Akampigia
simu mama yake. “Nanaa yupo hapa kwangu. Anaomba
umletee mtoto ili anyonye.” “Nanaa anajua kuniadhibu jamani! Sasa kwa nini anisumbue mimi wakati
aliyemkosea ni Geb?” Grace akacheka. “Kwanza kaja
analia. Danny anasema amemfungulia mlango alikuwa amekaa chini, hapo nje analia
sana. Anaonekana ametembea kuanzia kituoni mpaka hapa. Halafu usiku huu!”
“Amekwambia kitu chochote?” “Wala sikumuuliza. Unamjua Nanaa. Hawezi kusema
jambo alilomuudhi Geb. Ila aliniomba nisimwambie Geb alipo. Ndio nikamwambia
nilazima kumtaarifu alipo ila nitamuomba amwache kwanza.” “Nipe nizungumze naye
mwenyewe.” “Subiri.” Baada ya muda akamsikia Grace. “Mama
anataka kuongea na wewe.”
“Mama!” Akamsikia Nanaa.
“Sasa mbona unaniadhibu mimi wakati aliyekukosea ni Geb?” Nanaa akaanza kucheka. “Mimi nimechoka bwana. Njoo unyonyeshe mwanao. Na ukichelewa utamkuta
amelala.” “Sijisikii
vizuri mama.” “Nini tena?” Mama G akauliza
kwa wasiwasi. “Sijui! Lakini sijisikii vizuri.
Halafu…” Nanaa akanyamaza akamsikia analia. “Nini Nanaa? Niambie.” “Nimejikuta
nimelowa!”
“Maji au damu?” “Maji.” “Usilie. Nakuja
sasa hivi.” Mama G akakata simu.
~~~~~~~~~~~~~
Vichomi
vilishaanza kumsumbua Nanaa tokea yupo kwenye daladala anaelekea nyumbani kwa
Grace. Alipoteremka, akaanza kujihisi kuloa. Alitembea taratibu kutoka kituo
cha daladala mpaka nyumbani kwa Grace. Haikuwa shida kupita getini. Walinzi
walimruhusu. Alishazoeleka pale mpaka akapewa chumba chake.
Alipofika
mlangoni akagonga. Danny alipofungua tu mlango, akasimama na kuacha kulia.
Akapitiliza chooni huku akimwambia Danny, “Mimi nina shida na Grace.” “Hata
mimi mzima Nanaa!” Danny akamsikia akicheka huku anafunga mlango wa chooni. Grace
alishakuwa amepanda kitandani. Akamfuata. “Naomba taulo na nguo ya kulalia.” Bila
kuuliza kulikoni, usiku huo nyumbani kwake, akamletea kila kitu kama
alivyoagizwa. Tayari Nanaa alishakuwa kwenye moja ya chumba cha wageni, ambacho
ni chake. “Naomba mwambie mama aniletee mwanangu anyonye, lakini usimwambie Geb
kama nipo kwako.”
“Geb
atakuwa na wasiwasi kama hajui ulipo, Nanaa.” Nanaa akanyamaza. “Naomba
nimtaarifu kama upo hapa, lakini nitamwambia akuache. Namjua jinsi anavyopata
shida kama haupo naye.” Nanaa akanyamaza. Grace akamuona anafuta machozi.
Akajua amemuudhi. “Nenda kaoge, halafu upumzike. Nikuletee kitu ule?”
“Hapana. Nasikia tumbo limejaa
kama linavichomi. Nataka tu kuoga na kulala nipumzike.” Grace alimjua Nanaa
mpenda kula. Kabla hajaulizwa chakula, huwa anaomba mwenyewe. Kwa kukataa vile,
akaona amuache. Akaingia bafuni, akaoga na kurudi kitandani kulala, ndipo
akazungumza na mama G, baada ya Grace kuwapigia simu.
~~~~~~~~~~~~~
Geb
akabaki amesimama pale mlangoni anamwangalia mama yake akifungasha. “Ngoja basi
na mimi nikachukue wallet mara moja, nakuja.” “Wapi?” Mama yake akasimama huku
amemkazia macho. “Si tunaenda wote kwa Nanaa!” “Geb Magesa, usinitanie wewe
mtoto!” “Sasa unafikiria nitayamalizaje kama sitazungumza na Nanaa?” Mama G
akamgeukia vizuri.
“Unauhakika
upo tayari kuyamaliza?” “Ndiyo mama.” Mama G akamkazia macho. “Nakuuliza Geb,
na nataka ufikirie vizuri. Maana mlichogombana na Nanaa si kuondoka nyumbani
bila kukuaga au akijua ulimwambia utawahi kutoka kazini ili mtafute pamoja
sehemu ya fungate. Mimi na wewe tunajua hiyo ilikuwa sababu tu ya kumkera mtoto
wa watu. Hasira zako zimebeba wivu wakuona James anafanya uliyotakiwa kumfanyia
wewe Nanaa na kutofahamu cha kufanya na mali zako ukiwa na mtu mwingine ambaye
sio hawara ni mke. Unanielewa Geb?” Mama G hakumbakiza.
“Narudia
tena, upo tayari kumtoa Nanaa kwa kaka yake na kumpa yote anayopewa na kaka
yake? Maana sitakubali umchanganye Nanaa. Nanaa si mjinga, na wala James
hatakuruhusu hata kwa sekunde moja. Mimi na wewe tunajua. Yote anayojua mdogo
wake anahitaji na kuyastahili, halafu wewe umeshindwa kumpa, ujue James
hatatulia mpaka dada yake amepata.” Mama G akaendelea.
“Sasa
je, upo tayari? Nataka unijibu kama upo tayari kuona kambi mbili humu ndani?
Wewe ukipata mapenzi na watoto, halafu James na dada yake wakiwa timu moja
wakitafuta maisha ambayo unajua James alivyo. Atakushinda tu. Na taratibu
utajikuta wewe ndio utakosa nguvu na kupoteza kila kitu. Utabakia kuonekana ni
mwanaume bahili. Likitokea la kutokea, mimi si Mungu, wewe hufahamu kesho
ikoje. Hiyo sura yako utaiweka wapi? Ulimwengu wote utakujua ulimtenga mkeo
kwenye mali zako, kaka yake akaanza kumsaidia.” Mama G alizungumza naye bila
kumficha.
“Unakumbuka
historia ya baba yako na mkewe yule wa kwanza? Sijui alikuhusia nini! Lakini
walipomfilisi na kumshitaki mahakamani. Yule mama na watoto wake, walitaka baba
yako aondoke kama alivyo. Alikuwa na pakurudia, kwangu, kwa kuwa
alihusika kujenga. Hakupata shida hata kuja kumiliki na mimi kwa kuwa
alinisaidia kujenga. Kuanzia chini mpaka nilipokuwa. Alipokuwa mgonjwa,
nilimchukua na kumleta nyumbani kwetu. Na si kwangu. Palikuwa kwetu.
Kwa kuwa aliijenga ile nyumba. Akaweka miradi na alikuwa pia akija kupakarabati,
wewe ni shahidi. Japokuwa alirudi kwa mkewe, lakini alihakikisha hakuna
linalompita kwenye maisha yangu. Tena kwa kushiriki bega kwa bega. Kama
hakuwepo yeye, basi alihakikisha ananiachia mtu anayemwamini.” Mama G
akamwangalia tena. Kimya.
“Huwa
najiuliza ni kwa nini Magesa hajakupa busara zake, amekupa hayo macho tu ambayo
hayakusaidii!” “Unanitukana mama.” Hilo ndilo tusi alilopenda kumtukana nalo
Geb, na Geb alijua huwa akifika hapo ndio amechemka, hasira ipo mpaka mwisho.
“Sasa nisikilize Geb. Narudia tena. Wewe mtoto wa Magesa, nakuonya. Tena
nakuonya sana. Usiniondolee amani na kuniharibia mipango. Mwanamke atakayeishi
humu ndani na mimi ni Nanaa tu.” “Kwani mimi nimekataa?” “Basi, kaa
chini ujiulize ni nini unataka. Na ukishapata jibu, ndipo ujue jinsi ya kuishi
na sisi. Haswa Nanaa. Unanielewa Geb?” Kimya.
“Nisikuone
unanifuata nyuma. Alikufuata chumbani ili muyamalize, ukashindwa. Sasa tulia
hapo mpaka ujue chakufanya.” “Mbona nimeshajua cha kufanya?” Mama G akajiweka
sawa. “Nakusikiliza.” “Mimi mwenyewe ndio nitamnunulia gari. Nimeshaanza
kumtafutia gari. Zuri sana.” “Geb usinitanie wewe mtoto! Mimi muda wote
niliokuwa nikiongea hapa nilikwambia Nanaa anataka gari?” “Mengine taratibu
mama! Mbona unakuwa mkali kwangu?” “Sasa ndio hivyo. Wakati wewe unajipanga,
mwache Nanaa aendelee na kaka yake.”
“Kwa
nini na wewe usizungumze naye akawa na subira?” “Aliyekwambia anashida na mali
zako ni nani? Ushamsikia Nanaa anakuulizia unaingiza kwa mwezi pesa kiasi gani?
Ushamsikia anakuulizia unabiashara gani? Au leo unataka wote tuonekane wehu
nikurupuke nianzishe kitu ambacho wala hakikuwepo kwenye akili zake?” Kimya.
“Wewe
unasutwa na dhamira yako ndio maana unahangaika hivyo! Naomba mwache Nanaa.
Wewe endelea na mipango yako kama kawaida. Na wala sikulaumu. Wapo wanaoishi na
wao kama hivyo wewe tu na maisha yanaendelea. Wake zao hawajui chochote
kinachoendelea kwenye maisha yao, na ndoa bado zipo. Ila madhara yake naona
umeanza kuyaona mapemaaa. Mke utakuwa naye humu ndani, lakini akili zipo kwa
kaka yake na wanaume wengine watakaoweza kumsaidia. Ndipo kutoka nje ya ndoa
kunapoanza hapo. Atakutana na mwanaume mwingine anayeonekana anajali ndoto zake
kuliko wewe. Anamjali na kumsaidia kimawazo. Kwa nini asimpe kidogo ambacho
anakugawia na wewe?” Kimya.
“Sasa
baki hapa, usinifuate nyuma.” “Mimi siwezi kulala humu ndani bila Nanaa.”
“Geb!” Mama yake akamuita kwa kumtahadharisha. “Katika mambo kama haya, wewe
unatakiwa uwe upande wangu mama!” “Unanipotezea muda.” Walipogeuka kitandani
alipokuwa mtoto, wakakuta Liv alishalala. “Ona sasa!” “Sasa na hapo pia kosa ni
langu!? Wewe unamjua Liv jinsi anavyopenda kulala, halafu na wewe ukamuweka
kitandani!” “Nenda Geb kabla hujaniudhi zaidi. Kama sio wewe kumkera mama yake
mpaka kuondoka, huyu mtoto angelala ameshiba. Amelala na njaa sababu yako wala sio
mimi.”
“Basi
wewe baki hapa na mtoto mimi niende kwa Nanaa.” “Geb!” “Ni wazo tu mama!” Geb
akacheka kidogo. “Sitaki mawazo yako.
Jishauri mwenyewe na balaa lako. Wewe utabaki hapa na mtoto, mimi ndio nakwenda
kwa Nanaa.” “Mwambie namsubiria tulale.” “Hakika sitamwambia. Kwanza naona akae
tu huko huko kwa Grace mpaka akili yako itakapokukaa sawa au mpaka siku ya
harusi.” “Haa! Tafadhali sana mama. Hapo ndipo utakaponifanya nitembee uchi
barabarani.” “Unatembea uchi vipi wakati unapesa za kununua nguo? Hebu nipishe
hapo mlangoni.” Akamsukuma mwanae akapita ili aondoke.
Geb
akatumia akili ya haraka kumtuliza mama yake. “Ukirudi na Nanaa leo, mzigo wa
jumamosi ijayo nitakulipia mimi. Nitamwambia dereva akushushie mzigo halafu
pesa yote namlipa mimi, Grace.” Akamuona amegeuka. Akajua tayari amenasa.
Kabla hajafikiria vizuri, akamkatalia, Geb akamchanganya zaidi. “Tena
nitawaambia wakushushie oda yako kama ilivyo, wasikupunje.” “Na sitaki mchele
mbaya kwa kuwa ni wa bure.” “Sio bure, si ndio unaenda kumleta Nanaa!”
“Usinichanganye Geb!” “Basi mama yangu. Nitamwambia akuchagulie mchele mzuri.”
“Sasa mchele tu!?” Geb akaanza kucheka huku anatingisha kichwa.
“Kweli
mama unapenda pesa!” “Sio kupenda pesa. Wewe kama umeamua kutoa hongo,
toa hongo zakueleweka sio hongo za kitoto!” Mama G alishatulizwa. “Basi
nakuongezea na lita 20 za mafuta, kama utazungumza na Nanaa swala la
kukasirika, halafu anaondoka nyumbani. Mwambie akikasirika awe anatulia
nyumbani tuzungumze.” “Unamaanisha ukimkera, asiondoke?” Geb akacheka zaidi.
“Ukitaka
nizungumze naye hivyo labda unipe lita 40 za mafuta ya alizeti.” “Mama!” Geb
akashangaa sana. “Basi utaonana na Nanaa siku ya harusi. Kwanza nataka
apumzike.” “Jumatatu nitamtuma dereva akuletee mafuta halafu jumamosi mchele.”
Mama G akageuka na kuanza kuondoka. “Hujisikii vibaya?” Geb akamtupia swali. “Hata
bibilia inasema, ‘kila mtenda kazi
anastahili ujira wake’. Wewe unaharibu, mimi nina kazi
ya kujenga. Soma bibilia wewe mtoto wa Magesa.” Mama G akajibu huku anatoka. “Usichelewe
sasa!” “Unataka kuniongezea na malipo ya kuniharakisha?” “Hapana mama. Wewe
nenda, nitasubiri tu. Utanifilisi bure!” Akamsikia anacheka huku anafunga
mlango.
Kila Kazi Na Malipo Yake.
Nyumbani
kwa Grace na Geb hapakuwa mbali sana. Wote waliishi Tabata. Alipofika, akamkuta
Grace anamsubiria sebuleni. “Nanaa analalamika vichomi, mama. Hajala.” Mama
yake akaingia chumbani. Akamkuta amejifunika. “Vipi?” “Nasikia vichomi mama. Nahisi naendelea
kuloa.” “Tuone.” Mama G akamfunua.
Akakuta ameloa. “Hii sio ishara nzuri. Twende hospitalini moja kwa moja.” Grace
akamtolea nguo, akavaa. Wakatoka Grace, mama yake na Nanaa.
Njiani
akampigia simu Geb. “Sasa sio uanze kupaniki.
Tunampeleka Nanaa hospitalini kwa checkup.” Mama
yake akaanza kwa kumtahadharisha. “Kwa nini
tena?” Geb akauliza. “Tutajua
tukifika huko.” “Hapana mama. Nataka kujua kwa nini anaenda hospitalini usiku
huu!?” “Hajisikii vizuri.” “Hilo jibu halitoshi.”
Mama G akatulia kidogo. “Mama?” Geb akaita. “Kwa nini usisubiri mpaka tumuone daktari!” “Nipe Nanaa mwenyewe
nizungumze naye.” Mama G ndiye aliyekuwa akiendesha,
akampa simu Nanaa aliyekuwa amejilaza kiti cha nyuma. “Geb anataka kuongea na
wewe.” Nanaa akafungua macho akapokea
simu.
“Geb!” Nanaa akaita. “Vipi?” Akamsikia
ameanza kulia. “Pole. Nini kinauma?” “Sijui! Lakini nasikia vichomi vikali, sijisikii
vizuri, halafu maji yameanza kutoka.” “Unamaanisha
maji ya kumtunzia mtoto!?” “Sijui Geb! Nimeona
tu naloa.” “Naomba usilie Nanaa. Tulia
kabisa. Mungu yupo na sisi. Hatuwezi kumpoteza huyo mtoto.” “Naomba uniombee.” “Nakuombea
mpenzi wangu. Pole. Kila kitu kitakuwa sawa.” Nanaa
akarudisha simu kwa mama G. “Unipigie mkishafika tu
hospitalini.” “Sawa.” Mama G akakata simu.
~~~~~~~~~~~~~
Hapo
hapo Geb akaanza kubeba vitu vya mtoto wake na kuingiza kwenye gari. Akaenda
kumtoa mtoto pale kitandani na kumfunga kwenye kiti chake kwenye gari,
akaondoka mpaka nyumbani kwa Grace na mumewe. Danny akamfungulia mlango. “Naomba
nimuache hapa Liv. Haitaji chochote ila sehemu ya kulala mpaka bibi yake
atakapokuja kumchukua. Ila hataamka mpaka kesho saa nne asubuhi kama ikitokea
bibi yake hatawahi kurudi.” “Hamna shida.” Geb akamkabidhisha kwa Danny na yeye
akatoka kwa kasi akiwahi hospitalini.
~~~~~~~~~~~~~
Nanaa
alifikishwa hospitalini mapokezi. Alipoangaliwa, ni kweli maji ya kumtunzia
mtoto yalikuwa yakitoka na presha ilikuwa juu. Wakashauriwa alazwe ili apate
mapumziko na ashushwe ile presha. Wakati anaingizwa wodini, na Geb naye akawa
ameshafika. Mama yake akamueleza kwa kifupi. Wakaelekea kwenye chumba
alichopata cha kulazwa.
“Pole
Nanaa!” Geb akarudia. “Asante. Naogopa
Geb! Itakuaje kama mtoto akitoka?” Nanaa
aliuliza huku akilia. “Nimeambiwa presha ipo juu Nanaa. Naomba uache mawazo
yatakayokusababisha izidi kupanda. Huyo mtoto hatukumuweka sisi. Aliyemuweka
atamtetea. Naomba tufanye kwa upande wetu tu. Sasa hivi wewe unahusika
kumtunza. Naomba jitahidi kwa upande wako kutulia ili na presha nayo itulie,
yeye awe salama. Hilo ndilo tunaweza kufanya kwa sasa. Basi. Sawa?” Nanaa
akatingisha kichwa kukubali.
“Bado
una mamumivu?” Geb akamuuliza huku akimpapasa tumbo taratibu. “Sio sana.” “Lakini
bado yapo?” “Kama vichomi.
Wameniambia wamempigia simu daktari wangu. Aje, na kufanya ultrasound na
mengineyo, ili kujua ni nini kinachosababisha. Ila nimemsikia nesi akisema kama
presha ikizidi kuwa juu daktari anaweza kulazimika kumtoa mtoto. Lakini sitaki
Geb. Nimebeba miezi yote hiyo nakaribia kumaliza 8, sitaki kumpoteza mtoto ambaye
hata sijamjua! Sijui kama ni wakike au wakiume! Hata sijamfurahia mwanangu!
Hapana Geb. Mimi sitaki waje wamtoe huyu mtoto.”
“Basi naomba usilie, tumwambie Mungu.” Geb akapiga magoti pembeni ya kile
kitanda huku amemshika mkono Nanaa.
“Nakushukuru
Mungu kwa heshima uliyotupa mimi na Nanaa. Si kwa kustahili kwetu ndio maana
umetupa Oliva na kaka yake.” Mama G
akafungua macho akamtazama Geb. Hakuna aliyekuwa akijua jinsia ya huyo mtoto.
Kumbe wakati wote yeye alijua jinsia ya mtoto! “Wakati huu
Magesa anahitaji msaada ambao sisi hatuwezi kumpa, na madaktari wanaonekana
kushindwa. Namuombea mtoto wangu. Nakataa kifo cha Magesa kabla hajatimiza
kusudi lake hapa duniani. Magesa ataishi aje asimulie makuu yako wewe Mungu.
Natubu kwa lolote nililosababisha mimi binafsi mpaka kufikia hapa. Nakataa roho
ya uharibifu. Natakamka uzima juu ya mtoto wangu. Nakiri kuwa Magesa ataishi
wala hatakufa. Najua uweza ulioweka kwenye damu yetu. Kwa kuwa na yeye amebeba
damu yangu, ninaamini uliweka uwezo wa upambanaji ndani yake. Atapambana na
hali yeyote inayomkabili sasa.”
“Nakuamuru
Magesa, utulie mpaka siku zako za kukaa tumboni mwa mama yako zitakapotimia.
Hutatoka sasa hivi ili utunzwe kwenye vyombo vilivyoumbwa na kazi ya mwanadamu.
Utakaa pale Mungu alipokusudia ukae kwa miezi 9 kamili ndipo utakapotoka na
nikuone. Tunakupenda na tunakuombea ulinzi wa kiMungu ndani yako. Kila silaha
itakayoinuka juu yako, mimi ninaingamiza katika jina la Yesu Kristo. Kila ulimi
utakao tamka mabaya juu yako na kuleta uharibifu wowote, mimi baba yako na mama
yako, usiku wa leo, tunautengua na kuufuta katika ulimwengu wa roho, sasa hadi
siku utakapokamilisha kusudi lako hapa duniani. Natamka uzima ndani yako. Kila
kilichoanza kufa kwenye maisha yako, nakijenga na kukitamkia uzima na baraka.
Mungu akutunze na akujalie ukuaji mkamilifu huko tumboni. Ili mama yako
afurahie ukaaji wako.” Geb akaendelea.
“Nakuombea
uzima Nanaa mke wangu. Mungu akuponye. Amani ile ipitayo amani zoote, ikatawale
moyoni mwako. Umebarikiwa Nanaa kwa kuwa unafanya kazi kubwa ya kuleta kusudi
la Mungu hapa duniani. Nakuombea uzima ili ufurahie huduma hii ya umama.
Nakuombea uwezo wa Mungu ukawe juu yako ili ukaweze kustahimili kila kitu mpaka
mwisho. Naomba Mungu unijalie uwezo wa kuwa msaada kwa Nanaa na
watoto wangu. Naomba amani kati yangu. Nisamehe pale ninapokuwa kwazo. Nisaidie
niweze kusimama kwenye nafasi yangu. Amina.” “Amen!” Kila mmoja akaitikia.
“Ulijuaje
kama ni mtoto wa kiume!?” Nanaa akauliza mara baada yakusema Amen. “Tokea
ultrasound ya kwanza. Nilichukua namba ya simu ya yule….” “Ngoja kwanza Geb. Si
tulisema tusubiri?” “Wewe ndio ulitaka kusubiri Nanaa. Mimi nilitaka kujua.”
Grace na mama yake wakaanza kucheka. “Geb wewe!” “Kweli tena.” “Umenizunguka
bwana!” Mama G alizidi kucheka kuonyesha amefurahi. “Hataa! Wewe ulitaka
kusubiri. Nikakwambia sawa. Na ili nisiharibu matakwa yako, baadaye mimi
nikapiga simu kuulizia. Wakaniambia. Nikabaki na jibu langu. Leo nilitaka ujue
kwa kuwa ulionyesha kujutia kutojua jinsia yake mpaka leo.” “Lakini nimefurahi
sana. Nilikuwa natamani mtoto wa kiume, kupita kiasi.” Nanaa akajishika tumbo.
“Kwa
hiyo huyo ndio Magesa?” Mama yake akamuuliza. “Haswaaa! Magesa G. Magesa.” “Geb! Mpaka umempa mtoto jina
kamili!?” Grace alishangaa. “Nilimuomba huyo mtoto baada ya Oliva tu kuzaliwa.
Nilimuomba Mungu anijalie mtoto wa kiume angalau mmoja tu. Nikamuomba na
mengineyo. Nilipojua Nanaa ni mjamzito. Kwanza nilishituka kwa kuwa sikuwa
nimempigia mahesabu ili ashike mimba ya mtoto wa kiume. Nikajua atakuwa ameshika
tena mimba ya mtoto wa kike. Lakini alipoonyesha anampango wa kuendelea kuzaa
hata baada ya huyu, nikajifariji. Nikamkumbusha tena Mungu kuwa mtoto wangu wa
tatu basi awe wa kiume. Kumbe jamaa alishakuwa ametulia ndani. Nilipoambiwa ni
wa kiume, nilitamani kuruka ruka.” Geb aliongea akicheka.
“Geb
wewe ni
msiri sana! Mimi nisingeweza. Ningeshamwambia kila mtu.” Geb akacheka. “Mnakumbuka
siku ile niliwaambia mnisindikize kituo cha watoto yatima kule Mburahati ili
nipeleke chakula na pesa?” “Mimi nilijua kuna kilichokufurahisha tu ndio maana
unatoa sadaka. Lakini sikujua kama ni hilo. Maana niliona kuna kulazimishwa.
Kila nikikwambia tufanye juma linalofuata, nikaona unakuwa mkali. Na unataka
kila mtu awepo mpaka watoto kina Fillius!” Mama G akaongeza nakumfanya Grace
acheke zaidi.
“Mimi
nilimwambia Geb, muda huo ndio watoto wanakuwa wamelala, nikaona
amenikasirikia. Akawa mkali. Anataka watu wote tuwepo hata kama watoto watakuwa
wamelala, twende nao hivyo hivyo. Nikamwambia mama hii sadaka ya safari hii ni
ya kibabe!” Wote wakacheka. “Pale nilikuwa nafuraha, sikutaka mtu
anicheleweshe kumtolea Mungu sadaka yangu ya shukurani. Na hapo nilikuwa
nimeshaandaa jina kamili. Kwa hiyo pale tunakwenda kule kituoni, nilishakuwa na
jina. Nikafanya kama mama alivyotufundisha kabla ya kutoa sadaka kuzungumza na
Mungu. Nikamtajia Mungu jina la mtoto wangu, na nikamuombea baraka zote za siku
ile, ziwe juu yake. Basi.” Geb akamalizia.
“Hongereni
sana. Hongera Nanaa kwa kutuongezea kina Magessa. Usiogope. Huyo ni mbarikiwa.
Na asili ya kina Magessa ni wapambanaji. Utakuja kumuona tu mwanao. Jiandae
kunyonyesha mchana na usiku.” Nanaa akacheka. “Asante mama. Lakini tutamuombea
aje kuwa kama dada yake. Usiku tuwe tunalala.” Wakacheka. “Dume hilo! Huoni
unavyokula sasa hivi?” “Lakini leo sikula vizuri. Hata nilipokuwa na kaka,
niliagiza chakula ninachokipenda, nikashangaa kinanishinda!” “Kwa kuwa hukuwa
ukijisikia vizuri. Watakuangalia. Wakijua tatizo na kulitibu, utarudia hali
yako. Nashauri ulale sasa hivi. Pumzika kabisa. Hakikisha unapumzisha akili na
moyo wako ili hiyo presha ishuke. Tutakuona kesho.” “Asanteni mama na Grace.”
“Punguza mawazo Nanaa. Kila kitu kitakuwa sawa.” “Asante Grace. Nitajitahidi
kutulia.” Grace akamkumbatia na kumbusu. Nanaa akajisikia machozi yanamtoka. “Asante Grace.” “Damu ya Yesu ukifunike Nanaa. Nakuombea amani na
furaha.” “Asante.” Grace akamfunika vizuri, akatoka nje.
“Kesho
nitakupigia kujua daktari anasemaje. Kama wataendelea kukupumzisha, nitakuletea
Liv.” “Nitashukuru mama. Asante.” “Haya.” Mama G na yeye akatoka. Geb
akawafuata nyuma. “Asanteni mama na Grace. Nashukuru kwa kila kitu.” “Mungu
atawasaidia Geb. Na sisi tunarudi nyumbani, lakini njiani tutakuwa
tunawaombea.” “Asante mama. Usiku mwema. Akiamka Liv mlete tu.” “Sawa.” Wakaondoka
Geb akarudi chumbani alipokuwa Nanaa.
Nanaa & Geb!
Akavuta
kiti na kukaa pembeni yake. “Nakupenda Nanaa.” “Sasa tatizo ni nini Geb?”
“Nilikosa tu. Nahisi sijui napatwa na wivu!” “Wivu na kaka James!?” “Naona
ananiingilia Nanaa. Wewe ni mke wangu sasa. Natamani alijue na kuliheshimu
hilo. Mahusiano yenu kwa sasa sio kama zamani. Mimi na wewe ni kitu kimoja.
Kitendo cha kukutoa kwangu na kupanga naye mipango ya maisha bila mimi
kuhusishwa moja kwa moja, inanikera.” Nanaa akatulia.
“Lazima
James aelewe hilo na kuliheshimu Nanaa. Sio sawa kumchukua mke wa mtu na
kaunzisha mambo unayojua yatatugawa.” “Sidhani kama anania hiyo Geb.” “Sasa kwa
nini akupe wazo la kufanya naye biashara. Wewe peke yako angali akijua mimi
nipo na ninafanya biashara? Anaona kama vile mimi nakutenga kwenye mambo
yangu?” “Sidhani Geb. Nafikiri kaka anania ya kunisaidia tu.” “Kwani ulimwambia
una shida?” “Hapana!” “Sasa!?” Nanaa akanyamaza.
“James
ananifahamu vizuri zaidi yako Nanaa. Si sawa kufanya anayofanya.” “Labda hiyo
ndiyo sababu inayomfanya afanye anayofanya. Anaona mimi sikufahamu na huna
mpango wa kunifahamisha. Ukweli mimi na wewe tunatoka kwenye ulimwengu mbili
tofauti Geb. Umeanza kushika pesa nyingi kabla yangu. Ni ngumu kunifikiria kama
mwenzako katika maswala ya uchumi. Mimi naelewa. Na nafikiri hata kaka
anafahamu hilo ndio maana anajaribu kunisaidia. Siwezi kubakia hivi milele kama
mama yake Oliva tu! Oliva hatanyonya maisha. Watoto wote watakuja kwenda shule
na watakuwa na kwao. Nini itakuwa hatima yangu?” Wote walikuwa wametulia
wanazungumza taratibu.
“Mimi
nipo Nanaa.” “Sasa hivi upo. Hujui kesho yako Geb. Halafu mimi sijui kukaa
bure. Unanijua nilivyo muhangaikaji. Nitakapomaliza hili la kuzaa na kulea,
nitahitaji kitu chakufanya. Nitafanya nini, ndio kaka anajaribu kunisaidia.
Sidhani kama ni sawa eti nije kuanza maisha mapya nikiwa nimeshazeeka!
Nafurahia hivi mambo yote yanavyokwenda kwa pamoja. Wewe unafanya mambo yako.
Na mimi nifanye ya kwangu na kaka, wakati ninalea. Amesema atanisaidia kwa
asilimia kubwa tu ili nisihangaike na mambo ya biashara wakati nina watoto.”
Geb akawa anatingisha kichwa kukataa.
“Nini?”
Nanaa akauliza. “Sasa unafikiri mimi nitakuwa nahangaika kwa ajili ya nani?”
“Sijui Geb! Mimi nitajuaje? Labda unahangaika kwa ajili ya watoto wako!
Hatujawahi kukaa chini tukazungumza chochote juu ya maisha mengine mbali ya
mapenzi.” “Basi ni kuchelewa tu. Lakini mimi sihesabu eti kuwa mali zote
nilizo nazo eti zote ni za kwangu peke yangu. Nanaa hahusiki. Kazi ya Nanaa ni
kuzaa tu! Hapana Nanaa. Mimi nimekuchagua wewe kwa makusudi kabisa. Ni mtu
ambaye najua tutaishi mpaka tuzeeshane. Hakuna mipaka kati yetu. Kama unaswali
lolote wewe niulize tu nitakujibu.”
“Sina sababu yakufanya hivyo Geb. Wewe ukiwa tayari na ukiona ni sawa kunishirikisha mambo yako, itakuwa sawa. Na kama ukiona hivi tunavyoishi ni sawa, pia sitalalamika. Ila ujue ni lazima na mimi nifanye kitu.” “Mbona unafanya mambo makubwa na mazuri Nanaa? Unaendesha mambo ya nyumbani. Hapo ulipo upo kwa ajili ya kuhakikisha huyo mtoto anazaliwa salama.” “Unajua namaanisha nini Geb. Yule nesi aliyenipokea pale na kuniwekea hii dripu, na yeye ni mjamzito kama mimi. Anapete ya ndoa kidoleni. Ameniambia ana watoto wengine wawili wa kiume, walikuwa wanatafuta mtoto wa kike. Ndio hiyo mimba aliyonayo sasa hivi. Na yupo hapa kazini, usiku huu, amenihudumia mimi.” Geb akanyamaza kwa muda. Kisha akaongeza.
“Naomba
ujue, nahangaika pia kwa ajili yako Nanaa.” “Asante.” Nanaa akajibu kwa kifupi.
“Mbona kama huamini?” “Ulitaka nifanyaje Geb? Mimi nimekushukuru.” “Nataka
uamini, kuwa vyote nilivyo navyo ni vyetu sisi na watoto wetu. Na naomba ujue,
sifurahii vile James anavyotugawa.” Nanaa akanyamaza. “Hawezi kufanya biashara
na wewe bila mimi. Wewe huna kitu chako na mimi sina kitu changu. Yale magari
pale nje sio ya kwangu. Ni yetu. Chukua lolote utakalo uendeshe.” “Hata kama
sijui kuendesha?” “Mimi ndio nitakufundisha, sio James.” Nanaa akacheka huku
akimtizama asiamini. Tayari akaona amenaswa katikati ya mapenzi ya marafiki hao
wawili. Kaka yake na Geb.
“Kweli
wivu umekupata Geb! Ni kwa nini?” “Sitaki kuingiliwa na wewe. Mimi nina mipango
yote ya maisha yetu?” “Mipango gani? Kwa nini sasa huniambii?” “Utashika
mangapi Nanaa?” “Unajua nini ninamaanisha Geb.” “Nilifikiri tumegawana
majukumu. Wewe mambo ya nyumbani, mimi mambo ya kazini?” “Wewe unajua majukumu
yangu yote Geb. Lakini mimi sifahamu unachofanya zaidi ya kile anachokifanya
Grace. Nasikia tu kutoka kwa mama kuwa unabiashara nyingi. Nashindwa hata
kumuuliza. Naona ni kama wewe hutaki mimi nijue.” “Sio kweli bwana Nanaa.”
“Sawa.” Mara nesi akaingia.
“Samahani. Naomba usiku wa leo umpishe alale.
Pressure yake ilikuwa juu sana. Anahitaji mapumziko haswa. Nimekuja kumchoma
sindano ya usingizi. Anatakiwa alale kabisa. Wala hatajua aliyekuwepo pembeni
yake. Sisi tutakuwepo kumsaidia kama akihitaji msaada.” Nanaa akacheka huku
akimwangalia Geb. “Unafurahia mimi kufukuzwa?” “Wewe si umeniombea amani na
furaha? Ndio ujue nina amani kwa lolote lile.” “Mimi nitanyamaza. Sitamuongelesha
tena. Wewe mchome sindano.” “Una uhakika?” Yule nesi akamuuliza, Geb akabaki
akimtizama. “Hatarudia kukujibu alilokwisha kwambia wala hataondoka hapo
alipokaa. Unaona kile kibegi kidogo pale na begi la laptop? Ni mizigo yake yote
ile. Yaani hapa ndio amefika.” Yule nesi akacheka kidogo huku akitazama mizigo
ya Geb. “Wewe nichome hiyo sindano, ukapumzike.” Akamchoma sindano, akampima
tena na kumwangalia maji.
“Jitahidi
kupumzika.” “Asante. Kwani pressure umeonaje?” “Bado ipo juu. Sio vizuri hasa
ukiwa kwenye hatua hiyo.” “Asante. Nitalala ili kutulia. Usiwe na wasiwasi.
Nikitaka kitu, atakuja kukuita.” “Na sisi tutakuwa tukipita kukuangalia mara
kwa mara.” “Asante.” Nesi akatoka.
“Usiku
mwema baba Liv!” Nanaa akamtania. Geb akacheka na kutingisha kichwa. “Usimpigie
simu James mpaka mimi mwenyewe nitakapoamua.” Nanaa akazidi kucheka. “Unajitesa
bure mpenzi wangu.” “Sitaki kuingiliwa.” “Haya Geb! Lakini ujue akijua nimelala
hapa leo bila yakumwambia, hatafurahi.” “Ndio aanze kuzoea kuwa wewe ni jukumu
langu hakuhusu tena. Mtu anajua mpaka idadi ya watoto tutakao zaa kabla yangu
mimi mwenyewe!” Nanaa akazidi kucheka.
“Anachukua
mke wangu na kumpa mipango bila idhini yangu!? Hapo amenikosea sana.” “Nia yake
nzuri.” “Hainihusu mimi. Sasa hivi nitakuwa makini naye sana.” “Mwenzio
nimeanza kusinzia hapa. Na usiondoke hapo. Nikiamka nikukute hapo hapo.” “Si
ulinikimbia wewe?” “Kwa muda tu ili utulie Geb. Ulikuwa umekasirika sana.
Nilishindwa kukutuliza.” “Kwa hiyo ungerudi?” Nanaa akacheka na kufunga macho.
Hapo hapo akapitiwa na usingizi.
Nanaa na Bedrest
Aliamshwa
asubuhi na madaktari waliokuwa wanapita round. “Unajisikiaje?” Nanaa akafikiria
kidogo. “Vizuri. Lakini..” Akasita tena huku akijipapasa. “Nini?” Geb
akamsogelea. Alikuwa amesimama pembeni kuwapisha madaktari ili
wamwangalie. “Nahisi nimelowa.” Nanaa aliongea huku machozi yakimtoka. “Mnafikiri mwanangu ni mzima?” Nanaa akauliza kwa kilio. “Cha msingi utulie
kabisa. Tutakwenda kumwangalia kwenye Ultrasaound ili tujue anaendeleaje.” Daktari
aliyekuwa akimuona kwenye kliniki aliongeza. “Jana ulimsikia akicheza?” Daktari
akauliza tena. “Asubuhi. Lakini
mida ya usiku sikumsikia kabisa. Na anamtindo wakucheza kila siku asubuhi. Ni
kama ndiye anayeniamsha.” Nanaa alijibu
huku akijishika tumbo. “Unafikiri atakuwa
salama kama maji yakiendelea kutoka hivi?”
Nanaa akauliza tena.
“Cha
msingi ni kuhakikisha hiyo pressure yako inashuka, kwanza. Tutamwangalia mtoto,
kisha tutajua jinsi ya kumsaidia yeye na wewe. Sawa?” Nanaa akatingisha kichwa.
“Hakikisha unatulia kabisa. Pata mapumziko ya kutosha. Na sisi tutatafuta njia
ya kukusaidia ili pressure ishuke na mtoto atunzwe humo ndani mpaka akomae
zaidi. Anaweza kutolewa na kuwekwa kwenye chupa ya kumkuzia, lakini humo
tumboni kwako ndio sehemu ya pekee na salama kwake. Kwa hiyo kwa namna yeyote
ile, hakikisha umetuliza mawazo kumsaidia mtoto. Tutakuwa makini na vyakula
unavyokula, ili visizidishe hiyo pressure. Ukitoka kwenye chumba cha Ultrasound
nitarudi kuzungumza na wewe zaidi.” Wale madaktari na wanafunzi wanaosomea
udaktari walizungumza na Nanaa pamoja na Geb kuwafariji na kuwatia moyo. Ndipo
wakaondoka.
Walipotoka
tu, Geb akavuta kiti mpaka pale kitandani. “Usiogope Nanaa. Mungu yupo na sisi.
Hajawahi kutuacha. Hawezi kuanza leo.” Akaweka mkono tumboni kwa Nanaa.
Akasogeza mdomo pale tumboni kwa Nanaa. “Magesa! Hakuna sehemu sahihi unaweza
kukaa sasa hivi isipokuwa huko ulipo, tumboni mwa mama yako. Lazima utulie.
Mungu yupo na wewe, atakushindia. Una damu ya kupambana. Huu ndio wakati wako.
Lazima upambane na kila upinzani unaopitia humo ndani. Hakikisha wewe ndio
unashinda na unabaki huko mpaka siku ambazo Mungu amekuamuru ukae. Nakuombea na
mimi nipo na wewe. Haupo peke yako. Lazima tutashinda. Kwa kuwa Mungu
ametuahidia ushindi.” Akambusu Nanaa tumboni na kumpapasa mpaka yule mtoto
akaanza kucheza.
Nanaa
alianza kucheka mpaka akalia. “Mungu
wangu! Anacheza Geb!” Nanaa aliendelea kulia. “Asante Yesu. Anacheza!” “Safi sana. Usiwe unanyamaza ukamtia mama hofu.”
Geb akambusu tena kisha akamsogelea Nanaa. “Huyu hatoki humo. Ni mpambanaji,
hawezi kushindwa.” Akambusu Nanaa. Nanaa akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha
kama aliyepata aghueni. Walikuja kumtayarisha kwa ajili ya ultrasound, kisha
wakaenda akiwa amelala vile vile kitandani.
~~~~~~~~~~~~~
Baada
ya ultrasound daktari akashauri Nanaa asitoke pale mpaka siku ya kujifungua.
Geb alitamani kuchanganyikiwa. “Tuna harusi baada ya siku 13 tu!” Geb alijikuta
akiropoka mbele ya yule daktari aliyewafuata pale chumbani. “Geb!” Nanaa
akashangaa. “Kweli Nanaa. Lazima tufunge ndoa siku na muda tuliopanga. Hakuna
kusubiri tena.” “Mtoto wenu ni mkubwa sana. Kuanzi urefu mpaka uzito wake huyu
mtoto, ni mkubwa. Na Nanaa amepoteza maji mengi. Akitoka tu hapo kitandani, ipo
hatari ya huyo mtoto kutoka. Ni lazima apate total bed rest. Tena ya hapa hospitalini wala si nyumbani.”
Daktari akasisitiza.
“Basi
tutamleta mchungaji hapa hapa atufungishe ndoa.” “Hapana Geb. Tusubiri tu. Mimi
ndoto zangu tokea zamani ni kusimama kanisani nikiwa nimevaa shela ndefu. Sio
nikiwa hapa kitandani tena hospitalini! Hapana.” “Unaweza kabisa kuvaa shela
ndefu ukasimama na tukafunga ndoa hapa hapa pembeni ya kitanda. Mimi nataka
kukuoa.” “Hapana Geb. Sio hapa. Kama unataka kunioa mimi, basi subiri.”
“Nasubiri mpaka lini Nanaa? Nimesubiri vya kutosha. Hatuwezi kuahirisha tena. Oliva
amezaliwa bila ndoa na Magesa pia aje akute nacheza michezo ya kihuni!
Hapana Nanaa, tunaoana.” Nanaa na
Geb wakaendelea kubishana palepale mbele ya yule daktari na nesi anayemsaidia
Nanaa.
“Haya
ndio moja ya mambo ambayo itamlazimu Nanaa ajitenge nayo.” Wote wakanyamaza. “Itawalazimu
kuhakikisha mnafanya kwa upande wenu na sisi kwa upande wetu ili kuhakikisha
tunafikia lengo.” Daktari alijaribu kuzungumza nao kiuungwana. Mama G akaingia
na mtoto wao. Bila salamu Geb akamchukua mtoto wake na kutoka. Mama G akabaki
na mshangao. Daktari naye akaaga na kutoka. Nitarudi tena jioni kukuangalia. “Asante
sana.” Nanaa akashukuru.
~~~~~~~~~~~~~
“Haya,
kwema? Maana naona nimenyang’anywa mtoto bila salamu.” Mama G akauliza. “Kakasirika.”
“Nini tena?” “Eti mama, Geb anataka tufungie ndoa hapa.” “Kwa nini?” “Ndio
ushangae sasa!” “Hapana Nanaa. Nauliza kwa nini mfunge ndoa hapa na si
kanisani?” Mama G hakuwa anataarifa na kinachoendelea. Nanaa akamsimulia majibu
ya vipimo vyote. “Kwa kifupi Magesa ni mzima. Lakini nimeambiwa ni mrefu sana
na mzito ndio maana nilikuwa nasikia sana maumivu.
Hapa sitoki mama mpaka mtoto
atimize siku zake, azaliwe. Au angalau amalize hii miezi 8 yote. Ikishindikana
na pressure ikikataa kushuka, wanamtoa.” Mama G akakaa.
“Sasa
mbona husemi kitu?” Nanaa akamuuliza mama G. “Nafikiria.” “Nini?” “Geb hakiwezi
kile chumba bila wewe. Inamaana mtakaa hapa kwa karibia mwezi mzima!” Nanaa
akanyamaza. “Geb anakupenda Nanaa. Anakupenda sana. Hakuna sababu utakayompa
asikuoe wewe au asiwe karibu na wewe, akaridhika. Shida yake kubwa ni kuwa na
wewe. Hafikirii kama akikuoa hapa hatavaa suti au hatafika ukumbini kwenye
sherehe. Shida yake ni kukufanya uwe wake. Basi.” Nanaa akaanza kulia.
“Jipeni
muda wa kufikiria. Msiharakishe majibu.” “Ndoto zangu ni kuvaa shela ndefu kama ile aliyoninunulia Grace, mama.
Nataka na mimi kusimama kanisani. Nikiolewa hapa, ndio basi. Nitakuja kuolewa
tena lini?” Nanaa aliendelea kulia. “Naomba
utulie Nanaa. Umeniambia pressure bado ipo juu. Lazima utulie ili ishuke.
Isiposhuka watamtoa huyo mtoto. Si ndivyo ulivyoambiwa?” “Sasa nitafanyaje mama? Sitaki kumuumiza
Geb, na mimi natamani kutimiza ndoto yangu!”
“Hizi habari ndio mmepewa sasa hivi. Mambo mengi yanapita kichwani kwenu.
Maisha yenu yatabadilika kwa mwezi mzima, kitu ambacho sio wewe wala Geb
aliyetarajia. Mnahitaji muda. Naomba tulia kabisa. Geb alinitumia masharti yote
ya vyakula unavyotakiwa kula kuanzia sasa. Nimeleta uji, Grace ataleta chakula
baada ya muda mfupi tu. Kunywa uji ulale.” “Nataka kumnyonyesha kwanza Liv.” Mama
G akasimama na kutoka.
~~~~~~~~~~~~~
“Nanaa anataka kumnyonyesha huyo kabla
hajalala.” Geb akamkabidhi mtoto mama yake. “Niangalie mimi Geb.” Geb akageuka.
“Nataka ujijibu haya maswali. Unamtaka mtoto wako azaliwe salama? Maana maombi
peke yake hayatatosha kama usipokubali kutenda kazi na Mungu. Lazima.
Nasisitiza, ni lazima ufanye mazingira matulivu kwa Nanaa ili mpate mtoto
wenu.” “Nanaa hataki nimuoe mama.” “Tangia unazaliwa mpaka sasa, sijakuona
ukitaka kitu. Na ukamshirikisha Mungu, ukashindwa kupata wewe Geb Magesa.
Mwambie Mungu haja ya moyo wako. Weka hasira pembeni. Mtunze mwenzio. Namfahamu
Nanaa. Mtafikia tu muafaka. Nanaa ni muoga sana wa ugomvi. Ndio maana jana
ulipomgombeza tu kidogo, tayari pressure imempanda. Ukitaka atulie, ni akuone
na wewe umetulia.” Geb alipata faraja ya namna yake. Akajisikia ametulia
kabisa.
~~~~~~~~~~~~~
Wakarudi chumbani. Geb akamsogelea Nanaa.“Samahani.Nahisi nimepaniki.”
Nanaa akamuonea huruma. “Na mimi nataka unioe Geb!” “Najua. Naomba upumzike.
Tutapanga kila kitu pamoja, baadaye. Sasa hivi naomba upumzike.” Nanaa akajisikia
na yeye furaha. “Asante.” Wala hakunyonyesha tena, hapo hapo akalala. Usiku
walipobaki peke yao Nanaa akaanza.
“Geb!”
Geb alikuwa akila pembeni. “Vipi?” “Asante kwa kuwa hapa na mimi.” Geb
akasimama. “Hakuna sehemu natamani kuwepo isipokuwa wewe ulipo Nanaa. Nakupenda.”
Ilimgusa sana Nanaa. “Basi naomba unioe tu.” “Na shela?” Geb akauliza. “Naweza
kusubiri Nanaa. Hamna shida.” “Moja ya ndoto zangu nyingine ni kuolewa na
mwanaume anayenipenda. Maadamu nimekupata wewe, naona nisiendelee kusubiri.
Acha tuoane tu.” Geb akainama na kumbusu. Alimbusu kwa muda mrefu bila
kupumzika.
“Asante
Nanaa. Na samahani. Nina tatizo la kupanga mambo yangu. Baada ya kushindwa
kukuoa wakati ule, nikamuomba Mungu anisaidie niweze kukuoa kwenye siku yangu
ya kuzaliwa. Na kweli Mungu akafanya hivyo. Naomba iwe hivyo. Kwangu inamaana
kubwa sana. Sitajali utaonekana vipi mpenzi wangu. Nakutaka wewe. Naomba
tukamilishe hili. Nakuahidi tutafanya sherehe mara baada ya Magesa kuzaliwa.”
Nanaa akatingisha kichwa kukubali huku akifuta machozi. “Asante. Basi
nitazungumza na uongozi wa hospitali kama tunaweza kufunga ndoa yetu siku hiyo.
Sitataka watu wengi sana. Ni familia yetu na marafiki zetu wa karibu. Basi.”
Nanaa akatabasamu baada ya kumuona Geb amechangamka.
~~~~~~~~~~~~~
Ndugu
zao ndio walikuwa wametoka hapo. James, Danny na familia yake yote, Mama G na
Oliva. Na wote wakajua Nanaa hatatoka hapo mpaka ajifungue. James alipouliza
swala la ndoa, hakupata jibu. Kila mtu akanyamaza. Lakini baadaye Nanaa
alimwambia kaka yake yeye ameamua kusubiri mpaka ajifungue. Kwa hiyo wote
waliondoka tena na taarifa kuwa harusi hiyo inaahirishwa tena.
~~~~~~~~~~~~~
Geb
akampigia simu James wa kwanza. “Tutafunga ndoa
hapahapa hospitalini. Kesho nitazungumza na uongozi wa hospitali tuone
watakachosema.” Akamsikia James anacheka. “Daah! Umegoma kusubiri?” “Hapana aisee. Acha nioe James.
Mtoto wa pili huyu! Wote watakuja kujua ni kama sikuwa na malengo kabisa bwana!
Halafu Dume langu linakuja! Anakuja anamkuta baba yake hajaoa! Sio sawa.
Nitakuwa siweki mfano mzuri. Nilishakosea tokea mwanzo, basi maadamu Mungu
ametupa neema, acha niitumie vizuri. Nisiendelee kukosea. Naomba baraka zako.
Utuunge mkono katika hili tafadhali.” “Tupo pamoja.” Hata James alisikika akiwa
amefurahia.
“Nani
atawasimamia sasa?” James akauliza. “Wale wale. Nitaongea na Malii kama bado wanaweza kutusimamia yeye na
mkewe hapahapa hospitalini. Naona ndiye rafiki wa kweli niliyebaki naye na
angalau tunaendana.” “Sidhani kama Malii atakataa. Kwa umbali tuliotoka naye,
lazima atasimama na wewe, popote. Labda tatizo lije kuwa mkewe.” James
akatahadharisha. “Nitazungumza naye kesho, tuone.
Lakini sidhani kama kufungia hapa hospitalini itakuwa kikwazo kwao.” “Sidhani.
Wewe wasikilize. Kila la kheri.”
James akatoa baraka zake. “Asante. Sitakuwa na watu wengi.
Ni ndugu tu. Nanaa akijifungua, ndipo tutafanya sherehe na marafiki, kumshukuru
Mungu. Kwa hiyo kama mama na kina Viola wangependa kuhudhuria hapa hospitalini
siku hiyo nikimuoa Nanaa, wakaribishe tafadhali. Naweza kuwatumia dereva
akaenda kuwachukua.” James akanyamaza kwa muda. Geb akaona aage. “Siku njema.” “Asante na wewe.” Wakakata simu.
~~~~~~~~~~~~~
Mama
yake akawa wapili kupigiwa. “Naoa mama!” Mama G akaanza kucheka na kupiga vigelegele. “Subiri kwanza mama. Nisikilize.” “Niache nifurahie kwanza. Usinikere
wewe mtoto!” Mama G akaendelea kupiga
vigelegele. “Si usikilize kwanza ndio
uendelee kusherehekea?” “Usianze kunipa masharti ya hiyo harusi Geb. Maana wewe
nakujua.” “Hatutaki watu wengi mama. Ni ndugu tu.” “Hee!” Mama G akashangaa.
“Nanaa
akishajifungua ndipo tutafanya sherehe na utaalika watu wote unaotaka wewe.
Lakini sasa hivi ni familia tu kwa kuwa tutafungia hiyo ndoa hapa hapa
chumbani. Naomba usubiri.” Nanaa akaanza
kucheka. “Yaani huo ni msamiati wa kichina kwa mama G. Hawezi hata kidogo. Wewe
msikilize tu umsikie. Alivyopania hiyo harusi!” Nanaa aliongeza akiwa
anawasikiliza.
“Kwa nini
mfungie ndoa chumbani? Kwani Nanaa yupo mahututi? Usiniharibie shuguli kabisa!” Geb akajua
tayari ameshapokonywa shuguli nzima. “Sasa wewe
ulitakaje?” “Nitakuja mwenyewe kesho kuzungumza na uongozi wa hospitali.” Geb akashangaa. “Mama!” “Kumbe!
Wewe unafikiri hawana kumbi za kufanyia mikutano hapo? Unataka mashoga zangu
wakose harusi?” “Si watahudhuria sherehe baadaye!” “Nataka wahudhurie vyote.
Ndoa na sherehe. Sasa wewe niachie kila kitu.” Akamsikia
anaanza kupiga vigelegele tena.
“Huna
utakalomwambia mama akaelewa juu ya hiyo harusi. Wewe mwache tu.” Nanaa
akaongeza. “We Geb!” Geb akamsikia
mama yake akimwita. “Nipo mama.” Geb akaitika. “Tena nitataka kuonana na huyo daktari wa Nanaa. Aniambie masharti yote
juu yake. Ukaaji wake na..” “Mama, Mamaa!” Geb
akaita. “Nini?” “Nilishazungumza na daktari.
Nanaa anatakiwa alale asikae.” “Wewe niwekee miahadi na huyo daktari. Nitakuja
kuzungumza naye mwenyewe. Wewe vipi bwana!?” Akaendelea
kupiga vigelegele kwa muda.
“Ngoja nimpigie
Grace sasa hivi, ili tujue tunafanyaje?” “Juu ya nini mama? Acha hii iwe ndogo
tu!” “Naomba usinipangie kitu cha kufanya kwenye harusi ya mwanangu. Wewe
angalia swala la ugonjwa, basi. Mimi na Grace tutajua maswala mengine.” “Nilitaka kumpigia mimi
kwanza ili nimtaarifu.” “Kwani mimi nimekuzuia nini? Mimi nampigia na maswala
yangu na wewe mpigie na yako.” Akaendelea
kupiga vigelegele. “Naomba yasiwe maswala mengi
mama. Kumbuka hapa ni hospitalini.” Geb aliongea akisikika kuishiwa
nguvu, akamsikia mama yake amekata simu.
“Daah!”
Geb akabaki na mshangao. Nanaa akazidi kucheka. “Nilikwambia mimi.” “Yaani
shuguli nzima ameipora yeye! Ishakuwa shuguli yake yeye, mwenye mtoto. Kesho
anakuja kuzungumza na uongozi wa hospitali na daktari wako! Anataka marafiki
zake wote wawepo. Tena isifanyikie hapa! Hiyo ndoa anataka ikafungwe kwenye
ukumbi.” Geb alikuwa akieleza huku ameshikilia simu yake haamini.
“Nilijua
tu. Mama hana dogo.” “Najuta! Heri yeye ndio ningemfanyia surprise.” Geb
aliendelea kuwaza. “Na hapo mama Magesa huna utakachomwambia tena. Kashashika
usukani kwenye shuguli nzima. Utamsikia akitaka umlipe pesa yake tu.” Nanaa
alizidi kucheka. “Sio kwamba anakuomba kwanza?” Nanaa akauliza. “Umcheleweshe
kwenye mipango yake? Hathubutu. Atanunua vitu vyote anavyotaka kwa pesa yake,
baadaye ndio anakuletea risiti umlipe pesa yake. Subiri utamuona. Kesho tu,
risiti zake zitaanza kuingia hapa. Hajuagi kusubiri kwenye mambo yake. Akipanga
mipango yake leo, ujue inaanza hapo hapo.” Nanaa alizidi kucheka.
“Kanikatia
simu ili yeye ndio awe wa kwanza kumwambia Grace! Namwambia asubiri kwanza,
hataki. Mama! Tena anasisitiza eti mimi nisimuharibie shuguli!” Geb aliendelea
kulalamika huku akishangaa. “Hana jambo dogo hata iweje. Wewe muache tu
afurahie. Ni siku yake.” “We Nanaa!? Siku yake au yangu mimi na wewe?” “Si ndio
amekwambia yeye ndio mwenye mtoto?” “Daah!” Geb akavuta kiti na kukaa pembeni
ya Nanaa.
~~~~~~~~~~~~~
“Asante Nanaa.” “Asante ya nini tena?” Nanaa
akauliza huku akijiweka sawa. “Kukubali kuweka matakwa yako pembeni, na
kuolewa ukiwa hapa. Nimefurahi sana.”
Nanaa akamwangalia Geb. “Unahitaji msaada wa kiroho, Geb. Wewe ni mtu gani
huwezi kubadilika hata kidogo!?” Geb akacheka. “Eti siku nzima umepooza hata
kuongea, huongei kwa kuwa huoi siku uliyopanga wewe!” “Magesa hawezi kuja
akakuta baba yake bado sijaoa, Nanaa! Ni fedhea ilioje!? Halafu eti aje ajue
yeye ndio alisababisha! Unataka mwanangu ajilaumu?” “Unajua kufikiria mbali
wewe! Mimi hilo wala sikuwaza.” “Ndio hivyo. Wanangu watakuja kuniona baba
muhuni. Eti Magesa.” Akamshika Nanaa tumbo na kumbusu.
“Utavaa
suti yako?” Nanaa akamuuliza. Geb alikuwa amefurahi sana mpaka uso ulionyesha. “Kabisa.
Naoa mwenzio. Lazima nivae suti.” Nanaa akacheka kidogo na kufikiria. Geb
akamuona. “Vipi? Unataka kubadili mawazo nini?” “Hapana. Nafikiria tu.” “Nini?”
Geb akamuuliza na kumbusu kwenye kipanda uso. “Ningumu kuyatabiri maisha.
Sikujua kama nitapata mtu anayenipenda na kutaka kunioa kwa kiasi hiki! Haya, nilipokupata,
sikujua kama nitafunga ndoa hospitalini.
Tena nikiwa nimelala kitandani!”
“Unajuta?” “Hapana Geb. Hata kidogo.” Nanaa akatulia kwa muda.
“Mchana
nilipomwambia kaka kuwa nitasubiri mpaka nijufungue, nilikuona vile
ulivyohuzunika. Sio kukasirika kama jana. Nikakusikia ukiongea na Grace
ukimwambia umekubaliana na mawazo yangu, utasubiri mpaka nitakapokuwa tayari.
Lile neno likaniingia sana. Nikajiuliza ni ‘lini
nitakuwa tayari?’ Nikakumbuka ni miezi michache tu iliyopita, nilikuwa hapahapa
hospitalini. Kasoro chumba tofauti. Nikiwa nimeoza miguu. Na bado ulikuwa na
mimi ukitaka kunioa vile vile.” Nanaa akaanza kulia.
“Maisha yangu yamekuwa hayatabiriki Geb. Lakini mapenzi yako kwangu
hakika ni ya halisi. Unanipenda kwa dhati tena bila sababu. Wakati wote
unasisitiza unanipenda mimi vile nilivyo, hujali ninaonekana vipi. Sina sababu
yakunifanya usinioe Geb. Kama ni gauni lenye shela ndefu, nitalivaa hata hapa
kitandani tu. Sitajali tutakapofunga ndoa, ilimradi wewe upo, na ndiye
utakayeapa mbele ya Mungu utanichukua kama mkeo, hadi kifo! Hiyo itatosha
kwangu. Nakushukuru.” Geb akasimama na kukumbatia pale
pale alipokuwa amelala.
~~~~~~~~~~~~~
Walikumbatiana
kwa muda, mabusu yakafuata. “Docta amesema hakuna mapenzi Geb. Niache.” Geb
akahema kwa nguvu na kumuachia. “Daah! Hali mbaya.” Nanaa akamcheka. “Amesema
mpaka lini tena?” “Nijifungue!” Nanaa alijibu huku anacheka. “Daah!” Geb
alilalamika. “Sasa fungate tutafanya nini?” Nanaa akauliza.
Geb
akarudi na kukaa kwenye kiti. “Tutarudi hapa baada ya kila mtu kuondoka.
Tutapata muda wa kumshukuru Mungu. Siku tatu mfululizo, sitawasha simu wala
kompyuta. Sitaenda kazini hata kidogo. Tutakuwa wote siku tatu mfululizo. Mimi
na wewe tu.” “Na madaktari na manesi.” Nanaa akaongeza. “Na hao basi. Tutapata
muda mtulivu wa kuzungumza. Hapo ndipo utapata nafasi ya kumfahamu mumeo
vizuri. Ndani na nje. Maswali yako yote, yatapata majibu ya wazi na kina.
Utapata nafasi ya kushauri chochote katika yote tutakayozungumza. Nitahakikisha
baada ya hizo siku tatu, tunakuwa kitu kimoja. Kimwili, kiakili na kiroho
tunakuwa pamoja. Mtu akikuona wewe, anakuwa amemuona Geb Magesa.” Nanaa
akacheka.
“Unacheka
tena?” “Hapo haiwezekani Geb.Nimewasikia watu wakinong’ona siku ile pale kwenye
kikao cha Zena.” “Juu ya nini?” Geb akauliza. “Haupo kama ninavyokujua Geb.
Wewe sio mwenzangu hata iweje.” “Kivipi Nanaa!?” “Walikuwa wakisema wewe ni
milionea wa hapa mjini.” Geb akacheka. “Wewe hufahamu watoto wa mjini. Wanakuza
kila kitu.” “Jeff anafanya kazi benki. Alisema anahusika na moja ya akaunti
zako.” Geb akacheka kidogo. “Yaani dakika moja niliyokwenda kukununulia
chakula, tayari waliongea kila kitu!” “Wewe hukuona walivyokuwa wakituangalia?”
“Walikuwa wakikuangalia ulivyopendeza bwana!” Nanaa akampiga ngumi kidogo.
“Umoja
wetu hautakuwa na mipaka Nanaa. Yale yote Mungu aliyonibariki mimi, yatakuwa ni
yako pia. Na yale yote Mungu aliyokubariki wewe, tutayashiriki pamoja. Au
unafikirije?” Tayari machozi yalishakuwa yakimtoka Nanaa. “Si ndivyo hivyo?” “Mimi sina hata kitu Geb! Utanufaika kwa
lipi?” “Sina pesa inayoweza kumnunua
Oliva na Magesa. Pesa sio kila kitu Nanaa. Umenipa nyumba yenye amani na
utulivu. Una upendo wa dhati kwangu. Unanifikiria. Umetulia. Mwaminifu kwangu.
Hivyo vyote vinathamni kuliko pesa, mpenzi wangu. Na huwezi kuvinunua, hata uwe
tajiri wa namna gani. Wewe sio mwanamke wa kwanza kuwa na mimi. Lakini wewe ni
mwanamke wa kwanza kunivumilia na kunipenda.” Geb aliendelea.
Vya Sirini Vikiwekwa Mwangani Haibakii
Kama Ilivyokuwa.
“Sitasahau jinsi ulivyeweza kunisubiria kwa
uchungu wakati nalala na Liz, chumbani kwangu wakati na wewe upo palepale!
Nilikuwa najisikia vibaya. Sikuwa na jinsi. Halafu mama akawa ananiambia vile
ilivyo hatari ya kuendelea kuchelewa kufanya maamuzi. Akawa anazungumza kwa
mafumbo. Lakini nilielewa kuwa ulikuwa una watu wanao kutongoza mbali na Zinda
na Jeff. Nilijua kuna wanaume wengine ulikuwa ukienda kukutana nao, Nanaa.”
Nanaa akashituka kidogo. Akataka kukana.
“Nilikuwa
najua Nanaa.” Nanaa akanyamaza. “Kuna siku ulitoka mapema kidogo kazini.
Ilikuwa siku ya ijumaa. Ulibadilisha nguo ofisini tena baada ya kumuaga Grace.
Ulifuatwa na mwanaume alikuwa na gari ndogo, nyeupe. Ulivaa gauni fupi mpaka
kwenye magoti. Lilikuwa la rangi nyeusi. Lilichanua kuanzia chini ya maziwa.
Ukabadili na aina ya nywele. Vile ulivyokuwa umebana asubuhi wakati unaenda kazini,
haikuwa kama ulivyotoka. Ulibadili na viatu. Ukavaa viatu vya wazi, lakini
vilikuwa vya juu kidogo. Halafu ulitokea mlango wa nyuma. Stoo. Kama ambaye
hukutaka mtu akuone. Kwa kuwa hata nguo ulibadili baada ya kumuaga Grace.”
Nanaa alishindwa hata kumwangalia Geb.
“Nilipomuuliza
Grace unakwenda wapi, akaniambia hajui, lakini ulimuomba ruhusa tangia saa 6
mchana. Nilijiuliza ni wapi unakwenda ambako ilikulazimu uvae vile na usitake
mtu akuone! Nilijua kama umebadili nguo kwa kuwa nilikuona wakati unatoka
nyumbani asubuhi. Halafu nikakuona wakati unatoka ofisini na kupanda gari ya
yule Jamaa. Na mimi nilikuwa nimefika pale ofisini. Lakini sikuwa nimeshuka
kwenye gari. Nilikuwa nikizungumza na mtu kwenye simu ndani ya gari.” Nanaa
akanyamaza.
“Unakumbuka?”
Geb akamuuliza. “Lakini sikuchelewa kurudi nyumbani.” Nanaa akajitetea. “Sawa
sawa. Hukuchelewa hata kidogo. Ulirudi nyumbani muda ule ule unaorudi na Grace.
Kama mliingia tu pamoja. Lakini ulirudi nyumbani ukiwa umevaa tena nguo zile
zile ulizokuwa umevaa asubuhi wakati ukienda kazini na ukarudishia mtindo wa
nywele vile vile kama asubuhi. Ulinikuta nje, ukashindwa hata kunisalimia kama
kawaida yako. Ukapita kwa haraka, ukaingia ndani. Ulisema kichwa kinakuuma,
hukuweza hata kula. Ukalala mpaka asubuhi.” Geb alikuwa na hicho kitu moyoni.
Hakuwa amemwambia mtu yeyote yule. Akabaki nacho huku akiumia tu. Wakati huo na
yeye alikuwa na Liz.
“Nilijaribu
kumuuliza mama kwa makini ili asijue. Lakini nilitaka kujua kama alijua kama
ulitoka na ulikwenda wapi. Lakini mama alionyesha hajui naongea nini na alisema
siku hiyo hamkuzungumza kabisa. Alipokupigia simu mida ya jioni, hukupokea kitu
ambacho sio kawaida yako. Lakini ukamtumia ujumbe kuwa upo sehemu hutaweza
kuzungumza. Utampigia baada ya muda mfupi. Hukupiga ila saa 12 kamili ukawa
unaingia getini.” Nanaa alibaki kimya.
~~~~~~~~~~~~~
Mwanzo
wa Geb ulikuwa mzuri sana. Nanaa hakutegemea kama ataishia hapo. Nanaa alipanga
hiyo safari kwa siri sana. Hakuwa hata amemwambia mama G mshauri wake. Siku hiyo
aliamua kufanya kile akili yake imemtuma. Hakuchelewa kurudi, na wala hakukosea
kurudi nyumbani na nguo za tofauti na zile alizokuwa ameondoka nazo. Muda wote
aliokuwa na Geb, hakujua kama amebeba hilo jambo moyoni. “Sasa atakuwa amebeba mangapi?” Nanaa akajiuliza.
~~~~~~~~~~~~~
“Najua sikuwa na haki ya kuumia au kuona wivu. Lakini nilishindwa kulala Nanaa. Swali la ulikuwa wapi ambako uliweza kuwa huru kubadilisha nguo na kurudisha nywele vile zilivyokuwa asubuhi, ndilo lililokuwa likinitesa sana.” Kimya. “Nanaa?” Geb akamwita. “Abee!” “Tunakaribia kuanza maisha mapya. Si sawa kuanza kuwa na siri kati yetu. Najua hili lingeweza kusubiri, lakini nataka tuingie kwenye ndoa wote tukiwa kwenye ukurasa mmoja na tukiwa na amani. Nataka kujua ukweli.” Nanaa alitamani asingezungumzia hicho kitu. Hakutaka mtu ajue kabisa. “Nataka kujua ulikuwa wapi na ulikuwa na nani?” Geb alisisitiza kwa utulivu bila jazba.
“Naomba uniamini, siku ile hakuna kilichotokea
Geb.” Geb akakunja uso. “Sivyo nilivyokuuliza Nanaa. Nataka kujua ulikuwa wapi
na ulikuwa na nani. Basi.” “Naomba tusizungumzie hicho kitu Geb. Tukiache kama
kilivyo. Lakini naomba uamini hakuna nilichofanya.” “Mbona unanitia wasiwasi!?”
“Tafadhali Geb. Naomba tuyaache kama yalivyo. Nakuomba. Tafadhali sana. Naomba
maisha yetu tuliyoishi zamani, kama hayatatuathiri sasa hivi, basi tuyaache
kama yalivyo. Tuanze upya mimi na wewe.” Nanaa alisisitiza.
“Tunaanzaje
upya kukiwa na maswali ya nyuma ambayo hayataki kupewa majibu?” “Geb! Najua
huna asili ya kutaka kupitwa na mambo. Lakini katika hili, nakusihi acha
tu.” “Naachaje Nanaa!?” “Wewe unataka kuibua mambo ambayo hayaleti amani
hata kidogo.” “Labda hujaelewa Nanaa. Hili jambo nimejaribu kulisahau
lakini limekuwa likinisumbua sana. Kwa kifupi hiyo amani unayozungumzia, haipo.
Na sitaki tuingie kwenye ndoa katika hali hii. Kwangu ndoa sio mchezo. Ni kweli
tutakuwa mwili mmoja. Nataka iwe hivyo kiukweli. Nimekwambia utanifahamu kwa
asilimia 100. Watu wakikuona wewe, watakuwa wakiniona mimi. Nitajifunua kwako
kwa asilimia zote.”
“Sasa
na wewe huoni kama unahitajika kufanya hivyo hivyo? Huoni kama haitakuwa sawa,
eti mimi unifahamu mambo yangu yote. Mpaka wanawake niliokuwa na mahusiano nao,
halafu nikupe ruksa ya kuniuliza tena chochote! Na ahadi ya kukwambia ukweli,
halafu wewe ukatae kujibu swali kama hilo? Ni nini unaficha ambacho ni cha
hatari sana!?” Nanaa alitamani hilo lipite tu. Lakini Geb alionekana halitaweza
kupita kamwe.
~~~~~~~~~~~~~
Zikiwa zimebaki siku chache sana za kutimiza ndoto zao, Geb ana ibua
siri kubwa sana iliyokuwa imefichwa na kuendelea kufichwa Nanaa. Hata mama G,
msiri wake hakuwa amemwambia. Hakutaka mtu ajue. Kumbe Geb analo
moyoni. Leo anataka ukweli kwa Nanaa ambaye presha inamsumbua.
Tena yupo hospitalini.
Nini kitaendelea?
Nani alikuwa na Nanaa?
Geb & Nanaa wataweza kufuata masharti ya
daktari kusaidia kuzaliwa mtoto aliyekomaa huku wakiwa wamejawa wivu, hasira na
Kutojizuia?
Hapo nyuma vikwazo vilikuwa vinatoka NJE. Walimudu. Sasa ni wao
wenyewe.
Itakuaje!?
Usikose muendelezo…
0 Comments:
Post a Comment