Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Ni Wangu! – Sehemu Ya 43. - Naomi Simulizi

Ni Wangu! – Sehemu Ya 43.

“Mimi nahisi kuna kinachoendelea kwa yule msichana. Si bure. Naombeni mfikirie.” Grace akaongeza. “Kwa nini leo atoe vitisho badala ya kutekeleza kama mwanzo? Kwani mwanzoni kabla hajamdhuru Nanaa, alimuaga Nanaa? Alimtisha? Si alimdhuru tu?” Grace aliwafanya wafikirie. “Lakini kweli. Lipo jambo tu. Kama kweli yeye ni mtu wa kutekeleza mambo yake, kwa nini asifanye kama alivyofanya mwanzo? Inawezekana amekutana na nguvu za Mungu. Kumbukeni Nanaa alivyosema aliona watu wakipigana. Inawezekana alipigwa vibaya. Uchawi wake haufanyi kazi tena. Sasa hivi ameamua kutuma vitisho tu.” Mama G akaongeza. “Sawa sawa mama. Na mimi nahisi hivyo.” Grace akaongeza. 

“Lakini kama ni vitisho, basi amefika mbali!” James akaongeza. “Mimi najiuliza mwisho wa huyu binti utakuwa ni nini!? Mtu aliyehuru kuingia humu ndani. Mpaka akamfikia Nanaa! Mnafanya naye kazi! Ana uwezo wakuingia mpaka ofisini kwako na kupiga picha zote hizo! Inamaana ni mtu ambaye amefanikiwa kuwa karibu sana na nyinyi! Na amekusudia kumuangamiza kweli Nanaa. Na anaonekana anafanikiwa. Ameanza kwenye miguu. Amekuja kwenye hofu. Nanaa ameshindwa kuvumilia, amekimbia akiwa na mtoto na ni mjamzito. Sijui yuko wapi! Na hata kama atapatikana, hamjui ni nini tena atafanya kumdhuru Nanaa na mtoto! Nashauri mumuache kwanza Nanaa. Mwacheni kabisa. Maana ni kama mtamtafuta halafu mje mumtie tena matatizoni kwa watu wenu au watu wetu tuliokuwa nao kwenye maisha yetu! Wote ni mashahidi hapa. Watu wetu wote wamehusika katika kumuangamiza Nanaa na bado wanamtesa. Si Zinda, si huyo Mira!” James akaongeza hukumu mioyoni mwao. Likifika swala la dada yake, huwa haumi maneno.

Mungu naomba unirehemu. Nisaidie hili alilokusudia kunifanyia shetani lisinipate.” Geb alikuwa ameinama, wakamsikia akiomba. “Siwezi kuishi bila Nanaa na Oliva. Mungu nisaidie. Nitachanganyikiwa. Nisaidie Mungu wangu.” Geb alikuwa amejiinamia akiomba. “Pole Geb!” Grace alimuhurumia kaka yake. “Mungu yupo na wewe. Hata hili atawasaidia tu.” “Nahisi kuishiwa nguvu G. Sijui chakufanya tena! Ni kweli najiona nimemwingiza Nanaa kwenye matatizo.” Tayari shutuma za James zilishamwingia na kumnyima ujasiri.

“Fanya kile ulichokifanya mara ya mwisho ukafanikiwa.” Grace alimshauri mdogo wake. Na ni yeye peke yake hapo ambaye aliweza kuongea na James, kwa kuwa hakuwa mtuhumiwa wa moja kwa moja kwenye swala la Nanaa, japo Mira alimfuata yeye hapo nyumbani. Lakini na yeye linapofika swala la Geb, lazima asimame naye hata kama atamuonya kwa ukali, lakini huwa anasimama naye mpaka amuone ametoka kwenye tatizo. Mama G na Danny walikosa ujasiri kwa kuwa wao ndio walisambaza maneno. Wakaogopa wasije kuchangia hapo, nakuharibu zaidi. Huwa James hakawii kuwabadilikia.

“Eti Geb? Umepitia changamoto nyingi sana na Nanaa. Mlishindaje?” “Niliomba G.” Geb aliongea kwa upole huku akimwangalia dada yake. “Basi omba tena. Wewe umethibitisha nguvu ya maombi. Omba tena. Nanaa na Liv ni zawadi yako kutoka kwa Mungu. Usikubali kushindwa kirahisi hivi. Usikubali kutishwa kwa kelele na uongo wa ibilisi. Usikubali kutoa focus yako au macho yako kwa Mungu.” “Ni kweli. Basi naomba nikaombe.” Geb akasimama na kuelekea chumbani kwake. 

Walikaa hapo zaidi ya lisaa, hakutoka. James akaaga.

“Tunaomba akikutafuta, utujulishe na sisi.” Mama G alimsihi James. James akatulia kama anayefikiria. “Tafadhali James mwanangu.” “Najiuliza ili iweje mama? Mazingira haya sioni kama yapo tayari kumtunza Nanaa na watoto. Tumetibua sana hali ya hewa. Ni kama hakuna tena utulivu au mazingira mazuri kwa Nanaa.” “Hapana James. Na wewe usikubali uongo wa ibilisi. Asikutie hofu. Hakuna vita inayopiganwa na mtu mmoja. Ukidhani unamlinda Nanaa, ujue utamwangamiza zaidi. Mimi nimemuona Nanaa sasa hivi. Nanaa unayemfahamu wewe sio Nanaa huyu anayeishi na Geb sasa hivi.” Grace akaingilia mazungumzo ya James na mama yake. 

Akaendelea. “Hawa watu hakuna jinsi wakatengana sasa hivi eti ukasema maisha yao yatakuwa sawa. Haitakaa ikatokea tena. Si kwa Nanaa si kwa Geb. Nanaa hatakuwa sawa mbali na Geb. Hata kama ataenda kuanza kazi, akalipwa mamilioni ya pesa. Au hata kama Geb atakuwa anamtumia pesa, Nanaa hawezi kuwa na pumziko mbali na Geb. Tafadhali James. Tafadhali sana, naomba hili nalo lisikukasirishe na kukufanya ushindwe kusimama na Geb. Kama tulivyomsikia Geb, alifanya yote haya sababu ya kumlinda Nanaa. Si kumficha Mira kwa Nanaa. Naomba na wewe mlinde Nanaa kwa kumsogeza karibu na Geb mwanaume anayempenda na kumthamini, sio vinginevyo. Hawa watu sasa hivi ni familia. Wana watoto, hakuna jinsi ya kuwatenganisha tena. Nakusihi James usamehe na uwe upande wa kuwajenga. Nanaa anakusikiliza sana wewe. Chochote utakachomwambia wewe, atasikiliza na kukifanya.” Kwa mara ya kwanza Grace akamtolea uvivu James. Aliongea kwa ujasiri bila kuweka kituo na kumtaka James amsikilize. 

Mpaka James mwenyewe akatulia. Grace hakuwa mzungumzaji. Kwa hiyo akiongea ni lazima utamsikiliza tu, kama wewe ni muungwana. “Tafadhali James.” “Sawa.” Wakashangaa James amekubali kirahisi tu, akaondoka. Danny alikuwa kimya kabisa, akiwaza vyake. Alishindwa hata kuongeza neno. Majuto yalikuwa yakimsumbua sana. 

Nanaa Ndani Ya Basi.

Huko kwenye basi majuto yakaanza kumsumbua Nanaa. Akakumbuka vile Geb alivyokuwa akimuhangaikia. Jinsi alivyougua na kuwa naye pale hospitalini. Akakumbuka mapenzi ya Geb kwa Oliva. Jinsi alivyokuwa akifurahia anapokuwa ametoka kazini halafu awakute wakimsubiria barazani. Kitandani anavyolala akiwa amemshika au kumchora mgongoni. Mabusu ya shingoni na mgongoni. “Nitalalaje bila Geb!?” Nanaa akawaza. “Nimeondoka kwa haraka bila kufikiria. Sikutakiwa kumkimbia Geb. Heri ningemuaga tu. Geb ameniamini na mtoto, leo nimemsaliti!”  Nanaa akajikuta akilia. Aligeukia dirishani, akaendelea kulia. Akaanza kumuhurumia Geb akaamua kushuka njiani pindi basi litakapo simama.

“Lakini kwa nini amenificha kuwa anafanya kazi na mwanamke wake?” Wazo jingine likamjia. “Labda alikuwa na mimi hospitalini kwa kuwa alijua mwanamke wake ndiye aliyenisababishia yote yale! Dhamira ilikuwa ikimsuta.” Akajikausha machozi. Gari lilisimama maeneo ya Korogwe. Nanaa akataka kushuka, lakini akapingana na hilo wazo.

“Kwanza nilimuuliza kama anamfahamu ni nani aliyenifanyia hivyo, akasema anamfahamu. Alishindwa nini kunitajia kama sio alitaka kumficha mpenzi wake? Geb anapenda kutetea watu wake kama Danny na mama yake. Heri nikaanze maisha yangu.” Nanaa akatulia kwenye kiti. Akamfunika mwanae vizuri akajiegemeza kitini, akarudi kulala tena.

Kwa Geb.

Walikaa mpaka saa 11 jioni, Geb hajatoka chumbani kwake. Grace na Danny nao pia wakaamua kuondoka na watoto wao. Mama G akaona aende tu kumuangalia. Akamkuta amepiga magoti. Kichwa amekiegemeza kitandani. “Geb!” Mama yake aliita kwa upole. Geb akanyanyua uso. “Naomba unisamehe mwanangu. Najiona ninakusababishia maumivu kila wakati. Mara ya kwanza Nanaa aliondoka akiwa mjamzito, mimi nikiwa sababu. Mara hii ya pili anaondoka tena akiwa mjamzito, na mtoto juu, mimi nikiwa pia nimesababisha.” Geb akakaa kitandani.

“Njoo ukae hapa.” Mama G akaenda kukaa naye. “Naomba nisaidie kuomba mama. Naomba tuombe wote.” Mama G alimuonea huruma. “Kwani umeshindwa kuomba?” “Nimeomba. Lakini naomba tuombe wote tena. Maombi ya watu wawili wakipatana, yanakuwa na nguvu zaidi. Naomba tumuombee Nanaa wangu na watoto pia. Nanaa hajala tokea juzi. Alipoteza hamu ya kula kabisa baada yakuzungumza naye mambo yenu. Jana asubuhi pale hotelini hakula vizuri. Halafu ni mjamzito na ananyonyesha. Naomba tumuombee ulinzi wa Mungu. Popote alipo, Mungu amtie nguvu na kumlinda.” Machozi yalianza kumtoka mama G. “Nisamehe Geb. Naona vile ninavyokutesa mwanangu.” “Hata hili litapita tu. Naomba tuombe.” Wakapiga magoti.

Wema Huwa Hauozi!

Nanaa alifika Arusha, huku akikumbuka mapenzi ya Geb kwake. Mambo makubwa aliyokuwa akimfanyia. Upendo alio uonyesha kwake. Akakumbuka hakuwa akithaminiwa mpaka Geb alipoweka thamani kwake. Akajirudi. “Hata kama Geb ana mwanamke mwingine, sijawahi kupendwa na kujaliwa kwa kiasi hiki! Geb ananipenda kwa dhati. Anasisimkwa akiniona! Hawezi kulala bila kunigusa mimi. Anafurahi akiniona mimi na Liv.” Japokuwa mawazo mengi tofauti tofauti yalikuwa yakipita kichwani mwake akiwa njiani, lakini hilo ndilo likashindwa kupingwa au kupata upinzani mpaka anafika huko Arusha.

 Akaona kutomtafuta Geb ni kutokuwa na utu. Hata kama amekosea, basi angalau amjulishe yupo salama. Kumtoa wasiwasi. Wakiwa ndio wanapiga tu magoti ili aombe na mama yake simu yake ikaanza kuita. Geb akavuta simu yake kutoka mfukoni. Akaitizama ilikuwa namba ambayo haifahamu. Akasita kupokea. Lakini kama kitu kikamsukuma moyoni, akapokea. Huwa kama namba haifahamu, hapokei kabisa. Na ni mara chache sana hata kusoma jumbe za namba ambazo hazifahamu. Hufuta bila hata kusoma.

“Haloow?” Geb akaitika. “Geb! Nataka kukutoa wasiwasi. Nimefika salama. Na mtoto hajambo.” Akaweza kutambua kilio kwenye sauti yake. “Nanaa!” “Abeee!” Nanaa akaitika akijaribu kutulia. “Upo salama mpenzi wangu?” “Kuna baridi tu. Lakini nipo salama.” Nanaa akajibu. “Ulibeba nguo nzito za kujifunika?” Geb akauliza akisikika kumjali yeye bila kukimbilia lawama au kutaka kujua alipo kitu kilichomshangaza sana Nanaa na kuzidi kujutia kukimbia mapenzi mazito ya kiasi hicho. Akazidi kulia.

“Eti Nanaa? Ulibeba nguo nzito za kukuhifadhi usiumie na baridi?” “Hapana.Lakini mtoto nimemfunika vizuri. Usiwe na wasiwasi.” “Ungependa nikuletee nini cha kukusitiri kwa baridi?” Akamsikia Nanaa akiendelea kulia. “Nanaa!” Geb akaita. “Nina hamu na wewe Geb. Sijui nitalalaje leo?” Ndicho kitu Nanaa alifanikiwa kuzungumza. “Naweza kukufuata ili tuwe wote Nanaa.” “Naogopa Geb. Sitaki kufa niache watoto. Acha nianze tu maisha mapya. Nikitulia nitakutafuta. Lakini nisamehe niliondoka bila kukuaga. Niliingiwa na hofu.” “Unaanza maisha mapya bila mimi Nanaa?!” Nanaa akazidi kulia.

“Eti mpenzi wangu?” Geb aliendelea kubembeleza taratibu tu. “Nimeingiwa na hofu Geb. Mira ameapa kuniangamiza kabisa kama sitaachana na wewe. Amesema atamuua na Oliva pia.” “Pole mpenzi wangu. Naomba usilie. Umepata sehemu ya kulala wewe na watoto?” Nanaa alikuwa amembeba Oliva. Akajishika tumbo. Akakumbuka ni mjamzito. Akajifuta machozi. Mpaka hapo bado Geb hakuwa akijua Nanaa alipo. Lakini akajitahidi asikurupuke kuuliza hilo swali. Amchote taratibu tu, kwa upendo.

“Nanaa?” “Ndio nimefika tu. Bado nipo stendi. Nimepata mtu nimemuomba aniazime simu ili nikutoe wasiwasi. Niliacha simu nyumbani. Niliitupa kwa hofu Geb.” “Pole sana.” Geb aliongea kwa upole. “Nitakutafuta tena wakati mwingine. Ngoja nikatafute sehemu ya kulala. Sitaki Liv ashikwe na baridi zaidi. Nitakupigia wakati mwingine. Narudisha simu kwa mwenyewe.” “Unafikiria kulala wapi?” Geb akauliza kwa haraka kabla hajakata simu. “Kwa sasa nitachukua chumba hotelini. Huku nikitafuta chumba cha kupanga mahali. Nitatafuta kazi. Nakuahidi kukutumia pesa yako yote. Nitalipa kidogo kidogo.” Machozi yakaanza kumtoka tena.

“Unafahamu hayo mazingira vizuri?” Geb akamuuliza swali la kumtega ila kwa upendo tu. “Hapana Geb! Wewe unajua historia yangu. Sijaishi maeneo mengi zaidi ya Moshi na hapo Dar. Lakini nilikuja huku Arusha kwa sababu Alex, alikuwa au niseme anaishi huku. Alikuwa anapasifia sana. Anasema ni pazuri. Ndio maana nikaamua kuja kuanza huku maisha. Nahisi sitasumbuka. Usiwe na wasiwasi na watoto. Nitahakikisha watakua salama tu.” Nanaa akajikuta ametamka alipo. Geb akajua.

“Nafahamu hoteli nzuri itakayowafaa wewe na watoto.” “Mmm! Sitakuwa na hiyo pesa Geb. Najitahidi kubania pesa ili nipate sehemu nzuri ya kuishi na watoto. Na siku ya kujifungua nisipate shida yeyote hasa kifedha, kama nitakuwa bado sijapata kazi. Sitaki watoto waje wapate shida. Acha niende kwenye hoteli za bei ya chini. Halafu namaliza muda wa maongezi kwenye simu ya watu. Naomba nikuage kwa sasa ili nikatafute sehemu ya kulala.” “Basi nakata, halafu nitakupigia mimi sasa hivi, ili nisimalize pesa yake.” “Nataka kuondoka Geb. Hapa kuna kelele na Liv ameanza kutetemeka baridi, sitaki apatwe na vichomi kama mimi wakati ule mpaka nikalazwa! Nitakupigia simu wakati mwingine.” Nanaa akasisitiza.

“Basi chukua taksii, halafu muombe dereva wa taksii akuazime simu yake. Unipigie, halafu nitazungumza naye pia nimuelekeze sehemu ya kukupeleka.” “Sawa.” Nanaa akaitikia kwa haraka ili tu akate ile simu. Na Geb akajua. “Tafadhali usisahau Nanaa. Niahidi utanipigia ukiwa ndani ya taksii.” Nanaa akajua amekamatwa. Aliitikia bila kufikiria. Na Geb huwa hapendi kuahidiwa kitu, halafu usitimize.  “Sasa hapo itategemea kama nitapata dereva mwenye muda wa maongezi kwenye simu yake na kama atakubali, Geb.” “Kabla hujapanda kwenye hiyo taksii, hakikisha unapanda kwenye taksii yenye dereva mwenye simu.” “Geb! Nina masanduku mawili, na mtoto! Kwanza nilipanga kupanda daladala ili kubania pesa.”  “Hapana Nanaa. Kwenye daladala utawatesa zaidi watoto. Naomba uchukue taskii.” “Sawa. Nitafanya kama ulivyosema Geb. Asante na kwa heri.” Nanaa akaaga. 

“Nanaa!” Geb akaita. “Abee!” Nanaa akaitika akiwa anakaribia kukata simu. “Nakuombea ufanikiwe mpenzi wangu.” Hapo akaupata moyo wa Nanaa. Akajikuta machozi yakimtoka. “Nakupenda Geb.” “Najua Nanaa. Na mimi nakupenda sana, Nanaa wangu. Kila kitu kitakuwa sawa. Hakikisha unapanda taksii, na umwambie mwenye taksii anipigie.” “Nitafanya kivyo.” Nanaa akakata simu nakumrudishia mtu aliyekuwa amemuazima simu hiyo. Alikuwa kondakta wa basi hilo lililofanikisha kumfikisha jijini Arusha salama. 

~~~~~~~~~~~~~~

Baada ya kupingana na mawazo mengi akiwa ndani ya basi mpaka abiria wote wakashuka na kumuacha yeye peke yake na mwanae aliyekuwa amemkumbatia kama andazi ndipo huyo kondakta akamfuata na kumuuliza kulikoni kwani pale ndio ilikuwa mwisho wa basi. Na abiria wote walikuwa wameshuka. Mawazo ya wema wa Geb juu ya maisha yake, yakazidi ubaya wa kutokuambiwa habari za Mira. Akajikuta kosa la Geb ni dogo sana, kulinganisha na garama alizomlipia kwenye maisha yake.

 Kila alipojiambia kwa shahada aliyonayo, atapata kazi nzuri. Atalipwa mshahara mzuri. Atakuwa na uwezo wa kuja kumaliza deni la milioni 50 aliyolipiwa na Geb, lakini akakumbuka garama ya Geb aliyomlipia maishani si pesa peke yake. Alijitoa kwa hali na mali pia. Akagundua upendo mkubwa na wa dhati wa Geb maishani mwake. Akagundua kwa hakika hatakuja kupata mwanadamu anayempenda kama Geb.

Katika wanawake wengi waliotaka kuzaa na Geb, yeye ndio alichaguliwa na Geb! Ndipo akaona wema wa Geb unazidi ubaya alioleta Mira. Kwanza hata kama ni mwanamke wake, mbona muda mwingi anakuwa na yeye!? Kwa nini yeye Mira ndio awe wakutetea mahusiano yao sio Geb!? Hata Nanaa akajiuliza hilo. Nanaa akakumbuka vile Geb anavyopambana kuona wanakuwa pamoja. Alimuona anavyomlinda na mama yake mkubwa. Alilipa pesa yote ile ili awe naye. Akakumbuka visa vya  Zinda hata na Liz. Alimwambia alikubali yeye ndio atupiwe lawama, lakini sio yeye.

“Huyu Mira atakuwa muongo tu. Inawezekana alikuwa mpenzi wa Geb, lakini Geb alishamuacha, ndio sasa hivi anahangaika na mimi na mwanangu.” Ndio wazo la mwisho alilokuwa amefikia Nanaa na kuazimia kumtafuta Geb. Ndipo akaazima simu ya Kondakta huyo kumtaarifu Geb alipo. Lakini hakutaka kurudi kwa Geb, nikutaka tu kumtoa wasiwasi. Lakini kwenye simu aliyompigia Geb, akaibua hisia zaidi. Akajikuta anaongea hata ambayo hakupanga kuongea. Akatoa ya moyoni huku akilia. Geb alimlainisha mpaka Nanaa akaingia kwenye mtego yeye mwenyewe. 

~~~~~~~~~~~~~~

Akamrudishia yule kondakta simu yake, kisha akampa pesa kidogo kama shukurani ya kumshikia mizigo yake, akamuongezea pesa nyingine, akamwambia akanunua muda mwingine wa maongozi. Alipoona amepewa pesa nzuri, upendo ukaongezeka. “Naweza kukusaidia kukubebea mizigo mpaka kwenye taksii ili usisumbuke na mtoto.” “Nitashukuru kaka yangu.” Akambebea mizigo mpaka kwenye taksii. Nanaa akampa tena pesa nyingine, akaingia na mtoto ndani ya gari. Oliva alikuwa amejikunja kifuani kwa mama yake kwa baridi.

 “Tunaelekea wapi?” Mwenye taskii akauliza baada ya Nanaa kupanda na mwanae. Lilikuwa swali zuri sana, lakini hakuwa amejiandaa na jibu lake. Hakujua hata wanakwenda wapi. Akakumbuka Geb alimwambia ampigie simu mara baada ya kupata taksii. “Naomba unisaidie simu yako, nimpigie mtu atakuelekeza.” Yule dereva akatoa simu akampa. Nanaa akapiga. Ikaita mara mbili, akakata. Hapo hapo Geb akapiga.

“Samahani nakusumbua Geb. Lakini tupo kwenye taksii tayari.” “Hunisumbui hata kidogo. Naomba kuzungumza na dereva.” Akarudisha simu kwa dereva. Akapokea maagizo kutoka kwa Geb. Akasikia dereva akijibu, ‘nimeelewa’. Kisha akamrudishia simu Nanaa. “Nanaa!” “Abee!” “Nimemuelekeza sehemu ya kukupeleka wewe na watoto.” Wasiwasi ukamwingia Nanaa. Alimjua Geb na maisha anayoishi. Hakuwahi kumpeleka sehemu za bei ya chini. “Unakumbuka swala la pesa lakini? Naomba isiwe sehemu ya garama Geb! Nabania pesa mwenzio! Sitaki kuja kusumbuka na watoto.” “Usiwe na wasiwasi. Nimeshawapigia simu ili wawatayarishie chumba, mkikute tayari. Patakufaa wewe na watoto. Halafu ukishaingia chumbani, unipigie simu.” “Nimeacha simu nyumbani Geb.” “Hapo hapo chumbani kutakuwa na simu.” Hilo likazidi kumuogopesha.

“Hizo si zitakuwa hoteli zile za garama sana!?” “Naomba usiwe na wasiwasi juu ya pesa Nanaa. Fikiria usalama wako wewe na watoto kwanza. Sawa?” Kila wakati Geb alimkumbusha anao watoto wawili. Hajapuuza ujauzito wake kitu kilichozidi kumtuliza Nanaa. “Sawa. Nakushukuru Geb. Na samahani kwa usumbufu. Nakuahidi kukupigia Liv akishatulia. Sasa hivi anatetemeka baridi. Lakini kama nikikuta umelala, nitakupigia tena kesho. Umenisikia?” “Sawa.” Geb akajibu bila wasiwasi. Nanaa akashangaa safari hii hakulazimisha kupigiwa simu. Ikamuumiza moyoni.

Alitegemea kuambiwa lazima unipigie simu kabla hujalala. Lakini akaishia kusikia sawa! Ikabidi aage kwa upole. “Usiku mwema, Geb.” “Mama anataka kuongea na wewe.” Nanaa akanyamaza. “Nanaa!” “Bado nipo.” “Nakupa mama.” Kimya. Akamsikia anaanza kulia. “Nakuomba usilie tena. Pole mpenzi wangu. Pole sana.” Akamsikia akijaribu kuvuta pumzi mara kadhaa kujituliza. “Nanaa?” “Nipo Sawa, Geb.” “Utaweza kuzungumza na mama sasa hivi au baadaye?” Geb akatumia hekima. “Ni sawa tu.” Nanaa akajibu. 

          Geb akamkabidhi simu mama yake. “Pole na safari Nanaa, mwanangu.” “Asante mama. Samahani nimeondoka na mtoto gafla.” Mama G hakutegemea, lakini Nanaa alijua ukaribu wa huyo mama na Oliva mtoto wao. Alimpenda bila unafiki. “Usiwe na wasiwasi mwanangu. Sasa fanya hivi, ukifika tu hotelini, pale mapokezi waambie wakupe blangeti la umeme. Nimeshazungumza nao. Wamesema watakutayarishia. Ukifika chumbani, mwambie muhudumu alichomeke kwenye umeme. Uingie humo ndani na mtoto. Hakikisha unamnyonyeshea Oliva mkiwa humohumo ndani ya hilo blangeti ili apate joto. Usimuogeshe leo usiku. Na wewe utulie humo humo ndani ya blangeti kwa muda ili kutoa vichomi. Umesikia mama?” Nanaa alikuwa akilia. Mama G alishamuhangaikia mpaka blangeti! Hakutegemea.

Alijua atakuwa amemkasirikia baada ya kuondoka bila kuaga. Lakini akakuta anabembelezwa! Ilimuingia sana moyoni. Kutoka kwenye maisha ya kulaumiwa kwa kila jambo, sasa hivi anapata watu wanao mnyenyekea! “Asante mama.” “Pole mwanangu. Jitahidi kunywa hata mtori. Nimetoa oda jikoni. Nimewaambia wakuletee chumbani.” Mama G akaongeza. Nanaa alishindwa hata kujibu. Akabaki akilia. “Nakurudisha kwa Geb.” Mama G akampa Geb simu yake.

           “Nanaa! Kila kitu kitakuwa sawa mpenzi wangu. Tutaongea tena hivi karibuni. Huyo dereva mimi ndio nitamlipa. Usimlipe pesa yeyote. Nimemuomba akusaidie kubeba mizigo mpaka ndani. Usibebe mizigo na watoto. Yeye ndio atakusaidia. Akikufikisha mapokezi, ndipo anipigie, nikizungumza na wewe, ukiniambia amekufikisha salama, namtumia pesa yake kwa njia ya simu.” Nanaa aliendelea kulia. “Nanaa!” “Ninazo pesa Geb. Acha tu nitalipia. Nikifika chumbani nitakupigia.” “Basi mwache akubebee mizigo mpaka ndani. Naomba niahidi hutabeba hiyo mizigo wewe mwenyewe. Utajiumiza mgongo na kuhatarisha maisha ya mtoto tumboni.” “Nitamwacha anibebee, asante.” Geb akakata. Nanaa alimkumbatia mwanae zaidi huku akilia.

Nanaa Hotelini Jijini Arusha.

Baada ya muda, dereva alimwambia wamefika. Nanaa akabaki ametoa macho. “Hapa si patakuwa pa garama sana!” Nanaa akajikuta anaongea peke yake huku ametoa macho. “Sitapaweza!” Akaendelea kuwaza wakati dereva akimtolea mizigo yake. Akashuka kwenye gari. Akaongozana naye mpaka mapokezi. Akamlipa yule dereva. Akabaki ametoa macho akishangaa uzuri wa ile hoteli ya kisasa mle ndani huku amebeba mtoto wake mkononi.  

Wazungu ndio walikuwa wengi ndani ya hoteli hiyo. Kuashiria ni ya watalii. Waliokuwa na ngozi nyeusi kama yake, wote aliwasikia wakiongea lugha ya kigeni.

Kama sio kingereza, basi ilikuwa kifaransa na lugha nyingine ambazo hata hakuwa akijua wanazungumza nini. “Can I help you?” Nanaa akageuka. Akakuta muhudumu ametulia pale mapokezi akimuuliza kama anaweza kumsaidi. Alikuwa dada mrembo tu. Amevaa sare safi akaonekana nadhifu. Alimpa tabasamu la kumkaribisha.

Tarayi Nanaa alikuwa na wazo la kuondoka hapo. “Karibu.” Yule muhudumu mwenye sura ya kuvutia, akarudia kwa lugha ya Kiswahili baada ya Nanaa kubaki amekodoa macho. Akajua wazi ni mtanzania mwenzake. “Naitwa Nanaa. Nimeambi..” Nanaa akakwama. Hakujua aseme nini. “Nanaa Magesa?”Muhudumu akauliza huku akiangalia kwenye kompyuta.

“Si ni Nanaa Magesa upo na Oliva Magesa?” Si kwamba Nanaa hakuwa amemsikia tokea mwanzoni. Lakini hakutegemea kusikia akitambuliwa kama Nanaa Magesa. Moyo wake ukajawa furaha, akamwangalia mwanae. “Ndiyo.”  Akajibu na kurudisha macho kwa yule muhudumu. “Karibu sana. Chumba chenu kipo tayari. Alinipigia tena simu nakuniambia chumba kiwashwe heater kabisa na blangeti lenu la umeme pia lipo tayari kitandani. Na lenyewe alisema liwashwe kabisa. Naamini mtafurahia. Subiri kidogo nimwite mtu wakukubebea mizigo yako. Chakula kitaletwa baada ya muda mfupi. Ukihitaji kitu chochote, usisite kunipigia hapa mapokezi. Bonyeza namba sifuri tu, nitakuitika.” Nanaa alibaki ametoa macho, asiamini maandalizi yote yanayomsubiria yeye.

Akabebewa mizigo yake, akapelekwa kwenye chumba chake. Kilikuwa chumba kizuri sana. Chumba chenyewe tu ni kama nyumba! Ilikuwa na upande wa sebule. Makochi mazuri sana. Muhudumu alimuuliza mara kadhaa kama kuna kitu kingine anahitaji, lakini Nanaa alibaki anashangaa tu na mtoto wake mkononi. Akaamua kuzunguka kila mahali kwanza. Akaelekea chooni na upande vilipo vitanda. Akabaki ameduaa upande wa vile vitanda. Vilikuwa vimetandikwa vizuri sana lakini sio vitanda vizuri kushinda alivyoacha nyumbani kwa Geb. Geb alilalia kitanda kizuri sana.

Mlio wa kufungwa mlango na yule muhudumu ndio uliomtoa kwenye mawazo. Akajikuta amebaki peke yake na mwanae pale chumbani. Akarudi pale alipokuwa amemuacha yule muhudumu kuangalia kama mizigo yake ipo au aliondoka nayo. Akakuta alishaingiza mpaka kule chumbani upande wa makabati ya nguo. Akapumua kwa nguvu. Akafanya kama alivyoambiwa na mama G, akapanda kitandani kwa haraka. Akamfunika Oliva huku anamnyonyesha. Oliva alilala pale pale kwa haraka. Nanaa akajua alikuwa amechoka. Akamfunua tena, akambadilisha diaper yake. Ilikuwa imejaa sana. Akamuhurumia mwanae. Akajilaumu sana. “Nimemtesa mwanangu. Pole Liv. Kila kitu kitakuwa sawa.” Akambusu, na kumuweka sawa. Akahakikisha amemfunika vizuri. Ndipo na yeye akajilaza.

Baada ya muda kidogo, akasikia mlango unagongwa akajua tu ni mtu wa chakula maana aliambiwa ataletewa chakula. “Karibu.” Akasimama. Ni kweli alikuwa ameletewa chakula. Akamkaribisha ndani na kumwambia aweke chakula kwenye meza karibu na makochi. Akaweka na kutoka. Akakumbuka ni zaidi ya dakika 45 tokea azungumze na Geb. Na alimwambia ampigie mara atakapofika hotelini. Akaangalia. Akakuta kuna simu ya mezani. Akampigia. Haikuwa inapatikana. Akajaribu tena na tena hakumpata. Akaingiwa na wasiwasi. “Geb amenikimbia!” Nanaa akaanza kulia.

~~~~~~~~~~~~

Alilia na kusahau kuwa yeye ndiye aliyemkimbia Geb. Akajirudisha kitandani. Alilia na kulia. Akajua amebaki peke yake. Akaanza kupangia mahesabu pesa alizo nazo. Akapiga simu mapokezi kuuliza bei ya kile chumba. Akatajiwa kwa dola za kimarekani zisizopungua $185 kwa usiku huo ila akaambiwa inategemea na huduma ya ziada atakazopewa. “Dola!?” Nanaa akauliza kwa mshituko. “Dolla 185 na inategemea na huduma kama hivyo ya room service. Ukiletewa huduma chumbani ni tofauti na kuifuata. Kwa hiyo usijali. Jumla yote itawekwa kwa pamoja.” Akajaribu kumuelewesha kwa utulivu tu asijue ndio anazidi kumuongezea hofu. “Haya. Asante.” Akakata simu.

Usingizi wote ulimuisha. “Dola!? Nilimwambia Geb kuwa sina hiyo pesa! Nitafanyaje na watoto jamani! Watanifunga jela kama nikishindwa kulipa. Au nilipe ya usiku wa leo tu, halafu asubuhi niondoke? Sitaweza kuendelea kulala hapa.” Akamuona vile mtoto wake alivyolala vizuri. Akaridhika moyoni. “Hata kama nitagaramia pesa yote hiyo, angalau mwanangu amelala vizuri. Baridi inaonekana imemuweza!” Akamfunika vizuri akabaki akiwaza.

Akaamua kwenda kuoga. Akakutana na mabomba yanayotoa na maji ya moto huko bafuni. Akafurahia. Akiwa anaoga akakumbuka Mira alimwambia atamnyonga mtoto wake akiwa usingizini. Akafunga maji kwa haraka, akakimbilia taulo. Akatoka akikimbia mpaka kitandani alipokuwa amemuacha mtoto wake, akaweka kidole puani kwake. Akakuta anapumua. Akamshika homa. Akagundua hana homa. Akamfunua miguuni, pia akakuta miguu yake ipo sawa tu. Akaibonyeza mara kadhaa, akagundua ipo sawa tu. Akabaki anahema kwa hofu. Akaona pale alipolala hatakuwa salama. Akaamua amnyanyue mtoto wake alale mikononi mwake. Akakaa pale pale kitandani akiwa amempakata mwanae. Akapitiwa na usingizi. Kila wakati alishituka na kuweka kidole puani mwa mwanae kuhakikisha bado anahema.

~~~~~~~~~~~~

Akiwa amepitiwa na usingizi pale kitandani huku amempakata mtoto wake kwa hofu, akasikia mlango unagongwa. Akashituka sana. Akaangalia saa ya ukutani, ilikuwa inakaribia saa nne usiku. Akaingiwa hofu ya ajabu. “Labda wanataka kunidhuru mimi na mtoto wangu!” Nanaa akawaza. Hakuwa ameagiza kitu chochote kwani hata chakula walichokuwa wamemletea hakuwa amekula. Na tayari ilishakuwa karibu ni saa 4 usiku. Akavaa rob nyeupe iliyokuwa imening’inizwa pale chumbani.

Akasogelea mlango. “Nani?” Nanaa akauliza kwa wasiwasi. Akasikia tena mtu anagonga taratibu bila kujibu. Bado alikuwa amembeba mtoto wake. Akarudi kwa haraka kwenye simu ya mezani kujaribisha kumpigia tena Geb ili kuona kama safari hiyo angempata. Safari hii ikaita na kumfariji. Ilipoita mara ya pili, akapokea. “Samahani nakusumbua, Geb. Lakini naogopa. Kuna mtu anagonga mlango sasahivi. Hataki kuniambia yeye ni nani. Nifanyaje? Nipo na mtoto hapa. Kama wanataka kumdhuru je?” Geb alihisi hofu iliyomkamata Nanaa. Akamuhurumia. “Usiogope Nanaa. Hakuna mtu anaweza kukuingilia. Hiyo hoteli wanailinda sana ndio maana nilikuchagulia hapo. Fungua.” Nanaa akasita.

“Geb wewe! Unajua Mira amesema atamuua Oliva?” “Amekuogopesha tu. Ameshindwa tena kwako ndio maana anatumia lugha ya vitisho. Hawezi kumdhuru mtoto. Usiogope.” “Unafikiri hivyo!?” Nanaa akauliza kutaka uhakika.  “Kabisa. Hebu fikiria Nanaa. Kwani mara ya kwanza alipokudhuru, alikutumia kwanza vitisho?” “Hapana.” “Basi ujue ameshindwa kufanya madudu yake tena. Ndio maana akaamua kutumia njia ya kukuogopesha. Hana nguvu hiyo tena juu yetu. Tumefunikwa na ulinzi wa kiMungu, ndio maana anahangaika.” Kidogo Nanaa akafarijika. “Basi naomba usikate simu, Geb. Ili kama kuna kitu kibaya kitanipata, ujue halafu uwapigie simu watu wa mapokezi waje kunisaidia. Umesikia?” “Sawa.” Geb akamkubalia. Ndipo Nanaa akaenda kufungua mlango huku amembeba mtoto wake. Hakutaka kumuweka chini. 

Alumasi Husakwa Chini Kabisa Aridhini.

Na Atafutaye, Hachoki.

Alipofungua mlango, macho yake yakagongana na Geb aliyekuwa amesimama katikati ya mlangoni. Nanaa alirudi nyuma kwa mshituko. Kwa hakika hakutegemea. Akamwinamia mtoto wake nakuanza kulia. Hakuamini. Akanyanyua uso kuthibitisha kile anachokiona. “Geb!” Geb akaingia. “Umewezaje kufika huku kwa haraka hivyo!?” “Nilibahatika kupata ndege. Mara ya mwisho tulipokuwa tukiongea. Ukaniambia utanipigia simu hata kesho. Halafu ukaongea na mama pia. Pale tulikuwa tayari tupo njiani na mama ananisindikiza uwanja wa ndege kuja huku. Nilipojua tu upo huku Arusha, hapohapo nikamtumia ujumbe yule kijana anayekatisha tiketi, huku tunazungumza na wewe. Tulipoagana kwenye simu mara ya kwanza ukiwa unatafuta taksii, hapo hapo nikakusanya vitu nilivyojua nitahitaji kwa safari nikaingia kwenye gari kuelekea uwanja wa ndege. Nikamuomba yule jamaa anayetusaidiaga kupata tiketi za ndege kwa haraka bila shida. Nikamwambia nipo njiani naelekea uwanja wa ndege, lazima leo nilale Arusha. Mungu alikuwa upande wangu. Nimefika tu uwanja wa ndege nikapata tiketi ya ndege iliyokuwa inakaribia kuondoka.” Nanaa bado hakuwa akiamini. 

“Jamani Geb!” Nanaa aliendelea kulia. Asijue kama ni furaha au mshituko wa kumuona pale mida hiyo. Alijua ameshaachwa na watoto wake. “Unajua siwezi kulala bila wewe Nanaa.” Nanaa alilia sana. Geb akaweka mkoba wake chini, akamsogelea Nanaa. “Mbona umembeba huyo?” “Naogopa Geb. Yale maneno ya Mira kuwa atamnyonga akiwa usingizini, yananisumbua sana.” “Hilo ndilo alilokusudia. Anakutia tu hofu. Hana chakutufanya tena. Nipe nikupokee.” Geb akamchukua mtoto wake.

Kama kawaida. Akamuweka kifuani na kumkumbatia kwa nguvu huku akisikilizia furaha moyoni. Akambusu mara kadhaa. Akaanza kumuombea huku amemkumbatia. “Nakuombea usingizi mzuri Liv. Malaika wa Bwana wakafanye kituo kwako. Ulinzi wa Mungu ukawe juu yako. Kila ulimi ulioinuka na utakao inuka juu yako, nauhukumu mkosa. Umeshindwa katika jina la Yesu. Nguvu ya mauti juu yako ninaikataa. Haina mamlaka wala nguvu kwako, katika jina lipitalo majina yote. Jina la Yesu, Liv wewe utaishi ili ukayashuhudie na kuyasimulia makuu ya Mungu. Uhai wako ukafichwe ndani ya Kristo Yesu. Nakutamkia baraka. Umebarikiwa mwanangu, kwa baraka zote za rohoni na mwilini. Amen!” Geb akamaliza na busu kwa mwanae. Alimtizama kidogo, akamgeukia Nanaa. Akamkuta ametulia kimya.

“Naomba nimlaze. Apumzike.” “Nimefurahi umekuja Geb. Hofu imepungua.” “Nataka iishe Nanaa. Hakuna silaha itakayoinuka tena kwetu ikafanikiwa. Naomba uamini. Ni vitisho tu. Wanataka kukuogopesha.” Nanaa akatulia. Geb akaenda kumlaza mtoto wake kitandani. Akamfunika vizuri, akarudi kwa Nanaa.

~~~~~~~~~~~~

 “Njoo Nanaa wangu.” Geb akamvuta. “Nisamehe. Niliingiwa hofu, nikakimbia.” “Nimefurahi sana ulinitafuta, Nanaa. Asante.” Geb akamkumbatia. “Nina hamu na wewe Geb!” Geb akambusu kichwani akiwa amemkumbatia. Akamsikia Geb akivuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu kama aliyepata aghueni moyoni. Akafurahi kuhisi Geb anamtoa nguo. Akaanza kutoa ile rob ya juu. “Mbona upo na taulo bichi!?” “Nilikuwa naoga. Nikakumbuka maneno ya Mira, nikamkimbilia mtoto wangu. Niliogopa nisije nikatoka kuoga, nikamkuta Liv amekufa.” Geb akamuhurumia sana.

“Pole Nanaa. Anakutisha tu.” “Kwani alikuwa mpenzi wako?” Nanaa akamuuliza kwa upole. “Nimefurahia sana jinsi ulivyouliza hilo swali. Nimepata moyo kuwa unaniamini.” “Najua hunidanganyi Geb. Hilo ninauhakika nalo. Najua kwa sasa hivi nipo peke yangu kwako.” Geb alifurahi sana. Akambusu kichwani, akamtoa lile taulo bichi mwilini mwake, akamfunga tena ile rob, akamshika mkono, wakasogea mpaka kwenye makochi. Wakakaa.

Siri Ya Pili.

 Juu Ya Mira.

“Ni kweli niliishi na Mira nyumba moja.” Geb alianza kwa utulivu huku Nanaa akimsikiliza. “Lakini ilikuwa mwaka wa mwisho wa masomo yangu nilipokuwa nchini India. Mwaka huo wa mwisho, niliishiwa pesa. Na kwa kuwa malengo yangu yalikuwa mwaka huo nimalize masomo yote, na niondoke nchini hapo na shahada mbili, tena zote nzuri, ilinibidi kujibana sana ili kufanikisha malengo. Hapo mama alikuwa ameshamaliza kuuza mali zake zote. Hana kitu. Ukumbuke hapo ni kama alikuwa akisomesha watoto wawili, kwa shahada za juu, tena kwa ada ya nje, au kimataifa. Haikuwa pesa ndogo, Nanaa.” Geb akaendelea.

“Ikabidi sasa kutafuta watu wakuishi nao ili kubana matumizi. Ndipo nikapata chumba kwenye apartment aliyokuwa akiishi Mira na rafiki zake. Pesa ya pango ikapungua. Lakini bado haikutosha. Ikabidi kutafuta tena mtu wakuishi naye kwenye hicho chumba changu. Nikampata kijana mmoja kutoka nchini Nigeria. Tukawa tukiishi naye kwenye chumba changu, ndani ya apartment ya Mira na rafiki zake.” Geb akatulia kidogo.

Kisha akaendelea. “Nilikuwa nipo busy, ungeniona kipindi hicho, ungenihurumia Nanaa. Unajua kula yangu jinsi ilivyokuwa ya shida. Sasa ndio ikawa mbaya zaidi. Sikuwa nikikumbuka nilikula nini, wala sikuwa na mpango wa kula. Mimi na shule, shule na mimi bila kujua watu wananitizama. Mira akaanza kazi ya kunipikia na kuniwekea chakula. Siku moja nilitoka kujisomea, nikarudi kama saa tano usiku. Nikamkuta amekaa sebuleni anaangalia tv. Mimi nikajua yupo na mipango yake, kumbe alikuwa akinisubiri mimi. Akaniambia kipo chakula hapo mezani. Nile. Basi. Mimi nikakiangalia. Ilikuwa chapati sijui na mboga gani zile! Kwa kuzitizama tu kwa macho, nikawa nimekinahiwa. Nikachukua chapati moja, nikaingia chumbani kwangu huku nakula. Sikuwa hata nikijua kama yeye ni mpishi.” Geb akaendelea.

“Sasa kilichonishitua na kunifanya nijiulize, ni siku ya pili yake niliporudi pale tulipokuwa tukiishi, yule jamaa niliyekuwa nikilala naye chumba kimoja akaniambia Mira alikwenda hapo na kuchukua nguo zangu zote chafu akaenda kufua! Sijaingiza zile habari kichwani vizuri, akaniambia nisiwe na wasiwasi. Kwani alishazirudisha zote zikiwa zimepigwa pasi. Amenipangia kwenye kabati langu. Kabla hata sijaongea chochote, akaniambia na ameniletea chakula hapo chumbani. Ameniomba nile. Nikajua mambo yameshaharibika. Mira hakuwa wa kwanza kunifanyia hayo. Alishatokea tena na mwingine kama Mira nilipofika tu hapo nchini. Nikajiapia kuishi peke yangu bila mtu, lakini shida ya pesa ikanifanya nirudie kosa.” “Kosa gani tena?” Nanaa akauliza.

“Nilipokuwa tu nimefika hapo nchini India, ndio mgeni tu. Nilikutana na dada mmoja wa kitanzania. Na yeye alikuwa amekwenda kusomea mambo ya unesi. Akaniambia atanitembeza hapo, kwenye sehemu muhimu. Nikakubali. Nilijuta Nanaa. Nilikuwa sihemi wala sipumui! Aliniganda mpaka nilihisi sitaweza kuhema.” Nanaa akacheka. “Usifikiri utani Nanaa! Dada alining’ang’ania huyo! Tena huku anatangaza kuwa mimi ni mwanamme wake. Wakati mimi ndio nilikuwa nimetoka kujiapia wanawake tena basi. Ndio nilikuwa nimetoka tu kutendwa hapo chuo kikuu cha Mlimani. Najua mama yangu ameuza kila kitu ili nisome. Nikajiambia nina jukumu la kumrudishia vyeti vya maana. Nilijiapia kutokuruhusu kipingamizi chochote kile. Nikakusudia kujikana haswaa.” Nanaa akacheka.

“Ukafanyaje sasa?” “Kwa nani? Mira au huyu wa kwanza?” Geb akauliza. “Wote.” Nanaa akajibu huku akicheka. “Yule wa kwanza ilibidi kuanza kumkwepa. Lakini haikuwa rahisi. Maana alikuwa akinifuata na kutaka tuongozane kila mahali. Kwenye kula, sijui kusoma. Mara anifuate nimsindikize shopping. Ilimradi tu tuwe wote. Ikabidi kumkwepa. Tena kwa wazi kabisa, ili aelewe. Haya, Mira naye nilipoona shuguli za kufuliwa zimeanza na kuletewa chakula chumbani, nikaamua niweke kikomo mapema. Nikamwambia yule kijana niliyekuwa nikiishi naye, asiwahi tena kuruhusu mtu yeyote achukue nguo zangu chafu na kwenda kufua kama mimi mwenyewe sijaruhusu. Na nikamwambia, asiwahi kupokea kitu chochote alichopewa aje anipe kutoka kwa yeyote anayeishi pale nchini India. Awaambie wanitafute mwenyewe wanikabidhi.” Geb akaendelea.

“Lakini yule jamaa akanisihi sana nimvumilie kwa muda mpaka atakapotumiwa pesa kutoka kwao.” Nanaa akakunja uso. Geb akajua hajamuelewa. “Yaani yule jamaa niliyekuwa nikiishi naye, aliniomba aendelee kupokea chakula kwa niaba yangu, ili awe anakula yeye. Kwanza mimi mwenyewe sikuwa nikipenda vile anavyopika. Sikuwa hata nikila chakula chake. Nilisita sana Nanaa. Hasa nikizingatia naelewa wazi nia ya Mira kwangu. Nikamwambia yule jamaa, kwa kuendelea kupokea vile vyakula, ni kama kumwambia Mira, na mimi nimemkubali.

Nikamwambia haitakuwa sawa aone vyakula vyake navipokea, halafu nije kumkataa baadaye. Lakini yule jamaa akanisihi sana nimvumilie. Basi. Nikampa muda mfupi. Mambo yake yalipokaa sawa ndio…” “Subiri kwanza Geb!” Nanaa alimkatisha.

“Inamaana mliendelea kupokea vyakula vyake!?” Nanaa akauliza. “Ndiyo Nanaa. Lakini baada ya muda mfupi tu, nikaona nikomeshe hiyo tabia. Nikamwambia Mira tutoke kwa ajili ya chakula cha usiku.” “Geb!” Wivu ulishamwingia Nanaa. “Nia yakumtoa ilikuwa ni kwenda kuzungumza naye Nanaa. Si vinginevyo.” Nanaa akatulia. Geb akaendelea.

“Tulipokuwa tukila kwenye huo mgahawa, ndipo ikabidi kumueleza ukweli wote. Kuanzia mwanamke aliyenisaliti nilipokuwa nipo hapo chuo kikuu cha Mlimani. Malengo na viapo nilivyojiwekea. Na nikamwambia juu ya vyakula vyote alivyokuwa akileta pale chumbani, kuwa ni jamaa ndiye aliyekuwa akila. Tena nakumbuka kumtania kuwa jamaa anasifia sana mapishi yake na yeye mwenyewe. Akacheka. Sasa nisikilize kwa makini hiyo ndoa ilipotokea.” Nanaa akajiweka vizuri.

“Alipoelewa kuwa sitanii  wala sina mpango kwenye swala la mahusiano ya kimapenzi. Si kwake tu, ila ni kwa yeyote yule kwa wakati ule. Akaniomba kuwa, endapo nitafikiria kuoa mwanamke mwingine basi anaomba nimfikirie yeye. Mungu wangu nishahidi Nanaa. Sijasahau kitu hata kimoja. Kiiungwana tu, bila kutaka kumuumiza, nikamkubalia yule dada. Tukazungumza mambo mengine. Tukaachana kwa makubaliano asifuate tena nguo zangu chafu chumbani kwangu. Yaani nilimuomba asinifulie tena. Wala asinipikie. Basi. Nikaona ameacha. Mimi nikaendelea na chuo changu. Shule ikachanganya. Nikamaliza na kuondoka pale nchini. Yeye nilimuacha bado anasoma.” Geb akaendelea.

“Muda mrefu ukapita bila hata mawasiliano. Akaja siku moja kuniomba kazi. Hata sijui nani alimpa namba yangu. Sikutaka kujua, nikampa kazi nikiwa nahitaji mtu pale ofisini kwetu. Grace akamfanyia usahili. Akaniambia anaona atatufaa. Akaanza kazi. Ninavyokwambia mimi, na ninaomba uniamini. Sikuwa hata na habari naye. Alikuwa akinisalimia kwa heshima kama wafanyakazi wengine. Hapakuwahi kutokea na mazungumzo yetu  sisi binafsi hata mara moja. Kwa kuwa yeye  ni muhasibu, na yupo chini ya Grace, wala si mimi. Akiingia ofisini kwangu ujue ametumwa na Grace aniletee kitu ili nikague au kupitia kama ile ripoti uliyokuwa ukitengeneza wewe. Basi.” 

“Huwa hata hatuna mawasiliano mengi mimi na yeye. Inaweza ikapita hata siku sijawasiliana naye. Kwa kuwa na mimi nina sekretari wangu na nina shuguli zangu nyingine mbali na ile kampuni unayoifahamu wewe. Kama ninataka mambo au habari za ile kampuni, nitazungumza na Grace tu, wafanyakazi wengine wa ile ofisi, wanawajibika kwa Grace, sio mimi. Nina mambo mengi sana Nanaa. Siwezi kuwa nikizungumza na kila mfanyakazi, lasivyo usingekuwa ukiniona nyumbani saa 11 jioni au 12. Na wakati mwingine wa mchana tusingepata muda wa pamoja kama ningekuwa nikiwasiliana na kila mfanyakazi. Ndio maana Grace anahusika na kina Mira au wafanyakazi wote pale, mimi nafanya mambo yangu mengine labda Grace awe likizo kama hivi, ndipo atataka nimfanyie baadhi ya mambo, lakini pia hata akiwa nyumbani, anafanya mambo yake mwenyewe na ndio maana ulimuona Mira pale nyumbani siku ile ya kikao, alikuja nyumbani jana yake kumfuata Grace.”

“Ndio Grace anasema akamkaribisha kesho yake kwenye kikao baada ya Mira kuulizia yale maandalizi pale nyumbani. Lakini sio mimi.  Yaani kina James walipotoka kanisani siku ile ya kikao. Kuzungumza na mchungaji na Zinda. Ndio waliokuja kunishangaza nakunifanya nianze kukumbuka mambo ya Mira. Nilishasahau kabisaaa.” Nanaa hakuelewa.

“Sielewi Geb.” “Unakumbuka siku ambayo ndoa yetu ilitangazwa kanisani halafu Zinda na mama yako mkubwa wakaipinga?” “Nakumbuka.” “Si unakumbuka kesho yake mama akaomba kikao ili wamsikilize Zinda na kumlipa mama yako mkubwa pesa aliyokuwa akidai?” “Nakumbuka.” Nanaa akaitika kwa unyonge. “Basi ndio siku Zinda aliposimulia kuwa Mira ndiye anayekufanyia mambo yote hayo. Kwa kuwa umemchukulia mume, ambaye ndio mimi. Niliwasihi kina James wasikwambie kwanza, wakuache. Niliwaambia tutakutoa mawazo yako kwenye kumtazama Mungu, ukabakia na mawazo ya Mira. Nikawaambia ukweli wote juu yangu na Mira. Na nikawaambia Mungu atatushindia. Ipo siku nitakwambia. Lakini sio ukiwa kwenye ile hali.” Geb akaendelea.

“Wakanikubalia. Unakumbuka nilikupeleka Morogoro?” Nanaa akanyamaza na kuinama. “Nilitaka kupata muda na wewe Nanaa, lakini pia nilitaka kukwambia juu ya habari za Zinda na Mira. Niliishia kukwambia habari za Zinda tu, kwa kuwa unakumbuka mwenyewe jinsi ilivyokuwa.” Nanaa akanyamaza. Alikumbuka jinsi alivyokuwa amepaniki. Alilia. Hata chakula kilimshinda. Ni kweli Geb asingeweza kuongeza habari nyingine tena.

“Sikutaka kukuudhi zaidi Nanaa. Kumbuka na mimi ulinihesabu kama msaliti wako. Ukaona nawatetea watu waliokuumiza. Lakini Nanaa, nia yangu ilikuwa njema tu. Nilikuwa nataka amani. Nilijua wamekosea wao kama binadamu. Lakini sikutaka mgombane. Nilitegemea ungeumia. Lakini mimi ndio ningekuwa kimbilio lako kwa kuwa nimekwambia. Lakini ikawa tofauti. Nikaogopa kukupa habari za Mira kwa haraka. Nikaona nikuache kwanza. Mpaka utulie. Urudishe imani yako kwangu kama leo, ndipo nikwambie habari za Mira. Lakini jua hakujawahi kutokea mahusiano kati yetu. Na Mungu wangu ni shahidi. Neno la kumkubalia kuwa nitamfikiria nitakapokuwa tayari kuoa, ndio anasema niliingia agano naye na mizimu imejua kuwa nimemkubalia kuwa mimi ni mume wake.” Nanaa aliyekuwa ameinama kwa aibu, akainua macho kwa mshangao.

          “Anasema mimi na yeye tuna ndoa ya mizimu. Kwa hiyo ndipo aliposimamia hapo.” Geb akatulia huku akimwangalia Nanaa. “Umenielewa?” Geb akamuuliza. Nanaa akatingisha kichwa kukubali. “Nataka kujua kama umenielewa na kuniamini Nanaa. Hilo ndilo la msingi na nguvu yangu. Siwezi kufanya chochote, bila wewe kuwa upande wangu. Nazidiwa vita. Kwa kuwa najikuta nipo peke yangu bila wewe. Umoja wetu, ndio nguvu yangu. Kunapotokea tatizo, halafu unanikimbia mimi, ujue unaniathiri vibaya sana Nanaa. Nataka uniambie kama umenielewa.” “Nimekuelewa Geb. Na ninaomba unisamehe. Nilikukimbia.” “Ulikimbia, lakini ukanitafuta. Hilo limenifurahisha sana. Hujui tu.” Geb akambusu midomo yake kwa kifupi tu. Akamwangalia na kumfuta machozi. “Asante.” Nanaa akashukuru.

“Swala la Zinda na Mira ndilo ninalotaka kujua kama umenielewa na kuniamini. Kwanza ujue inapokuja swala la kuchagua, wewe utakuwa wa kwanza. Kwa namna yeyote ile Nanaa. Wewe ndio utakuwa wa kwanza.” Ilimgusa sana Nanaa. “Na katika swala la kusema kweli. Ujue ni kwako tu ndipo nitakapojificha uso wangu. Nitasema ukweli wote bila kificho ili ujue ni jinsi gani utanisitiri. Sina kimbilia jingine ila wewe Nanaa.” Nanaa akajifuta machozi. “Nimekuelewa na ninakuamini Geb. Samahani nilikukasirikia tulipokuwa Morogoro. Nilipaniki. Sikutegemea.” “Basi yaishe mpenzi wangu.” Akaanza kumbusu midomo yake. Akashuka  shingoni. Akambusu shingo nzima. Tena kwa kurudia rudia. Mwili mzima wa Nanaa ulikuwa ukisimkwa kwa yale mabusu ya mfululizo. Akamgeuzia uso, Geb akapokea midom, nakuanza kuifanyia kile kitu Nanaa anapenda. Wakahamia kitanda cha jirani. Geb akakata kiu zao, wakabaki wamekumbatiana hapo kitandani Geb akichezea maziwa yake taratibu ila si chuchu kuepuka kuzisisimua na kutoa chakula cha Liv. Nanaa alipenda sana jinsi alivyokuwa akishika maziwa yake, ilimfanya atulie kabisa akisikilizia raha yake.

~~~~~~~~~~~~

          “Sasa itakuje Geb?” Baada ya muda akauliza. “Kwanza ule. Nimeona vyakula pale hata hujagusa! Ukiendelea hivyo utajiumiza Nanaa. Kumbuka sasa hivi unaishi kwa ajili yako na huyo mtoto huko tumboni. Na Liv pia anategemea maziwa kutoka kwako. Lazima uhakikishe unakula vizuri na kushiba.” Geb akatoka pale kitandani. Akammiminia mtori. Bado ulikuwa wa moto vile vile. Akampelekea pale kitandani. “Asante.” Nanaa akashukuru wakati akipokea bakuli la mtori. “Karibu.” “Na wewe umekula sasa?” Nanaa akauliza. “Wewe unajua siwezi kula kama haupo au tukiwa hatupo kwenye maelewano Nanaa. Nashindwa hata kujifikiria.” Nanaa akamuhurumia.

“Nisamehe Geb. Niliingiwa na hofu. Nikaona heri mmoja wetu alipe garama ili kumnusuru Liv. Kumbuka kile alichonitenda Mira! Sikutaka kimpate na mtoto. Nikaona ni heri niondoke tu. Nikajua akipata habari kuwa nimeondoka, ataacha kumfuatilia mtoto wangu.” “Nilikuomba tuwe tunazungumza Nanaa. Ukipata kitu chochote kinachotaka ufanye maamuzi, naomba unihusishe na Mimi. Usichukue hatua peke yako bila mimi.” “Samahani Geb. Niliingiwa na hofu ya kupita kiasi. Nitajitahidi kufanya hivyo.” Wakatulia kidogo. 

“Naomba basi na wewe ule.” “Huo mtori sitauweza Nanaa. Nimeona karoti na maganda ya nyanya vinaniangalia kabisa. Siwezi.” Nanaa akacheka huku akimtizama. “Basi labda nikutolee hivyo vitu.” “Mmmh! Kwani siwezi kuagiza chakula hapa?” “Utakula?” Geb akacheka. “Ngoja nijue MENU yao kwanza. Ndipo nitajua chakuagiza. Kwanza muda umeenda sana.” “Lakini lazima ule Geb.” Geb akacheka huku akiiendea simu ili kuwapigia watu wa mgahawani. Akapata kitu anachotaka kula. Akaagiza kiletwe huko chumbani pamoja na chips yai ambayo haijakauka sana, na nusu kuku. Nanaa akacheka. Akajua ameagiziwa tu yeye.

Ukipenda Boga.

“Sasa itakuaje?” Swali hilo Nanaa alilikazania, akitaka kujua hatima yake. “Kwanza nataka ujue hivi.” Geb akarudi pale kitandani. “Adui au niseme shetani, anapenda sana kuishi sehemu isiyo na amani. Baba yangu alinifundisha kuwa, amani inamtindo wa kukaribisha kila kitu chema ndani ya nyumba. Na ikiondoka, pia inamtindo wakuondoka na kila kitu chema. Wakati mwingine mpaka utajiri.” Nanaa akaelewa kile anachotaka kuongea Geb.

“Najua mama amekuumiza Nanaa. Naomba msamehe. Namuombea mimi msamaha. Amekosa, naomba msamehe. Na kama huna sababu yeyote ya kumsamehe mama, basi naomba iwe mimi. Msamehe kwa ajili yangu. Naomba yaishe.” Nanaa akajisikia kuumia zaidi moyoni. “Nimesamehe Geb. Japo ni kweli sikutegemea! Lakini basi.” Geb akajiweka sawa. 

“Naomba usinifikirie kuwa namtetea. Nataka kukwambia ukweli Nanaa. Mama anakupenda sana wewe. Aliyasimulia hayo yote, akitaka kuonyesha ubaya wangu kwa Grace baada ya kufika nyumbani, kumkuta mtoto halafu wewe haupo, umelala hotelini sababu nilikupa masharti ya kutorudi nyumbani ikishavuka saa 12 jioni. Mama alikuwa akikutetea. Grace alichukia sana. Yaani wote, mpaka Danny, walinisema usiku ule mpaka nikajisikia vibaya. Wale watu wanakupenda sana Nanaa. Hakuna hata mmoja wao anae kuchukia.” “Basi Geb. Yameisha. Nitatafuta kuzungumza na mama pamoja na Danny pia.” “Hapo utakuwa umefanya vizuri. Nakushukuru.” Geb akatulia.

Suluhisho la Mira.

“Tukirudi kwenye swala la Mira. Huyo ni lazima nikaonane naye. Ameacha kuja kazini. Hata leo hakuja kazini. Nitaulizia nyumbani kwake, nita...” “Geb!” Nanaa akashangaa. “Itabidi kufanya hivyo Nanaa. Sina jinsi. Yapo mambo yakuombea na kumuacha Mungu afanye. Lakini yapo mambo inabidi kumruhusu Mungu kutenda kupitia wewe mwenyewe. Huyu binti anasema yupo kwenye ndoa na mimi kwa ahadi niliyomuwekea mimi mwenyewe. Sasa nilazima nizungumze naye, tuwekane sawa.” “Naogopa Geb!” Nanaa alishaweka mpaka bakuli la mtori chini, kwa hofu.

“Akikurushia tena madudu yake!?” “Hana nguvu hiyo tena. Nimekwambia. Hakuna silaha itakayoinuka kinyume yetu, ikafanikiwa tena. Mungu ameahidi kupigana vita yetu. Alipigana naye au alipigana na madudu aliyokuwa amekutupia, mpaka ameshinda. Mungu alikuletea ushindi pale pale hospitalini. Sasa unafikiri ni nini alichobakisha kama sio sisi kuendelea kutenda kazi pamoja naye?” Geb aliongea kwa kujiamini sana mpaka Nanaa akaanza kutulia.

“Kuna kitu Grace amekiongea leo. Anasema hadhani kama Mira yupo sawa. Anasema siku ya kwanza ulipokuwa hospitalini alikuwa na furaha sana pale kazini. Alikuwa akicheka, akiwa chini mpaka mtu wa juu anasikia. Lakini siku ya pili yake, alifika kazini kama mgonjwa. Na hajarudi tena. Sasa huwezi kujua vita hiyo aliyopigana na malaika wa Mungu alishindwa kwa namna gani! Hutujui yupo kwenye hali gani!  Halafu wanasema yale madudu yanamtindo yakurudia watu. Sasa ukute ubaya aliokutendea wewe, ndio umemrudi na yeye. Sasa hivi anatapatapa.” “Akirudi huku anakulilia shida? Au umkute mgonjwa ukamuhurumia? Labda hana kazi anahitaji msaada wako? Halafu anakukumbusha vile alivyokusaidia nchini India?” Nanaa akauliza.

“Nanaa! Nina jukumu mimi kama baba na mume. Nikishindwa kuwalinda nyinyi, ujue sistahili kuitwa baba wala mume. Sitaruhusu historia yangu ya nyuma iwaathiri watoto wangu wala wewe. Nahangaika ili nyinyi msipite nilipopita mimi. Siwezi kumruhusu tena kuwa karibu na nyinyi. Hata iweje. Kwanza nikirudi tu Dar, nitakwenda polisi.” “Geb!” Nanaa akashangaa.

“Kabisa Nanaa. Nitaenda kumshitaki kwa vitisho vyote alivyokutumia. Na kuomba ‘restraining order’ juu yake. Kwako na kwa familia yangu. Nitamfuata nikiwa na hiyo ‘restraining order’. Nitampiga marufuku na kumwambia, chochote kibaya kitakachokupata wewe, watoto wangu na ndugu zangu wote, yeye ndio atakuwa mtu wa kwanza kukamatwa.” “Akikuomba msamaha je?” “Nitamsamehe au nilishamsamehe tokea siku nilipojua amekutendea wewe ubaya. Lakini haibadilishi chochote kile. Bado sitamruhusu kuwa karibu yetu. Nitampiga marufuku na kumwambia wazi kabisa. Jumbe zake za vitisho na picha zote za mwanangu alizochukua ofisini kwangu bila ruhusa yangu, vimehifadhiwa polisi na kutaarifu vyombo vya usalama kuwa, chochote kitakachotupata sisi, yeye ni muhusika. Hata kazini au kwenye ofisi zangu, hataruhusiwa tena kusogea. Nikimuona tu, au nikiambia alionekana karibu na nyumbani kwetu au jengo letu lolote, nitamwakikishia atakuwa hatiani.” Nanaa akaridhika. “Asante Geb. Angalau moyo wangu umetulia.” Nanaa alisikika ametulia kweli kweli.

Suluhisho Juu Ya Zinda

Akamuona amekunja uso kama amekumbuka kitu. “Nini?” Geb akauliza. “Itakuaje juu ya Zinda?” Wakasikia mlango wao unagongwa kabla ya Geb kujibu. Geb akajua wanaletewa chakula. Akasimama. Akavaa rob  nyingine iliyokuwa imening’inizwa, akaenda kufungua mlango. Alikuwa muhudumu aliyekuwa amevalia nadhifu, na sinia la vyakula. Geb alipokelewa na tabasamu. “Naomba uweke hapo mezani tafadhali.” Geb akampisha mlangoni, yule muhudumu akapita. Harufu ya chakula, ikaanza kuenea hapo ndani. Nanaa akasimama.

“Kunanukia vizuri!” Geb akacheka. Alimjua Nanaa jinsi anavyopenda kula. Geb alimpa pesa kidogo yule muhudumu aliyeleta chakula. Ilikuwa tip nzuri iliyoonyesha kumfurahisha huyo muhudumu. Alitoa shukurani kwa Geb kwa kurudia rudia huku akisisitiza kama watahitaji kitu chochote, wasisite kupiga simu mapokezi na kumuulizia yeye, huku akirudia rudia kujitambulisha jina lake kwa kirefu na kifupi. Geb akashukuru tena, akatoka.

Akaenda kukaa kwenye kochi alilokuwa amekaa Nanaa. “Umeuliza juu ya Zinda. Niwe tu muwazi Nanaa, sijapata jibu. Sijajua nifanye nini juu ya Zinda. Ananisumbua kichwa changu, kwa kuwa nahisi kwa mara ya kwanza maishani mtu wa karibu yangu, anahusika katika kukwamisha mpango wangu. Au niseme, kwa mara ya kwanza maishani napanga mpango wa muhimu sana, uliobeba hatima yangu. Mpango uliojaa furaha yangu, naona unakwama. Na mbaya zaidi sijui chakufanya. Nimebaki kumuomba tu Mungu.” Nanaa alianza kunywea.

“Kwa hiyo hudhani kama tutafunga tena ndoa yetu?” Nanaa akauliza. “Sina mpango wa kumfikisha mwanamke mwingine yeyote yule kanisani na kumpa kiapo changu cha maisha au niseme sina mwanamke mwingine nitakayeweka naye agano la mpaka kifo, isipokuwa wewe Nanaa. Lakini sijui lini!” “Kwa nini tusiende kwenye vyombo vya sheria?” Nanaa akahoji. “Nimezungumza na mwanasheria. Nimemtumia mpaka picha ya kile cheti cha harusi ambacho Zinda anasema mlifunga ndoa. Yule mwanasheria akasema cheti kinaonekana ni halali, lakini tunaweza kumshitaki na kumkana. Kesi itapelekwa mahakamani na wewe utatakiwa kuonyesha ushahidi wako, kumpinga. Yeye anao mashahidi wa muhimu sana. Mwanamke anayetambulika kama mama yako, yuko upande wake. Achilia mbali huyo mama yako mkubwa, kina Viola pia wapo upande wake.” “Lakini na mimi nina ushahidi wa hospitalini! Kuwa siku ile nilikuwa kwa daktari.” Nanaa akaongeza.

“Nilimwambia hivyo huyo mwanasheria. Akasema inawezekana ukawa ushahidi. Au Zinda akatengeneza stori nyingine.” “Stori gani tena!?” “Nanaa, hivi unajua hapo Nairobi ni karibu sana? Na wala huhitaji Visa, au masaa mengi kufika hapo. Na kufungishwa ndoa hakuchukui muda mrefu. Hata dakika 15 ni nyingi. Mnaweza mkafungishwa ndoa na kurudi hapa nchini siku hiyo hiyo. Kwa hiyo anaweza kusema mlikwenda na kurudi.” Nanaa akapooza na kuishiwa maneno.

“Wewe ni mjamzito. Sitaki uanze kuhangaika mahakamani, unashindana na watu waliokusudia kukuangamiza Nanaa. Sitaki tena upitie kwenye kelele za kina Viola. Sitaki ile hali ya kunyanyasika, ujisikie wanakuonea maishani, ikurudie tena. Halafu sasa hivi iwe mahakamani, mbele za watu! Sidhani kama hata na wewe upo tayari kwa hilo. Sasa hivi tuna watoto, tupo pamoja, kitu kinachowaumiza wao. Ni mke wangu kihalali kwa kuwa nimeshakulipia mpaka mahari, na Mungu anajua.” “Na hicho ndicho nilijua kitatokea tu Geb. Tukishazaa ndio basi tena.” Nanaa aliongea kwa kulalamika kidogo.

“Hivi unafikiri ni wewe peke yako ndio unahamu ya ndoa? Au unafikiri unaweza ukanizalia watoto hawa, halafu nikaamua kuwatafutia wanangu mama mwingine!?” Nanaa akajifuta machozi. “Siwezi kufanyia hivyo wanangu wala nafsi yangu. Kwanza natafuta nini tena? Mwenzio katika swala la kutafuta mwanamke nimeshafunga hiyo shuguli. Kicho kipengele nimeshakitia tiki. Nimekimaliza. Sasa hivi nasonga mbele. Labda kama wewe mwenzangu bado unaangalia nje.” “Hapana Geb!” “Basi nakuomba tuwe wavumilivu tu kwa sasa. Tutunze kile Mungu alichotubariki nacho, huku tukimsihi atuvushe katika hili. Siku moja tuje kufunga ndoa. Lakini kwa sasa naomba tufurahie hii baraka Mungu aliyotupa. Upendo wa kweli katikati yetu. Jinsi alivyotuamini na kutupa watoto. Tufurahie uwezo aliotupa wa kuzungukwa na watoto wetu wenyewe wa kuwazaa. Mungu anajua nia yetu Nanaa. Hajawahi kushindwa. Na ninauhakika hana mpango wa kuanza kushindwa kwenye mambo yetu. Zaidi katika hili la ndoa. Maana mengine yote, ametuonyesha mkono wake upo juu yetu. Tusubiri tu.”

“Nitasubiri Geb. Na ninashukuru kwa kuanza kulifuatilia hata huko kwa mwanasheria. Na kunifikiria na mimi kutosimama mahakamani na kuendelea kudhalilishwa na mama mkubwa na watoto wake. Asante.” Nanaa akashukuru kwa upendo, Geb akajisogeza, na kumbusu begani.

~~~~~~~~~~~~

Kwa akili zao, wapenzi hao wamefika mwisho. Hawajui tena watafanya nini juu ya ndoa yao. Wamebanwa kila upande. Mazingira yote yamesema hapana kwa kuhalalisha ndoa yao. Nini kitaendelea? Hata jaribu hilo nalo aliokusudia shetani, kuwasambaratisha, ameshindwa.

Pengine Amani itarejea kwa kina Magesa kwa kuwa Nanaa amekubali kusamehe, lakini mambo mengine je?

Amani Hutafutwa Kwa Nguvu Ikiwemo kujishusha, na wakati mwingine hata kukubali mambo yaishe.

Itakuaje Mbeleni?

Mengi, Mazito yanakuja mbeleni.

Usiache kufuatilia.

 


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment