Geb alibaki akifikiria, wakati Nanaa akiendelea
kulia. James alikuwa ameinamisha kichwa pale alipokuwa amekaa. Amekishikilia kana kwamba kinataka kuanguka.
Walimsikia na yeye akivuta kamasi kama aliyekuwa akilia. Ukimya ukatanda tena.
Kila mmoja akiwaza lake. Mchungaji akakata simu. Bado jua lilikuwa likiwaka
nje. Hakuna aliyekuwa na wazo hata lakuangalia saa. Wazi walijua ndio mida ya
ibada kuisha. Inamaana hata bado hapo kanisani hapajapoa tokea mama yake James
na Zinda waamshe sakata la kipingamizi cha ndoa ya Nanaa na Geb.
Kwa alivyo mzungumzaji mama yake, James alianza
kupata picha moto aliowawashia hapo kanisani. Kwa fujo alizozifanya siku ile
pale baa na matusi aliyokuwa akiyamwaga kwenye kundi lao la whatsapp, Danny
akaanza kupata picha ya sakata alilolipeleka Zinda pale kanisani. Wote
walibaki kimya.
~~~~~~~~~~~~
“Milioni 20 nyingine!?” James alisikika akirudia kwa sauti iliyojaa
huzuni huku akifuta machozi. Mtoto huyo wa kiume, alifikishwa mahali hajui
atafanya nini na dada yake huyo hapo kitandani. “Labda
nitafute mteja wa kiwanja changu na ile nyumba ninayojenga. Nimlipe mama. Haya
mambo yaishe.” James aliendelea.
“Naombeni wote muondoke jamani.
Nataka kubaki tu peke yangu.” Nanaa naye akaongeza. “Naombeni
mniache. Geb, nakushukuru kwa kila kitu. Lakini kwa sasa nataka niachwe peke
yangu, tafadhali.” Nanaa alisisitiza huku akilia. “Nimechoka. Naona inatosha. Naomba niachwe
kabisa.” Nanaa akaendelea.
“Nilikwambia sitaondoka hapa hospitalini bila
wewe Nanaa.” “Mimi sikutaki tena Geb. Sitaki tena
mahusiano na wewe.” “Naomba usiwahi kurudia kuniambia hivyo tena Nanaa.”
Nanaa aliendelea kulia. “Mimi na wewe tuna maagano ya milele ambayo hayavunjiki
kwa changamoto za njiani.” “Tutafanyaje Geb!?” “Hilo
ndilo swali ulitakiwa kuuliza Nanaa. Sio kunikana!”
“Naona mambo yanazidi Geb! Sina
thamani ya milioni 50 mimi. Waambieni hao wote waje wanione sasa hivi kama bado
wataendelea kuning’ang’ania. Nimeanza kuoza nikiwa hai. Hakuna mwenye haja na
mimi zaidi yakutaka kunikomoa tu. Unafikiri Zinda atanitaka sasa hivi
jinsi nilivyo? Au huyo mama mkubwa unafikiri atavuna matunda gani hivi nilivyo?
Mwambieni aje anichukue muone kama atanikubali. Wameamua kunikomoa tu.” Nanaa aliendelea kulia
huku akiongea.
“Hawajui wanadai nini.
Hawajaniona.”“Mimi
na wewe Nanaa, ni mpaka kifo kitakapo tutenganisha. Hakuna pesa itakayokutoa
kwangu. Pesa yeyote wanayotaka nitawalipa. Kwa vyovyote ulivyo na
utakavyokuwa, wewe ni Nanaa Magesa. Ni wangu sasa hivi na ni jukumu langu.
Nitanunua uhuru wako kwa bei yeyote ile. Nakupenda wewe, na nimekuchagua wewe.
Hata iweje, utakuwa wangu tu. Wala pesa isikulize.” Geb akamgeukia Grace.
“Kitabu cha hundi ya akaunti yangu mimi binafsi,
sio ya kampuni, kipo kwenye mkoba wa laptop yangu. Mpe mama aniletee kesho
wakati anamleta Liv hapa hospitalini nishinde naye. Nitaweka saini tu bila
kuandika kiasi ili mama aende nayo wakati anakutana na mama James. Nataka kesho
tufikie hatima ya hiyo pesa mama. Nataka tumalize kumlipa huyo mama kiasi cha
pesa atakachoridhia yeye. Jaza hiyo hundi, hakikisha anasaini mahali kukubali
amepokea, kisha mkabidhi, yaishe. Tafadhali mama, naomba hakikisha kesho iwe mwisho
wa hayo madai. Sitaki kusikia tena.” Geb alitoa hayo maagizo.
“Mimi nitakuongezea pesa kiasi Geb. Ninayo
akiba.” “Nakushukuru James. Lakini hapana. Umeshahangaika sana na Nanaa
mpaka kumfikisha hapo alipo. Inatosha. Nilishawalipa mahari yenu.
Mkakubali. Nanaa ni mke wangu mimi. Nina jukumu la kumlinda kwa namna yeyote
ile. Hapo alipo ni mjamzito na mgonjwa. Naomba mambo mengine yote kuanzia leo
niambiwe mimi tafadhali. Nataka yeye ajifikirie yeye na mtoto aliyekuwepo
tumboni tu.” “Usisahau harusi pia.” Grace akaongeza wote wakamgeukia kama
kumshangaa. “Ni kweli Grace. Ajifikirie yeye mwenyewe, mtoto na harusi. Basi.”
Geb akakubaliana na dada yake.
“Mengine yote, yaishie hapo nje ya huo mlango.
Sitaki matatizo mengine yeyote yale yaingizwe tena ndani ya hiki chumba.
Nitamlinda Nanaa kwa kila namna.” Geb aliongea kwa kutulia. Akaendelea. “Na
ninaomba, mtu yeyote yule, asiambiwe hali ya Nanaa. Sitaki mtu yeyote
mbali ya nyinyi aje kumuona Nanaa. Sitaki wageuze hapa ni mbuga za
wanyama. Sitaki waje washangae na kuzidi kumtia hofu.”
“Danny, naomba endeleza mipango ya harusi kama
kawaida. Marafiki wote habari watakazopewa ni za harusi tu. Wakitaka kujua hali
ya Nanaa, waambieni…” “Nanaa amewekwa ndani anatayarishwa kwa ajili ya harusi.”
Mama G akadakia na kumalizia.
Wote wakamgeukia. “Kabisa. Hakuna mtu
atakayemuona Nanaa mpaka siku ya harusi yake. Kila mtu ajue hivyo. Mafunzo yao
ya ndoa yataendelea hapa hapa ndani mpaka siku yao ya harusi kama alivyosema
Geb. Mimi na Grace tutakuwa tukija kuzungumza na Nanaa juu ya ndoa. Hatutataka
mtu mwingine amfundishe kitu chochote Nanaa, isipokuwa mimi na Grace.” Mama G
akaongeza. “Asante mama.” Nanaa akashukuru. “Nakushukuru mama.” Geb naye
akaongeza.
“Na James, tafadhali sana. Hata mama yako naomba
asijue hali ya Nanaa. Niacheni tu mimi mwenyewe. Nitamlilia Mungu wangu mpaka
atakaponijibu. Na ninajua atajibu tu. Sitaki mtu yeyote yule ajue. Maana hata
wakijua, haitasaidia kitu.” Geb akaongeza.
“Inawezekana wanajua kinachoendelea sana tu.
Inawezekana mmoja wao ndio anahusika na kukuweka hapo Nanaa.” Mama G aliongea,
wote wakamwangalia. “Nawaambia kweli kabisa. Nyinyi mmeshawahi kuona ugonjwa
kama huo? Upo mkono wa mtu juu ya miguu ya Nanaa. Lakini mimi sitanyamza
Geb.” Mama G akaongeza wote wakabaki wakimwangalia.
“James, mimi nakutuma kwa mama yako. Mwambie kama
anahusika na ugonjwa wa Nanaa, ahakikishe huyu mtoto anapona. Huna haja ya
kumwambia anaumwa nini na yupo wapi, ila mwambie nataka atoe mkono wake kwenye
maisha ya Nanaa. Tutamlipa pesa yake, aachane na Nanaa. Anaanza vita kali sana,
ambayo mwambie namwakikishia hatashinda. Pesa yake yote tutampa kesho. Mwambie
aje ofisini kwa mchungaji majira ya saa 11jioni. Nitazungumza na mchungaji ili
aite na wazee wa kanisa, washuhudie tukimalizana na mama yako.” Mama G
akamgeukia Geb.
“Geb! Mpigie simu huyo meneja wa benki, mwambie
anitayarishie kopi zote za malipo ya hiyo milioni 30 aliyochukua mama James.
Nitapita hapo benki kesho kuchukua hizo kopi zote, wakati naelekea kanisani.”
Mama G akanyanyua tena simu akapiga mchungaji.
“Naomba mwambie Zinda, kesho akuletee
hicho kithibitisho cha ndoa yake na Nanaa. Kaka yake Nanaa, ambaye ni James,
mimi, mwanangu Danny tutakuwepo hapo kanisani saa 11 jioni kuangalia hicho
kithibitisho na aseme ni nani alimlipa hiyo mahari ya kumuoa Nanaa. Na
tafadhali sana mchungaji.” Mama G akaendelea.
“Ili kusiwe na kupindisha maneno hiyo
kesho na baadaye, naomba unisaidie kunitafutia baadhi ya wazee watakaoweza
kuwepo kesho kwenye hicho kikao.” “Ni wazo zuri mama. Poleni kwa matatizo.”
“Nashukuru. Lakini mpaka sasa, sijaona tatizo. Hatuna tatizo hata kidogo. Hiyo
ndoa itafungwa tu. Na ili kufanikisha hilo, naomba usimwambie Zinda kama sisi
tutakuwepo hapo. Anaweza asitokee. Nataka afike hapo, ndipo atukute
tukimsubiri. Nimemuomba na mama James pia awepo tumlipe pesa yake. ” “Sawa
mama. Mungu azidi kuwalinda.” “Amina.” Mama G akaagana na mchungaji. Akakata simu.
“Asante mama.” Geb alisikika akiwa amepata
aghueni. “Mungu yuko na wewe Geb. Uamuzi uliochukua ni wa busara. Binafsi
nikushukuru. Hisia nilizonazo kwa Nanaa, ni kama mtoto niliyemtoa tumboni
kwangu. Huwa najiambia ndio kiziwanda wangu.” “Mama wewe! Sio mimi tena?” Wote
wakacheka mpaka Nanaa na mama G, wakacheka. “Kweli tena. Nampenda Nanaa, kwa
moyo wangu wote bila unafiki. Na Nanaa, utasimama tu siku yako ya harusi. Na
utalea wanao mwenyewe. Wala usiogope.” Nanaa akaanza kulia tena.
“Kulia ni kukubali kushindwa Nanaa. Sasa hivi
simama kama Simba, ukitetea wanao. Kilio cha Oliva leo kikutie shauku ya kurudi
kwako na kulea wanao. Usikubali kushindwa kizembe hivyo. Simama mchana na usiku
ukimlilia Mungu, akutoe hapo kitandani. Najua inaogopesha. Lakini jiambie
tunae…” “Simba wa kabila la Yuda. Atanguruma tu. Na akinguruma, kila agano
na kila madhabahu iliyohusika na kuweka agano la hicho walichokutupia, hakika
Yesu atakipindua. Sitanyamaza, mpaka Mungu, mume wa wajane. Baba wa yatima, atakaponijibu.
Hakika atajibu Nanaa mwanangu. Wala hapo hutakaa muda mrefu. Utatoka tu.” Mama
G alimkatisha mwanae Grace, akaendelea yeye akiwa amejawa ujasiri.
“Umesikia Nanaa? Usilie tena.” Grace akaendelea.
“Ila hakikisha ukitoka hapo unaushuhuda mkubwa. Kukaa kwako hapo isiwe bure.
Lile baya alilokusudia shetani juu yako, Bwana akutendee mema. Badilisha hiyo
historia. Jiambie hapo upo kwenye shule. Lazima ukitoka hapo uwe watofauti.
Mungu amekutenga kwa muda. Badilisha mtazamo wako weka kwa Yesu tu. Kuanzia
sasa, mwambie Mungu aseme nawe kwa kuwa umekaa chini, umetulia,
unamsikiliza yeye tu. Inawezekana ulikuwa na mambo mengi. Wewe na Geb. Wote
mmeshindwa kumsikia Mungu. Sijui kama mlikuwa mkipata muda wa pamoja kumuomba
Mungu? Japo mama alishaniambia aliwafundisha.” Grace aliwatizama wote wawili
kutaka kujua.
~~~~~~~~~~~~
Wapenzi hao wawili walijawa kiu iliyokuwa haiishi
kati yao. Kila walipokuwa wakipata muda wao peke yao, ilikuwa ni mapenzi tu. Na
tena kila walipomaliza, waliwekeana ahadi ya kuendelea baadaye kana kwamba
hawakutumia masaa na masaa hapo kitandani au kwenye kochi lao hapo chumbani. Na
kwa kuwa walikuwa wakilala peke yao juu gorofani, walifanya mapenzi kwa raha
zao zote wakijinafasi.
Chumba chao kilikuwa na sebule ndogo tu. Geb
alitengeneza sebule hiyo iliyokuwa ikiangalia baraza kubwa la nje, la huko huko
gorofani. Lililokuwa limezungushiwa vyuma vizuri sana vya urembo na kioo
kizito. Mwanga wa jua ulikuwa ukimulika sebule hiyo ndogo iliyokuwa
imetenganishwa na milango ya kusukuma ya vioo. Mtu wa nje hakuweza kuona ndani
ila wa ndani tu. Kuliwekwa tv kubwa sana ambayo wakati wote walijiambia wanakaa
hapo kuangalia tv, na kuishia kufanya mapenzi kwa muda mrefu huku movie
ikiendelea.
Ndani ya hicho hicho chumba chao, kulikuwa na
chumba kikubwa tu cha nguo na viatu. Upande wa Geb, na upande mwingine wa
Nanaa. Napo huko walikutana wakati wa kuvaa baada ya kutoka kuoga. Kila
walipotizamana, walianza upya ndani ya chumba hicho hicho na kujikuta wanarudi
tena kuoga ambapo na huko bafuni kulikuwa na sinki kubwa la kuogea pamoja na
bafu. Na sehemu kubwa yenye sinki la kupigia mswaki lenye vitu vyao baadhi.
Upande wa Geb, kulikuwa na vifaa vya kunyolea ndevu na mafuta yake. Upande wa
Nanaa, vitu vya kike. Mbele ya hilo sinki kulikuwa na kioo kikubwa sana
ukutani. Napo pia Geb alijikuta akichelewa kutoka humo maliwatoni kuwahi kwenye
majukumu yake ya kila siku.
Kwani kila alipokuwa huko akimalizia kujisafi,
huku Nanaa naye amejifunga taulo akitaka na yeye kujipodoa mbele ya sinki hilo
lenye kioo kikubwa upande wake kisha atoke ili akasaidie kazi za humo ndani au
hata mtoto wake tu, Geb aliishia kumkodolea macho kwa kupitia kioo hicho,
mwishowe uzalendo humwisha, na kuishia kukwapua taulo hilo mwilini mwa Nanaa,
nakuomba kuagwa ili aweze kutulia kazini. Huku akimuahidi Nanaa, akimpa penzi
la mara ya mwisho hapo hapo bafuni, ataondoka kuwahi kazini. Mchana hatarudi mpaka
jioni akitoka kazini.
Lakini mchezo ukawa ni huo. Kazi zikipungua
kazini mida ya mchana, Geb anarudi huku akimwambia Nanaa, asubuhi wakati
wanaagana, hakufaidi hiki au kile. Anamtaka kidogo tu huko chumbani ili angalau
akatulize mawazo kwenye kikao chake cha jioni huko kazini na watu muhimu. Na
kwa penzi alilokuwa akipewa Nanaa. Sifa alizokuwa akipewa kuanzia nguo ya ndani
atakayokutana nayo Geb muda huo, Nanaa alikuwa akiomba Geb arudi tu, amfunue,
afurahishwe. Hata yale mapungufu aliyokuwa nayo Nanaa, kama mwanamke, akitamani
Mungu asingemuumba nayo, Geb alijigamba na kumwambia ndio starehe ya macho
yake. Akimuona tu hivyo, hajiwezi. Kwa hiyo hakuna jinsi ungemwambia Nanaa,
asimvulie nguo Geb, muda na wakati wowote akakubali.
Maombi, kusoma neno la Mungu, vyote vilisubiri.
Ushirika wao na Mungu kama walivyofundishwa na mama yao, walisogeza mbele. Kila
wakati waliambiana wataanza kesho. Walishapanga mikakati. Walishaweka
mipango ya kuanza kusoma bibilia kwa pamoja. Waanzie wapi, waishie wapi. Geb
alipokuwa kazini, Nanaa alipata ‘bible plan’
nzuri sana kwa wapenzi au wanandoa, kutoka online. Akaichukua ili waanze kusoma
pamoja na kuomba. Jioni hiyo baada ya Geb kutoka kazini, Nanaa alipokuwa
akimuelezea Geb juu ya hiyo ‘bible plan’, wakiwa
chumbani kwao, akimwambia waanzie hapo, walijikuta wakihema pembeni, baada ya
shuguli nzito na tamu ya mapenzi.
Geb alikuwa akiangalia midomo ya Nanaa wakati
akimuelezea, huku amejilaza kwenye kochi hapo chumbani kwao. Mikono ya Geb
ilikuwa ikitembea mwilini mwa Nanaa, wakati Nanaa ameshika simu yake anamsomea
hiyo ‘bible plan’ kutoka kwenye bibilia. Waliishia
kufanya mapenzi. Geb akamsifia kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kutafuta plan hiyo, na mkakati wa kuanza kusoma na kuomba
pamoja, akamwambia lazima kesho yake waanze. KESHO haikuwahi
kufika, mpaka hapo Grace anapowauliza.
~~~~~~~~~~~~
Alipowaona wanaangaliana, Grace akapata jibu
lake. “Nanaa na Geb, shetani yupo na nguvu zake ni halisi. Msifanye mchezo
jamani. Mkiishi hivyo mbali ya nguvu za Mungu, atawachezea kwa kadiri ya uwezo
wake. Na yeye huwa hachoki. Atatuma attacks kutoka nje. Akiona
mnashinda na mmeshikana kama sasa hivi, ataanza kuwajaribu nyinyi kwa nyinyi.
Ombeni bila kukoma. Ombeni msiingie majaribuni. Ombeni myashinde majaribu.
Yapo. Yatakuja. Msipuuze hata kidogo.” Grace alikuwa akiongea nao kwa taratibu.
Dada huyo mkimya, lakini kumbe alibeba nguvu ya
ajabu. Akianza kuzungumza mambo ya Mungu, utapenda kumsikiliza. Kwa kuwa
alijitolea mfano na kuwaambia ni maisha anayoyaishi yeye. “Mnadhamana ya roho
mbili sasa hivi kama sio tatu. Maana hatujui Nanaa ana watoto gani humo
tumboni. Kama ni mapacha au mmoja. Hizo roho mtadaiwa na Mungu! Mtazitolea
hesabu siku moja. Msizembee. Simameni kwa ajili yenu na watoto wenu.” Grace
akamaliza na kunyamaza.
“Mmeelewa Geb na Nanaa? Huu muda mtakao kuwepo
hapa, utumieni vizuri kama alivyosema Grace. Shetani hapendi familia. Ndio
maana wakati wote anasimama kupinga ndoa. Anajua akimpata mama au baba, amepata
taifa la kesho. Ambao ni watoto. Mmesikia?” “Nimeelewa Grace na mama. Nawaahidi
kufanyia kazi. Hii ni ‘wake up call’ yetu.
Akimaanisha kengele ya kuwaamsha kutoka usingizini. Hatutatoka hapa kama
tulivyoingia. Si ndio Nanaa?” Geb alimsogelea Nanaa, akainama na kumbusu. Nanaa
akatingisha kichwa akikubali.
“Basi kabla hamjaondoka,
naomba tuombeni tena pamoja.” Geb akapiga magoti pembeni ya kitanda cha Nanaa.
“Nipe mkono wako.” Nanaa akampa mkono ule ambao haukuwa na dripu. Geb
akaushika. Hakuna aliyemuona Geb akiomba vile. Japokuwa hakuwa akiomba, lakini
alikuwa akimuona mara zote vile mama yake alivyokuwa akimuombea. Usiku wakiwa
wanalala na mama yake. Enzi akilala na mama yake kabla Nanaa hajaanza kuishi
nao. Mama G alikuwa akimshika Geb mikono usiku anaomba. Mama huyo hakuacha
kutubu kwa niaba ya mwanae huku akimsihi Mungu amtakase. Wakati wote alibariki
mikono ya mwanae, nakumuombea katika kila eneo. Geb aliishia kusema ‘Amen’. Na kulala bila hata kuongeza neno. Lakini siku
hiyo aliomba kama mama yake.
Aliomba mpaka Nanaa
akashangaa. Akafungua macho na kumtizama Geb aliyekuwa amezama kwenye uwepo wa
Mungu. Alishakuwa ametubu kwa ajili yake, Nanaa na Oliva. Akamtakasa na mtoto
au watoto waliokuwepo tumboni. Akaomba uwepo wa Mungu. Danny mwenyewe hakuamini.
Aliomba kwa muda wa dakika 36, bila kupumzika. Ndipo akamaliza. Mama G
akafurahi sana.
“Sasa
hapo, hata nikiondoka sitakuwa na wasiwasi. Najua kiziwanda wangu yupo kwenye
mikono mizuri.” “Kweli mambo yanabadilika! Nanaa amenipokonya nafasi yangu hivi
hivi!” Angalau wakaanza kucheka. “Muda wakudeka umeisha Geb. Unaingia kazini.”
“Ni kweli. Nilishazoea kuombewa na mama.” Wakacheka.
“Mama!”
Geb aliita. “Naomba asubuhi Liv akiamka, ukishamlisha, umlete. Sitaki akae
mbali na mama yake. Hajawahi kuwa mbali naye. Na sitaki aone tofauti. Mimi na
mama yake wote hatupo! Haitakuwa vizuri. Kwa kuwa mimi nitakuwepo tu hapa,
mlete nishinde naye.” Watu wote wakanyamaza.
“Nini?” Geb akauliza. “Kwa nini usimuache kwa
muda mpaka mama yake apone?” “Nitachanganyikiwa mama. Naomba aje tu. Akiwa hapa
akili ndio itatulia.” Nanaa aliongeza. “Sawa nitamleta. Lakini sio asubuhi.
Angalau tumuache apate na ule usingizi wake wa saa tano. Akiamka hapo, ale
chakula kwanza. Halafu nitaenda naye benki kuchukua hizo karatasi, ndio nije
naye hapa. Sitaki akae hapa hospitalini muda mrefu. Atataka kutambaa. Na
sidhani kama kuna mazingira hayo, hapa.” “Basi ukija uje na kile kigari chake
chakutembea.” “Hapo sawa.” Wakakubaliana.
James akamsogelea Nanaa. “Nitakuona baadaye
kidogo. Ngoja nikafuate vitu vya Geb.” “Tutaongozana James. Na mimi naondoka
sasahivi.” Grace akaaga. “Asante kaka.” Nanaa
akaanza kulia. James akasimama pale kwa muda akimwangalia dada yake kwa
kumuhurumia. “Pole sana Nanaa. Pole. Nitakuona baada ya muda kidogo.” James
akaaga. “Na wewe Nanaa uletewe nini?” Mama G akauliza. “Uji
wa Geb, na chakula chake. Hajala vizuri mama. Anaweza kulala na njaa.”
“Basi itabidi James asubiri kidogo huko nyumbani, nipike haraka haraka.”
“Asante mama yangu.” Nanaa akashukuru. Kila mtu akacheka. “Asante Nanaa.” Geb
akamshukuru. Nanaa akatabasamu huku akifuta machozi mashavuni.
“Mwenyewe anamkumbuka Geb hata akiwa na
matat….”Danny akashindwa kumalizia. Akanyamaza kwa muda. “Nanaa na Geb, upendo
una nguvu ya ajabu sana. Mkiendelea hivyo. Mkichanganya na maombi. Mkajisogeza
karibu na Mungu. Hakuna litakalo washinda.” “Kama wewe na Grace?” Nanaa
akadakia. Wakacheka. “Na sisi mtuombee tuwe kama nyinyi.” Nanaa aliongeza kwa
upole. “Mungu ameshawasaidia Nanaa. Yupo na nyinyi.” “Amina na asante Danny.”
Wakaagana. Wote wakaondoka.
Usiku Wa Kwanza Nanaa Akiwa Hospitalini.
Geb
alijitahidi sana kumliwaza. Usiku huo aliutumia kumuwekea viapo vya milele.
Daktari alishapita. Na nesi naye akawa amechukua vipimo vyote. Nanaa hakuwa
amepandisha homa wala pressure. Kila kitu kilikuwa sawa tu. Daktari alimwambia
nesi aliyekuwepo zamu, ajaribu kufyoza yale maji kutoka kwenye malengelenge ya
miguu yake. Ili baadhi ya maji hayo yakafanyiwe vipimo. Yule nesi alishangazwa
na yale malengelenge. Alivyoyafyonza maji, muda ule ule yakajaa tena na kurudi
kama yalivyokuwa! Kwa mshituko akaongea pale pale mbele ya Nanaa na Geb. Nanaa
akaanza kulia.
Nesi alipoondoka, Geb akamfuata. “Tafadhali sana.
Naomba maendeleo yote ya ugonjwa wa Nanaa nijulishwe mimi. Naomba yeye aachwe
kwa sasa. Sitaki aanze kupandisha pressure na ujauzito alio nao. Nataka atulie.
Sijui itawezekana?” Geb aliongea kiugwana sana. “Samahani. Nikatika hali ya
mshituko tu kaka yangu. Sijawahi ona kitu kama hicho! Samahani sana.
Nitajulisha na wengine.” “Nitashukuru. Unaweza kunipa mataulo ya ziada ili niwe
nambadilisha mwenyewe. Kuwapunguzia usumbufu usiku.” “Basi nitakuletea. Lakini lazima
kuja kubadilisha mfuko wa mkojo na kumwangalia tena homa na pressure yake.”
“Hamna shida.” Geb akarudi chumbani alipokuwa Nanaa.
Bado alimkuta akilia. “Itakuwaje Geb?” Nanaa akauliza huku akilia sana
kwa hofu. “Sijui Nanaa! Lakini najua kitu kimoja.” “Nini?”
Nanaa akauliza kwa shauku kama aliyejua Geb anamajibu yote. “Ukiacha
kulia nitakwambia.” “Niambie tu Geb.” “Nataka
unisikie ukiwa umetulia.” “Siwezi. Naogopa.
Itakuaje maisha yangu yaje kuishia hapa kitandani?” “Tumezungumzia nini
juu ya swala la hofu Nanaa?” Geb akamuuliza.
“Umesema
ndio njia ya kuzidi kumfungulia shetani mlango. Lakini unajua kama binadamu
nashindwa Geb.” “Nakuelewa.
Na sikulaumu. Acha imani yangu ikubebe kwa sasa. Nitaamini kwa ajili yako.
Mungu atatenda tu. Naomba usiangalie hii hali sasa hivi. Tuangalie ahadi za
Mungu tu.” Geb akajaribu kumtuliza.
“Lakini
itakuaje kama nikibakia hivi hivi nisipone? Utafanyaje?” Nanaa akauliza.
“Ninachojua kwa hakika ninakupenda wewe Nanaa. Na nimekuchagua wewe uwe mke
wangu. Tutazikana. Kwa hali yeyote ile, wewe ni wangu. Tupo hapa kusubiri
majibu ya vipimo vyote walivyochukua. Yakitoka na kusema kila kitu kipo sawa,
tutakubaliana nayo. Tutaondoka hapa na kurudi nyumbani kwetu. Maisha ya aina
nyingine yataanza. Nikijua unahitaji msaada wa karibu zaidi, haswa mimi
ninapokuwa kazini. Na hapo ndipo itakaponilazimu kutafuta msadizi wa kutusaidia
mimi na Grace. Ili niwe na wewe muda mwingi. Basi. Hakuna kitakachobadilika
kati yetu sisi wawili. Mungu akizidi kutubariki siku, tutafunga ndoa yetu.
Wakati tukiendelea kumsubiria mtoto wetu.” Nanaa akavuta pumzi kwa nguvu
akijaribu kutulia.
“Kwa hiyo
niwe na uhakika kuwa hutaniacha peke yangu?” “Naanzia
wapi Nanaa? Niende kwa nani?” “Sijui Geb!”
“Haitakaa ikatokea. Ni kifo tu ndicho kitatutenga mimi na wewe mpenzi wangu. Na
nitamlilia Mungu atupe umri mrefu mimi na wewe.” “Nakushukuru
Geb.” Geb akambusu.
“Lakini nikuombe kitu Nanaa.” “Nini?” Geb akavuta shuka na kumfunika vizuri.
“Najua upo kwenye wakati mgumu sana. Uelewe hata mimi nipo kwenye wakati mgumu.
Nakuhitaji kuliko unavyofikiria wewe. Nakuhitaji sasa hivi. Ukiwa kwenye hali
hiyohiyo ujue nakuhitaji. Wewe ndio faraja yangu. Naomba isitokee ukanikana
tena.” “Sitarudia tena Geb. Niliingiwa hofu na hiyo
pesa. Ni nyingi sana.” “Naelewa. Lakini naomba katika kila changamoto,
tusimame pamoja. Leo ni wewe wanadai hiyo pesa, je ikitokea ni mimi?” “Unajua sitawahi kukukimbia Geb. Nakupenda.”
“Basi endelea kuonyesha kwa vitendo na maneno
yako. Nahitaji kusikia hivyo hata nyakati za shida. Tafadhali Nanaa.
Inaniogopesha kukuona upo tayari kuachana na mimi kirahisi hivyo!” “Nisamehe Geb. Tafadhali nisamehe mpenzi wangu. Nimepata
habari ngumu ngumu kwa wakati mmoja. Nikaona nikupunguzie mzigo. Labda
tukiachana, utapumzika. Nimeona vimezidi Geb!” “Hakuna pumziko mbali na
wewe. Wewe ndio pumziko langu.” Nanaa alilia sana.
Alijifikiria hali
aliyonayo wakati ule. Na maneno aliyokuwa akiyasikia kutoka kwa Geb, vilimgusa
sana. Ndipo akasadiki kuwa Geb ana mapenzi naye ya dhati. “Nakushukuru sana Geb. Asante mpenzi wangu. Sasa hivi
nimethibitisha. Maisha yangu yote nimejua ninaye kaka tu. Lakini angalau sasa
hivi najua umeongezeka na wewe. Asante mpenzi wangu.” Geb akamvuta
karibu akaanza kumbusu huku amemkumbatia. Alimnyonya midomo yake kwa utulivu
akiwa amelala palepale kitandani na dripu yake ya maji mkononi. Alimnyanyua
kiwiliwili kidogo tu, akahakikisha amemudu kumkumbatia vizuri.
“Nakupenda sana Nanaa.” “Nimeamini Geb. Asante.
Nakushukuru kuwa hapa na mimi. Asante kunilipia garama kubwa sana kutoka kwa
mama mkubwa.” “Karibu.” “Nakupenda Geb.” Geb akatabasamu. “Asante Nanaa.”
Akaanza kumbusu tena mpaka nesi akaingia kuleta mataulo. Akamkabithi Geb, na
boksi la gloves. Akatoka.
“Nataka upumzike. Leo umekuwa na siku ndefu sana.
Kesho tutaanza kutafuta majina ya mtoto.” Nanaa akacheka. “Sawa.” “Nilimisi
hizo dimpozi!” Geb akamshika mashavuni. “Usilie tena bwana. Unajua ni jambo
moja kujaribiwa. Lakini kukosa au kupoteza tumaini ndio mbaya zaidi. Naomba
amani yetu idumu. Amini kunamahali Mungu anatupeleka mimi na wewe. Tupo hapa
tunaandaliwa. Unasikia Nanaa?” “Sitalia tena Geb. Sasa hivi nitarudisha furaha
kwa ajili yako na wanangu. Sitaki Liv aje kesho anikute nalia au sina raha.” “Kabisa.
Na huyo wa tumboni sitaki ahisi anakuja kwenye mazingira ambayo hayajaandaliwa.”
“Nitabadilika Geb. Nakuahidi kupambana kwa ajili yako na wanangu. Na ninajua
hapa kitandani nitatoka tu.” “Sasa hapo unaanza kuongea. Endelea
kidogo.” Nanaa akampiga ngumi kidogo.
“Kweli tena. Rudia Nanaa. Mpaka hiyo hali isikie.
Akili ielewe. Na moyo upokee muujiza wa maneno yako. Kumbuka mama
alivyokwambia. Uzima na mauti upo kwenye kinywa chako. Jitamkie uzima.”
“Nitapona Geb. Nitamlilia Mungu kwa ajili yako na wanangu. Nataka kulea watoto
wangu mimi mwenyewe.” “Basi tushikane mikono tena tumwambie Mungu. Aturehemu.”
Geb akamwekea mito nyuma ya mgongo. Akapandisha kitanda upande wa kichwani.
Wakaanza kuomba. Waliomba, kila mmoja akimsihi Mungu kivyake. Ndipo Geb
akamwacha alale.
“Na wewe utalala wapi?”
Nanaa akamuuliza kwa kumuhurumia. “Najua usiku wa leo utakuwa mgumu sana kwangu.
Nimeshazoea kulala na wewe.” Nanaa akamuhurumia sana mpenzi wake. “Nishazoea
kukusikia mwilini mwangu, hata nikishituka usiku nakukuta pembeni yangu. Lile
kochi wameniambia linaweza kugeuka kitanda. Lakini pale napaona mbali sana na
wewe.” Nanaa akajifuta machozi. “Nitavuta kiti angalau nilale hapo pembeni
yako. Uniguse tu. Labda nitalala.” “Labda ukilaze
kichwa hapa pembeni yangu.” Nanaa akatoa wazo. “Labda hivyo.” Akavuta
kiti mpaka karibu kabisa ya kitanda cha Nanaa. “Hapa sawa. Ngoja nikasafishe
meno, nije tulale.” Nanaa alibaki akimwangalia kwa kumuhurumia.
Ndoto Ya Kwanza Ya Vita
Ya Nanaa.
Walilala wameshikana mikono. Nanaa akageuka
upande aliokuwa amekaa Geb. Alimchezea nywele mpaka akamsikia anahema kama
aliyepotelea usingizini. Na yeye akafunga macho. Akiwa anapitiwa na usingizi,
akaona amechukuliwa kutoka pale kitandani mpaka juu kabisa ya mlima. Akawa
amesimama peke yake. Hali ya mahali pale akaifurahia sana. Mara akasikia
mshindo na kelele kama ya watu wanaopigana sana chini ya ule mlima aliosimama.
Kwenye bonde. Akataka kushuka ili akaangalie kulikoni, sauti ikamwita na
kumkataza asishuke. Akiwa katika hali ya kutofahamu, kwa kuwa sauti ya vita
ilizidi kupanda kutoka bondeni, sauti ya mapanga makali yakisikika yakisuguana,
ile hali ya utulivu pale juu mlimani ikaanza kupotea. Nanaa akakosa raha
kabisa.
Akatamani kuondoka kabisa sehemu ile kwa hofu,
kwani cheche za moto zilianza kupanda kutoka chini kuashiria ni misuguano
mikali ya yale mapanga. Akageuza uso wake ili akimbie akiwa na hofu kubwa,
akasikia sauti ikimwambia, “Usiogope. Yupo
anayepigana badala yako.” Nanaa akashituka kutoka kwenye yale maono.
Akakaa huku machozi yakimtoka. Akamwangalia Geb, alikuwa amelala kabisa.
Akatamani kujifunua miguu yake ili ajiangalie. Akaogopa. Akabaki amekaa
akitafakari kile alichoona. Asijue kama ni ndoto, au ni maono. Lakini bado
mwili wake ulikuwa ukitetemeka asijue afanyaje na ile ndoto. Akatamani angekuwa
na simu, ampigie mama G, lakini Geb alishazima simu ya Nanaa tokea mchana, ili
asisumbuliwe na mtu yeyote.
Akamwangalia tena Geb. Akatamani amwamshe ili
amsimulie, lakini Geb alikuwa amelala kabisa. Tena alionekana amechoka. Nanaa
akamuhurumia. Akakumbuka siku nzima alikuwa na kazi ya kumliwaza yeye na
kuzungumza na madaktari na kila muuguzi aliyekuwa akimuhudumia yeye. “Anahitaji kupumzika.” Nanaa akawaza.“Mimi ndiye niliyeambiwa nisiogope. Lazima
nitulie. Nitafakari mimi mwenyewe. Niombe?” Nanaa mtoto aliyezoea kwenda
kanisani tokea mtoto, hakuwa akijua cha kufanya. Tokea yupo mdogo, akiwa
nyumbani kwa mama yake mkubwa, ilikuwa ni lazima siku ya jumapili kwenda
kanisani. Lakini hakuwahi kuwa na mahusiano binafsi na Mungu. Hata hakuwa
akijua ikitokea anakutanishwa na Mungu, anatakiwa afanye nini.
Akatamani aombe. Lakini anaombea nini? Ndilo
swali likaanza kumuumiza.
“Au nimuombee yule
niliyeambiwa anapigana vita kwa ajili yangu? Akishindwa?” Hofu ikaanza kumsumbua.
Lakini akakumbuka aliambiwa asiogope. “Inamaana
atashinda?” Akajiuliza. “Kwanza ni
nani anayepigana vita badala yangu?” Akazidi kuwaza. Akili zikaanza kufanya
kazi. Akaanza kutafakari mahusia aliyokuwa akihusiwa na Grace, mama G na Geb.
Akaanza kutafakari kitu kimoja hadi kingine.
Machozi yakaanza kumtoka
taratibu. “Huu
ni wakati wangu wakusimama mimi kama Nanaa. Lazima nipambane kwa ajili yangu,
Geb na watoto wangu.” Akakumbuka mimba aliyonayo. Akajishika tumbo.
Maneno ya Geb kuwa Mungu amemtumia kicheko wakati wa huzuni yake,
yakamrudia.
Kwa mara ya
kwanza, akiwa hajiwezi, Nanaa mbele za Mungu wake apata muda wakushukuru.
Machozi ya faraja yakaanza kumtoka. Moyoni
akajisikia kushukuru. Akajikuta akitamka shukurani zake mbele za Mungu huku
akilia. Alitamani ile hali ya shukurani ingemjia masaa machache kabla hajapata
yale maradhi. Ili aweze kupiga magoti, kumsujudia Mungu wake kwa matendo
makubwa maishani mwake. Akajaribu kusogeza miguu, akagundua bado imekufa ganzi.
Hakutaka kujifunua ajiangalie. Akakumbuka ni muda mfupi tu kabla Geb hajalala,
aliweka taulo safi. Akaona atoe mawazo yake kwenye ile hali, ampe Mungu wake shukurani
juu ya maisha yake.
Akamtizama Geb, mwanaume aliyemzuri wa sura na
akili. Ameacha kitanda cha mamilioni ya pesa nyumbani kwake. Amelala kwenye
kiti pembeni yake. Machozi yalizidi kumtoka Nanaa. Akakumbuka wanawake wengi
aliosimuliwa waliokuwa wakimtaka Geb. Tena wengine waliomba kuzaa naye tu, bila
kutaka matunzo ya huyo mtoto kutoka kwa Geb. Ila mbegu zake tu. Lakini Geb
amemchagua yeye! “Huyo ni wewe tu Mungu. Hakuna
mwingine.” Nanaa aliendelea kulia pale kitandani huku akimtizama Geb,
aliyekuwa hana hata habari.
Picha ya Oliva akicheka ikamjia. Akakumbuka jinsi
alivyokaa tumboni kwake akiwa mgonjwa. Akafanyiwa upasuaji huku anapewa madawa
mengi ya kukausha maji ya mapafuni kwake. Na bado Oliva akazaliwa akiwa mzima.
Hakuwahi kuumwa hata mara moja mpaka pale alipofika na miezi 6. Uelewa mkubwa
alio nao wakati ni mtoto. Kila Geb alipompeleka kliniki, alirudi na habari kuwa
mtoto wao yupo mbele ya hatua anazotakiwa awepo.
Alianza kutambaa akiwa bado mdogo. Alianza
kumtambua mama yake na watu wote aliokuwa akiishi nao mle ndani akiwa bado
mdogo sana. “Hakika huyo ni wewe tu Mungu. Si kazi
ya mikono ya mwanadamu.” Nanaa aliendelea kushukuru. Akajishika tumbo.
Hofu ya ukuaji wa yule mtoto tumboni kwake ikaisha. “Ulinipa
Liv kwa upendo. Hakuna daktari aliyejua, wala mimi kusema kuna kitu tulifanya
ili mwanangu azaliwe vile. Lakini Mungu, umethibitisha mkono wako juu ya Oliva.
Natubu kwa hofu iliyoniingia. Ulishanionyesha kuwa unaweza kunitetea hata kabla
sijakuomba. Umeshanionyesha wewe ndiye unapigana vita kwa ajili yangu. Hakika
wewe ni Baba yangu. Naomba nisamehe kwa kukutilia mashaka.” Nanaa
akatubu sana. Akamsihi Mungu amsamehe.
Hali ya shukurani juu ya kile kiumbe kilichopo
ndani yake ikamjia. Akajikuta akicheka huku machozi yakimtoka. “Bado unanionyesha unaniamini. Na nina uwezo wa kubeba
uhai wa kiumbe kingine. Kwa nini mimi!? Kama sio upendeleo wako kwangu?
Nakushukuru Mungu wangu.” Nanaa
akamshukuru sana Mungu.
Akakumbuka maono
aliyoyaona muda mfupi uliopita. Akiwa juu sana. Ile hali ya utulivu na amani
aliyojisikia akiwa pale juu mlimani. Akakumbuka alikuwa amesimama!
Akacheka. Wazo likamjia na kumkumbusha, vita inayopiganwa kwa ajili yake,
ilikuwa mbali kabisa na yeye. Chini sana. Akakumbuka akiambiwa asiogope. Yupo
anayepigana kwa ajili yake. “Vita si yangu. Nasubiri ushindi wangu. Mungu wangu
hujawahi kushindwa. Nasubiria vita yangu iishe, nishuhudie ushindi wangu kwa
macho haya ya nyama.” Nanaa akawaza huku akicheka. Akatamani arudishwe
tena kule kwenye ile vita ili ajue inaendeleaje. Lakini akajikuta macho
yanakuwa mazito, akalala.
Asubuhi Ya Jumatatu
Nanaa Alipokuwa Hospitalini.
Alihisi mtu akimnyanyua miguu yake. Akashituka.
“Geb!” “Pole, nimekushitua. Nakubadilisha. Umelowa.” Akatulia. Akakumbuka miguu
yake ndiyo inavuja maji. Akatulia kidogo. Hofu ikataka kumsumbua. Akakumbuka
usiku uliopita. Mwanga wa jua ulikuwa umeshaingia ndani, kuashiria
kumepambazuka. “Hata hivyo unatakiwa kuamka Nanaa. Umelala sana.” Nanaa
akacheka. Geb akamwangalia asiamini. Ile furaha ya Nanaa ilitoka ndani, si
usoni. Geb akamfunika vizuri. Akavuta kiti akakaa pembeni yake.
“Naona uso
mwangavu! Inaelekea ulilala vizuri.” “Namshukuru Mungu, nimelala vizuri
sanaaaa.” Geb akacheka. “Kweli naona ni sanaaaaa. Danny amepitisha
vyakula hapa, tumezungumza kidogo, naona hata hujashituka!” “Sikuwa hata na
habari!” “Ndio vizuri.” “Naomba ni busu hapa.” Nanaa akionyeshea shavuni. “Kwa
nini shavuni?” “Si ndio nimeamka tu! Kinywa kitakuwa kinanuka.” Geb akasimama.
Akambusu mdomoni.
“Asante sana Geb. Namshukuru Mungu kwa ajili
yako. Hata kama sababu zote hapa duniani zikiisha zakumshukuru Mungu, lakini
wewe, Oliva na huyu mtoto, mtabaki kuwa sababu pekee maishani mwangu, ya
kumtukuza Mungu wangu. Nyinyi ni muujiza wa kwanza kwenye maisha yangu. Na
ninajua Mungu ataniletea miujiza mikubwa zaidi maishani mwangu.” Geb aliona
kitu cha tofauti kwa Nanaa. Akabaki akimsikiliza.
“Nakupenda Geb. Na kitendo cha kuwa na mimi hapa,
wakati huu ukinihudumia bila kuchoka, hakika nitakienzi milele. Na Mungu
atakubariki.” Ilimgusa sana Geb.
“Kuna kitu cha tofauti kwako Nanaa! Nini
kimetokea huko usingizini?” Geb aliuliza na tabasamu. “Usiku wakati umelala,
nimepata muda mzuri sana na Mungu wangu. Lakini ni baada ya yale Mungu
aliyonionyesha.” Akamsimulia Geb kila kitu. “Sala zetu zimefika mbele za Mungu,
Nanaa. Mungu amekutumia mtu wa kupigana vita yako.” Geb na yeye akajawa na
furaha sana. “Hakika ipo nguvu ya maombi Geb. Natamani tungeanza zamani!”
“Nafikiri hatujachelewa. Kila jambo lina wakati wake. Naamini huu ndio wakati
uliokubalika na bwana. Kuna jambo mama alinifundisha juu ya ndoto.” Geb
akajiweka sawa.
“Aliniambia kila unapoota
ndoto. Kama ni nzuri, unajiunganisha nayo. Na kumuomba Mungu akulinde mpaka
ushuhudie kwa macho, yale uliyoyaota. Kama ni mbaya, unaikataa na kumuomba
Mungu aifute kwenye maisha yako. Basi tuombe kwa kifupi, kisha nikusafishe kinywa,
upate kifungua kinywa. Mama amekupikia vitu kama mzazi!” Nanaa akacheka.
“Amepiga simu na
kusisitiza unywe. Maziwa yakitoka, tukamue halafu tuyamwage. Anasema tusiache
yakauke. Ili Oliva aendelee kunyonya ukitoka hapa.” Nanaa akatulia kidogo.
“Umeambiwa usiogope Nanaa. Na yupo mtu anapigana kwa ajili yako. Amini
hapa hatutakuwepo kwa muda mrefu. Utatoka, na Oliva ataendelea kunyonya kama
ulivyopanga.” “Na mtoto huyu wa tumboni?” “Atamkuta dada yake akinyonya.”
Wakacheka. “Haya tuombe.” Geb akapiga magoti palepale pembeni ya kitanda,
akamshika mkono Nanaa, wakaanza kuomba pamoja.
~~~~~~~~~~~~
Nanaa na Geb walishinda vizuri. Madaktari
walipita kumungalia Nanaa. Bado hawakujua jinsi ya kumsaidia kwa kuwa vipimo
vilizidi kuonyesha hana tatizo. Na Nanaa mwenyewe alikataa kunywa dawa yeyote
kwani alisema hana maumivu popote. Ikabakia kipimo kimoja ambacho ni cha yale
maji yaliyotolewa na kwenda kufanyiwa uchunguzi.
Walikuwa wakiongea mambo yao huku wakicheka.
Walipata muda wakusoma neno kwa pamoja. Geb akawa anaendelea kufanya kazi zake
kwenye kompyuta yake huku akiongea na watu wa ofisini kwake. Alipiga simu huku
na kule. Nanaa akamsikia akizungumza na Grace pia. Akajua mambo yanakwenda
vizuri. Akabaki ametulia pale kitandani.
Mama G akaingia na Oliva akiwa amelala. Nanaa
akacheka alipomuona. “Umemsuka vizuri! Kimependeza ki binti Magesa!” “Nimeona
tunasumbuana kuchana. Nikaamua kumsuka hayo mabutu sita. Grace alimnunulia
hivyo vibanio muda mrefu tu. Leo ndio tumemfunga.” “Hakulia?” “Anavyopenda
urembo huyo! Alikuwa ametulia tuli. Alivyokuwa akitaka kujishika kichwani, Grace
alikuwa akimwambia subiri kwanza mpaka amalize. Basi akawa anacheka kama
anayeelewa vile! Mpaka tukamaliza. Grace akamuweka hivyo vibanio bila shida.
Akawa anamwambia asivitoe. Naona hajatoa.” Nanaa akacheka.
“Amependeza kweli! Asante mama. Naona na hereni
mpya!” “Sasa hujamuona shingoni na mkononi. Utamtaka bure. Usicheze na kina
Oliva Magesa. Tupo wawili tu mjini.”
Mama G akaanza kujisifia. Nanaa akacheka sana.
“Mwenyewe huyo!” “Kumbe! Ushakutana na Oliva
Magesa mwingine?” “Hata mara moja. Ni nyinyi tu wawili.” Nanaa akajibu. “Ndio
maana yake, na wala hatakaa akatokea mwingine.” Nanaa akazidi kucheka huku Geb
akimsikiliza mama yake anavyojisifia. Akasogea kumchungulia mwanae aliyekuwa
akisifiwa. Bado alikuwa amelala pale kwenye kigari chake. Akavuta kidogo ile
cheni shingoni kwa mwanae ili aione, akabaki akiangalia. “Nzuri sana mama.
Asante.” Geb akashukuru. “Karibu.” Mama G akajibu.
Kisha akamgeukia Nanaa. “Haya vipi Nanaa. Naona
uso wa furaha. Mambo yameendaje?” “Mwenzio nimeona maono mama. Nusu nikupigie
simu usiku.” “Sasa kwa nini hukupiga!?” “Geb alichukua simu yangu. Amezima.
Amesema nitulize mawazo.” “Haya. Anza.” Nanaa akaanza kucheka. “Unanicheka?”
“Mama na wewe unapenda stori kuliko mimi!” “Sikufikii Nanaa. Wewe unaweza
kuweka mtoto chini ili usikilize umbea.” Wakacheka.
Nanaa alimsimulia mama G kila kitu. Akamuona
machozi yanamtoka huyo mama. “Mungu wetu anaishi
Nanaa. Hasinzii wala hachoki kama sisi. Mungu wetu yupo vitani. Amekuahidia
ushindi.” “Kabisa mama. Yaani sina hofu hata.” Wakacheka kidogo, mama G
akajifuta machozi. “Nakuona. Na hiyo ndio silaha kubwa sana ya kumshinda
shetani. Kutokuwa na hofu. Na ndio uponyaji wako ulipo.” Mama G akakaa na Nanaa
na kuzungumza naye sana huku akimtia moyo yeye na Geb.
~~~~~~~~~~~~
Baada ya masaa mawili
Oliva akafungua macho. Akakuta baba yake akimwangalia. Akacheka akiwa anatoka
usingizini kama ambaye hakutegemea kukutana na sura ile. “Umependeza Liv!
Umependeza sana binti yangu. Hakika wewe ni mrembo.” Geb akamsifia. Liv akazidi
kucheka huku akionekana na usingizi. Bado Geb alikuwa akimtizama na tabasamu
usoni.
“Mlimpiga picha?” Geb
akauliza. “Si unajua Grace anavyopenda kumpiga picha? Kampiga picha nyingi
kweli.” “Njoo mama yangu mzazi. Nina hamu na wewe!” Geb akamtoa kwenye kiti
chake. Akamuweka kifuani kwake, akamkumbatia kwa muda huku akisikilizia ile
furaha. Liv alishazoea kufanyiwa hivyo na baba yake. Wakati wote Geb alimuweka
kifuani kwake na kumkumbatia kwa muda huku akigugumia. “Mmmmmmmmmh!” Kisha anambusu mara kadhaa. Liv hucheka sana huku
akimwangalia baba yake. Ndipo mengine yanaendelea.
“Sasa mimi niwaache.
Nitarudi baadaye kuja kumchukua huyo dada. Nikamalizane na mama James. Na huyo
Zinda anayejidai ni mumeo.” “Pole kwa
usumbufu mama.” “Wala usijali. Yataisha tu Nanaa. Na wewe utapumzika kwako. Siku
moja utasahau yote haya.” “Naamini hivyo mama yangu. Nakuombea hekima ya Mungu
ili ukafanikishe kila kitu huko kwenye hicho kikao.” “Na kweli nahitaji hekima
ya Mungu. Na nimefunga kwa makusudi kwa ajili hiyo. Maana wamenikera kweli!
Naweza nikaenda kuwachachafya, wasikae wakanisahau maisha. Heri Mungu
akaingilie kati.” Nanaa akacheka. “Nakuaminia mama yangu.” Mama G akacheka. Geb
akabaki akimwangalia mama yake.
“Leo nikirudi hapa, nataka niwe nimefika mwisho
na Zinda. Kama na mahusiano yanakufa, acha yafe. Amefika mbali sana. Sitaruhusu
aharibu maisha yenu.” “Utafanyaje mama?” “Tutampa muda wa kutoa vithibitisho
vyake. Na kujieleza. Tutakapofikia mwisho wa ushahidi wake, ndipo
nitakapomuomba nizungumze naye. Hakika hatakaa akanisahau. Yeye si anajidai
mlevi? Sasa leo atapambana na mimi. Hana adabu kabisa.” Nanaa aliendelea
kucheka.
“Wewe cheka tu. Mumeo anakuita.” “Akuuu!
Mimi mume wangu Geb. Hata wakisema nimempendea pesa, sawa tu.
Lakini mwambie mimi mke wa Geb. Akubali, akatae. Atajijua mwenyewe!” “Mimi
naona twende wote.” “Sitaki mama.” “Si ndio ukamkatae mbele za watu!” “Mimi
nakuaminia mama yangu. Wewe nenda ukaniwakilishe.” Mama G akacheka na kutoka.
Kikao Cha Kesi Ya
Kipingamizi Cha Harusi Ya Nanaa&Geb.
Mama James!
Mama G alifika hapo
kanisani akiwa nje ya ofisi ya mchungaji akasikia sauti ya mama James akiongea
ofisini kwa mchungaji. Alilalamikia hili na lile juu ya Nanaa. Jinsi alivyo
binti mbaya. Muhuni. Hana shukurani na mambo mengi ya kumchafua. Wakati anataka
kuingia ndani, akaona gari ya James na Danny na zenyewe zimeongozana. Wakaingia
ndani ya uzio wa kanisa. Wakaegesha magari yao pembeni ya gari ya mama G.
Wakashuka wote wakamsogelea mama G.
James akamsikia mama yake ndani akiongea vibaya
sana. Akaingia kwa haraka bila hata kumsalimia mama G. “Naomba unyamaze mama.
Tafadhali sana. Nyamaza.” “Nataka pesa yangu.” Mama G akaingia. Akamkuta
mchungaji na wazee wa kanisa mle ndani. Wote walikuwa kimya wakimsikiliza huyo
mama. James alijisikia vibaya sana. “Jamani naombeni mumsamehe mama yangu.
Sijui amepatwa na nini!” “Shika adabu yako James.” Mama yake alimkatisha.
“Jamani, naomba tusiendelee kumpotezea muda mama
James. Aongee kiasi cha pesa anachotaka alipwe. Tumalizane leo.” Mama G
akawakatisha wote. “Eti mama James? Umekataa kuwa hukupokea kiasi cha milioni
30 kama malipo yako ya kumlea Nanaa?” “Mimi nilitaka milioni 100. Ndio mkaomba
niwapunguzie. Nikawafanyia milioni 50. Nashangaa mnanizungusha! Mnataka Nanaa
aolewe bila kunilipa! Mnafaidi matunda ambayo hamkupa…” “Kwa hiyo ulipokea
milioni 30 au hujapokea?” Mama G akamkatisha kwa kumuuliza tena swali. “Iko wapi
sasa hiyo nyingine?” Mama James hakutaka kukiri.
“Mama, wanataka kujua kwanza juu ya ile pesa
waliyokuletea Moshi. Wanataka ukiri wako kama ulipokea au la. Maana jana
ulimwambia mchungaji hukupokea.” James naye akaingilia. Yule mama akaanza
kuwaka kama mkaa. “Huo ndio umbea. Mchungaji anatakiwa awe na kifua cha kubeba
mambo siyo..” “Nisikilize mama James. Hakuna mwenye muda wakupoteza hapa.
Nataka kujua kama ulipokea hiyo pesa au la. Basi. Hatutaki fujo hata kidogo.
Wote tunakuheshimu. Na binafsi ninakushukuru kwa kumlea Nanaa.” Kidogo akatulia.
“Maana mnaweza kusema natanguliza pesa mbele. Sio
utu.” “Hapana. Wewe tuambie kama pesa ya kwanza ulipokea?” “Ndiyo. Bado milioni
20. Ni jasho langu. Nilihangaika sana kumlea huyo mtot..” “Basi. Pesa yako
iliyobaki hii hapa.” Mama G akatoa ile hundi. Akaiandika vizuri. Akamuonyesha.
Akataka kuipokea. “Kabla hujaipokea hii pesa. Nataka upokee kalamu na karatasi
kutoka kwa mchungaji. Andika majina yako yote. Na ueleze kuwa tarehe ya leo
umepokea kiasi cha milioni 50. Kwa malipo ya kumlea Nanaa. Humdai tena Nanaa.”
Mchungaji akampa kalamu na karatasi. Akapokea kwa haraka sana bila hata shida.
Akaanza kuandika. James alibaki akimwangalia mama yake, asiamini
anachokifanya.
Akamaliza. “Naomba pesa yangu.” Akanyoosha mkono.
Mama G akapokea kwanza ile karatasi. Akasoma. Akaridhika nayo. Akamwangalia.
“Sasa nakupa onyo, mama James. Nanaa ameokoka. Na analindwa na Mungu. Usithubutu
kumsogelea kwa aina yeyote ile. Iwe kichawi au..” “Mimi nilipo hapa, hata
mganga simjui! Mdomo wangu ndio mganga wangu na Yesu wangu.” Mama
James alijibu kwa kujiamini. Kila mtu akatingisha kichwa kwa kumsikitikia.
Lakini mama G akawa amepata jibu kuwa Mama James hausiki kwenye gonjwa
la Nanaa.
“Hundi yako hii hapa. James atakupa tarehe ya
harusi ya Nanaa. Tungependa kukuona.” “Ili mniringishie?” Mama James akauliza
kishari huku akisimama. “Sina shida. Nimekabidhi mzigo. Simtaki huyo mtoto.
Kwanza anamkosi. Simtaki karibu yangu wala wanangu.” Kisha akatoka.
Ukimywa
wa muda ukatanda. “Naombeni mtusamehe mimi na mama yangu. Samahanini sana.”
“James, wala usiwe na wasiwasi. Hilo limeshapita. Kuwa na amani kabisa
mwanangu. Mimi bado nakuhesabu kama mtu muhimu sana kwenye maisha yetu. Na ujue
Nanaa anakuhitaji sana, zaidi sasa hivi. Usikubali hili jambo likakuondolea
ujasiri wa kuwa karibu na Nanaa. Umemsikia akikutaja wewe kama baba yake.”
“Daaah! Lakini najisikia vibaya sana mama! Sipati usingizi. Natamani kama
ningesaidia kidogo tu. Lakini uwezo sina mama yangu.” “Nanaa sio jukumu lako
tena James. Mlishapokea mahari. Kimila Nanaa ni mke wa Geb. Huwezi kuendelea
kutunza mke wa mtu. Geb hawezi kukubali hata kama ungekuwa na uwezo.
Halafu ujue kabisa, nafasi ya Nanaa kwenye maisha yetu ni kubwa
kuliko unavyofikiri.” Mama G akakaa.
James akamwangalia mama
G, kama asiyeelewa. “Geb ndiye mtoto wa kiume wa pekee kwa mzee Magesa. Yeye
ndiye anayebeba jina la baba yake. Kwa Nanaa kuendelea kumzalia watoto
vile, kwa Geb ni fahari kubwa sana. Kama hufahamu hilo, nataka leo
uelewe. Kwake Nanaa ni mtu wa thamani sana. Anaendeleza ukoo wa Magesa
kitu kilicho muhimu sana kwa Geb na kwetu pia. Hakuna pesa atakayoiona
ni kubwa kwa Nanaa. Na ujue Geb anafanya kama vile baba yake anamwangalia.
Yupo makini sana na kila hatua anayochukua. Kwa hiyo ujue anafanya kila kitu
kwa ajili ya heshima ya baba yake.”
“Hawezi akaruhusu
mtu aingilie hilo, hata iweje. Hata ungekuwa wewe ni milionea wa vipi,
Geb asingekubali umlipie Nanaa pesa. Anaona kuruhusu hilo ni kumwaibisha
baba yake, au kumwambia baba yake wosia wote na mambo yote aliyomfundisha ameshindwa
kwa kiasi cha juu sana.” Mama G akaendelea.
“Magesa alimpata Geb
kipindi cha uzee wake. Alijua atakufa na Geb akiwa ndio mtoto wake wa pekee wa
kiume. Alikuwa akimfundisha Geb kwa maneno na vitendo. Mchana na usiku. Hata
alipokuwa amelazwa hospitalini, Magesa alikuwa akizungumza na Geb kana
kwamba anaongea na mtu mzima. Walikuwa wakiachana jioni, anamwambia akirudi
kesho yake, arudi na maswali yote ambayo anafikiri atahitaji kumuuliza miaka
labda 10 au hata 20 ijayo. Yoyote yale. Uchumi, mahusiano, kila swali alimtaka
Geb aulize. Na kweli Geb alikuwa akimpa maswali mazito mpaka wakati
mwingine nilikuwa nikimtoa Grace nje ili kuwapa nafasi yakuzungumza. Naweza
kusema Magesa alizungumza na Geb kuliko mtu yeyote yule, au hata zaidi
yangu. Mpaka kifo chake, Geb alikuwa pembeni ya baba yake akimsikiliza.
Nahisi ndio maana akili ya Geb ilikomaa mapema sana, sababu ya baba yake.” Wote
walikuwa wakimsikiliza mama G.
“Kwa hiyo naomba uwe na
amani kabisa. Hata Danny alitaka kumsaidia, lakini amekataa kabisa. Mimi
mwenyewe amekataa nisimsaidie hata nusu ya mahari yake kwa Nanaa. Pesa za
mablangeti na vitenge nilivyokuwa nimenunua kwa pesa yangu, amenirudishia yote
kama ilivyo. Aliniambia ni baba yake ndio alitakiwa kumlipia mahari. Kwa kuwa
baba yake alimpa yeye jukumu la ukoo, basi yeye mwenyewe atalipa mahari ya
Nanaa.”
“Kwa hiyo uwe na amani
tu. Wala usijisikie mnyonge. Hakuna utakachofanya tena kwa Nanaa, Geb
akakuruhusu. Ameshajihesabu jukumu la Nanaa ni lake kama vile alivyo
Oliva. Jana aliniambia anasubiri mambo yatulie, akambadilishe Nanaa
jina, aitwe Nanaa Magesa. Ndio ujue mawazo ya mwenzio yalivyo.” Kidogo watu
wakacheka, na James akatulia. Maongezi mengine yakaendelea wakati wanamsubiri
Zinda.
Hakuna
Msiba Usiokuwa na Mwenzie.
“Zinda.”
Wakati wakizungumza wakasikia mlango unagongwa,
Zinda akaingia akiwa na sura ya hasira. “Huu ndio uthibitisho kuwa Nanaa ni mke
wangu halali.” Zinda akatupa cheti cha ndoa mezani, bila salamu wala tabasamu.
Kila mtu akashangaa. Hawakutegemea. “Sasa semeni jingine.” Akaongeza. Mchungaji
akaokota kile cheti, akaanza kukisoma. Kilikuwa cheti cha ndoa halali. Na
kilionyesha walifunga ndoa mahakamani.
“Ni kweli hiki cheti kinaonyesha Zinda ni mume
halali wa Nanaa.” Mchungaji aliongea huku akiendelea kukikagua kile cheti.
“Naomba kukiona na mimi.” James akasimama na kwenda kukifuata. Moja kwa moja
akakimbilia kwenye tarehe. Akasoma kwa makini. Wakaona anacheka. “Kweli
unatumia urafiki wetu vizuri sana Zinda.” James aliongea huku akimkabidhi Danny
kile cheti.
“Tokea siku uliponisaliti wewe na Danny, mkijua
jinsi nilivyohangaika na Nanaa. Lakini kwa kuwa mimi sina pesa kama Geb,
mkaamua mumtoe Nanaa kwangu na kumpa Geb mwanamke wangu, mmetangaza VITA
na mimi, James. Mimi sio rafiki yenu. Na ninawahakikishia, tutapambana
kufa na kupona hapa mjini. Nitafika popote itakaponilazimu, lakini nawaambia
Geb hatamuoa Nanaa.” Zinda alibadilika. Hakuwa Zinda wanae mfahamu.
Danny na James walibaki wakimtizama. Danny
akarudisha macho kwenye kile cheti. Akatingisha kichwa. “Jamani mimi nina swali
kwa Zinda. Sijui naruhusiwa kuuliza?” Danny akaongea. “Karibu.” Mchungaji
akamruhusu. “Unamkaribisha Danny kuuliza swali hapa kama nani?” Zinda
akaingilia. “Basi hakuna shida. Ila naomba mchungaji zingatia mambo yafuatayo
kutokana na hichi cheti cha ndoa, na ninaomba muulize wewe Zinda haya maswali.
Kutokana na tarehe hii iliyopo kwenye hichi cheti cha ndoa, inaonyesha tarehe hii 23/10/20XX, nchini Kenya, ndipo
Nanaa na Zinda walipofunga ndoa yao. Kitu ambacho nakuhakikishia sio kweli.
Nanaa alikuwa yupo chuo kikuu cha Mlimani. Anamalizia shahada yake ya mwisho!
Tena akiwa mjamzito wa mtoto wa Geb. Nanaa asingeweza kusafiri akiwa mjamzito wa
mtoto wa mwanaume anayempenda, Geb, na kwenda kufunga ndoa na Zinda. Hiyo ni
moja. Kutoka tu kwenye hiki cheti.” Danny akaendelea.
“Pili. Nanaa kama msomi wa chuo kikuu, kwa nini
hapa aweke saini ya dole gumba, badala ya saini yake halali? Achana na swali
atakalokuja kuuliza James, yeye ambaye Nanaa anamtambua kama baba yake,
atauliza mahari hiyo kama mila ya kitanzania, alimpa nani mpaka akapata ruhusa
ya kumuoa Nanaa? Naomba umuulize hilo swali Zinda.” Danny akamaliza na kumpa
kile cheti cha ndoa mama G.
Mama G akaanza kukiangalia. Kilionyesha ni cha
kutokea nchini Kenya. Mama G akaanza kutingisha kichwa. Zinda alikuwa ametulia
kana kwamba hakumsikia kabisa Danny. Mchungaji akayaweka yale maswali sawa,
akamuuliza Zinda. “Naomba kama utaweza kukaa, ukae Zinda ili tuzungumze
vizuri.” Mchungaji alizungumza kiustarabu. “Mimi nipo sawa tu. Naweza kuongea
wakati nimesimama.” Zinda akajibu kwa jeuri.
“Kujibu swali lako la
kwanza mchungaji ni hivi, baada ya Nanaa kuniambia hatutaweza kuwa na mahusiano
wakati ule, nikatulia. Siku moja ya harusi ya aliyekuwa rafiki yetu, Malii.
Nanaa akiwa ameachwa nje, usiku kwenye baridi, na hawa watu wote hao
wanajidai sasa hivi ni ndugu zake Nanaa, pamoja na Geb anayedai Nanaa ni
mkewe, mimi nilimkuta Nanaa nje peke
yake. Nilitoka ukumbini, nikiwa naelekea msalani. Watajwa wote hapo juu
walikuwa wakila na kucheza ndani wakati Nanaa wamemsahau nje ya ukumbi.
Nilimkuta akiwa anateseka nje na baridi. Nikamvalisha koti langu. Nikamwambia
anisubiri wakati naelekea msalani ili nikitoka nimuingize ndani. Lakini
sikumkuta. Nikauliza, nikaambiwa alishaondoka. Kumbe alizidiwa akaokwatwa na
watu wakampeleka hospitalini. Hao wote hapo, mpaka huyo anayejiita baba yake
Nanaa, walikuwa wakisherehekea ndani wakati wamemsahau nje ya ukumbi, Nanaa
wanayejidai kumgombania leo.” Zinda aliongea vizuri bila hofu.
“Kufupisha habari ndefu, Nanaa ambaye ni mke
wangu, akiwa hospitalini, alihudumiwa na huyo
mwanamke aliyemuoka siku hiyo walipomsahau nje mpaka akapona na kuhamia
nyumbani kwa huyo mama kuishi naye. Awali alikuwa akiishi nyumbani kwa
hawa matajiri unao waona wamekaa hapo,
nyumbani kwa Geb. Lakini Nanaa akaamua kuhama kwao na kwenda kuishi kwa huyo
mama sababu ya ubaya wa hawa watu waliomtendea. Akakata mawasiliano na
hao wote walio kaa hapo, mpaka na Geb aliyekuja kumfumania baadaye.”
Danny na James hawakuwa wakiamini.
“Nanaa akiwa ameumia sana, akanitafuta ili
anirudishie koti langu nililokuwa nimempa siku ya harusi akiwa ameachwa
nje. Nafikiri mnakumbuka. Aliniomba tukutane kwa chakula cha mchana.
Tukakutana. Tulipata muda mzuri sana. Akanieleza masikitiko yake ya usaliti
aliofanyiwa na hao watu wote. Kuanzia mama yake Geb aliyekuwa ndiye muhusika
wa kwanza, aliyemuacha nje. James ambaye alidhani ni kama baba
yake. Geb aliyekuwa amemdanganya anampenda, lakini akamfumania na
mpenzi wake aliyekuwa amemdanganya Nanaa waliachana. Kumbe Nanaa alikuja
kugundua ilikuwa ni janja ya kumuweka tu kitandani.”
“Nanaa akaniambia baada ya Geb kufanikiwa kulala
naye, ndipo alipoanza kumfanyia vitimbwi. Hakuwa akimjali kwa dhati.
Ikiwemo kuwepo kwenye kumbi wa harusi na mpenzi wake, badala yake yeye
Nanaa. Nanaa alijua wazi Geb alifanya makusudi kutomwingiza ukumbini.
Waligawa kadi kwa watu wote. Mpaka marafiki wa karibu, kasoro Nanaa, ili
asiingie ukumbini, awe na Liz mpenzi wake. Na mama yake Geb analijua hilo.”
Mama G alibaki akimtizama Zinda asiamini.
“Hata ukitaka ushahidi wa Liz nitaleta. Liz
alikuwa mpenzi wa halali wa Geb. Na alikuwa akienda kulala nyumbani kwa Geb,
mama yake Geb akiwepo! Nanaa pia alikuwa akiishi hapo hapo. Na ndugu zake Geb.
Hata huyo anayetambulishwa kwenu kama baba yake Nanaa, anajua kama Liz alikuwa mchumba
wa Geb, na walikuwa ni kama wakiishi pamoja! Sasa utawauliza kwa wakati wako
mapenzi au mahusiano hayo ya Geb kwa Nanaa yalianza lini? Wakati Geb alikuwa
akilala na mpenzi wake kwenye nyumba hiyohiyo aliyokuwa akiishi Nanaa na wote
hawa kasoro huyu anayejiita kama baba yake Nanaa, japo alikuwa ni kama akiishi
hapo maana kula yake pia alitegemea hapo nyumbani kwa tajiri yao Geb?” Zinda
akawa amemtukana na James kwa makusudi tu, akionyesha wote wapo mjini
kwa nguvu ya Geb, mwanaume mwenzao. Hawakumuingilia, wakamuacha tu
aendelee.
“Turudi kwenye habari yangu mimi na mke wangu.”
Danny alicheka na kutingisha kichwa. “Siku hiyo Nanaa aliponiomba tukutane ili
anirudishie koti langu, tulipata muda mzuri sana kama nilivyotangulia kusema. Penzi
jipya likazaliwa. Yakaanza mahusiano kati yetu, lakini alinisihi
nisimwambie hata James, kwa kuwa hawakuwa kwenye mawasiliano yeyote
yale. Na akasema hamtaki tena James kwenye maisha yake. Nikakubali, sisi
tukaendelea.”
“Nanaa alipojigundua ana
ujauzito wa Geb, aliogopa sana. Akataka kuitoa ile mimba. Nikamwambia asiue
kiumbe kisicho na hatia kwa kosa la baba yake. Nikamwahidi kuwa nitakuwa
tayari kumtunza yeye na mtoto. Na kumuhakikishia hivyo, nikamwambia nipo tayari
kufunga naye ndoa.” Zinda akaendelea.
“Swala likawa jinsi ya
kulipa mahari. Nanaa akakataa kata kata nisimshirikishe kaka yake huyu, ambaye
mmetambulishwa kwenu kama baba yake. Akanipeleka kwa mama yake mkubwa
Moshi. Ndipo nilipolipa mahari.” “Haiwezekani Zinda! Unadanganya
kabisa.” James akamkatisha. Zinda akatoa simu yake. Akapiga namba fulani,
ikapokelewa. “Naomba uingie ndani mama.” Akakata
simu.
Hata dakika moja haikuisha mama James akaingia. “Haiwezekani
mama!” James akashituka sana. “Juu ya
nini!?” Mama James akauliza bila hofu. “Mama aliyemlea Nanaa tokea anazaliwa
huyu hapa. Muulize kama hajapokea mahari yangu.” Mchungaji alimwangalia yule
mama, akabaki ameduwaa. “Unafanya nini mama yangu!? Ni mchezo gani unataka
kumfanyia Nanaa? Hujatoka kulipwa pesa ya kumlea Nanaa muda mfupi uliopita?”
James akamuuliza akiwa anaonyesha kuumia sana mpaka uso wake ulibadilika.
“Mmenilipa! Kwani nimekataa? Si ndio mnamtumia
sasa hivi huyo Nanaa! Sasa mlitaka mfaidi matunda msiyoyapanda wala kupalilia?
Zinda aliletwa na Nanaa nyumbani. Akamtambulisha kama mumewe mtarajia. Zinda
akalipa mahari yote. Na picha za ulipwaji mahari hizi hapa.” Yule mama
akafungua mkoba. Akatoa picha. Wakaanza kuzisambaza pale ndani kwenye ofisi ya
mchungaji. “Nanaa yuko wapi hapa kwenye hizi picha? Mbona kwenye picha zote
mnaonekana wewe, Viola, Vai na Zinda tu?” James akauliza.
“Kwani
mwanamke muda ule anapolipiwa mahari anakuwepo? Si anakuja baadaye baada ya
taratibu za mahari kukamilika! Ungekuwa umeoa, ungeyajua hayo.” Mama
James alimjibu mwanae bila hofu wala kubabaika. Picha zile zilionyesha vitu
vyote vya mahari kama alivyotoa Geb. Mama James na wanae hao wa kike
walionekana wakivipokea vile vitu hapo pichani.
“Ngoja kwanza mama. Zinda anasema alitoa hii
mahari Moshi. Sio kweli. Wewe na hao wanao wa kike wote mlikuwepo nyumbani
kwangu karibia mwaka jana mzima. Kwa nini mnadanganya?” “Hayo yakuwa
Moshi sifahamu. Ila ninachojua mimi Zinda ndiye mume wa Nanaa kihalali.
Kwa kuwa alinilipa mimi mahari, na kwenda kufunga ndoa na Nanaa, nchini Nairobi
Kenya. Tena Nanaa mwenyewe akisisitiza usiambiwe kabisa.” Akamjibu James
bila kupepesa kope.
“Kama hamna la nyongeza, nataka kuondoka.”
Alimgeukia Zinda. “Nakushukuru sana mama yangu. Asante.” Zinda akampa mkono
mama James. “Labda kabla mama James hajaondoka. Naomba mchungaji muulize kama
anakumbukumbu ya kupokea mahari ya Nanaa hapo majuzi kutoka kwa Geb.” Danny
akawahi. “Na kweli. Maana tulimfuata mpaka Moshi kwenda kulipa mahari ya Nanaa.
Na mimi nilikuwepo kupokea hiyo mahari kutoka kwa Geb. Ni kwa nini alipokea
mahari mbili mbili?” James naye akaongezea swali, kwenye swali la Danny.
“Hivi wewe James unalipwa
na huyo Geb? Umekuwa wazimu wa kunigeuka hata mimi mama yako? Nimesikia
anakujengea na nyumba. Ndio sababu ya kunivunjia heshima mbele za watu!?
Unanihoji kutaka kunidhalilisha mimi! Sasa nakuonya James, shika adabu
yako. Utatembea uchi hapa mjini. Endelea kumtumikia mwanaume mwenzako. Hata
baba yako atasikitika sana.” Aliwaka kwa kijana wake kama sio yeye. Na alikuwa
akifanana na James, hakuna jinsi James angeweza kumkana mama yake pale
mbele ya watu. Alimrisisha rangi ya weupe. Alikuwa mweupe sana kama James.
Urefu na sura ya duara kama mwanae James.
James alibaki akimtizama mama yake asiamini. “Ni
nini mama yangu unafanya!? Huyu Zinda amekulipa kiasi gani, kinachokufanya
ukose utu kiasi hicho!?” “Sina shida na kulipwa. Kwa taarifa yako tu, nina
nyumbani kwangu hapo Ubungo maziwa. Naishi na wanangu. Ninatarajia kufungua
baa, ambayo itakuwa ikipigwa miziki Live kila
siku. Sasa nina shida gani? Kwa nini nipokee pesa kutoka kwa mkwe
anayejiheshimu kama Zinda? Na umwambie Nanaa, tamaa itamponza. Atahama nyumba
moja hadi nyingine sababu ya kupenda pesa. Mkumbushe kiapo alichomwapia mumewe
Zinda.”
“Subiri kwanza mama. Yaani hii pesa uliyolipwa
hapa majuzi na leo na Geb, ndiyo hiyo inakufanya umwache baba peke yako huko
Moshi, uje uanzishe biashara hapa mjini!? Kwa nini usiende kufanyia biashara
kulekule Moshi?” “Kwa hiyo unanipangia na ni jinsi gani pia ya kuishi!? Kweli umelaaniwa
wewe mtoto! Sasa kabla sijakuvulia nguo hapa mbele za watu, naona niondoke.” Akatoka.
Walimuona James ameweka mikono kichwani, machozi
yakimtoka. “Sasa narudi kwako mchungaji. Ukitangaza tena ndoa ya mke wangu.
Ukitaka aolewe kwa mara ya pili. Ujue unatangaza VITA na mimi na vyombo
vya sheria. Sitakubali. Nitakushitaki kwa kupokea hongo kutoka kwa hao
mamilionea. Najua unaweza kuingia tamaa kwa kuwa umeona wameweza kumlipa mama
James bila shida. Nashauri usifanye hivyo. Kanisa hili litafungwa. Nanaa ni mke
wangu kihalali. Awe ameweka saini ya dole gumba au ameandika, hilo ni
juu yangu mimi na Nanaa mwenyewe. Haimuhusu mtu yeyote. Na kuanzia sasa, sitaki
usumbufu.” Zinda akataka kutoka.
“Naomba nikuulize swali la mwisho kabla ya
kuondoka Zinda.” Mchungaji akamuwahi. “Karibu.” Zinda akarudi. “Imekuaje kwa
muda wote huo mkeo alikuwa akiishi na Geb?” “Mpaka leo anaishi na Geb.” Danny
aliongezea kwenye hoja ya mchungaji. Wote wakamgeukia Zinda. “Kumbe sikumaliza
habari nzima? Samahani sana.” Zinda akajiweka sawa.
“Baada ya ndoa yetu. Nikawa nikiishi na Nanaa
nyumba moja huku amechukua chumba hosteli. Tunalea mimba huku anasoma. Mimi
ndiye niliyekuwa nikimpeleka Nanaa chuoni na kumrudisha. Alipokaribia
kujifungua, nikapata safari ya gafla. Ikanibidi nisafiri lakini huku tukijua
nitawahi kurudi kabla Nanaa hajajifungua. Ndipo ikamlazimu Nanaa kuhamia tena
hosteli ili asipate shida ya usafiri.”
“Siku ya pili yake baada
tu ya mimi kuondoka, Nanaa akajifungua. Geb alipojua kama Nanaa amejifungua,
Nanaa akiwa kwenye mtihani, Geb akamuiba mtoto. Ndipo ikabidi Nanaa
amfuate nyumbani kwa Geb. Nanaa alinipigia simu nikiwa safarini na kunisimulia
mkasa mzima. Kuwa Geb amemfungia mtoto. Na kuweka ulinzi mkali sana.
Akampa sharti kuwa, anakaribishwa kumlea mtoto wake hapo ndani, lakini haruhusiwi
kutoka na huyo mtoto.” Zinda alijieleza bila shida.
“Niliporudi safari
tukaonana na Nanaa. Akaniambia ukatili anaofanyiwa mle ndani na Geb. Lakini
akanisihi tukubali tuvumilie tu, mpaka angalau atakapomuachisha mwanae kunyonya
ndipo atarudi nyumbani. Kwa hiyo tukawa tukiwasiliana na Nanaa, na kukutana kila
tunapoweza.”
“Mwezi uliopita, Nanaa
alinitafuta tena akiwa analia. Akasema Geb anamlazimisha kufunga ndoa, lasivyo
anamfukuza mle ndani. Kwa kuwa hata hivyo mtoto ameshakuwa mkubwa, mama yake
anaanza kumuanzishia mjukuu wake chakula cha kawaida. Hana haja ya kunyonya tena.
Kwa hiyo akamwambia Nanaa, kitakachomuweka karibu na mtoto wake ni kama
atakubali amuoe, lasivyo anamfukuza mle ndani. Nikamtuliza Nanaa,
na nikamwahidi kumtetea. Kwa hiyo mchungaji, nakutuma kwa Geb. Mwambie
hatakaa amuoe Nanaa. Mvua inyeshe, jua litoke. Hatamuoa Nanaa. Kama
nitamkosa mimi Nanaa, ajue na yeye atamkosa.” Hapo ndipo wakahisi
pengine Zinda anahusika na ugonjwa wa Nanaa.
“Kwa hiyo wewe ndiye unayemtesa Nanaa sasa
hivi?” Mama G akarusha swali. “Siwezi kumtesa mke wangu! Hata hivyo kwa kuhamia
kuishi kwa Geb, ameshajitengenezea adui mmoja mkubwa ambaye ni mke
halali wa Geb, katika ulimwengu wa kiroho. Geb aliingia maagano
na Mira. Katika ulimwengu wa roho Mira ni mke halali wa Geb. Sasa labda huyo
ndiye anayemtesa Nanaa. Mimi sihusiki na ugonjwa wake.” Bila
kujijua Zinda akajikuta akiropoka.
“Umejuaje kama Nanaa ni
mgonjwa Zinda!?” James akauliza akiwa ameshituka sana. Kimya. “Zinda? Maana
hakuna mtu yeyote anayejua kama Nanaa ni mgonjwa. Wewe umejuaje?” Kidogo Zinda
akababaika. Wote wakamwangalia. “Mchungaji, nimemaliza, naondoka.” “Subiri kwanza
Zinda. Mira ni nani?” Mama G akauliza. “Kamuulize mwanao. Lakini ujue, ndiye mkweo
wa halali. Hata mizimu inamtambua kama ni mkewe. Waliingia maagano.
Sasa kama ni mizimu inamrudi Nanaa, kwa kuvunja agano la watu, shauri
yenu. Sihusiki.” Zinda akatoka akiwa amezua jambo jipya kabisaa.
~~~~~~~~~~~~
“Mira ni nani?” Mama G akamgeukia Danny na
James. “Mimi simfahamu!” Danny akajibu. “Na wewe James?” “Na mimi ndio namsikia
leo. Sijawahi kumsikia hata mara moja.” James akajibu. Pakazuka ukimya. Kila
mtu alikuwa akiwaza lake. Zinda aliongea mambo yote kwa hakika na uthibitisho.
Nani anakana? Ni kweli kuna kipindi Nanaa alikataa kuonana na kaka yake James.
Walipoteza mawasiliano kwa muda mrefu tu. Alikuwa wapi? Zinda aliibua
mambo mengi yanayofanana na ukweli mtupu kama kuwasuta mama G, Danny na James.
Na kweli aliwafunga mdomo.
Waliishiwa maneno kabisa. Vijana hao walikuwa
marafiki wa muda mrefu sana. Tena waliokuwa wameshibana. Hakuna walilokuwa
wakifichana. Analolijua Danny ndilo atakalolijua James, Zinda, Malii, Geb na
kundi lao wote. Waliambiana na kushirikishana kila kitu kwenye maisha yao.
Angalau Geb alikuwa mkimya sana. Lakini kwa kuwa alikuwa karibu na Danny
mzungumzaji, hata yeye habari zake zilifikishwa na Danny kwa kundi hilo. Bila
kujijua, walijikuta hata mambo yao ya ndani sana ya siri, yanajulikana na kila
mtu zaidi Zinda ambaye ndiye alikuwa rafiki mkuu wa Danny. Waliheshimiana kama ndugu
wa damu. Danny hakuwahi kumnyima neno Zinda.
Walijua kwa hakika Zinda anadanganya. Lakini
ilikuwa ni ngumu kumkamata uongo wake kwa kuwa aliongea uongo unao fanana na
kweli tupu. Na kila neno aliloliongea alilipata kutoka kwa Danny au James
mwenyewe. Au alishuhudia yeye mwenyewe.
Walibaki wamekaa pale kwenye viti kila mmoja akijiuliza lake. “Labda ni siku ile nilivyomsimulia Zinda…?”
Kila mmoja alijiuliza kimya kimya.
~~~~~~~~~~~~
“Jamani! Kama mlivyoshuhudia kuwa Zinda ni mume
wa halali wa Nanaa. Hatutaweza kutangaza tena habari ya ndoa ya Nanaa na Geb
labda mpaka mtakapoleta uthibitisho mwingine. Kama hati
ya talaka ya Zinda na Nanaa.” Mama G akacheka. Akasimama. “Nashukuru kwa muda
wenu. Mungu awabariki.” Mama G akatoka. Danny na James wakamfuata.
~~~~~~~~~~~~
Wakajikuta wamesimama
pale nje kimya kila mtu akiwaza lake. “Zinda ametuweza. Ametumia ukarimu
wetu kwake, vizuri sana.” Mama G aliongea huku akiwaza. “Najuta!” Danny alijikuta akiropoka. “Nahisi wewe hujuti kama mimi.
Naumia sana.” James akaongeza.
“Nisikilizeni James na
Danny. Zinda hakuwa adui. Zinda alikuwa ndugu yenu. Ndugu ambaye ni rafiki wa
karibu. Kuna mambo mengine mliongea kwake kwa imani mliyokuwa nayo kwake. Leo
amemruhusu shetani kutumia uaminifu wenu kufanya uovu.”
“Halafu umesikia mama?
Mungu amemuweka wazi mbaya wa Nanaa?” Danny akaongeza. “Lakini huyo Mira
ni nani!?” James akauliza. “Geb ndiye atakayekuwa na jibu. Twendeni
tukamuulize.” Mama G akatoa wazo.
“Lakini naomba isiwe mbele ya Nanaa. Tutazidi kumuumiza.” James naye akatoa
wazi. “Basi tukifika, tumpigie simu Geb atoke nje. Tuongee naye.” Wakakubaliana
na wazo la mama G.
~~~~~~~~~~~~~
Zinda
amewakilisha ushahidi wake. Mume halali wa Nanaa na mama James
kama mzazi husika wa Nanaa, amekubaliana naye. Nanaa
hayupo kwenye nafasi ya kupinga, ndoa imesitishwa.
Mira, ndiye
anayemtesa Nanaa? Ni nani?
Usikose
Muendelezo wa Kusikitisha na Kuumiza.
0 Comments:
Post a Comment