“Siku niliyomwambia tuagane,
nilikusudia aniache nikiwa mjamzito. Mimba yenyewe ilikuwa ndio ya hao kina
Geb. Tumbo kubwa. Halafu kumbuka hapo hata sijafikisha miaka 20. Akanikuta
nimelala sakafuni nipo peke yangu. Alinihurumia sana. Akaniuliza, ‘kliniki
wamekwambia nini?’ Nikamuelezea nikiwa nimelala pale pale chini. Nikamwambia
watoto hawajambo. Wapo wawili. Wameona wakike. Mwingine amejificha. Hapo
namjibu nikijua yeye anawatoto wakike tu. Akaniuliza kama nimekula, presha
yangu ikoje. Nikamjibu nikiwa nimetulia, nachezea funguo zangu za gari bila
hata kumwangalia. Akaniambia, ‘Sijakutupa Oli. Sikujua kama uliamua kushika
mimba. Nilikuomba tusubiri ili niweke mambo yangu sawa. Nilipojua upo mjamzito,
ilibidi kujipanga kwa ajili yako na watoto.’ Sikumjibu. ‘Oli!’ Akaniita.
Nikanyamaza. Akasimama pale kwa muda, akatoka nje.”
“Nikamuona anaingiza begi lake, akarudi
kukaa pale nilipolala. Ndio nikamwangalia. Alikuwa amekonda sana. Nikaanza
kulia, nikakaa. ‘Mbona umekonda hivyo?’ Nikamuuliza. Akasema anaumwa. Alianza
kuumwa miezi michache iliyopita. Lakini alishindwa kwenda hospitalini. Kwa kuwa
kuna mambo ilimbidi aweke sawa. Akaniambia alipojua ni mjamzito, ikabidi
akamwambie mchungaji wao. Akakiri kila kitu mbele ya kanisa. Wakamwambia kwa
umri wake na jina alilojijengea kwa jamii, ni lazima aniache. Kwanza ni aibu.
Anasema alikataa. Akasema mimi ni mkewe pia, na amekusudia kunioa mahakamani.”
“Mama!!” Nanaa akashangaa.
“Hata mimi sikuamini Nanaa. Basi,
wakamtenga na kumwambia asifike kabisa pale kanisani kwa kuwa anawafedhehesha.
Kurudi nyumbani mkewe na watoto wakamuita kikao, na kumwambia ni lazima achague
kati yangu na wao. Ndipo ikabidi awaeleze kuwa tayari mimi nilikuwa mjamzito,
tena wamapacha.” “Mama! Alijuaje wakati mlikuwa hamuonani!?” Nanaa akauliza kwa
mshangao.
“Asingeweza kuniacha bila kujua
linaloendelea Nanaa. Yule Mzee alinipenda kwa dhati. Kwanza wafanyakazi wote
aliokuwa amewaajiri pale walikuwa vijana wake. Sijui alikuwa akiwatoa wapi,
lakini walikuwa wake. Njovu nilihama naye kutoka Kibaha, akaja kunifanyia kazi
pale Posta. Na yeye ndio alikuwa mtu badala yangu pale kazini, na alikuwa kijana
wa Magesa. Kwa hiyo alikuwa akituma ujumbe kwa Magesa kumueleza kila kitu
kinachoendelea. Nani ananitongoza. Kama nimekubali au la. Kwa hiyo nilijua
ananiulizia. Basi. Akawaambia wanae hayupo kwenye hali yakuchagua tena. Yeye ni
baba kwao na kwa watoto hao wasio na hatia. Ambao hawakuchagua wazaliwe na
nani. Hapo anasema ni mwezi uliopita, na alishaanza kuumwa.”
“Basi, wakamfukuza pale ndani, na
kumwambia hawamtaki tena awe baba yao. Na mkewe akampokonya mali zote, akasema
kwa kuwa yeye ndio anaondoka, lazima aache kila kitu. Akawaomba wampe muda
wakufikiria, wakamwambia akiwachagua wao ndio arudi, lasivyo wao wanaondoka
kwenda kuishi na wazazi wa mama yao huko Machame. Basi anasema ikabidi yeye
ndio atoke kuliko kuwaharibia watoto wao maisha. Alikuwa akipenda sana binti
zake. Anasema aliishi hotelini huku akijaribu kuweka mambo sawa ya nyumbani
kwake, lakini hakufanikiwa. Walimwambia nilazima aachane na mimi. Sasa wakajua
kama alininunulia gari na amenipangishia nyumba. Mbaya zaidi ile biashara iliyokuwa
inashamiri hapo Posta.” “Sasa walijuaje?” Nanaa akahoji.
“Mtu yeyote anayekuletea habari za
umbea wewe, ujue hashindwi kutoa habari zako na wewe na kumpa mwingine. Hao hao
vijana wake ndio walikuwa wanamgeuka Magesa. Kila kitu kilichokuwa kikiendelea
kati yetu, walikuwa wakimwambia yule mama na wanae. Sasa wakataka Magesa
aninyang’anye vile vitu. Magesa alikataa kata kata. Wakashitakiana kila mahali,
Magesa akakataa kuninyang’anya. Uthibitisho wa zile documents zote za kununua
gari yule mama alikuwa nao. Akawa anawaomba wazee wamuulize Magesa gari
alilolinunua kwa pesa wanayohangaika wao wawili, mchana na usiku, liko wapi?”
“Mama!” Nanaa akashangaa.
“Yule mama alikuwa na haki, Nanaa.
Walihangaika na Magesa mchana na usiku bila kupumzika! Magesa akakiri kuwa ni
kweli amenikabidhi mimi. Lakini hawezi kunipokonya. Ni heri atoe gari yake
awape, kuliko kuchukua gari aliyonipa mimi. Hawakuamini. Gari ya Magesa ilikuwa
nzuri sana. Mpyaa. Safi sana. Akatoa funguo akamkabidhi yule mama. Yule mama
hakukubali. Akamshitaki Magesa kuwa hamuamini tena na mali zao, kwa kuwa
ameanza kuhonga nje. Kumbe muda wote huo alikuwa kwenye heka heka! Magesa
anasema hakutaka ugomvi na mkewe, akakiri kosa huko mahakamani. Na kukubali
mali zote ziende kwa jina la mkewe. Wakili wake akamwambia ni lazima iwe kwa
majina yao yote mawili, lakini Magesa akakataa. Akamwambia mali zinatafutwa,
lakini sio kitu alichonacho kwangu. Nililia Nanaa. Nililia siku ile. Sikuamini
kama Magesa amenichagua mimi na kuyatupa maisha yake.” “Jamani mama! Kwa hiyo
wakamfilisi?” Nanaa alitaka aendelee.
“Yaani vile alivyokuwa ameingia siku
ile, ndio alikuwa amemaliza.” “Hukujuta?” “Nilifurahi sana. Kwamba ndio mimi
nimesusiwa Magesa! Mungu anipe nini? Kwanza ukumbuke kuanzia mwanzo niiyekuwa
namtaka ni yeye. Sikuwahi hata kuchanganywa na mali zao. Alikuwa mgonjwa, na
mimi mjamzito, lakini sikumuachia siku ile. Kila saa ananiweka pembeni,
ananiuliza, hivi umeelewa nilichokwambia? Namwambia nimeelewa kuwa sasa hivi
wewe ni wangu. Magesa akawa anacheka tu. Akaniuliza akitokea mwanaume mwenye
pesa zaidi yangu. Nikamjibu kuwa hao wapo tu, na wala hawataisha. Niligaragara
naye hapo chini nafurahia siamini. Usiku nikampeleka hospitalini. Sijakaa sawa
tupo tunamsubiri daktari, akaanguka nakupoteza fahamu.” “Uwiii!” Nanaa akashituka.
“Acha Nanaa. Nilikuwa namdai Mungu kama
namjua vile au kama yupo hapo. Eti Magesa kapoteza fahamu siku tatu!
Nilizicheza ngoma zote. Nikamwambia Njovu awaambie familia yake wajue kama baba
yao mgonjwa, unajua walijibu walishafuta undugu naye! Mkewe akasema hataki
kumsikia yule baba. Nanaa, nilikuwa nazunguka pale Muhimbili kama mwehu. Tumbo
kubwa, namwambia Mungu namtaka Magesa. Muda wa kuona wagonjwa ukifika, naenda
kupiga magoti pembeni ya kitanda chake. Kuomba sijui, mtoto niliyelelewa na masista.”
“Tena hapo mwizi wa mme wa mtu! Sijali.
Namwambia Jesu ulizungumza na yule
mwizi pale msalabani, basi naomba azungumze na mimi. Watu wanajua ninamlilia
baba yangu, kumbe mme.” Nanaa akaanza kucheka gafla. “Tumbo kubwa kama nataka
kuzaa, kumbe ni miezi 5 tu. Tako na lenyewe limeumuka, nikipita unaona tumbo na
tako tu. Nilikuwa natembea pale Muhimbili asubuhi mpaka asubuhi. Njovu akawa
anakuja kunitoa pale kwa nguvu, ananirudisha nyumbani. Saa 11, nipo hospitali
ya Muhimbili kwa Magesa. Alikaa pale karibia mwezi ndio nikarudi naye nyumbani.
Nilimlisha, mpaka anatoka pale akawa kama kijana.”
“Bwana Magesa alinawili! Kazi yake
ilikuwa kula kulala. Mapenzi mazito. Sitaki mambo yakumkera. Usiku Njovu
anarudi nyumbani, analeta pesa, nyingine anakuwa ameshaweka benki.” “Mlikuwa
mkiishi na Njovu?” Nana akauliza. “Yule baba asingekubali niishi kule
Kinondoni, peke yangu. Alikuwa na wivu Magesa kuliko nitakavyokwambia. Njovu
aliwekwa pale kama mlinzi. Lakini alitusaidia sana na Magesa. Halafu alikuwa
mwaminifu sana.”
“Yuko wapi sasa hivi?” “Alikuja kufa
kabla hata ya Magesa. Alikuwa muhuni sana. Alikuwa anapenda sana wanawake. Ndio
ulikuwa ugonjwa wake. Magesa aliumia sana alipo athirika. Alikufa mikononi
mwetu. Halafu wakati ule madawa hayakuwa mengi kama sasa hivi. Ukiathirika
unakufa kwa haraka.” “Jamani! Eehe?” “Nanaa mtoto mbea huyu!” “Bwana nimalizie.” Mama G akacheka.
“Maisha yakaanza. Mimi na Magesa wangu.
Kuanzia asubuhi mpaka usiku. Kila kitu tunafanya pamoja. Kuanzia kuoga, mpaka
kulala. Mtoto deko, nadekezwa. Biashara yetu ya Posta ikachangamka. Si
nilikwambia Magesa ana akili sana?” “Kama mwanae Geb.” Mama G akacheka. “Hivyo
hivyo. Na alimwambia Geb. ‘Wewe una akili sana. Lakini utafanikiwa zaidi ukiwa
mfanyabiashara’. Naona hicho kitu kikamwingia sana Geb. Basi, tukaanza
kuendeleza ile biashara. Akaanza kuuza tena maziwa. Lakini safari hii akawa
anauza yaliyokwisha fungwa kwenye paketi. Kabla hata sijajifungua, akawa
amepata sehemu maeneo ya Chang’ombe. Anasambaza maziwa ya paketi jijini. Mtindi
kwa fresh. Kumbuka alianza biashara kwa pesa tuliyokuwa tunapata au
niliyoikusanya pale kwenye biashara ya Posta. Alichukua pesa yangu yote benki
akaiwekeza. Alikuwa na akili yule mwanaume, hujawahi ona Nanaa. Ukimuona
amenyamaza anaandika, mwache, ujue kuna
kitu cha maana anaandika.”
“Basi siku za kujifungua zikafika.
Nikashindwa kuzaa. Watoto wakubwa.” “Naona na Grace pia mrefu!” Nanaa
akaongeza. “Kama baba yao. Magesa alikuwa mrefu sana. Basi nikafanyiwa
upasuaji, Grace akatoka wa kwanza, akaja Geb wakiume ambaye hata sikumtegemea.
Mimi na Magesa tukamshukuru Mungu kwa pamoja. Akasema ni kwa rehema za Mungu tu
ndio alitupa wale watoto, hatukustahili. Ndio akamwita Grace, na mdogo wake
akampa jina la Geb. Lina asili la ki Egypt kuwa ni mungu wa ulimwengu huu. Akamtabiria
kuwa kila atakachoshika katika ulimwengu huu, kitastawi sana.” “Kumbe majina ya
wanao yanamaana kubwa hivyo!” “Magesa huyo.” “Lakini hata lako mama. Wakati
umesema tumwite Oliva mwanangu, nikakubali kwa haraka sana nikasema tutamwita
Liv kwa kuwa aliishi hata katikati ya yale matatizo. Walinifanyia mpaka
upasuaji, na kunipa madawa makali. Lakini akatulia tuli mwanangu mpaka
akazaliwa. Tena bila kasoro. Na uliponipa maana ya Oliva, naona kama mnafanana!
Wote mnastawi kwenye mazingira magumu.” Mama G, akacheka.
“Ikawaje sasa mama?” “Wewe Nanaa! Nenda
kanyonyeshe wewe mtoto acha umbea!” “Nimalizie bwana.” “Sasa wewe mtafutie Geb
sababu. Nenda kamchungulie mwanao. Unasubiri mpaka uuitwe! Shauri yako.” “Kwa
hiyo niende?” Nanaa akauliza. “Wewe si umekaribishwa huko chumbani? Nenda.
Mshike mwanao, jizungushe kisha toka.” Nanaa akasimama. “Lakini utakuja
kunimalizia stori?” “Yatakushinda wewe Nanaa!” Nanaa akatoka anacheka sio kama
vile alivyokuwa akilia.
~~~~~~~~~~~~~~
Kweli, Nanaa alitulia akaanza kumlea
mtoto wake. Akimsikia ameamka kwenye monitor, anaamka na yeye anakwenda
chumbani kwa Geb. Anamchukua mtoto, anakaa naye kwenye kochi, anamnyonyesha,
huku amemkumbatia kwa mapenzi na kumshika shika. Wakati mwingine alitulia akiwa
anamtolea tabasamu na kumchezea vidole vyake vya mkono wakati ananyonya. Wakati
mwingine alipokuwa akimsikia mtoto ameamka, anapokwenda, anamkuta Geb anampa
maziwa ya chupa aliyokamua.
Siku zikazidi kwenda, Liv anakunywa
maziwa ya mama yake kwa chupa na kunyonya. Taratibu yule mtoto akaanza kumjua
mama yake. Akimuona Nanaa, au akimshika anatulia kabisa na kuonyesha kufurahia.
Tayari alishamaliza miezi miwili, akawa amechangamka, lakini bado Geb hakuwa
akimuongelesha Nanaa. Nanaa alishaomba msamaha akaamua anyamaze. Kwa asili Geb
ni mkimya, ukichanganya na kiburi alichonacho, haikumsumbua kunyamaza.
Alikuwa akilala na mtoto wake. Asubuhi
wakati anaenda kazini anamuacha kitandani kwake, akijua lazima mama yake
atakwenda kumchukua na kumuhudumia. Na alitaka akirudi mchana au jioni amtawale
mtoto wake. Nanaa alilielewa hilo, kila siku asubuhi alipomsikia Geb anaingia
chumbani kwake na kumuachia pesa za matumizi kabatini kwake, alijua ndio
anaondoka, na yeye ndipo alipokuwa akiamka kwenda chumbani kwa Geb anamchukua
mtoto wake, anarudi naye kulala naye akiwa amemkumbatia chumbani kwake siku
nzima mpaka akisikia gari ya Geb.
Ilikuwa kila akisikia gari ya Geb,
anambemba na kumrudisha kitandani kwake kwa haraka, kabla Geb hajamkuta. Liv
alikuwa mtoto mzuri wa kutochosha kumwangalia. Kwa kuwa alikuwa akinyonya sana,
alikuwa na mwili mzuri, mkubwa. Hata Geb alipokuwa akimpeleka kliniki alikuwa
akisifiwa kuwa anamtunza vizuri. Alikuwa na nguo nyingi sana, hakuwa akirudia.
Kila Geb aliporudi kutoka kazini alikuja na nguo mpya na vitu vya huyo mtoto.
Macho yalikuwa kama ya Geb. Alikuwa na nywele nyingi sana kama baba yake. Kwa
kuwa alichukua rangi ya mama yake, kwa haraka sana mtu ungeweza kusema ni mtoto
aliyechanganyia na damu ya kiarabu.
Geb alimpiga picha za kila namna na
kutundikwa katika kila kona ya hiyo nyumba. Nyingine zilikuzwa zikawa kubwa
sana, nyingine za rangi ya nyeupe na nyeusi, ilimradi tu ile nyumba ilijaa Liv.
Muda mwingi aliutumia nyumbani na mtoto wake. Na akiwa nyumbani, hakutaka
kuingiliwa, alikuwa yeye na Liv tu. Bado alikuwa haongeleshani vizuri na mama
yake, kidogo alimuogopa kwa kumgombeza siku alipomfungia Nanaa nje. Lakini
afadhali yeye alimsalimia lakini sio Nanaa. Alipofungua mdomo wake kuongea na
Nanaa, ilikuwa ni kumpa maagizo tu. Hapakuwa hata na salamu.
~~~~~~~~~~~~~~
“Sasa na wewe uache kuzunguka na khanga humu
ndani.” “Naona rahisi kunyonyesha.” “Mambo yakishamba matupu hayo! Kwa hiyo
unaenda chumbani kwa Geb na makanga!?” “Si nakuwa naenda kunyonyesha?” “Uwiii!
Ndio maana hata ukimuongelesha hakujibu. Unamkera.” “Mama jamani!” “Kumbe!
Kuzaa imekuwa nongwa! Ulikuwa unapendeza mwenyewe, rangi yako nzuri, umbile
Mungu kakujalia, halafu unajiachia kwa mtoto wa kwanza tu! Wewe nenda kanunue
vigauni vyako vizuri, na vya maana. Vyenye zipu au vifungo mbele. Nunua sidiria
ya kunyonyeshea. Sio kutoa ziwa lote mpaka mtoto mwenyewe anakinahiwa!” Nanaa
akaanza kucheka.
“Mama nyie!” “Sasa je! Tengeneza
nywele, kuwa msafi.” “Mtoto ameanza kusumbua kunywa maziwa ya chupa. Nikitoka
itakuaje?” “Tutaenda wote huko madukani.” “Geb hawezi kuruhusu tutoke na
mwanae. Kliniki yenyewe anampeleka mwenyewe!” “Anajidai tu. Akitaka aache kazi
aje akae na huyo mwanae hapa. Lakini lazima kesho tutoke. Nitamwambia.”
Wakakubaliana.
Kesho yake Geb aliwahi kutoka kazini na
kurudi kukaa na mtoto wake. Nanaa na Mama G, wakatoka kwenda madukani. Mama G
akamnunulia nguo nzuri. Za kulalia usiku, na kuvaa wakati wa mchana.
Akamnunulia sidiria nzuri kwa ajili ya kunyonyeshea. Wakapitia sehemu
wanayosuka. Akaomba wasichana watatu, wafike nyumbani kwao asubuhi sana kwenda
kumsuka Nanaa. Akawaambia aina za nywele anazotaka kusukwa, Mama G akamlipa
mmoja wao kwenda kuzinunua hizo nywele, japokuwa zilikuwa za gharama sana,
lakini Mama G alikubaliana naye kuwa zitakaa muda mrefu.
Walirudi nyumbani mapema tu, mtoto
alikuwa bado amelala. Kama kawaida Nanaa alienda kuoga akaenda kumchukua mtoto
wake na kuanza kumnyonyesha. Geb akatoka bila kuaga, wakajua amerudi kazini.
Jioni akarudi, akamfuata Nanaa chumbani kwake. “Kesho utatoka tena?” Nanaa
akamgeukia kama kutaka kujua kwa nini anamuuliza hivyo. “Kuna mahali nataka
kwenda. Nitachelewa kurudi. Naweza kurudi usiku, na sitaki uzurule na mtoto
wangu. Kama unasafari zako, nataka uniambie mapema, ili niahirishe safari zangu
nije kukaa na mwanangu.” “Kesho sitatoka. Nitakuwepo.” Geb akatoka. Nanaa
alibaki akijiuliza. Ndio kwa mara ya kwanza ametoka pale ndani tokea aingie,
lakini Geb ameonyesha kutokufurahia!
~~~~~~~~~~~~~~
Geb alitoka asubuhi na mapema, Nanaa
akamsikia akimuaga mama yake kuwa anakwenda Morogoro, lakini atarudi usiku.
Kuna jambo anafuatilia. Lakini hakumuaga Nanaa, akaingia chumbani kwake,
akamuwekea pesa juu ya kabati kama kawaida, akaondoka. Wasusi wote watatu
walifika hapo saa moja asubuhi. Alitaka asukwe nywele ndogo ndogo sana, za
kusukwa chini na kuachia juu, kwa kutumia “100% human hair”. Iliyomgharimu sana
Mama G. Mpaka kufika saa tano asubuhi alikuwa ameshamalizwa.
Alipendeza sana. “Na hizo dimpozi huko
mashavuni, umezidi kupendeza mwanangu. Hapo ukimshika Oliva ndio watakubali
kabisa kama wewe ni mama yake. Maana manywele hayo ndio mmefanana zaidi.” Nanaa
akacheka. “Asante mama yangu kwa kunipendezesha.” “Halafu mtu hawezi kujua kama
sio zako! Zimekuwa kama zako kabisa!” Msusi mmoja aliongezea sifia. Walilipwa
pesa yao, wakaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~
“Mbona vidole kwenye simu muda wote?” “Si
unakumbuka jinsi nilivyoondoka chuoni? Sasa mizigo yangu yote nilimuomba yule
matron anitunzie.” “Antii?” Mama G akauliza.
“Huyo huyo. Ndiye aliyekwenda kunichukulia pale chumbani kwangu,
amenihifadhia kwake. Sasa ndio anauliza ni lini naenda kuvichukua? Nyumba yake
ni ndogo kweli! Vitakuwa vinamkera.” “Si twende sasa ukavichukue uje uvihifadhi
huko stoo!” Mama G. Akaonyesha utayari. “Sio hapa mama. Nipo kwenye makubaliano
ya bei na dalali, anachumba. Lakini wapo watu kama watatu wanakitaka hicho
chumba. Ndio nimemuomba akazungumze na mwenye
nyumba, kama atanipa mimi.” “Kwa nini ukakodishe chumba wakati nyumba
hii ipo?” Nanaa akaanza kutokwa na machozi.
“Hapa sio
kwangu mama. Unakumbuka jinsi nilivyofukuzwa siku ile? Nilifungiwa nje! Nipo
hapa ndani kwa masharti makali sana. Itakuaje siku nikiyavunja halafu vitu
vyangu nimefungia humu ndani? Hiyo mizigo niliyoiacha kwa Antii, ndio juhudi
yangu yote. Kuna vyeti vyangu kuanzia darasa la saba mpaka kidato cha sita.
Hivyo vyeti ndio ndugu, ndio mama yangu, ndio baba yangu. Ndio tumaini pekee
nililobaki nalo hapa duniani. Nimevipata hivyo vyeti kwa shida sana mama. Kwa
masimango, mateso, kulala bila kula, na dhiki ya kila namna. Kuna kipindi
nilikuwa natamani kukata tamaa, lakini nilikuwa najiambia shule atakuja kuwa
mkombozi wangu, ndio maana nilihakikisha nakosa kila kitu, lakini sio shule.”
Nanaa akaendelea huku akilia.
“Acha nivitafutie kwao, vikae hapo vikinisubiri.
Hata siku nikija kufukuzwa tena hapa, nitajua vipo kwetu vinanisubiri. Vitakaa
hapo kama ndugu. Acha na mimi niwe na kitu changu mama. Nimeshahangaika
vyakutosha. Nimenyanyasika vyakutosha. Mungu akinisaidia nikapata cheti kizuri
cha chuo, nitatafuta kazi, na mimi nianze kujitegemea.” “Na mtoto?” Mama G akauliza.
“Unafikiri nitakuwa na
kazi gani tena hapa kama Liv akianza kula? Geb ameweka mpaka kabisa kati yangu
na mwanangu. Amenionyesha kwa vitendo sihitajiki humu ndani. Ananihitaji kwa
kumnyonyesha tu mtoto, tena wakati mwingine hataki hata nimguse mwanangu yeye
akiwepo. Siku za jumamosi na jumapili kama unavyomuona. Anakuwa na mtoto
kuanzia asubuhi mpaka asubuhi. Akilia anampa maziwa ya chupa. Ananiambia
nikamue niweke kwenye chupa. Hebu niambie mama yangu, huyu mtoto akianza kula,
nitahitajika kweli hapa ndani?” Mama G, akanyamaza kidogo.
“Ulimjaribisha tena kuzungumza naye?”
Mama G, akauliza. “Japokuwa aliniumiza sana kunifukuza kwake na kunifungia nje,
nilikubali yaishe ili kulea mtoto kwa amani. Nimeomba msamaha, mpaka nimeamua
kuacha tu. Hanijibu kitu, akiongea na mimi ni kunipa maagizo tu. Hata akiingia
chumbani kwangu ni kuacha pesa, basi. Tena kuna mahali huwa anaziweka, juu ya
kabati langu. Kiasi chake ni kilekile, kila siku. Nimezikusanya, ni pesa
nyingi. Hivi nimemkusanyia nitamrudishia.” “Usifanye huo ujinga hata siku moja,
Nanaa. Wewe upo humu ndani, unalea mtoto, unafikiri pesa utapata wapi? Zitunze
hizo pesa, hujui ni lini zitakusaidia.” Nanaa akanyamaza. Akaenda kuoga,
akaenda kumchukua mtoto wake, akaenda kulala naye kitandani kwake.
Walikula hapo hapo chumbani huku
wakiongea na Mama G, mpaka ilipofika tena jioni, Nanaa akapitiwa na usingizi
akiwa amemkumbatia mtoto wake palepale kitandani. Hakusikia wakati Geb
anaingia, akaenda kumtafuta mtoto wake kitandani akamkosa. Akaenda chumbani kwa
Nanaa, akamkuta Nanaa amemkumbatia, wamelala. Aliingia kuoga akarudi kumchukua
mtoto wake mikononi kwa Nanaa, Nanaa alishituka sana, akakaa na kuanza kulia
alipomuona Geb amemchukua mtoto. “Nimekwambia mwache mtoto alale kitandani
kwake kama mimi sipo. Usinijaribu Nanaa!” Nanaa akaendelea kulia huku ameinama
bila kujibu kitu. Alilia, akarudi kujilaza.
Alishituka tena usiku akamsikia mtoto
wake analia kuliko kawaida yake. Nanaa akaenda chumbani kwa Geb. “Kwa nini
analia?” Akamkuta Geb anambembeleza. “Wewe ndio umeharibu kila kitu. Kwa nini
unalala na mtoto unamkumbatia? Sasa hivi ni kama amechanganyikiwa haelewi
anatakiwa kulala wapi!” “Naomba nimbembeleze.” Nanaa akasogea. Alipomshika tu
nakumuongelesha kidogo, mtoto wake akatulia. Nanaa akakaa chini, akatoa ziwa na
kuanza kumnyonyesha.
Aliponyanyua uso, macho yake
yakagongana na Geb, alimkuta anamtizama kwa kujiiba. Akajitengeneza nywele zake
vizuri, akavuta kitambaa, akajifunika yeye na mtoto, kama kujificha Geb asione
matiti yake. Liv aliendelea kunyonya kama mwenye njaa sana. “Kesho nataka
kutoka.” Nanaa akavunja ukimya wakati bado amempakata mtoto wake akinyonya.
“Lazima niende kwanza kazini, nikirudi ndio na wewe utatoka kwenda kuzurula.”
Nanaa hakujibu akainama na kuendelea kucheza na nywele za mtoto wake taratibu
kama kumbembeleza wakati bado akinyonya.
~~~~~~~~~~~~~~
Kesho yake Nana alijiandaa, akamuaga
Mama G, na kumwambia Geb akirudi tu, na yeye atatoka kwenda kufuatilia chumba,
na kama akifanikiwa, atakwenda kuchukua mizigo yake na kuihamishia kwenye hicho
chumba. Akachukua pesa zote alizokuwa akiziacha Geb juu ya kabati lake, akaenda
kuziweka kwenye kabati la mtoto chumbani kwa Geb. Akatoka akawa amekaa na Mama
G jikoni wakitaniana. “Leo sijui kama utarudi! Ulivyopendeza hivyo!” Nanaa
alikuwa anacheka tu. “Wakikuona huko, lazima wakuibe.” “Hapana bwana mama. Na
Liv wangu?” “Si yupo kwa baba yake!?” “Na kweli. Nitamtafutia mdogo wake.” “Na
ulivyopendeza hivyo, atakuja mdogo wake kwa haraka sana.” Wakaendelea kucheka.
Mara wakasikia mlango unafunguliwa, wakajua ni Geb, wakanyamaza.
Akaingia hapo jikoni akiwa na mifuko
mkononi. “Ni nini hicho?” Mama G akamuuliza. “Maziwa ya Liv.” Nanaa akashituka
sana. “Mimi bado nina maziwa mengi tu. Naomba usimuanzishie mtoto maziwa ya
kopo.” “Kama unamaziwa mengi kwa nini jana nimekuta chupa moja tu?” Geb
akauliza. “Liv ameanza kukataa kunyonya kwenye chupa, Geb. Nikiwa naye anataka
nimnyonyeshe tu.” “Labda hataki maziwa yako yakiwa kwenye chupa, haya
atayanywa.” “Tafadhali Geb, usimpe mtoto maziwa ya
kopo sasa hivi wakati mimi mwenyewe nipo.” Nanaa alishaanza kulia.
“Wewe Nanaa, niangalie mimi. Huyo mtoto
hatapewa maziwa ya kopo. Nyamaza uende uwendako ukiwa umetulia. Sio unakutana
na watu macho yamevimba! Umependeza sana, acha kujiharibia siku yako. Toka na
furaha yako, kafanye mambo yako uwahi kurudi umnyonyeshe mwanao. Si umeacha
maziwa mengine?” “Nimekamua chupa tatu mama.” “Haya
nyamaza, uende. Mwanao hatakunywa maziwa ya kopo, atampa ya kwako.” Geb akatoka
mle ndani kwa hasira, wakamsikia akipigiza mlango. “Wewe nenda. Achana naye.”
Nanaa akatoka akiwa ametulia.
Uchungu Wa Mwana, Aujue Mzazi.
Ilipofika saa 11 jioni Grace, Fili na
Danny wakaingia. “Naona tumbo linakaribia kuanguka.” Mama yake akamchokoza
Grace. “We acha tu! Watoto wenyewe wawili tu wapo humo tumboni, lakini
utafikiri nimebeba jeshi!” Grace akakaa. “Anakula huyo! Utafikiri anakwenda
vitani.” Danny akadakia. “Niache Danny. Unafikiri mimba ya watoto wa kiume
mchezo?” Grace na mumewe waliingia wakiwa wanaongea, Grace akajitupa kwenye
kochi, Mama yake akaanza kucheka.
Mara Liv akaanza kulia akiwa chumbani.
“Hee! Hii nyumba ina mtoto au mlio wa simu?” Danny akahoji, ndipo wakanyanyua
macho kuangalia ukutani. “Huyu mtoto wa kiukweli au ni zile picha za watoto za
kununua ndio mkapamba ukutani?” Grace akahoji na kujipinga tena. “Hataa! Haya
macho na nywele za huyu mtoto kama navifahamu! Fili alizaliwa hivi hivi kasoro
rangi tu! Huyu mweupe.” Danny akaanza. “Geb! Geb weee! Hebu njoo bwana. Acha
kutufanya mimi na mke wangu kama machizi, tunaulizana na kujijibu wenyewe!” Geb
akatoka amembeba mtoto. Wote wakanyamaza kwa gafla, macho yakawatoka.
“Huyu mtoto ni wa nani!?” Baadaye Grace
akauliza na mshangao mkubwa machoni. Akavuta suruali ya Geb ili amsogelee
karibu, amuone huyo mtoto. “Hebu nipe mimi huyu mtoto.” Akapewa, akaanza
kumchunguza taratibu. “Kwa kuwa huyu mtoto sio wangu, basi ni wa Geb.” Grace
akanyanyua uso na kumtizama mama yake. “Anaitwa Oliva.” Mama G, akaongeza. “Si ni jina lako mama?”
Grace akaendelea kuhoji. “Ndiyo.” “Kwa hiyo ni mtoto wa Geb?” Kimya. “Mbona
kama kunakufichwa hapa?” Danny akalalamika.
“Ndiyo ni mwanangu.” Grace akamwangalia
kaka yake kwa kukunja uso. “Sijaelewa. Yaani wewe Geb una mtoto, halafu
huniambii mimi wakati tunaonana karibia kila siku na tunakuwa wote siku
nzima!?” “Acha kunikasirikia Grace, huyu mtoto na mimi nilikuwa sijui kama
yupo.” “Wewe ulijua lini kama huyu mtoto yupo?” Grace akauliza akisikika
ameshakasirika. “Miezi miwili sasa.” Mama yao akajibu kishabiki.
“Ngoja kwanza mama. Yaani wewe upo na
huyu mtoto humu ndani, unashindwa kutuambia? Undugu umeisha kati yetu?” “Wala
usiende mbali Grace. Humu ndani kuna hekaheka, sio mchezo.” Mama G, akasogea
akakaa pale kwenye makochi. “Yaani Grace, pakikucha au pakiingia usiku mkapanda
kitandani kwa amani, mnashukuru Mungu. Kumegeuka kuwa kambi ya jeshi. Vilio
haviishi, ubabe ndio usiseme.” “Ngoja kwanza mama. Tuanze kwa hatua. Mama yake
huyu mtoto ni nani, na yuko wapi?” Danny akauliza.
“Mama yake huyo mtoto anaitwa Nanaa,
dada yake James.” Kila mtu akamwangalia Geb, aliyekuwa ametulia kimya, mikono
yake mfukoni. Grace akachukua headphone kutoka kwa mumewe, akamvalisha Fili
baada yakumuwashia simu acheze game.
“Hebu endelea mama. Maana nahisi ni stori!”“Huyo Nanaa katoka hapa muda sio
mrefu. Lakini kutokana na masharti aliyopangiwa humu ndani, haruhusiwi kurudi
tena leo. Labda mpaka tena keshoo kabla ya saa 12 jioni. Sasa hivi, yaani mida
hii, katoka kunitumia huu ujumbe hapa.” Mama G, akachukua simu yake akaanza
kusoma.
‘Mama, nimetoka hapo nyumbani
muda mbaya. Nimepelekwa kwenye hicho chumba. Ukweli nikizuri sana, na tupo watu
kama watatu tunakitaka. Ikabidi kumfuata mwenye nyumba, nyumbani kwake ili
nizungumze naye, mimi mwenyewe kujaribu kumshawishi ili anikodishe mimi.
Ameniambia nifuate jibu kesho. Lakini foleni ni kubwa sana mama yangu. Sasa
hivi ni saa kumi na mbili kasoro. Hakuna muujiza wa kufika hapo nyumbani kwenu
kabla ya saa 12. Ili nisimuudhi zaidi Geb, na nisivunje sharti jingine,
nikakosa hata hiyo nafasi yakunyonyesha, naona heri nichukue tu chumba
hotelini, nilale kwa usiku huu. Kesho nitajitahidi kuwahi kurudi mapema.
Nimeacha maziwa yakutosha. Nina uhakika yatamtosha Liv hata mpaka kesho.
Tafadhali mama yangu, hakikisha Liv wangu hanywi maziwa ya kopo. Tafadhali sana
mama. Simu inaishiwa chaji. Nazima mpaka nikipata hoteli ya kulala usiku huu,
ndipo nitawasha ili kukutaarifu nilipo mama yangu. Mbusu mwanangu kwa niaba
yangu. Mwambie ninampenda sana.’
~~~~~~~~~~~~~~
Mama G akamaliza kusoma na ukimywa
mzito ukatanda. Grace alisikika akivuta pumzi kwa nguvu akajiegemeza kwenye
kochi vizuri. Danny akamchukua yule mtoto kutoka kwa mkewe. “Bwana toto zuri
hili, kama toto la kimanga! Macho yake mazuri kama ya mke wangu!” Danny
akaendelea kusifia huku akimwangalia Liv. “Mbona kama nimechanganyikiwa zaidi
ya mwanzo! Ni nini kinaendelea?” Grace akauliza. “Acha nikueleze mwanangu,
maana mimi nipo kwenye uchungu wakupitiliza. Nimeongea na Nanaa kwa kituo.
Akanieleza mambo yote.” Mama G akaanza kuelezea kuanzia mwanzo anaitwa na Nanaa
chuoni.
“Yaani ndio alikuwa ametoka
kujifungua!?” Grace akahoji kwa mshangao mkubwa. “Haswaa. Alijifungua Jumatatu
alipotoka tu kwenye mtihani, sasa jumatano asubuhi ndio akanipigia simu
nikamshikie mwanae, kwa sharti nisimwambie mtu. Nikaona ameniamini mimi na
kunisamehe. Kumbuka tokea nimuache nje kwenye ile harusi ya Malii, sikubahatika
kupata muda naye nikaomba msamaha. Sasa kuja kunipigia simu na kunitaka msaada,
nikajiona nimebahatika na amenisamehe. Sasa nikasema nisivunje Imani yake
kwangu. Nimsaidie mpaka amalize mitihani ndipo tuzungumze naye.” Mama G
akaendelea.
“Nikaanza kazi ya kupika hapa na kwenda
kukaa naye na mtoto. Tena hapo nilimbembeleza kweli, baada ya kumuhurumia.
Maana alitaka msaada kipindi anaingia kwenye mtihani tu. Muda mwingine alisema
atakaa na mwanae, nisiwe na wasiwasi. Nikamuhurumia sana. Kwanza alikuwa
amekonda sana. Huku ananiambia alikuwa akila kama mchwa lakini manesi walikuwa
wanamcheka kuwa mtoto ndio alichukua chakula chote. Kazaa mtoto mkubwa kweli.”
“Hata sasa hivi huyu mtoto ni mkubwa, hafananii na wa miezi miwili. Ehhe?”
Grace akataka aendelee.
“Pili nikakumbuka jinsi Nanaa
alivyohangaika kumaliza chuo. Mnakumbuka alipokuja hapa kuchukua vitu vyake ili
aende chuo?” “Nakumbuka. Alikuwa kama anataka kukata roho!” “Ewaa. Sasa yote
hayo nikayakumbuka. Nikasema maadamu ameniita, lazima nimsaidie. Huku
nikijitahidi kukukwepa wewe na Geb. Sikutaka mtu yeyote amuingilie na mipango
yake ili atulie amalize mitihani yake.”
Mama G akaelezea kila kitu mpaka Geb alipomfukuza Nanaa, akamfungia nje,
jinsi anavyomnyanyasa Nanaa na mtoto wake, masharti aliyomuwekea Nanaa.
“Wakati na mimi nilishangaa siku ile
kumkuta Liz yupo uchi humu ndani wakati Geb ameanza mahusiano na Nanaa!” Grace
akaanza kulia. “Hata mimi nilikasirika sana,
nikamwambia Danny. Tena nakumbuka nilikutana na Liz yupo uchi hapo koridoni, na
mwenzie huyu yupo na boxer. Nikawalazimisha warudi chumbani wakavae, kwa kuwa
Fili na Danny walikuwa wakiingia. Na hiyo ndio ikawa moja ya sababu ya sisi
kuondoka humu ndani kwa haraka.” Grace aliongeza huku akilia.
“Basi, ndio Nanaa anatafuta chumba, ili
angalau awe na pakukimbilia. Vitu vyake aliviacha kwenye hicho chumba, huko
hosteli. Antii, yule matroni
aliyemuhudumia sana hospitalini, alivichukua ili amuhifadhie. Kwa kuwa
tuliondoka kama tunakimbizwa! Nanaa analia, anataka nimlete hapa kwa mwanae.
Hakuchukua vitu vyake, akaacha hivyo hivyo. Nafikiri alijua atarudi kwa
haraka. Sasa miezi miwili mingi, kukaa
na mizigo ya mtu! Si rahisi. Ndio amemtafuta anamtaka akachukue vitu vyake.
Sasa pakuviweka ndio shuguli.” Mama G akamalizia.
“Si angevileta hapa!?” Grace akauliza huku akifuta machozi.
“Sasa avilete hapa wakati mwenye nyumba ashamuonyesha hapa ni mpitaji?
Nilimuuliza hivyo hivyo. Akaniuliza swali gumu kweli yule mtoto, lililonifanya
nije kulia mwenyewe baadaye, na kumshukuru Mungu kwa uzima alionipa. Japokuwa
sikuwa na uwezo, lakini nikashuru Mungu alinipa uwezo wa kuwalea. Unajua Grace,
unaweza usione umuhimu wa uhai wako, lakini jilinganishe na Nanaa. Mtoto ambaye
hakuchagua kuzaliwa akiwa hana mama. Yule mtoto aliniambia maneno yananiuma
mpaka leo. Si unamjua Nanaa, alivyo na sauti ya upole? Akaniambia hiyo mizigo
yake ina vyeti vyake. Ambavyo kwake yeye ndio ndugu na kimbilio la pekee.
Akaniuliza itakuaje aje avilete hapa ndani, halafu Geb aje amfukuze tena?
Atavipataje tena? Akaniambia, ‘Mama,
acha niwe na kwangu, sehemu ya kukimbilia. Sina ndugu wala sina rafiki
wakunihifadhi, itakuaje nikija kutupwa tena nje?’ Nilishindwa chakujibu
ikabidi nimuache. Maana ni kweli nilimkuta hapo nje, asubuhi, amepiga magoti,
yule mtoto analia na kuomboleza afunguliwe mlango.”
“Nilikuwa nimelala, niliamka,
sikuamini! Ile picha inanitesa mpaka leo. Naamka usiku natubu kwa niaba ya Geb.
Namwambia Mungu amsamehe mwanangu, asimlaani. Naweza nikaamka nikajikuta
machozi yananitoka. Nasema labda ndio angekuwa Grace wangu, labda na mimi
ningekuwa nimekufa, wangemfanyia hivyo mwanangu! Kila siku usiku ile picha
inanijia Nanaa akilia na kuomboleza pale nje. Huu ni mwezi wa pili, kazi pia
imenishinda, nipo naye humu ndani namliwaza.” Grace alikuwa akilia kama mama
yake Nanaa.
“Lakini Grace, Mungu yupo. Yule mtoto
naona ana roho ya tofauti. Sijui kwa kuwa ameshapitia mengi! Amekubaliana na
yote, ametulia, na amependeza kweli kweli. Ukimuona hutaamini kama ni Nanaa
yule aliyekuwa amechoka. Si unajua ana ngozi nzuri? Basi amekuwa kama mtoto.
Nilikuwa namlisha mchana na usiku ili angalau arudishe mwili. Sasa naona na
uzazi umemkubali. Amependeza sana.”
“Lakini bado utamuhurumia. Asubuhi
mwenye mtoto akiondoka, anaingia kule chumbani kwa Geb, anaenda kumchukua mtoto
wake, analala amemkumbatia kama paka. Huwa nabaki kulia mwenyewe. Akisikia tu
gari ya Geb, hata kama yupo usingizini, ataruka kama swala. Anakimbia haraka
kumrudisha mtoto kitandani kwake, hapo baba yake anapotaka awekwe. Lakini
hajaacha ukarimu wake kwa Geb. Japokuwa nampikia vyakula vya uzazi, lakini
asubuhi lazima aamke asubuhi na mapema, anampikia Geb uji, na jioni
atahakikisha Geb anachakula ndio anarudi chumbani kwake.”
“Lakini mbona husimulii jinsi
alivyonitendea mimi Mama!? Mbona kama unanilaumu tu? Nanaa alinikimbia tena kwa
kunitukana!” Grace alinyanyuka kama simba. Akapiga teke meza ya kioo
iliyokuwepo mbele yake. “Wewe ni mbwa Geb. Mshenzi wa washezi. Unakimbiwa na
pesa, una uwezo wa kulala maporini kuzisaka pesa, mpaka unazipata, iweje leo
unashindwa kumtafuta Nanaa hapo Chuo Kikuu Mlimani? Tena baada ya kukufumania?”
“Usinitukane Grace. Nanaa alitukuta uchi, hakunifumania.” Geb akajaribu
kujitetea.
Grace alichukua kinyago cha kimasai
kilichokuwa kimepabwa pembeni ya makochi, kizito, akaenda kupiga meza ya kioo
yakulia chakula. “Pesa zimekufanya kuwa mnyama wewe
Geb. Kumbuka sisi tulipotoka. Kumbuka Mungu alipotutoa. Mavumbini, chini kabisa.
Kumbuka mateso tuliyopitia kabla hatujapata pesa.” Grace alivunja ile
meza, akahamia kwenye madirisha. “Leo unapata pesa
unamfukuza Nanaa? Unamuacha nje? Jeuri hiyo unapata wapi wewe?” Grace
alikuwa akivunja vitu huku akilia na kuongea.
“Mkeo atazaa leo.” Mama G, akamwambia
Danny. “Waache watoke. Mimi mwenyewe nimechoka kusubiri.” Danny akajibu. “Unafikiri watoto wanalelewa na maziwa ya kopo?” Grace
aliingia jikoni akatoka na yale makopo yote ya maziwa, akaanza kuyafungua na
kuyamwaga chini kwenye miguu ya Geb. Aliyamimina yote, mpaka akamaliza. “Mshenzi mkubwa wewe. Unafikiri watoto wanalelewa na
maziwa peke yake? Ingekuwa hivyo kila mwanamke sasa hivi ungemkuta ana mtoto.” Akaenda
kwenye friji akatoa maziwa yote aliyoyaacha Nanaa, baada ya kuyakamua, akaenda
kumwagia Geb mwilini mwake, akatupa nje zile chupa baada ya kuzipasua pasua.
“Wewe si mwanaume?
Mnyonyeshe sasa huyo mtoto leo. Mtoto anahitaji joto la mama, wewe unalala na
mtoto! Una joto gani wewe la kumkuza huyo mtoto? Unampangia Nanaa muda wakurudi
nyumbani halafu unakaa na mtoto wake? Unadai miezi 9 aliyokuwa na mtoto wako
tumboni kwake!? Hivi unajua unachoongea wewe au unaropoka tu? Unajua shida na
taabu mama anazopitia kwa hiyo miezi 9? Ungepewa wewe mimba na mwanaume
uliyemfumania, nina uhakika wewe ungeitoa hiyo mimba. Nakujua wewe Geb.
Usingevuka hata miezi 3 ile ya mwanzo. Hivi unajua shida ya kubeba mimba ya
mwanaume unayejua analala na mwanamke mwingine? Unajua shida yake wewe?
Ulimuacha nje kwenye harusi, na bado akakufuata hapa na kukuta na Liz. Ulitaka
akufanyaje? ” Grace akaanza
kuchana na makochi.
“Sasa hapo Danny mchukue mkeo. Tutakaa
wapi?” Mama G akashituka sana. “Mwache mke wangu aongee bwana! Anajua
anachoongea. Hapo ana usingizi wa siku kibao! Hawezi kulala chali, hawezi kulala
ubavu, havilaliki jinsi hao watoto huko tumboni wanavyomuendesha! Na Geb
analijua hilo. Umeshindwa kumuenzi mwanamke aliyekuzalia mtoto mzuri hivi!?”
Danny akauliza.
“Tena ngoja niwaambie nyinyi wote kama
hamumfahamu Geb. Halali na mwanamke kihasara. Liz alikuwa ananiambia, Geb
alikuwa anajua mzunguko wake wa hedhi wa mwezi. Yaani yeye mwenyewe Liz alikuwa
akisahau, anamuuliza Geb. Na mara zote Geb alikuwa akitumia kondomu na Liz, ila
zikiwa siku za hatari, hata hakuwa akitaka kumgusa Liz. Liz alikuwa akiniambia,
haamini hata kondomu huyo kwa jinsi alivyokuwa akiogapa mtoto na Liz. Mimba ya
Nanaa haikuwa ya bahati mbaya. Nina uhakika Geb alipanga mpaka na jinsia ya mtoto.
Geb anapenda sana watoto wa kike, na alikusudia kuzaa na Nanaa. Alimpa mimba
msichana wa watu kwa makusudi, halafu sasa hivi ndio anajiliza hapa, eti ‘Nanaa alinikimbia’! Tena ulijua
alikukimbia na mtoto wako tumboni kwa nini ulimuacha ateseke peke yake?” Grace
aliendelea kufanya fujo pale nyumbani kwa Geb.
“Tumeishi chumba kimoja sisi wote hapa
tena na marafiki zako. Muulize mama au rafiki zako kama kuna aliyewahi kuwekewa
sharti hata mmoja. Ubinadamu umekuisha kabisa sababu umepata kinyumba hiki!
Huna aibu, hukumbuki ulipotoka wewe?” Mtoto akaanza kulia. “Mnyonyeshe sasa.
Wewe si mwanaume? Mnyonyeshe na umbembeleze mpaka anyamaze leo.” Akamchukua
mtoto kutoka kwa mumewe, akamkabidhi Geb.
“Na mama, hakuna kumsaidia huyu, akome na ndio
ajue uthamani wa mama.” Mtoto aliendelea kulia. “Unashangaa nini? Si wewe
unajidai unagubu wewe. Huwezi kuongea jambo likaisha, unabeba visasi? Sasa
mbembeleze huyo leo mpaka anyamaze. Na hakuna wa kukusaidia.” “Jamani, ngoja
mimi nikaoge, nilale.” Mama G akasimama.
“Mama unaondoka?” Danny akauliza
akicheka. “Kumbe! Kazi yangu mimi ni Nanaa. Nanaa naye kachelewa kurudi,
kafungiwa geti. Huyo mtoto anashikwa na yeye mwenyewe tu. Mimi hataki nimshike
mwanae kwa kuwa kanikasirikia. Kama Nanaa anatoka humu ndani, basi ni heri aache
kazi, aje akae na mwanae. Hataki hata nitoke naye! Juzi nilimuomba nitoke naye
Liv, ili nikamnunulie mama yake nguo, akanikatalia bila aibu. Akaja kukaa na
mwanae mimi nikatoka na Nanaa. Sasa sina chakufanya hapa.” Mama G akaanza
kuondoka.
“Kamnunulie maziwa mengine ya kopo.”
Mama G alitoa ushauri wa kumsanifu, kisha akaondoka. “Naombeni twendeni Danny,
nisije nikaleta madhara makubwa zaidi bure.” Grace akamshika mwanae mkono bado
alikuwa na headphone masikioni. Alikuwa amezama kwenye game zake hakuwa hata
anajua kinachoendelea. Alimtoa pale kwenye kochi taratibu ili asikanyage vioo
alivyovunja mama yake.
“Na kazini kesho siendi. Nenda kafanye
kazi zako mwenyewe. Ukijidai kulala hapa na huyo mtoto wako, ujue kesho
unaingiza hasara ya mamilioni ya pesa.” Grace
akatoka na familia yake. Alimsikia akivunja meza nyingine ya kioo ya barazani.
“Hivi vitu ndio vinamtia wazimu huyu. Sijui nichome moto hii gari yake mpya?”
Geb alimsikia dada yake akiuliza. “Twende bwana Grace! Hasira zote hizo ni
usingizi tu wala sio Nanaa.” “Usiniudhi zaidi Danny! Unajua shida ya kubeba
mimba na kuzaa wewe? Tena maumivu yanazidi unapomzaa halafu upokonywe! Yule
binti yupo kwenye hali ngumu zaidi.” “Basi mama, twende.” Baada ya muda
akasikia gari ikitoka.
Nani Kama Mama!
Oliva alianza kulia kama amechapwa.
Aliongeza sauti na kulia kama kengele. Geb alimbembeleza huku anazunguka nyumba
nzima. Mwishowe Mama G akasikia wanatoka. Baada ya muda wakarudi huku mtoto
bado analia sana. Mama G, akatoka kwenda jikoni akijidai anataka kunywa maji
ili aone tu kinachoendelea. Akamkuta Geb amenunua maziwa mengine ya kopo na
chupa za maziwa. Akatengeneza yale maziwa, akayapima kama yana joto zuri. Mama
G akavuta kiti cha palepale jikoni akakaa huku anamwangalia. Akamfuta mtoto
wake machozi, akampa ile chupa.
Liv akapokea ile chuchu kwa haraka
sana. Alipoweka tu mdomoni, akatema na kuanza kulia upyaa. Mama G akaanza
kucheka. “Watu na mama zao! Hataki ujinga huyo mtoto. Unamdanganyishia unga wa
viwandani wakati maziwa ya mama yake yapo!” “Sasa Grace si kayamwaga.” “Basi
leo jasho litakutoka. Kama namuona sasa hivi Nanaa. Kalala kwenye kitanda
kisafi. Hakuna manyanyaso, hakuna ubabe wa usiku. Kwa raha zake!” Mama G
akaanza kucheka tena.
“Sasa ngoja apate bwana anayejua
kubembeleza, ampe mimba ya pili. Wee! Kama nakuona na mwanao huyo unayejidai
nae. Mtachina hapa. Na lile toto lilivyo zuri, tena sasa hivi ndio limezidi
kuiva, limenona! Akicheka na zile dimpozi utafikiri anakuita! Akiongea
utafikiri anakubembeleza! Sasa apate dume lenye upendo, likamkabidhi hata funguo
za chumba kimoja tu. Akamwambia Nanaa, hapa kwangu ndio kwako, kuwa huru.
Hutakaa ukamuona humu ndani. Atakuachia mtoto huyo, mbaki mnabembelezana mchana
na usiku.” Mama yake akazidi kumkera.
“Tena wanaume wenye akili walivyo,
wakimpata mtoto kama yule, hawamuachii mpaka wamzalishe mara mbili au tatu ndio
wanamuachia. Si umemuona Danny mwenzio? Anahangaika na Grace mpaka leo. Basi
unaona mwenzako mjingaa! Haya baba. Wewe si ulitaka mtoto ukadhani anachotaka
mtoto ni maziwa ya kopo tu? Sasa Nanaa kakuachia mwanao. Huyooo! Wewe mwanaume
wa shoka, hangaika naye leo. Ujue kazi ya mama ni nini.” Mama G, alimuacha hapo
jikoni akihangaika na mtoto wake.
Liv alikuwa kama ametumwa! Hakuweka
kituo, aliendelea kulia. Akarudi naye chumbani akamuwekea michezo yote kitandani,
lakini hakunyamaza. Akakumbuka hajambadilisha diaper. Akahisi ndio sababu.
Wakati anakwenda kwenye kabati ya mtoto, akakutana na pesa. Akafikiria kidogo,
akajua Nanaa ndio aliziweka pale. Akajua ni zile pesa zote alizokuwa akimuachia
Nanaa. Akasimama pale kwa muda akifikiria. Akashituliwa na sauti ya Liv akizidi
kulia. Akaenda kumbadilisha diaper akaamua ambadilishe na nguo, lakini
haikusaidia. Akamuweka kifuani kama alivyozoea zamani, lakini haikusaidia.
Akazima taa zote ili chumba kiwe giza kabisa labda mwanga wa taa ndio unamfanya
asilale, lakini haikusaidia. Liv alizidi kulia mpaka akapata joto. Yalishapita
masaa matatu mfululizo Liv akilia tu.
~~~~~~~~~~~~~~
Jeuri Ya Geb Itaishia Wapi? Baada Ya
Kumtenda Nanaa Kikatili, Hasira Ndio Zinamwisha Geb. Grace Amemjia Juu Na
Kumfungua Macho Pamoja Na Mama Yake. Liv Naye
Anamkumbusha Baba Yake Kuwa Yeye Hakuokotwa, Anaye Mama Yake. Nanaa Yupo
Kwenye Harakati Ya Kutafuta Kwake. Tena Safari Hii Akiwa Amehakikishiwa Pale Ni
Nyumbani Kwa Geb, Na Yupo Kulea Tu.
· Je
Nini Kitaendelea Kati Ya Wazazi Hao Waliobeba Jukumu La Oliva?
· Mahusiano
Ya Geb Na Grace Yatakuja Kupona?
· James
Hana Habari Kuwa Geb Amemzalisha Dada Yake. Mara Ya Mwisho Ilikuwa Ni Onyo Tu,
Lakumtaka Akae Naye Mbali. Leo Amemzalisha!
Nini Kitaendelea?
Usikose Muendelezo
0 Comments:
Post a Comment