Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Ni Wangu! - Sehemu Ya 40. - Naomi Simulizi

Ni Wangu! - Sehemu Ya 40.

 Giza lilikuwa limeshaingia wakati mama G, Danny na James  wanawasili hospitalini. Mishale ya saa ilikuwa ikionyesha ni saa mbili usiku. Mama G akampigia simu Geb, akamwambia atoke nje, lakini asimwambie Nanaa. Geb hakufurahia kabisa. “Kwa nini!?” Akamuuliza mama yake huku Nanaa akimwangalia. Alikuwa anacheza na Oliva hapo kitandani. “Nitakwambia tukionana.” Geb akafikiria kidogo. 

Hakutaka kumdanganya Nanaa. “Mama yupo nje, anataka nikazungumze naye. Nakuja sasa hivi. Sitakawia.” “Sawa. Naomba basi niachie Liv. Niendelee kucheza naye kabla mama hajamchukua.” Geb akaingiwa na hofu. “Naomba niondoke naye, tafadhali Nanaa. Liv anatambaa. Akienda mbali na wewe, halafu akataka kushuka, utamsaidiaje na wewe..” Akasita kumalizia. Nanaa akanyamaza.

Alimuona vile alivyoumia. “Nanaa, unajua sina nia mbaya.” “Nafahamu. Nenda naye tu.” Nanaa akajibu bila ya kumwangalia. “Naomba usinikasirikie. Nakupenda mpenzi wangu.” Nanaa akafuta machozi. “Asante.” Akavuta shuka akajifunika vizuri, asiamini ameshakuwa mlemavu wakushindwa hata kumtunza mtoto wake! 

Geb akambusu kwenye kipanda uso, akamnyanyua Liv. “Nitarudi muda sio mrefu.” Nanaa akatingisha kichwa kukubali. Geb na Oliva wakatoka. Nanaa alibaki pale kitandani akilia kwa uchungu. Gafla usingizi mzito sana ukamchukua. Akalala.

Historia ya Mira na Geb.

“Kwa nini mmenitoa kwa Nanaa? Ni kitu gani ambacho mmeshindwa kuzungumzia ndani!?” Geb aliuliza mara alipofika nje na kukutana nao wakimsubiri. “Unamfahamu Mira?” Mama yake akaenda moja kwa moja kwenye swali. Geb akakunja uso. “Mira yupi!?” Geb akauliza. “Wewe unamfahamu Mira yupi?” Mama yake akauliza tena. “Mira ambaye ni mfanyakazi wetu. Au muhasibu kwenye kampuni yangu. Kwani vipi?” “Ni msichana wa wapi?” Mama yake akadadisi tena na kumfanya bado Geb ashangae.

“Kama ni kabila nafikiri ni mtu wa huko kwa kina Zinda. Kwa sababu anafahamiana na Zinda. Kuna siku, zamani kidogo, Zinda alikuja pale ofisini kwangu. Mira akawa ameingia pale akitaka niweke saini kwenye karatasi fulani hivi. Zinda akamtamani yule dada. Nikamwambia amfuate tu ofisini kwake. Akamfuata. Baadaye Zinda akarudi tena ofisini kwangu na kuniambia amechukua namba zake za simu na kumbe Mira ni mtu wa kwao kabisa. Nikamtania na kumwambia ndio aoe kabisa. Akasema ni kama Mira ametokea kwenye ukoo wa kichawi kidogo. Huko kwao, kijijini kwao Tabora, ukoo wao kina Mira, hauna sifa nzuri, wazazi wake hawawezi kumruhusu kumuoa. Lakini akasema atamtafuta tu. Basi. Kwani vipi?” Bado Geb hakuwa ameelewa.

“Hujawahi kuwa na mahusiano naye?” Mama yake akahoji. “Huyo Mira!?” Geb akauliza kwa mshangao mkubwa sana. “Ndiyo.” “Hapana mama jamani! Si ungejua?” “Hujawahi kulala naye hata mara moja?” “Mama!!” Geb akashangaa zaidi. “Si unijibu tu?” James na Danny walikuwepo pale wakisikiliza. “Hapana! Kwani vipi, mbona maswali ya ajabu!?” Wote watatu wakaangaliana. “Jamani, naombeni mzungumze. Mimi natakiwa kurudi ndani kwa Nanaa. Nimemuacha peke yake.” Geb akasisitiza, akionyesha wazi hataki kupotezewa muda.

“Labda na mimi nikuulize kitu kingine Geb. Nani alimleta Mira kufanya kazi kwenye kampuni yako?” James akauliza. “Yeye mwenyewe alinitafuta. Nilikuwa nikifahamiana naye tokea nilipokuwa nchini India.” “Ooooh!” Wote watatu wakaitikia pamoja. “Kuna nini nyinyi? Mama!?” Bado Geb hakuwa anaelewa. “Huko nchini India mlikuwa na mahusiano gani na Mira?” Mama yake akauliza tena.

“Hatuku…” Geb akataka kukana kwa haraka, lakini akasita kidogo kama aliyekumbuka kitu. Akakunja uso kidogo. “Nini?” Mama yake akajua amekumbuka kitu. Kisha akatulia gidogo. “Mira ndiye anayehusika na kumtesa Nanaa? Maana na yeye alikuwepo siku ya kwanza ya kikao! Alikuja kumletea karatasi fulani Grace. Grace alimwambia azilete ili alinganishe na ripoti ya mwezi huo. Akaja siku ya ijumaa usiku. Akamkuta Grace yupo na heka heka ya kupigia watu wa chakula simu. Akiwasisitiza wasichelewe kesho yake. Tena hata mama utakuwa ulimuona ila utakuwa labda hukumtilia maanani. Watoto walikuwa wakilia. Grace alimwambia wazungumzie pale nje barazani ili wasikilizane. Baadaye Grace akaniita na mimi kuniuliza swali, mambo ya ofisini. Wakati Grace anazungumza na watu wa chakula, Mira alikuwa akisikiliza. Alipomaliza akamuulizia Grace, kuna nini. Nakumbuka kumsikia Grace akimtania na kumwambia kuna makulaji kesho kwenye kikao changu cha kwanza cha harusi. Halafu..” Geb akatulia kama akakumbuka tena kitu.

“Nini?” Mama yake akauliza. “Ni kama akabadilika kabisa. Sasa hivi ndio nakumbuka sura yake. Ni kama alikosa raha gafla na mawazo yake hayakuwepo tena pale. Nafikiri ndio maana Grace akamualika aje ahudhurie kesho yake. Akakubali bila ubishi. Lakini kwani nyinyi mmesikia nini?” “Subiri kwanza Geb. Mimi nakumbuka kumuona yule msichana siku ya ijumaa, lakini sio siku ya jumamosi kwenye kikao.” “Alikuwepo mama. Tena alikuwa amekaa karibu sana na sisi pale.” Geb akatulia kama anayewaza kitu.

“Turudi kwanza mlipokuwa nchini India. Mlikuwa na mahusiano gani?” Mama yake akaendelea kudadisi. “Nilipofika mwaka wa mwisho huko huko India, nilikuwa sina tena pesa za kuishi kwenye nyumba yangu peke yangu au ya watu wawili. Ikanilazimu kutafuta sehemu ya kujishikiza huku namalizia chuo. Nikapata chumba walipokuwa wakiishi Mira na wasichana wenzake. Nikahamia hapo mimi na kijana mwingine. Tukawa tukitumia chumba changu. Pesa niliyokuwa nikilipa hapo kwa ajili ya pango, ikawa ndogo sana. Kwa kuwa kwanza ilikuwa chumba kimoja tulichokodi kwa kina Mira, halafu tulikuwa na mwenzangu kwenye hicho chumba. Maisha yakaendelea kwa unafuu.”

“Mira akaanza kuhangaika mara aingie chumbani kwangu achukue nguo zangu chafu afue, mara atake kunipigia pasi nguo zangu. Akawa akipika anataka na mimi nile naye. Ikawa heka heka kweli. Nikawa nakosa utulivu. Narudi chumbani nakuta vitu vyangu vimepangwa, nguo zimefuliwa. Nikimuuliza yule jamaa, akawa ananiambia ni Mira. Na labda anakuwa ameleta na chakula. Ameniachia hapo chumbani. Sasa yule jamaa niliyekuwa nikiishi naye kwa kuwa alikuwa akinijua sipendi kula vile vyakula, yeye akawa anakula. Nikirudi alikuwa akiniambia, ‘nimekula chakula alichokuwa amekupikia Mira kwa kuwa nilijua hutakula.’ Nikamwambia ni lazima nimwambie Mira. Ajue ili asihangaike kunipikia. Mimi sitaki kufuliwa wala kupikiwa. Yule jamaa akanisihi niache kwa mwezi huo mpaka atakapotumiwa pesa kutoka nyumbani kwao. Hakuwa na pesa.” Geb akaendelea.

“Tena jamaa mwenyewe alikuwa ni mtu wa kutokea Nigeria. Basi. Nilipoona heka heka za Mira zinazidi huku anajitangazia kwa watu kuwa mimi ni mpenzi wake, ikabidi nimtoe kwa chakula cha usiku ili nikazungumze naye. Tulitoka. Nikwambia ukweli. Kwamba nipo pale kwa sababu nilifeli chuo sababu ya mwanamke mwingine niliyekuwa nae kabla sijahamia hapo nchini.”

“Nikamwambia kwa wakati huo sipo tayari kabisa kwa mahusiano na mwanamke yeyote yule. Akaniomba sana tena kwa machozi. Tena nakumbuka aliniambia, endapo nitafikiri kuoa, anaomba iwe yeye. Nikamwambia yeye ndio anaanza chuo hapo India. Mimi nimebakiza muda mchache naondoka hapo, nisingeweza kumuahidi mambo ya mbeleni. Mira akaniambia anaomba tu hata ahadi ya kuja kumfikiria baadaye. Nikamjibu sawa. Tukaachana. Yaani leo ndio mnanikumbusha!”

“Hata mwaka jana alipokuja kuniomba kazi ya uhasibu kuwa alimaliza chuo na akajaribu kuishi sijui ni India sijui wapi! Hata sikumfuatiliza, alikuja nikiwa na mambo mengi, sikumtilia maanani. Lakini ninachojua nilikuwa na shida na muhasibu. Nikamuajiri. Yaani hivi leo ndio hata nimekumbuka hayo mambo yote. Hata nilishasahau kama hata niliishi nyumba moja na Mira! Kwanza sijui nilikaa kwao muhula mmoja tu. Yaani kama miezi 4 tu!”

“Aaaaahhh!” Danny, James na mama G wakawa wameunganisha matukio yote. Wakawa wameelewa. “Kwani vipi!?” Wakamsimulia Geb mwanzo wa kikao mpaka mwisho. Kuanzia mama James, mpaka habari za Mira. Geb akabaki ametulia. “Kwa hiyo Mira anadai wewe ni mume wake. Na Zinda ametoa uthibitisho wa kweli kabisa ambao mchungaji amesema hawezi kutangaza tena ndoa yenu. Na Zinda ameapa pale mbele ya wote, amesema atahakikisha hutamuoa Nanaa.” Mama yake akaongeza.

“Mimi nitamlilia Mungu wangu, mama. Nimeamua kutulia kwa Mungu. Nanaa ni mke wangu mimi. Ananipenda na amenichagua mimi. Waacheni tu, na Mungu aliye hai. Najua kwa hakika atanitetea. Kwa kuwa nikweli sijamtendea mtu yeyote yule lililo baya.” Geb akajibu.

“Naombeni mimi nirudi ndani kwa Nanaa.” Wote walibaki kimya. “Kwa hiyo tufanyaje Geb? Mchungaji amesema hatafungisha tena hiyo ndoa!” “Naomba nipe siku ya leo na kesho Danny. Sasa hivi sina jibu la haraka. Ndio mmeniambia. Nahitaji muda wa kufikiria. Lakini, naomba mumuache kwanza Nanaa. Anayopitia sasa hivi yanatosha. Sitaki tena aongezee mambo mengine.” “Juu ya Mira? Labda ni vyema amjue mbaya wake.” James akaongeza.

“Itasaidia nini?” Geb akauliza huku amekunja uso. “Haitamsaidia kitu chochote. Sasa hivi Nanaa amefika mahali karibu sana na Mungu. Nanaa ameonyeshwa na Mungu na amemuahikishia yupo vitani kwa ajili yake. Nawaomba mumuache Mungu afanye kazi. Mtakapomtaja Mira sasa hivi kwa Nanaa, mtatoa macho yake kwa Mungu, mtamrudisha kwa wanadamu. Sina mpango wa kwenda kwa mganga. Naomba nimuachie tu Mungu. Naamini atapigana na adui zetu. Sijui kama mmenielewa?” Geb akauliza, kimya. 

“Labda ni weke hivi, siruhusu mtu yeyote yule azungumze na Nanaa jambo lolote lile, ila mimi mwenyewe. Kama hivi mlivyofanya, nashukuru. Umenisikia James?” “Nimeelewa Geb.” “Asante.” Geb akarudi ndani. Akawaacha wanaangaliana.

~~~~~~~~~~~~~

Alimkuta Nanaa amelala usingizi mzito hata hakujitingisha wakati wanaingia na Liv. Mama G akaingia. “Anaendeleaje?” “Ameshinda vizuri tu. Hata ameniomba kama ninaweza kumuombea arudi nyumbani. Lakini nimemwambia asubiri kidogo.” Geb alijibu huku akimwangalia Nanaa. Danny na James nao wakaingia. “Nampenda Nanaa, mama. Ni kila kitu changu kwenye maisha yangu.” “Najua Geb. Mungu atawasaidia.” Geb akabaki akimwangalia.

“Umemlisha huyo?” Mama G akauliza akimaanisha Liv. “Nimemlisha wakati mama yake anakula.” “Amekula vizuri?” Geb akanyamaza. “Geb?” “Alililia nyonyo sana. Mpaka mama yake akashawishika kumnyonyesha.” “Kwa hiyo amenyonya!?” “Imebidi mama. Wote wawili yeye na mama yake walikuwa wakilia sana. Nikashindwa chakufanya. Amenyonya na kulala hapo hapo kwa mama yake. Na ndio Nanaa naye akaweza kupata usingizi wa mchana. Sijui itakuaje mama!” “Wala usiogope Geb. Naomba urudie ujasiri uliokuwa nao jana na leo asubuhi. Sisi wote tunakutegemea wewe. Naomba usitetereke. Mwache Nanaa amnyonyeshe mwanae kama anataka. Mungu alishatuonyesha ulinzi wake kwa huyu mtoto, hakuna mwanadamu atakayeweza kumdhuru.” Geb akavuta pumzi.

“Kwa hiyo kesho utamrudisha?” Geb akauliza baada ya ukimya wa muda kupita. “Kama ananyonya, nitamleta na kile kitanda chake kidogo ili akae na mama yake tu. Na mimi nitakuwepo. Kwa hiyo na wewe unaweza kuondoka kurudi nyumbani ukapumzike kidogo.” “Siku nitakayorudi kulala pale kitandani, ni siku nitakayokuwa na Nanaa, mama. Siwezi kumuacha Nanaa hapa hospitalini, eti mimi nikalale nyumbani! Hapana. Wewe mlete tu Liv na vitu vyake, ukamsaidie Grace na watoto.” “Sawa. Mungu atawasaidia Geb. Tunawaombea.” Geb alimkabidhi mama yake mtoto, akamsogelea Nanaa. Akamvuta mkono, akaubusu.

“Atapona tu.” Geb aliongea huku akimwangalia Nanaa. “Hakika Mungu atawasaidia. Umebadilika sana Geb! Hakika umenipa somo. Na ujue najutia mambo anayofanya mama yangu.” “Usijali kabisa James. Ipo siku tutayaangalia haya yote, yatakuwa nyuma yetu. Tutasahau kabisa. Nashukuru kwa kuwa na sisi. Hasa Nanaa. Anakutegemea sana wewe. Usikubali uongo wa Zinda ukakuingia. Nanaa anakutambua wewe kama baba na kila kitu kwake. Na mimi naliheshimu hilo.” “Nashukuru.” James akaridhika na kutulia. Alishapoteza ujasiri kwa Geb.

          “Jamani! Ngoja  sisi tuondoke. Nitamrudisha huyu kesho.” Mama G akaaga. “Naomba kukuaga Oliva Magesa.” Geb akamsogelea mwanae na tabasamu. Liv akacheka. “Useme vizuri wewe Geb! Oliva Magesa tupo wawili hapa mjini!” Wakacheka. “Namaanisha mrembo wa Geb.” “Hapo sawa.” Mama G akajibu.

“Haya, njoo mbusu mama.” Geb akamuinamisha Liv kwa mama yake. “Mwaaa mama Liv.” Geb ndio akaongea kwa niaba ya mwanae. “Usimsumbue bibi. Ulale mpaka kesho. Sawa?” Oliva akacheka kama kawaida yake. Geb akamuweka kifuani. Akamkumbatia kwa nguvu.

Mhhhhh! Nakuombea usingizi mzuri. Mkono wa Mungu uendelee kuwa juu yako Liv. Ulinzi wa ki Mungu ukakuzingire. Nakubariki kwa baraka zooote, za rohoni na za mwilini. Uzima wako umefichwa ndani ya Kristo Yesu. Kila silaha itakayoinuka kinyume nawe, Liv, ikakutane na uwepo wa Mungu. Mungu apigane na adui zako. Kila ulimi utakao inuka kinyume nawe, Liv, Bwana auhukumu mkosa. Natamka uzima juu yako. Malaika wa Bwana wafanye kituo juu yako, Oliva Magesa. AMEN.” Geb alikuwa akimuombea mwanae huku amemkumbatia. Akamtoa kifuani kwake akamnyanyua juu. Olivia akaanza kucheka mpaka watu wote wakacheka. 

“Mchekaji kama mama yake!” Bibi yake akamsifia. “Niwasindikize mpaka kwenye gari?” “Hapana bwana! Atakulilia. Kwanza nipe Oliva wangu.” Olivia alichukuliwa na bibi yake huku akicheka. “Danny, nijie na mizigo yote.” “Sawa mama.” Mama G akataka kutoka. “Mama!” Geb akamuwahi. Akamkumbatia yeye na Liv. “Asante sana mama yangu. Nashukuru kwa yooote.” Geb akambusu kichwani.  “Asante kushukuru. Uniagie Nanaa akiamka.” “Sawa.” Ndipo akatoka.

~~~~~~~~~~~~~

 “Geb!” Danny akamwita. “Vipi?” Geb akamgeukia. “Naomba unisamehe sana. Nahisi mimi ndiye nimempa nyenzo nzuri sana Zinda, za kukuangamiza. Naomba unisamehe. Lakini unajua ukaribu niliokuwa nao na Zinda. Ni kama..” “Danny! Huko sipo akili zangu zipo kabisa. Naomba uniamini sipo hata kwenye kumlaumu Zinda mwenyewe. Naomba uwe na amani kabisa. Sisi wote tulikuwa marafiki wa karibu sana. Kutoa neno kwangu na kulipeleka kwa Zinda, sio kitu ambacho sikutarajia. Nilikuwa nikifahamu.” “Lakini nimekoma.” Danny aliongeza kinyonge.“Hata mimi nimejifunza sana. Aisee!” James akaongeza.

“Najua kwa hakika Mungu atatuvusha hapa. Ila sijui ni lini! Lakini najua kwa hakika tutatoka tu. Mungu atatusaidia.” Geb aliongea huku amerudisha macho kwa Nanaa. “Tunawaombea Geb.” “Asanteni sana. Nipeni muda na mimi nimuulize Mungu wangu. Nione atanijibu nini juu ya hili. Najua ipo njia. Ni mimi tu kutulia na kufungua macho ya kiroho ili kuiona na kuifuata. Mungu hakukusudia kunipa familia nzuri hivi halafu iangamie! Hapana. Iko sehemu atataka niifikishe familia yangu. Acha nimuulize Mungu njia.” Hakika Geb alibadilika na kuwashangaza rafiki zake. Wakamuaga, na kumuacha hapo amesimama pembeni ya kitanda cha Nanaa akionyesha wazi hataki kutolewa macho yake msalabani kwenye uponyaji nakusikiliza kesi au majuto yao. Kila walipotaka kumpeleka nje ya Mungu, alirudisha mawazo yake kwa haraka sana.

Usiku Wa Pili Hospitalini.

Kwa kuwa walikuwa wameshakula, akaingia kuoga hapo hapo bafuni. Akatoka. Alivuta kiti pembeni ya kitanda cha Nanaa. Akaanza kusoma neno la Mungu, bibilia. Kisha akapiga magoti pembeni ya kitanda, akamshika Nanaa mkono na kuanza kuomba. Geb aliomba kwa muda mrefu. Kwa machozi huku akimueleza Mungu yote aliyoambiwa yaliyotokea kwenye ofisi ya mchungaji. “Sijui nifanye nini Mungu wangu! Naomba nisaidie. Hakika nimekwama.”  Geb alilia mbele za Mungu. Alitamani kama malaika wa Mungu atumwe wakati huo huo ajibu kitu. Lakini hakuona malaika yeyote. Akatamani kama asikie sauti fulani ikimwambia wakati huo huo kitu cha kufanya. Akajaribu kutulia ili kusikiliza. Lakini kukawa kimya.

Nesi aliingia, akamkuta amepiga magoti pembeni ya kitanda cha Nanaa huku ameinamisha uso wake kitandani hapo. Nanaa alikuwa amelala usingizi mzito haswa hata hakuwa na habari na kinacho endelea. Nesi alimsafisha vizuri, akamuacha msafi. Akaondoka bila hata kumsemesha Geb. Aliendelea kuomba mpaka akamaliza, kisha akavuta kiti, akalala huku ameegemeza kichwa pembeni ya Nanaa. Alijiwekea mkono wa Nanaa juu ya kichwa chake. Hapo hapo akapitiwa na usingizi.

Ndoto Ya Pili Ya Nanaa.

          “Nanaa!” Alisikia mtu akimuita akiwa usingizini. Akastuka. Alimuona mtu amesimama pembeni yake akiwa amevaa nguo nyeupe. Akajua lazima atakuwa ni daktari. “Nimekuja, nimetumwa kwako.” Nanaa akakaa vizuri ili amtizame. Akajaribu kumuangalia usoni, akapata shida kumuona. Uso wake ulikuwa ukiwaka sana. Mwanga mkali. “Umetumwa na nani?” Nanaa akauliza huku akijaribu kufinya macho yake ili kumtizama. “Na Yupo, ambaye Yupo.” Mwili wa Nanaa ukaanza kutetemeka. Akaendelea kumtizima kwa shida, asiweze. “Upo tayari?” Akamuuliza. “Umesema umetumwa kufanya nini?” Nanaa akauliza. 

“Kuna vitu vyakutoa miguuni mwako.” Yule mtu aliyekuwa amevaa koti jeupe la kidaktari akasogea mpaka miguuni kwa Nanaa. Akamfunua akawa anaiangalia ile miguu. Nanaa alikuwa anaogopa kuiangalia miguu yake. “Unajua nimeshindwa kabisa kuingalia hiyo miguu? Geb mpenzi wangu, ndiye anayenisaidia kuingalia.” Nanaa aliongea huku amefunga macho kwa kutumia mikono yake. “Leo ndio mara ya mwisho. Hutaiona tena hivi ilivyo.” “Unauhakika unaweza kunisaidia? Maana daktari mwenzio aliwatuma hawa manesi kufyonza maji. Lakini hata jioni hii nimewasikia wakimwambia Geb hapo nje kuwa wamejaribu kunifyoza tena, imerudi kujaa tena. ” Nanaa alijieleza. 

“Kwa kuwa hawajatoa mzizi wake. Zipo sindano katikati kabisa ya kila mguu. Aliziweka katikati ya kila mguu wako. Ndio inabidi kutolewa kwanza.” Nanaa akashituka sana akafungua macho kujiangalia. “Wapi!?” Alipofungua macho kuangalia, akagundua kile chumba kimejaa mwanga mkali sana. “Mbona sioni miguu yangu? Punguza mwanga wa taa na mimi nione.” Nanaa alilalamika huku jasho likimtoka. “Huwezi kuona. Ni nyuma ya miguu yako. Geb atakapopima ukubwa wa upana wa vidole vyake, mara moja na nusu kwenye miguu yako. Utagundua kuwa ni katikati ya mguu wako. Atakapopasua ndani kabisa, ataona sindano katika kila mguu. Zilichomekwa hapo. Azitoe.” Yule mtu ambaye Nanaa aliyemtambua kama daktari kwa koti jeupe aliloliona Nanaa kwa shida,  akatoa hayo maelezo. Yakamchanganya Nanaa.

“Sijaelewa ni wapi! Kwanza na nani? Nani ameniwekea hizo sindano?Nanaa akaanza kulia huku akihangaika kutazama asiweze. Mwanga kutoka kwenye uso mkali wa yule mtu ulikuwa mkali sana. Aliona akiwa ameshamgeza, na mikono yake imegusa miguu yake. “Hizi hapa.” Yule mtu aligusa kwa nguvu kidogo. Alikuwa ameweka kidole sehemu ambayo kwa mara ya kwanza tokea siku ya kikao chake cha kwanza cha harusi, Nanaa alipopoteza uhusi wa miguu yake, hapo huyo mtu alipopagusa aliweza kuhisi ameguswa. “Nimehisi vidole vyako katika kila mguu wangu!” Nanaa aliongea kwa furaha sana.

          “Basi hapo ndipo zilipofichwa hizo sindano.” Moyo wa Nanaa ukajawa furaha. “Hakika wewe ni daktari bingwa. Wenzako wamejaribu kunisaidia wameshindwa. Naomba basi nitoe.” Nanaa alikuwa amelala fudi fudi. “Utanitoa?” Nanaa akauliza. Lakini kimya. “Tafadhali nisaidie. Geb anateseka. Nina mtoto mdogo anaitwa Oliva. Bado ananihitaji. Naomba nihurumie. Hapa nilipo ni mjamzito. Mungu ametubariki mtoto mwingine. Sitaki niwaache wanangu kama mama yangu alivyoniacha mimi. Tafadhli naomba nisaidie.” Nanaa alikuwa akilia sana. “Tatizo lako limekwisha.” Yule mtu akajibu hivyo, kisha kimya. Nanaa akashituka kutoka usingizini. Cha kwanza akajifunua miguu yake kwa haraka. Akajikuta yupo vile vile.

~~~~~~~~~~~~

Alilia, mpaka Geb akaamka na nesi akaingia. “Kuna nini?” Nanaa aliendelea kulia. Geb akapanda kitandani, akakaa upande. Akamvuta karibu akamkumbatia. “Nimeota nimepona Geb.” Nanaa aliendelea kulia. Alilia kwa muda mrefu. “Kabisa aliniambia tatizo langu limekwisha.” “Nani?” Geb akamuuliza huku yule nesi amesimama pembeni akimuhurumia Nanaa. Alijiambia ndio madhara ya kuomba sana. Alimuona vile Geb na Nanaa wakiomba. Akajiambia wamejiwekea tumaini la bure! Yule nesi alibaki kimya akisubiri Nanaa atulie, amfunike tena.

“Naomba utulie tuzungumze Nanaa.” Baada ya muda, Nanaa akatulia. Akamsimulia Geb habari nzima. Mwanzo mpaka mwisho. “Aliniita kabisa, nikashituka kutoka usingizini. Haikuwa ndoto mpenzi wangu. Naomba uniamini. Nilikaa. Akanishika kabisa.” Nanaa aliendelea kusisitiza huku akilia. “Hizo ni ndoto za kawaida hasa ukiomba sana. Akili inajiandaa kwa majibu. Lakini hakuna daktari mpya aliyekuja hapa. Kwa sababu kama angekuwa amekuja, sisi manesi ndio tungekuwa wa kwanza kum..” Yule nesi aliingilia. “Naomba unyamaze kwanza.” Geb alimkatisha. “Tafadhali nyamaza.” Geb akasisitiza.

“Nanaa! Mimi nakuamini. Lakini aliyekutembelea hakuwa ni daktari. Ni malaika wa Mungu. Hata mimi nimesikia ndotoni nikiitwa. Nilipoitika, nikasikia tu neno moja, ‘USIOGOPE’. Nikajua ni akili zangu tu, kwa maombi niliyoomba wakati nimelala. Lakini hakika ni Mungu.” “Asante kuniamini Geb. Sasa tufanyaje?” Nanaa akauliza. “Tuchukue hatua ya Imani. Hatuna cha kupoteza. Si umesema husikii maumivu kwenye miguu yako?” “Bado sihisi kitu. Imekufa ganzi vile vile.” “Basi naomba unipe tena maelekezo uliyopewa unipe. Mungu ameniambia nisiogope. Na amekutuma wewe uniambie mimi ndiye nitoe hizo sindano. Acha nizitoe.” Yule nesi akashangaa.

“Nashauri mumsubiri daktari. Usije ukamtoboa, halafu kesho ukanitafutia mimi matatizo kwenye uongozi!” Yule nesi akaweka kipingamizi. “Wewe si umeniambia kila ukimfyoza maji malengelenge yanajaa tena?” “Ndiyo.” Nesi akajibu kwa kujiamini asijue anaongea na Geb mwenye uwezo mkubwa sana wakufikiri.

“Basi. Kama hakuna sindano, inamaana nikimaliza, yatarudi tena vile vile. Naomba kaniletee kitu kikali, ambacho kitakuwa kipo sterilized. Mimi mwenyewe nitafanya.” Nanaa akambusu Geb. “Asante.” Geb akarudisha tena busu. “Mungu wetu anaishi Nanaa.” Kwa kuwa Geb alishawalisha na kuwanywesha. Halafu akawa akiwashukuru kila wakimfanyia kitu Nanaa, zaidi ya hapo yupo chumba cha peke yake kwenye hospitali hiyo ya kulipia. Inamaana pesa ipo. Heshima kutoka kwa wauguzi hao, ilikuwepo kwa Geb. Nesi akatoka.

~~~~~~~~~~~~

Ilikuwa yapata saa nane usiku, wakati nesi ameleta kila kitu na kumsaidia Geb kumgeuza Nanaa. Nanaa akalala kifudi fudi. “Naomba urudie tena maelezo yake.” Geb alikuwa tayari amevaa gloves na ameshika kisu cha upasuaji mkono wa kulia. “Fungua vidole vyako. Gumba na kile kinachofuata. Nyoosha kabisa. Pima mara moja na nusu, kuanzia chini kwenye kiungo cha mguu na nyayo kuja juu. Weka hapo kidole. Ninatajua.” Nanaa akatoa maelekezo kwa hakika.

“Sasa utajuaje akikugusa wakati miguu yako imekufa ganzi!?” Nesi alitoa neno jingine la kukatisha tamaa. Akamtia wasiwasi Nanaa. Akasita. “Lakini yeye aliponigusa, nilijua. Pengine na Geb akinigusa kama ni hapo, nitajua.” Nanaa akajibu huku akitetemeka. “Nanaa! Naomba usiogope. Hatuna chakupoteza. Tulia nikupime.” Nanaa akarudisha uso kwenye mto. Geb akaanza kumpima.

Hatua ya kwanza. “Unanisikia? Hiyo ni hatua ya kwanza.” “Hapo umenigusa?” Nanaa akauliza huku akilia kwa hofu maana hakusikia chochote. Inamaana yule nesi alikuwa sahihi. Ni mawazo tu. Haikuwa ndoto au maono kama alivyosimulia. “Lakini ndio hatua ya kwanza Nanaa. Usiogope.”  Geb akajaribu kumtuliza. “Labda huyo nesi yupo sahihi Geb. Ni ndoto tu. Sisikii kitu kabisa.” Nanaa aliendelea kulia akisikika amekata tamaa.

“Niliwaambia mimi. Naombeni muache tu jamani!” Nesi aliendelea kusisitiza hoja yake. “Mambo hayo mnayaona kwenye luninga tu. Wachungaji siku hizi wanafanya kama maigizo tu ili kuvutia watu. Hakuna kitu kama hicho!” Nesi aliendelea. Nanaa akazidi kulia. Geb akaweka kila kitu pembeni, akarudi kumtuliza.

Akapiga magoti pembeni yake. “Naomba niangalie na kunisikiliza mimi, Nanaa.” Nanaa alikuwa amejawa jasho, machozi na kamasi uso mzima, akamgeukia. “Naomba nipe nafasi ya kujaribu mpenzi wangu. Tafadhali. Uliniahidi utasimamia imani yangu. Basi mimi naamini. Naomba nifanye. Na hata kama huoni sababu yakufanya hivyo, basi fanya kwa ajili ya Oliva na mtoto.” “Haya.” Nanaa akakubali. “Haya?” Geb alimuuliza tena kutaka uhakika. “Nitafanya kwa ajili yako na watoto. Lakini nimeingiwa na hofu Geb. Kama kweli alikuwa malaika, kwa nini yeye mwenyewe asitoe!?” Nanaa akauliza swali ambalo lilikuwa ni kweli na maana. “Sijui Nanaa. Ila ninachojua, nataka kufanya.” “Sawa Geb.” Nanaa akakubali.

“Naomba rudisha uso kwenye mto. Tulia tu. Kama nikigusa, na wewe ukasikia, utaniambia.” “Kama asiposikia, bado utamtoboa?” Nesi akaingilia tena kwa swali. Geb akamwangalia. “Samahani. Nataka kujua tu.” “Nitafanya kutokana na imani sio vile atakavyojisikia.” Geb akajibu, na kurudi kule miguuni. Akapima mara moja na nusu, akaweka kidole. Akabonyeza mara ya kwanza. “Ni hapa?” Geb akamuuliza Nanaa. “Sisikii kitu Geb.” Geb akasogeza tena kidole pembeni.

“Hapa?” “Hapana.” “Hapa?” Geb akagusa tena kwingine. “Sisikii kitu.” Geb akatulia. Akarudia kupima tena akagundua ni pale alipogusa mara ya kwanza. Akabonyeza kwa nguvu zote. “Auuuuu!” Nanaa akalalamika. Geb akaruka. “Umesikia kitu Nanaa!?” “Umenigusa kwa           nguvu! Nimesikia    kama sindano.Imenich...” Nanaa akashituka. “Geb Sindano! Sindano Geb! Sindano!” Nanaa akapiga kelele.  Nesi akasogea karibu kushangaa.

Geb alikuwa ameshapapoteza kwa kushituka. Lakini akarudia tena kupima. Lakini safari hii akarudia kwa ujasiri, akijua ni hakika. Akaanza kumpima tena. Akafika pale pale. “Ni hapa?” “Bonyeza kwa nguvu Geb.” Geb akaongeza nguvu. “Sisikii tena.” “Subiri.” Geb akarudia mpaka akapafikia. “Hapo hapo.” Geb akakaza moyo. Akaanza kumkata. “Unasikia maumivu?” “Sisikii kitu kabisa.” Geb akaendelea. Akafika chini kabisa. Akahisi ni kama ule mguu wa Nanaa umevalishwa limfuko chafu. Akaendelea kukata mpaka chini kabisa. Ni kweli akakuta kichwa cha sindano kama pini ya ofisini ya kushikilia karatasi. Akavuta juu. Ikatoka. 

“Nanaa!” Geb akaita huku ametoa macho. Gafla ule mguu ukaanza kupasuka kuanzia juu ya ule uvimbe, mpaka chini. Maji yakamwagika, ‘pwaa!’ kama maji yaliyomwagwa. Yakatapakaa mpaka sakafuni. “Kuna nini Geb!?” Nanaa akauliza kwa mshituko. “Umepasuka! Maji yote yamemwagika! Inauma?” “Hata kidogo! Sisikii maumivu.” Nanaa akajibu huku akifuta machozi. Geb akasogea, akamfinya mguu akiwa ameshikwa na mshangao mkubwa usoni.

“Hapo je?” “Hapo nimesikia.” Geb akaanza kuruka ruka kwa furaha. “Nifanyie na huo mwingine Geb.” Nesi alikuwa ametoa macho karibu yaanguke. Geb akafanya kwenye mguu ule mwingine kama alivyofanya mwanzo. Ikawa kama mguu wa kwanza. Akafanikiwa kupata ile pini, akaivuta. Maji yakamwagika tena. “Naomba uchukue hatua nyingine ya imani, ugeuke Nanaa.” Nanaa akageuka kwa tahadhari, huku akilia kwa sauti ya juu. Bado kulikuwa na  ngozi zilizokuwa zikining’inia kwenye miguu yote miwili. Kama matambaa.

Nanaa alikuwa amefunga macho akilia. Wauguzi wengine wakaja kuangalia kulikoni. Wakabaki wameduaa. Geb alikuwa akijaribu kutoa yale mangozi yaliyokuwa yamening’inia. “Unaumia?” Geb akauliza. Nanaa akatingisha kichwa kukataa. Geb akakazana kuyavuta huku akiyatupa sakafuni. Mwishoe akaamua ayavue kama soksi. Akakwangua kuanzia chini ya goti, taratibu ili asimuumize, kisha akavuta. Lilianguka ngozi kama la kenge kutoka kwenye mguu wa kulia wa Nanaa. Geb akapata ujasiri kufanya hivyo hivyo kwenye mguu wa kushoto. Akavua lile ngozi. Lilikuwa likitisha sana. Akatupa sakafuni.

~~~~~~~~~~~~

Wakati mwingine Mungu huzungumza nasi kwa njia ya ajabu na tofauti na uelewa wa mwanadamu. Ni rahisi kupuuza na kutotilia maanani. Hasa unapokutana na vipingamizi vinavyofanana na kweli kama huyo nesi. Njia za Mungu zipo juu sana. Hazichunguziki kwa akili za kibinadamu. Bibilia inasema. {1kor 1:25 Kwa maana upumbavu wa Mungu una hekima zaidi kuliko hekima ya wanadamu, nao udhaifu wa Mungu una nguvu kuliko nguvu ya wanadamu.}  

Wakati mwingine Imani ya mtu mwingine inaweza kukutoa sehemu moja hadi nyingine. Kukushusha au kukupandisha. Kuwa makini nani anatembea karibu na wewe. Nani unampa sikio lako! Bibilia inasema {Muhubiri 4:9-11 Wawili ni afadhali kuliko mmoja, kwa sababu wana malipo mazuri kwa kazi yao. Kama mmoja akianguka, mwenzake atamwinua. Lakini ni jambo la kuhuzunisha kwa mtu yule aangukaye naye hana wa kumwinua!”

Bado Mungu anatenda miujiza. Hajawahi kuacha. Pengine alishajibu ni wewe kutembea kufikia muujiza wako. Tumekuwa tukitingwa na mengi nakushindwa kumsikia Mungu au kukubaliana na kile Mungu anachotujibu kwa kuwa hakileti maana kwenye ufahamu wetu.

~~~~~~~~~~~~

Miguu ya Nanaa ikarudi kuwa kama ya mtoto mchanga. Laini. Haina hata kipele wala doa! “Sasa hivi unaweza kufungua macho Nanaa. Mungu amekurejeshea miguu yako.” Geb mwenyewe hakuwa akiamini zile nguvu alizipata wapi. Akabaki ameduwaa kwa muda huku machozi yakimtoka kwa hofu ya Mungu iliyokuwa imemkamata. “Nanaa! Fungua macho ushuhudie kile Mungu ametutendea.” Akaikunja miguu yake na kuinyosha huku akilia. Kisha akafungua macho. Hakuwa akiamini. Ikabidi yule nesi asimulie manesi wengine kile kilichotokea. Wakaona na zile pini. Walioweza kuchukua video wakachukua. Lakini Geb akakataa kabisa Nanaa asichukuliwe video wala asipigwe picha.

“Ninahamu ya kuomba nikiwa nimepiga magoti, kama wewe Geb.” Geb akacheka. “Shuka basi kitandani. Nikushike mkono?” Nanaa akatingisha kichwa kukubali. Geb akaenda kumshika mkono. Akashuka. Akajaribu kutembea, akaweza. Nanaa alizidi kulia. Hapo hapo akasujudu chini. Alipiga magoti pembeni bila kujali yale maji machafu pale sakafuni akaendelea kulia huku akimshukuru Mungu. Geb aliomba wapishwe. Wote wawili walikuwa wakilia kwa furaha.

 “Mtataka nije kutoa catheter?” Nesi akahoji. “Tafadhali. Halafu nisaidie taulo safi na nguo za kubadilisha. Nataka akaoge. Kisha naomba utusaidie kusafisha hii sakafu.” “Hizi ngozi nitupe? Au mnataka niwahifadhie.” Nesi aliendelea kuhoji. “Huo ni uchafu wakutupa tu.” Geb akajibu. “Na hizi pini? Hamtataka kutunza kumbukumbu?” Nesi alihoji tena. “Sio mali yetu. Hututahitaji. Ila nitataka nizitupe chooni ili zisije zikatumiwa na mtu mwingine tena.” Geb akazichukua na kwenda kuzitupia chooni. Aka flush. Akahakikisha zimeenda ndipo akatoka.

“Njoo Nanaa. Nataka akutoe hiyo catheter ukaoge vizuri, ukiwa umesimama bafuni. Sio kufutwa ukiwa kitandani.” Geb alimnyanyua pale sakafuni. Nesi akamchomoa ile catheter na dripu. Geb akamchukua. “Nisaidie na shuka safi. Nitatandika tu mwenyewe. Nisikusumbue zaidi. Na wewe ukapumzike.” “Wala usijali kaka yangu. Mimi mwenyewe nimejawa furaha, nahisi usingizi umetoweka.” Nesi na Geb wakacheka.

Alimsubiria Nanaa akaoga, akamsaidia kumkausha. Wakatoka wote wakiwa kama wapepigwa na butwaa. “Naomba tuombe wote tena Geb.” Walikuwa wamekaa kwenye kochi. Wakapiga tena magoti. Wakaanza kuomba. Waliishia kulia mbele za Mungu. Hofu ya Mungu iliongezeka ndani mwao. Nanaa asiamini kama amemuona malaika wa Mungu. Na amepokea uponyaji wa namna ile. Magoti peke yake ikawa haitoshi. Wakainama kabisa kumsujudia Mungu wao kana kwamba wapo mbele ya kiti cha Enzi cha Mungu. Zilikuwa shukurani zilizojaa Imani ya ajabu. Iliwachukua dakika 40 kumaliza.

~~~~~~~~~~~~

Wakarudi kukaa. “Unataka kulala kidogo?” Geb akamuuliza Nanaa. “Nataka kurudi nyumbani.” Geb akaangalia saa. “Ni saa kumi usiku.” “Sitarudi kulala pale kitandani Geb. Mungu amenitoa hapo. Sitarudi tena.” “Basi ngoja nikamtafute daktari nizungumze nae.” “Unaniacha!?” Nanaa akauliza. “Nitarudi baada ya muda mfupi tu.” “Nataka kuwa na wewe Geb. Usiniache hapa tafadhali.” Geb akamkumbatia kwa muda. “Basi twende wote.” Wakatoka.

Walizunguka kumtafuta daktari wa zamu. Hata yeye hakuamini kumuona Nanaa na hali ile. “IMEWEZEKANAJE!?” Akauliza. Geb akasimulia kwa kifupi. “Kumbe haya mambo ni kweli!” Yule daktari wa kihindi akauliza kwa mshangao. “Hata sisi ndio mara yetu ya kwanza kushuhudia. Hatukuwahi hata kushuhudia mtu aliyekuwa na ugonjwa, akipokea uponyaji na sisi tukashuhudia kwa macho yetu. Ni kitu kipya na kigeni kabisa kwetu. Na wala sisi hatukuwa tukiishi maisha ya watumishi kanisani. Ni watu wa kawaida tu. Tena..” Geb akanyamaza. Akataka kusema wenye dhambi. Akakumbuka msamaha wa dhambi aliopewa na Mungu. “Mungu yupo. Na nguvu zake ni halisi. Hana upendeleo. Kwa mtu yeyote, wa taifa lolote, anayemcha na kumtii, hujidhihirisha kwake. Ametuthibitishia hilo mimi na Nanaa.” Geb akamalizia.

Ilibidi daktari awaruhusu tu. Hapakuwa na sababu ya Nanaa kuendelea kuwepo pale. Kwani tokea awali vipimo vilionyesha ni mzima. Hana ugonjwa wowote. Ila akamshauri arudi kwa daktari wa wakina mama kwa ajili ya kliniki. Walishasahau juu ya mtoto. Tangia wafike hapo, Mungu amekuwa akiwapa yaliyo mema tu. Baraka juu ya baraka. Geb akalipa garama zote. Wakarudi wodini kukusanya vitu vyote wakiwa wameshikana mkono na Nanaa. Wakawashukuru manesi, wakaondoka.

Mungu Wa Yasiowezekana Kwa Wanadamu.

Hapakuwa na maongezi mengi sana kati yao. Ni kama bado walikuwa kwenye mshituko. Kila mmoja akitafakari lake. Walitembea kimya kimya mpaka kwenye gari ya Geb huku wameshikana mikono. Geb akamfungulia mlango. Akamfunga na mkanda. Akasimama pale pembeni yake akimwangalia Nanaa. Mara Nanaa akamuona machozi yanamtoka. Akatoa mkanda, akamgeukia na kumkumbatia.

“Sijui maisha mengine tena bila wewe Nanaa.” Alimsikia Geb akiongea kifuani kwake. “Mungu amenirudisha tena kwako Geb. Anakusudi na maisha yetu. Najiuliza kwa nini yule malaika asinitoe yeye zile pini, akanituma nikwambie wewe ndio utoe?” Geb akatulia kama anayetafakari hilo.

“Si unaona eeh!?Mwenzio ndio swali najiuliza mpaka sasa hivi.” Nanaa akaongeza. “Umenifanya nifikirie! Sikuwa hata nimelifikiria hilo.” Geb akajibu. “Panda kwenye gari twende huku tunaongea. Lakini Geb, naomba nipitishe kwanza kwa kaka.” “Sasa hivi Nanaa!?” “Tafadhali Geb. Kaka huwa halali vizuri akijua nipo kwenye shida. Na ninajua sasa hivi ndio kabisa. Kwa hali ile, kuniacha hospitalini! Najua hatakuwa akilala. Naomba twende akanione ili atulie.”

“Sawa. Hata hivyo anastahili. James anakuhangaikia sana. Jana usiku ilimlazimu tu kuondoka. Alikuwa akikuangalia wakati umelala, mpaka machozi yalikuwa yakimtoka. Ilibidi nimtoe. Nikamwambia sitaki uamke, umkute analia. James anakupenda sana.” “Nafahamu. Mimi ni kama mtoto wake. Hivi nilivyo, ni kwa ajili yake. Nilikuwa nikiachwa na nepi chafu kuanzia asubuhi anaponibadilisha wakati anaenda shule, mpaka mchana anaporudi. Ndio anibadilishe tena na kuniogesha. Ilimbidi kunianzishia uji nikiwa mchanga kabisa, anasema ilimlazimu ili nisiwe nashinda na njaa wakati yupo shuleni. Na akirudi, alikuwa akinilisha tena. Amehangaika na mimi kwa muda mrefu sana. Sijui mapenzi ya mzazi ila kaka.” Waliendelea kuzungumza huku wakielekea nyumbani kwa James.

“Ungemuhurumia wakati ndio amefika tu pale shuleni. Tumefika kidato cha kwanza. Unajua tulipangwa cubic au chumba kimoja? Mimi, yeye, Danny na Zinda. Yeye alikuwa akilala kitanda cha juu yangu. Zinda juu ya kitanda cha pembeni yetu cha Danny. Alikuwa akitusimulia habari zako bila kuchoka. Alikuwa na wasiwasi sana na wewe, mpaka akabuni njia ya kusingizia ugonjwa. Ndio akawa anaweza kurudi nyumbani kukuona. Sisi tukawa na kazi ya kumsaidia kuandika darasani wakati yeye anakuja kukuona. Hakuwa akizungumza chochote isipokuwa wewe, Nanaa.” Nanaa akajifuta machozi.

          “Umemtaja Zinda, nimekumbuka. Mambo yaliendaje?” Nanaa akauliza. Geb akatulia kidogo. “Vipi?” Akauliza tena. “Naomba kwa sasa tufurahie yale Mungu ametutendea kwanza Nanaa. Mambo mengine tutazungumza wakati mwingine.” Nanaa akajua kuna jambo. Akaamua anyamaze. Ukimya ukapita. Kila mtu akiwaza lake.

Kwa James.

Walifika Kijitonyama, alikopangisha nyumba  James. Nanaa akashuka kwa haraka. Geb akajua anataka yeye ndio akagonge mlango. Akatembea nyuma yake taratibu tu. Nyumbani kwa James hapakuwa na geti. Moja kwa moja wakasogea mpaka mlangoni. Wakaona taa za sebuleni zinawaka. “Yupo sebuleni.” Nanaa akanong’ona. Kisha akagonga. Wakamsikia amesimama. Geb akamuhurumia James. Akajua kweli hakuwa amelala. Kwa kuwa alikuwa akifanya kazi karibu sana na kwake, ule sio muda wa kuamka na kujiandaa kwenda kazini.

Wakamsikia akifungua ndani, Nanaa akasogea pembeni kama kujificha. Akabaki amesimama Geb katikati ya mlango. James akafungua akabaki akimshangaa Geb. “Tafadhali usiniambie kama kuna jambo baya limempata Nanaa. Nipo kwenye kompyuta yangu usiku kucha natafuta ufumbuzi wa tatizo lake. Nimepata hospitali mbili nchini Afrika ya kusini. Nataka nikifika kazini niwapigie simu ili nione kama watanipa appointment ya karibuni, nimpeleke. Kama umeniletea habari mbaya, naomba uondoke Geb. Tafadhali sana.” Nanaa alimuhurumia sana kaka yake. Akajitokeza taratibu. 

Alimuona James machozi yakimchirizika. Alishabadilika rangi kwa hofu mara baada yakumuona Geb mlangoni kwake asubuhi ile hata kabla hapaja pambazuka. “Kaka!” Nanaa akamuita. James akabaki amesimama. Akafikicha macho, akayafungua. “Ni mimi kaka. Nimepona.” James alibaki kimya. Nanaa akamsogelea. Akanyanyua gauni alilokuwa amevaa.

“Ona miguu yangu! Mungu ameniponya muda mfupi sana uliopita. Hapa ndio tumetoka hospitalini, tukaja kwako moja kwa moja.” Nanaa aliendelea kujieleza lakini James akabaki ameduaa. Akaweka mikono kichwani. Akavuta pumzi kama aliyekuwa amekabwa koo. Geb akaingia. 

“Naomba ukae James.” Akamshika mkono akamsogeza mpaka kwenye kochi. Nanaa alianza kulia. Geb akaanza kumueleza mwanzo mpaka mwisho. Tokea alipoondoka pale wodini, mpaka hapo walipo. James alikuwa akitoa machozi na kamasi kama mtoto mdogo.

“Mungu ameniponya kaka! Amepigana vita yangu. Lakini amekataa kabisa kuniambia ni nani aliniwekea zile pini. Nilijaribu kumuuliza yule malaika. Tena kwa kurudia rudia ili anitajie aliyeviweka, lakini mpaka anaondoka, hakumtaja.” Nanaa akilalamika.

“Kama Mungu hakutaka umjue kwa wakati huo, basi ujue ni kwa faida yako Nanaa.” “Kweli kaka?” “Kabisa. Pokea kile alichokupa. Mengine amejua haupo tayari kuyapokea.” James aliongea kwa hekima. Geb akamshukuru Mungu kimya kimya. Hakutaka kuanza kutoa habari za Mira wakati huo. Na kuanza kuleta matatizo kati yake na Nanaa. Wakapata muda wakutulia wote wawili. Wakajikuta wanacheka.

“Naomba tukapumzike kaka. Geb hajalala.” Geb akacheka. “Wote hatujalala.” “Ni sawa nikija kukuona jioni?” Nanaa akakunja uso. “Kwa nini unaniomba ruhusa? Au Geb..” Nanaa akamgeukia Geb kama anayetaka kuuliza swali. “Unakaribishwa nyumbani muda na wakati wowote ule James. Huhitaji hata kukaribishwa.” Geb akaongeza kwa haraka. “Ulitaka kunitia wasiwasi kaka! Nakutegemea na ninakuhitaji sana kwenye maisha yangu, kaka yangu. Kama Mungu hatabadilisha hii hali, wewe ndio unaweza ukawa ndugu yangu wa pekee watoto wangu watakao kufahamu.” “Basi nitakuja jioni nikitoka kazini. Nimefurahi sana. Sijalala usiku kucha nahangaika humo kwenye hiyo kompyuta. Mpaka nikafikiria nikupeleke Nigeria ukaombewe!” “Pole kaka yangu. Basi tukuache na wewe ulale hata lisaa. Lakini Mungu ametudhihirishia kuwa yupo popote pale. Ukimwita, anaitika. Lala kaka. Tutazungumza vizuri jioni.” James akamsimamisha Nanaa. Akamkumbatia. “Asante Mungu.” Walimsikia James akishukuru. Wakaagana, wakatoka kuelekea Tabata.

Mungu Amrudisha Nanaa Nyumbani Kwake Akiwa Anatembea.

Ilikuwa majira ya saa kumi na mbili kasorobo wakati geti la nyumbani kwa Geb likifunguliwa na walinzi ili waingie. “Mama anaweza kuanguka kwa mshituko.” Wakacheka. “Hapo atakuwa anapika ili amtume Danny atuletee chakula hospitalini.” Nanaa akaongeza na kuzidi kucheka. Wakashuka na kuongozana mpaka geti dogo la kuingia ndani ya nyumba. Geb akabonyeza kengele.

“Danny! Kamfungulie huyo mlinzi mlango. Sijui anashida gani? Mimi namalizia hapa jikoni sasa hivi.” Walimsikia mama G akiongea kwa mbali sababu ya vioo vilivyozungushwa kwenye hiyo nyumba. “Mimi ndio nipo hapa mama. Danny amerudi chumbani.” Grace akajibu. “Basi wasikilize ujue wana shida gani.” Wakasikia Grace anafungua milango. Akatoka pale.

“Mamaaaa! Mamaa!” “Nini wewe?” Mama G na Danny wakatoka wakikimbia. Grace alikuwa akipiga kelele baada ya kumuona Nanaa amesimama pale. Mama G na Danny walifika pale wakabaki kama sanamu. “Mungu ameniponya usiku wa saa nane.” Nanaa aliongea  na kujifunua mbele ya taa kubwa iliyokuwa ikimulika hapo mlangoni.

“Oneni.” Akajifunua mpaka juu magotini. Akageuka nyuma kuwaonyesha. Kwa asili Nanaa hakuwa na miguu minene hata kidogo. Miembamba na mirefu isiyo na nyama nyingi popote. Lakini ilikuwa mieupe sana sababu ya kuvaa nguo ndefu wakati wote. Ile miguu ikarudi kuwa kama ya mtoto! Ngozi safi.

 Mama G akaanza kulia. Alilia huyo mama, mpaka Geb akamtoa pale na kumwingiza ndani. Badala ya kicheko, pakageuka kilio. Grace na mama G walilia sana. Geb akawasimulia mwanzo mpaka mwisho. Hofu ya Mungu iliwajaa. Kila mmoja wao mpaka Danny wakabaki wakitetemeka.

“Umemuona malaika Nanaa!” “Ila nimeshindwa kumtizama sura mama. Alikuwa akiwaka sana. Mpaka nikadhani ni dokta. Sababu niliona tu kama amevaa koti jeupe. Nikajua ndoto. Hivi Geb ndiye aliyeniambia ni malaika. Lakini mama, nilimuhoji sana ili aniambie ni nani amenifanyia ubaya wote huo lakini hajamtaja kabisa! Aliishia kunipa maelekezo ya nini Geb anifanyie. Basi. Hakumtaja!” Wote wakanyamaza. Nanaa wala hakuwa akielewa kama wenzake wanamfahamu.

“Halafu kingine. Najiuliza kwa nini yeye mwenyewe asinitoe hizo pini akataka Geb ndio azitoe! Tena kwa kurudia rudia kuwa ‘mwambie Geb, afanye hivi’. Halafu huku Geb akiambiwa kwenye ndoto yake asiogope! Kwa nini Geb!? Tangia nipo hospitalini najiuliza. Nikasema labda kwa kuwa ndiye aliyekuwa pale! Lakini roho ikakataa. Nikajiambia labda kwa kuwa Mungu anajua kuwa nampenda Geb. Lakini pia naona hapana mama. Si Mungu angejifanyia yeye mwenyewe ili kujipatia utukufu yeye mwenyewe!? Nakumbuka kuna kipindi tulikuwa tukizungumza mimi na wewe mama. Ukasema Mungu anapenda sana Sifa. Huwa hagawani utukufu na mwanadamu. Si ni kweli?” “Kabisa. Lakini labda tu alitaka afanye.” Mama G akajibu. “Hapana mama. Mimi nahisi kipo kitu cha ziada! Moyoni nashuhudiwa kabisa. Lipo jambo kati ya Mungu na Geb.” Nanaa alikuwa akiongea kwa utulivu kama akivuta hisia.

“Nashauri Geb aendelee kumuuliza Mungu juu ya hilo. Mungu amemtumia Geb kufanya jambo la kipekee na gumu sana. Geb hana elimu ya kidaktari hata kidogo na wala hajawahi kumuombea mtu hata kichwa tu. Lakini mama, ungemuona vile Geb alivyokuwa amejawa ujasiri! Yaani mimi na yule nesi tulimkatisha sana tamaa. Nilikuwa nikilia nikimsihi aniache tu.” “Sababu ya maumivu?” Grace akauliza. “Hapana Grace! Nilikuwa naogopa tu. Labda sijui niliogopa nisije kukatishwa tamaa kama visingefanya kazi au, sijui! Lakini alipokuwa kila akinigusa, halafu sisikii kitu, nilikuwa nikimuomba aniache. Ndipo Geb ikabidi atulie azungumze na mimi kwanza. Tena ni kama alijua. Akaniambia anaomba kwa wakati ule, nisimamie Imani yake. Yeye atanibeba.” Nanaa akatulia. 

“Mimi mwenyewe sijui ujasiri niliupata wapi! Hata wazo la kuvua lile ngozi sijui lilitoka wapi!? Nikajikuta navuta lile ngozi kama namvua Nanaa soksi! Sijui! Ila ninachojua Mungu hutenda kazi na wao wampendao au wamwaminio.” “Ila huu ugonjwa umenithibitishia kuwa Geb ni wangu mama.” Kila mtu akacheka. Lakini Nanaa akaanza kulia.

“Nanaaa!” “Kweli mama. Nilijua Geb ananipenda. Lakini si kwa kiasi hiki! Mungu amejenga kitu kipya kabisa ndani yangu juu ya Geb. Si upendo tu. Kuna kitu kingine amekiweka cha tofauti. Bado sijajua, lakini najua moyo wangu Mungu ameugeuza kabisa kwa Geb, mama.” Nanaa akatulia akijifuta machozi.

“Hata mimi nakubaliana na Nanaa. Geb unampenda huyu mtoto! Sijawahi kukuona ukiwa hivyo, tokea tunazaliwa. Ulibeba sura ya tofauti ili kukabiliana na tatizo lililokuwa limempata na halina ufumbuzi kabisa! Ulimshangaza kila mtu, mpaka James alikuwa akishangaa nakulia peke yake. Lakini baadaye tukaambiana ni mapenzi ya dhati kwa Nanaa. Utafanya kila uwezalo kwa huyu mtoto!” Grace akaongeza. Wote wakacheka, mpaka Geb mwenyewe. Nanaa akamwangalia huku akilia. “Asante Geb.” Akamshukuru kwa kunong’ona.

“Twende tukapumzike. Hatujalala tokea saa nane tupo macho! Nanaa najua amechoka. Tutazungumza zaidi baadaye.” “Mle kwanza ndio mkalale. Msilale bila kula. Hivi ndio nilikuwa nikimalizia kuwapikia.” “Msipandishe hata juu. Mkae hapo hapo. Napanga chakula sasa hivi.”  Mama G akakimbilia jikoni.

“Ngoja nikusaidie mama.” Nanaa akasimama na kumfuata jikoni kwa haraka. “Wee Nanaa! Hebu nenda kapumzike!” Mama G akamfukuza pale jikoni.  “Usinikataze mama yangu. Acha tu nifanye. Nilikuwa nikimlilia Mungu anisimamishe tena kwa ajili ya Geb wangu na wanangu. Amenisaidia, acha nimtumikie tu mpenzi wangu. Kwa kadiri ya Mungu atakavyonijalia. Nimegundua huu uzima tulio nao mama si kitu. Unaweza kupokonywa wakati wowote.” Mama G akabaki akimtizama.

“Usinifukuze mama yangu.” “Haya mwanangu. Uji wake huo hapo, upo tayari kwenye chupa. Kuna embe kwenye hilo kapu la hospitalini. Lisafishe tena umuwekee kwenye sinia lake. Na juisi ipo kwenye friji.” Nanaa akamtayarishia Geb, akamuwekea mezani.

~~~~~~~~~~~~~

“Maziwa yamejaa! Natamani Liv aamke anyonye.” Nanaa alikuwa akiongea na Geb pale mezani. “Na mwanao huyo kumuamsha ni shuguli nzito haswa! Akilala amelala.” Mama G akaingilia. “Grace! Wakina kaka wanaendeleaje?” Grace alikuwa amejiinamia akaanza kucheka. “Anawanywesha uji. Ndio maana unasikia pametulia.” Mama G akajibu yeye.

“Grace! Si ndio wametimiza miezi mitatu tu!?” Nanaa akashangaa. “Ndio wametimiza miezi mitatu juzi. Nilichoka Nanaa. Mimi kelele nyingi vile siziwezi. Nilihisi nitachanganyikiwa.” Nanaa akaanza kucheka. Akakumbuka vile Grace alivyokuwa akilia wakati wanae wanapokezana kulia.

“Kwa hiyo umeacha kuwanyonyesha?” “Niringe? Wananyonya kama sijui nini vile, na uji pia wanakunywa. Hapa niliamka mapema, angalau kupata muda na mume wangu kabla hajaenda kazini. Wakiamka nianze kuhangaika nao. Mpaka saa tatu ninakuwa nimewajaza matumbo yao uji. Hawawezi hata kulia! Ndio hata nikimuachia hapo mama na maziwa nikienda kazini masaa mawili, nakuta bado wamelala.” Nanaa akazidi kucheka. “Grace!” “Ningekufa nikawaacha Nanaa. Heri hivyo.” Grace akaongeza. Geb alikuwa akimwangalia tu dada yake huku akila. 

“Njoo basi ule kabla hawajaamka.” “Na kweli.” Grace akahamia mezani. “Danny amepigwa na butwaa. Njoo mume wangu ule ndio uende kazini.” “Namshangaa Mungu!” Danny akasimama na yeye akahamia mezani. Walikaa pale wakila.

“Zinda..” Nanaa akataka kuuliza. Akamwangalia Geb, akaona anyamaze tu. Alipoona wote wanaangaliana, akajua kuna kinachoendelea. “Geb amesema niache habari nyingine. Nipumzike kwanza. Lakini nilitaka kujua mambo ya Zinda yaliendaje!” “Nanaa!” “Basi Geb. Tutazungumza tukiamka. Au hata jioni.” Geb akanyamaza. “Si sawa?” “Jioni.” Geb akajibu, wengine wote wakanyamaza. Nanaa akajua lipo jambo tu ndio maana wengine hawachangii isivyo kawaida yao.

Alipomaliza kula akaenda chumbani kwa mama G moja kwa moja kitandani kwa mtoto wake. Akamkuta Oliva amelala hana hata habari. “Huyu binti Magesa kwa kupenda usingizi! Sasa hapo sijui ataamka saa ngapi?” Akabaki akijiuliza huku akimwangalia mwanae. Akambusu.

“Huyo mwanao ni wakumuamsha kwa nguvu. Usipomgusa hapo mpaka saa sita. Nitamuasha kwenye saa mbili. Aoge ndio ale.” “Hakusumbui kula?” Nanaa akatoka, akamuuliza bibi yake. “Hivyo hivyo. Ana kazi ya kucheka tu. Tena Fili asiwepo. Akiwepo Fili anataka wacheze. Fili anamtekenya, basi atacheka hapo wee. Mdomo hautafungwa tena. Na Fili akiondoka analia.” Nanaa akacheka. “Liv kwa kucheka! Kila kitu yeye kucheka! Na akicheka chakula hakikai tena mdomoni! Chote kinatoka. Itabidi afundishwe kutabasamu.” Nanaa alifanya wacheke.

“Nimechoka Nanaa!” Geb akalalamika kidogo. Akimaanisha wakalale. “Twende basi ukalale.” Akamsogelea Geb na kumsugua kidogo mgongoni. “Pole.” Geb akamgeukia, akampa tabasamu. “Mama! Asante kwa chakula.” Geb akasimama, akamkumbatia Nanaa na kumbusu. “Karibu tena nyumbani.” Aliongea huku akimwangalia Nanaa machoni. “Asante. Nina hamu na wewe Geb!” Nanaa aliongea sauti ya chini ya kudeka. “Hata mimi.” Pale pale Geb akainama na kuanza kunyonya midomo ya Nanaa. “Basi hapo tena kazi imeanza!” Mama G akafanya waanze kucheka. Geb akamnyanyua Nanaa. Akambeba na kupanda naye juu, kurudi chumbani kwao. 

~~~~~~~~~~~

Japokuwa walikuwa na hamu ya kufanya mapenzi. Kila mmoja alikuwa na uchu na mwenzake, lakini walipofika tu chumbani, Geb alimuweka Nanaa chini, wakapiga magoti pembeni ya kitanda chao, wakaanza kuomba. Walimshukuru Mungu kwa kuwarudisha nyumbani salama. Wakaomba ulinzi wa Mungu juu yao, watoto wao na familia yote kwa jumla. Wakamaliza, ndipo wakakumbukana sasa.

Walipata wakati mzuri sana hapo kitandani. Kwa kuwa walikuwa wamechoka, hayakuwa mapenzi ya muda mrefu. Wakaamua kulala. Nanaa alilala kifuani kwa Geb akiwa amemkumbatia. Alinyanyua uso wake, akambusu mara kadhaa. “Asante kwa kunipenda Geb.” Geb akiwa na usingizi. Alirudisha busu, hapo hapo akalala.

~~~~~~~~~~~

Waliamka jioni kwenye saa kumi, nyumba ilikuwa imetulia sana, kama hakuna mtu. Nanaa akatoka, akaenda chumbani kwa mama G. Alimkuta Grace na mama yake wamejilaza kitandani. “Mmelala?” Nanaa akauliza. Akakaa pembeni yao. “Tumepumzika tu, tunaongea. Oliva amerudi kulala muda sio mrefu.” Grace akajibu. “Nina hamu naye! Maziwa yamejaa mpaka yanauma.” “Labda ukakamue.” “Natamani anyonye.” “Sasa utanyonyesha mpaka ujifungue?” Nanaa akacheka. “Nilishasahau kama ni mjamzito!” Nanaa akajishika tumbo.

“Geb kafurahi huyo!” Nanaa akaongea huku akijiangalia. “Mwenzio anapenda kweli watoto. Usipoangalia, atakuzalisha mchana na usiku.” Grace alimfanya Nanaa acheke sana. “Hata mimi napenda watoto wengi.” “Basi hapo mmekutana.” Wakaendelea kuongea wakiwa huko chumbani. 

“Nanaa!” Wakamsikia Geb akiita. Nanaa akatoka. “Utataka kula kitu chochote?” “Nataka kukimbia ofisini mara moja.” Nanaa akanyamaza. “Sitakawia. Naenda kuangalia mara moja, nitarudi.” Grace akatoka. “Nimerudi sasa hivi. Nilikuwa huko. Kila kitu kipo sawa Geb. Leo pumzika.” “Una uhakika? Sitaki usumbuke. Kwa kuwa sasa hivi mimi nipo, nataka urudishe akili kwa watoto.” “Hayo madume ya Danny hayana neno. Wewe leo pumzika. Kesho asubuhi ndio uende mwenyewe.” “Mama yuko wapi?” Geb akauliza. “Nipo huku.” Geb akaingia chumbani kwa mama yake.

“Mzima?” “Nimejinyoosha tu.” “Pole. Najua unachoka sana.” “Wala. Kama hivi nimelala. Hamna hata ninachofanya!” Geb akakaa pembeni yake. “Nakushukuru mama.” Mama G akatabasamu. “Asante mama yangu. Asante sana. Bila wewe naona humu ndani wote tungekuwa tumechanganyikiwa!” “Namshukuru Mungu kuwa na nyinyi Geb. Uzima huu nilio nao, kama alivyosema Nanaa, ni wakutumia kwa kadiri tuwezavyo. Kwa hiyo hata mimi ninafurahi kuweza kuwa msaada.” “Sasa na wewe mambo yako?” Mama G akanyamaza.

“Kwa kuwa Nanaa amerudi, labda kesho uende ukaangalie kidogo.” “Nitafanya hivyo. Ni muhimu. Akiamka tu huyo dada, nikishamlisha. Nitatoka mara moja. Nikaangalie biashara inakwendaje. Naamini Mungu atakuwa amenilindia. Nilikuwa nazungumza na wafanyakazi wangu kila siku. Hawakuwa wakinipa taarifa mbaya. Ila kuna umuhimu wakwenda kutupia macho.” Geb na mama yake waliendelea kuzungumza. Nanaa na Grace wakiwa wameenda kukaa kwenye makochi na wenyewe wanaongea.

~~~~~~~~~~~

Ilipofika saa 11:30 jioni, James akaingia. “Kaka!” Nanaa akasimama. “Tuone tena hiyo miguu! Maana nilikuwa nahisi naota siku nzima.” Nanaa akacheka. Akamuonyesha kaka yake. “Imerudi kuwa kama ya mtoto mchanga!” James akasifia. Mama G, na Geb wakatoka. “Karibu James mwanangu.” “Asante mama. Za hapa?” “Bado tupo na mshituko wa uponyaji wa Nanaa!” Wote wakakaa. Geb akaenda kukaa pembeni ya Nanaa. Nanaa akajiegemeza kwake kidogo, akamvuta na mkono. Danny na Fili nao wakaingia.

          “Mbona huyo macho yamezidi kuingia ndani? Njoo baba.” Grace alilalamika. Fili akaenda kwa mama yake. “Danny umemfanyaje mwanangu?” Danny akacheka na kutingisha kichwa. “Maana wewe nakujua. Ukute hapo Fili alikuwa ametulia kwenye gari njia nzima. Hata hakuimba! Eti Fili mwanangu?” Wakacheka. Fili alikuwa mnyonge. “Hajala huyo. Mwalimu wake kaniambia tokea asubuhi hajaingiza kitu mdomoni. Mimi mwenyewe leo mpaka nimemuomba aniimbie huko njiani. Hataki kuongea mwanao.” Grace akamshika tumbo.

“Eti Fili. Tumbo linauma?” Fili akakubali. “Wewe Fili? Sijakuuliza mimi njia nzima, ukaninyamazia? Yaani mama yako kakuuliza kidogo tu, tena hata hajakubembeleza kama mimi, umemwambia!?” “Mwache mwanangu. Linauma wapi?” Fili akajionyeshea tumbo zima. 

“Labda ana gesi. Ngoja nimletee vidonge vya gesi. Labda litatulia. Si hana homa?” Geb akamuuliza Grace. “Wabaridii.” Geb akasimama. Akamletea vidonge vya kutoa gesi. Mama yake akampakata vizuri. “Pole na kazi.” Grace akamgeukia mumewe. “Asante. Naona kimya. Umewapa ugali nini?” Wakacheka. Danny akakaa. “Niwaletee basi kitu mle.” Mama G akasimama. Nanaa akafuata nyuma.

“Kwani leo tutakula nini usiku?” “Nilipika chakula kingi mchana. Tutakula hicho hicho. Wabebee hilo jagi la juisi kutoka kwenye friji. Weka glasi za kutosha. Ili kila atakayetaka ajimiminie. Sio tupate kazi ya kusimama kila wakati kufuata glasi.” Nanaa akafanya kama alivyoagizwa. Akatoka na sinia kubwa lenye jagi ya juisi na glasi. Akaweka kati kati yao. Kwenye meza kubwa ya hapo sebuleni walipokuwa wamekaa watu wote. Akamimina kwenye glasi, akawagawia.

“Naenda kumpashia moto chakula, Geb. Kuna mwingine atataka kula? Naweza kuwaletea hapo hapo.” Nanaa akauliza. “Mimi naomba supu yangu Nanaa.” Grace akaagiza. “Kama kuna chakula kingi, na mimi naomba. Sijala leo.” James naye akaongeza. “Sawa kaka.” “Na mimi.” Danny akaongeza na yeye. “Mimi naona pasha chakula chote, uweke mezani. Watu wajipakulie wale.” Nanaa akacheka. “Na kweli.” Akarudi jikoni. 

Kila Mwanadamu Mungu Humpa Mlango Wa Kutokea.

 “Naombeni niwashukuru nyinyi wote kwa kuwa pamoja na Nanaa, wakati anaumwa.” James alivunja ukimya. “Nanaa ni jukumu letu pia James.” Mama G akajibu, James akacheka kidogo. “Nahisi itanichukua muda kidogo kuniingia hiyo akilini. Nimemlea Nanaa kwa shida sana, huku nikiona watu wakimuona mzigo. Hata baba yangu mzazi nilimsikia akikataa katakata kujihusisha naye.”

“Nakumbuka baba alitaka atolewe pale nyumbani. Mama akaanza kuzunguka naye kama mzigo akitafuta sehemu ya kumtua huku akilalamika sana. Alizunguka naye kila mahali na kote walikuwa wakimkataa Nanaa. Nakumbuka mama alirudi naye akiwa amekasirika sana baada hata ya kituo cha yatima nao kumkataa. Akamuweka kwenye kochi Nanaa alikuwa akilia sana. Mama akasema hajui atafanya naye nini huyo mtoto. Nakumbuka nikajisogeza mpaka pale sebuleni alipokuwa amekaa baba na mama, nikawaambia mimi nitamlea Nanaa. Hawakuamini. Wakajua ni akili za kitoto tu.” James akafikiria kidogo.

Nikamnyanyua pale kwenye kochi, kwa kuwa alikuwa akilia mpaka akageuka kuwa mwekundu kabisa. Nilijua kuwa ni njaa.” James akacheka kidogo. “Nikamuwekea mdomoni, kidole changu hiki kidogo, akaanza kukinyonya. Alikuwa ananuka mikojo. Nepi imejaa! Nikaenda kumchukulia moja ya nepi za Viola, nikamwagia maji ya baridi tu. Wala sikuyapasha moto. Nikamkausha na kumvalisha ile nepi.”

“Nikaenda kumchukulia maziwa ya mbuzi. Pale nyumbani kulikuwa na ng’ombe na mbuzi. Baba hakuwa akitaka maziwa ya ng’ombe yaguswe. Sikutaka kesi na mtu. Nikaenda bandani, nikamuomba aliyekuwa akikamua. Tena alikuwa msichana wa kazi. Akaniwekea kwenye kikombe. Nikaenda kuyapasha moto. Sidhani hata kama yalichemka vizuri. Nikarudisha kwenye kikombe, nikampakata Nanaa, nikaanza kumnywesha na kijiko, mpaka akamaliza. Baba na mama walikuwa wakiniangalia tu.” Kila mtu alikuwa akimsikiliza James.

“Basi. Kuanzia hapo, nikaanza kuhangaika na Nanaa. Sikumbuki kumpeleka kliniki kwa chanjo yeyote ile wala kuangaliwa afya yake. Na sikumbuki kumuona anaumwa hata jino. Hakuwahi kunisumbua katika kukua kwake. Maisha yangu yakabadilika sana. Ilikuwa shule, na Nanaa tu. Niliachana na marafiki wote. Nikawa na kazi ya kuwa na Nanaa.”

“Nguo au nepi zake nilikuwa nikimkusanyia kutoka kwenye nguo za Viola. Kama nikiona mama amenunua nguo mpya kwa ajili ya Viola, namuomba za zamani, namvalisha Nanaa. Basi na yeye akawa ananijua. Hata kama yupo sebuleni, akisikia tu sauti yangu nimerudi kutoka shuleni. Labda nipo jikoni, atatambaa kuifuata hiyo sauti mpaka anikute.” James akatulia.

“Kwa nini nimesema yote hayo. Nataka kusema hivi, sijawahi kuona mtu anamtaka Nanaa kwenye maisha yake yote. Hata marafiki wa kike wamekuwa wakimsaliti Nanaa. Mpaka majuzi aliponipigia simu asubuhi amevimba miguu, nikakimbia kumbeba na kumkimbiza hospitalini. Hakika sikujua kwa hakika kama..” Wakamuona anafuta machozi akanyamaza kidogo.  

“Sikutegemea kabisa! Geb aliponipigia simu nikiwa njiani, alikuwa mkali kidogo kwangu. Lakini asijue ile ilikuwa faraja. Geb aliniambia lazima nimtambue na kuheshimu kuwa sasa hivi Nanaa ni jukumu lake. Zilikuwa ni habari ambazo sikuwahi kuzitegemea kuzisikia maishani. Au kama ningekuja kusikia, nilidhani nikipindi Nanaa akiwa mzima. Sio akiwa na miguu ya namna ile! Hata kidogo. Halafu Geb alisema yupo njiani anatufuata! Lakini bado upande mwingine sikuamini.” James akajaribu kufuta machozi ili atulie.

“Nilimfikisha Nanaa hospitalini, tukawa tumekaa naye. Nilikuwa nimeingiwa na hofu, nikijua tumebaki tena wawili. Lakini Geb akaingia. Kuanzia jinsi alipoingia pale mpaka leo asubuhi anamleta pale nyumbani, nimesadiki kweli Nanaa ni jukumu ambalo Mungu anaanza kulitoa kwangu.” “Sio ameanza James. Nanaa ni mke wangu MIMI. Narudia, na naomba ukubali tu. Nanaa ni jukumu langu mimi.” Wakacheka kidogo.

“Nakusikia Geb. Na namshukuru Mungu kwa hilo, ila najua itanichukua muda kuingia akilini.” “Naelewa. Na wala sio kwamba nakufukuza kwenye maisha ya Nanaa! Hapana. Anakuhitaji sana tu kwenye maisha yake. Ninachotaka ukijue tu, ni kuwa haupo tena peke yako. Na mimi nipo na wewe James.” James akavuta pumzi na kucheka kidogo.

“Kwa kweli hilo umelithibitisha kwa vitendo Geb! Na usifikiri ni kwa ile pesa uliyomlipa mwanzoni mama! Hata kidogo. Ile wala haikuwa imeniingia akilini. Kwani milioni 30 kwa Geb ni nini bwana?” Wakacheka kidogo.

“Usinielewe vibaya Geb. Ni pesa nyingi sana. Lakini najua unayo pesa. Na iliniuma. Lakini si kama ile milioni 20 uliyomlipa tena mama, kwa ajili ya Nanaa aliyekuwa ameharibika miguu! Unailipa, halafu huku madaktari wanakwambia hawajui jinsi ya kumtibu! Hapana! Nililia usiku kucha nisiamini kama umefanya hivyo Geb! Danny anakuuliza juu ya harusi, unasema harusi bado ipo! Ulizidi kunichanganya. Nikasema labda umechanganyikiwa.” Geb akacheka.

“Kweli kabisa Geb, muulize mama. Nilimpigia simu usiku wa saa sita. Nilikuwa nikilia kama mtoto mdogo, namuuliza iweje kesho Geb arudiwe na akili yake, halafu aje adai pesa yake, halafu amkimbie Nanaa pale hospitalini?” “Haiwezekani James!!” Geb alishangaa sana.

“Muulize mama huyo. Alikesha kwenye simu akinituliz…” James akanyamaza mara baada ya kumsikia Oliva anaongea kwenye kitanda chake. Aliongea kwa sauti. Bibi yake aliacha mlango wazi ili kumsikia. Chumba chake na bibi yake hakikuwa mbali na hapo sebuleni.

Geb akataka kusimama. “Sasa wewe usiende. Hatanyonya huyo. Mwache sasa hivi ananjaa, mama yake aende akamnyonyeshe.” Mama G akamzuia Geb. “Ninahamu naye kweli!” “Na yeye atakuwa na hamu na wewe. Ukimuweka hapo kifuani, hatakubali kutoka tena. Mwache Nanaa aende kwanza. Nanaa!” Mama G akaita. “Nimemsikia mama. Nakwenda sasa hivi. Namalizia kuweka chakula mezani.” Nanaa alikuwa akilia. Alikuwa akiwasikiliza mazungumzo yote.

Geb alipomsikia sauti yake ya kilio, akasimama. Akamfuata jikoni. “Njoo!” Nanaa akamsogelea. Geb akamkumbatia pale pale jikoni. Nanaa alilia kwa uchungu sana. Geb akamtuliza, akatulia. Akaanza kumbusu. “Mtoto anawaita huko chumbani. Wewe Nanaa?” Nanaa akacheka. “Naenda mama.” Kimya. Mama G akajua wamerudi kupeana mabusu. “Basi hapo mtoto mpaka aanze kulia, wakati mwenyewe si mlizi!” “Naenda sasa hivi mama yangu. Geb! Niwekee hivyo vyakula vyote kwenye  hiyo meza kubwa ya huko nje sehemu ya kulia chakula. Kila kitu kama kilivyo.” “Sawa.” Geb alianza kuhamisha. Nanaa akaenda kunyonyesha.

 ~~~~~~~~~~~

 “Jamani Nanaa amenipa kazi, nimemaliza. Naombeni tuhamie mezani.” Geb aliwakaribisha. Fili alishakuwa amelala. Geb akaenda kumchukua. “Ngoja nikammwagie maji mara moja, aje kula. Wewe nenda kaanze kula Grace.” “Asante. Maana njaa ilishaanza kuuma.” Grace akamshukuru kaka yake. “Fili! Fili!” Geb akamuita wakati amembeba. Akafungua macho wakati Geb anampeleka chumbani kwa wazazi wake kumvua nguo. “Vipi, tumbo limetulia?” Walimsikia Geb akizungumza naye. 

Hata dakika 15 hazikuisha, Geb akarudi naye akiwa ameshamvalisha nguo za kulalia. Lakini anatembea mwenyewe. “Njaa inauma?” Geb akamuuliza. “Kidogo tu.” Fili akajibu. “Njoo uje ule mwanangu. Naona umechangamka.” Grace akamuita mwanae. Fili akaenda.

“Shikamoo anko.” Akamsalimia James. “Marahaba Fili. Za shule?” “Nzuri. Nimepata zote kwenye hesabu.” Fili akajisifia. “Kumekucha!” Danny akadakia, wakacheka kidogo. “Safi sana. Lazima nikupe zawadi.” James akamwambia. “Asante anko. Lakini usifikiri nimekosa hata moja? Nimepata zote. Na sijaigilizia. Halafu nakumbuka mpaka sasa hivi. Nilimuomba mwalimu niwafundishe pale ubaoni.” “Sasa kazi watakuwa nayo huko shuleni.” Mama yake akaongea kwa sauti ya chini. Kila mmoja  akatamani kucheka, lakini wakajizuia.

“Sasa mwalimu alikuruhusu?” James akauliza. “Mwanzoni alikataa. Ndio nikamwambia kama hataki basi mimi naondoka, narudi kwa mama yangu. Nikamwambia ampigie simu mama yangu aje anifuate. Akasema mama atakuwa kazini. Nikamwambia mama yangu yupo nyumbani na wadogo zangu. Na mimi najua hesabu zote, anipe chaki niwafundishe. Akakataa. Sasa kuna mtoto mwingine yeye anapenda tu kulia. Kila mama yake akimshusha pale shuleni, analia tu. Nikajua atakuwa hajui hesabu. Ndio nikamwambia mwalimu basi nimfundishe yeye, pia akakataa. Ndio ikabidi ninyamaze.” “Ndio maana ukakataa kula?” Mama yake akamuuliza taratibu tu.

          “Kwani nilimwambia nataka kufundisha sana? Si kidogo tu! Sasa baadaye akaniambia nisome. Na mimi nikamkatalia. Nikamwambia najua sana kusoma, lakini na mimi sitaki kama yeye alivyonikatalia kufundisha hesabu. Nikawa nimekaa tu kwenye kiti changu.” Hapo kila mtu alianza kucheka. Mpaka Nanaa aliyekuwa akinyonyesha ndani alisikika akicheka.

“Wewe Fili!” Grace akashangaa sana. “Nilimkatalia mama. Halafu kila nikinyoosha mkono nijibu swali, hanichagui mimi. Nikaamua kusimama niongee. Nikamuuliza mbona hanichagui tena? Akasema nimeshajibu sana, niwape nafasi na wengine. Nikamuuliza mbona sasa hawanyoshi mkono kama mimi? Hapo hapo nikamjibia mwalimu nikamwambia akiona hawanyooshi mkono, ajue hawajui. Mimi najua, anichague. Akakataa.” Geb alikuwa akimwangalia Fili huku akitingisha kichwa. 

“Kazi watakuwa nayo huko! Watajuta kumpokea huyo.” “Na mwanao alivyo na hoja! Kama mwanasheria!” Mama G aliongea huku akicheka sana. “Sasa kama yeye alinikatalia, kwa nini atake nisome kwa sauti? Nikamwambia achague mtu mwingine. Mimi sitaki tena.” “We Fili! Hebu njoo kwanza.” Geb akamuita. Fili akaenda mpaka alipokuwa amekaa anko wake.

“Nisikilize halafu usiongee mpaka nimalize. Sawa?” Geb akamuuliza. “Hata kama nataka kuchangia?” “Hapana. Mpaka nikuruhusu kuongea ndio uongee.” “Sawa. Nitanyoosha mkono na unichague.” Kila mtu alikuwa akicheka. Akanyoosha mkono. “Hapana Fili. Bado sijaanza hata kuongea, na wewe unataka kuongea! Utasikiliza saa ngapi?” Fili aliendelea kunyoosha mkono bila kumjibu. Mpaka Geb mwenyewe akacheka. “Haya ongea.” Geb akamruhusu.

“Kesho nataka kwenda na mama shule. Ili amwambie yule mwalimu aniruhusu kujibu maswali na kufundisha kidogo. Haya sasa hivi nanyamaza. Na wewe ongea.” Fili akatulia kumpa nafasi anko wake azungumze naye. 

“Cha kwanza ujue unakwenda shule kufundishwa.” “Anayofundisha mimi nayajua.” Fili akamwingilia. “Nilikwambia nini? Nikiongea, wewe unanyamaza.” Akatulia. “Na sio kwamba unaenda kufundishwa kusoma tu na kuandika! Tumekupeleka shule pia ukajifunze kuwa msikivu, heshima, upendo, utii, vyote hivyo kwa walimu na wenzako. Unatakiwa kujua kuthamini na wengine. Sio wewe tu.”

“Unaweza kujua kusoma na kuandika, lakini hivyo vingine inabidi kujifunza pia. Na uelewe. Mwalimu akikwambia kitu, unatakiwa umtii. Umsikilize kwanza. Acha kujibizana. Hata kama akikwambia unyamaze wakati wewe unataka kuongea, nyamaza. Hapo ujue unafundishwa kuwa mtoto mtiifu.”

“Akisema uwape nafasi wenzio na wao wajibu, sio kwamba hakupendi wewe? Anakupenda, lakini ujue kuna watoto wengine wanajifunza taratibu, wanatakiwa kupewa nafasi wajifunze pia. Ukiwa unanyoosha mkono wewe tu, halafu unajibu kila wakati, utawanyima wenzio nafasi yakujifunza.”

“Yule mtoto anayemlilia mama yake, unatakiwa kusaidia kumtuliza na kumuonyesha shuleni ni sehemu nzuri. Mfariji. Mwambie atulie, atamuona mama yake baadaye. Wakati wakucheza, usimuache peke yake. Cheza naye ili asiwe mpweke. Umeelewa?” “Hapo nimeelewa anko.” Fili akakubaliana naye.

“Safi sana. Kwa hiyo kesho ukienda lazima umuonyeshe mwalimu wewe unaakili kuliko watoto wote. Uwe unanyoosha tu mkono. Usipochaguliwa, usiongee mpaka akuchague. Akikwambia ufanye kitu chochote, unafanya. Tena unafanya vizuri sana kuliko kila mtu. Halafu unatulia kwenye kiti chako. Hakuna kuongea hata na mtu wa pembeni yako mpaka mwalimu awaruhusu wote kuongea. Kucheza na kuruka, ni nje ya darasani. Sio kupanda juu ya meza na kuruka darasani. Umesikia?” “Siruki tena kwenye meza anko.” Fili akajibu kwa utulivu. 

“Sasa hapo ndio utakuwa mtoto mzuri na mwenye akili kuliko wote. Haya kaa sasa hivi, ule chakula chako hapo mezani mpaka umalize. Halafu uchukue sahani yako urudishe jikoni.” “Bibi Fili hatanilisha?” Fili akauliza kwa upole. “Hapana. Wewe una akili sana Fili. Inabidi uonyeshe watu wote kama wewe una akili kwa kuanza kujitegemea mwenyewe.” Wakamuona anacheka.

“Basi kuanzia leo nitakuwa nakula mwenyewe na kuwalisha na wadogo zangu. Nitawapa wali, ugali na..” Grace akashituka. “Mimi naona uanze tu kwanza wewe mwenyewe. Watoto mimi nitawalisha.” Grace akadakia kwa haraka sana. Watu wakaanza kucheka. 

“Naweza mama. Mimi nina akili.” “Kweli wewe unaakili mwanangu. Lakini naomba watoto niwalishe tu mimi.” “Kwani..” Fili akataka kubisha, Geb akamuwahi. “Nimekwambia nini juu ya kusikiliza na kutii? Hamna kumbishia mama. Mama anajua zaidi yako Fili.” “Sawa mama. Nitaanza kwa kula mimi mwenyewe. Si baadaye utaniruhusu kuwalisha wadogo zangu?” Grace akanyamaza kidogo kama anayefikiria. Alijua vile Fili alivyo mtundu.

“Cha kwanza, usiwalishe kitu chochote watoto mpaka umuulize mama au bibi Fili au Nanaa. Wakikuruhusu ndio uwalishe. Umenielewa?” Geb akamuuliza, akijua hofu ya Grace. “Hata kama nimeachwa na watoto peke yetu? Labda nimeingia chumbani nikakuta wanalia je? Si naweza kuwalisha?” Fili akauliza kwa makini. “Uwiii!” Grace alisikika. Watu wakazidi kucheka.

“Kimbia uje uulize kwanza kabla hujawalisha kitu chochote.” “Hata Oliva? Maana Oliva yeye ni mkubwa kidogo.” Fili alisisitiza. “Sasa hapo unamtaka anko wako maneno.” Baba yake akaingilia. Geb akacheka. “Hata Oliva usimlishe mpaka uulize.” Geb akamjibu.

“Lakini Liv anapenda sana pipi.” “Fili wewe jamani! Huwa unamlisha Liv pipi!?” Mama yake akashituka sana. “Namlambisha tu.” Kila mtu alikuwa akicheka. “Basi ndio maana Liv anampenda Fili! Akimuona tu, anamuita. Kumbe huwa anampa pipi!” Mama G aliongeza

“Nimeelewa anko. Nijilishe tu mimi mwenyewe. Halafu nikitaka kuwalisha watoto hata pipi ni... “ “Usimpe mtoto yeyote yule pipi.” Geb alisisitiza wengine walikuwa wakicheka sana. “Hata nikiwa nazo mbili?” Fili akauliza tena. “Nimekwambia nini juu ya kuuliza kwanza?” Geb akaumuuliza. “Basi anko. Nimeelewa. Umesema niulize kwanza kabla sijampa mtoto kitu chochote.”  “Safi sana. Hakuna kuweka kitu chochote mdomoni kwa watoto, mpaka uulize.” “Sawa.” Akakubali.

          Akakaa mama yake akamuwekea chakula kwenye sahani, akaanza kula taratibu. “Sijui wale wawili wao wamelishwa nini jamani! Naogopa hata kuuliza.” Grace aliongea kwa sauti ya chini. Kila mtu alikuwa akicheka. “Ngoja mimi niulize.” Mama G akajitolea. “Hivi sijui kina Fillius wao wanapendaga nini? Ili wakilia niwe nawapa.” Mama G akajidai kujiuliza kwa sauti. “Walambishe sukari bibi.   Ukiwapa sukari wananyamaza.” “Mungu wangu!!!” Grace aliweka mikono kichwani. Kila mtu alikuwa akicheka. Mpaka Nanaa akatoka.

“Fili Fili! Kwani huwa unawapa sukari?” Nanaa akauliza. “Mama akiwa bafuni anaoga, halafu wakilia, nawapa kidogo kidogo. Hawalii tena. Wanakuwa wanajilamba tu.” “Fili wewe jamani!” “Inasaidia mama. Si unaona siku hizi hawalii sana?” Fili akajitetea. Bibi yake ndio alikuwa akifuta machozi kwa kucheka. Mpaka Geb naye alishindwa kujizuia. James na yeye alikuwa akicheka sana. “Filiiiii!” James aliita akicheka sana. Danny alibaki akimtizama Fili. “Huyu mtoto ahame kabisa humu ndani.” Mwishoe Danny akaongeza. Hapo ikabidi bibi yake azungumze naye mpaka akaelewa.

~~~~~~~~~~~

Oliva alipomuona tu baba yake akaanza kunyoosha mikono. “Nina hamu na wewe Liv mwanangu! Njoo mama.” Geb akamuweka kifuani kama kawaida yake. Oliva naye akazungusha vimikono vyake kwenye shingo ya baba yake, akatulia kama anayesubiria kitu. “Mmmmmmmmhhhh!” Geb alisikika akisikilizia raha ya moyoni huku amemkumbatia mwanae na kufunga macho. Oliva aliposikia baba yake amemaliza, akajitoa shingoni akamwangalia huku anacheka.

“Hapo anasubiri mabusu ya baba yake.” Nanaa alikuwa akiwaangalia. “Baba yake ameshamzoesha. Mpaka ameshajua kinachofuata ni nini.” Mama G akaongeza. Wote walibaki wakiwatizama. Geb akaanza kumbusu mfululizo. Oliva alisikika akicheka sana. “Muone anavyofurahia!” Nanaa akaongeza. “Kazi yake ndio hiyo tu, kucheka.” Bibi yake akaongeza.

Wakakaa hapo na kula kwa pamoja mpaka walipo maliza. “Kama umemaliza kula Nanaa, naomba tuzungumze.” James alimtaka dada yake waongee. “Ngoja nimalizie kusafisha hapa mezani.” Nanaa akamaliza. Wakahamia kwenye makochi, wakati wengine wapo bado mezani wakiongea.

Nanaa Na Kaka Yake.

Nanaa akakaa. Akamuona kaka yake ametulia. “Kuna nini kaka?” “Nataka uniambie, kwa nini mwaka jana, hukuwa ukitaka tuonane?” James akauliza. Nanaa akakunja uso. “Mbona nilikwambia kaka? Huniamini?” Nanaa akauliza. “Hapana. Nataka urudie tena. Na safari hii kwa kina.” Nanaa akafikiria kidogo. “Unakumbuka baada ya kutoka hospitalini baada ya kufanyiwa ule upasuaji, na kupata nguvu kidogo, ulikuwa unanifuata kila siku za jumamosi au jumapili tunakwenda kula nje pamoja?” Nanaa akauliza.

“Nakumbuka, lakini baadaye ukaanza kunikatalia.” “Samahani kaka. Lakini kama nilivyokuwa nimekwambia. Nia ilikuwa nzuri kaka yangu. Nakumbuka hata nilipohamia hosteli kutoka kwa Antii, bado ulikuwa unataka tukutane mahali tule?” “Nakumbuka.” James akajibu. Watu wote walikuwa wakiwasikiliza pale sebuleni.

“Ukweli harufu za baa zilinza kunishinda kaka. Nikakwambia tuhamie kwenye migahawa. Nakumbuka ukasema twende kwenye ule mgahawa wanao uza samaki wazuri wa kuchoma. Pale napo pakanishinda kabisaa. Nikashindwa kukwambia kwa kuwa wewe ulionekana kupafurahia. Hali ya kichefuchefu na mabadiliko ya mwili wangu yakanipelekea kununua kipimo mimi mwenyewe na kujipima mimba. Siku ya jumapili ambayo tulipanga tukutane kwa chakula cha mchana, ndipo nilipojipima, nikajigundua ni mjamzito.”

“Niliingiwa sana na hofu siku ile. Nikajua endapo tukikutana tu, utajua kuna jambo ninalokuficha. Ndio nikakutumia ujumbe kukwambia sitaweza kuja tena. Ukapiga simu ukataka kujua kulikoni. Lakini niliogopa hata kuongea na wewe kwenye simu. Nikajua endapo utanisikia siku ile, ungejua kuna tatizo tu. Na ungelazimisha tukutane, nakutaka kujua kulikoni. Wakati hata mimi sikuwa nikijua nikwambie nini, kwa kuwa sikuwa kwenye mawasiliano na Geb. Na hapo nilijua Geb amerudiana na Liz. Nakumbuka nikakutumia ujumbe kukwambia siwezi kuongea kwa wakati huo, nitakupigia baadaye. Sijui kama ulielewa?” “Nilijua labda unasoma na wenzio.” James akajibu.

“Nilitaka nikishajua nini chakufanya na mtoto, ndipo nikwambie. Nikaamua nimwambie kwanza Geb mwenyewe. Akikubali mtoto, nikajua ndipo nitapata ujasiri hata wa kukwambia. Basi. Nilimfuata Geb pale alipokuwa akiishi zamani ili kumwambia. Nilimkuta na Liz. Nikashindwa kumwambia. Au tukashindwa kuzungumza. Nikajua wamerudiana kwa hakika. Nikaogopa kumwambia ili nisionekane namtumia Liv kama kigezo cha kutaka msaada kutoka kwa Geb au nataka kuharibu mahusiano yao. Nikaondoka nikiwa nimeamua wewe na Geb nisiwaambie mpaka nimalize chuo.”

“Nitafute sehemu ya kuishi. Nikipata kazi na kuweza kujitegemea, ndipo nije kuwatambulisha kwa Oliva. Kumfahamu tu, sio tena kuwa tegemezi kwako kaka. Najua umehangaika sana na mimi. Sikutaka tena ujue kama ni mjamzito, halafu ukaanza tena kututunza mimi na Oliva. Nilijiambia Oliva ni mzigo wangu, nitahangaika naye mwenyewe.” James alikuwa akimsikiliza kwa makini sana.

“Ndio nikaanza kukupa sababu yakutoweza kukutana mimi na wewe. Na bahati nzuri ukawa unaelewa, na kuniunga mkono. Lakini pia mambo hayakwenda kama nilivyotarajia, ndio Geb akaja kugundua nina mtoto wake. Kukazuka kutokuwa namaelewano kabisa kati yetu. Hapo pia nikaogopa kukwambia kaka. Kwa kuwa sikuwa nikijua ni lini tena Geb atanifukuza kwake. Nikarudi sifuri kabisa. Nikawa hata sijui kesho yangu itanikuta wapi.”

Nilikuwa siruhusiwi hata kutoka na mtoto labda useme nikuletee umuone! Hapo tena nikaingiwa hofu. Nikajua ukiniona tena wakati ule ungeumia zaidi kaka yangu. Maana nilijiona nimefanya kosa ambalo ulikuwa umenionya. Tena kwa kurudia rudia. Nikaogopa hata kukuona.” Nanaa akafuta machozi.

“Nilikuwa natamani sana kukuona kakak yangu. Lakini nikajiambia ni mpaka tena nitafute sehemu yangu ya kuishi. Nijijenge hata kidogo. Wakati nahangaika kujenga uaminifu tena kwa Geb ili aniamini na mtoto. Nikajiambia akiniamini na kuweza kuniruhusu niwe natoka na Oliva, ndio pengine nikukaribishe hapo kwangu uje umuone Oliva na uone sehemu ninayoishi. Lakini Mungu ndio akasaidia, tukapata na Geb. Ndio nikamuomba kitu cha kwanza, uje nyumbani ili tukutambulishe Oliva. Geb akakubali, ndio tukakuita wakati ule. Sijui kama unaniamini kaka yangu. Lakini niliogopa.” Nanaa akaanza kutokwa na machozi.

          “Mimi nakuamini sana Nanaa. Ila nina sababu ya kutaka kujua kwa undani kama hivi. Nina swali jingine. Katika kipindi hicho chote, ulikutana na Zinda wakati gani?” James akamuuliza Nanaa. Akashangaa anajaribu kuvuta kumbukumbu. “Hukumbuki ni lini umekutana na Zinda!?” James akauliza kwa kushangaa.  “Mmmh!” Nanaa akaguna akionyesha kutokumbuka kabisa. 

“Labda nikuulize hivi. Koti alilokuazima Zinda siku ya harusi ya Malii, ulimrudishia lini?” James akauliza. “Unakumbuka siku moja, ilikuwa jumamosi. Uliniambia kuna nyama ya mbuzi wanachoma vizuri sana maeneo ya Mbezi ya Kimara. Ukataka tukutane siku hiyo kama kwenye saa tano. Nikakwambia saa tano natakiwa kwenda dry cleaner ya Sinza. Ukaanza kucheka ukaniambia, ‘mdogo wangu siku hizi unafua dry cleaner? Mambo yako safi’. Nikakwambia namchukulia mtu nguo yake. Basi lilikuwa ndio hilo koti la Zinda. Nilimpigia, nikamuomba tukutane hapohapo kwenye hiyo dry cleaner. Nikamkabidhi koti lake, akaondoka. Ndio tukakutana na wewe pale Mwenge kituoni, mida ya saa 7 mchana, tukaelekea Mbezi. Sijui unakumbuka?” Nanaa akamuuliza kaka yake.

“Sasa ile si ilikuwa mwezi wa 9 sijui au wa nane mwishoni?” “Ndio wakati ule ule. Tena umesahau tu kaka. Unakumbuka nilichukua namba ya Zinda kwenye simu yako? Sema ulikuwa ukiongea na Antii. Sasa sijui kama ulikuwa ukijua kama nachukua namba ya Zinda! Nilikuomba simu yako tulipokuwa pale kwa Antii. Ulikuwa umeniletea Calculator. Baada ya ile yangu kuharibika. Ukasema tukutane kwa Antii ili umsalimie na yeye. Ilikuwa mida ya jioni, umetoka kazini. Nikachukua namba ya Zinda, nikakurudishia simu yako.” “Basi?” James akauliza.

“Ukisema, ‘basi’, ndio unamaanisha nini!?” Nanaa akauliza. “Namaanisha hukukutana tena na Zinda?” James akauliza akitaka uhakika. “Hapana kaka! Kwanza nilimpigia kwa namba ile ambayo kila mtu alikuwa nayo. Na nilikuja kuacha kuitumia kabisa ile namba. Sasa hata kama Zinda atakuwa alikuja kunipigia baadaye, basi hakunipata. Ule ndio ulikuwa mwanzo na mwisho wa mawasiliano na Zinda. Kwani kuna kitu amesema?” Ikabidi Nanaa aulize. James akawageukia kina mama G. 

“Mbona mnaangaliana na mnasita kuniambia? Maana nilimuuliza Geb, Geb akaniambia nisubiri kwanza. Eti Geb?” Nanaa akasimama na kumsogelea Geb pale mezani akiwa anacheza na Oliva. “Unafikiri huu ndio muda wa kuambiwa? Uliniambia nisubiri. Naanza kupatwa na wasiwasi. Kuna nini?” Geb akafikiria kidogo. “Mwambie tu James.” Nanaa akageuka, akarudi kukaa pale pale alipokuwa amekaa na kaka yake.

Nanaa Aambiwa Habari Za Zinda.

“Zinda ameibua stori mpya inayosababisha mchungaji kushindwa kutangaza ndoa yenu au kutotambulika uchumba wako na Geb.” Nanaa akakunja uso. “Stori gani tena!?” Nanaa akauliza huku akimtizama James kwa makini. James akabaki na yeye hajui aanzie wapi. “Kaka!?” Nanaa akaanza kupatwa na wasiwasi.  “Ameleta uthibitisho wa cheti cha ndoa.” James akajibu. “Cheti cha ndoa!? Ya nani? Na inahusiana vipi sasa na mimi kuolewa na Geb!?” Nanaa akazidi kuhoji. 

“Ndoa yako wewe na yeye.” Nanaa akatulia kidogo kama ambaye hajaelewa. “Sijaelewa. Ndoa yangu mimi na Zinda! Au?” “Ndiyo.” James akajibu. Nanaa akabaki amekodoa macho. “Yaani amesema wewe na yeye mlifunga ndoa.” “Kwa hiyo anasema mimi ni mkewe?” “Ndiyo.” James akajibu.

“Hivi kaka unajua Zinda sijawahi hata kumshika mkono? Kwanza siku niliyozungumza naye kwa muda mrefu, ni siku ya kwanza pale nyumbani kwa Geb pale nje. Tena watu wote walisikia.” “Alipokwambia atakupa magauni?” Kaka yake akauliza. “Na viatu!” Nanaa akamalizia, watu wengine wakacheka kidogo.

“Yaani siku ile ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza na ya mwisho kukaa chini na kuzungumza na Zinda. Na ninafikiri ndio siku tuliyozungumza kwa muda mrefu mimi na Zinda. Hata nilipomuomba tuzungumze pale Marangu, hatukukaa. Tulikuwa tumesimama. Nilimwambia wazi kuwa sipo tayari kwa mahusiano, kwa kuwa akili yangu haijatulia. Tena nikamwambia nashawishika sana kukubali ili kupata tu sehemu yakueleweka ya kuishi. Nikamwambia kama alivyosikia pale, sina mahali pa kuishi. Mimi na kaka tunatafuta mahali pakuishi.”

“Nikamwambia kwa yeye kuahidi kunipa nyumba na gari ni kitu kinachosikika vizuri sana kwangu kwa wakati ule ili kupunguza ile dhihaka. Lakini nikamwambia naogopa sana kumkubalia wakati ule kwa ajili ya kupata sehemu ya kuishi tu. Tena nikamwambia sitaki aje anipe sehemu ya kuishi na vitu vyote alivyoniahidi, halafu baadaye nafsi yangu ikapata kila kitu, nikaja kugundua simpendi. Nikamwambia itakuwa simtendei haki yeye wala mimi.”

“Akaniomba tena basi tuwe tu kwenye mahusiano. Nikamwambia kwa wakati ule hata mwili wangu na akili havipo kwenye mahusiano. Akili zimevurugika. Nikamwambia siwezi kumpa kitu ambacho sina. Tena nikamalizia kwa kumsisitizia kuwa mimi sio mkewe kabisa. Nikamuomba msamaha, na kumshukuru kwa nia yake nzuri kwangu. Nikaachana naye. Sijawahi kukaa tena na Zinda kaka. Hata siku niliyomkabidhi koti lake, tulikuwa tumesimama. Yeye ndani ya gari yake, mimi nje. Akaniambia twende sehemu tukale. Nikamwambia wewe unanisubiria twende Mbezi, kwa ajili ya kula nyama choma. Nikamshukuru kwa koti, nikapanda daladala mpaka Mwenge. Sijamuona tena huyo Zinda.” Nanaa akamalizia hivyo.

Akafikiria tena. “Tena amedanganya kabisa Zinda. Maana nilikuwa muwazi kabisa kwake. Sikutaka hata kumzungusha au hata sikuwahi hata kuwa na hisia na yule kaka.” James akacheka. “Sikudanganyi kaka. Unakumbuka siku ile nilirudi nyumbani nalia? Nilikuwa nimekuaga nikakwambia naenda kukutana na Zena Surrender Hotel. Basi siku ile unajua sikukutana na Zena. Alikuwa amenikutanisha na mwanaume mwingine. Sikuwa tu nimekwambia siku ile kwa kuwa nilikuwa kama nimechanganyikiwa.” Nanaa akaendelea.

“Nilipofika pale hotelini sikumkuta Zena kama tulivyokubaliana. Nikampigia simu kumuuliza kulikoni. Akanielekeza kwenye meza aliyokuwa amekaa mwanaume fulani hivi. Nikamfuata pale nikiwa sielewi. Nikamwambia Zena ameniambia nimsubirie hapo. Yule kaka akacheka. Alikuwa kaka labda umri wako hivi au mkubwa kidogo kwako. Alionekana ni kaka aliyetulia na anajielewa kimaisha. Na alikuwa mzuri tu kwa muonekanao.” James akacheka. 

          “Usicheke kaka! Nataka kukwambia kitu cha Zinda ndio maana nakusimulia hii stori. Basi, yule kaka akaniambia anafahamiana na Zena, alimuomba amtafutie mke. Akasema Zena amemsifia nimetulia. Na maneno mengi tu. Alijieleza yule kaka kwa muda mrefu tu. Historia yake ya maisha. Mwanamke aliyekuwa naye mara ya mwisho. Kwa kifupi alitaka kunioa.”

“Lakini kaka, nilishindwa kabisa kumkubalia. Yule kaka akanirudisha kwa gari yake, mpaka karibu na nyumbani. Nilimkatalia asifike nyumbani kwako. Aliniambia nimfanyabiashara. Hapo alipokuwa alikuwa na gari nzuri tu. Lakini nilichokuwa nikijisikia wakati ule kwa yule kaka, ni kama nilichojisikia kwa Zinda. Sikutaka hata kumpotezea muda. Akanishusha, na nikamkatalia namba yangu ya simu, kabisa.” Nanaa akaendelea.

“Nilishuka pale nikiwa nakuja nyumbani huku nikiwaza. Kwanza nilijichukia kabisa. Yule kaka nilijua angeweza kuniokoa na shida za wakati ule. Lakini nikajikuta namkataa! Ndio maana nilipokuja tu nikakukuta umekaa sebuleni ukaniuliza kwa nini nalia, nikakuuliza nitajuaje kama mtu fulani ndio atakuwa mume wangu? Unakumbuka kaka?” “Nakumbuka.” James akajibu.

“Tena tukazungumza kwa muda mrefu sana pale kwenye makochi. Ukazungumza na mimi mpaka nikalala pale pale kwenye kochi mpaka asubuhi. Unakumbuka?”  “Nakumbuka Nanaa.” James akajibu huku akimtazama dada yake.

“Basi vile vyote ulivyoniambia vile, nilikuja kuvisikia kwa mara ya kwanza kwa Geb.” Kila mtu alicheka mpaka Geb mwenyewe. James alicheka mpaka akapiga makofi. “Kabisa kaka. Vile vile. Kila kitu. Tena nikijua Geb hana kitu. Nikajua ile kampuni  ni ya dada yake. Geb anatumwa tu. Unakumbuka kwenye birthday ya Fili ya  mwaka jana Geb alinifuata nyumbani akasema ametumwa na Grace, aje anifuate?” “Nakumbuka.” James akajibu.

“Basi mimi mwenzio muda wote nilijua kazi aliyonayo Geb ni kutumwa tumwa tu na dada yake. Sikujua hata kama amesoma. Lakini moyoni nikawa najisikia kama vile ulivyoniambia.” Kila mtu akacheka tena.

“Sasa nikataka kukwambia kuwa vile ulivyoniambia nitajisikia nikimpata mwanaume ninayempenda, nikataka kukwambia nimejisikia kwa ndugu yake Grace. Hapo nilikuwa hata sijui kama mlisoma naye. Ndio nikajua ana mwanamke wake. Nikasema nimuache tu. Lakini bado nikawa namfikiria yeye tofauti na wanaume wote. Na hapo bado nilikuwa najua anamtumikia dada yake. Tena kuna kipindi nikajiuliza hivi inawezekanaje mapacha wakawa tofauti hivyo!? Yaani mmoja asome, mwingine asisome? Au mwingine afanikiwe sana kama hivyo Grace, halafu mwingine asifanikiwe?” Watu wakacheka. Mpaka mama G.

“Ni kwa vile nilivyokuwa nikimuona Geb anavyojishusha kwa dada yake! Mimi nikajua hana mbele wala nyuma. Lakini bado moyoni nilikuwa nampenda kaka.” James akacheka huku akimwangalia Nanaa. “Kama Grace atakumbuka, yeye ndio aliniambia kuwa Geb anafanya kazi BOT. Nilishituka sana. Tena nikarudia kumuuliza ‘Geb anafanya kazi BOT!?’ Nikamuuliza kutaka kujua kama nimesikia na kuelewa vizuri.” “Nakumbuka Nanaa.” “Afadhali. Asante Grace. Tena nakumbuka ndipo akaniambia hata ile kampuni ni ya Geb. Na akanipa historia fupi ya maisha ya Geb. Hapo ndipo nikakata tamaa kabisa. Nikajiambia nilazima nitoe hayo mawazo. Mtu kama Geb hawezi hata kuja kuwa na wazo na mtu kama mimi.” Nanaa akaendelea.

“Lakini kaka. Japokuwa nilikusudia kuachana na Geb, lakini nikawa nimepata ile hisia kama uliyokuwa umeniambia. Nikajiambia kwa hiyo alichoniambia kaka ni kweli. Nikajipa amani hata ya yule mwanaume niliyemkataa, aliyekuwa amenitafutia Zena. Maana kuna kipindi nilikuwa nikijilaumu sana kumkataa yule kaka.”

“Haya, wakaja na wengine. Akiwepo na huyo Zinda. Nikawa natamani kile nilichojisikia kwa Geb, nikipate kwa wengine ili niolewe na mimi nipate sehemu ya kuishi. Lakini ni kweli kaka yangu sikukisikia hata kidogo. Ndio maana nilikuwa nikiwakataa moja kwa moja bila kuwapotezea muda.” Watu walikuwa wakicheka.

“Watu wanaweza kusema nimempendea Geb pesa, lakini sio kweli kaka yangu. Baada ya kukutana na Geb, nimeshapata wanaume wengi sana wakinitongoza. Tena wenye pesa nyingi tu. Muulize mama huyo hapo. Ndio msiri wangu. Huwa namwambia wanaume wote wanao nitongoza. Eti mama, si wote waliokuwa wakija si hata wewe ulikiri ni matajiri?” Nanaa akamgeukia mama G, akitaka utetezi.

“Haswaa. Hata yule wa mwisho alionekana anapesa sana.” Mama G akamtetea. “Si umesikia kaka? Lakini sikuwa napata hisia zozote.” “Kama ulizokwisha zipata kwa Geb?” James akauliza nakufanya mpaka Nanaa mwenyewe acheke.

“Hata kidogo. Nilikuwa sisikii chochote zaidi ya ahadi zao tu. Kwa hiyo Zinda ni muongo kaka. Kwanza amesema tulioana naye lini?” “Kipindi hicho ulipokuwa na matatizo na Geb.” Nanaa akashituka sana. “Matatizo gani na Geb!?” “Vile ulivyomfumania Geb na Liz. Anasema baada ya kumfumania Geb, ukaamua kuachana naye. Kwa hiyo siku ulipomrudishia yeye koti lake ndio….” “Ngoja kwanza kaka. Yeye Zinda amefahamu vipi mambo yangu ya ndani hivyo!? Atakuwa amejuaje wakati mimi sikumwambia mtu yeyote. Hata wewe sijakwambia hata kwa kuropoka kama nilimfumania Geb na Liz. Mtu anayejua ni mama tu ambaye ndiye msiri wangu. Sijamwambia mtu yeyote yule! Sasa Zinda ameambiwa na nani mambo makubwa hivyo!?” Nanaa alishabadilika.

Akamgeukia Geb. “Ni wewe Geb?” Nanaa akauliza. “Hapana Nanaa.” Geb akajibu. Nanaa akamgeukia mama G huku machozi yakimtoka. “Ni wewe mama? Maana wewe ndio msiri wangu? Wewe ndio umemwambia Zinda?” “Hapana Nanaa mwanangu.” “Asante mama. Ningeumia sana. Mwenzio wewe ndio msiri wangu. Sina mtu mwingine ninayemwambia mambo yangu ya ndani isipokuwa wewe tu.” Nanaa akajifuta machozi, akatulia.

Lakini kama kitu bado kilikuwa kikimsumbua. Akaendelea kujiuliza. “Sasa atakuwa ni nani ameweza kutoa mambo makubwa hivi humu ndani na kumwambia Zinda!? Maana ni kama amempa fimbo ya kutuchapia mimi na Geb!” Watu wote wakawa wamenyamaza. Nanaa aliuliza swali lililozua ukimya wa hofu pale sebuleni. Kila mmoja alibaki akiwaza lake.

~~~~~~~~~~~

Geb alikuwa akimuwazia mama yake. Asingependa Nanaa akosane na mama yake hata kidogo. Mama yake ndiye aliyewasimulia Grace na mumewe siku walipoenda nyumbani kwake na kukutana na mtoto mgeni kwao, Oliva, halafu Nanaa hakuwepo alikuwa amelala hotelini baada ya kuchelewa kurudi nyumbani. Walipouliza mtoto wa nani, na kulikoni Nanaa hayupo ndipo Mama G alipowasimulia kila kitu. Wakamsema sana Geb, mpaka akamfuata Nanaa hotelini. ‘Sasa Nanaa ataelewa?’ Swali lililoanza kumsumbua kila mtu. 

Danny ndiye aliyetoa maneno na kuyapeleka kwa Zinda. Danny na Zinda hawakuwa tu marafiki. Walikuwa kama ndugu. Danny mtoto yatima, alipokelewa kwa kina Zinda kama mtoto wa nyumbani. Alishafanya biashara na baba yake Zinda kama baba yake. Nyumbani kwa kina Zinda, Danny hakuhitaji kwenda na Zinda au kukaribishwa. Wakati mwingine alichukua familia yake na kwenda kusalimia wazazi wake Zinda. Au akisikia mama yake Zinda ni mgonjwa, alimchukua Geb na kuwahi Tabora kumuwahi mama Zinda na kumkimbiza hospitalini. Aliweza kutuma pesa kwa kina Zinda bila hata kumwambia Zinda. Danny alikuwa mtoto wa nyumbani. Kaka wa hiari wa Zinda. ‘Sasa Nanaa ataelewa?’ Ni swali lililozidi kuumiza vichwa vyao zaidi vile jinsi Nanaa anavyouliza.

~~~~~~~~~~~

“Sasa atakuwa ni nani ameweza kutoa mambo makubwa hivi humu ndani na kumwambia Zinda!? Maana ni kama amempa fimbo ya kutuchapia mimi na Geb.” Hilo ndilo likabaki swali lakuumiza kichwa cha kila mtu hapo sebuleni.

~~~~~~~~~~~

Mungu bado anatenda Miujiza. Hajawahi kuacha, na wala hana mpango wakuacha. Hana upendeleo. Habagui wala kuchagua. Hufanya kwa kadiri ya apendavyo.

Nanaa na Geb wameshuhudia hilo.

KUPOKEA muujiza ni jambo moja, na KUUTUNZA ni jambo la pili. Ukifikiri shetani huwa analala au anasinzia, badili fikra.

Hawa wapenzi wawili ametoka kukutana uso kwa uso na nguvu za Mungu.

Si kusimuliwa! Hata masaa 24 hayajapinduka tokea Nanaa amuone malaika wa Mungu, LAKINI tayari shetani ametupa JINGINE.

Nanaa amerudi nyumbani, anataka kujua wabaya wake.

Sasa je, yupo tayari na ukweli? Nini kitaendelea kati yao? Alilokusudia shetani safari hii, watasimama?

Usikose kufuatilia.

 

 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment