Geb alilala usiku huo akiwa amefunga siku ya tatu. Akamuota
Nanaa analia sana. Akashituka. Akakaa. Akakumbuka vile James anavyokuwa
anamuota Nanaa akilia, na anakuwa kwenye shida. “Lakini haiwezekani. Hiyo kitu ni ya James tu.” Geb akabishia ndoto
yake. Akajitetea na mikasa mikali ya masaa machache yaliyopita. Kuanzia vile
Jeri alivyomsimulia hali aliyomkuta nayo Nanaa na jinsi alivyomuhurumia mpaka
kulia. Akakumbuka matusi makali ya Danny mpaka kumfukuza nyumbani kwake. Akajua
kwa hakika nafsi yake imeingiwa hofu nakushika tu hukumu, ndio maana akaota ile
ndoto. Akajifariji.
Maneno ya Danny. Tukio la
kuwatukana matusi mazito vile. Wote watatu. Bila hofu. Kwa maneno yanayoendana na kweli! Maelezo ya Jeri
juu ya Nanaa. Barua ya Nanaa. Kilio cha uchungu cha Liv, nakumuonyesha wazi
amemchukia. Mtoto aliyekuwa akikimbilia kifuani kwake, nakulala! Vyote hivyo
vilimnyima usingizi Geb. Alikaa kitandani kwake kimya akiwaza.
~~~~~~~~~~~~
Kwani walirudi nyumbani baada
yakutoka pale nyumbani kwa Danny, walishindwa hata kuongeleshana. Mama yake
alishindwa hata kumtizama Geb. Alimchukua Magesa. Akamlisha na kumbadili nguo.
Liv alishushwa kwenye gari, akakataa hata kushikwa mkono. Akarudi ndani,
akajilaza kwenye kochi huku akiangalia tv. Baba yake hakumuuliza kitu.
Akamkabidhi chupa yake ya maziwa.
Akaanza kuivuta taratibu huku amejilaza kwenye kochi,
amekumbatia mtandio wa mama yake, anaangalia tv. Alipopitiwa na usingizi, ndipo
Geb alipombadilisha diaper na nguo, akaenda kumlaza kitandani kwake, na yeye
akarudi chumbani kwake.
~~~~~~~~~~~~
Kesho yake Jeri alipofika tu
kazini, yaani nyumbani kwa Geb, akamuita nje. Akamwambia amtumie ujumbe Nanaa,
ajue anaendeleaje. Jeri akafanya hivyo. Lakini ikawa kimya. “Hata ujumbe
unaonekana haujafika!” “Endelea kujaribu. Lakini usimwambie mama. Nyamaza
kabisa. Usiropoke hata ujio wa Nanaa jana.” “Sawa bosi.” Jeri akapata kazi
yakutunza siri kwa mabosi wake wote wawili. Geb na mama yake.
Geb alipofika tu kazini
akampigia simu Jeri kujua kama alimpata Nanaa. “Hapana. Naona
bado simu imefungwa.” “Endelea kujaribu.” Geb akasisitiza. Mchana tena
akampigia simu Jeri. Majibu yakawa yale yale. Usiku wakati analala, Jeri
amerudi kwake, akampigia tena simu.“Bado simu yake
inaonekana imefungwa.” Jeri akamjibu bosi wake.
~~~~~~~~~~~~
Juma zima likapita. Bila
kumpata Nanaa. Geb akaanza kupaniki sasa. Akaona aanze kumsaka yeye mwenyewe. “Akija kufa, Liv wangu atateseka sana na
hatakaa akanisamehe.” Geb akawaza. “Ni
kweli nimekuwa kama baba! Grace hajakosea. Alipoteza binti zake wawili sababu
yakumuacha mama yao. Baba amekufa bila wale watoto wake.” Hofu ikamuingia
Geb. “Lakini Liv bado mdogo sana. Hawezi
kuja kukumbuka.” Akajifariji.
Juhudi za kumtafuta Nanaa
zikaendelea huku akijiambia anafanya kwa ajili ya Liv. Mchana ukaenda na usiku
haukuwa mbali. Kadiri siku zilivyozidi kusogea Nanaa hapatikaniki, akajiongezea
sababu zaidi ya kuendelea kumsaka. Safari hii akawa akimtafuta sababu ya watoto
wote wawili. “Magesa atakuja kunilaumu
sana. Atakuja kunichukia kwa kumtenga na mama yake. Liv naye hatanisamehe
kabisa. Bora tu nimtafute, nijue hali yake kwa ajili ya wanae tu.”
Akajiambia huku akiendelea kupiga simu ya Nanaa bila mafanikio.
Huku Kwa Grace Na Danny.
Maisha ya Sara yakaendelea
ndani ya nyumba ya Danny bila shida. Kuamka anavyotaka bila hata kujigusa na
chochote ila urembo wake tu. Alitoka bila kuaga, labda kama Danny yupo. Tena
wakati mwingine alitoka na Danny na watoto. Heshima hamna kwa Grace wala kwa
msichana wa kazi wa Grace. Grace alishazungumza na msichana wake wa kazi. Kwa
hiyo yule dada naye akawa anampuuza tu.
Na kweli, baada ya kama siku 10
hivi Danny, Sara na watoto wote wakasafiri. Grace alipotaka kuwasindikiza
kwenda huko Iringa, kwenye nyumba ya mapadri, alikokuzwa mumewe, Danny
alimkashifu na kumwambia ni mahali pa chini sana na watu anaoenda kukutana nao
ni duni mno. Matajiri kama kina Magesa hawawezi kufika huko wala hataweza
kuchangamana na wao. Hataki kiwingu, amuache tu. Grace alishuhudia wanae
wakiondoka na Sara kama mama yao.
Alisimama akitizama wanae
wakiondoka siku hiyo asubuhi, na yeye akapanda gari kuelekea kazini. Njia nzima
alikuwa akimlilia Mungu wake amrehemu. Alilia Grace mpaka anafika kazini kwake.
Hakuwa hata akikumbuka ni lini alikula. Alikuwa akifunga mfululizo. Alikaa sehemu
ya kuegesha magari, mwishowe akaamua aingie tu ndani aanze majukumu ya pale
yanayomtoa kwenye mawazo.
Geb akaingia. Alipomuona na sura ya kulia, akamuhurumia.
Asijue ampe pole au samahani. Ni kama yeye na mama yake ndio wamemuingiza
kwenye yale matatizo. Akabaki amesimama mlangoni kwake kwa muda akifikiria.
Grace alijua wazi kama kaka yake amesimama pale, lakini hata hakumtizama.
Aliendelea kuandika kwenye komputa yake.
Simu ya mama yake ikaanza kuita
mfululizo. “Mama anawasiwasi na wewe G. Zungumza naye hata kidogo. Amenituma
nikuombe upokee simu zake.” Grace akapokea. “Unaendeleaje Grace?” Mama G akauliza. “Namshukuru
Mungu. Lakini ujue tu, mke uliyemtafutia Geb, amekuwa mke wa mume wangu.
Tunapozungumza hapa, wapo njiani na wanangu wanakwenda Iringa. Kaburi ulilomchimbia
Nanaa, nimetumbukia mimi.” Grace alijibu na machozi
yakimtoka. Mama yake akakata simu. Geb akaondoka bila kuongeza neno.
~~~~~~~~~~~~
Geb alirudi ofisini kwake
akabaki amekodoa macho. Nyumbani hapakaliki. Kilio cha wanae, kazini nako kilio
cha dada yake. Magesa naye alishaanza kulia usiku. Lala ya Geb ilishaanza kuwa
ya shida. Akamuhamishia mwanae chumbani kwake ili usiku awe anamlisha yeye
mwenyewe ili asiendelee kumtesa mama yake.
~~~~~~~~~~~~
Binafsi Geb hakuwa akimlaumu
mama yake hata kidogo. Alijilaumu yeye mwenyewe kushindwa kuwa baba kwa watoto
wake na kusimama kwenye nafasi yake kama Grace alivyomwambia. Akachukuliwa na
jazba. Akajikuta yeye na mama yake wako ukurasa mmoja. Hakuna wakumsaidia
mwenzie. Wakahama na watoto. Akamuachia mama yake majukumu yote ya watoto, yeye
akaanza maisha yakujihurumia kuwa amedanganywa na kuumizwa na
Nanaa. Mama G ndio akashika usukukani. Anaamua watoto wafanyiwe nini na nani.
Yeye akiwepo hapo hapo akijihurumia hana habari na kinachoendelea.
~~~~~~~~~~~~~
“Danny anahaki yakukasirika. Ni kweli tumekuwa zaidi ya wanyama.” Geb
akawaza nafsini mwake akianza kujilaumu sasa. Akaamua kumpigia tena simu Nanaa
bila mafanikio. Ndipo wazo lakumtafuta daktari aliyejua huwa anamtibu Nanaa
kila akiwa mjamzito likamjia. Alikuwa na namba yake, kwani walikuwa karibu sana
kipindi Nanaa ana ujauzito wa Magesa. Yeye ndio alimwibia siri ya jinsia ya
mtoto aliyekuwa amembeba Nanaa, Magesa, bila hata Nanaa mwenyewe kujua.
Kwa Dokta Lyamu.
Akaitafuta kwa makini kwenye
simu yake, akaipata. Akampigia. “Namuulizia Nanaa. Huwa anakuja kukuona?” Geb
akauliza. “Ndiyo. Hivi hapa yupo kwenye matibabu. Lakini safari hii
sio Nanaa unayemfahamu wewe. Amejikatia tamaa. Na siunajua uponyaji unatoka
ndani? Sasa Nanaa hataki kujikaza kabisa. Dawa zinamkataa. Suluhisho pekee ni
kumtoa mtoto, lakini pia hataki kama unavyomjua. Lakini safari hii si kama
watoto wake wengine. Huyu wasafari hii amekata tamaa kabisa.” Lyamu
akamuelezea Geb.
“Yuko wapi?” Akauliza. “Nilikuwa
nimemlaza hapa hospitali ya Tumaini, lakini nikaona nimrudishe tu hospitali ya
Muhimbili.” “Kwa nini!?” “Hapa nilimuweka kwa juma zima nikijaribu kumshauri
jinsi ya kupona, lakini hakuwa akitoa ushirikiano. Nikaona tunaingia garama ya
bure. Heri tuhamie kwenye hospitali ya bure, tuendelee kubembelezana.”
“Usingemkatia tamaa.” Geb akajisikia kuumia, akajisahau na kulalamika.
“Sio mimi! Ni Nanaa mwenyewe.” “Naomba
nielekeze alipolazwa.” Akamuelekeza mpaka kitanda alicholazwa. “Na mimi
mwenyewe naelekea huko sasa hivi.” Geb akakata simu na kutoka
pale mbio bila hata kuaga. Hata muda wakuona wagonjwa ulikuwa bado haujafika wakati
Geb akiegesha gari yake katika hospitali ya Muhimbili. Ilikuwa saa 9 mchana.
Hakuruhusiwa kuingia. Akakumbuka daktari alimwambia na yeye anaelekea huko.
Akampigia simu. “Naomba nisaidie kama unaweza kuniombea nikaingia kumuona
Nanaa.” “Nipo huku kitengo cha mambo ya moyo. Najaribu kuzungumza na wataalamu
juu ya hali yake. Nitakuja muda sio mrefu.” “Nakushukuru sana.” Geb
akakata simu na kubaki amesimama pale nje ya wodi, akitamani aruhusiwe tu
aingie amuone Nanaa.
Atafutaye Hachoki.
Kadiri dakika zilivyozidi
kwenda, ndivyo shauku ya kumuona Nanaa ilivyomuongezeka. Sababu ya kumtafuta
Nanaa kwa ajili ya watoto wake, ikabadilika. Ikawa ni yeye ndio mwenye shida na
Nanaa kuliko hata wanae wanao lia huko nyumbani. Alikaa pale akimsubiria kwa
hamu kubwa dakatri aje aingie naye.
Kama baada ya dakika
20, ndipo Lyamu akafika pale. “Twende.” Wakaongozana mpaka alipokuwa amelazwa
Nanaa. Alikuwa amelazwa kitanda cha mwisho kabisa. Alikuwa amelala huku jasho
likimtoka sana. Daktari akamvuta mkono, akaanza kumpima presha. “Bado ipo juu!”
Daktari aliongea huku akiendelea kusoma.
“Anatokwa na jasho jingi!” Geb
akaanza kumfuta na kitambaa chake. Nanaa akafungua macho, akamuona Geb.
Akamtizama kwa muda, akarudi kulala. Geb akajua anafikiri anaota. “Mungu
atakusaidia utapona Nanaa. Pole sana.” Geb alijikuta akiongea. “Acha tuombe.”
Geb akapiga magoti pale pale pembeni ya kitanda, akaanza kuomba. Aliomba mpaka
Nanaa akaamka.
“Geb!” Aliita kwa upole huku akilia. “Nimechoka. Natamani Mungu anipumzishe. Nimechoka sana.” “Pole
Nanaa. Pole sana.” Nanaa akavuta pumzi. “Lakini Nanaa wewe ni mpambanaji. Sio
mtu wakuita kifo! Usikate tamaa.” “Safari hii
nimepigwa vibaya sana. Mpaka nafsi yangu imepondeka. Siwezi tena.” “Sio
wewe Nanaa.”
“Kweli Geb. Siwezi. Natamani kupumzika tu.
Nimepambana na haya maisha vyakutosha. Sina nilichobakiza.” “Ni
kwa sababu umekata tamaa mapema.” Nanaa akavuta tena pumzi kwa nguvu. Akafunga
macho. Geb akamfuta machozi.
“Asante.” Akashukuru
huku amefunga macho. “Karibu.” Geb akajibu. Lyamu alibaki akiwasikiliza huku
akiandika kwenye jarida la Nanaa. “Nitarudi baadaye tena kidogo. Ngoja nikazungumze
na wenzangu. Sijui nitakukuta?” Baada
yakumaliza kuandika, Lyamu akaaga. “Mimi nitakuwepo tu. Utanikuta kama
hawatanifukuza.” Geb akajibu. “Nitazungumza na manesi basi ili wasikutoe.
Kwanza muda wakuona wagonjwa umekaribia.” Akatoka.
~~~~~~~~~~~~
“Geb!” Nanaa akaita kwa upole. “Naam!” Geb akaitika. “Lile
tukio lilinisababishia nikapata mimba. Hapa nilipo ni mjamzito.” “Nafahamu
Nanaa. Najua.” Geb alimjibu nakumfuta machozi. “Lakini Nanaa, naomba umchukulie
kama ni mtoto wako. Uliyepewa dhamana na Mungu umlete hapa duniani. Kama
ulivyoniambia kwa Magesa. Unakumbuka?” Nanaa akatingisha kichwa akilia. “Basi
naomba ufanye kwa nafasi yako. Kama ulivyofanya kwa Magesa ndivyo ufanye na kwa
huyu. Najua unaweza Nanaa. Mungu hakuwa amekosea alipompitisha huyo mtoto
kwako. Si unajua wapo wengi wanalilia kupata watoto na wameshindwa?” “Kwa hiyo Mungu ameniamini mimi?” Nanaa akauliza. “Kabisa.
Anajua uwezo aliouweka ndani yako. Pambana, utoke hapo. Usikubali kushindwa
bila kupambana. Umenisikia?” Nanaa akatingisha kichwa kukubali.
“Lakini mwili
wangu umechoka sana!” “Unakumbuka umeshika mimba mara baada yakujifungua tu
Magesa? Tena hukua hata umepona vizuri. Mwili wako haukuwa umepumzika hata
kidogo. Bado ulikuwa upo kwenye madawa. Lazima mwili uchoke. Unachohitaji ni
mapumziko tu. Unahitaji mapumziko yakutosha, utakuwa sawa tu.” “Basi narudi kulala. Naomba ukiondoka, ukifika nyumbani unisalimie Liv
na mdogo wake.” “Nitafanya hivyo.” Akasinzia kidogo, akashituka.
“Geb!” “Bado nipo.” Akatulia
kidogo huku amefunga macho. “Asante kwa kuja.” “Karibu. Pumzika kidogo.” “Ila
nina kiu sana. Sijanywa maji siku nyingi na sina mtu wakumtuma maji ya kunywa.”
Geb akaumia sana. “Chakula je?” “Huwa wanapitisha cha wagonjwa wote, hichi
kinachotolewa na hospitali. Lakini mara nyingi nakuwa nimelala. Nashindwa
kula.” Geb akazidi kumuhurumia. Akajua anachoshwa na mengi. “Basi nisubiri
nakuja. Unahamu yakula nini?” “Chochote tu. Sichagui.” Akajibu kinyoge. Geb
akatoka kwa haraka sana.
~~~~~~~~~~~~
Kwa kuwa alijua Nanaa si
mchaguzi wa chakula. Anakula chochote. Akaenda kwenye maduka ya hapo nje ya
hospitali. Akanunua chupa ya chai, thermos, akakimbilia baa aliyojua atapata tu
chakula laini. Akapata mtori. Akachukua na fanta orange aliyojua Nanaa
anaipenda. Akabeba na chupa za maji mbili, akarudi hospitalini kwa haraka.
“Nataka kukukalisha ili ule.”
“Nimechoka Geb. Mwili hauna nguvu. Mikono inatetemeka.” “Mimi nitakulisha.
Nakusaidia kukaa.” Geb akamvuta, akamuegemeza kwenye mto. Akakaa mbele yake,
huku akiwa ameshaweka mtori kwenye bakuli. Akaanza kumlisha taratibu. Alionekana
alikuwa na njaa sana. Alikula ule mtori wote. Akafungua macho. “Asante. Nahisi
njaa ndio ilikuwa ikinichosha zaidi.” “Pole.” Nanaa akajiinamia.
“Nilikuletea na soda yako
unayoipenda.” Nanaa akaiangalia na kutoa tabasamu. “Asante. Nitainywa sasa hivi
ikiwa bado yabaridi.” Akamfungulia. Akaanza kumpa akiwa anavuta na mrija.
Alikuwa amemshikia. “Nakushukuru sana Geb. Asante.” “Karibu. Lakini bado mikono
inakutetemeka.” “Itapona tu.” Geb akacheka. “Huyo ndio Nanaa ninayemfahamu
mimi. Sio Nanaa anayeita kifo.” Akacheka nakuinama kama anayefikiria.
“Kesho asubuhi nikuletee nini?”
Nanaa akanyanyua uso na kumwangalia vizuri, akaona machozi yakimtoka. “Kwani utarudi tena?” Nanaa akauliza. “Ndiyo.” Nanaa akainama
nakuanza kulia. “Lazima kujaribu kutulia Nanaa ili presha ishuke.” “Lakini nina mimba ya Malii!” Nanaa akarudia kwa kumtahadharisha.
“Nafahamu Nanaa. Najua. Unataka nikuletee nini kesho?” “Chochote tu utakachoweza.” Nanaa akajibu nakujifuta
machozi huku akijua wazi itabidi anunue chakula. Geb hakujua kupika hata kidogo.
“Kabla hujaondoka, naomba
nikuombe kitu. Samahani lakini.” “Unataka nini?” “Sijui hata simu yangu ilipo.
Lakini yupo dada ninayeishi naye. Hajui nilipo tokea siku niliyomuaga nakwenda
kuona wanangu. Sijarudi tena nyumbani. Atakuwa na wasiwasi sana. Naomba
nimpigie.” Geb akamtolea simu. Nanaa akampigia.
Kwa Fifi.
“Ni mimi dada Fifi!” “Nanaa!” Fifi
akauliza. “Ndiyo dada.” “Kwa nini unanifanyia hivyo mdogo wangu?
Nimekwenda mpaka polisi! Nimezunguka mpaka mahospitalini. Nimekuwa kama mwehu!
Usinifanyie hivyo Nanaa. Watu wananipotea mimi kama upepo. Leo nakuwa na huyu
kesho wananipotea.
Sina
mtu..” Akamsikia
analia. “Pole dada. Pole dada yangu.” Nanaa akajaribu
kumtuliza.
“Uko wapi sasa? Au umerudi kwa baba watoto wako?” “Hapana
dada. Haitakaa ikatokea tena. Nilishakusimulia kila kitu, sikuwa
nimekudanganya. Hata kama ingekuwa hivyo, nisingehama bila kukutaarifu dada
yangu. Unisamehe.” “Uko wapi sasa?” “Hali ilikuwa mbaya. Si unakumbuka nilitoka
nikiwa sijisikii vizuri, nikakwambia nilazima nikawaone wanangu?” “Na wosia
ulishaniachia.” Nanaa akacheka.
“Usicheke bwana Nanaa! Umenipeleka mpaka
vyumba vya maiti!” “Dada Fifi wewe!” “Sasa je? Ulivyoondoka
ukiniaga kuwa unaweza usirudi tena kwa vile unavyojisikia. Heri ukaone wanao
angalau kwa mara ya mwisho. Halafu nisikuone tena! Sasa unafikiri ningeanza
kukutafutia wapi?” “Si wodini!” “Aliyekwambia sijafika huko mawodini ni nani?” Nanaa
akacheka tena. Nanaa huyu alishapewa mtori na soda. Tena alilishwa na Geb! Hata
sauti ilishaanza kutoka.
“Nimelazwa dada.” “Wapi!? Kweli
nimezunguka mimi mpaka wodi za wanaume. Na hivi ulikata nywele!” Nanaa
alicheka tena. “Na tumbo hili?” “Kwani hujaona wanaume wenye vitambi na
maziwa, bwana? Hebu niambie ulipo, ili nije. Umekula?” “Nilikuwa nimedhoofu.
Kumbe ni njaa. Presha pia ipo juu sana.” “Tulia Nanaa mdogo wangu. Wanao bado
wadogo mama. Usikiri kufa. Tulia ulee wanao. Tulia presha nayo itulie.” Nanaa
akaanza kulia.
“Unanisikiliza lakini?” Kimya.
Nanaa aliendelea kulia. “Umenitoa wodini kwa maneno yako ya imani. Umebadili maisha
yangu. Naomba hiyo imani yako itumie na kwako, mdogo wangu. Toka hapo ulipo.
Samehe, maisha yaendelee. Leo umekataliwa watoto. Hujui kesho. Uliniambia
unapambana ili wanao wakija kukutafuta, wakukute hai, sio waonyeshwe kaburi.
Ukaanza vizuri. Umejua ni mjamzito tu, mambo yote yamebadilika. Hutaki kila
kitu! Unajiandaa kufa! Umefikiria wanao uliokwisha wazaa?” Nanaa
aliendelea kulia.
“Nanaa!” “Nilikata tamaa dada.” “Hapana
bwana. Hizo ni kauli za kishamba kweli wakati wewe mtoto wa mjini.” Nanaa
akaanza kucheka tena. “Niletee uji kesho asubuhi. Njaa imeanza kunisumbua.”
“Afadhali kama hamu ya kula imerudi.” “Niletee na chai, sambusa, chapati na
maandazi.”
Akamsikia Fifi anacheka. “Wewe si ulikuwa ukitaka nile?” “Nakwambia
nitajuta!” Nanaa akacheka.
“Naomba mimi ndio niwe wakwanza bwana!
Ndio ukasambazie wengine.” “Hapa nahangaika kupika. Kutwa nilikuwa nakutaja.
Nasema huyu Nanaa kaanzisha mambo anayoyajua yeye, halafu ananiacha.” “Kama
nakuona jinsi ulivyokuwa unaongea peke yako hapo jikoni.” “Naongea, nakulia
kama mwehu!” “Pole dada yangu. Basi kesho unianze mimi.” “Lazima. Kwanza
nishapatwa na hamu na wewe. Sina mtu wakunisikiliza. Ngoja nimalize kupika,
nitakupigia tena kabla yakulala.” “Lakini hii simu sio yangu dada. Nimeazima
kwa mtu.” “Mmh! Sasa nakupataje?” “Wewe ndio wakupotea Muhimbili wakati ndio
maeneo yako haya!?” Fifi akacheka sana. Nanaa akamuelekeza alipo, wakaagana.
~~~~~~~~~~~~
“Asante Geb. Nakushukuru sana.
Ila naomba usihangaike tena. Maadamu dada Fifi amejua nilipo, ataleta tu
vyakula.” Geb akamwangalia. Nanaa akainama. “Jilaze.” Akajinyoosha vizuri.
Akamfunika. “Mnaishi wapi?” “Kawe mwisho.” Nanaa akajibu. “Fifi ameolewa?” Geb
akauliza. “Mumewe na watoto wake wakike wawili, na binamu wa mumewe, walipata
ajali mbaya, wakafariki papohapo. Kwa hiyo tunaishi sisi wenyewe, kwenye
nyumba ya uwani. Mumewe alimuachia mali nyingi ikiwemo hiyo nyumba ambayo
tunaishi sisi. Ila nyumba yao kubwa wanaishi wapangaji wengine. Amepangisha
familia moja tu, ndio wanaishi nyumba yake kubwa ya mbele. Nipazuri tu na yeye
ni dada mzuri sana.” “Nimemsikia.” Nanaa akacheka.
“Ukijitahidi ukapona, nitakuwa
nakuletea watoto, ukae nao kwa muda unaotaka wewe.” Nanaa akaanza kulia
asiamini. “Kweli Geb!?” “Lakini mpaka daktari
akuruhusu. Anihakikishie upo salama. Ndio nitakuwa nikikuletea watoto.” Nanaa
hakuamini. Alijifunika shuka mpaka kichwani akaanza kulia tena. Geb akamfunua. “Kulia
hakutasaidia kushusha presha Nanaa. Jaribu kutulia kabisa. Jipe muda wakutuliza
mawazo. Ukijua watoto wanakusubiri upande wa pili. Umesikia?” “Nakushukuru Geb. Asante. Halafu pia usiwe na wasiwasi hata ukiniacha
nao. Walishanipima UKIMWI na magonjwa yote hatarishi. Zinaaa na mengine yote
ambayo ningeweza kuambukizwa. Lakini wameniambia sina. Nipo salama kabisa.
Nakuhakikishia hata ukiniachia watoto, watakuwa salama.” Geb akanyamaza. Hayo yalikuwa ni maneno ya mama yake, sio yeye. “Nitakuona kesho Nanaa. Ngoja nimuwahi Liv.” “Nisalimie sana wanangu. Nakushukuru sana Geb. Asante.” Geb akamfunika vizuri, nakuondoka. Nanaa alilia kidogo, akakumbuka anatakiwa kupona. Akajituliza kimya pale kitandani.
Siku Inayofuata.
Asubuhi ya saa 12, Geb alikuwa
wakwanza pale wodini. Nanaa alikuwa anatoka chooni wakati Geb anangia. “Geb!”
Nanaa akashangaa asiamini macho yake. “Mbona mapema!?” “Ndio muda wakuona wagonjwa huu.”
“Sikujua.” Nanaa akajibu. “Vipi? Ulilala vizuri?” “Kama mtoto mchanga!”
Wakacheka. “Asubuhi hii wamenipima na kunipa dawa. Naona sio mbaya sana.
Karibu. Twende kwenye kitanda changu, au unawahi kazini?” “Bado ni mapema sana.
Nimeacha bado wamelala.” “Mpaka Magesa?” Nanaa akauliza wakati wakirudi
kitandani kwake.
“Yeye ndio anaratiba ngumu.
Inabidi usiku niwe namuhamishia chumbani kwangu ili mama awe anapumzika usiku,
mchana aweze kushinda nao vizuri. Lazima aamke mara mbili. Na akiamka anaanza
kupuliza na kulia. Bibi yake anahisi ameanza kuotwa meno. Fizi zinamsumbua.”
Nanaa akafikiria kidogo. “Nimemuona ana afya nzuri.” “Alikuwa mlaji mzuri sana,
ila ameanza kubadilika. Alikuwa akila kila kitu. Lakini naona anaanza kuwa kama
Liv. Liv anasumbua sana kula. Anaweza akaamka saa nne, akakataa kula kitu
chochote mpaka wakati mwingine inabidi niwe narudi mchana kumbembeleza kula
kitu chochote.” “Nimemuona. Amekuwa mwepesi sana. Kamebaki nywele tu!” “Nazo
hataki kuchana pia. Hataki mtu amshike kichwa. Amekuwa mkali kweli!” Kwa mara
ya kwanza Geb akajikuta anatoa dukuduku lake.
“Pole kwa kulea.” Geb
akamtizama, akanyamaza.“Nakuombea Geb. Sijaacha kukuombea.” “Unaniombea nini?”
“Kila kitu Geb. Nakuombea amani, faraja, kufanikiwa, kila kitu.” “Basi naona
Mungu hajayasikia hayo maombi yako. Hamna chochote kinachoendelea vizuri. Si
unaniona?” Geb alijibu kwa kujidharau. “Umepitia kipindi kigumu sana Geb. Jipe
muda. Mungu atakutendea. Mungu hawezi kukuacha. Jipe muda tu, kila kitu
kitakuwa sawa. Pole.” Geb akanyamaza, akabaki akifikiria. Alikuwa amesimama
kati kati ya kitanda cha Nanaa na mgonjwa mwingine kwenye wodi hiyo ya wazazi.
Fifi!
Fifi akaingia. Wakamsikia akisalimiana
na manesi wa hapo kama mashoga zake wa mtaani tu. “Huyo unayemsikia mwenye
kelele, ndio dada Fifi.” Akasalimiana na manesi wote na utani kidogo, ndipo
akaenda kwa Nanaa. “Umenitesa Nanaa wewe!” “Pole dada. Pole sana. Hali ilikuwa
mbaya. Nilianzia hospitali ya Tumaini, baada ya kama week hivi, yule daktari
akanihamishia hapa. Nahisi yeye ndio mwenye vitu vyangu vyote. Nilifika pale
nilikuwa sijiwezi!” Akamsimulia kila kitu. Kuanzia alipotoka pale mpaka siku
hiyo.
“Pole mdogo wangu. Pole sana.
Lakini si umshukuru huyo bwana kama amekubali hata ushike watoto? Maana wanaume
wengine ni washenzi, wangekutosa baharini.” Fifi akaanza taratibu. Nanaa
akatamani kumkonyeza kwa kuwa alimjua. Hana breki ya mdomo. Fifi akaendelea. “Lakini
naye anajishaua! Kinachomfanya amtume dereva wake ni nini, asiyeleta wanae yeye
mwenyewe? Nakwambia ingekuwa mimi mbona ningemzidi mahesabu. Hakika ningetoroka
na wanangu. Asilete wazimu wake! Anajua uchungu wa mwana yeye? Azae basi kama
yeye anajitia mwanaume kweli! Kwanza wewe ulibakwa. Kosa lako nini?” Geb
alikuwa kimya katulia na simu yake mkononi akiperuzi taratibu.
“Mimi sijawahi kuona mwanaume
anayeshindwa kumlinda mkewe, halafu eti ajidai kununa! Achana naye mdogo wangu.
Huyo bwana hakupendi. Nakwambia mimi mume wangu kwanza angekuomba msamaha. Tena
wewe ungeombwa msamaha wa herufi kubwa. Yaani umebakwa kwa kosa la kukataa
kulala na rafiki yake! Anakuadhibu nini kama sio wehu huo ni nini? Kuna watu tunaishi nao mdogo wangu, ni vichaa
wale wakulazwa mahospitalini. Hatuwajui tu. Jambo kama hilo likitokea, ndipo
unapojua uzima wa akili ya mtu.” Nanaa alitamani kumfunga mdomo, lakini Fifi
alionekana na jazba. Akajua wagonjwa wote wameshajua kama alibakwa.
Bado Geb aliendelea kuchezea simu yake. “Au hakuwahi kukupenda? Ulijilazimishia tu mdogo wangu? Maana hayo nayo yamo! Mwanaume hakutaki unajilazimishia unajua atakuja kubadilika baadaye. Yamemshinda, ndio kapata sababu yakukufukuza. Mimi nayajua mapenzi bwana. Tena nayajua mapenzi yakupendwa, si yakusimuliwa! Upendo unatabia ya kusitiri wingi wa dhambi mdogo wangu! Upendo unavumilia! Tena wanasema hautafuti mambo yake yenyewe! Nenda kasome sifa za upendo, ndio utajua kama huyo bwana alikupenda au alikuwa anakutumia tu!”
“Ila mimi nakwambia Nanaa mdogo wangu, huyo bwana ni MUONGO. Kakutafutia tu sababu. Achana naye. Wala usife sababu yake. Hakustahili hata kidogo.” Nanaa akajitahidi kumkonyeza lakini wapi.
“Kama ni hilo jumba hata mume
wangu alikuwa nalo. Kafa, kaniachia lote. Mwenyewe pia likanishinda mpaka uliponipa
wazo la kulikodisha. Achana naye. Atakuja kufa aliache hilo jumba na magari
yake. Kama alijua atazikwa nayo, basi amechemka. Aniulize mimi. Wewe jikaze,
utoke hapa. Zaa. Nikabidhi mimi huyo mtoto kama tulivyokubaliana. Mimi ndio
mama yake Jimmy. Au unasemaje Jimmy wangu?” Fifi akainama na kumshika tumbo
Nanaa.
“Nisalimie mwanangu. Sema na
mama yako mkubwa basi.” Akampapasa tumbo Nanaa mpaka mtoto akacheza. “Mambo si
ndio hayo mwanangu? Utasoma baba. Tena utakuwa msomi kuliko watoto wa matajiri
wote hapa duniani. Tutauza sambusa na chapati mpaka uwe daktari, uje ututibu
presha mimi na mama yako. Na kingereza utajua tu. Kwani ada shilingi ngapi
bwana! Kama mamilioni na sisi tutakuwa nayo tu. Tutauza hata ile nyumba usome
mwanangu. Wasitubabaishe.” Fifi akaendelea.
Nanaa akamvuta kidogo kama
kumtuliza. “Sasa je! Wewe tulizana, nizalie huyo mtoto uone atakavyokuwa kama
uyoga! Mapenzi yote tutampa. Na kama utataka mwanaume wa kukuoa mbona utapata
tu. Wapo kibao na mdogo wangu unalipa! Au vipi?” Akamgeukia jirani ya Nanaa.
Mama aliyekuwa amelazwa kitanda cha jirani. “Eti unamuonaje mdogo wangu?” “Si mchezo.Hapo
mwenyewe mjamzito na bado anavutia. Unalipa kabisa.” Fifi akafurahi sana.
“Heri mwambie wewe atakuamini.
Nikimwambia mimi huwa anasema ooh, dada Fifi wewe maneno mengi, sijui nini! Umesikia sasa?” Fifi
akamgeukia vizuri Nanaa. “Kwanza yule jamaa yako anayekutaka, ambaye akikuona
anachanganyikiwa, leo nampelekea sambusa
30. Kaniambia anataka wewe ndio uende ili akakuunganishe na mfanyakazi mwenzie,
anataka tuwapikie kwenye kichen party ya mwenzao. Sasa changamka mdogo wangu.
Mimi nikienda, nitamwambia Nanaa atakuja siku nyingine kama akitoa oda nzuri.
Najua kwa kuwa atataka kukuona, lazima aongeze oda kubwa na atupe tenda
yakuchanganyikiwa mtu. Sasa mama, changamka hapo. Toka tukatafute pesa za
Jimmy. Nataka mwanangu asome. Tena awe gumzo hapa duniani. Au unasemaje?” Fifi
akaweka kituo, Nanaa akavuta pumzi. Akafurahia lile swali.
“Eti Nanaa mdogo wangu? Tia
neno basi!” Fifi akasisitiza. “Huyo hapo ndio Geb!” Fifi akatulia kwanza. Geb
akamtizama. “Geb kwamba anafanana jina na yule baba watoto wako?” Fifi akauliza
kwa sauti iliyoishiwa nguvu. Nanaa akatingisha kichwa kukataa. Fifi akajua
amekamatwa. Akaweka kapu la chakula chini, akaondoka bila kuaga. “Kakamatwa
vibaya! Maneno yote yamemwisha.” Yule mgonjwa wa kitanda cha jirani akaanza
kucheka. “Yaani maneno yote yale aliyokuwa akiongea, kumbe bwana mwenyewe hata
sura hamfahamu!” Yule mama alizidi kucheka. Nanaa akabaki akicheka kimya kimya
huku akifikiria pakuanzia.
~~~~~~~~~~~~
“Angalia ni nini ameleta, ili
kama vimepungua nikanunue kabla yakuondoka.” Nanaa akavuta lile kapu. Alileta
kila kitu alichomuomba na zaidi. “Naona kila kitu kipo, asante.” Nanaa akataka
kujimiminia, Geb akamsaidia. “Naomba ule kidogo Geb. Huo uji ni mwingi sana.” “Hapana.
Wewe kula tu. Mimi nitarudi nyumbani. Nitakula, ndio niende kazini.” Nanaa
akamwangalia, akanyamaza. “Si kwa sababu nyingine yeyote ile, Nanaa. Nataka uwe
na chakula cha kukutosha siku nzima. Ili ukisikia njaa tena, ule. Umenielewa?”
“Nimeelewa. Naamini nitatoka.” “Ila naomba usilazimishie. Acha wakuruhusu
wenyewe.” Nanaa akanyamaza.
“Unanielewa? Kama ni swala la
kuwahi watoto naweza kuwa nakuletea hata hapa.” “Hapa sio sehemu sahihi kwao.
Bado wadogo sana. Sitaki waje hapa wachukue magonjwa. Nitakuwa sawa tu Geb.
Acha nitoke hapa nipate muda na wanangu. Magesa hanifahamu kabisa! Na Liv naye
bado anaonekana hanielewi kwa nini sipo naye. Nakuwa napotea kwenye maisha yake
na kurudi kwa sekunde chache, halafu napotea tena. Unakumbuka muda niliokuwa
hospitalini wakati wa ujauzito wa Magesa?” “Nakumbuka. Alikuwa anahangaika
kweli kukutafuta. Hata sasa hayupo sawa kabisa.” “Nimemuona. Naogopa
itamuathiri zaidi. Kama umenipa nafasi yakuwa naye, acha niitumie vizuri.
Nitajitahidi kunywa dawa na kupunguza au kugawa muda wa kazi. Ili niwe nao.” Nanaa
wa mipango akarudi.
“Unafanya kazi gani?”
“Tunatengeneza vitafunwa na kusambaza maofisini na kwenye masherehe.” Geb
akanyamaza. Nanaa akaendelea kula. “Mchana ungependa nikuletee nini?”
“Usihangaike juu yangu Geb. Umekuja hii asubuhi, inatosha. Maadamu dada Fifi
amejua nilipo, sitakuwa na shida tena. Atanihudumia tu. Halafu pia ana gari.
Hata nikiruhusiwa, atanisaidia usafiri. Kwa hiyo nikiruhusiwa hapo baadaye,
nitamtafuta Jeri, nimtaarifu kila kitu. Halafu nitamuelekeza kule tunapoishi
ili awe anawaleta watoto.” Geb alijua ndio hajakaribishwa hivyo.
“Lakini kama watanitoa leo,
nikarudi nyumbani kwangu salama, nitajitahidi kuweka mazingira mazuri kwa ajili
ya watoto. Usafi na kupanga vizuri ili kuwe na nafasi yakutosha. Ili wanangu
wakija hata kwa masaa machache, wapate pakucheza. Ni padogo, lakini najua
patatosha tu.” Nanaa akakumbuka kitu.
“Itabidi nikitoka hapa,
nimuombe dada Fifi anipitishe madukani kwanza ili ninunue tv kwa ajili ya Liv.
Ili akija akitaka kuangalia cartoons zake, asikose. Halafu itabidi ninunue na
feni. Ili..” “Nanaa! Naomba utulie.” “Sitaki wanangu waje wajisikie wapo kwenye
mazingira ya ajabu sana. Japokuwa hayatakuwa sawa na kwao, lakini angalau
wapate vitu vya muhimu.” “Wanakutaka wewe. Acha kufikiria mambo mengii. Kitu
cha msingi na maana ni uzima wako kwao. Basi. Wakukute unafuraha, ili wapate
pumziko. Jitahidi kufuata masharti ya madaktari, hilo ndilo la msingi.” Nanaa
akanyamaza.
Akaendelea kula. “Hujanijibu
unataka kula nini mchana.”“Naomba usihangaike Geb. Dada Fifi ata..” “Hutaki
nirudi tena hapa?” “Nakuonea huruma Geb. Najua una mambo mengi. Umechoka.
Unahitaji kupumzika.” “Nitapumzika ukitoka hapo kitandani.” Nanaa akaona
machozi yanamtoka. Akakumbuka vile Geb anavyokuwa naye wakati wote anapokuwa
hospitalini. Tena bila kuchoka.
“Bado unapenda vanila Ice cream
au unataka nikubadilishie?” “Nakula kila kitu Geb.
Sichagui.” “Basi mwambie Fifi, nitaleta chakula cha mchana.” “Sina simu. Labda kama daktari atapita mapema, nimuombe vitu vyangu.”
“Nikitoka hapa, nitampigia kuzungumza naye juu yako, nitamkumbusha juu ya simu
yako.” “Nakushukuru Geb.” Nanaa
akashukuru.
“Basi ngoja nikamuwahi na Magesa.
Napenda kumlisha mimi mwenyewe uji wa asubuhi kabla sijaenda kazini.” “Dada
mkubwa bado anaamka saa 4?” Nanaa akauliza. “Bado mpenda usingizi vile vile ila
hali kabisa.” Nanaa akabaki kimya, anafikiria. Akavuta pumzi kwa nguvu.
Geb akaona anazishusha taratibu. Huku anafuta machozi.
“Nawahurumia
wanangu! Wanalipa garama ya makosa yangu.” Nanaa akaanza kutokwa na
machozi. “Huwezi amini jinsi Roho wa Mungu alivyokuwa
akinisisitiza nikwambie ukweli wote lakini hofu ilinishika kabisa, nikaogopa
kukwambia. Hakuna siku inapita bila kujutia Geb. Najuta kupita
nitakavyokwambia. Ila basi tena. Najua itakuwa ngumu kuniamini tena, lakini
sikukusudia kukuumiza Geb. Ni hofu ndio ilinikamata. Niliogopa usije ukani…” Nanaa
akaona haitasaidia tena. “Daah! Basi tena. Mungu awarehemu wanangu tu
sasa. Sina jinsi tena. Nilishaharibu mimi mwenyewe.” Nanaa
akaona anyamaze tu. Wakabaki kimya kwa muda kila mtu akiwaza lake.
~~~~~~~~~~~~
Geb ndio alikuwa anajua sasa
matokeo au athari ya anachokiongelea Nanaa. Anaona shida wanayopitia watoto wao
kwa wakati ule bila mama yao. Mama yake alishachoka kwa hakika. Ule moto
alioanza nao wakati anapokonya watoto wa Nanaa, hata Geb aliuona ni kama
umeisha wote. Si kupungua tena, nikuisha kabisa. Ni kama alishalemewa. Watoto
wawili wadogo! Mmoja aliyekuwa akiyajua mapenzi ya mama aliyekuwa anauchu wa
kuzaa mtoto na kumpa mapenzi yote aliyokosa yeye. Ambaye ni Liv. Liv aliyajua
mapenzi ya mama yake kwa kushikwa na kuongeleshwa. Ungemkuta Liv mkononi mwa
mama yake, au akiwa na mama yake! Huwezi kuiga jinsi ya kuishi na huyo mtoto.
Ni kule maisha yalikompitisha Nanaa peke yake, ndiko kulikomuwezesha kumlea Liv
kwa namna ile.
Magesa alitolewa kwa mama yake
hata kitovu kilikuwa hakijaanguka. Mtoto anayehitajika mapenzi ya mama kwa
masaa 24. Ratiba zake za kulala zilikuwa bado zinabadilika. Wakati mwingine
mchana ndio usiku, usiku ndio mchana. Tena hata ulalaji wake ni wa masaa
machache machache, kwa kuwa alikuwa bado anakula vyakula vyepesi. Akikojoa tu,
tayari njaa. Ziwa la mama yake ndilo lilikuwa kitulizo.
Siku chache alipokuwa amezaliwa, haikuwa ikimsumbua mama G.
Hata kama atakesha naye usiku, basi alijua asubuhi atampelekea mama yake
hospitalini. Atamnyonyesha mpaka alale ndipo anarudi naye nyumbani. Akiamka
hata akilia, ni kwa muda mfupi, tena akizidisha kusumbua atampa maziwa ya chupa
na kumrudisha hospitalini kwenye nyonyo ya mama yake, anatulia. Akiwa na
shuguli zake, anawaacha watoto wote hapo hospitalini kwa wazazi wao. Anakwenda
kufanya shuguli zake. Akirudi, watoto wanakuwa walishalishwa mpaka chakula cha
usiku.
Tena wakati mwingine Geb alikuwa
ameshawaosha hata nakuwavalisha nguo zakulalia. Anamuwekea watoto kwenye gari, anakwenda kuwalaza akisaidiwa na Jeri.
Asubuhi anawarudisha kwa wazazi wao, Nana ana Geb. Au Jeri anawarudisha
hospitalini. Maisha yakawa rahisi sana.
Wakati anampokonya Nanaa,
watoto walikuwa wameshiba. Usiku uliopita walikuwa na wazazi wao. Liv aliambiwa
mama yake anarudi siku hiyo nyumbani. Akasaidia matayarisho yote yakumpokea
mama yake. Akaambiwa atakuwa akiendelea kunyonya na mdogo wake. Hapakuwa na
shida.
Mambo yalianza kumbadilikia
mama G, mara tu watoto wale walipoamka nyumba nyingine, bila mama yao.
Waswahili husema, ‘mtoto
wa mtu, mtamu akiwa amelala!’. Hayo ndiyo aliyopambana nayo bibi huyo.
Liv alitolewa kwa mama yake akiwa amelala. Ndani ya gorofa lenye kiyoyozi na
mazingira mazuri sana. Akahamishiwa kwenye gari ya thamani, akapelekwa kwenye
nyumba nyingine ya baba yake. Iliyojazwa thamani kama yazamani.
Geb alihakikisha kila kitu cha
nyumba aliyokuwa akiishi na Nanaa, kipo kwenye ile nyumba nyingine ili watoto
wake wasione tofauti. Aina ya vitu vya nyumba ya kwanza vikanunuliwa kwenye nyumba
hiyo waliyohamia. Tena na thamani zaidi, lakini bila Nanaa.
Yeye na mama yake walijua wale
watoto ni wa Nanaa tokea siku wanaamka upande wa pili, bila mama yao. Ubabe
ndio uliwasaidia siku za mwanzoni wakiamini watoto wale watazoea maisha mapya
na kuwa sawa. Nyumba ilikuwa ikijaa vilio kuanzia asubuhi mpaka asubuhi. Ndio
maana wakati mwingine mama G alipokuwa akilemewa, alikuwa akimtuma Jeri
awapeleke kwa mama yao lakini asiwaguse.
Kidogo Magesa akaanza kuzoea.
Akawa akipewa chakula kingi mpaka tumbo linasalimu amri, inabidi kulala tu. Ila
sio Liv aliyekuwa akimfahamu mama yake. Geb na mama yake walihangaika na huyo
mtoto mpaka wakasalimu amri. Vicheko vilikoma. Zile dimpozi walizozoea kuziona
kutoka kwa Liv zilikoma kabisa. Akawa mtoto mnyonge sana.
Afya ya mama G nayo haikukawia
kumkumbusha umri wake. Wakati akipambana kubeba watoto ili kuwatuliza na
kumuonyesha Geb kuwa kila kitu kipo sawa, mgongo haukukawia. Kutokulala vizuri
na vilio vya watoto wawili mchana na usiku. Na pia alimuongeza Sara kwa haraka
ili kuziba pengo la Nanaa. Akidhani pengine atasaidia ile hali, lakini kumbe
ndio akawa ameongeza tatizo jingine. Mtu mwingine anayemtesa kwa wasiwasi.
Akihangaika kufunika makosa yake kwa Geb, huku akiteswa na wasiwasi huko
anakokwenda siku nzima na kurudi amechelewa! Binti mdogo, aliyekabidhiwa na
wazazi wake kwa heshima. Akipatwa na matatizo huko anakokwenda, itakuaje?
Wasiwasi ukaongezeka kwa mama G. Akazeeka siku si zake.
Geb mwenyewe hakuna usiku
aliokuwa akilala masaa zaidi ya matano mfululizo sababu yakumuhurumia mama yake
usiku na mtoto mchanga. Wakati mwingine akimsikia ameamka, inamlazimu na yeye
kwenda kusaidia. Akirudi kulala na yeye, usingizi hauji kwa haraka. Alishazoea
kubembelezwa na Nanaa ndipo alale. Nanaa alimzoesha kumshika shika mwili wake
hasa kumchezea nywele mpaka analala. Ikabidi aanze tena kujizoeza kujibembeleza
kulala mwenyewe. Mpaka usingizi unarudi tena, na muda wakuamka tena Magesa
unakuwa umefika na kuhitajika kwenda kazini. Hamna tena kulala. Zilikuwa
zimejaa fujo kwenye maisha ya familia hiyo ya Magesa, Nanaa hakuwa na taarifa.
Kwa upande mwingine ni heri hata ya yeye Nanaa alikuwa akilala usiku na
kuendelea kuwaza watoto wake siku nyingine inapoanza. Tena wakati mwingine hata
mchana alilala sababu ya usingizi mzito wa mimba.
~~~~~~~~~~~~
Wakajikuta wote wapo kimya,
kila mtu anawaza lake. Ni hawa hawa wapenzi wawili Mungu alishawatumia
kujidhihirisha nguvu zake za uponyaji kwa kuwatumia wao. Alithibitisha kwao
kuwa upo mkono wake juu yao, hilo halikuwa swali. Lakini bado walikuwa na vitu
wamebeba mioyoni mwao. Nakujisahau kwingi.
“Pata muda wakupumzika. Jilaze.
Nitakuona baadaye.” Geb akagutuka kutoka mawazoni, akaona ni heri aondoke pale
awahi kurudi nyumbani. “Njoo mara moja Geb.” Geb akasogea. “Kaa hapa kwenye
kitanda tuombe.” Geb akamwangalia, akakaa. Nanaa akataka kumshika ili amuombee,
kama aliyekumbuka kitu, akamuachia. “Tuombe.” Nanaa akafunga macho. “Mungu
wangu na baba yangu. Najua hata sasa unatusikia! Tunatambua uwepo wako hata
sasa, mahali hapa.” Nanaa akaanza kuomba akiwa amefunga macho. Akahisi Geb
amemshika mikono.
“Tunakupa sifa na
utukufu kwa jinsi ya vile tu ulivyo. Tunatubu na kujitakasa…” Nanaa
akaendelea. Mwili mzima ulikuwa ukitetemeka kwa kushikwa na Geb. Lakini
akaendelea kuomba. “Tunaipokea siku ya leo kwa shukurani. Namkabidhi Geb
mikononi mwako. Mlinde na kila hila ya muovu. Mpe faraja na amani moyoni mwake.
Mbariki, mpe nguvu na shauku ya kuendelea kukupenda wewe. Msaidie..”
Akamuombea mpaka akamaliza. “Amen!” Geb
akafungua macho, yakagongana.
“Asante kwa maombi mazuri.” Nanaa akatoa tabasamu ambalo halijawahi kuongopa moyoni mwa Geb. Ni kweli akaanza kupokea faraja yake ile aliyoikosa kwa hasira kali na kumkimbia Nanaa. Akaona maombi ya Nanaa yameanza kujibiwa. Bado alikuwa amemshika mikono. “Naamini utakuwa na siku njema.” “Nakuombea na wewe Nanaa.” “Asante. Nisalimie wanangu.” Geb akasimama. “Nitakupigia picha. Nikuletee umuone Magesa, na dada yake akiwa amelala.” Nanaa akacheka. “Nitashukuru.” Geb akaondoka.
~~~~~~~~~~~~
Hata kama una presha ya namna
gani, lazima upone. Geb aliyerudi sasa hivi amepoa na amemkubali mpaka mtoto wa
Malii! Shida kwa Nanaa inatoka wapi tena? Watoto ataletewa. Ahadi ya Geb kurudi
mchana ipo. Tena anarudi na picha za watoto wao! Na ice cream juu! Mungu ampe
nini? Presha ikaanza kujitengeneza yenyewe. Akajigeuza mara mbili, ya tatu
usingizi ukamchua. Akalala kama mtoto mchanga.
~~~~~~~~~~~~
Haikuwa hivyo kwa Geb mara
aliporudi nyumbani. Wakati Nanaa anauchapa usingizi wa furaha kule hospitalini,
yeye alipokelewa na kilio cha Magesa. Alimkuta akilia mpaka dada yake akawa
ameamka anasikiliza kilio cha kaka yake. Sura ya mama G ilikuwa imebadilika.
Alionyesha wazi anaweza kupokea msaada wowote ambao angeweza kupewa. Alichoka,
na wazi alionyesha ana maumivu.
Geb akampokea mtoto maana
walikuwa wakizunguka nyumba nzima. “Mlete nikupokee.” Bila hata kujivunga,
akamkabidhi kwa haraka, akaanza kujinyosha. “Ni nini Magesa?” Geb akamuuliza
kwa kumuhurumia mtoto wake. Alikuwa mwekundu kama moto kwa kulia. “Au tumbo
limejaa gesi?” Alipogeuka kupata jibu kutoka mama yake, hakumkuta. Alishaondoka
zamani. Akawa amebaki na watoto wake wawili. Swali la kama amekula au la,
lilishapata jibu. Hakuona kibakuli chochote pale kwenye kiti cha Magesa. Na
ndio ilikuwa saa mbili asubuhi wakati Geb anaingia hapo ndani. Kwa hali ile,
Geb akajua kilio chake huko chumbani alipokuwa amemuacha amelala, ndicho
kilichomuamsha mama yake, na ndio walikuwa wakibembelezana wakati wote.
“Twende nje tukambembeleze
mtoto.” Alimwambia Liv. Liv akamtizama baba yake, akarudisha macho kwenye tv
aliyokuwa amejiwashia mwenyewe baada yakuamka nakumkuta bibi yake
anabembelezana na mdogo wake. Geb akajua amemsikia na kumuelewa, ila hataki.
Hata hivyo akajua hana nguvu. Alilala bila kula. Geb akatoka yeye na Magesa.
Akazunguka na huyo mtoto hapo nje akilia huku akimpiga piga mgongoni, mpaka
akalala.
Ilichukua kama dakika 10 mbele
ndipo akanyamaza. Tena akiwa anapingana na wazo lakumpeleka hospitalini
wakamwangalie ni nini kinamsumbua. Alirudi kukaa naye pale barazani akiwaza,
mwishowe akaamua amrudishe kulala. Yeye akatoka nje.
~~~~~~~~~~~~
Cha kwanza akampigia simu
dakatri wa Nanaa, Lyamu. “Inagarimu nini kumrudisha Nanaa kwenye hali yake yazamani?” Ndilo
swali la kwanza alilouliza Geb, mara daktari wa Nanaa kupokea simu. Lyamu
akatulia kidogo kama anayefikiria pakuanzia, Geb akatulia tu. Kisha akaanza. “Zipo njia
mbili. Japo sio kwamba ndio atapona kabisa lakini itasaidia. Ya kwanza ambayo
Nanaa anakataa au ambayo hajawahi kuikubali ni ile yakutoa huyo mtoto. Hapo
atapona kwa haraka. Kwa kuwa mimba na matatizo aliyonayo sasa hivi ndio
vinachangia kupandisha presha yake. Ata..” “Na ya pili? Maana hiyo najua
haitakaa ikatokea. Nanaa hawezi kukubali.” Geb akamkatisha.
“Kuna dawa nimeshauriwa na daktari wa
mambo ya moyo. Wamesema ni nzuri au zitakuwa salama kwake na mtoto pia,
zinaweza kumsaidia. Japo ni garama sana. Ndio najiandaa kwenda kuzungumza naye.
Ili..” “Naomba uzungumze na mimi.” Geb akamuwahi.
“Samahani Geb. Naelewa kwa sehemu mlipo
wewe na Nanaa kwa sasa. Amenieleza kwa sehemu kile mnachopitia. Ameniambia hampo tena pamoja. Na kama chochote
kikitatokea kwake, na mtoto akapona, Frida au Fifi kama anavyomuita yeye, ndio
anadhamana na huyo mtoto. Wanaonekana wamekubaliana kwa maandishi. Na amemuweka
Frida kama mtu atakayeingia naye chumba cha kujifungua. Wamelipia garama za
‘private delivary’. Kwamba niwepo mimi muda wa kujifungua na nilazima Frida
awepo kwenye hicho chumba atakachojifungulia. Ndiye mtu anayemleta kliniki
pia.” Moyo wa Geb ulinyong’onyea kabisa. Akapooza.
“Kwa hiyo hatima yake kwa sasa naomba
nikazungumze na yeye mwenyewe.” Daktari akaendelea. “Nimeelewa.
Lakini unafikiri kama atakubali hizo dawa, anaweza kuruhusiwa lini?” Geb
akauliza. “Wewe unamjua Nanaa. Sitashangaa nikamkuta ananisubiri hata
sasa hivi hapo kwenye mlango wa wodini, aniage.” Geb akacheka kidogo. “Lakini kama
angekuwa mgonjwa mwingine ungefanyaje?” Geb akaendelea kuuliza.
“Angeanzishiwa dawa mpya. Kisha akapewa
siku hata mbili mbele zauangalizi akiwa hapo hapo hospitalini. Ili kujua kama
dawa zinafanya kazi au la. Lakini kwa Nanaa utajua kama zinafanya kazi kwa kuwa
hatanitafuta tena. Au zimemkataa kwa kuwa atarudi akiwa anakaribia kufa, huku
ana masharti yake. Kwa hiyo kwa Nanaa, tutajua mbele ya safari. Ngumu kusema na
kutabiri. Lakini Geb!” “Nakusikiliza.” “Safari hii Nanaa ni mgonjwa. Sio sababu
ya mimba tu, lakini moyo wake umepanuka. Unakumbuka mara ya mwisho mlipokuwa
naye hospitalini nilikutahadharisha madhara yakutofuata masharti ya zile dawa?” Geb akanyamaza.
Akakumbuka wakati anamtoa Nanaa
hospitalini baada ya kujifungua Magesa, daktari alimsisitizia kumfuatilia Nanaa
kwa karibu sana. Kuhakikisha anatumia dawa kama alivyoandikiwa. Matokeo yake
kesho yake tu alimuacha na kumpokonya kabisa watoto, nakumuongezea madhara
zaidi. Alishindwa hata kumjibu dokta.
“Sasa moja ya madhara ya kukaa na presha ya juu sana
bila kuitibu kwa muda mrefu, ni hayo. Moyo wa Nanaaa umeanza kusumbua. Kwa
jinsi alivyozungumza na yule daktari wa moyo hakuwa hata akijua dawa zenyewe
zilikuwa wapi. Kwa kifupi hakuendelea na matibabu yeyote yale.” Geb
akakumbuka aliziacha kwenye gari lake.
~~~~~~~~~~~~
Kumbukumbu ilimjia siku
wanatoka hospitalini. Yeye ndiye aliyekwenda kuchukua dawa hizo na kulipia
garama zote za Nanaa na Magesa. Akaenda kuzifungia dawa hizo mbele ya gari,
kwenye dashboard draw, mbele ya kiti cha abiria. Jioni waliporudi nyumbani
wakakuta watu wakiwasubiria. Sherehe ya kukaribishwa Nanaa na Magesa nyumbani
pamoja na birthday ya Liv, vikachanganya. Akakumbuka Nanaa alikwenda kulala.
Akamuamsha ili ale chakula ndipo ampe dawa. Wakati Nanaa anakula ndipo Malii
akaingia na kusababisha maafa. Hakujali presha hiyo ya Nanaa hata baada ya
kubakwa kwake, akijua wazi aliruhusiwa akiwa bado mgonjwa. Lakini alisisitiza
mpenzi wake aruhusiwe tu, atahakikisha anafuata masharti ya daktari, atatumia
hizo dawa na yeye mwenyewe Geb, akatoa
ahadi ya kumrudisha Nanaa hospitalini kila inapotakikana ili kumuona
daktari wa moyo.
Ni kesho yake tu baada ya kumpa
huyo daktari ahadi hizo, ndipo alipoondoka kikatili sana akimuacha Nanaa akilia
sakafuni. Hakukumbuka dawa wala ugonjwa wa Nanaa, ila hasira kali juu yake.
Hapo ndipo daktari anamkumbusha juu ya hizo dawa alizotakiwa kumpa Nanaa.
Aliishia kuzinunua na kuzifungia kwenye gari.
Akajua kwa miezi hiyo sita,
zitakuwa pengine zilishatupwa wakati ameenda kusafishiwa gari yake. Kwanza
alishabadili aina ya gari alilokuwa akitumia. Lile alikuwa akilitumia mara
chache sana anapokuwa na Nanaa tu. Lilikuwa ni lile gari lenye milango miwili.
Lilitolewa pale alipokuwa akiishi Nanaa, na kuhamishiwa nyumba waliyorudi
kuishi na mama yake na watoto, akalisusa hapo kwa kuwa lilimkumbusha Nanaa kila
anapoingia humo. Akaona alitelekeze kabisa.
~~~~~~~~~~~~
“Kwa hiyo mbali na ujauzito alionao,
tayari Nanaa ana matizo ya moyo.” Daktari akamalizia. “Ameniambia
unaweza ukawa na simu yake.” “Ninayo. Niliificha kwa makusudi ili apumzike.
Ilikuwa ikiita nakuingia jumbe kila baada ya dakika. Ikabidi kuizima ili angalau
alale. Ila leo nitampelekea vitu vyake vyote. Sijui kwa nini, lakini hisia
zangu zote zinaniambia hatalala leo hospitalini! Ataondoka tu.”
Geb akacheka kidogo. “Na mimi nitarudi huko baada ya muda mfupi sana.
Sitachelewa.” Wakaagana.
~~~~~~~~~~~~
Geb akarudi ndani akakaa
pembeni ya Liv. “Unataka kunywa uji au maziwa?” Kimya. “Liv?” Hata hakugeuka
kumwangalia baba yake. Akabaki kimya macho kwenye luninga. “Twende
nikakubadilishe diaper.” Geb akaendelea. Baada ya sekunde kadhaa Liv akashuka
pale kwenye kochi kuelekea chumbani kwao. “Tunaenda kwanza kuosha uso na meno.”
Geb akaendelea kuzungumza naye akiwa nyuma yake. Mpaka anamalizia hiyo
sentensi, Liv alishafika bafuni. Akamuosha vizuri na kumbadilisha nguo.
Wakatoka.
Akarudi kukaa kwenye kochi. Geb
akamfuata. “Naenda kumuona mama Liv, unataka twende wote?” Liv akamwangalia,
akavuta mtandio wa mama yake vizuri. Akaushika nakurudisha macho kwenye luninga.
Geb akafikiria kidogo. Akamvuta na kumbeba. “Pole Liv.” Liv akajiegesha vizuri
pembeni ya shingo ya baba yake, akatulia. Geb akaona atoke naye. Akamchulia
begi lake lenye vitu baadhi vyakubadilisha, akatoka naye, kuelekea hospitalini
alikokuwa amemuacha Nanaa.
Katika swala la uelewa, Geb
hakulitilia mashaka. Japokuwa hata miaka miwili hakuwa ametimiza, lakini Oliva
alikuwa na uelewa wa hali ya juu. Hakuna aliyekuwa akizungumza naye kama mtoto
mdogo. Eti zile sauti za kitoto, kwa Liv hawakumfanyia. Walizungumza naye kama
mtu mzima, na yeye alielewa.
~~~~~~~~~~~~
Akiwa anaingia kwenye geti la
hospitalini. Ilishakuwa saa tano asubuhi. Hakuwa akikumbuka cha ice cream wala
chakula cha mgonjwa. Simu ya Nanaa ikaingia. “Ni mimi Nanaa.” Geb
akacheka nafsini mwake. Alikuwa na namba yake, alipewa na Jeri. “Vipi?” “Nilipiga
kukutaarifu kuwa ninatoka hospitalini.” Geb akakumbuka maneno ya Lyamu.
“Nanaa!” Geb
akashangaa. “Hapa nilipo nipo nasubiria dawa tu, niondoke. Nimempigia
simu dada Fifi. Atakuja kunichukua.” “Subiri kwanza Nanaa. Umeruhusiwa au
umeamua kuondoka?” Geb akauliza.
“Nina mambo mengi sana yakufanya Geb. Sina
muda wakulala hapa Muhimbili.” “Uko wapi?” Nanaa akamuelekeza alipo. “Mpigie simu
Fifi, mwambie mimi nitakuchukua. Ndio nipo hapa getini.”
Nanaa akatulia kidogo, kama aliyeshangazwa na ujio mwingine tena
wa Geb. “Nanaa?” Geb akaita. “Nampigia sasa hivi.” Wakaagana.
Alimuona kwa mbali amekaa na mizigo
yake yote, kuashiria hatarudi tena wodini. Akampigia simu. “Geuka.” Nanaa
akageuka vizuri. Akamuona yupo ndani ya gari yake kubwa aliyokuwa akitumia Jeri
kwa ajili ya watoto. Akampungia mkono. “Njoo.” “Bado sijapata dawa, Geb!
Nasubiria waniite jina langu.” “Njoo mara moja tu.” Nanaa
akaanza kutembea kumfuata. Wakakata simu. Kadiri alivyokuwa akiwasogelea,
ndivyo tumaini jipya lilivyokuwa likijengeka moyoni mwake. Geb alisikia
moyo unajaa furaha.
“Nilikwambia usihang..” “Mama!”
Kabla Nanaa hajamaliza sentensi yake mara alipofika kwenye gari upande wa
dirisha alipokuwa amekaa Geb, Liv aliyekuwa amekaa kiti cha nyuma, akamuona
mama yake. “Liv wangu!” Nanaa akazunguka upande wa pili akafungua mlango. “Beba mama! Beba.” Liv alishaanza kulia. “Usilie. Ndio
nakufungua nikubebe.” Nanaa akajaribu kutulia lakini akashindwa. Machozi
yakamtoka. Akamtoa pale kwenye kiti chake, akamsimamisha pale pale pembeni ya
kiti chake akamkumbatia. Liv alimbusu mama yake zaidi ya mara tano. Kichwani,
usoni mwa mama yake alimpa hayo mabusu bila kuchoka. Geb akabaki akimshangaa
Liv. Liv huyu siye wanaye ishi naye yeye na mama yake. Ni watofauti kabisa
anapokuwa na mama yake.
“Tumbo linanguruma njaa. Hebu
tulione.” Liv akanyanyua gauni. Mama yake akamtekenya, Liv akacheka. “Hili
tumbo halina kitu Liv. Lazima ule.” “Nyonyo!” Nanaa na Geb wakacheka. “Nyonyo
hamna tena. Imeisha yote. Lakini ninao uji na mtori. Tuanze kwanza uji.” Liv
akatingisha kichwa kukubali. “Beba.” “Nakubeba Liv. Lakini nisubiri nakuja sasa
hivi. Nimeacha mizigo yote pale…” “Mmhhh mama!
Beba. Beba mama!” Liv akaanza kulia tena. “Nitarudi sasa hivi Liv!
Sidanganyi.” Liv akazidi kulia akimshikilia mama yake. Nanaa akambeba. “Basi
ngoja mimi nikafuate. Wewe kaa hapo mbele, umpakate. Hawezi kuamini tena.” Geb
akateremka na kwenda kuchukua yeye hizo dawa. Nanaa akambeba huku akilia. “Pole mwanangu. Pole sana Liv.” Nanaa akaendelea kumbembeleza
wakiwa wamekaa kiti cha mbele.
Akashangaa Geb amechukua muda
kidogo kurudi. Maana ilikuwa ni kitendo chakuchukua kikapu na kugeuza tu.
Akahisi aliyemwachia mizigo yake amwangalizie amemkatalia. Kumbe Geb alifika
pale akakuta ndio na jina la Nanaa likitajwa akachukue dawa. Nanaa akampigia. “Nalipia
dawa.” Geb akajibu mara baada yakupokea. “Acha
usilipe. Nakuja sasa hivi. Ninazo pesa.” Nanaa akamuwahi. “Nimeshawakabidhi
pesa. Usiwe na wasiwasi.” Geb akakata simu.
Akarudi baada ya kuchukua kila
kitu. “Samahani Geb. Nakuingiza garama zisizo
kuhusu. Naomba nipe pochi yangu hapo nyuma, pembeni ya kiti cha Liv,
nikurudishie pesa yako. Najua ni garama sana.” Geb akakunja uso. “Kweli
naomba nikulipe tu Geb. Ninazo pesa. Huna sababu yakunisaidia.” Alipoona bado
Geb anamtizama tu, akageuka yeye mwenyewe akiwa bado amempakata Liv, akavuta
pochi yake nakutoa wallet yake kutoka kwenye hiyo pochi, akatoa pesa. “Nashukuru.”
Akawa anamkabidhi Geb. Geb akabaki akimwangalia. “Tafadhali naomba upokee Geb.”
Nanaa akasisitiza huku ameshika ile hela.
“Naomba upokee ili nimlishe mtoto.” Geb
alikuwa amesimama nje upande aliokuwa amekaa Nanaa na mtoto wake. Akazunguka
upande wake wa dereva bila kupokea pesa, akakaa kwenye kiti chake. “Nimuwekee
nini huyo?” “Tafadhali naomba upokee Geb.” Nanaa alisisitiza akiwa bado
ameshikilia zile pesa. “Naomba chukua tu. Ninazo pesa. Nina uwezo wakujitunza
sasa hivi.” “Ndio maana na jina umebadili? Umerudi kujiita jina la mama yako,
ukatoa Magesa. Na kumuweka Fifi kama mtu wako wa karibu? Yaani unaingia chumba
chakujifungulia na Fifi!?” Nanaa akajua ameshazungumza na Lyamu.
“Naomba usinilaumu Geb.
Unakumbuka mara ya mwisho unaniacha pale kwako uliniambia hutaki kuja kuiona
sura yangu tena, na wala nisiwahi kukutafuta tena? Unakumbuka Geb?” Kimya.
“Kana kwamba haitoshi, kuweka msisitizo wa ulichozungumza kwangu, mwezi uleule
ukakata pesa uliyokuwa ukinipa ya matumizi yangu binafsi ya kila mwezi. Sikuwa
nimepanga kubakwa wala kushika mimba. Yote yamenitokea bila hata kutarajia!
Hapa ninapozungumza na wewe, sijui kaka alipo wala sijamsikia tokea siku ile.
Hivi unavyoniona nilivyo, ndivyo nimemaliza. Sina ndugu wala rafiki.” Nanaa
akaanza kutokwa na machozi.
“Mungu alinipa
dada Fifi nikiwa nimelazwa hapa hapa hospitalini. Nililazwa pembeni yake.” Nanaa
akamsimulia historia yake na Fifi kwa kifupi mpaka siku hiyo walipoonana hapo hospitalini,
tena Fifi akimtukana Geb. “Niambie Geb, ningetakiwa
kufanya nini kama sio kushika pale Mungu aliponiletea msaada? Najiitaje tena
Nanaa Magesa!? Naanzia wapi mimi? Na mtoto atakayezaliwa wa Malii naye aitwe
James Magesa?” Nanaa akauliza akiwa analia kwa uchungu sana. Geb akajua
amebeba mtoto wakiume.
“Watu wote kwenye
maisha yangu hawatabiriki! Wanatoka na kurudi vile wanavyojisikia wao. Sina mtu
anayeweza kusimama na mimi kipindi cha shida yangu. Sasa hebu niambie Geb,
nikifa chumba cha kujifungulia! Au hata nikaja kufa siku chache baadaye, huyu
mtoto anakwenda wapi? Mimi niliangukia nyumbani kwa mama mkubwa. Yeye
ataangukia wapi? Ilikuwa nilazima kumtafutia pakwenda. Na imani ikaongezeka kwa
dada Fifi kwa kuwa kwanza hana familia, halafu akamtawala mwanangu hata kabla
sijamuomba. Anamsubiria huyu mtoto kama ulivyomsikia leo asubuhi.” Geb
akabaki kimya. Akageuka pembeni akiangalia nje ya dirisha. Nanaa akaziweka zile
pesa pembeni yake. Akajifuta machozi. Akatulia kwanza.
“Naomba unimiminie uji,
nimlishe kwanza ndio tuondoke. Anaonekana ana njaa.” Geb akamimina uji na
kuanza kupoozesha. “Geb!” Nanaa akamwita, Geb akamgeukia. “Nakushukuru sana,
kuniletea Liv. Nahisi ndio dawa pekee nilihitaji leo. Nimefurahi sana.” “Na
mdogo wake naona na yeye amenibadilikia! Nimemkuta analia sana. Amekuwa
mwekundu kwa kulia muda mrefu.” “Ungemleta tu na yeye.” “Unatakiwa kupumzika
Nanaa!” “Napumzika vipi huku najua wanangu hawana furaha, Geb? Natoa wapi hilo
pumziko?” “Kumbe ningejua nisingekwambia!” “Hapana. Ni heri umeniambia, ili
nijue chakufanya. Kama sio kuwaona, basi kuwaombea. Nashukuru.” Geb akamkabidhi
uji.
“Liv mama, usilale bila kula.
Amka.” Nanaa akambusu. “Anasinzia.” “Ameamshwa na kaka yake. Alikuwa akilia
sana.” “Pole mama eeh! Kaa vizuri ule.” Liv akambusu mama yake, akajirudisha
kulala. “Namimi nakupenda Liv. Haya kaa ule kwanza.” Akajiegemeza kwa mama yake
akaanza kula. “Naomba na wewe ule, Geb.” “Na njaa inauma kweli. Asubuhi
nilijivunga nikijua nitakula nikifika nyumani, lakini sikukuta hata uji wangu.”
“Pole. Kula kitu chochote humo. Nikifika nyumbani mimi nitapika tena.” Nanaa
akajiuliza huku akiwaza moyoni. “Kwa
nini huyo mke aliyemsikia ametafutiwa Geb, hakumpikia? Au ndio alikuwa
akibembeleza mtoto?” Nanaa akawaza wakati akiendelea kumlisha Liv, na Geb
akila.
~~~~~~~~~~~~
Liv alimaliza kula bila shida.
Akamfuta vizuri. Akabaki akimwangalia. “Unataka kulala?” Liv akamwangalia mama
yake. “Macho hayo yamejaa usingizi. Lala.” Liv akalala wakati mama yake
akimpapasa kama kawaida yake. “Anapenda kupendwa huyo! Hivyo unavyomfanyia
anapenda kweli ndio maana anakukumbuka.” “Jifunze na wewe umfanyie.” Nanaa
alitoa ushauri. “Anaakili huyo. Muone hivyo hivyo. Hakubali mtu amshike hivyo
ila wewe tu.” Nanaa akambusu, akaendelea kumbembeleza.
Alipolala kabisa, akamfunga
kwenye kiti chake akarudi kiti cha mbele, pembeni ya Geb. Akatulia kidogo. “Geb!”
Akamuita. Geb akamgeukia. “Sasa hivi nataka kwenda nyumbani. Tumepata oda kubwa
siku ya kesho. Nataka nikasaidiane na kina dada Fifi, ili kukamilisha.” Geb
akabaki akimtizama. “Naweza kumuachia dada Fifi na huyo msichana mgeni wafanye
peke yao pengine nipumzike. Lakini nazitaka sana hizo pesa kabla sijajifungua.
Nataka nikusanye pesa yakunisaidia kipindi hicho nipo na mtoto nyumbani.
Nitajipa mapumziko ya kama mwezi mmoja, angalau mpaka mtoto achangamke, ndipo
niendelee na biashara na kutafuta kazi. Lakini kwa hii miezi mitatu iliyobaki,
nataka nijitume sana. Ili nisiishiwe katikati.” Nanaa alijieleza vizuri sana,
kifasaha.
Geb akageukia dirishani
akafikiria kidogo, akamgeukia. “Hivi sasa hivi mtoto ambaye umebaki ukimfikiria
ni mmoja tu? Huyo aliyekuwepo tumboni?” Nanaa akakunja uso. “Eti Nanaa?” Nanaa
hakuwa ameelewa. “Hivi umesikia neno lolote nililokwambia juu ya Magesa na Liv?
Unaona afya ya Liv ilivyo?” Kimya. “Nanaa?” Geb akaita tena.
“Naona na nimekuelewa Geb.
Nitajitahidi kugawa muda.” “Kwa hiyo hivi unavyoniambia ni kwamba,
umeshamalizana na Liv. Umeshamnywesha uji. Niondoke naye. Akalale, akiamka alie
tena mpaka kesho, nikuletee tena, umyweshe uji, niondoke naye tena, wakati wewe
unauza sambusa?” Nanaa akawa hajui tena anatakiwa afanyaje wakati
alinyang’anywa watoto.
“Unakumbuka kitu chochote
nilichokwambia juu ya Magesa?” “Nakumbuka Geb, lakini sijui natakiwa nifanye
nini?” “Kweli Nanaa? Nakwambia mtoto analia sana, wewe unaniambia unataka
ukauze sambusa ili upate pesa! Kweli?” Nanaa akaona machozi yanamtoka. “Hivi
unawataka tena hawa watoto au ndio umeniziria? Na wewe umeamua iwe zamu yako,
unikomoe? Usipokee msaada wangu tena, uniachie watoto. Hata wakiteseka, haikuhusu
tena kwa sababu nilikupokonya na sasa hivi mtoto anayejaliwa ni mmoja tu. Liv
na Magesa hawana tena maana.” “Unavyonifanyia sio haki Geb!
Sio sawa.” Nanaa aliongea huku akilia.
“Kwa hiyo unataka usawa na
mimi? Na wewe ukasirike kama nilivyokasirika mimi. Uweke hasira mbele, utafute
kunikomoa kwa kuwa nilikukosea! Tuendelee kutesa watoto. Halafu wewe ukimaliza,
na mimi nitafute tena kosa lako, nikulipize.” “Geb!” Nanaa
akashangaa, asielewe. “Ndicho unachotaka kukifanya, kwa kuwa unaona
nilichokifanya mimi nikizuri sana. Kimeninufaisha mimi mwenyewe. Ndio maana
afya yangu nzuri. Nimependeza sana. Na nikanufaisha watoto pia. Ndio maana
wanaendelea vizuri. Sasa hivi ni zamu yako. Unikomoe.” Geb akambadilikia Nanaa.
“Uliniudhi Nanaa! Ukweli
ulinikosea sana. Tena baada ya kukusihi uwe unaniambia ukweli. Nilikwambia hata
kama unajua huo ukweli utaniumiza kwa kiasi gani, nilikuomba uniambie ukweli tu
kuliko kunidanganya. Haya, yakatokea yakutokea. Unanijua kabisa ninatatizo
la hasira. Nimefanya maamuzi mabaya, si kwamba yameathiri tu watoto! Mimi
mwenyewe nipo kama mgonjwa niliyekimbia hospitalini. Najirudi kwako,
nikiwa na watoto, na wewe unanipa mipango yako yakunionyesha unamaisha yako.
Hata kama mimi hunitaki tena, ndio nakuuliza, na hawa watoto wawili pia
huwataki tena?” “Nawataka Geb. Tena nawataka kwa garama yeyote
ile, nawataka.” “Ki vipi?” Geb akauliza.
“Niambie Nanaa. Unampango gani
na hawa watoto? Nimesikia mipango yako kwa James au Jimmy. Mpaka umemtafutia
mtu wakumchukua ukifa. Sasa naomba kujua mipango ya Liv na Magesa.” Nanaa
akajifuta machozi, akatulia kabisa na kuanza kufikiria akijieleza kwa makini. “Inategemea
utakuwa ukiwaleta saa ngapi na kwa muda gani. Hapo ndipo nitajua jinsi
yakujipanga. Lakini nakuhakikishia Geb, wanangu wanakuja kwanza ndio mengine.”
Nanaa akajibu.
“Nikiamua kukupa kabisa? Yaani
nikaamua wewe ndio uishi nao. Utafanyaje na biashara hiyo uliyoanza? Si
utashindwa au utaanza kuwaona mzigo?” “Sitashindwa kuwa na wanangu Geb. Na
ninakuhakikishia sitawashindwa na wala sitawaona ni mzigo. Wewe nipe kwa
majaribio hata ya siku tatu tu, utaona.” “Hawa watoto wanahitaji uangalizi wa
masaa 24, Nanaa. Mama mwenyewe kazi zake zote zimesimama tokea siku anawachukua
hawa watoto. Mpaka juzi nimemuonea huruma nakujisuta moyoni, nikamwambia atoke
kidogo. Nikabaki nao nyumbani. Hawa watoto tulizaa karibu karibu na ni jukumu
letu. Kama wewe unaingia kwenye biashara kama mimi, itabidi mimi nijipange
upya. Lakini nimekataa, na nimejionya, hawatalelewa na mtu mwingine tena
isipokuwa mimi au wewe kuhusika moja kwa moja. Nakiri nilizidisha hasira,
nakuchukua maamuzi yaliyowaumiza watoto. Lakini nimekusudia kubadilika. Kama
wewe upo busy basi itabidi mimi nihamishie ofisi nyumbani kwa muda, mpaka
angalau wakue kidogo.” Nanaa akavuta pumzi nakuzishusha. Geb amejirudi. Amekuwa
muwazi bila kificho.
“Basi naomba mimi mwenyewe niwalee,
lakini unisaidie pesa kidogo. Sio kwa ajili yangu mimi. Ni kwa ajili yao tu.
Kwa ajili ya chakula chao, mavazi na kama ikitokea wanaugua, basi niwe nina
pesa za matibabu mazuri na ya haraka. Ila malazi ninapo sehemu yakuwahifadhi.
Nilishamlipa dada Fifi kodi ya miezi sita mingine. Nilimpa miezi 6 ya kwanza.
Kabla haijaisha, nikamuongezea mingine 6. Kwa hiyo pakuishi hapata sumbua. Nipe
miezi hata mitatu tu, uangalie. Na si lazima ukawa ukinipa mimi pesa. Wanunulie
tu vitu wanao, uwe unaniletea. Hamna haja yakunipa pesa kabisa.” “Sasa na wewe
utaishije?” Geb akauliza.
Nanaa akafikiria tena kwa haraka
na kujibu. “Mimi nitafanya shuguli zangu kama kawaida. Nitakuwa nikipika usiku
wakati watoto wamelala, asubuhi wanaenda kusambaza, mimi nabaki na watoto.”
Akamuona Geb amenyamaza. “Au nimekosea? Wewe nikosoe chochote juu ya huo mpango
wangu, nitafanya tu. Ilimradi niwe na wanangu.” Geb akaonekana hana hoja. “Ngoja
nifikirie.” Nanaa anaye akanyamaza.
Walikaa pale kwa muda, mwishowe
Geb akawasha gari. “Naomba nielekeze huko unakoishi sasa.” Geb akaondoa gari. “Geb!” “Naam!” Geb akaitika. “Najua umeniambia
unafikiria, lakini naomba leo ukinishusha nyumbani, uniachie Liv kidogo.
Angalau akiamka leo, akutane na sura yangu.” “Sawa.” Geb akakubali bila shida. “Nilikuwa
bado sijamaliza.” Geb akamtizama.
“Naomba urudi nyumbani,
ukamwangalie Magesa. Kama bado analia tumpeleke hospitalini.” “Kwa hiyo kama
amenyamaza, ndio inakuaje?” “Nashindwa chakusema Geb. Umeniambia unafikiria
mpenz…” Nanaa alitaka kusema mpenzi wangu. Akasita. Wakanyamaza kidogo. “Lakini
Geb, hata ukiniambia unishushe sehemu, nikusubiri wakati unaenda kunichukulia
mwanangu, nitakushukuru sana.” “Unamaanisha sasa hivi?” “Kabisa. Mimi niache
hata kituo cha daladala pale karibu na kwako, nitawasubiri wakati unaenda
kumchukua Magesa.” Akaona gari inageuzwa, kutafuta njia ya Tabata. Nanaa akajua
hata wao wamelemewa. Akawacheka moyoni nakujiambia, debe
limevuja, nafuu kwake mchukuzi. Anapata wanae wote wawili
bila shida.
Debe
Limevuja.
“Utataka nikuchukilie nini?”
Geb akamuuliza mara alipokaribia nyumbani kwake. “Nguo ndio kitu cha muhimu.
Mengine yote, sio lazima. Ila naomba nishushe hapo soko dogo ninunue vitu
vichache vyakupika wakati unaenda kumchukua kaka.” Geb akamshusha, yeye
akaondoka na Liv akiwa amelala. Wakati anakaribia nyumbani, akaona mama yake
anampigia simu. Akapokea. Akasikia sauti ya Magesa, akilia. “Huyu analia
sana, nizaidi ya nusu saa sasa. Na homa imeanza kuwa kali. Naona nimpeleke tu
hospitali.” “Nakuja, nipo hapa karibu tu. Nitayarishie begi lake, mimi
nitampeleka.” Geb akakata simu.
Hapo hapo akampigia Nanaa. “Naomba
usinunue vyakula. Mama anasema Magesa homa ni kali, inabidi tumpeleke
hospitalini. Nisubiri nakuja sasa hivi.” “Sawa.” Nanaa akatoka
barabarani. Hata dakika 10 hazikuisha, akaona gari ya Geb. Akasogea. Wakati
anafungua mlango, akasikia kilio cha Magesa. “Naomba nimshike. Asilie peke yake
mpaka hospitalini.” Magesa alikuwa amefungwa kwenye kiti cha nyuma. Pembeni ya
dada yake. “Kaa basi, nimfungue. Nitakupa.” Gafla wakajikuta wamekuwa wazazi
wakujielewa. Akili zimewarudia.
Magesa alikuwa akilia kama
kengele. Geb akamtoa kiti cha nyuma, akamkabidhi mama yake pale mbele. “Pole
baba. Pole sana. Nini kinauma?” Nanaa akaanza kumbembeleza nakumuongelesha kama
ataelewa. Akajifunga yeye mkanda, akamlaza kifudi fudi tumbo lake mapajani huku
akimsugua mgongoni. Akaanza kutoa hewa. “Pole Magesa mwanangu. Ni tumbo ndio
linauma?” Magesa alianza kupunguza sauti kama ambaye ameanza kupata nafuu, huku
baba yake anaendesha.
“Haya, mwangalie mama.” Nanaa akamnyanyua. “Pole sana.”
Akambusu na kumuweka kifuani, akamkumbatia vizuri huku akimbembeleza. Mpaka
wanafika hospitalini, Magesa alishalala. Geb alikuwa kimya kabisa. Mawazo
yalikuwa mbali, hata hakuwa akijua ni muda gani huyo mtoto alinyamaza.
Baada ya vipimo vingi, Magesa
akagunduliwa ana UTI. Ugonjwa ambao mara nyingi unachangiwa na kinyesi, kuingia
njia ya mkojo. “Inamaana alikuwa hasafishwi vizuri!?” Wazazi hao
wakajiuliza kimya kimya. Nani wakulaumiwa? Geb au bibi? Labda mama mtu! Hakuna
ajuae. Ilibidi aanzishiwe matibabu kwa haraka, na kwakuwa homa ilishakuwa kali
sana, ikabidi alazwe ili waishushe kwa haraka isije leta madhara zaidi.
Wanafanyaje na Liv? Lazima wachukue chumba chao peke yao. Watajua wao wenyewe
wakishapewa chumba.
Uzazi Ni Kazi.
Nanaa
akakabidhiwa chumba yeye na wanae. Magesa akapewa dawa yakushusha homa,
akamlaza kitandani upande mmoja, upande mwingine Liv. Wakabaki wamekaa yeye na
Geb. Wazo likamjia Nanaa. Akampigia simu Fifi. “Naomba niletee chakula huku hospitali ya
Agakani.” “Wewe Nanaa! Asubuhi ulikuwa Muhimbili, ukaniambia umeruhusiwa, nije
nikufuate. Mara ukaniambia nisije tena, umepata lifti ya Geb. Sasa hivi upo
hospitali ya Agakani! Wewe mtoto vipi?” “Wakati tupo njiani tunarudi nyumbani,
Geb akapata simu kuwa Magesa anaumwa. Ikabidi kumfuata, ndio tumelazwa hapa
hospitalini. Sasa nataka chakula cha Liv. Na yeye yupo hapa. Nataka akiamka
ale. Ule mtori watokea asubuhi, sasa hivi utakuwa umeharibika.” “Umeona akili
yako ikikurudia unavyokuwa mama mzuri?” Nanaa akacheka.
“Ona sasa hivi unaweza kulea na wanao!
Haya, na wewe unataka kula nini?” “Chochote kile dada yangu.” Geb
akamgusa. “Subiri dada.” Nanaa akamgeukia Geb. “Wewe
nitaenda kukununulia.” Geb akaongea kwa sauti ya chini. “Kwa nini usimuache
dada Fifi akaleta, ili wewe upumzike?” Nanaa akamjibu Geb. “Ni lini mara ya
mwisho umekula mbuzi wa kuchoma?” Nanaa akacheka sana. Fifi akasikia. “Na unibakishie
Nanaa. Sio tena ule huyo mbuzi peke yako.” “Dada Fifi kwa nyama!” “Ndiyo. Sasa
kaka mdogo naye atakula nini?” “Wamesema wataniletea chakula chake akiamka tu.
Sasa sijui watamletea nini!? Naomba na uji mzuri. Ili akishindwa chakula cha
hapa, nimuongezee uji. Lakini pole dada yangu, nakusumbua!” “Wala
usijali. Nakuja sasa hivi. Ngoja nikupikie, nilete kabla hawajaamka.” “Ndio
maana nakupenda.” Fifi akacheka nakukata simu.
~~~~~~~~~~~~
Geb akatoka. Baada ya muda
akarudi na nyama ya mbuzi yakuchoma. Nyingi pamoja na chips na ndizi zakuchoma.
Soda 4, na maji ya kunywa. “Narudi nyumbani kuoga, nibadili nguo. Nitarudi
kulala na nyinyi.” “Naomba tuombe kwanza Geb. Mungu ametukutanisha pamoja. Japo
ni hospitalini, lakini ipo haja yakushukuru nakumuombea Magesa.” Nanaa na Geb
niwazuri sana wamaombi wanapokuwa kwenye shida.
Wakashikana tena mikono
wakaomba. Nanaa alitubu kwa popote yeye na Geb walipozembea kwa watoto hao
ambao Mungu aliwapa kwa upendo. Akashukuru kwa nafasi nyingine Mungu aliyowapa
na watoto hao. Kisha akaomba amani na uponyaji kwa Magesa na Liv. Waliomba
mpaka kila mmoja wao akajisikia vizuri. “Amina.” “Amen!
Asante kwa maombi mazuri, Nanaa. Nitarudi sasa hivi.” “Nashauri upumzike
kidogo Geb. Kalale kidogo, ndipo urudi. Jua watoto wapo salama, na mimi nipo.
Naomba ulale kabisa. Hata ukija kwa kuchelewa, hamna shida. Ila unahitaji
kupumzika.” Geb akafikiria kidogo, akatoka.
Kuliko
Ungua Mpini.
Mama G akashangaa Geb anaingia
bila watoto. “Vipi!?”Akamuuliza akisikika na wasiwasi. “Magesa amekutwa na UTI.
Wamemlaza.” Geb akajibu kwa kifupi. “Nilivyokuwa nikijitahidi kumbadilisha
diaper! Sijui kapataje huo ugonjwa! Sasa umewaacha na nani?” Mama G akauliza
tena huku akijisikia vibaya. “Wapo na mama yao.” Geb akajibu nakuingia chumbani
kwake. Mama G akabaki ameduaa kama dakika tano. Hajui aseme nini.
Ndipo akamfuata Geb chumbani. “Asubuhi
nililemewa nikakusahau chakula. Ila nimekupikia. Uje kula.” “Nataka kama lisaa
limoja tu lakulala. Nitakuja kula kabla sijarudi hospitalini.” “Niwapikie nini
huko?” “Usipike kitu chochote. Wewe pumzika tu.” Geb akajirusha kitandani vile
vile na viatu akalala. Alijirushia hapo kitandani saa 8 mchana, akaamka saa 11
jioni. Akaingia kuoga harakahara, akatoka akiwa na haraka.
“Naomba tuongozane.” Mama G,
alikuwa akisubiria kwenye makochi. “Naomba uje kesho mama. Leo pumzika tu.”
Mama G akajua hatakiwi. “Basi kula kwanza.” Geb akafikiria kidogo, akarudi
kukaa. Akatoa simu nakumpigia Nanaa. “Vipi?” “Safi tu.”
Nanaa kajibu. “Nilipitiwa na usingizi.” “Ndio vizuri umepumzika. Daktari
alirudi tena, wameona wamwanzishie dripu ya maji. Wamemuwekea na dawa humo
humo. Wameniambia itamsaidia kwa haraka, hata akikataa kula itamsaidia. Kwa
hiyo amerudi kulala. Halafu niliwaomba waniletee kitanda cha mtoto. Crib.
Wameleta. Naona dada nitamlaza hapo.” “Anafanyaje sasa hivi?” “Amekula vizuri
kweli! Nimemuogesha, yupo hapa tumepakatana, anaangalia cartoons zake.” Geb
akatulia kidogo.
“Sasa si utakuwa na wewe umechoka?” “Hapa nimejilaza kwenye kochi. Dada amejiegemeza kwangu huku anaangalia tv. Nilikuwa nasinzia. Yaani wewe ndio umeniamsha.” “Pole. Nikuletee nini?” “Nimeshiba. Dada Fifi alikuwa hapa. Akaongeza tena vyakula. Tumekula ndio akaondoka. Nipo tu sawa. Wewe pumzika. Tutaonana hiyo kesho.” Geb akakata simu. Akala vizuri akashiba, akatoka baada yakumuaga mama yake nakumuelekeza hospitali na chumba alicholazwa Magesa.
Njiani akampigia simu Grace. “Naomba
uendelee kushikilia kazini. Nitakuwa hospitalini na Magesa. Amelazwa.” “Poleni
Geb. Basi mwambie mama aniambie nini anataka niwaletee hospitalini.” “Mama yupo
nyumbani.” “Kwa hiyo upo mwenyewe hospitalini!?” Grace akaendelea kuhoji
akimuhurumia kaka yake. “Sasa hivi wote wawili wapo na mama yao huko hospitalini.
Mimi ndio naenda huko sasa hivi.” Grace
akapatwa na kigugumizi. “Mama yao Liv na Magesa au mama yetu sisi?” Grace
akahoji zaidi. “Wapo na Nanaa.” Grace akanyamaza, Geb akakata
simu.
Baada ya muda Grace akapiga
tena simu. “Wamelazwa wodi gani?” Geb akamuelekeza hospitali
waliyopo na chumba. “Lakini naomba labda uje kesho. Naomba leo tuwaache kwanza.
Hasa Liv. Anataka muda na mama yake.” “Sawa.” Geb akakata simu.
~~~~~~~~~~~~
Liv alikuwa akicheza mwilini mwa mama yake huku akiangalia cartoons zake wakati baba yake anaingia. Nanaa alikuwa amejilaza chali kwenye kochi. Liv alipomuona tu baba yake ameingia, akajificha nyuma ya mama yake. Nyuma kabisa. “Wala sikuchukui. Nataka tu unisalimie. Njoo.” Liv hakutoka hapo nyuma. “Njoo uchukue ice cream.” Liv alikataa kabisa. Akaendelea kujificha. “Nimekuletea na wewe ice cream.” Nanaa akakaa. “Hata hivyo ameshiba. Amekula sana.” Nanaa akatetea.
Mama G Na Grace.
Asubuhi wakati Nanaa na Geb
wanaomba. Mama G na Grace wakaingia. Walimkuta Geb na Nanaa wamepiga magoti
pembeni ya kitanda kingine kidogo alichokuwa amelazwa Magesa. Hawakugeuka
wakati wanaingia. Wakaomba kama dakika tano mbeleni, ndipo wakamaliza. Geb akamsaidia
Nanaa kusimama. Ile kuamka, mama G na Grace ndipo wakagundua Nanaa ni mjamzito.
Wakabaki wameduaa. “Shikamooni.” Nanaa akasalimia, nakuchukua kipochi chake
akatoka. Hata yeye aliwaona jinsi walivyomshangaa.
Alipotoka tu, Geb akamfuata. “Nanaa!”
“Nitarudi Geb. Nawapa nafasi na watoto.” “Naomba usiondoke tafadhali.” Geb
alisisitiza wakiwa wamesimama nje tu ya mlango. “Hawa watu wamekuja kuona
watoto, sio mimi. Ndio nawapa nafasi au uhuru na watoto. Watakapo ondoka,
unaweza kunipigia simu, nikarudi. Sitaki uwepo wangu uwe kero.” “Haiwezekani
Nanaa. Naomba uje. Wewe sio kero.” Nanaa akakunja uso akageuka vizuri.
“Geb! Naweza nikawa vitu vingi,
lakini mimi sio mjinga. Tafadhali, naomba watoto wangu wakiamka na ndugu zako
wakiondoka, nipigie simu nitarudi.” “Nanaa! Si tumetoka kuomba sasa hivi!?
Unafikiri maombi yetu yatajibiwa vipi kama unashindwa kusamehe.” “Nani amekosa
ambaye anahitaji msamaha wangu na nimeshindwa kumsamehe!?” Kimya.
“Hakuna aliyenikosea na
nikashindwa kusamehe Geb. Iwe nimeombwa msamaha au la. Huwa nasamehe kwa ajili
yangu mimi mwenyewe. Sina kinyongo na mtu. Ila nimeijua nafasi yangu na
nimeamua kutojidanganya tena. Hao wote wawili waliniacha kitandani nikilia
maumivu ya kubakwa wakati nimetoka kujifungua! Grace alishindwa hata kuja
kunipa pole, au hata kuja kuangalia niliumia kiasi gani ajue jinsi yakunisaidia
au hata kunisitiri. Alibeba watoto wake, akaondoka. Akajua mmenipokonya watoto
wangu, yeye anayejua uchungu wa watoto, akaniona nilivyoteseka, alinyamaza
kimya. Ndio namuona leo, ananishangaa na mimba yangu.” Nanaa akaendelea
“Mama yako ndio sitaki kurudia
matusi yake. Na wewe ulikuwepo. Yeye ni mwanamke kama mimi. Anajua uchungu wa
kuzaa. Nilimwamini kwa kumsogeza karibu yangu. Nikampa moyo wangu. Akatumia uyatima
wangu kama fimbo yakunichapa siku nilipokuwa na shida. Hata kama ningekuwa
mbaya kiasi gani, kama siku ile mimi ningekuwa Grace, nimefanyiwa vile, kweli
angenitukana kiasi kile na kunichukulia wanangu? Nililia usiku kucha na yeye
ananisikia. Asubuhi ananipokonya watoto niliowazaa kwa kumwaga si damu tu, ila
uhai wangu! Watoto nilio wazaa kwa kukubali kufa! Ananiambia mimi, mama
yao ni mchafu, sistahili kugusa wanangu!”
“Hakika nimesamehe, Geb. Na
nimemuachia Mungu. Sina kifua chakubeba uchungu wa ubaya mlio nitendea.
Sina. Na ndio maana nimeyaweka yote madhabahuni kwa bwana. Sina neno
lolote juu yenu, Mungu atashugulika na nyinyi wala si mimi. Lakini ndugu zako
sio watu watakaorudi kuwa sehemu ya maisha yangu.” Nanaa aliongea taratibu bila
jazba, lakini alisikika.
“Kama Grace
alivyoamua kuniacha siku ya msiba wangu, hakutaka kusumbuka na mimi. Basi.
Naahidi hatakaa akarudi kwenye maisha yangu. Mama yako analilia pesa zako!
Anasema kinachonisumbua ni pesa zako! Amenitukana matusi ya nguoni siku ile ya
maombolezo yangu! Akachukua watoto wangu bila hofu mbele za Mungu! Mtoto
wangu akiwa analilia ziwa langu! Hivi unajua jinsi nilivyoteseka na yale
matiti? Yaligeuka kuwa kama majipu Geb. Maziwa yalikuwa yanajaa,
mwanangu anashindwa kunyonya, kwa sababu mnaniadhibu mimi! Niliumwa mpaka homa,
kwa ajili yakumkatili mwanangu. Alimpa mtoto wangu maziwa ya kopo, akijua ni
kitu napingana nacho tokea kwa Liv. Lakini aliamua kufanya ili kunikomoa mimi.” Nanaa
alifuta machozi.
“Siku ya shida yangu,
alisimama kama mtesi wangu. Aliwatesa wanangu na mimi. Watoto wadogo wasio na
hatia aliwatenga na mimi kwa hila kabisa. Huku akiwatafutia mama
mwingine! Lakini Geb, hawa watoto ni wangu. Tena Mungu alinipa mimi kwa upendo
tu. Si wewe Geb, wala mama yako mtakao weza kunipokonya. Mungu ambaye ni Baba
wa yatima. Aliyenipa mimi hao watoto, ndio atakayenipigania. Atawarudisha
mikononi mwangu kwa kuwa sikuwatenda ubaya mkubwa wa kiasi hicho, ila tu
nilitaka kutunza mahusiano yenu, yangu na Malii. Hakuna cha ajabu sana
nilichokifanya ambacho nyinyi wote watatu hamkuwahi kufanya, chakustahili
adhabu mliyowaadhibu wanangu Geb. Mmemnyima Magesa mapenzi yangu, kwa makusudi.
Liv wangu ananililia mchana na usiku, mnamwangali tu! Hamjali kilio cha mwanangu, eti kwa kuwa
sikusema yote yaliyotokea kati yangu na Malii!” Nanaa akapata jukwaa.
“Hakika
nimewasamehe. Mungu wangu anajua. Sina nguvu ya kupambana na nyinyi. Kwanza
yeye Mungu ameweka mkono wake juu yenu katika kila eneo la maisha yenu. Kwenye
fedha, Mungu amewafanikisha. Utakatifu, amewafanikisha. Hamna dhambi. Nyinyi ni
wema sana. Ndio maana hamna hofu na watu kama sisi na mnaweza kuhukumu kwa
wepesi. Siwezi kushindana na nyinyi. Nilimwachia Mungu wangu ambaye
alinileta hapa duniani, akaninyima yale aliyowabariki nyinyi. Hakika
nimemuachia Yesu. Yeye ndio atashugulika na nyinyi, wala si mimi. Sina kinyongo
na hata mmoja wenu. Lakini hawatakaa kurudi kuwepo kwenye maisha yangu.
Tutaonana kama hivi ikitulazimu. Na kama ni wanangu, nitalea kwa upendo wote,
na unyenyekevu pale mama yako ATAKAPO KURUHUSU unipe niwalee. Lakini si
vinginevyo.” Nanaa akaondoka.
Ujumbe uliwafikia vizuri sana.
Nanaa alihakikisha haamshi wanae, lakini wengine wote ujumbe unawafikia. Na kwa
hakika ulifika. Geb alibaki amesimama pale mlangoni. Hajui aingie ndani au
atoke kwa muda. Akabaki amesimama pale, mpaka akamsikia Magesa ananung’unika.
Akaingia. “Vipi baba!” Geb akamsogelea. Akamshika kichwa. “Vipi homa?” Mama
yake akauliza. “Bado ipo juu. Lakini walituambia akipata dozi ya leo pia,
inaweza kushusha homa.” “Poleni Geb.” Grace aliongea kwa upole. “Atakuwa sawa
tu. Eti Magesa? Pambana baba. Pambana tutoke hapa.” Geb alimbembeleza kwa
kumshika shika.
“Nilileta chakula chenu wote.
Mpaka uji wa dada.” Mama G akaongeza. “Usihangaike tena mama. Yupo dada
anayeishi na Nanaa, naona ndiye anayemuhudumia Nanaa. Tokea Nanaa mwenyewe
alipokuwa hospitalini. Ndiye..” “Kwani Nanaa alikuwa amelazwa?” Grace akamkatisha.
“Yaani hata kwake hajarudi. Alikuwa amelazwa hospitali ya Muhimbili karibu ya
mwezi. Nimemtoa hapo, na kuhamia hapa kumuuguza Magesa. Kwa hiyo hajapumzika.”
“Alikuwa anaumwa nini?” “Presha.” Wakanyamaza.
“Kwa hiyo usingaike kupika.
Huwa anamwagiza huyo dada chakula anachotaka Liv ale, ndio anapika halafu kikiletwa
anakula naye. Kama leo alishapita alfajiri sana. Ndiye aliyetuamsha.
Ameshamletea chakula cha asubuhi, na amemuagiza chakula cha mchana pia. Kwa hiyo usisumbuke. Tumia huu muda
kupumzika, mama.” Mama G, akanyamaza.
Magesa akaanza kulia taratibu. Geb
akaendelea kumbembeleza lakini akazidi kulia mpaka Liv akaamka pale kwenye
kitanda. Akafungua macho. Akawaangalia kwa zamu watu wote waliokuwepo pale
ndani. Hakumuona mama yake. Akakaa. “Njoo nikubebe.” Bibi yake akamsogelea. Liv
akajivuta mpaka mwisho kabisa wa hicho
kitanda chake kama anamkatalia. Tayari machozi yakaanza kumtoka. “Mama anakuja
Liv. Wala usilie.” Geb akamuwahi, lakini alishachelewa. Liv alishavuta mtandio
wake, akajifunika kabisa huku kamekunja miguu yake.
“Mimi naona tuondoke mama, ili
Nanaa aje awe na watoto wake. Inatosha.” “Kwa hiyo naruhusiwa kuja kuwaona
watoto?” Mama G akauliza. “Tokea ujauzito ule wa Magesa mpaka leo, presha
inamsumbua sana Nanaa. Mnakumbuka ilibidi kumuombea atolewe tu hospitalini
baada ya kujifungua Magesa, ili arudi nyumbani awe na watoto? Walimruhusu kwa
kuwa niliwapa ahadi yakumrudisha hospitalini mara kwa mara kwa vipimo na
kumuona dakitari. Huku nikiwaahidi nitasimamia unywaji wake wa dawa. Wote
niliwaambia. Mnakumbuka?” Kila mtu kimya.
“Ndio yakatokea yakutokea.
Tukamuacha bila uangalizi wowote. Hata dawa alizokuwa ameandikiwa atumie,
niliondoka nazo. Nikazifungia kwenye ile gari ndogo. Jana ndio daktari wake alinikumbusha.
Na mbaya zaidi, hata Nanaa hakujua kama alitakiwa kutumia hizo dawa.
Alipoulizwa na daktari kama alikuwa akitumia zile dawa, hakuwa hata akijua huyo
daktari alikuwa akizungumzia nini, kwa kuwa mimi ndiye niliyekuwa nimechukua
maagizo yote ya dawa na dawa zenyewe. Daktari wake ameniambia kutotumia zile
dawa na Nanaa kuendelea kuwa na pressure ya juu kwa muda mrefu bila kuitibu,
imesababisha madhara makubwa zaidi kwenye moyo wake.”
“Hapo alipo moyo wake
umepanuka. Presha ipo juu sana. Dawa ya kwanza na ya haraka inayoweza kumsaidia
kwa sehemu, nikumtoa huyo mtoto. Lakini amekataa. Daktari anayemtibu sasahivi
ameniambia kwa hali aliyonayo sasahivi hawezi kuzaa tena kwa kawaida.
Akifanikiwa kufika hiyo siku zakutimia umri wa kukaa mtoto huko tumboni, kabla
uchungu haujaanza, watamfanyia upasuaji. Hana uwezo wakusukuma tena mtoto. Sasa
kuna dawa amepewa ndizo anatumia sasa hivi na ndizo zinamfanya aweze kuwepo
hapa na watoto na kumsogeza mpaka hizo siku za kujifungua. Naomba tumuache
kwanza.” “Mmmh!” Mama G
akaguna.
“Naomba mpe pole. Mtie moyo
mwambie Mungu atamsaidia atapona, na kumrudishia muda wake wote aliopoteza na
wanae. Na wewe msaidie ili atulie na watoto, mimi nitakuwepo kazini. Usiwe na
wasiwasi. Binafsi sitambugudhi kabisa, ili atulie. Ila ukipata nafasi
yakuzungumza naye, naomba niombee msamaha. Mwambie ni kweli najutia.
Najuta sana, lakini nampenda na ninamuombea.” Grace akatoka.
“Sasa nikiache hiki chakula au
niondoke nacho?” Mama G akauliza. “Kitamwagwa tu mama. Nenda nacho. Asante.”
Mama G akabaki amesimama. “Na wewe?” “Kama kipo chakula changu, naomba niachie tafadhali.
Mtoto akiendelea vizuri, jioni nitakuja kukuangalia nyumbani. Lakini kapumzike
tu.” Mama G akaacha kapu lote akatoka.
~~~~~~~~~~~~
Geb akampigia simu Nanaa.
Ikaita mpaka ikakata. Baada ya muda Nanaa akapiga. “Vipi?” Geb
alimuwahi mara tu baada yakupokea. “Namsikia Magesa analia. Naruhusiwa
kuja?” Nanaa akauliza kwa sauti iliyosikika alikuwa akilia. “Naomba usilie Nanaa.
Uzima wako ni muhimu sana kwa hawa watoto. Naomba utulie.” Kimya. “Uko wapi?” “Sipo
mbali. Kama unaniruhusu kurudi, naweza kuja sasa hivi. Sitachukua muda mrefu.” “Naomba uje basi. Na
Liv naye ameamka. Amejifunika, anakulilia.” “Basi nakuja.” Wakakata. Geb akaendelea kubembeleza watoto wake.
~~~~~~~~~~~~
Nanaa akashindwa kuelewa kama
yeye ndio mgonjwa au Magesa. Akili na mawazo ya Geb vyote vilikuwa kwake.
Hapakuwa na ahadi wala maneno mengi, lakini kila wakati alimuuliza
anavyojisikia. Kama ameshiba, amekumbuka kunywa dawa na kumtaka ajilaze, halafu
anamuwekea watoto pembeni yake. Alimfuata mpaka chooni kama atakawia kutoka. Na
akienda kuoga, alienda kusimama humo humo bafuni. Hata kama hatamuongelesha,
lakini Nanaa alishitukia anaingia nakujiegemeza hata kwenye sinki na macho
kwenye simu yake. Akifunga tu maji, Geb anamchukulia taulo na kumsogezea.
Atamsaidia kujikausha mgongoni au miguuni, kwamba asiiname. Ilimradi Nanaa
akamuona anajishugulisha naye.
Akabaki akijiuliza baada ya
mtoto kuruhusiwa, itakuaje? Ndio itakuwa mwisho wake na wanae? Akabaki kimya akiwaza.
Geb akamuona amepotelea mawazoni. Ilikuwa jioni ya siku inayofuata mara baada
ya ujio wa mama G, na Grace. “Nikupe maji ya kunywa?” Geb akamsogelea. “Naona
nakunywa maji mengi! Nina kazi ya kwenda chooni kila saa!” “Lakini unahitaji
maji mengi. Jitahidi kunywa. Ikifika kwenye saa 12 jioni ndio iwe mwisho.” Liv
alikuwa amemkalia mama yake huku akiangalia tv.
Ukimya ukapita kidogo. “Unawaza
nini?” Geb akavuta kiti karibu na alipokuwa amejilaza Nanaa. “Nafikiria tu.”
“Nini?” Nanaa akafikiria kidogo. “Nafikiria baada ya hapa, nitakuwa nawaonaje
tena wanangu?” Nanaa akaona machozi yanaanza kumtoka. “Naona Magesa ni kama ameanza kunizoea! Sasa hivi hata nikimshika mimi
anatulia. Nina wasiwasi tukija kupotezana tena kwa muda mrefu, atanisahau
tena.” “Kwa nini mpotezane tena?” Geb akauliza.
“Eti Nanaa?” “Sijui Geb! Hata sielewi tena! Hakuna kinachoeleweka tena. Nimebakiza
siku chache tu wanifanyie huo upasuaji ambao sijui kama hata huo moyo utakubali
kufufuka tena baada ya hapo! Sijui kama baada ya hapo nitawaona wanangu tena!” “Tunamuomba
Mungu Nanaa. Naomba na wewe ujipe moyo.” “Sijui kwa nini
Geb? Nimeingiwa na hofu sana.” Nanaa akavuta pumzi na kujaribu kutulia.
“Nimemwambia dada Fifi kuanzia
siku moja kabla sijalazwa kwa ajili ya huo upasuaji, asichukue oda yeyote ile.
Nataka niwe naye hospitalini wakati wote. Kuanzia mwanzo mpaka mwisho awepo.
Nikitoka tu hapa, nataka niende naye benki. Nikamuweke kama mtu wa pili kwenye
akaunti yangu. Ili chochote kikitokea kwangu, apate pesa za kujikimu na
mwanangu siku hizo za mwanzoni mpaka mtoto atakapochangamka. Ndipo atajua
mwenyewe chakufanya na huyo mtoto. Nimejitahidi kuandikia mambo mengi juu yangu
na maisha yangu. Kwa ajili yake yeye dada Fifi na Jimmy. Ili nisije kuondoka
vibaya kama mama alivyoniacha mimi. Naamini Jimmy akija kuwa mkubwa hatakuwa na
maswali mengi, kama mama alivyokuwa ameniacha nayo.” Geb akajua yapo mengi
yanayoendelea ndani ya kichwa na moyo wa Nanaa.
~~~~~~~~~~~~
Akatamani atoe ahadi,
akakumbuka ameshamuahidi ahadi nyingi sana, na amekuwa akizivunja muda mfupi
sana mara baada yakumuahidi. Siku aliyobakwa Nanaa, alikuwa naye hotelini zaidi
ya masaa matatu akimwaga ahadi tele kwake. Usiku wake alipobakwa, hata pole
hakumpa. Akaishia kumpokonya watoto na kukata msaada wa pesa alizokuwa akimpa
kila mwezi. Na kumpokonya watoto. Leo anarudi na ahadi gani tena!?
Akakumbuka ahadi zote alizokuwa
akimuahidi tokea hawana hata mtoto mmoja, nakuishia kuzivunja vibaya sana. Tena
alimuacha akiwa anamaumivu na inakuwa ni muda mfupi sana baada ya ahadi zake
kwake. Anarudi kwa kuomba msamaha, nakurudia tena kuahidi? Hakujua kama atubu
na kuahidi tena au anyamaze. Maana ni jana yake tu, Nanaa alimtahadharisha
nakumwambia yeye sio mjinga. Akaona anyamaze.
~~~~~~~~~~~~~~~
Mambo
yanazidi kuchanganya. Maji yamezidi unga kwa kina Magesa.
Nanaa naye
amewaambia amewaacha madhabahuni kwa
Bwana, Yeye
ndiye atashugulika nao. Amejipatia wanae lakini wakiwa dhaifu, na Magesa
mgonjwa.
Geb anakutana
na Nanaa aliyejeruhiwa sana. Anamipango mizito ambayo yeye wala pesa yake haihusishwi.
Nani wa Nani?
Endelea
kusoma kujua kitakachoendelea….
0 Comments:
Post a Comment