Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Ni Wangu! – Sehemu Ya 49. - Naomi Simulizi

Ni Wangu! – Sehemu Ya 49.

 Mwana Kulitafuta!

“Ni nini hicho kikubwa unachokificha kwa mtu kama mimi ambaye nipo tayari kusimama na wewe kila mahali, na kwenye kila hali!? Nimekuthibitishia kwa vitendo kuwa ninasimama nawewe hata iweje! Ulitaka nifanye nini tena ili uniamini?” Ikageuka lawama, lakini wazi Nanaa alimjua hayupo tayari na huo ukweli. Lakini kwa jinsi alivyomjua, alijua hakuna jinsi ya kupambazuka hapo, kama hatajua alichokianzisha. “Eti Nanaa? Mpaka unanitisha! Nani huyo mwenye thamani kubwa hivyo, yakufichwa kuliko mimi kujua ukweli?” “Mimi nakujua Geb ndio maana nimeamua kukulinda. Hauwezi kubaki hivyo ulivyo ukiendelea kuchimbua haya mambo. Yalitokea tukiwa hatuko pamoja, yaliisha, nakusihi Geb, yaache kama yalivyo.” Nanaa naye akamsisitiza, tena kwa kumtahadharisha kwa wazi kabisa.

 “Katika hili sitaki ulinzi wako. Wewe niambie tu.” Nanaa akamtizama vile ambavyo ameshabadilika. “Nanaa?” “Naomba maji kwanza.”Akampa na kuyanywa. “Umetosheka?” Akatingisha kichwa kukubali na kuanza. “Kuna siku usiku kabla ya kulala, nilipata simu. Iliita sana. Kwa kuwa ilikuwa usiku na sikujua namba yake, Sikupokea.” Geb akarudi kukaa. Nanaa akasita. Akamwangalia tena kwa makini. “Naomba uniahidi hutafanya kitu Geb.” “Mbona unanipa masharti wakati hata hujaanza kunisimulia habari yenyewe? Ni nani unayemtetea hivyo!?” “Sio kumtetea. Nalinda amani.” “Naomba endelea Nanaa.” Geb alisikika kutotaka kupotezewa muda.

“Akatuma ujumbe. Akajitambulisha kama yeye ni secret admire wangu!” Nanaa akaendelea. “Tuka chat usiku ule kwa muda mrefu tu. Vichekesho tu na mambo ya kawaida. Siku hiyo ikapita. Kesho yake akaniamsha na ujumbe mzuri sana. Tuka chat kidogo, tukaagana. Mchana ikawa hivyo hivyo na usiku, mpaka ikajengeka tabia. Kila nilipokuwa nikimwambia anitajie yeye ni nani, hakutaka kuniambia.” “Kwa hiyo ukaendelea ku chat na mtu usiyemjua!?” Geb akauliza kwa wivu akionekana kama anashangaa.

“Yalikuwa mambo ya kawaida tu, sikuona ubaya wake. Alikuwa akituma jumbe za kujengana, faraja na mambo mengine ambayo hata wewe ungependelea kuyajua.” “Ulimwambia mama?” Geb akauliza. Nanaa akababaika sana. “Nanaa?” “Hapana.” “Kwa nini?” “Sikuona sababu Geb. Mara nyingi nilikuwa nikizungumza na mama yale mambo niliyokuwa nikimtaka ushauri tu. Mwanzoni Malii alikuwa akituma jumbe za kawaida tu.” “WHAT!!??” Geb alishituka mpaka akasimama. Nanaa aliropoka jina, hakutaka kumtaja mpaka mwisho wa stori nzima.

“Naomba ukae chini Geb na utulie. Hakuna kilichotokea kati yetu. Tafadhali Geb.” “Hivi unajua Malii alikuwa anajua kuwa nakupenda? Malii ndiye mtu pekee niliyemtamkia kwa wazi tokea tupo sekondari kuwa ninavutiwa na habari zako anazozisimulia James! Nikamwambia ninaguswa na wewe kwa namna ya tofauti sana. Nikamwambia nina upendo wa ajabu sana kwako. Tena akaniuliza nampendaje mtu ambaye sijamuona, nikamwambia kuna kitu cha tofauti najisikia kila ninaposikia habari zako. Iweje leo aje kinyume nyume akutake wewe?” Geb alishakuwa amekasirika.

“Sasa hivi ndio naelewa ni kwa nini hakutaka nimwajiri mdogo wake tena, japo mimi nilikuwa tayari kumuajiri mpaka nikabadili mawazo. Nafikiri yule mdogo wake alipokuona na kukupenda, alimwambia Malii kwanza kabla hajaja kwangu kukuulizia baada ya Malii kumnyima habari zako. Malii akaamua amtenganishe mdogo wake na wewe ili asimzibie yeye. Akanitumia ujumbe ambao ulinishangaza, akisema nisimwajiri tena mdogo wake. Nilipomuuliza ni kwa nini, hakutoa sababu za kueleweka. Ila kwa kuwa alishafanyiwa usahili na Grace, ikawa lazima aje nikutane naye na mimi. Kesho yake alipokuja ofisini na kuanza kukuulizia kwangu, ndipo nikamnyima kazi. Lakini sikuwa nikijua nia ya Malii kwa wakati huo kuwa ni wewe kwa kuwa tayari alikuwa kwenye mahusiano na huyo mkewe!”

“Ndio maana sikutaka kuendelea naye Geb!” “Kuendelea naye!? Kwani mlifikia wapi!?” “Nitakusimuliaje hivyo ulivyo hamaki? Unaniogopesha mpaka mimi mwenyewe Geb! Naomba utulie usikilize mpaka mwisho. Tafadhali. Na sasa hivi nilazima ukae unisikilize ili usibakiwe na habari nusu nusu.” Geb akabaki amesimama.

“Geb! Naomba ukae.” Nanaa akamlazimisha kwa ukali kidogo. Akawa kama anayejishauri na kiburi chake, Nanaa akabaki akimtizama, mwishoe akarudi kukaa. “Na hakuna kuficha kitu.” Geb akaongeza kwa hasira. Wivu ulishaibua hasira zote ndani yake. “Naomba tulia Geb. Mimi huwa sikudanganyi.” “Uliishia pale anakufurahisha kwa jumbe zake za faraja na kukujenga.” “Geb!” Nanaa akashangaa. “Ndio nataka uanzie hapo. Maana unamtindo wa kusema ‘kwa kifupi’. Nataka habari nzima.” Nanaa akajua hapata kuchwa usiku huo utakuwa mrefu haswa.

“Endelea sasa.” Geb akasisitiza. “Ndio tukaendelea ku chat mpaka nika, au niseme tukapanga kukutana.” “Tafadhali sana Nanaa. Naomba malizia sentensi yako. Mpaka ukafanyaje?” “Nilivutiwa naye Geb! Kwanza ukumbuke mimi sikuwa nawafahamu rafiki zake wote kaka James. Hata Malii sikuwa nikimfahamu kihivyo. Basi. Siku ya kwanza tukakutana. Ilikuwa siku ya jumapili. Nyinyi mlikwenda kanisani, na mimi nikaenda kanisani kwetu. Wakati ule kabla hatujaanza kuabudu kanisa moja. Na nilisikia Liz akisema mchana mtakwenda sijui kwa ndugu yake gani sijui, alikuwa na sherehe ndogo. Aliamua kuifanya mapema kwa kuwa kesho yake ilikuwa siku ya kazi. Liz alikuomba muongozane siku ya jumamosi, tena mlikuwa mmekaa sebuleni, halafu mimi na mama tulikuwa tumekaa sehemu ya kulia chakula, ukamkubalia kuwa mkitoka kanisani utamfuata muende.” Geb akanyamaza. Hakukanusha wala kukubali.

Nanaa alipoona kimya, akaendelea. “Mimi nilivyotoka kanisani, nikaenda kukutana na Malii. Tulizungumza mambo mengi na mazuri tu. Ndipo akanitamkia kuwa ananipenda.” Nanaa alimtizama Geb vizuri. Alishakuwa amebadilika mpaka macho yalikuwa mekundu. “Lakini katika mazungumzo yetu nikaanza kufikiria nilimuona wapi? Ndio nikamwambia aniambie kwa hakika alipata wapi namba yangu. Akaniambia hataniambia ila alisisitiza anataka nijue kwa hakika ananipenda na amekuwa akinifuatilia kwa muda mrefu ndio maana ameamua kuvunja ukimya.” Nanaa akaendelea.

“Nilipomuuliza ni wapi aliponifahamu mpaka akapata moyo wa kuendelea kunifuatilia, akasema hataniambia. Ndipo nikamwambia bila hivyo sitataka kuwasiliana naye tena. Nikasimama na kutaka kuondoka. Ndipo ikabidi aniambie yeye ni rafiki ya kaka James. Tukazungumza mambo mengi. Tukaagana. Lakini jumbe zikaendelea kama kawaida. Kwa kweli mwanzoni nilianza kuvutiwa Geb. Naomba nikiri. Alikuwa mwema sana kwangu. Upendo. Na wakati wote alihakikisha ananijulia hali na kutaka angalau kunisikia.” Nanaa akanyamaza akasita. Akanyamaza.

“Nakusikiliza Nanaa.” “Siku ile ya ijumaa, ile uliponiona nimetoka. Tulipanga tokea siku ya jumatatu. Aliniambia ijumaa ni birthday yake. Nikamuuliza angependa zawadi gani, akaniambia angependa kuniona siku hiyo mapema kidogo, kwa kuwa jioni nilazima awe na wazazi wake, walikuja kutoka Moshi.” “Wewe kwa nini hukushangaa kwa nini hakukukaribisha huko kwa wazazi wake?” Nanaa akanyamaza.

“Ikawaje sasa?” Geb akaendelea kuuliza. Lakini wazi alishaonekana amekasirika sana. “Si ndio mambo hayakwenda kama tulivyotarajia nikarudi nyumbani.” “Nanaa please. Unajua kabisa mimi sipendi hivyo unavyokuwa unafupisha maneno. Inamaana kuna kitu unaficha.” “Umekasirika mpaka nashindwa kukwambia kila kitu.” “Lazima nikasirike Nanaa. Malii amenizunguka na wewe ulinificha.” “Alinisihi sana nisikwambie Geb. Akasema nikikwambia nitakuwa nimeharibu kila kitu. Ndio maana mimi sikutaka hata kwenda Marangu. Sikutaka hata kuja kumuona tena.” Geb alikunja uso.

“Naomba urudi nyuma Nanaa. Tafadhali sana. Nina hali mbaya kuliko ninavyoweza kukueleza.” “Sasa kwa nini uwe hivyo Geb na wakati kwanza ni historia ya nyuma! Hatukuwa kwenye mahusiano na wala…” “Naomba usiendelee kuniumiza Nanaa. Ulishajua nakupenda.” “Hapana Geb! Mimi ndio nilijua nakupenda. Mapenzi yangu kwako ndio yalinifanya nikatae kila mtu.” “Kama kweli ulijua unanipenda, sasa kwa nini ulitoka na Malii?” Geb akauliza.

“Hiyo ilikuwa mwanzoni kabisa nilipokukatia tamaa Geb! Nilikupenda kabla sijajua kama hata una kazi ya kueleweka. Kuja kukujua sivyo ninavyokufikiria kuwa ni mlala hoi, na kampuni ninayofanyia kazi ni yako! Nikaja kumuona na Liz. Anatambulika kwenu na mama yako anampa baraka zake, nilikata tamaa Geb. Malii alikuja wakati niliokuwa nikihitaji mtu.” “Kwa kuwa alikuwa akijua kinachoendelea. Alikusudia kunizidi mahesabu. Alijua ndio kipindi changu cha mabadiliko na yeye ndio aka…” Geb akasimama na kupiga teke kiti alichokuwa amekalia, na kutoka nje.

Mwili Ni Udongo.

Nanaa akaanza kujisikia vibaya. Akabonyeza kengele kumuita muuguzi. “Samahani. Naomba nipime tena pressure. Sijisikii vizuri.” “Hata hivyo muda umefika wa kukupima tena.” Yule nesi akaleta mashine ya kupimia, akampima pressure. Ilikuwa juu sana, ikabidi daktari wa zamu apigiwe simu. Akafika. 

“Hii pressure ipo juu sana, Nanaa. Huwezi kuendelea kumbeba huyu mtoto. Lazima atolewe lasivyo utahatarisha maisha yako.” “Huyu mtoto hatatoka humo ndani. Wewe nipe dawa nyingine ya usingizi, nilale.” Dokta alibaki akimwangalia Nanaa. “Ila ninachoomba. Uache maagizo kuwa haruhusiwi mtu yeyote kuja kuniona kwa muda wa siku tatu mfululizo. Nataka nilale tu. Lazima huyu mtoto azaliwe siku zake zitakapotimia. Ila sio leo wala kesho. Kama mkiweza kuniwekea dripu ya maji kwa ajili ya kuupa mwili wangu nguvu, ningeshukuru zaidi ili hata nisiamke kula.” Akajua labda Nanaa hajamuelewa.

“Labda hujaelewa Nanaa. Kwa hali yako hiyo ukiendelea hivyo, huwezi kuishi.” “Niamini mimi nikikwambia kuwa huyu mtoto hajaja kwa ajili ya kuniua. Kama kuna mahali unataka nisaini kuwa nimekataa nisitolewe mtoto, nipe nisaini. La sivyo mimi hapa nimefika na wala sitakufa. Hujaniona nikiwa nakaribia kufa wewe. Hapa sipo hata robo yake. Wala usitie shaka. Nipe dawa.” Hakutaka kubishana naye, kwanza alijua daktari wake atafika hapo, watamalizana. Yeye amalize zamu yake huo usiku, atoke. Akaandika dawa ambazo angetaka atumie, mara Geb akaingia.

“Kuna nini!?” Geb akauliza kwa mshituko mara baada yakurudi pale chumbani, na kukuta daktari na wauguzi wawili. “Naomba umpe ule ujumbe uliosema utawapa ndugu zangu wote.” Nanaa akamrushia mpira dokta. “Ujumbe gani!?” Geb akauliza. “Pressure yake ipo juu sana. Hataweza..” “Hapana. Huo sio ujumbe ninaotaka uwape. Hujui uwezo nilionao dokta. Hujui ni nini naweza na nini siwezi. Wewe waambie kwa muda wa siku tatu, haruhusiwi mtu kuja humu chumbani isipokuwa madaktari na wauguzi tu.” “Haiwezekani Nanaa!” Geb akashangaa.

“Sasa unataka kubaki hapa ili ufanyeje? Huna unachokifanya zaidi ya kunikorofisha tu. Nimekusudia kumzaa huyu mtoto akiwa mzima na siku zake zikiwa zimetimia kama Liv. Hakuna mtu wala mazingira yatakayonizuia. Kwa kuwa umeshindwa kuwa msaada wangu, naomba unipishe nitimize jukumu langu kwa mtoto wangu. Kwa sasa ananihitaji mimi kuliko wewe Geb. Daktari anafikiria atolewe humu ndani, akidhani anahatarisha maisha yangu. Nimekusudia kumpa uhai mtoto wangu. Nitapambana mimi mwenyewe kama nilivyofanya kwa Liv, ndivyo nitakavyofanya kwa Magesa, bila wewe. Kwa kuwa wewe umeshindwa Geb.” Nanaa alishakasirika.

“Sasa nataka kujua, unanipisha ili nitimize jukumu langu au mimi nikupishe nikatafute njia zangu za kumuokoa mtoto wangu? Halafu nitakuletea nikishamzaa, kama Liv.” Geb hakuamini. Nanaa alimbadilikia kama sio yeye. Alikuwa ni kama simba anayetetea mtoto wake. “Nitatulia Nanaa.” “Hapana. Kwa sasa tulipofika ni pabaya. Ni aidha wewe utoke au Magesa ndio atoke. Sasa mimi nimemchagua yeye abaki, wewe ndio utoke hapa. Maana Magesa hana kimbilio. Wewe unalo kimbilio. Una kitanda kizuri na cha fahari kinakusubiri nyumbani.”

“Hivi unajua watakapomtoa mtoto wangu sasa hivi ni wapi wataenda kumueka? Udongoni. Mtalia na kunyamaza, mimi nitaachwa na jeraha ambalo halitapona maishani mwangu kote. Mtasema alikuwa mtoto ambaye hajakomaa au mtoto si riziki. Kwangu mimi Magesa ni mtoto kama Liv. Sitaruhusu mwanadamu yeyote aharibu kusudi la Mungu kwenye maisha yangu. Umeshindwa kupambana pamoja na mimi, mimi ndio naanza mapambano. Na siwezi kuwa na wewe kwa kuwa unanishika miguu. Naomba uondoke Geb. Na uwaambie watu wote, nahitaji mapumziko ya siku 3 mfululizo. Sihitaji mtu yeyote aje anione wala aniletee chakula. Nitakula chakula cha hapa hospitalini.” Geb alibaki kama haamini.

“Na Liv je!? Nitamleta anyonye.” “Hapana. Liv atasubiri. Yeye anaweza kula ugali, mdogo wake hana tumaini jingine isipokuwa mimi. Anaweza kuishi bila kunyonya, kaka yake hawezi. Usiku mwema Geb.” Nanaa akajiweka sawa. Kila mtu mle ndani ya chumba alikuwa kimya wakisubiri wamalize. “Naombeni tuanze matibabu jamani. Mnichome hiyo sindano, nilale.” Geb akakusanya vitu vyake akamsogelea Nanaa. “Samahani.” Nanaa hakutaka kujibu. Akanyamaza kimya bila hata kumwangalia. Akabaki akiangalia shuka alilojifunika. Geb akambusu kichwani. Akatoka. Ilishakuwa saa sita usiku. Nanaa akachomwa sindano, hapo hapo akapitiwa na usingizi.

~~~~~~~~~~~~~~

Ni kweli pressure ya Nanaa ilikuwa juu sana. Hata daktari wake aliyekuwa akimuhudumia kipindi ni mjamzito wa Oliva, dokta Lyamu, alipopita kesho yake na kusoma matokeo ya pressure ya siku iliyopita na asubuhi hiyo, alimshauri mtoto atolewe. Akamwambia kwa miezi ile, wanaweza kumuweka mahali na anaweza akakua tu. “Siku zake alizoandikiwa na Mungu kukaa humo ndani bado. Wewe niandikie dawa za kutumia. Na waambie manesi waache kupita kila baada ya nusu saa na kunipima pressure. Wananifanya nashindwa kulala. Wanapishana humu chumbani kwangu mchana na usiku!” Dokta Lyamu alimfahamu tokea ujauzito wa Liv, akawa amemjua Nanaa na mpaka wakatengeneza kama udugu sababu ya kumuonea huruma juu ya historia ya kifo cha mama yake na kumuacha akiwa mchanga kabisa. Halafu kabila likawa moja na mama yake. Akaishia kuwa daktari kama mjomba wa Nanaa.

“Huyu mtoto hamtamtoa. Hilo wala halipo kwenye mjadala. Tuendelee na jingine.” Akacheka na kutingisha kichwa. “Nanaa! Naomba unisikilize. Tatizo la mimba ile ya kwanza, sio kama sasa hivi. Sasa hivi ni serious. Ni kweli utakwenda.” “Siendi popote. Mimi nipo hapa na wewe mpaka baada ya week 3 mbele. Siwezi kukubali mumtoe mtoto wangu halafu mje mniambie sijui joto la huko mlipomuweka lilipanda au likashuka, akafa! Au sijui alizidishiwa dawa, sijui nini! Hapana. Hapa alipo yupo salama. Mwache mtoto wangu.” “Wapo watu maalumu wakuhudumia watoto wa aina hiyo.” “Wangapi wanatoka salama huko?” “Wengi tu!” Akamjibu kwa kujiamini.

“Lakini kuna wanaokufa. Si ndio?” Kimya. “Sasa Magesa hatakuwa kwenye idadi ya hao wachache, wanaopatwa na bahati mbaya na kufa huko. Yupo hapa kwa makusudi. Wewe endelea kuhangaika na hii nyumba yake, ambayo Mungu amemuweka. Nitibuni mpaka muone nimekufa, ndipo mumtoe sasa. Lakini kwa kuwa kwa sasa yupo humo ndani. Umemuangalia, na kufanya vipimo vyote. Wewe mwenyewe ukaniambia yupo salama kabisa. Sasa hakuna atakayemtoa humo.” Waliposhindwa kumshauri madaktari hao waliokuwa wamepita round akiwepo na daktari wake wa kliniki, wakajadiliana jinsi ya kutatua tatizo hilo la pressure ili mtoto akae humo ndani. Wakazungumza kwa muda mrefu huku wanafunzi wengine wa udaktari wakisikiliza kwa makini na kumuuliza maswali mpaka Nanaa alipochoka, na kuwaambia analala.

~~~~~~~~~~~~~~

Ni kweli zilipita siku tatu mfululizo Nanaa hajaonana na mtu yeyote. Alikuwa akilala tu bila kuongea na mtu yeyote yule mbali na wauguzi wanao mtibu. Mungu bariki siku ya tatu, pressure ya Nanaa ilishuka ikarudi kuwa ya kawaida. Alijitahidi kutulia na kutowaza kitu chochote zaidi ya mwanae Magesa. Akakumbuka jinsi alivyokuwa akizungumza na Oliva wakati yupo tumboni. Akaanza kuzungumza na huyo mtoto kana kwamba ni mtumzima, wanaonana. Wakati wote mikono ilikuwa tumboni akimpapasa mtoto wake.

Alikuwa amefungiwa mashine ya kupima mapigo ya moyo ya mtoto. Nayo iliwapa matumaini ya huyo mtoto kuendelea kuwa humo ndani salama bila shida. Daktari alimtaka pia awe anakula, sio kuishi kwa dripu kama alivyotaka. Nanaa alikuwa akiletewa chakula maalumu cha pale pale hospitalini na kula. Hakumuona mama G wala wanae na wajukuu zake. Hata kaka yake hakuja kumuona. Akajua Geb alifikisha ujumbe. Kwa hiyo akapata mapumziko ya kweli.

~~~~~~~~~~~~~~

Alipomaliza siku tatu, siku ya nne alfajiri na mapema akiwa usingizini akahisi mtu anamchora mgongoni. Alikuwa amegeukia ukutani. Akafungua macho bila ya kugeuka. Akajua ni Geb tu. Akanyamaza. “Nina hamu na wewe Nanaa.” Akasikia sauti ya Geb. Akanyamaza. “Samahani nilikosea. Sikutakiwa kuwa mkali kwako.” Kimya. “Au tuseme sikutakiwa kuyaanzisha yale mazungumzo kipindi hichi ambacho unahitaji msaada wangu. Ningesubiri tu. Naomba unisamehe.” Kimya. Geb alijua kuwa Nanaa anamsikiliza. Akaendelea kumpapasa mgongoni.

“Daktari ameniambia bado hutaki kumuona mtu yeyote, unahitaji muda zaidi wa kumpumzika. Naomba tuwe wote. Nakuahidi nitabadilika. Sitakukera kwa maneno yeyote yale.” Kimya. “Nanaa please!” Kimya. Geb akatulia kwa muda, akaanza tena. “Pia daktari aliniambia Magesa anaweza kuzaliwa kuanzia baada ya siku 20 kuanzia sasa na akawa sawa tu. Naomba tumalize wote hizo siku.” Kimya. Nana hakutaka hata kugeuka. Akabaki amenyamaza. Geb alikaa hapo kwa muda bila kujibiwa kitu. 

“Bado hutaki uletewe kitu chochote kutoka nyumbani?” Kimya. “Liv anakutafuta Nanaa. Anatambaa kila mahali, mama anasema anakutafuta wewe. Hachoki kwenda kwenye kochi alilozoea kukuona umelala. Naomba nimlete baadaye. Japo kwa muda mfupi tu, anyonye.” Hapo akamsikia analia taratibu. “Sitakaa sana. Nitamleta, akuone kidogo tu. Ukiweza kumnyonyesha ni sawa, ukishindwa basi angalau mpate hata nusu saa na yeye. Naomba usimwadhibu mtoto kwa kosa langu. Nakuahidi sitazungumza chochote. Ni wewe na mtoto tu. Sawa?” Nanaa akatingisha kichwa kukubali. Bado alimpa mgongo.

“Naweza kukaa hapa kidogo?” Kimya. “Sitaongea Nanaa. Nakuahidi. Nakaa tu.” Kimya. Geb akanyamaza. Baada ya muda mfupi sana akamsikia anakoroma. Akajua alikuwa amechoka. Inamaana siku hizo zote tatu hakuwa amelala vizuri. Akageuka kumwangalia. Bado alikuwa amekaa kwenye kiti, pembeni ya kitanda chake. Kichwa amekiegemeza kitandani. Amelala hana habari. Nanaa akacheka mwenyewe. Akampapasa kidogo kichwani. Na yeye akapitiwa na usingizi.

 ~~~~~~~~~~~~~~

          Alipoamka hakumkuta Geb. Alishaondoka. Akajua amekwenda kazini. Baada ya kusaidiwa usafi wa asubuhi, akakaa ili ale. Akaona muuguzi mwingine anaingia na maua mengii na kopo la icream. Nanaa akacheka. Akajua yanatoka kwa Geb. Alikuwa na hamu ya ice cream. Akaomba apewe kijiko aanze kuila hiyo ice cream. Alikula ndio akasoma na kadi. Ilikuwa kadi kutoka kwa Geb akiomba msamaha. Akaomba yule nesi amuwekee maua yake kwenye chupa. Akamuwekea pembeni ya meza na kadi yake. Akala na kurudi kulala.

          Ilipofika jioni Geb akaingia na Oliva. Oliva alifurahi sana kumuona mama yake. Kwa mara ya kwanza alisema mama nzuri, bila kukosea au kuunganisha maneno na kumfanya mpaka Nanaa alie. Akakaa na kumpokea. “Mama!” Oliva aliita huku akitoka kwa baba yake na kutaka mama yake ampokee.  “Na mimi nina hamu na wewe Liv.” Tayari alishamsogelea kifuani. “Husahau kunyonya tu!?” Nanaa alimuuliza mwanae huku akifuta machozi. Oliva alianza kunung’unika akiashiria kutotaka kuchelewesha. Mama yake akamlaza pembeni yake. Alionywa asiwe anambeba kwa wakati huo. 

Kwa hiyo wote wakalala pale kitandani. Akaanza kumnyonyesha. Alinyonya huku akimtizama mama yake. Nanaa alikuwa akimwangalia kwa upendo. Ilisikika milio yake akimeza maziwa ya mama yake kwa nguvu zote. “Umependeza Liv. Bibi ndiye amekusuka?” Nanaa aliuliza kana kwamba atajibiwa. Oliva alibaki akimwangalia tu mama yake huku akinyonya.

“Ni Grace ndiye amemsuka. Alikuwa kwake tokea asubuhi anacheza na Fili.” Nanaa hata hakumwangalia. Geb akanyamaza akajua bado Nanaa hataki kuzungumza naye. Swali la kama harusi bado ipo au la, aliogopa hata kumuuliza Nanaa. Kuhofia jibu la hapana. Akabaki kimya.

“Asante kwa maua na Ice cream. Nilikuwa na hamu nayo!” Nanaa akavunja ukimya. Nusura asimame. “Naweza kuleta tena usiku.” “Naomba usitafute sababu ya kurudi kuja kulala hapa.” Geb akacheka. “Nitakuletea na nyama choma.” Tayari Nanaa akaanza kushawishika. Nanaa mmpenda kula alikuwa akiletewa vyakula visivyo na chumvi! Tena vyakula vya wagonjwa! Nyama choma ikasikika vizuri mpaka rohoni.  Halafu hata yeye alikuwa na hamu na Geb. Mara nyingi usiku wakiwa kitandani wao wawili walikuwa wakipata wakati mzuri sana. Vicheko na stori za hapa na pale. Tena mara nyingi baada ya kupeana penzi zito. Hata wakiwa hapo hospitalini, bado walitumia muda wao vizuri. Walipeana mabusu ya haja huku wakiliwazana vyakutosha. Hakuna jinsi Nanaa aliyesumbuliwa na wanaume, pamoja na ndugu waliomuona mzigo eti leo umwambie akae mbali na Geb muda mrefu akafurahia. Hata kidogo. Bado hakuzoea kuhitajika kwa kiasi kile.

          “Sijui nilete na chips au ndizi za kuchoma?” Geb akajidai anajiuliza kwa sauti. Akajua Nanaa ameshaingia line. “Halafu nimenunua movie nzuri. Naweza kuleta wakati nakuletea ice cream na nyama choma. Ila sasa sijui nilete na nini!?”  Geb akaendelea kutangaza hongo. “Kwani ukileta vyote kuna shida gani!?” Nanaa akajibu nakumfanya Geb acheke. Akajua ameshanasa kama mama yake. “Bwana usinicheke kwa kuwa unajua napenda kula!” “Mimi nimefurahi tu.” Nanaa akamwangalia. Alikuwa akiishi na wanawake hao wawili. Mashoga haswa. Nanaa na mama G. Na ndio wanawake aliowapenda sana. Aliwajua udhaifu wao wote wawili. Mama yake mmpenda pesa, hiyo ikawa hongo yakumtuliza. Na Nanaa chakula. 

“Nimekumiss Geb!” “Mwenzio hata silali vizuri. Nimekuwa kama mlinzi huko nyumbani.” “Nimekuona ulivyokuwa unakoroma hapa asubuhi.” “Si unihurumie usiku nije tu kulala hapa?” Nanaa akacheka. “Ukichelewa utanikuta nimeshalala.” “Naenda tu kumshusha huyu, narudi.” “Sasa sio urudi mikono mitupu!” Geb alicheka huku anatingisha kichwa. “Nanaa kwa chakula! Sitasahau mama. Najua hiyo ndio tiketi yangu ya kuingilia hapa?” Nanaa akacheka.

Usiku.

Geb alirudi akamkuta Nanaa amelala. “Nanaa!” Akafungua macho. “Nimepitiwa na usingizi sasa hivi. Nilikuwa nasubiria hiyo nyama choma kwa hamu! Halafu Liv ameninyonya mpaka ameniacha na njaa! Nikaona nisile chakula cha hapa hospitalini ili nije kufaidi nyama.” “Atakuwa alikuwa tu na hamu na wewe. Grace anasema alikula vizuri tu. Wala hakumsumbua kula.” “Aliamka njiani?” Nanaa akauliza huku akijiweka sawa. 

“Hapana. Atakuwa alikuwa amechoka pia. Amecheza sana na Fili. Na hivi anataka kutembea kama mwenzie, utamuonea huruma.” Nanaa akacheka. “Naomba umrudishe tena kesho. Leo ameniita mama!” “Nimemsikia. Juzi ameniita mimi da-da.” Nanaa akacheka sana. “Dada tena!” “Mimi sijali. Ilimradi najua ni mimi, nimefurahi sana.” Geb akajibu.

          Baada ya chakula, Nanaa akaanza tena. “Geb! Najua bado unataka kujua nini kilitokea kati yangu na Malii.” Geb akanyamaza. “Ungependa nimalizie?” “Sitaki iibue mambo mengine Nanaa. Nataka huyo mtoto azaliwe mimi nikiwepo. Maana sasa hivi mimi ndio nimegeuka mkosaji wala sio wewe! Naomba tuache tu. Tutakuja kuzungumza wakati mwingine.” “Sasa mimi nilikosea nini Geb!? Mwanzoni sikujua kama mnafahamiana na Malii! Pili hatukuwa kwenye mahusiano mimi na wewe!” “Nanaa please! Naomba tuache tu. Ulijua nakupenda. Na ulijua kama ni kosa ndio maana ulijificha hukutaka hata mama ajue na wala uliponikuta pale nje, ulishindwa kuniangalia usoni. Ulisalimia na kuingia ndani moja kwa moja kwa kuwa ulijua ulinikosea Nanaa. Dhamira ilikusuta kwa ulichotenda.” Geb alisisitiza kukosewa.

“Siku ile nilishindwa kukuangalia sababu ya kushindwa kufanya nilichotaka kufanya si sababu ya kufanya unachofikiria. Nilijichukia kwa kushindwa kufanya kile mwili wangu ulitaka kwa wakati ule sababu ya kubeba hisia za mwanaume ambaye alikuwa mpenzi wa mtu mwingine! Tena ambaye nilijua siku hiyo hiyo usiku, mpenzi wake anakuja kulala naye, humo humo ndani ya nyumba niliyomo mimi. Tena nikiwepo chumba cha jirani! Wakifanya kile mimi ninachoshindwa kufanya wakati huo.” Nanaa alianza kutokwa na machozi.

“Nikweli nilikwenda kukutana na Malii. Gari uliyoiona ilikuwa ni ya dereva taksii. Nilishazungumza naye na kumwambia aje anichukue na kunipeleka sehemu tuliyokubaliana na Malii. Haikuwa nyumba ya kulala wageni. Aliniambia ni nyumbani kwa rafiki yake. Ni kweli nilishavutiwa na Malii. Kwa jumbe alizokuwa akinitumia, alionyesha kunijali na kunihitaji. Nilifika kwenye hiyo nyumba, tukala na kunywa. Lakini mimi sio mtoto Geb. Nilijua mwisho wa yote ni mapenzi. Na nilikusudia kufanya hivyo. Siwezi kukudanganya.” Nanaa alimfanya Geb abaki akimtizama.

Nanaa akajifuta machozi. Akaendelea akiwa ametulia kidogo. “Na sio kwamba sikumwambia mama kwa kuwa niliogopa! Mama alijua upo na Liz. Na aliona vile Liz alivyokuwa akija kulala pale na wewe. Nilijipa muda ili nione tutakapoishia mimi na Malii. Malii alikuwa tofauti na wote niliokuwa nikimwambia mama. Ni mtu niliyekuwa nikifurahia mahusiano yake. Nilitaka kumchunguza kwa muda mpaka nione mwisho wake ndipo nimtambulishe kwa mama na kwa kaka. Sikutaka ushauri wa mtu, kwa kuwa nilikuwa nimekusudia kuwa naye. Malii ni mtu wa nyumbani. Hicho pia kilikuwa kigezo kingine kilichonifanya nivutiwe naye kwa haraka kuona ni kabila moja.” Nanaa akaendelea.

“Baada ya kula na kunywa, ulifika wakati ambao hata mimi nilikuwa nikiusubiria kwa hamu. Malii alininyanyua, akanikumbatia na kunibusu.” Nanaa alimuona Geb amefunga macho na kutingisha kichwa. “Naomba acha Nanaa. Tafadhali sana.” “Hapana Geb. Naomba nimalizie. Umeyataka wewe mwenyewe. Nilikubembeleza sana tuyaache, ukakataa. Sasa tulia nimalizie ili uamue leo kama bado unataka kunioa au utanihukumu kwa maisha niliyoishi zamani.” “Ukisema hivyo unakosea Nanaa.” “Kweli Geb. Huyu mtu nilikuwa naye kabla yako. Na hata hatukuwa kwenye mahusiano kwa muda mrefu.” “Kwamba unayatambua kuwa ni mahusiano!?” “Naomba nisimulie mpaka mwisho Geb. Tafadhali sana.” “Mimi najihisi sipo tayari kuzungumzia hili swala tena. Naomba tuache tu.” “Tunaachaje Geb?” Geb akasimama.

“Hunielewi   Nanaa. Malii alinifanyia makusudi.” “Makusudi kivipi wakati ulikuwa na Liz, Geb!?” “Huelewi Nanaa.” “Naelewa. Na yeye alinisimulia kwa upande wake ndio maana na mimi nikakubaliana na swala la kunyamaza, nisikwambie.” “Alikwambia nini?” Geb akauliza. “Ndio ukae sasa ili nikusimulie ukweli wote.” “Naumia Nanaa.”           “Unaumia nini sasa?”“Malii amenigeuka.” “Hajakugeuka Geb. Wewe kaa chini.” “Wewe zungumza tu.” Nanaa alijua ujeuri wa Geb umesharudi. Alibadilika. Akajua kiburi chote kimerudi vile vile.

Akabaki akimwangalia. “Wewe si unataka kumalizia? Malizia sasa. Uliishia kuwa mlikuwa mmekumbatiana, mnakisi.” “Unatafuta kujiudhi bure Geb.” “Sio natafuta. Nimeshakasirika sana Nanaa. Malii amenifanyia ubaya.” “Ubaya gani? Sio yeye aliyekuuliza  juu yangu?” Geb akakunja uso.

“Malii hakukuuliza utafanyaje juu yangu na Liz?” Kimya. “Unakumbuka jibu ulilompa?” Kimya. “Sasa kama hukumbuki, Malii alikurikodi na akanisikilizisha.” “Eti nini!?” Geb alishituka sana. “Ndio ujue hata mimi niliumia Geb. Lakini niliamua kunyamaza tu. Malii alinisikilizisha mazungumzo yenu yote, mliyokuwa mmezungumza siku ile. Niliyasikia majibu yako yote uliyokuwa ukimjibu Malii juu yangu. Kwa hiyo hakuna aliyekuzunguka Geb. Malii alifanya kwa haki, kwa yale uliyomjibu juu yangu.” “Kwa hiyo alinitega wakati ananiuliza ili anirikodi aje kukwambia?” Geb akauliza, lakini wazi alionyesha kuishiwa nguvu. Kumbukumbu juu ya mazungumzo yake na Malii juu ya Liz na Nanaa, ilimjia sawia kama alivyojaliwa na Mungu kutosahau. Akakumbuka kila kitu.

“Hakuwa amepanga kunisikilizisha. Ila baada ya kunibusu kwa muda, nilimwambia aniache tu. Akauliza kwa nini, nikamjibu, ‘hapana’ tu. Ndipo akajaribu kunibembeleza sana, lakini nilishindwa Geb. Hisia ambazo nilikuwa nikizisikia nikiwa na wewe, hata ukiniongelesha tu, sikuzipata kwa Malii siku ile. Ila sikumwambia. Aliniona nalia. Akadhani alikosea kitu. Nikamwambia hapana ni mimi mwenywe ndio nina tatizo. Kumbuka Malii sio mwanaume wa kwanza kumkataa tokea nikuone wewe na kukupenda Geb. Muulize mama. Lakini Malii nilitaka ndio nitulie naye baada ya kukukatia wewe tamaa.” Geb akarudi kukaa.

“Malii hakuwa ameelewa tatizo langu ni nini na mimi nilishindwa kumwambia. Ningeanzia wapi? Namwambia vipi nampenda mwanaume anayenihifadhi nyumbani kwake? Tena inajulika wazi mpaka kwa familia yake kuwa ana mpenzi? Tena anayekuja kulala hapo hapo na ni rafiki ya dada yake!? Nilishindwa kumwambia Malii na nilishindwa kuendelea hata kumruhusu anikumbatie kwa kuwa nilishajua zipo hisia za kweli ndani yangu. Kuendelea kufanya chochote na Malii, itakuwa nikutomtendea yeye haki na nafsi yangu pia. Nikabaki nikifikiria, nisijue cha kumwambia.” Nanaa akaendelea.

“Kwanza nilijisikia vibaya. Kwa kuwa aliniambia ile sehemu aliihangaikia makusudi kwa ajili yetu siku hiyo. Kwa hiyo sio kwamba alinishitukiza alichotaka tukifanye! Tulishazungumza na mimi nilimuonyesha kuwa nipo tayari. Sasa iweje tena nimbadilikie wakati tulikubaliana na yeye alikuwa tayari kabisa kwa mapenzi? Nikabaki nikifikiria na yeye akijiuliza kulikoni wakati ndio ulifika wakati mwafaka ambao wote tulikuwa tukiuusubiri kwa hamu? Nilikataa hata asiendelee kunishika. Ndipo akaropoka gafla na kuniuliza kwa kunishitukiza akasema, ‘au sababu ni Geb?’ Hapo ndipo nilishituka mpaka akajua jibu ni ‘ndiyo’. Maana ndio na mimi nilikuwa nikikufikiria.” Nanaa akaendelea. Hapo hata Geb hakutia neno.

“Alinicheka kwa dharau sana. Akaniambia wala nisijisumbue hata kukufikiria. Wewe huna mpango na mimi. Na wanawake kama mimi tunaokufikiria wewe na kusubiria labda siku moja utatukubali, akasema tuko wengi sana. Akanitajia majina baadhi ya wanawake wanaokusubiria na ambao hata walishakutongoza. Akaniambia wengine mlikuwa nao pale chuo kikuu cha Mlimani. Akanihakikishia kabisa huna mpango na mimi. Na kuweka msisitizo juu ya hilo ndipo akanieleza mahusiano yenu. Kuwa nyinyi mpo karibu sana kuliko watu wengine. Na huwa mnazungumza mambo mengi.” Nanaa akaendelea. 

“Ukweli alikuwa muwazi kwangu vya kutosha. Aliniambia pia alikuwa na mwanamke ambaye anataka kumuoa. Lakini baada ya kuniona, akavutiwa na mimi. Alisema nyinyi wote mnanifahamu kutokana na stori alizokuwa akisimulia kaka James. Wewe ulikuwa mstari wa mbele kuniulizia. Kwa hiyo aliponiona na kuvutiwa, akakumbuka swala la kwako la kunifuatilia kwa karibu. Ndipo akakuuliza vipi juu yangu? Akakuuliza, ‘kuniuulizia kule kulikuwa na maana nyingine yeyote, au ni undugu tu?’ Nikasikia akikuuliza tena, ‘ile hisia uliyosema unajisikia juu yangu na kukufanya kuniulizia wakati ule hata kabla hujaniona, imebadili chochote baada ya kunioana?’. Unakumbuka alikuuliza tena, ‘itakuaje juu ya Liz baada ya mimi kutokea?’ Nafikiri unakumbuka majibu yako yote kwa kuwa huwa husahau Geb.” Nanaa aliona vile Geb alivyotulia. Akajua wazi amekumbuka kila kitu.

“Nisikilize Nanaa. Mimi nilimjibu vile Malii kwa kuwa nilijua vile Malii alivyokuwa karibu na watu wengine. Nikajua jibu lolote nitakalompa ni kama nitakuwa nimetangazia uma. Ni kweli Malii nipo naye karibu kuliko wengine wote kama alivyokwambia, lakini huwa simwambii kila kitu. Na Malii najua yupo karibu yangu kwa sababu zake. Nazifahamu. Ndio maana haishiwi maswali kwangu kuliko marafiki zangu wengine wote. Kama umeshatuangalia, ni kama wengine wananiogopa kidogo. Ni sababu ya kuwa sana mkimya. Huwa nipo sana makini na kila neno linalotoka kinywani mwangu. Na wote wale najua tupo karibu, lakini wanamaswali mengi sana juu yangu. Mengine wanashindwa kuniuliza moja kwa moja. Niligundua huwa wanamtuma Malii kupata majibu fulani fulani kutoka kwangu kwa kuwa Malii amewahakikishia kuwa huwa nipo muwazi sana kwake.” Geb akaendelea.

 “Lakini huwa hajui. Huwa namjibu kutokana na kile ninachojua anapenda kusikia au ni sawa hata akiwarudishia majibu wenzie. Malii alishahangaika sana kuiba biashara zangu. Alishakuwa karibu sana na mimi ili kujua nini nafanya, ili afanye kama mimi ili anizidi. Kwa kuwa nilishamjua anahila ndani yake, kila alilojaribu kuuliza, nilimjibu kwa kiwango kidogo sana. Akidhani amefanikiwa, akaanza kuagiza malori nje ya nchi ili afanye biashara kama ninayofanya mimi na mbaya zaidi, kwa kutumia wateja wangu wale wale. Sikumuonyesha najua wala sikumuuliza japo nilijua kuwa ameingiza nchini hayo malori mawili kwa siri na kuanza kupigia simu wateja wangu. Alisajili kampuni kama yangu na kutafuta jengo kubwa.” Nanaa alitulia kumsikiliza.

“Vyote hivyo anafanya kushindana na mimi. Asijue mwenzie nilianzia wapi. Yeye akaanza kwa kishindo, tena kwa pesa ya wizi. Kampuni aliyokuwa akiwafanyia kazi ilikuwa ikihusika na mambo ya mtandao hapa nchini. Walikuwa wakimlipa vizuri sana. Kuja kushituka, Malii alikuwa akiwauzia huduma makampuni mengine, kwa kutumia vifaa vya hapo hapo kwenye hiyo kampuni, lakini aliwauzia kwa jina la kampuni yake kwa siri. Wamiliki wa ile kampuni walipokuja kumgundua, walimshitaki. Hawakutaka kesi kubwa ili wasiharibu jina la kampuni yao, lakini Malii akafilisiwa kila kitu mpaka yale malori na nyumba aliyokuwa amejenga.” Nanaa alibaki ametoa macho.

“Pale alipo Malii ni kama ameanza upya maisha. Kazi aliyonayo sasa hivi, nilimsaidia kumuunganisha na jamaa mmoja, ndipo wakampa kazi kwenye kampuni yao bila maswali mengi kwenye usaili kwa ajili yangu. Kwa kuwa pia ni mtendaji kazi mzuri, hakuna aliyejuta. Pale alipo hafahamu kama nafahamu alichokuwa akitaka kunifanyia. Niliamua kumuacha tu kwa kuwa nilishajua ni mtu wa namna gani.” Geb akaendelea.

“Naomba ujiulize Nanaa. Hata kama mimi nilimjibu kuwa wewe ni kama wasichana wengine tu kwenye maisha yangu, kama ni mtu mzuri kwetu, mimi au wewe, akijidai mimi ni rafiki yake, kwa nini anirikodi? Na kwa nini akusikilizishe mazungumzo yetu? Alishindwa nini kujitengenezea njia ya kukupata mpaka anichafue mimi?” Kimya.

“Eti Nanaa?” Geb alimuuliza. “Mimi sijui Geb. Lakini nakwambia kile nilichomwambia na yeye. Sijali unanifikiria nini, na sijali upo na nani. Sijui kwa nini hisia zangu zimekuwa kubwa kwako. Na nilimwambia pia sijui kwa nini iwe kwako. Akasema labda pesa. Nikamuhakikishia sio swala la pesa, kwa kuwa nilikupenda kabla hata sijajua kama wewe una pesa. Nilimwambia ninachojua nakupenda kwa dhati. Sijawahi kupata hisia za namna hiyo kwa mwanamme mwingine yeyote ila wewe Geb. Ila nilimwakikishia kuwa, endapo itatokea ukanipa hiyo nafasi, nitaitumia ipasavyo. Si kwa ajili yako tu, ila kwa ajili yangu mwenyewe. Nilimwambia nimekusudia kuupa moyo wangu kile kinachopenda. Nikamwambia nitakusubiri. Akitokea mwingine atakayeweza kuamsha hizo hisia kama zilivyoamka kwako, na akanifungulia mlango, nikamwambia sita, sita. Awe tajiri, awe fukara nitajitupia kwake.” Nanaa akaendelea.

“Aliponiambia niyape muda mahusiano yetu, nikamwambia nina uhakika sio yeye. Kwa kuwa wewe sikuwa nimekupa hata nafasi. Lakini nilipokuona tu, nikavutiwa mno. Nilimwambia mara ya kwanza nilishindwa hata kulala vizuri, nikitamani nije kukuona tena wakati mwingine. Haikuwa ni kwa muonekano tu. Nilimwambia nishatongozwa na wanaume wazuri sana kimuonekano. Waliobeba baadhi ya vigezo nilivyodhani navihitaji kwa mume wangu. Lakini nilipokutana na wewe, ilikuwa tofauti. Kwa mara ya kwanza, nilisikia kitu cha tofauti moyoni mwangu. Sina jinsi nikamueleza mtu, akanielewa. Lakini nikamwambia nilipojua uwezo wako na yupo Liz kwenye maisha yako, niliamua kukaa mbali kabisa na wewe, lakini bado hisia zangu ziligoma kubadilika. Nilijikuta unajengeka utayari wa kusubiri kitu ambacho sio kawaida yangu. Nikamwambia kwa kunishika siku ile na kunibusu, nimehakikisha yeye siye na wala hatakuwa ndiye. Tukaachana kwa makubaliano yaishie pale na wala tusitafutane tena. Akasema atamuoa mwanamke wake. Nikamtakia kila la kheri. Tukaachana.” Nanaa akamaliza. Geb akatulia kidogo.

“Kwa hiyo sijui umenielewa Geb? Mimi sikujua mahusiano yenu mpaka siku hiyo alipojifungua kwangu. Sikumwambia mama kwa kuwa aliniambia wanamahuasiano ya karibu sana na mama G. Akaniomba nisiwaambie, yasije kuharibika mahusiano yenu. Nilipomuuliza kama ningemkubali, je angeendelea kuwaficha? Akanijibu kwa wazi kabisa. Akaniambia wewe uko karibu sana na mama yako. Na upo makini sana kwenye maisha. Huwa huropoki. Kwa kumjibu vile yeye, inamaana hata mama G anajua hilo. Sio siri kuwa mimi unaniona kama mtu tu wakawaida tu. Na unanisaidia pale kama mdogo wake James.” “Sasa kwa nini akukataze tena kusema?” Geb akauliza.

“Kwa vile nilivyokuwa nimemwambia nitakungoja tu mpaka nitakapopata mtu mwingine au mpaka wewe utakaponipa nafasi. Na nilimuhakikishia Geb. Na ndivyo nilivyofanya. Nilimwambia ikitokea unanipa nafasi maishani mwako, nitahakikisha nitaitumia ipasavyo kwa kuwa nitakuwa nimepata uhakika kutoka kwa Mungu. Nitakupenda kwa dhati kwa kuwa ninajua wewe ni wangu, ambaye Mungu amenipa. Nilimwambia Malii, hakuna sababu ya wewe kuja kunipenda mtu kama mimi. Kwa kuwa umezungukwa na kila kitu unachokihitaji. Wanawake wazuri wanakugombania. Wengine mama alikuwa akinionyesha mpaka picha zao huko Facebook na Instagram. Nikamwambia, ukija kwangu nitajua wewe ni wangu kwa hakika. Malii alinitazama kama hivyo unavyonitazama wewe. Lakini alisema kama ningemkubali yeye, angenitambulisha kwenu bila shida, kwa kuwa ulishakataa mahusiano yetu kimapenzi. Ulimwambia baada ya kuniona, ukagundua ilikuwa ni huruma tu iliyokuwa ikikupelekea kuniulizia tokea zamani, ndio maana uliamua kuendelea kumsaidia kaka James, kwa kuishi na mimi.” Geb akatulia kidogo.

“Naomba nikuulize swali Nanaa. Na naomba uwe muwazi.” “Nini?” Nanaa akauliza. “Umeshawahi kutilia mashaka mapenzi yangu kwako hata mara moja?” “Ninachojua kwa hakika, nakupenda Geb. Hilo sijawahi kulitilia shaka hata mara moja.” “Kwa hiyo mimi umenitilia mashaka.” “Siwezi kusemea moyo wako Geb! Mdomo unaongea mengi. Inawezekana na mimi unanipa majibu ya yale unayojua ningependa kuyasikia kutoka kwako kama unavyofanya kwa Malii!” “Nanaa!!” Geb akashangaa sana.

“Kweli Geb. Mimi nawezaje kuusemea moyo wako?” “Basi naomba uyasemee matendo yangu kwako.” “Kwa matendo hapo naweza kukusemea.” “Nakusikiliza.” Nanaa akacheka. “Mbona unawasiwasi?” “Nataka kujua unafikiri nini juu yangu, Nanaa. Mengi yamesemwa. Si Malii tu, hata Zinda. Aliongea mambo mengi akithibitisha kuwa sikupendi kwa kuwa nilikuwa na Liz wakati nikiwa naishi na wewe.” “Mimi hayo siyajali. Na hata mama nilimwambia. Ilimradi nilikupata, inatosha. Mimi nilikuwa na maisha yangu ya mahusiano kabla yako. Sema mahusiano yangu yaliisha kabla ya kukutana na wewe. Na wewe mahusiano yako yaliisha baada ya kukutana na mimi. Mimi naona ni yale yale tu.” Nanaa akaendelea.

“Na huwa nakutetea hata kwa watu. Hata Grace alishaniuliza hilo swali. Mimi sio mwanamke wa kwanza kwenye maisha yako. Usingeweza kukurupuka kwangu mara baada ya kuniona na kuacha wanawake zako wote.” “Ni Liz tu, Nanaa.” Nanaa akacheka. “Huyo huyo Liz. Eti ukamuacha bila hata kunifahamu mimi ni nani! Nina tabia gani! Kama kweli nakupenda wewe kwa dhati au nipo kama wanawake wengine wanaopenda hayo macho yako na pesa.” Geb akacheka.

“Si ni kweli?” Nanaa akauliza. “Nakupenda Nanaa. Niamini nikikwambia nakupenda na nilikusudia wewe ndio uwe mke wangu. Hamna sababu yeyote inayonifanya niwe hapa sasa hivi na wewe. Au uwe na watoto wangu kama mimi sikuamua Nanaa. Nilikwambia na ninarudia, mimi sikurupuki. Hasa kwenye mambo yanayohusu maisha yangu. Watoto unaozaa na mimi sio bahati mbaya. Nimekusudia. Nimekuchagua wewe uwe kwenye maisha yangu yote hapa duniani. Lasivyo ungenikuta nilishaoa au nilishakuwa na watoto tokea zamani maana wewe sio mwanamke wa kwanza kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mimi. Niliamua watoto wangu wote watokane na wewe.” Geb akasisitiza.

“Malii aliniambia majuzi tulipokutana na mkewe tukizungumzia swala la kuwa ukurasa mmoja kwenye harusi, wao kama wasimamizi wetu wa harusi. Unakumbuka pale hotelini mkewe alikwenda chooni na wewe ukatoka kwenda kuzungumza na simu? Mlituacha mimi na Malii pale mezani. Unakumbuka?” Geb alibaki akimtizama Nanaa, akitaka aendelee ili ajue ni nini tena kilitokea. “Geb?” “Nakumbuka Nanaa.” “Basi aliniambia unanioa kwa sababu ya rangi yangu tu. Au rangi ya ukoo wetu,  wala si mapenzi.” Nanaa akaongeza na kumuudhi sana Geb. 

“Yeye ndio alikuwa akipenda wanawake weupe tokea zamani. Hata alipotutambulisha huyo mkewe, kabla ya kumuoa, tena nakumbuka hata Danny aliongea hili. Akamwambia ugonjwa wake tokea tupo shule ni wasichana waupe. Malii hajawahi kuwa na msichana mweusi hata mara moja. Tena alikuwa anasema wasichana weusi wote anawaona kama dada zake wakuzaliwa tumbo moja. Hawezi hata kuwatongoza. Liz alishawahi kumpiga na kiatu sababu ya kusema hivyo siku moja tukiwa pamoja.” “Danny alimwambia nini?” Nanaa akauliza.

“Danny alimtahadharisha na kumwambia ndoa ni kifungo cha maisha. Yeye hajawahi kuwa na mwanamke mweusi hata mara moja. Tena akiwa amekusudia sio kwa bahati mbaya kuwakosa wanawake weusi. Ni alikuwa hawatongozi kabisa. Akimuona msichana mweusi anayempenda yeye, au yupo karibu naye, alikuwa akiwafanya marafiki tu. Alikuwa akisema anaogopa kuwatongoza kabisa. Sasa Danny akamuuliza iweje leo aoe mwanamke mweusi? Akasema yule dada ni watofauti. Amembadili mtazamo kabisa. Anasifa zote za kuwa mkewe. Danny akamuuliza je yeye anasifa za kuwa mumewe? Akasema amebadilika, sasa hivi ametulia. Atakuwa mume mzuri. Kumbe huku nyuma anakutongoza wewe! Mimi sikuwahi kuchagua mwanamke kwa rangi hata siku moja. Mbona Liz alikuwa mweusi? Kwanza naweza kusema mama ndio alivutiwa na rangi yako kuliko hata mimi mwenyewe.” Nanaa akacheka sana.

“Namsikia anavyosema nimeleta damu nyeupe kwenye ukoo.” “Basi ujue ni mama na Grace ndio wanakusifia rangi yako kuliko hata mimi mwenyewe.” “Kwa hiyo wewe hupendi rangi yangu!?” Nanaa akauliza kwa kulalamika kidogo. “Nanaa!” “Wewe sema tu.” “Nilishakwambia nilikupenda hata kabla sijakuona. Nakupenda Nanaa. Nakupenda sana mpenzi wangu. Na nilizidi kukupenda baada ya kukuona. Sasa sijui kama na rangi ilichangia, lakini jua nakupenda.” Nanaa akacheka kuonyesha kuridhika.

“Kwani kaka hakuwahi kuwaonyesha picha zangu?” Nanaa akauliza huku akijirudisha kulala vizuri. “Kwani wewe ulishamuona kaka yako akipiga picha?” Nanaa alicheka sana. “Kweli bwana! Kaka hapendi picha. Utambembeleza week nzima kumpiga picha ndio anakubali.” “Basi umepata jibu. Ila nakumbuka kumdadisi kidogo tu baada ya kuona hisia zinanisumbua, nikamuuliza kama mnafanana naye. Akasema labda rangi tu. Lakini akasema hata sura hufanani na mama yako kabisa.” Nanaa akafikiria.

~~~~~~~~~~~~~~

“Eti Geb. Unafikiria ni sawa nije kumtafuta baba yangu?” “Sio vibaya. Lakini kwa jinsi alivyonisimulia James, hata na wewe pia, mlisema alikana mimba na wewe mwenyewe wakati ni mtoto mdogo kabisa. Sasa hutaumia ukimtafuta halafu akukatae tena?” Nanaa akafikiria tena. “Lakini safari hii sitamtafuta kwa mahusiano. Nikutaka tu kumuona. Nimfahamu. Sihitaji kitu kutoka kwake. Angalau nijue nafanana na nani, kabila langu na mambo ya kawaida tu. Wala sitamuomba mahusiano.” “Sawa. Tutazungumza na      James.” “Asante Geb.” Nanaa akashukuru.

 “Lakini Nanaa, nimeamua Malii na mkewe hawatatusimamia tena harusi.” Nanaa akabaki kimya akimtizama. “Malii bado anaonekana anakutaka na hatatulia mpaka akupate.” “We Geb! Yaani unamaanisha nitamkubali!?” Nanaa akashituka sana. “Ujue mimi sio muhuni? Hata kama hukunikuta bikra, ila ujue najiheshimu sana. Acha..” “Hapana Nanaa! Subiri kwanza. Acha kupaniki. Sijamaanisha hivyo.” Geb akamkatisha maana Nanaa alishabadilika.

“Unamaanisha nini sasa?”  “Namaanisha ataendelea kutusumbua sana. Hasa wewe. Hatakata tamaa. Mimi namfahamu Malii kwa wanawake. Na zaidi wawe wangu na ni mweupe! Itatusumbua tu.” Kimya. “Sasa mbona husemi tena kitu!?” “Unataka kunisikia nikisema nini Geb? Mimi sijali nani anatusimamia harusi. Ilimradi wewe uwepo siku hiyo, basi.” Geb akacheka kidogo.

“Kwa hiyo bado unataka nikuoe?” Nanaa akamwangalia na kucheka kwa kuguna kidogo. “Wewe ni mkorofi sana Geb.” Geb akacheka. “Mimi ndio mumeo bwana. Ni hasira tu.” “Unakasirikaga bila hata sababu!” “Nilijua utasema unaomba nibadilike.” “Aiii! Mama yako alinisimulia habari za baba yako. Anasema alikuwa hivyo hivyo.” Geb alicheka sana. “Mama bwana! Anapenda kuniharibia!” “Ndio ukweli wenyewe. Wakati mwingine unakasirika mpaka nakuhurumia. Na mara zote mimi ndio sababu!”

“Basi usiwe unaniudhi.” “Nitafanyaje Geb jamani? Hutaki nitoke na kaka yangu. Hutaki niwe kwenye mitandao. Hutaki niwe na marafiki. Nikichelewa kurudi nyumbani, nikikukuta wewe ni shida. Hata kama nitarudishwa na kaka au Grace dada yako pia ni shida!” “Nakuwa naacha mambo yangu ili nirudi nyumbani tuwe wote, halafu na wewe sikukuti! Hata wewe usingefurahia Nanaa.” Nanaa akabaki akimwangalia.

“Wewe niangalie hivyo hivyo. Lakini nataka niwe nakukuta nyumbani.” “Ndio ukampiga marufuku na mama kutembea na mimi jioni?” “Mimi nilimwambia kwa vizuri tu. Shuguli zake za jioni za kina mama, wewe hazikuhusu. Asiwe anakuchukua, akuache nyumbani na mtoto.” Nanaa alicheka na kutingisha kichwa. “Unashida wewe! Mpaka kwa mama yako mzazi!” “Wewe ukianza heka heka za mama G, mambo ya nyumbani yatakushinda. Wewe mwache azunguke mwenyewe. Nimemwambia akitaka mtoke, iwe asubuhi, ili jioni uwepo nyumbani.” Nanaa akapumua kwa nguvu. “Mbona hujibu?” “Hilo mbona kila mtu alishalielewa. Hata nikiwa na Grace mahali inabidi anirudishe haraka nyumbani kabla ya saa 11 na nusu jioni. Kila mtu ananikwepa kwa masharti yako, Geb!” Geb akacheka.

“Unafikiri nivizuri? Unakuwa mkali kwa kila mtu! Utafikiri wanaenda kuniuza kwa wanaume wengine wakati ni ndugu zako!” “Mama na Grace wanashuguli nyingi sana wale. Hutaweza. Kila weekend wanashuguli! Mara Kitchen party, sijui wagonjwa hospitalini. Mambo kibao. Hapana. Nimewaambia mara moja moja tena iwe muhimu.” “Sawa baba.” Nanaa akaitika na kulala vizuri.

          “Lakini Geb, Nataka kukuhakikishia swala la Malii. Tafadhali usiwe na wasiwasi juu yangu. Japo anaonekana anania na mimi, lakini naomba uniamini. Hakuna kilichotokea na sita…” “Kipo kilichotokea Nanaa. Naomba tusikatae ukweli. Malii alikuchukua ukiwa na mimi. Mkatafuta sehemu ya siri ya kwenda kufanya naye mapenzi. Mkaishia kukiss. Hilo sitalisahau na wala sitalipuuza. Malii amembusu na kumkumbatia mke wangu. Ndilo nitakalobakia nalo. Awe alitumia kigezo kuwa sikutaki kimapenzi au la. Lakini ujue wazi, alifanya kusudi akijua ukweli na ndio maana alirikodi mazungumzo yetu na kukukataza usiseme.” Geb akasimama.

Akamfunika Nanaa shuka vizuri. “Na kuthibitisha hilo, ndio maana anahangaika na wewe mpaka leo. Malii ni mpinzani wangu wa wakati wote. Wala hataishia kwako.” “Kwa hiyo unanilaumu?” Geb akanyamaza. Nanaa akapata jibu lake. “Naomba unisamehe Geb!” Geb akamtizama. “Nisamehe. Na ninakuahidi hakuna kitu kingine nitakachofanya kwa siri tena. Nakuhakikishia Geb. Mimi sina tabia yakutoka nje ya mahusian..” “Nanaa! Naomba uishie kwenye msamaha tu. Basi.” “Lakini..” Nanaa akaona anyamaze tu, akubali yaishe.

“Basi Geb. Nimekubali kosa. Nilienda kwa Malii, huku nikijua kile kinachoendelea kati yetu, japo hatukuwa tumezungumza. Lakini nilijua hisia zako kwangu. Naomba nisamehe, na ninakuahidi na kwa msaada wa Mungu, sitarudia tena.” Akamuona kidogo ametulia. Geb huwa hakubali kushindwa na chochote maishani. “Nisamehe Geb. Nilikosa.” “Basi, yamekwisha.” Geb akajibu. “Yameishaje?” Akanyamaza. “Mbona huniambii kama umenisamehe?” Nanaa akalalamika. “Sasa mbona unalazimishia majibu unayotaka wewe, Nanaa? Wewe umeomba msamaha. Nimekusikia na kukwambia yameisha. Naomba tuache yaishe hivyo.” Nanaa akaona anyamaze tu. Alimfahamu Geb. Akajiingiza ndani ya shuka vizuri, akalala bila hata kupewa busu.

Ukweli Huwa Ni Mchungu.

Baada yakujua ukweli, kweli mambo yalibadilika. Mabusu yalikoma kati yao. Kitu kilichomshangaza sana Nanaa. Alimuona akimuhudumia vizuri. Kumletea vitu vizuri, lakini sio kumbusu. Hakuonyesha hasira wala kuzungumzia chochote. Kabla ya kwenda kazini asubuhi, aliamka na kumsaidia kumsafisha pale pale kitandani. Alihakikisha amekula vizuri ndipo alipomuacha na kwenda kazini. Wakati wa mchana alirudi na Oliva ili apate muda na mama yake. 

Nanaa alikuwa akicheza na mwanae pale pale kitandani akimsikiliza maneno mapya aliyoweza kuzungumza wakati Geb akiendelea na shuguli zake. Kama ni kupiga simu au kurudi kwenye ipad au laptop yake na kufanya kazi baadhi humo mpaka jioni anapomrudisha Oliva nyumbani. 

Usiku alikuwa akirudi akiwa ameshaoga na vyakula ambavyo anajua Nanaa anapenda. Na baadhi ya DVD ambazo anajua Nanaa angefurahia usiku huo na kesho yake anapomuacha kwenda kazini. Wataangalia hizo movie usiku. Atamfunika tu, nakujirudisha kitini kuendelea na shuguli zake mpaka analala. ~~~~~~~~~~~~~~

Juma moja lilishapita tangia Geb abadilike. Hofu ikaanza kumuingia Nanaa. Ile midomo aliyokuwa na hamu ya kuinyonya akigugumia kama anakula pipi, aliikwepa kama sio yeye. Hakuendelea kuzungumzia habari za harusi wala hakuwa amemuona mtu yeyote kutoka nyumbani kwa kina Geb. Ila kaka yake alishapita hapo mara kadhaa. Akiwa anaelekea kazini na jioni alimpitishia vitu vidogo vidogo vyakula.

Kwa kuwa Geb alisema yameisha. Na Nanaa alimjua Geb, akisema jambo amesema. Hakutaka kurudia yale mazungumzo na kumuhoji kama bado anahasira. Alishindwa kudai mabusu, kwani Geb alionyesha wazi hahitaji busu lolote. Alizungumzia mambo ya kawaida kabisa, zaidi watoto wake hao wawili Nanaa anaomzalia. Alimuonyesha Nanaa video alizokuwa akimchukua Oliva akifanya mambo mapya kila siku na kumuonyesha kumfurahia binti yake. Alimwaga sifa za Oliva pasipo kuchoka. Hapakuwa na mazungumzo ya mapenzi kati yao. Ilikuwa ni kula na kuangalia movie basi.

~~~~~~~~~~~~~~

 Wasiwasi ukazidi kumtesa Nanaa. “Kuna kuolewa kweli hapa!” Nanaa akawaza nafsini mwake. “Au ndio nitaishia kuzalishwa tu?” Ndio swali lililozidi kumuumiza Nanaa. “Au anaona kinyaa baada ya kumwambia Malii alinibusu? Maana tangia nimwambie hivyo, hajanibusu wala kunikumbatia tena!” Machozi yakazidi kumtoka Nanaa kila anapokuwa peke yake, asijue wakumuuliza. Mwanzoni yeye ndio alionyesha hayupo tayari, Geb akabembeleza. Safari hii uliwekwa ukimya wa namna yake. Zilikuwa habari za watoto tu. Mama G wakumuuliza hakuwepo asubuhi wala mchana.

~~~~~~~~~~~~~~

Uzalendo ukamshinda, mwishoe akaona aulize tu. “Mbona mama na Grace hawaji kuniona?” Nanaa akauliza usiku huo wakati Geb alipoingia. Alisubiri mpaka akachoka. Ilikuwa siku ya ijumaa. Hakuletewa mtoto. Geb alimuaga asubuhi na kumwambia siku hiyo atakuwa busy sana. Ila atarudi usiku. Arudi mchana. Akamletea ice cream, akionyesha anaharaka. Hata hakukaa sana, akatoka wakati Nanaa anakula. 

Alirudi usiku huo akionyesha amechoka sana. Alionekana alitokea nyumbani, kwani alinukia vizuri. Kuonyesha alishaoga na yupo tayari kulala. Nanaa alibaki akimtizama. “Kwanza umeshindaje?” “Vizuri. Nimelala siku nzima.” “Afadhali. Magesa ameshalala?” Geb akauliza huku akisogelea tumbo la Nanaa. “Alikuwa akicheza hapa muda sio mrefu. Naona na yeye amemsubiri dad mpaka amechoka.” “Nilikuwa na siku ndefu sana leo.” Geb akambusu tumboni na kupapasa taratibu tumbo la Nanaa.

“Nina hamu na mama!” Nanaa akarudia. “Niliwaambia wakuache upumzike, kama ulivyokuwa umeomba.” Geb alijibu na kujirudisha kwenye kiti. “Ilikuwa ni kwa kipindi kile tu!” Nanaa akajitetea kidogo. “Basi kama unataka waje, nitawaambia ili kesho waje kukuona.” Nanaa akanyamaza kwa muda. 

 

“Wamefanya ultrasound leo.” “Daah! Nimepitwa. Magesa anaendeleaje?” Geb akauliza. “Daktari anasema anaendelea vizuri. Namshukuru Mungu nimebakiza siku 12 tu. Nimeshachoka kukaa hapa.” “Naelewa. Kukaa sehemu moja inachosha. Pole.” Geb akajibu hivyo tu. Akatulia kidogo. “Kwa hiyo maji hayatoki tena?” Akauliza tena Geb. “Nilisahau kuuliza. Lakini ni kama alisema yapo maji yakutosha kumuweka mtoto kwa hizo siku 12.” “Afadhali. Basi tuombe halafu tulale. Nimekuwa na siku ndefu sana. Nipo hoi.” “Pole.” Nanaa akaongea kwa kunyongea. Akionyesha kukosa raha kabisa.

Wakaomba kwa pamoja. Geb akamshukuru Mungu kwa ripoti nzuri aliyopewa na daktari. Akamuombea mtoto wake huyo Magesa. Kisha akamuombea na Nanaa huku akiwa amemshika mkono, yeye amepiga magoti pembeni ya kitanda. Akamuombea na kumbariki Nanaa. Ndipo akamuombea na Oliva huku akimwaga sifa za huyo mtoto mbele za Mungu kana kwamba Mungu hamfahamu huyo mtoto. Akamsifia na kumuombea. Akamaliza. 

“Asante kwa maombi mazuri.” Nanaa alishukuru wakati Geb akisimama. “Na mimi nakushukuru kwa kulipa garama ya kuwa hapa kama kifungoni kwa ajili ya mtoto wangu. Unajua ndio mbeba jina la Magesa?” Nanaa akacheka kidogo. “Huwa namfikiria baba yangu. Nasema angekuwa hai, angekuthamini sana. Aliniambia alisharidhika na watoto wake wakike. Hakutegemea kama Mungu angemzawadia mtoto wa kiume wa kuendeleza jina lake. Alijua angekufa, halafu jina lake lingepotea tu. Hapo ndipo nilipojua ni kwa nini alikuwa akizungumza sana na mimi.” Geb akarudi kukaa.

“Alikuwa akinifundisha mambo mengi sana mpaka nilikuwa nashangaa. Ni kama alitaka aache picha yake halisi hapa duniani. Japokuwa tulikuwa watoto wa nje ya ndoa, lakini alijitahidi sana kuwekeza kwangu. Nilikuwa mdogo kuliko wote, lakini alikuwa akinihusia mambo mengi kana kwamba sitamuona tena kesho yake. Hakuwahi kuniona mimi ni mtoto. Grace ndio alikuwa kiziwanda wake, mpaka mama alikuwa akinihurumia. Siku ambazo nilikuwa siendi shule, alikuwa anakuja kunifuata pale kwa mama. Alfajiri sana. Tunaenda kwenye kazi zake. Halafu alikuwa mtu wa kazi za mikono sana. Basi nitakuwa naye huko mpaka jioni, ndipo ananirudisha kwa mama.” “Kumbe ndio maana unafanya sana kazi!?” Geb akacheka.

“Sijui maisha ya kubahatisha. Yule Mzee aliniambia bahati zangu zote, zitakutana na juhudi zangu. Akaniambia nimfundishe na Magesa hivyo hivyo.” Nanaa akashangaa sana. “Haiwezekani Geb! Yaani baba yako alikwambia jina la mtoto wako wa kwanza wa kiume!?” “Kabisa Nanaa. Ndio maana nilikuwa makini sana katika swala la kuzaa. Sikutaka kuzaa hovyo. Baba aliniambia mtoto wangu wa kiume wa kwanza, nimpe jina la Magesa. Hao wengine nipo huru kuwaita majina nitakayo. Akamuombea kabisa. Na akaniambia nimfundishe katika misingi ya kimungu. Aliniambia siri ya mafanikio yote ni kwenye kanuni za kibibilia. Alikuwa akifanya kazi huku akitumia maandiko ya kimungu. Yule Mzee alikuwa akifanya kazi Nanaa! Hujawahi ona. Na alikuwa na bahati sana. Hakuna alichofanya asifanikiwe.” “Unahisi ndipo uliporithi?” Nanaa akauliza na kumfanya Geb acheke kidogo.

“Sijui! Labda.” Geb alijibu huku akicheka. “Sema ukweli.” “Kwa kweli siwezi kulalamika au kukufuru. Naona mkono wa Mungu katika kila eneo la maisha yangu. Wakati mwingine najiambia labda kwa kuwa nafanya kama baba alivyonifundisha! Sijui!” “Ndio unafanyaje?” Geb akacheka tena. “Leo una maswali!” “Nataka kujua.” Nana akasisitiza. 

“Sio vitu vigeni. Ni zile zile kanuni ndogo ndogo tu za maisha zinazojulikana na kila mtu. Lakini huwa ni rahisi kuzipuuza. Sasa hizo baba alinifundisha na kunisisitiza nisijaribu kuzipuuza hata mara moja.” “Zipi?” Nanaa alizidi kuuliza. “Moja wapo aliniambia hakuna pesa ndogo. Milioni moja haikamiliki bila shilingi moja. Akasema kama ninajiwekea malengo ya kuwa kila mwaka niwe na kiasi fulani cha pesa. Tuseme, milioni 50. Aliniambia kila mwanzo wangu wa mwaka nitakaochagua mimi. Sio lazima ikawa mwezi wa kwanza. Hata kama nikisema nafunga mwaka kila mwezi wa sita. Lakini lazima niweke malengo ya kiasi cha pesa ninachotaka nifunge nacho mwaka.” Geb akaendelea.

“Akasema. Kama nitataka kufunga mwaka na milioni 50, lazima ndani ya huo mwaka niheshimu kila senti na kuitafuta kwa bidii. Hata kama itakuwa ni biashara ya kuuza karanga stendi ya daladala, nihakikishe ninauza kwa bidii, ili nipate hiyo shilingi moja ya kukamilisha malengo ya milioni 50. Akaniambia nisiwahi kuridhika kuvuka mwaka kama sijatimiza malengo. Hata kwa kupungukiwa na hata shilingi moja. Akasema huko ni kushindwa, ambako kutakaribisha kushindwa kwenye mambo mengi zaidi.” Nanaa alibaki ametoa macho. Ndipo akajua siri ya Geb.

“Kumbee!” Geb akacheka baada ya Nanaa kuhamaki. “Lala Nanaa. Acha kupenda stori.” “Ndio maana watu wanakuita mfanikiwa! Kumbe unasiri hivyo! Kesho niambie nyingine.” “Nyingine ya mwisho, aliniambia, nisilale hata dakika moja, kama sijatimiza malengo ya siku hiyo. Lazima kila siku iwe nimejipangia malengo yangu ambayo nihakikishe ninayatimiza. Nisilale mchana au usiku, kama zijatimiza malengo ya siku hiyo. Lasivyo nikukaribisha kushindwa. Inamaana malengo ya siku hiyo, yatakutana na malengo ya kesho. Yataenda kujilundika mpaka yatafika ya mwaka mzima. Ndipo kupuuza kutakapoingilia kati maana itabidi kuyaacha ya jana ili nifanye ya leo. Halafu nitashindwa kuweka malengo mapya sababu ya kupambana kukamilisha malengo yazamani. Wakati kila siku Mungu anayotupa, baba aliniambia inakuwa ni mpya. Kila siku Mungu anaweka baraka mpya. Siwezi kutembea na malengo ya jana kwa kutumia baraka za leo. Nitashindwa vibaya sana.” “Magesa unasikia mwanangu?” Nanaa akajishika tumbo. Geb alicheka sana.

“Yaani sasa hivi ndio naelewa kila kitu! Ujue una mambo yako Geb wewe! Mpaka Grace anakuita mkoloni. Unakanuni ambazo utafikiri Mzee! Ukiamua jambo umeamua.” “Kwa kuwa sikurupuki Nanaa. Na hilo baba alinitahadharisha. Kutokuyumbishwa na matukio.” Nanaa alimwangalia Geb hakummaliza. “Kwa hiyo na huyu Magesa atakuwa kama wewe?” “Zaidi ya mimi. Ataijua bibilia zaidi yangu. Kama babu yake alivyoniambia. Atatembea katika neno mchana na usiku.

Namuombea uzima na roho ya utii. Mambo mengi nimemwandikia. Akikua na kuweza kusoma, atakutana na wosia wa babu yake. Nimemuandikia mambo mengi sana. Yale aliyoshindwa babu yake, alisema nimwambie ili na yeye asije pita huko.” “Geb wewe!” “Kweli tena. Mimi ni mjumbe tu. Napitisha ujumbe kwa vizazi vya Mzee Magesa.” Geb alijibu huku akicheka.

“Umenifanya nijisikie wa muhimu! Kumbe nimebeba kitu cha maana hivyo!” Nanaa aliendelea kujipapasa tumboni. Geb akacheka. “Ndio maana ulivyonifukuza siku ile nilishindwa hata kulala. Lazima huyo azaliwe mimi nikiwepo. Mbeba ukoo huyo!” “Sasa mama yako anajua?” Nanaa akadadisi. “Kwa sehemu. Yale baba aliyokuwa akimuhusia juu yangu. Hasa shule. Alimwambia ahakikishe nasoma kwa garama yeyote ile. Halafu ahakikishe nakua kanisani. Alimwambia nimebeba ujumbe wa muhimu sana. Lazima ahakikishe sipotei.” Geb akacheka kama anayefikiria.

“Unafikiri mama alikuwa anafurahia maisha ninayoishi na wanawake pale ndani? Hasa Liz? Hata kidogo. Mama anampenda Yesu, Nanaa. Anajua ninaishi maisha ambayo hayampendezi Mungu. Lakini anasema ni afadhali nimlete msichana pale ndani ili awe anamfahamu, kuliko niishie nao nje. Alikuwa akitaka kumjua kila mwanamke ninayekuwa kwenye mahusiano naye na alijitahidi kumfahamu huyo binti mpaka kwa wazazi wake. Anasema ni kwa faida zake mwenyewe. Kwa hiyo ilinifunga nisiwe natembea hovyo na wanawake. Kwa kuwa inabidi mama ahusike. Ni Liz tu ndio walishindwa na mama. Lakini wengine wote walikuwa karibu na mama.” “Wa ngapi?” Geb alicheka sana. “Usiwe na wasiwasi. Hakuna msafara mrefu sana. Ila wewe ndio kiongozi wa wote, mbeba ukoo.” Nanaa akaguna.

 Jumamosi.

Ilikuwa siku ya jumamosi walipoamka baada ya maongezi marefu ya usiku uliopita. Geb akimuelezea Nanaa juu ya baba yake. Alimsaidia Nanaa kuoga, lakini pale pale kitandani kama alivyokuwa amefundishwa na manesi. Akambadili nguo, akaruhusu manesi waingie wabadili mashuka, wakabaki wamekaa wakizungumza. Bado hapakuwa na mabusu wala mambo ya mapenzi kati yao.

Mama G, Oliva, Grace na familia yake wote wakaingia. Nanaa akajikuta machozi yanamtoka. “Mlinisusa.” Akalalamika. “Wala sio sisi. Geb alipiga marufuku kila mtu. Akasema tusije, wala tusikupigie simu.” “Simu yenyewe alishachukua.” Nanaa aliongeza huku akifuta machozi. “Haya. Kumbe unajua? Basi Grace akamwambia, kama hataki upigiwe simu, akifika hapa yeye apige tukusalimie. Kama unavyomjua Geb, akajibu ‘inategemea’. Na nini? Hakusema. Tukabaki tunasubiri. Jana usiku kanitumia ujumbe kwamba leo tunaruhusiwa kuja kukuona.” “Tena mimi kaniandikia kwa msisitizo,  ‘kwa muda mfupi’.” Grace akamkatisha mama yake. Nanaa akacheka. 

“Hata mimi nimeambiwa naruhusiwa kuja, lakini ni kwa muda mfupi. Nikampigia simu Grace, nikamwambia leo tuamkie hapa hapa hospitalini. Asubuhi tuwe tumefika kabla madaktari hawajapita.” Mama G akamaliza huku anaweka vitu chini. Nanaa akacheka, Geb alikuwa kimya kama hazungumziwi yeye. Alishamchukua mtoto wake.

“Mbona huyu anasinzia!?” Geb akauliza. “Hujanisikia? Nimekwambia tuliamua kuamkia hapa. Kwani huu ndio muda wa mwanao kuamka?” Mama yake akamuuliza. “Liv kwa kupenda usingizi!” Nanaa akaongeza. “Hapo nimemuogesha huku amelala. Na ameshindwa pia kula.” “Basi mlete nimnyonyeshe.” “Ndio atalala kabisa.” Bibi yake aliongeza huku akienda kumchukua kutoka kwa Geb ili amkabidhi mama yake.

“Nina hamu na wewe Liv! Jana hukuja kuniona.” Nanaa alilalamika. “Nilimvalisha na kumwandalia begi lake kabisaa. Baba yake ndio hakutokea. Na mimi kumleta nikaogopa nisije nikamkorofisha mtoa masharti.” “Nilikuwa na kazi nyingi sana jana.” Geb akajibu. Nanaa akajifunika nakuanza kumnyonyesha mwanae.

“Mbona Fili wangu leo hana raha?” Fili alikuwa ametulia sana, kitu ambacho si kawaida yake. “Danny huyo!” Nanaa akacheka. Alimjua Fili na baba yake. “Nisalimie Fili kipenzi changu.” Fili akaanza kulia. “Njoo mwaya. Panda hapa kitandani ulale na mimi. Nyamaza mtoto mzuri.” “Wakati mwingine masikio yake huyo anayahamishia miguuni.” Danny aliongeza. “Njoo Fili.” Fili akamwangalia baba yake kama anayeomba ruhusa. “Nenda sasa. Unaniangalia nini?” Fili akaenda kupanda kitandani kwa Nanaa. Akajilaza vizuri kwenye mto. “Mfunike mama. Anaonekana ana usingizi.” Bibi yake akamfunika. 

“Basi ndio haya tuliyokuwa tunakatazwa kuja hapa. Sasa na huyu naye atakutwa amelala hapa hapa!” Grace akaongeza. “Na Liv naye akilala, nitamlaza hapa hapa.” “Na wewe?” Mama G akauliza. “Nitalala pembeni yao.” “Hata hivyo hawatakaa muda mrefu.” Geb akaongeza, mama yake akaguna. “Bwana waache. Ninahamu na nyinyi kweli! Mlienda kwenye kichen paty ya Suzy?”  Nanaa akauliza. “Mama wewe umepitwa! Ilikuwa si mchezo. Muulize Grace. Tuliserebuka mpaka Grace akanitoa pale mbele.” Nanaa akaanza kucheka. 

“Yaani mama! Utafikiri ndio alikuwa mama yake bibi harusi!” Grace aliongeza. Nanaa akazidi kucheka. “Ngoja nikuonyeshe picha.” Mama G akatoa simu. Nanaa akaanza kuangalia huku Liv ananyonya ndani ya mtandio ambao Nanaa aliozoea kumfunika wakati akimnyonyesha, huku wamelala pale pale kitandani. Fili pembeni, Oliva kati kati na Nanaa pembeni. “Mlipendeza!” Nanaa akasifia.

Maji Yametibuka.

Mara wakaingia James na Malii pamoja na mkewe. James na Malii walikuwa wakicheka. Nanaa akawaangalia kidogo tu akarudisha macho kwenye simu. Wakasalimiana. “Mbona midomo imekukauka mwanangu?” Mama G alimuuliza mke wa Malii. “Mama wewe!” Grace akashituka sana. “Nauliza tu. Mimi ndiye mama yake Malii. Sasa kama ameanza kumnyima chakula, aniambie nimuweke Malii sawa.” “Hapana mama. Unajua ulinilea vizuri. Siwezi kumnyima mke wangu chakula.” “Mbona unamjibia wakati nimemuuliza yeye? Eti mama?” Mama G akasisitiza swali lake. “Hapana mama. Nakula.” Alijibu na tabasamu la kinyonge. 

“Au mambo tayari?” Mama G akauliza tena. “Mama Magesa Wewe!” Grace akashangaa kwa kushituka. “Bwana wee! Kila mtoto anakuja na vyake. Kuna mimba nyingine zinakuja hutaki chakula kabisaaa.” “Sio Nanaa.” Danny aliongeza na kufanya wote wacheke. “Maana mjamzito huyu na msosi! Hatari.” “Naomba niache Danny. Mwenzio ni mjamzito.” “Basi ndio sababu yake hiyo! Ngoja ujifungue tuone.” “Si nitakuwa nanyonyesha! Lazima kula chakula kingi!” Kila mtu alicheka zaidi. “Basi sababu hazimwishi. Hajali wembamba wala unene. Namwambia unatakiwa kuwa model, msichana mwembamba. Lakini wapi! Hapo James una dada!” James alikuwa akicheka tu huku akimwangalia dada yake.

“Kwanza hapa njaa inauma. Kaka mtu anakula huko ndani, na dada yake anakula hapa nje. Mimi wembamba huo naupatia wapi!?” “Kula mwanangu. Ushakuwa mama. Utapungua wakishakua hao. Sasa hivi hakikisha wanapata chakula chakutosha. Mambo ya diet mpaka wajukuu zangu wakue.” “Ndio maana nampenda mama yangu. Haya, nimiminie uji basi.” Kila mtu akacheka.

“Na wewe mama unywe kidogo. Naona hujala bwana.” Mama G akimaanisha mke wa Malii. Akamkabidhi kikombe. “Hapana mama. Mimi nipo tu sawa. Mwachie tu mgonjwa.” “Huyo sio mgonjwa. Wewe kunywa tu. Upo mwingi. Kaa hapo ule bwana. Utasimamiaje harusi ukiwa kama mgonjwa? Kula kidogo angalau umfikie mwili bibi harusi wako.” Mama G akasistiza. “Heri upokee tu. Mama hajui jibu la hapana. Pokea tu unywe.” Mke wa Malii akapokea huku akicheka.

 “Hayo ndio mambo. Kula ili kwenye harusi na wewe utokee mwanangu. Watasema unateseka kwenye ndoa bure.” Mama G akasisitiza. “Hawatasimamia tena harusi yetu.” Geb aliongeza na kufanya kila mtu amgeukie. “Unamaanisha Malii na mkewe!?” Mama yake akauliza. “Si ndio hao tuliokuwa tumewaomba wasimamie harusi yetu! ” Geb akajibu, tayari hasira zilionekana kumpanda. Hakuwa ameongea neno lolote tangia  kina Malii wanaingia hapo, wala hakuwasalimia.

 “Kwa nini!?” Malii akamuuliza Geb kwa mshangao. “Kwa sababu mimi nimesema hivyo.” Alijibu kwa jeuri, kila mtu aliona na kushangaa. Alijawa na hasira za gafla. Nanaa ndipo alipoiona hasira ya Geb waziwazi. Akanyamaza na kuendelea kuangalia picha kwenye simu ya mama G. Bado walikuwa wakimwangalia. Akarudisha macho kwa mama yake aliyekuwa bado amekodoa macho. “Sasa ni nani anasimamia?” Mama yake akamuuliza na kumwangalia yeye na Nanaa kwa zamu. Alipoona hata Nanaa hamtizami, akajua kuna jambo la ziada na hatajibiwa tena. Alishaishi na baba yake Geb, kwa hiyo kwa kumtizama tu Geb, akajua amekasirika sana na hataongea tena. Akageukia upande mwingine, na Geb akainamia simu yake. Pakazuka ukimya wa gafla.

“Vipi mtoto na wewe mwenyewe?” James akabadilisha mazungumzo. “Naendelea vizuri. Jana walimwangalia mtoto. Wanasema mrefu kweli!” James akatabasamu. “Ila hajambo?” “Hajambo kabisa. Hapa anacheza. Na siku hizi akigeuka hata kama upo usingizini utaamka tu.” “Unapata maumivu?” Mama G akauliza. “Sana mama.” “Umemwambia daktari?” “Ndio maana ikabidi kuangalia tena. Wameniambia kila kitu kipo sawa, ila napata maumivu sababu mtoto ni  mkubwa sana.” “Hata hivyo siku zimebaki chache. Jikaze mwanangu. Tunakuombea.” “Asante mama.” Pakazuka ukimya mwingine.

Geb akasimama na kutoka upande wa barazani. Malii akamfuata. “Vipi!?” Wakamsikia Malii akiuliza. Kimya. “Mbona unabadilisha mambo kienyeji? Ni jana tu James ametoka kuzungumzia swala la sisi kusimamia harusi hapa hospitalini. Mimi na mke wangu tukakubali. Leo unasema hatusimamii tena harusi! Halafu hutaki kutoa sababu? Ni nini?” Kimya. “Geb!” “Usiniguse tafadhali.” Wakamsikia Geb akijibu. “Kwa nini unanipuuza? Nakuuliza hunijibu, ni kama hunisikii!?” “Kwa kuwa unarudia maswali ambayo nilishajibu pale ndani.” Geb akajibu, mama yake akasimama kwa haraka akatoka nje kuwafuata pale barazani.

“Malii! Naomba utulie kwanza.” “Hapana mama! Geb ananidharau. Iweje jana James aniambie tusimamie hapa hospitalini, halafu leo Geb anifanyie hivi? Tena kwa kiburi! Yeye mwenyewe na Nanaa ndio waliotufuata kutuomba. Leo analeta jeuri!? Kwa nini anatufanya sisi kama watoto wadogo? Anatuzungusha vile atakavyo!”

James akatoka. “Jamani naomba mnisamehe. Mimi nilizungumza na Malii bila kuwasiliana na Geb mwenye shuguli. Kwa hiyo Malii, naomba unisamehe bwana. Kama kuna garama yeyote mliingia, mimi nitalipa.” “Kwa nini unafikiria swala la pesa tu na kuondoa ubinadamu? Kwani kinachomshinda Geb kutuambia sababu ni nini?” “Jamani nashauri mtulie. Geb ameshajibu kwamba ameamua hivyo. Kwa kufanya fujo hapo, wala haitasaidia kubadili jibu lake. Nashauri Malii uliache hilo jambo liishie hapo.” “Hapana mama. Huko ni kumwendekeza Geb. Hiyo ni dharau.” Malii aliendelea kulalamika.

Geb alikuwa ameshageukia upande wa bustanini. Akionekana pale alishahama wala hasikilizi tena. Malii alimtizama kwa hasira. “Usije wahi kunitafuta tena. Leo iwe mwisho.” Malii alitoa onyo kali. Hata Geb hakujisumbua kumtizama. Alimuonyesha jeuri na kana kwamba hilo onyo ndio kitu alitamani kitokee kati yao. 

Akarudi ndani kwa mkewe. “Twende.” Malii alimuongelesha mkewe kwa jeuri. “Wewe tangulia na gari yako. Mimi namalizia kunywa uji.” Kila mtu akashangaa.

“Sasa unaniangalia nini? Wewe umekuja na gari yako. Umeniambia mimi nipande daladala, nikufuate hapa. Kwa nini kunitoa hapa kwa hasira wakati hata usafiri hatutumii pamoja! Mimi siondoki sasa hivi. Nasubiri fujo za daladala zipungue na jua litulie, ndipo nitarudi nyumbani.” Kila mtu akabaki anashangaa. Mkewe akaendelea kunywa uji wake taratibu.

Malii akabaki bado amesimama. “Hakika mimi siondoki sasa hivi. Wewe tangulia tu. Hapa nilipo nimechoka kwa kutembea. Unataka nitoke tena hapa nianze kutembea wakati mimi ndio nimefika! Hata Malii! Acha nipumzike. Kwanza huwezi jua, naweza nikabahatika lifti hapa hapa, nikasogezwa hata karibu ya kituo cha daladala kama sio nyumbani kabisa.” Walizidi kushangaa. Malii alikuwa na usafiri. Iweje watoke nyumba moja, halafu mkewe atembee wakati Malii alikuja na gari!

James aliyeingia nao akabaki ametulia pale nje. Alimkuta Malii amekaa ndani ya gari, mkewe yupo nje ya gari. Akasema ndio amefika. Kwa haraka James akajua ndio wote wamefika, maana hata Malii alisema ametokea nyumbani. “Malii mwanangu, mimi nitakusaidia kumrudisha nyumbani. Mwache azungumze na wenzie na amalizie huo uji.” Mama G akaingilia. Malii akatoka. Mkewe akaendelea kunywa uji taratibu kama hamna kinachoendelea.

~~~~~~~~~~~~~~

Madaktari waliingia nakukuta kitandani kwa mgonjwa, wamejaa watoto. “Unaendeleaje Nanaa?” Daktari wake, Lyamu, alimuuliza baada ya kusalimiana na kila mtu. Geb aliposikia sauti ya dokta Lyamu, akaingia ndani. “Naendelea vizuri.” Nanaa akajibu kinyonge huku ameangalia chini. Dokta Lyamu aliyemzoea Nanaa mcheshi akaona mabadiliko. Akavuta chati ya Nanaa na kuanza kusoma. “Naona tangia nikuache jana, mambo hayajabadilika. Pressure ipo vizuri, hata ya asubuhi imeonyesha vizuri.” Daktari aliongea huku akiendelea kusoma ile chati ya Nanaa.

          “Endelea kupumzika na kujtahidi kunywa maji mengi.” “Sawa.” Nanaa akajibu. “Naomba nikupime tena kidogo kabla sijaondoka.” Daktari akamsogelea. “Ngoja nimtoe mtoto.” Geb akasogea pale kitandani ili kumtoa Oliva. “Bado dada ananyonya vizuri?” Daktari akauliza. Alikuwa ni daktari wake Nanaa tokea ni mjamzito wa Oliva. “Zile siku tatu za kumwachisha ili kaka yake anyonye peke yake sijui kama itawezekana. Ananyonya kama mwenye njaa ya mwaka mzima!” Lyamu akacheka. “Ndio vizuri. Bado anahitaji maziwa.” Geb akamtoa Oliva na kwenda kumfunga kwenye kiti chake. “Ngoja nimtoe na huyo kaka yake.” Danny akasogea. “Hamna shida. Hapo alipo hanizuii.” Daktari Danny kumtoa mtoto.

Nanaa akatoa mkono, daktari akapima. Watu wote wakiwa wamenyamaza kabisa wakimwangalia daktari. Wakamuona amekunja uso. Akamtoa kile kipimo. Akaminya mkono wa Nanaa kidogo, na kurudishia ile mashine tena. Akapima, wakamuona amekunja tena uso.

“Usiogope, mimi nitakuwa sawa.” Nanaa alisikika akimwambia daktari. “Vipi?” Geb akasogea. “Usifanye mchezo Nanaa!” Daktari akasisitiza. Nanaa akanyamaza. “Umekula ng’ombe mzima, umebakisha mkia tu. Sina dawa nyingine ya kukupa, lasivyo itabidi tumtoe huyo mtoto. Hata hivyo ameshakomaa.” “Nimekwambia usiogope. Hizo siku 11 tulizobakisha na huyu kaka, zitafika tu.” Nanaa alisisitiza huku akishika tumbo lake. “Kwani pressure ikoje?”  Geb akauliza tena. “Ipo juu sana. Yaani imerudi vilevile! Lakini kwa sasa, huyu mtoto ameshakomaa. Ni heri atolewe tu. Jana nilimwangalia, ni mtoto anayeonekana ana nguvu. Kumuacha huko ndani ya mama yake, ni kuhatarisha maisha yake bila sababu. Tafadhali zungumza na Nanaa. Hamna sababu ya kumuweka huyo mtoto huko. ” James akaingia akamsogelea Nanaa.

Mipango Ya Mungu Si Ya Wanadamu.

“Vipi?” Kaka yake akamuuliza. “Nataka kwenda chooni. Naomba nisaidie nisimame niende chooni.” Akimaanisha kutaka msaada wa kutolewa Fili pale kitandani ili atoke. Danny akaenda kumtoa mtoto pale kitandani, Nanaa akashusha miguu kitandani. Akasikia kichomi kikali sana kinapita tumboni. Akakunja uso huku ameshika tumbo. “Vipi mama?” Mama G naye akamsogelea kwa haraka na Geb pia. “Kimepita kichomi hapa.” Nanaa akaonyeshea tumboni kwake. “Pole. Kimepita?” Geb akauliza huku akijaribu kumshika tumboni. Nanaa akabaki amejishikilia tumbo. “Ngoja niende chooni.” Akasimama.

Aliposimama tu, maji mengi sana yakamwagika. Chupa ikavunjika. “Haa!” Nanaa akashangaa, na kumwangalia yule daktari. Kama aliyechanganyikiwa yule daktari akabonyeza kengele kuita manesi. Akapiga simu chumba cha upasuaji kwa haraka. “Nakuja na mama mzazi. Hawezi kuzaa. Pressure ni 170 kwa 110. Naomba mniandalie kila kitu. Nakuja sasa hivi.” Tayari manesi walishafika. Wakamrudisha Nanaa kitandani. 

“Nimeingiwa na hofu. Mtoto atakuwa salama?” Nanaa akamuuliza daktari kwa sauti ya chini kuhu akilia. “Nitajitahi wote mtoke chumba cha upasuaji salama. Usiogope.” “Kama ikikulazimu kuchagua kati yangu na mtoto, naomba iwe mtoto tafadhali.” “Nanaa!” Geb akamsogelea. “Usiogope. Kila kitu kitakuwa sawa. Umesikia?” “Nisamehe Geb. Tafadhali nisamehe mpenzi wangu. Sikukusudia kukuudhi.” Nanaa aliendelea kulia. Hakuna aliyeelewa. Tayari hofu ilishajaa ndani ya kile chumba. Hofu ya kumpoteza mtoto na Nanaa mwenyewe. “Nini kinaendelea?”  Ndilo likawa swali la kila mtu katika kile chumba kwa wakati ule.

Nanaa alikuwa akilizwa na mengi. Alihofia anaweza kwenda huko chumba cha upasuaji na asitoke tena. Hofu juu ya mwanae aliyemuhangaikia pia ilimsumbua. Pia alijua ameshapoteza penzi la Geb. Hilo ndilo lilipoteza hata ladha ya kila kitu. Alitarajia mtoto aje akiwa ameshaolewa. Lakini hapakuwa na mazungumzo tena ya ndoa. Ni week ilishapita, hajapata hata busu kutoka kwa Geb.

~~~~~~~~~~~~~~

Nini kitaendelea? Nini hatima ya Nanaa na Magesa? Pressure ipo juu sana. Na pressure ikiwa juu, mama mjamzito hawezi kuzaa kwa njia ya kawaida, kuepuka kusukuma kwa nguvu wakati pressure imeshakuwa juu.

Geb je? Siku hiyo ndipo Nanaa aliona hasira iliyokuwa imejificha ndani

yake. Hakujua kama harusi imesitishwa au la! Si mama G wala

Geb mwenyewe waliozungumzia tena swala la harusi kwa Nanaa, zaidi ya kumsikia Geb akiwakataa wasimamizi wa harusi.

Hata akipona, je bado atamuoa?

Mke wa Malii naye azua jingine jipya.

Je, ni nini kinaendelea kwa wana ndoa hao?

Usikose. Muendelezo

 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment