Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Ni Wangu! – Sehemu Ya 47. - Naomi Simulizi

Ni Wangu! – Sehemu Ya 47.


“Utakuwa umechoka na hivi leo hujapata muda wakulala mchana!” “Nitajitahidi tusikae sana. Nitawaaga mapema. Na tumbo hili, watanihurumia tu.” “Tutakuona Nanaa. Na unavyopenda stori wewe!” “Sio na hawa watu, Geb. Kina Zena wananidharau sana. Ukisikia wanazungumza na mimi kwa muda mrefu, ujue wananiringishia kitu, ili kuniumiza tu. Basi. Lakini si vinginevyo. Wananiona mchemshaji sana wa maisha. Sasa nishajionya. Sitawapa nafasi tena. Nina kwenda hapo kwa kuwa tunafahamiana nao. Yasini na yeye. Nawapa mchango wangu. Nawaambia sitaweza kushiriki vikao vingine. Kama ni swala la kunialika, nitamwambia nitamtafuta muda utakapo karibia.” Geb akamtizama.

“Ulitaka kumchangia kiasi gani?” Geb akamuuliza. “Kikubwa tu kama kumsuta. Ameshaninyanyasa sana Zena. Kujua sina kazi na bado sijaolewa! Nayo pia imekuwa nongwa. Nimekuta jumbe kama 20 leo asubuhi.” “Na wewe ukasoma?” Geb akamuuliza. “Nimekwambia nimeachana naye. Sitaki tena kumpa sikio langu. Jana ndio mwisho, sitaki tena. Kwa hiyo kujibu swali lako, sijasoma.” Kidogo Geb akatulia.

“Twende basi. Tena nawaona wale pale.” “Hujaniambia unataka kuwapa kiasi gani!” Geb akasisitiza swali lake. “Nataka kwanza nikaone kitabu cha majina ya watu walioahidi na bajeti yao. Ndio nitaamua. Hawana adabu! Wale wote pale waliokaa, walikuwa wakinicheka kweli na mimba ya Liv. Walikuwa wanasema nimepewa mimba, kisha nikakimbiwa. Walikuwa wakinisema vibaya sana Geb. Kila ninapopita na tumbo langu walikuwa wakinicheka. Ijumaa ilikuwa ikifika ndio utachoka hivyo vishindo vyao hapo darasani. Wanaaga kwa sauti kwamba wanaenda kwa wapenzi wao. Wasio na wapenzi, ndio wanabaki. Chuo kikifunga halafu wajue nilibaki chuoni, wakirudi ndio utachoka zaidi. Watanitangaza hata kwa watu ambao hawanijui! Walikuwa wanasema hata kwa kaka nilifukuzwa ndio maana sina pakwenda. Ilimradi tu kuniumiza.” Kidogo Geb akaanza kuelewa wasiwasi wa Nanaa usiku uliopita. Akamuhurumia. “Pole.” Nanaa akacheka. “Twende. Naona wanaongea huku wanaangalia huku. Tusiwape sababu.” Geb akashuka na kumfungulia mlango.

~~~~~~~~~~~~~~

“Umesikia harufu ya mshikaki?” Geb akacheka. “Nilijua tu. Sijui kama tutaondoka leo!” “Tutaondoka bwana. Tukimaliza tu kula, tunaondoka. Sasa chamsingi ni kumuita muhudumu wa jikoni kwanza. Tumwagizie mishakaki na ndizi za kuchoma. Ndio mambo mengine yaendelee. Nikishiba tu, tunaondoka zetu.” Geb alikuwa akimtizma Nanaa huku anacheka na kutingisha kichwa. Nanaa alishakula chakula cha mchana kama masaa mawili yaliyopita. Akamalizia na chips alizokuwa ameletewa Geb, ambazo hata hakugusa. Lakini hapo anaongelea chakula kingine kama ambaye hajala siku nzima.

Wakasogea mpaka pale kwenye kikao. Wakamuona Yasini anasimama na kumsogelea Geb. Kidogo Jeff naye akasimama. “Karibu Mkubwa!” Wote walitoa tabasamu la heshima. “Asante. Kumbe wewe ndio unaoa!?” Geb akamuuliza Yasini akishangaa kidogo. “Ni mimi bwana. Ndio tunabembelezana michango hapa.” Yasini akajibu kinyenyekevu sana. “Hongera sana.” Geb akampa tena mkono. Nanaa akabaki anashangaa.

“Jeff ameniambia mnafahamiana.” Yasini aliongeza akisikika wazi anajikomba kwa Geb. “Tumeshakutana mara kadhaa nafikiri.” Jeff na yeye akaongeza kuthibitisha aliyosema rafikiye Yasini. “Basi huyu ndio mshenga wangu. Mtu wangu wakaribu sana. Ndio anaongoza mambo yote hapa.” Yasini aliendelea wote wakipokezana kwa Geb. “Safi sana. Naona sisi ulitunyima harusi, ila naona wife hapa, amepata habari. Ndio nimemsindikiza.”  Geb akaongeza kama akilaumu lakini nia ilikuwa kuwafikishia wote ujumbe kuwa yeye ndio anamiliki Nanaa.

“Nanaa!?” Yasini akauliza kwa mshangao wa wazi kabisa. Geb akacheka kidogo. “Ndio mwenyewe. Mama watoto wangu huyo. Binti yule niliyekuonyesha kwenye picha, ndio binti yetu wa kwanza.” “Naona kweli rangi zimefanana! Hongereni sana kaka. Familia nzuri.” Yasini akasifia. “Namshukuru Mungu.” Geb akajibu. Nanaa akaona heshima pale imeongezeka. Akajua wazi Yasini anafahamiana na Geb. Na muda waliotumia kuzungumza pale ndani ya gari mara baada ya kuwasili, akajua wazi Yasini atakuwa amesha waambia habari za Geb. Kwani wote waligeukia lile gari la Geb kabla hawajashuka garini.

~~~~~~~~~~~~~~

Ni kweli magari aliyokuwa akiendesha Geb, yalikuwa machache sana jijini. Likisimamishwa   mahali, utajua ni nani atakayeshuka humo ndani. Kama sio Geb, basi ni mtoto mwingine wa milionea hapo jijini. Tena mtoto mdogo tu, wakichotara. Huyo ndiye alijulikana kwa kuendesha magari mazuri na ya thamani. Lakini huwa akiingia yeye mahali, anajulikana. Ujana mwingi. Kwa hiyo kwa usimamishwaji ule wa gari, wazi alijulikana ni Magesa ndiye mmiliki wa chombo hicho. Na kwa kuwa Yasini na Jeff walimfahamu Geb, waliposimamisha tu gari wakalisifia na kumtaja mmiliki wake.

Ni kweli wote waliokuwepo kwenye kikao hicho waligeuka kushangaa gari, lakini zaidi walitaka kumuona huyo Geb Magesa aliyekuwa akisifiwa na Jeff na Yasini kuwa wamwangalie akishuka. Ni kijana mdogo, mwenye pesa nyingi sana. Walitegemea kumuona Geb, lakini sio na Nanaa! Na wakajua Geb hawezi kuwa alifika pale kwa ajili ya mtu kama Yasini na Zena. Walijua pengine yupo pale kwa shuguli zake. Sasa kushuka na Nanaa, na kusema amemsindikiza hapo kwenye hicho kikao! Kila mtu alifunga mdomo wakabaki wamenywea.

~~~~~~~~~~~~~~

“Sikujua kama mnafahamiana!” Nanaa alimwangalia Geb na Yasini. Kama kawaida yake Geb, aliacha Yasini mwenyewe azungumze. Bado walikuwa wamesimama wanaangaliana. “Asilimia kubwa ya mazao ya Mkubwa hapa kutoka mikoani, yanauzwa kwenye ile kampuni ambayo mimi ni muhasibu. Kwa hiyo mimi huwa nahusika sana na malipo yake. Napata neema yakumsikia mara moja moja.” Yasini alijibu na kucheka kidogo. Jeff naye akatoa cheko la heshima tu. “Kumbe!” Nanaa akajibu.

“Na mimi nilishawahi kumuona kama mara moja au mbili pale kwenye tawi la posta.” Wote wakamgeukia Jeff. Nanaa na Geb wakabaki kama hawajaelewa. “Si unajua Jeff anafanya kazi benki? Sasa nafikiri huko kwenye tawi la hiyo benki, maeneo ya Posta mpya, ndiko alipomuona Mkubwa hapa.” Yasini akasaidia. “Aaaah!” Nanaa akaitika. “Kumbe mnafahamiana!” Akaongeza na kusogea. Akamuacha Geb, Yasini na Jeff.

          Yeye akaenda kusalimia wenzake. “Habari zenu jamani!” Nanaa akapita na kuanza kusalimia. “Hongera mwali. Naona mambo yako mazuri.” Maneno ya Zena alipomfikia. Nanaa akacheka tu. “Hongera na wewe kwa hatua kubwa.” Zena akacheka cheko la kinafiki. Wazi alionekana kuna kilichomkamata rohoni. “Naona siku hizi mambo yako si mchezo. Sio viwango vyetu tena.” Kwa kuwa Nanaa anamfahamu Zena, hakutaka kuendelea kusimama na kuendelea kuzungumza naye zaidi. Akaendelea kusalimia wengine kwa kuwashika mkono. “Hongereni jamani. Niliona picha zenu za harusi. Mlipendeza sana.” Couple nyingine iliyokuwa imekaa. Geb alimsikia Nanaa akiwasalimia na kicheko.

“Tulikutafuta ili kukualika. Hatukuwa na mawasiliano yako.” “Ukweli nilipotea kwenye ulimwengu wa mawasiliano. Ila ni jambo la kumshukuru Mungu kuwafanikisha.” Nanaa akaongeza. Bado Geb alikuwa amesimama. Alimfahamu Nanaa kwa kupenda kuongea. Yeye hakupita kumsalimia mtu hata mmoja. Alitoka pale na kuelekea jikoni wakati Nanaa akisalimia watu.

“Mtusamehe jamani. Tumechelewa. Tulikuwa kwenye kikao kingine. Nikaona tuje tu hivyo hivyo. Angalau na sisi tusikose. Lakini hatutakaa sana. Mkiona tunaondoka katikati ya kikao, naomba mtuelewe. Hata mtoto tumemwachia bibi yake amrudishe nyumbani ili sisi tuwepo hapa. Kwa hiyo hatutakaa sana.” “Kwanza hongera Nanaa. Sikujua kama umejifungua.” Rafiki yake mwingine alidakia.

“Tumefanya harakaharaka. Bandika bandua ili asikose mwenzie wakucheza naye.” Wote wakacheka kiheshima. Mwenye pesa akisimama sehemu, hata akiwa kimya pesa yake itazungumza tu. “Ndio vizuri.” Mwigine akaongeza. “Hongereni sana.” Yasini naye akaongeza lakini Zena alishindwa hata kumpongeza. Alibaki akimwangalia tu kama asiyeamini.

Geb akarudi wakaenda kukaa mwisho kabisa, yeye na Nanaa. “Au tuwapishe hapa?” Jeff akauliza na tabasamu la heshima usoni. Akimaanisha mbele kabisa. “Asante sana. Hapa panatosha. Panatufaa sisi wachelewaji.” Akajibu Geb na kufanya hata hilo liwachekeshe. Ni kama muongoza kikao akawa amepoteza dira. Kubabaika kukawa kwingi. Kama hakuna la maana lililokuwa likizungumzwa kabla.

Muhudumu akamletea Geb kile chakula. “Naomba msogezee meza hapo pembeni yake.” Akinyoonyeshea kidole pembeni ya Nanaa.

“Vinanukia hivyo!” Nanaa akanong’ona. Geb akatingisha kichwa huku akimwangalia. “Utakula kidogo?” Geb akatingisha kichwa kukataa. “Basi nambakishia mama.” “Wewe kula tu. Nimemwagizia cha kwake.” “Ndio maana nakupenda. Maana hapa nisingeshiba.” “Vyote hivyo Nanaa!?” “Unaona vingi!? Hapa napunguza tu njaa. Nikifika nyumbani ndio nitakula vizuri.” Nanaa alishaanza kula kwa uchu. Geb alikuwa akimtizama hammalizi.

           “Onja kidogo mpenzi wangu. Nyama yao hapa tamu sanaa!” Nanaa aliendelea kunong’ona. “Mmmh! Kuna chakula ambacho si kitamu kwako?” Nanaa akacheka sana. Lakini kwa sauti ya chini ili asisumbue wengine. “Bwana hii tofauti! Onja uone Geb. Kidogo tu.” “Kipande kimoja tu.” Nanaa akamuokotea na kukiweka mdomoni kwake. Geb akatafuta. “Mbona sasa husifii.” “Kawaida sana.” Nanaa hakumshangaa. Alimjua ushirikiano wake na chakula. Akaendelea kula kwa shauku kubwa huku wakisikiliza.

“Omba daftari la michango.” Geb akamnong’oneza Nanaa. Jeff akawa amesikia. Akasimama kwa haraka, akalichukua kutoka kwa katibu na kumpa Geb. Ndipo wakajua walikuwa wakisikilizwa muda wote. Nanaa akamwita muhudumu akamnawisha mkono. “Asante sana dada yangu. Nyama yenu nzuri sana. Laini, imekolea viungo. Nzuri sana. Nimekula nikafurahi. Na asante kwa kunihudumia.” “Karibu. Nimefurahi kama umeridhika.” Yule muhudumu alijibu huku  akicheka wakati akiendelea kummiminia maji ya vugu vugu.

Alipojikausha, akajivuta kwa Geb ili na yeye asome kilichoandikwa. Akaona Geb ametuliza macho kwenye budget. “Ipi?” Nanaa akauliza. Geb akaweka kidole kwenye garama ya chakula. Nanaa akamtolea macho. “Unataka kulipa yote au sijaelewa!?” “Naomba uwaandikie hundi, tuondoke tukapumzike, Nanaa. Mwenzio nimechoka!” “Kwa hiyo huo ndio utakuwa mchango wetu?” “Unaonaje? Ni sawa?” Geb akauliza. Nanaa alijawa nafuraha mpaka Geb akaiona usoni. Hakuwa akiamini. Akambusu begani. “Asante.” Akanong’ona. “Ni sawa?” Geb akamuuliza tena. Nanaa akatingisha kichwa kukubali. 

Nanaa akatoa pochi yake iliyokuwa na kitabu chahundi, ambacho benki ilichapisha juu jina lake yeye kwenye kila hundi. Na ndiko Geb alipokuwa akimuwekea pesa huko. Akaandika kiwango hicho chote cha pesa, na kuiweka ile hundi katikati ya kile kitabu cha michango kilichokuwa na budget nzima ya harusi pia, walichokuwa wamepewa na Jeff. Alijisikia vizuri kuona ameweka heshima mbele ya wenzie ambao alisimuliwa habari za maendeleo yao. Wote waliomaliza pamoja, Zena alimringishia kuwa wanakazi nzuri. Kasoro yeye. Kitendo cha kuandika hundi ya pesa iliyonona vile. Tena kwa jina lake yeye sio Geb. Na Geb kumtambulisha pale kama mkewe. Tena baada ya kuona vile Jeff na Yasini walivyobabaika, akaongeza ujasiri moyoni. Yaani yeye ndio atalisha watu kwenye harusi ya Zena! Nanaa alifurahi sana.

“Twende.” Geb akasimama na kumsaidia kumshika mkono ili asimame. Wakasogea mpaka kwenye meza aliyokaa Jeff, Yasini, Zena na msichana mwingine. Geb akawakabidhi kile kitabu. Wote walisikia kina kundi ndani. Wote kwenye ile meza wakasimama. “Jamani! Naomba sisi tuwahi nyumbani. Tupo pamoja.” Geb akatoa mkono na Nanaa pia. “Kila la kheri Zena. Tutawasiliana.” “Naomba namba yako ya simu, basi.” Zena aliomba pale mbele za watu. Nanaa akasita kidogo. “Tutaongea basi.” Nanaa akajibu jibu ambalo wazi kila mtu akajua amemkatalia. Wanawasiliana vipi, wakati hajampa namba! Kila mtu aliwaza. “Tuwaache muendelee. Tusiwacheleweshe.” Nanaa akaongeza na kumgeukia Geb. Wakaondoka.

Baada Ya Kikao Cha Zena.

“Nakushukuru mpenzi wangu. Angalau wataniheshimu.” Nanaa aliongea mara baada ya Geb kuondoa gari. Geb akamwangalia na tabasamu. “Umeona lakini Zena alivyobabaika? Kawa mwema kama sio yeye anayependa kunirusha roho!” Wakazungumza kidogo, Nanaa akalala hapo hapo na kumuacha Geb akiwaza. Alijiuliza mengi kama umuhimu wa kumshirikisha Nanaa juu ya mali zake zote au aache. Alijiuliza hili na kujijibu. Lakini majibu yake yote yalimridhisha juu yakutomshirikisha chochote. Hakuona sababu.

          Walifika nyumbani, Geb akamwamsha.“Usingeniamsha bwana Geb!” Nanaa akalalamika. “Tumefika nyumbani. Twende ukalale ndani.” “Nahisi huyu mwanao ananilemea bwana! Napata maumivu makali nikisimama. Natamani nikikaa nisiwe nasimama, kwa jinsi maumivu yanavyokuwa makali.” “Pole. Tutaenda kumuuliza daktari. Aangalie kama kuna tatizo. Twende ukapumzike ndani.” Nanaa akashuka na kuelekea ndani taratibu.

Walimkuta Mama G chumbani kwake. Nanaa hakutaka hata kuingia. “Wewe Nanaa?” Akamuita. “Nina usingizi mama. Acha kupenda stori.” Akamsikia mama G anacheka. “Njoo bwana. Ukoje Nanaa wewe?” “Ngoja nikalale kidogo, ndio nije kukwambia yaliyojiri. Nimewarusha roho vilivyo! Muulize Geb.” “Mmmh! Huyo? Hana cha maana atakachoniambia. Hajui kunisimulia stori, nikaridhika.” Akamsikia Nanaa anacheka huku anapandisha ngazi. “Geb! Nenda kamsimulie mama kila kitu.” “Mimi sijaona cha kusimulia pale.” Geb akajibu huku akiingia chumbani kwa mama yake. “Si nilikwambia mimi? Hayawezi.” “Basi nakuja mwaya mama. Yapo mengi tu yakusimulia. Kuanzia tulipofika mpaka tunaondoka. Nimeweka heshima mjini. Usinione hivi.” “Nakuaminia Nanaa.” Mama G akamsifia. “Wewe nipe kama lisaa. Nikapunguze usingizi nakuja. Geb amekuletea chakula. Kula wakati mimi napumzika.” Nanaa akaingia chumbani kwake.

Ukweli Unaopenda Kuepukwa

Mama yake alipomwangalia tu usoni, akajua lipo jambo. Akajilaza pembeni ya mama yake. Kimya. “Haya, kuna nini?” Mama yake akamuuliza. “Hamna kitu. Vipi nyinyi? Naona Liv amelala hana habari.” “Bwana wee! Acha kunipoteza malengo. Nijibu swali langu.” Geb akaanza kucheka. “Si nimekwambia hamna kitu?” “Usinichoshe Geb. Maana unajua wazi nilazima uniambie tu. Naomba uanze kujieleza, usinipotezee muda.” Geb akajiweka sawa.

“Labda nikuulize swali.” Geb akaanza. “Nakumbuka historia yako na baba. Ulimkuta baba ameshaanza maisha. Naamini umenielewa.” “Kwamba alishakuwa na mali halafu mimi sina kitu?” Geb akacheka. “Sio kwa maana hiyo lakini kama hivyo.” “Wewe nenda kwenye swali.” Geb akatingisha kichwa, alimjua mama yake. “Mlipoingia kwenye mahusiano, alikushirikisha kila kitu?” Mama G akatulia kwa muda kama anayefikiria.

“Sio kwa haraka na haikuwa moja kwa moja. Kwanza ukumbuke mimi nilishafanya kazi kwake. Halafu kwa kuwa nilimpenda tokea mwanzo, nikaanza kumchunguza. Kwa hiyo nilimfahamu kwa haraka, kwa utundu wangu tu mimi mwenyewe na nikamwambia kila kitu ninachofahamu juu yake. Alipojua ninaakili ya maendeleo na mimi ni muhangaikaji, unakumbuka biashara alizokuja kunifungulia baadaye na kuanza kufanya naye kazi pamoja?” “Nakumbuka.” Geb akajibu.

“Basi. Kwa hiyo kwa kifupi hapakuwa na siri sana kati yetu. Nilikuwa nikifahamu kila kitu cha Magesa. Iwe kutoka kwake mwenyewe au mimi mwenyewe nilifanyia uchunguzi na kuja kumuuliza kwa uthibitisho.” Geb akatulia. Mama yake akamtizama vizuri.

“Hutaki kumshirikisha Nanaa juu ya mali zako?” Mama yake alimtupia swali la moja kwa moja. “Sio kwamba sitaki. Lakini sioni muhimu.” “Kama huoni umuhimu, kwa nini unataabika rohoni?” Geb akanyamaza. “Ni kwa kuwa unajua kuna umuhimu wa hilo, ila unasita kwa kuwa wewe ni msiri sana Geb.” “Sio kama ni msiri. Ila naona hamna umuhimu.” “Basi acha. Sio lazima uishi kama mimi na baba yako tulivyoishi. Wewe una uhuru wa kufanya kile unachopenda. Kwani Nanaa amekuuliza?” “Hapana.” Geb akajibu kama anayeficha jibu zima. Na mama yake akajua.

“Nisikilize Geb. Mimi nakufahamu. Nafahamu umbali uliofika kwenye maisha yako. Ni ngumu sana kumfungulia milango yote msichana kama Nanaa ambaye kwanza amekuonyesha wazi ni kama amejitenga na mali zako kabisa. Nanaa hana shida na mali zako. Anakupenda wewe kama wewe. Ni rahisi sana kupuuza umuhimu wake kwenye upande wako mwingine wa maisha. Kwa kuwa unajua humuhitaji sasa hivi. Biashara zako zinaenda vizuri. Unaakili nzuri yakufikiria. Kila unalofanya wewe sasa hivi, mkono wa Mungu umekuwa juu yako. Huoni umuhimu wa kujifungua kwa mtu mwingine.” Mama yake akaendelea.

