Nanaa alikuwa amejifunika shuka
amelala. Geb na yeye akavua nguo akapanda kitandani. Akamsikia analia taratibu.
Akajisogeza karibu naye. Kwa kuwa alikuwa amegeukia ukutani, akajinyanyua mpaka
kwenye masikio yake. “Nakupenda Nanaa! Amini ninakupenda na ninathamini kila
muda Mungu anao nijalia kuwa na wewe. Unisamehe pale nilipoonyesha upendeleo
wowote. Nia yangu ni kuhakikisha kuna amani. Najua mama anakupenda kwa hakika.
Ila kuna maisha ambayo tulikuwa tukiishi zamani, hapakuwa na usiri kati yetu.
Nahisi ni udhaifu wetu. Na wote wamejifunza kwa hiki kilichotupata. Ndio maana
unaona ni kama pale nyumbani amani imepotea. Danny anajilaumu sana. Nilichokuwa
nikitaka kutoka kwako ni uwasamehe, yaishe. Sikuwa na nia yakuwatetea. Hata
mimi nimeathirika Nanaa. Wamechangia kwa asilimia kubwa kusimamishwa kwa harusi
yetu. Lakini namuamini Mungu, atatufanikishia tu. Naomba usinichukie. Nipo
upande wako mpenzi wangu. Sipo kinyume na wewe.” Nanaa akanyamaza. Geb alimuona
anajifuta machozi, bila kujibu kitu. Akambusu shingoni na kujivuta zaidi karibu
yake, akamkumbatia.
~~~~~~~~~~~~~
Nia ya Geb ilikuwa kuzungumzia
mambo mawili. Juu ya hilo la Zinda, Danny na Mama yake, pamoja na la Mira.
Lakini kwa jinsi Nanaa alivyopokea habari za watu walioshiriki kutoa habari za
ndani na kumpa Zinda, akaona habari za Mira zisubiri kwanza. “Hata malaika alishindwa kumwambia. Heri na
mimi ningojee kwanza. Nisije nikaharibu zaidi.” Geb akawaza. Akaamua
kulala.
Usiku huo hapakuwa na mapenzi
wala busu. Hapakuwa na kuomba pamoja wala Geb hakukumbuka kuomba peke yake.
Tayari na yeye alisha changanyikiwa na shutuma alizotupiwa na Nanaa. Nanaa
alimuweka na yeye kwenye kundi la wasaliti wake. Hakumuhesabu upande wake kitu
kilichomuumiza na kumchanganya Geb zaidi. Mpaka Nanaa analala, amekiri kwake
ile safari yote aliyokuwa akiifurahia pale mbugani, akidhani ilikuwa kwa ajili
yake ili kumfurahisha, kumbe nia ilikuwa kuja kutetea familia yake. Hilo nalo
lilimuumiza Geb. Inamaana furaha yote aliyojenga moyoni mwa Nanaa kwa siku tatu
mfululizo, imefutika!
~~~~~~~~~~~~~
Nanaa aliamka asubuhi na mapema.
Hiyo ilikuwa siku ya 4, tokea wafike hapo. Ilikuwa ni siku ya jumapili. Geb
akamsikia, amekaa kitandani. “Mbona mapema hivyo?” Akauliza. “Si ulisema
tunaondoka leo? Ndio nakusanya vitu. Samahani nimekuamsha.” “Hamna neno.
Nilifikiria tuondoke hata jioni.” “Kwani kuna kitu kingine tena unataka
kuniambia?” “Nanaa!” Geb aliumia zaidi. “Nauliza tu!” “Sikukuleta huku kwa
ajili ya kukupa habari zitakazo kuumiza! Nilitaka muda na wewe.” “Naomba
usinidanganye Geb.” “Sawa. Nilitaka tuje tuzungumzie na hilo pia. Lakini zaidi
nilitaka muda na wewe.” “Basi nitakuwa hapo nje. Nataka nitembee tembee kidogo
wakati nyinyi mmelala. Nitarudi baadaye kidogo.” Geb akajirudisha kwenye mto,
akafunga macho.
Nanaa alisimama pale kwa muda.
Geb hakuwa amesema ndiyo au hapana. “Geb! Natoka nje.” Akamgeukia. “Nakuhitaji
Nanaa.” Akamuona Nanaa anavua nguo zote, anarudi kitandani. “Sio kwa namna hiyo
Nanaa! Kufanya mapenzi na mimi sio lazima. Sitaki uone unawajibika. Si jukumu
unalotakiwa kulitimiza kwangu. Na nikikwambia nakuhitaji sio kwamba nakuhitaji
kufanya mapenzi. Nakuhitaji kwenye maisha yangu.” “Sawa.” Nanaa akapanda
kitandani, akajifunika shuka, akatulia.
“Nanaa!” Nanaa akageuka, machozi
yakimtoka. Akajifuta. “Abee!” “Pole.” Geb
aliongea kwa upole na upendo. “Pole sana. Lakini naomba tusitengane sababu ya
makosa ya watu wengine. Naomba usinichukie. Kumbuka na mimi nimuhanga wa hayo
makosa. Harusi ilikuwa ni yangu pia. Ninataka sana kukuoa Nanaa. Nakuhitaji
kwenye maisha yangu.” “Sijakuchukia Geb. Ila nimeumia sana.
Sikutegemea. Nilijua nimepata mtu wa kumueleza chochote kinachoendelea kwenye
maisha yangu au hata moyoni mwangu. Nimeumia kujikuta narudi kuishia kuwa na
kaka tu! Maisha yangu yameshindwa kabisa kuniongezea mtu mwingine!?” Geb alizidi kuumia. Akaona hata yeye
hakutajwa hapo. “Pole.” Ndilo neno aliloweza kujibu akiogopa kuongeza neno
jingine asije haribu.
Nanaa alipanda kitandani kwa
hasira akiwa uchi kabisa. Kama aliyekuwa akitaka kutimiza wajibu. Lakini Geb
akamtuliza. Alimsogelea karibu, akambusu kidogo tu shavuni. “Pole sana.”
Akabaki akimwangalia. “Asante.” Akamfunika
shuka vizuri. Nanaa akashangaa anajilaza kwenye mto bila hata kumpapasa. “Njaa
inakuuma?” Akamuuliza. “Hamu ya kula imeisha kabisa. Nasikia tumbo limejaa.
Sina hamu ya kuweka kitu chochote mdomoni.” Geb akajua bado ana hasira. “Basi
tulale kidogo. Labda ukiamka utasikia njaa. Na sio lazima tule hapa. Tunaweza
kwenda kula sehemu nyingine. Jaribu kupumzika.” Mikono ya Geb ilikuwa juu ya
shuka. Akamtengeneza lile shuka vizuri. Kama anayemtayarisha kulala. Nanaa naye
akajiweka sawa, akarudi kulala.
~~~~~~~~~~~~~
Waliamshwa na Oliva saa 4:37asubuhi. Alikuwa akiongea
huku akipuliza. Nanaa akacheka. “Fizi zinamuwasha huyo!” “Naomba ukaongee naye
kidogo. Jana alijua nimekuudhi. Hakutaka hata kunichekea!” Nanaa akatoka. Alipomuona
tu mama yake akaanza kucheka. Akakaa. “Na mimi nina hamu na wewe Liv!” Geb
akamsikia anacheka. “Ulilalaje?” Liv aliendelea kucheka. “Njoo upate nyonyo
kwanza.” Akamtoa pale kitandani. Akambusu. “Muone unavyotokwa mate! Meno
yanataka kutoka ndio maana fizi zinawasha Liv. Pole kipenzi chagu. Ukinyonya
nitakupa ile toy yako yakukunia fizi. Sawa?” Oliva alizidi kumchekea mama yake.
“Unapendeza ukicheka wewe! Usiwe unanuna bwana. Umesikia Liv?” Geb alisikia
wakizungumza. Akabaki akiwaza pale kitandani.
Alijua kwa hakika Nanaa ameumia
sana. Maisha yatakuaje baada ya hapo kati yake na mama yake! Ndio kitu kikaanza
kumuumiza kichwa. “Nanaa atarudi kuwa
rafiki wa karibu tena wa mama?” Geb akawaza. Kwa ukaribu aliokuwa nao Nanaa
na Mama G, ungependa tu uwepo nyumbani kwao. Vilijaa vicheko kila wakati. Nanaa
alikuwa akiishi na mama G kama rafiki yake wa karibu wala si mkwe. Alifanya
chochote mbele yake bila hofu. Ukiwakuta pamoja, ungeweza kufikiri Geb ndio
mkwe halafu Nanaa ndiye kiziwanda cha Mama G. Oliva alilelewa na bibi yake kwa
mapenzi makubwa sana. Lakini hapo napo kukatupwa jaribu lake.
Geb akaendelea kuumia. Alichukia
ile hali. Wasiwasi ukazidi kumtesa. Kwa Danny haikumsumbua. Nanaa hakuwa karibu
sana na Danny, lakini si mama yake. Akabaki akiwaza. Akamchukia shetani na kazi
zake zote. Hakuacha wapumzike hata kidogo! Ni jumapili iliyopita tu, siku kama
hiyo, Nanaa aliamka na miguu iliyoharibiwa vibaya sana. Huwezi kusema imeoza,
kwa kuwa haikutoa harufu. Lakini na jumapili hiyo nayo, wameamka wakiwa
wamesambaratishwa mioyo. Nanaa hakumuhesabu upande wake. Akazidi kuumia.
Akachukia visasi alivyovianzisha Zinda. Swali la atafanyaje likaanza kumsumbua.
Akajua kama harusi haitafanyika kwa haraka, ndio Nanaa ataona madhara yake
zaidi.
~~~~~~~~~~~~~
“Twende ukamsalimie dad.” Wakamtoa Geb kwenye
mawazo. Nanaa akaingia na mtoto wake pale chumbani. Hapakuwa na mlango. Kwa
hiyo alipitiliza na kumuweka Liv kifuani kwa baba yake pale alipokuwa
amejilaza. Oliva akaanza kumchekea. “Unatoa tu maziwa!” Geb akamfuta. “Naona
alikuwa na njaa. Amenyonya kama anakimbizwa!” Nanaa na yeye akajiweka pembeni.
“Au ulikuwa na hamu na mama?” Geb alimtekenya kwa kuweka kidole chake kwenye
dimpozi yake.
“Halafu fizi zinamuwasha. Anahangaika
kweli!” “Hivi tulikumbuka teething toys zake?” Geb akauliza. “Nilibeba. Sema
zile anazozipenda, zakuweka kwenye friji ndio niliacha. Nilijua huku hakutakuwa
na friji.” Nanaa akajibu huku akimfuta maziwa na mate yaliyokuwa yakimtoka
Oliva. Meno ya mbele mawili ya juu na chini yaliyokuwa yakimpendeza sana Liv,
yalishatoka tangia anatimiza miezi mitano. Geb akasimama akiwa amemkumbatia
mwanae. “Twende tukafuate toys zako nyingine utafune.” Nanaa akaamua kuvaa.
Alikuwa amejifunga khanga wakati ameenda kumfuata Liv.
Geb alimuona akivaa. Akatamani
aombe penzi la mwisho hapo hotelini, lakini akaamua ajikaze tu. Na yeye Nanaa
akajiuliza mbona haombwi tena! “Naona nivae kabisa, ndipo nimuhudumie na Liv.”
Akajisemesha akitarajia kuambiwa subiria. “Sawa. Wakati unamvalisha yeye, na
mimi nikaoge. Ndipo tukapate kifungua kinywa.” Geb akajibu. Nanaa akatulia
kidogo. “Kwani ulitaka tuondoke saa ngapi?” “Najua hamu ya kukaa huku na mimi,
imeshakuisha.” “Hapana Geb.” “Naelewa Nanaa. Sikulaumu. Muda wowote utakaotaka
tuondoke, tunaweza kwenda tu.” Nanaa akanyamaza. Hakujua ajibu nini.
Dar.
Waliingia jijini mida ya saa kumi
jioni. Mlinzi akafungua geti bila kuchelewa. Lakini hawakukuta magari ya watu
wengine ila ya Geb. Hapo hapo Geb akampigia simu mama yake. “Uko wapi!?” “Kwa
Grace. Namsaidia kuweka mambo sawa. Walirudi kwao jana. Sasa namsaidia usafi,
kupika na mambo mengine. Nitarudi kama kwenye saa moja hivi. Vipi nyinyi?” Mama
G akauliza. “Salama. Lakini sikujua kama kina Grace wataondoka mama! Hajaniaga!”
Geb alilalamika kidogo. “Mwache mwinzio atulie kwake. Ulitaka akae hapo mpaka
lini?” “Naona ni mapema sana mama.” “Hivi unajua huyu Grace ni mke wa mtu?
Mwache ajenge kwake.” “Watoto watatu bila mtu mwingine!?” Geb aliendelea
kulalamika. “Ndio kukua huko. Tutaongea vizuri baadaye.” “Kuna kitu mnataka
niwasaidie nije?” Geb akauliza. “Sidhani. Kama kipo watakupigia. Lakini wewe
pumzika na familia yako. Mimi nitarudi kwenye saa moja.” “Usichelewe sasa mama!”
“Umeanza Geb.” “Naomba usichelewe.” Nanaa alikuwa akiwasikiliza bila ya
kuongeza neno.
Alikuwa amekaa kiti cha nyuma na
mtoto wake, akamtoa. Liv akafungua macho. “Bado una usingizi?” Nanaa
akamuuliza. “Twende ukalale na mama.” Alimbeba mtoto wake mpaka juu chumbani
kwake. Akambadilisha diaper na nguo, akapanda naye kitandani. Geb akamkuta
amemkumbatia Oliva wamelala. Kitu ambacho sio cha kawaida. Liv alishazoezwa
kulala peke yake, kitandani kwake. Kitanda hicho ni cha Geb na Nanaa tu.
Akilala hapo Oliva ni mara chache sana, tena wanacheza na baba yake tu. Hata
mchana alilala kitandani kwake.
Geb akabaki amesimama pale
akimwangalia Nanaa na mtoto wake. Akaamua anyamaze tu. Akaenda kujilaza kwenye
makochi. Usingizi wa mimba ulimchukua Nanaa, akalala kama mzigo. Alilala akiwa
na mawazo. Na ni kweli alipoteza hamu ya kula kabisa.
Geb alimuasha ilikuwa saa mbili
na nusu usiku. Akaangalia pale kitandani Oliva hakuwepo. “Twende ukale.” Geb
alimuongolesha kwa upendo. “Nataka nioge kwanza. Najisikia mwili umechoka
sana.” “Pole. Labda safari. Ukioga utajisikia vizuri.” Nanaa akajitoa pale
kitandani kwa shida, akaenda kuoga. Alipotoka bafuni, Geb hakuwepo pale
chumbani. Akaamua arudi tu kulala. Hakujua akitoka pale chumbani, ataenda
kuongea nini na mama G. Akaona ni heri arudi kulala tu.
Alipojiweka tu kitandani,
akapitiwa tena na usingizi. “Nanaa!” Geb akaingia tena na kumuamsha. “Amka
ukale japo kidogo. Mama amerudi na chakula.” “Sijisikii vizuri Geb. Naomba
nilale tu. Nitakula kesho.” Nanaa ambaye alikuwa hashibi masaa machache
yaliyopita, gafla hawezi kuweka kitu
mdomoni. Hataki tena kula. “Jikaze kidogo tu.” “Nina usingizi sana. Nataka
kulala tu. Ila naomba uniletee Liv aje anyonye kabla ya kwenda kulala.”
“Sidhani kama ataweza kunyonya. Bibi yake alimpikia ndizi. Amezisaga na samaki.
Nimemlisha, naona amekula sana.” Nanaa akacheka kidogo. “Basi kesho. Naomba
nilale.” Geb akabaki amesimama pale kwa muda. Nanaa alishafunga macho kuashiria
anataka kupumzika sio tena maongezi. Baada ya muda akamsikia Geb anatoka.
Jumatatu.
Akiwa usingizini, kwa mbali
akasikia busu la mdomoni. Nanaa akafungua macho. “Nataka kwenda kazini.” “Kwani
sasa hivi ni saa ngapi?” Geb akacheka. “Saa moja asubuhi.” Nanaa akakaa kwa
haraka. “Sasa umekula nini!?” Nanaa alipitiwa na usingizi, hata uji wa Geb
hakuamka kuupika. “Mama alishaniandalia.” “Samahani nimepitiwa na usingizi.”
Geb akambusu. “Usijali. Ila uamke hapo kitandani ukale.” “Nitaamka. Maziwa
yamejaa, nataka nioge, Liv akiamka anyonye.” “Basi toka hapo kitandani sasa
hivi, lasivyo utapitiwa tena na usingizi.” “Nitaamka. Kazi njema.” “Nitarudi
mchana tuje tule wote.” Nanaa akatulia kidogo.
“Unataka nikuletee nini?” Geb
akauliza. “Nimepoteza hamu ya kula kabisa Geb. Sijisikii kula hata kidogo!”
“Labda ni hiyo hali ya ujauzito.” Geb akamshika tumboni. “Labda. Nitamtafuta
yule daktari aliyenisaidia wakati wa ujauzito wa Liv.” “Naomba na mimi
unishirikishe kwa karibu Nanaa. Nataka tuwe tunakwenda wote.” Nanaa akacheka
kidogo. “Sawa. Uwe na siku njema.” Geb akambusu tena, na kutoka.
~~~~~~~~~~~~~
Aliingia kuoga. Akasafisha meno,
ndipo akashuka huku akiwaza kukutana na mama G. Hakuwa amemuona tokea watoke
safari. Alimsikia akiimba jikoni. Akaingia. “Shikamoo mama.” Hapakuwa na
tabasamu wala kicheko. Salamu hiyo aliitoa Nanaa akiwa mlangoni, tena amepooza
sana. “Marahaba Nanaa mwanangu. Umeamka salama?” “Ndiyo.” Nanaa akajibu, kisha
akanyamaza. “Kaa ule.” “Asante.” Nanaa akaingia ndani. Akasogea mpaka kwenye
jiko. Akamimina uji aliokuwa amepikiwa Geb. Akaweka kwenye microwave ili
kupasha. Mama G akaona ule ukimya usio wa kawaida. Akajua Nanaa amemkasirikia
tu. Wakati anasubiria uji wake upate moto, akaendelea kuchezea simu yake bila
kuongea chochote. Kidogo kengele ya kuashiria uji wake umekuwa tayari hapo
kwenye microwave ikalia. Akautoa uji, akaenda kukaa mezani. Hapo hapo ndani
jikoni. Kimya.
Hakuna Kulala.
Wakati mama G anataka kuzungumza
na Nanaa, simu yake ikaita. “Haloo!” Nanaa akapokea. “Ni Nanaa?” Mtu wa upande wa
pili akauliza. “Kwani wewe unamtaka nani?” Nanaa akauliza. “Nina shida sana ya
kuongea na Nanaa?” “Wewe ni nani?” “Mira.” Akajitambulisha.
“Mira!?” Nanaa akauliza
akiwa kama hajaelewa vizuri hilo jina. “Ndiyo mimi naitwa Mira.” Mama G akashituka
sana. Akaangusha mpaka glasi. Nanaa akamwangalia, na kurudisha mawazo kwenye
simu.
“Umesema Mira kama kioo!?”
“Ndiyo.” Mira akajibu. “Mmmh! Mbona mimi
sikufahamu? Unasemaje?” “Nataka kukutaarifu kuwa mimi ni mke halali wa Geb.” Nanaa akatulia. “Unanisikia Nanaa?”
“Nakusikiliza.” “Ndio hivyo. Unatakiwa ujue na uachane na mpenzi wangu. Geb
nimetoka naye mbali sana. Tokea tunasoma nchini India tulikuwa tukiishi naye.
Aliniacha nchini India nikiwa nasoma. Yeye alipomaliza akaniaga kuwa anarudi
kuanza kutafuta maisha huku. Ameniacha na baraka zangu zote. Nikikata tu simu,
nitakutumia picha zangu na Geb ili uamini vizuri na ujue sio kwamba nakurusha
tu roho. Ni kweli ni mume wangu.” Mira akaendelea.
“Nimemaliza chuo, nikarudi huku
akanipa na kazi. Tupo naye kwenye biashara zetu. Maisha yetu yanaendelea kama
kawaida. Sitaruhusu wewe wala mwanamke mwingine aingilie mapenzi yetu. Nakuonya
ukae mbali na Geb. Tuna maagano ya mpaka kwa mizimu inanitambua mimi kuwa ni
mke wa Geb. Nakuonya na kukutaarifu kabisa. Mizimu haitakubali wewe ukavunja
agano letu.” Nanaa alibaki akimsikiliza.
“Bila shaka umeshapata onyo la
kwanza. Umerudishiwa miguu yako kwa kupewa nafasi ya pili ya maisha. Nakusihi
uitumie vizuri. Itakapo kurudia tena, utajuta Nanaa. Hutakaa ukatoka kitandani
mpaka kifo chako. Nakusihi acha kucheza na ndoa za watu. Mwache Geb. Kama ni
huyo mtoto, tutamlea. Lakini ujue sitarudia kukuonya tena. Kaa mbali na Geb. Ni
mume wa mtu.” Mwili mzima wa Nanaa ulianza kutetemeka. Akagundua
kumbe mwanamke wa Geb ndio alihusika kumuwekea ukilema! “Kwa nini Geb hakuniambia?” Nanaa akajiuliza na kuumia sana.
Wakati akimsikiliza Mira,
akamsikia Oliva akilia. Akakata ile simu, akakimbilia chumbani kwa mama G
alipokuwa amelala mtoto wake. Akakuta amesimama. “Kwani umeita sana?” Nanaa
akamuuliza mwanae wakati anamchukua. “Pole. Nilikuwa naongea na mtu kwenye
simu. Umeamka salama?” Nanaa aliendelea kuongea na mwanae. “Njaa inauma? Eti
Liv? Usikasirike bwana. Sikukusikia kipenzi changu. Njoo unyonye, labda
utajisikia vizuri.” Akambusu, na kumuweka kwenye ziwa.
Mama G akaingia wakati Nanaa
ananyonyesha. Akabaki ameduwaa. Nanaa hakuongeza kitu chochote. Akabaki
ameinama akimnyonyesha mtoto wake huku akimchezea nywele. Liv alikuwa akinyonya
kwa uchu wote, Nanaa ametulia kimya. Mama G alijua wazi mambo yamebadilika.
Nanaa wa zamani angeshaanza kumsimulia juu ya ile simu. Lakini Nanaa huyu
alitulia kana kwamba hapakuwa na jambo. Akasimama pale kwa muda mfupi, akaamua
atoke.
“Nataka nimuogeshe huyo, niende
kwenye biashara yangu mara moja. Sitakawia.” “Hamna neno mama. Wewe nenda tu.
Nitamuogesha. Ukirudi ukiona sijamtakatisha mjukuu wako, mtaogeshana tena
usiku.” Mama G akacheka kidogo. “Ule basi. Chakula kipo kingi tu kwenye friji.
Na cha Oli nimeweka kwenye chupa yake. Leo nimemsagia kiazi na mboga za
majani.” “Haya. Asante mama.” Nanaa akarudisha macho kwa mwanae, akanyamaza.
Kwa
Geb.
Kitu cha kwanza alipoingia tu
kwenye gari yake, akampigia simu Geb. “Kwema?” Geb akauliza. “Hivi ulishazungumza na
Nanaa, habari za Mira?” “Hapana mama. Nilianza na kuzungumza naye habari za
Zinda kwanza. Mambo ya Mira nimeona yasubiri kwanza.” “Kwa nini!?” Mama G akahoji. “Nanaa ni mjamzito
mama. Ametoka kwenye kuumwa, akakutana na habari za Zinda. Zote zikionyesha
kuwa wewe ndio umetoa maneno humo ndani. Ilibidi kumuweka kwanza sawa na
kuandaa mazingira ya kumwambia mambo ya Mira.” Mama G
akanyamaza kidogo.
“Kwa nini unaniuliza?” Geb akauliza,
lakini kimya. “Mama?” “Mmmh! Sijui nifanyaje Geb! Nashindwa kukwambia. Asije akasema
tena nimekwambia mambo yake.” “Kwani kuna nini? Mbona sauti yako si yakawaida,
imejaa wasiwasi?” “Nitakwambia. Lakini naomba uniahidi hutamwambia Nanaa habari hizi.”
“Nini?” Geb akahoji zaidi. “Mira amempigia simu
Nanaa sasa hivi. Ameongea naye kwa kirefu tu. Nimemsikia akijitambulisha kama
yeye ni mke wako na mpo kwenye maagano ambayo hata mizimu inatambua. Amemuahidi
kumtumia picha kama uthibitisho wa mahusiano yenu. Na amemwambia alishapewa
onyo la kwanza akalazwa mpaka hospitalini. Onyo jingine, amemwambia hatakaa
atoke tena kitandani mpaka kifo.” “Mungu wangu!” Geb alisikika
kwa sauti ya juu ya kushituka sana.
“Sasa sijui utafanyaje Geb! Ni
mbaya sana kwa Nanaa kusikia kutoka kwa Mira. Ni heri angekusikia wewe mwenyewe
kwanza. Na nimemsikia akimtambia kuwa anafanya kazi na wewe. Yaani ni kama
umemuweka hapo kama mwenzio. Amemwambia ni biashara yenu.” “Mungu wangu nisaidie!” Geb
alisikika akimwita Mungu wake. “Sasa Nanaa amesemaje?” Akauliza tena. “Amenyamaza tu.
Anaonekana wazi amenikasirikia. Mbali ya salamu na kuitikia ‘ndiyo’, nakusema
atamuogesha Liv yeye mwenyewe, hajaniongelesha kitu kingine chochote.” “Wewe
uko wapi?” “Naelekea dukani kwangu. Wamenipigia simu nakuniomba niende. Kuna
tatizo kidogo. Ila nashauri usiende sasa hivi. Mwache kwanza kidogo. Fikiria
chakufanya au chakuongea naye kwanza.” “Sawa.” Geb akakata
simu akiwa amechanganyikiwa, hajui chakufanya. Tokea alipofika kazini siku
hiyo, Mira hakuwepo.
Shetani Hana Usiku Wala Mchana.
Hanaga Usingizi. Hachoki.
Wakati akimvalisha mtoto wake
baada ya kumuogesha, akasikia ujumbe unaingia kwenye simu. Akamvalisha mtoto
wake haraka haraka, akachukua simu yake. Mira alianza kumtumia picha za Oliva. ‘Huyu mwarabu wako
nitamnyonga usingizini kama hutamtoa wewe mwenyewe kwenye maisha ya mume
wangu.’ Ulikuwa ujumbe wa vitisho ulio mugopesha sana
Nanaa. Alituma picha kama tatu za Oliva, kisha akatuma nyingine alizokuwa
amepiga yeye mwenyewe Mira na Geb. Baadhi walikuwa na watu wengine. Mazingira
ya pichani, yalionyesha ni kweli walikuwa wote nchini India. Hapo ndipo Nanaa
alipomtambua Mira. Akaogopa sana. Mwili mzima wa Nanaa ulikuwa ukitetemeka
kadiri kumbukumbu ya Mira ilivyokuwa ikimjia akilini.
Alimuona siku moja kabla ya kikao
chao cha kwanza cha harusi, akizungumza na Grace na Geb. Tena akakumbuka
waliongea na kucheka. Siku ya kikao, Nanaa akakumbuka vile Mira alipomsogelea
kumsalimia. Kwa kuwa alikuwa amekaa na amempakata Fili, Mira alichuchumaa mbele
yake baada ya kusalimiana na Geb. Alichuchumaa kumsalimia. Aliongea kwa sauti
ya chini ili watu wengine wasisikie. Kuna vitu alizungumza mara kadhaa, Nanaa
hakuwa akimsikia wala kumuelewa. Akainama ili kumfikia pale alipokuwa
amechuchumaa akampa sikio. Maana Mira aliongea mara tatu bila Nanaa kumsikia.
Ndipo akakumbuka kusikia mikono ya Mira ikimpapasa miguuni. Akashituka kidogo na
kumuuliza vipi, akamwambia anamtoa uchafu miguuni. Mira alisimama, akaondoka
bila Nanaa kumuelewa vizuri. Lakini kwa kuwa alimuona na Grace siku iliyopita,
na wakasalimiana na Geb vizuri tu bila tatizo, hakuingiwa na wasiwasi. Akajua
ni watu wakaribu ya kina Geb.
Ile picha nzima na yale aliyokuwa
akimfanyia Nanaa siku ile, ilianza kumjia vizuri. Kama aliyefunguliwa macho,
akawa amejua kabisa. Hata kule kumpapasa miguuni, Nanaa akagundua hakuwa
akimtoa uchafu miguuni, bali alikuwa akimuweka zile pini. Nanaa akashituka na
kusimama kama mshale, karibia kuanguka. Olivia alibaki akimwangalia mama yake.
Picha zake na Geb wakiwa nchini
India ziliendelea kuingia. ‘Huu ndio uthibitisho wa ndoa yangu. Sasa litakalo kupata tena na
kifaranga chako, usilaumu. Jua ulionywa.’ Ujumbe mwingine ukaingia. Nanaa
alipousoma ni kama alipigwa na shoti ya umeme, akarusha ile simu kitandani.
Akabaki akitetemeka huku akimwangalia mwanae kwa hofu.
~~~~~~~~~~~~~
Kwa haraka sana kama aliyekuwa
ametumwa, akakimbilia stoo ya ndani ambayo huweka vitu wasivyotumia. Akachukua
mabegi makubwa mawili. Akaingia chumbani kwa Oliva na bibi yake. Akaanza
kukusanya nguo za mtoto wake na kuziweka kwenye begi moja. Akatoka kwa haraka.
Akapiga simu getini na kumuagiza mlinzi mmoja akamchukulie taksii. Akakimbia
juu chumbani kwao. Akakusanya baadhi ya nguo zake. Akashuka kwa haraka. “Mungu wangu nisaidie.” Nanaa alikuwa
akiongea huku akihema na kukimbia juu na chini ya ile nyumba, kama
aliyechanganyikiwa. “Huyu msichana
atakuja kuniulia mwanangu. Heri mimi hata nikifa hakuna atakayepata hasara.”
Nanaa aliendelea kukusanya vitu vyake.
Simu kutoka kwa mlinzi iliita
kumtaarifu Nanaa wamepata taksii. Akaamuru iingie ndani kabisa. Akapandisha
mabegi yake mawili kwenye ile taksii, akarudi ndani, akachukua kalamu na
karatasi.
Geb!
Sikuwa nikijua kama una mke ambaye anakuhitaji kiasi cha kunidhuru
mimi. Nimeamua kuondoka mapema kabla Mira hajamdhuru mwanangu. Sihofii juu
yangu. Kwani hata akiniua mimi, hakuna atakayepata hasara. Najua itakuwa
pumziko kwa wengi, lakini si Liv. Nitamtunza na kumlinda na kila hatari. Hata
kama itagarimu furaha yangu. Nimeamua kwenda kuanza maisha yangu sehemu
nyingine nikiwa na watoto wangu wote. Nina kuahidi kukutafuta nitakapo tulia.
Inaweza kuchukua muda kidogo. Lakini nakuahidi kukutafuta nikipata kazi na
sehemu nzuri ya kuishi na watoto. Nakuahidi kumpa Liv na mdogo wake maisha
mazuri kama unayotamani. Nitahangaika. Naamini nitafanikiwa mapema tu. Niombee
uzima na nguvu. Nina kuahidi sitakutenga na watoto wako. Nikitulia
nitakujulisha nilipo. Ili kama utapenda, uwe unakuja kuwaona wanao.
Najua ulininunua kwa pesa nyingi
sana. Lakini Geb, nakuahidi kukurudishia pesa yote. Nikianza tu kazi, nitakuwa
nakutumia kila mwezi pesa kiasi kupunguza deni. Naomba usiumie ukadhani pesa
yako imepotea bure. Nitairudisha kama ilivyo. Tafadhali sana, nakuomba Geb,
usimdai kaka. Mimi mwenyewe nitairudisha. Tafadhali nivumilie. Najua hii pete
imekugarimu sana. Nakurudishia pamoja na cheni aliyokuwa amenikabidhi mama.
Tafadhali mrudishie mama mwenyewe. Naona mimi sio mtu sahihi aliyetakiwa kunipa
hiyo cheni iliyobeba historia nzito hivyo. Nashukuru sana kwa kila kitu.
Nakuombea uzima na furaha.
Nanaa!
Akaiweka ile karatasi pale mezani
pamoja na cheni na ile pete ya uchumba, akaondoka kwa haraka kama anayekimbizwa.
~~~~~~~~~~~~~
“Tunaelekea wapi?” Yule dereva
taksi akauliza. “Stendi ya mabasi yaendayo mikoani.” Dereva akaaondoa taksii.
Swali anakwenda wapi baada yakufikishwa stendi, likaanza kumsumbua. Nanaa hakua
akijua kokote zaidi ya Moshi alikozaliwa, hapo jijini Dar ambapo napo ni shule
ndio iliyomtoa mkoani Moshi na kumfikisha hapo, na Morogoro ambako alipelekwa
na Geb.
Wazo la kukimbilia Morogoro lilipomjia,
akapingana nalo kabisa. “Morogoro
hapana. Hapo ni karibu sana. Anaweza kunifuata bila shida.” Wazo la
kikimbilia Moshi hakutaka hata kulipa nafasi hata kidogo. Ni mkoa ambao
haukuwahi kumtendea vyema. Tokea anazaliwa mpaka anaondoka mkoani hapo. Ilikuwa
machungu matupu. “Moshi hata kwa fimbo,
sitarudi.” Nanaa aliendelea kuwaza wakati dereva taksii akiendelea
kuendesha.
Ilikuwa ni saa 4 kamili asubuhi
wakati dereva taksii huyo akiingia standi. Mpaka wanaingia hapo, Nanaa hakuwa
akijua akimbilie wapi na mwanae. Aliposikia mtu mmoja akiwakimbilia huku
akitangaza kuuza tiketi ya mwisho ya basi linaloelekea Arusha muda mfupi sana
kuanzia hapo, Nanaa akashawishika. Hakuwahi kufika jijini Arusha. Lakini Alex,
mpenzi wake wakwanza, alikuwa akilisifia jiji hilo nakumwambia ipo siku
atampeleka huko wakatembee. Lakini mpaka anamsaliti, hakuwahi kumpeleka.
Waliishia kulala naye kwenye nyumba za wageni hapo hapo Moshi.
Akamuomba dereva taksii
asimamishe gari pembeni ili anunue hiyo tiketi ya kuelekea Arusha. Hakutaka
hata kujua ni basi gani. Ilimradi alisikia ni basi litakalomtoa jijini hapo kwa
haraka, Nanaa akanunua tiketi. Yule kijana aliyemuuzia akamwambia amebahatika
nafasi ya dirishani. Nanaa akamshukuru na kumwambia kwa kumuhakikishia kuwa
hamwibii, waongozane mpaka kwenye basi hilo ndipo atakapomlipa hiyo pesa. Yule
kijana akiwa anatembea, Nanaa bado yupo ndani ya taksii amekumbatia mwanae kama
alumasi anayoogopa asipokonywe, akakubali.
Wakaongozana mpaka kwenye hilo basi.
Ni kweli akamsaidia na kupandisha mizigo yote, akamlipa na pesa ya ziada kama
shukurani, Nanaa akakaa na mtoto wake huku akihema. Baada ya dakika chache
sana, basi hilo lilifanikiwa kumtoa Nanaa na Oliva jijini Dar es salaam, kwa
ahadi ya kuwafikisha jijini Arusha salama. Hakuwa akiamini wakati basi hilo
linaacha jiji. Akamtizama mtoto wake kama yupo salama. Wakagongana macho. Oliva
alikuwa ametulia akimtizama mama yake. Akamshika kichwa kama kupima homa na
kuhakikisha yupo salama, akamkuta ni mzima, ila tu ametulia kama anayejua
kinachoendelea. “Asante Mungu wangu!” Nanaa
alijikuta akishukuru kama aliyeokoka na ajali ya moto.
Akambusu mtoto wake. Oliva
alikuwa ametulia tuli. Hata Geb alishamjua mtoto huyo. Ni kama anajua kama mama
yake hayupo sawa. Alikuwa mchekaji sana. Lakini mama yake asionyeshe kutokuwa
na furaha usoni hata kidogo. Oliva hatacheka hata iweje. “Liv!” Nanaa akamwita
kwa upole. “Unakumbuka nilikuahidi hakuna kutengana?” Akamuuliza kama anaelewa.
“Basi, bado natunza ahadi yangu. Sitakuacha popote pale mwanangu. Na wala
sitakubali mtu akudhuru. Nitakulinda. Umesikia eeh! Usiogope. Kila kitu
kitakuwa sawa.” Nanaa alishazoea kuzungumza na huyo mtoto tokea yupo tumboni.
Ukiwa nje ya chumba walichopo wao, unaweza fikiri Nanaa anazungumza na mtu
mzima. “Lala tu, mama atakukumbatia.” Akamuweka sawa mwanae. Akamkumbatia kama
alivyomuahidi. Akamfunika na mtandio wake ambao huwa anamfunika wakati wote
akimnyonyesha. Na yeye akajiweka sawa akiwa amempakata vizuri. Liv alilala hata
kabla hawajafika mjini Kibaha. Baada ya muda mfupi tu alipomuona mtoto wake
amelala na yupo sawa, na yeye akalala.
Huku Nyuma Nyumbani Kwa Geb.
Geb alipata wakati mgumu sana
kusubiri kazini mpaka mchana kama alivyoshauriwa na mama yake. Alishindwa hata
kumpigia simu Nanaa, kuogopa asije piga na kuropoka na kuharibu mambo
zaidi. Kazi zilikuwa haziendi. Kila
wakati macho kwenye simu ya mkononi, ukutani na kompyuta kana kwamba kuna moja
inaweza ikampa muda usio sahihi. Ilipofika saa saba mchana, akarudi nyumbani
akiwa na makopo ya ice cream mawili. La Vanilla na Chocolate na chakula.
Alimnunulia Nanaa kuku wa kuchoma.
Alijua ni mpenzi sana wa nyama.
Akafungiwa na Chips, akarudi nazo zikiwa zimefungwa vizuri tu. Akajua hata kama
Nanaa hasikii njaa, ile harufu ya yule kuku lazima atamshawishi tu. Alirudi
akiwa ameshajiandaa kwa hoja zake zote. Alishazipanga, akazirudia akiwa peke
yake mpaka akaridhika kuwa lazima Nanaa ataelewa tu na kusamehe. Alipoingia
akakimbilia juu baada ya kukuta nyumba ipo kimya. Akajua atakuwa amelala na
mtoto wake chumbani kama usiku uliopita walipotoka Morogoro. Lakini hakuwepo
chumbani.
Akampigia simu. Akasikia ikiita
chumbani kwa mama yake. Akajua amelala na Oliva chumbani kwa mama yake.
Akashuka ngazi akikimbilia chumbani kwa mama yake. Hakumkuta Nanaa. Akapiga
tena simu yake, akasikia mlio ukitokea mwisho kabisa wa kitanda cha mama yake,
uvunguni upande wa ukutani. Akapanda na kuitoa.
Macho yake yakakumbana na picha
zake akiwa na Mira, nchini India. Akaendelea kuangalia. Picha hizo alikuwa ni
yeye na Mira. Nyingine akiwa na watanzania wengine. Geb akakaa. Akaendelea
kuziangalia. Macho yake yakatua kwenye picha za Oliva. Zote alizitambua ni
picha alizokuwa amempiga mwanae na kuzipenda sana. Oliva alikuwa akicheka.
Akaenda kuzi print. Akaziweka kwenye fremu nzuri sana na kuzitundika ofisini
kwake. Geb alishangaa sana.
“Huyu msichana anaonekana
alikuwa akinifuatilia kwa muda mrefu sana bila ya mimi mwenyewe kujua!
Ameingiaje ofisini kwangu na kupiga picha, picha za mwanangu!” Geb akaendelea
kujiuliza akizidi kushangazwa na kumbukumbu za muda mrefu alizotunza Mira.
Na yeye akakumbana na jumbe za
vitisho kutoka kwa Mira. “Hapana. Hapa amefika mbali sana!” Geb aliendelea
kuzungumza akiwa peke yake pale chumbani kwa mama yake huku akisoma na
kuangalia zile picha kwa kurudia rudia. “Atakuwa amemuogopesha sana Nanaa, ndio
maana ametupa na simu. Nanaa atakuwa yuko wapi?” Geb akasimama nakutoka pale chumbani.
Ndipo macho yake yakatua juu ya
meza aliyozoea kuweka funguo zake za gari kila anapoingia ndani. Wakati
ananyanyua zile funguo za gari ili atoke akamwangalie Nanaa huko madukani
akidhani pengine alitoka kufuata kitu dukani ndipo akaona karatasi imeandikwa “Geb!” Akajua
ni ujumbe kutoka kwa Nanaa. Wakati anaingia, alirusha tu funguo bila kuangalia
mezani kwani alikuwa na haraka yakumuwahi Nanaa.
Akaanza kusoma. “No no no
noooo!” Alijikuta akikataa kile alichotaarifiwa na Nanaa. Akahisi hakusoma
vizuri. Akarudia kusoma tena. “No way! This is not happening to
me. No way!” Gafla akahisi dunia imemuangukia. Nanaa ameondoka na faraja
yake! Nanaa amebeba mipango mizima ya Geb. Bila kujijua yeye ndiye akawa amebeba
ratiba na mipango yote ya maisha ya Geb yaliyobaki hapa duniani. Nanaa
ameondoka! Kwa sekunde kadhaa dunia iliacha kuzunguka mbele ya macho ya Geb.
Akahisi ni kama giza limemfunika machoni.
Kwa gafla sana kila kitu
kikakosa maana hapa duniani. Aliliangalia lile jumba na thamani yote mle ndani.
Gafla ikawa ni kama amesimama jagwani kwenye jua kali. Hata kiyoyonzi
kilichokuwa kinapuliza mle ndani, hakukisikia tena. Akaanza kuhisi joto kali.
Magari yote yaliyokuwa hapo nje ya hilo jumba. Ambalo alilijenga kwa mamilioni
ya pesa alitamani yawe msaada kumtoa hapo na kumpeleka alipo Nanaa na watoto
wake. Lakini yalishindwa. Yalihitaji kuongozwa. “Amekwenda wapi Nanaa?”
Lilikuwa swali ambalo hata hayo magari, yasingeweza kumsaidia, kumtoa hapo na
kumfikisha alipo Nanaa.
Akakumbuka mamilioni ya pesa
aliyonayo benki. Akajua hayatasaidia kitu chochote kukamilisha furaha yake tena
hapa duniani. Yangekuwa na maana tu kama yangeweza kutumika kumwambia Nanaa
alipo na watoto wake. Akakumbuka pesa alizolipa kwa ajili ya kumpata Nanaa,
siku alipomsahau nje ya ukumbi wa harusi ya Malii. Alimlipa Mlinzi wa benki
akamsaidia kwenda naye kwenye kampuni ya simu, akafanikiwa kupata namba ya
Antii na kumkuta Nanaa hospitalini. Lakini leo pesa yake imekuwa bubu. Haiwezi
kuongea. Nanaa ameacha simu. Labda angekimbilia kwenye kampuni ya simu ili
awalipe mamilioni ya pesa wamwambie ile simu inaonyesha ipo wapi kwa wakati ule
ili amfuate Nanaa na Oliva, furaha ya moyo wake. “Mungu wangu
naomba usiniache!” Akajikuta amepiga magoti pale pale, machozi yakimtoka.
Hapakuwa na tumaini tena.
Akarudia tena kusoma ule ujumbe
alioachiwa na Nanaa. Akagundua ameelewa kile kilichoandikwa. Akajiambia kabla
hajarukwa na akili, watu wasijue ni kwa nini, basi amtaarifu mama yake.
Walishaongea muda mfupi kabla hajarudi hapo nyumbani. Mama yake akamwambia yeye
bado yupo kwenye biashara yake. Geb alikuwa sawa tu mara ya mwisho alipokuwa
akizungumza na mama yake. Lakini safari hii alipiga akiwa analia.
Kwa Mama G.
“Mama!” Geb
aliita mara baada ya mama yake kupokea. “Kuna nini wewe!?” Mama G
akauliza kwa mshituko. “Nanaa amenikimbia mama. Nimemchelewa kidogo
tu!” “Mungu wangu!” Mama G akaweka mikono
kichwani. Simu ikaanguka. Geb akarudi kwenye kochi akakaa. Geb yule wa mipango,
mwenye majengo yanayoingiza pesa wakati wengine wakilia njaa. Ambaye akifika
mahali hata wazee wanasimama. Anayeongoza wanaume na wanawake wasiopungua
ishirini kwenye biashara zake tu. Ambao wanategemea kupokea kutoka kwake kila
mwisho wa mwezi ili nao watunze familia zao. Geb ambaye walio kwama kifedha
wanamkimbilia kukopa mamilioni ya pesa.
Jumatatu hiyo, mchana, siku ya kazi, mwanamke amemfanya apige magoti na
kujikuta akilia kama kitoto cha kike.
Kwa James.
Baada ya muda, akampigia simu
James kumtaarifu. Ndani ya lisaa limoja nyumba ya Geb ilishakuwa na wageni.
James, Grace, mama yake, Danny na watoto wote. Kila mmoja alisoma ule ujumbe
kwa kurudia rudia. “Kwa nini hukumwambia Geb? Ujue aliponipigia simu kuniambia mnakwenda
Morogoro kupumzika, nikajua mnakwenda kuzungumza!” James akalaumu.
“Kama ulikuwa huwezi kuzungumza
naye, ungeniambia tu mimi mwenyewe nikajua jinsi ya kuzungumza naye. Unajua ni
mjamzito, halafu ana mtoto. Unafikiri ataishije sasa!? Nanaa haifahamu kabisa
hii nchi!” James aliendelea kulaumu kama kawaida yake kwa dada yake.
“Kwa nini hukumwambia Geb? Huyu
Mira atakuwa amemuogopesha sana ndio maana ameamua kukimbia.” Grace aliongea
kwa unyonge akimuhurumia kaka yake. “Jamani, Nanaa aliyaona mabadiliko ya Danny.
Akaanza kuwa na wasiwasi. Akaniuliza mbona Danny hana furaha. Ndipo ikabidi
kumuelezea mahusiano ya Danny na Zinda. Nia yangu ilikuwa ni kumtoa hapa,
nimpeleke sehemu iliyotulia ili niweze kuzungumza naye. Kwanza ili kujibu
maswali yote aliyokuwa nayo Nanaa juu ya ugonjwa aliopata wa gafla, na habari
za Zinda.” Geb akaendelea.
“Nilipokuwa nikimuelezea
mahusiano ya Danny na Zinda tu, hata sikuwa nimemaliza habari nzima, tayari
Nanaa alishakuwa amepata majibu yake. Alilia sana, akihisi amesalitiwa.
Ilimchukua muda mrefu sana kutulia. Ilibidi kumueleza taratibu kwa nini maneno
yalimfikia Zinda.” “Mimi nilimuona tokea mwanzo jinsi alivyomuuliza mama kama
yeye ndiye aliyemwambia Zinda. Mama unakumbuka? Akasema ningeumia sana kama ni
mama. Maana mama ndiye msiri wake.” Grace aliongeza.
“Nakumbuka. Na amerudi kutoka
safari, ameshindwa hata kuniangalia usoni. Najuta! Unajua Mira alizungumza naye
nikiwa hapahapa! Ingekuwa zamani angeniambia. Lakini alinyamaza kabisa. Mpaka
namuaga nakwenda kazini, alionyesha yupo sawa tu na hana kitu chakuzungumza na
mimi.” “Nimekuta hizi picha na jumbe za vitisho sana kutoka kwa Mira. Mira
amemtumia kwenye simu yake. Nina uhakika hizi ndizo zimemkimbiza.” James
akachukua ile simu kutoka kwa Geb. Akaanza kuziangalia.
“Mbona ulisema ni kama hamkuwa
na mahusiano!?” “James! Huyo dada hatukuwa na mahusiano naye, ila tumeishi
naye.” “Picha zako zinaonyesha tofauti Geb! Kama hii mmepiga akiwa amekuegemea
begani! Hapa mmekaa karibu kabisa! Na picha za Oliva amezipata wapi!?” James
aliendelea kuhoji huku akiperuzi kwenye simu ya dada yake. “Sidanganyi James. Huyo dada sikuwahi hata
kumfikiria kimapenzi. Na Mungu wangu ni shahidi. Na picha zote hizo zimepigwa
kwenye mikusanyiko ya watanzania. Sio kwamba nilikuwa nikipiga naye mimi peke
yangu! Na picha zote hizo nikiziangalia, nakumbuka kabisa ni picha tulizopiga
siku tulizokuwa watanzania tunakutana kwenye sherehe au mikutano ya watanzania.
Sasa labda yeye alikuwa akinitega kwa madhumuni yake. Lakini sikuwahi hata kuwa
na wazo naye.”
“Amekuja kuomba kazi kwangu,
nikamuajiri kama mfanyakazi wa kawaida tu. Muulize hata Grace. Hata sina muda
naye. Mungu wangu ni shahidi. Grace ndiye anayemsimamia na tuseme yuko chini ya
Grace. Sipo karibu naye kabisa labda atumwe kitu kwangu na Grace, basi. Nisingemdanganya Nanaa. Nampenda Nanaa. Na
picha zote hizo za Oliva ni picha nilizo tundika ofisini kwangu. Hizo mbili
nimening’iniza ukutani, pamoja na za Nanaa, na hii ni picha ambayo nimeweka
mezani kwangu. Tena ipo nyingine ya Nanaa akiwa amembeba Liv. Muulize Grace. Au
twende ofisini kwangu hata sasa hivi utaona. Ofisi yangu imejaa picha za Nanaa
na Oliva tu. Nina uhakika ndiko alikoziona hizo picha. Niamini nampenda Nanaa.
Siwezi kumchanganya na mwanamke mwingine yeyote yule James. Sithubutu.” Hilo
James alilithibitisha pale Nana alipougua. Akanyamaza.
“Sasa unafikiri atakuwa ameenda
wapi?” Mama G akamuuliza James. “Sijui! Mimi ndiye familia ya pekee ya Nanaa.
Hana pakwenda na hafahamu hii nchi vizuri. Kwanza hana uzoefu wa kusafiri
kwenye mabasi. Kwanza hata sikumbuki kama alishawahi kupanda mabasi makubwa
kumpeleka sehemu yeyote. Labda HIACE. Kumtoa pale Moshi mjini kumpeleka
vijijini. Hata kuja hapa Dar kwenyewe mimi ndiye nilimleta na gari yangu. Nanaa
hafahamu mambo mengi na hicho ndicho kinachoniogopesha, tena akiwa ni mjamzito
na mtoto juu! Sijui kama anapesa yakumtosha au la!”
“Nanaa anazo pesa. Anapesa
nyingi tu. Huwa nampa kila mwisho wa mwezi kama mshahara, kwa matumizi yake
binafsi ili asiwe anashida ya pesa. Huwa nampa pesa nzuri tu. Grace akilipa
mishahara, nahakikisha na yeye namgawia kutoka kwenye mshahara wangu.
Namwingizia asilimia 80 benki halafu 20 huwa namletea hapa nyumbani. Kwa hiyo
swala la pesa hilo usiwe na wasiwasi nalo. Na nitaendelea kumuwekea tu, hata
kama sitampata.” Geb alijibu kinyonge akisikika amekata tamaa.
“Kama ni hivyo, ni sawa. Lakini
nashauri mumpe muda. Mwacheni atulie tu. Amesema atakutafuta. Basi
atakutafuta.” James alisikika amepata aghueni baada ya kusikia dada yake ana pesa.
Akasahau pesa si kila kitu. “Lakini
ataishije mwenyewe akiwa na mtoto na ni mjamzito? Hata akiwa na mamilioni ya
pesa yanayoingia kila siku bila kuzungukwa na watu wanaompenda na kumthamini,
haitamsaidia chochote. Mbaya zaidi akiwa amejawa na hofu! Halafu amejazwa
maneno yaliyojaa uongo na usaliti kutoka kwa Mira bila yakusikia upande wangu!
Najua sasa hivi amejawa hofu, usaliti na majuto.” Geb alisikika akiwa
amenyong’onyea.
“Na lazima atajisikia hivyo.
Ameona picha. Halafu amejua unafanya naye kazi siku zote. Kwa nini usimwambie
siku zote, mpaka yeye mwenyewe ndiye amekuja kumwambia? Hujui amemwambia nini
mbali ya hizo jumbe zakutishia maisha yake na mtoto wake. Nanaa yupo kwenye
hofu sana. Ameshuhudia kile huyu anayejiita mke wako, akimtendea
yeye. Unyama mkubwa. Lazima sasa hivi anajua hizo jumbe sio za vitisho. Anajua
ni kweli ana uwezo wa kuja kumdhuru tena yeye na mtoto wake pia. Lazima aogope
na kujiweka mbali. Hasa akijua kwa kutomtaja Mira kwake ni kwa kuwa upo upande
wake Mira.” James aliendelea kupalia makaa ya moto.
~~~~~~~~~~~~~
Ni bandika
Bandua. Likiisha hili, linaanza jingine.
Jamani! Nani ni wa Nani?
Hata Nanaa
amechanganyikiwa na kupoteza dira, akaamua kuachia gazi.
Zinda amedai Nanaa ni mkewe, huku Mira naye
anadai Geb ni wake!
Geb
anamwambia Nanaa amemchagua yeye, huku anapata habari kutoka kwa Mira kuwa ni
wa Geb!
Walikuwa
mbuga za wanyama kwa takribani siku tatu, kwa nini asimwambie? Alimuona pia na
Grace, inamaana hata Grace anamfahamu wifi yake Mira. Usaliti wa namna gani?
Nanaa
aliwaza wakati anaondoka.
Anaelekea
wapi?
Ø Ni Nanaa
huyu huyu aliyekuwa ametokewa na malaika siku chache zilizopita. Akaamuona mtu
akipigana vita yake na kumwambia yupo mtu anayepigana badala yake. Lakini ndio
huyu huyu leo anakimbizwa na simu na ujumbe kutoka kwa Mira.
Ø Alisimamia
Imani ya Geb mpaka akapokea muujiza wake, leo ameweka kila kitu chini. Pete ya
Geb na cheni ya dhahabu ya mama G, anakimbia na faraja ya Geb, Oliva!
Usikose
kufuatilia Visa na Mikasa ya Simulizi hii ya kusisimua.
0 Comments:
Post a Comment