“Mimi
mwenyewe nitajua jinsi ya kuzungumza naye.” “Basi mjitahidi kuamka mapema
mumuandae na mtoto. Mnamjua Oliva anavyopenda usingizi wa asubuhi. Lazima
mumtoe kitandani mapema ili achangamke, ale. Lasivyo mtakuja naye hajala na
amevaa nguo zake za kulalia. Nitaandaa nguo zake za kanisani tayari kabisa.
Hapendi..” “Mama! Mama G! Atakuja Liv ameoga na amevalishwa nguo utakazo.” Geb
alimkatiza mama yake.
“Bwana
nyinyi hamtabiriki bwana! Mnaweza kulala mkapitiliza muda. Mkaniletea mtoto
mchafu.” “Wewe usiwe na wasiwasi.” “Lazima niwe nao. Nawafahamu wewe na Nanaa.
Hamuwezi kutoka huko chumbani kwenu kwa haraka.” Grace na Danny wakaanza
kucheka.
“Jamani!
Na sisi tunaondoka. Tutaonana kesho.” Danny akaenda kuchukua wanae chumbani
walikokuwa wamelala akaanza kuwapandisha kwenye gari mmoja baada ya mwingine
mpaka alipomaliza ndipo akaenda kumwamsha na dada yao anayewasaidia kazi, wakaondoka.
Mama James
Mama
James hakutaka kupotezewa muda. Walipotoka tu pale kwenye kikao, akatembea
mpaka kituoni, akaenda kupanda daladala kuwahi wateja wake. Alijua kabisa
ugomvi utakao kuwa ukiendelea ndani ya gari ya Zinda. Kwani alimuacha Vai na Viola,
wakipanda gari ya Zinda. Akajua huo ugomvi humo ndani ya gari, unaweza
kumchelewesha kwenye shuguli zake. Akamwachia Zinda ahangaike nao. Akimkuta Vai
nyumbani, atajua ameachwa. Asipomkuta atajua Zinda alimchukua.
James.
James
alipohakikisha wanatoka tu getini na mlinzi amefunga geti dogo, na yeye
akapanda gari yake akaondoka. Hakutaka kujua wanapoelekea wala kinachoendelea.
Aliwapita hapo getini na akamuona mama yake anatembea kufuata daladala, lakini
hakusimama. Akaamua arudi tu kwake, akapumzishe akili zake. Kwa muda mfupi
aliokuwa nao walishampa habari mbaya tupu. Aliondoka pale akimlaumu sana mama
yake. Amehusika kwa asilimia zote kuharibika kwa dada zake. Walipo vile kwa
umri ule, hawana elimu yeyote na wala hawawezi kuwekwa ndani kama Nanaa na kuwa
wake. Hawajui kuzungumza. Hawana adabu. Shule hamna kichwani. Hawana ustaarabu.
Hawajui kazi na wazi kabisa wanaonekana ni binti ambao hawajatulia. Wasichana
wazuri lakini hawana maadili. Na ndio siku hiyo na yeye James akajua kuwa mdogo
wake, Vai alitoa mimba na kuoza karibia kifo! James aliumia sana. Aliondoka
pale asijue hatima ya hao dada zake. Alishaishi nao, lakini akashindwa
kuwasaidia.
Zinda & Vai
Zinda
aliwatoa hapo hao mabinti wawili akiwa amekusudia kabisa kumtoa Vai kwenye
maisha yake. Kwanza alishajua hatazaa. Mapenzi ya kitandani pekee hayatamsaidia
kitu. Vai hajui kupika wala kusaidia usafi! Vai hataki ndugu! Zinda akawa
ameshapata majibu yake yote usiku ule. “Vai
hawezi kuja kuwa mke wangu! Uzuri huo hautanisaidia chochote. Utageuka kama
mwiba kwangu.” Zinda aliendelea kuwaza wakati akikanyaga mafuta.
Vai
akashangaa wanaelekea nyumbani kwao. Alipokuwa akiishi zamani na mama yake na
Viola. Alikuwa amekaa kiti cha mbele. “Umeamua kumrudisha kwanza Viola?” Vai
akamuuliza Zinda kwa upole. Alishangaa walivyokuwa wametulia garini. Hawakuwa
wakitukanana tena. Kimya. “Zinda?” Vai akauliza tena. “Tafadhali naomba
nyamaza. Nyamaza hata kwa dakika chache niweze kufikiria. Unaongea sana Vai,
mpaka unanifanya siwezi kufikiria!” “Mbona nimeuliza tu?” “NIMEKWAMBIA NYAMAZA!” Zinda aligomba kwa sauti kubwa sana
mpaka wakaogopa.
“Wewe
ni mtu gani huambiliki? Eti Vai? Itakugarimu nini kumsikiliza mtu kidogo tu, na
kutii bila kujibu kitu?” Kimya. Zinda aliendesha mpaka nyumbani kwao. “Naombeni
mshuke wote.” “Na mimi!?” Vai akauliza kwa upole. “Naomba ushuke Vai. Vitu
vyako nitampa kaka yako akuletee.” “Nitabadilika Zinda.” Vai akaanza
kulia.
“Nimekusudia
kuanzisha familia Vai. Nataka watoto na wewe unaonekana umechezea sana kizazi
chako. Huna uwezo wakuzaa.” “Viola
amekudanganya.” “Mbona hujashika mimba sasa
wakati tumeishi wote kwa miezi takribani mitano sasa?” “Ni kwa sababu nilikuwa nikitumia njia
yakuzuia mimba.” Vai alijitetea. Hakuwa tayari
kurudi kuishi tena hapo kwenye nyumba ya kupanga ya watu wengi. Kurudi tena
uswahilini? Inamaana itabidi aanze kuishi na Viola na kina mama wa pale
uswahilini. Mama yao alikuwa busy na baa yake. Kutoka asubuhi kurudi saa nane
za usiku.
Kule
kwa Zinda alikuwa peke yake na alikuwa akiachiwa pesa kila siku. Anakula
atakacho. Anamlipa jirani kuja kumfanyia kazi. Kazi yake ilikuwa kulala
akimsubiria Zinda. Leo aje kurudi kuishi na kina Viola tena! Uswahilini! Nyumba
ya watu wengi! Hakuwa tayari.
“Njia
ipi ya kuzuia mimba uliyokuwa ukiitumia?” Zinda akamgeukia na kumtizama kwa
makini. Viola akaanza kucheka. “Mwambie sasa njia ipi ya uzazi wa mpango
uliyokuwa ukiitumia kuzuia mimba!” Viola alishabikia. “Naomba utupishe Viola.”
Zinda akamgeukia Viola aliyekuwa amekaa nyuma. Akataka ashuke kwenye gari yake.
Kwani walikuwa wameegesha nje ya hiyo nyumba waliyokuwa wakiishi. Viola
akashuka.
“Umeshanidanganya
vyakutosha Vai. Naomba usiendelee kunidanganya. Mimi nilikupenda, nikaamua
tuishi wote. Ni kweli wote tulikosa. Mimi nimekusudia kubadilika. Naanza upya
bila kinyongo na mtu.” “Na mimi pia Zinda. Nitamuomba Nanaa msamaha. Nitatulia.
Hayo ni maisha niliyokuwa nimeishi zamani. Nakuapia Zinda, nimebadilika mpenzi
wangu. Tokea nimepata yale matatizo, sijarudi kulala na mwanaume tena. Yaani
wewe ndio mwanaume wangu wa kwanza na wala sina tena mpango wa kujichanganya
tena.” Vai akaendelea kujitetea.
“Sawa.
Lakini tatizo litabaki pale pale Vai. Mimi ndio kaka mkubwa nyumbani kwetu.
Nataka familia ambayo wewe huwezi kunipa. Huna uwezo wa kuzaa. Nilikuwa
nikikuangalia na kukufuatilia kwa makini sana Vai. Tulifanya mapenzi kwenye
siku zote za mwezi. Sijawahi kukuona hata ukipata siku zako! Inamaana walikutoa
kabisa kizazi.” “Hapana Zinda.” “Wewe kaa chini jifikirie. Mara ya mwisho kuona
siku zako ilikuwa ni lini?” Kimya.
“Mimi
nakufuatilia kuliko unavyofikiria Vai. Kwa kuwa mwenzio naishi na wewe kwa
akili nikitaka uje uwe mke wangu kihalali. Lakini si kwamba huzai ila huna
kizazi kabisa. Nilishajiuliza sana hilo swali. Inakuaje hupati siku zako?
Mwanzoni nikajifariji labda umeshika mimba, lakini leo ndio Viola amenifungua
macho. Huna kizazi Vai. Tena si kwa kuwa
umezaliwa hivyo au ni bahati mbaya! Hapana. Ni mambo uliyojitakia. Ni mchezo
uliokuwa ukicheza na kizazi chako. Leo unataka na mimi nilipe garama ya maisha
uliyoishi nyuma! Hapana Vai. Sitakuwa tayari kufanya hivyo. Siwezi kukuoa. Mwenzio
ni lazima niwe na watoto. LAZIMA.” Vai aliumia sana.
Yalikuwa
maneno makali ambayo Zinda aliyatamka bila kupindisha. Alijilaumu na kujuta
hata kuanza kuishi na Zinda. Pengine kama sio kuanza kuishi naye angemuoa,
swala la kuzaa wangelijua mbele ya safari!
Zinda
hakumumunya maneno. Mbele ya uso wake alimkataa. “Nakutakia maisha mema. Mizigo
yako itakufuata hapa. Tafadhali usirudi pale kwangu. Nakusihi sana Vai.
Tumeshachafuana vyakutosha. Tushapotoshana vyakutosha. Huwezi kuniongoza kwenye
jema, na mimi nilishindwa kukuongoza kwenye jema. Wote tumeishi maisha ya
kudanganyana tu na kuumiza wengine. Tafadhali shuka kwenye gari yangu.” Vai
hakuwa akiamini kama yule ni Zinda aliyekuwa akihangaika kumpa penzi mchana na
usiku. Tena wakati mwingine alijituma zaidi ya uwezo wake ili tu kumfurahisha.
Leo Zinda anampasukia bila huruma wala aibu!? “Vai!” Zinda akamshitua. Vai
akafungua mlango na kutoka.
Zena Tena Kwenye Maisha Ya Nanaa.
Geb
aliingia chumbani akamkuta Nanaa amejilaza kwenye kochi na tv ipo wazi. “Mbona
hujalala?” Geb akauliza. “Si umesikia nimefukuzwa pale chumbani kwa mama?” Geb
akacheka. “Kwa hiyo hapa navuta muda ili nichelewe kulala, usiku nisiamke.”
“Ukiamka, niamshe mimi.” “Nakuonea huruma Geb. Unakuwa umechoka halafu wakati
mwingine unatakiwa asubuhi kwenda kazini. Kama leo ndio siku yako ya kulala kwa
kuwa huendi kazini na ibada ni saa 4 asubuhi. Naona heri ulale tu. Lakini mama
najua hata mchana anaweza kurudi kulala kama asipoamua kwenda kazini.” Geb
akakaa.
“Sasa
mbona na simu mkononi?” “Nilikuwa na chat na Zena. Wameamua kuona na Yasini.
Wazazi wao wamewakubalia ndoa ya mahakamani. Wamemkubalia kuolewa na mkristo,
lakini wamemkataza kubadili dini. Anasema walifanya kazi ya ziada mpaka
kukubaliwa na wazazi pande zote mbili. Namuonea wivu!” Nanaa akaongea kwa
unyonge. Geb akamtizama na kuamua kuuliza.
“Wivu
wa nini?” “Amepata mwanaume anayempenda na anamuoa.” Geb akanyamaza. “Kesho
ameniomba nihudhurie kikao chao cha harusi. Kila nilivyojaribu kumkatalia, kama
unavyomjua Zena, hajuagi jibu la hapana. Ni nusu saa sasa tokea tuanze
kubembelezana. Anasema amenitafuta sana bila mafanikio. Anasema alimuomba Jeff
amlete mpaka pale tulipokuwa tukiishi zamani. Mlinzi akawaambia tumehama na
hawezi kuwaambia tulipohamia. Alinipigia simu, hakunipata. Si unakumbuka
nilibadilisha namba ya simu? Ukasema
nitoe mpaka Whatsapp? Nilitoa mpaka Facebook na Instagram. Leo nimekaa tu hapa nikasema nirudishe Facebook,
ndio akaniona online akaanza kuninyeshea mvua za jumbe za kutaka nihudhurie
kikao cha kesho.” Geb akabaki kimya anasikiliza.
“Mbona
sasa husemi kitu?” “Nakusikiliza Nanaa.” “Nataka kesho kwenda na mimi kwenye
kikao chao cha harusi.” Geb akabaki kimya. “Geb?” “Umesema unataka. Sasa
sijui natakiwa kusema nini Nanaa! Ndio nakusikiliza. Maana unanipa taarifa.
Sijui natakiwa kusema nini?” Nanaa akatulia kidogo. “Basi nimekosea kuongea
mpenzi wangu. Nahisi ni kama nimechanganyikiwa, sijui!” “Nini chakukuchanganya?”
“Naona wenzangu wote wanaolewa Geb. Mimi nimebaki…” Nanaa akasita kidogo.
“Halafu
wote wanakazi! Wameajiriwa! Mimi nipo tu.” Nanaa aliongea kwa kulalamika.
“Unataka na wewe kufanya kazi?” Geb akamuuliza taratibu tu. “Sijui! Naona nakaa
tu bure. Hamna maendeleo yeyote yale! Nipo tu.” Geb alimjua Nanaa. Muda mfupi
tu aliofungulia mtandao, tayari walishamchanganya. Alishapitia page za marafiki zake huko Facebook.
Akaona hili na lile. Wengine wakijinadi wamesafiri kikazi nchi hii. Wengine
wakionyesha pete za uchumba walizovalishwa na sherehe kubwa. Kuna waliomaliza
nao chuo ameona picha zao wakiwa wanaolewa.
“Kama
Natuja. Hakuwa hata na mchumba. Nimeona amepata mchumba. Amevalishwa pete ya
uchumba. Wakafanyiwa sherehe kubwa. Mwezi uliopita ameolewa. Nimeona picha zao.
Alipendeza kweli! Na akatuma picha zao za honeymoon. Sijui walienda wapi!?
Lakini zilikuwa nzuri kweli. Zena ndio aliniambia niangalie. Na kesho nae
atakuwepo kwenye kikao. Halafu kumbe na Tia naye amechumbiwa! Alipata kazi hapa
hapa Dar. Anaishi hapa. Kesho pia atakuwepo kwenye kikao na mchumba wake. Tena
nasikia amepata kazi nzuri tu. Yaani anatumia elimu yake na inamwingizia pesa
yake.” Geb alibaki akimsikiliza Nanaa anavyolalamika na kujiona ameshindwa na
kupitwa na kila mtu.
~~~~~~~~~~~~~
Pete yake ya uchumba alivalishwa kitandani na Geb.
Hapakuwa na sherehe yeyote ile. Wala hakuwa na kumbukumbu ya picha wakati
anavalishwa. Alishasahau furaha aliyoipata siku alipoamka na kuikuta ile pete
kidoleni mwake. Geb alipomtambua kama ni wake wa milele. Kwa muda mfupi sana
alipowasiliana na Zena, akasahu wajibu mkubwa unaomkabili wakati huo. Nanaa
alikuwa akiingiza pesa nzuri tu kila mwezi. Ni kama Geb alikuwa akimlipa
mshahara bila yeye kujua. Alikuwa akimwambia ni pesa yake ya matumizi. Lakini
kwa kiasi kile cha pesa kupewa kila mwezi, Nanaa ambaye hakuwa akinunua chakula
wala kulipa kodi na garama yeyote pale ndani, pesa yote ile haikuwa ya matumizi
tu. Ulikuwa mshahara kabisa.
Geb
alifanya vile ili asijione tegemezi na kujikuta anamuomba pesa mara kwa mara.
Alikuwa akimuwekea benki, na nyingine alikuwa akimletea nyumbani. Na bado
hakuacha kumgaramia mahitaji yake binafsi. Lakini kama kawaida ya Zena. Aliweza
kuingia kwenye akili za Nanaa, na kumshawishi vilivyo. Alijikuta muda wote
aliokuwa akizungumza naye Zena alikuwa akimpa maendeleo ya huyu na yule, lakini
akashindwa kujisemea chochote. Hakuweza hata kumwambia habari za Oliva na kama
anatarajia mtoto mwingine na anaishi na Geb. Aliishia kumwambia, ‘nipo tu.’ Akaonea aibu kila kitu kinachoendelea kwenye maisha
yake.
~~~~~~~~~~~~~
“Sio
kama nalalamika. Nilikuwa nakwambia tu.” Baada ya mazungumzo ya ulalamishi na
kugundua Geb ametulia akimsikiliza bila kuongeza neno, akaona atulie. “Zena
anahabari za kila mtu. Kwa hiyo ni kama alikuwa akiniambia maendeleo yao.”
Nanaa akaendelea. “Anasema hata Jeff naye anatarajia kufunga ndoa.” Akaendelea.
“Halafu Jeff na Yasini walifungua biashara yao. Wanashirikiana. Anasema sasa
hivi wanapesa sana. Biashara inawaendea vizuri, japo bado wameajiriwa.
Ameniambia wakioana tu wanahamia kwenye jumba lao. Anasema Yasini alinunua
jumba huko maeneo ya Mbezi beach. Yaani karibu kabisa na baharini. Ilikuwa ikiuzwa
kwenye mnada. Nasikia mwenye nayo alishindwa kuilipia, yeye Yasini akainunua.
Ipo kwenye marekebisho kidogo tu, wahamie. Anasema kuna mambo hawajayapenda
kwenye hiyo nyumba ndio wameona wayabadilishe. Hasa vyumbani na jikoni.
Wametafuta ‘contractor’ ndio
anayewashugulikia. Hawakutaka hawa mafundi wa kawaida. Mwenyewe Zena anawaita ‘fundi njaa’. Wamekodi kampuni ya ujenzi
kabisa ili kushugulikia hiyo nyumba yao.” Geb alibaki akisikiliza.
~~~~~~~~~~~~~
Geb
mtoto wa mjini. Anajua pesa. Anajua maisha jinsi yalivyo. Alishaujua udhaifu wa
Nanaa wakumwamini Zena hata anapomdanganya, haoni. Habari nyingi alizokuwa
akieleza Nanaa pale, alizoambiwa na Zena, zilikuwa na maswali mengi sana,
lakini si kwa Nanaa. Nanaa aliendelea kusifia huku akijiona yeye duni.
~~~~~~~~~~~~~
“Na
amesema Yasini amemwambia ni kama wameanza nae maisha. Kwa hiyo kila kitu
wanachonunua sasa hivi, kinaandikwa majina yao yote mawili. Kama hiyo nyumba,
ni ya kwake yeye na Yasini. Wameshashugulikia hati ya nyumba. Ina majina yao
yote. Yaani kila kitu chao wanachonunua, ni cha wote wawili. Anasema kasoro
gari alilomnunulia ndilo ameandika jina la Zena tu. Ujue sijaamini Geb!? Zena
mpanda daladala kama mimi, eti sasa hivi anaendesha gari! Tena gari yake kwa
jina lake!” Nanaa akaendelea.
“Lakini
wao wameanzia mbali. Si unakumbuka nilivyokusimulia juu yao? Alimkuta Yasini
hana kitu. Kwa hiyo kwao wao nirahisi. Yaani kama ni vitu, wameanza kununua
pamoja. Inakuwa rahisi. Hakumkuta Yasini na mali yeyote. Nafikiri ndio maana
Yasini anamthamini sasa hivi. Ujue sio rahisi kupata msichana anayekuvumilia
wakati wa shida mpaka ukafanikiwa?” Nanaa aliendelea kuongea bila kujibiwa, na
kwa kuwa alikuwa na mengi yakuongea hakutaka kupoteza muda. Alimjua Geb ni
mkimya sana. Ni heri aendelee kuongea tu.
“Sasa
nafikiri ndio maana Yasini anamthamini sasa hivi. Anasema alimvumilia sana.
Ndio maana sasa hivi anamuenzi. Anasema amemnunuliwa gari nzuri sana. Nimesahau
jina. Ila amesema baada ya harusi, wataenda kupumzika nje ya nchi. Wapo kwenye
kutafuta ni nchi gani waende kwa fungate. Si unajua wao ni rahisi? Hawana cha
mtoto wala Zena hana mimba. Kwa hiyo hawana mtu wakumfikiria ila wao tu.
Wanaweza kwenda popote baada ya harusi yao.” Tayari Zena alishafanikiwa
kumuonyesha Nanaa kuwa, swala la kuwa na watoto wakati ule ni mzigo. Na yeye
hakukosea kutoa ile mimba iliyokaribia kumuua mpaka akalazwa hospitalini, Nanaa
akamuhudumia mpaka akapona.
“Yaani
Zena amejawa furaha!” Nanaa akaendelea. “Ameniambia nguo zake za harusi na
Yasini wanafikiria kwenda kutengenezewa China. Anasema ndugu yake mmoja Yasini
amewaambia China wanatengeneza nguo nzuri sana. Na watapata vitu vizuri zaidi
vya harusi. Kwa hiyo ameniambia wanatafuta weekend moja wakimbilie China kwa
kufanya shopping. Ila Zena ana roho nzuri! Ameniambia kama nataka kumuagiza
kitu, nisiwe na wasiwasi. Japokuwa atakuwa na mizigo mingi ya kubeba wakati
anarudi, lakini atanibebea na ya kwangu. Yaani Geb, ukimsikiliza Zena, hapo
ndipo utajua Mungu yupo. Na humpa yeyote amtakaye. Zena anazungumzia kupanda
ndege! Tena sio ndege za lisaa! Ndege ya kwenda nchi yeyote. Yaani kama utani
tu. Zena tulikuwa naye kwenye maisha kama haya haya tu. Lakini ona Mungu
alivyomwinua!” Tayari Nanaa alishasahau utajiri mkubwa unaomzunguka hapo.
~~~~~~~~~~~~~
Muda
mfupi sana kabla hajazungumza na Zena wala kuingia Facebook,
Nanaa alikuwa kwenye shukurani kubwa sana. Aliingia pale chumbani kutokea chini
alikowaacha kina Viola. Alipokuwa akijinadi mbele za watu Mungu amempa masikio
mengine na mdomo mwingine, yaani Geb. Ameamua kumpumzisha yeye. Aliingia
hapo chumbani kwa furaha na shukurani akifurahia vile Mungu alivyombariki
kutoka mavumbini mpaka gorofani.
Akiwa
na ndugu mmoja tu James. Aliyekuwa amebeba kofia zote za ubaba, mama, rafiki wa
kweli, dada na kaka. Gafla Nanaa anajikuta Mungu amempa mama wa kweli, mama G.
Dada ambaye anampenda wala hamuoni kama ni wifi, Grace. Rafiki wa kweli wa
wakati wote. Mume na mfariji wake ambaye hawezi kulala mbali naye. Furaha yake
ni kumuona yeye anafuraha. Hata akifanya naye mapenzi, alimuonyesha ni kama
ndio amebahatika mara ya kwanza ya kulala na yeye mrembo. Na alifanya naye
mapenzi kana kwamba hatabahatika tena. Geb.
Nanaa
alikuwa akimshangaa vile anavyofurahia penzi lake hata kama akimkuta bafuni au
hapo kwenye kochi. Vile anavyomfurahia mikononi mwake! Hakukosa sababu ya
kusifia mchezo aliopewa. Kama hakusifia joto la siku hiyo, basi ulaini wa mwili
wa Nanaa, mikononi mwake. Vile alivyofurahia kumshika kila sekunde waliyokuwa
wakifanya naye mapenzi. Ilimradi tu, kumfurahisha Nanaa.
Lakini
Zena aliyabatilisha yote. Akamfanya ajione na kusahau kila kitu. Akajiona
amepitwa. Hana anayemjali yeye kama anavyojaliwa Zena! Akaona mkono wa Mungu
juu ya Zena wala si kwake! Akaona maisha yake yeye mwenye mtoto na kupata
bahati ya ujauzito tena, si kitu! Nanaa akasahau kabisa orodha ya wasichana
wengine wanao jielewa. Wazuri na wasomi waliokuwa wakitamani bahati na heshima
aliyopewa yeye na Geb. Kuzaa naye na kumtamka kuwa ndiye mwanamke wa pekee
maishani mwake!
Tokea
atendwe na msichana. Tena akiwa bado kijana mdogo tu. Chuoni. Geb alipokutana
na Nanaa, ndipo anajikuta ni msichana wa pekee anayeweza kuishi naye. Ni kweli
alishakuwa na mahusiano na wasichana wengine. Lakini hisia alizozipata kwa
Nanaa, akajua ni wake. Na akaelewa ni kwa nini nafsi yake ilikuwa ikimtafuta
Nanaa kabla hata hajamuona. Alijikuta popote alipo, yeyote aliyenaye kwa wakati
huo, haondoi haja yakutaka kujua pale alipo Nanaa. Alimuulizia mara kwa mara,
hata yeye mwenyewe asijue ni kwa nini anamuulizia.
Alishajua
Nanaa alikuwa kwenye mahusiano ya wanaume tofauti tofauti. Lakini hakuacha
kuulizia maendeleo yake. Hakuwa akijua ni kwa nini anajikuta anasukumwa
kumtafuta James na kumuulizia alipo mdogo wake huyo, mpaka siku alipomuona
Nanaa, na kupata nafasi ya kuzungumza naye. Ile hali ya kuwepo na Nanaa kwa
mara ya kwanza na kufanya naye mazungumzo mafupi pale beach wakaingiliwa na
Grace akimtaka Geb amrudishe mtoto wao Fili nyumbani, iliibua shauku yakutaka
kupata nafasi ya kuzungumza na Nanaa zaidi.
Busu
alilolipata siku ya kwanza Nanaa akiwa amelala kitandani baada ya Liz kuingia
na kumkuta Nanaa anatoa mwiba kidoleni mwake, liliamsha hisia za tofauti!
Aliipenda midomo ya mwanadada huyo. Hakuna jinsi au mahali ambapo Geb alitaka
kumbusu Nanaa, akajizuia. Aliipenda kuinyonya midomo yake kila wakati. Wakati
mwingine Nanaa alimuona akifika kileleni kwa haraka akiwa anambusu yeye.
Siku
ya kwanza kuonja penzi la Nanaa, wakiwa mjini Morogoro, Geb alijua ni kwa nini
alimtaka sana Nanaa. Alikata kiu yake na kuibua kiu nyingine ambazo ni penzi la
Nanaa pekee lilimwakikishia ndio lina uwezo ya kukata kiu hiyo. Hakuwahi
kuchoka kumpapasa pale alipofanikiwa kumuweka mikononi mwake. Macho yake
hayakuweza kufunga pale Nanaa alipokuwa uchi mikononi mwake. Akili zake
zilitulia kwenye mwili wa Nanaa, nakujikuta hatosheki kutazama pale macho yake
yalipoangukia. Nanaa alikuwa akimuona vile anavyofurahia akimpapasa. Alimuona
vile hisia kali zilivyokuwa zikiibuka kwa Geb kila ampapasapo. Kwa muda mfupi,
Zena alifanikiwa kuweka giza kali kwenye kumbukumbu zote za Nanaa. Akabaki
akimuona yeye tu na mafanikio yake.
~~~~~~~~~~~~~
“Naona
tulale tu. Najua umechoka.” Nanaa akaona ahitimishe. Hata yeye alishachoka
kuongea. Kwanza ni kama aliyamaliza yote. Akasahau kuwa jumapili ndio siku ya
familia. Geb aliipenda hiyo siku. Kwa kuwa ndio siku pekee yenye uhakika, mara
nyingi hakuwa akihitajika kazini. Aliitumia hiyo siku na Nanaa na Oliva. Siku
nyingi za jumamosi alikuwa akienda kazini. Tena wakati mwingine mpaka jioni au
usiku.
Akajiweka
sawa. Akakaa. “Umeniletea nini hapo. Nataka nile ndio tulale.” Geb akasogolea
bakuli alilopewa na mama yake, lilikuwa kwenye sinia na kufunikwa vizuri.
“Amenipa mama. Hata sijafungua! Aliniambia nikifika huku nikuwekee kwenye
friji.” Nanaa akacheka. “Kweli amekusudia kunifukuza!” Geb akafunua. “Ni
matunda.” Kisha akamtizama Nanaa. “Anajua wazi mimi sishibishwi na matunda.
Hapo ndio ananitaka nimfuate usiku.” Geb akacheka kidogo. “Lakini haya matunda
ni mengi Nanaa.” “Siwezi kushibishwa na matunda hata kidogo. Yaani hicho ni
kianzio cha kudhibiti njaa.” Geb alimjua Nanaa jinsi anavyopenda kula. Hata
kabla ya ujauzito, Nanaa mpenda kula.
“Kwanza
hujanijibu Geb.” “Juu ya nini?” Nanaa aliongea mambo mengi sana mpaka Geb
hakujua anatakiwa kujibu nini. “Nazungumzia juu ya kuhudhuria kikao cha harusi.
Wala huna haja ya kunipeleka. Ni muda wa jioni. Tukitoka kanisani, tuwe wote.
Hiyo jioni nitachukua hata daladala nitaenda na kurudi. Ili wewe upumzike tu.”
“Sasa hapo nilitakiwa kujibu nini?” Geb akauliza. “Geb jamani! Labda
nilizunguza tu vibaya. Lakini ndio nilikuwa nikikuomba ruhusa mpenzi wangu! Sio
kwamba nilikuwa nakutaarifu. Naona umuhimu wa mimi kuwepo. Kwanza itakuwa njia
moja wapo yakukutana na wenzangu. Japo naona aibu kidogo.” “Aibu ya nini?” “Si
unajua na mimba ya Liv niliibeba chuoni? Walinisema sana. Zaidi Zena na Tia
ndio walikuwa viongozi. Wakasema nimeshikishwa mimba halafu nikakimbiwa. Sasa
wataniona tena safari hii naenda na tumbo jingine sina ndoa!” Nanaa akaongea
kinyonge kidogo.
“Naona
labda nisiende tu. Nitulie. Nitamwambia mchango wangu nitatuma.” Akabadili mawazo.
“Kwa hiyo unatuonea aibu mimi na watoto wangu?” Geb akamuuliza. Nanaa akashituka
kidogo. “Hapana Geb! Siwaonei aibu kabisa. Kwanza namshukuru Mungu kwa ajili
yenu. Ni vile naona kuepusha maswali mengi na kujiumiza.” “Kujiumiza!?” Geb
akauliza huku akimtizama. Akapoa.
“Nanaa?”
“Sio kwa nia mbaya Geb!” “Unaogopa kuonekana na mtoto wangu!? Sijawahi kukukana
wewe wala mtoto wangu. Sijawahi kukuonea haya mbele ya mtu yeyote yule Nanaa!
Sijawahi kukuficha kwa yeyote! Wakati wote nimekutanguliza wewe na watoto wangu,
tena bila kificho! Sina kitu wala mtu ninayemuona wathamani maishani mwangu ila
wewe.” “Hata mimi Geb. Samahani kama umeona kama nakukana au nakuonea haya. Ni
vile nilitamani nikija kuonana na hao watu angalau niwe nimewafunga midomo
katika hili. Sasa najiona ni kama nitaenda kuwapa sababu ya kunisema zaidi.
Naomba usinielewe vibaya.” Nanaa akajisogeza karibu ya Geb.
“Nakupenda
Geb. Na wewe unajua kabisa sina maisha mengine wala mtu mwingine ila wewe.”
“Hayo ulimwambia na Zena?” “Zena ni mbea Geb. Anahamisha maneno hapa na pale.
Sikutaka habari zangu na zenyewe ziwe gumzo.” “Au ulijisikia kama huna
kitu kizuri cha kumwambia?” Nanaa akababaika sana. “Nanaa? Au unahisi una maisha mabaya ambayo
huwezi kuwaambia watu?” “Hapana Geb. Zena ni mbeya sana. Msambaza maneno.
Huwezi amini kwa muda mfupi tu nimezungumza naye amenipa habari za watu karibia
darasa zima.” “Kama unalijua hilo, kwa nini unamfungulia mlango mpaka wa moyo
wako? Kwa nini unamruhusu kuharibu akili zako? Kwa muda mrefu sana tokea
umetoka kwenye mitandao, ulikuwa umetulia Nanaa!”
“Ni
juzi tu ulikuwa ukinishukuru kwa fulsa niliyokupa yakukaa nyumbani na kumlea
Liv. Ukasema huna mtu ambaye unamfikiria kumwamini kumuachia Liv, kama ikitokea
wote, wewe na mama mnatakiwa kwenda kazini! Ulishukuru kwa machozi Nanaa.
Nikakwambia tumshukuru Mungu pamoja kwa uwezo aliotujalia. Hasa nguvu. Mimi amenipa
nguvu yakufanya kazi, na wewe uwezo wa kumudu hii familia.” Geb akaendelea
kumkumbusha.
“Nikakwambia
hakuna mtu sahihi ambaye anaweza kulea watoto wetu na kuendesha mambo ya hapa
nyumbani vizuri isipokuwa wewe Nanaa. Wote tukakubali huku tukimshukuru Mungu
kwa pamoja. Tena tukiwa kwenye kochi hili hili tulilokaa sasa hivi. Unakumbuka
tukamshukuru Mungu kwa pamoja na kumsihi Mungu aendelee kubariki biashara zetu,
na kutuimarisha sisi wenyewe? Unakumbuka Nanaa?” Nanaa alishaishiwa nguvu.
Machozi yalishaanza kumwagika.
“Leo
Zena anakufanya uyatupilie mbali maisha Mungu aliyotubariki nayo!” “Hapana Geb. Sijasahau.” “Kweli Nanaa?” Geb akauliza kama kumsuta kidogo. “Labda nimepitiwa tu Geb. Nisamehe mpenzi
wangu. Nimepitiwa tu. Sikuonei haya.” Geb
akatulia kidogo.
“Unakumbuka
nilikuuliza uniambie chochote unachotaka. Ukasema unataka ndoa tu?” Kimya huku
akifuta machozi. “Leo unajiita mpanda daladala! Unataka uache magari hapo nje,
ukapande daladala! Ili iweje Nanaa? Unajitenga na kila kitu changu! Kutoka
kwenye kutambua kuwa hizi mali zote ni zetu. Mungu ametupa kwa upendo, leo
imekuwa vyangu kwa kuwa nilianza maisha kabla sijawa na wewe!” “Sijamaanisha hivyo Geb!” Nanaa akajitetea.
“Kweli
Nanaa?” “Naomba
unisamehe. Na Mungu anisamehe. Unafikiri nimekufuru?” “Ndiyo Nanaa! Umekufuru sana.” Geb alimjibu bila
kumumunya maneno. “Naomba unisamehe
Mungu wangu. Nimekosa. Nimenung’unika. Nisamehe. Nisamehe mpenzi wangu. Kuna
jinsi nimeruhusu maneno ya Zena yaniingie. Nikasahau yale yanayonizunguka.
Nisamehe.” Nanaa akajirudi kwa haraka. “Naumia
kukuona unanung’unika Nanaa! Najitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu kukuridhisha.
Na ninakuomba kama unaona kuna mahali napelea, uniambie.” “Hupelei Geb. Ni kweli unanipa kila
ninachotaka na hata mengine sikuwahi kuyafikiria.” Geb akamtizama vizuri.
“Kweli Geb.” Nanaa alijaribu kumuhakikishia.
“Naomba uwe muwazi Nanaa. Kama unataka kazi, mimi nafahamiana na watu wengi tu.
Naweza kukutafutia kazi. Na ukitaka pia, unaweza pia kuja kufanya kazi pale
ninapofanya kazi mimi. Nitamtafutia Oliva mtu wakunisaidia mimi kumtunza
mtoto wangu. Nitagawa muda wangu. Kazi na Oliva, ili uwe huru kufanya
unachotaka. Sitaki ujihisi mimi na watoto wangu tunakufanya usiishi
ndoto zako.” Nanaa alilia sana. Alijua Geb ameshakasirika. “Nisamehe Geb. Nisamehe mpenzi wangu. Nahisi
nimekuudhi. Nisamehe. Tafadhali. Naomba nisamehe. Nimekukosea. Nisamehe Geb.” Nanaa aliombeleza akapiga na magoti.
“Nimekuudhi Geb, nisamehe mpenzi wangu! Ninataka kumlea Oliva mimi mwenyewe.
Naomba usinikasirikie Geb.” “Hapana Nanaa.
Mimi sijakasirika. Ila nataka tuwekane sawa. Sitaki umuone Liv ni mzigo. Huyo
mtoto nina mthamini kuliko kila kitu changu. Nampenda sana. Hata huyo
aliyekuwepo tumboni namsubiria kwa hamu sana. Binafsi najiita mbarikiwa
kwa sababu ya hao watoto pia. Hawapo hapo kwa bahati mbaya Nanaa! Nilipanga na
kumuomba Mungu. Kwangu sio mzigo na wala hawapo kwenye maisha yangu kwa bahati
mbaya.” “Nisamehe tu Geb.
Naomba nisamehe. Hakika nimeongea bila kufikiria. Naomba nisamehe. Nimekiri nimekosa.
Naomba yaishe.” Nanaa aliendelea kuomba msamaha
wa machozi huku amepiga magoti.
“Nisamehe Geb.” “Yameisha. Ila achana na Zena.
Anakuchanganya akili. Kesho unajua ni siku yangu na nyinyi. Siku pekee kwenye
juma! Lakini ulikuwa radhi kuniacha kwa aibu ili uende kwake peke yako! Naomba
mwombe budget yao ya kikao. Tuchague kitu kimoja, tuwasaidie basi. Lakini sio
wewe kwenda huko kesho. Ikitokea unataka kwenda iwe ni siku nyingine ambayo sio
siku yangu, na tunakwenda wote. Ni sawa?” “Nimeelewa. Samahani.” Nanaa akarudia.
“Naomba
basi ukae hapa na umtumie ujumbe. Atume hiyo budget nzima, halafu umwambia
atuambie ni wapi kesho atakuwepo, tukitoka kanisani tumpitishie hiyo pesa au
hundi.” Nanaa akabaki amepiga magoti huku ameinama anafuta machozi. “Niangalie
Nanaa.” Nanaa alianza kulia tena. “Mimi sitakudanganya, kwa kuwa nakupenda.
Nipo kukuongoza na kukusaidia. Hivyo hivyo na wewe kwangu.
Zena sio rafiki unayemuhitaji kwa
sasa. Anakuchanganya tu. Umenielewa?” Nanaa akatingisha kichwa kukubali. “Kama
unaona muda umekwenda sana, utamtafuta kesho.” Nanaa akajifuta machozi, akavuta
simu yake.
Akakuta
bado Zena anamtumia ujumbe. “Bado yupo macho. Ametoka kunitumia picha za hoteli
wanazofikiria kwenda mara baada ya fungate.” “Basi mtumie huo ujumbe.” Akiwa
amepiga magoti vile vile akaanza kutuma ujumbe. ‘Picha ni nzuri
Zena. Hongera. Lakini kesho sitaweza kuhudhuria kwenye kikao. Ni siku yangu na
familia yangu. Huwa tunaitumia kuwa pamoja na mpenzi wangu, baba watoto wangu
na watoto wetu. Ila nimezungumza naye sasa hivi, amekubali kusaidia kwenye
harusi yako. Naomba unirushie budget yenu, halafu sisi tutachagua kitu cha
kuchangia.’ Akatuma huo ujumbe.
Nanaa
aliona kabisa kuwa alisoma. Akamuona anaandika, kisha anaacha. Akafanya hivyo
mara kadhaa, mwisho ukaingia ujumbe mwingine. ‘Budget yetu
ipo juu sana. Tumeamua kufanya harusi nzuri na ya kisasa. Sidhani kama mtaweza.
Hata hivyo hamna haja. Kama hutaweza kufika basi.’ Geb na yeye alikuwa akisoma. Nanaa akamwangalia
Geb. “Atakuwa amekasirika.” Nanaa akaongea kwa upole. “Tunaweza kupitia kwenye
hicho kikao kesho kwa muda mfupi wakati tunampeleka Liv kucheza. Si lazima mimi
na Liv tukaingia. Tunaweza kukusubiria kwenye gari.” “Uliniambia umenisamehe
Geb!” “Nakwambia kwa nia nzuri tu. Sina hila ndani yake.” “Sasa kwa nini ubaki
kwenye gari tena?” Nanaa akauliza akijua wazi bado Geb anamfikiria anamuonea
aibu.
“Hujanikaribisha
Nanaa! Wewe ndio umekaribishwa huko. Ukitaka tukusindikize mimi na Liv,
tutakufuata. Unajua hakuna sehemu ningependa kuwepo isipokuwa sehemu ulipo
Nanaa.” Nanaa akaanza kulia tena.
“Basi naomba mnisindikize Geb. Nitafurahi tukiongozana wote.” Geb akamvuta mkono na kuubusu. “Nakupenda Nanaa.” “Na mimi nakupenda Geb. Nisamehe tu. Sijui
niliingiwa na nini! Naona nilishakuwa nimechanganywa na kina Vai, halafu nikaja
hapa nikakutana na Zena naye. Nikajirudisha kule Mungu aliponitoa. Nisamehe.
Najua unanipenda sana na kunijali Geb. Nimekufuru kujishusha kwa kiasi hicho.
Nisamehe.” “Yameisha. Kula basi tulale.”
Nanaa akajifuta machozi.
Akamuona
anacheka kama mwanae Liv. “Unacheka nini sasa?” Geb akamuuliza. “Kusimama hapa
ndio shuguli. Naona huyu mtoto atatoka mrefu kama wewe. Miezi saba ndio tumbo
lote hili!” Geb akacheka kidogo, akasimama na kumsaidia kusimama. “Usikimbilie
kupiga magoti bwana! Hukuwa na sababu ya kufanya hivyo.” “Nilijisikia vibaya
Geb. Sikutaka nikuumize. Najua unanijali sana na kunihangaikia. Sitaki
nikuudhi.” “Yameisha.” “Mbona sasa hata hunikumbatii?” Nanaa akalalamika. “Wewe
unajua nikikukumbatia sitakuacha hivyo hivyo. Nataka ule kwanza.” “Mimi
nakutaka wewe kwanza.” Geb akacheka. Wakasahau hata habari za Zena. Wakahamia
kitandani. Mapenzi yakaanza.
Jumapili.
Nanaa
alimka akaanza kumtafuta mama G. “Mbona mama hayupo?” Geb alisahau kumwambia.
“Mama alitangulia kanisani. Anamazungumzo na mchungaji.” Nanaa akakaa kama
aliyeishiwa nguvu. “Kwani ulitaka nini?” “Kila kitu! Mimi sijui chakufanya hapa
ndani bila mama. Atarudi?” “Acha kupaniki Nanaa. Kila kitu ameandaa ndio
akaondoka. Tutamkuta huko huko kanisani.” “Na huyo Liv? Ujue ndio anashida humu
ndani kuliko kila mtu!” Geb akaanza kucheka.
“Kweli
Geb. Huyo mtoto anamuwezea mama tu. Liv hapendi kuchana nywele wala kubadilishwa
nguo. Bibi yake ndio anamuwezea.” “Mimi nitakusaidia.” “Haya twende ukajaribu
uone. Kwanza kumuamsha hapo ni shuguli. Na akiamka ujue hutamgusa kichwa.
Ataishia kukuchekea huku akiweka mikono yake kichwani anakuzuia usimchane. Na
unamjua mama. Ukimpelekea mtoto asivyotaka yeye, atakasirika.” “Olivia hawezi
kunishinda. Wewe twende tukale, tukiwa tayari tumwamshe.” Wakashuka chini.
Walishakuwa
wameoga na kuvaa tayari. Wakala. Ilipofika saa tatu kamili ndipo Geb akaenda
kumwamsha Oliva. Alimwamsha mpaka akachoka. Akamtoa kitandani bado amelala. “Si
nilikwambia mimi. Huyo shuguli yake mpaka bibi yake. Hapo hatafungua macho
mpaka aamue mwenyewe.” Geb akaanza kucheka. “Jamani Liv wewe!? Amka bwana.” Liv
aliendelea kulala. “Mimi nambadilisha diaper nambeba hivyo hivyo. Tutambadili
mbele ya safari. Hatuwezi kuchelewa kanisani sababu ya nywele. Kwanza hivi
alivyo anapendeza tu” “Geb wewe!?” “Sasa wewe unafikiri tutafanyaje Nanaa?
Amegoma.” “Shauri yako! Wewe utaenda kupambana na bibi yake.” Geb akacheka huku
akimwangalia mwanae. Hakuwa hata na dalili ya kumka.
~~~~~~~~~~~~~
Walifika
kanisani mama G nusura aanguke. “Mnanitania nyinyi wawili!?” “Mama, huyu Liv
ameamka hapa hapa kanisani. Yaani Geb anazima gari ndio na yeye amefungua macho
na kuanza kucheka. Alikataa kabisa kumka.” Nanaa akatetea. Liv alikuwa akipiga
makofi huku anacheka. “Liv wewe jamani!” Nanaa hakua akiamini. “Yaani nyinyi
watu wazima wawili mnashindwa na huyu mtoto!?” “Mama! Nimemuamsha sana huyo
mjukuu wako. Nimemtoa kitandani nikampeleka mpaka sebuleni, lakini akagoma
kufungua macho. Nimembadilisha mpaka diaper hajafungua macho. Kama alivyosema
Nanaa, ameamka hapahapa.” Liv akamtaka bibi yake. Vimikono vyote juu huku
akimwita bibi yake.
Grace
akawasogelea akiwa na familia yake. Wote walikuwa wamependeza. “Mbona bado dada
ana nguo za kulalia?” Grace akauliza. Nanaa akamkonyeza anyamaze. Grace
akacheka. “Watu wazima wawili wameshindwa na mtoto mdogo huyu! Yaani
wameniletea mtoto mchafu kabisa huyu. Nywele hazijachanwa halafu waone wao
jinsi walivyopendeza! Aibu tupu hii.” “Ni Geb huyo.” Nanaa akamtupia Geb mpira.
“Na mimi nilimwambia mama atakasirika.” “Naombeni mnipishe. Mmenikera sana!” “Lakini
nimebeba vitu vyake vyote kama ulivyoweka pale kitandani kwako. Hapa ndio
nilikuwa nimfungue kumtoa kwenye kiti chake, nianze kumtengeneza. Usikasirike
mama yangu.” Geb akajaribu kumtuliza. “Naombeni muondoke, mnipishe.” Grace
alizidi kucheka.
“Sasa
amekula?” Grace akauliza tena, Nanaa na Geb wakaangaliana. Mama G akawageukia.
“Msiniambie mmemleta huyu mtoto bila kumlisha!” “Nilikwambia alikataa kuamka
mama. Liv aligoma kabisa. Yaani nilimnyanyua mpaka kwa mkono mmoja! Akakataa
kufungua macho.” “Naomba muondoke Geb.” “Ila tumeleta na chakula chake.” Geb
akasisitiza. “Ondokeni Geb.” “Mimi naondoka mama.” Nanaa akasogea pembeni. Geb
akampisha pale mlangoni. Mama G akazunguka upande wa pili wa lile gari akiwa na
mjukuu wake.
Grace
alizidi kucheka. “Liv anakusudi bwana! Mama anatukasirikia bure.” Geb
aliendelea kuongea asiamini aliyowafanyia Liv. “Huyo mtoto anakila kitu cha
tofauti cha kanisani. Bibi yake ananunua kila leo! Tena ananunua kwa pesa
nyingi tu. Sasa leo umletee mtoto na nguo za kulalia! Hamtaelewana.”
“Nilimwambia Geb.” “Bwana Liv leo kanikosanisha na mama yangu. Mimi nilijitahidi
kweli kumuasha. Tena nikamwimbia na nyimbo zake zote. Lakini wapi!”
Wakatangulia kanisani.
Baada
ya kama dakika 25 mama G akaingia na Oliva akiwa amependeza sana na cheko lake
kama kawaida. Nanaa akamkonyeza Geb ili amwangalie mama yao na Liv. Akawageukia.
Liv alishangilia alipoona baba yake anamwangalia. Geb hakuamini. Kwa muda
mfupi, yule mtoto alibadilika! Mama G akaenda kuwakabidhi mtoto. “Hivi ndivyo
nilitaka aletwe. Na akiwa ameshiba. Nakuja kumchukua sasa hivi.” Akawaambia
hivyo na kuondoka. Geb akampokea mtoto huku anatingisha kichwa.
“Sasa
mama naye, alitegemea mimi nimletee mtoto akiwa hivi! Naanzia wapi?” Nanaa
akacheka huku akiangalia vile huyo mtoto jinsi alivyokuwa amepangiliwa. Kuanzia
kichwani mpaka miguuni. Ungependa umshike tu. Lakini cheko hilo la Liv lilikuwa
lakibaguzi haswa. Huwapa wachache anaowajua yeye. Akiwa hakufahamu, ujue
hutamgusa.
Hayawi Yamekua.
Baada
ya kusifu na kuabudu Nanaa akashangaa linatoka tangazo la kwanza la ndoa.
Hakuamini. Akamwangalia Geb. “Umesikia!?” Nanaa akauliza kwa kunong’ona.
“Ndiyo.” Vigelegele vikasikika. Mama G akiwa anashangilia na wakina mama
wengine pale kanisani. Nanaa alijikuta akiinamisha kichwa na kuanza kulia.
Hakuwa akiamini. Habari za mwisho alizojua ni kuwa hataweza kuolewa tena kwa
kuwa anandoa na Zinda. Geb alimwambia wamsubirie tu Mungu. Alipouliza mpaka
lini, hata Geb hakuwa akijua anasubiria mpaka lini. Ila alimsisitiza kutulia.
Ukweli moyoni kwa Nanaa hakuwa ametulia. Alitamani sana kuolewa.
~~~~~~~~~~~~~
Hamu
ya kumtambulisha Geb kama mumewe ilikuwepo, lakini alikosa ujasiri kabisa. Japo
walikuwa wakiishi pamoja na wana watoto. Oliva na huyo aliyekuwepo tumboni,
lakini ujasiri wa kumtambulisha kama mume, haukuwepo. Uwezo wa kupaita nyumbani
kwa Geb ni kwake, na kutambua mali za Geb kama zake. Tena akiwa amemkuta na
kila kitu chake. Magari na nyumba. Pale kwa Geb alikwenda na sanduku
lililochakaa na nguo za kawaida sana, ambazo alishatupilia mbali muda mrefu
sana Geb alipomfanyia shopping ya nguvu.
Hata
Oliva alimpatia hapo hapo kwa Geb. Kwa ujumla kila kitu anachomiliki kwa wakati
huo, alikutana navyo hapo kwa Geb. Utajiri mkubwa uliokuwa ukiongezeka na
kumsikia mama yake akimsifia mwanae kuwa anaakili sana ya biashara. Huku
akisema ni yeye na Grace wanaendesha hiyo kampuni vizuri sana. Hakuwa akijua
hata anatakiwa aongee nini au ajiweke kwenye nafasi gani. Kama mmiliki pamoja
na Geb au msikilizaji tu! Anaanzia wapi sasa wakati amevikuta! Hana ndoa na
Geb. Umwili huo mmoja unatambulikana wapi!
Japokuwa
Geb alijitahidi sana kumfanya Nanaa ajisikie vizuri, lakini haikuondoa ile hali
ya kujishuku na kutomiliki moyoni mwa Nanaa. Shauku yake kubwa ni kutaka
kuolewa na Geb. Pengine angekuwa hata na ujasiri wa kuulizia mambo fulani
fulani. Kuna maswali mengi aliyokuwa nayo juu ya Geb, lakini yalikosa nguvu kwa
kuwa alijiona hana haki ya kuyauliza. Kama alivyoachwa Liz na wengineo, ndivyo
na yeye alijua angeweza kuachwa siku moja. Hakuwahi kujiaminisha. Amani yake
ingetimia tu siku ya harusi atakapotamkwa ni mke halali wa Geb.
Kama
mtu angelifungua moyo wa Nanaa, nakujua kilio chake kikubwa mbele za Mungu
akiwa peke yake, ilikuwa ndoa. Kila aliyekuwa anamuona anamzunguka, akiwepo
kaka yake James, ni kama walishalipuuzia hilo swala. Ilimradi maisha
yanaendelea. Nanaa anaendelea kuzaa. Hakuna aliyekuwa akizungumzia swala la
ndoa tena. Miezi ilishapita, vikao vya harusi navyo vilishavunjwa. Hapakuwa na
dalili ya ndoa tena.
Geb
kijana aliyekuwa akiwindwa na historia yake ya nyuma na sasa, alikuwa akimfanya
Nanaa asilale usingizi mzuri kwa wasiwasi wa kuibiwa penzi. Ujasiri wa kumuaga
asubuhi na kumuacha kwenda kazini kwa amani, ni vile alivyokuwa akimuona Geb
anapiga magoti kila siku asubuhi akimuomba Mungu. Alimuona Geb akibadilika na
kuwa karibu na Mungu kuliko walivyokutana. Kama Nanaa alishindwa kuamka asubuhi
kuomba naye, Geb alihamia upande wa sebuleni hapo hapo chumbani. Basi atasoma
neno na kupiga magoti pembeni ya kochi. Akishamaliza kuomba na kuoga. Hapo
ndipo alipoenda kitandani na kumshika Nanaa mkono na kuomba naye kwa ufupi
kisha kukimbilia kazini. Kidogo ilikuwa ikimtuliza Nanaa.
“Mwanaume anayepiga magoti mbele ya Mungu
kwa unyenyekevu hivi, lazima Mungu na yeye atamwinua.” Nanaa alikuwa akiwaza kila alipokuwa akishituka
usingizini na kumuona Geb anaomba. Lakini bado haikuondoa shauku ya kuja kuwa
mke kihalali. Ashajifikiria mara nyingi ameachika pale na mwanamke mwingine
amechukua nafasi yake mle ndani. Alikubali kumsubiria Mungu, lakini kila
alipokuwa peke yake hakuacha kumkumbusha Mungu na kumlalamikia katika swala la
kuchelewa. Alimwambia Mungu anamchelewesha.
Usiku
uliopita ndio ulikuwa mbaya zaidi pale alipozungumza na Zena, na kuambiwa
anaolewa. Huku Zena akimpa habari za wenzao waliomaliza nao chuo, vile
wanavyoolewa na kufanikiwa. Nafikiri unakumbuka mwisho wake pale jana. Aliishia
kupiga magoti na kumuomba Geb msamaha. Akiwa bado na uchungu mwingi moyoni,
bado shauku yake ikiwa pale pale, baada ya kuridhishwa kitandani pale na Geb,
akajikuta akimuahidi Geb kuwa atakuwa sawa tu hata ikitokea wanaendelea kuishi
vile vile. Haikuwa kweli. Lakini ilimbidi kutoa ahadi ile, ili kumridhisha Geb.
Alimuahidi kumtambulisha kwa marafiki zake wote hiyo kesho watakapokwenda
kwenye kikao.
~~~~~~~~~~~~~
Ukweli
hakuwa akiamini. Ni kama ilitokea kufumba na kufumbua. Gafla kutoka kwenye
kukata tamaa, na kuamua kuacha kabisa kufikiria swala la ndoa, hata masaa 24
hayakuwa yamepita, tangazo lao la kwanza la ndoa likawa limetoka! Bado alikuwa
na pete yake ya uchumba mkononi. Waliitwa pale mbele ya kanisa ili waombewe.
Bado Nanaa alikuwa ameinama. Mama G alikuja kumchukua Oliva aliyekuwa
ameshalala kifuani kwa baba yake wala kelele hazikumsumbua.
Geb
akasimama na kumsaidia Nanaa kusimama, wakaenda kupiga magoti pale mbele
kuombewa baada ya mchungaji kuuliza kama kuna kipingamizi chochote. Hakukuwepo
mtu wa kupinga hilo kwa wakati huo ambapo Mungu ameruhusu. Wakaombewa.
Hakuna
sala wala wimbo alikuwa akisikia Nanaa kwa wakati huo. Bado alikuwa amebaki
kwenye bumbuwazi. Kilichomshangaza Nanaa ni pale tangazo lake la ndoa
lilipotoka siku hiyo hiyo. Mchungaji akatangaza na tarehe ya harusi mara baada
ya kuwaombea na watu kumaliza kushangilia. Hasa mama yake Geb ndio alionekana
anafuraha zaidi. Nanaa akagundua itakuwa siku ya birthday ya Geb ambayo ilikuwa
mwishoni mwa mwezi huo. Hakuweza hata kuzungumza au kuangalia watu kwa machozi
yaliyokuwa yakimwagika mfululizo.
Akiwa
ameinama palepale mbele kanisani na kushindwa hata kunyanyua uso na kupokea
pongezi zake, akasikia sauti ya kaka yake. “Kaka!” Nanaa
akanyanyua uso. Akamuona James anacheka. “Usilie sasa.” James akamsogelea na
kumpa mkono. “Hongera sana.” Nanaa akashindwa hata kujibu. James alibaki
kucheka. Nanaa hakutegemea kumuona kaka yake pale. Ndipo alipojua wote walikuwa
wakifahamu hilo isipokuwa yeye tu. Kama alivyomwepesi kucheka ndivyo alivyokuwa
mwepesi kulia. Aliendelea kulia mpaka mwisho wa ibada. Wakatoka. Alikuwa kimya
huku akifuta machozi wakati wote pembeni mwa Geb.
“Kichwa
kitakuuma Nanaa! Usilie bwana.” Grace alimsogelea kujaribu kumtuliza. “Unataka
kwenda kula wapi?” Grace alimuuliza lakini Nanaa akashindwa hata kujibu. Geb
akamshika mkono na kurudi naye kwenye gari. Mama G alimchukua Liv akaenda naye
kwenye gari yake. Grace na familia yake nao wakaingia kwenye gari yao,
kadhalika James. Wakaondoka Nanaa asijue wanaelekea wapi.
~~~~~~~~~~~~~
Alipoingia
tu kwenye gari Nanaa akajifunika uso na kuendelea kulia kwa uhuru. “Naomba
usilie bwana.” Nanaa hakujibu. Baada ya muda akasikia gari linasimama. Akajua
labda wamefika nyumbani, akabaki amejifunika uso. Akasikia Geb akishuka,
akamfungulia mlango. “Njoo hapa.” Geb akamfungua mkanda na kumgeuza pale pale
kwenye kiti akamsogeza na kumkumbatia. “Asante Geb! Nakushukuru sana. Sikutegemea!” Geb alimsikia wakati amemkumbatia. “Nilishakata tamaa. Sikutegemea!” “Nilikwambia tumsubiri Mungu Nanaa. Mungu hakawii
wala hachelewi. Hujibu kwa wakati wake. Hakuna siku ilishawahi kupita
nisimkumbushe Mungu juu ya shauku yangu.” Nanaa akajitoa na kumtizama.
“Ulifikiri
na mimi sina hamu ya kuoa?” Geb akauliza na tabasamu usoni. “Na mimi sifurahii
kuishi hivi Nanaa. Na mimi nilitaka kumaliza hili tufikirie mambo mengine.
Kitendo cha wanangu kuzaliwa pasipo ndoa takatifu unafikiri ni jambo
ninalolifurahia? Unafikiria mimi kama baba naweka mfano gani kwa wanangu? Yaani
Liv leo anakuwa mkubwa, halafu anakuja kukuta naishi na wewe bila ndoa!
Inamaana namtuma na yeye akafanye hivyo hivyo. Yaani akikua na yeye aende
akaishi na mwanaume bila ndoa! Hapana Nanaa. Tumepewa watoto kuwaongoza.
Hawatakuwa kingine na kile watakachokiona kwetu au kile tunachowafundisha.
Lazima kuweka juhudi za makusudi kuweka mfano wa kuiga.” Akambusu.
“Sikutegemea! Mbona sasa hukuniambia?” “Na mimi sikuwa nimetegemea kama Zinda atasimamia
ahadi yake mpaka mwisho. Mama alimwambia jana ni lazima aje leo azungumze na
mchungaji na wazee wa kanisa kufuta pingamizi lake. Sikutaka kukwambia halafu
leo asingetokea, nilijua ungeumia sana.” “Nakushukuru Geb.” Geb
akatabasamu.
“Kwa
nini?” Akamuuliza huku akimfuta machozi. “Unanilinda na kila kitu. Unahangaika mchana na usiku kwa ajili yangu
kuhakikisha mimi na watoto tupo salama na tunafuraha. Hulali kama mimi
sinafuraha. Unasimama kwenye nafasi zangu zote za huzuni. Umebeba huzuni zangu
zote ili mimi niwe nafuraha. Nakushukuru. Asante.” Geb akambusu. “Asante kama umeona hilo. Na asante
kushukuru. Sasa twende tukale. Mama ametuambia tukutane hapa kwa ajili ya
chakula cha mchana. Tutakuwa sisi tu kama familia.” Nanaa akajiweka sawa,
akaona kila mtu anatoka kwenye gari yake. Wakawasogelea.
Kikao Kingine Cha Familia Kwa Ajili Ya Harusi Ya
Nanaa & Geb.
Walikaa
mezani wakila na kuweka mipango ya harusi. Mama G ndiye aliyekuwa akiweka
mikakati, alionekana kuhamasika kweli kweli. Danny alirudi kuwa mwenyekiti wa
kamati yao ya harusi. Wakakubaliana kuitisha tena kikao kingine. “Lakini sio
pale nyumbani.” Geb alitahadharisha. “Naona safari hii tukutane sehemu nyingine
kama kwenye hoteli. Na hatutamwitaji Nanaa.” Danny akaongeza. “Mimi niachieni
Nanaa. Mambo ya saluni na nguo. Ni mimi na mama.” Grace akaongeza.
“Au
labda tusubiri mpaka nijifungue.” “Nanaa please!”Geb akashituka kweli. “Sasa
tumbo hili linakua kila siku. Muulize mama. Kila week nanunua nguo mpya. Tumbo
linakuwa sana tofauti ya mimba ya Oliva. Sasa hiyo nguo nitanunua ya namna
gani? Mpaka siku ya harusi siitabana?” “Hapana Nanaa! Gauni la harusi na
lenyewe haliwezi kutuzuia kufunga ndoa. Nunueni mengi hata mkitaka 50. Kuanzia
kwa saizi itakayomuenea sasa hivi na makubwa zaidi yake. Sitajali unaonekana
vipi hiyo siku ya harusi. Hata ukiwa kama hivyo ulivyo sitajali, nataka kukuoa
wewe Nanaa. Sio gauni.” Nanaa akacheka na kuinama.Mama G akaanza kupiga
vigelegele. “Basi hapa tutafukuzwa!” Grace akaongea. James akawa anacheka tu.
Walikuwa
Grace na familia yake, James, Geb na familia yake tu. “Mimi mwenyewe nimefurahi sana.” Nanaa aliongeza huku machozi yakimtoka. “Siamini! Nahisi ni ndoto! Nilijua sita..” Hapo Nanaa akashindwa kuendelea kuongea.
Akanyamaza kama anayefikiria. Kaka yake alicheka tu huku akimwangalia. “Umekuza
James. Hongera!” “Asante mama. Mimi mwenyewe siamini hata kama ana watoto!
Nikimwangalia Liv hivyo! Siamini kama ni mtoto wa Nanaa!” Kila mtu alikuwa
akicheka.
“Mungu
ana mambo yake ya ajabu! Yaani nikimfikiria hapa Mungu alipomuweka Nanaa,
ungeniuliza miaka 5 iliyopita na kuniambia nitabiri atakuwa wapi baada ya miaka
5, nisingesema hivi hata kidogo! Hiyo siku nikitoka kanisani. Nikahakikisha
ameolewa! Nahisi naweza kulala hata masaa 10.” “James! Kwani sasa hivi bado
huna amani?” Grace akashangaa. “Huwezi amini Grace. Na yeye anajua. Lazima
nimsikie asubuhi na usiku wakati naenda kulala ndipo nipate amani. Nijue
ameamka asubuhi salama, na usiku nijue siku yake iliisha salama hamna baya
limempata. Ndio napata amani.” Hawakuwa wakiamini. Walibaki wakishangaa.
“Hata
anitumie ujumbe wenye mstari mmoja tu, ndipo najua yupo salama. Ikifika saa 4
asubuhi sijamsikia, basi napiga. Ni heri anitumie ujumbe wakusema tu, ‘kazi njema kaka!’ Basi hapo
napata amani najua yupo mahali anapumua.” “Sasa wewe si ulishapokea mahari?”
Mama G akauliza.
“Mahari
sio ndoa mama. Viola alilipiwa mahari na akaachwa na mtoto wake mpaka leo.”
James akajibu. “Lakini ni kweli!” Mama G na Grace wakaitika kwa pamoja. “Lakini
mimi nilikuhakikishia nitamuoa Nanaa, James! Sijawahi kukudanganya!” “Ikifika
kwenye swala la Nanaa, huwa siamini maneno Geb. Hata siku moja. Na kama
nilivyokwambia, itabidi kuanza kujifunza na kuzoea. Sijawahi kumuamini mtu
yeyote na Nanaa. Huwa nahisi ataonewa tu sehemu. Na kwa kuwa namfahamu kwa
kumsikia sauti yake, nakuwa makini sana. Huwezi kunificha ubaya unaomtendea
Nanaa, hata umwambie asiniambie. Ukiwa naye pamoja. Kwa kuwaangalia tu, nitajua
unaishije na Nanaa. Mama alilijua hilo, kwa hiyo akawa anajitahidi kumuondoa
pale nyumbani kila akimfanyia ubaya halafu ajue ninakwenda hata kama ni kesho yake atamtoa nyumbani.”
James aliendelea.
“Kuna
siku alimtoa pale nyumbani nikiwa nimemwambia kabisa nitakwenda, lakini nataka
kumkuta Nanaa. Nilikwenda baada ya kama siku tatu baada ya kuzungumza naye.
Nilifika usiku, sikumkuta Nanaa. Akaniambia amekwenda kwa bibi. Kwa kuzungumza
naye tu usiku ule, nikajua kuna kinachoendelea. Nikamwambia nakwenda kwa bibi
usiku huo huo, nilazima nizungumze na Nanaa. Nikamwambia nimeota mama mdogo
analia sana. Akasema Nanaa mzima, hana shida. Nikamwambia nitapata jibu nitakapo
muona Nanaa mwenyewe. Akawa ananizuia sana nisiende kijijini. Kumbe alikuwa
amemficha kwa rafiki yake hapo hapo mjini. Akajua nikienda kijijini sitamkuta.”
“Kumbe
siku ile nilipompigia simu mama, kabla sijamwambia nakwenda na ninataka kumkuta
Nanaa, walikuwa wametoka kumpiga na kumuumiza jicho. Tatizo likawa Nanaa
mweupe, jicho lilivilia damu. Walilikanda lile jicho siku tatu mfululizo ili
kabla sijafika nimkute mzima. Lakini lile jicho liligoma. Na mama alishajua
hawezi tena kunidanganya juu ya Nanaa. Wote walishajua hata Nanaa akinidanganya
amejigonga, huwa najua ukweli.” James akatulia.
“Sasa
wakafanyaje?” Mama G akauliza. “Haikuwa shuguli ndogo. Ilibidi wanipeleke
alipo. Halafu mama akaniwahi kwa kumpigia simu rafiki yake, kuwa nikifika huko
na baba, wasifungue mlango, wajidai wamelala.” “Kwa hiyo ukaondoka?” Mama G
alizidi kudodosa. “Nakwambia niliota mama Nanaa analia ndio maana nikampigia
mama simu kutaka kuzungumza na Nanaa. Wakanidanganya Nanaa hayupo. Kumbe
alikuwa nje analia. Akajua nikizungumza na Nanaa nitajua kuna tatizo.
Nilipomkosa Nanaa, ndipo nikamwambia sasa nitakwenda na ni lazima nimkute Nanaa
nyumbani. Nilishawishika sana kwenda siku ile ile au inayofuata, lakini
nilikuwa na kazi ofisini iliyonilazimu niimalize kwanza. Halafu nikajipa moyo
kwa mazungumzo yale na mama, inamaana bado yupo hai, hawajamuua.”
“Nikiwa
naota mama yake Nanaa analia au yeye mwenyewe analia, huwa najua lazima kuna
tatizo limempata Nanaa. Sijui Mungu amefanyaje hiyo! Wala sijawahi kuelewa.
Lakini huwa mara nyingi sana, au niseme, sijawahi kukosea. Labda Nanaa mwenyewe
aamue asiniambie lakini nikisha ota hivyo, ujue ni kweli. Na nilazima nimuone
au nizungumze naye yeye mwenyewe ili nijue kulikoni. Hamna mtu mwingine naweza
kuzungumza naye nikaridhika isipokuwa Nanaa mwenyewe.” “Ikawaje sasa?” Mama G
akauliza tena.
“Mama
kwa kupenda stori!” Nanaa akacheka. “Wewe ndio umenifundisha bwana. Haya
ikawaje?” Akamgeukia James. “Muulize Nanaa mwenyewe.” James alijibu huku akicheka
kidogo. “Alivunja mlango.” Nanaa akajibu huku ameinama na kucheka. “James
wewe!” Grace akashangaa. “Kabisa. Sijui ninakuwa na nini linapokuja swala la Nanaa.
Siwezi kufikiria. Yaani siku ile ilikuwa mbaya sana. Nilifanya fujo, mpaka
wakamtoa Nanaa. Kwanza walimuumiza jicho vibaya sana. Nikahisi atakuwa chongo.
Hilo jicho haliwezi kuja kuona tena. Nilikuwa nimepaniki. Nusura nimpige mama.
Ndio baba akaniambia nitajilaani. Nisimguse mama. Heri aolewe, labda na mimi
nitaweza kufikiria jambo jingine.” James akamalizia.
“Hutaweza
James. Labda uongeze mtu mwingine utakayeweza kumfikiria kama Nanaa, na huku
ukiamini sasa hivi anaishi na Geb. Mwanaume anayempenda na kumjali. Hata sisi
tunampenda Nanaa. Mwenyewe nahisi kama Mungu amenipa mdogo wa kike.” Grace
aliongeza huku akimwangalia Nanaa. “Na mimi hilo nimeliona. Nitazoea tu. Lakini
acha afikishwe kwanza kanisani. Akitoka hapo, ndipo labda atatafutwa mwingine
wakufikiriwa.” Wote wakacheka.
“Oa
mwanangu James. Huyu Nanaa umeshakuza. Tuachie sisi.” James akacheka. “Nitaoa
tu mama. Acha hili likamilike kwanza labda ndipo naweza hata kufikiria. Kwanza
nahisi hiyo siku nitakayohakikisha ameolewa pale kanisani. Sherehe ikaisha kwa
amani. Nafikiri ndio siku ya kwanza kwa muda mrefu sana naweza kulala au hata
kuwa na simu iliyoishiwa charge na nikawa na amani, pale Nanaa anapokuwa mbali
na mimi.” “We James!?” Bado mama G hayakuwa yakiingia akilini.
“Kweli
mama. Huwa ni simu ya Nanaa tu huwa napokea wakati wowote na popote. Na nina
hakikisha simu yangu ipo hewani wakati wowote ili isijetokea anashida mahali,
halafu akanikosa. Ni namba yake tu niliyoitengenezea mlio wa tofauti kwenye
simu yangu. Nikisikia huo mlio hata kama bosi wangu amenisimamia mbele yangu
huwa namwambia asubiri kidogo.” “Hata kama anatoa mada mbele ya kikao na
wakubwa wapo, simu ya Nanaa ikiingia tu, anaacha kila kitu. James ataomba
udhuru na kutoka nje hapo hapo bila yakusubiri jibu la muongoza kikao. Atatoka
tu. Anapokwambia simu ya Nanaa haisubiri, ujue hatanii. Mimi nilishaliona hilo,
japo hatujawahi kuzungumza naye.” Danny aliongeza na kuzidi kuwashangaza.
“Siku
moja tulikuwa kwenye kikao kinachohusu kitengo chetu. Mimi na James tulitakiwa
kuelezea mambo yaliyokuwa yanaendelea pale. James alitakiwa aanze, mimi ndio
nimalizie. Unajua tulikuwa tunawakilisha kwa wamiliki wa kampuni? Sijui kama
unaelewa mama. Walikuwa wamefika hapa nchini. Kwa hiyo na viongozi wote wa zoni
zote walikuwepo. Ile James amesimama na kusalimia, ameanza tu, simu ya Nanaa
ikaingia. Akapokea pale pale kisha akatuambia anaomba kama dakika tatu hivi,
atarudi. Hakusubiri jibu la ndiyo au hapana. Akatoka nje na kutuacha wote
tunamsubiria. Ikabidi kutoka na kumuuliza kama ni kwema. Akasema ni Nanaa. Amemuacha
nyumbani hajisikii vizuri. Nilimtizama James kama vile nimuulize anajua
alichofanya. Lakini nikaona tuokoe muda, arudi ndani amalizie anachohitajika kufanya.
Ndipo aondoke.” Kila mtu alicheka. Geb alikuwa akimtizama Nanaa, aliyekuwa
ameinama akicheka kwa aibu.
“Nyinyi
hamkumuona siku ile asubuhi alipoamka miguu imevimba?” Grace akauliza. “Mimi
nilishangaa James amenipita pale mlangoni chumbani kwao hawa, akaenda kumbeba
Nanaa na kuondoka bila hata kuzungumza na mtu. Nikabaki kujiuliza kwani alilala
hapa au ametokea wapi huyu?” Kila mtu akacheka.
“Ujue
siku ile usiku kama panaelekea kupambazuka hivi, niliamshwa na ndoto ya mama
mdogo. Mama Nanaa. Nilimuota analia sana. Nikashituka. Na kama nilivyowaambia.
Mara nyingi nikiota hivyo, Nanaa analia au yeye mama mdogo analia, nakuwa najua
Nanaa anatatizo popote alipo. Na mara nyingi ninakuwa napatia. Hata alipokuwa
anaishi na mimi pale nyumbani, nilikuwa nikiota hivyo hata kama ni usiku.
Nakwenda kumgongea. Nikienda kumgongea, nakumta hajalala. Labda tumbo linamuuma
au anatatizo tu. Sasa nilipoamka baada ya hiyo ndoto, nikaangalia simu.
Sikukuta ujumbe wala simu kutoka kwa Nanaa. Nikajiambia itakuwa ni mawazo tu.
Kwa kuwa nilimuacha Nanaa usiku uliopita ameshindwa hata kusimama, Geb akambeba
mpaka kitandani.”
“Nikasubiria
simu na ujumbe wowote kutoka kwa Nanaa. Ikawa kimya. Nikaamua kuoga kabisa kama
kujiandaa kama atanipigia. Kimya. Nikajithibitishia ni mawazo tu. Niliposita
kumpigia simu ili kumuuliza, nikaamua kurudi kulala kwenye kochi. Sikutaka
kuwaamsha. Nafikiri nililala kama masaa mawili tu hivi, simu ya Nanaa ikaingia
huku analia. Nikajua tayari. Kwa hiyo kilikuwa kitendo cha kupanda tu kwenye
gari ndio maana sikuchelewa kufika.” Kila mtu alishangaa huku akicheka.
“Basi
huyu hatakuwa!” “Wala hujakosea mama. Sijawahi kumuona amekuwa hata siku moja.
Kila nikimwangalia namuona kama bado mtoto anayehitaji uangalizi wa karibu tu.
Siku Geb anamlipia mahari ilikuwa ni kama kengele ya kutolewa usingizini.” Wote
walicheka. “Na bado hujaamka!” Grace akaongeza. “Naona naanza kuamka. Nikimuona
Liv anacheza vile na nimjamzito tena, najiambia amekuwa sasa.” Walikaa hapo mpaka jioni.
“Huyu
amelala!” Geb alikuwa amemuweka mwanae kifuani baada ya kucheza na Fili mpaka
kuchoka. “Hata hivyo tumeongea mengi. Inatosha. Tukapumzike tu.” Mama G
akajibu. “Kuna mahali nataka kumsindikiza Nanaa. Tangulia na Liv nyumbani.
Naona amechoka na ishakuwa jioni. Hatutatoka naye tena.” “Hamna shida. Hata
hivyo amecheza vyakutosha. Akaoge alale.” Wakaendelea kuzungumza kidogo,
wakaagana.
Nanaa na Geb njiani kuelekea kwenye kikao cha harusi ya Zena.
Nanaa afunua ukurasa mpya ulimgusa Geb.
Akiwa
anajua amechelewa, akampigia simu Zena. “Mmeshaanza
kikao?” “Bado. Kwani unakuja?” “Tupo njiani. Tutapita hapo kidogo. Si umesema
mpo Sinza Bar?” “Ndiyo. Tupo tu hapa nje. Ukishuka kwenye daladala tu, tutakuona.” Zena akajibu. “Basi tupo
njiani.” Nanaa akajibu na
kukata simu. “Anasema wapo tu nje. Tukifika watatuona.” Nanaa akamwambia Geb
wakati anaendesha. Geb akamtizama.
“Unatamani
kujua kuendesha gari?” Geb akamuuliza. “Hiyo ni ndoto ambayo lazima nitimize,
Geb. Nilimwambia hata kaka. Akaniambia nikimaliza tu chuo nikiwa tayari
nimwambie, atanifundisha yeye mwenyewe. Alinikumbusha kipindi fulani kama miezi
miwili iliyopita hivi, lakini nikamwambia bado akili hazijatulia. Mambo ya
watoto na maisha kwa ujumla. Nikamwambia nataka nikija kujua na mimi niwe nina
gari yangu. Sio anifundishe halafu nibakie na ujuzi tu. Unakumbuka kuna siku
alikuja kunichukua tukatoka naye kwa chakula cha usiku? Ilikuwa siku ya
jumamosi.” Nanaa akajaribu kumkumbusha.
“Nakumbuka.”
“Basi siku ile alipowahi alinipitisha pia sehemu wanazouza magari. Nikapata
nafasi ya kuangalia magari mbali mbali.” Nanaa akacheka mwenyewe. “Yaani pale
ndipo nilipoamini nina ushamba wa magari. Ujue sijui kabisa aina ya magari!
Yaani mwenzio nilikuwa najua kuwa kuna magari makubwa na madogo tu. Kumbe tena
sijui kuna sijui Toyota, Suzuki, Honda na majina mengi hata sikumbuki. Haya,
wakaniambia kuna magari ambayo yanakuwa yanatumia mafuta sana na mengine
hayatumii mafuta mengi. Halafu mwenzio nikajua kuwa magari ambayo ni makubwa
ndio garama halafu madogo ndio rahisi. Wakaniambia kuna madogo ambayo ni garama
sana kuliko hata makubwa. Nikajikuta nachanganyikiwa zaidi.” Nanaa akaanza
kucheka tena.
“Basi
nikamvuta kaka pembeni. Nikamuuliza mbona hapa sioni magari kama yale ya Geb?
Acha kaka acheke. Akaniambia eti magari ya Geb hayo hayauzwi kwenye sehemu kama
hizo. Eti unaagiza magari yako nje ya nchi. Halafu akaniuliza swali
lililonifanya nifikirie. Akaniuliza eti nishaonana na magari kama yako, wapi!
Nikawaza wee, mwishoe akaniambia tuondoke tu. Kwa kufikiria vile bila kutoa
jibu la haraka, basi eti nijue ni machache sana hapa nchini. Na pesa yake pia
ipo ndefu. Nikajiona nachanganyikiwa tu. Magari yenyewe garama! Halafu hata
wakiniuliza nataka lipi, sijui! Nikamwambia kaka niache tu kwa wakati huu.
Nifikirie kwanza maswala ya watoto huku tukikusanya pesa. Ameahidi kuniongezea
pesa nitakapokuwa tayari.” Nanaa alitabasamu alipokuwa akimalizia na
kumwangalia Geb. Macho yakagongana. Kimya.
Ukimya
wa muda ukapita. Geb akiendelea kuendesha. Nanaa akafikiria kidogo, akawa
hajaelewa kwa nini hachangii kitu. Akaona anyamaze asije akaharibu kama usiku
uliopita. Kidogo akaanza kusinzia. “Kwa nini hukuniambia hayo? Au kwa nini
nilipokwambia uniambie kitu chochote unachotaka nitakununulia, ukasema unataka
tu ndoa? Nilipokuuliza maswala ya gari, ulisema kwa sasa huna haja ya gari.
Labda mpaka utakapojifungua. Ukaniahidi popote utakapotaka kwenda, utaniambia
mimi nikupeleke au Jeri. Tena ukasisitiza kuwa hata mama atakufaa kwa kuwa huwa
anakusindikiza sehemu nyingi tu bila shida. Na imekuwa hivyo wakati wote! Kabla
sijamgawia kazi za siku Jeri, huwa nakuuliza kama utamuhitaji!.” Nanaa akakunja
uso akajiweka sawa.
“Nimekutajia
kitu ninachojua unaweza kunipa Geb. Ndoa. Sifahamu chochote juu yako isipokuwa
mapenzi ya dhati uliyonionyesha. Sijui hata kama una uwezo wa kununua gari
jingine hasa baada ya kuninunua kwa mapesa yote yale! Kwanza najisikia vibaya,
nashindwa hata kukuuliza kwa hofu la kupata jibu ninalolifikiria. Sijui kama
uliua biashara gani kuweza kuninunua kwa mapesa yote yale! Sijui kama
nilikufilisi kwa kiasi gani! Sijui ni umbali gani umefika Geb, kuninunua!
Naishi mimi na wanangu bure. Tunakula tunachotaka. Navaa kile ninachota na
vingine hata sikuwahi kufikiria kama nahitaji. Unanipa pesa kila mwisho wa
mwezi, achilia mbali na za matumizi pale nyumbani. Sijui hiyo pesa unatoa wapi!
Sijui kama unabiashara gani, isipokuwa zile ninazosikia kutoka kwa mama. Sijui
unaingiza kiasi gani kwa mwezi! Sijui kama mwezi huo umeingiza hasara au faida!
Kama nilivyokwambia, sijui kama pesa uliyonilipia imekuathiri vipi! Hebu
niambie Geb, naanzia wapi kukutwika mzigo wa gari tena?” Nanaa akamuuliza kwa
utulivu tu.
“Kuwa
mkweli Geb. Hata wewe ungekuwa kwenye nafasi yangu, ungeanza kudai vitu
vinavyogarimu mamilioni ya pesa tena? Binafsi siwezi. Nipo huru kutumia ule
upande ambao nimekuona upo huru nao kwangu. Na umeufunua kwa umbali ambao
sikuwahi kufikiria kama ninastahili. Mapenzi. Umekuwa muwazi na umejitoa kwangu
kupita kiasi. Najua chochote nitakachokuomba kwa upande huo, hutasita kunipa.
Kwa kuwa najua uwezo wako katika penzi lako kwangu. Utajiri uliopo kwenye
mapenzi unaonipa na ambao upo tayari kunipa. Lakini si vinginevyo.” Ulikuwa
ukweli mtupu uliomwingia sawia Geb.
~~~~~~~~~~~~~
Ni
kweli Geb hakuwahi kuzungumza lolote juu ya utajiri wake kwa Nanaa. Ni jambo
ambalo hakuwahi hata kufikiria kama anahitajika kumshirikisha mtu yeyote juu ya
pesa yake. Grace mwenyewe alifahamu pesa anayoingiza kaka yake kwa pale kwenye
ile biashara tu. Ambayo yeye Grace amewekwa kama msimamizi wa upande wa
biashara hiyo inayokusanya mazao mikoani na kuuza pale mjini. Basi.
Geb alikuwa na biashara nyingine.
Alikuwa na hilo jengo analokodisha kwa wapangaji wengine. Pesa yake iliingia
kwake yeye tu. Alinunua mafuta mikoani na kuyaleta pale jijini. Alikuwa na
kiwanda kidogo ambacho kilikuwa kikiyasafisha mafuta hayo na kuyahifadhi kwa
ujazo tofauti tofauti ambao aliuza kwa jumla na reja reja. Nayo hiyo biashara
yeye mwenywe ndiye aliyekuwa akisimamia. Grace hakuwa akihusika.
Kwenye
jengo hilo hilo ambalo kulikuwako ofisi yake na Grace, chini alikuwa na duka
kubwa sana ambalo liliuza vinywaji ambavyo havina kileo. Kwa bei ya jumla. Nayo
hiyo biashara, ilikuwa ni yeye pekee ndio msimamizi. Grace hakuwa hata akijua
kinachoendelea huko. Achilia mbali biashara zake nyingine ndogo ndogo ambazo
ungeweza kuzihesabu ni za kipuuzi, lakini si kwa Geb. Alikuwa na vitega uchumi
mbali mbali kama alivyokuwa akiambiwa na baba yake akiwa mdogo. Huweki shilingi
zote sehemu moja. Unasambaza. Ili upande mmoja ukikwama, uweze kunufaika na
kwengine. Nanaa hakuwa akijua analala kitanda kimoja na milionea mkubwa kwa kiasi
hicho.
Hakuwahi
na wala hakuwaza kumshirikisha mtu juu ya pesa anayomiliki. Ila waliojua
akaunti zake huko benki, alipoingia kutaka huduma za kibenki, ilibidi meneja wa
tawi amuhudumie yeye mwenyewe. Kijana huyo mkimya ambaye usingemkuta kwenye
majumba ya starehe isipokuwa nyumbani kwa mama yake na jumapili kanisani,
alikuwa amebeba utajiri mkubwa sana. Na alijitahidi kuweka pesa zake kwenye
benki tofauti, tofauti.
Aliitafuta
shilingi kuanzia chini. Yeye peke yake na shule aliyopewa urithi na mama yake
akiwa msaada mkubwa. Anaanzia wapi kumwambia Nanaa maisha yake? Amwambie nini,
aache nini? Je, Nanaa anao uwezo wa kumfahamu kwa ukubwa huo? Ni maswali ambayo
Geb hakutaka mtu ayajibu kwa kuwa hakutaka kumshirikisha mtu yeyote juu ya
hilo. Mali ni zake. Nanaa anampa atakacho. Basi. Inatosha.
Huo
ni upande ambao Nanaa aliona wazi hakuwa tayari Geb kuuzungumzia. Hakuwahi
kuzungumza mambo ya kazini akiwa nyumbani. Hata mara moja. Ila Nanaa alikuwa
akisikia, ‘kuna mtu nataka kuonana naye leo’ au ‘Jumamosi hii itakuwa ndefu
sana. Naweza nikachelewa kurudi nyumbani’. Basi. Hakumsikia akilalamikia
mfanyakazi, wala biashara. Ila Grace tu ndiye aliyekuwa akiongea mambo ya
kazini anapokuwa na mama yake au anapofanya mambo yake hapo nyumbani. Japokuwa
alikuwa na ofisi na wafanyakazi karibu kila mkoa Tanzania, Nanaa hakuwahi
kumsikia Geb anazungumza na simu za kikazi nyumbani. Ila Grace. Alitoka
nyumbani saa 1:30 asubuhi. Na kurudi saa 11 jioni. Akichelewa sana 6 jioni
mwisho. Jumapili ndio hafanyi kazi kabisa. Na wote walijua. Kama kunatatizo,
alitafutwa Grace, lakini sio Geb. Ni heri akae kazini siku ya jumamosi mpaka usiku,
ilimradi tu, jumapili apumzike.
~~~~~~~~~~~~~
Swala la uchumi ni kipengele kigumu sana kwenye ndoa nyingi. Hupuunzwa
lakini ndio eneo kubwa linaloleta matatizo kwenye ndoa nyingi hata kama ndoa
ilianza na msingi wa penzi la kweli.
Madhara ya kupuuzwa au kuwekwa misingi mizuri ya uwazi wa kiuchumi kwa
wanandoa, huwa haiepukiki. Kama si leo, basi ujue ipo siku lazima watakuja
kuona madhara yake.
Mama G atakuja kuzungumzia hilo. Usiache kufuatilia simulizi hili.
Mambo yameanza kunoga kwa Nanaa na Geb. Mambo ya ndoa ndio yanapamba
moto. Nanaa yu mjamzito wa miezi 7, anaelekea mwezi wa nane. Geb ataka na yeye
ndoa kabla ya mtoto huyo naye hajazaliwa.
Wakiwa ni kama wamevuka vipingamizi vyote, watu hawa wanaona mwanga.
Ni nini tena kitakachowazuia kuhalalisha ndoa yao?
Pengine huu ndio wakati muafaka wa milionea Geb, kuoa na kupumzisha
wadada wa mjini. Na kufunga wanaume midomo juu ya Nanaa. Watafanikiwa?
Zena anamsubiria mlalahoi Nanaa, ashuke kwenye
daladala ili ahudhurie kikao chake cha harusi.
Asilolijua Zena, maisha ya mtu ni Mungu pekee awezaye kuyabadili.
Haihitaji kikao wala ruhusa kumbariki mtu.
Mungu Humpa ampendaye na hakuna wakumuuliza kwa
nini?
Endelea kufuatilia.
0 Comments:
Post a Comment