“Muongo
kabisa huyu kaka. Huko Kenya mimi hata sijui kunafananaje! Tena kipindi hiki
ndio nilikuwa nikisumbuliwa sana na kizunguzungu. Nakumbuka ni mwezi huu huu wa
kumi ndio kizunguzungu kilinitesa sana. Nitaenda kuangalia tarehe kwenye mfuko
niliokuwa nikiweka vitu vya hospitalini kipindi mjamzito wa Oliva. Nilikuwa na File maalumu la hospitalini. Nilikuwa nikiweka kila
kitu humo ndani mpaka risiti kama nilinunua dawa au nililipia kumuona daktari.
Nitaangalia kuthibitisha. Nakumbuka kuna weekend
moja ilinilazimu kurudi kumuona daktari sababu nilianguka nikiwa peke yangu
kwenye ngazi, sababu ya kizunguzungu. Nilipoamka tu, nikampigia simu daktari
nikamuomba anione.” Nanaa akaendelea kukumbuka.
“Sasa
kwa kuwa yule daktari nilishampa historia yangu na nikamsihi anisaidie kwa
karibu sana ili nisije kufa nikamuacha Oliva peke yake, basi alikuwa
akinisaidia sana. Muda na wakati wowote nilikuwa nikimpigia simu, anapokea.
Ilikuwa siku ya jumamosi. Nakumbuka nilipanda daladala akaniambia nimfuate
alipo. Alikuwa yupo hospitali ya Tumaini. Nikamwambia nilianguka sababu ya
kuona giza. Akaniambia nipime damu. Ndio akagundua sina damu kabisa. Akataka
kunilaza ili niwekewe damu. Ndio nikamwambia siwezi kulazwa. Kwanza nilikuwa
sina pesa. Akasema atanisaidia lakini lazima niwekewe damu.” Nanaa akaendelea.
“Nikamwambia
pia sina mtu wakuanza kuniuguza pale hospitalini. Maana nilijua yupo busy sana.
Asingeweza kuniuguza. Halafu nikamwambia nipo chuo. Nina mitihani mingi sana,
siwezi kulazwa. Baada ya kumkatalia swala la kulazwa, ndio akaniandikia
vidonge, na kuniambia lazima nipate muda wa kupumzika. Nile vyakula vya
kuongeza damu, halafu nirudi kumuona ili kujua kama damu imeongezeka. Kwa hiyo
Zinda ni muongo. Ngoja nikuletee uthibitisho kaka. Nilitunza kila kitu.” Nanaa
akasimama.
Akaelekea
stoo alipokuwa amehifadhiwa vitu vyake vyote vya chuoni. Akaanza kupekua humo
ndani. Pale sebuleni palikuwa pamezuka ukimya mkubwa sana. Nanaa alikuwa
akimtaka kumjua mtoa siri zake. Geb naye akaongezewa mawazo. Akaumizwa
kujua Nanaa alikuwa na matatizo ya afya kipindi mjamzito wa kuyo mtoto
aliyezoea kucheza kifuani kwake.
“Faili
lenyewe hili hapa kaka.” Nanaa akarudi na faili kubwa. Macho yake yalikuwa
yakisaidia kutafuta. “Amesema tulifunga ndoa tarehe ngapi?” Nanaa akauliza
tena. James akamtajia. “Tena kila kitu nimekipanga kwa tarehe!” Nanaa akakaa
chini huku akitafuta hiyo tarehe. Akakutana na picha za Ultrasound. Akacheka.
“Unataka nikuonyeshe picha za Oliva wakati yupo tumboni?” Akamuuliza kaka yake.
James akacheka. “Hembu tumuone.” Nanaa akampa kaka yake.
“Na
mimi naomba kuona, Nanaa.” Geb akasimama. Akamsogelea James. James akaangalia,
akamkabidhi Geb. Geb akacheka. “Nilikuwa nafurahi kweli nilivyokuwa
nikionyeshwa kwenye machine!” “Nashukuru umezitunza Nanaa. Ukumbusho mzuri
sana.” “Kweli Geb? Maana mimi nilikuwa naweka tu.” “Muhimu sana. Asante.” Nanaa
akamtizama Geb, akacheka. Akaenda kukaa pembeni yake. “Pole kwa matatizo yote
yaliyokuwa yakikupata peke yako wakati ulipokuwa mjamzito.” Nanaa akacheka
kidogo. “Asante Geb. Namshukuru Mungu kuniwezesha.” Wakataka kupena mabusu,
Nanaa akakumbuka kitu.
“Subiri
kwanza kaka. Sasa kama Zinda anasema alinioa, aliwezaje kuishi na mimi nikiwa
na mimba ya Oliva!?” “Anasema ulimwambia, akakukubalia kuwa atamtunza mtoto.”
“Zinda ni mwendawazimu! Sasa anasema baada ya ndoa ikawaje?” Nanaa aliendelea
kuhoji. “Anasema mlienda kuishi naye.” Nanaa akaanza kucheka. “Sasa kama
nilikuwa nikiishi naye, iweje leo niwe hapa?” “Anasema ulipokaribia mitihani
yeye akiwa nje ya nchi kikazi, ilikulazimu uhamie hosteli. Ndipo ukajifungua.
Ulipojifungua, Geb akajua una mtoto wake, akaja kukupokonya mtoto. Wewe ndio
ukamfuata. Ndio Geb akakufungia. Ukamwambia..” Nanaa akakunja uso. “Subiri
kwanza kaka. Zinda anaonekana anaongea uongo unao sindikizwa na ukweli! Hayo
mambo nani amemwambia!? Maana hata wewe hukuwa ukijua! Hayo mambo yalitokea
kati yangu mimi, mama na Geb tu. Hakuna mtu mwingine alijua! Ni mambo ya ndani
sana. Nani atakuwa anaongea mambo mazito hivyo, tena ya ndani sana,
kwa watu wa nje!?” Kimya. Nanaa akashangaa watu wote wameinama.
“Naomba
nikuombe kitu kaka. Nimekuwa na maswali ambayo hakuna mtu anayenipa majibu.
Kuanzia mtu aliyetaka kuniangamiza, mpaka mtu anayetoa maneno humu ndani. Hiyo
ni tabia mbaya sana. Kuna mambo ambayo huwa yakitokea, hayafai
hata kuja kuzungumzwa tena! Lazima nijue. Nijue nani anataka kuniangamiza. Na
kwa nini! Nani anatoa maneno humu ndani. Na anayapataje! Maana humu ndani watu
wanaokuja ni watu wa kusafisha. Na wanakuja mara mbili kwa week tu. Na mara
nyingi wakija huwa tunawapisha. Sasa nani anakuwa anatusikiliza? Jibu atakuwa
nalo Zinda. Naomba unisindikize kuzungumza na Zinda. Nitamuomba tuonane naye.
Akikataa nitamfuata hata kwake.” “Akikushitaki?” “Mimi si ni mkewe?” James
akacheka.
“Si
ndio vyeti vinavyosema? Sasa nataka nikazungumze naye. Si ni sawa Geb?” Geb
akabaki akimwangalia. Nanaa akajua wazi huko ndiko kukataliwa. “Naomba usikatae
Geb, tafadhali. Zinda hawezi kuwa sababu ya mimi kutokuolewa na wewe. Au
umebadili mawazo.” “Hapana Nanaa. Unajua jinsi ninavyokupenda. Natamani hata
kesho nikuoe.” Nanaa akacheka. “Basi sasa kwa nini huniungi mkono katika swala
la kutafuta suluhisho? Au umekata tamaa?” Nanaa aliendelea kumuhoji Geb
taratibu. “Sijakata tamaa Nanaa. Lakini unakumbuka ulimuuliza hata malaika ni
nani amekuweka zile pini, lakini hakukwambia?” “Kwa sababu alikuwa akinielekeza
kila kitu kwako Geb. Mungu anataka wewe ndio uhusike na mimi si vinginevyo.”
“Hudhani
kwamba anakulinda? Labda anadhani haupo tayari na ukweli.” “Sidhani Geb. Mungu
amekuamini na maisha yangu. Anajua wewe utaniongoza vizuri. Ndio maana anataka
kila kitu kizuri, kianzie kwako.” “Una uhakika?” Nanaa akacheka. “Kabisa. Sasa
unafikiri ni kwa nini alitaka wewe ndio uwe chanzo cha uponyaji wangu? Mungu
anakuamini na maisha yangu Geb.” Geb akamtizama.
“Mbona kama huamini!?” Nanaa akauliza. “Hilo
naliamini. Lakini je wewe unaniamini?” “Nakuamini sana Geb!” “Una uhakika?”
“Zaidi ya asilimia 100, Geb. Mungu amekutumia sana kwenye maisha yangu. Na
nimetumia Imani yako kama ulivyoniambia pale hospitalini nikiwa nimekata tama,
nikiwa hata simwamini Mungu. Lakini nikakuamini wewe, umenisaidia nimerudi kwa
Liv. Nakuamini sana.” Nanaa asijue anajifunga mwenyewe.
“Basi
naomba tulia kwanza kwa sasa hivi. Acha tutafute njia nyingine yakumaliza hayo
matatizo na kufunga ndoa yetu. Ukitafuta nani amefanya nini sasa hivi,
haitasaidia. Utapoteza muelekeo mzima wa kwa nini upo hapa leo.” Nanaa akatulia
kidogo. Hakutegemea jibu la namna ile kutoka kwa Geb.
Akamgeukia
vizuri Geb, akamtizama. “Wewe unafahamu ni nani amefanya hayo yote?” Lilikuwa
swali la moja kwa moja lililozua ukimya wa gafla. “Geb?” Nanaa akaita kwa
upole. “Ndiyo nafahamu.” Geb akajibu. Wakabaki wakiangaliana. Nanaa akakunja
uso, akainama. “Nanaa! Naomba nipe muda. Nipo kwenye maombi. Namuomba Mungu
atusaidie hekima juu ya hili.” “Sasa
unajuaje labda kwenda kwangu kwa Zinda ndio msaada wetu?” Nanaa akauliza huku akifuta machozi. “Umesikia
habari nzima juu ya Zinda. Amekusudia kutukomoa, Nanaa. Amekwenda umbali mkubwa
sana kutengeneza uthibitisho utakaozuia nisikuoe. Amekusudia. Lazima kuwa
makini kwa kila tunachotaka kufanya. Najua sasa hivi anategemea sisi tufanye
mambo fulani fulani kujibu mashambulizi yake. Na kwa kahika amejipanga. Tena
amejipanga vizuri tu. Naomba tupate muda wa kumsikiliza Mungu. Tujue anataka
atusaidiaje katika hili.” Geb alimvuta mkono.
“Wewe
si unasema unaniamini?” Geb akamuuliza. Nanaa akatingisha kichwa kukubali. “Lakini nataka kujua. Geb.” “Nafahamu. Basi naomba nipe muda. Sawa?” Nanaa
akanyamaza. “Nanaa?” “Huniamini Geb!” “Nakuamini sana Nanaa. Lakini naomba tupate muda na
Mungu kwanza. Tukikubali kuwa wepesi wakusikia au kusikiliza kila mtu,
nakuhakikishia anguko letu halitakuwa mbali. Tutaanguka na kutengana kwa haraka
sana. Zinda sio adui yetu wa kwanza. Anatumiwa na shetani. Na usifikiri
atakuwa mtu wa mwisho kumtuma kwetu kutuchafua. Bado tutakutana na makwazo
mengi na watu wa aina ya Zinda ni wengi tu. Tukiwa watu wa haraka kujibu kila
mashambulizi, hatutafika mbali. Umemuona Mungu alivyotutoa kwenye mtego mkubwa
sana wa shetani. Amepigana vita vikubwa sana kwa niaba yetu.” Geb akaendelea.
“Hatuwezi
kitu bila msaada wa Mungu. Hatutafika mbali. Nahitaji muda wetu sisi na Mungu
kwanza. Kumbuka kwa nini Mungu ametutoa hospitalini. Kumbuka kilio chako.
Naomba usipoteze muelekeo. Tafadhali Nanaa.” “Nitasubiri Geb.” Nanaa akajifuta
machozi. “Asante. Nakuahidi kwa wakati unaofaa, nitakwambia kila kitu. Lakini
sio sasa hivi. Mungu ametupa nafasi yakuwa pamoja. Hata masaa 24 hayajaisha
tokea upokee uponyaji tuliokuwa tukililia kwa ajili yako mwenyewe na familia
yetu. Naomba urudishe mawazo kwa mtoto aliyekuwepo tumboni na sisi.” Nanaa
akajishika tumbo.
Akamuona
anatabasamu. “Halafu kila saa nasahau hata kama ni mjamzito!” “Kwa kuwa akili
yako ina mambo mengi. Naomba urudishe mawazo humu ndani. Halafu mambo mengine
niachie mimi. Sawa?” Geb alikuwa akizungumza naye taratibu tu. Kila mtu
akiwasikiliza. Nanaa akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu huku
akijirudisha nyuma. Akajiegemeza pembeni ya Geb. Akambusu begani. “Sawa.
Nitatulia kabisa. Chukua hili faili. Pengine litakusaidia utakapoamua kutafuta
ushahidi. Au mimi naweza kukusaidia.” “Nanaa!” “Basi Geb. Naachana kabisa na
hayo mambo.” James akacheka taratibu. Nanaa akacheka na kuinama.
Geb
alibaki akimtizama. “Kweli tena nimeacha Geb. Sasa hivi natulia na nyinyi tu.
Sihangaiki tena. Ilimradi unihakikishie utakuja kunioa mimi hapa.” Watu wote
wakacheka kidogo. “Hapo kafika huyo. Hata kaka yako alipopiga simu usiku ule
ananiuliza sasa iweje akili ije imrudie Geb, ampigie simu amdai pesa yake!
Halafu akukimbie hospitalini! Nikamuuliza James, huyo Geb akimbilie wapi?
Nikamwambia Geb ndio kafika pale. Hajiwezi kwa lolote. Hata kama mama yake
akirudi adai tena pesa nyingine, atamlipa tu.” “Mama wewe! Naomba temea mate
chini, asirudi tena!” Nanaa alishituka sana. Wakacheka tena kidogo.
“Nimesema
ukweli.” Mama G akasisitiza. “Mungu
asaidie asirudi tena. Sasa hivi mambo yake safi. Hata simu zangu hapokei tena.
Wamepanga nyumba na amefungua baa.” “Kaka wewe!” Nanaa akashangaa sana. “Kweli
tena. Anashida gani na pesa anayo. Ashakuuza wewe, sasa hivi ametulia tuli. Amemkimbia
baba. Anaishi na wale wanae wakike.” Nanaa akasikitika sana. “Jamani!” “Lakini
waache tu Nanaa. Mungu yupo.” Wakanyamaza kidogo.
~~~~~~~~~~~~~
Nanaa
akamgeukia Geb. “Asante mpenzi wangu kwa kunilipia garama zote hizo.” Geb
akacheka. “Nakupenda Nanaa. Hakuna thamani inayoweza kulinganisha na yale
unayonipa. Ona sasa hivi nilivyokumbatiwa hapa.” Wakamuona Liv ametulia kifuani
kwa baba yake. Uso ameweka shingoni kwake. Ametulia kimya. Wakacheka.
“Hiyo
furaha yake, huwezi kuipima kwa pesa. Hakuna kiasi cha pesa kinaweza kununua
hii hali ninayo jisikia moyoni.” Nanaa akammchungulia Liv. Mwanae akajitoa pale
kwa baba yake, akamwangalia na yeye. Akacheka kisha akajirudisha tena kwa baba
yake. Geb alikuwa akimkuna mgongoni. Akamgeukia mwanae, akambusu tena.
“Umeyabadilisha maisha yangu kabisa Nanaa. Unanipenda bila unafiki.
Umenivumilia hata kipindi kile nipo na Liz!” Nanaa akainama.
“Unakumbuka
kuna siku nilikwambia kwa mafumbo upendo huvumilia?” Nanaa akatingisha kichwa,
huku akicheka. “Pale nilikuwa nikikusihi univumilie Nanaa. Ndio nilikuwa
nakuomba usimkubali mtu mwingine, hata Jeff. Unisubiri niweke mambo yangu
sawa.” Wakacheka.
“Nilielewa
Geb.” “Haiwezekani Nanaa! Sasa wewe ulielewa nini wakati Liz aliendelea kuwa
anakuja kulala pale pale ndani? Mimi nisingeweza.” Grace akauliza kwa mshangao.
“Wakati mwingine nilikuwa naumia sana. Lakini muda mfupi niliokuwa nikiupata na
Geb, ulikuwa unanifanya nipate moyo wakuendelea kumsubiria.” Wakacheka.
“Kweli.
Tulikuwa tukipata muda mfupi mfupi. Lakini kwa namna fulani, nilianza kujisikia
upendo wa Geb kwangu. Kuna jinsi alivyokuwa akiwa kwangu, hata nilikuwa
nikimuona akiwa na Liz hawi hivyo.” “Sawa sawa Nanaa. Basi kweli kumbe ulikuwa
ukimwangalia Geb. Mimi mwenyewe mpaka nikawa namwambia mama. Huyu Geb
anakaribia kukamatwa na Liz. Alishindwa kabisa kuficha mapenzi yake kwako.
Unajua hata siku ile Marangu Liz alipomuuliza Geb mbele za watu, nilimkonyeza
Danny. Nikamwambia, leo bomu linapasuka. Lakini nikamuona amejikaza sana
kutosema.” Grace akaongeza.
“Aaaah!
Ndio maana.” Nanaa akaanza kucheka. “Nini?” Grace akauliza. “Ujue Geb
aliniambia hivi. Baada ya wote kurudi kutoka Marangu. Siku ile nilikuja
kuchukua vitu vyangu ili nihamie kwa Antii. Geb akanikatalia nisihame. Tukabaki
tukizungumza muda mrefu chumbani akinisihi nibaki. Sasa nikawa nipo kama
nimechanganyikiwa tena. Maana ni kama nilimuacha amekumbatiana na Liz! Hata
tumaini dogo nililokuwa nalo moyoni likawa limeisha kabisa. Nikaamua niondoke
kabisa pale kwake.” “Na yeye Geb alijua.” Mama G akaongeza.
“Kweli
mama?” Nanaa akauliza. “Kabisa. Alijua hutasamehe tena. Wala hutataka
kumsubiria tena. Basi muda wote uliomuacha kule Marangu alishindwa kula wala
kulala huyo.” Nanaa hakuamini. “Geb!?” Akauliza kwa mshangao sana. “Kumbe! Huyo
huyo Geb. Hali ilikuwa mbaya sana. Heri usingeondoka.” “Basi mimi sikuwa hata
najua. Niliondoka nikiwa nimekusudia kuanza upya. Niondoke. Nitulie na shule,
basi. Nakumbuka akaingia pale chumbani kwangu, akaniambia hakuna mtu yeyote
kati yetu. Si mimi, wala kaka, au Zinda na Liz, tuliokuwa tayari kwa ukweli.
Ndio maana akaamua kunyamaza tu. Sasa mimi sikumuelewa. Nikamuuliza ni ukweli
gani? Akasema kama nikiamua kubaki naye. Yaani nisihamie kwa Antii, niendelee
kuishi pale kwake, nitajua tu.” “Na unavyopenda umbea wewe. Hapo ukahisi labda
atakuja kukwambia wakati mwingine. Ukaona usipitwe.” “Kama ulikuwepo kwenye
akili zangu mama. Nikasema labda atakuja kuniambia kesho au baada ya muda
mfupi. Heri nibaki tu.” Wakacheka.
“Nanaa
kwa kupenda stori! Lakini zitakusaidia kupata mume.” “Umeona sasa? Ningekimbia
wakati ule nisingekuwa hapa.” Kila mtu akacheka. Lakini Nanaa akashangaa Danny
amepooza kabisa. Akahisi kuna kinachoendelea.
Wakazungumza mpaka James
akaaga. “Sasa na huyo anywe uji ndio akalale.” Mama G akimaanisha Oliva. “Mpaka
uje mtoe hapo shingoni kwa baba yake! Tena kwa kumpa uji! Labda tumwite Fili
ampe pipi.” Nanaa akafanya kila mtu acheke. Fili alishaenda kulala. Baba yake
alimpeleka ilipofika tu saa mbili. “Fili bwana! Sisi tunajua watoto wanampenda
tu, kumbe anawapa sukari na pipi!” Grace akaongeza. Wakazidi kucheka. “Utamkuta
ametulia nao kitandani wapo kimyaa. Tena huwa ananiambia, ‘usiwe na wasiwasi mama. Wewe nenda tu kaoge. Nitakaa na watoto.’
Basi nikawa najua nimekuza yaya wa Watoto! Kumbe mwenyewe ana njia zake!” Wakacheka. “Lakini amekusogezea. Si hao sasa
hivi wanakunywa uji? Watakuwa tu.” Mama G akampa moyo.
Nanaa
aliona hali imebadilika. Mazungumzo hayakuwa kama kawaida. Kulikuwa na hali ya
ukimya. Baada ya muda mfupi Danny akaaga, akaondoka. Wakati Grace anataka
kuondoka, Geb akamuita. “Naomba tuzungumze kidogo.” Grace akamsogelea. “Vipi?”
“Unafikiri unaweza kunivumilia nikaanza kazi jumatatu ijayo? Nataka nitoke na
familia yangu kwa kama siku tatu hivi. Tutarudi jumapili mchana. Jumatatu
nitakuwepo kazini. Halafu na wewe unaweza kuchukua hata siku mbili za
mapumziko” “Unataka muondoke lini?” “Kesho asubuhi.” Geb akajibu. “Hamna shida.
Wewe nenda kapumzike na familia yako. Mimi nitakuwepo.” “Nakushukuru sana.” Geb
akamshukuru, Grace akaondoka.
Aluta
Kontinua.
Ilikuwa
siku ya jumatano asubuhi wakati Geb akiondoka na familia yake kuelekea mbuga za
wanyama Mikumi, mjini Morogoro. Nanaa alikaa kiti cha nyuma na Oliva. Kwa kuwa
walimsubiri mpaka saa tatu akawa hajaamka, ikabidi kumtoa tu kitandani akiwa
bado na usingizi. Kwa hiyo baada ya kuogeshwa na kunyweshwa uji na bibi yake,
alianza kusinzia. Geb alipomfunga tu kwenye kiti cha gari na kumpa busu, alitoa
tabasamu la kichovu, na kupotelea usingizini. Nanaa aliendelea kuzungumza na
Geb njiani huku Geb akiendesha.
Walifika
Mikumi hoteli, wakachukua chumba. Geb akaanza kutengeneza kitanda cha Oliva walichokuwa
wamekichukua nyumbani. Alikifungua na kurudishia kwenye boksi lake maalumu
akakiweka nyuma ya gari mpaka hapo hotelini. Baada yakupata chumba na kuangalia
sehemu nzuri ya kufunga kitanda hicho cha mtoto, ndipo Geb alipoanza
kukirudisha kwenye muundo wa kulalika. Nanaa alikuwa akimlisha Liv wakati Geb akifunga kitanda.
“Geb!”
Nanaa akaita. “Nimeona kuna tofauti kwa Danny. Kila kitu kipo sawa?” “Hapana.”
Nanaa alipata jibu ambalo hakutegemea. Na Geb akajibu tu kwa kifupi, akaendelea
na kazi. Nanaa akabaki ameduwaa. Akaendelea kumlisha mtoto wake. Akambadilisha
nguo na diaper akabaki akicheza naye.
Geb
akamaliza kila kitu, akaenda kukaa karibu yao. Liv akataka ambembe. “Nanaa,
unajua nimekuja huku kwa kuwa nilitaka muda na nyinyi. Nataka tuwekane sawa.
Tunaishi pale na watu wengi. Ni rahisi mahusiano yetu kumezwa na watu wanao
tuzunguka. Mwishowe tukasahau nafasi zetu kwetu. Namaanisha ikawa rahisi
kupoteza muelekeo. Kwa kifupi, nilitaka kukumbusha wewe ni nani pale ndani na
kwenye maisha yangu.” Nanaa alikuwa akimsikiliza.
“Nahesabu
ni baraka kuwa na wewe mpaka sasa hivi Nanaa. Sitaki mambo tutakayopambana nayo
njiani, yakachukua kile kilichopo ndani yetu. Naamini bado unanipenda.” “Sana
Geb! Wewe unajua kama nakupenda.” “Basi naomba siku ya leo iwe kwa ajili yangu
na Liv tu. Naomba tuwe wote hapa. Akili zako, mawazo na kila kitu chako.
Unakumbuka mapenzi tuliyofanya mara ya kwanza tulipokuwa wote huku Morogoro?”
Nanaa akacheka kwa aibu. “Basi nakuomba tena. Nina hamu na wewe Nanaa.” “Hata
mimi Geb. Nakuahidi nitatulia.” Geb akatabasamu na kumbusu. “Nakuahidi kesho
tutapata muda mzuri wa mazungumzo. Nitakwambia kila kitu. Halafu tutajua kwa
pamoja kitu cha kufanya.” “Sawa.” Wakahamia sakafuni kuanza kucheza na mtoto
wao wakati Geb ameagiza chakula hapo chumbani.
~~~~~~~~~~~~~
Mtoto alipolala tu, Nanaa akachangamkia kazi.
Akaanza mabusu kwa Geb. Geb akacheka. “Nina hamu na wewe Nanaa! Nina kiu.”
“Itaisha leo.” Nanaa akamnong’oneza masikioni. Geb akamnyanyua kutoka pale
sakafuni na kumuweka kitandani. Akamfunua gauni yake akambusu tumboni. “Akiwa
wa kiume, nitamuita Magesa Junior.” Mara zote Nanaa alikuwa akisahau kama ni
mjamzito.
“Akiwa
wa kike je?” Nanaa akauliza huku akitoa tabasamu. Macho ya Geb yalikuwa tumboni
kwa Nanaa. Akambusu tena na tena tumboni. “Oliva ulimlea ukiwa peke yako. Huyu
nitamlea mimi. Zamu yangu.” Nanaa akacheka. Hakuwa amepewa jibu lake. Lakini
akaamua kunyamaza. Alijua wazi Geb amesikia swali lake.
“Nataka unitajie kitu kimoja.
Kikubwa unachotaka kutoka kwangu Nanaa. Nitakununulia. Chochote kile. Wala
usiwe na wasiwasi juu ya pesa.” Nanaa akakaa. “Chochote kile?” Nanaa akauliza.
“Chochote kile.” Nanaa akacheka huku akifikiria. “Kwanza niulize kwa nini?”
“Kwa sababu nakupenda.” Nanaa akacheka sana. “Hiyo ndiyo sababu pekee?”
“Huniamini?” Geb akauliza. “Nakuamini Geb. Ila najiuliza kwa nini sasa hivi?”
Geb akakaa pembeni yake.
“Ngoja
nikwambie kitu. Ulipokuwa hospitalini, ndipo nilipojua sina maisha mengine bila
wewe Nanaa. Thamani yako kwangu iliongezeka mara zote pale nilipoona hatari ya
kukupoteza. Nikajiambia Mungu akinipa nafasi ya kuja kuwa na wewe tena,
nitakufanyia chochote utakacho. Lakini kiwe kikubwa kitakachonigarimu. Ili kila
nikikumbuka, nikumbuke uthamani wako. Si kwa kuwa nitasahau, lakini..”
“Unamaana zaidi ya milioni 50 ulizo nilipia!?” Geb akacheka.
“Namaanisha
kikubwa.” Nanaa akabaki ametoa macho. “Hivi unajua kitu ulichonipa kwenye
maisha yangu? Au unajua kitu ambacho unaendelea kunipa kwenye maisha yangu ni
cha thamani kuliko mtu anavyoweza kufikiria?” “Unamaanisha watoto!?” Nanaa
akauliza. “Ulimpata Liv na kulea mimba kwa mateso ukiwa peke yako. Sasa hivi
nafurahia mapenzi ya huyo mtoto. Hakuna jinsi naweza kukwambia furaha yake
ukaelewa.” Nanaa hakuwa ameelewa.
“Jamani
Geb! Mbona nimesikia watu wengi walikuwa wakitaka kuzaa na wewe!?” “Kwa kuwa
walitaka kunitumia tu! Walitaka kwa faida zao wenyewe. Wengine walijua wakizaa
na mimi watanufaika na pesa yangu. Wengine ni kwa mashindano ili kujivunia kuwa
wamelala na mimi! Wengine walijua wakizaa na mimi watazaa watoto wenye akili
kama zangu! Lakini sio wewe Nanaa.” Geb akawa kama amekumbuka kitu cha
kumwambia.
“Unakumbuka
zile siku ambazo tulikuwa hatupo kwenye maelewano? Kama ile siku ulikuwa
umeniomba nikusindikize mahali. Ukajiandaa kabisa. Akaja Liz, nikaishia kutoka
na Liz, nikakuacha wewe?” Nanaa akanyamaza.
~~~~~~~~~~~~~
Alikumbuka jinsi alivyokuwa ameumia. Alitoka
kwenye birthday aliyokuwa amealikwa na Zena kigamboni. Jeff akamtambia na
mwanamke wake. Akaamua kurudi nyumbani. Akamkuta Geb akiwa anafanya kazi juani.
Akamwokoa na ile hasira. Wakapata muda mfupi, mzuri. Wakakubaliana watoke.
Lakini Geb akaishia kutoka na Liz badala yake yeye ambaye alikuwa
ameshajiandaa. Nanaa aliumia sana, na kuamua kukaa mbali na Geb. Mpaka mama
yake Geb alipombembelezea mwanae, ndipo Nanaa akamtumia ujumbe kwa mara ya
kwanza, Geb akatulia.
~~~~~~~~~~~~~
“Nikiwa
nimekuumiza, ulikuwa unaweza kuweka hisia zako pembeni na kunifikia mimi.
Kutaka kujua ninaendeleaje! Kuhakikisha nipo sawa, ndipo mambo mengine
yaendelee. Wakati wote unaniangalia mimi kama Geb. Uwe katika uzima au
matatizo. Akili zako zipo kwangu mimi kama Geb. Umeweza kutenga hisia zako na
mali zangu. Unanipenda mimi kama Geb. Sijawahi kufanya mapenzi na mwanamke
mwingine kama ninavyofanya mapenzi na wewe Nanaa. Nikiwa nafanya mapenzi na
wewe, moyo wangu, akili zangu na hisia vyote vinafunguka kwa kuwa najua nafanya
mapenzi na mwanamke anaye nithamini. Hamu na wewe haijawahi kuisha. Ni vile tu
kwa kuwa na mimi ni mwanadamu wa kawaida, nachoka.” Geb alikuwa akiongea naye
taratibu na kwa hisia.
“Lakini
Nanaa, kiu ya mapenzi kwako haijawahi isha. Nilikuwa nikikutamani wakati nikiwa
na Liz. Niliacha kufanya naye mapenzi, nikijua wewe ndiye utakayeniridhisha.
Nilijaribu baada ya wewe kuhamia pale nyumbani, lakini nilikuja kushindwa
kabisa. Nilikuwa siwezi kulala na Liz, eti nikijua Nanaa yupo chumba kingine!
Tena pale pale ndani! Nilishindwa kabisa.” Geb akacheka kidogo kama
aliyekumbuka kitu.
“Kitendo
cha kukufikiria unaweza kuja kuchoka kunisubiri. Ukaamua kuachana na mimi,
ukawa na mwanaume mwingine. Akaona kwa macho kile nilichokuwa nikikitazama mimi
na kukitamani. Nilikuwa siwezi kula Nanaa. Nikijua umetoka mle ndani eti mama
aniambie au anitumie ujumbe kuwa Nanaa ametoka, kazi zilikuwa hazifanyiki!”
Nanaa akacheka kidogo. “Nilikuwa ni kama nashindwa kufikiria. Kile kitendo cha
mimi kumpigia mama simu, nimkute peke yake nyumbani wakati najua unatakiwa wewe
uwepo nyumbani, halafu aniambie umetoka! Au
hata kama nakuwa nimetoka na Liz. Halafu labda nimtumie ujumbe nimuulize
Nanaa anafanya nini sasa hivi, aniambie ametoka! Pengine kuna mtu ulienda
kuonana naye, akili zilikuwa zinavurugika kabisa.” Nanaa akashangaa.
“Geb
wewe! Yaani kumbe ulikuwa ukiniulizia hata ulipokuwa ukitoka na Liz!?” “Kabisa
Nanaa. Nilikuwa nikiondoka lakini moyo wangu umejaa wasiwasi. Najiambia unaweza
kupata mwanaume mwingine. Halafu mama naye alikuwa anakusifia huku akiniambia
una bahati sana na wanaume wenye uwezo. Swali la wewe utanisubiria mpaka lini,
lilikuwa likininyima usingizi na kushindwa hata kula.” “Basi mimi sikuwa na
habari hata kidogo!” “Nilikuwa na wakati mgumu sana Nanaa. Unajua mpaka Grace
akaniambia ni lazima niweke kikomo. Najiumiza mimi mwenyewe.” “Sasa Grace
alijuaje!?” Nanaa akauliza akiwa na mshangao wa kilichokuwa kikiendelea bila ya
yeye hata kuhisi kama anamtesa Geb aliyeonyesha maisha yake yanaendelea kama
kawaida.
“Yeye
alijua kinachoendelea kwa kuwa Liz alikuwa akimlalamikia. Halafu ujue Grace ni
pacha ambaye ni kama hisia zetu zipo pamoja. Nikiwa kwenye mateso, na yeye
anaumia sana. Anaumia sana Grace akijua kama sina raha. Nikiumwa ndio ujue na
yeye ataumwa. Basi, alipoona vile ndio akaniambia yale sio maisha ninayotakiwa
niendelee kuishi kwa muda mrefu.” “Sasa kwa nini ulikuwa ukiishi hivyo?” Nanaa
akauliza taratibu tu.
“Unaona
hiki kinachotokea sasa hivi na Zinda? Sikutaka wewe ndio utupiwe lawama.
Mwanzoni sikutaka Liz ageuke kuwa adui yako. Nilitaka aje anichukie mimi
mwenyewe. Nilitaka kukutoa kabisa kwenye lawama, ajue mimi ndiye niliyekutaka
au kukuchagua. Sio aje akuzushie wewe.” “Asante Geb. Lakini sasa hivi imekuwa
kinyume. Zinda anasema nimekupendea pesa.” “Sio kweli. Hata watu hawaamini
hilo. Hata Liz hakulaumu wewe. Nilihakikisha anaelewa ni mimi ndiye
nimekuchaguwa wewe.” Nanaa akabaki kimya.
“Niambie
nini unataka Nanaa.” “Nataka niwe mkeo kihalali Geb. Nataka niitwe Nanaa
Magesa. Kama mkeo sio heshima ya kuishi na wewe. Nataka uhangaike mpaka
uhakikishe mimi ndio nasimama na wewe kanisani. Nataka uahidi mbele za watu na
mimi mwenyewe kwamba mimi ndio nitakuwa mkeo mpaka kifo kitakapotutenganisha.
Nataka hata iweje, nibakie kwako mimi peke yangu. Kwako wewe Geb.
Hilo ndilo nataka kutoka kwako. Hiyo ndiyo garama nataka unilipie. Iwe katika
shida na raha. Ukinipa hilo, ndio nitafurahi. Hakuna thamani ya mali
itakayoweza kununua hiyo furaha yake. Nataka uwe wangu mimi Nanaa. Mimi
peke yangu nisiwahi kukushiriki tena na mtu. Na watu wote wajue Geb ni wa
Nanaa.” Hapo ndipo alipoanza kumng’ang’ania Nanaa. Alifanya naye mapenzi kana
kwamba ndio wanaagana na hawataweza kuja kuwa tena pamoja hapa duniani.
Kwa
hakika siku hiyo ilikuwa ni yao tu. Nanaa na Geb waliweza kuridhishana kila
walipokuwa wakifanya mapenzi. Oliva alipokuwa akiamka walipata muda wa pamoja
naye wakicheza. Walitoka kidogo mida ya jioni kuzunguka hoteli hiyo ya Mikumi.
Geb akiwa amembeba mtoto wake kwa mkono wa kushoto huku wa kulia akiwa
amemshika Nanaa. Wakiongea na kucheka.
Alijitahidi
kutuliza akili za Nanaa. Akirudia rudia umuhimu wake kwake na wanae. Vile
anavyomuhitaji. Furaha aliyompatia kwa kumpa watoto. Tena mtoto kama Oliva mzuri
na mwenye uwezo mkubwa wa kiakili. "Naami hata huyo anayekuja Mungu
atamsaidia furaha kama Liv.” “Hujaniambia kama ni mtoto wa kike tutamuita nani!”
Geb akamtekenya kidogo mwanae, wakacheka. “Eti Liv? Jina la kaka si liwe Magesa
Jr? Utalipenda?” Nanaa akajua Geb anataka mtoto wa kiume. Akaingiwa na hofu. “Iweje nije kuzaa mtoto mwingine wa kike?
Haya mapenzi na sifa zote si vitaisha?” Hofu akafanikiwa kuchukua furaha
yote ya Nanaa.
Kuanzia
muda huo mpaka wanaingia kitandani kulala, Nanaa hakuwa akiongea sana. Geb
alikuwa akicheza na Liv. Akajaribu kumlisha Liv chakula alichokuwa
ametayarishiwa na bibi yake. Akala vizuri tu. Geb akampigia simu mama yake
akijisifia kuwa ameweza kumlisha Liv kwa urahisi tu bila hata kupoteza muda
mrefu akimbembeleza. “Nimezungumza naye tu. Mwanangu
akakubali kukaa kwenye kiti chake, akawa anafungua mdomo. Amekula mpaka
akashiba.” “Mmmh!” Mama yake akaguna. “Kweli mama.” “Ukute amekula vijiko vinne tu!” “Ngoja nikuchukulie
video uone kibakuli chenyewe.” “Nataka kuona na tumbo lake. Msije mkamlaza na
njaa!” “Sawa mama. Ila ujue mimi nimewashinda wote. Na mjue mwanangu anaelewa
kila kitu. Ni kumwambia tu ale, anakula.” Nanaa akacheka.
“Unavyojisifia
Geb wewe! Ngoja akubadilikie kesho. Mwanao hatabiriki huyo!” Nanaa akaongeza.
“Bwana nyinyi hamjui kumlisha mwanangu. Mnamkaba badala ya kumkalisha tu kwenye
kiti chake ale! Eti Liv wa Geb?” Geb akakata simu akaendelea na mwanae.
Alimsafisha
na kumbadilisha nguo. Akamuweka kitandani kwake. Akaanza kumsomea kitabu mpaka
Liv akalala. Nanaa alikuwa akimsikiliza wakati anamsomea. Kila mtu alijua Liv
akisomewa kitabu na baba yake alikuwa akilala kwa haraka kuliko yeye mama mtu
au bibi yake. Wakati wao wakimsomea alikuwa akichukua muda mrefu akicheka au
hata kusimama. Mpaka watarudia mara mbili au tatu ndipo anaweza kulala lakini
si baba yake. Wakati mwingine Geb anakuwa hata hajafika mwisho wa kitabu, Liv
anakuwa alishapotelea usingizini. Akamsikia Geb akicheka peke yake. Akajua
anamcheka mwanae. Akatoka.
~~~~~~~~~~~~~
Nanaa
alikuwa amejilaza kitandani, Geb alijua wazi amekosa raha. Akambusu tena na
tena. Nanaa akarudisha busu kidogo, Geb akampa tabasamu. “Unakumbuka
nilikwambia huwa napanga mambo yangu, halafu namwambia Mungu?” Geb akamuuliza
Nanaa huku akimtizama vile alivyonyong’onyea pale kitandani. “Nakumbuka.” Nanaa
akajibu taratibu tu akitaka kujua anapoelekea.
“Basi
ni tabia niliyofundishwa na baba yangu. Aliniambia kamwe nisiwahi kuishi bila
kujiwekea mipango. Kisha nimshirikishe Mungu. Basi ndivyo ninavyoishi. Kila
kitu napanga, halafu huwa namwachia
Mungu. Ikitokea inaendana na mapenzi ya Mungu kwenye maisha yangu, basi
huwa inatimia. Na ikitokea...” “Kwa hiyo ni kweli kama alivyosema Grace? Kuwa
ulitaka mtoto wa kike ndio awe wa kwanza.” Nanaa akawa ameshamuelewa hata kabla
hajamaliza.
Kabla
hajajibiwa akaongeza swali jingine. “Lakini unataka awe wa kike mmoja tu?” Geb
akajua ameshaingiwa hofu. “Kama nilivyokuwa nikisema. Nikiona havijatokea kama
nilivyopanga, baba alinifundisha kushukuru kwa kuwa mipango ya Mungu kwa
wanadamu ni bora kuliko yetu. Akanifundisha kupokea kila Mungu atakachonipa.”
Nanaa akatulia.
“Nikweli
nilimuomba Mungu kuwa mtoto wangu wa kwanza awe wa kike. Halafu wa pili ndio
awe wa kiume. Akaja Liv. Nikajua mpango wangu uliendana na wa Mungu.
Nilikuvizia siku za mtoto wa kike, na nikafanikiwa. Tangia umerudi, nilishindwa
kuhesabu mzunguko wa hedhi yako. Nilikuwa siwezi kusubiri siku hata moja ya
kutofanya mapenzi na wewe.” Nanaa akacheka na kujifunika uso. “Kwa hiyo huyo
mtoto wa sasa hivi, ni yule Mungu atakaye nijalia. Hakuna juhudi zozote
nimefanya kumpata wa kiume. Nitampokea vile atakavyonijalia Mungu. Wewe huusiki
na jinsia ya mtoto yeyote utakaye zaa.” Kidogo Nanaa akatulia. “Niliogopa Geb!”
“Nilijua. Nilikuona vile ulivyobadilika. Huna haja ya kuogopa. Akiwa wa kike,
tutamtafutia jina utakalotaka wewe.” “Ndio maana nakupenda!” Wakajikuta wameangukia
kwenye mapenzi tena.
Wakaendelea
usiku huo, wakalala na kuamkia alhamisi. Siku hiyo na ijumaa wakatumia hapo
hapo hotelini wakizunguka tu, kula na kucheza na mtoto wao huku wakizungumza
mazungumzo yasiyoweza kuibua hisia za majonzi.
Jumamosi,
Mjini Morogoro.
Waliamka
siku ya jumamosi Geb alikuwa amelipia gari ya kuwapeleka mbuga za wanyama.
Nanaa alikuwa akishangaa na kufurahia kila kitu. Kila wakati Geb alikuwa
akiwapiga picha yeye na mwanae. Mwishowe yule aliyekuwa akiwazungusha mbugani
akawasaidia kuwapiga picha kwa pamoja. Wakapata muda mzuri sana huko mbugani.
Hasa Nanaa ambaye hakuwa akijua starehe.
Kwa
muda mfupi aliokuwa ameishi na mama G na Geb, alikuwa akinukia pesa. Kila kitu
cha Nanaa kilikuwa kizuri. Alikuwa akienda kununua vitu na mama G mpenda vitu
vizuri. Kwa hiyo hapo alipo alifanania na Oliva na utajiri wa Geb. “Anasinzia
huyo!” Nanaa akamwangalia Oliva mikononi kwa baba yake. “Naona turudi tu
hotelini. Hata hivyo ni kama tumeshaona wanyama wote.” “Nakushukuru Geb.
Nimepata wakati mzuri sana.” Nanaa akatupia na busu la shukurani. “Nimefurahi
kama umepafurahia. Nimefanya hivi makusudi kwa ajili yako.” “Najua Geb.
Asante.” Wakarudi hotelini.
Mpaka
wanatoka bafuni kuoga, tayari muhudumu akawa ameshaleta vyakula pale chumbani.
Wakakuta vimeandaliwa vizuri hapo ndani. “Chumba chote kinanukia chakula!”
Nanaa akasifia. “Husikii kichefuchefu?” “Hata kidogo. Ndio naona njaa inazidi
kuuma.” “Vaa basi!” Geb alianza kucheka. Maana Nanaa alikaa pale pale na taulo
lake na kuanza kula. “Acha kwanza nishibe bwana!” Geb akajua mimba ya safari
hiyo haitamsumbua. Wakakaa na kuanza kula.
~~~~~~~~~~~~~
“Mbona unaniangalia hivyo?” “Kuna kitu nataka
kukwambia.” Nanaa akavuta tena bakuli la matunda, akajisogeza vizuri kwenye
kochi akajiweka sawa. Akakumbuka Geb alimwambia hiyo ndiyo siku atamwambia
ukweli wote. “Umeshiba kweli? Naona bado unajilamba vidole!” Geb akamuuliza.
“Nahisi nina tatizo Geb. Nimeanza kutokushiba! Ile siku tunaondoka nyumbani,
ile asubuhi tulipokaa wote pale nyumbani
na kupata kifungua kinywa, ujue mwenzio nilianzia kula jikoni! Nilikunywa uji
wako pia. Supu ile aliyotengeneza mama. Chapati alizokuwa ameleta Danny jana
yake usiku na yale mayai niliyokula pale mezani. Halafu si ulinisikia njiani
nilivyokuwa nakula?” Geb akaanza kucheka.
“Usinicheke
bwana! Sishibi hata! Yaani ninakula naona sishibi!” Nanaa akaendelea kulalamika.
“Kumbuka unanyonyesha na una mtoto anayekutegemea tumboni.” “Unahisi ndio
sababu?” Nanaa aliuliza huku akimalizia juisi ya matunda iliyobakia kwenye
mabuli baada ya kumaliza matunda yote. Geb akazidi kucheka. “Tuagizie chakula
kingine.” “Naona wazo zuri. Sijashiba hata! Na safari hii waambie walete chips
za kutosha Geb. Wanapunja sana bwana!” “Nitaagiza sahani mbili. Unataka na
nini?” “Ndio maana nakupenda. Sasa moja iwe chips na mayai. Wasiunguze wala kukausha.
Waache mbichi kidogo.” Geb alikuwa akimtizama Nanaa na kucheka.
“Usinicheke
bwana! Halafu sahani ya pili iwe chips na kuku. Walete na kachumbari yenye kila
kitu walichonacho huko jikoni. Na waweke na limao. Sio jingi.” “Sasa kwa
maelezo hayo. Nafikiri niende mimi mwenyewe kuzungumza na mpishi.” “Udumu Geb
wangu. Lakini nahisi nitanenepa sana jamani! Utanichukia?” Geb akambusu.
Alipotaka kumuachia. Nanaa akamng’ang’ania midomo yake.
“Kidogo
tu, halafu ndio uende.” “Si umesema una njaa wewe? Ngoja nikalete kwanza chakula.”
“Sio kuwa nina njaa! Ila sijashiba. Njoo kidogo bwana. Nina hamu na wewe Geb.”
Geb hakujivunga. Akachangamkia penzi. Haikuwa kidogo kama alivyoomba Nanaa.
Walihamia kitandani. Nanaa alinogewa hapo kitandani. Hakutaka Geb amwachie. “Ni
busu tena.” Nanaa aliomba taratibu mara baada ya Geb kumalizia na yeye. Geb
akambusu midomoni kwa muda mrefu kidogo, akamwachia. Nanaa akajivuta pembeni
yake. Karibu kabisa na ubavuni kwake. “Usilale sasa!” “Nikumbatie kidogo tu.”
Nanaa akajigeuza ukutani. Geb akasogea mpaka nyuma ya mgongo wake. Akambusu
nyuma ya shingo.
“Nakupenda
Nanaa.” “Nakupenda sana Geb. Namshukuru Mungu kuwa hapa na wewe. Nashukuru kwa
wazo la kuja hapa. Najisikia vizuri. Sikujua kama nitafurahia hivi. Ni kweli
sisi wote watatu, tulihitaji huu wakati. Asante mpenzi wangu.” “Asante
kushukuru.” Geb akapitisha mkono juu ya kiuno chake. Kiganja kikatua tumboni.
Akaanza kumpapasa taratibu, akamsikia Nanaa ameanza kukoroma taratibu.
Akacheka. Akambusu tena mara kadhaa mgongoni. Akabaki akiwaza.
~~~~~~~~~~~~~
Nanaa
alikuwa mwingi wa furaha. Kadhalika Oliva aliyekuwa akicheka kwa sauti huko
mbuga za wanyama. Walipata wakati mzuri sana. Wakati wote Nanaa alikuwa
akimgeukia Geb na kumnong’oneza neno, “Asante”. Akionyesha kufurahia kile Geb alichofanya.
Alikuwa amebadilika usoni kwa furaha. Ni Nanaa aliyekuwa amedidimizwa na
kutamkiwa ni mzigo. Leo Geb amempokea na kuongeza uthamani wake. Nanaa amekuwa
gumzo kwenye jamii! Thamani imeongezwa, kila mtu anamtaka yeye! Mwenye kisu
kikali ndio anakula nyama sasa hivi. Ni Nanaa Magesa.
Joto
la mwili wake liliongezeka na kumfanya Geb kutaka kufanya naye mapenzi kila
wakati. Hakutaka kubanduka hapo kwenye mwili wa Nanaa, ni vile Mungu alifupisha
starehe hiyo, na huwa mwili unachoka, vinginevyo Geb angekesha. Hofu ya kutaka
kumwambia kila kitu Nanaa ikaanza kumwingia. “Nisije kuharibu kila kitu!” Geb akawaza wakati Nanaa na mwanae
wamelala bila hata habari, sababu ya uchovu wakuzunguka siku nzima mbugani.
Geb
akambusu tena mgongoni huku na yeye amelala kwa ubavu ili kumkumbatia kwa
urahisi Nanaa aliyekuwa na yeye amelala kwa ubavu. Akampapasa tena tumboni mara
kadhaa. Hamu yakutaka kumuamsha apate starehe aliyopewa muda mfupi uliopita
ikamjia kadiri alipokuwa akimpapasa Nanaa. “Usiku
wa leo utakuwa mfupi. Na hivi amelala mchana!” Geb akawaza na kucheka. “Lakini nikimwambia. Anaweza kuumia sana.”
Wazo jingine likapita. Likamtia hofu kuzungumza yote aliyotaka kuongea na
Nanaa. “Lakini nilazima asikie kutoka
kwangu. Si vinginevyo.” Geb akajirudi. Wakati anawaza, akapitiwa na
usingizi pale pale kitandani alipokuwa amemkumbatia Nanaa.
~~~~~~~~~~~~~
“Njaa
inauma!” Geb akasikia Nanaa akiongea. Akahisi anaota. “Geb!” Nanaa akamtingisha
kidogo. Akafungua macho. Akakuta giza limeingia mpaka chumbani. Taa ya nje
kwenye balcony, ilikuwa ikimulika kitanda cha Oliva. Chumba hicho kilikuwa
kimejazwa thamani za mbao na viti vizuri vya miti. Geb alichukua kama kinyumba
kidogo, chenye chumba kikubwa kilichogawanywa mara mbili. Kulikuwa na vitanda
viwili humo humo ndani na sehemu kubwa iliyotengenezwa kutoshea meza na viti
vilivyokuwa vimesukwa kwa ustadi mzuri tu. Vyote vilipangiliwa kwenye hicho
kinyumba kilichokuwa kimetengenishwa katika sehemu tatu ndani. Vyumba viwili
na sehemu ya kukaa. Walikuwa na Balcony/
baraza moja kwa nje.
Akamsikia
Oliva akiongea kitandani kwake. “Ameamka huyo!” Geb aliongea akiwa anatoka
usingizini. “Hajaamka muda mrefu. Pole nimekuamsha. Lakini njaa inauma.”
“Twendeni basi wote tukale huko huko sehemu ya kulia chakula. Hata Liv nitaenda
kumlishia huko huko.” Geb akatoka kitandani. Nanaa alioga hata dakika
haikuisha. “Nanaa!” Geb akashangaa ametoka. “Njaa inauma bwana. Nitaoga vizuri
nikirudi.” Geb akacheka tu. Na yeye akaingia bafuni kwa haraka akatoka.
Alimkuta Nanaa alishavaa na amemtayarisha Liv. “Kweli una njaa!”
“Nimeshawapigia simu. Nikawaambia oda yangu. Nataka nikifika tu, nikute
chakula. Siwezi kusubiri tena.” Akaenda
kumpokea Oliva. Akachukua mfuko wake, wakatoka. Walimbebea cerelac ambayo
ilikuwa niyakuchanganya tu na maji ya vuguvugu.
Walipofika
ni kweli hawakukaa muda mrefu, chakula cha Nanaa kikaletwa. Geb akaagiza maji
ya moto na baridi. Alikuwa ameleta na kiti cha Oliva, maalumu cha kumlishia
chakula. Akawa amemfunga hapo. Amemvalisha na aproni yake. Liv alikaa pale
akijua chakula kinakuja. Alikuwa akimtizama baba yake vile anavyomchanganyia
chakula chake. Kila Geb alipokuwa akimwangalia, Liv alimrudishia tabasamu.
Nanaa alikuwa akiendelea kula kwa juhudi zote wakati Geb akimlisha mtoto huku
anazungumza naye.
Nanaa
alikuwa akishangaa vile Oliva alivyokuwa akila bila shida. “Liv unamakusudi
wewe! Unavyokula kwa bidii kama sio wewe!” “Hamjui kumlisha mwanangu.
Mnampakata na kutaka kumkaba! Liv hapendi fujo mwanangu. Akikaa mwenyewe na
kumlisha anakula vizuri tu. Mnatumia nguvu nyingi bila sababu! Mnaishia kumkera
tu. Ndio maana hali.” “Ngoja niwachukue video nimtumie bibi yake aone ubaya wa
mjukuu wake.” Nanaa akaanza kumchukua video. Liv akacheka. “Tabia mbaya hiyo
Liv! Wala usinichekee.” Oliva alizidi kucheka. “Wala sio mazuri!” Geb alikuwa
akicheka.
Alipokuwa
akilishwa na bibi yake, wote waliishia kuchafuka. Oliva alikuwa akicheka wakati
wote huku chakula kikitoka. Hakuwa akitaka kutafuna wala kumeza. Mama G akaona
awe anamlisha kwa kumpakata. Oliva alikuwa akipaliwa nakuishia kutapika au
kukohoa na kumlowesha uso mzima bibi yake. Walikuwa wakimlalamikia Geb kuwa
mtoto wake anataka nyonyo tu, hataki kula. Lakini Geb alikuwa akiwabishia na
kuwaambia jinsi wanavyomlisha Liv, ndio maana hali. Akamnunulia kiti na
kuwaambia watumie njia ya kumuweka ale, napo haikusaidia. Sasa siku hiyo baba
yake alimuweka kwenye kiti chake, akaamfunga vizuri na kumlisha bila shida.
Tena Liv alikuwa akifungua mdomo yeye mwenyewe.
Walikuwa
na wakati mzuri sana hapo sehemu ya kulia chakula. Walikuwa wakizungumza mambo
yao na kucheka na mtoto wao huku Nanaa akiendelea kula. Walizungukwa na wazungu
watupu hapo. Wao peke yao ndio walikuwa weusi kwenye eneo hilo la kulia
chakula. Nanaa aliagizia chakula kingine tena, safari hii akawa anaendelea kula
taratibu, Geb akijipanga kuzungumza la moyoni bila kutibua hali ya hewa.
Siri ya kwanza.
“Unajua
Danny ni yatima?” Geb akaanza. “Najua. Alisema na yeye alilelewa kwenye nyumba
ya mapadri. Ila sijui historia yake ni kwa nini ilikuwa hivyo! Na wazazi wake
wako wapi!” Nanaa akajibu huku akiendelea kula, hana habari. “Wazazi wake wote
walifariki. Lakini wote walikuwa wakifanya kazi hapo hapo kanisani. Alianza
kufa baba yake wakati ndio Danny tu amezaliwa. Baada ya kama mwaka mmoja akafa
mama yake pia. Lakini kwa kuwa wazazi wake walikuwa wakitumika hapo kanisani
kwa muda mrefu, Danny alipoachwa peke yake, hao mapadri wakamlea Danny. Ni
historia ndefu kidogo. Lakini ndio hivyo.” “Oooh!” Nanaa akaitikia bila
kufikiria. Akaendelea kula.
“Alipofaulu
sekondari kwenda Iliboru.” Geb akaendelea na kumfanya Nanaa amwangalie kwa
makini. “Kwani kuna nini tena!?”
Nanaa akawaza. “Kwa nini habari za Danny
sasa hivi, katikati ya mapumziko yetu!?” Nanaa akaendelea kujiuliza wakati
amenyanyua uso akimtizama Geb aliyeonekana anataka kuzungumza jambo muhimu.
“Ndipo
tukakutana huko. Asilimia kubwa ya marafiki kwenye lile kundi tulikutana kidato
cha kwanza kwenye sekondari ya Iliboru. Lakini kwenye kubic yetu, au chumba
chetu tulikuwa tukilala wanne. Mimi, James, Danny na Zinda. Tulikuwa
tukifuatana sisi wanne. Ndipo Malii na Goz wakajiunga. Marafiki wengine
tulikutana nao kidato cha 5&6. Kundi likazidi kuongezeka. Wachache hasa
wanawake wa lile kundi, tulikutana Chuo Kikuu Cha Mlimani.” Nanaa akabaki
ametulia akimsikiliza, akitaka kujua mwisho wa yale mazungumzo katikati ya
mapumziko yao, yataishia wapi.
“Zinda
na Danny wakaanza urafiki uliowapelekea kuwa kama ndugu. Likizo nyingine kubwa,
Danny alikwenda nyumbani kwa kina Zinda kwanza, ndipo kisha huko kwa hao
mapadri, Iringa. James hakuwa akipoteza muda wowote ule. Shule zilipokuwa
zikufungwa tu, alikimbilia nyumbani ili awe na wewe.” Nanaa akatabasamu.
Akachukua
soda yake akanywa. Mara hiyo ya pili, Nanaa aliomba muhudumu amletee chips na
yai. Lakini isikaushwe hata kidogo. Kwa hiyo hapo alikuwa akiendelea kula kwa
kufurahia rojo rojo hilo. Alishamaliza sahani ya kwanza ya chips kuku, hiyo
ilikuwa sahani ya pili aliyokuwa akila taratibu bila haraka. “Kwa hiyo kuanzia
hapo, Danny akawa amepata sehemu mbili za kuishi. Nyumbani kwa kina Zinda
Tabora na huko Iringa, nyumbani kwa wale mapadri waliokuwa wamemlea tokea
mtoto.” “Kwa hiyo kabila la Danny ni muhehe?” Nanaa akauliza.
“Sina
uhakika sana. Sikuwahi kudadisi hilo. Lakini ni kama wazazi wake walihamia hapo
Iringa kutafuta maisha. Katika hangaika zao, wakajikuta wote wakifanya kazi
kwenye nyumba hiyo ya mapadri. Mama yake alikuwa mpishi. Kama sijakosea. Baba
yake alikuwa akifanya kazi za nje. Usafi, maua na kadhalika. Na nafikiri kama
nakumbuka vizuri, mama yake Danny na yeye alikuwa yatima. Kwa hiyo alikulia
maeneo hayohayo mpaka akaja kukutana na baba yake Danny. Alivyoambiwa Danny ni
kwamba mama yake alishika mimba kabla ya ndoa. Ikamlazimu baba yake kutafuta
chumba na kumchukua. Kumbe baba yake tayari alikuwa na maambukizi ya virusi vya
ukwimwi. Akamuambuza mama yake. Yaani pale unapomuona Danny ni mtoto
aliyezaliwa na wazazi waliokuwa wameathirika. Kwa kuwa mama yake alikuwa binti
mwaminifu na alilelewa hapo hapo au kwenye mazingira ya namna hiyo, ikabidi
Danny apitie kulelewa kwenye mazingira hayo hayo.” “Maskini Danny!” Nanaa
akamuhurumia.
“Ndio
maana Danny hata mwanamke awe vipi, hawezi kumtaka kimapenzi. Sisi tulijua
atakuja kuwa padre. Tulikuwa naye akiwa hana msichana. Mpaka alipokuja kukutana
na Grace. Kila mtu alishangaa vile alivyochanganyikiwa. Hatukuamini kama ni Danny.”
Nanaa akacheka. Akakumbuka historia ya Danny na Grace.
“Ndio
maana anamchunga sana Grace!” Nanaa akaongeza huku anacheka. “Nafikiri.
Anakumbuka kosa la baba yake. Hataki waje wawaache watoto wao. Wosia wake
wakati wote kwa kila mtu ni kuwa makini. Muoga hata wakuweka pombe mdomoni.
Anasema anaogopa kuweka kitu chochote mwilini mwake kitakachomfanya afanye kitu
cha kuja kujutia baadaye.” Nanaa akacheka.
“Kwa
hiyo Danny na Zinda, wakageuka kuwa ndugu. Nikisema ndugu namaanisha ni kama
waliokuwa wametoka kwa baba na mama mmoja. Danny haitaji kualikwa nyumbani kwa
kina Zinda. Anaweza kutoka Dar na kukimbilia Tabora japo kwa siku mbili tu,
kuwaona wazazi wa Zinda. Haitaji kumtaarifu Zinda tatizo la nyumbani kwao ili
asaidie. Anatuma pesa nyumbani kwa kina Zinda kila inapolazimu. Akisikia mama
yake Zinda mgonjwa, atawasha gari na kukimbilia Tabora kumchukua yule mama na
kumpeleka hospitalini. Awe na Zinda asiwe na Zinda, atafanya hivyo. Ndugu wa
Zinda hawahitaji ruhusa ya Zinda kumuomba pesa Danny. Ni kaka yao. Kukiwa
na tatizo nyumbani kwao, wasipompata
Zinda kwenye simu, basi Danny atapigiwa simu.”
“Mimi
ndio nimeharibu mahusiano yao.” Nanaa akajilaumu. Asielewe historia hiyo nzima
itakapoishia. “Wala si wewe Nanaa. Ni Zinda mwenyewe. Zinda alikuwa akijua
kabisa ni kwa kiasi gani nakupenda. Zinda anafahamu. Sijui ni roho gani
imemuingia na kumfanya awe hivyo alivyo. Na ametumia urafiki wake na Danny
vibaya au niseme vizuri, ili kuniharibia mipango yangu.” Nanaa akatulia kidogo.
Ni kama akatoka usingizini. Geb akajua ameanza kupata picha fulani.
“Kama
ulivyokuwa ukiona jinsi Danny na Zinda wanavyoishi. Kufuatana kila mahali.
Kuambiana kila kitu. Kwenye kundi zima wao ndio walikuwa karibu zaidi ya
wengine.” Nanaa akaumia sana. Tayari akawa ameelewa kila kitu. Akainama. “Kama
unavyonijua mimi si mzungumzaji sana. Lakini hawakuacha kunishirikisha katika
mambo yao. Na japokuwa sikuwa kama wao, wacheshi na mambo mengine, lakini kwa
kuwa wote walikulia pale nyumbani sababu ya Danny, tukajikuta kama ndugu. Hata
mimi nisipokuwepo nyumbani, wao wanaweza kuja tu. Kama alivyosimulia Grace
maisha waliyoishi wakati mimi nipo nchini India. Wote waligeuza nyumbani kwetu
kama kwao.” Nanaa alibaki ameinama.
Geb
akaendelea tu. Alikusudia afikishe ujumbe wake. “Mama na yeye ni yatima kama
alivyokwambia. Alipojua historia ya Danny na mapenzi aliyokuwa nayo kwa Grace,
akamfanya Danny kuwa kama mtoto wake. Anampenda sana Danny. Na kwa kuwa wote
wamekutana wacheshi, basi wamekuwa karibu muda mwingi kuliko hata mimi.” Nanaa
akazidi kuumia. Akahisi usaliti wa hali ya juu.
“Kwa
hiyo mama ndiye aliyemwambia mambo yote Danny, na Danny ndiye
aliyemwambia Zinda?” Nanaa akauliza moja kwa moja na kumfanya Geb atulie
kidogo. “Kwamba mama ametumia uaminifu wangu kwake, akatoa mambo ambayo
nimemuamini nayo, akawa anamwambia Danny!?” Nanaa akatengeneza swali lake na
kulifanya lisikike vibaya zaidi akionyesha maumivu ya usaliti.
“Haikuwa
kama hivyo Nanaa. Unakumbuka siku niliyokufuata hotelini nikiwa na Liv, akilia
sana, kipindi kile cha matatizo yetu?” Kimya. “Unakumbuka hata mama ulimwambia
asimwambie mtu kama unamtoto?” Kimya. “Kwa hiyo hata Grace hakuwa akijua kama
tuna mtoto. Alikuja siku ile ulipokuwa umechelewa kurudi nyumbani. Ukaenda
kulala hotelini kwa kuwa nilikwambia ikifika saa 12 jioni usirudi tena nyumba.
Grace na Danny walipokuja na kukutana na mtoto wasiyemjua. Anafanana na mimi.
Mama hawamjui wala hakuwepo pale. Grace alichukia sana. Akajua moja kwa moja ni
mtoto wangu mimi, halafu yeye akafichwa. Aliumia sana. Alianza kulalamika ni kwa
nini mimi na mama tumeanza kumficha mambo! Ndipo mama ikabidi amuelezee kila
kitu. Wakati akimuelezea alikuwepo
Danny na Fili pia.” “Lazima amtetee. Si ni mama yake?”
Likapita wazo kichwani mwa Nanaa, likamchafua kabisa moyo wake.
Geb
aliendelea kumuelezea lakini Nanaa alibaki ameinama. Akaanza kufikiria mambo
yote aliyokuwa akimshirikisha mama G. Akagundua ndio maana Zinda amefanikiwa
kutengeneza uongo unao fanana na kweli. Alijua amepata rafiki wa kweli, na siri
zake zipo salama. Lakini akagundua amemuamini mtu ambaye anaye watu wake. Geb
akaendelea kuongea.
“Kwa hiyo mambo yote anayozungumza Zinda sasa hivi, ameyatoa kwa Danny,
na Danny ameyatoa kwa mama?” Nanaa akanyanyua
uso na kuuliza wakati Geb akiendelea kuongea. Machozi yalishaanza kuchirizika
kama mvua. “Usifikiri kwa hivyo Nanaa!” Nanaa akacheka kwa kuguna huku akifuta
machozi. “Unajua nilimwamini
sana mama! Nilikuwa nikimwambia kila kitu change! Nikajisikia nimejenga
mahusiano mapya. Nikajiona ni kama nimepata sehemu yangu peke yangu. Kumbe
nilikuwa najidanganya tu! Na sijui ni kwa nini nimekubali kujifanya mjinga wa
kiasi hichi jamani! Nikasahau na kufumbia macho mahusiano niliyoyakuta kwenu!
Mna umoja ambao mimi nitabakia mtu wa nje tu.”
“Sio
kweli Nanaa.” “Ni kweli Geb. Hata
kama utatetea familia yako. Mimi nitabakia mtu wa nje tu. Hata wewe unahaki ya
kuwatetea. Mnamahusiano makubwa. Historia zenu zina mizizi. Mimi nimekuja
kwenye maisha yenu hata miaka miwili sijamaliza. Kwanza nimekuja ni kama
nimewatibulia mambo. Mimi nimekuwa mtu wa kuzungumziwa kati kati yenu. Habari
zangu zinazungushwa vile mtakavyo kwa kuwa nimekuwa mgeni niliyeongezeka na
matatizo yangu.” “Unakwenda mbali sana Nanaa.” Geb
akashangaa vile Nanaa alivyochukulia lile jambo. Hakutegemea.
“Usingewatetea, hata mimi ningekushangaa Geb.” “Siwatetei Nanaa!” Hamu ya chakula ilishamuisha
Nanaa. “Mama anakupenda sana.” Geb akaongeza. “Kiasi cha kutoweza kunifichia siri zangu? Kiasi cha kushindwa
kunisitiri kama anavyomsitiri Grace au wewe? Ananipenda kiasi cha
kunidanganya?” “Nanaa!” “Nini? Au mimi ndio nakosea sasa hivi? Ni
juzi tu, nimemuuliza mama tena mbele yako na kaka kama ni yeye ndiye ametoa
mambo yangu na kumpa Zinda. Akakataa mbele yako. Au umesahau?” Nanaa aliendelea kuongea taratibu huku akilia.
Sauti yake ilijaa uchungu wa namna yake.
“Hakukudanganya
Nanaa! Mama siye aliyetoa maneno na kuyapeleka kwa Zinda. Danny ndiye aliyetoa
hayo maneno.” “Naomba mimi
nikapumzike Geb.” “Tafadhali Nanaa!” “Nini Geb? Hakuna nitakachoongea hapa kikawa
sawa na kile unachotaka nifikirie wewe juu ya familia yako. Naogopa hata
kuendelea kuzungumzia juu ya hili jambo. Naomba yaishe.” “Yanaishaje Nanaa?” “Unataka kusikia nini Geb? Niambie kile unachotaka kusikia, ili
nikirudie uelewe yameisha.” Hawakuwa
wakiongea kwa sauti ya juu, lakini Geb hakupenda kumuona Oliva akimuona mama
yake akilia. Alibaki ametulia kimya akimwangalia mama yake. Kicheko kikaisha
kama anayeelewa. “Naomba twende chumbani Nanaa.” Nanaa akasimama. Akamchukua
mwanae, akatangulia chumbani.
Geb
alikusanya vitu vya mtoto wake, na kile kiti cha Liv, walichokuwa wamekuja
nacho, kwa ajili ya kumlishia chakula, akawafuata chumbani. Nanaa akafungulia
maji ya moto. Akatengeneza kwenye beseni la Liv kwa ajili ya kumuogeshea.
Akamtoa nguo. Akaenda naye bafuni. “Nikusaidie?” Geb akamfuata bafuni. “Hapana.
Asante.” Nanaa akaendelea kumuogesha mwanae. Kwa muonekano wa Liv, Geb akajua
mwanae amehisi mama yake hakuwa na furaha. Oliva alikuwa ametulia akimwangalia
mama yake muda wote. Hapakuwa na kucheka tena. Geb akajua amani imeshapotea.
Akamtoa
mtoto wake kwenye maji, akarudi naye kitandani kwake kumvalisha nguo za
kulalia. Akabaki amembeba kama ambaye hajui chakufanya. Geb akampokea mtoto.
“Nanaa! Tafadhali naomba yaishe.”
“Nimekwambia yameisha Geb. Au unataka kusikia nimeongea nini? Au hata nikisema
hayajaisha, unafikiri ndio itakuaje sasa? Sina chakufanya. Nimeshajua nafasi
yangu kwenye familia yenu. Basi, inatosha.” Geb
akanyamaza kidogo akamgeukia Oliva. Akamuona ametulia kabisa, nay eye anamwangalia
mama yake. Akambusu. “Nakupenda Liv!” Geb akamwambia mwanae lakini akapata
tabasamu badala ya kicheko alichozoea. Mpaka Nanaa akashangaa.
Geb akamuweka shingoni kama
alivyozoea, lakini Liv akajitoa akamgeukia mama yake, akabaki akimwangalia.
Nanaa alipomuona vile, akahisi kitu kimemkaba kooni. Akanyanyuka akatoka kwenda
nje kwenye baraza. “Kwanza wameninunua kwa pesa nyingi sana. Sina chakufanya.” Nanaa aliwaza wakati amesimama pale nje peke yake,
akiangalia asione chochote kwa mawazo. “Nilijua nimepata mtu wangu wa uhakika! Nilijua mama ndio atakuwa kama
mama yangu! Lakini naona nimejidanganya. Hawa watu wana mahusiano yao ambayo
hayawezi kuvunjika wala kuingiliwa. Mimi ni mgeni, na nitabakia kuwa mgeni tu.
Kwanza ujio wangu kwenye maisha yao umesababisha kuvunjika kwa mahusiano yao.” Akaendelea
kuwaza. “Nimebakiwa na kaka tu!”
Kila alipojitahidi kumuongelesha
Oliva, alionekana akili na macho yake yapo kule alipoelekea mama yake. Alibaki
akikodoa macho kama anayesubiri mama yake arudi. Geb akajua Nanaa analia huko
nje. Hakutaka kumtoa mwanae pale. Akajua atazidi kumuhuzunisha mtoto wake.
Akamuweka kitandani pamoja na michezo yake, yeye akatoka kule alipokuwa Nanaa.
Akaenda
kusimama pembeni yake. Akajifuta machozi. “Nataka nikalale. Usiku mwema.”
Nanaa akataka kuondoka. “Nanaa!” Nanaa akageuka. “Naomba tuzungumze.” Nanaa
akageuka vizuri. Akacheka kwa masikitiko. “Unajua nilidhani safari ya kuja huku ilikuwa kwa ajili yakutaka muda
na mimi, kumbe umegaramia pesa zote hizi ili kuja kuwatetea ndugu zako!” “Sio kweli Nanaa. Naomba hasira zisikufanye hivyo.”
Nanaa akaingia ndani, akabadili nguo. Akapanda kitandani akalala.
Habari nyingi za kukatisha tamaa
na kuharibu moyo wa Nanaa ziliendelea kupita akilini mwake na KUHARIBU THAMANI
NA GARAMA NZIMA ALIYOLIPIWA KUANZIA NA GEB mwenyewe, Mama G kusafiri mbali
akipambana mpaka kumlipia mahari, na kumalizana na mama James tena kanisani. Lile
jambo likakuzwa nafsi mwake na kusahau kabisa na yale aliyotendewa na Mungu.
Moyo wake ukaumia kupita kawaida, akasahau yote kwa hilo kosa lililomkumbusha
makuzi yake ya uchungu.
~~~~~~~~~~~~~
Maisha Hayatakosa Sababu ya Kukuyumbisha.
Kutoka kwenye mikakati ya kutulia, macho kwa
familia tu, wapenzi hawa waliokuwa na wakati mzuri sana mpaka kushuhudia Ukuu
wa Mungu, leo imetokea sababu nzuri inayoungana mkono na
hasira ya kuvunjika kwa amani.
Usikose Muendelezo.
Maji yametibuka..
0 Comments:
Post a Comment