~~~~~~~~~~~~~~~
Akamfuata
kwa haraka Vai chumbani. Akamkuta anafungasha vitu vyake. “Acha hasira Vai.
Unataka kuharibu amani yetu bila sababu.” “Ninayo sababu Zinda.” Vai alijibu
huku akiendelea kukusanya vitu vyake na kuvitupia kitandani. Ni kitanda hicho
hicho kilitoka kumtoa jasho Zinda masaa machache yaliyopita kabla yakupata
kifungua kinywa. Alipotoka tu bafuni kuoga asubuhi hiyo wakati Vai bado
amejilaza kitandani akichezea simu yake, alipomuona anajikausha, akamvutia hapo
kitandani na kumuanza mapenzi. Zinda alifurahia penzi la asubuhi hiyo.
Akamshukuru sana Vai kwa bao la kushitukizwa. Vai akacheka huku akielekea
bafuni.
Sasa
ndio kitanda hicho hicho ndicho kinachohusika kumsaidia Vai kuondoka! Zinda
akaona endapo Vai akiondoka, atajipunja mwenyewe. Akaka pale kitandani. “Tulia
kwanza Vai.” “Hapana Zinda. Acha tu niondoke. Umenitamkia wazi kuwa Nanaa ni
bora kwako kuliko mimi.” “Sio kweli!” “Sasa kwa nini unamng’ang’ania?” Vai
akasimama na kumrushia swali. “Simng’ang’anii bwana! Njoo mpenzi wangu.”
“Usitake kunifanya mimi mtoto mdogo Zinda.” Zinda akacheka huku akitaka
kumvutia pale kitandani. Vai akakataa.
“Kama
unataka kuwa na mimi, twende ukamkane Nanaa mbele yangu. Mwandikie talaka au
ukamwambie rasmi mnaachana naye na unataka jumatatu mkutane kwa mwanasheria
msainishane makaratasi yakuachana. Lasivyo naondoka.” Vai akaanza kuvua kigauni
alichokuwa amevaa. Kilikuwa kifupi sana. Alikuwa akikivaa mle ndani kwa ajili
yake huyo Zinda huyo.
“Nabadilisha
nguo. Navaa nguo zangu, naondoka. Endelea na Nanaa wako.” Vai alifungua zipu na
kukishusha mpaka miguuni. Lile tendo la kuinama na kuokota lile gauni, akiwa
amempa mgongo Zinda, tayari ulikuwa mtihani. Binti huyo mchanga, akageuka akiwa
na chupi tu, matiti yako wazi. Akasogea mpaka pale kitandani pembeni ya Zinda
kwa madai anatafuta nguo ya kuvaa ili aondoke.
~~~~~~~~~~~~~~~
Kwa
asili Zinda hakutofautiana sana na Malii. Tabia yao yakupenda wanawake weupe.
Hata wanawake aliokuwa akitongoza baa, lazima awe mweupe. Tofauti yao ilikuwa
moja tu, yeye Zinda hakujali kama umejichubua au la. Ilimradi uwe na hiyo
rangi, basi atakulipa ulale naye. Alipomuona Nanaa anawaka kama kaka yake.
Kiuno chembamba, akajiambia akimuweka ndani ndio ataridhika. Na Vai naye akajua
huo ugonjwa wake. Akatumia mwili wake kama fimbo kwa Zinda.
Sio
kwamba Zinda alisahau penzi la Geb kwa Nanaa, hata kidogo. Alijua wazi kuwa Geb
alikuwa akimfuatilia Nanaa kwa karibu sana hata kabla hawajamuona Nanaa
mwenyewe. Lakini alichanganyikiwa na
kujitoa akili pale alipotokea Nanaa mwenyewe. Wakati Geb anamuulizia Nanaa
tokea wakiwa shuleni, picha ya Nanaa kwa Zinda ilikuwa tofauti kabisa. Alijua
atakuwa ni msichana wa kawaida sana, asiyekuwa na sura wala umbile lakueleweka.
Mate yalimtoka alipotokea Nanaa mwenyewe. Akili zikaenda mbio nakuanza mchakato
wa kummiliki huku akimsahau Geb aliyekuwa akimsubiria.
Nanaa
alipomkataa ndipo akahamia kwa dada zake James. Zinda alibaki kuuliza, ‘nyinyi
ni wachaga wa wapi tena?’ Asiamini kuwa wale ni wachaga wa asili. Ukweli dada
zake James walikuwa wazuri. Hata uhuni waliokuwa wakifanya ulizidishwa na
usumbufu waliokuwa wakipata kutoka kwa wanaume. Walikamilika kwenye maeneo
mengi ya kike kasoro yao ni moja na kubwa, mtu wa ndani. Huyo ndio alikuwa
ni shida. Kama Mungu angeruhusu huyo mtu wa ndani akaonekanika nje,
hakuna mwanadamu angewasogelea kina dada hao warembo.
~~~~~~~~~~~~~~~
Zinda alibakia akikodolea macho mwili huo
mtupu uliokuwa pembeni yake. Akakumbuka Vai akiondoka hapo, usiku huo atakuwa
peke yake. Akanyoosha mkono angalau amguse. “Niache Zinda. Huna tofauti na
matapeli wengine.” “Sikutapeli Vai! Mimi nina nia ya kweli.” Zinda akajitetea
kwa upole ili angalau Vai atulie, aanze utundu wake hapo, amtulize. Vai naye
alishamuona vile suruali ilivyotuna. Akajua hali yake mbaya.
“Kwanza
ngoja nitafute viatu vyangu niviweke kwanza ndio nivae.” Akiwa vile vile na
chupi ndogo iliyoshikiwa na vimikanda tu, Vai akaanza kuinama anatafuta viatu
vyake. Alijua wazi anamtesa Zinda. Na hilo ndilo lilikuwa lengo. Hakuwa na
mpango wakurudi kuishi na Viola na kelele za mtoto wake, hata kidogo. Pale kwa
Zinda alikuwa akipewa pesa za matumizi kila siku. Maisha mazuri, matulivu.
Alitaka kumwingiza mtegoni tu ili atangaze ndoa kwa haraka.
Zinda
akasimama. “Nisikilize Vai. Kama shida yako ni kumwambia Nanaa kama wewe ni
mpenzi wangu, nitamtaarifu. Njoo.” “Hapana. Ninachotaka ni wewe uende na mimi
mpaka kwa Nanaa. Unitambulishe mbele za watu, kama mimi ndio mkeo mtarajiwa.
Mpe talaka yake. Uwe huru.” Vai akaongeza jambo jingine. Hawakuwa hata
wamezungumzia swala la ndoa. “Kama hutaki ndoa na mimi, huu mwili hutakaa
ukagusa tena. Leo asubuhi ndio ulikuwa mwisho wako.” Hapo Vai alisimama na
kujionyeshea mwili wake. Zinda akabaki amekodoa macho.
“Si
unaona? Haupo tayari. Mimi naondoka.” “No no noooo!” Na
kingereza kikapanda. “Unanichanganya Vai! Njoo kidogo tu. Talafu tuongee tukiwa
tumetulia.” “Nimekwambia mwili huu hutagusa tena. Naondoka.” Ukweli Zinda
hakuwa amepitisha wazo la kumuoa Vai kwa asilimia 100. Bado alihitaji muda
wakumchunguza zaidi haswa upande wa familia ambao ndio kipaumbele kwa Zinda
kaka wa familia. Kitendo cha Vai kushindwana na ndugu zake, kila akijaribu
kuwataja yeye mwenyewe Vai aliwazungumza vibaya sana, kilimfanya Zinda kuendelea
kusita kumfanya wake moja kwa moja. Ikawa ni hilo tu lakini mengine yote
hakuona kasoro kubwa sana. Alijiambia ni kuvumiliana tu. Mpaka lini? Hamna
ajuaye. Lakini katika swala la kitandani, hapo alitaka kuendelea kufaidi bila
ndoa.
“Hilo
mbona halina shida. Njoo utulie hapa.” “Sio mwilini kwako Zinda. Leo
umeniogopesha sana. Nitatulia tukitoka kwa Nanaa?” Zinda akanyong’onyea.
“Unamaanisha twende leo!?” Zinda akauliza kwa mshangao. “Kwa nini leo
tusipumzike halafu tupange siku nyingine?” “Hamna shida Zinda. Ukiwa tayari,
unajua pakunipata. Lakini mimi sitaendelea kupoteza muda hapa na mume wa
Nanaa.” “Mimi sio mumewe bwana! Mimi wako, Vai.” “Haya, chukua funguo za gari,
twende kwa Nanaa sasa hivi ukamweleze hayo. Na jumatatu mkaandikishane talaka mahakamani.”
Zinda akarudi kukaa kitandani.
Huku Kwa Nanaa.
Oliva alikuwa akimchokoza mama
yake wakati amelala kwenye kochi. Alikuwa akicheza na Fili pembeni kabisa ya
sebule. Akatambaa mpaka alipokuwa amejilaza mama yake kwenye kochi. Nanaa
alipitiwa na usingizi wakati Geb akiongea na kucheka na mama yake. Grace na
familia yake walipita jioni hiyo. Japokuwa vicheko vilikuwa vikiendelea, Nanaa
alilala muda mfupi sana baada ya kula vitumbua vyote alivyokuwa ameletewa na
Grace. Alikuwa na kochi lake refu alilopenda kutumia kwa kulala akiwepo hapo
sebuleni. Watu wote walijua ni kochi la Nanaa. Akikuta mtu yeyote amekaa,
atakutaka usimame umpishe kwenye kochi lake.
Oliva
akasimama mbele ya uso wa mama yake kwa kujishilia kwenye kochi hilo. Geb
alikuwa akimtizama kila anachofanya. Akamwangalia mama yake kwa muda, akagundua
amelala. Akaanza kumfungua macho. “Bwana Liv! Niache bwana!” Nanaa akalalamika
akiwa ameamshwa. Oliva akaanza kucheka kwa sauti mpaka watu wakamgeukia yeye
aliyekuwa akicheka kwa sauti. Lakini Nanaa alisharudi kulala.
“Anapenda
kucheka huyu! Hapo anamcheka mama yake jinsi alivyo lala.” Grace akaongea.
Wakamuona ananyosha tena kidole chake mpaka kwenye macho ya mama yake. Akaanza
kumchezea kutaka afungue macho. “Liv jamani!” Nanaa akalalamika tena. Oliva
alianza kucheka tena. Geb akaanza kucheka na kumchukua video. Kila tukio la
huyo mtoto alilofanya walilirikodi. “Huo uchokozi kachukua kwa mama yake tu,
sio mimi.” “Wala sio mimi. Ni wewe tu.” Nanaa akamjibu Geb, akakaa. “Geb
alikuwa mpole sana.” Mama G akaongeza. “Ujue siamini mama wewe! Sasa huyu mtoto
hapa anafanana nani kama sio Geb?” “Lakini tabia za mama yake.” Mama G
akaongeza.
Geb
akacheka “Liv! Liv! Niangalie basi.” Oliva akamgeukia baba yake. “Mwache mama
bwana. Njoo.” Liv aliendelea kucheka akiwa amesimama pale pale mbele ya mama
yake. “Muone! Kama mazuri vile! Na nikisimama hapa, nikakukamata!” Oliva
alicheka kwa sauti ya juu zaidi. “Mpaka Oliva mwenyewe amekucheka mjukuu wangu.
Hujiwezi kwa lolote.” “Hivi unafikiri nashindwa kumkamata huyo Liv? Unanidharau
mama! Jana tumeenda kutembea wote, mwenyewe ukashindwa.” “Mimi! Sio wewe
ulikuwa ukihema kama unataka kufa?” “Huyo mimi? Umenifananisha bwana.” Nanaa
akapinga kabisa. Kila mtu alikuwa anacheka.
“Basi
hapo mwenzio anataka nyonyo. Anakuchekea ili umpe nyonyo.” “Wewe Liv? Si
umepewa ugali na bibi yako? Umeshiba bwana.” Oliva alizidi kucheka mbele ya
mama yake. Nanaa akamnyanyua. “Una hamu na mama? Eti Liv?” Mara wakasikia simu
ya mezani.
~~~~~~~~~~~~~~~
Geb
akasimama, akabonyeza sehemu ya kupokea, lakini akaweka spika. “Kwema?” Geb akamuuliza mlinzi wa getini.
“Salama kabisa. Ila kuna wageni wa mama.”
Wote wakamgeukia Nanaa. “Mimi!?” Nanaa akauliza. “Sasa hapa mama nani kama sio
wewe? Miye ni bibi?” “Mgeni!? Muulize ni nani?” Geb akarudi kwenye simu. “Kina nani?” Geb akamuuliza mlinzi. Maana kama ni mtu
anayemtembelea Nanaa hapo ni James tu. Na akifika hapo, hasimamishwi getini.
Anapita moja kwa moja.
“Wamesema
wakionana na Nanaa, atawatambua.” Jibu hilo la mlinzi lilisikika na wote. Nanaa
hakuwa akitoka humo ndani labda na Geb, Grace, Jeri dereva au Mama G. Alikuwa
ni kama anafungiwa humo ndani. Geb hakutaka mtu yeyote hasa marafiki zake
wamfikie Nanaa kipindi hicho cha ujauzito, na vipingamizi kila kona. Akataka
atulie kabisa. Na baada ya kuahirisha harusi na ugonjwa wa miguu waliompa
wageni wake siku walipokuja kwenye kikao, ndio ilikuwa kabisaa. Hakuwa na
wageni wengi. Kwanza ni kama Zinda aliharibu kikundi chao.
“Sasa waambie
kama hawataki kujitambulisha, watakaa sana hapo. Sitaki kuonana na mtu
nisiyemfahamu.” Nanaa akajibu, na mlinzi
akasikia. “Kata simu Geb. Wasinichezee akili.” Nanaa akaongeza. Geb alipokata
tu, mlinzi akapiga tena.
“Acha nipokee mimi Geb.
Wasikusumbue mpenzi wangu.” Nanaa akataka kusimama, lakini Geb akamsogezea
simu. Akafanya kama alivyofanya Geb. Akaweka kwenye spika ili wote wasikie.
“Unasemaje?” Nanaa akaitika. “Wamejitambulisha kama Zinda na Vai.”
Ukimya ukazuka. Wakaanza kuangaliana. Nanaa akamwangalia Geb kama kumtaka
ushauri, Geb akanyanyua mabega juu kumwambia hajui. “Wanataka nini?” Nanaa akauliza tena. “Wamesema
wanashida ya kuzungumza na wewe.”
Mlinzi akajibu. “Si bado wapo nje?” “Ndiyo.
Sijawafungulia geti bado.” “Safi sana. Sasa waunganishe na simu ya hapa.
Waongelee kwenye hiyo hiyo nguzo hapo nje, waambie mimi nawasikia.
Usiwafungulie hata geti dogo.” “Sawa mama.” Mlinzi akajibu kwa heshima.
Akawaunganisha bila wao kujua. Kwa hiyo ndani walimsikia Mlinzi, na wao watu wa
nje.
“Zungumzeni na
mama hapohapo mliposimama, anawasikia.”
Mlinzi aliongea nao yeye akiwa ndani ya kibanda cha ndani, wao nje. Huku
akiwatazama kwa kamera. “Unachoogopa nini? Zungumza naye sasa kama unania kweli
ya kunitambulisha.” Wakamsikia Vai akiongea. Wakaangaliana na kushangaa ni nini
kinachoendelea.
“Kwa
nini nisizungumze naye uso kwa uso?” Walimsikia Zinda anamjibu Vai. “Acha
tupate wasaa wakumuona ndio itakuwa vizuri Vai.” Zinda alisikika akibembeleza.
Hata Danny hakuwa ameelewa. Wakabaki wakiwasikiliza. “Nisikilize Zinda. Kama
wewe unamuogopa Nanaa, mimi naondoka.” Wakasikia vitisho. Watu wote wa ndani
walitulia kabisa ili kina Zinda wasijue kama wanasikilizwa ili angalau wajue
kilichowaleta. Hapo ndipo wakajua wamekuja na shida yao. “Usiondoke Vai bwana.
Tumekuja mpaka hapa. Huoni kama nina nia?” “Mbona sasa unajiumauma?” Vai
akamuuliza. “Hapana. Ila sijui naongelea wapi!” Zinda akaongeza. “Zungumzeni tu, anawasikia.” Ukimya ukatanda nje. Wakajua
wameshituka kusikia walikuwa wakisikilizwa. “Naomba kama
hamna kitu cha kuzungumza mpishe hapo getini.” Wakamsikia mlinzi akipiga mkwara.
Alijua wazi tajiri yao anasikiliza. Huyo alikuwa mke wa tajiri wake. Lazima
kuonyesha kujali. Kwanza alijua wazi kwa majibu ya awali kutoka kwa Nanaa, sio
watu wanohitajika humo ndani. Hakuogopa.
“Nazungumzia
wapi?” Wakamsikia Zinda akiuliza. Hakuwahi kusimamishwa getini kwa Geb. Alikuwa
akifika na kufunguliwa geti. Leo anaambiwa kuzungumza tu hapo hapo nje! “Hapo hapo uliposimama ukiongea anakusikia.” Mlinzi akajibu huku watu wa ndani wakiwasikiliza. “Nanaa!” Zinda akaita. Nanaa akanyamaza.
“Mbona haitiki sasa!?” Walimsikia Zinda akilalamika. “Wewe ongea mkuu.
Anakusikia.” Mlinzi akajibu. “Nanaa? Ninaomba
kuzungumza na wewe. Tafadhali.” “Tafadhali ya
nini? Mwambie atoke tuongee. Anajifungia nini humo ndani kwa watu?” Walimsikia
Vai akizungumza. “Tulia basi Vai!” “Naona unaanza kubabaika!” “Sibabaiki. Si
ndio naongea.” Wakabaki wakiwasikiliza.
“Nanaa,
unanisikia?” Zinda akaongeza. Wote pale ndani
walikuwa wakimwangalia Nanaa. “Nisikilize Zinda.” Nanaa akajibu. “Mimi sikufahamu wewe isipokuwa
kwa kupitia kaka. Ukitaka kuzungumza na mimi, mtafute kwanza kaka. Muombe aje
hapa, ndio nitazungumza na wewe. Lasivyo sitaki kuwaona hapo getini tena. Iwe
mara yenu ya mwisho kusimama hapo bila kaka. Nikisikia sauti zenu, kaka awepo pembeni
yenu. Lasivyo mpo matatizoni. Haya, ondokeni.” “Ungenisikiliza Nanaa,
tafadhali.” Zinda alibembeleza kama sio yeye. “Deo!” Nanaa akamwita yule mlinzi aliyekuwepo zamu muda
huo. Walikuwa na walinzi wanne tu waliokuwa wakipokezana hapo. Mchana anakuwepo
mmoja, usiku wawili. “Nipo mama.” Mlinzi akaitika. “Sitaki kuwaona
hao hapo getini, labda warudi na kaka James.” “Sawa.” Mlinzi akajibu.
Ya sirini Mwangani.
“Si
ungemwambia tu? Nakuona kama huna nia Zinda!” “Nia ipo lakini ni uzungumzaji
gani huo? Naongea na nguzo!” “Kwani hapa anafanya kazi za ndani?” Wakamsikia
Vai akimuuliza Zinda. “Hapana Vai. Si umesikia anaitwa ‘mama’ hapo?” “Itakuwa huyo mlinzi
amemwita mama mwenye nyumba sio Nanaa. Na ushamba ule apate wapi mwanamme
anayeweza kumiliki jumba kama hilo?” “Acha ubishi Vai!” “Sasa unanibishia nini?
Mimi namfahamu Nanaa zaidi yako. Mshamba yule hata kuvaa hajui. Nguo zenyewe
alikuwa akisubiria anazotaka kutupa Viola ndio achukue yeye. Mpaka chupi zangu
na za Viola zilizochakaa alikuwa anaziokota ndio avae yeye.” Wakamsikia Vai akiongea
na kuongeza na cheko juu kama anayemdhihaki Nanaa.
“Sasa
unacheka nini?” Wakamsikia Zinda akiuliza. “Nimekumbuka kitu.” “Kitu gani kama
sio unanicheka mimi?” “Sio wewe bwana Zinda! Ni Nanaa. Kuna siku Viola alitupa chupi
zake. Machupi mabaya, halafu yakawa yamechakaa. Si Nanaa akaenda kuyaokota jalalani!
Viola akamuona. Acha amsemee kwa mama! Tena akamwambia amemwibia. Bwana
alitandikwa kama mbwa!” Mpaka Zinda aliumia lakini Vai alizidi kucheka.
“Sasa
hapo unacheka nini Vai!?” “Hee! Si nimefurahi! Na ndio nakuhakikishia hapa sio
kwa Nanaa. Wewe mwambie huyo mlinzi azungumze na huyo mama mwenye nyumba,
wamtoe hapa. Tumpe habari yake, tuondoke zetu. Tena unaweza sema chochote kwa
huyo mama mwenye nyumba, ili amtoe humo ndani kama paka jizi. Tena mimi naweza hata kumuhakikishia huyo mama
kuwa Nanaa ni mwizi, wamtoe humo ndani, atawaletea majambazi wawaibie. Mgongee
tena huyo mlinzi mwombe kuzungumza na huyo mama mwenye nyumba, halafu mimi nitazungumza
naye huyo mama. Nitampanga mpaka atamtoa tu huyo Nanaa. Asijidai amefika!”
“Vai!?” Walimsikia Zinda akiongea kwa unyonge zaidi.
“Nini
sasa na wewe!? Changamka au mimi mwenyewe nikamgongee huyo mlinzi?” “Kwa hiyo
hivyo ndivyo mlivyokuwa mkiishi na Nanaa?” Zinda akauliza kwa unyonge. “Vipi!?”
Vai akauliza. “Lakini hivi sivyo mlivyonieleza juu yake! Mliniambia ni tabia ya
Nanaa kuiba vitu na wanaume za watu hasa wenye pesa! Sasa hivi umeongea wewe
mwenyewe kuwa Nanaa ni mjinga, mshamba na amezubaa! Hawezi kupata
mwanaume mwenye pesa! Na ukasema mlikuwa mkimsingizia wizi! Mbona unakuwa na
kauli nyingi? Nikuamini kwa lipi?” Nanaa alikuwa akifuta machozi. Mpaka walinzi
walikuwa wakisikiliza.
“Sio
mimi wewe Zinda! Vuta kumbukumbu zako vizuri. Ni mama na Viola. Viola ndio
alikudanganya alipokwambia Nanaa alimpokonya mwanaume wake. Sasa kwa taarifa
yako tu, ni Viola ndiye aliyempokonya Nanaa mwanaume aliyetaka kumuoa. Akambebea
mpaka mimba ili kumfanya amuoe yeye. Ila kibao kikamgeukia. Yule
mwanaume akamgeuka wakati mimba ina miezi 7 sijui! Ambapo Viola alishindwa
kutoa. Alex akamwambia Viola anajutia kitendo cha kumsaliti Nanaa.
Hamtaki tena Viola ila mtoto wake atamtunza. Ndio mtoto yule! Mimi siku ile
sikuongea sana. Ni mama na Viola wenyewe. Usiniingize.” “Kama wewe ni mkweli,
kwa nini baadaye hukuja kuniambia ukweli?” Zinda akahoji.
“Hee!
Nije kusutwa? Mama alitaka umuoe Viola sio Nanaa. Sasa ulitaka mimi nije
niongee halafu waje wanione mimi mchonganishi? Kwani wewe mwenyewe huna akili?
Ulitakiwa kufikiria tokea mwanzo. Kwa nini uliwasikiliza?” “Kweli mimi ndio
sikuwa na akili tokea mwanzo.” Sauti ya Zinda ilisikika ya majuto.
“Sasa
hayo yamepita Zinda. Hata mimi sikupenda walivyokudanganya. Ndio maana mpaka
leo sitaki mama wala Viola na mwanae wafike kwetu. Nimewakatalia kata kata. Sitaki
kuona sura zao pale kwetu.” Vai aliongea kijasiri. “Sikujua kama unawakatalia
Vai! Uliniambia unawaandalia mazingira mazuri ndio waje!” “Akuuu!
Kwanza ujue bado Viola anakutaka.
Na ninamjua jinsi anavyopenda mabwana wa watu. Huyo mwanaume wa Nanaa
aliyemchukua, huyo Alex wala sio wa kwanza. Walishakuja wanaume zaidi ya wawili
pale nyumbani wakitaka kumchumbia Nanaa. Lakini mama akawa anawasukumia
kwa Viola. Tena kwa uhakika nilio nao ni wawili ndio mama alihangaika nao.
Kwakuwa walikuwa na pesa. Huyo mmoja wakamfukuza kwa kuwa alikuwa lofa, hana
kitu. Lakini hao wawili kwa kujua na kuona kwa macho, Viola aliwashikia mimba
ili wamuoe yeye. Akaona hawana muelekeo na yeye akazitoa mimba. Sasa ulitaka
nimlete nyumbani halafu anigeuke kwako?” “Vai! Vai! Vai!” Zinda alisikika.
“Ni
nini?” “Sio wewe uliyeniambia haya yote ndio anayoyafanya Nanaa tokea mkiishi
naye?” “Aaa- aali ali!” Vai akawa amekamatwa uongo. “Vai? Wewe uliniambia mbele
ya mama kuwa lazima tukomeshe tabia ya Nanaa kubebea watu mimba ili wamuoe.
Mkanishawishi na mama yenu nikimbilie haraka kanisani kusimamisha ndoa. Tena
wewe ukaniambia nitakuwa nimeua ndege wawili kwa jiwe moja. Nanaa atalipa
kwa uovu aliomtendea Viola wa kumchukulia wanaume waliokuwa wakitaka
kumuoa Viola, Nanaa akaishia kuwabebea mimba na kuzitoa. Na mkasema nitakuwa
nimelipa kisasi kwa rafiki yangu pia, kwa kunigeuka! Mkanipa mbinu nyingi
zakunitia moyo katika yote. Mkanipandisha na kunijengea chuki kali zaidi. Leo unabadilisha
maneno unasema ni tabia ya Viola! Nikuamini katika lipi?” Zinda akauliza. Vai
akabaki kimya. “Tafadhali naomba msiendelee
kusimama hapo. Naomba muondoke.” Zinda na Vai walimsikia mlinzi
kwa kupitia nguzo hiyo hiyo iliyokuwa na spika, akiwafukuza. Wakaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~
Nanaa
akazima simu. Geb akairudisha sehemu yake. “Huna haja yakulia Nanaa. Unatakiwa
kushukuru. Mungu anaanza kupambana na adui zako. Unakumbuka maombi
tuliyoomba leo asubuhi? Hakika Mungu wako anajibu kwa moto Nanaa! Wamejirudi
wenyewe! Na yaliyo sirini Mungu ameyaweka mwangani.” Geb akamfariji. Akakaa
pembeni yake. “Ni kweli Geb. Si Vai wala Zinda waliojua tunawasikiliza.
Wameongea yote tukiwasikiliza! Na ni kweli kuwa hiyo ni kazi ya Mungu peke
yake. Amewaleta adui zako mbele yako. Pole.” Grace akaongeza kwa upole.
“Zinda
anaonekana ameanza kujuta.” Danny akaongeza. “Sana. Anaonekana hata yeye
ameumia. Unajua Geb aliponiambia juu ya kumsubiria Mungu, nikawa najiuliza
moyoni. Nikasema hivi atakuja kumuoa Nanaa kweli? Maana kila nilipokuwa
namwambia Geb ni lini hiyo harusi inafungwa, akawa ananijibu namsubiria Mungu.
Nikajiambia haya majibu mbona ya jumla jumla hivi! Hamna tarehe wala
mipango!?” Mama G akaongeza
“Kwa
kuwa kweli hata mimi sikuwa najua chakufanya mama! Kilikuwa ni kitu ambacho
kinanisumbua sana. Kwanza ukumbuke ni kama ndio jambo langu la kwanza na la
msingi ambalo nilishapanga maishani halafu likakwama. Siku namwambia Danny
awataarifu watu kuwa tunaahirisha harusi mpaka hapo watakapojulishwa tena, hakika
machozi yalinitoka. Niliumia kuliko nitakavyokwambia. Niliegesha gari pembeni
na kuanza kumwambia Mungu anitetee. Nilimwambia Mungu mimi na Nanaa
hatukumtendea mtu ubaya wowote ule. Nikamsihi aingilie kati hili jambo. Hapo
nilikuwa nimeshazungumza na yule mwanasheria zaidi ya mara mbili tukitafuta
jinsi ya kumshinda Zinda kisheria. Kila mbinu alizokuwa akinipa, nikaona
zitazidi kumdhalilisha Nanaa. Ndipo nikanyanyua mkono nikajimbia sitaweza mpaka
Mungu aingilie kati. Sikutaka Nanaa asimame mahakamani halafu aishie
kudhalilishwa tena. Nikajiambia hapana. Acha Mungu apigane kama alivyopigana
pale hospitalini tukatoka na Nanaa akiwa mzima. Wote tukashuhudia kwa macho.”
“Na kweli Mungu ameingilia kati. Amewaleta mbele zetu wote.” Mama yake akajibu.
“Sasa
unafikiri Zinda atajirudi baada ya kujua ukweli?” Nanaa akauliza kwa upole.
“Nina mjua Zinda. Kwa kusikika kule, anaonekana akili zake zimerudi. Anaweza
asimtafute James leo, lakini namjua. Atamtafuta tu.” “Kweli Danny!?” Nanaa akauliza huku machozi yanaendelea kumtoka.
“Mwamini Mungu Nanaa. Mimi naamini huu ndio wakati wenu. Leo ni mwanzo wa
majibu yenu. Kitu kikubwa kitatokea.” “Amina Danny. Hiyo ni ishara ya kwanza na
kubwa kuwa Mungu ameanza kutenda.” Geb akadakia.
Nanaa
akabaki ameinama anawaza huku akichezea nywele za mwanae. Hakujua kama ni aibu
ya historia yake ya nyuma kusemwa wazi wazi. Kuwa alikuwa akiokota chupi zilizochakaa,
au la. Alibaki akiwaza. “Nanaa!” Geb akamuita kwa upole. “Abee!”
Nanaa aliitika na machozi. “Tafadhali usilie.” Geb akaongeza. “Tena huna haja
hata ya kuhuzunika Nanaa. Mimi naona Mungu amekuinua sana mpaka hata wao
wenyewe hawaamini. Si umeona jinsi Vai alivyokuwa hakubali kama hapa ni kwako?”
Mama G akaongeza kama kumtuliza.
“Amenikumbusha tu mbali mama yangu ndio maana nalia. Lakini ni kweli
namshukuru Mungu. Alinitoa mavumbini! Jalalani kabisa. Na wala usifikiri Vai
amedanganya. Nimeishi kwa kuvaa kutokea jalalani kwa muda mrefu tu. Walikuwa wakiona
shida kunipa hata nguo zao zilizochakaa! Walikuwa wakiona ni bora watupe kuliko
kunipa! Sasa baada ya kuwa nikichapwa kwa kuokota halafu wananisingizia wizi,
nikawa nikiokota nawafuata wote wakiwa pamoja na mama mkubwa, naomba kuichukua
hiyo nguo ya jalalani. Wakinicheka ndio najua nimeponea hapo, nafua, nakuifanya
yangu. Na masweta yao hivyohivyo. Vikanisaidia mpaka nimekua. Kwa hiyo hapa nilipo ni huruma za
Mungu tu.” Nanaa alifuta machozi na kutulia.
“Sasa
kwa nini hukuwa ukimwambia James awe anakusaidia pesa ndogo ndogo?” Grace akauliza.
“Ukumbuke na yeye kaka alikuwa akisoma. Hakuwa na pesa nyingi. Halafu sikuwa na
simu ya kumtafuta. Nilikuwa nikimwandikia barua. Na nikiandika barua nakuwa
namahitaji ya msingi kuliko kuomba nguo za ndani ambazo nilikuwa najua naweza
kutumia hata za kina Viola. Nilikuwa naona ni heri anilipie ada nisome, kuliko
mambo ambayo hayakuwa yamsingi.” Kila mtu hapo akajisikia kuumia.
“Mbona
mojawapo ya madai ambayo mama yako mkubwa aliyomdai Geb ilikuwa ni ada!?” Mama
G akauliza. “Ni kweli alikuwa akinipa pesa. Lakini unaweza kuta hazitoshei ada
na michango ya shule. Kuna kipindi nakumbuka wakati nipo kidato cha pili
nilirudishwa nyumbani. Nililipa ada nusu na pia sikuwa nimelipia michango ile
midogo midogo ya shule. Nilikaa nyumbani karibia majuma mawili mama mkubwa ananiambia
yeye hana pesa, mpaka barua yangu ilipofika kwa kaka. Alipojua nimerudishwa
nyumbani sina pesa, nakumbuka akaja kwa haraka. Akanirudisha shule na kunilipia
kila kitu. Sasa hapo utaanza tena kumwambia sina nguo za ndani au taulo sijui,
wakati mtu analipa pesa yote hiyo!? Nilikuwa siwezi mama. Mambo mengine
nilikuwa najihangaikia tu mwenyewe.” “Pole Nanaa mwanangu. Pole sana.” Nanaa
akavuta pumzi kwa nguvu kama kusafisha kifua. Kila mtu alikuwa kimya akiwaza
lake huku wakiumia moyoni.
~~~~~~~~~~~~~~~
Geb
akambusu begani. Nanaa akamwangalia kwa tabasamu la kinyonge. “Asante.”
Akashukuru kwa sauti ya upole. “Naomba utulie Nanaa. Tafadhali. Jaribu
kurudisha mawazo hapa tulipo. Kwa ajili ya mtoto huko tumboni na wewe
mwenyewe.” Geb aliongea naye kwa upole huku amemuegamia begani akimtizama.
“Sawa?” Geb akamuuliza. Nanaa akakubali kwa kuitikia kwa kichwa. Liv alikuwa
kimya ametulia mikononi mwa mama yake. Wote wakamwangalia wakakuta akimtizama
mama yake kwa makini kama anayejua mama yake anahuzuni.
“Twende
mwanangu ukanyonye.” Nanaa akataka kusimama. “Ngoja nikupokee mtoto kwanza.”
Geb akasimama kwa haraka. Oliva akakunja uso kukataa. “Namsaidia mama kusimama
Liv! Sikutoi kwenye nyonyo.” Oliva akajificha uso kwa mama yake kuonyesha
msisitizo wa kukataa kabisa. “Hivi ujue wewe Liv utatoka kwa mumeo uje unyonye
wewe! Ukoje jamani?” Nanaa akafanya wacheke na kuwaangalia.
“Kama
shangazi yake! Mpaka leo yupo nyuma ya mgongo wangu! Naona hivyo ni vya
kurithi.” Mama G akaongeza. “Mama wewe! Mimi nipo nyuma ya mgongo wako jamani!”
Grace akauliza kwa kulalamika. “Niambie ni lini yamepita hata masaa 4,
hujasikia sauti yangu ukatulia, wewe?” Kila mtu akacheka. “Usiku.” Grace
akajibu. “Si kwa kuwa unaenda kulala? Hata ukiwa kazini unapiga, Grace!” Geb
alimjua dada yake, akamtizama na kucheka. “Sasa ampigie simu mama, halafu
amkose! Unaweza dhani nyumba itawaka moto. Kama mpo ofisini utamuona
amekusimamia mbele yako na simu yake mkononi. Anakwambia hampati mama kwa simu.
Hapo na mama anakuwa amekwambia ametoka kuzungumza naye. Basi atakutia wasiwasi
mpaka na wewe umpigie mama!” Geb akaongeza, Danny na yeye akacheka.
“Sasa
unacheka nini na wewe Danny?” Grace akamuuliza mumewe. “Mimi nimefurahi mke
wangu. Kwani kosa?” “Wewe sema tu. Najua kuna ulilokumbuka.” Grace akaongeza
huku akicheka. “Na hawezi kulala mpaka awe amezungumza na mama yake. Yaani ndio
awe mtu wa mwisho kuzungumza naye ndio ataweza kulala. Lasivyo huo usiku huna
utakalomwambia Grace, akalielewa.” Kila mtu akacheka. “Anazidisha bwana Danny!”
“Mmmh!” Mama yake akaguna.
“Basi
kumbe huyu ninaye huyu!” Nanaa akaongeza akimaanisha Oliva. “Si nimekwambia
vipo kwenye damu? Nilikusimulia mambo ya Grace. Basi yupo hivyo tokea mtoto.
Wote tunamjua. Yaani wewe unatakiwa mfikirie yeye. Asikwambie lolote, ila kama
anaumwa, basi ujue ugonjwa wake na uwe unamuulizia ulizia kila wakati na umpe
dawa. Usipofanya hivyo ujue ni machozi. Basi mimi na Geb tukawa tumeshamjua.
Tukimuona analia peke yake, tunaanza kuulizana na Geb. Mpaka tujue tatizo lake
ndio kuanza kumbembeleza.” “Na hajawahi kubadilika G, mpaka leo. Wewe
ukibahatika kumsikia analalamikia kitu, basi hiyo ujue ni bahati yako. Hangaika
kwa haraka kutatua hilo tatizo. Maana hatarudia kulalamika tena, ila kulia.”
Geb akaongeza nakufanya wazidi kucheka.
“Usiige
vya shangazi yako wewe Oliva. Mwache abakie yeye peke yake mwenye tabia hiyo,
kwenye hii familia, tupumzike.” “Kwani mmenichoka?” Grace akauliza na sauti
yake ya upole. “Hata kidogo mwanangu.” Mama G akajibu kwa haraka nakufanya kila
mtu azidi kucheka. “Nenda kamnyonyeshe Oliva wangu bwana! Kalifuata hilo nyonyo
tokea mbali! Halafu kasubiria sana. Mpe nyonyo.” Bibi yake aliongeza. Nanaa
akamwangalia mwanae. “Eti Liv? Umesubiria sana?” Oliva akamshika kifuani kutaka
kutoa ziwa. “Subiri kwanza. Nenda kwa dad ili nisimame.” Oliva akagoma
akaendelea kumng’ang’ania mama yake.
“Sasa
hapa tunasimamaje mwanangu? Basi nikuweke pembeni ili nisimame. Tutaanguka wote
hapa.” Oliva akakataa. “Wadogo zangu pia wananyonya mpaka leo.” Fili akadakia kule
alipokuwa akicheza game. “Yamempata.” Mama yake akaongeza kwa sauti ya chini,
wote wakacheka. “Si kweli mama eeh?” Fili akamuuliza mama yake akitaka ungwaji
mkono. “Ni kweli mwanangu. Wala hujakosea.” Grace akamtetea. “Si nilikwambia
mimi?” Fili akamgeukia Nanaa.
“Wale
ni wadogo kuliko Liv.” Nanaa akajibu. “Mbona na wao wanakula kama Liv na bado
wananyonya?” Nanaa akajua hatamuweza Fili. Mpaka Geb akacheka. “Hapo umefika.
Mtoto kwa hoja huyo!” Baba yake akadaikia. “Ni kweli Fili. Haya nenda kitandani
kwa Liv, chukua mtandio mkubwa upo palepale utauona. Ulete ili aje anyonye.” Fili akasimama kwa haraka
akaenda chumbani kwa bibi yake kufuata huo mtandio kitandani kwa Liv. “Bora
ulivyokubali yaishe. Hapo asingemaliza.” Mama yake akanong’ona wakati Fili
ameondoka.
Akarudi
na mtandio mkononi. “Sasa mtandio wa nini wakati wa kunyonyesha?” Fili
akamkabidhi Nanaa na swali. “Ili nijifunike anyonye.” Nanaa akajibu huku Geb
akimsaidia kuzungusha ule mtandio mabegani kwake. Afunike matiti yake wakati
ananyonyesha. “Mbona mama yangu hafanyi hivyo? Ananyonyesha bila kujifunika.”
“Wewe Fili wewe!?” Grace akashituka sana. Mama G akaanza kucheka. “Leo
mtakoma.” Mama G akaongeza huku akicheka. Geb alikuwa akimtizama huku
anatingisha kichwa.
“Ni kweli
mama. Wewe hufuniki watoto wakati wananyonya.” “Mimi naona ukaendelee kucheza
tu.” Baba yake akaingilia. “Nilikuwa..” “We!” Baba yake akamkata kwa ukali.
“Sawa dad. Nilitaka..” “Nimekwambia kacheze, au unataka kwenda kulala sasa
hivi?” “Sina usingizi.” Fili akajibu kwa upole. “Basi cheza, mwache mtoto
anyonye.” “Atahemaje sasa!?” Fili akarusha swali jingine. Mama G alizidi
kucheka. “Hapo hatanyamaza mpaka hoja yake yeye ishinde.” Mama yake akaingilia.
“Basi anakwenda kulala sasa hivi.” Danny aliongeza kwa mkwara.
“Wanasema
inabidi kuvuta hewa safi na kutoa hewa chafu.” Fili aliendelea kwa upole huku
akisogea taratibu kama kumkwepa baba yake. Mpaka Nanaa akaanza kucheka. “Ni
kweli anti. Mimi sidanganyi. Wanasema usipovuta hewa safi, ukijifunika mpaka
kichwani, unakufa. Mimi nikilala sitaki mama anifunike mpaka kichwani. Nahakikisha
natoa pua nje. Sasa Liv…” Liv aliposikia anatajwa jina lake na Fili akatoka kwa
haraka huku akichuruzika maziwa kutoka mdomoni.
Alipomuona
Fili karibu yake akashuka miguuni kwa mama yake kwa haraka. “Bora uende tupunguze
hizi shutuma.” Nanaa akajirudisha vizuri huku kila mtu anacheka. “Are you okay
Liv?” Fili akachuchumaa kwa haraka pale alipokuwepo Liv. Oliva alikuwa
akitambaa kumfuata yeye huku akicheka. Ni kweli alimpenda Fili. Kila alipokuwa
akija hapo, alitaka kucheza naye tu. “Twende tukaendeshe magari. Usiwe
unajifunika mpaka pua.” Fili alitangulia, Oliva akawa anamfuata kwa nyuma huku
akitambaa kwa haraka.
“Unajua
kufa?” Walimsikia Fili akimuuliza Liv. “Wewe Fili wewe!?” Baba yake alimuwahi.
“Ungemuacha amwambie tusikilize.” Nanaa akamuwahi. “Kwani nimefanya nini mimi?
Namfundisha tu, dad!” Fili alijiteta kwa baba yake. “Bwana mtoto huyu!” Danny akalalamika.
Grace alikuwa akicheka sana. “Nataka kumfundisha asijifunike pua atakufa.”
“Ukikazania jambo wewe! Basi hapo mpaka wewe ndio uwe mshindi! Haya sema
yaishe.” Danny akamalizia. “Namwambia Liv, dady!” “Sasa kwa nini umwambie mambo
hayo?” “Ni mtoto, mimi mkubwa. Najua mambo yote.” Mama G alikuwa akicheka mpaka
anafuta machozi kama Grace. Geb alicheka huku akitingisha kichwa.
“Tutajuta
Fili kuzaliwa wa kwanza. Haya mfundishe, halafu mcheze.” Geb akaongeza. “Liv!
Liv!” Fili akamuita. Oliva mwenyewe alikuwa akitafuna gari la Fili.
“Nilikwambia usile gari. Sio chakula. Kama unataka nyonyo, nenda kwa mama yako
unyonye, lakini usifunike pua.” Walizidi kucheka na Oliva naye alikuwa akicheka
huku akimtizama Fili. “Umesikia?” Oliva alikuwa anacheka tu huku mate
yakimtoka. “Lazima uelewe. Ukifa unakuwa unalala moja kwa moja. Hakuna tena
kucheza na mimi wala kunyonya. Umesikia?” Fili alimsisitiza Oliva kama anayeelewa
vile.
“Hapo
roho ndio imemtulia na ndio atanyamaza. Hakubali kushindwa huyo!” Danny
aliongea kwa sauti ya chini kidogo. Kila mtu alikuwa akicheka. Geb akanyanyuka.
“Unaenda wapi tena?” Nanaa akauliza. “Nakuletea Ice cream yako. Au hutaki?”
“Njaa imeanza kuniuma. Naona nile tena ndio nipate ice cream.” Nanaa
akajitahidi kusimama. “Mmmh!” Mama G akaguna. “Unavyokula! Utafikiri una mapacha
huko tumboni! Au ni dume hilo?” Nanaa akacheka. “Naijua shida yako mama.
Unataka kujua jinsia ya mtoto.” Wote wakacheka.
“Umejuaje?”
“Nakujua sana. Wewe umevumilia muda wote huo, miezi imebaki michache tu,
utamjua mjukuu wako tu.” “Kwa nini kutuweka roho juu Nanaa? Basi jumatano
nikupeleke mimi kliniki. Namuuliza daktari ukiwa wewe haupo. Nabakia siri yangu
tu.” Mama G alizidi kubembeleza. “Naomba usubiri mama.” Wakamsikia Geb anajibu
yeye huko jikoni. “Basi hapo ndio basi tena! Akiongea huyo, ujue tutakuja
kumkuta huyo mtoto siku hiyo.” Nanaa akacheka.
“Afadhali
Geb. Mama atulie.” “Kwanza najua sana ni mtoto gani. Ni kutaka tu uhakika.”
“Hapana mama bwana! Hujui. Unavyonibembeleza hivyo! Ungekuwa unajua wewe,
usingekuwa ukihangaika hivyo.” “Nikwambie halafu twende tukamwangalie jinsia?
Kama mimi nimepatia, unanilipa milioni moja?” Nanaa akabaki akifikiria mlangoni
akitaka kuingia jikoni alipokuwepo Geb akimpashia chakula moto.
“Ukikosea
wewe ndio utanilipa mimi hiyo pesa?” Tayari Nanaa akashawishika. “Ndiyo.
Nakulipa hapo hapo. Yaani jumatano tunaenda wote kliniki na hiyo pesa kwenye
pochi. Naweza kukupa kabisa ukaishika.” Nanaa akacheka. Geb akajua anakaribia
kushawishika. “Kuwa na msimamo Nanaa. Acha kupenda pesa.” Geb alifanya kila mtu
acheke. “Milioni sio ndogo Geb!” “Wewe subiri kama ulivyopanga tokea mwanzo.”
Geb akasisitiza. “Basi mama. Sitaki tena.” Wakaendelea kuzunguza huku wakicheka
na kutaniana.
Kila Jambo Na Wakati Wake.
Mara
simu ya Danny ikaanza kuita. Akaitoa mfukoni wakamuona ametoa macho. “Nani?”
Mkewe akamuuliza. "Zinda!” Kila mtu akabaki kimya. “Sipo tayari kuzungumza
naye.” Danny aliongea huku akiitizama ile simu. “Hapana.” Danny akazidi kukataa
kwa sauti. Simu ikakata. Baada ya muda tena, ikaanza kuita. “Msikilize tu
Danny. Si ndio kitu ulikuwa ukitaka? Usikubali hasira ikutawale mume wangu. Na
wewe ndio Mungu amekujibu. Pokea muujiza wako. Jishushe, mambo yaishe.” Danny
alibaki kimya akiitizama ile simu. Mpaka mishipa ya pembeni ya macho
ilimsimama. Mikono yake ilianza kutetemeka mpaka wakaona.
Akaiweka
simu chini. Ikaita tena na tena, Danny akabaki akiitizama. “Danny!” Mkewe
akamwita kwa upole. “Nazungumza naye nini, Grace?” “Msikilize ndio utajua kitu
cha kuzungumza naye.” Mkewe akajibu akijua wazi umuhimu wa Zinda kwenye maisha
ya mumewe. Zinda kwake hakuwa rafiki tu. Hata watoto walijua ni baba mdogo.
Alishampeleka Fili mpaka kwa wazazi wa Zinda, mjini Tabora. Fili anawatambua kama
babu na bibi zake kabisa mzaa baba. Sikukuu nyingine, Danny alibeba familia
yake na kwenda kusherehekea nyumbani kwa kina Zinda, Tabora. Grace alijua jinsi
Danny alivyokuwa ameumia.
Simu
ikakatika. Danny akamtizama mkewe. Grace akabaki akimtizama na yeye. “Sidhani
Grace. Naomba muda mke wangu. Katika haya yote yaliyotokea, ni kama Mungu
alinifungua macho katika maeneo mengi sana.” “Danny!” Mkewe akamwita. “Kweli
Grace. Si Zinda tu aliyeniumiza. Hata wazazi wake. Sikutaka kukwambia, lakini
mama yake alinijia juu vibaya sana. Nilimpigia simu kutaka tu kumsalimia kama
kawaida. Ilikuwa mbaya sana, nilishindwa kuamini kama mwanadamu anaweza
kumbadilikia mtu aliyekuwa naye karibu kwa kiasi kile. Alikuwa mkali. Yule mama
alinitolea maneno mabaya sana. Mbaya zaidi hakutaka kunisikiliza hata kidogo.
Aliamini upande wa Zinda tu. Ilibidi kukata simu kwa sababu ya matusi mabaya
aliyokuwa akinitukana bila kutaka kumaliza.” Wote wakashangazwa. Hawakutegemea kwa
jinsi Danny alivyokuwa amejitoa kwenye hiyo familia.
“Pole
Danny! Kwa nini hukuniambia!?” “Isingesaidia Grace. Nilikuwa nimeumia sana. Au
tuseme wameniumiza. Sitaki kuhesabu, lakini wale watu nilijitoa kwao kama ndugu
wa damu! Lakini wamenigeuka vibaya sana. Wakati mwingine maneno ya yule mama
yanajirudia masikioni mwangu. Hivi unajua alitukana mpaka wazazi wangu?” Grace alishaanza
kulia.
“Aliniambia
nimelaaniwa kwenye huu ulimwengu ndio maana hata Mungu hakuona sababu ya
kuniachia wazazi wangu! Alinitamkia kuwa mimi ni balaa, nina mkosi, sina uwezo
wakutunza familia. Na sitaweza kuishi na familia yeyote ile kwa laana
Mungu aliyonipa. Aliniambia nina roho chafu ya kuharibu mahusiano yeyote yale.”
“Jamani!” Grace alilalamika. “Kweli walisahau kila kitu sababu ya chuki ya Zinda!?” “Hakika walisahau Grace. Yule mama alinitukana
matusi ya nguoni. Tena kwa sauti kali sana kana kwamba nilikuwa adui yake
wakati ndio nilikuwa nimetoka kumtumia pesa! Ilikuwa mbaya sana. Ilinichukua
siku tatu, kufunga na kuomba. Tena mama huyu anajua.” Wote wakamgeukia mama G.
“Nini
sasa? Habari njema ndizo zinasemwa.” Mama G akajibu. “Lakini mama akanishauri
vizuri sana. Akanishauri tufunge. Tulifunga naye siku tatu. Akaniambia tufute
maneno yote aliyosema. Laana zote alizonitamkia mimi na wanangu, pamoja na
wewe. Tukatubu kwa kila baya tulilotenda na kufuta kila neno chafu lililotamkwa
juu yetu. Siku ya mwisho ambayo ni ya tatu ndipo tukatamka uzima na baraka juu
yetu. Tulikutana na mama muda wa mchana. Tukaomba. Mama alinibariki sana mpaka
nikafarijika. Akaniachia neno ambalo nalikumbuka mpaka leo. {Kutoka 14: 13. Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa
Bwana atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo, hamtawaona tena
milele. 14 Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.’} Danny alisema hiyo mistari miwili ya bibilia kwa
kichwa na kuendelea.
“Mama
akaniambia hivi, naweza nisione majibu yale leo wala kesho. Lakini Mungu sio
muongo. Akaniambia ninyamaze kabisa. Nisianze kujitetea kwa lolote. Ilikuwa
ngumu sana. Nilikuwa nimeumia. Zaidi kuona nimesababisha hata kutofungika kwa
ndoa ya Geb na Nanaa. Nikatamani nije nijieleze kwao, mama akasema niache
kwanza. Niwape nafasi. Tukashangaa na mama, Geb na Nanaa wakanitafuta wao
wenyewe wakaomba kuwe na amani. Nanaa akaomba yaishe kabisa.” Danny akaendelea.
“Halafu
Geb naye akaniambia neno jingine kutoka kitabu cha Mhubiri 3: ‘1. Kuna wakati uliowekwa wa kila jambo,Wakati wa kila shughuli chini ya
mbingu: 2 Wakati wa
kuzaliwa na wakati wa kufa; Wakati wa kupanda na wakati wa kung’oa
kilichopandwa; 3 Wakati wa kuua
na wakati wa kuponya; Wakati wa kubomoa na wakati wa kujenga; 4 Wakati wa kulia
na wakati wa kucheka; Wakati wa kuomboleza kwa sauti na wakati wa kucheza
dansi; 5 Wakati wa
kutupa mawe na wakati wa kukusanya mawe; Wakati wa kukumbatia na wakati wa
kuacha kukumbatia; 6 Wakati wa
kutafuta na wakati wa kuacha kutafuta kilichopotea; Wakati wa kuhifadhi na
wakati wa kutupa; 7 Wakati wa kurarua na wakati wa kushona,Wakati wa kunyamaza na wakati wa
kuongea; 8Wakati wa kupenda na wakati wa
kuchukia;Wakati wa vita na wakati wa amani.’ Akaniambia
na yeye ndio ametoka kufundishwa na Mungu.” Danny akatingisha kichwa.
“Wao
hawakujua tu. Lakini ndio ikawa kama Mungu ameanza kunijibu. Nikapata amani ya
ajabu. Nikampigia mama simu nikamueleza kila kitu juu ya ujio wa Geb na Nanaa.
Tena Geb aliniomba kwa chakula cha mchana nikiwa kazini. Nikatoka, nikakutana
nao kwenye hiyo hoteli. Ndio tukafanya hayo mazungumzo. Nakumbuka kushindwa
hata kuongea au kuwajibu kitu. Nilibaki kimya kama kitu kimenikaba kooni.
Nilipotoka tu hapo nikampigia mama simu nikiwa njiani narudi kazini. Machozi
yalikuwa yakinitoka kama mtoto mdogo. Sikutegemea kuitwa na kupewa msamaha
wangu. Basi, mama akarudia kunisomea tena ile mistari aliyonipa Geb huku
akiielezea taratibu mpaka nikatulia nikaweza kuingia ofisini na kufanya kazi.”
Danny akatabasamu kidogo.
“Ndio
nikashangaa na Nanaa naye hataki kubanduka kwetu! Akazidi kunizoea. Anaongea na
mimi kana kwamba hakuna kilichotokea. James naye akawa ndio yupo karibu na mimi
zaidi ya zamani! Mungu akanirejeshea amani. Lakini nilijiuliza kwa kukumbuka
maneno ya mama yake Zinda. Ni kwa nini yule mama alipandisha hasira kwa gafla
tena kwa maneno tu ya kupewa kama kweli alikuwa akinihesabu mimi kama mwanae?
Ipo jinsi mzazi anakasirika mtoto anapokosea. Anajawa na hasira. Lakini hasira
yake inakuwa imebeba upendo ambao sikuuona kwa yule mama hata kidogo!
Alinilaani na kunilaumu sana hata kwa maendeleo ya Zinda! Huwezi amini yule
mama aliniambia nafurahia vile Zinda anavyolipwa mshahara mdogo zaidi yangu.”
“Danny!” Grace akashangaa sana kama wengine.
“Kweli
G. Nikashangaa hata mambo ya mshahara yanaingiaje hapo! Akasema namnyonya Zinda
kwa pesa ndogo alizo nazo mpaka nimeweza kujenga jumba la kifahari.” “Danny!”
Grace akazidi kushangaa. “Na yule mama hajawahi kufika nyumbani kwetu wala
sikuwahi kumtajia mshahara wangu! Hapo ndipo nilipojua yule mama na Zinda
wamebeba wivu mkubwa ndani yao. Hata kicheko walichokuwa wakinipa kilikuwa
hakijajaa upendo. Ilikuwa hila. Yule mama aliniuliza iweje mimi nikue pamoja na
Zinda. Nisome darasa moja na yeye, halafu mtoto wake aishie kuwa chini yangu?
Eti namloga Zinda, nachukua bahati zake. Namfunga ili asioe ili asijekuwa na
familia kama mimi!” “Jamani!” Grace aliendelea kulalamika.
“Ndio
hivyo. Sikutaka kukwambia maana mama alisema ninyamaze kabisa. Nisubirie kuona
kile Mungu atafanya katika hilo. Najua tutasameheana na Zinda. Lakini haitakuwa
kama zamani Grace. Nimejifunza. Na nimejua sina jinsi yakubadilisha kile wazazi
wake wanachofikiria juu yangu mpaka waridhike na maendeleo ya mtoto wao. Au
wajue Zinda amenipita kwenye maeneo wanayoyataka wao. Nilifanya kwa sehemu
yangu kwenye ile familia. Lakini wale wazazi walinitamkia wazi, hawataki
kuniona tena, na wala hawataki ukaribu wangu na Zinda. Tena waliniambia siku
nitayorudi kuwa karibu na Zinda, ndio mwisho wangu. Wakaniambia nimeiba bahati
za Zinda vya kutosha. Sasa nikae nae mbali.” Grace alizidi kuumia.
Kila
mtu alikuwa kimya akiwaza lake huku wakimsikiliza Danny. “Zinda nitamtafuta.
Lakini haitakuwa sasa. Kama wazazi wake watakuja kunitafuta, nitawasikiliza.
Nitawaomba msamaha kwa lolote nililotenda, basi. Sitarudisha mahusiano kama
zamani. Sitarudi tena Tabora kwenda kuwatembelea. Wakinihitaji kwa
msaada, nitafanya kwa nafasi yangu, lakini sio kama zamani. Nimeshawafuta
katika undugu ule wa zamani. Watakuwa ni watu kama watu wengine tu kwenye
familia yangu. Mungu aliruhusu mimi kuwa yatima. Akanipa nyinyi, basi ndio
ndugu wa pekee watoto wangu watawafahamu. Na wao Mungu awasaidie washikamane,
wajenge ukoo wao. Nimemaliza. Sitaki tena undugu na wao.” Danny akamaliza. Wote
wakanyamaza.
~~~~~~~~~~~~~~~
Nanaa
akasimama na kwenda kuandaa chakula. Ilipofika saa moja na nusu usiku akawa
ameshapanga vyakula mezani mpaka cha Geb. “Muone anavyorembua macho!” Nanaa
akatoka akamkuta Oliva ameshaenda kwa baba yake. Amebebwa. “Hapo tukichelewa
kidogo tu, atalala huyo. Nipe nimlishe haraka, akaoge, alale. Naona siku yake
ishaisha.” Mama G akasimama. Oliva alivyoona anamsogelea akaanza kucheka na
mikono yake juu. “Muone!” Bibi yake akainama. Akambusu na kumbeba. “Mchana
umekula ugali, sasa hivi unakula kitu laini. Au unasemaje?” Mama G akamuuliza
mjukuu wake huku akielekea kumfunga kwenye kiti chake ili ale. Mtoto huyo
hakuwahi kubahatika kuongeleshwa kitoto. Kila aliyekuwa naye karibu
alimuongelesha kama mtu mzima mwenye uelewa. Tokea yupo tumboni mama yake
alikuwa akizungumza naye kama mtu mzima.
“Na
mimi naenda kuoga nitoe harufu ya vyakula mwilini.” Nanaa akaaga. “Ngoja
nikusindikize.” Geb akasimama. “Jamani, sisi njaa zinauma. Naombeni mrudi.” Geb
akaanza kucheka. Kila mtu akacheka. “Mama!” “Mama nini? Kwani mimi siwajui?
Mkichelewa tu sisi tunaanza kula. Hatuwasubiri.” “Hatuchelewi mama. Si kuoga
tu?” Nanaa akaongeza huku akimalizia kupandisha ngazi.“Mhhhhh!” Mama G akaguna
nakufanya kila mtu acheke zaidi. Nanaa alipoingia tu chumbani, Geb akiwa
anataka kumalizia kupandisha ngazi, simu ya Geb ikaanza kuita mfukoni.
~~~~~~~~~~~~~~~
Akaitoa
na kuingalia. Akapokea bila kuchelewa. “Vipi James?”
“Safi tu. Upo sehemu tunaweza kuzungumza?” Geb
akaangalia mlango wa chumbani kwao alipoelekea Nanaa. Akajiridhisha kuwa
umefungwa. Akashuka chini na kurudi kukaa. Kina Danny wakamgeukia. “Kwema?” Geb akauliza. “Kwema. Lakini
kuna jambo Zinda anaomba kuzungumza na Nanaa. Ameomba nimlete yeye na kina
mama.” “Nisingependa kesi, James.” Geb
akatahadharisha.
“Nimezungumza
nao sana. Hasa mama. Wameahidi hapatakuwa na kesi.” Geb akabaki kimya akifikiria. “Nashauri kuwakaribisha tu Geb, ili mambo yaishe.” James
akasisitiza. “Haya mambo yangeweza kuisha
tokea muda mrefu kama ningetaka, James. Lakini sikutaka kutumia njia ambazo
nilijua Nanaa ndio angeishia kuathirika. Sitaki fujo zitakazomtibua sasa hivi.
Ametulia na akili yake ipo hapa nyumbani kwa familia yake. Sitaki kesi za
kumnyima raha ili Zinda na wengineo wajisafishe dhamira zao.” “Mimi nitakuwepo
Geb. Zikianza fujo tu, nitawafukuza.”
James akasisitiza.
“Sawa kama
unaniahidi hivyo. Lakini nataka uwaambie wote utakao kuja nao hapa. Hii ni
nyumba ya Nanaa. Kwa kuwa wanamfuata wao wenyewe, tafadhali naomba heshima
iwepo. Maneno ya kejeli na dharau, sitayaruhusu James. Naomba unielewe.”
“Sawa.” James akakubali bila shida. “Kuna nyongeza.” Geb alimuwahi kabla hajakata
simu. “Nipo.” James akaitika. “Ni gari yako tu ndio itaruhusiwa kupita getini. Mwambie Zinda aache
gari yake nje, mlinzi ataingalia. Hawaruhusiwi kupita getini na pochi hata
wallet.
Atakayekubali
kukaguliwa hapo getini, ndiye atakayepita.” Kila mtu akashangaa. “Hawataruhusiwa kuingia wakiwa na kitu chochote mkononi wala kwenye
mifuko ya nguo. Hata funguo za gari waambie waache getini kwa mlinzi. Simu za
mkononi hazitaruhusiwa humu ndani. Msisitizie hilo Zinda. Na wasije wakiwa
wamejifunika khanga wala mitandio. Atakayeona anaweza hayo masharti,
anakaribishwa.” Mpaka mama G akabaki ametoa macho. “Kwa heri James. Kama mtakuwa na mpango wa kuja, tafadhali msikawie.
Tutawahi kulala kwa ajili ya ibada kesho.” Geb
akamaliza. “Sawa.” James akajibu. Geb akakata simu. Hapo hapo akapiga
simu getini na kuanza kutoa maelezo juu ya ugeni wa kina Zinda na nini mlinzi
afanye. Aliporidhika kuwa walinzi hao wawili wameelewa, akakata simu.
~~~~~~~~~~~~~~~
Grace akaanza kucheka. “Nini?” Geb akamuuliza. “Ujue wewe Geb ni mkorofi sana?” “Huwezi jua Grace! Wakiingia na silaha? Tukadhani wanakuja kuleta amani, wakaishia hata kudhuriana wao kwa wao humu ndani?” “Na kweli. Maana wananonekana ni wazungumzaji sana!” Grace akamkubalia kaka yake. “Na wazungushaji wa maneno pia. Mmoja anaweza akaongea jambo, wakaanza fujo hapa.” Danny akaongeza. “Hakika hawatakaa. Nikisikia mtu anamsema vibaya Nanaa, nitamtoa nje. Wakianza kugombana, nje! Sitaki fujo humu ndani.” Mama G akaanza kucheka. “Naona Mzee Magesa amerudi. Hataki utani mwanangu.” Mama yake akaongeza, kila mtu akacheka mpaka Geb mwenyewe.
“Sasa
hapa ndio mje kula. Wakija hapa, hamtaweza kula tena.” Mama G akaongeza. “Ngoja
nikamwite Nanaa.” Geb akanyanyuka. “Sasa huyo ukimwambia kuwa wanakuja, anaweza
asile. Mwache kwanza ale ndio umwambie.” Mama G akamuwahi Geb wakati
anapandisha ngazi kuelekea chumbani kwao alipokuwa ametangulia Nanaa. “Ni
kweli.” Geb akaitikia, akaingia chumbani kwao.
~~~~~~~~~~~~~~~
Kama
baada ya dakika 45 hivi, ndipo Geb na Nanaa wakashuka chini kuungana nao. “Liv
yuko wapi?” Geb akauliza. “Mmmhhh!” Mama G akaguna kila mtu akaanza kucheka.
Nanaa akavuta kiti akakaa huku anacheka. “Mbona sasa hamjala?” Nanaa akauliza.
“Tunakula vipi wenye nyumba hampo?” Grace akajibu. “Bwana mngekula tu.”
“Tulikuwa tunawasubiria.” Grace akajibu. “Na tukasema kama mnajificha ili
tuondoke bila kula, imekula kwenu. Tuliamua kusubiri mpaka hata asubuhi.” Danny
akaongeza huku akianza kupakuwa.
Vikaanza
vicheko huku wakila. Gafla wakasikia geti linafunguliwa. “Kaka huyo!” Nanaa akasimama kwa haraka. “Si
umsubiri hapa? Anakuja ndani Nanaa!” Nanaa akacheka. “Bwana mimi nishazoea
kumpokea. Acha tu niende Geb.” Nanaa akabaki akitizamana na Geb. “Geb!” Akamuita
kama anayemuomba ruhusa. “Nenda tu.” Mara wakasikia kengele ya mlangoni.
“Karibu.” Nanaa akakimbilia mlangoni. Akafungua mlango.
“Karibu
kaka!” “Naona unazidi kuwa mkubwa!” “Ninavyokula!
Kama mchimba migodi! Shikamoo kaka.” Nanaa akasalimia. “Marahaba. Mzima lakini?”
“Mzima. Wote hatujambo. Karibu ndani.” Akaingia. James akakuta watu wote ametulia mezani. “Shikamoo mama.”
“Marahaba James mwanangu. Sogea mpaka mezani.” “Na njaa inauma kweli! Wamenipigia
simu nikiwa nimepitiwa na usingizi niliamua kulala bila kula. Hekaheka tu.”
“Heka heka gani tena?” Nanaa akauliza, James akashituka kidogo akakuta Geb
akimwangalia. Nanaa akaingiwa na wasiwasi akajua kuna jambo anataka kufichwa
tena.
“Kaka!
Kuna nini tena!?” “Naona ni kama wanajirudi. Wanataka kuweka mambo sawa.” Nanaa
akanyamaza. “Njoo umalizie chakula, Nanaa.” Geb akamuita. Nanaa akarudi kukaa.
“Kaa kaka ule.” James akasogea mezani. “Ngoja nile haraka haraka kabla hawajaja.
Mrembo wa Danny upo?” Grace akacheka. “Nipo James. Mzima?” “Njaa! Mmemchukua
Nanaa, basi mimi nakufa na njaa!” Wakacheka. “Na hicho chakula pia kapika
yeye.” “Najua mambo yake.” Nanaa akamsogezea sahani kaka yake.
“Naona
bado unakaba tu. Hutaki kuongea!” James akamchokoza Danny wakati anakula. Na
kweli alikuwa akila kwa haraka. “Wewe si unaona? Siku zikizidi kwenda ndio na
mwenyewe anavyozidi kuvutia.” “Na mimi nitaoa jamani!” “Afadhali James
mwanangu.” Mama G akadakia. “Utapumzika sana. Ndoa ina baraka zake na utulivu.”
“Upate wa kukutuliza mama yangu. Unaweza juta!” James akajibu nakufanya wacheke
kidogo. “Mungu atakusaidia tu. Nakuombea mwanangu.” “Amina mama.” James akajibu
huku akila.
Hakuna Ajuae Kesho Ya Mtu.
Mara
wakaanza kusikia kelele kwa mbali getini. Geb akamtizama James. James akaelewa,
akasimama na kutoka. Nanaa alikuwa amebaki kimya kabisa. Baada ya dakika chache
wakamsikia James. “Mama, Viola na Vai, kama nilivyowaambia, hapa ni nyumbani
kwa Nanaa. Mumewe amesisitiza heshima kwa Nanaa. Tafadhalini sana angalieni
kila neno litakalotoka mdomoni kwenu. Naheshimiana nao sana. Mama yake Nanaa pia yupo humo
ndani.” “Mama yake Nanaa yupi, wakati mama yake ndio huyu? Au kwa kuwa amepata
pesa ndio anamkana mama?” Viola alisikika.
“Nyinyi
si mlimuuza Nanaa kwa milioni 50? Sasa mwanamke aliyeona thamani ya Nanaa, na
kumnunua ndio huyo yupo ndani. Alikuja mpaka Moshi kumlipia Nanaa mahari baada
ya nyinyi kukimbia hapa Dar. Mama anafahamiana naye zaidi maana ndiye aliyekuwa
naye kanisani kumlipa mama pesa alizozidi kudai mpaka kusimamisha harusi
yao. Anaishi na Nanaa kama mtoto aliyemzaa! Tafadhalini sana, heshima iwepo.”
Kimya.
“Tumeelewana
Zinda?” “Sawa. Mimi nimeelewa. Sitaki ugomvi. Nimekuja kurekebisha.” Zinda
akasikika akiongea kwa utulivu. “Mama?” James akasikika akimuuliza mama yake
kuhakikisha ameelewa. “Mama nini?” Mama yake akasikika akiuliza kishari.
“Nataka kujua kama umenielewa mama yangu. Kama unaona hutaweza kunyamaza au
kuzungumza kwa heri ni bora tuondoke. Maana mmenipigia simu nyinyi wenyewe!
Mimi sikuwa na nia ya kuja huku na kuvunja amani kwenye nyumba ya watu.”
“Nisikilize James. Hata mimi sikuwa na nia ya kuja huku. Nilishamalizana na
huyo mtoto. Unafikiri mimi ndio nafurahia udhalilishwaji huu wakupekuliwa
getini kama mwizi!?” “Basi naomba mgeuze hapahapa muondoke. Sitaki muingie
ndani.” James akawabadilikia.
“Hapana
kaka James. Naomba hili jambo na mimi unikamilishie kama unavyomsaidia Nanaa.
Limeshika hatima ya maisha yangu. Nataka niondokane na hawa watu, kaka.
Nimechoshwa na maisha yao. Na wewe mama, tafadhali sana. Nilikwambia nini juu
ya kunyamaza? Unataka kuniharibia maisha yangu? Mambo uliyaharibu wewe mwenyewe
na Viola, leo nataka mnitengenezee niendelee na maisha yangu niachane na nyinyi
kabisa.” “Unikome Vai.” “Nini Viola? Sio wewe uliokuwa ukileta maneno ya uongo
na ya uchonganishi kwa mama juu ya Nanaa tokea mpo wadogo? Mlimjaza Zinda
maneno ya uongo juu ya Nanaa. Leo unaruka nini?” Watu wote wa ndani waliendelea
kuwasikiliza.
“Muongo
tu Vai! Na wewe pia ulikuwa ukimpa maneno ya uongo mama na baba? Unakumbuka
ulivyokula ada yako ya shule halafu ukamwambia baba ni Nanaa ameiba! Baba
akamfuata mpaka shuleni kwao Ashira akaenda kumchapa mstarini mbele ya
wanafunzi wote? Sio wewe?” Viola naye akamjia juu mdogo wake.
“Ni wewe na mama ndio mlikuwa
wabaya zaidi kwa Nanaa kuliko mimi. Msijidai watakatifu hapa mbele ya kaka
James. Tena kaka, hawa wawili walishampigaga Nanaa mpaka karibia ya kumuua.
Mara ya kwanza Viola alimsingizia amemuibia. Mama akampiga Nanaa huku
wakimchangia na Viola. Ndio mama akambabiza uso kwenye mlango wa jikoni madamu
yakaanza kuvuja. Alimpasua mdomo. Hapo hapo na wewe ukapiga simu ukasema
unakuja kesho yake. Mama akamsafirisha Nanaa na Viola kwenda kwa bibi ili usije
muona Nanaa vile alivyopasuka. Tena alikwenda bila hata kupelekwa hospitalini!
Ulipokuja ukamuulizia Nanaa, mama akakudanganya kuwa Nanaa mzima, ameenda
kusalimia kijijini kwa bibi.” Vai aliendelea kusemelea.
“Halafu
mara nyingine tena wakampiga hivyo hivyo kwa kumchangia mpaka akazimia. Halafu
wakamtupa pale nje upande wa banda la ng’ombe, tena alikuwa anavuja damu za
pua. Wakamuacha hapo mpaka yule kaka anayeleta majani akaja ndani, akamwambia
mama kuwa Nanaa yupo pale nje anaonekana ameumia vibaya. Anatoka damu za pua na
masikioni. Wakamwangalie labda wamuwahishe hospitalini. Mama akamtuma ili
amshike kama ashakuwa wa baridi. Yule kaka akarudi akamwambia bado wa moto, wamuwahishe
hospitalini. Mama akasema amwache afe. Nanaa ni mwizi na Malaya. Walimuacha
hapo mpaka usiku. Tena tulienda kulala, mama akasema afungiwe nje. Akalala hapo
hapo mpaka asubuhi akaamka mwenyewe na kurudi ndani. Halafu..” “Naomba nyamaza
Vai. Nyamaza. Tu.” Walimsikia James akimnyamazisha kwa uchungu sana.
“Ndio
uwajue ubaya wao hawa kaka!” “Wewe kama ni mwema, kwa nini hukuwa ukiniambia?”
“Niliogopa kaka. Nilikuwa namsikia mama akimwambia Nanaa asithubutu kukwambia.
Lasivyo atampasua kichwa.” “Muongo kaka! Muongo mkubwa huyo. Tena yeye ndio
alikuwa mbaya zaidi. Alikuwa akimsemelea na kwa baba pia, ili apigwe zaidi.
Acha unafiki Vai! Anajidai sasahivi kwa kuwa wewe upo, na anataka azidi
kumdanganya Zinda ili amuoe.”
“Namdanganya kwa lipi Zinda?” Vai akauliza.
“Wote
tunajua hujui kupika wala kufanya usafi. Unamlipa jirani yako akupikie na
kukufanyia usafi ili Zinda akitoka kazini akute chakula kipo tayari afikiri ni
wewe umepika. Bisha kama hiyo sio tabia yako kwa wanaume wote?” “Wivu tu kwa
kuwa unajua umezalishwa huwezi kuolewa tena.” “Bora mimi nimezaa kuliko wewe
ambaye hutawahi kuja kushika mtoto maishani. Mimi nimefanya yangu nimepata
mtoto, wewe umefanya umalaya na kizazi wamekitoa tena kikiwa kimeoza!
Haya sema jingine.” Hapo Viola akawa amemmaliza mdogo wake kabisa. Alinywea Vai
kama aliyemwagiwa maji.
“Mbona
kimya? Wewe si jeuri huna shukurani! Hututaki mimi na mama wakati sisi
tulikusaidia ulipokuwa umeoza? Wewe si jeuri? Sema sasa.” “Wala sikuwa nimeoza!”
Wakaendelea kubishana. “Haya, Zinda chukua timu yako mkasutane kwenu. Sio hapa.
Niliwaambia mumewe Nanaa, hataki fujo na nyinyi. Tokeni.” James akaanza
kusukuma wadogo zake akiwatoa nje. Mlinzi akasogea “Hamruhusiwi kufanya fujo za
aina yeyote hapo. Naombeni mtoke tafadhali.” Mlinzi akaongeza msisitizo.
“Tafadhali
James. Mimi nilazima nionane na Nanaa. Na Nanaa amesema hawezi kuzungumza na
mimi kama wewe haupo.” “Si kwa staili hii Zinda. Mmeshamuumiza Nanaa
vyakutosha. Siwezi kuruhusu muendelee kumnyanyasa mpaka sasa hivi. Tena
nyumbani kwake! Hapana Zinda. Akapumzikie wapi!?” “Mimi nimenyamaza James.” “Hii
timu yako uliokuja nayo haijanyamaza. Nafikiri wanahitaji muda na sehemu nzuri
itakayowafaa kusutana. Sio hapa na si mbele yangu. Wananiumiza nafsi yangu tu.
Hapana. Tokeni.” “Nipe muda na Vai. Vai hebu njoo.” Zinda akasogea na Vai
pembeni.
Walizungumza
kwa kunong’ona kwa muda, Vai akarudi akiwa ametulia kimya. “Sisi tupo tayari.”
“Mna uhakika?” James akauliza huku akiwatizama kila mmoja wao. “Mimi nitatulia
kama na yeye atatulia. Asijidai mtakatifu hapa sababu anajua Zinda yupo hapa.
Anataka amtapeli ili amuoe. Akinisingizia na mimi nitatoa siri zake.” Viola
aliongea kwa kujiamini.
“Mama!
Nashauri uondoke na wanao. Sina muda wa kupoteza.” “Hee! Mimi!?” Mama yake
akashangaa sana. “Kama yamewashinda waliyoniitia, mimi naondoka narudi zangu
kazini kwenye baa yangu. Wamenitoa huko mbio mbio nimeacha wateja wangu
wakitaka niwasaidie. Leo jumamosi, siku yangu ya kuvuna pesa. Kama
wameshindwa hapa, mimi naondoka sasa hivi. Sitaki waje wanilaumu baadaye.”
“Mama naomba usiondoke. Mimi ndio nimekuita. Viola anafanya makusudi ili
aniharibie kama Nanaa. Mimi..” Wakasikia kibao cha nguvu. James alimpiga Vai
kibao cha uso. “Nimekwambia acha kumtaja Nanaa.” Wote walishituka.
James
hakuwahi kuwapiga dada zake. Akamgeukia na Viola na yeye akampiga kofi la uso
la haraka haraka bila kujua. “Nyinyi ni watu wa namna gani!? Kwa nini nawaambia
jambo moja hamnielewi? Masikio yenu yako wapi? Miguuni!? Hamjui kumsikiliza mtu
na kutii!? Ala!” Wote walikuwa wameshika mashavu yao.Vai alianza kulia.
“Sasa
nauliza kwa mara ya mwisho. Mnaondoka au mnabaki? Kama hamna shuguli za
kufanya, mimi nina shuguli zangu. Mlinipigia simu nyinyi wenyewe, tena Vai
ukiwa unalia na kunisihi nikulete hapa kwa Nanaa. Sasa hivi mnanifanyia michezo
ya kitoto! Sina muda wakupoteza wa kusikiliza uchafu wenu. Umenisikia Vai na
Viola?” Walishangaa mama yao amenyamaza kimya. “Mimi natulia kaka. Naomba twende.” Vai
alisisitiza. “Na wewe Viola? Kwanza hebu jiangalie jinsi ulivyo mchafu!” “Si
nilikuwa napika ndio mama akaniambia niache kila kitu, nije?” James alimtizama
kwa hasira. “Sasa nisikie mtu anaongea hovyo huko ndani. Nitatoa huu mkanda
kinoni, niwatandike wote.” Kimya.
Baada
ya muda mfupi wakasikia kengele. Geb akasimama. Akaenda kufungua mlango.
“Karibuni.” “Asante.” James akashukuru akapita. Zinda alishangaa kumkuta Danny
amekaa kwenye makochi ametulia kimya na mkewe. Mama G naye alikuwa amekaa kimya
akiwatizama. Geb akawaonyeshea sehemu ya kukaa. Wote wakabaki kama wanashangaa
mle ndani. Walibaki wamekodoa macho huku wakizungusha vichwa. Wakishangaa kwa
wazi kabisa, mpaka wenyeji wao wakajua.
Mbio Za Sakafuni.
Nanaa
hakuwa hata ameongea neno wala kusalimia. Pakazuka ukimya kidogo. Geb
alisharudi kukaa pembeni ya Nanaa ameweka mkono wake juu ya mapaja yake. Nanaa
akamshika kiganja, akamvuta kidogo kama kumuita. Geb akamgeukia kwa kuinama.
“Naomba mimi nikapumzike.” Nanaa alimnong’oneza. “Sawa.” Bila kubisha, Geb
akakubali. Nanaa akampa tabasamu la kumshukuru. “Nakushukuru.” Akanong’ona. Geb
akanyanyua ule mkono uliomshika, akaubusu.
“Kaka!”
Nanaa akaita. “Vipi?” James akaitika. “Naomba mimi nikajipumzishe, kaka yangu.
Nikuachie masikio yangu haya na mdomo wangu.” Akimuonyeshea Geb, waliyekuwa
wameshikana mkono. Wote wakabaki kimya wakishangaa. Nanaa akataka kusimama.
“Nataka kuzungumza na wewe Nanaa.” Zinda akamuwahi. “Hunifahamu, sikufahamu
Zinda. Nimekufahamu kupitia kaka James, Danny na Geb. Sina kitu chakuzungumza
na wewe tena. Mara ya mwisho kuzungumza na wewe ilikuwa Marangu. Ukaniambia
umenielewa. Tukaagana kwa amani. Siku nakurudishia koti lako uliloniazima,
ulikuwa ndani ya gari yako na mimi namuwahi kaka. Nikakupa koti lako.
Nikakushukuru, tukaachana kwa amani kabisa. Sina kitu cha kuzungumza na wewe.
Na kama kipo, basi narudia tena. Naacha masikio yangu na mdomo wangu
hapa. Akisikia Geb, ndio ujue na mimi nimesikia. Jibu lolote ambalo ningetoa
mimi, ujue lingekuwa limetoka kwa Geb. Siwezi kuongea kinyume naye.” Nanaa
akaendelea.
“Sasa
nakupunguzia safari. Ongea na Geb moja kwa moja. Maana kama asingekuwepo hapa,
ningekwambia subiri mpaka nizungumze na Geb, sasa kwa kuwa mwenyewe yupo hapa,
naomba nikuachie yeye anayekufahamu, uzungumze naye.” Nanaa akataka kusimama.
Geb akasimama kwa haraka, akanyoosha mkono. Nanaa akaupokea, Geb akamvuta
kumsaidia kusimama. “Nakuja sasa hivi. Sitachelewa.” Geb aliongea kwa sauti ya
chini wakati anaweka sawa gauni hilo la Nanaa na kumtupia begani kitenge chake
anachojifunika akiwa analala hapo sebuleni. “Asante.” Nanaa akashukuru.
Wakati
anataka kuondoka, Geb akiwa amerudi kukaa, Vai akamuwahi wakati anataka kupanda
ngazi. “Ungetusikiliza kwanza Nanaa!” Nanaa akageuka. “Nimewasikiliza tokea
nazaliwa mpaka sasa hivi nakusikiliza. Nimechoka nafsi na roho yangu. Mungu
amenipa mtu wa kunipokea. Huyo hapo Geb. Nimewaachia. Atawasikiliza mpaka
mtachoka nyinyi wenyewe kuongea. Na mimi ni zamu yangu ya kupumzika.” “Ni mambo
mema Nanaa, sio ubaya!” Vai aliendelea kusisitiza. “Mbona kama huelewi wakati
naongea Kiswahili!?” Nanaa aliongea kwa ukali kidogo huku amekunja uso.
“Nikutaka
tuwekane sawa tu. Hatutakuchelewesha.” Vai akaendelea. “Nanaa! Nanaa!” Mama G
akaita. “Abeee mama!” Nanaa akamgeukia mama G. “Nenda kapumzike mwanangu. Usiku
mwema. Tutaonana kesho.” “Kesho tena!? Wakati usiku mimi mgeni wako?” “Hapana
Nanaa. Wewe tulia chumbani kwako. Sitaki ugeni wa usiku.” “Nikisikia njaa je!?”
“Geb atakupandishia vitu vyako vyote vya
kula.” Nanaa akacheka.
“Bwana
mimi sitaki!” “Hapana Nana. Usiku nisikuone chumbani kwangu.” Nanaa akazidi
kucheka. “Bwana mimi nishakuzoea!” “Hata! Unanidanganya tu. Wewe umalize
usingizi wako wote mchana, halafu eti usiku ndio uje ukeshe na mimi kwa stori
zisizo isha! Leo utaletewa haja zako zote huko huko juu chumbani kwako. Sababu
za kuamshana zikuishe.” “Nikisikia kiu je?” “Nakwambia na maji yatakufuata huko
huko chumbani kwako.” Nanaa akazidi kucheka huku akipandisha ngazi. “Lazima
utasahau tu kitu. Nitakifuata mwenyewe usiku, kwenye saa 8 hivi!” “Nazijua kiu
zako na njaa zako zote. Utakutana na kila kitu pembeni ya kitanda chako kama si
kwenye friji yenu hukohuko juu ukose sababu ya kushuka.” Nanaa alizidi kucheka.
“Sawa
bwana mama! Na sio kesho utake stori zangu.” “Stori gani za usiku bwana?” “Usije
sema unapitwa tu!” “Unanidanganya tu, huna lolote. Wewe tulia kitandani kwako
mpaka asubuhi.” Wakamsikia akicheka,
akafunga mlango. Pakazuka ukimya.
Zinda!
“Nilikwambia
tumepewa muda mfupi sana Zinda. Na umeona nusu yake ni kama tumeshamaliza pale
nje. Kwa hiyo kama kuna la kuzungumza, uliongee sasa hivi.” James akavunja
ukimya. Zinda akabaki kimya. “Labda hakutegemea kukuta watu wote hawa.” Vai
akadakia. “Ukinyanyua tena mdomo wako Vai bila ruhusa yangu, utatoka hapa
unalia. Nyamaza. Hujui ni nini unaongea. Hakuna mtu mgeni hapa kwa Zinda. Na
hawa unaowaona hapa ni kama kitu kimoja. Hawajawahi kutengana. Na Nanaa ametoka
kukwambia sasa hivi. Naona huelewi. Sasa nakutahadharisha kwa mara ya mwisho,
nyamaza.” Vai akainama.
“Zinda?”
James akamwita kwa ukali kidogo. “Nafikiria pakuanzia.” Zinda akajibu. “Basi
naomba tuondoke hapa, tuwapishe wenyewe wapumzike. Wewe nenda kafikirie vizuri.
Ukiwa tayari utatujulisha.” James akasimama. “Usiondoke kwanza James. Unajua
tulipotoka. Tumetoka mbali sana. Imetokea mwenzenu nimeteleza. Naomba
msinitupe. Kuteleza sio kuanguka. Na mimi ni binadamu Yapo..” “Samahani Zinda.
Binafsi sina muda wa nahau na mithali. Nenda kwenye kilichokuleta.” James
akamkatiza.
“Naombeni
msamaha.” Zinda akaongeza. “Danny! Naomba..”
“Tafadhali. Niache kabisa. Usiniingize huko. Wewe zungumza kilichokuleta hapa
nyumbani kwa Nanaa na Geb. Kwangu unapafahamu. Tumekutana hapa kwa bahati mbaya
tu. Usipotezee watu muda.” Danny aliongea bila utani. “Basi nitakufuata
nyumbani.” “Tafadhali usifike nyumbani kwangu. Nitakutafuta kwa wakati wangu.
Sio sasa.” “Sawa Mkubwa. Nakuelewa kabisa. Najua nilifika mbali. Ila kama
utapunguza hasira, utagundua nimejirudi Danny. Sisi ni ndugu.” “Nisikilize
Zinda. Sidhani kama ulinitoa kwangu kuja hapa kwa ajili ya Danny. Nipo hapa kwa
sababu ya Nanaa, basi. Usipoteze muda. Naomba tufanye kilichotuleta hapa
tuondoke.” James akasisitiza.
“Sawa.
Nilitaka kumuomba Nanaa msamaha. Sasa naona ameondoka, sijui inakuaje?” Akamgeukia
James. “Acha masihara Zinda! Yaani umekuja hapa kuomba msamaha kwa Nanaa tu?
Ulimuona vile huyu mama alivyokuwa akihangaika na Nanaa! Najua ulisikia jinsi
alivyohangaika naye kuanzia swala la mahari mpaka kumnunua Nanaa kwa mapesa
mengi na pesa nyingine nasikia ni wewe ulitoa wazo la kumdai Geb zaidi. Najua
ulijua kama vilianza mpaka vikao vya harusi hapa. Na Danny akiwa mwenyekiti wa
kikao. Harusi mliisimamisha kanisani wewe na mama yangu. Achilia mbali historia
ya Nanaa uliyokuwa ukiijua waziwazi tokea mtoto mdogo mpaka siku unamkatili.
Ulijua kabisa jinsi nilivyohangaika naye.” James akaendelea.
“Ulijua
Nanaa ni yatima. Ulijua fika anahitaji familia kama hii iliyokuwa imempokea kwa
mikono yote miwili! Tena ukifahamu hisia za Geb kwa Nanaa, kabla hata
hawajafahamiana, ukaamua kuharibu vibaya sana. Mimi na Danny tulikufuata ili
kuzungumza na wewe. Unakumbuka fujo ulizofanya pale baa? Ukisema upo hapa mbele
ya Geb na ndugu zake kumuomba msamaha Nanaa. Ambaye humfahamu kama alivyosema
yeye mwenyewe. Utakuwa hujaamua kukiri kosa. Na hapa tunapoteza muda. Na kama
kweli nia yako ni Nanaa tu, basi. Amekuachia Geb huyo hapo. Omba msamaha
tuondoke.” Kimya. James akasimama.
“Subiri
kwanza James. Usiondoke kwanza.” “Mbona huzungumzi kitu cha maana Zinda!? Kwa
nini ulinipigia simu kutaka nikusindikize wewe na kina mama hapa kama
unashindwa kufanya yaliyokuleta? Au nikuulize, kwa nini umekuja na watu
wengine?” “Labda nianzie mbali kidogo.” Zinda akajiweka sawa.
“Zinda!”
Mama G akaita. “Hatuna huo muda hata kidogo. Umenielewa?” Mama G
alishabadilika. “Wewe si familia yangu kama zamani. Nilikupa hiyo nafasi,
umeiharibu vibaya sana. Umetumia upendo wetu kumwangamiza zaidi Nanaa. Najua
unajua ubaya Mira aliokuwa amemtendea Nanaa.” “Ni hasira mama.” “Nitajuaje kama
huu ndio mwisho wa maangamizi yako kwa wanangu? Hasira zikikupanda tena?”
“Nimekoma mama.” “Basi Zinda. Itabidi ujenge tena uaminifu wako kwetu. Kwa
kifupi tu, hakuna neno hata moja utakaloongea wewe na hao uliokuja nao tunalotaka
kulisikia. Wote tumeshawajua nyinyi ni wazungushaji wa maneno. Na sisi hatutaki
watu wa namna hiyo kwenye maisha yetu. Jenga upya uaminifu wako. Uaminifu
hautamkwi. Unajengwa. Na hujengwa kwa vitendo. Si kwa maneno. Ushaharibu mara
ya kwanza, umefuta kila kitu. Anza upya. Lakini ukiwa mbali na sisi.” Mama G
alishakuwa mkali.
“Umenielewa
Zinda?” “Nimeelewa mama. Ila naomba utambue ninajutia. Kina Vai walitumia
hasira zangu kuendelea kumuangamiza Nanaa. Nakuhakikishia mama yangu, ni leo
ndio nimejua ukweli. Sikujua kama ndio ubaya waliokuwa wakimfanyia Nanaa.
Walinipa maneno mabaya sana juu ya Nanaa, ndio maana nikaapa na mimi
kumuangamiza. Na hata Mira aliponitafuta kutaka kumfahamu Nanaa zaidi, nikiwa
nimejawa na hasira na maneno mabaya juu yake, nilishindwa kuchuja maneno ya
kumwambia Mira. Nikakuta natumia maneno yao hawa, kusambaza chuki juu ya
Nanaa.” Zinda aliongea kwa unyenyekevu kama apige magoti.
“Kwanza
Mira yuko wapi? Mbona hamna anayejua alipo, na kazini hafiki tena?” Grace
akauliza. “Leo ndio na mimi nimejua alipo. Mama anasema amerudi nyumbani
anajaribu kuaguliwa.” “Ndio nini?” Grace akauliza. “Kwa jinsi mama
alivyonieleza, anasema kuna mambo yamemrudia. Alifanya uchawi kwa mtu
ukamrudia. Ndio nikamtuma mama jioni hii kwenda kumuangalia. Akarudisha majibu
kuwa Mira ameoza miguu kabisa. Hawezi hata kutoka kitandani.” Mama G na wanae
wakaanza kutizamana.
“Kwa
hiyo umejua mabaya aliyomtendea Nana, yamemrudi Mira ndio maana umekuja kuomba
msamaha?” Kimya. “Kwa hiyo isingekuwa hivyo usingekuja hapa au usingeng’ang’ania
kuwepo hapa?” Mama G aliendelea kuhoji kwa ukali. “Haya, naombeni mtoke humu
ndani.” “Hapana mama yangu. Nimekuja kwa yangu lakini na Mira naye amenituma.
Anaomba yaishe.” “Anataka yaishaje?” Mama G akahoji kwa ukali lakini hapo
ndipo wakajua Zinda ameletwa na mengi.
“Anasema
kama mmemuendea kwa mganga ili hayo mambo yamrudie, anaomba msameheane
yaishe.” Mama G akacheka. “Kamwambie Mira, sisi tunaye Mungu aliye hai. Uchawi
wetu sisi ni jina la Yesu. Basi. Mwambie yeye atubu, amlilie Mungu wake
atamsamehe na kumponya. Ninachokutaka wewe ufanye.” Mama G akawa amebadilika
kama sio yeye. Akaanza kutoa amri sasa.
Ukorofi ukarudi kama kawaida yake.
“Unanisikia Zinda?” “Nakusikiliza mama.” “Kesho, siku ya ibada. Nataka saa moja na nusu asubuhi tukutane pale kanisani, ofisini kwa mchungaji. Nakutaka ukakiri kuwa Nanaa hakuwa mkeo, ulidanganya na ukilete kile cheti cha ndoa, tukichane pale pale ofisini. Ili kesho hiyo hiyo litoke tangazo la kwanza la ndoa ya Nanaa na Geb.” “Sawa mama.” Zinda akakubali kwa haraka mpaka akamshangaza kila mtu.
“Lakini
nilitaka na hawa wamuombe Nanaa msamaha. Kwa jinsi nilivyowasikia na kusimuliwa
na Vai, hawa watu wanatakiwa kutubu mama. Kwa Nanaa mwenyewe tena kwa magoti.”
“Sitawahi kumpigia Nanaa magoti. Ulimwengu mzima ulimkataa, mimi nikamlea! Eti
leo nipige magoti kwake!? Hata mara moja.” Mama yake James kwa mara ya kwanza
akaongea kwa jeuri. “Hata hivyo ni vile humfahamu Nanaa, Zinda. Hana tabia
yakubeba vinyongo. Atakumbuka kama mwanadamu mwingine yeyote ambaye
anakumbukumbu. Lakini anatabia yakusamehe hata kabla hujamuomba msamaha. Huwezi
ukamsikia analalamikia watu walio mkosea. Kwa hiyo hamna haja yakuomba msamaha.
Alishasamehe.” Mama G akajibu na kuendelea.
“Ila
nawasihii acheni kushindana na Nanaa. Mungu atawachapa, mtarudi hapa kwa magoti
au mtashindwa hata kurudi kama Mira. Upo ulinzi wa ajabu sana unao mzunguka
yule mtoto. Kila anayemdhuru Nanaa, ni Mungu mwenyewe ndiye anayeonekana akishuka
na kumponya yule mtoto. Sijui inakuaje lakini tokea nasikiliza mazungumzo yenu.
Yakumpiga na kumuacha nje nusu mfu, anaamka mwenyewe amepona! Sasa ndicho hicho
hicho alichokifanya Mungu, pale Mira alipojaribu kumuweka hospitalini. Hakupewa
hata kidonge kimoja! Malaika wa Mungu akatumwa kumponya Nanaa.”
“Yule
malaika alitumwa kumwambia na mpaka Nanaa
mwenyewe alionyeshwa mtu anayepigana vita yake. Sasa nakutahadharisha Zinda na
wengineo. Msicheze na mkono wa Mungu. Hamtaweza. Haya. Usiku mwema naomba
mtupishe tulale.” Mama G akamgeukia James. “James mwanangu, usiku mwema.
Tutaonana kesho kanisani kwenye tangazo la kwanza ya ndoa ya Nanaa na Geb.”
“Asante mama. Usiku mwema.” James akasimama.
“Sasa
vipi kuhusu mimi wewe Zinda?” Vai akadakia kabla kila mtu hajasimama na kutoka.
“Nahitaji muda Vai. Nimesikia mambo mengi sana juu yako na maisha yenu.
Unabadilika badilika kutokana na mazingira. Kauli zako hazieleweki. Leo
unaongea hiki, kesho kile. Hutaki ndugu zako hata mmoja! Huna unayeweza
kumuongelea vizuri, hata mama yako mzazi! Unatukana kila mtu. Kasoro James tu
ndio nimekuona unamuogopa. Nahitaji muda. Nitakutafuta.” “Jamani Zinda.
Naomba..” “Naombeni isiwe hapa jamani. Tokeni. Kamalizaneni nje ya hii nyumba.
Mimi nataka nikapumzike.” James akamkatisha dada yake. “Tokeni.” James
akasisitiza. Wakasimama na kutoka.
~~~~~~~~~~~~~~~
Wanasema, Msubiri bwana kwa Saburi. Hakuna shujaa wa kusubiri. Wala hakuna mwanadamu shupavu
anayekuwa imara kwenye kusubiri hasa ukiwa
kwenye shida. Lakini wakati mwingine inalazimu.
Katika hilo na la Ugonjwa iliwalazimu Nanaa na Geb kumsubiria Mungu wao
ili awatetee.
Geb angeweza kutafuta njia nyingine za kumshinda Zinda. Na angekuwa na nafasi
ya kushinda tu, lakini si kwa ushindi mkubwa
kama huu. Mungu ameleta adui wa Nanaa mbele yake. Wamepigana vita yeye
akiwatizama na kupokea ushindi.
Jina lake limesafishwa mbele ya kila mtu! Tumaini
jipya.
Hata hili nalo wamelishinda. Limepita wakiwa bado wamesimama pamoja
kama familia.
Je, Zinda hatabadili mawazo? Atatokea kanisani kama alivyomuahidi mama
G? Hasira ya wazazi wake kwa Danny Itaishia wapi?
Usikose muendelezo Mkubwa, wakusisimua na kuumiza mbeleni.
Yapo Mengi Mazito Yanakuja.
Endelea kufuatilia.
0 Comments:
Post a Comment