“Ni sawa. Kuna faida zake hasa sasa hivi ambako mambo yako yanakuendea vizuri. Upo peke yako. Huhitaji ushauri wala pesa ya mtu kukufanikisha. Unafanya maamuzi kwa haraka. Upo kwenye kisiwa chako cha salama kabisa. Unajua mali yako ipo salama kwa kuwa ni wewe peke yako unayejua unakiasi gani au mali kiasi gani. Unampa Nanaa kile unachoamua wewe. Halafu na yeye hawezi kukuhoji kwa lolote, maadamu anapewa na halalamiki, ni rahisi sana. Yeye atulie tu hapa nyumbani, akuzalie watoto na wakue. Safi sana. Maisha mazuri na marahisi. Hakuna maswali. Upande wa nyumbani ipo amani kwa kuwa unajua yeye yupo na watoto wako. Atakupa unachotaka. Na wewe utampa kile unachotaka. Hiyo ni safi kabisa. Hata mimi mama yako nafurahia hiyo. Mali zako haziguswi na mtu mwingine. Ni wewe tu.”

Geb akatulia akisubiria madhara ambayo hata hakuona tatizo liko wapi. Maana alianza na faida. “Lakini?” Geb akauliza pale alipomuona mama yake ametulia. “Lazima ujiandae. Kipimo hicho hicho unachompimia Nanaa, ujie na wewe utapimiwa. Jiulize na kujijibu. Upo tayari kumfahamu Nanaa nusu nusu kama yeye anavyokufahamu? Upo tayari kuujua upande mmoja tu wa maisha yake? Yaani umuone tu na pesa, halafu hujui anakozipata! Na hautakuwa na haki yakumuuliza anakozipata pesa zake kwa kuwa kwanza hayakuhusu, pili huna hiyo haki kwa kuwa hata wewe hajui anakozipata pesa.” Mama G akamuona ameanza kubadilika.

“Hiyo ni sehemu ya kwanza.” Mama G akaendelea. “Sehemu nyingine ambayo nataka kukutahadharisha, kwa kuwa mwili unatabia ya udanganyifu. Ukiwa umekaa hapo na una uhakika wa kwenda kazini kesho, haukwambii ukweli juu yake. Mwili ni udongo Geb. Udongo kabisa. Nafikiri unakumbuka kilichompata Nanaa. Kufumba na kufumbua, alipoteza uwezo wa kutembea. Akawa na miguu iliyooza. Achilia mbali mifano hai uliyonayo. Unaamka mzima, unatoka hapa kama kawaida kuelekea kazini, unapata ajali. Unapoteza viungo vyote. Anabakiwa na Nanaa wakukuhudumia. Unafanyaje na mali zako zote unazozificha kwake?” “Mungu anatulinda mama. Usiniogopeshe.” Mama G akakaa.

          “Unasoma bibilia gani wewe!? Unakumbuka yaliyompata Ayubu. Milionea wa wakati ule. Tena mcha Mungu na Mungu aliruhusu mwili wake uguswe na magonjwa! Yakikufika kama ya Ayubu? Unakumbuka kila kitu chake kilikufa? Unakumbuka aliyetajwa kubaki naye ni nani?” “Mkewe.” Geb akajibu kwa haraka. “Ewaaa. Unakumbuka ushauri wa mkewe?” Geb akatulia. Mama yake akajua ukweli umeanza kumwingia.

“Kasome vizuri kitabu cha Ayubu 2:9, uone yaliyomkuta mwenzio. Mkewe alimshauri amkufuru Mungu ili afe. Ushajiuliza ni kwa nini mkewe aliongea vile? Halafu mumewe, yaani Ayubu kwenye mstari wa 10, anamtukana mkewe. Ukiwaangalia kwa karibu hawa wanandoa wawili hawakuwa kwenye upande mmoja. Anamuuliza kwa nini wao ndio wapate tu mema, wasipatwe na mabaya? Pengine halikuwa kosa la yule mwanamke! Ukute yeye hakuzoea kupata mengine yoyote kutoka kwa mumewe isipokuwa mema kama hivi unavyomfanyia Nanaa. Unampa kila kitu. Hajui ni kwa taabu gani unapata unachompa. Kesho tatizo linapotokea, ndio unataka akupe ushauri mzuri! Anautoa wapi wakati hafahamu upande wako mwingine? Alimtukana mkewe bure kama ni mwanamke mpumbavu. Lakini unafikiri kama angehangaika na huyo mwanamke tokea mwanzo. Anatoa naye sadaka na kumlilia Mungu pamoja na mkewe, unafikiri Imani ya yule mama isingekuwa kama yake yeye Ayubu?” Kimya.

“Maana bibilia inamtaja Ayubu tokea mwanzo kama yeye ndiye aliyekuwa mkamilifu na mcha Mungu. Ndiye aliyeepuka uovu. Hawajasema Ayubu na mkewe! Kasome Ayubu 1:1. Nenda kasome mlango huo huo wa kwanza mstari 5. Bibilia inamtaja Ayubu peke yake aliyekuwa akiwatakasa wanae. Na bibilia inasema alikuwa akiamka asubuhi na mapema. Yeye mwenyewe kwenda kumtolea Mungu sadaka kwa niaba ya wanae, ili kuwatakasa. Haijasema Ayubu na mkewe. Amekuja kupata matatizo, ndipo sasa anakuja kuonekana mkewe akimpa ushauri mbaya! Sasa huo ushauri mzuri angeutoa wapi wakati hajajengwa kama mumewe? Mumewe ndiye aliyeonyesha juhudi kwa Mungu. Utavunaje jema wakati hujapanda?” Geb akajigeuza upande wa pili. Akatulia kimya. Mama yake akajua yamemuingia akilini. Wakatulia.

“Nimekuletea chakula. Kipo jikoni. Twende ukale.” Baada ya muda Geb akabadilisha mazungumzo. “Mimi bado nimeshiba.” Wakaendelea kuzungumza mambo mengine tu. Geb hakutaka tena kuzungumzia lile jambo. Na mama yake akajua. Geb alikuwa na msimamo sana kama baba yake. Mama yake alijua hilo ni jaribu ambalo litamsumbua sana. Ni kweli alikuwa msiri sana, na alimiliki mali nyingi.

Mambo Yanaendelea

Ni kweli Geb alikusudia kumuoa Nanaa. Huo mwezi ulikuwa upo busy sana kwa familia yake na marafiki wa karibu wa Geb kukamilisha harusi hiyo. Alitaka mtoto huyo wa pili angalau azaliwe ndani ya ndoa. Kuendelea kuishi na Liv, mtoto wake wa kike aliyekuwa akimpenda, bila ndoa! Ni kitendo kilichokuwa kikimsuta sana. Kila alipojiuliza kama atakubali mwanaume yeyote aishi na binti yake huyo bila ndoa, alihisi kunyonga mtu. Akajikuta anawajibika kufunga tu ndoa na Nanaa ili kusafisha dhamira yake.

Kwa kuwa Grace alikuwa na msichana mzuri wa kazi aliyekuwa akimsaidia watoto, akili zake aliweza kuzigawa na kumsaidia Geb kwenye maandalizi hayo ya harusi. Hasa upande wa Nanaa. Walijitahidi kutafuta nguo nzuri ambayo hata kama tumbo litaendelea kuwa kubwa, basi bado itamkaa vizuri na kumpendeza. James na Danny walisaidiana bega kwa bega kuhakikisha mambo yanakaa sawa, na kukamilisha hilo swala la ndoa.

