“Tafadhali Geb. Kabla sijaingia
chumba cha upasuaji naomba nikusikie kuwa umenisamehe. Naweza nisitoke tena.
Naomba angalau nife nikiwa najua nimekuacha na watoto wangu ukiwa huna hasira
na mimi.” Manesi walishaanza kusukuma
kitanda kumtoa Nanaa pale ndani, daktari akionyesha hataki kupoteza hata dakika
moja mbeleni. “Geb please!” Nanaa akasisitiza huku akilia. Geb akawasogeza
wale manesi kwa haraka, akainama pale kitandani na kumbusu Nanaa midomoni.
Nanaa alisikika akiendelea kulia, wasijue ni furaha au uchungu.
Alimbusu
kwa muda kidogo. Akamwangalia. “Nilishakusamehe Nanaa. Lakini lazima utoke,
ujue nakusubiri tufunge ndoa.” “Bado
utanioa!?” “Kabisa. Nilitaka kukufanyia
surprise. Nilitunza busu langu mpaka siku ya harusi yetu.” Nanaa akazidi kulia.
“Nilijua umenikasirikia Geb!
Ungeniambia.” “Ilikuwa surprise Nana! Magesa
ndio ameharibu.” Nanaa akacheka huku akifuta machozi. “Siogopi tena.” Nanaa akaongea nakufanya kila mtu acheke.
“Lazima
twende sasa hivi.” Daktari akarudi pale walipokuwa wamesimama. “Nimemwacha mtu
ameshikilia lifti. Twendeni tuwahi.” Daktari akasisitiza. “Naruhusiwa kuingia
na mimi tukifika chumba cha upasuaji?” “Hapana! Ingekuwa ni labor, hapo sawa.”
“Daah!” Geb akasikitika. “Nitakuwa nikikusubiri nje ya chumba cha upasuaji. Ukijifungua
tu, tunafunga ndoa, tunaenda kupumzika.” Kila mtu alikuwa nyuma ya hicho
kitanda wakimsindikiza Nanaa, kutoka chumba alichokuwa amelazwa kwa mapumziko
hapo hospitalini, chini kwenda chumba cha upasuaji jengo hilohilo lakini gorofa
ya juu. Walikuwa wakiiendea lifti ili iwatoe hapo wodini.
“Tutawaacha
watoto, wakati tunaenda honeymoon?” Nanaa akauliza huku akikunja uso. “Mama
atabaki nao. Vipi mbona unakunja uso?” Geb akajibu na kuuliza. “Nasikia maumivu makali.” Nanaa alianza kulalamika huku akilia. “Nasikia mtoto wangu anatoka jamani!” Nanaa aliongeza sauti iliyojaa kilio. “Mtoto
wangu mimi!” “Nisikilize Nanaa. Pressure ipo juu sana. Tumaini
pekee alilobakisha Magesa ni wewe kutulia ili akitoka awe salama na wewe
akukute. Unaweza kutulia.” Nanaa akatingisha kichwa na kufunga mdogo hapo hapo
huku akifunga miguu.
“Hapana
Nanaa. Huwezi kufanya hivyo.” Daktari akarudi kutoka ilipokuwepo lifti.
Ilishakuwa imejifunga. Kuashiria inatumika kwenye magorofa mengine.
Walichelewa. Daktari akaingiza mkono ndani ya ile shuka.
“Nimeshika
kichwa! Hatutafika chumba cha upasuaji. Turudini chumbani kwake.” Kwa haraka
wakageuza kile kitanda kurudi chumbani kwa Nanaa. Hapakuwa mbali sana na hapo
kwenye lifti. “Naombeni wote mnisubiri hapo nje.” Daktari alitoa amri hiyo
akionyesha wasiwasi usoni. “Geb
njoo. Nimeanza kuogopa tena.” Nanaa akamuita akiwa
amenyosha mkono. “Wewe unaruhusiwa.” Daktari alimgeukia Geb. “Usiogope Nanaa.
Kila kitu kitakuwa sawa.” Geb akamshika mkono na kumbusu. Nanaa ndio alikuwa
amebeba hatima ya mtoto wake. Mtoto aliyetabiriwa tangia Geb ni mtoto mdogo.
Ilimlazimu Geb kutulia sana, ili kuwa faraja kwa Nanaa, ili kuhakikisha kusudi
la Mungu linatimilika. “Tunakuombea Nanaa, wifi yangu. Na ujue tunakusubiri
hapa hapa nje.” “Asante Grace.” Nanaa alijibu huku akiingizwa ndani ya kile
kile chumba alichokuwa amelazwa. Mama G akakimbia na kumbusu Nanaa.
“Nakusubiria mwanangu. Jikaze. Umefikia mwisho wa hayo mateso. Wewe nitolee tu,
nitalea mwenyewe.” Nanaa akacheka huku anafuta machozi. Akatoka na kuwapisha.
~~~~~~~~~~~~~~
Kila
mtu alikuwa kimya akimwita Mungu aingilie kati kwenye ile hali. Mtoto alikuwa
anatoka huku kwa kiutalamu, Nanaa mwenye pressure iliyo juu sana, hawezi kuzaa
kwa njia ya kawaida tena kwa wakati huo. Funga na kufungua chumba cha Nanaa
kilishajaa madaktari. Alikuwa amelazwa first class, kwenye hospitali hiyo ya
garama za juu sana nchini. Kwa hiyo hata uangalizi wake ulikuwa wajuu. Manesi
wenyewe walikuwa wakimuheshimu kwa kuweza kumudu chumba hicho tena kwa
mapumziko ambayo Geb alikuwa tayari kulipia kwa siku 21 ambazo Nanaa angetakiwa
awepo mpaka ajifungue.
Chakula
na usafi wa hospitalini hapo, ungeona. Ungejua ipo pesa inayofanya kazi.
Alikuwa akihudumiwa kwa hali ya juu sana. Uzuri ni kuwa, daktari huyo huyo
aliyekuwa akimuhudumia kipindi cha ujauzito wa Oliva, aliyekuwa amempata kwenye
hospitali ya bure ya taifa, kumbe alikuwa akifanya na hapo kama ‘part time’.
Kwa hiyo Nanaa alibadilisha tu mazingira, ila huduma ya daktari wake aliyekuwa
amemzoea tokea zamani ilikuwa ile ile. Kutoka kwenye kumtibu bure na kumsaidia
vitu vingine, safari hii daktari huyo anavuna wema wake kwa kula pesa ya Geb,
aliyemwambia ahakikishe huyo mtoto anazaliwa salama na Nanaa anaishi.
Alishazungumza
naye baada ya kutoka kliniki. Wakati mimba ya Nanaa bado ndogo tu. Geb akiwa
amemfuata kwa siri kujua jinsia ya mtoto huyo. Alipomtajia kuwa ni wakiume, Geb
akamwambia yule daktari kuwa huyo mtoto anaitwa Magesa. Alishatabiriwa na babu
yake tokea hata yeye mwenyewe Geb hajakuwa kijana mkubwa. Kwa hiyo afanye juu
chini, kuhakikisha kwanza huyo mtoto anazaliwa salama. Na mama yake awe salama
ili aje amlee huyo mtoto.
Mwanzoni dokta Lyamu alijibu bila shida kwani Nanaa alikuwa mzima kabisa. Alimtoa hofu Geb. Na kumwambia alishamuona Nanaa akibeba mimba akiwa hana damu. Na akajifungua bila hata yeye kuwepo, na akajifungua salama tu. Hofu yao ilikuja pale mwishoni pressure ilipoanza kumsumbua Nanaa akiwa na miezi karibia kumaliza 8. Hapo hofu ndipo ilipomwingia huyo daktari na ahadi aliyokuwa amempa Geb, ambaye walishaanza kuzoeana kwa kukutana mara kwa mara hapo hospitalini wakati Nanaa alipowekwa mapumzikoni. Kila ushauri aliotaka Nanaa afuate, alimtumia Geb kuweka msisitizo kwa Nanaa, kwa sababu Nanaa alikuwa mbishi sana. Kwenye hatari, yeye ndiye aliyekuwa amkimsisitiza dokta Lyamu akimwambia asiogope.
Mwenye Hatima Ya Kila Kitu Ni Mungu.
Hapo nje ya chumba alicho lazwa Nanaa kila mtu
alikuwa ameshikilia roho yake kwa hofu, wakati ndani kukisikika kuna heka heka zakutia hofu zaidi. Geb
alikuwa ndani na Nanaa, kitu alichofurahia kama alivyokuwa amepanga kwamba huyo
mtoto azaliwe yeye akiwepo. Baada kama ya dakika 8 hivi, kilio cha mtoto
kikasikika kutoka ndani ya kicho chumba. Mama G akawa kama amechanganyikiwa. Akaanza
kupiga kelele. Grace alijikuta machozi yakimtoka. Oliva alimka kwa kelele za
bibi yake. “Amka mama. Umepata mdogo wako.” Mama G alimtoa kutoka kwenye kiti
chake. James alikuwa akipumua kwa hofu. Hakufurahia kama wengine, alibaki kimya
tu.
Baada
ya muda alitoka nesi. James akamkimbilia kwa haraka. “Vipi Nanaa?” James
akauliza akionyesha wasiwasi. “Anaendelea vizuri. Usiwe na wasiwasi. Mtoto
mwenyewe naona ametoka bila shida. Hajahangaika sana kuzaa. Ila madaktari ndio
wanahangaika kushusha pressure yake na kushonwa. Alichanika sana. Mtoto alikuwa
mkubwa sana. Ila na yeye mzima, amepakatwa na mama yake huku akihudumiwa.”
James akapumua kwa nguvu.
“Anafananaje?
Namaanisha huyo mtoto.” Grace akamsogelea na yeye huyo nesi, akauliza. “Ana macho
kama hayo yako. Dume la nguvu. Mrefu kama baba yake.” Wote wakacheka. Mama G
akaendelea kuruka ruka. “Jamani Magesa amezaliwa!” Akaendelea kupiga vigelegele
huku amembeba Oliva. “Mama tulia bwana! Unapiga sana kelele!” Grace alijaribu
kumtuliza bila mafanikio.
Geb
akatoka akiwa amembeba mtoto. “Nanaa amesema nikuletee kidogo umuone ndio
akashugulikiwe.” Haraka haraka akamkabidhi Oliva kwa James. “James mwanangu, nishikie
mara moja.” “Hapo shuguli imempata mama!” Grace aliongeza na kumpisha mama
yake. Geb akamsogezea mama yake mtoto, akamkabidhi. “Magesa mzungu amezaliwa
jamani!” Mama G aliendelea kupiga kelele. “Basi mpaka Nanaa amekusikia mama,
kwa kelele!” Grace aliongea huku akimsogelea na yeye ili kumuona Magesa. Mama G
akampokea na kumyanyua juu. “Umebarikiwa
Magesa. Wewe ni shujaa. Utaishi maisha marefuuuu, usimulie makuu ya Mungu.” Machozi yalikuwa yakimtoka Grace na Geb. “Baba angekuwepo, angefurahi sana kumuona
Magesa.” Grace aliongeza huku akifuta
machozi ya furaha.
“Hongera
Geb!” Grace alimpongeza kaka yake. “Asante. Nimefurahi sana. Siamini! Nahisi
kama sikuwa nimejiandaa vizuri! Nilijua siku bado!” Geb aliongea akimtazama
mtoto wake. “Sikutegemea kama angekuja anikute bado sijaoa!” Aliongea kwa
kulalamika kidogo. Akamsogelea tena mwanae. “Hebu tumuone, mama.” Mama G
akamuweka vizuri, wote wakamsogelea. Wakawa wamemzunguka mama yao,
wanamwangalia Magesa kwa karibu na makini. “Amefanana sana na mimi, kasoro
rangi tu.” Wote wakacheka.
“Nanaa
anadamu kali sana ya rangi. Lakini huyu ni Geb mtupu. Anaendeleaje?”
“Wanamsafisha na kujaribu kushusha pressure. Ila wanataka alale kabisa.
Wanaamini akija kuamka tena, atakuwa sawa tu. Amejitahidi sana mpenzi
wangu. Hata daktari amemsifu. Angechelewa kidogo tu, Magesa angekosa hewa.
Kumbe alishaanza kutoka bwana!” “Maskini mwanangu Nanaa! Sasa hapo ni kukazana
na vyakula. Anakuwa na kazi ya kunyonyesha watoto wawili! Na dume hili, sio
mchezo.” Mama G aliongeza huku akimuweka vizuri Magesa.
“Ngoja
nirudi ndani kwa Nanaa.” Geb aliaga huku akimchukua mtoto wake. “Mwambie Nanaa
asante kuniletea mtoto. Nimefurahi sana. Mpe pole. Mwambie namsubiria kwa hamu
nimpe pongezi zake, mwanamke wa shoka!” Mama G aliongeza, wakacheka.
Geb
akarudi ndani na mtoto. Wakati akishonwa ndipo Nanaa alipomwambia atoke na
mtoto nje. Ampelekee mama G aliyekuwa akimsikia akipiga kelele. Geb alirudi akakuta nesi aliyekuwa akimuhudumia
Nanaa ameshamaliza kila kitu. “Nimekurudishia mkeo kama binti mdogo!” Geb na
Nanaa wakacheka. “Nakushukuru sana. Asanteni kunisaidia.” Nanaa akashukuru tena.
“Karibu. Pole na hongera. Pumzika ili ujisikie vizuri. Kazi ndio imeanza.
Mapumziko ya mwisho hayo! Si unamuona mwanao ameshaanza kunyonya kidole?” Nanaa
akacheka. “Nipe nimuone tena, Magesa wangu.”
Nanaa akajiweka vizuri. “Mama kafurahi huyo!” “Nimemsikia akipiga
kelele.” “Ameshindwa hata kukaa.” Nanaa akacheka huku akimpokea mwanae.
“Magesa
ni mzuri sana. Mkubwa! Ndio maana ulikuwa ukiniumiza mwanangu! Urefu huu
unaupeleka wapi?” Nanaa alimgusa mwanae kwa upendo. Akambusu. “Nimefurahi sana kukuona.” Nanaa akaanza kulia nakushangaza hata madaktari
waliokuwa wakijadiliana juu ya pressure yake. Muda wote wa kuzaa alikuwa jasiri
akikazana kusukuma kwa makini kama alivyokuwa akielekezwa na daktari wake ili
asiipandishe pressure zaidi na asimdhuru mtoto ambaye alishatanguliza kichwa.
Alitoka na nywele nyingi sana kama za baba yake.
“Usilie
bwana Nanaa! Unatakiwa ufurahi.” Geb alijaribu kumbembeleza. Nanaa alikumbuka
siku alipojifungua Oliva, akiwa peke yake hospitalini. Hofu ya itakuaje
ikimuandama. “Namuomba Liv.” Nanaa akamgeukia Geb. “Naruhusiwa kuwaita watu
ndani?” Geb alimuuliza dokta Lyamu. “Hali yake bado haijatengemaa. Anatakiwa
alale kabisa.” “Kwa muda mfupi tu
tafadhali. Namtaka mtoto wangu.” Lyamu
akatabasamu huku akimwangalia Nanaa. “Unanichanganya wewe! Yaani muda
unaotakiwa uwe unalia, huwa unacheka. Muda wa kucheka ndio unalia!” Nanaa
akacheka huku akifuta machozi.
Akainama
kumwangalia mtoto wake. Akamuweka kwenye ziwa ili anyonye. Magesa akaanza
kuvuta ziwa kama aliyezaliwa na ujuzi wa kunyonya. “Asante kwa kunisaidia na
kunivumilia.” Nanaa akamshukuru Lyamu, daktari wake. “Kumbe unajijua ulivyo
mkorofi?” Nanaa akacheka. “Asanteni wote jamani. Isingekuwa nyinyi wote kuwa
hapa na mimi, wala nisingeweza. Nawashukuru sana, tena sana.” Nanaa akashukuru
wauguzi wote pale ndani. “Karibu. Pole na hongera.” Wakaitikia huku wakiendelea
kukusanya vifaa vilivyokuwa vikiingizwa mle ndani wakati wa kujifungua Nanaa,
ili kuacha chumba hicho kisafi na nafasi ya wageni wake.
“Kabla hamjatoka, naombeni mnipe muda mfupi sana nimshukuru Mungu pamoja na nyinyi.” Geb akawasimamisha wote. “Sitachukua muda mrefu. Wewe Nanaa andelea tu kunyonyesha.” “Ni kweli Geb. Mungu anastahili kupewa sifa kwa huu muujiza.” Nanaa akaunga mkono. Hapo hapo Geb akaanza kuomba tena akiwa amepiga magoti. Akashangaa anashukuru na machozi yanamtoka. Akamshukuru sana Mungu kwa ule muujiza pale. Akamtambua kuwa bila mkono wake, Nanaa asingeweza. Akawaombea baraka wale wauguzi wote waliomsaidia Nanaa na Magesa. Baada ya muda mfupi sana akawa amemaliza. Akawapa mkono kila mmoja. Kwa kurudia kuwashukuru. Kwani aliwaona jinsi walivyokuwa wakihangaika.
Utabiri Juu Ya Magesa.
Mama G alikuwa na furaha isiyo kifani. “Magesa aliniambia habari za huyu mtoto. Ndio maana nilikuwa nina hamu sana yakujua kama Nanaa amebeba mimba yake au bado niendelee kusubiri.” “Ndio maana ulitaka kumrubuni Nanaa mkaangalie jinsia halafu umlipe milioni?” Grace akauliza. “Kabisa. Maana nilikuwa namsubiria kwa hamu huku nikimuomba Mungu nisife kabla sijamuona. Maana Magesa alisema alishamuombea sana. Nikamuuliza kwa nini asimkazanie Geb ambaye ndio mtoto pekee wa kiume na tumeshamuona? Akasema Mungu alimuonyesha huyu mtoto. Akampa kabisa na jina lake yeye mwenyewe. Akasema nihakikishe Geb anakuwa katika njia nzuri, ili aweze kumlea huyu Magesa.” Mama G akaendelea kueleza huku wamerudi kukaa kwenye viti, wakisubiri waingie kumuona Nanaa.
Kila
mtu alikuwa akimsikiliza mpaka mke wa Malii. “Sasa siku ile usiku tulipomleta
Nanaa hapa hospitalini. Geb akatukuta hapa na kuanza kumuombea. Akamtaja ni
Magesa..” “Ndio maana ukashituka sana mama!” “Kumbe unakumbuka Grace?
Nikamwambia Mungu asante kwa kuweza hata kuona ujauzito wake. Sasa kuja kusikia
Nanaa anasumbuliwa na pressure itahatarisha maisha yake na mtoto, ndipo maombi
ya kufunga na kuomba yalipoanza. Kuharibu kazi ya ibilisi. Maana kila
tulipokuwa tukimpeleka Nanaa kliniki, tulikuwa tukiambiwa ni mzimaa. Iweje karibu na mwisho uzuke ugonjwa mkubwa
hivyo wakati hata mama mtu hakuwahi kuwa nao!? Sasa leo kumsikia Magesa analia
hapo ndani, hakika nimemtukuza Mungu wangu.”
Mama G akafuta machozi.
“Hongereni
sana.” Mke wa Malii aliwapongeza kinyonge. “Asante Manka.” Grace alijibu. “Ndio
maana Nanaa alikuwa akipata sana maumivu. Mtoto mkubwa sana. Hapo hata
hajatimiza siku zake lakini yuko hivyo!” Grace aliongeza. “Nakwambia huyo ni
Magesa mtupu.” Mama G akasifia. “Ni mzuri kama dada yake! Nywele na macho
utafikiri ni mapacha! Nanaa amebahatika sana.” Manka mke wa Malii akaongeza.
James alikuwa na Oliva amempakata. Wote wakamgeukia. “Hongera James mwanangu.
Umekuza. Naona nazidi kuletewa wajukuu! Zote hizo ni juhudi zako baba. Hongera
na asante.” James akacheka. Wazi alionekana amefurahi na yeye. Akamwangalia
Oliva aliyekuwa ametulia tu akionyesha bado ana usingizi.
Madtari
walitoka na manesi nao pia wakatoka wakiwa wanasukuma kigari kilichojaa vifaa
vingi walivyovitumia wakati wa kujifungua Nanaa. “Asanteni sana jamani. Mungu
wangu awabariki.” Mama G akasimama kwa haraka akawakimbilia wale madaktari na
manesi. “Asanteni sana, tena sana. Naombeni mrudi jioni, ili tule na kunywa
tumshukuru Mungu pamoja.” Mama G akaongeza.
“Mimi
sitakuwepo mama. Natakiwa kwenye hospitali nyingine. Naomba mfurahie kwa niaba
yangu.” Lyamu akajibu kwa upande wake. “Basi naomba mwanangu Danny akusindikize.”
Danny alijua mkwewe anachomaanisha. “Nyinyi wengine naomba mpitie chakula chenu
hapo kwenye ofisi ya manesi. Grace atahakikisha wote mnapata chakula na
vinywaji. Mmefanya kazi kubwa sana ambayo lazima Mungu aliwahitaji kuwatumia
ili kukamilisha ujio wa mjukuu wangu. Hatuna jinsi nyingine ya kuwashukuru ila
kusema asante.” Grace naye akasogea na kuongeza. “Asanteni sana.” Wote waliwapa
mkono wa kushukuru.
“Ila
Nanaa anahitaji muda wa kupumzika. Bado pressure ipo juu.” Lyamu akaongeza kabla
yakuondoka. “Na sisi hatutakaa sana. Tunamuona tu na kutoka, mpaka usiku ndipo
tutarudi. Asante baba.” Mama G aliendelea kushukuru.
“Nanaa
anamtaka Liv.” Geb akatoka. Ndipo wote wakaelekea chumbani. James ndiye alikuwa
amembeba Oliva. Oliva alipomuona tu baba yake akanyanyua mikono. “Dadii!” “Njoo
mwanangu, nikutambulishe kwa kaka yako.” Geb akampokea. Mama G alishaingia
ndani akaenda moja kwa moja kitandani kwa Nanaa. Nanaa akaanza kulia. “Nimechanika sana mama!” Nanaa alinong’ona kwenye sikio la mama G. “Utapona
Nanaa mwanangu. Pole mama. Umefanya kazi ngumu tena ukiwa mgonjwa.” “Basi pole hiyo ingeenda na bakuli la uji.” Kila mtu akacheka. “Na mzazi tumempata!” Mama G
akaongeza.
“Mchukueni
huyo mtoto, nimkumbatie Nanaa wangu.” James akampokea Magesa, mama G
akamkumbatia Nanaa. “Hongera sana Nanaa. Hongera mama.” “Asante mama yangu.
Nimefurahi sana.” Grace naye akamsogelea na kumkumbatia. “Pole wifi yangu.”
Nanaa akacheka. “Nimefurahi umeniita wifi.” Wote wakacheka. “Kwa kuwa anaandaa
harusi mwenyewe ndio maana na uwifi umenoga.” Mama G akaongeza.
“Jamani
pole na maandalizi! Basi mimi nilijua hamna tena harusi. Geb aliacha
kuzungumzia kabisa.” “Surprise!” Geb akaongeza. “Na ni surprise kweli. Mbona
utapenda?” Nanaa akacheka. “Mniombee uzima.” “Utapona mama. Utapona tu na
utalea wanao.” Mama G akamfariji.
Manka
mke wa Malii akamsogelea na yeye. “Hongera sana Nanaa. Hakika Mungu
amekubariki.” Nanaa akajikuta machozi yanamtoka. Furaha ya ajabu ilimjaa
moyoni. Hakuwa anaamini kama ni yeye Nanaa. Gafla akaona vile Mungu alivyoweza
kuongeza uthamani wake. Bado hakuwa akiamini yanayomtokea. “Asante Manka. Na wewe umebarikiwa.” Akacheka kwa kuguna kama asiyesadiki. “Usigune
Manka mwanangu. Sema amina. Umebarikiwa.” “Mmmh mama! Tuyaache tu kwa kuwa sasa
hivi tunafuraha ya mtoto. Acha tufarijike kwa hili. Bado Mungu anajidhihirisha
yupo na wala hajaacha kutenda miujiza. Ni dakika chache tu hapa tulikuwa
tunazungumzia hatari ya kifo iliyokuwa inatukabili. Lakini ona furaha
aliyotushushia Mungu! Ni kwa neema na upendeleo mkubwa alionao kwa Nanaa.”
Mwisho wa hayo maneno ya Manka, ukafanya kutulie kidogo, wasijue wajibu nini
tena.
“Amina!
Nashukuru Mungu. Geb namuomba Liv wangu.” Nanaa akavunja ukimya uliotaka kuzuka
mle ndani na kumgeukia Geb. Nanaa akampokea na kuanza kulia tena. “Kama ni
hivyo namchukua mtoto.” Geb alimsogelea Nanaa. “Mwaka jana, siku kama ya leo wakati najifungua Liv nilikuwa peke yangu
Geb. Nikiwa nimejawa hofu. Sijui itakuaje na nitamuweka wapi. Nilikuwa
nikimuhurumia kweli. Acha nikae naye kidogo nifurahie.” Nanaa alikua akiongea huku akimwangalia Oliva
ambaye na yeye alikuwa akimtizama na macho ya kusinzia.
“Jamani
watu wamesahau birthday ya dada mkubwa! Mama Mzazi!” Grace akashituka sana.
“Jamani Liv wangu! Pole mama, nimekusahau!” Bibi yake akaongeza. Geb alikuwa
kama ameduwaa kwa muda. “Nimewezaje kusahau hili!” “Wala usijilaumu Geb. Tangia
sisi tumeingia hapa ile saa moja mpaka sasa, ilikuwa ni heka heka tu. Akili
zako zilikuwa hazijatulia.” “Hapana Mama, sikutakiwa kusahau birthday ya Liv.
Namuomba.” Geb akamchukua.
“Happy
birthday Oliva Magesa.” Oliva akacheka huku akimtizama baba yake. Akambusu mara
kadhaa kisha akamuweka vizuri ili kumuombea. “Nakupenda
mwanangu na ninakuombea heri kwenye maisha yako yote. Uwezo wa kimungu ukawe
juu yako daima. Ukafanikiwe kwa kila utakachogusa. Kila utakapopita wakamwite
heri mwanamke aliyekuzaa wewe. Nakuombea ulinzi katika kila jaribu
atakalokutupia muovu. Mungu akakushindie. Wakati wote wewe ndio ukasimame
mshindi. Nakuombea afya njema na baraka zote za mbinguni na duniani zikawe juu
yako. Hatua zako ziongozwe na Bwana. Amen!” “Amen!” Kila mtu aliitika na kuanza kumpongeza Oliva.
“Jioni
tukileta vyakula, nitaleta na keki yake aje akate hapa hapa mbele ya mama
yake.” Grace akatoa wazo liliondelea kumgusa Nanaa. Bado machozi yalikuwa
yakimtoka Nanaa. “Pole Nanaa mwanangu. Mungu anakufuta machozi sasa hivi.” “Kweli mama. Kaka! Umemuona Magesa?” James akacheka. “Mwenzio alikuwa na wasiwasi na
wewe huyo! Ndio anacheka sasa hivi.” “Jamani kaka yangu! Pole.”
James akamwangalia Nanaa. “Pole wewe.” “Asante kaka. Pole na wewe kwa wasiwasi.” Nanaa akajibu na kufuta machozi. James akarudisha
macho kwa Magesa aliyekuwa amemshika. “Mtoto mzuri sana, Nanaa. Hongera.” James
alirudia huku akimtizama yule mtoto. “Asante kaka.” Oliva akataka arudishwe kwa
mama yake. Nanaa akampokea na kumbusu mara kadhaa. “Happy birthday Liv!” Oliva
akacheka na kuhamia kwenye ziwa la mama yake.
Oliva
akataka nyonyo. “Mchukue bwana asinyonye ili amwachie mwenzie kwa hizi siku
mbili. Akianza kunyonya huyu ni mpaka ahakikishe amemaliza.” Geb akataka
kumchukua Oliva akaanza kulia. “Jamani Liv! Nenda bwana. Maziwa ya mtoto. Nenda
bibi akupe uji.” Akajificha uso kwa mama yake. “Basi tabia hizo za baba yake.
Akitaka jambo lake mpaka apate. Jasho litakutoka.” Wote wakacheka. Mama G
akamsogelea. “Bibi! Bibi!” Oliva akamwangalia bibi yake, akacheka na kurudisha
uso kwa mama yake akajificha. “Basi akikuchekea hivyo, utafikiri amekukubalia.
Kumbe ndio anakwambia hadanganyiki.” Mama G aliongeza.
Manka, Mkewe Malii, Atoa Siri Nzito.
Manka
akasimama. “Jamani, naombeni mimi nitangulie kabla jua halijawa kali sana.” “Si umpigie simu Malii!? Jua limeshakuwa kali
Manka. Huwezi kutembea sasa hivi wakati gari ipo!” Grace alimuwahi. “Gari ile
ni ya Malii, wifi yangu. Mimi nimeambiwa nilikwenda pale na daladala, nisijitie
ufahari wa ukubwani. Acha tu niende.” Manka alifanya kila mtu ashangae. “Subiri
kwanza Manka. Huyo aliyekwambia hivyo ni Malii mwenyewe au nani!?” Gafla Mama G
akawa hajaelewa.
“Mwanao Malii huyo.” “Haiwezekani!” “Mmmh!
Acha tu mama. Mimi mwenyewe ningeambiwa kabla, nisingeamini. Hivi ni bibilia
ndio ilionya mwanadamu asiolewe na mnyama au ni mimi tu mwenyewe nimepata huo
msemo?” Manka akaanza. “Usiseme hivyo Manka mwanangu.” “Nakwambia nimejiingiza
kwenye ndoa na mnyama mama. Mwanadamu wa kawaidia hawezi kuwa kama Malii.” Kama
aliyekuwa amepewa ruhusa. Akarudi kukaa.
Ni
kama aliyekuwa amekabwa na kitu kooni. Akaanza kuongea bila kificho kina Danny,
James, Geb, Grace na mama G, wakisikiliza. “Mimi huwa najiuliza labda yule
mwanaume nilibadilishiwa siku ya harusi! Si wakawaida hata kidogo! Hivi
ushawahi ona mwanaume mshenzi hapa duniani?” Manka akauliza. “Manka!” “Basi ni
kwa vile yupo mmoja tu hapa duniani, na ninaishi naye mimi. Malii.” Manka
akajiweka sawa. Mama G akamkabidhi Nanaa bakuli la uji. “Kunywa wakati huyo
anasinzia.” Nanaa akapokea.
“Kwanza
mimi nilikuwa najua naolewa na mwanaume mcha Mungu. Kumbe naolewa na mnyama
ambaye hana Mungu ndani yake na wala hajui kama yupo Mungu aliye muumba!
Akianza kunitukana, utafikiri mie mke mwenzie.” “Kwa nini!?” Mama G akauliza
kwa mshangao. “Weusi! Nakwambia mwanaume anachukia rangi yangu hii, utafikiri
hakuniona kabla hajanioa au utafikiri nilikuwa na Mungu wakati ananiumba,
nikafanya kosa la kuchagua niumbwe mweusi.” Grace na Danny wakatizamana. Grace
na mama yake pia walikuwa weusi.
“Malii
jamani! Amepatwa na nini?” Mama G akauliza. “Ni mshenzi tu yule mama. Samahani
kusema hivyo. Lakini hujawahi ona mtu kama Malii. Ila nashukuru Mungu,
nishakuwa na wanaume wanosifia rangi yangu, kwa hiyo nimejua tatizo wala sio
rangi, anapepo chafu sana. Na asiposaidiwa mapema, hakika atakufa kifo kibaya.
Sio kawaida.” Manka akaongeza. “Kwa nini?” “Sema kuna watoto mama. Na mimi
nataka kuondoka. Lakini ujue wazi, pale nimenawa mikono, naondoka hivi
karibuni.” Manka akasisitiza.
Akataka
kusimama, akawa kama amekumbuka kitu. “Ujue mie mwanzoni nilikuwa simfahamu
huyu Nanaa. Mara ya kwanza kumsikia ni kwa Malii mwenyewe tukiwa tunafanya
mapenzi.” Nanaa akashituka sana. Akapaliwa na kuanza kukohoa mfululizo.
“Samahanini jamani. Lakini acheni tu niongee. Amenichosha nafsi na roho.” Geb
akampa Nanaa maji ya kunywa. Kila mtu akabaki ametoa macho. Grace akawaangalia
wanae. Wote walikuwa wamelala. Fili alikuwa amepakatwa na baba yake tokea
zamani.
Hata
mama G akashindwa kuhoji. Akabaki kimya. “Basi mwanaume yule akamtaja Nanaa.
Nikamuuliza Nanaa ni nani? Akakataa katakata kuwa yeye hajasema Nanaa.
Akaniambia alikuwa anagugumia nananaa! Wakati mimi nilisikia kabisa ni
kama jina Nanaa. Nikanyamaza kwa kuwa sikuwa namjua. Nikajiambia labda ni
mwanamke wake wa zamani. Hapo hata hatujaoana. Sikutaka ugomvi, siku ile
ikapita. Lakini ukweli nikaumia sana. Nikajiambia huyu mwanaume anafanya
mapenzi na mimi huku akimuona mwanamke mwingine! Basi nikatulia.” Manka
akaendelea.
“Kwani
iliishia hapo. Ukaanza mchezo wa kusifiwa wanawake weupe, wanalinganishwa na
weusi. Kama utani vile. Mimi nikawa nacheka. Najua utani! Huwezi amini mama,
usiku ule wa honeymoon, alikuwa anatajwa Nanaa tu. Mpaka kesho yake ikabidi
nimkalishe chini nimwambie aniambie ukweli. Akaanza kuniambia atakuwa ameropoka
tu. Nikamkazania na kumwambia si kwa kurudia mara zote hizo tena usiku wetu wa
kwanza wa ndoa! Nikamwambia anitajie Nanaa ni nani na kama ni mwanamke wake
ambaye yupo naye kwenye mahusiano. Basi ndio safari yangu ngumu ya ndoa ikaanza
hapo. Nilitamani kuondoka pale hotelini mama yangu, lakini aibu. Narudije
nyumbani nilikoacha wazazi wangu na mimi ndio nimeolewa hata masaa 24
hayajapita!” Manka hakunyamaza.
Akasahau
kama ndio yeye aliyesema siku hiyo wafurahie tu baraka kutoka kwa Mungu. Manka
akaendelea. “Tukarudi nyumbani, nikaanza kulinganishwa sasa na Nanaa. Chuki
ikanijia juu ya huyo Nanaa. Shauku ya kutaka kumjua Nanaa, anayetajwa mpaka
kwenye kitanda changu cha ndoa, ikaibuka. Nikaanza kuuliza taratibu. Nikaanza na
Goz. Maana Goz kidogo ndio akawa amebaki na sisi baada ya kundi letu
kusambaratika na uzuri Gozi ni mtu wakuhamisha maneno. Nikajua hataninyima
majibu yangu kama na yeye anamfahamu huyo Nanaa. Nikamuuliza unamfahamu Nanaa?
Gozi akacheka sana. Akasema , ‘siku hizi
Nanaa ndio habari ya mjini!’ kama mnavyomjua Gozi. Utani haumwishi, maneno
mengi. Akaendelea. Akasema, ‘sasa hivi
Nanaa anawaendesha akili wahandisi wa mjini, hapashikiki. Kampiga chini Miss
Africa, jasho linamtoka!’. Akimaanisha Liz. Mimi si sipo kwenye hilo kundi
lenu la Whatsapp!” Manka akaendelea.
“Acha
Gozi anipe mikasa ya mjini. Kinachoendelea. Na yeye akaanza kusifia. ‘Nanaa anawaka kama jua, kiuno ng’e!
Wanaume walio liana amini, na kuapiana urafiki kama undugu, wanashikana mashati
sasa hivi!’. Aliposema tu Nanaa ni mweupe, nikajua tayari. Ndicho
alichomkamatia Malii. Nikamuuliza kwani huyo Nanaa anaishi wapi, au wazazi wake
wako wapi? Nyinyi mmemfahamuje? Na iweje marafiki wote wamgombanie mwanamke
mmoja? Sasa hivi yuko na nani? Si ndio akasema mwenye kisu kikali ndio
anayekula nyama! Kafichwa na milionea wa mjini. Nikamuuliza nani? Na yeye
akaniuliza kwani mamilionea vijana hapa mjini ambao hawajaoa, mimi ninao wajua
ni wangapi? Hapo tena macho yakanitoka. Kama anavyojisemeaga Malii. Mwanamke
mimi wa migombani. Mamilionea wa jijini nawajulia wapi? Nikabaki nawaza.” Manka
alikuwa amekaa kwenye kochi hapo hapo chumbani mbele ya Nanaa.
Anaongea
huku akimtizama mama G. Watu wote wakimsikiliza. Nanaa akaendelea kunywa uji
taratibu. James kimya. “Basi. Sasa hapo mimi hata sikujua kama Geb ndiye
milionea! Lakini jina hilo halikuwa geni. Nilikuwa nimeshalisikia hilo jina
mara nyingi tu. Wakitaka kukopana pesa, wanaambiana mpigie simu Milionea. Basi,
ndio Goz akasema ni Geb. Nikashikwa kama na bumbuazi. Akaniuliza vipi? Nikawa
kama nimemsahau tena Geb! Maana Geb ninayemfahamu mimi ukikutana naye
anakusalimia kwa kukupa mkono. Halafu akiwa katikati ya watu, hazungumzi kabisa.
Katulia wakati wote wala sikuwahi kumjua kama ni yeye milionea. Ndio Gozi
akaniambia ndiye huyo huyo alisimamia harusi yetu na Miss Africa sijui mwenyewe
anamwita Face of Africa. Kuna jina lao wenyewe wamempa Liz.” Manka akaendelea.
“Ndio
nikaambiwa na habari za Liz zote. Mtoto asiyejua shida. Hataki maskini,
ananyata kama malaika. Sasa nikaambiwa, ndio kwa mara ya kwanza akapata kiboko
yake, ambaye ni Nanaa. Hamu ya kumfahamu huyo Nanaa ikaongezeka. Nikauliza
kwani huyo Nanaa na yeye yupo kama Liz? Ndio nikapewa tena habari za James.
Kuwa James ndio mama, baba, dada na kaka ya Nanaa. Wanaume hao ambao wote
waliapishana katika shida na raha, wamesambaratishwa na Nanaa, waliyemsikia
kutoka kwa James tokea anamiaka sijui 4, sijui hata sikumbuki vizuri maana na
yeye Gozi alikuwa na mengi ya kuongea na mimi nilitaka kusikiliza. Wote nasikia
walikuwa shule ya bweni huko jijini Arusha, Iliboru.” Manka akaendelea kama
asiyetaka kukatishwa.
“Gozi
akasema mate yaliwatoka paleee, James alipowatambulisha huyo Nanaa. Unaambiwa
mpaka wanaoweza kutumia tunguri walitumia. Kila mtu akadai Nanaa wake. Gozi
akasema kuna ambao hawakutaka kuingia kwenye ugomvi mkubwa, lakini nasikia pia
walimfuata huyo kaka mtu, sijui mzazi mtu wa Nanaa, yaani James. Kulalamika
nakuomba James awaunganishie kwa Nanaa. Akasema sasa hivi watu hawazungumzi
hapa mjini sababu ya Nanaa. Nikamuuliza vipi na yeye? Akasema yeye mnyonge.
Hata akisema, hamna atakayemsikia. Nikamwambia niambie mimi. Akasema yeye ni
machozi ya samaki. Haitasaidia. Gozi akamalizia kwa kusema, ‘Nanaa maji marefu mama!’ Akaondoka
kama mnavyomfahamu Gozi.” Nanaa alikuwa ameinama kimya.
“Basi
tena pale ikabidi na mimi niwe mpole. Niunge msafara wa Gozi. Nikajinyamazia
kimyaa. Lakini mama! Mmmh! Usiombe. Malii mnyanyasaji! Akianza kutukana viungo
vyako vya mwili, utajuta kuzaliwa mwanamke. Halafu taratibu mwenyewe hana
haraka. Hapo karudi nyumbani, kalewa. Basi atakuchambua wewe, mpaka utashindwa
kulala. Halafu anamalizia kukwambia hataki kukugusa amechoka. Heri tu alale. Mara
ya kwanza nilitamani ninywe sumu nife.” “Usifanye hivyo Manka mwanangu.” “Sasa
hivi siwezi kufanya hivyo tena mama yangu. Nimeshamuelewa. Hanisumbui tena.”
Manka akaongea.
“Afadhali.
Maana unaweza kujikuta unachuki na watu bure.” “Wala nisiseme uongo mama.
Nilimchukia Nanaa kupita kiasi. Sasa nikawa sijui kama alishakuwa na mahusiano
naye au la. Nilionyeshwa picha yake. Nikakumbuka ndiye msichana wa mwisho
kukutana naye siku ya harusi yetu wakati tunaingia ukumbini. Tulimkuta
amesimama pale nje. Bwana msichana alikuwa amependeza huyu! Mpaka Malii
alishindwa kujizuia. Mbele yangu alimsifia kama amependeza sana. Basi ile picha
ndio ikawa inanitesa. Nikajua ni mwanamke wake Malii. Alikuwa anamsubiria pale
nje ili waonane na mpenzi wake.” “Hapana Manka mwanangu. Usiingie dhambini.
Sisi ndio tulimsahau Nanaa pale nje. Pale alikuwa amezuiliwa kuingia ukumbini.”
Mama G akamueleza kwa kifupi.
“Kumbe!
Basi mimi na hilo nikalibeba. Nikawa najiambia kama sio Nanaa kumuonjesha penzi
Malii, wala tusingekuwa hapa. Sasa akanipa kubwa kuliko! Acha Malii anivue nguo
mbele ya watu mama!” “Nini tena?” Mama G akauliza. “Bwana mwanaume yule
nimemvulia kofia. Asiende kuanzisha mahusiano na yule msichana aliyenisimamia
harusi! Sio kulala naye mara moja, mahusiano haswa. Na yule dada alikuwa rafiki
wa tokea watoto. Tulizaliwa kijiji kimoja pale Marangu. Yaani wazazi wake ni
kama wazazi wangu. Tumelelewa pamoja. Ila mwenzangu akapewa rangi nyeupe. Yule
dada ndio akageuka kuwa mke wa Malii. Mama! Walinitoa jasho.” Manka akacheka na
kupiga makofi.
“Yule
Mary si mnafanya naye kazi ofisi moja!?” “Sawa sawa wifi yangu. Basi
walinichezesha ngoma nilizokuwa sijui kuzicheza. Nakwambia mapenzi ya wazi
wazi. Malii anamfuata kazini kwenda kula mchana.” “Si ameolewa? Yule
aliyemsimamia Malii si ni mumewe yule?” “Bwana kumbe wifi Grace unakumbukumbu!
Sasa yule bwana wake hana kitu. Hali yake kama yangu. Alijisemea Malii. Kwetu
tunalalia machalali na kuamkia mtori tu. Hamna chakula kwetu. Basi yule kaka
uwezo wake mdogo. Lakini walikuwa wanasikilizana sana na Mary mpaka nikawa
nawaonea wivu. Nikienda kwao nilikuwa nawaambia waniombee na mimi nipate ndoa
kama yao. Haaa! Malii si akaingilia kati. Nikamwambia nimempongeza. Maana Mary
na uzuri ule aliwaliza wanaume, lakini mapenzi ya dhati ndio yakamfanya aolewe
na Chalii. Tena nakumbuka Malii akanijibu kwa kiburi kuwa yeye ni mwanaume wa
shoka, hatongozi na kukataliwa. Nikamtupia swali la haraka ili kujiridhisha,
nikamwambia mbona Nanaa anamtoa jasho? Akajibu na ndipo nilipojua Nanaa
alimkataa. Akasema, ‘atafutaye hachoki,
akichoka kashapata’. Hapo ndipo nilipojua bado anahangaishwa akili na
Nanaa.” Manka akaendelea. Hakuna aliyemkatisha.
“Sasa
Malii akaniambia Geb anaomba tukutane naye kwa chakula cha mchana hotelini.
Atakuwa na Nanaa. Akasisitiza nivae vizuri nisije mtia aibu. Nisivae nguo zangu
za migombani. Kwa kuwa Geb akikutoa kwenda kula mahali sio kwenye chips vumbi.
Ni hoteli za maana. Mimi nikacheka tu. Tulipofika hapo, ndipo nikamuona kwa
karibu dada huyo!” Manka akamnyoshea kidole Nanaa.
“Mjamzito
wa huyu mtoto wake mpya. Mwenyewe kapendeza. Kajaa dhababu mwili mzima. Alivaa
kigauni chake cheusi mwenyewe, mpaka magotini. Bwana Nanaa alipendeza mpaka
nikasema leo Geb atamkamata Malii. Bwana yule alikuwa akihangaika, basi bibi
huyu katulia kimya. Anawaka kama alivyosema Gozi. Akiongea tu, mashavu
yanabonyea! Mbona niliamini alichokisema Gozi! Lakini tena mimi mwenyewe pale
nikawa kama sijielewi. Hoteli kama ile sijawahi kufika. Soda kwenye glasi! Kwa nini
bwana!?” Kidogo watu wakacheka.
“Kumejaa
visu na vijiko vya kila namna. Meza imekuwa kama kabati la vyombo! Basi pale
mimi nikasema heri nikapumzikie chooni. Nikaaga, nikawaacha hapo mezani ili
nikirudi, angalau nikute wameshika vile vifaa pale mezani, nijue wanatumiaje.
Nikakaa huko weee, kurudi nikakuta kila mtu ana kisu na uma kasoro Nanaa
kashikilia paja lake anakula kwa mkono.” Kila mtu akacheka. “Kwa msosi huyu!
Hawezi kutumia kisu na uma! Vitamchelewesha.” Danny alimchokoza. Nanaa akacheka tu huku akimpapasa mwanae
aliyekuwa ameshalala na yeye alishamaliza uji wake, akawa amejilaza pembeni
yake. Geb alishampokea bakuli tupu alilokuwa amemalizia uji.
“Basi pale na mimi nikasema nimwige Nanaa.
Nilipaliwa, pale, Geb alipotuomba tumsimamie harusi. Hakika nilipaliwa mama.
Muulize Nanaa na Geb. Mpaka ilibidi niletewe maji ya kunywa. Bwana Malii
alikasirika nusura apasuke.” “Kwa nini sasa?” “Wakati tupo njiani tunarudi
nyumbani ndipo akaniambia nimemtia sana aibu.” “Jamanii!!” Grace na mama G
wakaongea kwa pamoja.
“Nilishamzoea
hanipi tena shida. Hapakuwahi kuwa na mapenzi pale. Hata sijui ni kwa nini hata
alinioa! Lakini ukweli nilishituka sana. Nikasema huyu kaka na akili yake yote
anataka kumkabidhi fisi bucha! Asichokiona na kutojua ukweli kutoka kwa Malii
rafiki yake ni nini mpaka kumfanya awe msimamizi wake!? Nikakumbuka majigambo
ya Malii akisema, ‘atafutaye hachoki, na lazima atampata tu Nanaa. Kwanza Nanaa
alishampenda yeye, lakini akazinguliwa na pesa ya Geb.’ Akasema walikuwa kwenye
mahusiano ya muda mrefu sana na Nanaa. Mpaka Nanaa alishamtamkia anampenda
sana. Lakini sijui Nanaa alihamia nyumbani kwa Geb sijui, ndio Geb akamzidi
mahesabu! Kuna kajistori alikizungumza, sikukielewa vizuri kwa kuwa alikuwa
amelewa sana siku akinisimulia. Alikuwa anachanganya maneno, lakini ni kitu
kama hicho. Na yeye alitoa malalamishi yake hapo juu ya Nanaa.” Manka akazua
ganzi mwilini mwa Nanaa.
“Sasa
nikajiambia Geb anafanya kosa la mwaka. Anamrudisha Nanaa kwa Malaya yule!
Lakini nikajirudi, nikamkumbuka shoga yangu Mary. Nilimuomba anisimamie harusi
yangu, akiwa rafiki wa karibu sana kwangu. Mwaminifu niliyekuwa nikimwamini na
chochote, lakini akaishia kuwa mke mwenzangu. Nikajiambia wanadamu
hawatabiriki. Nikasema nisubiri nione mwisho wake. Basi Malii akawa amefurahi
kweli. Akawa anatamba kuwa tunasimamia harusi, halafu tutalipwa.” “Hee! Kumbe
ilikuwa uwalipe?” Mama G akamgeukia Geb.
“Alisema
tarehe hiyo angetakiwa asafiri kikazi. Anabiashara yake sehemu. Akasema
asipoenda weekend hiyo atapoteza hiyo pesa. Ndio nikamuuliza ni kiasi gani
aka..” “Muongo. Tena tapeli mkubwa mwenzio yule. Alikuwa anakupangia pesa kubwa
ili umpe amalizie mambo yake. Pale alipo hana cha biashara wala nini! Bado
tunaishi kwenye nyumba ya kaka yake yule
aliyehama hapa nchini na familia yake. Basi ile nyumba yake, ndio sisi tunaishi
hapo mpaka leo. Tunaishi bureee. Pesa yake yote, starehe. Tena kuna wakati mama
yake alikuja kutusalimia hapa mjini. Akakutana na hali hiyo ya mwanae. Yule
mama alienda sokoni Kariakoo kununua vyakula kwa uchungu. Akiondoka asubuhi
Malii hajali hata huku nyuma mama yake anakula nini.” Manka alimkatisha Geb akaendelea
yeye.
“Mimi
nilishamzoea. Haachi pesa pale ndani. Na akirudi anakuwa ameshiba na kalewa. Ni
matusi tu kwenda mbele mpaka mnalala. Sasa mama yake akawa anaumia kuona vile.
Mimi kimya. Nanunua ninachoweza, nampikia namwachia hapo, naenda kazini. Na kwa
kuwa nilishamjua ni mshenzi, nikaanza kupanga mipango yangu mingineee!
Ikikamilika tu, atanisikia mitandaoni. Sitaki ujinga.” Manka akajisifia.
“Kwa
hiyo mama wala usinione nimekaukwa mdomo bure. Sina cha mimba wala nini. Yule
bwana hanigusi, kwanza hata nishasahau mara ya mwisho ni lini. Ila,
Mungu atamlipa Malii. Atamlipa
vibaya sana.” “Mama yake alijaribu kuzungumza naye?” Mama G akahoji.
“Kwani
unafikiri mama yake aliishia hapo? Alirudi kwao, akarudi tena pale na baba yake
Malii. Na yeye akajionea. Malii alijitahidi siku mbili tatu, akashindwa.
Akarudia wehu wake vilevile mbele ya wazazi wake. Yule Mzee alikuwa anaongea
kichaga kitupu, Kiswahili kilimpotea. Mpaka ungemuhurumia. Walimuonya sana.
Yule baba alimwambia asipobadilika, atakufa bado mdogo. Ni mchafu yule, mama!
Hujawahi kusikia. Hakuna mwanamke mweupe anayempita. Mpaka unamuhurumia.
Analala kwenye kochi kwa kuchoka kwa pombe na wanawake. Kwa hiyo Geb! Ni Mungu
ndio alikusaidia kututoa kwenye harusi yenu. Ulikuwa unatumbukia shimoni. Toa
sadaka kanisani. Analala akimuota Nanaa yule. Wala sio siri. Hakuna siku
asimtaje Nanaa. Hata Gozi anajua hilo ila anasema hatakwambia. Hataki kuonekana
mchonganishi. Na ameapa atampata Nanaa tu. Sasa Nanaa jiandae.” Manka
akataka kusimama.
“Aendelee kuota hivyo hivyo. Hatawahi kunipata
hata iweje.” “Kwani wewe Nanaa ulikuwa ukimfahamu Malii kabla ya Geb!” Grace
akauliza, Nanaa akanyamaza kidogo. James akamgeukia vizuri.
“Nanaa?”
James akamuuliza kwa ukali kidogo. “Abee.” Akamwitikia kaka yake, James akabaki
akimtizama. “Ndiyo na hapana.” Nanaa akajibu akiwa anaangalia chini. “Ndio
nini!? Ulishakuwa na mahusiano naye?” James akauliza kwa ukali kidogo. “Hebu
subiri kwanza James. Unawezaje kumuhoji mke wa mtu maswali kama hayo? Huko ni kunivunjia
heshima. Mnavuka mipaka na sitaruhusu. Nanaa ni mke wangu mimi. Nashauri James
uanze kuelewa hilo na kuliheshimu. Anawajibika kwangu tu, si kwa mtu mwingine
yeyote.” Geb akawabadilikia. Kila mtu akabaki kimya.
“Hata
hivyo muda wakumuona umeisha. Daktari ameshauri alale.” Geb aliongeza na
kumfunika vizuri Nanaa. “Lakini jioni nilitaka tuje kula chakula cha usiku
pamoja, baba. Kama kumshukuru Mungu na kusherehekea birthday ya Oliva.” Mama G
akajua ameshakasirika. Akaongea naye kwa upole. “Naomba tuwasiliane kwanza
mama. Akiamka nitawajulisha hali yake ilivyo. Bado pressure yake ipo juu.
Anahitaji utulivu. Kwa nini tusisubiri akitoka ndipo tukamshukuru Mungu pamoja
nakufanya hiyo sherehe ya Liv?” “Hata hivyo mimi mwenyewe nitarudi baadaye
kuleta vyakula na kumwangalia Nanaa. Nataka kujua anaendeleaje.” Kimya. “Hata
mimi pia nitarudi baadaye.” Grace akaongeza. Nanaa hakujibu.
James
akamkabidhi Magesa kwa Nanaa, wakatoka. Geb na yeye akamchukua Liv pale
kitandani akamsindikiza mama yake akiwa amembeba. Nanaa akaanza kumnyonyesha
tena. Nesi akaingia tena, akampima nakutoka akiwa ameonyesha uso wa wasiwasi.
Nanaa akajua majibu ya presha aliyompima hayakumfurahisha. Hakujali. Akaendelea
kumnyonyesha mtoto wake huku amejawa furaha na hofu ya Malii.
Magesa
alinyonya bila kumaliza. Nanaa akajua hashibi sababu Liv alishanyonya maziwa
yote muda mchache uliopita. Geb akarudi baada ya kuhakikisha amemfunga vizuri
mtoto wake kwenye gari. Akamfunika nakumbusu mara kadhaa. Liv alikuwa amelala.
Akawaaga mama yake na dada yake na watoto, akarudi chumbani kwa Nanaa.
~~~~~~~~~~~~~
“Naona
hapati kitu huyu. Anavuta bila kupumzika.” Nanaa akamuwahi Geb mara alipoingia.
“Liv huyo! Amemaliza maziwa yote.” “Sijui nitamfanyaje ili kumuachisha ziwa. Na
hasahau! Hata mkitengana siku tatu, akirudi analilia nyonyo.” “Lakini itabidi
aachishwe kwa nguvu. Hutaweza kuwanyonyesha wote wawili. Na hivyo alivyo Liv,
na ninavyomuona kaka yake, utachoka sana.” Geb akaongeza huku akimsogelea
karibu mtoto wake. Nanaa akamuona anacheka.
“Nini?”
Akamuuliza. “Nilikuwa nikimsubiria kwa hamu huyu? Nilikuwa natamani sana
kumuona. Nilijua atafanana na mimi na baba.” “Hata hivyo naona mmefanana.” Geb
akamtizama vizuri. “Sidhani. Una rangi kali sana Nanaa. Huyu mtoto atakuwa kama
Liv. Naona wanakuwa kama mapacha!” Nanaa akabaki akimtizama mwanae kwa makini.
“Kweli atakuwa kama Liv. Natamani aniangalie.” Nanaa akaongeza. “Macho yangu
hayo.” Geb akaongea kwa kujisifu. “Na manywele kama dad. Kila kitu ni wewe Geb,
nahisi ni rangi tu. Ngoja tumsubirie tuone.” Wakaendelea kuongea huku mtoto
akisikika kunyonya kwa kutoridhika.
Mara
daktari wake akarudi. “Lazima kumuweka chini huyo mtoto ulale, Nanaa. Naomba
safari hii unisikilize. Umempata huyo mtoto kwa bahati sana. Usifikiri ndio
umepona. Nesi amenipigia simu, imebidi nirudi. Presha bado haijashuka. Naomba
upate muda wa kupumzika kabisa.” “Akishiba huyu, nitalala. Nahisi maziwa
hayatoki.” Nanaa akajitetea.
“Ndio
hicho nimekuja kuzungumza na nyinyi. Najua Nanaa hupendi maziwa ya kopo. Lakini
safari hii itabidi tu ukubali. Kwanza sababu ya aina ya mtoto uliyejifungua. Ni
wakiume. Na nilikwambia tokea yupo tumboni, mwanao anaonekana ni mlaji.” Nanaa
akacheka. “Alikuwa akila vidole hapa.” Nanaa akaongeza huku akimwangalia.
“Ehee!
Sasa nataka kwa siku saba mfululizo, ulale tu. Utapata muda na mtoto wako.
Utamnyonyesha, lakini najua kwa sasa hatashiba. Lazima aongezewe maziwa ya
kopo, kuepusha kuamka wewe mara kwa mara. Katikati ya usiku na mchana. Nataka
uwe unapata masaa yasiyopungua 8 usiku. Bila kuamka. Kulala moja kwa moja.
Nitakuwa nakupa dawa. Na mchana pia..” “Nitamnyonyesha mwanangu na nitalala.”
Nanaa akaingilia.
“Umeanza
ubishi Nanaa.” “Sasa kwa nini mwanangu ale maziwa ya ajabu wakati mimi nipo?
Ningekuwa nimekufa hapo sawa.” Nanaa akabisha. “Naomba unisikilize mimi Nanaa.
Mimi ndio daktari wako kwa sasa, na kesho nitakuletea daktari wa mambo ya moyo
azungumze na wewe labda yeye utamuelewa vizuri.” “Mimi nakutaka wewe.” “Hapana
Nanaa. Mimi huwa hunisikilizi. Acha nikuletee daktari ambaye ni mgeni kwako,
labda utamuelewa. Geb!” Akamgeukia Geb.
“Hali
ya Nanaa si nzuri. Sikutaka kuwatia wasiwasi, lakini lazima ujue presha yake
sio nzuri. Anaweza hata kupata kichaa cha mimba, kifafa na mengineyo, hata
kifo. Kama hamtanisikiliza, atakuachia hawa watoto wakiwa bado wadogo sana.”
Hapo ndipo Nanaa akatulia. Daktari akaanza kuwaeleza kwa utulivu. Mpaka Geb
akaelewa. Aliuliza maswali mengi na yule daktari akayajibu na kuwaahidi daktari
wa kesho yake atazungumza nao zaidi.
“Usiwe
na wasiwasi. Mimi nimeelewa. Na Nanaa atapumzika. Kama kuna maziwa yeyote
unayojua ni mazuri kwa Magesa, niandikie nikayanunue sasa hivi.” “Kwa sasa nesi
atakuja kumchukua mtoto. Atoke kabisa hapa. Watamlisha na kukusaidia kila kitu.
Ukienda kuwaletea hayo maziwa, utawakabidhi wao. Watakuwa wakimuhudumia wakati
wote. Watakuwa wakimleta kwa mama yake kwa masaa fulani. Ili amnyonyeshe na
kukaa naye kidogo, kisha watamchukua ili Nanaa apumzike kabisa. Akiruhusiwa,
anaweza kuacha kumpa hayo maziwa ya kopo. Akaendelea kumnyonyesha kama
alivyofanya kwa Liv.” “Nimeelewa na nitahakikisha anafuata masharti yote. Muda
mwingi nitakuwa naye hapa. Atapumzika tu.” Geb akatoa matumaini.
~~~~~~~~~~~~~
Alikuwa
ni daktari aliyekuwa akimuhudumia Nanaa tokea yupo chuoni. Nanaa alimzoea sana.
Na kwa kuwa alijua historia ya kuzaliwa kwa Nanaa, akajikuta ni mgonjwa wake
anayemuweka karibu sana. Na utundu wa Nanaa, ukawafanya wazoeane kwa karibu.
Kasoro alisumbuka na ubishi wa Nanaa. Angalau Geb alipoingia kwenye picha,
kidogo ikaleta nafuu.
~~~~~~~~~~~~~
Mtoto
alipokuja kuchukuliwa na nesi kama alivyoongea daktari, akamtaka Nanaa alale
kabisa. Geb naye akatoka kwenda kununua maziwa aliyoagizwa na daktari. Nanaa
akalala usingizi mzito. Lakini baada ya muda akashituliwa na ndoto yake na
Malii. Akaogopa sana. Akabaki akiwaza pale kitandani. Picha ya akiwa na Malii
na yale aliyoyafanya naye siku ile wakiwa wawili tu yakaanza kumsumbua. Akajua
kwa hakika ndio maana Malii anateseka mpaka sasa. Alimkatili vibaya sana. “Nimwambie ukweli wote Geb?” Nanaa
akawaza huku amejilaza hapo kitandani. Palikuwa pametulia sana. Hapakuwa hata
na dalili ya kuwepo mtu.
“Geb akijua ukweli wote, atachanganyikiwa.
Heri niache tu.” Nanaa akakataa wazo la kumwambia
ukweli wote Geb. Walipokutana na Malii, kabla hajamkatalia penzi, ni mengi
yaliendelea kati yao kabla ya hatua ya penzi. Lakini Nanaa akajiambia
hatathubutu kumueleza yote Geb. “Kama
busu tu lilimfanya apige teke kiti! Akijua yote atarukwa na akili.” Nanaa
akakusudia kunyamaza. “Hata hivyo
hatukwenda mbali san..” akasita kidogo.
~~~~~~~~~~~~~
Ni nini kilitokea kati ya Nanaa na Malii kinachomchanganya
Malii kwa kiasi hicho? Geb Hapendi Siri, Nanaa anaogopa kumwambia ukweli,
itakuaje mbeleni atakapojua ukweli ambapo hakuna siri duniani?
Malii aliyeapa lazima atampata Nanaa hata iweje, atafanyaje
akiwa ameshatoka kwenye maisha yao ramsi hata usimamizi wa harusi amekataliwa
na Geb?
Usipitwe…
0 Comments:
Post a Comment