Kwa Kina
Magesa.
Yeye
Danny ndio hakusikika kabisaa. Tokea siku ya mkasa, walipita na mkewe mara moja
tu, hakurudi tena. Tena Danny na watoto wake walibaki kwenye gari hakutaka hata
kushuka garini. Mama G naye alikuwa busy na ulezi wa watoto akisaidiana na
Sara. Geb yeye ndio alibadilika kuliko kawaida kasoro tu kuchanganyikiwa sababu
ya jukumu la watoto na kazi. Ikawa hata ngumu kumuongelesha au kumwangalia
usoni. Kupishana kukawa kwingi kati yao kama wanao kwepana. Maisha yakaendelea
wasijue yanayoendelea nyumbani kwa Grace na Danny.
Chachu Ndogo, Huchachua Donge Zima.
Kumbe
maneno ya Malii yalimuingia na kuharibu akili ya Danny kabisa. Walimtoa pale
siku ya tukio, Malii akiendelea kumsema mpaka walipomshusha kwenye mataa. “Wasijekuwa wamenitoa kweli kafara!”
Danny aliendelea kuwaza. “Utajiri wa Geb
ni kweli umekuwa wa gafla sana. Kwa nini Grace amekazania kufanya kazi huko?
Hata ukimwambia kuna kampuni nyingine itamlipa zaidi, au tufungue kitu chetu,
hataki! Ukute kweli wameungana pamoja wakifanya biashara kwa njia ya ushirikina
wakinitumia mimi!” Danny akaendelea kuwaza.
Ni
kweli ‘chachu ndogo, huchachua donge zima’. Danny akaanza kujiwinda nafsi yake na familia ya
mkewe. “Wana kijiumoja ambacho
hakieleweki eleweki hivi! Inakuwa ni wao tu!” Yale yote yaliyokuwa
yakimvutia Danny kwenye familia ya mkewe, yakaanza kuleta maswali. “Kwa nini nimng’anganie hivi Grace!? Kuna
walichonifanyia tokea zamani kama alivyosema Malii. Itakuwa ni kweli mimi ndio
waliona katika kundi letu wote mimi ndio nina nyota kali, wakanifanyia kweli
uchawi kwa kunitoa kafara. Nikawa kama mjinga kwa Grace. Sikuwa hivyo
mimi! Sikuwa mtu wa wanawake kabisa! Kwa nini nikawa nimepagawa na mwanamke
kama Grace!” Akaendelea kuwaza kila iitwapo
leo. Hata mkewe akaanza kumtilia mashaka. Yale mazuri yote ya Grace akaanza
kuyaangalia mara mbili mbili huku akijiambia zile sio akili za kawaida. Akaanza
kumshusha thamani mkewe.
Matatizo
ambayo Grace hakuwahi hata kuwaza yanaweza kumpata ndani ya ndoa yake,
yakaanza. Kila kitu anachoongea yeye, Danny anakipinga. Tena kwa ukali sana
akiamini ndio anajitoa kwenye ushirikina wa familia ya mkewe. Ukali kwa Grace
ukazidi pasipo sababu. Kuchelewa kurudi kutoka kazini bila taarifa kukawa kitu
cha kawaida. Yale mambo yakutaka awe na Grace wakati wote yakaisha kabisa kitu
ambacho kilikuwa mateso makubwa sana kwa Grace. Akawa anamkwepa sana.
Akimpa
hata maji ya kunywa, anayaangalia mara mbili mbili mwishowe anayamwaga hata
mbele ya Grace na kwenda kuchukua glasi nyingine na maji mengine au anaacha
kabisa kunywa maji. Chakula ndio alikuwa anakikataa waziwazi huku akimtamkia
mkewe aondoe limbwata lake, mbele ya macho yake. Akimaanisha aondoe chakula
ambacho atakuwa amekiweka madawa ya ushirikina ili kumpumbaza yeye. Grace
hakuchoka kumwambia kuwa hajawahi kumloga, lakini napo pia huwa panazuka ugomvi
mkubwa zaidi.
Mambo
yaliharibika zaidi pale alipojua kuwa Nanaa alipokonywa watoto.
Alichukia na kuwa kama amechanganyikiwa kwa Grace. Akawa kama anamlipiza Grace
kisasi kwa walichofanya ndugu zake kwa Nanaa. Na yeye ni kama akampokonya
Grace watoto. Siku ambazo yeye haendi kazini, anaweza kuchukua wanae kuanzia
asubuhi akarudi usiku bila kumtaarifu Grace alipo. Hataaga wala kumtafuta mkewe
kumjulia hali au kumwambia walipo na watoto.
~~~~~~~~~~~~~
Ikafika
birthday ya kutimiza mwaka kwa mapacha wa Grace, ikabidi kumuomba Geb, watoto
wake wahudhurie. Akamfuata ofisini kwake. “Nitamwambia mama. Wataletwa tu.
Sidhani kama kutakuwa na shida. Si umesema itafanyika nyumbani?” Grace akabaki
kimya kwa muda. “Ndiyo.” Akajibu. “Wewe hutafika?” Grace akauliza. “Najua
unanikwepa Grace.” Grace akavuta pumzi na kuzishusha taratibu. “Kwanza nina
matatizo yangu binafsi. Pili Sifurahii maamuzi yako na mama Geb. Mnaniumiza
nafsi yangu. Ndio maana naona ni heri nikae tu mbali na nyinyi. Siyawezi maisha
mnayoishi sasa hivi. Naumia sana hasa nikimuona Liv! Siwezi Geb.” Geb
akanyamaza.
“Najua
unampenda sana mama na unamsikiliza kwa kila kitu. Lakini kuna mambo nilazima
usimame wewe mwenyewe kama baba, Geb. Wanawake wengi Malaya au niseme wale
wachafu kupindukia, au hata mwanamke fukara, akiamua, anaweza kulea
watoto vizuri tu. Tena yeye peke yake bila msaada wa mtu, kuliko hata mwanaume
msomi na tajiri. Mwanamke mmoja anaweza kulea watoto 10 bila shida. Hata akiwa
maskini vipi, anaweza kuwasogeza hao watoto wakafikia ngazi yeyote hata kuwa
madaktari au maraisi wa nchi. Lakini mwanaume mmoja milionea anaweza kushindwa
kulea hata mtoto mmoja tu. Angalia matajiri wengi na wasomi. Watakwambiwa
walilelewa na mama tu. Aidha baba alikimbia au alikufa. Fanya utafiti wako Geb.
Utagundua.” Grace aliongea kwa upole sana lakini kinyonge.
“Najua
mimi huwa hunisikilizi. Lakini nataka kukwambia ukweli Geb. Unaharibu maisha ya
watoto wako. Huyo Sara anayekupikia hapo ndani, hatakaa akawa mama wa Liv, hata
ufanyeje Geb.” “Nani amesema Sara atakuwa mama yake Liv?” “Basi fungua macho
yako, uone. Sikulazimishi chakufanya. Lakini nakushauri urudi magoti. Umemuacha
Mungu Geb. Unaangamia. Mungu pekee ndio atakutoa hapo ulipo. Umekonda. Wewe na
mtoto wako Liv, wote mmechoka kama wagonjwa! Umezeeka gafla, umekuwa
kama babu wa miaka 80, wakati unaishi na wanawake wawili ndani ya nyumba. Na
wote wanakuhangaikia wewe!” Geb akabaki kimya.
“Vipo
viatu vya watu wengine, havivaliki na wengine. Hata ufanyaje. Kuna mapengo huwa
hayazibiki daima. Labda kwa rehema za Mungu tu. Mrudie Mungu Geb. Umefanikiwa
sana kwenye mambo ya pesa. Unaakili sana upande huo. Kwa nini maisha ya upande
mwingine yanakushinda? Jiulize, jichunguze wewe binafsi kabla hujanyoshea mtu
mwingine kidole. Inawezekana shida inaanzia kwako. Nakuombea Mungu akusaidie
kukufungua macho ili uweze kufanikiwa na huo upande mwingine wa maisha ambao ni
muhimu sana hasa sasa hivi ukiwa ni baba. Ninakwambia bila kukuficha Geb. Umeshindwa.
Mama hawezi kukwambia ukweli, lakini mimi nakwambia. Umeshindwa kuwa
baba kama ulivyoshindwa kuwa kimbilio katika upande wa mapenzi.” Grace
akapasua moyo wa Geb.
“Hunitendei
haki Grace!” “Ndio maana nakwambia jichunguze Geb. Mimi sitasema mengi kama
Danny anavyotusema. Lakini naanza kumuona kwa upande mwingine yupo sahihi. Sisi
sio watu wakutegemewa wala wakukimbiliwa wakati wa shida. Tatizo
linapotokea, tunajitenga na mtu. Danny anasadiki kwa asilimia mia ni
kweli tunamloga! Tunataka watu tunaoona wanatusaidia tu. Tukiona hawana faida
kwetu, tunawatupa nje. Anaamini hata yeye tupo naye karibu,
tukimshikilia, kwa sababu tuna nufaika naye.” “Ndio maana umekonda hivyo?” Geb
akamuuliza dada yake.
“Mimi
nakondeshwa na mfungo Geb. Namlilia Mungu wangu. Ipo siku najua atanijibu tu.
Hayo mengine najua ni majaribu tu. Lakini Geb, rudi magotini. Vunja roho za
kurithi. Muombe Mungu akusaidie urithi mazuri tu kutoka kwa baba. Mabaya
uyavunje. Si kwako tu, hata kwa Magesa wako. Ni roho. Nakuhakikishia ipo kwako.
Usiposimama imara na kutulia magotini, utakuwa kama baba kwa asilimia zote.
Utafanikiwa kipesa, lakini maisha mengine yatakushinda kabisa. Na kama
hujagundua, unatesa watoto wako wewe mwenyewe. Ukishirikiana na mama,
aliyekuwa kwenye maisha ya baba. Anahamisha maisha ya baba kwako wewe.
Nampenda mama, lakini kuna mambo lazima uwe naye makini sana. Kwake
haitamsumbua kukuona unayafanya au unaishi maisha fulani aliyomuona baba
akiishi.” Grace akaendelea.
“Atakusaidia
kuyaishi hayo maisha bila shida. Na atakubariki huku akikufariji na kujaribu
kukupa yale yote uliyotakiwa kupewa na mkeo. Atahakikisha unakula na kuvaa
vizuri. Atakutafutia mwanamke anayempenda yeye. Umemfikiria Magesa na Liv?
Ukishuhudia vile Nanaa anavyoteseka na mimba zake. Inakuwa kufa au kupona ili
kuzaa hao watoto. Leo unaungana na
mama kumpokonya mtoto wake akiwa hata hajamnyonyesha!” Grace akaanza kutokwa na machozi.
“Tena kwa kosa ambalo alilifanya kwa ajili yako! Hujijui vile ulivyo
nahasira Geb. Yule binti alikuficha ili asikuumize au kwa kuwa alikuogopa! Leo
unamuadhibu kwa jambo alilolifanya wakati akikuona wewe ukiishi na Liz nyumba
moja, ambayo na yeye alikuwa akiishi! Hamkuwa pamoja! Wewe ulikuwa na Liz, na
yeye alikuwa huru kuishi maisha yake. Leo mnamuadhibu bila huruma! Unaruhusu
wivu wako na hasira zako zitese watoto wako! Na kwa taarifa yako tu, na wewe
unateseka. Jiangalie kwenye kioo ndipo utajua.”
Grace aliendelea taratibu huku akitokwa na machozi.
“Danny ametuogopa kuliko nitakavyokwambia. Anashindwa kuelewa hata
tunawezaje kumtaja Mungu kwa kitendo tulichokifanya kwa Nanaa. Alijua
tungemuhurumia na kujutia hata kushindwa kumlinda siku ile usiku! Mlikuwa
wanaume wanne pale na walinzi wako. Lakini wote mlishindwa kumlinda Nanaa
tuliyekuwa tukimsikia akilia kwa uchungu sana. Leo mnamuadhibu na kumfukuza!
Danny ameshindwa kuelewa kabisa. Anatuogopa, hataki hata kutusogelea. Anatuona
wote sisi ni wanyama si binadamu. Ananitangazia kuwa inabidi aanze kujiandaa
yeye na wanae. Kwa kifupi, Danny anatafuta kuanzisha familia yake. Ndoa yangu
ilishaisha Geb. Kinachotufunga sasa hivi ni ile nyumba na watoto, basi.” Grace alifuta machozi.
“Anasema
amewekeza pesa zake nyingi sana pale. Hawezi kuondoka na kuniachia ile nyumba.
Anatoka na kurudi nyumbani atakavyo.” “Si urudi tuishi wote?” Geb alitoa wazo.
Grace akacheka huku akitingisha kichwa. “Hilo ndilo tatizo lako Geb. Kukitokea tatizo linalokuumiza wewe,
unakimbia. Hujui kumlipia mtu garama. Hujui kupigania kilicho chako. Hujui na
hutaki kujifunza.” Grace akaona asimuache, avute
kiti kabisa akae mbele ya meza yake.
“Hivi
unakumbuka walimtoa Danny nyumbani kwako huku wakimtukana na kumuaminisha
tumemloga? Unakumbuka walimtoa huku wamemshikia risasi ya tumbo na kumwambia
wanaenda kumuua? Unakumbuka muda ambao Nanaa alikuwa akilia akiomba msaada na
tukashindwa kumsaidia?” Kimya. “Basi Danny anajua mpaka dakika ya mwisho aliyoshuhudia
yeye, Nanaa aliyolia akiomba msaada. Danny anajiweka kundi moja na Nanaa.
Yatima wasio na msaada. Kuwa familia yetu tunawatumia tu. Anasema wewe
umeshapata watoto uliokuwa ukiwataka, basi. Ndio maana tumemtupa Nanaa nje.” Grace
akaendelea
“Hivi
unajua kuwa James anaogopa hata kumuona Nanaa? Yeye anamaumivu yakushindwa
kumsaidia mdogo wake siku ile usiku. Danny anasema James amekonda yupo kama
kijiti. Anamwambia Danny, halali. Sauti ya Nanaa akimlilia akimuomba msaada,
inamuweka macho. Anasema mdogo wake alimlilia akimuomba amuokoe lakini alishindwa.”
Grace akaendelea. Alikusudia kuzungumza na Geb. Akaamua aongee tu hata kama
hatajibiwa.
“Sasa
Danny yeye anasema haelewi roho hiyo mbaya yakumpokonya Nanaa watoto waliokuwa
wakimtesa karibu kufa, sisi tumeipata wapi? Tumewezaje? Anasema
ameshindwa hata kumwambia James kama mdogo wake amepokonywa watoto. Anasema kwa
hali ya James ilivyo sasa hivi, anaweza kufa kabisa. Anamdanganya kuwa Nanaa
yupo na anaendelea vizuri.”
“Kwa
hiyo Geb, inawezekana ile nyumba ambayo inamfanya Danny anashindwa kuondoka,
ukute ndio muujiza wangu. Sitamkimbia mume wangu. Kwanza mimi naujua ukweli wote. Sijamloga
Danny ili anipende. Najua maumivu aliyonayo. Nitamuombea mume wangu.
Sitamkimbia kipindi hichi ambacho amechanganywa na maneno ya Malii na matendo
yako wewe na mama kwa Nanaa. Mchana na usiku nitamlilia Mungu wangu. Hata kama
ameanza umalaya huko nje. Basi, namuombea Mungu amlinde, asipatwe na magonjwa.
Naamini ipo siku atanijibu na nitampata Danny na hata kama sitampata tena,
sitakuwa na pakulaumu, kwa kuwa ninajua nilivyopambana. Ataniacha nikiwa sina
lawama moyoni. Nitajiambia niliomba, nikavumilia, lakini ameshindwa kunipokea
tena. Lakini bado sijamaliza kupambana Geb. Nipo kwenye kupigania ndoa yangu
mpaka nione huo mwisho. Huwa hatukimbii mmoja anapoanguka. Na upo usemi unasema, mtoto akinyea mkoni,
hukati. Ndoa hazijengwi kwa hisia Geb. Ni upendo. Na unajua sifa za upendo. Nenda kasome bibilia yako kama umesahau tabia za
upendo. {1 koritho 13:4-8}.” Grace akasimama na kutoka. Alimuacha Geb hoi.
Hakutegemea.
~~~~~~~~~~~~~
Akachukua
simu akapiga simu nyumbani. “Mbona
Liv analia!?” Akamuuliza mama yake. “Naona ameamka tu vibaya. Lakini ni mzima.
Nimempima hana hata homa.” “Amekula?” Geb
akamuuliza tena mama yake. “Kidogo
sana.” “Naomba kuzungumza naye.” Liv
akakataa. Geb akakata simu. Ilikuwa ni saa tano asubuhi. Lakini Geb akaona
arudi tu nyumbani. Akaenda kumuaga Grace, akatoka.
Alirudi
nyumbani kwa haraka. Akamkuta Liv amekaa chini ya meza, akilia. Maneno na
hukumu ya Grace vikaanza kumrudia. Kama aliyefunguliwa macho. Akaona yeye ndio
amesababisha machungu yote yale kwa mwanae. Akachuchumaa, akamuona amekaa peke
yake mwisho kabisa wa ile meza, ameshika kitambaa cha mama yake alichokuwa
akijifunika wakati ananyonya. “Njoo Liv.” Geb akamwita. Liv akaendelea kulia
kwa kwikwi, taratibu, bila kutoka pale chini.
“Njoo mama yangu. Njoo mama eeh!” Liv hata
hakujivuta. Akabakia akimwangalia baba yake huku akilia taratibu. Kama
aliyekuwa akimuhukumu zaidi. Maneno ya Grace yakaleta maana zaidi. Geb akaingia
chini ya ile meza. Liv akajivuta mbali zaidi, akajifunika kitambaa cha mama
yake kama kujificha. “Nitakaa hapa hapa na wewe. Sitakugusa.” Liv hakutoka
pale. Akatulia vile vile alivyokuwa amejiweka. Mama G alikuwa amekaa kwenye
makochi akiangalia.
“Unaumwa?”
Geb akamuuliza kwa upendo. Liv kimya. “Unataka twende kwenye ice cream?” Kimya.
“Niambie unataka nini Liv, mwanangu.” Kimya. Hata hakunyanyua uso kumwangalia
baba yake. Akaamua na yeye kunyamaza. Ukimya wa muda ukapita, Geb akajua
ameshalala. Akamtoa pale chini ya meza. “Grace amekwambia birthday ya wanae
itakuwa jumamosi hii?” Geb alimuuliza mama yake wakati akipita na mwanae
kuelekea chumbani kumlaza. “Amenitumia ujumbe.” Mama G akajibu. Geb akaingia
chumbani.
~~~~~~~~~~~~~
“Nataka
kumuomba dereva anipeleke saluni. Sijaosha nywele muda kweli!” Geb alimsikia
Sara anaaga. “Si ndio umekurudisha sasa hivi?” “Alinisindikiza kwa sonara.
Unakumbuka ile pesa uliyonipa jana? Basi nilikuwa naenda kummalizia sonara
wangu. Lakini wala sitakawia. Kwanza hamna kitu chakufanya hapa. Huyo mtoto wa
kike ndio kagoma. Kaka yake ni maziwa na uji tu. Huwezi kushindwa kummudu huyo,
bwana bibi! Acha na mimi nikajisopu sopu nifananie na hapa kidogo. Halafu
nimesikia kuna birthday party ya watoto wa Grace. Nataka nikashonee wiving
ndefuu, nipendeze. Sio natokea kwenye birthday naonekana wakuja. Au unasemaje
bibi!?” Sara akacheka nakutoka bila kusubiri vikwazo.
Baada
ya muda akarudi. “Nahisi kama pesa haitanitosha vile! Naomba niongezee kidogo.”
Mama G akasimama. Sara akamfuata nyuma. “Yaani pesa yote ile ya jana,
umemaliza?” “Bibi na wewe? Pesa gani ile yakujiliza bwana?” “Sio kwamba
najiliza Sara. Pesa ngumu.” “Kwa wengine. Hapa pana neema bwana! Acha kubania
mipesa hiyo, niache nipendeze bwana! Nataka kushonea wiving original ili ikae
muda mrefu halafu nikitokea watu wajue zangu. Uzuri garama bwana.” Sara
alisikika akicheka kwa utani. Akapewa pesa, na kutoka na dereva. Geb akatoka
taratibu na kurudi chumbani kwake.
~~~~~~~~~~~~~
Maneno
ya Grace yakaanza kujirudia taratibu. Miezi mitano ilishapita tokea Nanaa aondoke.
Lakini utafikiri ilishapita miaka 3. Geb akarudi chumbani kwake. Kilio cha Liv
na maneno ya Grace vilimnyima raha yakurudi tena kazini. Akasogelea kioo
nakujitazama. Ni kweli alikuwa amechoka. Akarudi kukaa kitandani akiwa amejawa
mawazo. “Mungu nisaidie.” Kwa mara
ya kwanza baada ya muda mrefu, Geb akamkumbuka Mungu wake. Akazivuta pumzi kwa
nguvu, nakuzishusha taratibu.
Akaamua
kupiga magoti kabisa. “Najua unanisikia Mungu wangu.
Nisaidie. Ni kweli nimezama.” Ndilo neno
aliloweza kuliongea. Akabaki akiwaza jinsi yakujinasua. Aliachana na Mungu
lini, ni swali ambalo alishindwa kulijibu. Alikumbuka mara ya mwisho alipokuwa
na Nanaa, aliweza kupiga magoti na kuomba. Nini kilimpata? Hasira!
“Liv anaakili kama za kwangu. Hapotezi kumbukumbu. Bado
anamkumbuka mama yake. Sasa sijui
nilaana au ni baraka kwake! Mungu wewe
ndio ulimuumba huyu mtoto. Msaidie. Asiendelee kuteseka.” Geb aliomba na kuwaza akiwa amepiga
vile vile magoti ameinamia kitandani. Alimsikia mama yake anataka kuingia.
Lakini alikuwa amejifungia mlango kwa ndani. Hakutaka kumfungulia. Akataka muda
wa peke yake mle ndani. Alikaa pale akiwaza asijue aombe nini.
Nanaa!
Mimba
ya Nanaa ilipofikisha miezi mitano presha ndio ikazidi kuchukua hatamu. Alirudi
kutoka hospitalini, akajitupa kitandani. “Mbona huna raha?” Fifi akaingia na
kumuuliza. “Daktari ameniambia hali yangu sio nzuri. Presure ipo juu sana. Hivi
hapa ilibidi waniwekee dripu moja ndio nimeweza kufika hapa. Walitaka kunilaza,
lakini nimekataa.” “Kwa nini tena na wakati uliniambia mimba zako zote ndivyo
zinavyokuwa!?” “Sijui dada. Najiona kama sina nguvu za kupambana tena.
Najisikia kuishiwa nguvu kabisa. Sasa sijui kwa kuwa sio mtoto wa Geb? Sijui
dada! Nimejiachia tu. Liwalo na liwe. Nikifa au tukifa wote na huyu mtoto,
najionea ni sawa tu. Naomba nijipumzishe kidogo.” Fifi alibaki akimwangalia.
Nanaa akajigeuza, akalala.
Uzuri
hata Fifi alishakuwa mtaalamu wa mapishi. Na kadiri siku zilivyokuwa zikizidi
kwenda ndivyo hali ya Nanaa ilivyozidi kuwa mbaya. Presha juu kila wakati.
Mikono kutetemeka, mara kufa ganzi. Hawezi kushika chochote. Mbaya zaidi,
hakuwa akijali tena. Fifi alijua ni kama amejizira. Alishatafuta msichana
mwingine wakuwasaidia. Biashara ikaendelea. Nanaa akiwa nusu nusu. Nanaa
aliyeanza hiyo biashara, siye Nanaa huyu. Utafikiri ni watu wawili tofauti.
Aliyokuwa akiongea na anavyoishi sasa ni tofauti. Mimba hiyo ilimuharibu akili
zake kabisa. Akasahau yeye ni nani, anakwenda wapi na anataka nini.
Kwa Kina
Magesa!
Siku
moja kabla ya birthday ya watoto wa Grace, Geb aliwahi kutoka kazini. Akaamua
kupitia kwenye nyumba aliyokuwa akiishi na Nanaa. Walinzi walimfungulia geti.
Akaegesha gari, akashuka nakutembea taratibu wala asijue kwa nini yupo pale.
Akajikuta amekaa pale nje akiwaza. Alikaa kwa muda mrefuu. Mlinzi akamfuata.
Geb akamsalimia. Alikuwa ni mlinzi wa muda mrefu hapo. Mzee kwa walinzi wote
waliokuwa wakifika hapo kulinda. Wengine walikuwa wakibadilishwa mara kwa mara,
lakini yule mzee alikuwepo hapo mara kwa mara. Na Geb alikubaliana na hiyo
Kampuni kwa kuwa alikuwa ni mzee aliyejaa busara, ilikuwa rahisi kunyoosha
walinzi vijana waliokuwa wakifika hapo.
“Mambo
yanabadilika mwanangu! Na ni kwa kila mtu.” Geb akanyamaza. “Watu wengi wanajua
wakishapata majumba makubwa hivi, wakayajaza mavitu ya thamani, ndio maisha
yamekamilika. Hawajui nyumba si jengo wala huwa hazijazwi na vitu vya thamani.”
Geb akabaki kimya akaendelea kusikiliza tu. “Na mimi wakati wote huwa nawaambia
hawa vijana hapa wanaokuja kulinda na mimi. Si hivyo. Maana kutwa wanatamani na
wao wangekuwa wamelala ndani, wanalindwa nje. Nawaambia si heri wao asubuhi
ikifika au jioni wakitoka kazini, wanaenda kulala kwa wake zao. Japo si kama
hapa, lakini wanajua wanarudi makwao. Mke na watoto wanawasubiri. Haijalishi ni
wapi. Iwe uswahilini, iwe chumba kimoja, bora maelewano. Sasa waliyaona majuzi
hapa wakati mama watoto anakimbia hili jumba. Hawakuamini. Si uliona barua yake
aliyokuaga na wewe?” Geb akashangaa kidogo.
“Ulimpa
nani?” “Si yule dereva wenu? Jeri! Alileta watoto. Nikamwambia kabisa kuwa
asihangaike kuleta tena watoto hapa. Mama yao ameamua ni heri aondoke kuliko
yale masharti uliyokuwa umemuwekea. Kwa hiyo..” “Subiri kwanza Mzee
Nyundo.” Geb akamkatisha. “Masharti gani na barua gani?” Geb akauliza.
“Si
vile ulivyomwambia awe analeta watoto, lakini asiwaguse? Mwenzio alishindwa
vile watoto walivyokuwa wakilia, lakini hawezi kuwabembeleza. Hasa kale karembo
kenu. Alikuwa akimlilia sana mama yake. Walikuwa wakilia hapa, kama msibani.
Mama mtu analia nje ya gari, basi na mwanae analia ndani ya gari. Na yule
dereva naye akasimamia masharti yako bila huruma. Hakuna mtoto kumshika
mama yake, wala mama haruhusiwi kumshika mtoto. Kuwaangalia tu dirishani kama
anatizama mfungwa jela! Mwishowe naona mwenzio akaona ameshindwa. Akaniaga.
Tena hapa mbele ya wale vijana. Akasema hawezi kuendelea kumtesa mtoto wake. Ni
heri aondoke tu. Mbona alinipa hata barua yakukuaga! Nilimkabidhi yule kijana
wako. Hakukupa?” Geb hakujibu kitu chochote, mpaka yule mlinzi akaamua kuondoka.
Lakini na yeye akawa ameongezea kitu kingine.
Geb
alikaa kwa muda pale akiwaza. Zilikuwa habari mpya na ngeni kabisa kwake.
Akaunganisha hili, akajumlisha nakutoa. Akakumbuka maneno ya Grace. Akajua watu
wote wanajua yale yote yanayoendelea kasoro yeye. Akaelewa ni kwa nini watu
wanawachukia. Akachukia mateso aliyokuwa akiyapitia Liv na yeye kuwepo kwenye
maisha ya huyo mtoto bila taarifa! Akachukia sana. Akajua ndio maana amegeuka
kuwa mtoto asiye na furaha. Kwake yalikuwa ni mateso ambayo hakujua ni kwa nini
anafanyiwa hivyo na kwa hakika hakustahili. Magesa yeye hakuwa hata na habari
na kinachoendelea. Nanaa ni nani? Hakuwa hata na habari na anachokikosa
maishani. Bora apewe chakula, maisha yanaendelea.
Geb
akataka kumchukia mama yake, lakini akajua yeye ndio anawajibika kwa asilimia
zote. Alishindwa kusimama kwenye nafasi yake kama alivyoambiwa na Grace pia.
Alizidi kuumia kushindwa kujua yaliyokuwa yakiendelea na kule walikokuwa
wakipitishwa wanae, hasa Liv na yeye akiwepo ila hana habari. Akabaki akiwaza.
~~~~~~~~~~~~~
Alitamani
kuendelea kukaa pale hata asionane na mama yake kwa muda ili apate muda na
Mungu, lakini akakumbuka watoto wake. Jinsi Sara anavyowalalamikia, hasa Liv.
Akaona heri tu arudi, aanze kuwa baba. Akamkuta Magesa analishwa na mama yake. “Nipe
nikusaidie kumlisha.” Geb akamsogelea. “Mbona na wewe hauli tokea juzi?” Mama
yake akauliza. “Nipo kwenye maombi.” Geb akajibu kwa kifupi tu. Akaendelea
kumlisha mtoto wake. Alikuwa akila bila shida. Bibi yake alishamwanzishia uji
kwa kuwa alikuwa hashibi. Alikuwa na afya nzuri. Ungependa kumwangalia kila
wakati.
“Kesho
ndio ile birthday ya mapacha. Grace anataka iwe mapema.” Mama yake
akamkumbusha. “Nakumbuka. Kwa kuwa sitakwenda kazini, tutaongozana tu.” Geb akajibu
na kuongeza. “Kesho nataka na wewe
utoke, ukafanye mambo yako. Hata kama utaenda kutengeneza tu kucha, lakini
utoke ukapumzike na kujiandaa na hiyo party.” “Sasa nani atakusaidia swala la
watoto? Sara si mkaaji ndani.” “Usiwe na wasiwasi. Liv na Magesa
hawatanishinda. Wewe chukua mapumziko tu. Hata hivyo nataka muda nao. Nimekuwa
na mambo mengi, nimeshindwa kutulia nao.” Geb akaendelea. “Halafu naona
nimekuachia majukumu yangu ambayo nilitakiwa kuyafanya mimi mwenyewe kama baba.
Unahangaika sana juu ya watoto wangu. Umeacha shuguli zako, upo hapa kwa ajili
yao tu! Kweli nakushukuru. Pole na asante mama.” Yale maneno yalimuingia mama G,
yakawa kama hukumu tena, wala si faraja. Akabaki kimya kabisa.
Sara!
Ilipofika
mida ya saa mbili usiku, Sara akawa anaingia. Alimkuta Geb yupo na mama yake hapo
sebuleni. “Nimechelewa kweli sababu ya foleni.” Akajiongelesha. Kimya. “Hata
hivyo nimerudi tu. Lakini sijamaliza mambo yangu. Vitu garama kweli! Labda
kesho nitamalizia.” Sara alipita na
mifuko yake. “Ukishaweka mizigo yako, nakuomba uje tuzungumze.” Mama G
akamuwahi. “Powa, nakuja.” Sara akajibu.
Baada
ya muda akatoka. “Kwema?” Akauliza Sara wakati anakaa. “Nimezungumza na
shangazi yako, tumeona ni heri urudi tu kuishi kwa wazazi wako.” Sara akashituka
mpaka Mama G akamuona. “Kwa nini!?” Sara akauliza. “Naona nimezidiwa na
majukumu. Sitaweza kukuangalia wewe na watoto.” “Kwani mimi unatakiwa kuniangalia!?
Mimi mtumzima na akili zangu. Nimeishi Morogoro kwa miaka mitatu bila wazazi,
sihitaji kuangaliwa na mtu.” “Hilo ndilo tatiza Sara. Mimi nimelea watoto humu
ndani. Sijapata ambaye ananirudia saa mbili usiku. Nimekuza bila shida.
Nikiheshimiwa. Na..” “Kama ni swala la kuwahi kurudi nyumbani, hilo mbona
linazungumzika tu. Wewe niambie saa ngapi unataka niwe narudi nyumbani,
nitarudi. Wala usitokwe jasho.” Sara aliongea bila hofu huku akicheka nakutaka
kugonga.
“Sioni
sababu ya wewe kuendelea kuishi hapa wakati wazazi wako wapo. Unahitaji kurudi
kwa wazazi.” “Si nakusaidia swala la watoto!?” “Sara!” Mama G akashangaa maana
hata hakuwa akishinda nyumbani. Na anapokuwa nyumbani busy kwenye simu. Hakuwa
akitaka kufanya kazi. Kila kitu alimwachia mama G. Ataamka saa 4 asuhuhi au saa
tano. Ataoga na kujitengeneza. Kama Jeri yupo, basi atataka amsindikize kila
mahali. Zaidi kwa mashoga zake aliomaliza nao chuo, kujionyesha utajiri na gari
hiyo yakifahari ya Geb iliyoachwa hapo nyumbani kwa matumizi ya watoto wake. Lakini
Sara ndio akaanza kulitumia yeye rasmi baada yakuona muda mwingi Jeri anakuwepo
tu pale hana kazi.
~~~~~~~~~~~~~
Kazi
kubwa ya Jeri aliyokuwa akifanya na hiyo gari ilikuwa nikuchukua hao watoto
kuwapeleka kanisani na nyumbani kwa Grace. Walikuwa wakimpeleka hasa Liv,
kwenda kucheza na Fili kabla Danny na yeye hajapora wanae na kuwatawala. Mara
kadhaa walikuwa na Sara. Wakati mwingine Sara alipokuwa akifika hapo nyumbani
kwao na kuwakosa Danny na watoto wake, alikuwa akimpigia simu. Danny
akiwaelekeza walipo, Sara alimwambia Jeri wawe wanawafuata. Lakini mwishowe
wakaacha kwani Oliva aliacha kucheza kabisa. Mara nyingine aliishia kukaa
kwenye gari tu. Hakuwa akitaka hata kushuka acheze na watoto wa Grace. Hata
Fili amfuate ndani ya gari ambembeleze, Liv alikuwa akikataa. Ndipo Jeri
akamshauri mama G, waache tu kuwapeleka. Lakini sio Sara.
Sara
alifurahia kule kutoka na kukutana na kina Danny pamoja na watoto wake kwenye
mahoteli mbalimbali. Wakati mwingine walikuwa wakipanga na Danny labda jumamosi
fulani au siku fulani wapeleke watoto sehemu fulani. Wakikubaliana ndio ikawa
furaha ya Sara, ili tu kutoka. Lakini Jeri akaona haina maana. Kwa kuwa walikuwa
wakiishia kukaa kwenye gari yeye na Liv, Sara yeye ndiye aliyekuwa akishuka
kwenye mahoteli hayo kuungana na Danny na watoto wake. Jeri na Liv watakaa humo
ndani ya gari wakisubiri mpaka Sara achoke ndipo wanarudi nyumbani.
Pesa
alizokuwa akipewa na mama G hazikuwahi kumtosha. Kila siku alilalamika shida ya
pesa. Nywele aliyokuwa amesukia ni ya laki 350. Ametengeneza na kucha.
Ukimwangalia unaweza sema mtoto wa kisomali anayetumikiwa na mama G mle ndani.
Yeye alionekana bora kuliko hata mama G aliyekuwa amechoka akawa bibi
kwelikweli.
~~~~~~~~~~~~~
“Kweli mama. Sema yule mtoto wenu wa
kike ni mkorofi sana. Jeuri, haambiliki. Mtoto mdogo anataka yeye ndio awe kama
malkia humu ndani! Anaongea anapojisikia yeye. Akiamua kuwa kisirani, hakujibu
kitu.” Geb akasimama, nakuondoka pale. Akawaacha pale wao wawili wakizungumza.
Gafla mama G akageuka kuwa mama usiku huo, si bibi tena kwa Sara
aliyezoea kumwita bibi. Mpaka mama G, mwenyewe akashangaa.
Siku Ya Birthday
Kesho
yake asubuhi Sara aliamka yeye wa kwanza. Akasafisha na kusaidia kazi zote.
Mpaka mama G anaamka, yeye akawa amemaliza kila kitu. Mama G hakumuongelesha.
Akapita na Magesa wake, akaendelea na shuguli zake. Aliposikia sauti ya mtoto
wake, Geb akatoka. “Njoo.” Akamchukua mtoto wake. “Nimeshampikia uji.” Sara
akaongea kwa upendo, akimpa taarifa hizo Geb asijue alikorithi Liv. Kimya. Geb
hakujibu kitu. “Na dada mkubwa nimemtayarishia vitu vinono. Naamini atakula
leo.” Geb akampita nakuelekea sebuleni.
“Umeamkaje?
Eti Magesa?” Geb alimuongelesha mwanae. Mara dereva akaingia. “Ndio nimekuja
kukuchukua dada Sara.” “Kwenda wapi!?” Jeri akabaki kimya, akamgeukia mama G. “Anakurudisha
nyumbani, Sara.” “Mbona nimebadilika mama? Sitakawia kurudi tena. Kuanzia leo
nitabadilika.” “Wazazi wanakusubiri nyumbani. Nimeshazungumza na mama yako.
Nenda tu. Utakuja wakati mwingine.” Alishaishi na Grace mtoto wa kike wakumzaa.
Akawa na adabu zake. Akaja Nanaa, wakawa marafiki. Adabu na msaada bila hata
kuombwa. Sara ni waina ambayo hawezi kuvumilia.
Sara
aliondoka huku amekasirika sana. Aliongea maneno ya kashfa kabla yakuondoka na
kuomba alipwe kwa kazi na muda wote aliokuwa ameishi nao pale. “Karibia miezi
mitano sasa! Mmenizubaisha, nikashindwa kuanza kazi ofisini. Ningekuwa napokea
karibia milioni mbili kila mwezi. Nikabaki nikiwapangusa mavi watoto wenu!
Halafu leo mnanifukuza bila kosa!? Naombeni pesa yangu.” “Unataka kulipwa kiasi
gani?” Kwa mara ya kwanza Geb akaingilia.
“Kweli
Sara unasahau pesa zote nilizokuwa nikikupa!?” “Shilingi ngapi na wewe? Mtoto
wenu yule wa kike kiburi wakati hata choo hajui kutumia! Kumtoa diaper yenyewe
anaringa! Halafu hata shuku..” “Unataka ulipwe kiasi gani?” Geb akamkatiza. “Labda
milioni.” “Unapokea hundi?” Geb akauliza. “Nitafanyaje sasa kama nyinyi hamna
pesa tasilimu na hamuwezi kunirushia kwenye simu yangu?” Geb akamuweka mtoto
wake kwenye kiti chake chakulia, akaenda kwenye gari yake. Baada ya muda
akarudi na hundi.
“Nakuomba
Jeri, usipitie popote pale. Mshushe nyumbani kwao, hakikisha unamkabidhi kwa
wazazi wake, ndipo urudi nyumbani moja kwa moja. Kuna kazi nataka kukupa.” Geb
akatoa maagizo. “Sawa.” Jeri akatoka na Sara. Sara alikuwa akiishi kwa wazazi
wake Kitunda. Akakanyaga mafuta kuelekea Kitunda. Sara alitaka apelekwe benki,
lakini Jeri alimkatalia. “Natakiwa kurudi nyumbani mapema.” Jeri
akamkatalia katakata. Akakusudia
kumrudisha kwao.
Mama G!
“Mama,
wewe usiguse chochote leo. Pata kifungua kinywa. Nenda saluni. Tutakutana kwa
Grace. Leo nataka upumzike.” “Naona pia nipitie kwenye biashara zangu.
Nikachungulie kidogo, ndipo niende saluni. Sitakawia kufika huko nyumbani kwa
Grace.” Mama G alikuwa kama ameokota alumasi. Alikuwa na hao watoto masaa 24.
Mpaka alishachoka. Umri ulishakwenda, hana msaada wowote wakusaidiwa watoto wa
Geb. Kupata likizo ya siku ile, ilikuwa muujiza aliotamani utokee. Lakini kwa
kuwa aliyataka mwenyewe, hakuwa na namna. Ilibidi abebe mzigo wote bila
kulalamika huku akimuonyesha Geb inawezekana kabisa na ni rahisi sana.
Hakupoteza
muda, wala hakutaka kula. Akaoga na kutoka kwa haraka na gari yake. Hakuwa hata
akikumbuka siku aliyotoka humo ndani bila hao watoto. Hata kanisani alishaacha
kwenda. Hata kuomba tu yeye mwenyewe alikuwa akishindwa sababu ya watoto na
shuguli za humo ndani. Alihakikisha anahangaika sana kumwaminisha Geb kuwa
maisha yanaweza kuendelea vizuri tu bila Nanaa. Kumbe asijue garama anayolipa.
Alindwa
kukutana hata na marafiki zake sababu ya majukumu ya pale ndani. Hakuwa akienda
tena saluni wala kwenye sherehe kama zamani. Hakuwa akijua yanayoendelea huko
ulimwenguni. Yeye na watoto tu na shuguli za mle ndani kuhakikisha mambo
hayakwami na wala hayaharibiki. Akasahau pia kuwa umri ulishakwenda. Akawa
anajituma zaidi ya anavyotakiwa kama binti mdogo, akihakikisha mambo yote ya
mle ndani yanakwenda sawa. Chakula cha watoto na Geb mwenyewe, huku akihangaika
kumridhisha Sara atulie, ili Geb amuone ni kama binti wa kawaida, amuoe. Kumbe
Sara ni mapepe, mtoto ambaye hajui kutulia sehemu moja.
Sirini
Mwangani.
Jeri
alirudi akamkuta Geb amekaa na watoto wake nje, barazani. Akatoka kwenye gari
akaingia mpaka pale barazani. “Mama ametoka?” Akamuuliza Geb. “Ndiyo. Kwani
vipi?” Jeri akasita kidogo. “Kwani unashida na mama?” Geb akamuuliza tena
alipomuona anasura ya wasiwasi. “Hapana. Ni dada.” “Dada gani tena?” Geb
akauliza. “Mkeo!” Moyo wa Geb ukapasuka. “Nanaa!?” Akamuuliza. “Ndiyo. Tumekuwa
tukiwasiliana. Anaulizia hali ya watoto wake. Lakini nimekuwa nikimwambia tu
wanaendelea vizuri ili nisimuhuzunishe. Alikuwa akilia sana nilipokuwa
nikimpelekea watoto na kukataza asiwaguse. Sasa tokea jana ameniomba niwapige
watoto wake picha, kisha nimtumie.
Lakini kwanza nilisita kumpiga Liv. Alikuwa akilia sana, karibu siku nzima. Na
pili nikaona sio sawa kufanya bila kumuomba bibi yao. Maana aliniambia nisiwe
nakwambia wewe chochote, ila yeye.” Jeri akajieleza.
“Lakini
kaka, mama ni mama tu. Hata kama anatabia mbaya au chafu, lakini mama anayetaka
watoto wake, ni mama mzuri. Mkeo yule ni mzuri sana. Wasura, umbile na moyo.
Angeweza kuondoka kwako akaolewa kwingine na asikumbuke wanae. Lakini hajaacha
kuulizia watoto wake. Mruhusu awaone wanae, na awashike. Itamsaidia dada Liv.
Anazidi kunyongea kila siku. Hafananii hata na mtoto wa humu ndani. Amekonda
kama wale watoto wanaoishi kwenye nchi zenye vita! Bado anakumbukumbu zile
mbaya za mimi kumpeleka kwa mama yake na kumkatalia asiguswe na mama yake. Ni
kumbukumbu mbaya sana kwa mtoto yeyote yule. Najua ni ngumu, lakini bosi wangu,
kaza moyo kwa ajili ya wanao. Futa hiyo kumbukumbu mbaya kwa mwanao. Mwache
mama yake amshike. Hata kama utataka amshike sehemu ya nje. Hadharani tu. Hata
dakika moja tu. Mwache. Mnawaadhibu watoto wenu nyinyi wenyewe.” Kimya.
“Samahani
lakini kama nimevuka mipaka. Na mimi ni baba. Tunapitia changamoto kama zenu,
lakini zinatofautiana tu majina. Usifikiri mtoto wako huyo ni mdogo. Hapana.
Liv ni mkubwa na anaelewa kila kitu. Kama ukimchunguza vizuri, utagundua
hanipendi kabisa. Nikiingia tu, na akajua nipo mahali, hataniangalia kabisa,
kwa kuwa anajua ubaya niliokuwa nikimtendea yeye na mama yake. Nafikiri
anakubali nimchukue akidhani pengine namrudisha tena kwa mama yake, lakini
najua kwa hakika asingekubali hata niwe naye sehemu moja.” Jeri akaendelea.
“Na
pia nafikiri ameanza kujua ninakompeleka siko kwa mama yake, ndio maana kila
nilikokuwa nikimpeleka akaanza kukataa kushuka kwenye gari. Aligoma kushuka
mara kadhaa kucheza na Fili na wadogo zake. Kanisani ndio mara ya mwisho
ikabidi turudi tu nyumbani. Bibi yake alipomlazimisha kushuka kwenye gari,
alilia huyo mtoto, mpaka watu wote waliokuwepo pale nje kanisani walituzunguka
pale kwenye gari. Tukarudi nyumbani na hatukuwahi kwenda tena kanisani. Sasa
huwezi kujua hata wewe anakufikiriaje, akijua unajua anakopitia, na wewe uko
kimya tu! Utamuharibu kabisa mtoto wenu ambaye ni mzuri, sababu ya matatizo
yenu. Mmemuadhibu huyo mtoto vyakutosha. Sijui lakini, ni ushauri tu kaka.”
Jeri akanyamaza na Geb akanyamaza. Liv alikuwa kimya, akiangalia cartoon zake
kwenye tv, pembeni ya baba yake palepale nje barazani, huku Magesa akizunguka
kwenye walker yake. Akicheza.
“Kaka
mtu anakua haraka huyo! Anampita dada yake sasa hivi.” Jeri alisifia kama
kubadili mazungumzo. “Barua uliyopewa unikabidhi mimi, iko wapi?” Geb akauliza
bila maelezo mengi, lakini Jeri alielewa ni barua gani. “Nilimpa bibi. Lakini
alinionya nisikwambie. Tafadhali usiniharibie mahusiano yangu na bibi.”
“Unaweza kumwambia anaruhusiwa kuja kuwaona watoto.” “Hiyo dada alikataa
kwa kuwa bibi alinionya asiwaguse. Na yeye akasema hawezi kumtesa mtoto wake.”
“Mwambie utamruhusu kuwashika.” “Kweli bosi wangu!?” Jeri akajisahau. Geb
akabaki akimwangalia kwa jicho la tangia lini mimi na wewe tunataniana.
Lile
jicho likamsaidia kurudisha akili za Jeri
kazini. “Ngoja nimtumie ujumbe sasa hivi.” Jeri akajirudi kwa haraka na
kutuma ujumbe kwa Nanaa. ‘Kwa nini usije kuwaona tu?’ Akamtumia huo ujumbe Nanaa. ‘Niheri nisiwaone kabisa, kuliko niwaone wakiwa wanalia. Siwezi Jeri.
Nitakufa mapema sana.’ ‘Naweza kukuruhusu uwashike.’ Nanaa akakaa kwa haraka. ‘Kweli Jeri?’ ‘Kweli dada.’ ‘Basi nisogezee mpaka nyuma ya ukuta.
Sitaingia ndani.’ ‘Kwa nini dada?’ ‘Shida yangu ni watoto Jeri. Sitaki kuja
nakuibua matatizo mengine mwishowe nikazuiliwa kabisa hata kuona wanangu.
Naomba niletee wanangu kama ulivyoniahidi, tafadhali usinibadilikie.’ ‘Hapana
dada, siwezi kubadilika. Wewe njoo. Ukifika unijulishe nitoke.’ ‘Hapa nishatoka
nyumbani.’ ‘Sawa dada. Lakini kuwa mwangalifu.’ Geb akamuona Jeri anacheka.
“Nini?”
Akauliza. “Dada anaonekana amefurahi huyo! Tayari yupo njiani. Ona jumbe zake.”
Geb akapokea ile simu. Akazisoma na kumrudishia simu yake Jeri bila kuongeza
neno. Jeri akarudi kwenye gari kama kulisafisha kidogo ili watoto wa bosi
wakiingia wakute pasafi. Baada ya muda Jeri akarudi tena. “Bibi amefanya vizuri
kumtoa yule dada hapa. Japokuwa alitaka umuoe, lakini hakuwa akipenda watoto
kabisa. Na yeye alikuwa akikuogopa sana. Anasema huingiliki.” Geb akanyamaza.
Jeri akaona aondoke tu.
Chako Ni Chako
Tu.
Baada
ya kama dakika 45 hivi, Nanaa akawa amefika. Akampigia simu Jeri. Jeri akarudi
kwa Geb akiwa anakimbia. “Dada amefika.” Geb akamsaidia kuwapandisha watoto
kwenye gari. “Naomba kuwa mwangalifu.” “Sawa bosi.” Jeri akatoka na watoto. Geb
akarudi ndani kwa haraka sana. Moja kwa moja chumbani kwa mama yake akitafuta
barua aliyokuwa ameachiwa na Nanaa. Akahangaika bila mafanikio.
Huku
kwa Jeri akazunguka nyuma ya ukuta, akamuona Nanaa. Akashituka sana kumuona na
tumbo kubwa, akajua ni mjamzito. Akasimama. “Nakushukuru Jeri.” “Mama!” Liv
alishituka sana kumuona mama yake. Nanaa akamsogelea
Liv. “Nina hamu na wewe Liv.” “Beba mama! Beba!” Liv akaanza kulia. Nanaa akaingia ndani ya lile
gari akapiga magoti mbele ya kiti cha mwanae, akajikuta akilia sana. Akamkumbatia
Liv kwa muda mrefu. “Mama!” Liv akaanza kumbusu mama yake kila mahali. Nanaa
alikuwa amekata nywele. Lakini Liv aliweza kumtambua mama yake.
Akamwangalia
Magesa wakati Liv akiendelea kumbusu. “Hata siamini kama ni mwanangu huyu! Amekuwa mkubwa sana. Ana afya
nzuri! Sidhani hata kama ananijua mimi kama ni mama yake.” Akarudisha macho kwa Liv, alikuwa akimvuta. Nanaa
akamtoa kwenye kiti chake huku akifuta machozi. Akahamia naye kiti cha mbele.
Akakaa akiwa amempakata.
“Nyonyo!” Liv alivuta gauni la mama yake. “Husahau
tu! Maziwa hamna tena Liv. Yameisha yote. Unakula vizuri? Mbona umekwisha
hivyo? Tumbo linauma?” Nanaa akamuuliza kwa upendo. Lakini Liv akatingisha
kichwa akikataa kuwa haumwi. Akamlalia mama yake kifuani.
“Njaa
inauma?” Akakubali. “Naomba kaniletee chakula chake nimlishe. Tafadhali Jeri.
Nitakusubiri hapa hapa.” “Nikuache naye!?” “Hata kama ukiondoka naye, lakini
kaniletee chakula chake nimlishe mimi mwenyewe.” Kwa kuwa Jeri aliogopa kurudi
kwa bosi wake bila watoto wote. Akamtaka
Nanaa amrudishe na kumfunga kwenye kiti chake ili akafuate chakula. Liv alilia
sana. Hakutaka mama yake amuache. Mwishowe Jeri akaamua amuche tu na mama yake,
akimuomba asiondoke pale. “Siwezi kukimbia naye. Nitakuwa mwaminifu kwako Jeri.
Nenda tu ukaniletee chakula chake. Anaonekana ananjaa kweli. Nijie na begi lake
la diaper, nimbadilishe kabisa baada ya kula. Nisaidie Jeri.” Jeri akaondoka
kurudi kwa Geb.
Geb
akashituka sana. “Ameniambia hataweza kukimbia naye. Mtoto amelia sana bosi
wangu. Nimeshindwa kumchukua. Lakini amemwambia mama yake ananjaa. Ndio
amenituma chakula. Anataka akamlishe, akilala ndio tumrudishe. Sidhani kama ni
jambo baya.” “Na siku hizi hali vizuri. Ngoja nikupe chakula chake umpelekee.”
Geb aliandaa kwa haraka chakula cha Liv alichokuwa amekataa kula tokea asubuhi.
Akakiweka kwenye bakuli lenye mfuniko, akampa Jeri na begi lake. Jeri akatoka
kwa haraka huku akiomba Mungu Nanaa awe ametunza ahadi yake asiwe amekimbia na
mtoto.
Na
kweli, akamkuta Nanaa amesimama na mtoto wake akimsubira. “Asante dada yangu.”
“Nisingeweza kukimbia naye.” Nanaa akaingia tena ndani ya gari. Akaanza
kumlisha Liv chakula huku yeye amepiga magoti, mtoto wake amekaa kwenye kiti
chake. Magesa alikuwa akimwangalia tu mama yake. “Umekua mkubwa baba! Nakuombea
sana. Ipo siku Mungu atatupa nafasi yakufahamiana. Umesikia Magesa? Mimi ni
mama yako. Na ninakupenda sana.” Jeri alijikuta machozi yakimtoka. “Mungu yupo na nyinyi Liv. Umesikia mama?
Kila kitu kitakuwa sawa. Nawaombea kila siku. Mkono wa Mungu upo juu yenu.
Hakuna silaha yeyote itakayosimama juu yenu ikafanikiwa.” Nanaa aliendelea kuongea na watoto wake taratibu
huku Liv akimwangalia.
Liv
alikula chakula chote huku akimwangalia mama yake kwa makini sana. “Bado unao
tu mtandio wako wakunyonyea?” Nanaa akamuuliza huku akicheka kwa upendo. “Huo
hauachi popote. Ukitaka alie, mpokonye huo mtandio. Atalia mpaka awe mwekundu.”
Jeri aliongeza nakumfanya Nanaa alie sana. “Nirehemu Mungu wangu. Warehemu
wanangu. Usiwalipishe wanangu kwa kosa nililotenda mimi.” Jeri alimsikia Nanaa akiomba kwa kuugua sana
kwenye hicho kiti cha nyuma alichokuwa wamekaa watoto wake, yeye amepiga
magoti. Gari ilikuwa kubwa na ina nafasi yakutosha tu. Kutoka kiti hadi kiti
kingine kulikuwa na nafasi.
“Dada!
Naomba usilie. Utaliza na watoto. Muda ulipewa na hao watoto ni mfupi sana.
Jaribu kutumia vizuri.” “Ni kweli Jeri.
Nakushukuru.” Akamtoa Liv kwenye kiti, akaenda
kukaa naye kiti cha mbele baada ya kumbadilisha diaper na nguo iliyokuwa
imechafuka kidogo. Alishamfuta vizuri. Akamkumbatia huku akimbusu kila mara.
Nanaa alikuwa na namna anayomshika huyo mtoto. Wakati wote alimpapasa mwanae
mpaka analala. Na Liv aliitambua mikono ya mama yake tokea mtoto. Akamrudisha
kwenye kiti chake. Akamfunga vizuri. Akambusu mara kadhaa, akashuka.
“Mungu wangu akutendee mema Jeri. Akuonekanie siku utakayomuhitaji kama
mimi. Nakushukuru sana, tena sana.” Machozi
yalikuwa yakimtoka Nanaa. “Amina dada. Unafikiri lini utakuja kuwaona tena?”
“Mmmh! Sidhani. Sijui lini nitaamka vipi. Afya yangu kama unavyoniona. Mbaya
zaidi nimeishiwa nguvu kutoka ndani. Sina nguvu na sina sababu ya kupambana
tena. Sidhani hata kama huu mwezi nitamaliza Jeri.” “Usiseme hivyo dada.” “Kwa jinsi ninavyojisikia na vipimo vya huko
hospitalini! Madaktari wenyewe hawajui nimebakisha siku ngapi. Ndio maana
nilikuwa nikikusumbua unitumie picha za wanangu niwoane. Sijui kama nitakuja
kuwaona tena. Naumwa tokea ndani ya moyo. Nimepigwa haswa, tokea ndani ya nafsi
yangu. Lakini Mungu akiniongezea siku, nitakujulisha tu. Nije kuona tena wanangu.” Nanaa
akafuta machozi.
“Nakuelewa
dada yangu. Nakuombea uzima. Upone. Uje ulee wanao.” “Amina na asante Jeri.” Akaona Magesa anamwangalia kwa makini sana.
Alimsindikiza kwa macho kila mahali na kumtizama kila anachofanya kwa dada
yake. “Naomba ni mbembe hata kidogo, kama atakubali.” “Hamna shida.” Jeri
akamruhusu. Akaenda kwa haraka kule alikokuwa amekaa Magesa. Akafungua mlango. “Naomba
nikubebe kidogo tu mwanangu.” Magesa alitulia kimya huku akimtizama na macho
kama ya baba yake. Rangi ya mama, sura kama Geb. Nanaa akambusu, kisha akamtoa
pale kwenye kiti. Akambeba kisha akamuweka kifuani. Alipitisha mikono yake yote
juu yake, akamkumbatia kwa nguvu sana.
“Sijawahi
kukusahau Magesa mwanangu. Nakupenda na ninakuombea sana.” Nanaa aliongea na
mwanae huku amemkumbatia. Alipomuona ametulia, akarudi kukaa naye kwenye gari
pale pale mbele. Akamfanyia kama anavyomfanyiaga Liv. Jeri akashangaa analala
hapo hapo. Wote wakacheka. “Alikuwa amechoka.” Nanaa akanong’ona huku anashuka.
“Ipo nguvu ya ajabu kwenye mikono ya mama, dada yangu. Ni siri ambayo Mungu
mwenyewe ndio anajua.” Jeri aliongea kwa hisia huku akimuhurumia Nanaa.
Geb!
Huku
nyuma baada ya Jeri kuondoka tena, Geb akarudi tena chumbani kwa mama yake.
Akaanza kuisaka tena ile barua. Akaikuta chini kabisa kwenye droo aliyokuwa
anasita kufungua tokea mwanzo. Lakini ilibidi ajikaze baada yakufungua na
kupekua kila mahali na kuikosa. Kumbe ilifichwa kwenye droo ya chupi na sidiria
za mama yake. Alijua wazi Geb hawezi kufika huko.
“Geb!” Ndio neno alilokutana nalo juu ya
bahasha. Mwandiko wa Nanaa. Akajua ndio yenyewe. Akaifungua hiyo bahasha kwa haraka
kama asiye na imani kama bado ipo. Ilionyesha wazi ilisha funguliwa. Akajua
mama yake alishaisoma. Akaipiga picha kwa kutumia simu yake. Mbele na nyuma.
Akairudisha vile vile, pale pale alipoikuta. Akatoka kwenda kusoma nje barazani,
alipokuwa amekaa na watoto wake.
~~~~~~~~~~~~~
Wakati
anatoka tu, na Jeri naye akawa anarudisha watoto. Geb alimuona kama aliyekuwa
akilia. “Kwema?” Geb akauliza huku akitoa watoto kwenye gari. Alianza na Liv. “Amekula
vizuri kweli. Mama yake amempakata, akalala.” “Na Magesa naye?” Geb akauliza. “Utashangaa
nguvu ya mama. Si unamjua Magesa asivyopenda kushikwa na mtu? Basi leo
amemuangalia mama yake mpaka akambeba. Alimpakata na kumbembeleza kama vile
Liv. Si unajua vile dada anavyomshikaga Liv?” Geb hakujibu.
Alishachukuliwa
na hisia mpaka vile Liv alivyokuwa anapenda mikono ya mama yake, huku
akibembelezwa na nyonyo. Hapo anakuwa hana rafiki wala undugu. Mpaka aridhike
ndipo anatoka kwenye mikono ya mama yake. “Basi ndio leo alivyomfanyia na
Magesa. Alilala hapo hapo mpaka tukamcheka. Lakini…” Jeri akanyamaza. Geb
akamwingiza Liv ndani. Akarudi kumchukua kaka yake. Kisha akatoka tena.
“Ulisema
lakini. Lakini nini?” “Dada ni mgonjwa. Halafu hivi unajua ni mjamzito?” Nusura
Geb aanguke. “Anatetemeka mikono kweli! Hata sijui amefikaje hapa!” Kimya. “Nilimwambia
ni lini aniambie atataka kuwaona tena watoto. Lakini nimemsikiliza, ni kama
amejikatia tamaa. Ni kama aliyekuja kuaga wanae. Hadhani kama atakuja kupona tena.
Anasema ameishiwa nguvu kutokea ndani kabisa. Hawezi kupambana tena. Na huko
hospitalini wanamuhesabia siku za kuishi. Inaonekana majibu aliyopewa huko
hospitalini si mazuri. Ila dada ni mgonjwa sana. Anaonekana amejikaza tu kufika
kuona wanae.” Jeri alimsimulia kila kitu, akamuacha na habari zilizovunja
mifupa ya bosi wake. Akamuaga, yeye akarudi ndani.
~~~~~~~~~~~~~
Alipiga
magoti nakuanza kulia mbele za Mungu, asijue chakufanya. Ni kweli Nanaa
amemuumiza sana. Leo anasikia ni mjamzito wa mtoto wa Malii! Lakini ni mama wa
watoto wake. Grace naye alishampitisha kwenye maandiko ya bibilia 1koritho
13:4-8. Geb alibaki amepiga magoti. Asijue afanye nini. Akakumbuka anayo barua
kutoka kwa Nanaa. Ipo kwenye simu yake. Hamu yakumsikiliza ikamwingia. Akatoa
simu yake, akaanza kusoma akiwa pale pale amepiga magoti.
‘Geb mpenzi
wangu, nimekukosea sana. Najua hakuna jinsi unaweza hata kunisikiliza tena,
lakini naamini ipo siku Mungu atakupa rehema yakunisamehe. Nashukuru kwa
kuniruhusu kuendelea kuishi hapa, lakini Geb, kumbuka hii nyumba tulihamia mimi
na wewe. Wote wawili ndio ilikuwa mara yetu ya kwanza kuhamia hapa. Nakumbuka
usiku wetu wa kwanza chumbani kwetu, ulinisisitiza na kuniomba nikutengenezee
‘home’. Ukasema hili jengo halina maana kama sisi wote hatutakuwepo humu ndani
na kama hakutakuwa na amani. Nakiri kuivunja hii nyumba kwa mikono yangu mimi
mwenyewe. Sina chakujitetea. Nakutetea hata mbele za Mungu, ulifanya kwa nafasi
yako. Tena kiuaminifu sana. Sijawahi pata mapenzi kama uliyonipa Geb. Nakiri,
na ninakutetea mbele za Mungu, hata mbele za watoto wetu hapo baadaye. Hakika
huna hatia Geb. Upo sahihi kuniacha.
Japokuwa nimeshindwa
kutimiza nilichokuahidi, lakini nakuahidi kukuombea. Nimetubu. Na nitaendelea
kutubu kwa kutokukwambia ukweli wote na kuishia kukuumiza mpenzi wangu. Najua
Mungu atanisamehe na kunisikiliza. Nimeambiwa unatafutiwa mke ili uoe.
Nakuahidi kukuombea mpenzi. Nitakuombea bila kuchoka ili Mungu akupe mwanamke
atakayekupa yale yote niliyoshindwa mimi kukupa. Na asikuumize kama
nilivyokuumiza mimi. Nakuombea faraja na amani ile ipitayo fahamu zote,
ikufunike Geb. Najua unaweza ukaona haitawezekana kwa yale niliyokusababishia.
Lakini Geb, Mungu yupo. Jipe muda tu, ipo siku Mungu atarejesha furaha
yako kwa upya.
Hili jengo na vitu vyote
vilivyomo humu ndani ni vya thamani sana. Lakini haviwezi kukamilika kama wewe
na watoto hampo humu ndani. Sitaweza kuishi humu ndani peke yangu. Hata hivyo
naona itakuwa mateso makali zaidi kwa Liv. Analia sana akiniona. Anataka nimshike,
wakati umeweka masharti magumu sana kati yangu na wanangu, Geb.
Ni heri
niondoke wazoee kuwa hawana mama, kuliko hivyo wanavyolia nakushindwa
kuwabembeleza wanangu. Inaniuma kuliko nitakavyokueleza. Unajua jinsi
nilivyokuwa nikiwazaa kwa shida. Ilikuwa kufa nakupona ili wao wazaliwe.
Sikubahatika kuwa na mama. Ningependa wanangu wanione. Lakini sio kwa mateso ya
kiasi hicho Geb. Sitaki wanangu walipe garama ya kosa langu. Ni heri niondoke
tu. Naamini Mungu atawasaidia kwa namna nyingine.
Sitarudi tena
hapa. Kuwa huru kuuza tu. Najua hutaweza kuja kuishi tena humu kwa yale
yaliyotokea humu ndani. Hata mimi sijaweza kupata usingizi tangu usiku ule.
Imekuwa mateso matupu. Kwa hiyo kuwa huru kufanya chochote na hii nyumba yako.
Mimi nakwenda kuanza upya, sehemu nyingine.
Hakika
nakushukuru Geb. Asante kwa mapenzi ya kweli uliyonipa. Nakuombea kila la
kheri. Mungu akujalie hekima ya kuwalea watoto wetu vizuri. Mungu azidi
kukufanikisha katika kila eneo la maisha yako.
Nanaa.’
Hiyo
barua haikuwa faraja hata kidogo kwa Geb, ila hukumu ambayo hakujua afanye
nini. Alikaa pale akirudia kuisoma bila kuridhika. Alikumbuka pressure kali
sana iliyomsumbua Nanaa kipindi ni mjamzito wa Magesa. Lakini akapambana mpaka
akamzalia mtoto. Nanaa sio wakutangaza kifo. Hata madaktari walimkatia tamaa,
lakini yeye alisimama akitia moyo kila mtu hata wauguzi akiwaambia wasiogope.
Lakini leo anasikia amepoteza tumaini kabisa! “Lakini mtoto sio wangu!” Geb akajitetea nafsini kwake.
Ni
yeye pekee, mwanamke wa kwanza aliyemuonyesha kumpenda kwa dhati. Hata barua
yake ilijaa mapenzi matupu. “Hakuna
mwanamke atakayekuja kunipenda kama Nanaa.” Geb akawaza. “Lakini ni muongo, Malaya. Alikuwa akinionyesha
kunipenda na kunijali mimi kumbe huku anavulia nguo wanaume wengine na…”
Akanyamaza. Akabaki pale chumbani akiwaza hili na kujitetea kwa lile, mpaka
muda wa kwenda nyumbani kwa Grace ulipofika.
Kilio cha
Liv!
Wakati
anakaribia kuamsha watoto wake ili awaandae waende nyumbani kwa dada yake, Liv
aliamka nakuanza kumuita mama yake akiwa palepale kitandani. Geb akamsikia.
Akajua anaota. Liv alilala akiwa amekumbatia na mama yake, anaamka yupo
kitandani kwake, mama yake hayupo! Akaanza kulia akimtaka mama yake. Geb
akaenda. Liv alipomuona tu akajisogeza mwisho kabisa wa kitanda chake, hataki
baba yake amguse, anamwita mama yake. “Mamaa!”
Kilio
kikali chakukataa hata asiguswe na baba yake kikamuamsha Magesa. Akakaa
akisikiliza huku akimwangalia dada yake akilia huku akishindana na baba yake
asimguse. Hakutaka kabisa Geb amguse. Magesa alipoona ile hali na yeye
akaongeza nguvu. Geb yupo peke yake, watoto wote wawili wanamlilia. Liv
haonyeshi ushirikiano hata kidogo. Hataki hata baba yake amguse, tena alilia
kwa ukali huku akimtizama kama kumuonya asimsogelee. Ndipo akaamini aliyosema
Jeri juu ya hasira ya Liv kwa baba yake. Geb alikaribia kuchanganyikiwa. Alikaa
hapo zaidi ya nusu saa, Liv akilia kwa uchungu sana. Alifanikiwa kumtuliza
Magesa, akamlisha na kumbadilisha nguo. Mpaka anamaliza, Liv alisha jibembeleza
na kupitiwa na usingizi pale pale kitandani akiwa amejikunja, na kushikilia
mtandio wa mama yake. Geb hakutaka hata kumbadilisha. Akambeba kwa tahadhari,
na kumwingiza kwenye gari mpaka nyumbani kwa dada yake.
Nyumbani
kwa Danny na Grace.
Alimkuta mama yake na Grace wapo kimya na msichana wa kazi, watoto hawapo. Kulikuwa na vyakula, vinywaji, mpaka keki ya mapacha ilikuwepo. Grace alishaiandaa, lakini hakuwepo Danny wala watoto wao. Geb akawashusha watoto wake, Liv alimuweka kwenye kiti pale pale nje bustanini, na Magesa alimuweka kwenye walker yake akawa anatembea kila mahali huku akimlinda asigonge meza na kuangusha vitu. Liv alijikunja kwenye kiti akanyamaza kimya. Bibi yake alimuita mara kadhaa akitaka ambebe, lakini Liv hata hakumtizama. Wakaamua kumuacha. Kimya kikazuka.
Lisaa
la kwanza likapita. La pili na la tatu. Geb hakutaka kuuliza kwani mbali na
salamu, hata wenyeji wake walikuwa kimya kama alivyowakuta. Walikaa pale mpaka
saa tatu usiku ndipo wakaona gari ya Danny ikiingia getini. Grace akasimama
kuwasogelea.
“Mbona
umechelewa kurudisha watoto mpaka wamelala, wakati nilikwambia nimewaandalia
sherehe hapa?” Grace aliuliza kwa upole tu. Lakini mama yake, Geb na msichana
wakazi waliweza kusikia. “Nimekwambia nimechoka na matambiko ya kwenu.
Umekusanya ndugu zako mje kuwalisha wanangu madawa yenu? Haitakaa ikatokea tena
Grace. Nimekwambia inatosha, naomba uniamini mimi kuwa inatosha. Wanangu
wameshasherehekea sherehe yao na watu wakaida. Wamecheza, wamekula na
nakufurahi na watu wakaida, inatosha.” Walimsikia Danny akijibu kwa jazba.
Grace akanyamaza.
Mara
wakamuona Sara anashuka kwenye gari. Alikuwa amevaa nusu uchi. Kikaptura
kilifika kwenye hips, na kiblauzi chepesi. “Nikusaidie watoto?” Sara akamuuliza
Danny. “Wewe shusha mizigo yako tu. Nitabeba watoto.” Danny akajibu
nakumshangaza Grace. Sara akazunguka nyuma ya gari nakuanza kushusha mabegi
yake.
“Ni
nini kinaendelea Danny? Kwani Sara anahamia hapa?” Grace akauliza tena. “Ndiyo
na kumfukuza kama walivyomfukuza mama yako na Geb, hutaweza na sitakuruhusu.
Hapa ni kwangu na mimi nina uhuru wa kumwalika nimtakaye. Huwezi kuishi naye,
ondoka uniache nifanye ukarimu kwa ninayemtaka. Nenda kaishi na watakatifu
wenzako.” Danny akajibu huku akimfungua Fili mkanda.
“Watu
msioweza kuishi na watu. Mmezoea kutumia kila mtu! Mkiona hamnufaiki na huyo
mtu, mnamfukuza. Mmemfukuza Sara kwa kuwa ameshindwa kuwa kijakazi wenu. Hawezi
kuwatumikia kama mlivyozoea kututumia wengine. Mkamfukuza kama mlivyomfukuza
Nanaa. Kawazalia watoto, mmeona idadi ya watoto mnaowataka imetimia, tena Mungu
naye akafanya kosa la milele. Kawapa wakike na wakiume, harakaharaka. Mmeshamkamua
mtoto yatima. Mnayejua hana pakulilia wala kushitaki, mkamnyang’anya
watoto wake. Akiwa bado na maumivu yote. Yakuzaa na kubakwa, mkamfukuza kama
mbwa! Sasa hapa ndio mmefika. Sara atakaa humu ndani atakavyo yeye. Ni kwangu,
na hamna wakuniambia kitu. Nyinyi si mnajidai ni wachawi sana, kalogeni sasa.”
Danny alikuwa akiongea kwa jazba. Ukali ulizidi mara tatu yake. Alikuwa
akiingia na kutoka huku akiongea.
Alipomaliza,
akaenda kupiga teke meza ya keki. “Mmefanikiwa kunilisha mimi
mauchawi yenu, komeni kwa wanangu.” Akaisambaratisha ile keki yote huku
wakimwangalia. Akaimwagia na mchanga kabisa. “Marufuku kuja kufanya ibada zenu
za matambiko hapa. Mlinipata mimi, sitaki muwafikie wanangu. Komeni kabisa.”
Danny akaingia ndani kwa hasira.
Hapo
ndipo walipojua kwa nini hawawaoni watoto wa Danny wala Danny mwenyewe nyumbani
kwao. Na kujua kwa nini Grace anakonda. Danny akatoka tena. “Naombeni muwatoe
hao watoto nyumbani kwangu. Tafadhali sana. Mnaninyima usingizi.” Danny akaanza
tena. “Kwanza nawasifu. Mnaroho mbaya ambazo ni nyinyi tu watatu ambao
mnazielewa roho zenu. Na mnajijali nyinyi tu watatu. Hata watoto wenu wenyewe,
damu zenu, mnashindwa kuwajali! Halafu eti leo ndio mnakuja nyumbani kwangu
mnajidai mnataka kusherehekea birthday za watoto wangu, kama si uchawi wa
mchana kweupe ni nini!?” Danny akawasogelea.
“Yaani
leo mnajidai mnaupendo wakuwapenda wanangu wakati watoto hao wawili tu,
mmeshindwa kuwajali! Liv amekwisha kama kitoto chenye ugonjwa wa mifupa. Mtoto
amebaki mifupa mitupu! Mbavu zinahesabika! Halafu bila aibu, mmemjaza dhahabu
na magauni ya garama! Nyinyi ni binadamu gani jamani! Hamumuogopi huyo Mungu
wenu mnayejifanya mnamfahamu? Watoto wadogo hivyo, mnawatoa kwa mama yao, eti
wanalelewa na bibi! Kwa kipi na kwa nini? Ndivyo mganga wenu alivyowatuma nini?
Ili muendelea kutajirika. Ukute mlikuwa mnatafuta watoto wakuwatolea matambiko
ili muendelee kutajirika.” Danny akaendelea.
“Sasa
kama Grace hakuwaambia, ndio nawatangazia wazi kabisa nyinyi kina Magesa.
Hamtakaa mkawa karibu na wanangu. Hata iweje, ninawatenga na kuwafuta kwenye
maisha ya wanangu. Logeni hao hao watoto wenu. Sitaki niwaone karibu na mtoto
wangu hata mmoja. Na nishaongea na walezi wangu, jumapili ijayo nawapeleka
Iringa, wakabatizwe kabisa. Watulie kwenye dini iliyonilea mpaka leo. Haya,
naombeni ondokeni.” Geb akasimama bila kujibu kitu.
Akambeba
Magesa. Akaenda kumfunga kwenye gari, Liv akajua zamu yake inakuja. Hakutaka
kushikwa. Akateremka pale kwenye kiti taratibu, akaongoza njia kwenye gari. Geb
akamfungulia mlango. Akaanza kuhangaika kupanda akionyesha wazi hataki
kusaidiwa. Geb alibaki akimwangalia. Alipambana mpaka akaweza kupanda mpaka
kwenye kiti chake. “Naweza kukusaidia kufunga mkanda.” Geb aliongea naye kwa
upole. Liv akanyamaza. Geb akajua hata yeye anajua hawezi kufunga mkanda.
Akamfunga. Wakati anamalizia, akasikia gari ya mama yake ikitoka getini. Na
yeye akapanda gari yake akaondoka. Grace alikuwa kimya kabisa. Hakujibu kitu,
akaingia ndani.
Baada
Yakuona Wanae.
Nanaa
akatoka pale akampigia simu daktari wake anayemuona kliniki. “Nimeamua tu kutoa huyu mtoto kama ulivyoshauri.” “Unauhakika Nanaa?” Lyamu akauliza.
Kimya. “Uko wapi wewe Nanaa? Unatetemeka
mpaka mimi huku nakusikia! Utakufa barabarani. Hebu njoo huku hospitali ya Tumaini.
Chukua taksii.” Nanaa akashuka tena kwenye
daladala, akapanda taksii kama alivyoshauriwa na daktari wake. Akaomba apelekwe
hospitali ya Tumaini.
Ukweli
alikuwa na hali mbaya. Kila alipokumbuka sura ya Liv, alizidi kulia asijue kama
aishi au afe. Kuendelea kuishi na ile mimba nikukubali kufa. Kuitoa, ndio
kupona kwake. Presha ikazidi kupanda. Mara nyingi pressure inapokuwa juu, mimba
huwa hutoka zenyewe. Lakini sio watoto wa Nanaa, kitu kilichokuwa kikimshangaza
kila mtu aliyekuwa akimpima akiwa mjamzito na pressure aliyokuwa nayo. Alizidi
kutetemeka, hata yeye akajua safari hii anapata stoke. Yule dereva taksi
akamfikisha pale hospitalini, lakini akashindwa hata kumuacha aende peke yake.
Akamshika mkono mpaka ndani ofisini kwa dokta Lyamu.
Daktari
alipomuona tu akaomba nesi ampe sehemu ya kupumzika. Akaomba achomwe sindano ya
usingizi. Lyamu akachukua vitu vyake vyote, akafungia kwenye ofisi yake. “Mwacheni
alale leo. Kesho nitakuja kumwangalia.” Daktari akamwandikia dawa. Akamuacha alale.
~~~~~~~~~~~~~
Aliporudi
tena kesho yake nakumuuliza swala la kumtoa mtoto anayehatarisha maisha yake,
Nanaa akasema amebadili mawazo. “Mbona hata sishangai!” Nanaa akacheka
akionyesha amedhoofu. “Sasa hivi nipo tayari kufa. Sina hofu tena.” “Na Liv?” Lyamu
akamuuliza akijua kilio chake ni Liv. Nanaa akanyamaza. “Unajua sijawahi
kukutana na Nanaa huyu! Nanaa ninayemfahamu mimi ni mpambanaji. Mbishi mpaka
kwa kifo! Ni nini kimekupata Nanaa?” “Huyu mtoto sio wa Geb, dokta. Geb hataki
hata kuniona. Amenifukuza na kuninyang’anya watoto wangu wote mpaka yule
uliyenizalisha wodini.” “Magesa?” Daktari akauliza. “Huyo huyo. Kwani na wewe
umenizalisha wangapi?” Lyamu akacheka nakutingisha kichwa.
“Niliwaona jana kwa kuibiwa na dereva wao.
Magesa amekuwa mkubwa, hata hanifahamu. Huyu mtoto nilibakwa na rafiki yake
Geb, tena mbele yake Geb. Sina sababu ya kuishi. Sina kinachonibakiza hapa
duniani. Kama huyu ananiua, acha nife naye tu, nirudi naye huko alikotoka.” Lyamu akamwangalia Nanaa. Akamuongezea dawa.
Akalala.
~~~~~~~~~~~~~
Mambo yanazidi kuwa mambo.
Nani amelikoroga na nani analinywa sasa hivi?
Kila nyumba inawaka moto. Hakuna kwenye amani wala utulivu. Si kwa
Nanaa aliyebakwa, wala kwa kina Magesa. Sasa hivi Nanaa yupo tayari na kifo
huku mwanae Liv, yu mahututi - mzima.
·
Sara aliyetakiwa kuwa mke wa Geb,
Sasa yuko na Danny, kwenye nyumba yake na Grace. Kwa makubaliano Yepi? Hata
Grace hafahamu.
·
Mama G, amelemewa. Danny
amempasukia bila hofu kama aliyetumwa. Umri umeenda watoto wanahitaji ungalizi
zaidi, na Liv ndio hawataki kabisa.
·
Geb amejua ukweli wote, lakini
akajitetea nafsini kwake kwa yale aliyoumizwa na Nanaa. Lakini Grace
alimwambia, kuna mapengo hayazibiki. Hata Liv amemthibitishia hilo. Cheko na dimpozi vya Liv, vimepotea
kabisa. Hataki hata baba yake amguse.
Nini kitaendelea? Nani wa Nani
kwenye simulizi hili?
Mahesabu yameshapandana.
Grace amesema ndoa yake
ilishaisha ila anaendelea
kuomba, mpaka lini!?
·
Sara ambaye alikuwa aolewe na
Geb, sasa yupo kwa Danny.
·
Nanaa anasubiria kifo chake
hospitalini.
·
Geb ameamua kuwa baba wa watoto
wanaonza kumbadilikia. Liv
aliyezoea kuwekwa kifuani na baba
yake akisikilizia furaha, huku
akigugumia ‘Mhhhhhh!’ siye Liv huyu.
Nani wa Nani?
Endelea kufuatilia.
0 Comments:
Post a Comment