Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Ni Wangu! - Sehemu Ya 32. - Naomi Simulizi

Ni Wangu! - Sehemu Ya 32.

Oliva alilia mpaka baba yake akasalimu amri. “Naomba nisaidie mama. Mtoto wangu anapandisha homa.”  Mama G, akashitukia Geb amemsimamia pembeni ya kitanda chake, amechoka kama anayetaka kulia na yeye. Geb huyu ni baba wa mtoto anayempenda sana lakini kwa usiku huo yeye mwenyewe na vyote alivyonavyo vimeshindwa kumsaidia mwanae. “Nakusaidia vipi wakati hutaki nimshike mwanao?” Akaona machozi yanamtoka. Akajua ameshapatikanika. Geb si mliaji kama Grace. Akajua ubaba umemuingia kama si majuto.

“Naomba nisamehe mama. Nisaidie.” “Sasa sikiliza. Huyo mtoto ameshamjua mama yake. Anajua maziwa ya mama yake na anajua joto na harufu ya mama yake. Hakuna tutakachomfanya sasa hivi akatulia, mpaka mama yake.” “Sijui Nanaa alipo.” “Wewe si ulimwambia ikifika saa 12 asirudi hapa?” Geb kimya. “Mwenzio amelala sasa hivi.” “Wewe unajua alipo?” “Ndiyo.” Mama G akamjibu huku akimwangalia machoni. Bado Liv alikuwa akilia chumbani kwa baba yake.

 “Naomba niambie alipo.” “Kwani maziwa ya kopo ameyakataa kabisa?” “Mama jamani! Si umeona pale amekataa!” “Kamjaribishe tena.” Mama G alikuwa akimkejeli tu. “Naomba niambie Nanaa alipo. Tafadhali mama!” Akajifuta machozi. “Si umpigie simu mwenyewe umuulize kama atakubali umfuate? Kama yupo na mtu wake wanataka kupata muda mtulivu je?” Alizidi kumkera. “Sina namba ya Nanaa?” “Hee! Huna namba yake!?” “Naomba usiniadhibu mama. Ujue unamuadhibu mjukuu wako mwenyewe?” “Lini umelitambua hilo? Si ulikuwa ukininyima huyo mtoto? Leo iweje ukumbuke kama ananihusu?” “Nimekuomba msamaha!” “Msamaha wa nini?” Geb alitamani kulia tena lakini mwanae akamzidi. Alikuwa akilia kupita kiasi. Akatoka kwenda kumchukua.

Akarudi. “Naomba msamaha  wa kukugombesha na kukukatazia mtoto.” Geb akamalizia hapo. “Usinitanie Geb!” “Sasa nimefanya nini tena!?” “Uliniambia nini juu ya Liz? Kwa nini alikutwa uchi humu ndani?” “Na mimi nilimkuta uchi pale pale kitandani kwangu. Mungu wangu ni shahidi, mama. Nilikuwa nimetoka safari, nimechoka, sikutaka hata kuzungumza naye, na mimi nikapitiliza bafuni kuoga. Nimetoka bafuni na Nanaa anaingia. Nilijaribu kumtuliza Nanaa ili tuongee lakini hakutaka, akaondoka.” 

“Ulijua amekasirika. Kwanza hamkuwa mmemaliza tukio la kukuona umemshika Liz mkono siku ya harusi, na ukamsahau. Pili akakukuta naye wote mpo uchi. Tena na wewe unajua alishadanganywa na wanaume wengi kwenye matukio kama hayo, kwa nini hukumtafuta tena baadaye ukaweka mambo sawa, tena baada ya kujua atakuwa mjamzito?” “Sikuwa bado nimepata uhakika kama ameshika mimba. Na nilijiambia hata kama alishika mimba itakuwa ilitoka kwa ile hekaheka ya kufanyiwa upasuaji na madawa makali aliyokuwa akipewa. ” Geb akajaribu kujitetea.

          “Kwa nini hukumtafuta?” “Kwa nini tusiendelee na kesi baadaye ukaniambia mahali alipo Nanaa, nimpeleke mtoto?” “Wewe kama una haraka ya kuondoka hapa, jibu maswali yangu yote.” “Nilikosea mama. Nilikuwa nimekasirika. Niliona ananiadhibu bila kosa! Tena ukumbuke ndio nilikuwa nikijiiba kwenda kuwa naye usiku kucha wakati mgonjwa.” “Mwenzio wala hajui kama ulikuwa ukikesha ukimuuguza.” “Ndio nimekuja kugundua hilo mama. Hakuwa hata akijua kama nilimuuguza muda wote huo. Sikufikiria vizuri mama yangu na kipindi hicho na mimi nilikuwa na mambo mengi ya kupanua kwenye biashara ili niache kazi. Nilikosea. Naomba unisamehe kwa kumfukuza Nanaa, najisikia vibaya sana. Najua nimekosea.” Akamsikia mama yake anapumua kwa nguvu kama amepata aghuheni. Akajua ameshasamehe. Akamwambia Nanaa alipo. Geb akatoka kwa haraka.

~~~~~~~~~~~~~

          Bado Nanaa alikuwa akiwaza anakopitia wakati ule, asiamini kama anaweza kunyang’anywa mtoto wake kirahisi kiasi hicho! Usingizi uligoma kuja kila alipofikiria usiku huo atalala mbali na mtoto wake. Aliendelea kukumbuka shida alizopata wakati wa ujauzito wa Liv! Leo Geb anammiliki mwanae yeye anakuwa kama mtu baki tu! Akachukia umasikini kupita kiasi. Alijuta kutokubaki siku ile alipomkuta na Liz, ili kuyamaliza. Alikuwa amejilaza hapo kitandani akiwaza wakati muhudumu wa mapokezi alipompigia simu chumbani kwake, kwa kutumia simu ya mezani ya hotelini hapo.

Simu yake ilishazima kabisa mara baada ya kumtumia ujumbe wa mwisho Mama G, kumtaarifu alipo. Nanaa alishituka aliposikia simu ya mezani ikiita. Akafuta machozi, akapokea. Ndipo alipoambiwa  ana mgeni anataka kwenda hapo chumbani kwake, kumuona. Akasikia sauti ya mtoto akilia sana kwenye simu, akajua ni mtoto wake. Bila kujibu Nanaa alitoka huku anakimbilia mapokezi na yeye akilia. Alimkuta Geb amembeba Liv akilia kama kengele. “Namuomba nikusaidie kumbembeleza.” Geb akampa bila ubishi.

Nanaa akampokea mwanae, akamkumbatia huku akilia sana. Alilia huku akimbembeleza na kumbusu mtoto wake. Gafla yule mtoto akanyamaza. “Naomba nikamnyonyeshe.” Aliomba kwa upole huku akilia kwa uchungu sana. “Naona atakuwa na njaa sana.” Geb akajibu kwa upole kama sio yeye! Nanaa akaongoza njia mpaka kwenye chumba alichokuwa amekodisha. Haraka haraka bila hata kupoteza muda, akamtolea mtoto ziwa, Liv alilipokea, nakuanza kuvuta kwa nguvu. Ulisikika mlio wa Liv tu akinyonya kwa uchu. Nanaa alianza kumchezea nywele zake huku akifuta machozi yake. Alishika mikono ya Liv huku akiibusu. “Pole Liv.” Nanaa aliongea kwa sauti ya chini akimbembeleza mtoto wake kwa upendo.

Geb alibaki amesimama na begi la mtoto begani. “Samahani nimechelewa kurudi.” Nanaa akaomba msamaha huku akilia. “Nilikutana na foleni. Saa 12 imenikuta bado nipo barabarani. Siku nyingine sitachelewa.” Geb alizidi kujisikia vibaya. “Hamna shida.” Geb akajibu. “Hata hivyo uliondoka muda mbaya.” Nanaa hakuamini. Tokea arudi nyumbani kwake, hiyo ndio ilikuwa sentensi ya kwanza na ndefu sana, tena yenye amani kuizungumza kwake. Akajifuta machozi, akabaki akimwangalia mtoto wake. “Naona anahoma!” Nanaa aliongea taratibu huku akimpapasa mwanae. “Nafikiri ni sababu ya kulia. Amelia sana leo. Sikujua kama ni mkali hivyo!”

 “Geb!” Nanaa aliita kwa upole huku machozi yakianza kumtoka tena. “Nakuomba uniruhusu leo nilale naye. Tafadhali sana. Akipona nitamrudisha.” “Unaondoka!?” Geb alishituka sana kama siye yeye aliyemfukuza. “Bado sijapata chumba. Labda kesho ndio naweza kufanikiwa.” “Kwa hiyo ukipata chumba utaondoka?”  Nanaa alianza kulia tena kwa uchungu sana. Akijua ndio anafukuzwa rasmi. “Naomba nikae naye kidogo. Angalau akiacha kunyonya ndio naweza kuondoka. Tafadhali Geb. Niache nimlee hata akifikisha mwaka ndio unifukuze kwako. Nitajitahidi kufuata kila masharti, ili tu nilee mwanangu. Naomba usimkuze hivi kama hana mama! Ni ngumu! Mimi nimepita huko. Nina uhakika hutataka Liv akue hivyo. Ni maisha mabaya sana! Tafadhali usinitengenishe na mtoto wangu.”  Nanaa akaendelea.

“Sikukusudia kukuficha Geb. Siku niliyokuwa nataka kukwambia ndio siku nilikufumania na Liz. Nilikuja kukwambia lakini nikashindwa. Naomba unisamehe.” “Mungu wangu ni shahidi Nanaa, na mimi nilimkuta Liz yupo uchi pale kitandani kama ulivyomkuta wewe. Sikutaka kubishana naye kwa kuwa nilikuwa nimechoka sana, na njaa ilikuwa ikiniuma. Nikaamua nioge, ndio nitoke niende jikoni kutafuta chakula. Nimetoka kuoga, ndio na wewe unaingia pale. Sikumgusa wala kumuongelesha Liz. Mpaka ulipoondoka ndipo nikamuomba funguo zangu za nyumba, na kumwambia asirudie kufanya kitendo alichokifanya tena. Aliomba msamaha, akanipa funguo zangu za nyumba na chumba, akaondoka. Sisemi uongo.” Nanaa alishikwa na kigugumizi asijue anatakiwa aseme nini. Machozi yakakauka gafla, akabaki kimya kwa muda.

“Kwa hiyo naruhusiwa kurudi nyumbani kwako?” Nanaa akauliza kwa wasiwasi kidogo. “Muda na wakati wowote.” Nanaa akakunja uso kidogo, akainama kama anawaza. “Hata ukitaka sasa hivi tunaweza kurudi wote.” Nanaa akamwangalia Geb kama asiyeamini. “Kweli!?” Nanaa akauliza huku machozi yakimtoka tena.  “Kweli Nanaa. Huyo mtoto siwezi kumlea peke yangu na sitaki akue hivyo bila wewe. Liv anaonekana anakuhitaji wewe zaidi sasa hivi kuliko hata mimi.” Nanaa aliinama nakulia sana. Alilia kwa kwikwi na kushindwa kujizuia. 

“Naomba nisamehe Nanaa. Nimekukosea sana. Nashindwa hata nianzie wapi! Naomba unisamehe. Nisamehe kwa masharti niliyokuwa nimekuwekea. Nisamehe kwa kukufukuza kinyama. Nisamehe kwa kukupokonya mtoto. Nisamehe kwa kutokutafuta tena baada ya kunikuta siku ile na Liz, nikakuacha ukiteseka peke yako. Nisamehe kwa kushindwa kutunza ahadi yangu kwako.” Kwa wakati huo Nanaa hakuwa akikumbuka tena ni ahadi gani anayoizungumzia. Akamwangalia akiwa na uso wa kuuliza ni nini anazungumzia. “Nilikuahidi mimi nitakuwa nikikufuta machozi daima. Lakini nimeshindwa. Ile hali yakunikataa huku ukinitukana iliniumiza sana, nikashindwa kujizuia. Iliibua hasira kali sana moyoni kuona mimi nakupenda kwa dhati kumbe mwenzangu huthamini chochote kile! Niliumia sana Nanaa. Yote nilifanya kwa hasira tu.” Nanaa aliinama na kuendelea kulia. Geb alijirudi, akajishusha mpaka akamshangaza, asijue kinachoendelea.

 “Naomba unisamehe. Nisamehe kwa kila kitu. Nimekukosea sana. Naahidi nitabadilika. Nahisi ninahasira sana. Nina tabia yakuweka vitu moyoni na kushindwa kuviachilia kwa haraka.” Baada ya kulia kwa muda, Nanaa akaamua yaishe ilimradi apate mtoto wake. Akafuta machozi akatulia huku akimshukuru Mungu kumpata mtoto wake. “Yameisha Geb.” Geb akabaki na maswali kwa ukubaliji ule wa jumla. “Yameisha umesamehe au umekubali yaishe?” “Vyote. Chamsingi ni mtoto wetu akue na tumpe yale sisi tuliyoyakosa. Nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kumlea tena mwanangu. Nakuahidi kuitumia vizuri.” Geb alipooza toka rohoni. Akaelewa Nanaa ndio anachora mstari bayana. Haitakuwa kama zamani, ameharibu kwa Nanaa. Hawezi kumpokea tena kama mpenzi ila mzazi mwenzake.

“Kwa hiyo usiku wa leo tunafanyaje? Unaniruhusu kulala naye hapa halafu asubuhi ndio nirudi naye nyumbani kwako au unataka turudi sasa hivi?” Nanaa akauliza. Lile swali liliendelea kuonyesha wazi msamaha ule ni wakurudiana kama wazazi wa mtoto lakini sio wapenzi. Akakumbuka ile hali aliyoiacha pale nyumbani kwake. Meza zilizovunjwa na pacha mwenzie, makochi yalivyochanwa akaona asimrudishe pale Nanaa. “Ngoja nitoke kidogo, nitakuwa hapo nje kuna simu nataka kupiga. Kisha nitarudi na jibu kamili.” Geb akatoka.

Baada ya muda akarudi. “Kuna kitu nataka kurekebisha pale nyumbani. Naomba nivumilie kwa siku chache, tutarudi nyumbani. Lakini naomba tuhame hapa hotelini twende kwenye Apartment kwa muda. Nimepata nafasi, wameniambia tunaweza kwenda hata sasa hivi. Hapa kuna kelele za baa, siwezi.” Nanaa akacheka kidogo. “Nilipachukua kwa kuwa bei ni rahisi, halafu nilipanga kulala usiku wa leo tu.” “Kwa hiyo ni sawa tukihama?” “Hamna neno. Ila bado sijamaliza mambo ya chumba, Geb. Nilazima kesho nikamilishe, nifunge mkataba wa kile chumba. Nihakikishe napewa funguo kabisa. Kuna watu wengine wanakigombania. Nikikamilisha hilo, nitaenda kuchukua vitu vyangu kwa Antii, nivifungie hapo. Nikikamilisha hilo nakuahidi nitatulia. Vitu vingine vya hicho chumba, nitanunua taratibu. Siku ambazo najua utakuwepo nyumbani kama jumamosi na jumapili, ndio nitakuwa nikitoka kwenda madukani. Sitarudia kutoka tena jioni. Hata kesho nataka kumuomba huyo mwenye nyumba, tukutane asubuhi.” Geb akanyamaza kwa muda. 

“Nitajitahidi nisichelewe kurudi.” “Ni wapi?” “Kipo mtaa wa Temeke, karibu na benki ya NMB. Ni chumba kizuri tu.” “Utataka tukusindikize mimi na Liv?” “Mmh! Wewe na mwanao huyu mmekaa kitajiri sana bwana. Mtaniponza kama wakati ule. Unakumbuka?” Geb akacheka kidogo. “Unatukimbia mimi na Liv?” “Mwanao huyo ndio kabisaa. Nikienda naye watajua nimezaa na mzungu mwenye pesa. Labda nimvue hizo cheni na hereni zake za dhahabu. Nimfunge kitambaa kichwani na..” “Basi. Mimi naona wewe uende tu.” Nanaa akaanza kucheka. 

“Utarudi, Nanaa?” “Kwa nini unauliza hivyo Geb, jamani!?” “Nauliza tu.” “Hata nikitaka niondoke, sina pakwenda. Lazima nirudi kwa Liv. Nimekuwa bila mama, Geb. Najua ugumu wake, na umuhimu wake. Nitalipa garama zote kuwa na Liv. Hata ikigarimu furaha yangu! Sitajali, nitakaa na mwanangu. Niambie tu muda gani utakuwa na nafasi ili uje ukae na mtoto mimi niende. Nitajitahidi kufanya haraka sana ili nirudi.” “Natamani kukuomba tena usitafute chumba!” Nanaa akanyamaza.

“Nina nyumba mbili za kuishi, Nanaa.” “Ni zako Geb. Mimi siku ile uliponifukuza na kuniambia nitoke, nilikuwa nikilia mengi! Kwanza nilikuwa sijui niende wapi asubuhi ile. Kulikuwa na baridi na tayari nilikuwa nimeshachafuka kwa damu. Pili niliingiwa na hofu ya mtoto wangu. Ile baridi pale nje ilivyokuwa ikinipiga, nilikumbuka vile mama mkubwa alivyokuwa akinifungia mlango nje, ananiambia nilazima nifue mpaka nimalize ndipo nirudi ndani. Sitasahau Geb. Ilikuwa ni baridi kali mpaka vidole vilikuwa vikiganda. Unakuta hapo sina sweta, na nimeambiwa nifulie nguo nje. Upepo mkali, unafua huku unatetemeka baridi! Na huwezi kufua vibaya, kwa kuwa ukimaliza, unatakiwa kumwita atoke nje akague kwanza, ndipo akiridhika uingie ndani uendelee na kazi za ndani. Ukichelewa kumaliza ukakuta mlango umefungwa, ndio ujue nitalala hapo nje mpaka kesho yake asubuhi wao wakiamka, ndio wanifungulie.” Nanaa akaanza kutokwa na machozi.

Nilikuwa nikilia siku ile pale nje kwako, nikiomba Mungu anirehemu. Nilikuwa nikimwambia Mungu ni heri angeniua siku namzaa huyo mtoto, kuliko kuruhusu nipokonywe. Niliingiwa hofu, nikawa najiambia ukifungua mlango, nitakuomba hata unipe kazi ya kusafisha kama wale vijana wanokuja pale kukusafishia nyumba yako, ili tu niwe karibu na Liv wangu. Na nikajiambia, kama hutanifungulia mlango, ule ndio ungekuwa mwisho wangu. Ningejiua Geb. Nilijua hamna mtu angepata hasara, na hamna mtu angejua. Nilipanga nikajiulie sehemu ya mbali ili watu wasihangaike na maiti yangu. Ndio maana hata ulipokuwa ukinipokonya mtoto, hutaki nilale naye kitanda kimoja, nilijiambia ni afadhali hivyo kuliko kukosa kabisa.” Geb akanyamaza kimya na Nanaa akanyamaza, akabaki akifuta machozi.

“Tunaweza kuondoka sasa hivi?” Geb akavunja ukimya. “Hamna shida. Lakini bado hujaniambia kesho utakuja kukaa na mtoto saa ngapi ili niweke miahadi na huyo baba mwenye nyumba.” “Nafikiria swala la Liv.” “Nitahakikisha nakuachia maziwa yakutosha.” “Hataki chupa kabisa huyo mwanao.” Nanaa akamwangalia mwanae aliyekuwa amepitiwa na usingizi huku chuchu ya mama yake ipo mdomoni. Akabaki akimwangalia nakumpapasa taratibu. “Asante Geb.” “Kwa nini tena? Maana najisikia vibaya sana Nanaa. Natamani kama ningebadili lile tukio.” “Nakushukuru kwa nafasi uliyonipa ya kumlea mwanangu.” Geb akabaki kimya, akashindwa hata kujibu.

Nanaa & Geb Kwenye Apartment.

W

alitoka hapo, wakahamia kwenye apartment nzuri na ya kisasa. Ilikuwa na vyumba viwili tu, jiko zuri na sebule iliyojazwa na kupangwa makochi na meza nzuri. Nanaa alienda kukaa sebuleni akiwa amempakata mtoto wake. “Kabla sisi hatujaenda kulala, naomba simu yako nimtaarifu mama kuwa tupo hapa.” Geb akamwangalia kidogo, akampa simu yake. Nanaa akampigia Mama G. “Pole mama, nimekuamsha?” “Wala usijali mwanangu. Umemuona cha ulizi wako? Wamekuletea huko huko.” Nanaa akacheka. “Mimi sijui huyu Liv amefuata wapi kulia hivi! Mimi si mlizi hivi. Amelia hoteli nzima wakajua kama amefika!” Mama G, akacheka. “Jike la nguvu huyo. Akifika mahali lazima watu wote wajue kama Oliva Magesa yupo. Sio watu wakae kihasara hasara.” “Mwenyewe huyooo!” Nanaa alimtania Mama G.

“Kumbe! Unamuona kwa wasiwasi?” “Hata kidogo, mama. Basi alivyo huyu mjukuu wako, ametulia sasa hivi kama sio yeye. Hataki hata kuamka. Tumehama hotelini tumehamia kwenye apartment, njia nzima namwita aamke ili tuongee, ameninyamazia kimya. Tabia gani hiyo!?” “Mwache apumzike. Amelia sana.” “Jamani Liv wangu! Siku nyingine sitamuacha tena.” “Wakati kesho unamuacha tena!?” Geb akaingilia mazungumzo. 

“Halafu kweli. Ujue amekataa kunyonya kwenye chupa?” “Ameshakujua huyo. Na unavyombembeleza wakati ananyonya, basi anajua ndio anatakiwa afanyiwe hivyo hivyo! Mbona unae huyo.” Nanaa akacheka. “Naona raha mwenyewe!” “Nakusikia hata sauti imebadilika.” “Asante mama yangu.” “Asubuhi nitakupitishia chakula.” “Mama wewe! Pumzika bwana! Nitaagiza chakula hapa hapa, kuna sehemu ya mgahawa.” “Basi maziwa yatakauka. Huko hotelini hawawezi kukutengenezea uji kama ninaokupikia mimi! Mbona unataka kunipunguzia shuguli?” Nanaa alicheka mpaka machozi. 

Geb akabaki akimtizama anavyoongea na mama yake. “Mimi nilitaka upumzike.” “Hata! Acha nimuhudumie wajina wangu. Nataka awe kama mimi. Mungu amjalie afya njema, ampe umri mkubwa, ashike wajukuu na vitukuu vyake.” “Amina mama yangu. Basi nakusubiri hiyo kesho.” “Nikuletee nini?” “Ngoja nitakutumia kwenye ujumbe.” Wote wakacheka, wakaagana.

~~~~~~~~~~~~~

“Mama amefurahi sana kumpa mtoto jina lake.” “Eti eeh!” “Sana. Lakini pia anakupenda. Mama anakupenda sana Nanaa.” “Ni kweli. Nilihisi hivyo. Ndio maana nilipokwama na mtoto, yeye pekee nilijua ndio atakuwa kimbilio langu. Na wala hakubisha. Nilimpigia tu nikamwambia naomba uje, nina shida sana. Hakuuliza hata maswali mengi, akaja. Alinifariji sana. Bila yeye nahisi nisingeweza kufanya mtihani. Nilikuwa namfukuza aondoke akapumzike lakini hakutaka kuniacha peke yangu na mtoto. Alihakikisha aninisaidia na Liv mpaka wewe alipokuja kumchukua. Namshukuru sana Mungu kwa kunipa mama kama huyu, sikuwahi kupata mtu kama yeye.” Geb akabaki kimya.

“Geb!” Nanaa akaita. “Naomba kesho mama akija, anisindikize kwenye hicho chumba nikiwa na Liv ili nisimuache tena peke yake. Kama ukikubali, nataka nimuombe mama twende naye, halafu abaki na Liv kwenye gari, mimi wanishushe mbali kidogo, nitatembea mpaka kwa huyo mwenye nyumba.” “Naomba mimi nilipie, Nanaa.” “Hapana Geb. Una mambo mengi sana. Usiwe na wasiwasi na mimi, nina pesa.” “Unapata wapi pesa na wewe huna kazi?” “Unakumbuka nilikuwa na mkopo wa chuo wa asilimia 85? Kaka naye alikuwa akinitumia pesa, halafu ule mshahara mliokuwa mkinilipa wakati ule nawafanyia kazi kwenye kampuni yako, nilikuwa najiwekea akiba. Halafu Liv nilijifungulia hospitali ya serikali, wala sikutumia pesa nyingi. Kwa hiyo ninayo pesa yakujitunza kwa sasa. Wewe mwangalie mtoto wako tu. Usinifikirie mimi hata kidogo. Nipo sawa kabisa.” “Wala hunisaidii hivyo. Unazidi kuniumiza.” “Naomba kabisa uwe na amani Geb. Kwa sasa ni kweli sihitaji msaada wa mtu yeyote yule. Nilichokuwa nataka ni mtoto wangu, na umenipa. Asante.” Geb akanyamaza.

“Hujajibu Geb.” “Ni sawa. Nyinyi nendeni tu.” Nanaa akatulia tena kidogo. “Naomba nikuombe kitu cha mwisho.” Geb akamwangalia. “Naomba usiku wa leo nilale na Liv. Kesho nitakuachia, lakini angalau leo tumfanye asilie tena.” Tayari machozi yalishaanza kumtoka Nanaa. Geb aliinama kwa muda. “Naomba iwe kwa usiku wa leo tu. Tafadhali Geb.” “Ni sawa. Hamna neno. Hata hivyo sasa hivi naona anakufahamu na kukuhitaji wewe zaidi.” “Asante. Nakushukuru sana.” Nanaa akajifuta machozi, akanyanyuka na mtoto wake.

 “Sisi tutachukua hiki chumba kidogo.” Nanaa aliongea akiwa katikati ya hivyo vyumba na Geb yupo sebuleni lakini hakujibu. Akaingia kwenye hicho chumba, akamlaza mtoto wake vizuri baada ya kumbadilisha, akapanda kitandani. Akamkumbatia mtoto wake, akaanza kulia taratibu. Geb alisimama nje ya mlango akimsikiliza jinsi anavyolia. Alikuwa akitoa kilio cha sauti ya chini. Lakini alilia kwa uchungu sana. “Nakupenda Liv. Unakumbuka nilikuahidi hatutaachana? Ona Mungu ametusaidia tupo wote pamoja! Na leo tunalala wote tena. Mungu akitusaidia hatutatengana kwa muda mrefu. Nakuombea uzima mwanangu. Hata hapa tutapita tu.” Aliendelea kuzungumza na mwanae kwa upendo, kwa sauti ya chini yenye kilio. Geb alisimama pale akisikiliza, uzalendo ukamshinda akaamua kuingia. 

Nanaa akakaa kwa haraka kama aliyekosea. Akabaki anababaika. “Nimekushitua?” Geb akamuwahi kama kumtuliza, akaenda kukaa kwenye kile kitanda. Nanaa akajiweka sawa, akamfunika mtoto wake vizuri na kumsogeza pembeni kidogo kama kumuonyesha Geb kuwa hakuwa amemkumbatia. “Naomba unisamehe, nilikukosea.” “Yameisha Geb! Hakika nimesamehe.” Alijibu huku akifuta machozi. “Unauhakika?” “Kweli Geb. Nimeshatendwa sana. Nimeumizwa mnoo. Nikajifunza kusamehe kabla sijaombwa msamaha. Nilielewa na kukusamehe kabisa. Huwa nafanya hivyo kwa ajili yangu mwenyewe. Nimejawa na furaha ambayo siwezi kueleza. Siamini kama nimepata bahati ya kulala na mwanangu hivi. Niliingiwa hofu sana. Sikujua kama ipo siku nitarudi kulala na Liv wangu na kumkumbatia kwa uhuru hivi. Niamini kuwa nalia kwa furaha, sio kwamba nina uchungu na wewe.” “Sasa kwa nini hukutaka mama aniambie kama una mtoto wangu kama ulishanisamehe?” Nanaa akafuta machozi, akajiweka sawa.

“Unakumbuka nilikwambia niliwaona siku ya harusi mmeshikana mkono mnaingia ukumbini pamoja? Tena mlionekana mmetulia kama wapenzi tu. Kuja kunisahau pale nje, huku nikijua upo na Liz ndani, ukweli niliumia sana. Nakumbuka tulizungumza kwenye simu muda mfupi kabla ya pale ukumbini. Ulijua wazi nilikuja pale kwa ajili yako Geb, na bado ukanisahau! Halafu kilichoniumiza zaidi ni wewe Geb unayesifika kutosahau! Nikajiona kweli nina mkosi. Mtu aliyeumbiwa kutosahau kila kitu ila Nanaa tu! Kwa hiyo ikaniuma na bado nilikuwa na hasira. Lakini nikajiambia ni haki yako na Liv kufahamiana. Nikaamua kuja kukwambia tu. Sasa tena nikaja, nikawakuta tena  na Liz! Halafu wote mpo uchi! Nilijua mlisameheana na kuamua kurudiana. Nikaona nisubiri kwanza ili nisije kuonekana kama natumia mtoto kama chambo ya kukuvutia kwangu. Kumbuka nilikwambia nilimtaka mtu anayenipenda mimi kama Nanaa. Awe anajua madhaifu yangu yote, na bado anichague mimi.” Nanaa akaendelea taratibu. 

“Sikuta kuja kuishi na wewe sababu ya mtoto. Lakini ningekuja kukwambia siku moja baada ya kutulia. Sikutaka kujichanganya. Yaani nipo kwenye  mitihani, halafu niwe nakabiliwa na kesi za kujibu kwako au ndugu zako! Sikutegemea kama Liv angekuja katikati ya mitihani Geb. Ulikuwa mshituko kwangu. Halafu sikujua utamchukuliaje. Kama utamkubali au la. Kwa hiyo hayo yote nilijiambia nitakuja kujua baadaye. Nikiwa nimeshatulia kwangu, nimepata kipato cha kueleweka ndipo ningekutafuta kukutaarifu tu, sio kuanza kukulia shida.” Nanaa akafikiria kidogo, kisha akaendelea.

“Sikutaka kuzunguka na Liv kama mzigo ambao nataka kumuachia mtu, halafu akaishia kukataliwa kama mimi nilivyokataliwa au ninavyokataliwa na watu. Geb, niamini nikikwambia kuwa inauma sana kujua watu wanakukataa. Wanakuona mzigo, hawakutaki! Inauma kuliko kitu chochote. Na maumivu yake hayana tiba hata iweje, hayaponi. Inaathiri kila eneo la maisha yako. Sikutaka Liv apite nilipopita mimi. Kwa kuwa nilishafanya kosa kama la mama yangu kumleta duniani bila makubaliano au tuseme bila ndoa, sikutaka kuendelea kurudia historia yangu na mama yangu kwa Liv. Sijui umenielewa?” “Nimekuelewa Nanaa. Nahisi hata mimi ningefanya hivyo hivyo.” Wakatulia kwa muda. “Tutaongea zaidi kesho. Pata muda wa kupumzika. Naomba usilie.” Nanaa akanyamaza. “Usiku mwema.” “Asante na wewe.” Geb akatoka.  

~~~~~~~~~~~~~~~~

Asubuhi Mama G alifika hapo na vyakula. Geb alipata kifungua kinywa akaondoka kwenda kazini na kuwaacha hapo. Vilijaa vicheko kati yao, mwishowe wakatoka. Alisindikizwa na Mama G, akakamilisha mambo yake ya chumba. Alilipia pesa na kukabidhiwa funguo. Alirudi kwenye gari alipokuwa amemuacha mama G na mwanae, machozi yakimtoka. “Ni nini tena? Umekosa hicho chumba?” Mama G akauliza. “Sasa hivi na mimi nina kwangu mama. Nanaa naye ana kwake!” Mama G akacheka. “Nimelipia kila kitu. Nimemalizana na dalali pamoja na mwenye nyumba wangu. Ona funguo hizi hapa. Funguo za nyumbani kwangu mama. KWANGU!” Nanaa akaweka msisitizo. “Hongera.” Mama G alikuwa akicheka huku akimwangalia jinsi alivyofurahia.

“Naomba unisindikize kuchukua tena mizigo yangu. Au umechoka?” “Mimi leo nipo kwa ajili yako. Nizungushe utakavyo.” Nanaa akacheka. “Basi twende kwa Antii.” Mama G akaondoa gari, Nanaa akamuelekeza mpaka nyumbani kwa Antii, Chuo Kikuu cha Mlimani. Walipofika, Nanaa akamwambia mama G asisumbuke, akae tu kwenye gari yeye ataleta vitu. Akashuka. Hakumkuta Antii, lakini alijua wapi pakuchukua funguo. Akaanza kuingiza vitu vyake kwenye gari ya mama G, huku akivipanga vitoshee. Bado Liv alikuwa amelala. 

Nanaa akaendelea kusombelea na kuvipanga taratibu kwenye gari ili asimsumbue mtoto wake mpaka akamaliza. “Nimemaliza mama. Naomba kabla hatujavipeleka hivyo vitu vyangu kwangu, tupitie kwenye ofisi za utawala, kuna kitu nataka nikaweke sawa.” Nanaa akatoa tabasamu aliposema neno ‘kwangu’. “Naona umefurahi!” “Sana mama yangu. Angalau sasa hivi nina kimbilio. Hata nikifukuzwa, ninapo pakwenda.” “Sasa mbona huna hata kitanda?” “Taratibu mama. Kwa kuwa sasa hivi ninapo pakuishi, nitanunua vitu vyangu kimoja baada ya kingine mpaka nikamilishe kuwe kwa kueleweka.” Nanaa alijibu kwa upole lakini akiwa amejawa na furaha.

“Nakuhakikishia Nanaa, Geb hawezi kurudia tena upuuzi alioufanya. Anajutia sana.” Nanaa akanyamaza wakati mama G akiendelea kuendesha wakielekea kwenye ofisi za Utawala chuoni hapo. “Msamehe.” “Nimesamehe mama, hata yeye nimemwambia nimeshasamehe kabla hata hajaomba msamaha. Huwa nafanya hivyo kwa ajili yangu mwenyewe, mama. Nimepita pagumu sana. Kama ingekuwa kuweka visasi moyoni, nisingeweza kuwa hapa. Ningeshindwa kuendelea na maisha.” Nanaa akacheka kidogo. “Nimejiwekea kama katabia. Kama mtu ameniumiza sana, nikaumia, huwa namtafutia sababu ya kwa nini alinifanyia hivyo, ili tu kupata sababu ya kusamehe, kujipa amani moyoni, au kujifariji ili niendelee na maisha.” Mama G akamuhurumia sana Nanaa. 

Walifika kwenye ofisi za utawala, Mama G akaegesha kwenye kivuli, Nanaa akashuka akamuacha Oliva akiwa bado amelala kwenye kiti chake. “Kama watu sio wengi, sitakawia mama yangu. Nivumilie.” “Wewe usiwe na wasiwasi na sisi. Maliza mambo yako kwa utulivu.” Nanaa akatabasamu huku akichukua pochi yake, akaondoka. Alibahatisha kujikuta yupo peke yake pale ofisini. Akamuulizia muhusika ambaye angeweza kumsaidia kumpatia matokeo yake yote ya nyuma. Trascript. Akaambiwa lazima kujaza kwanza form baada ya siku mbili ndipo arudi kuchukua transcript yake. Alipomaliza kujaza, akatoka.

Wakati akiliendea gari ya Mama G, aliangusha karatasi na kalamu alizokuwa ameshika mkononi. Akainama kuokota, lakini karatasi ilianza kupeperushwa na upepo. “Ngoja nikusaidie.” Kijana mmoja mtanashati alianza kukimbiza karatasi ya Nanaa huku akiacha harufu nzuri nyuma, alimfanya Nanaa asimame abaki akimsubiria arudi na ile karatasi, na Mama G alibaki akiwaangalia kwani Nanaa alikuwa amekaribia kabisa garini. Kila aliposogelea ile karatasi na yenyewe ilisogea, na yeye hakukata tamaa. “Lazima nikupate wewe karatasi, huwezi kunishinda.” Walimsikia akiongea, Nanaa akacheka taratibu huku akimwangalia kwa nyuma. Alihangaika mpaka akaikamata. “Told you!” Yule kaka alianza kuiongelesha ile karatasi kwa sauti ya ushindi baada ya kuiokota. Nanaa akacheka akainama huku ameficha mdomo kwa kiganja. 

Ya Kale…

“Penye nia, pana njia. Karatasi yako hii hapa.” Nanaa akanyanyua kichwa kupokea. “Zac!” Nanaa alishituka sana, hakutegemea. “Nanaa!” Yule kijana alijibu. Alikuwa Zac, kipenzi wa zamani wa Nanaa. “Zac!” Nanaa alirudia safari hii akiwa na machozi. “Nanaa mpenzi!” Zac alimkumbatia. Hakuwahi kuruhusu Nanaa alie mbele yake. 

~~~~~~~~~~~~~

Mara ya mwisho wapenzi hao waliachana Zac akiwa amepiga magoti nje ya daladala, Nanaa ndani ya daladala akilia. Zac aliumia kumuona Nanaa akilia na yeye kushindwa kumbembeleza. Alishawishika kuingia na yeye ndani ya daladala, lakini akajua Nanaa anarudi nyumbani kwa kaka yake, hakutaka mwanzo wa mahusiano yake na shemeji yake uwe wa habari ya fumanizi lake. Alimbembeleza Nanaa ashuke wayamalize, lakini Nanaa hakutaka hata kumgeukia. Aliendelea kulia ndani ya daladala hiyo akikumbuka ahadi kemkem alizokuwa ameahidiwa na Zac. Penzi alilokuwa akipewa na Zac. Kitanda kile kile alichokitumia kumridhisha Zac, ndicho hicho hicho alikitumia classmate mwenzake Zac, kumpa yale yale aliyokuwa akiyapokea kutoka kwa Nanaa. “Nibaki au nirudi? Ili iweje wakati anauwezo wa kupokea kwa msichana mwingine, kile nilichodhani ni cha thamini, alichoahidi kukipata kutoka kwangu tu?” Nanaa alijiuliza wakati akiendelea kulia ndani ya daladala.

          Ni kweli alijua kwa hakika Nanaa ndiye atakaye kuwa mkewe. Lakini ni nini kilimpelekea kulala na msichana mwingine, tena aliyemjua Nanaa kwa muda wote? Ni swali ambalo alishindwa kuwajibu wengi walio yajua mahusiano mazuri aliyokuwa nayo na Nanaa na wengi waliitamania couple yao. Walishangaa kuweza kumsaliti msichana kama Nanaa aliyekwisha kujigamba kwa kila mtu kuwa ni lazima atamuoa yeye. Kwa kumwangalia tu Nanaa, utajua ni binti aliyetulia. Hata rafiki wa Zac walimpongeza na kumsifia Zac wazi wazi kuwa Nanaa ni ‘wife material’. Kwamba ni mke wa kuoa na kuweka ndani. Zac naye alishajisifia nyumbani kwao kuwa akimaliza tu chuo, atawapelekea kifaa chakufunga mwaka. Kwa hiyo hata nyumbani kwa kina Zac, walishazisikia habari za Nanaa, wakabaki wakisubiria atokee. 

~~~~~~~~~~~~~

Zac alizidi kumkumbatia Nanaa kwa nguvu akimvutia karibu kabisa na mwili wake, huku ameinamisha kichwa chake kwa Nanaa akimbusu kichwani, kwenye nywele zake. “Nanaa!” Zac aliendelea kuita taratibu kwa sauti iliyojaa hamu, mapenzi na hakika alionekana ni mwanaume anayempenda Nanaa. Nanaa aliendelea kulia huku amekumbatiwa. Alikuwa na machungu ambayo alijua kwa Zac, ndio sehemu sahihi ya kuyatolea. Zac alijua kumbembeleza.

Mama G alikaa sawa akabaki akiwaangalia na kusikiliza. Kwa hakika vile walivyokumbatiana haukuonyesha kama ni ukaribu wa kawaida. Mama G, alijua wazi walikuwa wapenzi. Nanaa alishindwa kujitoa kwenye mikono ya Zac. Wazi alionekana ni mahali anapofurahia kuwepo. Alijisahau kabisa kama yupo mbele ya macho ya mama yake Geb. Alilia huku akikumbuka shida zake zote tokea waachane na Zac. Zac alijua kumtuliza Nanaa. Kwa kilio kile, Zac alijua wazi lipo jambo kwa Nanaa. Je bado anamaumivu ya kumfumania au kuna jingine linaendelea ndani yake? Hilo ni swali Zac aliendelea kujiuliza wakati akishindwa kumuachia.

“Lakini anaonekana na hali nzuri sana kimaisha! Nanaa amependeza zaidi. Hiki kilio ni cha nini tena kwa mpenzi wangu?” Zac alijiuliza huku akiendelea kumkumbatia na kumbusu Nanaa aliyekuwa akiendelea kulia kwa kwikwi. Aliendelea kumkumbatia huku akipitisha mikono yake mgongoni taratibu, kama kumbembeleza huku akimbusu kichwani. Nanaa alitamani kuongea kitu lakini akashindwa. Ni kama kitu kilimkaba kooni. 

Zac alimvuta mbele kidogo kumwangalia. “Pole mpenzi wangu. Nimekuacha peke yako!” Mama G, alisikia Zac akimwambia Nanaa aliyebaki ameinama huku akifuta machozi. “Sijawahi kukusahau Nanaa. Bado nilijua nitakupata tu. Umeolewa?” Nanaa akatingisha kichwa kukataa. “Una mchumba?” Mama G akajiweka sawa kusikia jibu la lile swali. Alitamani kujua Nanaa atajibu nini. “Nanaa!” Zac akaita tena. “Naomba usilie mpenzi. Unajua nachukia kukusikia ukilia.” Nanaa akafuta machozi. 

Zac alivuta mkono wa kushoto wa Nanaa. Alipoona hauna pete, akaubusu. “Afadhali. Nilidhani nimeshachelewa!” Nanaa akacheka huku akifuta machozi. “Nilizimiss hizo dimpozi zako!” “Nilibahatika kupata mtoto.” Nanaa akaongea kwa upole. “Hongera.” Nanaa akatoa tabasamu, wakabaki wakiangaliana kwa muda. “Nina hamu na wewe Nanaa!” Nanaa akanyamaza, kama anayefikiria kitu. Alipokonya simu ya Nanaa, akajipigia na kuandika namba yake. “Sitaki kukupoteza tena.” Kisha akamrudishia na busu la kichwani. “Usilie Nanaa wangu. Usilie mpenzi.” Nanaa akajifuta machozi. 

“Unafanya nini hapa?” Nanaa akauliza taratibu. “Nimekuja kufuatilia transcript yangu. Yakwanza nilipoteza, nikaandika barua ya kuomba nyingine. Leo waliniahidi itakuwa tayari, ndio nimeifuata. Umependeza sana Nanaa.” Nanaa akacheka na kuinama. “Na wewe unafanya nini hapa?” “Na mimi nilifuatilia transcript.” “Unataka kuendelea na chuo?” Zac akauliza. “Hapana. Hali yangu haijabadilika sana Zac. Ni Nanaa yuleyule uliyeniacha. Naishi kwa rehema za Mungu. Sina uwezo wakurudi tena chuo. Sasa hivi nimepata bahati ya kumlea mwanangu, nalea, akikua kidogo nahisi baba yake atamchukua, ndipo naweza kutafuta kazi.” Zac aliona machozi yakimtoka tena Nanaa.

 Zac alikunja uso. “Baba yake akimchukua tena? Sijaelewa.” “Ni habari ndefu Zac. Lakini kwa sasa, naishi na baba wa huyo mtoto wangu. Kwa ajili ya kumlea mtoto wetu. Ni mdogo sana, bado nanyonyesha, ndio maana nipo nao. Lakini..” Nanaa akashindwa kuendelea kuongea akainama nakuanza kulia kwa kwikwi. Zac akamuhurumia, akajua yapo mengi yanaendelea. Nanaa alikuwa mpole kwa asili. Alimvuta tena akamkumbatia.

Alimbembeleza kwa muda. “Naweza kuingia hapo ofisini nikachukua hayo matokeo yangu, kisha twende mahali?” “Hapana Zac. Nipo na mama yangu na mtoto, wapo…” Nanaa akageuka ili kumuonyesha alipokuwa ameiacha gari ya Mama G, akashituka sana kujikuta kumbe wamesimama hatua chache sana kutoka lilipo gari hiyo. Wakabaki wakiangaliana na Mama G. Zac akamwangalia Mama G, akamwangalia Nanaa aliyekuwa ameinama.

“Nanaa! Umesema mama!?” Zac aliuliza kwa mshangao kwani aliijua historia ya Nanaa vizuri sana. “Ni mama yake huyo mzazi mwenzangu. Lakini nimemzoea sana, mpaka najisahau.” “Ohh! Nimeelewa. Shikamoo mama.” Zac akasalimia. “Marahaba Zac mwanangu.” Nanaa akashituka akanyanyua uso kumwangalia Mama G. “Amelifahamu vipi hilo jina la Zac, wakati bado sijamtambulisha?” Akajiuliza, Zac akatoa tabasamu la mshangao huku akimwangalia Mama G, Nanaa aliona.

 “Kwani mnafahamiana?” Nanaa akauliza kwa upole. “Nimesikia jina lake sasa hivi wakati unamtaja.” Mama G, alijibu akiwa ametulia kabisa. Nanaa aliinama akajua wazi Mama G, amesikia kila kitu. Ukimya ukapita kwa muda kati yao, huku Nanaa akiendelea kupokea taarifa kuwa yule alikuwa mama yake Geb. Akabaki ameinama akifikiria itakuaje baada ya hapo. Alikumbuka vile alivyokuwa akilia kifuani kwa Zac, na kupokea mabusu mfululizo muda mfupi uliopita, tena bila kupinga.

Ukweli mama G alikuwa mama yake Geb. Alimpenda Nanaa kwa upendo uliokuwa ukimfanya Nanaa asahau kama yule si mama yake. “Itakuaje tena baada ya hapa? Bado ataendelea kunipenda na kuniheshimu kama zamani? Atamsimulia Geb! Lakini sitajali hata kama Geb akijua. Sio mpenzi wangu na amenionyesha wazi hanihitaji. Liv wangu je? Bado atampenda?” Nanaa aliendelea kuwaza. 

“Nanaa!” Zac akamuita kama kumtoa mawazoni. “Abee!” Aliitika kwa upole akanyanyua uso huku ameegemea gari ya mama G. “Naomba tuonane baadaye.” Zac aliomba kwa utulivu. Sauti yake ilionyesha mapenzi makubwa kwa Nanaa. “Saa ngapi?” Bila kufikiria, Nanaa alijikuta akiuliza swali lililomshangaza Mama G, wazi alionyesha anataka kumuona tena Zac. “Muda na wakati wowote. Niambie wewe.” Nanaa akafikiria kidogo. “Hata sasa hivi.” Zac akaongeza. “Sasa hivi sitaweza, Zac. Kwa mara ya kwanza nimepata kwangu.” Nanaa alimtolea Zac kicheko. Zac akaonekana kuelewa kile kicheko. “Finally!” Zac alijibu kwa kucheka. “Finally, Zac! Hatimaye na mimi nina kwangu.” Nanaa aliweka msisitizo. “Hongera sana. Am proud of you!” Nanaa akacheka.

Kama aliyekumbuka kuwa kuna mama Geb pale anawasikiliza, akaacha kujichekesha. Akaendelea. “Kwa hiyo leo ndio nimekabidhiwa funguo. Usifikiri ni nyumba, ni chumba!” Zac akacheka. “Hata kama ni chumba kimoja, bado nakupongeza Nanaa.” “Asante.” Nanaa akajibu kwa furaha. “Kwa hiyo leo ndio nahamia huko.” “Naweza kukusaidia kuhama.” Zac aliongeza nakumfanya Nanaa acheke. “Hujabadilika Zac!” Zac akatabasamu. “Nifanye niwe mikono yako. Wewe ongea tu, nitakuwa nakufanyia kila kitu. Nitakubebea vitu vyako, na tukifika nitakupangia.” Nanaa akacheka, akainama kama anayekumbuka kitu.

~~~~~~~~~~~~~

Mawazo yalimrudisha zamani akiwa na Zac. Wakati mwingine alikuwa akimuomba kazi. “Naomba nipe kazi, Nanaa.” Zac alikuwa akimwambia nakumfanya Nanaa acheke. Wakati mwingine alipokuwa akila, alimuomba kazi yakumlisha, huku akimwambia yeye afanye kazi ya kutafuna tu. Na alimlisha mpaka chakula kinaisha. Siku alizokuwa na Zac, hakujigusa. Zac alimfanyia kila kitu. Yeye alikuwa akilala kitandani tu, huku Zac akimuomba amtume. Zac alimpenda na kumtumikia Nanaa bila kuchoka. Ndiye mwanaume aliyeonyesha kumsikiliza kila wakati na kujali hisia zake. Hakuchoka kumtafuta na kumjulia hali. Tena endapo atapiga na kumkuta Nanaa hana furaha, ni lazima atamtafuta ili ajue kulikoni. Swali ni kwa nini alimsaliti, ndilo lilimtesa sana Nanaa. 

~~~~~~~~~~~~~

Alinyanyua uso ukiwa na tabasamu, akakuta wote wanamtizama. Akajaribu kujibaraguza kwa kujishika hapa na pale akitafuta neno la kuongea tena, akababaika kidogo kwa kuwa Mama G, alikuwa ametulia ndani ya gari akimtizama tu. Akakumbuka ombi la Zac. “Sina vitu vya kuhamisha Zac. Ndio naanza maisha.” “Hata kitanda tu nitabeba.” Zac akaendelea kubembeleza. “Huwezi amini hata kitanda sina. Naanza kupeleka urithi wangu, upo hapo nyuma ya gari. Vitabu na madaftari.” Zac akakunja uso. 

“Utalala wapi sasa?” Akamuuliza. “Nilikwambia kwa sasa naishi kwa mzazi mwenzangu, nikimlea mtoto.” Nanaa akajibu nakuongeza. “Njoo umuone mwanangu Zac.” “Ngoja kwanza Nanaa, sasa kama unaishi naye, nitakuona vipi? Akikukatalia kuja kuniona?” Tayari Zac alipatwa na wivu na Nanaa akajua, akacheka. “Tutaonana tu. Usiwe na wasiwasi. Tunaishi naye tu, sio kama tuna mahusiano. Na sio kwamba tunaombana ruhusa. Hapana. Ni kuagana tu. Hata yeye huwa akitoka hasemi anakwenda wapi, au anarudi saa ngapi. Kikubwa ni mimi niwepo pale na mtoto, au yeye mwenyewe awepo na mtoto. Hajali wapi ninakwenda, ilimradi nisichelewe kurudi.” Zac akashangaa sana, lakini kwa upande mwingine akashukuru Mungu.

“Daah! Lakini afadhali yangu.” Nanaa akacheka. “Nitakuona jioni, Zac. Ngoja tuwahi, nisimuweke mama.” “Saa ngapi sasa?” “Mpaka yeye arudi, ili nimuachie mtoto, ndipo nitakutafuta.” “Una uhakika Nanaa? Naomba usinidanganye.” “Sina sababu ya kukudanganya. Hata mimi nataka kukuona.” Zac akacheka kwa furaha. “Basi nitakuwa na simu karibu sana kusubiria simu yako. Naomba nimuone mtoto.” Nanaa akasogea mpaka mlango wa nyuma, akafungua na kumpisha Zac.

Zac alisimama pale akabaki akimwangalia yule mtoto. “Anaitwa Oliva.” Zac alivuta pumzi kwa nguvu, akatulia. Alimwangalia Liv kwa muda. “Alitakiwa kuwa ni mtoto wangu huyu!” Zac aliongea kwa sauti ya chini kama anayejutia. “Unakumbuka jina tulilokuwa tumepanga kumpa mtoto wetu wa kike?” Zac alimgeukia Nanaa aliyekuwa kimya nyuma yake akimsikiliza, akamuuliza lile swali. Nanaa akabaki tu kimya. “Daaah! Nilichezea shilingi chooni. Najuta sana, Nanaa. Natamani nirudishe ile siku, lakini siwezi. Hamna siku inapita nisijutie. Maisha yangu yameharibika kweli baada ya kuachana na wewe. Lakini tutapata muda tutazungumza.” Nanaa akanyamaza, Zac akarudisha macho yake kwa yule mtoto, akabaki akimtazama akiwa ametulia.

“Unamtoto mzuri sana Nanaa. Jamaa amebahatika, ameibuka mshindi! Natamani ndio ningekuwa mimi!” Nanaa akacheka kidogo. “Hongera mpenzi wangu.” Zac alitoka pale akasimama nje ya gari akimwangalia Nanaa. “Asante Zac.”  “Nategemea kukuona jioni, Nanaa. Tafadhali usiache kunitafuta.” “Nitafanya hivyo.” Zac akatulia kwa muda kama anayefikiria kisha akaongeza. “Nimefurahi sana kukuona Nanaa. Sana.” Nanaa akacheka. “Tutaongea zaidi baadaye. Uwe na wakati mzuri. Mungu akutangulie.” Ni usemi wa Nanaa aliokuwa akiupenda sana kwa Zac. “Amina mama. Nimeshaanza kusubiria simu yako.” Nanaa akacheka. “Hata hatujaachana!?” “Ndio ujue ni kiasi gani nina shida ya kuongea na wewe.” Nanaa akacheka tena. “Haya. Akija tu baba yake Liv, nitakupigia tukutane.” Waliagana, Zac akaondoka kuelekea ofisi za Utawala, Nanaa akapanda kwenye gari asijue anaanzia wapi na Mama G.

~~~~~~~~~~~~~

Alitamani kama Liv angekuwa ameamka ili ajibaraguze naye, lakini Oliva alikuwa amelala kama malaika! Akajiweka sawa kitini. “Lakini hakuna nilipokosea.” Akajitetea nafsini mwake. “Kwa hiyo huyo ndio Zac?” Alishituliwa na swali kutoka kwa Mama G. “Ndiyo.” Nanaa akajibu kwa upole. “Anaonekana anakupenda sana.” Mama G akaongeza. “Kipindi nipo naye, kama hata Mungu angeshuka, akaniambia Zac asingekuwa mume wangu, ningesema sio Mungu. Alikuwa…” Nanaa akatulia kidogo. “Nashindwa hata kusema. Alinipa mapenzi ambayo sijawahi pata maishani. Hakutaka hata anihisi nilikuwa ninalia. Nikilia alikuwa anachanganyikiwa. Alikuwa akipiga simu kutaka kusikia sauti yangu kila mara ili apate nguvu ya kuendelea kufanya alichotaka kukifanya. Kama hakuwa akipiga simu, basi atatuma ujumbe. Alikuwa akipenda kunisikiliza nikiongea, nikicheka ndio kabisaa.” Nanaa akacheka na kumfanya Mama G, na yeye acheke kidogo. Aliongea kwa hisia.

“Una sauti nzuri, Nanaa. Inatia raha kusikiliza.” “Sio kwa kila mtu mama.” Nanaa akajibu nakuinama. Mama G, akajua anamaanisha sio kwa Geb. “Nini kilitokea?” Mama G akauliza swali. “Na yeye nilimfumania.” Mama G alishituka kidogo, akamgeukia Nanaa, Nanaa akacheka. “Kweli mama. Nilimfumania akifanya mapenzi na msichana waliyekuwa naye darasa moja! Tena kwenye kundi moja la kujisomea! Wakati mwingine alikuwa akimfuata Zac amfundishe peke yake. Lakini sikuwahi hata kuhisi. Kwa kuwa yule msichana alikuwa na pete ya uchumba kidoleni, yaani alikuwa anasubiriwa na mchumba wake amalize chuo, wafunge ndoa. Mchumba wake alikuwa akifanya kazi. Hakuwa mwanafunzi kama sisi. Na vikao vya harusi vilishaanza. Yaani sikuwa hata nikiwahisi chochote. Alijitahidi sana kujificha.” “Unafikiri walikuwa na mahusiano ya muda mrefu?” “Sijui mama. Na wala sikusubiri kutaka kujua ilikuaje. Niliondoka pale pale.” Nanaa akacheka.

“Mbona unacheka?” Mama G akatupia swali jingine. “Nakumbuka vile Zac alivyokuwa akinikimbiza huku yupo nusu uchi. Kweli Zac alinipenda mama. Alikuwa akinikimbiza kama mwehu huku ananiita mpaka kituoni. Tulipofika kituoni mimi nikapanda ndani ya daladala yeye alibaki amepiga magoti nje ya daladala akinisihi nishuke tuzungumze. Hakutaka niondoke nikiwa nalia. Lakini nilishindwa kushuka mama.” “Kwa nini?” “Sikutaka anidanganye na pia sikuwa tayari kwa ukweli, ili asinivunje moyo. Kwa kuwa nilijiambia lazima nije kuolewa na kuanzisha familia. Niwe na watoto, niwape kile nilichokikosa.” Akatulia kidogo. 

“Unajua mama, ipo hisia ndani yangu inaniambia au najihisi kuwa nina upendo mkubwa sana ndani yangu. Naona kama nikibahatika kupata mume na watoto, ninajiona nina uwezo mkubwa sana wakupenda. Nikawa mke na mama mzuri tu. Najihisi hivyo. Sitaki kuja kuishia kwenye mikono isiyo sahihi ya mwanaume asiyenithamini mimi, mama. Nimeteseka sana tangia nazaliwa mpaka leo. Nahangaika kupata pumziko ambalo nahisi hakuna mwanadamu atanipa tena, labda mimi mwenyewe. Naogopa kusema nimekata tamaa.” “Na wala huna sababu ya kufanya hivyo.” “Unafikiri hivyo mama?” “Kabisa Nanaa mwanangu. Huna sababu yakukata tamaa.” “Asante mama yangu.”

“Eti hata hivi kuonana na Zac, na kuonyesha bado ananijali, imenifurahisha kidogo! Angalau nimefarijika. Nitamtafuta tena ili nipate naye muda wakumsikiliza.” Mama G, akabaki kimya kama aliyenywea. Alijua utabiri wake umetimia. Mwanae ndio ameshakosa.

~~~~~~~~~~~~~

Walifika kwenye hicho chumba ambacho Nanaa alikuwa akimiliki kwa wakati huo. Akashusha vitu vyote kwa haraka bila hata kuvipanga. Akafunga mlango, akarudi kwenye gari kwa haraka. “Pole mama yangu. Nakusumbua eeh?” “Wala usijali. Kwanza mbona kama vitu vyenyewe ulikuwa ukivitupa tu. Umepanga kweli?” Nana akacheka huku akihema kama mtu aliyekuwa akikimbia. “Nimefanya haraka ili nisiendelee kukuweka mama yangu. Na wewe ukapumzike. Nitarudi hata jioni au kesho kuja kuvipanga vizuri. Nafikiria nivinunulie kwanza kabati. Kitanda kisiwe kitu cha kwanza. Maadamu sasa hivi mimi nina pakulala, basi vitabu vyangu na vyenyewe nivisitiri. Nitavinunulia kabati zuri, nivipange humo. Ndipo ninunue kitanda. Lakini pazia zuri kwanza na….” Nanaa akaendelea kutaja vitu alivyoona angehitaji nakumuacha Mama G, akiwaza vyake. 

~~~~~~~~~~~~~

Mara simu ya Nanaa ikaingia ujumbe. Akaona uso wa Nanaa ulivyojawa furaha. Haraka sana Nanaa akajibu huku na tabasamu limejaa usoni. Waliendelea kujibizana kwa ujumbe kwa muda mrefu. Wakati mwingine alimuona Nanaa akicheka nakugeukia dirishani kama anayekumbuka kitu, kisha anarudisha macho kwenye simu yake na kuendelea kuandika ujumbe mwingine, kisha anatulia kama anayesubiri majibu. Mama G alijua wazi atakuwa akiwasiliana na Zac tu. Kwani ni jana yake tu Geb alimwambia hakuwa hata na namba ya simu ya Nanaa! Na alimsikia Nanaa akimwambia Zac kuwa hawana mawasiliano na baba watoto wake. Nanaa alishamwambia hata Geb akiondoka asubuhi huwa hamuagi. 

Na kweli mama G alishuhudia hata alipokuwa mbali na nyumbani, anapotaka kuulizia hali ya Liv, alimpigia yeye wala si Nanaa. Alizidi kukumbuka vile  Nanaa alivyomwambia kuwa Geb hakuwa akimuongelesha. Na hata alipomuomba msamaha, hakuwahi kujibu. Kwa hakika aliyekuwa akiwasiliana naye kwa wakati ule hakuwa mwanae Geb, ni Zac tu. Mwanaume aliyeonyesha kwa muda mfupi sana alipowaona pamoja, kumpenda na kumjali sana Nanaa. Nanaa aliendelea kuchat na Zac nakujisahahu kabisa alipo na yupo na nani mpaka walipofika.

~~~~~~~~~~~~~

“Tumefika mwanangu.” Alishitushwa na sauti ya Mama G. Akaangalia nje, akagundua kweli wamefika kwenye apartment. “Asante mama.” Nanaa akashukuru tena kama kawaida yake. “Asante hizo zinakaribia kumwagika kwenye pipa.” Nanaa akacheka. “Bwana mama! Usichoke. Kweli nakushukuru, na ninakuahidi leo mwisho kukufanya dereva wangu.” “Wala usijali. Ndio nafurahia kupata muda na nyinyi wote wawili.” Akamsaidia kumshusha mtoto, yeye akabeba vitu vingine. 

“Huyu naye itabidi kumuamsha anyonye.” Mama G, aliongea wakati anaweka kiti cha Oliva kwenye kochi. “Jamani Liv analala! Mpaka ananitia wasiwasi.” “Na baba yake alikuwa hivyo hivyo. Nyumba inakuwa kimya kama hamna mtoto. Nenda kaoge, uje umnyonyeshe.” “Utamuamsha?” Nanaa akauliza. “Lazima. Amelala sana. Lazima aamke anyonye.” Mama G alianza kumchezea wakati mama yake yupo bafuni akioga, mpaka akaamka. 

Alitoka akamkuta mwanae ameamka. “Muone vi macho vyake! Unalala mpaka nakuwa na hamu na wewe! Njoo kwanza unichekee ndio nikupe nyonyo.” Nanaa akamchukua. Akambusu na kumkumbatia kifuani. “Na anaonekana ana njaa kweli!” Mama G, akaongeza. “Lazima awe na njaa. Analala sana.” Alibaki akimtizama Nanaa na mwanae. Alikuwa akimuongelesha kama watu wanao elewana vizuri. 

“Eti Liv! Huna hamu na mama!?” Alimuweka chini, akawa akizungumza naye huku akimwangalia mwanae. Nanaa huyu wa sasa hivi aliongezeka furaha na uchangamfu sio kama alivyomkuta asubuhi.  “Ngoja mimi niwaache. Naondoka.” Mama G, aliaga akiwa amenyongea moyoni. Ilishakuwa jioni. “Si tukae kidogo?” “Nataka nipite dukani nikaangalie kidogo kabla hawajafunga mahesabu ya siku.” “Haya mama yangu. Nakushukuru sana, tena sana. Mungu akutangulie. Ukute kila kitu kipo sawa huko kwenye biashara yako.” Mama G akacheka. “Amina.” Akatoka.

~~~~~~~~~~~~~

Alitaka kuondoa gari, lakini akashindwa kabisa. Mawazo yalimrudisha Chuo Kikuu cha Mlimani, akamuona Nanaa vile alivyokuwa amekumbatiwa na Zac. Akazima gari. Alikaa pale zaidi ya nusu saa, Mama G akisikilizishwa na mawazo yake, ile sauti iliyojaa penzi, ya Zac kwa Nanaa. Akakumbuka miahadi ya Nanaa na Zac. Maneno ya Nanaa akimwambia Zac maisha yake na Geb jinsi yalivyo. Kwa Nanaa aliongea kama kitu cha kawaida sana, lakini yeye aligundua udhaifu  mkubwa au mapungufu ya mwanae yatakayomkosesha mke mzuri kama Nanaa. Kwa Nanaa kuongelea sifa za Zac kwake, akajua ndio udhaifu wa Geb, mtoto wake kipenzi. “Hasira imemponza mwanangu!” Akawaza kwa kumsikitikia kiziwanda wake.

Geb Kwa Mama Yake.

Simu yake ilianza kuita, akaitizama, ilikuwa ikitoka kwenye duka lake. Akajua wafanyakazi wake wanamtafuta. Akabaki akiingalia. Hakuwa na nguvu hata yakutoka pale. Bado alikuwa ameegesha gari yake kwenye majengo hayo marefu ya apartment. Akakumbuka furaha ya Nanaa akiwa kwenye gari wakati ana chat na Zac. “Mhh!” Simu ya Geb ikaingia. Akaipokea. “Shikamoo mama.” “Marahaba.” “Mnaendeleaje na mtoto?” “Kwa nini unaniuliza mimi na sio mama yake?” Geb akatulia kidogo. Hakutegemea kusikia hivyo kutoka kwa mama yake. Kwani alijua Oliva mwanae ndiye anayemfanya mama yake acheke na kuongea hata kama amechoka.

“Wewe Geb?” “Mbona leo hivyo mama!?” Alihisi sauti ya ukali kwa mama yake. “Tokea umeondoka nyumbani, umempigia simu Nanaa kumjulia hali yake yeye mwenyewe binafsi na mtoto?” Kimya. “Utajuta Geb wewe! Shauri yako.” “Basi mama. Mimi mwenyewe nitarudi nyumbani muda sio mrefu. Nitamuona mwanangu.” Mama G, aliona kwa wazi utofauti kati ya mwanae na Zac aliyekuwa akimwangalia Nanaa kama alumasi. 

“Nikuulize swali Geb?” “Uliza tu.” Geb akajibu akiitambua sauti ya hasira kutoka kwa mama yake. “Hivi unampango tena na Nanaa au ndio kama ulivyotuonyesha kuwa yupo kwa ajili ya mtoto tu?” “Kwa nini unaniuliza hivyo, tena unasikika ukiwa na hasira? Kwani nimefanya nini tena!? Mbona kama nilishakuomba wewe msamaha na kumuomba Nanaa mwenyewe msamaha! Tena wote mkasema mmenisamehe! Grace pia leo nimezungumza naye na kuomba msamaha! Sasa natakiwa kufanya nini tena? Eti mama?” Geb akawa haelewi.

“Nisikilize Geb. Nanaa ni msichana ambaye hutakaa ukapata mwanamke kama yeye. Yule mtoto unampuuza Geb.” “Simpuuzi mama jamani! Tulikuwa na matatizo ndio nipo kwenye kuweka mambo sawa.” “Kwa njia ipi, na mpaka lini? Utachelewa, uje kukuta mwana sio wako! Wewe fanya mchezo. Wanaume wenzako wanaotambua uthamani wa yule binti, hawachezi kama wewe. Wewe umeondoka tokea asubuhi hujui alipo, yupo na nani, anaendeleaje au hata basi kutuma ujumbe tu! Kwanza hata huwa unamuaga wakati unapokwenda kazini au unapotoka tu kwenda kwenye shuguli zako?” Kimya.

“Mimi ni mama yako Geb, nakwambia utanikumbuka. Fanya mchezo tu. Huyu binti leo amekutana na mpenzi wake wazamani, anaitwa Zac. Kijana kachanganyikiwa, anamtaka mpenzi wake. Nimesikiliza mazungumzo yao. Mmh! Sijui. Sijui Geb mwanangu. Nakuhisi kama umeshachelewa. Zac anaonekana anampenda sana Nanaa, na ni kama anafanikiwa kumpa Nanaa alichokuwa anahitaji maishani. Nanaa uliyemuacha leo asubuhi, siye Nanaa niliyemuacha sasa hivi hapo ndani mida hii. Mwanaume anatuma ujumbe kila wakati na anaonekana anamjulia Nanaa. Nanaa amejawa na furaha usoni. Nimejaribu kumuuliza maswali machache, anaonekana ni kijana anayempenda sana. Hata leo nilivyokuwa nikiwatizama, sio uongo, pale lipo penzi la kweli.” Mama G, alimsimulia kila kitu Geb, mwanae kipenzi. Tena kwa kituo. Neno kwa neno. Kila Zac alichokuwa akimfanyia Nanaa, na vile Nanaa alivyokuwa akilia kwa furaha, na kuonyesha amepata sehemu ya kutulia mzigo wake. Geb alibaki kama amenyeshewa mvua kwenye baridi.

“Nakwambia mzee Magesa atakuwa akizunguka huko kaburi. Wewe sio mtoto aliyetegemea uwe. Hakukutabiria hivyo. Hakujua kama utakuwa mwehu wa kiasi hicho!” “Naomba usiseme hivyo mama!” Geb akalalamika. “Nakwambia kama Mungu angemfufua baba yako leo, akampa dakika moja ya kuzungumza na wewe, hakika angekukana kama wewe sio mwanae. Na wala asizungumze na wewe tena maishani. Baba yako alikufundisha kwa vitendo, wewe mtoto! Uliona kule tulikopita na baba yako lakini akasimama kama mwanaume. Umerithi macho tu hayo, ukamuachia busara zote.” Mama G akakata simu bila kutaka kumsikiliza tena mwanae. Hata hivyo Geb alishukuru vile alivyokata simu. Alijua kama angeendelea kuongea, angemtukana zaidi ya vile.

~~~~~~~~~~~~~

Ni kweli kila Geb alipojilinganisha na Zac aliyesimuliwa na mama yake, akajiona ni kama ameshachelewa. Ni kama mchana na usiku. Alimkumbuka Zac aliyekwisha kusimuliwa na Nanaa. Zac aliyejua kumjali Nanaa. Akabaki kimya upande wa pili. Afanyaje tena wakati alishakosea kwa kiasi kile? Aanzie wapi kurekebisha baada ya kumfanyia unyama mkubwa Nanaa aliyekuwa amejitoa kwake kwa kiasi kile? Ni kweli Nanaa alikuwa na haki ya kumkasirikia baada ya kumfumania kama Zac. Lakini angalau mwenzake alionyesha kujali, akamkimbiza Nanaa mpaka kituo cha daladala, akiwa uchi, akitubia kosa. Lakini yeye hakuweza hata kumtafuta tena Nanaa. Alimkasirikia. 

“Lakini na yeye Zac alikuwa wapi miaka yote hiyo!?” Geb aliwaza baada ya kukatiwa simu na mama yake. “Huyu ni shetani kabisa anataka kuniharibia mipango yangu yote!” Aliendelea kuwaza, akachukua funguo zake za gari kwenye droo, akatoka kuwahi nyumbani.

Kakumbuka Shuka, Kumekuchwa..

G

eb alifika nyumbani, ilishakuwa tayari ni saa 11 jioni. Akafungua mlango akaingia ndani akamkuta Nanaa amekaa upande wajikoni akiwa anajibu jumbe zake kwenye simu na tabasamu usoni. Ukweli alikuwa amependeza. Hakuwa amevaa nguo za kuonyesha amekamia kwenye hiyo safari yake. Lakini alivaa jumpsuit ya rangi moja nyeupe tupu. Iliishia juu ya maziwa, bila mkanda wowote. Ili isianguke, fundi aliyeitengeneza hiyo nguo aliiunganisha na lastiki pana iliyopita kuzunguka mgongoni na kujichora vizuri juu ya matiti ya Nanaa yaliyokuwa yamejaa vizuri. Bila shaka ukubwa uliongezwa sababu ya kunyonyesha. Nywele zake alichana bila kuweka mtindo wowote, akaziachia tu. Ile nywele yenye mawimbi mazuri, ilianguka mgongoni, ikafunika mabega yake. Hakuwa na mkufu wowote shingoni. Labda sababu ya hereni ndefu alizokuwa amezivaa zikakaribia kushika mabega. Aliweka rangi nyekundu kwa mbali kwenye midomo yake, iliyofanya azidi kuwaka usoni. 

Akasimama kwa haraka alipomuona Geb. “Pole na kazi.” Mwili mzima wa Geb ulisisimkwa, asijue kama ni wivu au ni la! Alishaambiwa na mama yake kuwa anasubiriwa, aachiwe mtoto ili Nanaa akaonane na Zac.  Nanaa aliongea kwa sauti iliyoonyesha hofu kwa Geb. Taratibu ile sura ya furaha aliyokuwa nayo, ikaanza kubadilika. “Nikupokee?” Aliongeza Nanaa baada yakuona kimya. “Hapana. Asante.” Nanaa akatulia kidogo huku akijaribu kuweka simu yake chini kwa tahadhari. 

“Vipi mmeshindaje, wewe na mtoto?” Geb akavunja ukimya. “Liv ameshinda vizuri. Amelala karibu siku nzima! Imebidi mama amuamshe ili anyonye. Nimejitahidi kumuweka macho ili angalau ukija umkute, lakini amelala muda sio mrefu.” Nanaa alijibu kama anamjibu mwalimu wake au anatoa ripoti kwa bosi wake. Tena bosi mnoko! Haikuwa hivi tokea zamani. Geb na Nanaa walikuwa wapenzi, tena alimfanya ajisikie vizuri. Wakati ule kila wakiangaliana walitoleana tabasamu.

“Geb!” Nanaa akaita kwa upole. “Naomba nitoke. Sitakuwa mbali. Kuna mtu nakutana naye hapo kwenye mgahawa wa apartment. Sitakawia kurudi. Lakini ikitokea Liv anaamka kabla sijarudi, na ananihitaji, tafadhali naomba unipigie simu. Nitarudi kwa haraka. Chakula chako kipo mezani. Na uji pia upo.” Kitu kilimkaba Geb, akashindwa ajibu nini. Anamkatazaje leo, wakati alishamruhusu kwenda kwa mabwana zake lakini asichelewe kurudi? Anamuuliza anakwenda wapi, wakati hata yeye kuwa anaondoka bila kuaga? Tena hata hakuwa akimwambia anapokwenda!

Wakati mwingine Nanaa alimsikia akimuaga mama yake, sio yeye. Alimpa ruhusa yakutoka, lakini isizidi saa 12 jioni. Tena akitamka wazi huku akimpa baraka zake na kumuonyesha hajali hata kama anakwenda kwa wanaume wengine, yeye hana neno. Alianzisha hiyo tabia baada ya Nanaa kurudi na mtoto nyumbani, akiwa amemkasirikia. 

Aliondoka asubuhi bila kumuaga na wala hakumpigia simu. Ujumbe uliingia kwenye simu ya Nanaa. Nanaa akachukua simu yake. Akarudisha majibu ya ule ujumbe ulioingia, kisha akamgeukia Geb. “Sitachukua muda mrefu, nitarudi.” Wazi Nanaa hakuwa akiomba ruhusa, na alionekana ni safari ambayo lazima aende. Kwanza alionekana alitumia muda wakutosha kwenye kioo. 

“Nimeandika namba yangu ya simu hapa kwenye kikaratasi kama ikitokea inabidi unipigie kama mtoto akiamka.” Nanaa aliongeza. Inamaana huyu Geb hakuwa hata na namba ya simu ya Nanaa! Hata yeye mwenyewe alijisuta nafsini mwake. Hakuwahi kumpigia simu hata mara moja tokea arudi na mtoto. “Umependeza sana.” Ndilo neno pekee alilofanikiwa kulitoa Geb, nakumfanya Nanaa ajiangalie kidogo na tabasamu. “Asante, hata mimi nilifikiri hivyo.” Alijibu kwa sauti yake nzuri na ya upole. Akapita pembeni ya Geb aliyekuwa amebaki amesimama vilevile, akatoka. Geb alimsindikiza kwa macho. Akabaki akikodolea macho mgongo wa Nanaa. 

Hiyo jumpsuit ilimkaa vizuri sana mgongoni. Kiuno chembamba cha Nanaa kilionekana kwa nyuma, huku kikishikiliwa na supu nzuri ya kumtoshea. Hips zake ziliungana na matako na kutengeneza duara zuri lililokuwa limetuna na kushiliwa na jumpsuit hiyo ambayo ilimchora vizuri na kuruhusu yeyote kuona na kuvutiwa. Urefu wa Nanaa uliongezeka kwani nguo hiyo ilikuwa ndefu mpaka chini kabisa. Haikuonyesha kumbana kwa chini, isipokuwa hapo katikati ya kiuno na mapaja tu. Geb alibaki ametoa macho asiamini aliwezaje kuruhusu hasira kumtenga naye. Ni yuleyule Nanaa. Mwanamke aliyezaa naye. Aliyeruhusu hasira zikubali kulala chumba cha pili yake. Ashindwe kupokea msamaha wake, yaishe, akafaidi kile anachoenda kupewa Zac jioni hiyo.

~~~~~~~~~~~~~

 “Hata kama hatampa mapenzi kwa usiku huu, lakini mwenzangu ataliwazwa. Watacheka na Nanaa. Atapata nafasi kuyaona kwa karibu yale niliyojidai nimeyasusa. Pengine atambusu!” Geb alianza kuwaza akiwa amesimama palepale. Akakumbuka midomo mitamu ya Nanaa. Iliyokuwa ikimtoa ofisini kwake BOT na kuifuata popote alipo Nanaa, na kuinyonya hata kwa dakika 5 tu, huku amemkumbatia. Alivuta pumzi, akaenda kukaa kwenye kochi. 

Sio kwamba ilihitaji Visa kukutana na Nanaa. Nanaa alikuwa hapohapo kwenye eneo la apartment, tena analala chumba cha pembeni yake. “Nimechelewa kidogo tu. Leo ndio nilipanga nizungumze na Nanaa kila kitu. Ni heri jana nilipomkuta akilia, ningeongea yote, labda angenielewa kwa haraka, kuliko nije kuanza tena baadaye, tena akiwa na penzi jipya la Zac! Ameshindwa hata kujibu swali dogo tu la ‘umeshindaje wewe na mtoto’! Akaishia kumzungumzia Liv, yeye akajitoa kabisa!” Geb aliendelea kuwaza akiwa amejiweka kwenye kochi. “Daah!” Alijikuta akiongea mwenyewe kwa sauti. Giza lilianza kuingia mpaka sebuleni, lakini hakuwasha taa, akabaki amekaa tu gizani. “Kweli Mzee Magesa atanikana. Sio kwa upuuzi huu!” Geb akajikejeli mwenyewe.

~~~~~~~~~~~~~

Ukisema cha Nini, Zac analilia atakipata Lini!

Zac amerudi kwa kasi mpya. Na Nanaa naye hana kipingamizi.

Alishaomba msamaha mpaka amechoka. Geb alimuonyesha hana shida naye. Usikose mwendelezo kujua yatakayojiri.




CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment