiku hapa. Utakuja kuwaua wanao Nanaa! Hao watoto hawatapaweza hapa. Hata nikisema nikutolee mizigo yote hapo chumbani kwako, bado hapatoshi.” Geb aliendelea kukanyaga mafuta, kuitafuta Kawe.

“Sasa nitafanyaje dada? Nataka kuwa na wanangu.” Tayari Nanaa alishaanza kulia. “Wewe mwenyewe ulinifundisha kuwa kila jambo lina wakati wake, Nanaa. Huu sio wakati wa kuchukua hao watoto. Ungekuwa umewazaa huku kama wale wangu, hapo sawa. Au kama huyo Jimmy, hapo sawa. Lakini sio kuwahamisha kutoka kwao, ukawaleta hapa! Kwanza unakumbuka tunakopikia lakini? Tunapikia nje. Moshi wote unaingia ndani ya vyumba. Wewe mwenyewe mwenzangu na mimi ulikuwa unalalamika na kuniambia niwe nahamisha jiko kila pande ya huku uwani, ili uweze kulala ndani. Sasa ushafikiria hao wanao lakini?” Kimya. Nanaa akabaki akifuta machozi.

“Unataka kuleta balaa bure! Mrudi tena hospitalini. Wewe jiachie tu. Omba kwenda kutembelea wanao. Kila unapoweza, nenda. Mimi nitakuwa nakusaidia kazi za hapa ndani, wewe uwe unaenda kutembelea wanao. Hata kama utakuwa unapika vitu vigumu usiku, ili asubuhi uwe unaenda kwa wanao, pia ni sawa. Mimi nitahangaika na kusambaza. Lakini sio kuwaleta hapa hao watoto. Jiachie tu mdogo wangu. Mambo yetu yakiwa safi, tunawafukuza wale wapangaji mle ndani, tunahamia kwenye nyumba kubwa. Hapo ndipo tunaenda kuwafuata watoto wa uzunguni.” Nanaa akacheka kidogo.

“Sikutanii Nanaa. Nakwambia ukweli. Umenielewa mdogo wangu?” Nanaa kimya. “Basi ulivyombishi wewe!” “Nafikiria dada.” “Unachofikiria nini sasa?” Kimya. “Wewe Nanaa?” “Nataka kutumia muda niliobakiza na wanangu dada. Magesa bado mgonjwa.” “Ndio garama watakayolipa hao watoto, Nanaa. Wanasema, ‘tembo wakigombana, manyasi ndio yanaumia’. Sasa garama yakutokuelewana kwenu nyinyi wazazi, ndio wanalipa watoto wenu sasa hivi. Lazima wataumia tu. Hamuwezi kuepuka hilo. Watailipa hiyo garama kwa uzima na ugonjwa. Maumivu yake watayasikia mchana na usiku. Mbaya huyo mkubwa ambaye mlimlea pamoja. Anauelewa mkubwa sana Liv. Anajua kabisa kila kinachoendelea. Heri kaka yake. Yeye ataweza kuuguzwa na yeyote na akawa sawa tu.” Nanaa akazidi kulia, Fifi akakata simu.

Akasikia gari linaegeshwa pembeni. “Naomba usilie Nanaa. Sisi tunayemtaka ni wewe. Sitajali mazingira utakayotaka kuwaweka watoto. Ilimradi wewe ukiamua wawepo hapo, watakuwepo tu.” “Ni kweli pale hapatawafaa watoto Geb. Nenda nao tu. Mimi nirudishe kwangu. Nikajipange, halafu nikiweka mambo sawa, ndipo nitakutafuta tena.” “Basi usilie. Naamini huo ndio uamuzi unaokupa amani. Tulia. Sitaki Liv aamke, akukute na hali hiyo. Itakuwa ngumu zaidi kumuacha. Nimeshawatesa wanangu vyakutosha. Nimekubali kulipa garama yeyote ile. Naomba Mungu anisaidie, kuwasaidia watoto wangu. Naamini watakuwa sawa tu.” Nanaa akajaribu kutulia, Geb akatoa gari.

Uswazi.

Alimuelekeza Geb, mpaka wakafika. Kweli nyumba ya mbele ilionekana ni kubwa tu, na nzuri ya kawaida. “Unaweza kuegesha gari hapo nje tu. Nitamuomba dada Fifi aje anisaidie kushusha mizigo.” “Tunaruhusiwa kuingia ndani?” Geb akauliza kiungwana. “Kabisa Geb. Karibu. Nilifikiri unataka mrudi nyumbani ili mkapumzike.” “Hamna neno. Tutakaa kidogo.” “Ila kuna joto!” Nanaa akamtahadharisha. “Hamna shida.” Geb akafungua mlango, Fifi naye akatoka.

Wakasaidiana kushusha mizigo, wakaingia ndani. Fifi alisafisha vizuri chumba cha Nanaa. Ni kweli kulikuwa na joto, na nzi nje. Ndani Fifi alijitahidi kutoa nzi. Pakawa hamna nzi wengi. Pasafi ila padogo. Geb akamuacha Liv kwenye kigari chake akiwa amelala, akamuweka Magesa kitandani kwa mama yake. Yeye akakaa kwenye kochi refu la mbao lililokuwepo hapo hapo chumbani. Akatulia. Nanaa akababaika vyakutosha. Kilikuwa chumba kimoja, kilichojazwa mizigo yake yote. Ila kulikuwa na  choo na bafu humo humo ndani. Sakafu ilikuwa yakawaida tu. Haikuwekwa hata marumaru.

Watoto wamelala, Geb amekaa kwenye kochi. Hamna tv, wala radio. “Kuna feni. Sijui niwashe au watoto watakohoa?” “Labda usiwaelekezee.” Geb akajibu taratibu. Nanaa akawasha feni, akaelekeza upande mwingine. Akabaki akifikiria. “Mbona hukai?” Geb akamuuliza. “Nataka kupika kwanza. Najua njaa zitakuwa zikiwauma.” Kimya. “Liv akiamka atataka kula. Ngoja niende nikawashe mkaa. Nitarudi. Unataka soda au maji?” “Mimi nipo tu sawa. Asante.” Geb akajibu.

Mtihani ukawa pakuwashia moto. Akajua moshi wote na harufu ya mafuta ya taa vitaingia ndani alipo Geb na wanae. Fifi akabaki akimtizama. Akahamisha jiko kulia na kushoto bila kuwasha. “Nahofia moshi utaingia ndani!” Nanaa akajiongelesha. “Si ndicho nilichokuwa nikikwambia mimi? Mwanaume wa watu hajabisha. Yupo ndani na wanae. Jasho linakutoka mwenyewe!” “Usiseme hivyo bwana. Nisaidie dada.” “Mbona hamna shida. Wewe nipishe hapo nifanye vitu vyangu. Dakika 20 tu chakula kipo mezani.” “Sasa utaniamshia wanangu kwa harufu ya mafuta ya taa.” “Wala si kuwaamsha tu. Wataondoka hapa wananuka moshi kama wachoma mishikaki.” Nanaa akacheka.

“Wala hunisaidii wewe!” “Tatizo lako wewe Nanaa mbishi na huyo bwana hapo ndani mjuaji. Basi wanaoteseka watoto.” “Sasa mimi ubishi wangu ni upi?” Fifi akamsogelea Nanaa. “Kinachowashinda kuzungumza mambo mkamaliza na mwenzio ni nini? Jumba limewashinda, mmelifunga, mmekuja kujibana hapa uswahilini sababu ya wote hamtaki kushindwa. Wewe mbishi na mwenzio mjuaji. Wote mmeshika kwenye mpini, watoto wenu kwenye makali!” “Acha kusema hivyo dada!” Nanaa alizungumza kwa sauti ya chini.

“Nanaa mdogo wangu. Maisha ni karata. Ukizicheza vibaya tu, imekula kwako. Nilikwambia tokea mwanzo. Kama Mungu angenipa mimi hata dakika kumi tu na familia yangu, ningezitumia vizuri sana. Fifi huyu unayemuona hapa, nisingekuwa hivi. Hakuna garama. Narudia na nilikwambia Nanaa. Hakuna garama itakayonishinda kulipa ili niwe na familia yangu. Hapa najiuliza hata nikipata mamilioni ya pesa, yana raha gani? Sina mtoto sina mume. Hata nikivaa dhahabu nikawa na magari tisini, havina raha Nanaa. Maisha ni watu.” Fifi alitoa machozi.

“Hujakaa upande wangu ndio maana hujajua ninachoongelea. Niliiacha hii nyumba nikawa nashinda nazurula kwenye majumba ya watu sababu ya upweke. Nanaa, mimi nilikuwa naitwa naringa! Huwezi kunikuta napoteza muda na mtu wakati mume na watoto wangu wapo hai! Kwanza utanikuta wapi na saa ngapi? Sina ujinga na mtu ndio maana watu na wenyewe walikuwa hawanitaki kipindi nilipobaki peke yangu.” Fifi akaendelea.

“Na sio kwamba nilikuwa na ndoa nzuri ya ajabu! Lakini nilikuwa na mwanaume aliyekuwa akijua kujirudi. Na hivi alishanizalisha, na tumetoka mbali, basi maisha yalikuwa yakiendelea. Sikuolewa na malaika, lakini tulipendana sana na Manase. Upendo ulinifunza kuvumilia, kutohesabu na kutojitafutia mambo yangu mwenyewe. Ndio andiko alilokuwa akilipenda sana Manase. Na hakuacha kunikumbusha. Hasa yeye akikosa.” Nanaa akacheka huku akilia.

“Usicheke. Alikuwa akiniudhi, lakini mwenyewe alikuwa ananiambia ni neno la Mungu wala si lake. Akawa ananiambia nikishaona kunatabia yakuhesabu hesabu kila wakati, ujue hapo hamna upendo. Nyinyi bado wadogo sana Nanaa. Hivyo hivyo watoto wenu bado ni wadogo. Wanawahitaji sana. Wewe unaweza kuolewa hata na hilo tumbo lako.” “Dada wewe!” Nanaa akamfinya.

“Hujaona wanavyohangaika huko maofisini na wewe? Kila tunakopeleka vitafunwa wanakuomba wawe baba wa mtoto wako.” “Wale wana tamaa tu.” “Lakini ndio ujue bado unalipa. Na mwenzio hivyo hivyo. Wote mnaweza kuendelea na maisha yenu, mkapata wenza mkawa na furaha tu. Lakini Nanaa, jua wazi, hakuna atakayeweza kulea watoto wako isipokuwa wewe mwenyewe. Hata baba yao hataweza. Watoto wanaolelewa na baba peke yao, hawafanani na watoto waliolelewa na mama peke yake. Wapo tofauti. Na hiyo imeanza tokea mwanzo wa kuumbwa mwanadamu. Uchungu wa mtoto ni mama. Na haviishi siku yakuzaa tu. Ni mzigo wako huo. Sasa akili kichwani mdogo wangu. Ujue umama ni garama. Tena garama yakukana nafsi. Hatima ya wanao iko kwako. Maneno na tabia yako yakuaga aga eti unaenda kufa, ujue utakufa kweli na uache wanao wanateseka. Shauri yako.” Fifi akataka kuondoka.

“Sasa itakuaje nikija kujifungua? Nataka tuwe wote hapa ili nikijifungua uweze kuwa karibu na Jimmy.” “Unaanza kuishi miezi mitatu baadaye wakati hata leo hujamaliza! Si wazimu huo? Wewe ulizungumza na Mungu akakwambia mimi nitakuwepo hapa duniani baada ya miezi mitatu ijayo?” “Usiseme hivyo dada!” “Niambie Nanaa. Kesho yangu wewe unaijua? Nikianguka kesho nikafa? Mimi nilijua kama Manase atakufa siku ile wakati tulikuwa tukizungumza muda mfupi kabla hajapata ajali!? Unajua mipango niliyokuwa nayo na Manase juu yetu muda mfupi kabla hajafa? Hakuna anayejua linalotokea hata baada ya dakika moja kuanzia sasa. Sasa eti wewe unataka utese watoto wako sasa hivi, kwa ajili ya mtoto unayemtegemea miezi mitatu ijayo! Huo sio wazimu?” Nanaa akanyamaza.

“Yaani hawa ulionao sasa hivi ushindwe kuwalea, halafu ujidai unamsubiria Jimmy ambaye hata hujamshika mkononi! Akizaliwa amekufa?” “Usimtamkie mwanangu mabaya bwana!” “Mimi nataka kukufungua akili, Nanaa. Wewe bado mdogo. Hujayajua maisha mdogo wangu. Unadandia treni kwa mbele. Utakufa siku si zako. Haya mama, mimi njaa inauma. Changamsha mkono huo. Wanao wanaamka sasa hivi. Bwana kakaa ndani. Haya. Ivisha tule.” “Na huo moshi sasa?” Nanaa akauliza.

“Ndio watajijua. Si mama yao kaanza maisha! Tena kayaanza maisha kwa kasi zote. Changamsha mkono sasa.” Nanaa akanyamaza. Alijuta kumsimulia Fifi mkasa mzima wa Geb. Jana yake mara baada ya kutoka kuzungumza na Geb, akatoka kwenda kumpigia simu Fifi, nakumueleza kila kitu, akitaka Fifi awe upande wake. Lakini ameshangaa Fifi amembadilikia! Akaenda kukaa pembeni anamwangalia Nanaa. Baraza lenyewe lilikuwa na jua.

“Watu wanakimbia shida, wengine mnazikimbilia!” Fifi aliendelea kuongea kwa mafumbo. “Ona unavyotokwa jasho hapo juani. Uzuri nimejaza gari yangu mafuta. Ukiangaka tu hapo, nakutia kwenye gari, nakupeleka hospitalini. Wakakuchome chome sindano, halafu nakurudisha hapa.” Nanaa akacheka. “Si mbishi wewe! Basi endelea hapo hapo.” “Njoo unisaidie bwana dada! Kawashe mkaa hapo nje ya geti, halafu uje upikie ndani.” “Sawa. Mimi sikujaliwa ubishi kama wewe. Ila kumbuka hapo nje kuna gari ya baba watoto wako. Na ninawasha moto kwa kutumia mafuta ya taa. Sasa likiwaka moto, ujue chakumueleza!” “Acha kuniogopesha bwana dada! Wewe nenda kawashie huo moto mbali na hilo gari la watu.” “Sawa. Ila ujue nilikutahadharisha.” Fifi akatoka na jiko lenye mkaa, mafuta ya taa na kiberiti.

~~~~~~~~~~~~~~~

Nanaa akarudi ndani. Akakuta wanae wamelala, lakini wamelowa jasho. Geb alikuwa amepandisha miguu juu ya lile kochi, akiwa bado amevaa viatu vyake. Amejilaza na kufunga macho. Nanaa akamuhurumia. Akainama na kumfungua viatu. Akaanza kumtoa taratibu. Geb akafungua macho akabaki akimtizama. “Pole. Nimekuamsha?” “Hapana. Nilikuwa nimejipumzisha tu. Vipi wewe?” “Nipo sawa tu. Nimekutoa viatu ili kupunguza joto. Naona unatokwa na jasho kweli.” “Asante.” Geb akabaki akimwangalia. Nanaa akainama. Geb akamvuta mkono, akaushika.

“Hongera kwa hatua kubwa. Naona umepambana mpaka umepata kwako.” Nanaa akacheka. Akakaa vizuri pale sakafuni wakati Geb amejilaza kwenye kochi. “Mbona unajicheka tena? Kweli mimi nakupongeza.” “Asante Geb. Lakini kila kitu unachokiona hapa ni cha dada Fifi.” “Taratibu. Kila kitu utanunua kutokana na uhitaji. Kama hivi unaona wageni wako tunatokwa jasho, ukipata pesa, unaongeza feni jingine. Taratibu. Huwezi kuwa na kila kitu kwa wakati mmoja.” Nanaa hakuamini kama yale maneno yanatoka kwa Geb. Bado alikuwa amemshika mkono akimwangalia.

“Asante kwa kunitia moyo. Naona na wageni wangu mmekuwa wavumilivu!” Wakacheka na kuwageukia watoto wao. “Unaratiba gani jioni?” “Sina. Mkiondoka, nitakuwepo tu mpaka usiku ndio nianze kuandaa vitu vyakupika.” “Unakumbuka lakini kunywa dawa zako?” “Nakunywa usubuhi na usiku wakati nalala.” Geb akamvuta mkono zaidi. Nanaa akacheka.

“Baadaye jua likipungua, tunaweza kutoka kidogo na watoto?” “Unataka twende wapi?” Nanaa akauliza. “Tukatembee kidogo. Tumekuwa kwenye mazingira ya hospitalini kwa muda mrefu. Kama utaona sawa, tuwapeleke watoto sehemu wacheze kidogo. Hasa Liv. Hajapata muda wakucheza tokea uondoke. Amekuwa ndani tu. Hata ukimpeleka mahali, alikuwa hachezi. Au unafikiri utakuwa na kazi nyingi, hutaweza?” Geb hakutaka kulazimishia.

“Ningefurahi kuwa nao, Geb. Asante.” “Basi baada ya kula. Wakiamka, twendeni.” Nanaa akacheka kwa furaha. Wakabaki wamekaa kimya. Nanaa akainama kama anayefikiria. “Umekata nywele, umependeza.” Nanaa akacheka. “Kweli!?” “Mmmh!” Geb akamshika kichwani. “Alinikata dada Fifi, hapo nje!” “Alikukata vizuri.” Nanaa akacheka kwa aibu kidogo huku akijishika shika. “Ngoja nikamsaidie dada Fifi.” Nanaa akaona atoke tu pale.

Alipotoka tu, akamsikia Magesa anaongea kitandani. Akarudi. “Magesa!” Mtoto alikuwa amelowa jasho kama amemwagiwa maji hapo kitandani. “Vipi baba? Pole na joto.” Akamtoa pale kitandani akampakata. “Amelowa jasho! Kama amenyeshewa mvua! Pole.” Nanaa akaendelea kuongea, Geb akiwa kimya pale kochini. Akamtoa nguo zote akambakisha na diaper tu. “Njaa inauma?” Nanaa akamuuliza mwanae. “Ule kwanza, ndio uoge.” Nanaa akaendelea kuzungumza na mwanae.

Mama yake akamiminia uji kwenye bakuli, akaanza kunywa. “Nilitaka kumuanzisha nyonyo, lakini naona sitaweza.” Geb akacheka. “Huyo hana utani na chakula. Usiposema wewe basi, ujue mwenzio ataendelea kula tu.” Wote wakacheka. Magesa alikuwa akiendelea kula kana kwamba yupo kijiko cha kwanza, wakati ndio amemaliza bakuli la uji. Cheko ilimjaa. Alionekana ni mtoto ambae hasumbui. Ilimradi ashibe. “Naona homa imemuisha kabisa. Amekula vizuri.” Geb akasifia. “Namuonea huruma jinsi anavyotokwa jasho! Halafu naogopa kumuelekezea feni asije kukohoa.” Geb kimya.

“Huyo dada hapo mpaka umtoe. Atalala siku nzima. Na hivi alishiba vizuri kabla hajalala, hataamka.” Nanaa akacheka. “Liv kwa kupenda kulala! Kama wewe Geb.” “Naona mwenzangu amezidi. Huyo hata umuweke sakafuni, atalala tu. Hapo alipo hana habari ya alipo. Mpaka aamke ndio utamuona anahangaika. Kama ni njaa au kwenda chooni. Lakini sio huo muda wake hapo.” Baba yake akasimama, nakumfuta jasho. “Naona nimtoe tu hiyo nguo.” Geb akaanza kumtoa. “Mgeuzie na feni kidogo. Nzi wanamsumbua.” Nanaa akaongeza. Geb hakuchangia.

~~~~~~~~~~~~~~~

Jioni Geb akawatoa. Akawapeleka sehemu ambayo alijua watoto wake wote watafurahia. Nanaa hakuwahi kumuona Geb wa namna hii. Alijawa kicheko. Akawa anacheza na wanae kwa sauti ya juu kabisa. Walikuwa na wakati mzuri sana. Vilijaa vicheko visivyoisha. Liv ndio alikuwa akicheka mpaka anaanguka chini. Geb alikuwa akimkimbiza kulia na kushoto, ilimradi tu mtoto wake acheke na kupata wakati mzuri.

“Naona Magesa wangu na yeye anaona wivu. Amebaki anaruka ruka tu hapo kwenye gari yake.” “Ndio akazane kutembea. Eti Magesa?” Geb akamtoa kwenye gari yake akaanza kumkimbiza Liv huku amembeba Magesa. Magesa alikuwa akicheka kwa sauti mpaka watu wengine walikuwa wakiwaangalia wao, nakucheka. Kila Geb alipomfikia Liv, alitumia mkono wa Magesa kumshika. Wote wawili walikuwa wakicheka sana. Mshikwaji na mshikaji. Magesa na Liv. Mama yao na yeye alikuwa akicheka kama Geb.

Wakapata muda wakula pamoja. Walikuwa wamebeba vyakula vya watoto wao. Nanaa akaagiza samaki wakuchoma na chips. Akataka aletewe kachumbari yenye limao jingi. Geb yeye akaagiza samaki wa kuchoma kama Nanaa. Akataka tango zima. Lisikatwe. Nyanya kubwa moja na ugali. Nanaa akacheka. “Hujabadilika tu?” Akamuuliza. “Nimebadilika mno. Imenibidi kubadilika kwa nguvu. Lasivyo ningekufa kwa njaa. Hapakuwa na wakumringia tena. Mama alikuwa busy na watoto. Mpaka aje anifikirie mimi, ilikuwa labda baada ya siku mbili au tatu. Hapo watoto wananiangalia mimi. Sikuwa na ujanja ila kula kilichopo.” “Pole Geb.” Geb akajicheka na kunyamaza.

Wakaendelea kuwalisha watoto wao wakati wanasubiria chakula chao. Geb alikuwa akimlisha Magesa mpenda kula, Nanaa akamlisha Liv huku wanaongea na kucheka. Chakula chao kikaletwa. Nanaa akaanza kula. Akamuona anajikatia nyanya na tango, akaanza kula bila shida. Hakulalamikia ugali wala samaki. Kweli Geb alibadilika. Akala karibia kumaliza ugali wote. Tango na nyanya vikamwishia. “Nimwite akuongezee?” “Hapana. Inatosha. Nimeshiba.” Akakusanya sahani zake, akatulia. Alikuwa akila na kisu na uma, kwa hiyo hakuhitaji kunawa.

Muhudumu alikuja na bili yao. Nanaa akaiwahi. “Acha mimi nitalipa.” Geb akamuwahi. “Ngoja tu mimi nilipe.” Nanaa akaendelea kusoma huku ananawa. Muhudumu akaondoka na vyombo, akisema atarudi kuchukua pesa. “Nanaa! Mimi nitalipa.” “Acha tu mimi nitalipa.” Nanaa akakazania. “Kwani unataka kushindana na mimi?” Nanaa akashituka kidogo. “Hapana Geb! Nataka kukusaidia. Umekuwa ukinilipia mara kwa mara.” “Hayo ni mashindano.” “Hapana. Usinielewe vibaya.” “Mimi ndiye niliyekuomba tutoke. Haikuwa kwenye ratiba yako wala bajeti yako. Unaposema nimekuwa nikilipa mara kwa mara, ni kwamba unahesabu. Mimi na wewe tulipofika hatuwezi kulipana tena. Si kwa wema wala kwa mabaya. Hatutaweza hata kidogo. Hatutafanikiwa. Hatujengi, tutazidi kubomoa na kuumiza watoto. Niulize mimi, nimejaribu. Najua matokeo ya unachotaka kufanya, Nanaa. Ni maumivu matupu.” Geb aliongea kwa utulivu.

Nanaa akaweka ile bili chini, akamsogezea karibu. “Sio katika hili tu Nanaa. Katika kila kitu. Naomba kuanzia sasa na kuendelea fanya maamuzi yako ukifikiria watoto zaidi. Mimi nipo radhi uniadhibu kadiri upendavyo. Lakini sio watoto.” “Sikuadhibu Geb.” “Unaniadhibu Nanaa. Unaniadhibu kwa mabaya niliyokutendea tokea mwanzo nakufahamu, mpaka sasa. Jana uliniambia. Lakini najua ninastahili hayo yote. Lakini Nanaa, nakuomba ufikirie watoto wetu. Tafadhali sana.” Nanaa akanyamaza.

Muhudumu akaja, Geb akalipa. “Turudi nyumbani ukanywe dawa, upumzike.” Hawakuwa mbali na nyumbani kwa Fifi. Walienda Kawe Club. “Nikitoka kusambaza mzigo wa kesho, nitakuja kukuona na watoto. Ni sawa?” Nanaa akamuuliza Geb wakati wapo njiani. Safari hii akasema ‘kukuona na watoto’. Na yeye Geb akasikia ametajwa. Geb akavuta pumzi na kuzishusha taratibu. Akanyamaza kama anayefikiria.

“Nitajitahidi kuwahi kabla watoto hawajaamka. Halafu nitakaa nao mpaka hata jioni. Ndio nitaondoka. Unaweza hata kwenda kazini ukaniachia kwa siku nzima.” “Nikichelewa kurudi je? Maana sijakwenda kazini zaidi ya siku 3.” “Hamna shida. Wewe kuwa huru tu. Nitakusubiri mpaka urudi Geb. Kama kuna vitu vyakupika, naweza kupika nikiwa kwako, baada ya watoto kulala. Kisha nikarudi  navyo nyumbani tayari kwa kesho. Usiwe na wasiwasi.” Geb akamtizama.

“Hiyo ‘usiwe na wasiwasi’ unamaanisha au unaongea tu kama sentensi nyingine yeyote.” “Namaanisha Geb.” “Basi ujue nina wasiwasi Nanaa. Nina wasiwasi wa afya yako. Ambayo niliipuuza sababu ya hasira. Nina wasiwasi sijui itakuaje kabla na baada ya kujifungua kwako. Madhara yote hayo najiona mimi ndio nilikusababishia.” “Hapana Geb! Usifikirie hivyo.” “Niambie kwa nini Nanaa. Kwa nini? Mimi ndiye niliyemuomba daktari akuruhusu urudi nyumbani. Nikapewa masharti ya jinsi yakuangalia hiyo presha yako isipande tena na dawa. Kesho yake nikakuacha. Leo daktari ananiambia madhara yakutokufuata masharti na kutokutumia zile dawa, kumepanua moyo wako. Wewe mwenyewe una wasiwasi hudhani kama utaishi. Niambie Nanaa, naachaje kuwa na wasiwasi? Hata kama nina roho mbaya ya namna gani, nawezaje kwenda kulala, nakukuacha na hali hiyo?” Nanaa hakutegemea kama ndicho anachojisikia Geb.

“Halafu kwa vile nilivyokutenda vibaya, watoto wale wale ulikuwa ukiwalilia, unapata nafasi yakuwa nao, unashindwa! Upo radhi kuacha mtoto mgonjwa, ili tu kuwa mbali na mimi.” Nanaa akashituka mpaka akamgeukia Geb. “Sio kweli Geb!” “Sasa ni nini? Mtoto huyo huyo uliyekubali kutoa maisha yako ili azaliwe, leo ni mgonjwa, haujali, unamuacha akalale bila wewe! Kweli nimekuudhi Nanaa na umenichukia mimi na watoto wangu.” “Hapana Geb. Nahisi nikuchanganyikiwa tu. Naona mambo yamekuwa mengi na yote yananiangalia mimi.” “Kwa hiyo hivyo unavyofanya ndio njia pekee yakutatua hayo mambo mengi?” Nanaa akageukia dirishani. Akanyamaza.

Wakafika mpaka nyumbani kwa Fifi. Wakabaki wametulia ndani ya gari. “Geb!” Nanaa akaita. Geb akamwangalia. “Naomba nishauri kitu.” Moyo wa Geb ukapasuka. “Nataka kumuomba dada Fifi kama tunaweza kugawana vitu vya kupika. Ili hata nikiondoka na nyinyi, niwe napika huko huko. Asubuhi nakutana naye mahali. Tunagawa hizo oda, na kuwapelekea wateja. Unafikiri ni wazo zuri?” Geb akavuta pumzi kama amepata aghueni. “Hata kama tutakuwa tunabadilishana naye, ili asichoke. Unafikiri ni sawa? Halafu nimpe yeye nafasi ya kwanza yakuchagua ni nini anataka kutengeneza.” Nanaa akaendelea.

“Litakuwa wazo zuri sana. Utakuwa ukiendelea kujiingizia pesa na watoto hawataendelea kuteseka.” “Ila siku kama ya jumamosi ambayo tunakuwa na tenda kubwa kama kitchen party, itabidi kulala kwangu. Kwa kuwa tunakuwa tunachelewa kutoka na ninakuwa nimechoka sana.” Nana akaanza tena. “Naomba tufanyie kazi wazo la kwanza, kwanza. Tafadhali Nanaa.” “Sawa. Basi kesho nitakuja na jibu lakueleweka. Au nikizungumza naye, kama bado itakuwa nimapema, nitakutumia ujumbe. Ni sawa?” “Si sawa.” Geb akajibu kwa haraka kama aliyekuwa akisubiri aulizwe. Nanaa akashangaa.

“Si umesema nikazungumze na dada Fifi!?” Nanaa akauliza kama asiyeelewa tena. “Ndiyo. Na sisi tunakusubiri hapa.” “Geb!” Nanaa akashangaa. “Au ulikuwa humaanishi?” “Namaanisha. Lakini nahitaji muda wakujiandaa. Nijue nabeba nini na nini naacha!” “Utahitaji kujiandaa usiku kucha?” Nanaa akanyamaza. “Sikuharakishi. Ila kama utataka usiku kucha, basi tuingie tukalale mpaka kesho.” Nanaa hakuamini. “Kwamba na wewe ulale kwenye kile chumba!?” “Si niliyataka mwenyewe? Ndio garama yakulipa hiyo. Twende.” “Hapana Geb. Sio sawa kwa watoto.” “Kwa hiyo ni sawa kwa Liv kuamka asubuhi aanze kukulilia? Na ni sawa kumuacha mtoto mgonjwa?” Nanaa akaona kila kitu kinamgeukia yeye.

“Basi ngoja nikazungumze naye, nakuja.” “Sawa.” Wakati anashuka, Liv aliyekuwa akisinzia huku anaangalia cartoons zake akashituka sana. “Mama beba!” “Nakuja Liv. Nisubiri.” Liv akataka kutoka kwenye kiti huku analia. “Beba mama. Beba!” “Nisubiri Liv. Nakuja sasa hivi, sikudanganyi.” Liv akazidi kulia. “Hawezi kukubali. Ngoja nimtoe hapo kwenye kiti chake. Atembee mwenyewe, umshike mkono, uende naye tu. Usimbembe.” Geb akatoa wazo. “Haya nyamaza mama. Nyamaza twende wote.” Liv akaendelea kulia mpaka akatolewa kwenye kile kiti, akaenda na mama yake ndani.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Umerudi nao tena? Hawakuachii hao! Hata ushupaze shingo vipi. Unao hao.” Nanaa akacheka. Fifi alimpokea na maneno. “Njoo Liv mwanangu. Njoo kwa mama mkubwa.” Liv akacheka huku anajificha kwa mama yake kama kawaida yake. Nanaa akakaa na kumpakata. “Sasa inanibidi niende dada yangu. Naomba usijisikie vibaya.” “Mbona mimi nakuelewa Nanaa. Tena mimi ndio ningekuwa wewe, hata nisingechelewa.” “Lakini mimi sio kwamba narudiana na Geb. Hapana. Narudi kwa ajili ya wanangu tu. Tushaharibu sana. Ni ngumu kuja kuaminiana na kuishi tena kama wapenzi. Kama ni ahadi, tushapena zote tumeshamaliza mimi na Geb. Hatuna jipya. Heri tulee tu watoto.” “Watu wanakosa na watu wanamapungufu yao Nanaa. Hutakaa ukapata mwanaume mkamilifu. Wanatofautiana vijimambo tu. Huyu atapungua katika hili na yule lile.” “Mmmh!” Nanaa akaguna.

“Usigune Nanaa. Huyu bwana anakupenda mdogo wangu. Kitendo cha kuja kujilaza hapa kwenye joto na nzi, eti ili awe na wewe, wakati ameacha jumba la maana! Sio kitu kidogo.” “Hakuwa hapa kwa ajili yangu dada, ni kwa kuwa wanae wananililia.” “Naona wewe umeamua kufanya maisha kuwa tu magumu. Na sijui shida yako ni nini!” Fifi alisikitika.

“Mimi nawajua wanaume dada. Nishadanganywa vyakutosha. Achana na hayo mambo. Naomba tuzungumzie biashara yetu.” “Unahangaika kulisha wanaume za watu wakati wa kwako hata hujamshibisha! Tulia Nanaa wewe.” “Nataka pesa dada. Nimeshazungumza naye, hana neno kwa sisi kuendelea na biashara. Tujipange tu. Leo unaweza kupika hiki, na mimi nikapika kile. Tunakutana mjini, asubuhi na mapema. Tunawatengenezea wateja wetu oda zao. Au unasemaje?” “Wazo zuri. Lakini naomba tuliza mawazo Nanaa. Hizi pesa huwa hazitoshi.” Fifi akasisitiza.

“Sasa ulitaka niache kabisa! Nitaishije dada yangu? Halafu ikitokea nakuachia Jimmy, mtafanyaje wakati tutakuwa tumepoteza wateja wote?” “Kwanza ujue hii biashara ni yako Nanaa. Mimi sasa hivi ukiniambia tuache, naacha nahamia kwenye miradi yangu ya zamani.” “Dada!” Nanaa akashangaa. “Kweli tena Nanaa. Mimi nakupika wapi na wapi!?” “Sasa utafanya nini?” “Nilikwambia tulikuwa tunafanya biashara ya kuku. Niliacha sababu ya kuomboleza.” Wote wakacheka.

“Dada Fifi wewe! Yaani mimi siku ile unajiliza pale hospitalini nikajua umefiwa jana yake au hata majuma mawili! Heee! Kumbe miaka!.” “Bwana mimi nimefiwa.” “Acha bwana dada!” “Si ndio nimeacha sasa. Namsubiria Jimmy wangu, nilee.” “Hayo ndio maneno. Lakini tenda ya watu tuliyochukua lazima tuitimize. Tusiwe matapeli.” “Hamna shida. Nimekwambia mimi nakusikiliza wewe. Ila usiache mambo ya wanao, sababu ya pesa. Shukuru Mungu umepata pakuweka kichwa leo na kula, basi fanya ya leo. Usiharibu leo, kwa ajili ya kesho. Ukijenga msingi mbaya, hata kama utaweka gorofa zuri la namna gani juu, ipo siku itakupasukia tu. Kuwa makini.” “Nimekuelewa dada yangu. Basi ngoja nichukue nguo baadhi, ila kesho kutwa nakuja tulale hapa, ili tujiandae na hiyo tenda ya jumamosi.” Fifi akacheka.

“Sasa unacheka nini?” Nanaa akauliza huku anasimama. “Hivi ulisema wanaitwa kina nani tena?” Fifi akauliza kwa kejeli. “Kina nani?” “Huyo mwanao na baba yake.” “Kina Magesa?” “Ewaaah! Hao kina Magesa wamekuganda, huthubutu kurudi hapa. Hata kama utapata tenda ya ikulu, hawatakuachia.” “Nitawapanga dada, ili nipate kijipesa changu.” “Sawa mama. Tutakuona. Ila ujue mwenzio naanza kufufua biashara yangu.” “Usinikatie tamaa mapema bwana. Vuta subira.” Nanaa akaingia ndani kuchukua baadhi ya vitu alivyojua angehitaji.

 ~~~~~~~~~~~~~~~

Huku nyuma Geb alishatafuta sehemu ya kwenda kuishi na familia yake kwa muda wakati wanajiweka sawa. Akabahatika pale pale maeneo ya Msimbazi centre, lakini apartment tofauti. Akazungumza nao. Kwa kuwa alikuwa akifahamiana na mwenye apartment, na alishaishi hapo kwa muda, hakupata shida kukamilisha mambo yakuhamia usiku huo huo.

Awamu Ingine Tena.

Walifika hapo ilishakuwa usiku wa saa tatu. Liv na mdogo wake walishalala. “Itabidi kuwafuta, ili niwabadilishe nguo. Liv amejaa michanga kweli.” Geb aliongea wakati wanaingia ndani. “Nikusaidie yupi?” “Wewe ingia kuoga, upumzike tu. Nataka kukuona umelala kabisa Nanaa. Ulishakunywa zile dawa?” “Tayari. Najisikia uchovu!” “Nenda kaoge ulale.” Kulikuwa na vyumba viwili. Akajua kimoja nilazima kitakuwa cha watoto, na kingine? Akaweka mizigo yake kwenye chumba ambacho Geb aliweka mizigo ya watoto. Geb alimuona. Hakuongea chochote. Akatoka na taulo, akaenda kuoga bafu la nje ya hicho chumba. Akatoka ameshavaa nguo za kulalia, akaenda kujilaza kwenye kochi wakati Geb anabadilisha watoto.

Alipomaliza, akamfuata pale sebuleni. “Ndio umeshalala?” “Nitalala sasa hivi. Najisikia uchovu.” “Sasa kwa nini ulale hapo?” “Nimeona nikuachie wewe kule chumbani. Mimi hapa pananitosha tu. Usiwe na wasiwasi. Nenda kaoge na wewe upumzike.” Geb akapiga magoti pembeni ya pale alipojilaza. Akavuta mkono wa Nanaa, akaanza kuomba. Aliomba taratibu, lakini Nanaa alimsikia baadhi ya maneno. Kisha akasema ameni. “Usiku mwema Nanaa.” “Na wewe. Ila nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuwa na watoto wangu.” “Karibu. Ukitaka kitu chochote usiku, usiache kunigongea.” “Nitafanya hivyo.” Akaenda chumbani kwake, akamtolea shuka. Akamfunika vizuri, Geb akaondoka.

 ~~~~~~~~~~~~~~~

Maisha ya pale kwenye apartment yakaanza. Kesho yake Geb hakwenda kazini. Wakashinda hapo wakicheza na watoto. Vilijaa vicheko siku nzima. Watoto walipolala mchana, wao walibaki wakiangalia tamthilia na Nanaa kusinzia kidogo. Siku ya kwanza ikapita, ya pili siku ya ijumaa. Geb pia hakwenda kazini.

Nanaa akashangaa anamfuata jikoni. Yeye aliamka alfajiri ili kupika vyakula vya wanae na Geb. Geb naye akawahi kuamka. “Ndio unaenda kazini?” “Nataka kujifunza jinsi unavyopika uji.” Nanaa akacheka sana. “Usinicheke bwana! Najifunza.” “Haya. Lakini ndio unatakiwa kusimama hapo jikoni mimi nitakwambia kitu chakufanya.” “Haaa! Wewe Nanaa ualimu huo umejifunza wapi bwana? Ndio mwanafunzi nimefika tu, unaniachia kila kitu.” “Kwa kuangalia tu, hutakaa ukaivisha uji hata siku moja. Kila siku utaona rahisi. Lakini siku ukitaka kupika wewe, utaishia kumwaga. Wewe shika mwiko na sufuria uanze kufuata maelekeze.” Geb akakubali. Wakapika mpaka wakamaliza. “Sasa inabidi tule tuonje mapishi.” Geb akacheka. Wakakaa mezani wakaanza kunywa uji aliokuwa amepika Geb. Wote wakapenda.

“Geb!” Nanaa akamwita. “Jioni inabidi kwenda kulala kwangu. Ili tujitayarishe na tenda ya kesho. Kwa kuwa nitachelewa kutoka kwenye hiyo shuguli, nitalala na kesho. Kwa hiyo nitarudi tena hapa siku ya jumapili. Nitajitahidi kufika asubuhi.” Kama aliyemwagiwa maji yabaridi, Geb akapooza mpaka usoni, Nanaa akaona.

“Nahitaji hiyo pesa Geb. Naomba unielewe. Nataka kujifungua Private. Nataka madaktari wote wawili wawepo hiyo siku ya upasuliwaji. Daktari wangu wa moyo na huyu wa wakina mama. Nataka niwe na uangalizi wakaribu kama walivyonifanyia kwa Magesa ndio nataka huduma kama hiyo wakati najifungua Jimmy, ili chochote kikitokea, niwe na watu wakunisaidia kama kipindi namzaa Magesa. Nilishazungumza na yue daktari, akasema ni wazo zuri. Ila ni garama sana. Akaniambia kiasi kilichokugarimu wewe wakati ule wa Magesa. Ni kweli nahitaji kukusanya pesa, Geb. Sikujua kama ilikugarimu kwa kiasi kile! Yule daktari akasema ndio maana nilipata huduma nzuri  na kwa haraka kwa kuwa nilijifungulia ‘first class’, lasivyo ningempoteza Magesa na pengine hata mimi kudhurika vibaya zaidi. Kwa hiyo nahitaji kupambana ili kufikia lengo. Na hivi nitajifungua kwa upasuliwaji, garama ndio kubwa zaidi.” Geb akanyamaza kwa muda.

“Kesho mnahitajika kufika huko kwenye hiyo shuguli saa ngapi?” “Saa 12 ndio wamesema wataanza kula. Lakini tutataka muda wa ziada wakuandaa meza.” “Unajiangalia afya yako lakini?” “Nitakunywa dawa. Naamini kwenye saa 4 usiku tutakuwa tumeshamaliza kila kitu, mpaka kusafisha ili niwahi kurudi kulala.” “Unaenda kuandaa nini hicho ambacho huwezi kuandaa hapa mpaka uwe kule kwa Fifi?” Geb alionyesha wazi kutoridhika. Nanaa akakumbuka maneno ya Fifi.

“Hii biashara ni yangu Geb. Nikizembea mimi, ujue ndio ninaua biashara yangu kabisa. Lazima nijitoe, ili kufanikisha. Hata kama nitaacha kwa muda, lakini nataka nikija kurudi, nisiwe niliacha nikiwa nimeharibu. Nitunze wateja wangu. Dada Fifi amesema ataacha hii biashara. Hapendi kupika kabisa.” “Sasa kama wewe ndio mwenye biashara, mwambie Fifi yeye ndio aje hapa. Alale hapa, mfanye hicho ulichotaka mkafanye huko kwake. Lasivyo wote tukalale huko huko kwake.” “Geb!” Nanaa akashangaa sana.

“Kabisa. Ni aidha yeye aje hapa, au sisi wote wanne twende kule.” Nanaa alibaki akimwangalia. “Mpigie simu mwambie akija aje na kila kitu. Mtapikia hapa na mtaondokea hapa. Kwanza hapa hamtahangaika na maswala ya mkaa. Kuna gesi. Mtapika kwa haraka na hutatuacha kwa muda mrefu.” Bado Nanaa hakuwa ameelewa. “Yaani hapa naona ndio nimefika! Geb hataki hata nitoke dakika moja!” Nanaa akawaza.

“Lakini lazima nitoke jioni kwenda kununua mahitaji, Geb.” “Unataka nini?” Geb akauliza. “Kila kitu nimeandika. Lazima niende leo na kuanza kuandaa baadhi ya vitu mimi mwenyewe.” “Naomba kuona hiyo orodha ya vitu unavyotaka.” Nanaa akasimama, akaenda kufuata simu yake. Akafungua sehemu aliyokuwa akiwasiliana na Fifi. Wakitajiana mahitaji mpaka wakafikia muafaka. Geb akaanza kusoma taratibu.

Wakati anasoma, na jumbe za Zena zikawa zinaingia. Bila kujua nini kinaendelea kwenye simu yake. Nanaa amezama kunywa uji kwa bidii kama mwanae Magesa, Geb anasoma zile jumbe. Akatoka pale kwenye ile orodha, nakuhamia kwenye mazungumzo ya Zena na Nanaa. Akasoma jumbe za mwishoni, akarudi kwenye orodha.

“Sikujua kama bado mnawasiliana na Zena!” “Hakuna jinsi yakumkwepa huyo msichana Geb. Uliponiambia niachane naye wakati ule, nilimfungia mpaka simu zake. Lakini sijui alifanyaje, akajua kama nimem ‘block’ kila mahali. Akatafuta njia nyingine yakuwasiliana na mimi. Ila hanisumbui kwa kuwa nimeshamjua kuwa nia yake nikushindana na mimi. Haniumizi kichwa.” “Sio kweli Nanaa. Zena amefanikiwa kuingia kwenye kichwa chako. Na anakuendesha kwa vile atakavyo.” “Sio kweli Geb!” Nanaa akakataa.

“Pale hospitalini ulipokuwa ukisema wenzako wameolewa, wana watoto, kazi nzuri na ndoa zilizotulia japo hawana pesa nyingi, ulikuwa ukimzungumzia nani kama sio Zena? Maana yeye ndio anakuamsha asubuhi hii na habari za ndoa yake na vile Mungu alivyomjalia mtoto mzuri. Ni asubuhi sasa hivi Nanaa. Hata saa 4 haijafika. Yupo mtandaoni anajisifia kwako. Hiyo familia anayokwambia ni nzuri, Mungu amemjalia, anaihudumia saa ngapi? Yuko kila mahali huko mitandaoni anakutag wewe picha zake na familia yake. Kweli Nanaa?” Kimya.

“Anyway. Naomba turudi kwenye hii orodha. Hivi vitu naona tunaweza kuvigawa kwenye makundi mawili. Vyakula na vyombo. Najua vyombo ungependa kununua mwenyewe ili uchague. Lakini vyakula unaweza kumtuma hata Jeri.” “Hapana Geb. Acha tu nitafanya mwenyewe!” Geb akamgeukia vizuri.

“Ni nini Nanaa!? Unafanya nini? Katika maisha huwezi kufanya kila kitu wewe mwenyewe. Lazima kufika mahali na kukubali kuamini watu ili usaidiwe. Ni siku ngapi nipo na wewe na watoto? Zaidi ya siku 4. Ni sawa?” Kimya. “Nipo hapa na pesa yangu inaingia kama kawaida kwa kuwa nimekubali kusaidiwa. Nisingeweza kufanya kila kitu mwenyewe na niwepo hapa sasa hivi. Unakumbuka kuna kipindi nilikwambia nahangaika kufanya hii biashara iweze kujiendesha bila hata mimi kuwepo kila wakati?” Nanaa akatingisha kichwa kukubali.

“Nimefikia hapo kwa kuwa nilipata muda mrefu wa kuchunguza wafanyakazi wangu. Nikajua mapungufu yao. Nikajua nani awe wapi na akiwa hapo atanifanikishia mambo yangu na kwa kiasi gani. Nimejitengenezea timu yangu. Najua nani anacheza wapi na nimfuatilie vipi. Ndio maana nipo hapa. Nahitaji kupiga simu asubuhi. Wanitumie mipango ya siku. Grace anipe mipango ya siku nzima ili kujua nini kitaendelea kwa wafanyakazi wangu wote leo. Napokea ripoti zangu. Nasoma kwa muda mfupi. Najua kitu gani cha kurekebishwa siku hiyo. Ikifika saa 4 asubuhi, nishajua nini chakuzungumza na nani. Na jioni nipewe ripoti. Nipo hapa na wewe na watoto wangu. Biashara zangu naziendesha mimi mwenyewe, kupitia watu wengine. Bila shida. Lakini kwa kuwa nimekubali kuamini watu.” Kimya.

“Unanielewa Nanaa?” “Nimeelewa ila nilitaka kufanya kwanza mimi mwenyewe kama wewe ulivyofanya.” “Mimi sikuwa mjamzito wala mgonjwa. Sikuwa na majukumu ya watoto kipindi naanza hii biashara. Niliweka mipango yangu kabla hamjaja kwenye maisha yangu. Niliiona siku ya leo, kabla hamjaja kwenye maisha yangu. Ndio maana wakati ule uliniona nalala maporini, nasafiri mchana na usiku. Nafanya kazi kwa bidii ili leo niwe hapa na nyinyi.” Geb akaendelea.

“Nilikwambia ile ramani ambayo baba yangu aliniachia. Niliifuata kwa bidii sana. Tena nilipokupata wewe, ndio nikaongeza juhudi ili hiki ninachokifanya sasa hivi kisichelewe. Namshukuru Mungu nimefanikiwa. Kila kitu kipo kwenye kiganja changu. Elimu yangu ya kompyuta imenirahisishia kila kitu. Nikitaka kujua nani yupo wapi na kama anafanya ninachomlipa kila mwisho wa mwezi, nafungua tu simu yangu. Nawafuatilia bila wafanyakazi wangu wenyewe kujua. Kisha nawapigia simu. Najua na kufuatilia kila kitu nikiwa hapa hapa na wewe. Najua kama pesa yangu imeingizwa benki au kuna mtu anachezea sehemu na huwa najua ikiwa kwenye mkono wa nani kwa muda mrefu, itakuwa hatarini. Najua pesa yangu iwe wapi na kwa wakati gani. Na nikigundua haipo sehemu na muda uliotakiwa iwepo hapo, basi ninajua ni nani wakumpigia simu kwa haraka kuhakikisha inapelekwa kwa wakati huo. Lakini nililipa garama. Na wewe uliona kwa sehemu. Sasa wewe huna huo muda. Lazima utaumiza familia Nanaa. Kubali kusaidiwa.” Nanaa akanyamaza.

“Namuamini Jeri kwa asilimia zote. Nilikwambia habari zake. Jeri ni mwaminifu wa hata ukiacha shilingi sehemu, atakutafuta akupe.  Kwa tabia yake ile, ndio mtu wa pili ninayemlipa mshahara mkubwa mbali na Grace. Na ndio maana leo unamuona anaendesha watoto wangu. Namlipa kama meneja wa kampuni fulani. Lakini utashangaa jukumu alilonalo kwa sasa hivi. Ni Magesa na Liv tu. Hata nimpigie simu saa sita usiku, nimwambie afanye jambo fulani. Nitarudi kulala bila shida. Kwa kuwa najua Jeri atalifanya kwa uaminifu. Na ndio huyo nakupa na wewe umtumie. Sasa najua kwa kuwa mimi umenikasirikia, hutaki kupokea msaada wangu wowote. Umeniziria kila kitu au kila aina ya msaada nitakao kupa. Lakini nakuhakikishia Nanaa, Jeri atakusaidia kama ukiamua kuweka mbali tofauti zetu. Atakuwa msaada mkubwa sana kwako. Na hatakubali kukuharibia kazi. Mtumie kwa ajili yako na watoto. Na kwa kuwa tayari anakukubali, hamtapata shida.” Nanaa akamfikiria Jeri.

“Kweli Jeri ni mwaminifu. Japokuwa alikuwa akinihurumia mimi na Liv, vile tulivyokuwa tukilia. Lakini alisimamia amri yako. Nisimguse mtoto. Alikuwa akinibembeleza huku akiniambia ni amri amepewa, hawezi kuvunja.” Nanaa akakumbuka kilio alichokuwa akilia ili amguse mtoto wake, halafu wakamkatalia. Akaona machozi yanamtoka. Akashindwa kuendelea kunywa ule uji, akaamua atoke kabisa pale ndani. “Unaenda wapi?” “Nitarudi.” Nanaa akafuta machozi nakutoka pale ndani. Alishangaa kitu kimemkaba kooni, akashindwa hata kutembea. Akaamua akae tu hapo nje ya mlango wa ile apartment yao, ajaribu kutulia. Geb akajua ndio maana bado anahasira naye.

Geb Ajieleza Kwa Nanaa.

Akatoka kumfuata. “Nilipoondoka siku ile, sikupanga kukupokonya watoto, Nanaa. Nilimwambia mama lazima upelekewe watoto asubuhi, wakae na wewe kidogo, halafu warudishwe kwa mama, kisha jioni uletewe tena. Wakishiba, warudishwe kulala. Sitaki uchonganishi, lakini nataka unielewe na usinifikirie vibaya Nanaa. Mwanzoni kabisa, kuna siku nilirudi nyumbani mchana nikamkuta Liv analia sana. Nikamtuma Jeri amlete kwako. Tena nikampa mpaka begi lake lile dogo lenye kila kitu. Nikamwambia amwache alale na wewe siku hiyo. Jeri akarudi nakuniambia walinzi walimwambia ni siku ya tatu kujaonekana pale nyumbani. Liv akarudishwa. Nikawa namtuma Jeri aje kukuangalia pale karibia kila siku, ndipo nikaja kupewa jibu la kuwa uliamua kuondoka.” Geb akaendelea.

“Nilishangaa na kuumia zaidi. Nikajiuliza umewezaje kukimbia watoto uliowahangaikia kwa kiasi kile? Hapo nilikuwa sijui chochote kilichokuwa kikiendelea kwa upande wako.” “Nilikuachia barua Geb.” Nanaa akajitetea huku akilia. “Sikupewa. Na Mungu wangu ni shahidi. Nilikuja kujua habari zako kutoka kwa babu Nyundo, yule mlinzi. Tena alikuwa akizungumza na mimi kama vile najua kila kilichokuwa kikiendelea. Mpaka kwamba ulikuwa ukiletewa watoto na hutakiwi kuwashika. Ni yule babu ndiye aliyeniambia. Ndio maana nikajua sababu ya Liv kunichukia mimi na bibi yake.” Geb akaendelea.

“Baada ya yale mazungumzo na yule babu. Na Grace naye akanifuata ofisini na kuzungumza na mimi sana, nikawa sijui chakufanya Nanaa. Sikuwa nimekusudia utengwe na watoto. Ile hasira yote niliyokuwa nimeibeba juu yako, ikageuzwa hukumu, nikawa nashindwa kufikira wala kulala. Ikabidi kuingia kwenye kufunga na kuomba, kutafuta uso wa Mungu. Angalau anitazame kwa upya, anisaidie nijue chakufanya. Maana niliweza kuhisi jinsi tulivyokuumiza. Hata mimi nilikasirika sana Nanaa. Nilitamani kumchukia mama yangu kwa kukutenga na watoto, lakini nikajisuta mimi mwenyewe. Nikajiambia mimi ndio nina makosa. Nilishindwa kusimama kama baba kwa watoto wangu. Na nilishindwa kusimama kama mume kwako. Sikuwa na wakumlaumu. Ila kutubu na kuomba rehema za Mungu.”

“Gafla watoto wote wakanigeuka. Hawanitaki mimi wala bibi yao. Akianza kulia Magesa, ujue Liv lazima ataamka. Na akiamka, hamtaki mtu. Anataka ashike ule mtandio wako tu. Hali wala kunywa. Hataki aguswe na mtu. Akiniangalia ni mara moja, tena ni kama ananilaumu. Hakuna utakachomwambia akajibu ila matendo tu, tena akitaka. Hapo sijui pakukupata wala sijui kama kuna mtu anataarifa zako.”

“Nikaendelea kumuomba Mungu mpaka Jeri akaja kufunguka kwangu. Akaniambia kuwa huo mnawasiliana, unataka picha za watoto. Ndio nikamtuma akwambie uje uwaone watoto na unaruhusiwa kuwashika. Siku anakuletea watoto na kukupa ruhusa ya kuja kuwaona watoto wakati wowote ule, ndio siku niliipata na barua yako. Ilikuwa imefichwa mahali.  Ndipo nikaisoma na kuelewa kila kitu. Sasa nikamwambia Jeri akutafute ili kusisitiza uwe unakuja kuona watoto. Ukawa hupatikaniki.” Geb akamueleza mkasa mzima mpaka walipokuwa wamesimama pale.

“Ni kweli nilikasirika Nanaa. Uliniumiza sana kwa kutoniambia ukweli. Kama vile unavyonijua. Huwa napandwa sana na hasira nashindwa kujizuia. Ila nakiri nilivuka mipaka. Niliongea maneno ambayo yaliletwa na hasira tu. Haikuchukua hata siku nyingi kujutia nilichokuwa nimekiongea kwako nakujua ni makosa. Tena wakati ule ambao unanihitaji. Ukiwa umeumizwa na Malii. Nikataka kurudi. Nikiwa nimejipongeza kuwa angalau katika hasira zangu za safari hii, sikukufukuza. Nilikuacha pazuri, lakini ukawa umeshaondoka Nanaa.”

“Nikaamua kurudisha kukuwekea pesa. Muhasibu akaja kuniambia benki wamempigia simu kuwa cheki zote zimekubali kuingia kwenye akaunti husika, isipokuwa ya kwako. Akaunti yako ilikuwa imefungwa. Nikampa muhasibu namba yako ya simu. Nikamwambia akupigie simu, akuombe akaunti yako nyingine. Akaja kunijibu ile namba nayo pia imefungwa. Hapo nikazidi kukasirika. Kwa kuwa ndio ilikuwa mwanzoni kabisa. Sijajua hata kwa nini uliondoka. Nikakasirika kuona wewe sio mtu wakuvumilia wala kutegemewa. Umeweza kukimbia watoto na kubadili mawasiliano kabisa! Kwa hiyo hayo ndio yaliyokuwa yakiendelea kwa upande wangu.” Nanaa akatulia.

“Simu iliibiwa kwenye daladala. Nililala, kuja kuamka nikawa nimepitishwa kituo, na sina pochi.” Wakacheka kidogo. “Ikabidi hapo hapo kuelekea ofisi za Voda ili kuwaomba wafunge ile namba ili wasiniibie chochote. Nikaomba wanipe namba nyingine. Nilifunga ile akaunti benki kwa kuwa unakumbuka ile akaunti ni wewe uliifungua Geb. Unakumbuka nilishakulalamikia makato wanayonikata kila mara? Ukasema unapenda ile benki kwa kuwa ni waaminifu na unauhakika pesa ipo salama. Sasa nilipoona umekata matumizi, nikajiambia ni heri nifunge ile akaunti kuliko waje wanimalizie vijihela vyote vilivyokuwa vimebaki kwa wakati ule. Ndio nikahamisha pesa zote kwenye ile akaunti niliyokuwa natumia tokea nipo chuoni. Ni rahisi na hawana makato mengi. Na ndio hiyo nataka nikamuongeze dada Fifi ili chochote kikitokea apate zakumsaidia yeye na Jimmy.” Geb akatulia

“Nashukuru kwa msaada unaotaka kunipa wa Jeri.” Nanaa akavunja ukimya. “Kwa hiyo nimpigie simu nimwambie aje saa ngapi?” “Mapema tu. Lakini mimi itabidi nimpigie simu dada Fifi aje anichukue tukanunue hivyo vyombo kama ulivyosema.” “Sawa. Naamini hautachelewa kurudi nyumbani.” “Nitajitahidi.” Wakarudi ndani.

Kulikoungua Mpini.

Wakati Nanaa anametoka na Fifi, Geb akaamua aende kumsalimia mama yake na watoto. Alipofika Liv akakataa kushuka garini. “Twende ukamsalimie bibi.” Akabaki akimwangalia baba yake akiwa amekaa pale pale ndani ya gari kwenye kiti chake. “Twende halafu tutarudi kwa mama.” Kimya. Geb alishakuwa amemtoa Magesa kwenye kiti chake. “Liv! Lazima kushuka.” Geb akamkazia sauti. Liv akakunja uso. “Twende. Na uache kukunja uso.” Liv akanza kutaka kulia. “Haya, shuka hapo.” Liv akashuka taratibu huku ameshakuwa mwekundu. Geb akafurahi amemuweza mwanae.

Wakati wanaingia Liv yupo anatembea pembeni ya baba yake, bibi yao akafurahi sana kuwaona. Akasimama. “Mbona dada amekasirika?” Grace naye aliwaona wakati wanaingia. Na yeye alikwenda kumsalimia mama yake. “Nenda kasalimie.” Geb alimpa amri mwanae. “Bibi chapa.” Liv akaanza kutokwa na machozi. Geb akashituka sana. Yeye na Grace wakamgeukia mama yao. “Mama wewe!” Grace akalaumu. “Nilimchapa mara moja tu. Tena kibao cha matakoni akiwa na diaper.” Geb akakasirika sana.

“Kwa nini ulimchapa, mama jamani?” Grace aliendelea kulalamika. “Nahisi siku hiyo nilikuwa nimechanganyikiwa tu. Wote walikuwa wanalia na yeye akakataa kutoka kitandani. Hata mimi nilishangaa nilivyomchapa. Ni kama nikagutuka. Lakini nilimuomba sana msamaha.” Mama G akajitetea.

“Usingemchapa mama. Ni heri ungenipigia simu mimi mwenyewe nirudi nyumbani nije kumtoa kitandani kuliko kuendelea kumwadhibu mwanangu.” “Kumuadhibu au kumfundisha! Nyinyi mngekuwa hapo bila kuwachapa? Alifanya ukorofi ndio maana nikakasirika. Najua sikutakiwa kumchapa kwa haraka, lakini nilikuwa namfundisha kutii.” Mama G akawa mkali.

“Ungeelewa kipindi wanachopitia kwa wakati ule mama! Ulikuwa ukiwapeleka kwa mama yao, huku hutaki mama yao awaguse! Huoni kama ulikuwa ukiwaadhibu mara mbili?” “Jamani mama wewe! Ulikuwa ukifanya hivyo tena?” Grace alilaumu zaidi. “Jamani nyinyi mnamjua Malii jinsi alivyo Malaya yule mtoto. Nilikuwa nawalinda hawa watoto. Kama Nanaa angekuwa ameathirika, hamuoni kwamba hawa watoto wangeambukizwa pia kila wanapokwenda kwake na kuwanyonyesha? Leo mnanilaumu kwa kuwa kila kitu kipo sawa. Lakini wakati ule kama angekuwa ameathirika, akaendelea kunyonyesha watoto, hakika wote wangeathirika na tungekuwa tukizungumza habari nyingine sasa hivi.” Kimya kwa muda.

“Ila ujue huyo mtoto anaakili kama za Geb, mama. Hasahau. Ndio maana nikawa najiuliza, nini kimetokea kati yako na Liv? Maana alikuwa akikupenda sana. Gafla akawa kila akikuona anajificha.” Grace akaongeza. “Ni hasira tu na nahisi nilikuwa kama nimelemewa. Lakini sio kwamba nilikuwa nawatesa watoto Geb. Nawapenda sana watoto wako, hata nyinyi ni mashahidi.” Geb akanyamaza.

“Nashukuru kwa kuja kuniona.” Mama G akabadili mazungumzo. Bado Geb alikuwa amesimama. Hajui kama akae au aondoke. Mama yake alijua ameshakasirika. “Usingemchapa mwanangu.” Geb akalalamika. “Samahani Geb. Liv, samahani mama yangu. Nisamehe mama. Njoo.” Liv akamchungulia. “Umependeza! Nani amekusuka?” “Mama!” Liv akajibu huku anacheka na kujishika kichwani. “Jamani mama Liv anajua kusuka! Umependeza kweli. Njoo unionyeshe mimi na aunt.” Liv akacheka nyuma ya baba yake akichungulia katikati ya miguu yake. “Njoo Liv kipenzi changu. Njoo.” Grace akamwita. Akamwangalia bibi yake na aunt yake akarudi nyuma ya miguu ya baba yake.

“Nenda kambusu bibi na anti.” Geb akamwambia mwanae. Liv akaenda kumbusu bibi yake na anti yake akarudi kwa baba yake. “Twende dad.” Liv alishafika mlangoni. Wakacheka. “Njoo nikupe zawadi kwanza.” Liv akakataa. “Twende dad.” “Subiri kidogo. Kakae pale kwenye kochi unisubiri.” Liv akatoka, wakabaki wakimtizama wasijue anaenda wapi. Kwa kuwa baba yake alijua anaelewa vizuri, hakutilia mashaka na anapokwenda. Wakamuona anakwenda kukaa kwenye kochi la barazani.

“Japokuwa Liv anaweza asitamke maneno yote kwa ufasaha na mkamuona ni kama hayupo. Au hasikilizi sababu ya ukimya wake, lakini nimekuja kugundua anasikia na kuelewa kila kitu. Chochote mnachozungumza mbele yake, anaelewa na hasahau. Naombeni muwe makini na kila kitu mnachoongea mbele ya Liv. Na sitaki mtu amchape. Mkishindwa kumuelekeza kitu, niambieni mimi mwenyewe.” “Sawa baba. Hata hivyo nilimchapa mara moja tu, tena kidogo.” “Kwa Liv alivyo, anaweza asiwe ameumia kwa kumchapa, ila ile hasira uliyokuwa nayo wakati ule, ukamuonyesha na kuishia kumchapa. Na pengine ulimgombesha kwanza wakati ukimlazimisha afanye kitu ambacho hakutaka kufanya kwa wakati ule.” Geb aliendelea kulalamika.

“Basi baba. Nipe basi mume wangu nimsalimie. Yeye na mimi hatuna ugomvi.” “Lakini hatutakaa sana. Nimepita tu kukuona mara moja.” “Nanaa hajambo?” “Anaendelea vizuri.” Geb akajibu kwa kifupi wakati anataka kumkabidhi mtoto kwa mama yake. Magesa akamng’ang’ania baba yake kama hataki amshushe. “Hee! Wewe Magesa! Yameanza lini!? Hebu njoo bwana.” Bibi yake akamsisitiza. Lakini Magesa akafunga mpaka miguu akimng’ang’ania baba yake, akisisitiza hataki kushuka au kutoka pale kwa baba yake kwenda kwa bibi yake. Wote wakashangaa.

“Wewe Magesa ndio wakunikataa mimi! Yaani umeondoka hapa juzi tu, gafla unajidai hunifahamu!? Hebu njoo bwana.” Yule mtoto akamkataa bibi yake kabisa mpaka kilio. “Basi baba.” Baba yake akambembeleza akamuweka kifuani. Akakaa naye. “Labda kwa kuwa ametoka usingizini.” Geb akatetea.

~~~~~~~~~~~~~~~

Kile kitu kilimuuma sana mama G. Akaumia mpaka watoto wake wakajua. Akabadilika na kuwa mpole sana. Magesa ni kama mtoto wake. Ni kama alivyomtoa Geb hospitalini baada ya kumzaa ndivyo ilivyokuwa kwa Magesa. Alimlea kwa mapenzi yote kama mtoto wake kabisa. Kitendo cha kukesha naye mchana na usiku, kuanzia anazaliwa mpaka siku tano zilizopita ndio anakuja kumkataa, akasikia kabisa ni hasira ya Mungu iko juu yake. Magesa ni mtoto ambaye hakujua mapenzi ya mtu mwingine isipokuwa bibi yake na baba yake. Leo amemkataa! Ilimuuma sana.

~~~~~~~~~~~~~~~

“Vipi familia?” Geb akamuuliza dada yake. “Naona Mungu amenipumzisha na ulezi. Bado Danny anahangaika nao. Utamuonea huruma.” Grace aliongea safari hii akionekana kama amesharidhika. “Mbona sasa unaongea kama jambo la kawaida?” “Sasa nifanyaje Geb? Hebu niambie. Nimeshamuomba Mungu kwa kufunga na kuomba zaidi ya miezi mitano sasa. Heka heka haziishi! Danny kawa kama kapagawa na wale watoto na huyo Sara. Imebaki kushukuru tu. Lasivyo naona nitachanganyikiwa nishindwe kuwa na wanangu pale ninapopata nafasi ya kuwa nao.” Grace alieleza taratibu.

“Kwani wamehama?” “Tupo wote tunaishi humo humo ndani. Tumejaa tele.” Grace aliongea kama kitu cha kawaida. Geb akamtizama kwa kumshangaa. “Mimi napata muda na wanangu kama kawaida. Siku za jumamosi na jumapili ndio anatoka na watoto na mimi napata muda wakufanya mambo yangu binafsi. Hapa nimetoka kutengenezwa nywele na kucha. Nasubiri saa 10 jioni ifike, niende kwenye masaji. Nikakae huko nipumzishe mwili wangu, nirudi nyumbani. Jumapili kanisani. Jumatatu kazini. Tena hivi umeondoka, ndio nafurahia nimepata kitu chakunifanya nisiwaze. Nafuatilia hata yasiyonihusu huko kazini. Ilimradi jioni ifike, nikaone wanangu. Basi.” Grace akaongeza.

“Sasa na wale wadogo?” Geb akauliza. “Danny kapandishwa cheo. Anapesa inayomchanganya, hana ndugu hana pakuipeleka, zaidi yakunikomoa mimi. Kawatoa watoto nyumbani, kawaanzisha shule. Pale pale anaposoma Fili, ndiko wapo wadogo zake. Anamwaga mipesa kama hana akili nzuri. Anatoka na wanae wote asubuhi, anarudi nao jioni. Siku hizi humo ndani kwetu lugha inayozungumzwa ni kingereza tu, kama tupo London!” Grace akaongea kama mazuri. Akacheka, lakini Geb akanyamaza.

Wakakaa kimya kwa muda, kila mtu akiwaza lake. Mwishowe Geb akaona aondoke. Hakukaribishwa hata maji ya kunywa. “Naona sisi tuondoke, tuwahi kurudi kabla Nanaa hajarudi nyumbani.” “Mmerudi kwenu?” Grace akauliza. “Hapana. Sio sasa hivi. Namuacha kwanza. Nimegundua Nanaa anapaogopa sana pale nyumbani. Anaonekana baada ya lile tukio alishindwa kuja kulala tena. Kwenye mazungumzo yake, ni kama hajawahi kurudi kulala kwenye kile chumba tena. Sasa, kwa sasa hivi naona heri atulie pale wakati nikiendelea kumuomba Mungu. Pengine atanisamehe, atataka turudiane. Hapo ndipo naweza kuzungumza naye swala la kurudi nyumbani. Lakini kwa sasa namchukulia taratibu sana ili atulie na watoto na aweze kujifungua salama.” “Umefanya vizuri.” Mama yake akaongea kwa upole.

“Naomba tuombe kabla sisi hatujaondoka.” “Pole. Mnaondoka na njaa! Sikupika, kwa kuwa nipo kwenye maombi. Grace naye amekuja hapa, tukaishia kuomba tu, na mazungumzo.” Mama G akaongeza. “Hamna shida. Naona hamna mwenye njaa hapa. Eti Magesa?” Geb akamuuliza Magesa aliyekuwa amejiegemeza begani kwa baba yake, akiangalia nje.

“Liv!” Geb akamuita. Akaja na kuchungulia. “Njoo tuombe.” Liv akiwa amesimama pale pale mlangoni, akafunika macho na vimikono vyake viwili, kama yupo tayari kwa maombi, akainama. Wote wakacheka. “Njoo ndani bwana!” Baba yake akamwita. “Njoo ukae hapa karibu na mimi.” Akaenda kujificha ubavuni kwa baba yake. Geb akaongoza yale maombi. Alianza kwa kutubu. Alitubu kwa niaba ya kila mmoja wao pale. Akawatakasa mpaka watoto wake, akiomba Mungu awarehemu wote. Aliomba Mungu awabariki na kuwapatia yale yote ambayo pesa na elimu haviwezi kuwapa. Wakaomba wote watatu kwa kupokezana, mpaka wakamaliza. Geb akaondoka na watoto wake.

~~~~~~~~~~~~~~~

Sababu ya maombi ya muda mrefu na foleni barabarani wakawa wamechelewa kurudi nyumbani. Wakamkuta Nanaa alisharudi, Fifi alishaondoka. Liv akamkimbilia mama yake. “Mama!” “Mpaka nimepatwa na hamu na nyinyi! Mbona mmechelewa kurudi? Mbusu mama.” Liv akambusu mama yake na kumkumbatia. “Mmetoka kwa sonara? Naona una hereni na bangili mpya.” Nanaa akamuuliza mwanae wakati Geb anaweka vitu vya watoto chini. “Bibi!” Nanaa akajua wametoka kwa bibi yao. Hapo hapo na yeye akabadilika mpaka Geb akajua.

Kwanza Geb hakumuaga kama atawapeleka watoto kwa bibi yao, nalo likawa kosa lililomuudhi. Amepewa dhahabu wakati yeye hana uwezo huo. Nalo likawa kosa lililomuudhi. “Anawadanganyishia wanangu kwa zawadi ili wanikatae mimi, wamtake yeye!” Nanaa akawaza wakati mwanae akiendelea kumsimulia habari za huko. Akamwambia na auntie yake alikuwepo, ila Fili hakumuona. Akamuelezea pia kuwa walimuomba Mungu kwa pamoja. Na yeye akaomba pia.

Geb alimuona wazi amekosa raha. “Naomba nimshike kaka.” Akimaanisha Magesa. Magesa akaenda kwa mama yake. Wakaanza kuzungumza pale wote watatu. Yaani Nanaa na wanae. Akajilaza kabisa kwenye kochi wanae wakawa wamemlalia huku akizungumza nao. Geb alijaribu kuingilia kwenye hayo mazungumzo akaona yeye anapewa majibu mafupi mafupi tu. “Vipi huko, mlifanikiwa?” Geb akauliza. “Ndiyo.” Nanaa akajibu bila hata kumtizama. “Jeri alikuletea vitu vyote unavyotaka?” “Ndiyo.” Akajibiwa tena kwa kifupi. “Nilidhani Fifi atalala hapa leo ili msaidiane kazi.” “Atakuja kesho asubuhi.” Geb akaona anyamaze kwanza. Hapakuwa na maongezi ya ziada.

Wakalisha watoto na kuwaweka kitandani baada ya kuomba nao. Nanaa alishakuwa amepika mapema tu, akaoga kabisa. Akachukua mashuka yake chumbani akarudi kujilaza kwenye kochi. Tena safari hii aligeukia pakuegemezea mgongo hapo kwenye kochi. Hakutaka kuona sura ya Geb.

Geb alipotoka kuoga, akakuta taa zote za sebuleni zimezimwa Nanaa ameshalala. Akajua amekasirika. Akaenda mpaka pale alipolala, akapiga magoti akajiegemeza kichwa pembeni ya Nanaa, akatulia kwa muda. “Ulipotuacha hapa, nikapata wazo la kwenda kumuona mama mara moja. Nikaona nisikusumbue kukupigia simu kukwambia. Nikimbie mara moja na watoto, nikijua nitawahi kurudi kabla yako. Naona sababu ya maombi na foleni, nimechelewa kurudi na watoto.” Kimya. Geb mbabe sio huyu wa sasa hivi. Hata Nanaa hakuwahi kuona aina hii ya Geb.

“Umeshakula?” Geb akauliza. Kimya. “Njaa inaniuma mwenzio.” “Nilijua umekula kwa mama yako. Chakula nilishapika. Nimekirudisha kwenye friji wakati umeingia chumbani kwako.” Nanaa akajibu kwa sauti ambayo Geb akajua huko alikogeukia analia.

“Nilienda kuoga. Lakini Sikula. Nilitaka tuje kula wote.” Geb akajibu kwa upole na unyenyekevu kama si Geb! Kimya. “Unataka nikupashie moto chakula na wewe, ili tule huku tunaangalia movie?” Kimya. “Nimekuudhi?” Geb akauliza kwa upole akibembeleza, mpaka Nanaa akajisikia vibaya. “Naomba nisamehe Nanaa. Sikujua kama nitachelewa na watoto. Ulitusubiri kwa muda mrefu?” Nanaa akatingisha kichwa kukubali. “Pole.” Geb akambusu mgongoni.

Akamuona anageuka taratibu. Akampangusa machozi. “Unarudi kuishi na mama yako?” Nanaa akauliza huku akitokwa machozi. “Hapa duniani zipo falme mbili tu, ambazo zinazofanya kazi. Lazima uchague moja ili kuweza kuishi maisha fulani. Hakuna pande ya katikati. Lazima uchague. Na ukiwa katikati huwezi kufaidi mema ya famle hizo mbili. Lazima ukubali kumtumikia Mungu kwa uaminifu ili ufaidi mema yote, au shetani ili akupe yale awapayo wafuasi wake. Hakuna katikati.” Nanaa hakuelewa anachotaka kuongea Geb. Havikuendana na swali lake.

“Sasa mimi nimekuwa nikiishi katikati kwa muda mrefu sana. Nikiogopa kwenda kwa shetani kwa sababu nyingi tu. Lakini sasa hivi nimeamua Nanaa. Nimekusudia kumfuata Mungu kwa moyo wangu wote na akili zangu zote. Kwa kuwa najua hata nikirudi kwa shetani, kwa hivi nilivyo, mapungufu niliyonayo, atanichoka kwa haraka sana, na nitaendelea kuteseka. Ni Mungu mwenyewe ndiye nimemuona anaweza kuchukuliana na mapungufu yangu na kunisaidia.” Geb akaendelea huku Nanaa akimsikiliza akiwa amejilaza kwenye kochi.

“Nimeamua kusoma neno lake, huku nikimsihi Roho wake anijalie kuishi vile neno linavyosema. Nipo kwenye kujifunza. Najua kutakuwa na kukosea kwingi, lakini najua Mungu ni mwaminifu na wa haki, kile alichokianzisha ndani yangu, hatatulia mpaka akikamilishe. Katika kusoma maandiko nikakutana na maandiko ambayo ni magumu sana kwangu. Na si kwamba ni mageni. Lakini nafikiri Mungu alitaka au aliona ndio wakati wa mimi kuishi hilo neno.” Geb akakaa.

“Naweza kuwasha taa?” Akamuuliza Nanaa. Akiwa haelewi, akakubali. Geb akaenda kuwasha taa, akarudi na simu yake mkononi. Akaenda kunyanyua miguu ya Nanaa ili akae. Nanaa akataka ampishe, lakini Geb akamzuia. “Nitaipakata tu. Hamna shida.” Geb akakaa, na kuipakata miguu ya Nanaa. Akaiminya minya kidogo  kama kuipapasa. Nanaa alisikia faraja ya pekee, akauma midomo yake na kutoa tabasamu. “Asante.” Akashukuru, Geb akamwangalia na kurudisha macho kwenye simu.

“Ngoja nikusomee kile Mungu anachokiwekea msisitizo kwangu, sasa hivi.” Akafungua bibilia ya kwenye simu. Akasoma{Mwanzo 2:24 Kwa hiyo mwanamume atamuacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakua mwili mmoja” } “Niliposoma hiyo, nikatulia kwanza. Roho wa Mungu akanichukua tena taratibu mpaka hapa.” Geb akafungua tena andiko jingine kwenye bibilia. Akasoma. { Mathayo 19:5-6 Akasema, kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe, na hao wawili watakua mwili mmoja? hata wamekua si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, Hapo napo ikawa ni mafundisho magumu zaidi. Maana Mungu alishugulika na kila eneo la maisha yangu na yale yaliyotokea kwako na mimi nikakuacha.  {mwanadamu asiwatenganishe.} Hapo Mungu akahakikisha anaparudia sana tena sana.” Geb akaendelea.

“Hapo ujue nilikuwa kwenye maombi ya siku tatu. Nimefunga. Hata maji sikuwa nakunywa, natafuta uso wa Mungu tu. Sijui ulipo, sijui chakufanya. Watoto wote wamenigeuka. Bibilia ndio kimbilio langu. Naisoma mchana na usiku labda Mungu atazungumza na mimi. Ndio nakutana na hayo maandiko! Mungu hakuishia hapo Nanaa. Akaendelea tena kwenye hilo eneo. Nikakutana na huu mstari tena. {Waefeso 5:31 Kwa sababu hiyo mtu atamuacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao watakua mwili mmoja.} Hapo nikajua lipo tatizo ambalo Mungu ameliona ndani yangu, anataka nilishugulikie. Hakuna jinsi ungemwambia Geb aachane na mama yake akaelewa. Wewe unanijua, Nanaa. Umenikuta nalala na mama.” Nanaa akacheka kidogo.

Nikaanza maombi kumsihi Mungu anifundishe kwenye hilo eneo. Mungu mwingi wa rehema, akaanza kunifundisha taratibu na kwa upole. Akanichukua hatua kwa hatua kunifundisha mimi ni nani na nafasi yangu kwake na kwa jamii ni ipi. Mpaka anamalizana na mimi kwenye hilo eneo, nikaishia kulia nakuomba toba. Nikajikuta nimeshindwa kusimama kwenye nafasi hata moja wapo. Kwanza kama mtoto kwa mama yangu. Mume kwako, baba kwa watoto wangu na kijana kwenye jamii. Vyote hivyo nilikuwa nimevichanganya na kuharibu kabisa mpaka nikafika mahali, majukumu yangu yote, kasoro pesa ambazo nalo hilo ni eneo Mungu ameshugulika nalo pia. Bado sijapona, lakini bado ananishugulia. Naamini nitapona tu.” Nanaa hakuwa ameelewa ni nini ambacho Mungu anatakiwa ashugulike kwa upande wa pesa kwa Geb. Maana ni kweli alimbariki na pesa. Wakati watu wengine wakilia njaa, akaunti za Geb zilikuwa zikiingia pesa za halali zisizo na maswali.

“Kwa hiyo kama nilivyokwambia, nikagundua nilikuwa nimeshakoroga kila eneo. Majukumu yote au yale ambayo nilitakiwa kuyafanya mimi, nikawa nimemkabidhi mama yangu, ndio maana hakuna kilichokuwa kikienda sawa, kasoro pesa tu ambazo niliweka uangalizi wa asilimia 100, chini yangu. Huwa siamini mtu na mipango yangu ya pesa, hata Grace. Nikishajiwekea mipango, ni mimi tu ndio nitaisimamia na kuhakikisha inatimia. Imeniathiri sana, lakini Mungu ni mwaminifu. Na hapo atanirehemu tu siku moja.” Geb akaendelea.

“Kwa hiyo Nanaa, umepata jibu la swali lako?” Nanaa akainamisha macho chini kama anayefikiria. “Nanaa?” “Nimekusikia Geb.” Nanaa akajibu taratibu. “Na je, umenielewa?” Akamuona analia. “Najua kila kosa lina adhabu au madhara yake, siwezi kuepuka hilo. Nimeshakukosea mara nyingi sana. Najua hata unatilia mashaka upendo wangu kwako kwa sababu nimeshindwa kuishi kile nilichokuahidi tokea mwanzo. Umeweka wazi na kwa vitendo, kuwa upo hapa kwa ajili ya watoto tu. Silaumu. Lakini Nanaa, kumbuka wewe ni mke wangu. Nilishalipa mahari. Ndoa yetu ilishatangazwa kanisani mara tatu na tukaenda kuombewa na mchungaji kanisani. Tulishawekeana viapo mbele za Mungu. Bado tu kuweka viapo mbele za mashahidi ili tupewe hati za ndoa.” Geb akaendelea.

“Nimeamua kusimama kwenye nafasi yangu kama mume, baba na mtoto kwa mama yangu. Nasubiri adhabu yangu iishe ili tuendelee na maisha yetu.” “Mimi sikuadhibu Geb.” Nanaa akajibu huku akifuta machozi. Geb akamwangalia kidogo, akaendelea. “Kama mume, kusimama na wewe wakati wote. Sitachoka kukusubiri Nanaa. Nitakusubiri mpaka utakapo nisamehe. Mpaka utakapoona nafaa kuwa mume wako tena. Mpaka utakapoona ipo sababu ya kuwa na mimi. Nataka ujue, ninakusubiri.” Nanaa akashindwa hata kumtizama.

“Nitachua nafasi ya kuwa baba kwa wanangu. Sitamtupia hilo jukumu tena mtu mwingine yeyote, zaidi mama. Hatakuwa mlezi wa watoto wangu isipokuwa bibi yao. Nitawaongoza kwenye njia iwapasayo kuishi. Kwa maombi na juhudi zangu zote. Kuwapatia kile ninachojua wanastahili na kuhitaji. Kwa garama yeyote ile. Iwe pesa au mimi mwenyewe kutoa uhai wangu kama vile ulivyokuwa ukiwapigania wewe hospitalini ili wazaliwe. Ndivyo nitakavyohangaika kusimama kuwa baba kwa wanangu kuwapa kile wanachostahili. Ukiwemo wewe.” Akashika miguu ya Nanaa aliyokuwa ameipakata.

“Lakini katika hayo yote, nikakutana na ukweli fulani fulani hapo katikati ambao nilifichwa, nikaumia sana moyo. Aliyekuwa ameniumiza zaidi alikuwa mama. Nikataka kumchukia sana. Kwa kuwa ile barua uliyokuwa umeniachia kwa walinzi ukataka nipewe mimi, Jeri alimpa mama. Mama akaificha. Nilikuja kujua baadaye sana kama nilivyokwisha kukusimulia. Hasira ikaniwaka ndani yangu. Nikamchukia mama. Lakini tena, Mungu akanibana.” Geb akamuachia Nanaa. Alikuwa akimpapasa miguu huku akiiminya minya kwa mkono mmoja. Alijua wazi Nanaa anafurahia.

Akachukua tena simu yake. Akafungua bibilia. “Akanipeleka sehemu ngumu kweli. {Marko 11:25–26 “Nanyi mnaposimama kusali, sameheni kila mtu aliyewakosea ili Baba yenu wa mbinguni apate kuwasamehe ninyi makosa yenu. 26 Lakini msipowasamehe wengine, basi makosa mliyofanya ninyi hayatasamehewa na Baba yenu wa mbinguni.”} Hapo napo pakawa pagumu. Nikakumbuka dhambi nilizonazo. Nikajiambia inamaana nisiposamehe, na mimi sitasamehewa!” Hapo napo na Nanaa akaanza kuhukumiwa.

“Nikashupaza shingo kidogo. Kama unavyonijua nilivyo mwingi wa hasira. Lakini Mungu hakuchoka na mimi. Akaniletea tena andiko jingine. {Matayo 5:23-24 “Basi, kama ulikuwa tayari kutoa sadaka yako madhabahuni, ukakumbuka kuwa ndugu yako amekukasirikia, 24 acha sadaka yako hapo hapo, uende kwanza ukapatane naye, kisha urudi kumtolea Mungu sadaka yako.”} Kwa hiyo nikajua hata sadaka zangu hazitakuwa zikipokelewa. Ikabidi kujirudi tu, na kusamehe. Kwanza Nanaa, kumbuka makosa yalikuwa yangu tokea mwanzo. Sikuwahi kuachana na mama yangu, na haikutosha, majukumu yangu yote ya nyumbani, nikamkabidhi yeye. Ikabidi kuwa mpole na kujirudi tu.” Geb akamaliza. Ila yale maneno yote yalimuingia Nanaa vizuri sana. Na yeye hayo maandika mawili ya mwisho yakawa yanamuhusu. {Marko11:25-26 na Mathayo 5:23-26} Akabaki kimya.

Geb akamsugua sugua tena miguu. “Ulitembea sana?” Akamuuliza kwa upendo huku akimminya miguu kama kumfanyia masaji. Nanaa akakubali kwa kutingisha kichwa. “Lakini hivyo unavyonifanyia, utanifanya nilale sasa hivi!” Geb akacheka. “Basi ngoja nilete chakula, tule kwanza ndio ukalale.” “Wapi tena? Mimi hapa ndio nimeshafika mwenzio. Wala sijisogezi.” “Tupeane zamu yakulala kitandani.” “Hamna sababu Geb. Mwenzio nafurahia hapa kwenye kochi. Najigeuza nitakavyo, halafu wanangu wakiamka pale ndani, nawaona. Kwa hiyo wewe furahia tu kitanda. Mimi nipo sawa kabisa.” Geb akaenda upande uliopo jiko, ambako kuna friji.

~~~~~~~~~~~~~~~

·      Haya, Nanaa amerudi kuishi na wanae, akionyesha wazi ameshindwa kumpokea Geb kama mpenzi. Kwanza hana historia yakumuona anaahidi na kutekeleza ahadi zake. Amemwambia wazi bila kificho kuwa huwa anaanzisha mambo mazuri na kuishia katikati pindi anapokuwa amekasirika. Lakini Geb huyu anaonekana ni watofauti. Hata Nanaa mwenyewe amemuona amebadilika. Itakuaje?

·      Usikose kujua yatakayoendelea kwenye ndoa ya Grace & Danny. Wapenzi wa tokea zamani. Kaburi alilochimba mama G, hakika ametumbukia mwanae mwenyewe bila kujua, Sara amehamia kwenye ndoa ya mwanae. Je, nini kitaendelea? Grace aliyekuwa ametangaza kumuombea mumewe, ni kama na yeye amesalimu amri.

Usikose muendelezo.

 


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment