Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Ni Wangu! – Sehemu Ya 38. - Naomi Simulizi

Ni Wangu! – Sehemu Ya 38.

Alipoona hakuna msaada hata Geb amekimbia kitanda, ndipo akamkumbuka mtu pekee ambaye amekuwa akimbeba katika shida na raha. Hajawahi kumkimbia daima. Akachukua simu yake na kumpigia James akiwa analia sana. Mama G akaingia akakuta ile hali, akaganda hajui chakusema wala chakufanya. Akawa kama amepigwa na kibumbuazi. Grace akaingia na yeye. Alipomuona vile, bila yakusema kitu, akaenda bafuni kuchukua mataulo kadhaa, akarudi pale chumbani akanyanyua ile miguu ya Nanaa, akatandika yale mataulo chini yake. Bado ilikuwa ikitoa maji. Ilihitaji moyo kugusa au hata kuitizama hiyo miguu.

Geb naye alikuwa akilia kama mtoto pembeni ya kitanda. Bado mama G alibaki ameduwaa. Grace akamfunika shuka Nanaa kama kumsitiri, maana usiku uliopita Geb alimsaidia kumbadilisha nguo za kulalia. Na nguo hiyo yakulalia ilikuwa ni kama imemuweka nusu uchi. Ilikuwa nyepesi sana.

 Danny naye akaingia. Grace akasimama na kuwatizama kwa zamu. “Kwanza naombeni wote mtoke. Hasa wewe Geb na Danny. Nataka nimsafishe na kumbadilisha nguo. Nikikuita hapa Geb, nataka uwe umetulia kabisa. Nisione chozi hata moja. Ukoje lakini, unakuwa kama Fili!? Haya naomba mtoke. Danny na Geb tokeni.” Wakatoka.

Mama G akabaki amesimama kama sanamu. Hajajigusa wala kuongea. Grace akamgeukia na yeye. “Kweli mama jamani!? Ni nini sasa!?” Grace akamshangaa. “Yaani huu ndio unafikiri ndio muda wa wewe kuchanganyikiwa wakati wote tunakuangalia wewe? Nanaa anakulilia na wewe ndio upo kwenye hali hiyo! Hebu acha bwana!” Mama G ndio akawa kama  aliyeamshwa kutoka usingizini. Akaingia bafuni kwa Geb na Nanaa, akatayarisha maji kwenye beseni akatoka nayo kumfuta Nanaa aliyekuwa akilia pale pale kitandani. 

Wakati ndio wanamalizia kumsafisha na kumbadili nguo, wakamsikia James ameingia. “Yuko wapi?” “Juu chumbani kwao.” Danny akamjibu. Wakamsikia James anapandisha ngazi huku anakimbia. Akagonga na kuingia. “Kaka mimi nakufa!” James akaangalia ile miguu, haraka sana akambeba kumtoa pale kitandani.

“Unampeleka wapi James!? Ndio tumemaliza kumsafisha mwili na kumvalisha. Hata chai bado hajanywa.” James hakujibu, akatoka amembeba dada yake. “James!?” Grace akamuita. “Nampeleka hospitalini.”“Hospitali gani?” “Nitawajulisha.” James akajibu huku akiendelea kushuka ngazi huku amembeba Nanaa aliyekuwa akilia. Baada ya muda mfupi sana wakasikia gari ya James inatoka getini kwa kasi. Ndipo akili zao zikaanza kufanya kazi sasa. Bado Geb alikuwa kwenye nguo zake za kulalia

~~~~~~~~~~~~~

Geb akakimbilia chumbani kuoga na kubadili nguo kwa haraka, akatoka huku anakimbia na yeye. “Unijulishe mtakapokuwa Geb. Nikimlisha Liv, nitakuja.” Geb alimwitikia mama yake huku anatoka bila hata kujua hospitali aliyopelekwa Nanaa. Njiani ndipo akampigia simu James. Iliita zaidi ya mara tatu bila kupokelewa. Hapo ndipo jasho lilipoanza kumtoka Geb. Hakuwa akijua aelekee wapi. Akajaribu tena.

Ikapokelewa. “Uko wapi James?” “Bado nipo njiani.” “Unaenda hospitali gani?” Kimya. James hakujibu ila akamsikia Nanaa akilia sana. “James?” “Nafikiria.” James akajibu. “Kwa nini tusimpeleke..” “Nisikilize Geb. Nimekwambia nafikiria. Nataka nimpeleke sehemu atakayopata huduma kwa haraka. Acha kuniita mara kwa mara, nashindwa kufikiria.” “Namimi nataka unisikilize James. Nanaa ni mke wangu mimi. Sasa hivi yupo chini yangu mimi. Nataka ulitambue hilo na uniheshimu.” Kimya.

“Sasa mimi natangulia Agakhani, nataka umlete mke wangu pale.” Kimya. “Unanisikia James?” “Naona mimi nitakutangulia. Sipo mbali na hapo.” “Basi baada ya muda mfupi sana na mimi nitakuwa hapo.” Geb mwenyewe hakuamini kama safari hii amemmudu James. Ikifika kwenye swala la Nanaa, James anakuwa mkali sana. Pengine ni yale mamilioni ya pesa aliyopokea mama yake siku chache zilizopita ndiyo yamempunguza ujasiri James! Au ameshatambua Geb haepukiki! Nani ajuaye! Lakini kwa mara ya kwanza alimkubalia Geb.

Walifika mapokezi, Nanaa akaanza kufanyiwa huduma ya kwanza. Alipimwa homa na pressure wakati wanasubiri kumuona daktari. Muuguzi waliyemkuta hapo aliwaambia kila kitu kipo sawa kabisa. Hakuwa na homa na pressure yake ilikuwa nzuri tu. James alikaa na Nanaa pale nje wakisubiria kumuona daktari. Bahati nzuri hawakukuta watu wengi sana siku hiyo ya jumapili. Wakajua kwa vyovyote vile watamuona daktari kwa haraka. Wachache waliowakuta pale wakabaki wakiangalia miguu ya Nanaa kwa kujiiba. Aliwekwa kwenye wheelchair. James akamuomba muuguzi ampe shuka amfunike. “Naogopa kaka.” Nanaa aliongea wakati kaka yake akimfunika huku akiendelea kulia. “Pole Nanaa. Lakini naona kuna dalili nzuri. Mpaka sasa kila kitu kipo sawa. Hawajakukuta na tatizo. Mungu atakusaidia. Usiogope.” James alijaribu kumtuliza lakini hata yeye aliingiwa hofu. Haikuwa hali ya kawaida.

Mara Geb akaingia. Akaenda moja kwa moja kwa Nanaa. “Pole.” “Naogopa Geb! Naogopa sana.” Midomo ya Nanaa ilikuwa ikicheza kama yupo kwenye baridi kali sana. Yeye na kaka yake wote walishabadilika rangi wakawa wekundu kama moto. Geb akapiga magoti, akambusu palepale alipokuwa amekaa kwenye wheel chair. Akambusu midomo yake kidogo, kisha akamkumbatia huku akiongea naye sikioni taratibu. “Usiogope. Kila kitu kitakuwa sawa. Sawa?” Nanaa akatingisha kichwa. “Nitakuwa hapa na wewe wakati wote.” “Naogopa kujiangalia.” Nanaa alikuwa akitetemeka sana mpaka meno yalikuwa yakigongana. “Basi usiangalie. Nitakufunika wakati wote ili usione. Huna haja yakuangalia. Mimi nitakusaidia kila kitu. Na nitakuwa hapa na wewe wakati wote. Hautakuwa peke yako.” Geb alizungumza naye huku amemkumbatia. Akatingisha kichwa. 

“Haya, niangalie Nanaa.” Nanaa akamwangalia. Akamfuta machozi. “Naomba uinue imani yako kwa upya. Jua hata hili tutalipita tu. Sawa?” “Pamoja!?” “Mimi na wewe, Nanaa.” Watu wote walikuwa wakiwasikiliza. James alikuwa kimya ameinamisha kichwa. “Nikifa?” “Sio sasa hivi na wala si kwa hili. Bado hatujafanya mambo mengi sana. Mungu hawezi kukuchukua sasa hivi. Kwanza unakumbuka hata bado hatujafunga ndoa?” Nanaa akaanza kulia tena.

“Sasa tunafungaje ndoa nikiwa hivi? Wakinikata miguu? Nikifa?” “Unakumbuka tulimuomba Mungu na mama akatuombea, Mungu atusaidie tufunge ndoa?” Nanaa akatingisha kichwa kukubali huku akilia. “Basi naomba tuwe na imani kuwa atajibu maombi. Uwe na miguu usiwe na miguu, lazima Mungu atatujalia tutafunga ndoa yetu.” Watu wote wakapata ujasiri wa kuwageukia vizuri kuwasikiliza. “Kweli Geb!?”  Nanaa akauliza kama asiyeamini. “Kabisa. Kwa hiyo naomba utulie. Tujue kuwa sasa hivi tupo hapa tunahitaji msaada wa madaktari. Tusubiri tuone watakacho tuambia. Lakini naomba kabisa ujiambie na tukatae kuwa hili sio jaribu la kututenganisha wala la kutushusha chini.” Kidogo Nanaa akaanza kutulia.

“Hili sio jaribu lakunishusha wala kunitenganisha na wewe Geb.” “Mbona kama sijakusikia vizuri, Nanaa? Au huna uhakika?” Geb akamfuta machozi, akambusu tena midomo yake kwa muda kidogo, kisha  akamuachia. Nanaa akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu. “Hili sio jaribu la kunishusha wala la kunitenganisha na Geb.” Geb akatabasamu. “Hapo sawa na usilie tena kama umeamini hilo. Sawa?” Nanaa akatingisha kichwa kukubali. Geb akambusu tena na tena. Akasimama. 

“Niliingiwa na hofu. Nikajua utaniacha. Maana uliruka kitandani, ukanikimbia.” “Nisamehe Nanaa. Nilishtuka sana. Unajua tulilala nikajua tukiamka utakuwa sawa tu. Sasa kuja kukutana na picha hiyo, ndio nikashituka sana. Akili iliponirudia, nikajuta sana. Nikajua nilikuogopesha zaidi.” Nanaa akacheka kidogo.

“Usinicheke bwana. Kwanza niambie kama inauma?” “Hata kidogo. Wala sijihisi kama nina miguu.” “Utakuwa tu sawa. Pole na samahani kwa kukuogopesha.” “Nimefurahi umekuja.” Wakaanza kucheka. Nanaa huyu siye aliyetoka nyumbani. Alianza kuongea na James na Geb akijaribu kujituliza.

Geb alikuwa akiandaa maneno ya kuzungumza naye akiwa njiani huku akimuomba Mungu amtie nguvu. Ni kweli Nanaa alikuwa anatisha sana. Geb alijitahidi kuzungumza naye ili kumtoa mawazo yake kwenye ile miguu. Aliifunika vizuri ili Nanaa asiiangalie tena au hata ikitokea anainama, asiione. Na Nanaa naye hakutaka hata kufanya kosa hata lakugusa magoti. Mikono aliiweka juu tu, na macho yaliangalia pembeni wakati wote. Hakujitizama. Wakati mwingine Geb alikuwa akiishika mikono yake na kuibusu, huku akiisugua mikono hiyo iliyokuwa ikitetemeka sana, mpaka Nanaa akatulia.

 “Pole kaka. Nilikuogopesha.” “Pole wewe. Lakini nimefurahi hofu imeisha. Ikiwa hivyo, itakusaidia kupona haraka.” Nanaa akacheka, akisikika ametulia kwa asilimia kubwa. Dimpozi zikaonekana. Geb akaweka kidole chake, Nanaa akamgeukia akacheka. “Asante Geb.” Nanaa akanong’ona. Geb akampa tabasamu akamshika mkono wake na kuanza kubusu viganja vyake tena. Kwa mapenzi hayo, huwezi kuogopa tena.

~~~~~~~~~~~~~

Zamu yake ya kumuona daktari ikafika. Nesi akamuita jina lake. Geb akamsukuma mpaka kwenye chumba cha daktari huku James akiwafuata nyuma. Hata daktari mwenyewe alishituka alipoona ile miguu. “Ameungua na maji ya moto au mafuta ya moto!?” Akauliza. “Hapana. Imeanza jana akiwa amekaa. Akaniambia miguu yake inakufa ganzi. Alikuwa amempakata mtoto. Nikamchukua yule mtoto nikidhani labda amelemewa na uzito wa mtoto, maana mtoto mwenyewe ni wa miaka sita. Baada ya muda nikataka asimame ndio akaniambia hawezi. Tukaenda kulala, ameamka akawa hivyo.” Geb alijieleza. Nanaa alikuwa akiangalia pembeni huku machozi yakimtoka.

“Hii kitu ni ngeni kabisa! Au amekula kitu ambacho kimemkataa?” Daktari akauliza. “Hajabadilisha chakula.” Geb akajibu. “Basi inabidi afanyiwe vipimo. Itabidi alazwe wakati tunamfanyia uchunguzi.” “Kuna jinsi yeyote yakumpatia chumba chake yeye mwenyewe? Sitaki wawe hata wawili kwenye hicho chumba. Nisingependa  watu wageni au nisiowafahamu mimi wawe wanaingia humo kwenye hicho chumba halafu wamtie hofu.” “Ila garama itaongezeka.” Daktari akamtahadharisha. “Hamna shida. Ilimradi yeye atulie tu.” Geb alijibu bila wasiwasi.

“Nimebanwa na mkojo. Nitafanyaje Geb?” Nanaa alinong’ona huku akilia. “Kwanza naomba usilie Nanaa. Ndio maana tupo hapa hospitalini ili kupata msaada. Hayo yote watatushauri nini chakufanya. Usiwe na wasiwasi kabisa. Sawa?” Nanaa akatingisha kichwa kukubali. “Basi naomba usilie.” “Siwezi. Naona machozi yanatoka tu.” “Basi nitakufuta. Jitahidi kuondoa hofu moyoni.” Nanaa akatingisha kichwa. Daktari na James walikuwa wakisikiliza tu. Geb akamtizama huyo daktari kama kutaka asimshangae Nanaa, na afanye wajibu wake. “Inabidi avalishwe catheter. Itamsaidia kutoa mkojo bila shida ya yeye kuhangaika kwenda chooni. Watamvalisha na diaper.” Daktari akatoa huo ushauri ulimfanya Nanaa kuongeza kulia.

“Hiyo itakusaidia Nanaa.” “Nakuwa kama Liv jamani! Watu wanaanza kunisafisha!” “Sio watu. Ni mimi. Usiwe na wasiwasi. Unakumbuka nilikwambia tutakuwa wote wakati wote? Geb alijaribu kumtuliza kwa kumuuliza swali. Nanaa akatingisha kichwa kukubali. “Sitakubali udhalilike Nanaa. Mimi nipo na manesi watakuwepo. Usiogope.” Kidogo Nanaa akatulia. Lakini alijua wazi maisha yake ndio yameshabadilika. Kutoka kujitegemea, akifika atakapo kwa uhuru wote. Gafla ameanza kuwa tegemezi! Mpaka lini? Ni swali lililoanza kumsumbua kabla hata hajapewa kitanda pale hospitalini.

Nanaa Akiwa Hospitalini.

Alichukuliwa damu kwa ajili ya vipimo vingi sana huku daktari akisisitiza lazima kufanyiwa culture ili kujua kinachoendelea kwa undani. Majibu mengine aliambiwa watapewa siku hiyo hiyo mengine waliambiwa yanaweza kuchukua mpaka majuma mawili. Geb hakuwa na wasiwasi, ilimradi kijulikane kinachomsumbua Nanaa. “Labda hayo majibu mengine nikasubirie nyumbani.” Wasiwasi wa garama ukamwingia. “Nanaa! Ndio tumefika tu sasa hivi, tayari unataka kuondoka mpenzi wangu! Naomba tuwape muda wa kukufanya uchunguzi wa kutosha.”

“Itakuwa pesa nyingi sana Geb! Maadamu majibu ya awali yameshaonyesha hakuna tatizo kubwa. Tukipata na haya ya leo, mimi naona tuondoke tu.” Nanaa akaongeza kabla Geb hajajibu. “Halafu nitakaa hapa peke yangu mpaka lini?  Mwanangu?” Tayari ile hofu ilionekana imerudi tena usoni. “Niangalie Nanaa. Nilikwambia mimi nitakuwepo hapa na wewe muda wote. Yale yote tuliyokuwa tukiyafanya nyumbani, tutayafanya tukiwa hapa. Na kama unavyomuona mama hayuko hapa, kwa kuwa yupo na Liv. Na unamjua Liv anampenda sana bibi yake.” “Naona kuliko hata mimi!” Geb akatabasamu. “Si unaona sasa? Usilie bwana! Hakuna kitakachobadilika.” “Na wewe kazini?” “Naomba usianze kuniwekea vikwazo vingi Nanaa. Nimekwambia tutakuwa wote hapa.”

“Lakini itabidi uwe unaenda kidogo. Sitaki huu ugonjwa ukufilisi.” “Kila kitu kitakwenda vizuri tu. Kwanza ujue Grace atakuwepo ofisini muda wote. Kitu kitakachonihitaji mimi atafanya yeye au tutajua kitu chakufanya muda huo utakapofika. Naomba sasa hivi utulie kabisa. Acha mawazo mengii, tena ya baadaye. Naomba tukabiliane na la sasa hivi kwanza.” Nanaa akatulia.

Alishakuwa amewekewa catheter kwa hiyo mkojo ukawa unatoka tu. Mama G akapiga simu, akataka kuzungumza na Nanaa. “Vipi Liv wangu?” “Anakazi ya kucheka tu mwanao.” Angalau Nanaa akafarijika. “Vipi na wewe?” “Nasubiri majibu ya vipimo mama.” “Lakini nimefurahi umetulia. Nitakuja muda sio mrefu. Namalizia kazi hapa ndani ili nikimuachia watoto Grace, asiteseke peke yake. Danny yupo njiani. Nimemtuma uji wenu.” “Mimi sioni umuhimu wa kunywa huo uji tena mama. Nitarudi kula vyakula vya kawaida bila kula  vitu vya kuongeza maziwa. Sitaki Liv aje aninyonye tena. Sijui nimepatwa na gonjwa gani! Sitaki kumuambukiza mwanangu. Naona mumuanzishie tu maziwa ya kawaida.” Nanaa alianza kulia tena. Mama G akanyamaza.

 Hata yeye aliona ni kweli. Hawakujua ni nini kinamsumbua Nanaa. Kimemuathiri kwa kiasi gani! Hawakujua kama ni gonjwa ambukizi au la. Nanaa aliendelea kulia pale kwenye simu, mama G akiwa kimya. Geb akachukua simu, akazima. “Hata hivyo amenyonya vyakutosha. Miezi sita bila kula kitu ila maziwa yako tu, nafikiri amepata kinga yote. Atakula vyakula vingine. Usiwe na wasiwasi.” “Nilitaka anyonye mpaka hata miaka miwili.” “Haaa! Yote hiyo! Na mimi?” Geb aliropoka mbele ya James. Nanaa akacheka nakujificha uso kwa mto. James akatoka. 

“Heri nimegundua hila zoko, Nanaa.” “Geb wewe!” “Miaka miwili si michache Nanaa. Ngoja nimwambie mama aanze kufikiria kitu cha kumnywesha huyo mjukuu wake. Hapa biashara ndio imekufa.” Nanaa alizidi kucheka. “Sasa utamwambia nini mama?” “Tunatumia huu huu ugonjwa.” “Ujue Geb huna akili wewe!” “Weee, nimevumilia sana. Acha na yeye anipishe.” Nanaa alikuwa akicheka. “Inasaidia kinga na kujenga akili.” “Anaakili zakumtosha yule mtoto. Naona hayo maziwa yako yameshamjenga vyakutosha. Aache utani na mimi kabisa! Kwanza pale alipo anakumbukumbu ya mtoto wa miaka 2, inatosha. Acha aanze kupewa ugali.” Waliendelea kuongea huku wakicheka.

Akaingia James na Danny. “Afadhali kama Nanaa anacheka. Maana nilikuwa nimeingiwa hofu kweli!” Nanaa akamwangalia Geb. “Atakuwa tu sawa.” Geb akajibu. Wakaendelea na stori nyingine. “Sikuwa hata nimejua kikao kiliishaje jana!” Geb aliingiza mazungumzo ya kikao. “Watu wameahidi pesa ya kutosha bwana. Mpaka nikashangaa! Ila watu wana wasiwasi na Nanaa.” Danny akaongeza. “Waambie Nanaa anaendelea vizuri, na harusi ipo palepale kama tulivyopanga.” Danny akamtizama Geb kama haamini. 

“Vipi?” Akamuuliza Danny kama na yeye anamshangaa kwa kusita kwake. “Naona kama tungesubiri tujue hatima ya Nanaa.” Danny akashauri. “Miguu ya Nanaa haitanizuia kumuoa Nanaa, Danny. Siku na tarehe ile ile tuliyopanga kufunga ndoa, ndio hiyo hiyo. Iwe hapa hospitalini au kanisani, namuoa Nanaa. Sitasubiri tena. Ninachotaka kutoka kwenu ni ushirikiano tu. Nitamuomba mama aniombee kwa mchungaji aliyeahidi kutupa mafundisho ya ndoa, aje hapa hospitalini atupe hayo mafundisho mimi na Nanaa. Tena kwa muda uleule ambao kanisa limepanga wa mafundisho, ndio huo huo tutafundishwa. Wapi harusi itafungwa, ndio itategemea na wapi bibi harusi atakuwepo siku hiyo. Basi.” James na Danny wakaangaliana kwa muda wakiwa hawajaelewa. Nanaa hakuwa akiamini.

“Unauhakika Geb?” James akauliza. “Juu ya nini!?” Geb naye akamuuliza. “Kumuoa Nanaa akiwa kwenye hali hiyo?” “Ipi?” Geb akauliza tena. “Mengi yaweza kutokea Geb.” “Lini?” Geb akauliza tena, akiwa ametulia tu. James akanyamaza. “Naomba unielewe James. Sina uwezo wakujua kesho inakuwa nini. Na siwezi kuruhusu hofu ndio itoe tathimini ya maisha yangu. Sipo hivyo na wala sijawahi kuwa hivyo. Mimi ni mtu wa mipango. Napanga kila kitu, halafu namuachia Mungu. Kwa mfano, leo nilipanga kuwa Nanaa. Imetimia. Nipo na Nanaa. Lakini ni wapi, hapo Mungu amepanga yeye kuwa nitakuwa naye hapa. Japo mimi nilijua ningekuwa naye mida hii kanisani. Nikiwa nimembeba mtoto wangu pembeni ya familia yangu. Sehemu, sio kama nilivyotarajia, lakini nipo naye hapa. Na baadhi yenu nyinyi kama familia tupo pamoja. Kwa hiyo kwa sehemu kubwa mipango yangu imekamilika.” Geb alizungumza akiwa anaonekana anajielewa.

“Mipango yangu ni kuwa Nanaa ndiye atakayekuwa mke wangu kihalali. Sitaruka hatua hata moja. Nimekamilisha kwa wazazi. Bado kanisani tu. Mipango yangu siku hiyo ya harusi yetu ni niwe nimesimama naye kanisani. Baada ya hapo twende ukumbini tukafurahie na watu watakaoweza kuhudhuria. Tena isizidi siku 40 tokea jana. Nimepanga hivyo. Na nitasimamia hivyo. Mengine namwachia Mungu. Ninayemtaka ni Nanaa tu. Wapi, na kwa staili gani, nitaona mbele ya safari, siku itakapofika. Naomba mnielewe katika hilo. Sijawahi na sitaki kuyumbishwa na matukio.” “Nimekuelewa Mzee.” Danny akajibu. James akatoka tena pale chumbani. Nanaa akabaki amejifunika akilia.

“Wala usilie Nanaa. Na hili tutavuka tu. Tutavuka kwa staili gani, hatujui. Tumuachie Mungu. Yupo pamoja na sisi. Umesikia?” Nanaa akatingisha kichwa ndani ya shuka. Geb akamfunua. “Naomba usilie hata kidogo. Kulia ni kumtangazia shetani ameshinda. Hajawahi kushinda, na wala hataanzia kwetu kushinda. Nimuongo tu. Sasa hivi ananguruma, kwa vitisho vya macho haya ya nyama. Anakutupia vitu vya kukuogopesha tu. Lakini alishashindwa.” Geb akamfuta machozi huku Danny akiwasikiliza asielewe ule ujasiri Geb aliupata wapi! Nanaa hakuwa akitizamika miguuni. Tayari taulo alilokuwa amewekewa chini yake na shuka la juu vilishalowa. Geb akamwita nesi. Akaja kubadilisha, wakamfunika tena. Nanaa akawa ametulia.

~~~~~~~~~~~~~

Baada ya muda, Mama G akaingia. “Hivi Grace amegoma kubaki. Tumekuja na watoto wote, wapo kwenye gari. Utafikiri amefungua shule ya chekechea hapo kwenye gari.” Danny akacheka. “Ngoja nikampokee.” Daktari akaingi. “Vipi?” “Anaendelea vizuri.” Geb akamjibu yule daktari. “Sasa nimerudi na baadhi ya majibu ya vipimo tulivyovichukua.” “Naomba usubiri kwanza nimwite kaka yake kabla hujatuambia. Ndio kama baba yake Nanaa.” Geb akampigia simu James. “Njoo, daktari yuko hapa, anamajibu ya Nanaa. Nataka na wewe usikie.” Geb akakata simu.

Baada ya muda mfupi sana, James akaingia. Macho yake yalikuwa mekundu sana. Wazi alionekana alikuwa akilia. “Majibu yakoje?” James akamuuliza daktari mara alipoingia. “Vipimo vyote vinaonekana Nanaa hana tatizo lolote. Hata mkojo ni msafi kabisa. Ila tumekuta ni mjamzito.” “Asante Mungu wangu kwa faraja. Hata wakati huu umetukumbuka. Asante Yesu wangu. Asante ku…” Geb aliendelea kumshukuru Mungu akaacha kila mtu kimya.

Zile habari zilimshtua kila mtu pale ndani. Kwa hali ya Nanaa ilivyo, halafu kusikia ni mjamzito tena, hata mama G, akashituka sana. Lakini ikawa tofauti kwa Geb. Zile shukurani alizokuwa akizitoa huku akifurahia, kulianza hata kubadilisha moyo wa Nanaa. “Si umeona Nanaa? Katika hili pia Mungu ametukumbuka. Ametutumia faraja.” Hata yule daktari akabaki kimya.

“Hivi unaona hali yangu Geb? Mimba hiyo naibebaje? Mtoto huyo anakujaje sasa hivi?” Nanaa akauliza huku akilia. “Nanaa! Hivi wewe unafikiri Mungu hakuwa ameiona siku hii ya leo? Hakuna jambo linalotokea sasa hivi eti likamshangaza Mungu! Hata kidogo. Alijua leo tutakuwepo hapa tukiwa kwenye hali hii ya ugonjwa, ndipo akaamua kutukumbusha kuwa yupo na sisi. Ametubariki na mtoto mwingine. Hiyo ni faraja Nanaa. Jiulize kwa nini huyo mtoto aje kwetu wakati huu? Au unafikiri ni bahati mbaya?” “Na maradhi haya Geb!?” Nanaa akauliza.

“Mbona kama unasahau Nanaa wewe!? Unakumbuka mimba ya Liv? Unakumbuka ulivyougua mpaka ukafanyiwa na upasuaji! Madawa uliyokuwa ukinywa! Lakini mwangalie Liv sasa hivi. Anakuwa kwa haraka kuliko watoto wa umri wake! Si kwa nguvu zako wala uweza wa madaktari tumekuwa na Liv. Mungu ametaka kukuhakikishia yeye ni Mungu. Na humpa amtakaye. Hata huyo naomba tumuachie Mungu, na tuchukue kama faraja. Hakuna jinsi Mungu angekupa pole, ukaelewa kama si kukupa huyo mtoto sasa hivi. Jua hiyo ndio pole ya kipekee kutoka kwa Mungu. Na anatujulisha bado mkono wake uko juu yetu.” Geb akaendelea.

“Kama unafikiri huyo mtoto amekuja kwa bahati mbaya, uliza wanaolala mahospitalini na makanisani wakililia kushika mimba. Muulize Sara mke wa Ibrahimu, mama yake Isaka kwenye bibilia atakwambia vile ilivyo shida kushika mimba. Muulize Hana mke wa Elkana kwenye kitabu cha 1 samweli 1. Mama yake Nabii Samweli. Kama ungepata bahati ya kukutana na hao wanawake wawili tu. Waliokuwa wameolewa na wanaume wema, safi mbele za Mungu. Ndipo ungetambua na kuelewa hichi Mungu alichokutendea wewe.” Geb akaendelea. 

“Sio kitu kidogo kilichotokea kwetu Nanaa! Usipuuze hata kidogo. Usikubali hii hali ya leo ikakufanya ushindwe kuona baraka na faraja Mungu aliyotutumia. Tumshukuru Mungu kwa majibu haya ya kwanza kuwa huna tatizo. Damu yako safi. Inamaana hata mtoto yupo salama huko tumboni. Nalo hilo ni la kumshukuru Mungu. Naomba Danny akatuletee vinywaji, tusherehekee mtoto wangu. Leo tunahabari njema tu. Tuna mtoto anayekuja na hawajakuta tatizo. Umenielewa Nanaa?” Nanaa akatingisha kichwa huku akifuta machozi. 

“Ni kweli unaamini Nanaa? Mbona sikusikii ukisema kitu?” Nanaa akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha. “Leo ni habari njema za mtoto wetu na kuwa sijakutwa na tatizo lolote.” Nanaa akarudia. “Mbona kama sikusikii vizuri? Halafu bado unalia? Naomba hizi habari ziingie moyoni, na zipate nafasi kama habari nyingine zozote zile.” Kila mtu alikuwa akisikiliza, nakushindwa kuchangia. Daktari mwenyewe alikuwa kimya. Geb akamfuta machozi na kumbusu kichwani. “Leo ni habari njema za mtoto wetu na kuwa sijakutwa na tatizo.” Nanaa akarudia tena kwa sauti iliyotulia. “Ewaaa!” Geb akainama na kumbusu midomoni. “Naomba utulie na uingize habari njema tu. Kwa ajili yako na mtoto. Basi.” Nanaa akatingisha kichwa kukubali.

Akamgeukia mama yake. “Umemsikia Mungu wetu tunayemuabudu? Amegeuza huzuni yetu kuwa kicheko! Oliva amepata mdogo wake.” Mama G akaendelea kujifuta machozi, asiamini ni nini kimempata Geb. Alihisi ni kuchanganyikiwa kwa hali ya Nanaa. Lakini kila alipokuwa akiongea, alionekana anajua anachokizungumza. Danny na James walikuwa kama wamepigwa na butwaa. “Danny! Naomba chakula kizuri na vinywaji mpaka kwa manesi. Vije humu ndani. Mwambie Grace alete watoto humu ndani. Lipo jambo Mungu ametutendea mimi na Nanaa. Lazima tumtukuze yeye Mungu. Na nitamrushia mchungaji sadaka yetu ya shukurani. Tunaitoa leo leo. Haitangoja.” Geb alibadilisha ile hali ya huzuni, wakaanza kutulia.

“Nitakusindikiza Danny.” James akaona na yeye atoke tu, ili wasiharibu hali ya pale iliyojaa furaha na shangwe tupu. Ukweli wote walikuwa na hofu. Lakini sio Geb. Hata mama yake hakuwahi kumuona Geb huyu. Alijawa kujiamini na yeye ndiye alikuwa akiongea mistari ya bibilia kama Grace! Mama G akaanza kuona amekuza vijana. Tokea asubuhi Grace aliingilia ile hali ya Nanaa, akamsaidia wakati yeye amepatwa na mshtuko asijue chakufanya. Kufika hapo hospitalini, anakutana na Geb naye ametulia. Ikabidi na yeye atulie tu.

~~~~~~~~~~~~~

 “Ni sawa  watoto wadogo kuwepo humu?” Geb akauliza kabla daktari hajatoka. “Mpaka sasa hakuna hatari yeyote ile ya maambukizi. Kama nilivyowaambia, damu na mkojo wake ni visafi kabisa. Hakuna ugonjwa wowote kwa mkeo.” Daktari alijibu lakini wazi alionekana yupo kwenye mshangao. Geb alielewa. “Nakushukuru sana.” Geb akampa mkono. Akatoka. “Naomba ukaniletee Liv, mama.” Mama G akatoka kimya kimya bila hata kuongeza neno. 

“Msamehe mama. Hivyo ndivyo anavyokuwa wanae wakiwa wagonjwa. Utampenda hekaheka zake mtu mwingine akiwa mgonjwa! Lakini asiwe mwanae. Hapo akili itakuja kumrudia baadaye.” Alibaki Geb na Nanaa pale chumbani. “Alishaniambiaga tokea kipindi kile tulipohamia kwenye apartment. Halafu nikamuona wakati wa uchungu wa Grace.” Wakacheka kidogo. Wakamkumbuka mama G alivyokuwa amechanganyikiwa wakati Grace anahangaika na uchungu. “Basi ndivyo alivyo. Ujanja wote huwa unamwisha.” Akamuona Nanaa ametulia akiwaza.

~~~~~~~~~~~~~

James, Danny, na mama G wote wakajikuta wamesimama kwenye gari alilokuwepo Grace. “Mbona wote mpo kama mabubu?” Grace akawauliza huku akiwaangalia kwa zamu. Kimya. “We Danny?” Grace akatoa mkono nje akamsukuma kidogo mumewe. “Sijawahi kumuona Geb yule tuliyemuacha mle ndani!” Danny aliongea kama anajaribu kuvuta taswira. “Au amechanganyikiwa?” James akauliza. “Na mimi nilidhani hivyo. Lakini hasikiki kama mtu aliyechanganyikiwa hata kidogo.” Danny akajibu wakati mama G amejiegemeza kwenye gari pembeni.

“Amefanyaje?” Grace akauliza. “Bwana ametulia. Na anasema mipango yao ya harusi inaendelea kama ilivyo!” Danny akajibu. “Sasa nyinyi mlitaka iweje!?” Grace akauliza kwa kushangaa. Wote wakamgeukia. Wakamuona Grace anawaangalia. “We Danny? Ulitakaje? Asimuoe Nanaa!?” “Sio asimuoe. Angalau asubiri aangalie hatima yake.” “Kumbe nyinyi mmeishi na Geb lakini hamjamfahamu! Geb sio mpangaji wa mipango halafu asihakikishe inatimia. Labda Mungu aseme hapana. Na ndio maana hanaga mipango mingii  na hanaga mipango ya kijinga hata mmoja. Hajui kuahidi kitu anachojua hataweza kukisimamia. Akisema anamuoa Nanaa, ujue hajakurupuka. Na ni lazima atamuoa Nanaa, labda Nanaa afe kabla ya hiyo siku. Na akiamua kuwa hatakuwa na watoto nje ya Nanaa, ujue hata Nanaa akishindwa kuzaa mjue Geb hatawahi kuwa na watoto hapa duniani. Ndio Geb alivyo. Na labda ndio maana anafanikiwa san..” “Kwanza Nanaa amekutwa ni mjamzito.” James akamkatisha.

“Jamani Mungu ni mkubwa! Ona katika hili pia amewatumia faraja!” Wote watatu wakasogea pale dirishani wakabaki wakimwangalia Grace mpaka mama yake. “Nini!?” Grace akashangaa. “Kweli nyinyi ni mapacha! Geb naye amesema hivyo hivyo! Yaani maneno hayo hayo kama uliyosema wewe! Ndio maana tunakwambia amechanganyikiwa.” “Heee! Amechanganyikiwa tena!? Hakika huyo ni Mungu, Danny! Si mtu mwingine. Ameamua kumfariji Nanaa katika kipindi hiki kigumu.” Grace aliendelea kushangilia huku akimtukuza Mungu.

“Mimi naona tuondoke James.” “Mnaenda wapi badala turudi ndani tukasherehekee?” Wote wakarudi kumwangalia tena Grace. “Nyinyi vipi jamani!?” Grace akashangaa. “Mbona mpo hivyo!? Shetani hana uwezo wakutoa vitu vizuri hata siku moja. Kelele zake huwa zinaishia kama vile mnavyoona miguu ya Nanaa. Basi. Hawezi kutoa baraka hata siku moja. Huyo ni Mungu ameamua kujidhihirisha kwetu kama kutuonyesha mkono wake bado upo juu ya Nanaa.” Grace akaendelea kurudia aliyozungumza Geb.

“Basi nahisi sisi ndio tumechanganyikiwa!” Danny akaafiki. “Kwa nini?” Grace akauliza. “Maana mwenzio huko ndani anaongea maneno kama hayo hayo unayozungumza wewe! Utafikiri mmeambizana! Hapa tumetumwa vyakula kwa wauguzi wote wanao muhudumia Nanaa, na sisi.” “Usisahau na vinywaji Danny. Tumeambiwa tukalete vinywaji vyakutosha, tusherehekee mtoto aliyekuwepo tumboni.” James akamalizia wakacheka kwa pamoja.

“Haya, watoto wa Danny, mjiandae tunatoka. Fili vaa viatu tunaenda kwa anti Nanaa. Ana mtoto mwingine tumboni.” “Kama vile Fillius na Fillan walivyokuwa tumboni kwako wanacheza?” Fili akamuuliza mama yake huku akitafuta viatu vyake. “Eheee! Lakini wa aunt hawajaanza kucheza. Bado wadogo. Umefurahi?” “Sana mama. Mimi ndio kaka mkubwa. Nitakuwa nacheza na wadogo zangu wote. Nitawafundisha kuruka ngazi.” “Nini?” Danny akashutuka sana na kumgeukia mwanae. “Mbona anko Geb anasema ni sawa tu.” Fili akajitetea. “Wewe ruka peke yako na anko wako. Usifundishe wenzio kuruka. Unataka kunichanganya akili wewe Fili. Sitaki wawe watundu kama wewe.” “Anko amesema mimi ni brave. Nina uwezo wa kuthubutu mambo magumu na sishindwi.” Fili alijibu kifasaha. Grace akaanza kucheka.

“Sasa hapo Grace unacheka nini bwana?” “Wewe usinigeukie mimi. Endelea kupambana na Fili.” Grace akaendelea kucheka. “Hicho kichwa kwa hoja, ukiwezi.” James akaongeza na kuondoka kuelekea lilipokuwa gari yake. “Danny na maneno yote, hapo kwa Fili amefika mwisho. Haya dad, unalanyongeza?” Grace akazidi kumchokoza mumewe. “Hamna kufundisha wenzako kuruka ruka kama wewe. Unanisikia wewe Fili.” Danny aliongea kibabe kidogo.

“Kwa nini?” Fili akauliza kwa utulivu na macho yake kama mama yake. “Wataumia.” Danny akajibu. “Mbona mimi sijawahi kuumia? Naruka kwa kutumia akili dad. Siruki kijinga. Na nitawafundisha kuwa makini kabla hawajaanza kuruka.” Grace alizidi kucheka mpaka akainamia usukani. “Mimi naona niondoke tu.” Danny akaanza kuondoka. 

Mpaka mama G akaanza kucheka. “Danny! Danny mume wangu!” “Sitaki Grace. Mimi naenda kuleta vitu vya sherehe. Geb ataanza kupiga simu sasa hivi, kuulizia.” Danny akaelekea alipokuwa ameegesha James gari yake. Wakaondoka.

“Njoo mama G.” Grace akamuita. “Niambie mama yangu. Kibumbuazi kimekuisha?” “Mmmh! Naona nyinyi watoto mmenipita. Imebidi kiishe tu. Maana huko ndani ukiingia, hata ukiwa na huzuni zako zinaisha.” Grace akacheka. “Kwa nini?” “Huyo Geb! Kila neno analoongea ni kinyume na hofu. Anasema yale shetani aliyokusudia kuwa mabaya, Mungu anayabadilisha kuwa mema. Anasema kilio chao, Mungu amekibadilisha na kuwa kicheko. Amefurahi huyo! Kama Nanaa amepona!” “Jambo la kumshukuru Mungu mama! Unafikiri kama yeye angeendelea kupaniki kama vile asubuhi, wewe ungekuwa kwenye hali gani? Ingekuwa mbaya zaidi!”

 “Na ni kweli. Ila Grace, umekuwa mwanangu. Sikutegemea kama ungekuwa shupavu hivyo! Yaani leo asubuhi pale chumbani kwa Geb na Nanaa, niliona sura ya Magesa hivi. Nikasema katika hali hii ngumu, Mungu amemrudisha Magesa kupitia wewe. Ulifanya kama vile baba yako angefanya! Utulivu usoni mwako, maneno ya kutokatisha tamaa, na kuchukua hatua kwa haraka kwenye wakati mtatanishi kama ule ambao wote tulikuwa hatujui chakufanya!” Mama G akacheka.

“Unacheka nini sasa?” Grace akamuuliza. “Ulimuona Geb lakini?” Wote walizidi kucheka. “Lakini Nanaa anatisha mama! Kuamka na kukutana na miguu ya hali ile! Mimi mwenyewe sijui ujasiri nilipata wapi?” “Nikaona kwa masaa machache wewe ukawa Magesa, basi kiziwanda wangu akawa kama mama yake!” Wakazidi kucheka. “Lakini ukimuona humo ndani sasa hivi, utafikiri Magesa amefufuka. Mimi mpaka nimeondoka. Alivyosimama! Anavyoongea! Ule ujasiri! Ni Magesa mtupu! Na sura ile na macho, hakika utafikiri Magesa mwenyewe Mungu amenirudishia.” “Sasa Nanaa yupo na hali gani?” “Ametulia kabisa. Hayo mabusu anayopewa!” Grace akacheka sana.

“Na Geb anavyojua kubembeleza!” “Basi na maneno yake hayo, mpaka Nanaa ametulia. Lakini Geb ameomba afunikwe ile miguu asiione kwa sasa hivi. Habari walizonazo humo ndani wanasema ni njema tu. Nanaa amepimwa hajakutwa na tatizo na Mungu amewabariki mtoto mwingine. Basi.” “Afadhali. Twende basi.” “Ujue nilitumwa nimpeleke Oliva?” “Hivi wewe mama ukoje bwana!? Naomba ubadilike. Nanaa alikuwa anakulilia na wewe ukabaki umeduaa!” “Bwana ananijua huwa naishiwa nguvu. Anajua sana.” “Hapana bwana.”

“Basi sasa hivi nguvu zimerudi.” “Kweli? Maana sio turudi tena ndani, uanze tena kufa ganzi na kugeuka kuwa bubu wakati haya ndiyo mambo yako ya kuombea.” “Halafu hatujaomba hata mara moja, Grace!” “Shetani huyo. Jana nilitaka kuanza kuomba, Danny akaingia na jeshi lake.” Wakacheka. “Lazima leo tupige maombi ya nguvu.” “Kabisa.” Mama G akafungua mlango. “Kumbe wote wapo macho!?” “Wameshiba hapo. Liv nilimlisha tena, na hao kina kaka nimewapa uji.” “Wewe Grace!?” “Kweli mama. Nimeona hawashibi. Huoni walivyotulia? Nimewapa uji wa Liv.” “Umewalevya bwana!” “Heri hivyo walivyolewa. Na mimi nipumzike.” Mama G akacheka.

“Hawajakataa?”“Wapo kama Danny hawa watoto. Naona hawa sitasumbuka nao kama Fili. Wamekula mpaka nikaona basi. Hapo nimewawekea nyimbo za watoto, wanaangalia huku wanasinzia. Kimyaa, kila mtu anashuguli zake.” Mama G akatingisha kichwa. “Nilijua nikiwaambia wewe na Danny, mngekataa.” “Kwa hiyo ukaona ufanye siri?” “Kumbe!” “Watoto wadogo hao Grace. Ungewaanzishia maziwa mengine.” “Hayakai tumboni. Bora wanywe uji na kunyonya. Nitachanganyikiwa mama. Wananiliza kila siku! Sina hata muda na Danny wangu? Hapana mama. Namtaka mume wangu.”

“Na watoto?” “Watakuwa tu. Nikiona huo uji umewakataa, basi. Nitatafuta njia nyingine. Yaani sina muda na mume wangu hata kidogo! Watoto wakilala, na sisi tumechoka. Hapana mama. Ni mwezi unaenda watatu huu, hata hatujapata muda na Danny!” “Ni hivi tu limetokea hili. Ningekushikia hata kwa masaa matatu mrudi kwenu kwa muda mfupi mpumzike, ndio mrudi pale.” “Mbona itabidi ufanye tu.” “Grace wewe mtoto?” “Kweli mama. Na hivi wameshaanza kunywa uji. Baadaye tukirudi nyumbani, nitatoka na Danny kidogo.” Mama G akatingisha kichwa.

Liv alipomuona tu bibi yake akaanza kuhangaika pale kwenye kiti huku anacheka na kunyanyua vimikono vyake juu. “Muone alivyofurahi kukuona.” Mama G akacheka. Akapita mpaka kiti cha nyuma kabisa alipokuwa amekaa Oliva. Grace alinunuliwa na mumewe gari nyingine ya Toyota Van. Yenye njia ya katikati. Kwa hiyo ilikuwa rahisi kufikia kiti chochote. Ilikuwa ni gari ya viti 7. Waliita gari ya watoto. Waliwaweka kwenye viti vyao na kuwafunga mikanda. Wakawa wakizunguka nao bila shida ya kupakatana.

Akambusu Liv. “Salamu kwanza Oliva. Wewe vipi bwana?”  Bibi yake alimwambia. “Anataka umbembe?” Grace akauliza huku akiwatoa wanae Fillius na Fillan, na kuwaweka kwenye kigari chao cha kuwasukuma wakati wakitembea. Na chenyewe kilikuwa cha mapacha watatu. Wakati mwingine walimuweka Liv humo kama bibi yake na baba yake hawapo. Wakiwepo, atataka wambebe tu, sio kumsukuma kwenye kigari. 

“Nakwambia! Anataka salamu hiyo tupeane nikiwa nimembeba! Haya njoo.” Mama G akamtoa Liv kwenye kiti chake akambeba, kisha akambusu. Liv akaanza kucheka huku akiongea kwa lugha ya kitoto. “Unamtaka dad?” Mama G akamuuliza. Liv akacheka. “Haya, twende kwa dad yako.” Wakatoka pale, Fili akiwa anafuraha zote.

~~~~~~~~~~~~~

Walimkuta Geb anaomba na Nanaa. Maombi yalikuwa ya shukurani tu. Isivyo kawaida, Oliva alivyoingia tu akamtaka mama yake na wala si baba yake. Nanaa alianza kulia kwa uchungu sana. Kwani mkono mmoja alishawekewa dripu ya maji ili kufidia yale maji anayopoteza kwa wingi miguuni. Oliva alilalamika akimtaka mama yake mpaka Geb akamtoa nje. Hapo ndipo alipoanza kulia. Mama yao naye akatoka. “Labda ni njaa mama.” “Hana njaa. Amekula vizuri tu. Labda anahamu na mama yake. Mweke pale akae naye tu.” “Nanaa anaogopa mama. Hataki amuambukize.” “Mweke kidogo tu hata kifuani atulie. Unamjua mwanao yupo kama wewe. Hawezi kutaka kitu akatulia mpaka akipate. Muweke kwa mama yake.” Wakarudi ndani.

Liv alishakuwa mwekundu. “Mshike kidogo tu, atulie.” Geb akamuweka kwa mama yake. Akamlalia mama yake kama alivyokuwa akimlalia baba yake kifuani, Nanaa akamkumbatia kwa mikono yote miwili. Nanaa ndiye aliyebaki akilia. “Nitakufa nimuache mwanangu!” Nanaa alisikika akilia taratibu.

“Nisikilize Nanaa. Uzima na mauti upo kwenye kinywa chako. Unachokiri ndicho kitakacho kuwa. Ukikiri mauti, na kweli mauti ndiye atakayekuja. Ukikiri uzima, uzima ndiye atakayekuja. Pambana. Tena pambana sana kwa ajili yako na wanao. Una sababu kubwa ya kupambana. Kama si kwa ajili yako basi ya wanao. Liv, na huyo ambaye yupo tumboni anayekutegemea kwa asilimia zote. Ujue sasa hivi unaishi kwa ajili yako na huyo mjukuu wangu. Nataka upambane haswa. Kiri uzima. Jiambie hutakufa bali utaishi. Ambia hiyo hali hutakufa, hutakuwa kilema, iambie utaishi uyashuhudie matendo makubwa ya Bwana. Umenisikia Nanaa?” Mama G akaongea kijasiri, Nanaa akatingisha kichwa.

“Hapana Nanaa. You can do better than that.” Geb akaingilia. “Sitakufa, bali nitaishi. Niyashuhudie makuu ya Mungu.” Nanaa akarudia. “Hiyo ni kwa ajili yako. Sasa iambie hali yako. Na lazima kuwa jasiri. Tena ongeza kuwa, ‘uhai wangu umefichwa ndani ya Kristo Yesu’.” Geb akasisitiza. “Tena bila machozi.” Mama G akaongeza. Geb akamsogelea nakumfuta machozi. Nanaa akatulia na kurudia. “Sitakufa. Bali nitaishi. Niyashuhudie makuu ya Mungu. Si mimi ninayeishi, bali Kristo ndani yangu. Na uhai wangu umefichwa ndani ya Kristo Yesu.” Nanaa aliongeza na kufanya mama G na wanae wacheke na kumpigia makofi. 

“Safi sana. Sasa tumwite huyo aliyeficha uhai wako. Tumkumbushe juu ya afya yako. Hakuna atakayetulia tena, mpaka tuone Bwana atakavyotujibu katika hali ya kulalamika kwetu. Tuombe.” Yakaanza maombi pale chumbani. Mama G ndiye aliyekuwa akiongoza. Waliomba bila kupumzika. Danny na James walipoingia na vyakula, na wao wakaungana nao kuomba mpaka  wakamaliza.

“Tumeshagawa vyakula na vinywaji kwa wauguzi wote wa hii gorofa.” “Nashukuru sana Danny. Asante.” Wakakaa wote wakamshukuru Mungu na kuanza kula huku Oliva amelala kifuani kwa mama yake. Kila walipotaka kumtoa, Nanaa alikataa. Alibaki akimpapasa mgongoni huku wengine wakiendelea kula na kuzungumza. Wakamaliza kula wakabaki wakizungumza tu. 

~~~~~~~~~~~~~

Mambo yakaanza kubadilika pale Geb alipoaga. Akamsogelea Nanaa. “Nitarudi baada ya muda mfupi. Nakimbia nyumbani mara moja.” “Utarudi?” Nanaa akauliza. “Sitakawia.” Geb akajibu. Tayari Nanaa alishaanza kutetemeka kwa hofu. “Najua utarudi tu. Si ndio?” “Nitarudi Nanaa!” Nanaa akaanza kumpigapiga mtoto wake mgongoni kama anayembembeleza, wakati Oliva alikuwa ameshalala. “Najua. Najua unaenda mara moja tu, halafu utarudi. Hutachelewa.” Watu wote wakatulia. 

James akamsogelea. Akajua ameingiwa na hofu. “Nipe nikupokee mtoto.” “Geb anakwenda nyumbani mara moja kaka. Atarudi.” “Ndiyo Nanaa.” James akamjibu kwa upole kutaka atulie. Maana hata midomo yake ilishaanza kucheza kama aliyeshika baridi kali. “Nanaa! Nanaa! Niangalie.” Geb akamuita. James akamchukua mtoto. “Kuna vitu naenda kuchukua mara moja nitarudi baada ya muda mfupi sana.” Geb akarudia taratibu akijaribu kumtuliza  “Hata mimi najua utarudi Geb. Huwezi kuniacha hapa peke yangu.” Nanaa alianza kutokwa machozi huku akitetemeka sana. Akavuta shuka akajifunika mpaka mabegani huku machozi yakimtoka. “Nenda tu. Mimi nitakuwa hapa hapa nakusubiri Geb. Nitakusubiri. Hamna neno kabisa.” Kila mtu alikuwa akimwangalia kwa kumuhurumia. Wakajua ameingiwa hofu.

“Nanaa!” “Nenda tu Geb. Nakuamini utarudi.” Geb akamshika mkono. Akakaa pembeni ya kitanda. “Kwani unataka nini huko nyumbani?” Grace akauliza.

“Begi langu lile la kazini. Lenye laptop. Na..” “Nenda tu kachukue Geb. Nitasubiri.” Nanaa akarudia huku bado midomo ikimcheza. “Naona nitamtuma Grace akanikusanyie vitu ninavyovitaka, halafu..” “Mimi nitarudi navyo.” Akawahi James kwa kumkata Geb na kuendelea. “Mimi niende na Grace. Anipe hivyo vitu vyako vyote. Nitakuletea Geb.” James aliongea kinyenyekevu sana kama anayesihi na kuomba Geb abaki tu na dada yake. “Nafikiri hilo wazo ni zuri. Halafu tumuache Nanaa sasa hivi apumzike.” Mama G akaongeza.

Geb akamfuta machozi, akamwinamia pale kitandani nakuanza kumbusu pale mbele za watu. Nanaa akaanza kutulia. “Lala mimi nitakuwa hapa hapa.” “Niliingiwa na hofu Geb. Samahani.” Geb akambusu tena kwenye kipanda uso, akampa na tabasamu. “Nenda tu.” Walimsikia Nanaa akiongea akisikika akiwa ametulia kidogo. Bado Geb alikuwa amemwinamia. “Naelewa. Usijali. Hata mimi sitaki kuondoka tena.” “Kweli?” Nanaa akamuuliza kwa upole. “Nikitoka hapa, tutatoka wote.”  “Sasa kazini?” Nanaa akauliza. “Mimi nitakuwa nikienda hata kama ni nusu siku. Ili kuhakikisha kila kitu kipo sawa. Usiwe au msiwe na wasiwasi.” Wote wakamgeukia Grace mpaka mumewe.

Grace akacheka. “Nitawabeba wanangu wala msiwe na wasiwasi. Wakiamka vizuri, tunaenda asubuhi. Wakiamka na akili kama za baba yao, naenda nao mchana. Tutakuwa tunawasiliana Geb. Wewe tuliza mawazo tu hapa hospitalini. Mambo mengine yatakuwa sawa.” Geb aliinama kwa muda kama anayefikiria. Kisha akamgeukia tena Grace. “Nakushukuru sana Grace. Asante. Asante sana.” “Asante Grace.” Nanaa naye akaongeza.  “Wala msijali. Kwanza likizo yenyewe ilikuwa imeshaisha. Nilikuwa nikivuta tu muda huku nikitafuta msichana wa kazi. Watoto wenyewe wameshakuwa.” Grace akaongeza. “Afadhali. Utakuwa umempunguzia mwenzio mzigo mkubwa sana. Hata yeye atatulia.” Mama G akaongeza. Geb akamgeukia tena Nanaa, akamvuta mkono na kuubusu.

Hakuna Msiba Usio Kuwa Na Mwenzie.

Wakiwa wanataka kutoka, mchungaji akampigia simu mama G. “Upo sehemu nzuri tunaweza kuzungumza?” Mchungaji akauliza. “Nipo na wanangu. Tunaweza kuongea tu.” “Mlikumbuka kama leo ndio lilikuwa tangazo la kwanza la harusi ya Geb na Nanaa?” “Tunakumbuka mchungaji. Lakini tumepata matatizo. Hapa tupo hospitalini ndio maana tumeshindwa kuja kanisani. Ulifanikiwa kutangaza?” Mama G akauliza. Wote walikuwa wakisikiliza. 

“Kabla sijakwambia kilichonifanya nikupigie, niambie kwanza nani ni mgonjwa?” Mchungaji akahoji tena. “Kuna nini tena?” Mama G akauliza. “Nafikiri ushugulike na tatizo moja baada ya jingine.” Mchungaji akashauri. “Mpaka sasa sijaona tatizo lakunifanya nishindwe kukabiliana na changamoto nyingine, Mchungaji. Tafadhali niambie tu. Kuna nini?” Mama G aliendelea kusisitiza. Mchungaji akasita. “Au tuonane?” “Hamna shida. Sasa hivi tupo hapa hospitalini ndio tunajiandaa kuondoka. Naelekea nyumbani. Lakini kabla hatujapanga muda na wakati wa kukutana, nataka kujua tunakutana kwa ajili ya nini! Na tafadhali usinifiche.” Mama G akasisitiza zaidi.

“Tangazo la kwanza tu, limepata kipingamizi.” Mchungaji akaongea. “Unamaanisha nini?” Mama G akauliza. “Leo wakati natoa tangazo la kwanza la ndoa ya Geb na Nanaa, nikapata vipingamizi viwili. Wapo watu wawili wanaopinga hiyo ndoa isifungwe. Kwa hiyo hatuwezi kuendelea mpaka tufikie muafaka.” Mama G akavuta pumzi kwa nguvu na kuzishusha taratibu.

“Vipingamizi kutoka kwa nani?” Mama G akauliza. “Labda tukutane. Ili tuzungumze.” Mchungaji akasisitiza. “Kwa nini ulinipigia simu?” Mama G alishabadilika. “Kama sijakosea, ulinipigia simu ili kunijulisha. Simu ni nusu ya kuonana. Tafadhali tusiendelee kupoteza muda zaidi.” Mama G aliongea kwa ukali kidogo huku wote wakimsikiliza. “Ni kweli.” Mchungaji akajishusha. Mama G akaweka ile simu kwenye speaker ili kila mtu asikilize.

“Kipingamizi cha kwanza kinatoka kwa mama yake Nanaa.” “Nanaa ni yatima, mimi ndio mama yake.” Mama G akajibu kibabe. “Amekuja hapa mama mmoja. Wakati natangaza, yeye na kijana mmoja wakapinga kuwa ndoa isifungwe. Ndipo baada ya ibada ikabidi kukaa nao ofisini. Huyo mama amejitambulisha kwa jina la ‘Mama James’. Anasema yeye ndiye aliyemlea Nanaa tokea mama yake amefariki. Amemlea kwa tabu sana. Alipowaambia anataka alipwe fidia, mmemkatalia.” “Subiri kwanza. Mama James amesema tumemkatalia kumlipa!?” “Labda sijaongea vizuri. Amesema mmemkatalia kumpa pesa aliyowadai, mmemlipa kidogo sana.” “Mungu wangu mama!” James alisikika akisikitika.

“Amekwambia yeye alitaka kiasi gani?” “Anavyodai alitaka milioni 100. Akamtuma mwanae kwenu. Mkaomba mpunguziwe mpaka milioni 50. Akakubali. Matokeo yake mmempa hundi ya milioni 30 tu. Tena anasema alipoenda benki wamemkatalia kumpa hiyo pesa.” “Mama James hasemi ukweli mama.” Geb aliingilia. “Jumatatu tulipokuwa Moshi. Tena kabla hata hatujaondoka Moshi, meneja wa tawi la benki alilokuwa amekwenda kuchukua hiyo pesa, alimpigia simu meneja wa benki yenye akaunti yangu hapa Dar. Tena huyo Mzee naheshimiana naye sana. Naweza hata kuwapa namba yake. Alinipigia simu kuniuliza kama kweli nimehidhinisha hiyo pesa itolewe kutoka kwenye akaunti yangu huko Moshi. Akaniambia yupo kwenye simu nyingine na meneja wa tawi la Moshi, yaani bado hajakata simu. Na mama yake James yupo hapo ofisini na binti mwingine.”

Tena alinisomea jina kamili la mama yake Jemes kutoka kwenye kitambulisho chake. Maana huyu meneja wa hapa Dar alimwambia akitoe kopi kitambulisho cha huyo mama amtumie saa hiyo hiyo kwa Fax. Nikamwambia ampe hiyo pesa. Mimi ndiye nimemwandikia hiyo hundi. Lakini nikamsisitiza ahakikishe wanasahihishana vizuri, halafu wanitumie kopi zote. Yule meneja wa hapa alinipigia simu baadaye akaniambia ameshakamilisha kila kitu na kopi zote za kuthibitisha amechukua malipo, anazo. Nikipata muda niende ofisini kwake nikachukue. Sijakwenda mpaka leo, kwa kuwa nimekuwa na mambo mengi. Kwa hiyo amechukua hiyo pesa.” Geb akamaliza kujitetea.

“Umesikia mchungaji? Kwamba kithibitisho kipo?” Mama G alikuwa kwenye spika. “Nimesikia. Sasa na hilo salio?” Mchungaji akauliza. “Salio gani tena!?” Mama G akauliza. “Amesema aliwadai milioni 50, lakini mkampa milioni 30. Hivi amesema yupo hotelini amekuja kudai malipo yake. Anasema mmemchukua Nanaa, mnaishi naye bila kumlipa. Amelalamika kuwa yeye ndiye aliyehangaika naye tokea mtoto, lakini nyinyi ndio mnafaidi matunda yake. Amesema hatatulia, mpaka apate haki yake. Atafanya lolote na kwenda popote mpaka apate haki yake.” “Mungu wangu mama!” James alikuwa ameshika kichwa. Nanaa ndiye alikuwa akilia sana.

~~~~~~~~~~~~~

Kila James alipokuwa akitizama hali ya dada yake pale kitandani, haikuwa ikifanania kabisa na mamilioni ya pesa waliyokuwa wakidaiwa. Nanaa alikuwa akivuja maji pale kitandani! Vipimo vya awali vilishaonyesha hana tatizo. Inamaana ataendelea kuwepo hapo ili lijulikane tatizo na ndipo matibabu yaanze. Akajua na hapo tena kwenye hiyo hospitali yakulipia, patagarimu pesa nyingi sana. Sasa wanalipaje tena mamilioni ya pesa ya mahari wakati pale tu alipolala dada yake, James alijua ni pesa nyingi sana zitamtoka Geb!?

Chumba alicholazwa Nanaa na huduma alizokuwa akipewa ni za hali ya juu sana. James alijua ni mapesa mengi yatamtoka Geb. Japokuwa yeye mwenyewe alikuwa akilipiwa matibabu na kampuni yake, lakini alijua hata kama angelazwa kwenye hospitali hiyo, kampuni hiyo ingemudu kumuweka kwenye chumba cha angalau watu wawili tu. Sio chumba cha peke yake kama vile.

Ni mapenzi ya dhati kwa dada yake kutoka kwa Geb ndiyo yamemlazimu kumlaza Nanaa pale. Ili kupata huduma ya haraka na makinifu. “Hawa watu watajitoa hivi kwa Nanaa mpaka lini? Mwishowe watamchoka au wataanza kumuona ni mzigo.” James aliwaza.

“Hali yangu hii sio yakulipiwa mamilioni ya pesa. Geb atashindwa. Ataniacha.” Nanaa aliendelea kulia huku akiwaza. Alijifunika shuka akawa analia kwa uchungu sana.

Ni kweli mtu huchagui uzaliwe wapi na nani. Na wala huchagui uzaliwe kwenye mazingira yepi. Huchagui ndugu, wala kabila. Sasa kwa nini Mungu anaweka wengine kwenye mazingira kama ya Nanaa? Nanaa alizaliwa na kujikuta mikononi kwa mama yake James. Hakumbuki alipokuwa akilia wakati mchanga! Hakumbuki siku wala muda alipokuwa akinyonya ziwa la mama huyo analodai malipo ya pesa nyingi hivyo! “Kwani mimi nina mkosi gani jamani!?” Ndilo swali ambalo Nanaa hakuweza kupata jibu lake.

~~~~~~~~~~~~~

 Ukimya ulikuwa umetanda pale chumbani wakimsikiliza mchungaji. “Huyu mama anaonekana anamaanisha anachoongea mama G. Amesema bila kulipwa pesa yake, hiyo harusi haitafungwa na wala hakuna atakayeweza kufaidi jasho lake.” “Anamaanisha nini?” Mama G akauliza. “Alikuwa akiongea kwa jazba sana. Ilichukua muda kumtoa hapa ofisini kwani alikuwa akionyesha vitisho.” “Vitisho gani?” Mama G aliendelea kuhoji. “Ni mambo mengi. Ikabidi kumtoa tu hapa. Maana watu hata wamtaani walinza kujaa hapa kanisani. Lakini amesisitiza kama hatalipwa hiyo pesa yake yote, hakuna mtu atakayefaidi matunda yake.” Wote wakavuta pumzi.

“Na mwingine ni nani?” Mama G akahoji. “Kijana mmoja amejitaja kwa jina moja tu, Zinda. Anasema Nanaa ni mkewe ila Geb amempokonya.” “Amekuletea cheti chake cha ndoa aliyofunga yeye na Nanaa?” Mama G alitumia akili ya haraka sana. Akauliza hilo swali. “Amesema atakileta kama tutataka uthibitisho. Lakini na yeye amesema hiyo ndoa isifungwe, kwa kuwa Nanaa ni mke wake kihalali. Ila Geb anatumia pesa yake kumrubuni mkewe.” Wote wakashangaa.  “Umesema amekwambia anacho cheti chao cha ndoa?” Mama G akauliza tena kuthibitisha. “Ndiyo.” Mchungaji akajibu.

“Ndoa aliyofunga yeye na Nanaa!?” Mama G akahoji tena kwa mshangao. “Amesema nikikihitaji kwa uthibitisho zaidi, atakileta. Na anasema kama sitachukua hatua maalumu, anakwenda kwenye vyombo vya sheria. Na amesisitiza na yeye kuwa, Nanaa hatakaa akaolewa na Geb, labda kama yeye sio mwanaume.” Hapo ndio kila mtu akabaki anajiuliza ni mchezo gani Zinda anataka kucheza! Mama G akavuta pumzi kwa nguvu.

~~~~~~~~~~~~~

Bado mambo yanazidi kumuwakia moto Nanaa. Hata hapo kitandani bado changamoto zinaendelea kumfuata tu. Mwanzoni Geb

alionekana akiweza. Akalipa milioni 30 kwa haraka sana. Sasa zinahitajika milioni 20 nyingine kwa ajili ya Nanaa aliyeoza

miguu na kuvuja maji hapo hospitalini.

-       Je, bado ipo thamani ya kuendelea kulipia mipesa yote hiyo? Pengine ndio kimya cha Geb akitafuta thamani hiyo na kujishauri kama akimbie au abaki!?

Zinda naye amedai Nanaa ni mkewe halali na anacho Kithibitisho.

-       Kipi? Maana ni kweli Nanaa alipotezana na familia hiyo ya

Magesa na kaka yake, akatokezea na Liv.

-       Alikuwa wapi?

-       Ni kweli alifunga ndoa na Zinda?

-       Je ni kweli Zinda anacho kithibitishi?

-       Hao wote walijuaje kama siku hiyo ndiyo siku ya Tangazo la kwanza la Ndoa ya Nanaa na Geb wkati hawakuwepo siku ya kikao cha kwanza cha harusi?

Kikulacho, kinguoni Mwako. Nani Ndumi La Kuwili?

Usikose kufuatilia ili kujua.

 

 


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment