Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Ni Wangu! - Sehemu Ya 33 - Naomi Simulizi

Ni Wangu! - Sehemu Ya 33

Ukisema Cha Nini.

 Nanaa alimkuta Zac bado akimsubiria hapo mgahawani. Tokea mchana wakati wanatumiana ujumbe, alishamuuliza wapi anaishi kwa wakati ule. Nanaa akamuelekeza na kumwambia upo mgahawa mzuri sana hapo kwenye hizo apartment, wanaweza kukutana hapo. Waliafikiana

wakutane hapo, kwa kuwa muda ulishakuwa umeenda na Nanaa alimwambia lazima saa 12 kamili awe amerudi kwake. Wasingeweza kukutana mbali na hapo kwa siku hiyo. Hiyo siku ilikuwa ya salamu tu, kisha wangepanga siku nyingine, wakutane mahali patulivu wakiwa wawili tu. Wakumbushie enzi.

          Alisimama baada yakumuona Nanaa. “Umependeza sana Nanaa.” Nanaa akacheka. “Asante. Na wewe amependeza kama kawaida yako. Hujikosei!” Zac akacheka. “Nilirudi nyumbani, nikajiandaa rasmi kukutana na wewe.” Nanaa alizidi kucheka. “Kwa hiyo hapo umevaa hivyo kwa ajili yangu?” “Unafanya mchezo nini? Nimevunja kabati kama mtoto wa kike!” Nanaa akazidi kucheka. “Basi umepatia.” “Afadhali kama juhudi zangu sio bure.” Wakatizamana kwa muda kama wasio amini.

“Nina hamu na wewe Nanaa!” Zac akaanza. “Naomba unisamehe mpenzi wangu. Nilikosa.” Nanaa alibaki kimya kwa muda, akabadili mazungumzo. “Umerudi lini?” “Hata sijamaliza week. Nimerudi kwa ahadi ya kazi. Baba aliniunganishia kwenye kampuni moja ya mambo ya simu. Nimefanya usahili huko, wameonekana kuvutiwa na mimi, wamesema watanipigia simu. Lakini ikitokea sijabahatisha, nataka kurudi shule, nimalize kabisa mpaka PHD. Kwanza nani alikwambia kama sipo nchini?” Nanaa akatabasamu. “Nilikutana na Tondi, yule rafiki yako. Ilikuwa maeneo ya Posta Mpya, akawa ananilaumu, eti nilikuchanganya mpaka ukakimbia nchi.” Wote wakacheka. 

“Lakini hakukosea. Niliingiwa na chuki. Nikajichukia sana kwa kitendo nilichokifanya. Unajua japokuwa sikuwa nimekutambulisha nyumbani, lakini kila mtu alikuwa akikufahamu na wakajua lazima nikuoe. Tena niliwaambia tutafunga ndoa ukiwa mwaka wa pili. Kwa hiyo kila mtu alijua naoa mwaka ule unaofuata baada ya kumaliza. Sasa kuja kuharibu, nikaona heri nikaanze kwingine. Nilijilaumu sana.” Nanaa akanyamaza kwa muda kama anayefikiria.

Alishamuagizia kinywaji alichojua Nanaa anakipenda. Aliagiza mara alipopokea ujumbe kutoka kwa Nanaa akimtaarifu kuwa Geb amefika nyumbani, avute subira kidogo, ataungana naye muda si mrefu. Yeye alikuwa amefika hapo lisaa kabla ya Nanaa kufika hapo. “Nanaa!” “Kwa nini ulinisaliti, Zac?” Nanaa akauliza huku machozi yakianza kumtoka. “Uliwezaje kusahau ahadi zote na mipango yote tuliyowekeana mimi na wewe!? Ni nini nilikuudhi au nilikunyima ukakipata kwake? Ulikuwa na mahusiano naye kwa muda gani? Mara ngapi ulilala naye kabla sijawafumania? Mliendelea naye baada yakuwafumania? Alikuwa mzuri kitandani kuliko mimi? Ilikuaje Zac?” Nanaa akajikuta yale maswali aliyokuwa akijiuliza siku zote juu ya Zac, yanatoka bila kituo.

          “Uliwezaje kunisaliti ungali ulijua nilikuwa nikikuhitaji kiasi kile? Uliwezaje kunionyesha mapenzi yote yale, halafu ukaweza kulala na msichana mwingine? Na yeye ulikuwa ukimfanyia kama ulivyokuwa ukinifanyia mimi kitandani? Na yeye ulimwambia unampenda? Hivi uliwezaje hata kudiriki kumvulia nguo msichana mwingine ambaye sio mimi!? Tena akijua mimi nipo! Halafu na yeye alikuwa anamchumba wake! Akitoka kwako, anarudi na kwa mpenzi wake, halafu mnaniacha mimi peke yangu! Uliwezaje kunisaliti Zac? Uliwezaje kusaliti makubaliano yote yale? Au yalikuwa ni maneno ya uongo kwangu? Pengine ndiyo maneno uliyozoea kuwaambia wasichana wote!” Nanaa hakuwa akisubiri ajibiwe.

Aliendelea kuuliza tu. “Hivi unakumbuka kuwa kile kitanda ulichokuwa ukilala na mimi, ndicho ulichokuwa umelala na yule msichana!? Ni nani uliyekuwa ukifanya naye mapenzi wakati wote ulipokuwa na mimi? Uliona upo na Nanaa kweli au ilikulazimu unifikirie mimi ndiye yule msichana uliyekuwa ukitembea naye kila mahali huku ukiniaminisha ni mwanafunzi mwenzako kama wanafunzi wengine tu? Uliiona sura yangu wakati ukifanya mapenzi na mimi au ni ya yule msicha wako? Eti Zac?”

“Kwa nini ulinidanganya na kunivua nguo zangu bila penzi la kweli? Umenisababishia ugonjwa mkubwa sana maishani. Nashindwa kupenda na kuamini mtu yeyote! Umenisababisha kutupa mbali penzi la kweli lililokuwa limekuja kwangu mara moja katika maisha yangu, sababu ulivunja uwaminifu wako kwangu. Wanaume wote nawaona waongo! Tena mbaya zaidi ulinitenda nikiwa nimekusimulia usaliti niliotendwa na mwanaume niliyekuwa naye kabla yako! Ukanifurahisha kwa muda mfupi, halafu ukarudia kosa lile lile! Tena na mtu wakaribu yetu! Uliwezaje kunitendea ubaya wa kiasi kile? Nilikufanyia nini kibaya cha kunilipa kwa kiasi kile?” Nanaa alijikuta akitokwa na maswali yaliyosindikizwa na machozi kama mvua.

Alimnyeshea mvua ya machozi na maswali, Zac akabaki amenywea hajui aanzie wapi kujibu. Hasira za kusalitiwa zilimrejea Nanaa, alilia asijue atajisaidia vipi. Ukweli hakuwa tayari kupokea jibu hata moja kama alivyodhania hapo awali. Bado hakutaka kudanganywa na wala hakuwa tayari na ukweli. Zac alitaka kumfuta machozi, Nanaa akakwepesha uso akasimama mbali zaidi. “Nakutakia maisha mema Zac. Lakini sio na mimi. Tafadhali usinitafute tena hata kwa ujumbe. Leo ndio nakuaga rasmi. Na kama kweli ulishawahi hata kunipenda maishani mwako, utaheshimu maamuzi yangu. Kwa heri.” Nanaa akaondoka bila hata kunywa kinywaji chake. Hakugeuka nyuma, na wala safari hii Zac hakumfuata. 

Tangia mchana wake anakutana na Zac, mpaka muda mfupi kabla ya kuja hapo, walikuwa wakiwasiliana vizuri sana na Nanaa. Akajua Nanaa amesamehe, nikwenda kuwekana tu sawa, waanze upya na kuendeleza penzi lao. Lakini Nanaa alibadilika gafla. Swali la kwanza na la pilli alionekana ametulia. Lakini kadiri alivyoendelea kuzungumza ndipo Zac alivyozidi kuona jeraha kubwa alilomsababishia moyoni mwake. Akaamini na kukubali huo ndio mwisho wake na Nanaa.

~~~~~~~~~~~~~

Akiwa bado amekaa palepale gizani, akimuonea wivu Zac anavyofaidi na Nanaa wakati huo, akashangaa mlango unafunguliwa kwa tahadhari. Kidogo alishituka akijua mwizi. “Mwizi na funguo?” Geb akajiuliza. “Atakuwa ni Nanaa? Lakini mbona mapema hivyo! Hata nusu saa haijaisha!” Geb akatulia baada ya mwanga wa nje, ulipoingia kwa kupitia mlango, na kumsaidia kumuonyesha Nanaa. Geb akashukuru Mungu. Nanaa naye alishukuru baada ya kuingia hapo ndani na kukuta giza. Akajua Geb alishakula, akaenda kulala. Asubiri nini tena, wakati walishapoteza mtiririko mzima wa maongezi yao! Alimuonyesha wazi mahusiano yao yalikufa akabaki Liv tu kati yao.

Akaingia mpaka jikoni kwa tahadhari kama asiyetaka kusumbua mtu, akakaa chini kabisa sakafuni. Akajikunja hapo na kuanza kulia taratibu. Nanaa alikuwa mzoefu wa kulia. Tokea mtoto mpaka hapo, hakuwahi kunyimwa na maisha sababu ya kulia. Maisha yalijua kumpiga, nakumliza bila huruma. Alijua jinsi ya kutawala sauti yake. Akiamua mtu mwingine asijue kama analia, hutajua. Ataruhusu kutoa machozi bila sauti, ili kuruhusu uchungu wake moyoni utoke, angalau baada ya hapo aendelee na maisha mengine. 

Geb alijua wazi analia, japo hapakuwa na sauti. Alimuhurumia Nanaa, asijue ni nini tena kimemsibu. Akaamua kutoka sebuleni, akasogea jikoni taratibu kama asiyetaka kumshitua. Alipofika tu jikoni, Nanaa akashituka sana. Akasimama. Ilibidi Geb awashe taa, ndipo akaona vile Nanaa alivyojaa machozi kila mahali. Nguo hiyo nyeupe ilikuwa chapachapa kwa machozi. “Samahani nimekusumbua.” Nanaa aliongea huku akijipangusa machozi kwa viganja vyake. “Hata kidogo.” Nanaa alibabaika kidogo asijue aseme nini. “Samahani sikujua kama umekaa kwenye makochi. Nilijua umeshakwenda kulala.” Geb akamsogelea. “Hujanisumbua, Nanaa. Ila sikutaka ukae hapo chini peke yako.” “Liv aliamka hata mara moja?” Tayari akabadili mazungumzo. Geb akavuta pumzi kwa nguvu akabaki akimtizama.

“Nimechelewa sana?” Nanaa akauliza kwa upole baada ya kuona kimya. “Samahani kwa kuchelewa.” Akarudia kuomba tena msamaha. Tena safari hii ulikuwa wa unyonge, na machozi juu yake. Geb akazidi kuumia. “Liv hajaamka Nanaa. Na hujachelewa hata kidogo. Hujamaliza hata dakika 30, tokea uondoke mpaka sasa. Upo sawa?” “Ndiyo. Basi ngoja nikaoge ili niwe tayari akiamka, nimnyonyeshe moja kwa moja.” Akapita pembeni yake, akaingia chumbani kwenda kuoga na kubadili nguo. Geb akasimama pale kwa muda, akaamua na yeye kwenda kuoga angalau kutoa uchovu wa siku nzima.

 ~~~~~~~~~~~~~

Nanaa alioga, akapanda kitandani, akajilaza pembeni ya mwanae. Geb alimaliza kuoga, akapitia simu yake, akajibu jumbe mbili tatu kutoka kwa marafiki zake, akatoka nakukuta nyumba imetulia. Akajua lazima Nanaa yupo chumbani kwake analia. Akaamua kumfuata chumbani kwake. Akabaki akimwangalia vile Nanaa alivyomkumbatia Liv kwa mapenzi huku amelala. Akamuhurumia na kuzidi kuhukumiwa. Nanaa alichoka na mizunguko ya siku nzima, ukichanganya na kilio, hakuhitaji kubembelezwa na chochote au yeyote ili alale. Alijikuta hata anashindwa kulia tena, ila kupitiwa na usingizi muda na sekunde aliyopitisha mkono juu ya mwanae. 

Geb alibaki amesimama akimwangalia. Nanaa akashituka akamkuta bado Geb akiwaangalia. Geb alimuona vile alivyoingiwa na hofu. Alikumbuka vile Geb alivyomwambia asilale na mtoto kitanda kimoja, amzoeshe kulala kitandani kwake. Akakaa huku akijaribu kumsogeza Liv mbali kidogo kama kuepusha ushahidi. “Alikuwa amelala kitandani kwake, nikamtoa hapo ili nijaribu kumbadili diaper nikidhani ataamka ili anyonye, lakini hajaamka. Nilitaka kumrudisha kitandani kwake, lakini nimepitiwa na usingizi.” Nanaa akajitetea huku akionyesha uso wa wasiwasi, kama aliyefumaniwa. 

“Naona Liv mwenyewe anapenda hivyo mnavyolala.” “Lakini naweza kumuweka kitandani kwake tu.” “Hamna shida. Nyinyi laleni tu. Vipi lakini na wewe?” Nanaa akajiweka vizuri, akakaa. “Anaendelea vizuri. Homa iliisha kabisa. Alikuwa akitoa kicheko tu kwa bibi yake.” Nanaa akajibu huku macho yote yakiwa kwa mwanae, mikono ikimpapasa kwa tabasamu zito.  Geb akatulia, akijua wazi Nanaa ameelewa swali ila anakwepa. Ujumbe ukaingia kwenye simu ya Nanaa, ikatoa mlio mara kadhaa, kulazimisha kupewa na yenyewe kipaumbele. Ilikuwa pembeni kwenye meza. Wote wakaingalia ile simu.

Kabla hajafikiria chakufanya, ukaingia ujumbe mwingine uliotoa sauti kama ya mara ya kwanza. Ukaingia ujumbe wa tatu na wa nne. Ikamlazimu Nanaa kuchukua simu yake. Akaanza kuzisoma zile jumbe taratibu. Zote zilitoka kwa Zac. Geb aliona machozi yakimtoka mara kadhaa na kuyapangusa, kisha akataka kujibu, lakini simu ikaingia. Iliita mara kadhaa huku Nanaa akiangalia sura ya Zac juu ya simu yake. Akafikiri kwa haraka, akapokea huku akijiandaa kutoka ili akazungumze na simu yake nje. “Nanaa mpenzi! Nashukuru umepokea simu yangu.” Zac alisikika upande wa pili. “Naomba subiri kidogo.” Nanaa akaongea kwa upole huku akitaka kutoka hapo chumbani. “Huna haja yakutoka. Mimi ndio natakiwa kutoka.” Geb akatoka, akafunga mlango, akamuacha Nanaa ameduwaa na simu yake sikioni, Zac upande wa pili. “Nanaa!” “Nipo Zac.” Nanaa akajibu kwa utulivu huku akijirudisha kitandani.

“Naomba nafasi ya kunisikiliza. Tafadhali mpenzi wangu. Naomba nisikilize tu. Naweza nisiwe na majibu ya maswali yote kwa kina, lakini nipe nafasi mpenzi. Siwezi kuruhusu mwisho wa machozi kwako. Hata kama nimeshindwa mengine, basi naomba nipe nafasi ya kutimiza ahadi moja niliyokuwekea, sitakubali kuyaona machozi yako tena, zaidi mimi nikiwa nimesababisha. Nipe nafasi. Nisikilize tu. Hata kama tunaagana, tuagane tukiwa tuna amani. Nakuahidi safari hii tukimaliza mazungumzo yetu, ukanipa masharti, nitafuata, ila kwa sharti moja tu. Kama tutaagana ukiwa una amani na mimi, na sivinginevyo.” Nanaa aliendelea kufuta machozi, huku akisikilizia faraja moyoni. 

“Nanaa!” Kimya. “Tafadhali mpenzi wangu.” “Utaniambia nini Zac, ambacho hujawahi kuniambia? Naogopa kuumia zaidi.” Nanaa akajibu kwa uchungu na machozi yakizidi kumbubujika. “Nakuomba nipe nafasi mpenzi. Nisikilize tu.” Kimya. “Sasa hivi nimeshaondoka hapo. Lakini kesho siku nzima nitakuwa hapo kwenye huo mgahawa nikikusubiri. Ukipata nafasi muda wowote, iwe jioni, au asubuhi, jua nipo hapo nikikusubiri. Naomba urudi tuzungumze.” Nanaa akafikira kidogo. Akakata ile simu na kuizima kabisa. Geb aliyekuwa nje ya mlango akisikiliza aliposikia kimya, akaondoka kwa haraka ili kama Nanaa anatoka asimkute pale nje. Akaenda kusimama jikoni. 

~~~~~~~~~~~~~

 “Kweli jamaa ameamua kupambana! Akifanikiwa tu kufikia moyo wa Nanaa, ndio nimekwisha na mwanangu.” Geb aliwaza. Akajua sababu ya Nanaa kumpenda Zac, ni kujua kumbembeleza kitu alichoshindwa yeye. “Mama yupo sahihi, Nanaa ataondoka au watamzalisha, nibakie na Oliva wangu nikiteseka.” Geb aliendelea kuwaza. Geb mtoto wa mama. Kijana mwenye pesa. Mzuri na yeye anavutia kwenye macho ya wanawake. Amezoea kubembelezwa na sio kubembeleza. Kwa swala la mchezo wa kitandani, hata yeye alijua ni hodari. Aliujua mchezo wa mapenzi, hata Liz alizunguka lakini ilimlazimu kurudi kukata kiu kwa Geb. Kila alipokuwa akijishauri kuachana na Geb moja kwa moja, alikumbuka penzi la Geb, akajikuta akijirudisha mwenyewe. Liz alishakiri hata kwa mashoga zake, hakuna mwanaume aliyewahi kuutendea haki mwili wake huo wa thamani, kama Geb.

“Bwana Geb akikuvua nguo, hujuti!” Ndio ilikuwa kauli ya Liz kwa mashoga zake wakati wote. Japokuwa hakuwahi kufanya naye mapenzi bila kinga, kama wanaume wengine waliokuwa wakipagawa na kuchanganyikiwa mara Liz akiwakubali, nakuona kuvaa kondom ni kupoteza ladha nzima ya kimwana huyo, lakini alifaidi penzi la Geb, alilokuwa akipewa pipi kwenye ganda lake. Kilichokuwa kikimpagawisha zaidi, ni ule uwezo wa Geb kumfikisha kileleni hata mara 4, kwenye mchezo mmoja, tena akiwa ametulia, bila heka heka nyingi katika eneo la tukio.

~~~~~~~~~~~~~

Geb alitoa chakula alichokuwa amewekewa na Nanaa, akataka kula, akashindwa. Akataka hata kunywa uji wake kama dawa, lakini pia akashindwa. Akataka kurudi chumbani kwa Nanaa, lakini akagundua Nanaa alishazima taa, amelala. “Hata nikiingia, nikamuamsha, nitamwambia nini wakati wazi nilimuonyesha simjali? Sijui kama anakula au la. Nilishamuonyesha kumsusa muda mrefu sana. Ndio maana anashindwa hata kujibu maswali yangu. Kesho ndio hatima ya Zac, Nanaa na mimi. Zac anayejua kumbembeleza Nanaa, akifanikiwa kukutana na Nanaa kesho tena, mimi ndio niandike maumivu. Au nimkataze asiende? Naanzia wapi? Sina mamlaka hayo tena juu yake. Mama hajakosea. ‘I sow a  seed for my own destruction’. Lazima kujishusha kama mama alivyosema. Nanaa alinitamkia kuwa kwa mara ya kwanza maishani amejikuta akipenda. Ni mimi ndiye aliyenipenda. Mimi ndiye nipo kwenye nafasi nzuri na kubwa kuliko Zac. Ananipenda na nimefanikiwa kumzalisha. Kesho tukiamka salama, nitatumia silaha zangu zote mpaka kieleweke.” Geb aliendelea kuwaza akijaribu kuweka mikakati aliyokuwa akijikatisha nayo tamaa. 

“Hakika kesho lazima nichukue changu mapema.” Akazidi kujiwekea mikakati mingi, akachukua simu na kumtumia ujumbe mama yake. ‘Mama, naomba kesho usiingie ndani. Niachie chakula cha Nanaa hapo mapokezi nitakifuata. Naomba nipate muda na Nanaa. Nampenda sana Nanaa, na sipo tayari kumpoteza. Naomba uende kazini uwe na Grace kumsaidia kazi. Kesho sitaki kutoka kabisa humu ndani. Nitahakikisha narekebisha makosa yangu yote. Nitajishusha kama ulivyonishauri wewe mama yangu. Siwezi kumpoteza Nanaa. Nahisi nachanganyikiwa mama. Sijui lakufanya! Siwezi kula, wala kulala wakati nimechoka. Nimeshindwa hata kuacha kuangalia mlango alipolala mwanamke ninayempenda. Naumia kuona anathaminiwa na kuonyeshwa mapenzi na mwanaume mwingine wakati mimi nilikuwa nikilala naye nyumba moja! Mwanaume ambaye hata nakosa ujasiri wakumwita ni mpinzani wangu, kwa kuwa mwenzangu amenipita mbali sana kwa Nanaa. Lakini mama, nilikuwa au ninayo mipango mikubwa na ya kudumu kwa Nanaa. Ni hasira tu ndizo zimenifanya kupitisha kipimo.’ Mama yake alisoma huo ujumbe kwa makini.

Akaamua kumjibu. ‘Ulijisahau na kumpuuza Nanaa, Geb. Ulijua atakuwepo wakati wote kwa kuwa ana shida. Mwenzio anatumia matatizo ya Nanaa kumpata Nanaa. Na kumfanya awe karibu naye. Lakini wewe umeyatumia matatizo ya Nanaa kama fimbo ya kumchapia mwanamke mtulivu, asiye na makuu, aliyehitaji kupendwa tu! Nanaa sio kama hao wanawake zako wengine waliokuwa wakitaka mali zako tu, bila kukujali. Japokuwa ulikuwa ukimfanyia ubaya, lakini huyo mtoto alihakikisha halali bila ya kuhakikisha una chakula, Geb. Huendi kazini bila kula! Ulijua hilo na ukapuuza.’ Mama G aliandika huo ujumbe akautuma kwa mwanae. 

Geb akasoma majibu ya mama yake na kuzidi kuhukumiwa moyoni. ‘Nimetambua kosa mama. Kesho nitarekebisha.’ Akarudisha majibu kwa mama yake. ‘Kama bado hujachelewa!’ Mama yake nae akamjibu kwa kifupi. ‘Naomba usinikatie tamaa mama. Wewe ndio nguzo yangu. Kila ninapokosea wewe ndio unakuwepo kuniinua. Hujawahi kunitupa, naomba usinitupe sasa hivi. Nitachanganyikiwa zaidi ya hivi.’ Geb alijikuta akizidi kukosa nguvu kila alipokumbuka ukali kutoka kwa mama yake kila linapokuja swala la Nanaa. Wazi mama yake alionekana kuwa upande wa Nanaa kila wakati kitu kilichokuwa kipya na kigeni kwa Geb. 

Alizoea kuonwa kama malaika na mama yake. ‘Mama! Nimekuomba usinitupe. Nimekukosea, nimekosea kila mtu, naomba mnisaidie wewe na Grace, kwa namna yeyote ile nimpate tena Nanaa.’  Jumbe zote aliona zimeingia kwenye simu ya mama yake, akaona wazi amesoma, na hataki kujibu. Geb alizidi kuumia. ‘Tafadhali mama yangu. Naomba usinitupe sasa hivi!’ Geb alituma ujumbe mwingine akiendelea kusihi.

Japokuwa alikuwa amemkasirikia mwanae, ikabidi ajirudi kidogo. Akamuhurumia. Akajua amekuwa mkali sana kwake. Alimjua jinsi anavyoweza kuchanganyikiwa na kuwa hata mgonjwa. Alikumbuka madhara makubwa aliyoyapata kwa msichana aliyemkimbia kwa ajili ya mwanaume mwingine akiwa chuoni. Akaogopa historia kujirudia, akarudisha ujumbe kwa haraka, ‘Geb! Penye nia pana njia. Sijawahi kuona ukishindwa jambo. Sasa hivi naingia kwenye maombi kukuombea mwanangu. Hujawahi kunidanganya, na ninaamini ulichosema kuwa unampenda Nanaa. Tulia, hakikisha unapata usingizi wakutosha ili kesho uwe na familia yako. Nitakuletea vyakula asubuhi, na kwenda ofisini kwako kumsaidia kazi Grace. Usiku mwema.’ Ilikuwa kama dawa, moyoni kwa Geb. Alifurahia sana, akarudi chumbani kwake moja kwa moja. ‘Asante sana mama yangu. Usiku mwema.’ Alituma huo ujumbe, akabaki akiwaza. Wakati akiwaza huku, Nanaa naye alikuwa akiwaza, na Zac hivyo hivyo. 

Kwa Zac!

Z

ac naye alianza kupanga sera zake. Akajiapia kurudisha penzi la Nanaa. Akapanga maneno ya kumwambia huku akijaribu kukumbuka maswali yote aliyoulizwa na Nanaa jioni hiyo. Akaanza kuyafanyia mazoezi majibu yake. Huku akiyapa hisia kutokana na kile alichojua Nanaa angependa kusikia, na kugusa hisia zake kwa haraka. Alijiambia endapo kesho atabahatika kukutana naye tu, basi atahakikisha anauza sera zake kama mwanasiasa. Kwa utulivu sana bila papara ili asiharibu akiweka hisia nzito, mpaka Nanaa ataingia kwenye anga zake. Akakusudia kumbana katika kila eneo alilojua Nanaa anaweza kutaka kumponyoka. Na kwa kuwa alimjulia Nanaa, hakika alijua atashinda tu.

Akaweka mkakati wa kumuoa kwa haraka sana hata ikimlazimu ndoa ya serikalini ambayo alijua haitakuwa na mlolongo mrefu. “Jamaa kaniwahi kwa mtoto, mimi namuwahi kidoleni.” Akajisemea Zac usiku huo. “Halafu namfungia. Nikishamfungia, simtoi humo ndani mpaka nihakikishe amebeba mtoto wangu na mimi.” Akaendelea kujiwekea mikakati. “Lakini jamaa anaonekana mambo yake safi. Nanaa ana hali nzuri. Nitaweza kweli kushindana naye?” Akajivunja tena moyo. “Hapana. Hata kama anapesa za kunizidi mimi, mbona Nanaa anaonekana bado hana furaha? Jamaa anaonekana ni kweli hamjali. Mimi bado nipo kwenye nafasi nzuri tu.”  Akajitia tena moyo. Akapandisha ujasiri. Akajitia morari zaidi.

“Kama kweli angekuwa yupo kwenye mikono sahihi, nina uhakika asingetulia mikononi mwangu kwa kiasi kile. Ni kweli nimechezea shilingi chooni. Lakini bado najiona nina nafasi kubwa sana kwa Nanaa. Mimi ni Zac bwana! Mtoto wa mjini. Lazima nikieleweshe.” Akachukua simu, akamtumia ujumbe Nanaa. ‘Usiku mwema mpenzi wangu. Nitakuona kesho.’ Mpaka anapitiwa na usingizi, ujumbe haukuonekana kufika.

Kwa Nanaa!

“Nakosea wapi kwa hawa wanaume jamani!?” Nanaa aliwaza huku machozi yakimtoka gizani pale alipokuwa amelala na mtoto wake. “Geb amenionyesha wazi hanihitaji, nipo hapa kwa ajili ya mtoto. Mpaka lini? Ikitokea anaoa kesho, inamaana nitabaki humu ndani na mkewe kwa ajili ya kunyonyesha tu. Nitaweza? Heri niendelee na maisha yangu. Peke yangu? Oliva wangu je? Nimuache kweli? Zac alinipenda sana na bado anaonekana kunihitaji. Alikosea wapi? Ni nini kilimsababishia anisaliti? Alipatwa na nini? Nimpe nafasi nyingine tena?” Nanaa aliendelea kuwaza huku akifuta machozi. 

“Labda nikamsikilize ili nijue. ‘jini likujualo, halikuli, likakwisha’.” Nanaa alijiambia. “Heri nirudi kwa Zac ninayejua ananipenda, hata kama ananidanganya, lakini hajawahi kunifanyia unyama kama Geb. Geb hanihitaji mimi maishani. Nisije nikamkataa Zac sasa hivi, Geb akanifukuza, nikaishia kuwa peke yangu. Sitaki kuja kuanza mahusiano na mwanaume mwingine tena. Kwanza Zac alinionyesha wazi amempokea Liv.” Nanaa akajifariji, ili tu kujitia moyo kwenye maamuzi yake. 

“Hata kama nikiondoka hapa, Geb akanikatalia kuondoka na mwanangu, nitamuomba kazi ya kumlea mwanangu, mimi mwenyewe. Niwe naingia asubuhi, natoka usiku wakati Oliva wangu analala. Nitahakikisha hatahisi kama sipo naye. Nitashinda na mwanangu siku nzima! Usiku narudi kwangu na Zac. Nianzishe familia yakueleweka na Zac.” Nanaa aakaanza kujiwekea mikakati. ‘Lakini itakuaje kama Zac akiamua tuondoke nchini? Itakuaje kama Geb akinikatalia kuondoka na Liv? Hata iweje sitawahi kutengana na mwanangu. Labda kifo pekee.’ Tayari akaanza kuona ugumu wa mikakati yake.  Lakini akaendelea kuwaza. 

~~~~~~~~~~~~~

Akaamua kuwasha simu yake, akakutana na ujumbe wa Zac. Akausoma na kuamua kurudisha majibu kumwambia Zac usiku mwema na yeye. Wakaanza kuchat tena kwa muda mrefu. Nanaa akitoa vipingamizi vyote anavyoona vipo mbele yake hata kama akimsamehe. Zac naye alitumia hiyo nafasi vizuri sana. Akijibu na kumtoa Nanaa wasiwasi. Alimpa mikakati kabambe, endapo watakuwa pamoja. Nini watafanya wakiwa pamoja ili kuwa na amani na pia wasimpoteze Oliva. Alimbembeleza Nanaa na kumuonyesha anamuhesabu kwenye maisha yake. Vile anavyomuhitaji. Vile maisha ambavyo hayajakuwa sawa tokea waachane! Akampanga mpaka Nanaa akaanza kuingia kwenye mstari. Akajikuta wanakubaliana, kesho kuonana tena ili wazungumze zaidi.

~~~~~~~~~~~~~

Kikubwa alichokuwa akikwepa ni upweke. Alijiapia hatawahi kuja kuwa peke yake maishani. Kwa garama yeyote ile, ataolewa na kuanzisha familia na mwanaume yeyote atakayekuja kuwa tayari kumuoa. Yeye kama yeye Nanaa hakuwahi kufungulia moyo wake kwa wanaume ila mwili tu. Angalau kwa Geb alihisi kupenda kwa mara ya kwanza, lakini Geb alimuonyesha hamuhitaji! 

~~~~~~~~~~~~~

Oliva alianza kuhangaika, akamtoa mama yake kutoka mawazoni, akakaa kwa haraka. Moyo wake ulijaa furaha mara baada yakuwasha taa, na Liv kumpa tabasamu. “Nina hamu na wewe Liv mwanangu! Punguza kulala basi ili tuwe tunaongea! Muone unavyojinyoosha. Utaachika! Mwanamke gani unapenda kitanda hivyo? Eti Liv mama? Njoo kipenzi changu. Njoo eeh!” Geb akamsikia Nanaa akiongea na mtoto, akajua ameamka. Na yeye akapata sababu ya kuamka.

          “Na mimi naomba nimuone. Nina hamu naye!” Nanaa alishitukia Geb anaingia, akakuta ananyonyesha. Macho yake yakatua kwenye matiti yaliyokuwa yakimpa usingizi kabla Oliva hajayamiliki. Nanaa akamuona amekodolea macho matiti yake, akavuta mtandio wake aliozoea kumfunikia Oliva wakati akinyonya, akajifunika yeye na mtoto. Geb akagutuka akaona ajibaraguze tu. “Ukimaliza kumnyonyesha utaniita basi. Nipo hapo chumbani.” Oliva akaanza kuhangaika mle ndani. “Amesikia sauti yako naona hataki kunyonya tena, anakutafuta.” Nanaa akamtoa, akaona vile Geb alivyofurahi. “Nimshike kidogo. Ninahamu naye kweli! Asubuhi niliondoka akiwa amelala.” Geb akajisogeza.

“Njoo mama. Njoo mama yangu mzazi.” Geb akampokea, akambusu, nakumuweka kifuani. Nanaa alimuona akifunga macho kama anayesikilizia furaha moyoni, akanyanyua mkono wake akaubusu nakumuweka mbele ya uso wake. “Unalala sana Liv jamani! Mpaka tunakuwa na hamu na wewe!” Geb aliongea na mwanae, Liv alibaki akimwangalia baba yake. Geb akambusu mara kadhaa huku akimchezea. “Manywele haya, tutaanza kuyakata na kuyauza. Tufanye biashara. Eti Liv wangu? Naona yanazidi kujaa kichwani.” Geb aliongea akisikika akimsifia mwanae. Nanaa akacheka. “Naona mimi nitakuwa mteja wenu wa kwanza.” Geb akacheka. “Eti Liv? Tuanze biashara? Mteja wa kwanza tumeshampata.” Geb aliendelea kumchezea.

“Changamka basi mama! Mfanyabiashara gani mpole hivyo? Tuchangamkie pesa, mchana kweupeee!” Liv alianza kucheka na kumfanya Geb azidi kucheka kwa furaha.

 “Angalau roho imetulia. Sasa hivi nenda kanyonye, halafu tukacheze, tumpishe mama apumzike.” “Kesho hutakwenda kazini?” Nanaa akauliza, akishangaa kwa nini Geb achelewe kulala wakati kesho yake ni siku ya kazi. “Kesho sitakwenda kazini.” Nanaa akafurahi sana. Akajua mambo yake yatakaa sawa. Atamuachia mtoto, yeye akamalizane na Zac. Hata hivyo alikuwa na hamu naye. “Kesho nikakate kiu.” Nanaa aliwaza akatoa tabasamu aliloliona Geb. Akaona ni bora atoke ili kumpa nafasi ya kunyonyesha kwa uhuru si kujifunika. “Nitakuwa hapo chumbani.” “Sawa, nikimaliza, nitamleta.” Geb akatoka.

Nanaa na yeye akacheza na mtoto wake kwa muda mrefu, Geb akiwasikiliza Nanaa akiongea na kucheka. “Hamna kunyonya mpaka tuongee leo.” Nanaa alisikika. Alimuimbia taratibu huku akimtania mtoto wake, mwisho akasikia anapewa ziwa. “Njoo ule mwanangu. Usilale ili ukacheze na dad. Sawa Liv? Hamna kulala.” Nanaa aliendelea, kimya kikazuka, Geb akajua ameshaanza kunyonya. Akacheka.

Hakumaliza hata dakika mbili, tayari Oliva alisharudi kulala. Nanaa aligutuka kutoka mawazoni akichezea nywele za mwanae, aliyekuwa amelala bila habari. Akagundua alishalala  “Jamani Liv wewe! Amka bwana!” Lakini hata hakufungua macho. Kila mama yake alipomkuna miguuni ili aamke, yeye aliongeza kunyonya kwa nguvu bila kufungua macho. Akamuona ameachia chuchu, akajua ameshashiba. Akamuweka begani ili ateuke. Akateuka. Akamwangalia tena diaper, akamuweka kitandani kwake, akabaki akicheka. “Unaturingia wewe!” Nanaa akatoka.

~~~~~~~~~~~~~

“Geb!” Akasikia sauti tulivu mlangoni kwake. Akakaa. “Ingia tu.” “Nilihisi umelala, kumekuwa kimya!” “Hapana. Nawasubiri wewe na Liv.” “Mwanao amelala hana hata habari!” Wote wakacheka. “Ndio atakuwa haraka. Ilimradi ananyonya, mwache alale. Karibu.” Nanaa alishangaa anakaribishwa. “Asante. Ngoja nikuache upumzike.” “Nanaa!” Geb aliita kwa utulivu akabaki akimwangalia Nanaa aliyekuwa amesimama pale mlangoni, ameshikilia mlango. “Abee.” Akaitika kwa upole na heshima zote. Alivaa nguo nzuri ya kulalia. Ilikuwa na kitambaa cha silk, nyeusi. Kilikuwa kigauni, kama shumizi. Geb alibaki akimtizama kwa uchu, Nanaa akainama. Alibana nyele zake sehemu moja ili zisimsumbue wakati analala. Alivutia kumtizama. Ukimya wa muda ulipita.

“Usiku mwema.” Nanaa alinyanyua uso, akaaga. “Nilikuita Nanaa.” Nanaa alibaki akibabaika asijue aongee nini, Geb akabaki akimtizama. “Abee.” Akarudia tena kuitika huku akimtizama kwa shida. Nanaa alipenda kuangaliwa na Geb. Macho yake yalikuwa kama moto unaoyeyosha matatizo yote moyoni mwake, hasa akimwangalia akiwa ametulia kama wakati huo. Akaingia ndani, akafunga mlango na kusimama mlangoni huku amekusanya mikono yake pamoja asijue aseme nini. Akamkumbuka Zac. Kwa kuwa Geb hakuwa amesema kitu, akaona avunje ukimwa ili kuyatoa macho yake kwenye mwili huo wenye nguo ya kulalia tu. 

“Geb!” Nanaa akaita akanyanyua uso, macho yake yakagongana na Geb aliyekuwa bado amejiegemeza kitandani akimwangalia. “Kesho umesema huendi kazini?” “Ndiyo.” “Naomba asubuhi nitoke nikuache na Liv kwa muda mfupi kidogo, nitakwenda mahali, kama baada ya lisaa au lisaa na nusu nitakuwa nimerudi. Nitajitahidi nisichelewe.” Mapigo ya moyo yalianza kwenda kasi. “Unarudi tena kwa Zac?” Geb aliuliza swali la moja kwa moja lililombabaisha Nanaa, nakushindwa aseme nini. Akajua mama yake amemwambia kila kitu, akainama. 

“Eti Nanaa? Umeamua kurudi tena kwa Zac?” “Sijui Geb.” “Hujui nini?” “Nilikutana naye leo nilipokuwa na mama, akaniomba tukutane tuzungumze. Zac yeye ananonekana bado ananihitaji kwenye maisha yake.” Lile neno lilizidi kumuuma Geb. “Nilikwenda kuonana naye jioni hii nilipokuaga, lakini nilishindwa kuzungumza naye.

Ameomba kuniona tena kesho.” “Kwa hiyo unaenda?” Nanaa hakujua anamaanisha nini wakati ametoka kumuomba abaki na Liv, yeye atoke. Wazi alishamjulisha anakwenda kukutana na Zac. “Sasa anamaanisha nini tena!?” Nanaa akajiuliza.

“Naona nimekimbia vyakutosha Geb. Najihisi ni wakati mwafaka wa kusimama na kusikia ukweli. Umri umekwenda. Sitarudi tena kuwa msichana mdogo. Siwezi kubadili yaliyotokea, kwa kuwa nimekuwa nikikimbia bila kujua ukweli. Japokuwa naumia, lakini naona nimpe Zac, mwanaume aliyeonyesha kunipenda na kunijali, nafasi ya kumsikiliza.” “Ili muanze naye maisha?” Geb akauliza. “Sijui Geb! Sijui atanipa sababu gani ya kwa nini alilisaliti penzi letu.” Geb alitamani kuchanganyikiwa. 

“Halafu kwa Zac sitakuwa naanza Geb. Nitakuwa nikiendelea. Nilikwambia jinsi Zac alivyokuwa akinipenda na kunijali. Hajabadilika. Mpaka naachana naye leo, alinionyesha ananipenda na kunijali, mimi. Nimejiuliza kwa nini arudi tena kwangu, tena baada yakunikosea. Au kwa nini amenitafuta tena? Jioni hii wakati nimemuacha pale mgahawani, nilimpiga marufuku asinitafute tena. Lakini Geb, Zac amenitafuta tena. Zac ananionyesha kwa vitendo ananihitaji. Hawezi kulala vizuri, akihisi nitalia. Hawezi kuniacha ninalia, hata kama itamlazimu kuahirisha mtihani au vipindi, atabaki na mimi mpaka nitulie ndio ataondoka! Zac alikuwa akitaka kunisikia kila wakati!” Nanaa akaendelea taratibu.

“Japokuwa alinisaliti, lakini Geb, nimeshakaa na wanaume baada ya Zac, nimeona wachumba wa rafiki zangu, bado sijapata wakumlinganisha na Zac. Anafurahia akiniona ninafuraha. Hata kama ananidanganya, lakini najisikia furaha na amani katika huo uongo. Napata kile ninachokitafuta, ndani ya huo uongo wake. Zac ananithamini kuliko ambavyo nitakueleza. Nimeamua kumpa nafasi ya kumsikiliza. Ikitokea anaomba radhi, najihisi kuruhusu nafsi yangu kumpa nafasi ingine tena. Ili nione tutakapofika tena.” Geb alikuwa ametulia pale kitandani kama aliyekufa ganzi. Nanaa akaendelea.

          “Sina chakupoteza tena, sina haraka. Sasa hivi nina Liv, na yeye amempenda mtoto wangu. Nimemueleza maisha yetu. Mimi, wewe na Liv. Zac amekubali na ameahidi tutafikia muafaka tu ili nisimkose Liv kama nikiwa naye. Amepata ahadi ya kazi yenye mshahara mzuri. Ameniambia Mungu akimbariki hiyo kazi, itatusaidia kipindi hichi ninacholea. Amenishauri kama nitamsamehe, nakurudiana naye, ameniahidi tutafunga ndoa. Kisha tutakuomba badala yakuajiri msichana wa kazi, basi unipe mimi kazi ya Liv.” Nanaa alianza kulia. 

“Atakuwa akinileta nyumbani asubuhi na mapema kabla hujaenda kazini. Nitakuwa na Liv siku nzima mpaka usiku atakapokuja kunichukua Zac, turudi nyumbani. Sitataka chochote kutoka kwako, Geb. Nitafanya kwa bure kabisa. Ilimradi tu unipe nafasi ya kumlea Liv kama sasa hivi. Na sitazaa mtoto mwingine, mpaka Liv awe mkubwa. Nitafanya chochote utakacho ilimradi tu naomba unipe kazi yakumlea mwanangu.” Geb alishangaa na yeye machozi yanamtoka.

Nanaa akashituka kidogo. Akakausha ya kwake. Akabaki hajui ni nini kimempata, ‘Bosi dad wake’.  “Geb! Sio kwa haraka. Pata muda wakufikiria.” Geb hakujibu. Nanaa hakuwa anaelewa. Alisogea mpaka pale kitandani, akakaa. Geb akainama, akafuta machozi. “Nimekosea?” Nanaa akauliza kwa upole na wasiwasi. “Geb! Nimekosea nini?

Nimekuudhi?” Nanaa akauliza tena. “Kama ni juu ya Zac, usiwe na wasiwasi naye. Sitamruhusu hata amsogelee Liv. Nitamwambia asifike hata ndani nyumbani kwako. Kama nikunishusha, atanishusha nje ya nyumba yako. Hataingia.” Kimya. “Tafadhali Geb, niambie kitu chochote. Usiniache njia panda, nikiwa sijui unawaza nini!” Nanaa akabembeleza. Asijue wivu na hukumu aliyoiacha kwenye moyo wa Geb. 

~~~~~~~~~~~~~

Anajirudije tena kwa Nanaa baada ya vituko vyote alivyomfanyia? Ndilo swali lililomziba mdogo Geb, nakushindwa kutoa neno hata moja na kwa mara ya kwanza kujikuta akitoa machozi mbele ya mwanamke, tena baada ya kujiapia hatalizwa tena na mwanamke. Historia inajirudia tena! Anaachwa na mwanamke mwingine, kwa sababu ya mwanaume mwingine. Geb aliinama. Akajikuta machozi yakimtoka tena. Hisia zilimrudisha kwa msichana wake wakwanza aliyemlilia mpaka karibia kutaka kujiua. 

Sasa hivi tena ni Nanaa. Lakini Nanaa hakuwa na kosa. Alimfukuza yeye mwenyewe. Anajirudije tena kwa msichana, aliyekwisha muomba msamaha wa machozi kiasi kile, nakushindwa kumsamehe? Leo Nanaa anatangaza kurudi kwa mpenzi wake wa zamani, atamzuia vipi?  Si utakuwa ubinafsi tu!

~~~~~~~~~~~~~

Geb alishindwa hata kunyanyua uso kumuangalia Nanaa. Nanaa aliogopa hata kumshika. Walikaa pale kwa muda, Nanaa akiwa pembezoni kabisa ya kitanda, Geb amekaa katikati ya kitanda chake ameinamisha kichwa chake. Alipotulia tu, Nanaa akasimama kama mshale. “Usiku mwema. Nitakuona kesho.” Akatoka, bila kujibiwa.

Nanaa alikwenda kulala, asijue kinachomliza Geb. Akajiuliza maswali mengi akihisi amemkosea, lakini akajiaminisha kuna lake linamliza sio yeye. “Asubuhi nikiamka tu, naenda zangu kwa Zac.” Nanaa alijiambia wakati anapitiwa na usingizi. Geb aliendelea kuwaza hili na lile akihesabu hasara zote. Akijutia hili na lile. Akaliona anguko lake kwenye maisha. “Ndio maana Zac mwenzangu amerudi. Hakuna mwanaume aliyeishi na Nanaa, akamuacha na kufanikiwa kimaisha. Nimekwisha Geb, mimi.” Geb aliendelea kuwaza huku machozi yakimtoka. 

~~~~~~~~~~~~~

Ilishakuwa saa nne asubuhi wakati Geb alipoamshwa na maongezi ya Nanaa na Liv. “Hakuna kulala tena Liv. Lazima dad akuone. Amebaki leo kwa ajili yako. Usinichekee bwana! Twende tukampikie dad uji. Nitakufundisha ili uwe unampikia kila siku, asiwe analala na njaa. Umesikia Liv? Twende.” Geb aliwasikia wakitoka chumbani, akatoka. “Jana hukula Geb.” Nanaa alimuwahi mara Geb alipotoka chumbani kwake. Geb akabaki akimwangalia Nanaa. Alipendeza, akionyesha wazi yupo tayari kutoka.

“Mama ameleta vyakula, vipo mapokezi.” “Jamani mama yangu! Anahangaika kweli! Angeacha tu nikapika. Halaf..” Nanaa akanyamaza kidogo kama anayefikiri. “Kwa nini aache vyakula mapokezi, asiingie humu? Ni nini nimemuudhi? Au..” Nanaa akapooza. “Nimekosea? Niambie ukweli Geb. Sitaki kumuudhi mama, wala wewe. Nilipokesea nitarekebisha haraka. Nini kimemuudhi mama, nakushindwa kuja kuniona mimi na Liv!? Sio kawaida yake!” Nanaa akaanza kulia kama kawaida yake, machozi ya karibu. “Hajawahi kuacha kuniona tokea nimerudi na Liv.” “Nanaa! Nanaa!” Geb alimkatiza kutaka atulie asiendelee kulia.  

“Mimi ndiye nimemuomba leo asije.” Nanaa akafuta machozi akamwangalia Geb kwa kushangaa. “Kwa nini!?” “Sikujua kama unamiahadi mingine tena na Zac. Nilimuomba mama leo anipe nafasi na nyinyi. Nilitaka muda na wewe Nanaa, pamoja na Liv. Nilimuomba jana kabla hujanitaarifu kuwa unakwenda na leo kukutana na Zac!” Hilo likamtuliza. “Niliingiwa na wasiwasi nikajua nilimkosea!” Akamsogeza Liv kwa baba yake. “Naona anakaribia kusinzia huyu. Leo ameamka mapema! Nimeona bibi yake anachelewa kuja kumuogesha, nimecheza naye tu sikutaka nimuogeshe. Maana akioga tu angelala kabla hujamuona. Na akilala sasa hivi, atachukua muda kuamka. Pata naye muda sasa hivi kabla hajarudi kulala.” Nanaa akamkabidhi. Geb akamtizama kidogo, akarudisha macho kwa mwanae.

~~~~~~~~~~~~~

Alijua Nanaa anamkwepa. “Nitarudi muda sio mrefu. Nakwenda kufuata hivyo vyakula mapokezi.” Nanaa akaaga, hakusubiri jibu, akatoka. Alipofika tu mapokezi kabla hajamfikia muhudumu, Zac naye akasogea. “Hee! Ulilala hapa hapa!?” Nanaa akamuuliza kwa mshangao. “Nimefika muda sio mrefu.” Akamsogelea na kumkumbatia kwa upendo. Akiwa kifuani kwa Zac, akajikuta machozi yakimtoka. “Zac anaonekana kunipenda sana. Kwa nini alinisaliti?” Hilo swali bado lilimsumbua na kumfanya ashindwe kujizuia. “Natamani ingekuwa kama zamani Zac!” Nanaa aliongea kwa upole akiwa bado amekumbatiwa. Zac alisikia, akamvuta mbele kidogo akabaki amemkumbatia huku akimwangalia. “Nilikosa Nanaa.” “Hilo ndilo tatizo Zac.” Nanaa aliendelea kulia taratibu huku macho yake yakiangalia kifua cha Zac, kama aliyeinama. Zac alitoa mkono mmoja nyuma ya mgongo wa Nanaa na kuanza kumfuta machozi.

“Ndio umekuja ili tupate muda wa mazungumzo?” Zac akauliza. “Hapana. Nimefuata chakula.” Nanaa akajibu huku bado amekumbatiwa. “Unataka tukae hapa tule wote?” “Geb leo yupo nyumbani. Hiki chakula mama yake ndio ameleta sio chakununua. Huwa hali vyakula vya kununua, kwa ufupi hapendi kula kwa hiyo vyakula vyake vina jinsi yakupikwa.” Akatoa tabasamu. “Kwa hiyo mama yake huwa anampikia mara zote. Ngoja nikichukue, nimpelekee. Nimemuacha na Liv. Nitarud..” Akamuona Zac ametoa macho yake anaangalia kwengine kama aliyeona kitu.

          Akiwa bado amekumbatiwa na Zac, akageuza kichwa, ndipo alipomuona Geb na Liv na wao wanaingia hapo. Kidogo alibabaika, lakini akagundua hana kosa analofanya. Geb si mpenzi wake tena, ni mzazi mwenzake tu. Lakini akakumbuka alimuaga anakwenda kuleta chakula, akaishia kukutwa amekumbatiwa! Akajitoa mikononi kwa Zac. “Samahani nimechelewa kurudi.” Ndilo neno lililofanikiwa kutoka mdomoni mwake huku akionyesha wasiwasi na hofu ya wazi kabisa. Akahisi anashikwa mkono taratibu. Akamgeukia Zac, akamkuta na tabasamu lililoashiria kumtuliza, asiogope. Nanaa akamgeukia Geb aliyekuwa amesimama na yeye akiwaangalia kwa utulivu tu bila paniki.

“Naenda kuchukua sasa hivi, nikilete ndani.” Nanaa akarudia. “Hamna shida. Niliamua kukufuata ili kumtoa Liv ndani. Nataka kumtembeza kidogo asirudi kulala kwa haraka.” Geb alirudisha macho kwa mwanae, ukimya ukapita. Nanaa akahisi mkono wake umeminywa na Zac, akageuka akamtizama. Bado walikuwa wameshikana mikono. “Geb! Huyu ndio Zac.” Nanaa alimtambulisha kwa unyonge, Geb alinyanyua macho kutoka kwa mwanae akayatupia kwa Zac bila kusema kitu. Nanaa alivyoona hivyo, akageuka kwa Zac. “Huyo ndio Geb, baba yake Oliva.” “Asante kwa utambulisho. Nimefurahi kumfahamu.” Zac alimjibu Nanaa, tena kwa kumwangalia yeye wala sio Geb. Kimya.

“Ngoja nikachukue chakula, halafu nikamnyonyeshe Liv, ndio nitakuja tutoke.” Nanaa akaaga. “Sawa, nitakusubiri. Lakini kuna zawadi zako kwenye gari. Nilikununulia kabla sijarudi hapa nchini. Naweza kukusaidia kuzibeba mpaka ndani, kama utakuwa na mzigo mkubwa. Tuziache kwako, sitaki kuendelea kuzunguka nazo.” Nanaa akacheka kwa deko. “Ulijuaje kama utanipata sasa?” “Penye nia pana njia Nanaa, mbona unakuwa msahaulifu?” Wote wakacheka kidogo. “Haya bwana, asante kunikumbuka. Nenda basi kafuate zawadi wakati mimi nachukua chakula. Nitakusubiri hapa.” Zac alitoka kwenda kwenye gari lake, Nanaa akaelekea mapokezi bila hata kumtizama Geb.

Baada ya kusalimiana na kijana aliyemkuta hapo mapokezi, akamuomba mzigo wao. Geb akamsogelea. “Kama ni mzito, naweza nikakusaidia kubeba.” Nanaa akageuka baada yakusikia sauti ya Geb nyuma yake. “Wewe mbebe Liv, mimi nibebe hivi vyakula. Kwanza atakuwa na hamu na wewe. Muone anavyoshangaa.” Wote walirudisha macho kwa Liv aliyekuwa amebebwa kwa kugeuziwa mbele ili asilale kifuani kwa baba yake. “Eti Liv? Ulikuwa na hamu ya dad?” Geb alimtekenya kidogo na kumbusu mgongoni. Wakati makapu mawili ya vyakula yamewekwa juu ya kaunta, Geb na Nanaa wakishangaa vyakula vilivyo vingi, Zac naye akarudi na mfuko mzuri, ulionekana ni wa zawadi. 

Nanaa akamgeukia vizuri na kucheka kumuonyesha amefurahia ile zawadi, kisha akarudisha macho kwenye vile vikapu vya vyakula. “Jamani mama! Sijui hata kama amelala leo. Vyakula vyote hivi! Nitampigia simu nimshukuru. Kwanza nimeshapatwa hamu naye. Lazima aje atuone kidogo. Siku haiwezi pita bila kuonana na mama.” Nanaa aliendelea kuongea peke yake bila kujibiwa na mtu. Wanaume wote wawili walikuwa wamemsimamia pale nakumfanya azidi kubabaika. Kuongea pekee ndiko kulikokuwa kukimtoa hofu.

Akamgeukia Zac akampa tena tabasamu. “Nashukuru, lakini hukuwajibika kufanya hivyo bwana.” “Wewe nenda kafungue kama hujarudi unarukaruka kwa furaha. Mambo yako matupu humo ndani.” Zac alimfanya Nanaa acheke zaidi. “Haya Zac. Nashukuru.” “Niwasaidie kubeba mpaka ndani?” Zac akauliza, Nanaa akamgeukia Geb, Geb akamtazama Zac. 

Shilingi Imepinduka.

“Naweza kuwasaidi mizigo.” Zac akarudia huku akimtizama Geb. “Hukaribishwi kwetu, na wala nisingependa kukuona karibu ya mlango wa nyumbani kwetu.” Geb alijibu kwa utulivu huku akimtizama Zac machoni. Nanaa akashituka sana, nakuogopa zaidi. “Nimekosa nini!?” Zac akauliza kiungwana. “Kucheza na hisia za Nanaa, hilo ndilo kosa lako. Unamdanganya. Huna mapenzi ya kweli kwa Nanaa. Kwa kuwa unamfahamu anataka nini, shida yake ni ipi, ndio maana unacheza na hisia zake vile utakavyo. Unajua ni lugha gani sahihi utakayo itumia kwa Nanaa na kumfurahisha au kumfanya ashindwe kufikiria kitu kingine chochote ila wewe na uongo wako tu.” “Sio kweli. Mimi nina mapenzi ya dhati kwa Nanaa.” Zac akajitetea kwa ujasiri.

Geb akamuweka mtoto vizuri, kisha akaendelea. “Unatumia machozi ya Nanaa, kujinufaisha naye. Unatumia upweke wake, kujinufaisha nae. Tena kwa muda, ukiwa huna mipango ya kudumu na Nanaa. Acha kumdanganya Nanaa, na sitakuruhusu uendelee kucheza na hisia zake.” “Sichezi na hisia za Nanaa. Nampenda Nanaa.” “Kama kweli unampenda Nanaa, mwambie ukweli wa maisha yako yote. Usimdanganye.” “Ndio nataka nikamwabie ukweli.” “Anza kwa kuwa muwazi sasa hivi. Hapa hapa mbele yangu. Anza kwa kitu kidogo tu. Anza kwa kumweleza ukweli  kati yako wewe na Ndina.” Wote wakashituka na kumgeukia Geb.

Nanaa akarudisha macho kwa Zac. “Amemfahamuje Ndina?” Nanaa akamuuliza Zac kwa upole. “Naomba umuulize maswali sahihi, Nanaa.” Geb akaingilia. Nanaa akamuangalia Geb kisha akarudisha macho kwa Zac. “Zac! Ukweli gani juu yako wewe na Ndina?” “Ulitaka kujua kipengele gani?” Zac aliropoka, na kumchanganya zaidi Nanaa, Geb akacheka kwa kicheko cha kumkejeli. “Kipengele tena? Kwani vipo vingapi!?” Nanaa akauliza, lakini Zac alinyamaza akamgeukia Geb. “Shida yako ni nini Geb? Kwa nini unafanya hivyo?” Zac akamlaumu Geb.

 “Kwani mnafahamiana na Zac?” Nanaa akauliza. “Kama kweli unampenda Nanaa, mwambie ukweli.” Geb akajibu. “Ni habari ndefu Nanaa, twende tukazungumze.” Zac akabembeleza. “Hata sio ndefu! Msimulie tu kwa kifupi. Akikubali na kukuelewa, akaondoka na wewe sasa hivi, sitakuwa na neno. Lakini sitakuruhusu utoke na Nanaa leo, kabla hajajua ukweli wote. Mtatoka naye tu, endapo utamwambia ukweli, akakujua vizuri, halafu bado akaamua kutoka na wewe.” Geb aliongea huku akimsogelea yule kijana pale mapokezi.

          “Naomba nisaidie kikombe.” Alizungumza na muhudumu. Alipopewa kikombe, akachukua kapu lililokuwa na chupa ya uji, akakaa kwenye meza ya pembeni yao akafungua chupa ya uji, akajimiminia na kuanza kunywa uji aliokuwa ameletewa na mama yake taratibu huku akiwatizama. “Unamfahamu Zac?” Nanaa akamuuliza Geb kwa upole. “Ndiyo. Lakini sikujua kama Zac huyu, ndiye Zac uliyekuwa ukimzungumzia wewe. Mpaka hivi leo nilipowakuta mmekumbatiana hapa. Ndio nikajua Zac huyu unayemwita wewe mpenzi wako, ndiye…..

 ~~~~~~~~~~~~~

Usikose Muemdelezo.

Zac Ni Nani?

Amefahamiana Vipi Na Geb?

Yote Na Mengine Mengi Yapo Mbeleni.

 


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment