“Wewe
Geb tokea tunakutana sekondari, kidato cha kwanza, mpaka mwaka jana
hamjamchukua Nanaa kuishi naye hapa, nilikuwa nikikwambia habari za Nanaa. Kwa
wazi bila kukuficha. Ni kwamba mnasahau au mmeamua kupuuza?” “Nakumbuka kila
kitu James.” “Kwa hiyo ni umeamua kupuuza
tu? Maana usingefanya unayoyafanya. Mnajua kuwa Nanaa ni kama yatima. Hana
pakwenda, na alipolelewa nako wanamsubiria akosee mahali ili wanibeze au
wamcheke. Leo umezaa na mdogo wangu, unamvalisha pete uchochoroni na kumficha
hapa kwa kuwa unajua hana pakwenda!? Katika kuishi kote hapa duniani ndivyo
unavyoona watu wanafanya? Yaani unazaa na binti ya watu, unamvalisha pete,
halafu unamficha, ndio inakuwa basi? Unaishi naye kama mkeo kwa ruksa ya nani?”
“Ndio maana upo hapa leo, James! Sijakusudia kumficha Nanaa.” Geb alianza akiwa
ametulia tu.
“Unakumbuka
nilikufuata ofisini kwako nikakwambia kuwa nampenda Nanaa?” “Ndio ulikuwa
ukiomba ruhusa ya kumzalisha?” James akauliza kwa jazba, Geb akatulia kidogo.
Hakuna aliyejua kama Geb alishamfuata James kumwambia maswala ya Nanaa. Wote
wakabaki kimya wakisubiria kuona mwisho wa Geb na James. “Nakufahamu Geb. Wewe
sio mtu wakukosea. Kumbuka ni kama tumekuwa pamoja.” “Sikujua kama Nanaa ni
mjamzito. Alinikataa, akaondoka kwangu akiwa mjamzito bila kuniambia. Alinipiga
marufuku nisimtafute tena maishani, kama vile na wewe ulivyonifuata rasmi na
kunionya nisisogee pale chuo kikuu cha Mlimani kumfuata Nanaa, labda niende kwa
shuguli zangu.” James alianza kutulia. Nanaa hata hakuwa akijua kama kaka yake
alimkataza Geb asimtafute.
“Sasa kwa kuwa ulikuwa mwaka wake wa mwisho
chuoni, nikakubaliana na onyo lako na nikaona ni vyema kumuacha, nisimbugudhi.
Sikukutana na Nanaa, mpaka miezi miwili iliyopita, akiwa na mtoto wangu.
Alijifungua, akamtafuta mama nakumuomba amuhudumie kwa siri. Nilipoona nyendo
za mama hazielewiki ni kama za siri, ndipo nikamfuatilia. Alikuwa akitoka
asubuhi na vyakula, anarudi usiku. Ndipo nilipoingiwa na wasiwasi. Ndio siku
moja nikaamua kumfuatilia mpaka hosteli za Mlimani ambako alikuwepo mtoto wangu
na Nanaa. Kwa kuwa Nanaa hakutaka kunihusisha na mtoto wangu, nilimchukua mtoto
wangu kwa nguvu, ndipo Nanaa akanifuata nyumbani. Nilimkatalia mtoto kwa
makusudi ili Nanaa abaki nyumbani, atulie.” Geb akaendelea.
“Tulikuwa
kwenye hali mbaya sana James. Nisingeweza kumwambia mtu yeyote juu ya Nanaa au
mtoto kwa wakati ule, kwa kuwa sikuwa najua hatima yetu. Tumepata na Nanaa, na
kuwekana sawa, hata week haijaisha! Jana ndio tumerudi kutoka kwenye apartment.
Tulikuwa tukiishi huko na ndiko tulikopatana na Nanaa. Leo upo hapa ili
kukutambulisha mtoto, lakini pia kutaka kujua taratibu za kulipa mahari.
Nimekusudia kumuoa Nanaa, na wewe unanijua James, huwa sidanganyi.” James akabaki
kimya kwa muda.
“Usingemzalisha
kwanza, Geb! Si ungesubiri!” “Nanaa asingekubali nimuoe James. Na wala leo
asingekuwa hapa na mimi. Muulize
mwenyewe. Hata alivyorudi na mtoto, alijaribu kunitoroka. Nakuhakikishia na
nyinyi watatu wote mnanijua kasoro mama, nisingezaa na Nanaa kama sina nia ya
kumuoa. Weka hasira pembeni James, halafu kuwa mkweli. Unanijua mimi, huwa
sifanyagi kosa kama hilo.” Geb akajitetea tena. Kwa kuwa James alimjua Geb,
akatulia kidogo.
“Pole
sana mwanangu, lakini mtoto mwenyewe ungemuona, ingekusaidia. Nanaa katuletea
toto la nguvu. Damu nyeupe peee. Kitu hadimu kwenye ukoo wetu.” Kidogo James
akatabasamu.“Yuko wapi?” “Amelala, lakini ngoja nikuletee labda utafurahi
kidogo.” Mama G akasimama kwa
haraka. “Nashindwa kukuomba
msamaha James, nitakuwa nakudanganya tu. Haikuwa bahati mbaya. Hivi ilivyo,
ndivyo nilikusudia iwe. Nisaidie kunipa tu taratibu inayofuata ili kukamilisha
utaratibu wakumfanya Nanaa kuwa mke wangu wa halali.” James akacheka,
akatingisha kichwa.
“Unajua
siamini kabisa! Aisee Geb wewe niking’ang’anizi! Labda ndio maana umefanikiwa
kuliko sisi wote.” Angalau watu wakacheka. “Nilikuwa namuonya Geb huku
nimemtolea macho, aachane kabisa na Nanaa. Yaani nilikuwa namkaripia mpaka
mwenyewe najua. Lakini ukakazana tu! Nilikuwa najua sana kama ulikuwa ukikesha
pale kwa Antii wakati Nanaa alipotoka hospitalini.” Geb akacheka. “Nilimsihi
sana Antii asikwambie.” “Asingeweza. Lakini nikamwambia akuache tu.” Kidogo
Nanaa akapumua.
“Sijui
kwa nini tokea unaanza kumsimulia Nanaa tukiwa shule, nikaanza kujiona na mimi
nawajibika kama wewe! Unakumbuka Danny?” “Nakumbuka vile James alivyokuwa
anadanganya shuleni anaumwa ili arudi kumuona Nanaa. Wakati huo Nanaa kalikuwa
hakajatimiza hata miaka 5.” “Nilimuacha nyumbani ndio ameingiza miaka 4.
Nikamuomba Mzee anihamishie shule ya sekondari ya Old Moshi, mama akakataa.
Nilikuwa nakaribia kuchanganyikiwa! Maana ndio kalikuwa kadogo. Halafu likizo
nzima ile ya darasa la saba, nilikaa naye kama yaya wake. Kumlisha, kumuogesha
na kumfanyia kila kitu. Sasa matokeo kutoka, naambiwa natakiwa kwenda kusoma
bweni! Nilihisi nitarukwa na akili. Maana tokea kanatolewa hospitalini mimi
ndio nilikuwa nakitunza. Wakati mwingine natoka shule nakikikuta kimelowa,
inabidi kukibadilisha. Hapo nipo la 5. Nanaa hajui mtu ila mimi. Nahisi ndio
maana nilipokutana na nyinyi nilikuwa nikimuongelea sana Nanaa ili kujifariji
tu. Nilikuwa na wasiwasi naye kweli.” “Labda na mimi ndio maana nilianza
kumfuatilia kwa kumuonea huruma.” Geb akaongeza.
“Lakini
Geb ulikazana! Unakumbuka James?” “Sana tu. Unakumbuka mpaka tukalizungumzia
hili?” James akauliza. “Nakumbuka. Kila mtu alijua kama Geb anamfuatilia
Nanaa.” Danny akaongeza. “Sasa utata ukaja pale ulipoanza mahusiano na wanawake
wengine. Nikajiambia labda ni upendo wa kikaka.” Wote wakacheka. “Lakini hata
mimi nilidhania hivyo hivyo mwanzoni. Kuwa ni upendo kama wa James kwa Nanaa.
Lakini kadiri siku zilivyozidi kwenda, ndivyo nikawa nikimfikiria Nanaa kwa
zaidi. Mambo yaliharibika nilipokuja kumuona Nanaa mwenyewe. Ndio nikajua ni
mke wangu.” Walizi kucheka.
“Nisaidie
tu kujua hizo taratibu za mahari.” “Nitaongea na mama, tuone atasemaje.”
“Asante kaka, na samahani sana kwa kutokukwambia mapema.” Akamgeukia Nanaa.
“Daah! Ushukuru kwa kuwa ni Geb. Sijui tungejificha wapi!?” “Samahani kaka
yangu.” James akatingisha kichwa na tabasamu usoni. “Umekosea pazuri.” James
akajibu, wakacheka.
~~~~~~~~~~~~
Mama
G akatoka na Oliva, akamkabidhi James. James akaanza kumwangalia kwa makini
kisha akauliza. “Una uhakika huyu mtoto ni wa Geb wewe Nanaa?” “Kaka wewe!”
Wote wakacheka. “Mbona mtoto kama wakiarabu!?” James alijawa na tabasamu kila
mtu aliliona lile tabasamu. “Wangu huyo, James. Angalia nywele hiyo. Hata umpe
mchina miaka 7 hawezi kuitoa nywele kama hiyo kiwandani. Na akifungua macho,
utafikiri Fili.” Geb alijisifia huku na yeye akimsogelea yule mtoto.
“Fungua basi hayo macho mama, ili
wakuone!” Geb alimuongelesha mwanae taratibu huku akimkuna miguu. “Na anajua
kulala huyo!” Mama G aliongeza. “Hongereni sana.” James akawapongeza. “Asante.”
Mama G akadakia yeye kwa haraka.
“Mama
wewe! Mtoto wa kwako!?” Grace akamuwahi. “Kumbe wako? Huyo mtoto anajina langu
na ninamlea mimi mwenyewe tokea anazaliwa. Mama yake hajawahi hata kumuogesha
huyu mtoto! Muulize. Anajua kunyonyesha tu, kazi nyingine zote za huyo mtoto ni
mimi.” “Basi na biashara pia imemshinda, mama huyo! Anakazi yakulea tu” Grace
aliongeza nakumfanya James acheke.
“Mama
umeacha kazi?” “Kazi zipo James mwanangu. Nikienda kesho au kesho kutwa,
nitaikuta tu. Lakini huyu wajina wangu, siku ikipita moja, ujue haitakaa
ikarudia milele. Sitaki kupitwa.” James alijisikia vizuri sana. “Asante sana
mama kwa kumpokea Nanaa. Nafarijika nikiona mnamjali, anahitaji familia.
Nitaenda kuzungumza na mama kujua taratibu za mahari.” James alikuwa akiongea
huku macho yote yakiwa kwa huyo mtoto.
~~~~~~~~~~~
Chakula
kiliwekwa mezani, Nanaa akawakaribisha watu wote pale mezani. Akakaa pembeni ya
kaka yake. Akaonekana kama ana kitu anataka kumwambia. James akamwangalia. “Vipi?”
Nanaa akacheka kisha akainama. “Unataka tutoke tukaongee hapo nje?” James
akauliza. Nanaa akatingisha kichwa kukubali. “Sasa si umuache mwenzio amalize
kula?” Mamaa G akaingilia. “Chakula hakitapita huyu. Namfahamu akiwa na jambo
lake. Twende.” James akaweka kijiko kwenye sahani, akasimama na dada yake.
Wakatoka nje, wakakaa barazani.
“Ni
nini?” James akamuuliza. “Namuhofia Zinda.” Nanaa aliongea kwa sauti ya chini,
lakini Danny ndani akaanza kucheka kwa sauti. “Yaani Danny ni mbea wewe mume
wangu! Sasa si ungenyamaza tu?” Grace naye alikuwa akicheka. James naye akaanza
kucheka. “Mimi naona mje tu mmalizie hayo mazungumzo humu humu ndani. Dada yako
hajuagi kunong’ona huyo!” Mama G akaingilia kila mtu akaanza kucheka, mpaka
Geb.
“Kweli
tena James mwanangu. Nanaa hajui kunong’ona hata. Sisi wote tulijua tutasikia
tu.” Nanaa alikuwa akicheka. James akamshika mkono wakarudi ndani. Bado James
alikuwa akicheka. “Bwana mimi sipati picha! Zinda lazima akumind Nanaa.
Umemkataa! Tena alishakuwa amekununulia bangili za dhahabu, ukaenda kuzaa na
Geb!” Danny aliongeza kichochezi. “Mimi sikujua kama alininunulia!” Nanaa akajitetea
nakufanya watu wazidi kucheka. “Kwa hiyo ungejua kama amekununulia bangili za
dhahabu, ungemkubali?” Danny akamuuliza. “Akuuu!” Nanaa alikataa kwa kupandisha
mabega juu. Watu wakazidi kucheka.
“Yaani
sijui utamwambia nini Zinda! Maana zile sababu zako ulizompa, ni kinyume kabisa
na ulichoenda kufanya!” Danny alizidi kumuogopesha. “Sio mimi ni Geb huyo!”
Hapo mpaka Grace alipaliwa. Mama G, ndio alikuwa akicheka mpaka machozi. “Acheni
kumuogopesha mpenzi wangu jamani. Zinda alikuwa akijua tokea zamani kuwa
nilikuwa na nia ya dhati kwa Nanaa. Kwanza nilikuwa nikimshangaa alivyokuwa
akihangaika na Nanaa wakati alijua wazi mimi ndio nilikuwa na nia naye. Wala
usiwe na wasiwasi Nanaa. Hakuna baya ulilolifanya. Rafiki zake James wote
walikuwa wakijua nilikuwa nakufuatilia tokea tupo Iliboru sekondari. Tena kuna
kipindi mpaka Malii akaniulizia juu yako. Kwa hiyo wanajua sana.” Geb akamtuliza.
“Afadhali.
Maana nilikuwa naogopa kweli. Nilisema wasije wakakuona wewe umewasaliti.
Wakati ni mimi mwenyewe niliamua.” Nanaa aliongeza taratibu kama anayefikiria. “Wala
msingemtuliza huyu. Aliyemwambia amdanganye mwanangu Zinda ni nani? Mngemuacha
Zinda aje amsute.” “Mwaya mama sijui yukoje! Saa nyingine anakuwa rafiki yangu
saa nyingine ananirusha roho!” Kila mtu alicheka. “Ule uongo wako kwa Zinda
mwanangu, ndio huo unaniuma mimi.” “Hayo mambo ya kale mama. Sasa hivi kuwa
upande wangu mimi.” “Nimgeuke Zinda mwanangu aliyeingia mpaka deni la kununua
dhahabu!?” Nanaa akacheka sana.
“Yaani
kumbe mpaka alikopa?Asingefanya hivyo!” Nanaa alizidi kucheka na kufanya
wengine wacheke zaidi. “Kumbe je? Si anakupenda.” “Mimi nilishasema Zinda
simpendi. Kwanza anakunywa pombe. Mimi sipendi harufu ya pombe. Muulizeni hata
kaka.” Kila mtu akacheka. “Sasa si ungemwambia mwenyewe?” Mama G, akamuuliza. “Hata
mimi nimemuhurumia Zinda. Amehangaika kweli, halafu akaja kuambiwa shule
kwanza! Hata mwezi haujaisha, nashangaa Geb amekubaliwa!” Danny aliongeza Nanaa
akazidi kucheka huku amejificha uso.
“Mimi
Geb ndio nilikuwa namtaka tokea mwanzo.” Nanaa akajibu, nakufanya mpaka James
acheke na kushangaa. “Nanaa!?” “Kweli kaka. Wala sio Zinda.” Nanaa alizidi
kujitetea. “Haya dada yangu. Mimi nitamalizana na Zinda. Wala usiwe na
wasiwasi.” James akamalizia. “Asante kaka yangu. Angalau nikikutana naye
nitakuwa sijifichi.” Viliendelea vicheko kati yao mpaka James alipoaga. Aliondoka
kila mtu akajua ameridhika.
Penzi lililokusudiwa na kusubiriwa kwa hamu!
Penzi
la Nanaa na Geb ndio likaanza rasmi. Moto uliokuwa ukiwaka ndani yao, ni wao
wawili tu ndio walijua. Muda wa kitandani ukawa mfupi. Hilo wote walikiri na
kulalamika kunapambazuka mapema, na weekend haina huruma kwao. Iliisha bila wao
wawili kufaidi vilivyo. Nanaa alikuwa akisubiri muda wa kurudi kwa Geb
nyumbani, kana kwamba anasubiri kutunukiwa ulimwengu wote! Kila alipowasili Geb
kutoka kazini, alianza mabusu kwa Nanaa, popote atakapomkuta binti huyo. Na
hayakuwa mabusu ya sekunde kadhaa, mabusu yakumtoshea. Kisha wataongozana
kwenda kuoga. Haijalishi muda. Huo wakati atakao fika Geb, ndio wakati wa kuoga
kwao. Napo hapakuchukua muda mfupi. Mpaka wapangaji wao walikuwa wakiwasahau
kama wapo humo ndani. Wakipandisha juu, watatumia muda wakutosha, ndipo Geb
atashuka chini kuzungumza na mama yake na watu wengine.
Geb
awapo nyumbani, alikuwa nyuma ya Nanaa wakati wote. Atamshika na kumkumbatia.
Hata akiwa yupo kwenye sinki la jikoni, basi Geb atamfuata na kuanza kumpapasa
pale anapoweza au kuzungumza naye. Ilimradi tu mikono yake iwe juu ya mwili wa
Nanaa. Muda mwingi walitumia chumbani. Na kwa kuwa muda mwingi Oliva alikuwa na
bibi yake, basi Nanaa alikuwa huru. Jumbe za mapenzi na simu za kujuliana hali
kilikuwa kitu cha kawaida sana kwao. Muda mwingi walikuwa waki chat. Wakati Geb
yupo kazini, Nanaa yupo nyumbani.
‘Umevaa nini
sasa hivi?’ ‘Upo wapi sasa hivi?’ ‘Piga picha nikuone.’ ‘Nina hamu na wewe!’
‘Asubuhi muda ulikuwa mfupi, bado nakuhitaji.’ ‘Naomba kusikia sauti yako.’
‘Liv ananyonya? Naomba kuona.’ ‘Nikirudi sasa hivi, tunaweza hata kupata nusu
saa tu tukiwa peke yetu?’ ‘Tengeneza mazingira ya kumuachia mama mtoto. Nakuja
nipo njiani, nikukute chumbani.’ ‘Kumbuka leo ni ijumaa, Nanaa. Hakikisha
unalala mchana. Ili usiku tupate muda wa pamoja.’ ‘Na wewe hakikisha
hujichoshi.’ Hizo zilikuwa jumbe zisizoisha kati yao.
~~~~~~~~~~~~~
“Mimi
naona huyu James alete tu hizo taratibu za mahari. Watu walipe hiyo mahari,
tupumzike.” Geb na Nanaa wakacheka. Grace aliwakuta jikoni wanapeana mabusu
mfululizo. “Halafu mimi nashauri honeymoon ya hata mwezi mzima. Angalau kuwe na
amani humu ndani.” Danny alidakia akiwa nje ya jiko. “Mimi pia nitachangia hiyo
honeymoon. Wakae hata miezi 3. Watu tupumzike! Maana jikoni hapafikiki, wenye
nyumba kutwa wamekumbatiana. Ukisema ukakae barazani, na wenyewe wapo
wamepakatana. Ukipita koridoni, na wenyewe wapo wamekumbatiana!” Geb na Nanaa
wakazidi kucheka.
“Sasa
nikienda honeymoon miezi 3, si tutarudi tumekuwa masikini?” “Kwani hata sasa
hivi kuna unachokifanya kule ofisini?” Grace akauliza. “Grace unapata dhambi
wewe!” Geb akashangaa. “Kutwa upo kwenye simu Geb. Mpaka sekretari wake
amehamishia kazi zake kwangu. Na akianza simu zake kwa Nanaa, hataki mtu aingie
ofisini kwake. Basi kama kuna kitu cha muhimu, inabidi yule mama aje anifuate
mimi, mimi ndio niingie huko ofisini kwake. Siku hizi anasaini cheki bila hata
kuuliza maswali kwa kuwa akili zote zipo nyumbani. Dakika moja yupo, dakika ya
pili anakugongea ofisini anakwambia anatoka kidogo. Ukipiga simu nyumbani,
unaambiwa yupo chumbani na Nanaa. Bora aoe, aende akapumzike labda akirudi
akili itakuwa imetulia.” Grace aliongeza.
“Hapa
nyumbani napo kazi ni hiyo hiyo. Simu mkononi kila wakati. Sasa iite, halafu
yeye yupo mbali. Utamuonea huruma. Unaweza ukadhani atavunja mguu.” Mama G
akaongeza. “Sasa unakuta mwenzio ameacha kazi zake zote, anakupigia wewe! Lazima
kuheshimu hilo.” “Mmmh!” Mama G akaguna, kila mtu akacheka.
Mwenye Kisu Kikali, Ndio Mla
Nyama.
Mambo hayakwenda kama alivyotegemea James na kina Magesa. Zinda alilalamika sana kuwa Geb ametumia pesa yake au utajiri wake kumnyang’anya mwanamke wake. Ambaye ni Nanaa. Alilalamika bila kuchoka. James alipoona wameshindwa kuelewana na Zinda ikabidi kumuita Danny. Wakakutana na Zinda baa. Danny akaanza kumkumbusha tokea zamani. “Unakumbuka wakati tupo “O” Level? Kipindi James anaenda kwao kumwangalia Nanaa? Geb ndiye aliyekuwa akimwandikia masomo yote darasani kama anakosa vipindi. Na yote hayo alifanya kwa ajili ya Nanaa.” Danny akatetea. “Kwani mimi sikumsaidia James wakati tupo shuleni? Mlijua kuwa nafanya kwa ajili ya nani?” Zinda aliuliza akiwa na hasira. “Au leo ndio mnajidai kuniruka sababu sina pesa kama Geb?”
“Hapana
Zinda. Wewe unajua mimi ni mtu wako!” Danny alijaribu kumtuliza. “Acha
kunidanganya Danny. Umemuoa dada yake, lazima utamtetea tu.” “Simtetei Geb! Kumbuka
vile Geb alivyoendelea kumfuatilia yule mtoto kwa karibu hata alivyokuwa India?
Hakuacha kumfuatilia.” “Wewe unajuaje kama na mimi sikuwa nikimfuatilia?” “Sema
umekasirika tu Zinda. Lakini sikumbuki wewe binafsi kumuulizia Nanaa kwangu
kama Geb.” James akaingilia.
“Utaacha
vipi kutetea wakati dada yako anaolewa kwenye neema, James? Unajua atafia
pazuri kwenye majumba ya maana sio mimi. Lakini kumbukeni mimi nimekuwa na
nyinyi tokea zamani sana. Geb alishawaacha hapa akaenda kusoma nje ya nchi,
mimi nilikuwa na nyinyi. Danny wewe tumekuwa kama ndugu. Mama yangu mimi ndio
mama yako wewe. Leo pesa inakutoa ubinadamu unaniruka! Sikuchagua kuwa
masikini.” “Acha hizo Zinda!” “Kwani uongo? Tuambizane ukweli sisi wote hapa.
Kama mimi ndio ningekuwa Geb, nina pesa kama alizonazo Geb. Kila mkiwa na shida
ninawakopesha. Na Geb angekuwa mimi. Leo mngenifuata kunituliza wakati
amenichukulia mwanamke wangu?” “Hapo unatutukana Zinda!” James akaingilia.
“Hapana.
Kuweni tu wakweli. Nanaa ananikataa mimi kwa kuwa sina pesa. Na James umeamua
kumpa baraka zako Geb kwa kuwa unajua undugu utakolea, atakusaidia popote
ukikwama. Na..” “Nisikilize Zinda. Najua umekasirika. Lakini unapokwenda,
unakaribia kuvuka mipaka, na sitaruhusu. Huwezi kumtukana dada yangu. Huwezi
kusema amempendea Geb pesa.” “Kwani uongo? Alinikataa mimi kwa kunidanganyia
maswala ya shule. Mimi nimekaa nimetulia, sijatafuta hata mwanamke! Namsubiri
Nanaa amalize shule tuzungumze naye tena. Kumbe alikuwa akinitoa njiani tu na
nyinyi wawili mkinikejeli!” “Kivipi Zinda!?” Danny akauliza.
“Sio
nyinyi wawili niliowashirikisha nia yangu kwa Nanaa? Mlijua ninaingia deni la
pesa nyingi tu kwa ajili ya Nanaa. Mlijua nimekopa pesa yakumnunulia Nanaa
vitu. Danny ulinisindikiza mpaka kwa sonara. James na wewe ukaungana na sisi
kwenda kununua nguo, viatu na vitu vingine! Tena mkijua ni kwa pesa niliyokopa!
Hamkusema kitu! Mlinyamaza kimya. Kumbe James unang’ata meno. Hunitaki mimi
mkopaji. Unataka dada yako akaolewe na tajiri!” “Zinda jiangalie!” James
alimtahadharisha.
“Kwa
lipi James? Naweza nikawa masikini, pengine sijui hata kutongoza lakini si
mjinga. Unakumbuka wakati tupo njiani kwenda Marangu niliwaomba nyinyi wawili
mnisaidie kuniunganisha kwa Nanaa? Haswa wewe James. Nilijua wazi hakuna
utakachomwambia Nanaa, asikusikilize. Lakini ukajibaraguza kama mtoto wa kike
ili tu kunikwepa huku ukimsogeza mdogo wako kwa Geb. Umemtoa kwako
ukamuhamishia nyumbani kwa Geb ili tu akambebee mimba Geb, kisha wapate sababu
ya..” James alirusha ngumi ikampata Zinda sawia.
Danny
alisimama kwa haraka akamshika James. “Nakwambia ukweli ndio maana unakasirika
James. Ubinadamu unakuisha wewe na dada yako sababu ya pesa!” James alitaka kumrukia tena, lakini Danny
akamshika kwa nguvu. Kelele zilifanya watu wengine waanze kuwatizama na kutaka
kujua kulikoni, lakini Danny akamvuta James nje. “Naomba ondoka James.
Tafadhali sana. Ondoka.” Danny akamsihi James. Bila kuongeza neno, James
akaingia kwenye gari yake akaondoka.
~~~~~~~~~~~~~
Katika
yote hayo Zinda hakuwa amelewa hata kidogo. Alionekana wazi ameumizwa. Danny
alirudi kule alikokuwa amemuacha Zinda. Akakuta ameshaagiza bia. “Tumetoka
mbali sana mimi na wewe Danny. Walishakufukuza hao nyumbani kwao, mimi
nikakupokea. Nilikukaribisha kwetu ukiwa huna pakwenda. Leo unanigeuka mimi!
Tena nikiwa nimekuomba unisaidie kumpata Nanaa!” “Zinda umekasirika. Angalia
sana maneno yanayokutoka ukiwa na hasira.” Danny akamsihi.
“Kwani
ni uongo kuwa walikufukuza?” “Sikuwahi kufukuzwa nyumbani kwa kina Geb hata
siku moja. Mimi mwenyewe niliondoka kwao kipindi kile tulipo maliza wote chuo,
sababu sikutaka kushuhudia Grace akiolewa na mwanaume mwingine. Yule mama tokea
zamani alinipokea kama mtoto wake.” “Utaacha vipi kuwatetea wakati wanakuweka
mjini? Geb ndiye anakulisha na kukulaza wewe na mkeo nyumbani kwake, utaachaje
kumtetea? Hata mimi ningelipa fadhila ya kumsogezea Nanaa.” Danny alipandwa na
hasira.
“Ila
nakutuma kwao Danny, na wewe Kibara wao usikie. SITAKUBALI hata kidogo.
Nitafanya nini na lini, hiyo mtaona matokeo. Hakika mtalipa kwa usaliti
wenu. Nyinyi wote. Nyinyi si mnapesa sasa hivi? Geb ameshakuhonga na kukusaidia
kukamilisha mjengo wako? Sasa hivi zamu ya James. Na yeye atasaidiwa
kukamilisha kinyumba chake alichokuwa akihangaika nacho miaka yote hiyo. Sasa
mimi nitawakomesha Danny. Kawafikishie ujumbe wangu. Na wewe sitaki kukuona
tena kwenye maisha yangu. Msaliti mkubwa wewe. Nenda, labda na wewe utapewa na
hilo jina la Magesa. Wewe na mkeo wote muitwe Magesa.” Danny hakutaka kujibu
kwa kuwa alikuwa amekasirika sana, akaamua kuondoka.
~~~~~~~~~~~~~
Danny
alirudi nyumbani mkewe akajua kabisa amekasirika. Aliingia isivyo kawaida yake,
akasalimia na kupitiliza chumbani. Maneno ya Zinda ya kumkashifu kuwa anatuzwa
yeye na familia yake, na Geb, yalimuumiza sana. Yaliharibu akili zake na
kuchafukwa kabisa moyo. Kwa kuwa ni kweli alikuwa akiishi nyumbani kwa Geb.
Tokea wahamie hapo kwa mara ya pili hakuwa hata akikumbuka lini alinunua
chakula hapo ndani. Hata chumvi! Aliamka akakuta chakula kimeandaliwa, na
aliporudi jioni alikuta chakula mezani. Yeye na familia yake walikula na kusaza
hapo ndani bila hata kufikiria mara mbili.
Leo
Zinda ameibua kitu kipya. Ikamfanya ajifikirie. “Kumbe ndivyo jamaa wote wanavyonisema hivyo!” Danny akawaza,
akiyachukua maneno ya Zinda kama ndio kauli ya kila mtu. Akajidharau sana.
Akajua wenzake wote wanamsema hivyo kuwa anatunzwa na Geb. Aliumia zaidi kwani
kwa sehemu ilikuwa ni kweli. Lakini ni kwa ajili ya maisha waliyokuwa wakiishi
hapo. Waliishi kama ndugu bila kuhesabiana. Wewe fanya hiki, mimi kile,
ilimradi siku iende warudi nyumbani wakutane wacheke.
Lakini
haikuwa hivyo kwenye macho ya Zinda rafiki au kama mtu wa karibu sana kwa
James. Aliibua kitu cha tofauti ndani ya Danny, tena hakutegemea wala hakuwa
tayari kwa wakati ule ambao mkewe anakaribia kujifungua na hawana msaada wa
msichana wa kazi. Akajuta hata kwa nini alimkubalia James atoke naye mapema
kazini kwenda kuzungumza na Zinda. James na Danny walitoka kwenye hicho kikao,
Zinda akiwa amewachafua mioyo yao vibaya sana. Aliwadhihaki na kuwakashifu kila
mmoja kwa vile alivyowajua na akagonga msumari palepale, kuhakikisha anawafunga
midomo na wao waonje maumivu anayojisikia.
~~~~~~~~~~~~~
Grace
alimuona vile mumewe alivyoingia, wakaangaliana na mama yake. Grace akageuka
kulia na kushoto, kutafuta balance ya kusimama huku akigugumia akiashiria
anafanya kazi ngumu mpaka akafanikiwa kusimama. Hata hivyo alikuwa amechoka.
Ndio na yeye alikuwa amerudi nyumbani kutoka kazini. “Hiyo siku ya kutoa hawa
watoto huko tumboni, naisubiri kwa hamu sana!” Mama yake akacheka. “Waache
wakomae wajukuu zangu!” “Basi ujue mwanao ndio nazidi kukoma. Heri uniombee
watoke tu. Watakomaa hukuhuku nje.” “Siku zimebaki chache. Jikaze.” “Mmmh!”
Grace akaguna huku akielekea chumbani kwao.
Aliingia
chumbani akamkuta mumewe anasoma jumbe kwenye simu yake huku anatingisha
kichwa. “Kwema?” Grace akauliza huku akipapasa tumbo lake. Akajivuta mpaka
alipokuwa amesimama mumewe. “Vipi? Mbona macho kwenye simu hata huniangalii!?”
Grace akauliza kwa kulalamika. “Samahani bwana. Nahisi nimechanganyikiwa. Vipi
nyinyi? Mmeshindaje?” Danny akamgeukia mkewe, akamgusa tumbo.
“Tupo
tu.” “Umeweza kunywa maji?” Danny akamuuliza mkewe. “Ndio ilikuwa kazi ya leo
hiyo. Mama kila akipiga simu ananikumbusha kunywa maji. Angalau nimepitisha
lita mbili. Ila mbavu zinauma!” “Pole. Lakini si ndio siku za lala salama
hizi?” “Mmmh! Bado. Ndio nimeanza mwezi wa 9!” “Utafika tu mama. Jikaze.” Danny
akambusu mkewe. “Nini kinakuchanganya?” Grace akauliza. “Wewe ingia huko kwenye
group letu la Whatsapp, utajionea na kujisikilizia mwenyewe.” Danny
alijibu wakati anajitupa kitandani na viatu vyake.
“Vua bwana viatu Danny! Wewe ndio umemfundisha Fili! Anacheza na viatu kitandani!” “Wewe soma hizo jumbe humo ndani ya group, ndio utajua kwa nini napanda na viatu kitandani.” “Kaniletee basi simu yangu. Nimeacha sebuleni.” “Basi tumia ya kwangu.” “Sitaki bwana Danny! Nenda kaniletee yangu. Nikianzia kusoma kwenye yangu ndio vizuri.” Danny akatoka, akakutana na Geb naye anasoma huku akitingisha kichwa. “Njoo huku huku sebuleni Grace. Nilitaka kumficha Geb, lakini naona ameshapata ujumbe wake.” Danny akamuita mkewe. “Kuna nini tena!?” Akauliza mama G, baada ya kutoka chumbani kwake akiwa na Oliva na Fili. Nanaa alikuwa ameinama wakati anasikilizishwa jumbe alizojirikodi Zinda na kutuma kwenye group.
Alia Wivu!
Hasira
ya Zinda ikaendelea. Akaanza kusambaza sumu ya chuki katika kundi lao la
marafiki. Wale waliokuwa pamoja tokea wapo sekondari mpaka sasa wakiwa wameoa.
Lilikuwa kundi kubwa tu. Kwani walitafutana baada ya chuo kuisha wakawa
wakishirikiana. Waliongeza hata wake zao kwenye kundi hilo. Kwa hiyo kama
kulikuwa na jambo lolote lile, liwe la kheri au la simanzi, walishirikiana na
kuwasiliana kwa kutumia kundi hilo. Wakaweza kukutanika mara moja na
kushirikiana kwa wepesi. Na Danny ndiye aliyekuwa kiongozi wao.
Zinda
alijirekodi kuanzia mwanzo wa mahusiano yake na watu wote waliokuwepo mle
ndani. Alieleza vile alivyojua wao ni ndugu. Wakisaidiana bila hila. Akaeleza
vile alivyojitoa kwao, hata pale Geb alivyokuwa hayupo kwenye maisha yao,
lakini yeye alikuwepo. Zinda alieleza kusikitishwa na usaliti wa watu waliopo
humo ndani. James na Danny ambao waliheshimiana sana. Akaeleza vile walivyojua
tokea mwanzo anakusudia kukopa na wakajua amekopa pesa nyingi kwa ajili ya
kununua zawadi za Nanaa. Aliwakumbusha watu wote mle ndani juhudi zake zote
safarini kuelekea Marangu mpaka walipofika Marangu. Wao wakiwepo, na Geb
akiwepo na Liz. Tena walilala chumba kimoja kama wapenzi.
Akawakumbusha
usaliti wa familia hiyo kwa Nanaa. Jinsi walivyomdhalilisha kule Marangu na James
kuonekana kukasirishwa na kitendo kicho. Akawakumbusha ule mkasa mzima. Nanaa
hakuwa hata amejua kama kulitokea ugomvi alipoondoka Marangu, ndio siku hiyo na
yeye akasikia hapo kwenye malalamiko ya Zinda. Akanyanyua uso kumtizama Geb,
lakini Geb hakutaka kukatiza. Akataka kuendelea kusikiliza rikodi hiyo ya
Zinda.
Zinda
akamlaumu sana Geb kutumia mali zake kumnyang’anya mwanamke wake. Tena watu
wote kwenye hilo kundi wakijua hilo. Aliendelea kusema wakati Geb akimfaidi
Liz, yeye Zinda kwa mara ya kwanza akaonyesha nia ya kuwa na mtu wake maishani.
Akataka kutulia na Nanaa.
Zinda
anasema yeye anafahamika kuwa hakuwahi kuwa na mwanamke wa maana. Au
aliwakumbusha wote kipindi anamtongoza Nanaa, hakuwa na mwanamke. Ila Geb
alikuwa na Liz. “Kwa kutumia pesa zake, Geb
amehakikisha mimi ambaye sina kitu. Sina mwanamke, ananichukulia mwanamke
wangu. Leo Danny na James kwa kuwa wananufaika na pesa ya Geb, wanatoa baraka
zao kwenye ukatili kama huu! Wanasema Geb alimpenda Nanaa tokea zamani wakati
wote tulishuhudia Geb akimkana Nanaa mbele yetu wakati tupo Marangu! Geb alikuwa
akilala na Liz wakati Nanaa alikuwepo! Mimi nahangaika kumtongoza Nanaa, na
kumfanya awe wangu, Geb akiwa anamsaidia Nanaa na kaka yake, kimali,
akanipokonya mwanamke wangu.” Zinda
aliendelea kwenye rikodi yake.
“Ubinadamu
unawaisha watu niliohesabu kama ndugu sababu ya pesa! Danny akiwa kama kiongozi
wetu na ndugu yangu mimi wa karibu, leo sababu ya kutunzwa hapa mjini yeye na
familia yake na Geb, anaamua kufumbia macho hilo, anamtetea Geb! Anasema Geb
alimpenda Nanaa tokea mwanzo! Mbona sikumuona Geb akimsubiria Nanaa? Akaendelea
kuwa na mahusiano ya wanawake watatu tofauti tofauti! Tena mmoja alitaka mpaka
kujiua kwa ajili yake wakati tupo chuo kikuu cha Mlimani! Najiuliza mapenzi
hayo kwa Nanaa alianza lini wakati Nanaa alikuwepo kabla ya wanawake wote hao
kuwepo kwenye mahusino na Geb? Ni kipi kigumu watu wameshindwa kukiona na kuwa
wawazi? Jamani pesa ya Geb isitufumbe macho na kusahau mambo!” Akaendelea kulalamika akisikika na uchungu mwingi.
“Ni juzi juzi
tu, kwenye harusi ya Malii, huyu huyu Geb mwenye sifa ya kutosahau, alimsahau
na kumuacha nje ya ukumbi mwanamke anayesema anampenda! Akapigwa na baridi
zaidi ya masaa manne mpaka Nanaa akaugua karibia kufa! Nanaa aliugua na sisi
tukimuuguza bila familia hiyo ya matajiri, kina Magesa. Eti gafla leo James na
Nanaa wamelisahau hilo!” Zinda akaendelea.
“Kweli leo Geb
haoni hata aibu kutudanganya sisi watu tunaomjua kabla hata hana kitu! Tena akiwa
masikini wakutupwa, kama paka la mtaani tu anadanganya bila aibu! Anadiriki
kusema anampenda Nanaa! Anamchukua
mwanamke wangu wakati nyinyi wote mnajua nilikuwa nikisubiri Nanaa amalize chuo
nizungumze naye tena! Mpaka leo nimetunza zawadi nilizomnunulia Nanaa na ni
mwezi uliopita tu ndio nimemaliza kulipa deni ya pesa niliyokopa kununulia
zawadi hizo! Na nyinyi wote mnajua! Lakini mnashindwa kuwa upande wangu mimi
ambaye sijawahi hata kuonekana na mwanamke! Leo mnakuwa upande wa Geb
aliyekwisha kuwa kwenye mahusiano tena yakueleweka na wanawake wengine, tena
hata Nanaa mwenyewe akiwepo! Kama sio upendeleo wa waziwazi tu sababu ya pesa
yake ni nini?” Zinda aliendelea kulalamika.
“Mapenzi gani
hayo ya dhati kwa mwanamke huyu, huku ukitaka kujiua kwa mwanamke yule!? Geb
anatumia pesa yake kukandaniza watu. Aliyempa yeye pesa, ndiye aliyetunyima
sisi. Na kwa kuwa ni Mungu, basi Mungu atatuhukumu kwa haki. James mpe dada
yako huyo Geb, lakini nakuhakikishia, pesa sio kila kitu. Mtanikumbuka tu. Upo
umbali nimeshakwenda na nyinyi, nina uhakika Geb hawezi kwenda na nyinyi. Danny
wewe ni mnafiki, ndumi la kuwili. Na Mungu atakulipa kabisa. Najitoa rasmi
kwenye maisha yenu. Sitaki tena mnitafute. Sitaki kupigiwa simu na yeyote.
Nyinyi mliojaliwa unafiki endeleeni kuwakumbatia hao kina Magesa ili waendelee
kuwakopesha pesa. Wengine hatukujaliwa unafiki. Na tutawaona mtakapoishia na
hao kina Magesa. Wakiwageuka, msinitafute. Na yatakayowapata pia, msinitafute. Leo
ndio mwisho wenu na mimi.” Zinda akamaliza
rikodi yake.
Akaongeza na baadhi ya jumbe
zakuzidi kulalamika. Na kutukana watu wa mle ndani. Tena kwa majina.
‘Najua hata
Malii utatetea kwa kuwa nusu ya bajeti yako ya harusi alibeba Geb. Hata gauni
la harusi la mkeo, yeye ndio alilinunua, wote tunajua.’ Ujumbe huo ukawa wa Malii. ‘Danny wewe ndio siongei kabisa. Kwa kuwa mnalishwa na kulala bure hapo
kwa Geb. Una kazi yakupiga picha vyakula unavyolishwa na Geb, na kuturingishia
sisi mboga moja. Hata mimi ningelipa fadhila. Lazima uwe upande wake.’ Na huo ujumbe
nao akaurushia kwa kundi.
‘Na wewe James,
najua unafurahia kuwa Neema imemshukia dada yako. Kwamba na wewe
utaponea hapo hapo. Labda atakusaidia kumalizia kile kijumba chako ulichokuwa
ukihangaika nacho miaka yote. Unamshikilia vizuri ili akutoe kwenye nyumba za
kupanga. Lakini wanaume sisi tunapambana kivyetu. Hata kama hatujateremsha
magorofa hapa mjini. Tunakula na kulala makwetu. Hatufungwi macho na pesa.’ Akatuma ujumbe mwingine.
‘Na wewe
Jerome. Mzee wa kuchomekea. Kutaka makuu, pesa huna. Najua lazima utatetea tu
kwa kuwa Geb anakudai na huna mpango wa kulipa pesa yake. Lakini ujue wazi mkeo
anajitongozesha kwa Geb. Masela wanakuchora tu. Wote wanajua kuwa mkeo anamtaka
Geb. Kundi limejaa unafiki. Wanashindwa kumwambia ukweli, wamebaki kukucheka
pembeni wewe na mkeo.’ Na huo nao akaurushia hapo
kundini.
‘Na wewe Tuli,
jamaa kashakuonyesha hakutaki. Acha kujichekesha kwake kwa mambo ya kipuuzi.
Najua hata hili utataka kumfariji nalo kwa cheko lako lakijinga. Fungua macho
uone na ujue majira. Tafuta mwanaume wako akuoe. Acha kuomba omba ujinga na
kujikiria Geb ni mumeo. Geb alishakiri kwetu hajawahi kuwa na wazo na wewe wala
hana mpango na wewe. Kama masela wangekuwa waungwana wangeshakwambia.
Wanakuchora tu. Tena wanasema unamtakia vijisenti vyake.’ Huo nao Zinda akaurushia hapo hapo.
“Anaandika
ujumbe mwingine. Ngoja nimtoe kabla hajazidi kuharibu.” Danny alipoona
anaandika tena, akaamua kumtoa kabisa kwenye kundi kabla hajatuma ujumbe
mwingine na kuzidi kuchafua watu. Akatulia. Yeye Danny ndiye alikuwa akiwasomea
wote pale sebuleni. Wakawa wanasikiliza. “Mmmh!” Grace alisikika akiguna. “Sijui
nijibu nini humu ndani!?” Danny akauliza. “Hapana. Usijibu kitu chochote. Tulia
kwanza.” Mama G akatoa wazo. Wote wakamwangalia mama yao.
~~~~~~~~~~~~~
“Nisikilizeni
kwa makini sana. Shetani anataka kuwafarakanisha. Anajua wazi kila kwenye
umoja, ndipo Mungu anapoamuru baraka zake. Someni kitabu cha Zaburi 133:1-3.”
Geb akafungua bibilia yake ya kwenye simu. “Zaburi 133:1-3 Inasema hivi, {{1.Tazama, jinsi ilivyo
vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja. 2.Ni kama mafuta mazuri
kichwani, Yashukayo ndevuni, ndevu za Haruni, Yashukayo mpaka upindo wa mavazi
yake. 3 Kama umande wa Hermoni shukao milimani pa Sayuni. Maana ndiko BWANA
alikoamuru baraka,Naam, uzima hata milele.}” Geb
akamaliza. “Nataka na Danny naye asome. Taratibu tu. Kwa makini. Neno kwa
neno.” Mama G akataka Danny arudie kusoma. Danny akasoma.
“Sijui
kama mmeshatambua hila ya muovu? Shetani ni muongo. Na hakuitwa muongo
kwa bahati mbaya. Anayoongea yanayofanana na kweli kabisa. Ni mfitini. Hawezi
kuruhusu zile baraka Mungu anazoamuru juu yenu kama mstari wa 3 kwenye hiyo
zaburi, itimie kati yenu. Hawezi. Na hatalala mpaka awafarakanishe. Danny wewe
umebeba jukumu zito sana. La kundi zima na hapa nyumbani pia. Ukiruhusu tu hayo
maneno yakuingie, ujue utavuruga umoja kati yetu na kundi zima. Sio Geb wala
wewe ambaye anaweza kufika hapo mlipo bila mmoja wenu. Geb anakuhitaji sana
kwenye maisha yake, na wewe hivyo hivyo. Siku utakapomtizama Geb kama Zinda
anavyotaka uanze leo, nawaambia kabisa, hakuna kati yenu atakaye simama. Si Geb
wala wewe Danny.” Mama G akaendelea.
“Pesa
ya Geb itakuwa na thamani tu, sisi wote tukiwa kwenye maisha yake. Na yeye
amejitahidi kutuonyesha hivyo kwa vitendo. Si kweli Danny?” “Kweli mama. Na
Mungu wangu ni shahidi. Si mtetei Geb. Amekuwa mnyenyekevu kwetu sisi wote.
Kwanza hazungumzi.” “Nashukuru kwa kuwa mkweli Danny. Nakusihi mwanangu,
usilisahau hilo, ukakubali uongo wa ibilisi. Sina utofauti kati yako wewe na
Geb. Hata Nanaa nilimwambia. Nitamlilia Mungu juu yako kama nitakavyomlilia
Mungu juu ya Geb. Haupo hapa sababu ya shida. Ni umoja na amani ambayo Mungu
alitujalia. Wewe ni shahidi. Alipita Liz hapa, alishindwa kuwa na sisi. Shetani
ameshindwa kumtumia Nanaa kututenganisha, leo anatutumia nguvu ya nje
kutusambaratisha. Msikubali.” Mama G aliongeza.
“Kwa
nini leo ndio iwe ni siku ya kujulikana mabaya yote kama kweli yalikuwepo? Kwa
nini leo ndio tukumbushwe mabaya tuliyomtendea Nanaa? Tena akiwa Nanaa mwenyewe
na kaka yake wamesamehe na wala hawajatuhesabia? Ipo hila, na msikubali.”
“Daah! Afadhali mama umeongea. Nilishafikiria kesho nirudi nyumbani kwetu na
mke wangu na mtoto. Nilikuwa najiambia nitajua mbele ya safari hapo Grace
atakapojifungua. Nikajiambia hapa nilazima nitoke.” “Basi ndio shetani angekuwa
ameshinda. Usiruhusu neno hata moja likuingie Danny. Sio kweli kama wewe unamtegemea
Geb sasa hivi. Una mshahara wako mzuri tu. Na hata mkiondoka leo, sisi tutapika
humu ndani na kutaliwa. Na hicho chumba mnacholalia kitabaki na kitanda chake
na AC itaendelea kupuliza hata kama nyinyi hamta itumia. Unanielewa Danny?”
“Nimeelewa mama.” “Basi tulia.” Danny akavuta pumzi kwa nguvu.
“Nijibu
nini kwenye group?” Danny akauliza. “Tulia kwanza. Sasa hivi kila mmoja wenu
ana hasira na Zinda. Mwacheni kwanza. Tumwiteni Mungu ataingilia kati hii
hali.” Nanaa alibaki ameinama tu. Zinda alizungumza ukweli mtupu. Tayari na
yeye akaanza kusononeka moyoni. Mama G akamwangalia.
“Nanaa!”
Nanaa akanyanyua uso akamwangalia. Tayari machozi yalishakuwa yamejaa machoni
kwake. “Unakumbuka uliniuliza kitakachokufanya usitulie sasa hivi wakati unaye
Geb na Oliva, ni nini?” Akashindwa kujibu. “Basi mambo kama haya ndiyo
yatakufanya usitulie. Shetani ameshakuona umeingia humu ndani, umetulia.
Sasa anahangaika kukufanya mateka wa fikra zako. Amecheza na hisia zako.
Ameshaingiza uongo unaofanana na ukweli. Amerudisha mambo ya nyuma, aliyojua
yalikuumiza ili kukutesa. Ni kweli wote tulikukosea kwa namna moja au nyingine.
Na ukasamehe. Kwani ulisamehe sababu ya pesa?” Mama G akauliza.
“Hapana mama.” Nanaa alijibu kinyonge. “Sasa!?
Sisi wote tumekuona jinsi unavyompenda Geb. Na ulitaka kujitenga kabisa na mali
ya Geb mpaka sisi tulipokulazimisha usitafute kwako, hapa ndio kwako.” “Tena
mimi ndiye niliye kulazimisha Nanaa. Kwa kuwa mimi ndiye nakupenda.
Nilikusimulia kila kitu. Tafadhali Nanaa, usinichukie sababu ya makosa ya nyuma
ambayo Zinda anayatumia sasa hivi. Tafadhali mpenzi wangu.” Geb alimkatisha
mama yake, akapokea usukani wa kusihi. Nanaa akafuta machozi, akainama.
“Nanaa!” Geb akamuita. “Abee!” “Umenielewa?” Geb akamuuliza kwa upole. “Niamini nakupenda Nanaa, sina sababu yakudaganya. Naomba uniamini mimi kuliko maneno ya hasira ya Zinda. Zinda amekasirika tu, lakini anajua ukweli wote. Naomba niamini mimi Nanana. Tafadhali.” Kila mtu alijua Geb ameingiwa na hofu. Na ni mara chache sana Geb akiwa katika hali hiyo. Akajikuta amekamatwa kwenye ukweli uliotengenezewa hila kali ya kumuaminisha yeyote yule hata ambao walikuwa wakijua ukweli wangeweza kubadili walichokuwa wakikifahamu na kuelewa ukweli mpya wa Zinda na kumuona kweli Geb ni mbambaishaji tu. Sio mkweli. Zinda alimbana Geb kwa vile anavyomfahamu mpaka Geb akatingishika na jeuri yote ikamuisha. Hata mama yake akamuona. Ile haiba ya kunyamaza ikamtoka gafla akabaki akijitete akibabaika. “Tafadhali mpenzi wangu. Mimi nakupenda kwa dhati.” “Najua Geb. Nafahamu kama unanipenda. Laki…” Nanaa akaanza kulia kwa kuumia sana.
“Njoo Nanaa.” Mama G akamuita. Nanaa
akamsogelea. “Kaa hapa.” Akakaa pembeni ya mama G. “Niambie chochote kile
unachosita kuongea.”“Mimi najijua nina
mkosi mama. Naona nimeanza kumuingizia Geb na Oliva pia! Hawa watu walikuwa
kwenye umoja mzuri tu. Ona mimi nilivyoleta machafuko! Haya, jana uliniambia
unataka Oliva abarikiwe jumapili hii inayokuja. Ukasema utamfanyia tafrija.
Mwanangu anaanza mwanzo wa maisha yake kwenye machafuko hivi! Najisikia vibaya
mama yangu.” “Usilie Nanaa. Kwanza nataka
ufute hiyo kauli kwamba wewe unamkosi. Nanaa wewe ni mbarikiwa. Maisha yako
yalianza siku ile nilipokuongoza sala ya toba. Soma bibilia Geb. Fungua 2 koritho
5:17.” Geb akaanza kusoma. “{Hata imekuwa, mtu
akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; yakale yamepita tazama! Yamekuwa
mapya.}” Geb akamaliza.
“Umesikia
Nanaa? Hata kama ulikuwa na mkosi, siku ulipomkabidhi Yesu maisha yako,
ameondoa kila kitu. Kama ulivyoaminishwa wewe unamkosi, ndivyo unavyotakiwa
kuamini kuwa wewe ni mbarikiwa. Umenielewa?” “Nimeelewa mama.” “Sasa kwa
taarifa yako tu, vita yako ndio imeanza. Kama ulifikiri kufika hapa ndio
utamaliza, basi ulikosea Nanaa. Umama ni kazi kuliko kazi yeyote ile hapa
duniani. Hivyo unavyoumia kwa Oliva kwamba anaanza kwenye machafuko, huwa
haviishi na wala havitakuwa na nafuu. Badala ya kulia, unajiweka na kusimama
kwenye nafasi yako. Ukijua wewe unaye Simba wa kabila la Yuda.
Atakupigania, hutashindwa. Faida yake ni moja tu, humtegemei shetani na kazi
zake, zenye mateso mengi. Mara kwa mganga wa kienyeji au hata kutizama mambo
kwa jicho la wengine wanavyotazama mambo. Wewe kimbilio lako ni magoti.
Kumtwika Yesu fedheha zako zote. Mlilie Mungu katika kila hali. Mwambie hofu
yako. Amuru mambo yasiyoonekana katika ulimwengu wa Roho, yadhihirike katika
ulimwengu wa mwili. Niliwaambia wewe na Geb, hamtasimama, kama hamtamtanguliza
Mungu. Umeona sasa?” Mama G aliwaangalia wote.
“Mungu
pekee awe kimbilio lenu Nanaa na Geb, ndipo mtaweza kusimama. Mtajaribiwa sana,
lakini mkimtanguliza Mungu mtashinda tu. Unanisikia?” “Nakusikia mama, lakini
mimi nataka Liv abarikiwe hiyo jumapili kama ulivyopanga mama! Hata kama watu
wasipokuja, sisi wenyewe tutatosha. Na kaka James.” “Safi sana. Hayo ndiyo
mambo. Maisha yetu hayasimami sababu za hila za ibilisi. Tunasonga mbele.
Nitazungumza na mchungaji. Sasa hii itakuwa tofauti. Si Nanaa unaniruhusu
kufanya kile ninachotaka na Oliva.” “Chochote mama yangu. Wewe fanya kile
unachojua kitampendeza Mungu. Si ni sawa Geb?” Nanaa akamgeukia Geb. “Sawa.”
Geb akakubali.
“Basi.
Nashukuru. Sasa huyu shuguli yake nataka iwe tofauti. Tumuombee baraka,
kwa kuwabariki watoto wengine. Geb utaenda kituo kile cha watoto yatima
kilichopo pale Mwenge. Nataka ukazungumze na uongozi. Waombe wakuandikie
mahitaji yao yote. Hata kama ni ujenzi wa kitu, wewe waambie waandike tu.
Tukishapata mahitaji yao yote. Tutakuja kukaa hapa kama familia. Tutachagua
vitu tutakavyoweza kufanya sasa hivi. Kabla ya jumapili, tutawapelekea. Ndipo
tukamuombee Oliva baraka kwa Mungu siku ya jumapili halafu tutaenda kula
chakula na hao watoto yatima hiyo siku ya jumapili.” Nanaa akaanza kucheka.
“Ndio
maana nakupenda mama yangu.” Wakacheka kidogo. “Halafu mahitaji mengine
yatakayo baki, tutamwamini tena Mungu kukamilishia hicho kituo, wakati tunaenda
kutoa sadaka ya shukurani wakati hao wakina kaka wakishazaliwa. Au unasemaje Danny?”
“Maana nilishaanza kuona wivu!” Danny akajibu. Wakacheka. “Ni wazo zuri sana
mama. Tumekuwa tukitapanya mapesa huko kwenye birthday zao hawa! Kwanza hata
wenyewe hawaelewi! Bora hata umri wa Fili huo.” Danny akaongeza.
“Na
kama tukiweza kumaliza mahitaji yote, sasa kwa wanangu wakizaliwa tutawapelekea
nini?” Grace akahoji akionyesha wasiwasi kidogo. Gafla wazo la mama G likawa
lamaana kila mtu analitaka. “Grace, hao watoto ni yatima. Wanaishi kwa
kusaidiwa tu na watu. Hawawezi kuishiwa mahitaji yao kwa msaada wa mara moja tu.
Hata kula yao ni ya msaada. Sidhani kama wanawadhamini wakutosha kukidhi
mahitaji yao. Usiwe na wasiwasi. Huu ni mwanzo tu. Na kila jambo tujue Mungu
anatuletea kwa wakati. Tushirikiane sasa hivi tukamilishe hili la hiyo jumapili
na tuendelee kufanya ili kuwafundisha Fili, Oliva na wadogo zao, kujali
yatima.” Danny na Grace wakaridhika.
“Mama!
Kibinafsi mimi nakushukuru kwa kweli. Sikuwahi kujiona nina upungufu wa wazazi
tokea nimekuwa na wewe. Umeniongoza vizuri sana. Nakiri bila wewe, pengine
nisingekuwa hapa. Sijui kama unakumbuka wakati nataka kuacha chuo ili nitafute
kazi nimtunze mwenyewe Grace?” “Nakumbuka Danny mwanangu.” “Lakini ukataka
nivumilie, huku ukinihudumia kwa jasho lako, kama ulivyofanya kwa Geb, mpaka
nikamaliza shule yangu. Ni kweli upendo wako kwangu ni kama wa Geb tu. Kwa muda
mfupi nilichanganyikiwa. Zinda akanichanganya kabisa. Lakini nimekaa hapa sasa
hivi, ni kama Mungu amenirudisha hatua kwa hatua. Akanionyesha jinsi
ulivyohangaika na mimi bila kuchoka. Tena nikiwa mkorofi kuliko hata watoto
wako ulio wazaa.” Grace na Geb wakacheka. “Kweli! Si mimi mwenyewe najijua.
Nakushukuru mama yangu. Asante kunituliza.” Danny alisikika akiwa ametulia
kabisa.
“Basi
na mimi namshukuru Mungu kwa hilo. Haya, njooni wote tushikane mikono tuombe.” Wakasogea
wakashikana mikono mama G akaongoza maombi. Alianza kwa kutubu. Aliwatakasa
wanae kwa majina. Kila mmoja wao akiowaombea toba na utakaso. Akaomba amani
iliyokuwepo kati yao, iendelee kudumu. Akabariki kazi za mikono yao kila mmoja
wao. Akamuombea Fili, Oliva na watoto walioko tumboni mwa Grace na wengine
watakao kuja. Akaomba hekima juu yao yakupambana
na changamoto zote zitakazo wakabili maishani. Kisha akaomba ulinzi juu yao.
Wakamaliza wote wakiwa wametulia.
~~~~~~~~~~~~~
Baada
tu ya maombi Geb akamgusa Nanaa. “Naomba twende tukazungumze.” Nanaa
akatingisha kichwa kukubali. “Naomba Nanaa anyonyeshe kwanza.” Wakacheka. “Mara
moja tu, tutarudi!” “Hapana Geb. Mimi nawajua nyinyi. Hamtarudi leo. Huyu mtoto
lazima ale ndio arudi kulala, hawezi kusubiri.” Mpaka Grace akacheka, Geb
akatingisha kichwa. “Mama anakosa imani na Geb!” Danny akachokoza. “Mimi
nawajua hawa. Watakuachia mtoto hapa kwa ahadi ya kurudi baada ya muda mfupi
sana. Tena Geb ndio ataingia hapa anakimbiakimbia akijifanya anaharaka, anataka
akazungumze kitu kwa muda mfupi tu na Nanaa. Basi wapandishe hizo ngazi!
Hutakaa ukawaona tena. Na yeye mtoto wa watu asivyo na makuu, analala kimya na
njaa yake. Wazazi hawa utawasikia wanacheka juu.” Geb alimtizama mama yake kama
haamini.
“Mama!”
Geb akashangaa. “Mama nini! Mwache mwenzio anyonyeshe.” “Basi na huko kazini
ndio hivyo hivyo. Utaagwa. Anakwambia anarudi baada ya muda mfupi sana.
Unamkumbusha watu watakaokuja hapo ofisini. Tena walioweka miahadi ya kumuona
labda hata siku tano kabla. Anakwambia sitakawia. Ujue usahau. Na utafute kitu
cha kuzungumza na hao wageni wake. Harudi Geb. Ukipiga simu huku nyumbani
kumtafuta, unaambiwa yupo chumbani kwake, simu kazima. Yaani hapo ndio ujue
ananifikishia ujumbe kuwa nimalizane na watu wake mimi mwenyewe. Wenye
kukasirika wanakasirika, wanaona wamepuuzwa. Wenye uvumilivu wanaomba miahadi
mingine tena ili wajaribu kama watakuja kuonana na Geb mwenyewe.” Geb akarudi
kukaa huku akitabasamu bila kukanusha.
“Basi
nanyonyesha kwanza mama!” “Au twende naye juu. Tuongee wakati unanyonyesha.”
Geb akatoa wazo. “Hapana Geb. Wewe tulia hapo kwenye kochi, mwenzio
akanyonyeshe hapo chumbani kwangu. Mtoto akishiba nyinyi nendeni kokote
mnakotaka, hakuna hata atakaye wasumbua. Haya Nanaa nyanyuka nenda.” Danny
alizidi kucheka.
“Kwani
wewe mama unahisi mtoto anaweza kwenda kulazwa bila kula?” “Yaani Danny kwa
kupenda kushabikia mambo!” Mkewe alimjua. “Si nimeuliza tu!?” Danny alizidi
kucheka. “Hapana Danny. Wewe nyamaza tu mume
wangu.” “Sawa. Lakini kwani wewe mama unahisije?” Kila mtu alianza kucheka
upyaa. “Mwanangu Danny, mimi huwa nashinda humu ndani na huyu mtoto. Acha tu
alishwe sasa hivi, nimuogeshe ndio alale. Maana wakati mwingine kama baba yake
akirudi hapa mchana, basi mwanae ndio aandike maumivu. Utasikia ‘Nanaa, njoo mara moja.’ Hapo
yeye kashapandisha ngazi yupo juu kule. Basi bibi huyu naye akishasikia jina
lake limetajwa, popote ulipo, anakuletea mtoto, au utamsikia anakwambia ‘Nimemuacha Liv hapo kitandani. Narudi sasa hivi.’ Basi huyo mtoto atalala hapo, kuja kukumbukwa na
mama yake ni baada ya baba mtu kuondoka. Utafikiri alilishwa ugali kabla ya
kuachwa.” Danny na Grace walikuwa wanacheka, Nanaa akajificha uso.
“Ni
mazungumzo ya muda mfupi tu!” “Hapana Geb. Acha hayo mazungumzo yasubiri. Haya
Nanaa, chukua mtoto, nenda kanyonyeshe.” Nanaa akasimama kwenda kumchukua
mtoto. “Labda ungempa muda kabisa wakutulia humo ndani.” Grace akamfinya
mumewe. “Ukoje Danny wewe!?” “Nazungumzia ushibaji wa mtoto Grace mke wangu! Si
unajua mawazo yakiwa yamegawanyika! Nanaa anaweza asinyonyeshe vizuri.” Nanaa akakimbilia
chumbani na mwanae.
“Wala
usiwe na wasiwasi. Atashiba tu mjukuu wangu. Hivi ninavyohangaika kumnywesha
supu huyo Nanaa, mbona atatulia hapo mpaka mtoto ashibe. Nikiridhika ndio
ataenda kwenye hayo mazungumzo.” “Mama bwana!” Danny alizidi kuchochea. Angalau
utani ukazidi. Wakaanza kucheka.
~~~~~~~~~~~~~
Mara
James akaingia akionekana amepaniki haswa. Akakuta pale ndani kumejaa vicheko,
asielewe. “Karibu James mwanangu.” “Asante mama.” Akakaa. Akamwangalia Danny,
Geb na Grace akaona wametulia na tabasamu usoni. “Mnacheka nini?” James
akauliza. “Danny anamchokoza Geb na Nanaa.” “Grace naye hana siri!?” “Umezidi
wewe.” “Sio wewe uliyekuwa ukitusimulia habari za Geb hapa? Kwamba jamaa ofisi
kahamishia nyumbani? Mimi kosa langu kuuliza maswali?” “Mchochezi Danny.
Anataka kukuza visa.” Wakaendelea kubishana Danny na mkewe.
“Subirini
kwanza. Hivi nyinyi mmesikia yanayoendelea kwenye kundi?” “Kuna mapya mbali ya
yale ya Zinda?” Danny naye akauliza. “Kwa hiyo mmesikia kila kitu!?” James
akauliza kwa kushangaa. “Si nilimtoa?” “Bwana si padogo humo ndani. Liz
amemrudisha. Wamejaza kurasa za matusi. Nahisi kama nimevuliwa nguo zote.” Wote
wakacheka na kumshangaza James.
“Wameamua
kuungana?” Danny akauliza huku akicheka. “Yaani mpaka sasa hivi hapa,
wanapokezana kuandika. Hakuna walichobakiza naona wanarudia rudia.” James akaongea.
“Naombeni msimwambie Nanaa tafadhali. Itamchanganya sana.”
“Mbona anajua! Ameingia ndani
sasa hivi kwenda kunyonyesha.” Mama G akajibu bila wasiwasi. “Mbona sasa nyinyi
hamna paniki yeyote!?” James akauliza akiwa haelewi.
“Tumemuachia
Mungu.” James akakunja uso huku akimwangalia Danny. “Kweli tena James. Wewe
jiulize tu mwenyewe, shutuma zote anazokushutumu Zinda ni kweli?” “Hata kidogo
Danny! Na wewe ni shahidi. Sijamuuza Nanaa kwa Geb mimi sababu ya pesa. Kwanza
sikuwa hata nikijua kinachoendelea wakati ule wa mambo ya Marangu.
Nilimsindikiza Zinda kununua vitu bila hila nikitaka Nanaa mwenyewe aamue japo
nilijua wazi Nanaa hawezi kumkubali Zinda sababu ya pombe. Nanaa hapendi kabisa
harufu ya pombe. Na ndio maana kama utakumbuka wakati tumemsindikiza Zinda,
nilimsihi sana asubiri kwanza, asinunue kitu chochote mpaka azungumze na Nanaa.
Unakumbuka Danny?”
“Basi
mimi nilijua na wewe hicho kipengele umesahau. Nikajiuliza kwa nini pale baa
hukumkumbusha wakati analalamika na kukutukana?” “Nilikuwa nimeshakasirika,
maneno hayatoki tena. Nikaona heri nimrushie tu ngumi ya mdomo anyamaze.” James
alijibu wakacheka.
“Ujue
siku ile pale kwa sonara ulipompa lile wazo, kuwa asinunue mpaka azungumze na
Nanaa, nilitaka kukuuliza pale pale, kwa nini, lakini unakumbuka Zinda
akakubishia kwa haraka sana wala hakutaka kukusikiliza?” “Tena alikuwa mkali
haswa! Nikaamua ninyamaze nimwache na ubishi wake. Leo analaumu kwamba
tulimuacha aingie garama bure wakati nilikuwa na mpango wakumuuza kwa Geb!
Mjinga sana Zinda.” James akaongeza kwa hasira kidogo. “Kwani pesa Geb kapata
leo? Tangia nampiga Geb marufuku kuwa karibu na Nanaa, Geb si alikuwa na pesa! Wewe,
Malii na Zinda wote mlijua jinsi nilivyomfukuza Geb na kumpa onyo kutokuwa
karibu na Nanaa.” Grace akamgeukia mumewe.
“Sasa
nini Grace?” “Kwa nini hukuniambia?” “Kweli mke wangu? Ulitaka nije kukwambia
kuwa James ameniambia amempa ONYO kaka yako asimuone mwanamke pekee ambaye wote
tunajua anampenda?” Grace akanyamaza. “Nilijua ingekuumiza tu. Tena baada ya
wote kumkosea Nanaa! Niliona wewe na mama mlivyoumia wakati Nanaa mgonjwa.
Nilijua ningekwambia wewe, na wewe ungemwambia mama, mkazidi kuumia. Zaidi mama
ambaye alikuwa akimuomba Geb msamaha kila siku kwa kusababisha kukimbiwa na
Nanaa. Nisingeweza kukwambia. Ingekuwa ni kama nawaongezea hukumu.” Grace akaridhika.
“Asante kutufikiria Danny. Kweli ingetuongezea hukumu tu.” Danny akatoa
tabasamu kwa mkewe.
“Sasa
ndio najiuliza, hayo yote Zinda amesahau kweli au ni hasira tu?” James bado
hakuwa ameelewa. “Nisikilize James mwanangu. Ndio maana mimi nilifundisha
wanangu kunyamaza wakati umekasirika. Ukiwa na hasira unaweza kuongea chochote
kile. Zinda amekasirika. Akija kutulia, atakuja kukumbuka hayo yote, na atajua
amekosea. Kumjibu sasa hivi, hakutasaidia hata kidogo. Mpeni muda wa kupokea
taarifa za Nanaa kuzaa na Geb. Mpeni muda tu. Atakuja kuzikubali baadaye.
Lakini kwa wakati huu, mwacheni.” “Sasa na Liz je!? Maana naye analalamika
sana. Ananiita majina mabaya kweli huko mtandaoni likiwepo Msaliti!”
James akaongeza akisikika kuumia.
“Shauku
ya Liz ilikuwa ni kuzaa na Geb tokea zamani. Na aliniambia alishamuomba Geb
kama hana mpango wa kumuoa basi angalau wazae naye mtoto hata mmoja tu. Geb
hakusema ndiyo au hapana. Si ni kweli?” Grace akamuuliza Geb. Geb
akanyamaza. “We Geb?” Dada yake akamuuliza tena kwa msisitizo. “Ni kweli.” Geb
akajibu kifupi tu. “Aaaaah! Basi ndio maana anasema hivyo huko kwenye group!”
James akadakia akikumbuka shutuma za mtandaoni. Wakataka kumuuliza amesema
nini, lakini wakaona ni heri wanyamaze tu.
“Nashauri
mtulie.” Mama G akasisitiza ushauri wake. “Nisijaribu kumtafuta Liz ili
nizungumze naye?” James akauliza. “Naomba mimi nikwambie James.” Grace akawahi
kabla ya mama yake. “Japokuwa sijasikiliza rikodi alizotuma huko kwenye kundi
letu au hatujasoma jumbe zake, lakini mimi namfahamu sana Liz. Nafahamu jinsi
anavyojithamini mwili wake. Na mnajua kwa Liz, hakuna mwanamke bora na wa
thamani kama yeye mwenyewe. Kwa hiyo naweza kuhisi chuki yake ipo wapi. Kitendo
cha Geb kukataa kuzaa na yeye, na kujua wazi ameamua kuzaa na Nanaa! Tena watu wote
tunajua kuwa Geb hakukosea. Maana wote sisi tunajua tabia ya Geb. Kufikiria, na
kupanga mambo yake kabla hajatenda jambo lolote. Wote tunajua huwa halali na mwanamke
kwa kukosea, na halali na mwanamke yeyote bila kinga. Kwa yeye kuzaa na Nanaa
na si Liz, watu wote wanajua Geb alikusudia. Na ni kama kumdhalilisha Liz kwa
hali ya juu wakati watu wote tunajua Liz alishambembeleza sana Geb azae naye,
lakini japokuwa Geb hakusema hapana, minong’ono ilizuka kuwa Geb alikataa. Hata
Danny alisikia. Si ni kweli Danny?” Grace akauliza akitaka uungwaji mkono wa
mumewe.
“Mimi
nilikuta wanamcheka. Sijui nani alifikisha hizo habari kwa kina Goz na Malii.
Wakawa wanamcheka waziwazi kwamba anataka urithi. Lakini Liz akasema ni wivu
tu, yeye anataka mbegu ya Geb kwenye maisha yake. Akasema anataka kuzaa mtoto
mwenye akili nzuri. Kwa kuwa yeye anaakili na Geb anaakili sana, kwa hiyo
anauhakika akizaa mtoto na Geb, atakuwa tishio ulimwenguni. Goz akawa
anamcheka. Liz akaondoka kwa hasira, ndio mimi nikauliza kulikoni. Ndio Malii
akanisimulia kuwa Liz anamkataa Goz kwa kuwa hana akili kama za Geb, anamtaka
Geb. Sasa Goz akawa anamcheka Liz kuwa hata afanyaje Geb anapita tu kwake, ni
heri amkubali yeye. Yeye atamuoa na kumthamini.” Geb alibaki kimya.
“Si
umesikia James?” Grace akauliza. “Mimi hilo mbona najua? Goz mwenyewe
alishaniambia kuwa anamtaka Liz, lakini Liz anamng’ang’ania Geb sababu ya pesa.
Kwa hiyo najua. Hata sasa hivi huko kwenye kundi, Goz anatuma picha za watu
wanaocheka mpaka machozi.” James alijibu nakufanya wacheke. “Gozibeth ni chizi!
Anafanya makusudi tu kuwacheka Liz na Zinda.” Danny aliongeza. “Ndio kazi yake
hapo. Liz akituma tu ujumbe, na yeye anatuma katuni na ile video ya yule mtoto
mdogo anayecheka sanaaaa.” Wakazidi kucheka.
“Sasa
kwa hali kama hiyo, Liz akiwa na hasira hivyo, unafikiri utamwambia nini
akaelewa? Liz hajawahi na wala hafikirii kushindwa. Kwa Nanaa kufanikiwa kuzaa
na Geb, wewe tayari ni adui mkubwa sana kwa Liz. Nashauri umwache tu atulie.
Wote wanahitaji muda wakuingiza hizo habari akilini. Watatulia tu kama mama
alivyosema.” Grace akamaliza.
“Sasa
hali ya Nanaa?” Akili ya James ikarudi kwa dada yake. “Mzimaa. Katulia. Hivi
hapa anataka mwanae akabarikiwe jumapili.” James akacheka. “Kweli nimekuza!”
James akajisifia. “Mimi nilikuwa nakuja kumtuliza!” “Ametulia tuli. Na wewe
tulia tu. Wala usimuonyeshe wasiwasi. Mtie tu moyo na msaidie mpaka afunge ndoa
yake.” “Nahangaikia hizo taratibu mama.
Hivi sikutaka ajue ugumu ninaopitia ili tu kuweka mazingira ya mahari yake
kupokelewa huko nyumbani.” “Ni nini tena!?” Mama G akauliza.
“Daah!
Naomba nisiongee mama yangu. Lakini naomba mniombee. Hili jambo sio rahisi kama
nilivyodhani. Lakini Mungu yupo nami. Atanisaidia tu. Sijawahi kutulia tokea
Nanaa analetwa nyumbani kutoka hospitalini akiwa ametoka kuzaliwa na mama yake
amefariki, mpaka leo! Na hili najua nitalikamilisha tu.” Hata uso wa James
ulishabadilika akaonekana kuna kinachoendelea.
“Unajua
tokea mama yake amekuja pale nyumbani kwetu akiwa mjamzito, mpaka yule mama
anapelekwa hospitalini kujifungua, alikuwa akilia sana! Sitamsahau. Halafu
kalikuwa kabinti kadogo sana. Kila nikimfikiria najiuliza sijui alikuwa
akiogopa! Au kwa kuwa alikataliwa na mwanaume aliyempa mimba! Au sijui kwa kuwa
alifukuzwa nyumbani kwao! Hakika sijui! Lakini sura yake akiwa analia akiwa
amekaa nje peke yake, haijawahi kunitoka mpaka leo. Na kila nikimkumbuka,
ndivyo ninavyojitahidi kumsaidia Nanaa, asipitie kule alikopita mama yake.
Sitaki hata awe na uchungu au awe na mawazo huyu mtoto. Wakati mwingine nahisi
nakuwa over protective kwake. Sitaki hata mtu amuudhi kidogo.” James
alikuwa akiongea huku akionekana kufikiria.
“Mungu
atakusaidia na kukubariki James. Umebeba jukumu la Nanaa ukiwa bado mdogo sana.
Mungu hatakupungukia kwa hilo. Kila ulichofanya kwa Nanaa, ujue umemkopesha
Mungu.” “Amina mama. Kwa hiyo msione kimya. Napambana kupata taratibu za
mahari. Nikikamilisha tu, nitawajulisha. Sitaki waje wapate sababu ya kunilaumu
au kumlaumu Nanaa. Naomba tusubiri ili tufuate hatua zote.” “Usijali James.
Mimi nitasubiri tu. Na ninakuahidi nitamuoa Nanaa, na nitamtunza vizuri tu.
Hutasikia tatizo lolote.” Geb akaongeza. “Nashukuru Geb. Asante sana.” Wakati
wanamalizia mazungumzo yao tu, Nanaa akatoka.
“Kaka!”
Nanaa akaonyesha kufurahi. “Shikamoo.” “Marahaba. Vipi mtoto?” “Alikuwa
anakula. Naona anarembua tu. Anataka kulala.” Akamkabidhi kaka yake. “Anakua
kama uyoga! Unamlisha nini?” “Namkazania kunyonya.” Mama G akadaikia wote
wakacheka, Grace akatingisha kichwa. “Mama wewe!” “Kumbe uongo? Mimi ndiye
namkazania kunyonyeshwa. Mambo ya huyo mtoto yote, niulize mimi James
mwanangu.” James akacheka. “Na mimi nimeona mama.” “Tena umbile kachukua langu
kabisa.” “Mama wewe! Sio mama yake?” “Hata kidogo! Hapo Nanaa katupa rangi tu.
Mimi nina damu kali kweli! Basi na yeye huyo Oliva akija kuzaa, atazaa watoto
kama mimi!” Grace alikuwa akimwangalia mama yake hammalizi. Kila mtu alikuwa akicheka.
“Sasa
Geb itabidi apandishe huo ukuta. Maana kama huyo mtoto atakuwa kama mke wangu!
Jasho litawatoka.” Danny aliongeza kwa kumsifia mkewe. “Wala si ukuta huo wa
kazi ya mikono ya mwanadamu. Huyo nitamuwekea ukuta wa kiroho. Maisha yake
naenda kuyatoa wakfu kwa Bwana! Akaombewe. Nguvu ya Mungu imzingire kila
aendapo. Nataka…” “Mama hamalizagi na mipango ya huyo mtoto! Akianza hapo,
tutakesha. Naombeni tule jamani.” Grace alianza kuhangaika kusimama. “Wivu tu!”
Mama G akasimama na kwenda kumpa mkono Grace ili asimame. “Hivyo ulivyokonda
mama yangu! Nitakuumiza tu.” “Nakuhurumia. Nipe mkono nikusaidie kusimama.”
Mama G akanyoosha mkono ili amsaidie Grace kusimama. Danny akasimama, akamsadia
mkewe kusimama. Wakacheka.
Kikao
kikahamia mezani. Wakaanza kucheka. Hakuna aliyekumbuka tena kashfa
zinazowakabili. Danny aliendelea kuwachekesha, mpaka James alipotaka kuaga. “Oliva
anabarikiwa, kaka.” “Nimeambiwa. Hongera.” Nanaa akacheka. “Si utakuwepo?”
Nanaa akauliza. “Lazima. Siwezi kukosa.” Nanaa akafurahi. “Lakini tutaenda
kuwabariki watoto yatima kwanza siku ya jumamosi, ndipo jumapili tunafanya
ibada.” Nanaa akamuelezea kaka yake mpango mzima. “Mpango mzuri sana. Basi na
mimi nitataka kushiriki.” James
akasisitiza.
“Mimi
nashauri hivi. Sijui kama itakuwa ni sawa. Geb akishapata hayo mahitaji yote.
Danny aandae tangazo dogo tu la mwaliko. Litakaloeleza ratiba nzima kuanzia
jumamosi huko kituo cha watoto yatima, mpaka jumapili. Alitume hilo tangazo kwa
marafiki wote, pamoja na mahitaji yote. Atakayetaka kuchangia, ajibu palepale
kwenye kundi. Ili kushirikisha watu wote hizo baraka. Vitakavyo baki vyote,
itakuwa sisi. Danny na Grace nyinyi iwe chakula. Mtanunua vyakula kwa ajili ya
kituo. Kadiri muwezavyo. Mahitaji mengine ni Geb na Nanaa. Na wengine
tutachagua hapo. Au mnaonaje?” “Mbona mimi nilishafurahia hilo wazo kabla
hujauliza!” James alifanya wacheke. Wakakubaliana hivyo.
Ubarikio wa Oliva Magesa.
Geb
alifanya kama alivyoshauriwa na mama yake. Akakusanya mahitaji yote kutoka
kwenye hiko kituo cha watoto yatima. Wakakusanyika tena kama familia.
Wakayapitia, ndipo Danny naye akaamua kufanya kama alivyoshauriwa na mama G.
Akayatuma kwanza kundini kabla wao hawajachagua, ili kusiwe na kulalamika tena.
Alituma kwenye kundi lile lile walilotukanwa, bila kujibu shutuma. Tokea
watukanwe ndio Danny anarudi na ujumbe wa kumshukuru Mungu na kuwataarifu juu
ya kubarikiwa kwa mtoto wa Geb na Nanaa. Alieleza mpango mzima wa kubariki
kituo cha watoto yatima, na kuwaambia na wao wanakaribishwa. Atakayependa
kuungana nao, basi achague kitu hapo na aandike hapo hapo, ili wasirudie
kununua vitu vilevile.
Hapo
hapo Zinda na Liz wakatoka/left
kwenye lile kundi. Danny akatulia tu, hakujibu kitu. Lakini wakashangaa kuona
watu baadhi wanajibu na kuchagua vitu vya kuleta siku hiyo. Danny akashukuru na
kuwataarifu muda wa kukutana siku hiyo ya jumamosi kwenye kituo hicho cha
watoto yatima, sehemu ya kuegesha magari kabla hawajaonana na uongozi. Vitu
vilivyobaki kina Magesa wakamaliza wao wenyewe.
Jumamosi
hiyo walipokutanika kwenye kituo hicho cha watoto yatima, mama G akaomba waombe
kwanza. Wakashangaa maombi ya mama yule ni juu ya watoto hao yatima na watoto
wao tu. Akawaombea baraka watoto wao wote. Kisha ndio akasema waingie ndani. Hakutaka
kuuliza mambo yaliyopita, na wala kina Danny hawakuweka mazingira yakuzungumzia
shutuma za Zinda na Liz. Kwa hiyo hapakuwa na hayo mazungumzo kabisa.
Watu
walifanya kilichowapeleka pale, na kesho yake baada ya ibada, Oliva
alipobarikiwa akiwa amesimamiwa na bibi yake, walirudi kunywa na kula na watoto
hao yatima. Napo pia walishangaa baadhi ya marafiki zao waliwaunga mkono.
Walifika kanisani na kwenye chakula cha mchana. Hilo nalo wakafanikiwa
kulimaliza. Lakini wazi kulikuwa na ukimya wa namna yake. Kama kuwindana hivi!
Hakuna kutizamana machoni. Hapakuwa na vicheko vingi, na walifika wachache.
Mama G aliwashukuru walioweza kufika, wakaagana.
~~~~~~~~~~~~~
- Hawa watu walikuwa ni marafiki wa muda mrefu sana. Wamekua pamoja,
wakageuka kuwa kama ndugu. Leo kumeingia tatizo ambalo kwa mara ya kwanza
hawajui watalitatua vipi katikati ya jambo ambalo baadhi yao waliliona ni la
heri.
- Kwa Mara ya kwanza James anamuona dada yake akiwa na furaha
nakupokelewa kwenye familia inayomjali. Anamjua Nanaa. Anajua wazi wale ndio
watu ambao Nanaa angewahitaji maishani. Alimuona jinsi mdogo wake akihangaika
tokea anazaliwa. Leo amempata Geb, lakini kumeingia dosari kubwa sana. Tena
akiwa ametupiwa shutuma zinazo fanana na kweli!
- Zinda akiwa ndiye kama ndugu wa Karibu wa Danny, leo ndio anampa maneno
machungu ya kiasi kile. Kejeli na matusi yaliyogusa hisia za Danny. Zinda
anamuhesabu ni msaliti kwake. Amesimama na Geb wala si yeye. Amempa ujumbe wa
vitisho kuwafikishia kina Magesa. Ameahidi
kutokukubali na litakalo wapata wasimtafute.
-Nini Zinda atafanya?
-Nini kitaendelea kwa vijana hao waliokuwa pamoja?
Mama G aliwahusia hawa wapenzi
wawili, {Geb & Nanaa}, juu ya vita inayo wakabili mbeleni. Aliwasihi
wamtangulize Mungu katika kila jambo, lakini mapenzi yamenoga. Hakuna
anayetosheka na mwenzake. Si mchana, si usiku, penzi tamu haswaaaa!
- Je, wataweza kuendelea kusimama katika kila kombora litakalotupwa kwao
wakiwa na msingi imara wa kitandani tu?
Wote wanaujua mchezo wa kitandani vilivyo. Tena hakuna asiyetosheka na
mwenzie wawapo kitandani. Ndio maana kazi hazifanyiki tena kwa Geb, mikono yake
inataka kushika mwili wa Nanaa wakati wote! Hakuna sehemu nimeona wakiomba
pamoja kama walivyoshauriwa zaidi ya penzi.
- Nini kitaendelea kati ya penzi hilo zito la Nanaa
& Geb?
USIKOSE MUENDELEZO. Mambo ndio kwanzaaaa Yanaanza.
0 Comments:
Post a Comment