~~~~~~~~~~~~~~

Wakati maandalizi ya harusi yamepamba moto wazo likamjia James. Alipiga simu siku ya jumamosi asubuhi Nanaa akiwa na mama G pamoja na Geb. “Tunaweza kuonana baadaye?” James akauliza. “Utakuja kunichukua?” Nanaa akauliza na cheko usoni kama mwanae Liv. “Nikitoka kazini basi.” “Sawa. Ila niambie muda ili unikute tayari.” “Nitakuwepo hapo kama kwenye saa nane. Naamini nitakuwa sijakuvurugia mipango yako. Kuna kitu nataka kukushirikisha.” “Hamna shida kaka. Nipo tu hapa nyumbani. Wala sikuwa na mpango wa kutoka.” “Sawa. Nitakuona baadaye. msalimie Liv.” “Zimefika. Kazi njema kaka yangu.” “Asante na wewe.” James akakata simu.

“Kwema?” Mama G akauliza. “Kwema. Lakini mchana atakuja kunichukua. Anataka tukazungumze.” Nanaa akajibu. “Utachelewa kurudi? Maana ndio muda na mimi natoka kazini.” Geb akauliza kama ambaye hataki Nanaa atoke. “Nafikiri sitakawia. Au nitajitahidi nisikawie. Kwani kuna mahali unataka twende?” “Hapana! Sasa si na mimi ndio nitakuwa nimerudi?” Geb alionyesha wazi hafurahii Nanaa kuondoka. Alitaka akiwa anarudi nyumbani amkute Nanaa na yeye anamsubiria. “Sitachelewa Geb.” Geb akasimama na kutoka baada ya kuaga.

Vita Ya Ndani.

Mida ya saa nane kasoro James alikuwa akiegesha gari mbele ya nyumba hiyo anayoishi mdogo wake. Nanaa akatoka. “Liv yupo wapi?” “Amelala na bibi yake. Anapenda kulala huyo! Labda Fili awepo nyumbani.” James akacheka huku akiondoa gari. “Kwa kuwa anampa pipi?” Nanaa akacheka sana. “Geb alirudia kumuonya na akahakikisha Fili ameelewa. Hataki kabisa ale pipi. Naona siku hizi ameacha.” James akacheka. “Una hamu ya kula nini?” “Kila kitu.” Kaka yake akacheka. “Yaani nakula kaka. Kama sijui nini!” “Hata hivyo ni haki yako. Unanyonyesha na huyo mtoto humo ndani ni mkubwa.” “Basi ndio twende tukale chakula kingi.” James akacheka.

Walifika kwenye mgahawa wa kawaida tu uliokuwa ukiuzwa vyakula mbali mbali. Nanaa akaagiza kuku wa makange na ugali. Kaka yake akaagiza na yeye kama Nanaa. “Kuna nini kaka?” Nanaa akauliza. “Nilikuwa nikifikiria. Sipendi hivyo unavyoishi. Unakuwa tegemezi tu. Huna kitega uchumi chochote! Kuna leo na kesho Nanaa. Sitaki ubweteke. Ukiwa na chako ni chako.” “Lakini Geb ameniomba nibaki nyumbani na watoto. Nikamkubalia. Siwezi kubadilika kaka.” Nanaa aliingiwa na wasiwasi kidogo.

          “Zipo njia nyingi tu za kuingiza pesa. Sio lazima wewe uwe unafanya kazi mahali ili kuingiza pesa.” Nanaa akajiweka sawa kusikiliza hiyo njia anayoweza kujiingizia pesa bila kufanya kazi. “Mimi ninafanya biashara. Ninaweza kukusaidia. Ukawekeza pesa kwangu, nikawa nakupa faida.” “Kweli kaka!?” Nanaa hakuamini. “Kabisa. Unaishi pale na watu ambao wanaakili sana. Kila mmoja anaingiza pesa yakueleweka. Sio sawa wewe kuwa tu pale kama tegemezi. Hata kama wanakupenda na kukuthamini. Chako ni chako tu mdogo wangu. Asikudanganye mtu. Umebahatika kupata mwanaume mwenye pesa. Sawa. Lakini ukumbuke umezikuta. Hata iweje, ni vya Geb.” Nanaa akatulia.

“Ni kweli anakupenda sana. Lakini lazima kuna sehemu atajiwekea mipaka ambayo itakuwa ngumu kwako kuvuka. Mimi ni mwanaume. Najua na ninaelewa. Kuna mambo ambayo hata mimi nisingeyafanya kwa mwanamke aliyenikuta nina kila kitu. Labda kama mngekuwa mmeanza naye. Bado kuna mambo utakuwa mgeni tu kwake. Hata iweje.” James akasisitiza. Na aliongea kama aliyekuwepo kwenye akili za Geb. Au kama anayejua kinachoendelea kwa Geb, kwa wakati ule. Au pengine ni kwa kuwa walikuwa wakifahamiana tokea vijana wadogo.

“Hata hivyo, huna sababu ya kutokuwa na chako Nanaa. Wewe sio mjinga wala hushindwi kujijenga. Sasa kwa nini usijijenge?” “Ni kweli kaka. Na kama ulivyosema. Kuna leo na kesho. Sio mbaya watoto wetu wakawa na sehemu mbili za kutegemea. Kwa baba na mama. Sijui ya kesho.” “Basi. Naona somo umelielewa.” Nanaa akacheka. Waliendelea kuzungumza na kucheka wakipanga mipango. Kuja kugutuka ni saa 12 jioni. Nanaa akamuomba kaka yake amrudishe nyumbani.

~~~~~~~~~~~~~~

James aliingia ndani. Akasalimia na kumbeba Liv kidogo. Wakacheza pamoja kidogo. Akaondoka. Geb alikuwa ametulia kwenye kochi. Nanaa akajua amekasirika. Akaenda kukaa pembeni yake. “Kwani nimechelewa sana?” Nanaa akamuuliza huku akimshika. Geb akamgeukia kidogo, akamtizama na kugeuza shingo kwengine. Nanaa akaelewa. “Samahani. Nilijisahau kabisa mpenzi wangu. Pole na kazi.” “Asante.” Geb akajibu kwa kifupi tu. “Umerudi saa ngapi?” “Saa 8 mchana.” “Basi itakuwa tumepishana kidogo tu mpenzi wangu. Kaka aliwahi.” “Kwema?” “Kwema kabisa. Umekula?” Geb alitamani jibu zaidi, lakini akashindwa kuuliza zaidi kwa kuwa mama yake alimwambia kama atakuwa anamficha mambo Nanaa, na yeye awe anapokea kile anachoambiwa. Asitake undani.

“Nilikula.” Geb akajibu. “Umeoga?” Nanaa aliendelea kuhoji kwa kujikomba. Geb akamtizama kidogo akageukia pembeni. Ukweli ndio mambo waliyokuwa wakizungumzia na Nanaa. Ya hapo tu nyumbani. Wajibu wake ilikuwa kuhakikisha nyumba ina amani, ametoa penzi kwa Geb, amekula anachopenda. Ameoga na kulala sehemu safi. Mazungumzo yao yalikuwa ya kifamilia tu. Na ni kweli walikuwa na amani na upendo ulitawa. Wala Nanaa hakuwahi kuona tofauti na wala hakutaka mali ya Geb. 

“Twende tukaoge. Hata mimi nasikia joto.” Nanaa aliongea kwa kubembeleza kidogo, akijua wazi Geb amekasirika. “Niliwahi kutoka ili nikukute, angalau tuagane kabla hujatoka na James. Sikujua kama umebadilisha muda!” Geb aliendelea kulalamika. “Samahani mpenzi wangu. Nafikiri tumepishana kama dakika tano tu. Pole. Kumbe ningejua ningekupigia! Samahani mpenzi wangu.” Mama G aliyekuwa akicheka na mjukuu wake alijua kinachomsibu Geb. Alijua wazi anataka kujua yale waliyozungumza Nanaa na kaka yake. Kila alipolalamika akionyesha hakufurahia kutomkuta nyumbani, Nanaa aliomba msamaha tu, hakuonyesha utayari wa kumwambia kabisa, kipi cha muhimu kilichomtoa siku hiyo wakati akijua wazi ni siku yeye anafanya kazi nusu siku tu. Alitegemea Nanaa ajieleze kile kilichoendelea huko alipokuwa na kaka yake. Lakini hakusema.

Hata swala la James kumtoa pale na kumpeleka sehemu wanayo uza magari. Na ahadi ya kumuongezea pesa Nanaa ili amiliki gari yake, lilimkera sana Geb. Alitamani ashirikishwe. Lakini alimsikia Nanaa akiongea katikati ya mazungumzo tu.

Geb akasimama na kuelekea chumbani. “Kwani umemfanyaje mpenzi wangu!?” Nanaa alimnong’oneza mama G baada ya kuachwa peke yao. “Mie huyu!?” “Kumbe? Si ndiye niliyekukuta naye hapa? Umemfanyaje?” “Nanaa naomba uniche wewe mtoto. Wewe ukazurule huko halafu uje uniulize mie?  Kama ungetaka kumkuta anafuraha, ungetulia hapa umsubirie hasa ukijua mwenzio leo anarudi hapa mchana.” Nanaa akabaki ameduwaa. “Ulisahau kama leo jumamosi na jana alikwambia atawahi kurudi ili mzungumzie swala la wapi mtakapoenda baada ya harusi?” Nanaa alisahau kabisa.

“Mama wewe!?” “Mama wewe nini?” “Sasa kwa nini hukunikumbusha pale pale asubuhi?” “Wee! Yaani mimi niingilie mazungumzo yako na kaka yako? Wewe umelikoroga, nenda kalinywe mwenyewe.” Nanaa akaanza kucheka. “Wewe cheka hapo wakati katangulia ndani. Ndoa unataka au hutaki?” “Ninavyoitaka hiyo ndoa! Ngoja niende nikajibembelezeshe. Tena naenda kumwambia nimepata na majina ya sehemu ya kwenda.” “Wapi?” “Kwani hata najua mimi? Ndio pakushikwa uongo. Bora nijinyamazie.” Mama G akaanza kucheka. Nanaa akasimama.

Alimkuta Geb amekaa kwenye kochi na nguo zake vilevile. “Hivi unaona umuhimu wa hii ndoa kweli?” Geb akarusha swali pale tu Nanaa alipofunga mlango. Nanaa akajua bado anahasira. “Sana Geb. Ninavyosubiria kuja kuitwa Nanaa Magesa! Acha tu mpenzi wangu. Hapa nawaza pakwenda tukafurahie baada ya ndoa yetu. Nimekuandalia mambo moto moto yakukupa kwenye fungate.” Nanaa akamuona ametulia kidogo kama anataka kucheka. “Mambo gani?” “Sasa nikwambie halafu iweje?” “Hivi umeliona hilo tumbo lakini?” “Basi ndio usubiri uone.” Akaenda kukaa pembeni yake.

“Unajua wazi mimi sipendi kurudi nyumbani halafu nisikukute Nanaa.” “Pole mpenzi wangu. Haitatokea tena. Nitahakikisha nakusubiri kwanza. Tuagane ndio niondoke. Umenisamehe?” Geb akabaki anamtizama. “Nijibu basi. Hasira za nini mpenzi wangu? Kwanza niambie wapi tunakwenda kwa fungate.” “Nitajuaje wakati nakuona mwenzangu kama haupo tayari!” “Mie tena! Utaona utayari wangu tukifika huko. Twende basi tukaoge. Au bado unahasira?”  Nanaa akambusu mkono wake kisha akaanza utundu wake pale pale kwenye kochi, wakajikuta kitandani.

“Ndio ulikuwa ukiomba msamaha?” Nanaa akacheka. “Sipendi ukiwa umekasirika bwana. Mimi nilijua vile tulivyozungumza asubuhi ndio nilishakuaga. Vipi lakini? Mambo yameenda vizuri huko kazini?” Akimaanisha labda zile hasira ni za ofisini amekuja nazo nyumbani. “Mambo yameenda sawa tu.” “Hata mimi nimekuwa na wakati mzuri na kaka. Twende tukaoge halafu tukacheze na Liv kabla hajalala.” Nanaa hakueleza kwa undani. Akaishia hapo hapo kama vile Geb ambavyo hakutoa maelezo ya ziada. Geb akazidi kuumia rohoni.

Wakati wanaoga, Geb akaamua aulize moja kwa moja asizunguke tena.

“James anataka nini?” Nanaa akatulia kidogo. “Au ndio anataka kukununulia gari?” Akasisitiza. “Hapana. Ni maswala ya maendeleo tu.” Akajibu kwa kifupi, akionyesha wazi hakuona umuhimu wakumweleza kila kitu. “Maendeleo na kaka yako?” Geb akaendelea kudadisi. “Tulikuwa tukizungumzia maswala ya biashara tu. Hamna hata jipya.” “Kwamba mlishazungumzia kabla ndio maana hamna jipya?” Nanaa akamtizama Geb. Akajua anataka kujua kila kitu. Akanyamaza kwa muda kama anayefikiria.

“Nanaa? Au huoni umuhimu wa kuzungumza na mimi?”“Ni mambo ya kawaida sana Geb.” “Ambayo sitakiwi mimi kujua?” Geb akauliza tena. “Alikuwa akinishirikisha maswala ya biashara zake. Si unajua kaka na yeye anafanya biashara na kazi?” Nanaa akauliza huku akifunga maji wakiwa wamemaliza.

“Nafahamu kuwa anabiashara. Wewe hukuwa ukijua?” Geb akauliza. “Nilikuwa nikifahamu. Lakini alitaka kunishirikisha, yaani kama kufanya naye biashara ili na mimi niwe na kitega uchumi. Kwa kuwa anajua nipo hapa nyumbani na watoto, ameamua kunisaidia niwekeze kwenye biashara zake. Anaona wazo la kununua gari kabla ya kuwa na kitega uchumi ni wazo la kijinga. Ameniambia nahitaji kitega uchumi ambacho kitaweza kununua gari. Ananiambia nisitumie pesa kwa kununulia vitu tu, bali kwa sasa kwa kuwa nyinyi mpo, mnanisaidia usafiri, nitumie pesa ndogo niliyonayo kuizalisha kuliko kuongeza tena gari ambalo hata halina matumizi makubwa.”  Nanaa akaendelea kumsimulia mambo yote mpaka waliporudi chumbani.

“Kwa hiyo kwa kifupi amenishauri au amenikataza kununua gari. Ameniambia lazima kutumia akili kwenye maisha. Bado sijafikia uwezo wa kuwa na gari. Gari litakuja, lakini sio sasa hivi. Sasa hivi natakiwa kufikiria jinsi yakuwekeza kwanza.” Nanaa akatulia kidogo. “Ujue Geb, kaka ananifikiria sana juu ya maisha yangu kwa kila upande. Namshukuru Mungu kwa ajili yake. Mara nyingi huwa najisahau, lakini yeye ananirudisha kwenye mstari. Wakati mwingine najiuliza maisha yangu yangekuwaje bila kaka, sijui Geb!Kuna       mambo nachelewa kufikiria. Kama ungeniambia maswala ya kuwekeza sasa hivi, wala nisingefikiria.” “Labda ukute sio wakati wake.” Geb akaona aongezee.

Alishaona wivu kati ya Nanaa na James. “Unamanisha sio wakati wa mimi pia kutengeneza pesa? Yaani kuendelea kuwa nasubiri kupewa tu pesa nisiwe na kitu changu na mimi!?" Nanaa akauliza na mshangao. Geb akaona anyamaze. “Sidhani kama kuna wakati sahihi na usio sahihi  kwangu Geb. Kwanza ni yeye ndio atanisaidia kufanya hiyo biashara wakati mimi naendelea kulea. Kwa kuwa nilimwambia natamani kuwa na watoto hata watano. Na nikamwambia kama utakubali nitawaunganisha. Kwa hiyo nafikiri aliona nitakuwa nyumbani kwa muda mrefu sana, ndio maana ameamua kunisaidia.” Geb akabaki anashangaa.

“Ni mtu ambaye anataka akinufaika, na mimi ninufaike kwa kila namna. Ana…” “Subiri kwanza Nanaa. Unazungumza idadi ya watoto tutakao zaa mimi na wewe na kaka yako sio mimi mwenyewe?!” Nanaa akatulia kidogo. “Sio kwamba ni mazungumzo yaliyokuwa rasmi. Ni katika maongezi tu ndipo nilipomwambia, shauku yangu! Kwanza aliniuliza kama nafikiria kurudi tena shule. Nikamwambia sifikirii kabisa. Nikamwambia kwa wakati ule nafikiria swala la watoto tu. Ndio akacheka na kuniuliza kwani nataka watoto wangapi? Ndio nikamwambia natamani hata watano kama wewe utakubali.” “Sasa kwa nini hukuniambia mimi mwenyewe?” Geb alishabeba wivu. Alitafuta tu sababu ya kulalamika.

“Geb mpenzi wangu! Mbona kama leo unatafuta sababu ya kukasirika? Kuna nini!?” “Huoni kama ni makosa kuzungumza na kaka yako juu ya idadi ya watoto tutakao zaa mimi na wewe pamoja kabla yangu mimi?” Nanaa akafikiria. “Naomba unisamehe Geb. Tafadhali naomba yaishe. Nilikueleza mazingira ya hayo mazungumzo. Hayakuwa rasmi. Halafu wewe unamjua kaka. Yupo sana karibu na mimi. Hana asichokifuatilia kwangu.” “Kwa hiyo mimi sipo karibu na wewe?” Geb akaendelea.

“Namaanisha nazungumza naye kila kitu! Siwezi kujificha kwa kaka. Anajua kila eneo la maisha yangu tofauti na wewe Geb. Labda niwe muwazi zaidi. Haijawahi kutokea mimi na wewe tukazungumzia maswala ya uchumi. Hata mara moja. Lakini nazungumza na kaka. Ninaishi hapa na wewe. Hatujawahi hata kuzungumzia kesho yangu inakuaje isipokuwa maswala ya sasa hivi tu. Silalamiki wala sioni tatizo kwa kuwa ndivyo mahusiano yetu yalivyo. Lakini kaka ananifanya nisibweteke katika jambo lolote. Anajitahidi kunikumbusha mimi ni nani na ninatakiwa kufanya nini katika kila eneo la maisha yangu. Kuanzia nakua mpaka sasa.” Nanaa akaendelea.

“Yale mapenzi unayoyapata kutoka kwa mama yako. Mafunzo na ulinzi unaopata kutoka kwake, mimi napata kutoka kwa kaka James. Yale unayoyapata kutoka kwa Grace, na mimi nayapata kutoka kwa huyo huyo kaka James. Sina mtu mwingine kwenye maisha yangu isipokuwa kaka. Mungu amempa nafasi zote kwenye maisha yangu. Ndio maana na yeye amekuwepo kwenye kila eneo la maisha yangu bila kuchoka. Watu wote wameshawahi kunisahau hapa duniani isipokuwa kaka James. Hajawahi kutoona umuhimu wangu hata kwa sekunde.” Nanaa akaanza kulia.

“Pale wengine wanaponisahau, na kutoa kipaumbele kwenye mambo mengine, kaka amekuwa na mimi. Na sio kwa kuwa nimekuwa mkamilifu kwake. Kuna mambo mengine nimekuwa nikikosea. Kaka akasimama kama mzazi kwangu kunikaripia na kunijenga. Ulitaka nifanye nini Geb? Mambo yangu mengine ambayo hayapo kati yetu, ulitaka nizungumze na nani? Kosa langu au la kaka ni kunionyesha ananijali au tatizo lipo wapi? Mbona wewe huwa unapata muda mwingi tu wa faragha na mama au Grace, na sijawahi kulalamika na wala huniambii ni nini mmezungumzia, na sijawahi kulalamika? Hapa kosa langu mimi ni lipi? Na si kwamba natoka na kaka kila siku! Mara moja moja tu! Nimeomba msamaha, lakini bado umekasirika.” Hormones za ujauzito zilishapanda. Nanaa alishakasirika mpaka mwisho. Machozi yalikuwa yakimtoka kama mvua.

“Sijakasirika Nanaa.” Nanaa akavaa. “Naomba tulia tuzungumze Nanaa. Sikuwa nimekasirika.” “Naomba nitoke, nikupishe upate muda wakufikiria na mimi nipate muda wakufikiria. Sijui ni nini kinaendelea kwako Geb. Naona umebeba hasira ambayo hutaki tuzungumze yaishe! Naona ni kama unanikandamiza bila sababu! Hivyo, sitaweza. Nimejaribu kukutuliza muda wote. Nimekwambia mpaka mambo ambayo hayakuhusu, pengine utatulia, lakini bado! Acha nikupishe na mimi nitoke hapa nisije nikajiletea madhara.” “Unaenda wapi usiku huu? Usinikasirikie Nanaa.” Nanaa akachukua pochi yake.

“Naomba basi nikusindikize huko unakokwenda.” “Hapana. Nitatumia tu daladala.” Nanaa akatoka huku anafuta machozi.  Geb bado hakuwa amevaa, bado alikuwa na taulo kiunoni. Akaona Nanaa anaondoka, ikabidi kumkimbilia vile vile na taulo kiunoni. “Nanaa! Nanaa!” Nanaa akawa anashuka ngazi huku analia. Akampita mama G pale sebuleni akimlisha mtoto. Akatoka nje bila hata kuzungumza naye. 

~~~~~~~~~~~~~~

“Umefurahi sasa?” Mama yake akamuuliza Geb aliyekuwa katikati ya ngazi. Geb akanyamaza. Alikuwa uchi na taulo tu, asingeweza kutoka. “Nakuuliza wewe Geb. Ulichokuwa unakitaka umeshakipata?”  Kimya. “Shida yako hivi wewe ni nini? Unachotaka hasa hapa duniani wewe ni nini?” “Kwani mimi nimefanyaje? Kwa nini unanilaumu mimi? Kama kosa ni lake je?” “Kinachokufanya umkimbilie ni nini kama kosa ni lake? Mambo uyafanye na kuyapanga mwenyewe, sasa hivi unatapatapa. Sio wewe niliyekupa madhara ya unachokifanya wewe? Sasa hivi wivu unakupeleka kama gari bovu! Wewe si milionea? Basi tulia na mali zako, mwache na yeye atafute mali zake na kaka yake. Acha kujidai umechanganyikiwa.” Mama G akambadilikia.

“Wewe umesahau kama James ni Mchaga na Nanaa amebeba damu ya kichaga? Umemuona vile mama yao anavyohangaika kuitafuta pesa. Unafikiri watamuacha Nanaa amekaa tu hapa kwenye hili gorofa lako, eti kwa kuwa anabiashara ya kukuzalia wewe watoto!? Na usifikiri James hajui kama umejitenga wewe na mali zako! Ametusimulia kwa makini sana jinsi anavyomuhangaikia na kumtazama Nanaa kwa karibu na watu anao ishi nao. Anajua na ndio maana anataka kumjenga na mdogo wake pia!” “Sasa kwani tumeshaoana?” Geb akajaribu kujitetea.

“Sasa kama unajua hamjaoana na kuna mambo hutaki kumshirikisha, unachomkera sasa hivi mtoto wa watu ni nini? Mwache basi. Si unasema bado hamjaona ndio maana unaishi hivyo unavyoishi? Basi acha wivu. Mwache kaka yake amjenge. Mimi nilikuwa na maisha yangu na biashara zangu kabla sijaanza mahusiano na baba yako. Na nilianza biashara akiwa anajua. Alichokifanya alinitafutia mfanyakazi kwa siri ili anifanyie kazi mimi na kumpelekea habari yeye. Tulipoanza mahusiano akatumia akili, akajiingiza kwenye biashara zangu tukawa kitu kimoja. Akili zako wewe ziko wapi? Kama hutaki mshirikiane mali, basi mwache ashirikiane na kaka yake! Acha kujidai umechanganyikiwa wakati nilikwambia kwa mapana madhara yake.” Geb akanyamaza.

          Alimjua mama yake akikasirika. “Kwa hali aliyonayo sasa hivi maamuzi yake mengi yapo ‘so emotional’. Anaamua vile mimba inavyompeleka. Sasa ngoja akatae hii ndoa, ndio utanieleza vizuri.” “Hawezi kukataa. Ni kutoelewana kwa kawaida tu, tutayamaliza.” Mama yake akasimama. Alishamaliza kumlisha mtoto. “Na uombe Mungu yaishe Geb. Utajuta, mimi nakwambia. Utabakishiwa mihela yako hiyo, ndio ujue pesa sio kila kitu. Umepewa msichana anayekupenda na kukujali, basi roho yako haitulii mpaka uharibu!” Mama yake alimbadilikia. Lakini Geb alishamjua akikasirika. 

“Mtoto huyu anakwenda kulala bila kumuona mama yake. Roho yako ikutulie sasa.” “Naenda kumfuata mama!” “Unajua alipo?” Kimya. “Nakuuliza wewe Geb.” “Sijui. Lakini nitaenda kumwangalia hapo nje. Hawezi kuwa ameenda mbali.” “Mungu akusaidie iwe hivyo.” Geb akageuka  akaanza kupanda ngazi. “Na ninakuomba unisikilize Geb. Nataka harusi ifungwe kama tulivyopanga na Nanaa ajifungue mtoto wake akiwa anaishi humu ndani. Sitaki uanze kutibua mambo. Alikuwa ametulia tuli, umeona tunafaidi humu ndani, ukaanza ukorofi wako. Mtoto wa watu hakuwa hata na wazo na mali zako! Umeanza kujishuku wewe mwenyewe, na kutibua amani iliyokuwepo humu ndani. Sasa nikusikie tena. Umenielewa?” Kimya, na yeye hasira zilikuwa zimeshampanda. Kiburi kimerudi. Akaona anyamaze.

“Usinitanie Geb wewe!” “Si nakusikiliza mama!” “Ndio nakuonya. Sitaki ukorofi wako. Umenielewa?” “Kwani mimi nimesemaje?” “Geb usinitibue wewe!” Mama G akasimama na kumtizama kwa hasira  “Nimeelewa. Haya mambo yataisha mama. Naomba usikasirike, presha ikapanda bure. Naomba yaishe.” Geb akajirudi kwa haraka sana. Mama yake akaondoka na yeye akarudi chumbani kwake.

~~~~~~~~~~~~~~

Akavaa kwa haraka, akachukua simu yake ili atoke. Akakutana na ujumbe kutoka kwa Nanaa. ‘Nafikiri inabidi tufikirie kwa upya swala la ndoa. Naona tunataka kuingia kwenye maagano makubwa sana, tukiwa hatujajiandaa. Lazima tukubali kuwa tumetoka kwenye ulimwengu miwili tofauti. Nimeona itakuwa ngumu sana mimi na wewe kuja kuishi pamoja na tukaelewana. Nashauri tupate muda wakufikiria zaidi ili kujua hatima yetu.’ Mwisho.

“Nanaa bwana! Hajanielewa tu.” Geb akawaza na kumpigia. Simu yake ikaita mpaka ikakatika. Akapiga tena. Ikaitaa. Mwishowe ujumbe ukaingia. ‘Nipo sehemu ambayo siwezi kuongea. Nitakutafuta wakati mwingine.’ Geb akashituka sana. ‘Nanaa please! Naomba rudi nyumbani tafadhali. Hukuwa umeelewa.’ Kimya. ‘Nanaa!’ Geb akatuma ujumbe mwingine. ‘Nahitaji muda wakujifikira Geb. Tafadhali nipe muda wakufikiria.’ ‘Unafikiria nini ukiwa peke yako Nanaa? Mwishowe utasikilizishwa sauti nyingine za shetani. Naomba urudi nyumbani.’ Kimya. Wasiwasi ukamwingia, akajua Nanaa hatanii. Akajaribu kupiga, simu haikuwa hewani tena.

~~~~~~~~~~~~~~

Akatoka. “Yuko wapi, maana nataka mtoto anyonye kidogo ndipo alale? Hajala vizuri.” Mama yake akamdaka kwa swali. “Nani?” Geb akauliza akijua wazi ni nani mama yake anamuulizia. “Usinitanie Geb wewe!” “Nanaa amefika tu mbali mama. Yalikuwa mazungumzo ya kawaida kabisa.” “Sasa huu ndio ule wakati wa ile pesa yako na mali zako kufanya kazi. Nenda kaninunulie mwanamke mwingine, aje aninyonyeshee Oliva, akalale.” “Mama!” “Kumbe! Wewe si umegoma kujifunza kutokana na makosa? Unakumbuka huyu mtoto wakati ana mwezi sijui! Unakumbuka ulifanya ukorofi wako mpaka Nanaa akalala hotelini? Sasa naona historia inajirudia. Umeachiwa jumba lako na magari yako hapo nje. Tukuone sasa wewe tajiri.” Geb akatoka nje.

 ~~~~~~~~~~~~~~

Haya tena. Karibu ya harusi, Geb atibua mambo,

Nanaa ameondoka akihitaji muda wakufikiria hatima yao.

Damu ya kichaga bila pesa, huyo si mchaga na wala si James.

Kijana aliyekomaa akili akiwa bado mdogo, sababu ya majukumu ya kulea.

Geb amefika mbali sana kimaendeleo. Anaanzia wapi kujifunua kwa Nanaa? Yeye si anakula na kulala tu? Hata akifa, haoni mtu wakumpokonya mali Nanaa. Sasa tatizo ni nini? Kwa nini James kumwingilia na maisha yake na Nanaa ambaye hakuwa hata na wazo!

Geb & Grace dada yake ni Sawa, lakini Isiwe Nanaa na James!

Usiache kufuatilia kujua yatakayojiri kwenye Mkuki Kwa Nguruwe.

 

 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment