Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Ni Wangu! - Sehemu Ya 30. - Naomi Simulizi

Ni Wangu! - Sehemu Ya 30.

Nanaa aliendelea kulia mpaka Mama G akaamka. Alidhani anaota, lakini ni kweli alikuwa Nanaa akilia nje. Akatoka. Akakuta milango imefungwa, Geb anazo funguo. Akaenda chumbani kwa Geb. “Nataka funguo za milango sasa hivi, Geb. Usinichezee akili.” Geb kimya. “Usiniletee kiburi na ukorofi kama baba yako. Nipe funguo.” “Huwezi kuniambia hivyo mama wakati wewe ulinificha juu ya mtoto wangu!” “Nisikilize Geb. Nimekuficha, ndiyo, na huna utakalo nifanya. Acha kuwa kama umechanganyikiwa! Huwezi wewe kunipangia nini chakufanya na nini nisifanye. Umenielewa Geb? Nipe funguo sasa hivi kabla hujajuta milele. Na kama unafikiri nakutania, usinipe funguo.” Mama G, alimbadilikia Geb, na yeye hakuamini.

“Unaniletea ujinga mimi!? Unafikiri watoto wanakuzwa na maziwa tu? Kama ndio hivyo si kila mwanaume ungemuona hana mke ana watoto tu! Kama unafikiri hizo pesa ndio kila kitu, mbona nilivyowazaa baba yenu asiwachukue akawalea nyinyi kwa maziwa ya kopo au ya ng’ombe kwa kuwa alikuwa mfugaji? Acha ujinga wako. Umenisikia Geb?” “Nanaa alikuwa anatoroka.” “Kinachomuweka hapa nini, nawakati wewe umekuwa kama mwehu? Hata mimi ningetoroka. Nipe hizo funguo haraka. Unamfungia mzazi nje? Hata damu ya uzazi haijakatika, unamfungia nje na baridi hii! Umechanganyikiwa wewe!? Huyo mtoto hata kitovu hakijakauka unataka kumtengenisha na mama yake! Umelaaniwa wewe? Haraka sana nipe funguo.” Geb akampa funguo mama yake.

“Ulipokuwa ukizunguka naye kwenye mahoteli, nakujiiba kuingia chumbani kwake usiku, unafurahia, hukuwa ukijua kutunza? Ulitaka kujiridhisha tu halafu umuache, utegemee akae anakulilia wewe?” “Nanaa mwenyewe ndio alinikataa mama, sio mimi.” “Kama wewe mwanaume kweli kwa nini hukwenda kumtafuta na kumbembeleza? Si alikuwa hapo chuo kikuu? Sasa hivi ndio unajidai kulalamika umefichwa! Umefichwa! Umefichwa nini wakati ulijidai wewe unakiburi? Wenzio tunajua kubembeleza ndio maana amesamehe.” Mama G alikuwa akiwaka kama moto. “Sasa nikusikie tena.” Mama G akamchimba mkwara. Geb akanyamaza akionyesha amekasirika sana.

 Akatoka pale chumbani kwa Geb kwa hasira kuelekea nje kwa Nanaa. Alifungua milango yote akamnyanyua Nanaa pale alipokuwa amekaa chini, aridhini akilia. “Njoo Nanaa mwanangu.” “Geb amenifukuza mama.” “Acha kusema uongo Nanaa. Sio wewe uliondoka humu ndani tena huku ukinitukana? Nilikubembeleza ubaki, ukasema unaondoka mimi ni ukurasa uliofunga! Leo unataka kuondoka tena na mwanangu, umpeleke kwa mabwana zako! Hujui kutulia sehemu moja Nanaa. Umezoea kuruka ruka, unataka ukaanze kuhangaika na mwangu!” Mama G akamwingiza ndani.

“Wewe ndio muongo. Uliniahidi nini tulipokuwa Morogoro? Uliniahidi utakuwa na mimi wakati wote.” “Sasa kwa nini uliondoka kama uliamini? Wewe uliniambia ungekuwa mlinzi wangu. Sijakuona ukilinda chochote zaidi ya kukimbia kimbia!” “Ulitaka nikulinde hata ukiwa na mpenzi wako?” “Nilikwambia Liz, ni msichana niliyekuwa naye zamani na hata yeye nilishamwambia basi! Tukaachana kwa ajili yako.” “Sasa mbona niliwafumania?” “Hujawahi kunifumania Nanaa, acha uongo. Mimi sio muhuni. Najiheshimu. Siwezi nikawa na lala na wewe huku na lala na Liz. Sina ujinga huo, naomba uniheshimu. Kama wewe unaweza kufanya hivyo ni wewe, acha kuniingiza kwenye huo uchafu.” Nanaa akashangaa sana.

“Unataka kukana nini wewe Geb wakati niliwakuta wote mpo uchi chumbani kwako?” “Leo ndio unauliza, wakati siku ile nilikubembeleza unisikilize ukakataa ukasema nitakudanganya kama wanaume wengine waliokudanganya! Sasa hata nikikwambia, kitakachokufanya uniamini leo ni nini? Kutukuta uchi ndio umenifumania? Tena unazidi kudanganya wakati nilikuomba usidanganye!” “Sasa hapa nimedanganya nini?” “Wewe siku ile umemkuta Liz yupo uchi kitandani kwangu, na mimi natoka bafuni kuoga. Sasa hapo ndio ulinifumania?” “Sasa je? Kwa hiyo ulitaka mpaka niwakute mkifanya mapenzi?” Mama G alitafuta mahali akaaa ili asikilize vizuri.

“Sasa nisikilize Nanaa. Wewe sio mtu wa kuaminika. Hujui kupenda wala hujui kutulia sehemu moja. Kitu ambacho sitaruhusu kitokee kwa mtoto wangu. Wewe hangaika na wanaume wote unaowataka hapa duniani. Fungua kila kurasa na kufunga. Hama kitanda kimoja mpaka kingine mpaka uje ufe kwa magonjwa. Lakini sio na huyu mtoto wangu. Umenielewa Nanaa? Nakupa nafasi ya mwisho. Nataka uchague wewe mwenyewe, tena ukijua wazi, huyu mtoto hapa ni kwao. Hatawahi kuishi kwenye nyumba za kupanga na wanaume zako. Hatakaa atoke humu ndani bila idhini yangu. Nilikufungulia mlango mpaka wa moyo wangu, ukaamua kunitesa na kuniacha nikiwa nakuhitaji. Nilikuwa silali nakuja hospitalini na nyumbani kwa Antii usiku kucha nipo na wewe nikikuuguza bila kulala. Japokuwa James alinifukuza lakini sikuacha kuwa na wewe Nanaa. Kama ningekuwa na Liz, kwa nini nilikufuata niwe na wewe wakati hukuwa hata unajua kama nipo?” Nanaa akanyamaza hakujua hata kama Geb alimuuguza. Akanywea kabisa.

“Umepona hata kunitafuta! Nimekuwa na kazi ya kukupigia kama mwehu! Unawasiliana na watu unaowataka wewe, mimi unanipuuza. Nimekuwa kama mwehu kwa ajili yako! Mara ya mwisho nimekupigia simu, ukanishutumu. Nilijaribu kukuelezea kila kitu na kukuomba msamaha wa kukusahau pale nje siku ya harusi. Usifikiri kukuacha nje ukumbini ni kitu nilichokifurahia Nanaa. Kiliniuma kuliko ambavyo ningefungua mdomo wangu kukueleza. Nilikwambia nina hamu na wewe, ukanikatia simu. Matokeo yake ukaja hapa, ukanisingizia na kuniacha huku ukinitusi na kunifananisha mimi na wanaume zako wengine. Sijakusamehe kwa hilo, kwa kuwa ulinidhalilisha sana. Mimi sina mchezo wa kuhama vitanda na wanawake tofauti tofauti, halafu nikajisifia. Naumia sana kuona naachana na mwanamke ambaye nilishamvulia nguo. Naumia sana Nanaa. Mimi sio kama wewe. Sijisifii kubadili wanawake. Inaniuma sana. Hasa wewe kwa kuwa nilikupenda kwa dhati, na nikakutanguliza kwenye kila kitu. Umenisaliti Nanaa. Na ninarudia tena, sijasamehe.” Mama G ndio alikuwa akisikia mambo mengine kwa mara ya kwanza. Akawa anasikiliza kwa makini.

 “Sasa, leo mbele ya mama. Nakupa nafasi ya mwisho, ili ukiharibu na mama awe shahidi yangu. Na pia ili usinikosanishe na mama yangu.” Nanaa alibaki akilia.“Unakubali kukaa hapa ili kulea mtoto wangu kwa masharti yangu au hutaweza kuishi hapa? Sitakusumbua na wanaume zako, ila ujue saa 12 jioni uwe umeingia humu ndani. Ikipika hata dakika moja hujapita pale getini, usirudi tena siku hiyo. Siku utakayorudia kutoka na mtoto bila idhini yangu, ndiyo siku yako ya mwisho kukanyaga humu ndani. Hutakaa urudi na ndio utakuwa mwisho wako na huyu mtoto. Nitakushitaki kwa kuzaa mtoto wangu na kumficha hosteli za chuo akiwa hana uangalizi mzuri. Na wala huna mahali pa kumuweka. Najua nitashinda kesi kwa kuwa huna hata uwezo wa kifedha wa kumlea huyu mtoto, wakati mimi nipo na nina uwezo.” Huo ulikuwa ukweli ulioanza kumuogopesha Nanaa.

 Geb akaendelea. “Haruhusiwi kuleta mwanaume yeyote humu ndani, isipokuwa James, kaka yako. Sasa je, unabaki humu ndani au unaondoka ukaendelee na maisha yako uliyokwisha kuzoea kuyaishi?” Kimya, Nanaa alisikika akilia kwa uchungu sana.  “Naomba tusipoteze muda Nanaa. Unaondoka au unabaki.” “Mimi sio malaya.” “Ulinimbia mwenyewe, tena kwa kujisifia. Sasa, unaondoka au unabaki?” Mama G, alikuwa kimya akiwasikiliza.

“Namtaka mtoto wangu Geb. Nipe nikamlee hata miaka mitano tu, ndio umchukue.” “Haitakaa ikatokea Nanaa. Kama kuna mwanaume ulimdanganya huyu ni mtoto wake, nashauri tafuta uongo kama uliokuwa ukinidanganya mimi, na yeye ukamdanganye. Nina uhakika atakuamini tu. Maana na mimi nilikuamini.” “Sijawahi kukudanganya Geb, na Mungu ni shahidi.” “Nanaa! Naomba tusirudie mambo. Mimi nikiongea sana, mdomo na kichwa vinaniuma. Nataka jibu la mwisho. Unabaki au unaondoka?” “Naomba kubaki.” Nanaa alijibu kwa upole huku akiendelea kulia. “Tafadhali zingatia masharti. Sitakusamehe endapo utavunja hata moja wapo.” Geb akarudi ndani chumbani kwake, akawaacha hapo sebuleni.

~~~~~~~~~~~~~~

“Mama, mimi sio muhuni na wala sijamdanganya Geb. Mungu wangu ni shahidi.” “Naomba utulie Nanaa. Umechagua jambo zuri, kubaki na kumlea mtoto wenu. Naomba akili zako zihamie kwa mtoto tu, hayo mambo mengine yaache kwanza. Lea mtoto wako. Ni bahati ambayo wanawake wengi wanatamani kuipata. Lakini wengine wanakufa hata kabla hawajanyonyesha watoto wao. Wengine wanashindwa uwezo, hamna mazingira mazuri ya kulea watoto wao. Na mambo mengine mengi najua wewe unajua. Maadamu Mungu amekupa nafasi hiyo, upo hai, unamaziwa, na afya njema, weka kila kitu pembeni, mlee mtoto wako tu. Umesikia mama?” Mama G akaenda kumnyanyua pale na kumuingiza chumbani.

Alikuwa amejaa michanga mwili mzima kwa kugaragara chini alipofungiwa nje na tayari alishakuwa amelowa damu. Akamchemshia maji ya moto, akaenda kumsaidia kuoga na kumkanda, akamrudisha kitandani. Akamfunika mashuka mengi na blangeti juu, akampa uji, akanywa, akarudi kulala.

~~~~~~~~~~~~~~

Aliamshwa na Geb. “Mchukue mtoto, naenda kununua vitanda.” Nanaa alikuwa amepooza. Geb alimpa maneno ya hukumu, akajuta siku ile kuondoka bila kumsikiliza Geb, aliyekuwa akimsihi atulie wazungumze. Hakuwa hata akijua kama Geb alikuwa akijiiba kukaa naye usiku wakati mgonjwa.  Alimpokea mtoto, Geb akatoka. Akakumbuka wosia wa Grace. Alimwambia asikubali hisia zake zimtawale. Alijuta. Akatamani kama angerudisha siku nyuma, abaki amsikilize Geb. Alijiona mjinga vile alivyoteseka na mimba ya mwanaume ambaye alitaka mtoto wake. Alikejeliwa na wanafunzi wenzake, bure tu. Akabaki akiwaza.

~~~~~~~~~~~~~~

Alirudi na kitanda kama kilekile alichokuwa akilalia mwanzoni, godoro jipya, mashuka mapya na kitanda cha mtoto wake kilichokamalika. Alitoa kile kitanda cha zamani, akaweka kipya. Na kitanda cha mtoto wake alikifunga pembeni ya kitanda chake, chumbani kwake. Akaingia chumbani kwa Nanaa, akamkuta amelala kitandani amemkumbatia mtoto wake. Akamchukua yule mtoto na kutoka naye.

Nanaa alianza kulia tena. Alilia kwa muda mpaka akasikia mlango unafunguliwa tena, Geb akarudi. “Sikuwa nimeenda kwa mwanaume mwingine, Geb! Naomba usiniadhibu bila kosa.” “Nimebadili kitanda kizima. Kila kitu ni kipya. Nimemnunulia Liv kitanda chake. Kipo pembeni ya kitanda kikubwa, chumbani kwangu. Na hii ni monitor yake akiwa amelala, unaweza kumuacha kwenye kitanda chake, wewe ukaenda popote ndani ya hii nyumba ukiwa na hii monitor, akiamka utamsikia. Kama utataka kulala pembeni yake, unakaribishwa kulala kwenye kitanda ambacho sijalalia na wanawake zangu.” “Kwa nini tumlaze mtoto peke yake Geb? Naomba nilale na mwanangu!” “Huyu mtoto atakuwa mkubwa zaidi ya hivi alivyo sasa, na si muda wote atakapotaka kulala na wewe utakuwa unataka kulala. Huwezi kumuacha kwenye kitanda peke yake, ataanguka. Ndio maana nimemnunulia kitanda chake ili aanze kuzoea kulala peke yake.” “Kwa hiyo kwa sasa naruhusiwa kulala naye?” “Sasa hivi nitakuwa naye. Ukitaka kumnyonyesha, unaruhusiwa kuja kumnyonyesha na kumuacha kwangu. Kila siku usiku nitakuwa nalala naye mimi, mchana namlaza kwenye kitanda chake.” “Yaani mimi siruhusiwi kulala na huyo mtoto?” Nanaa aliuliza huku akilia. Geb akatoka.

Baada ya muda mfupi Mama G akaingia. “Unalia nini tena?” “Geb amenipokonya mtoto mama.” Nanaa akamuelezea kila kitu. Mama G, akacheka. “Wala usilie. Yatamshinda tu.” “Hawezi mama. Jana usiku kuchwa alikaa pale kwenye kochi amemkumbatia mwanae.” “Wewe tulia wala usilie. Fuata kila kitu anachotaka, mpaka mtoto wako achangamke, akufahamu wewe vizuri. Jifunze kucheza na kucheka na mwanao. Mfanyie vitu ambavyo ni wewe tu unaweza kumfanyia. Akishakuelewa wewe, nitakufundisha kitu kingine. Sasa hivi jifanye mjinga, fuata kila anachokwambia. Mimi namjua Geb akiwa amekasirika. Huwa najua ni wapi pakumbania. Wewe tulia kabisa. Achana na tabia za kulialia. Akikuita umnyonyeshe mtoto, wewe nenda tena ukiwa umetulia.” “Kaniletea kimashine hiki hapa! Eti mtoto akiamka nitamsikia. Inamaana anachojaribu kuniambia hatakuwa akiniita, nikimsikia mtoto ameamka niende mimi mwenyewe.” Mama G alicheka akatingisha kichwa.

~~~~~~~~~~~~~~

Mama G akamtuliza akatulia. “Kwani siku hizi hafanyi kazi tena huko BOT?” “Aliacha kazi. Siku hizi anafanya biashara tu. Kanunua jengo moja la gorofa hapo Ubungo, kalitengeneza vizuri. Ofisi zote kahamishia kwenye hilo jengo. Hata ofisi ya Grace ipo hapohapo. Chini ametengeneza maduka, juu ndio zipo ofisi zao. Kila duka la hapo chini linamwingizia pesa nzuri tu. Ana sehemu amejaza mashine ya kutolea kopi, anauza vitabu na mambo kama hayo ya Stationary.  Upande mwingine ameweka duka la jumla la vinywaji. Siku hizi anasambaza vinywaji karibia mji mzima huu wa Dar. Upande mwingine anauza mazao kwa jumla na rejareja. Kama lile duka langu, lakini yeye ameongeza mafuta. Anakusanya mafuta ya kila namna kutoka vijijini, anakuja kuyaweka kwenye madumu ya kila ujazo, kisha anauza. Kuanzia mafuta ya mawese, alizeti, mzeituni, na mengineyo. Ana mashamba ya asali huko Tabora. Kwa hiyo anauza ile asali nzuri. Watu wengi wanapenda asali yake, wanasema ni nzuri hachanganyi na vitu vingine. Ndio na huo Mchele, mahindi, na maharage pia anauza.” “Na ile ofisi ya Grace kule kwa zamani?” Nanaa aliendelea kuhoji.

“Si unajua pale walikuwa wanakodi?” “Sikujua!” “Pale walikuwa wanakodisha kutoka kwenye kampuni ya muhindi mmoja hivi. Wamepaachia. Akahamishia hiyo ofisi kwenye hilo jengo hapo Ubungo. Tena aliamua kununua godauni huko Buguruni, naona huko ndiko wanakohifadhia mazao na dada yake. Pakubwa sana. Ndiko wanakoweka mali zao zote. Naona mambo yao sio mabaya. Grace anapesa kweli siku hizi. Na siku hizi Geb hasafiri sana kama zamani. Amefungua ofisi huko mikoani, ameweka wafanyakazi wanao msaidia kumkusanyia mazao na kumtumia huku. Kila mkoa ambapo anapata mazao mengi, amefungua ofisi.” Nanaa akanyamaza.

~~~~~~~~~~~~~~

          “Wewe usiwe na wasiwasi hata kidogo. Ni hasira tu za kumuacha. Hana lolote!” “Sikumuacha mama. Siku nilipokuja kumwambia ni mjamzito, ndio siku nilimkuta chumbani na Liz, tena wote wako uchi. Nilishituka sana mama yangu. Nahisi sijui ni hasira, sikutaka hata kumsikiliza, nikaondoka. Matukio kama hayo yameshanitokea mara nyingi sana kwenye maisha yangu. Sijawahi kubahatika kupata mwanaume mwaminifu.” Nanaa akafikiria kidogo.

“Unajua siku ile ya harusi mliponiacha pale nje, nilimuona Geb na Liz wakiingia pamoja huku wameshikana mikono! Geb aliniahidi wakati nipo saluni kuwa japokuwa atasimamia harusi, lakini atakuwa akija tukae wote. Nilikaa pale nje zaidi ya masaa 4, mama! Hakuna hata aliyetoka kunitafuta! Zaidi Geb aliyejua nipo pale kwa ajili yake! Nikajua ni kwa sababu yupo na Liz. Kuja tena kumkuta tena yupo uchi na Liz, nikajua ni yaleyale. Sikutaka kudanganywa tena mama. Nikaamua niondoke tu. Hata hivyo nilijiona mimi ndiye niliyeingilia mapenzi yao. Nilianza mahusiano na Geb, mimi nikiwa sababu ya kuvunjika hayo mahusiano yao. Nikajua waliamua kusameheana, ili waendelee na mapenzi yao.” Mam G akashangaa kidogo.

“Ngoja kwanza Nanaa. Wewe unahusika vipi kwa kuvunjika kwa mahusiano yao?” “Moja ya masharti ambayo Liz alimpa Geb, ili waendelee kuwa wapenzi, ni kunitoa mimi hapa ndani. Ndio Geb akamwambia hatanifukuza mimi humu ndani kama ulivyomsikia Danny akisimulia siku ile asubuhi ya harusi ya Malii, pale jikoni. Hilo ndilo lilikuwa sharti mojawapo na mengine.” “Yapi?” Nanaa akasita kumwambia Mama G. Akaona anyamaze tu.

“Naomba nisikwambie mama yangu. Tuyaache tu. Lakini Geb aliniambia kuwa alipomkatalia ndio akasema basi, hawezi kuendelea tena na Geb. Yeye hawezi kuishi kwenye nyumba yenye watu wengi.” “Yule msichana ni mwehu tu. Hata hivyo nisingekubali aolewe na Geb.” “Mama wewe!” “Nakuhakikishia. Geb asingethubu kumuoa. Niliwaacha tu nikijua ni mambo ya muda. Unafikiri ingekuwa kuolewa si angeshaolewa muda mrefu sana? Huyo Geb anasubiri nini sasa hivi asiyeoa tukapumzika? Au mabinti wa watu nao wakapumzika? Anatongozwa mchana na usiku mpaka unawahurumia hao wanawake! Huyo Liz nilimuona sio mke wa kuwekwa ndani. Hafanani na maisha yetu hata kidogo.” Nanaa akamwangalia asiamini.

“Sasa Geb angemng’ang’ania amuoe?” “Nakwambia asingemuoa. Au kwa kuwa unaniona nipo kimya? Naangalia kila kitu. Kinachotokea ni kwa kuwa nakiruhusu. Geb na Grace hawawezi kufanya chochote bila kuniambia. Wananiambia kila kitu, na hawawezi kufanya jambo mpaka waone nimewapa baraka zangu. Kwa hilo namshukuru Mungu nimepata watoto wanao nisikiliza. Kwanza ujue mimi huyo Liz sijawahi kumuona tena humu ndani tokea siku ile alipokuja akataka kuingia chumbani kwa Geb, Geb akamkatalia?”  “Kweli mama!?” Nanaa hakuamini.

“Kweli tena. Tangia siku ile, sijamuona Liz humu ndani. Na wala sijamsikia Geb akimtaja. Geb hanifichi kitu. Mimi ndio msiri wa Geb. Na pia sikutaka akuchezee wakati nilijua yupo Liz. Ikabidi kumuhoji mapema. Ndio akanihakikishia aliachana na Liz kabisa na hata iweje hatamrudia tena. Na mimi namjua Geb, anamsimamo sana. Hawezi kujipinga na si muhuni hata kidogo. Kama ingekuwa wamerudiana, angeshaniambia. Kuna kilichotokea tu siku hiyo na Liz. Mwache kwanza.” Nanaa akabaki akiwaza.  Mama G, akacheka.

~~~~~~~~~~~~~~

“Unacheka nini?” “Geb ananikumbusha sana baba yake. Mzee alikuwa mkorofi yule! Hujawahi kuona. Halafu mkali kama pilipili. Geb amerithi kila kitu kutoka kwa baba yake, kasoro ukimya. Ukimya wao hawa wawili,  yeye na dada yake, umezidi. Baba yao alikuwa akiweza kugomba haswa mpaka nyumba ikatikisika sio kama Geb anayekasirika kimya kimya. Lakini tabia hizo za hasira za Geb, ni kama baba yake. Hivyo hivyo. Kabla yakunifanya kuwa wake, alinijaribu sana.” Mama G akacheka tena huku anavuta hisia.

“Hakika alinijaribu yule Mzee! Isingekuwa kuwa mkorofi, na nina msimamo, nisingefanikiwa.” Nanaa akajiweka sawa huku akicheka. “Acha umbea wewe mtoto!” “Bwana nisimulie.” “Na usicheke.” “Kidogo tu mama.” Mamaa G, akaanza kucheka tena. “Ona. Wewe mwenyewe yanakuchekesha!” “Yaani nakaaga mwenyewe najiuliza hivi akili zangu Mungu aliziumbaje!? Huwa sielewi. Nilifanya kituko cha mwaka. Mimi mwenyewe nilikuwa najishangaa.” “Ilikuwaje?” Nanaa akahoji kwa shauku zaidi.

Historia ya Mama G.

“Mimi hivi unavyoniona, sijui kabila langu wala sijui wazazi wangu. Nasikia tulizaliwa mapacha. Mwenzangu alikuwa wakiume. Unapajua Peramiho, ipo Songea?” “Nimeshawahi kupasikia.” “Basi hapo Misheni ndipo tulipoenda kutupwa mimi na mwenzangu wa kiume. Aliyetutupa hatumjui. Wanavyosema, itakuwa tuliachwa hapo usiku, padre aliyekuwa ameenda kufungua kanisa, akatukuta hapo. Kwa kifupi mwenzangu alifariki masaa machache tu tulipofika hospitalini, mimi nikaishi. Ndio chanzo huyo padre kunipa jina la Oliva. Kama vile Olive tree. Unajua asili ya miti ya mizaituni inastawi vizuri kwenye udongo usio na rutuba. Ukiweka kwenye udongo wa rutuba, haitengenezi mafuta mazuri. Sasa kaka yangu alikufa sababu ya mazingira yale mabaya, lakini wanasema wakanikuta mimi nipo nacheka.” Nanaa akacheka.

“Nikarudishwa pale kituoni nikaanza kulelewa. Unaambiwa nikawa kama mtoto wa kila mtu. Unibebe, uniweke chini, mimi nipo sawa tu. Siumwi wala silii. Chakula chochote kile mimi nakula. Nikawa napenda vile vitu vya hatari zaidi. Ukiniambia nisishike moto ni hatari, basi ndio kama umenituma! Nikaendelea hivyo mpaka nimekuwa. Mkorofi kweli kweli. Masista na padre  wote walikuwa wakinijua Oliva. Nikaanza shule. Lakini nikajikuta sipendi sana shule. Nikamaliza darasa la 7 kwa shida sana. Tena kwakusukumana na masista. Wakataka kuniingiza kusomea usista, nikawaambia mimi nataka mwanaume.” Nanaa akacheka sana.

“Usicheke. Tena nilikuwa nikiwaambia bila woga. Nikakataa kwenda sekondari. Wakanilazimisha kwa kuwa nilikuwa nimefaulu vizuri, nikachaguliwa kwenda Kilakala Sekondari. Wao wakaamua kunihamishia Songea girls ili niwe karibu nao. Nikasoma mwaka wa kwanza, wa pili mwishoni nikatoroka nikaamua kuhamia Dar. Hapo napasikia tu. Simjui mtu yeyote yule. Nikawa nasikia sifa zake kuwa jiji la Dar ni zuri sana, ila maisha ni magumu. Nikasema napataka hapohapo. Shule zikafungwa, badala ya kurudi kwa masista nikaamua kutorokea Dar.” “Mama wewe! Sasa shule?” “Nimekwambia mimi shule nilikuwa sipendi. Sio kwamba nilikuwa mjinga, lakini sikupenda tu kukaa darasani.” Nanaa alikumbuka aliambiwa na Geb mama yao ni mkorofi. Akaanza kumwangalia mara mbili mbili huku akicheka.

“Bahati yangu ilivyokuwa nzuri, wakati nipo njiani kuja huku jijini nikakaa na kijana mmoja hivi. Alijitambulisha kwa jina la Chalii. Lafudhi ilikuwa ya kichaga kabisaa. Kama kawaida yangu nikaanza kumchokoza kwa kuwa nilijua amenipenda. Hapo binti mdogo, umbile kama vile unavyomuona Grace. Akachanganyikiwa kweli kweli. Akaanza kujisifia alivyo na pesa na nikimkubali atanitunza. Basi nikamwambia akitaka nimkubali, anitafutie kazi. Akasema dada yake na mumewe wana shamba kubwa sana nje kidogo ya jiji la Dar, Kibaha. Wana kituo cha maziwa hapo hapo Kibaha, atanitafutia kazi hapo. Basi nikamuahidi kama akinitafutia kazi na sehemu ya kuishi, ningefanya naye mapenzi. Ahadi hiyo nampa usiku, tupo njiani. Tunakuja Dar. Wakati huo mabasi yanasafiri usiku. Kuja kupambazuka aliponitizama vizuri, akazidi kuchanganyikiwa. Basi akawa kama kapagawa. Akaninulia vyakula njiani huku anajigamba kweli kweli. Mimi nimetulia tu namsikiliza.” Nanaa akabaki anatingisha kichwa.

“Tukashukia Kibaha, akanitafutia chumba kwenye nyumba za kulala wageni. Eti na yeye akataka tulale naye.” Mama G akaanza kucheka. “Ulifanyaje mama wewe!” “Nilimuadabisha! Hakika hatasahau. Nikamwambia makubaliano ni anitafutie kazi kwanza na mahali pakuishi ndio nitampa mapenzi. Basi akaondoka pale chumbani na maumivu. Kesho yake akaja kunifuata akaniambia natakiwa kwenda kwenye usahili wa kazi. Basi, ilikuwa asubuhi tu. Nikatoka naye. Kwanza sikuamini kama atarudi jinsi nilivyomfanyia usiku uliopita.” “Kwani ulimfanyaje?” Nanaa akazidi kudadisi.

“Mbea huyu!” “Bwana niambie mama!” “Nilimpiga teke la nguvu huku chini. Alilala chini kama dakika 5, anaugulia maumivu.” “Mama wewe!” Nanaa akaanza kucheka. “Kumbe! Makubaliano yetu ilikuwa anitafutie kazi na sehemu yakuishi. Sasa leo iweje atake kuvunja makubaliano? Nikampiga nakumfukuza.” Nanaa akazidi kucheka.

“Ehe?” Baada yakutulia Nanaa akataka aendelee. “Basi, akanipeleka mpaka kwa Mzee Magesa.” “Baba yake Geb!?” Nanaa akauliza na mshangao kidogo. “Ndiyo! Yaani ile kumuona tu yule Mzee, nikajiambia lazima yule ndio aje awe mwanaume wangu wa kwanza.” Nanaa akaficha uso. “Sasa ulimpendea nini?” Nanaa akauliza kwa aibu. “He was tough. In every way. He was tough and very handsome. Yaani kwa kumwangalia tu, unaona vile mwanaume yule alivyokuwa amesimama na nguvu kama dume kwelikweli. Macho yake ndio yalinimaliza kabisa! Tena nilimkuta anagombesha wafanyakazi wake. Chalii akanitambulisha, akamwambia anipeleke ofisini kwake, nikamsubirie huko. Nikaenda, nikakaa. Baada ya muda akaja. Akawa anafanya mambo yake hapo kwenye meza yake huku mimi namwangalia. Akaandika wee, huku amekunja uso.” Mama G akacheka.

“Yaani yule mzee hakuwahi kunisahau. Unajua wakati anaandika na mimi nikamwambia naomba kalamu na karatasi. Akanyanyua uso kunitazama. Nikarudia, ‘Naomba kalamu na karatasi nataka kuandika kitu.’ Yule mzee akanipa. Nikaanza kuandika.  Nikaandika huku nasema, ‘Chai nzito au maziwa ya cocoa, maji ya kunywa, juisi, nyama za kukaanga pamoja na kitafunio kizuri. Mboga za majani.’ Yule Mzee akaacha kuandika alichokuwa akiandika, akabaki akiniangalia, maana nilikuwa naongea kwa sauti.” “Ni nini sasa?” “Yule Mzee naye akaniuliza hivyo hivyo.” Mama G akaanza kucheka.

Kisha akaendelea. “Nikamwambia naandika vitu ambavyo kama mimi ningekuwa mkewe, ningehakikisha unavipata asubuhi kabla hujaja kazini. Nikaandika tena chini huku akinitizama. ‘Kufanya akili zake zitulie, ili ajifikirie yeye mwenyewe.’ Kisha nikamaliza.” “Mama wewe!” Nanaa akatoa macho kwa mshangao.

“Ujue yule Mzee alibaki kama hivyo wewe unavyo niangalia! Ni kamwambia tena. ‘Lakini hiki cha mwisho kinaweza kuwa cha kwanza. Ukijifikiria wewe mwenyewe, utajaribu kutafuta mazingira ya kula vizuri, kulala vizuri, kunywa maji ya kutosha, halafu utajithamini wewe kuliko pesa. Kwa kuwa pesa hainunui uhai. Kwa hiyo nitahakikisha unaondoka nyumbani ukiwa umetulia. Ili ukija huku kazini ukikutana na watu wajinga kama hawa wafanyakazi wako, hujimalizi mwenyewe kwa kukasirika. Kwa kuwa kila ukikasirika, unapunguza muda wa kuishi hapa duniani. Halafu unagombesha watu ambao hawastahili.’ Nikamaliza nikabaki nikimwangalia.” “Jamani mama wewe!” “Ujue yule Mzee alikaa kama dakika tano ananiangalia hanimalizi. Nikamsogezea kile kikaratasi.” Nanaa alikuwa haamini.

“Akasemaje?” “Akaniuliza jina langu nani. Nikamwambia Oliva. Akaniuliza jina kamili. Nikamwambia bado ndio najaribu kulitengeneza. Yule baba alibaki hanielewi. Akaniuliza, ‘Unatengeneza jina lako?’ Nikamwambia, ‘ndiyo’. Akabaki ananiangalia. Akaniuliza shule ulikuwa ukitumia jina la nani? Nikajibu kwa kifupi tu ‘la Padri’. Yule baba alizidi kutonielewa. ‘Una miaka mingapi?’ Akauliza tena. Nikamwambia andika mwaka wowote lakini uishie na 1, au 3, au 5 au 7. Akaniuliza kwa nini hizo namba. Nikamjibu huwa sio rahisi kugawanyika. Ni ngumu, na hazigawanyiki kwa mbili. Yule Mzee akabaki ananitizama.” “Jamani wewe mama ni mkorofi!” “Sana. Sijajipatia mwenzangu. Hivi nashukuru nilikutana na Yesu. Lasivyo!” Wakacheka.

“Akaniuliza tena. ‘Kwani una miaka mingapi?’ Nikaanza kufikiria. Akaniuliza kwa hiyo hata umri wako hujui? Nikamwambia kuna umri walinipa, lakini siamini. Nahisi walinipunja. Akaniuliza unataka uwe na miaka mingapi? Haraka sana nikamjibu 19. Akacheka na kutingisha kichwa. Akauliza tena, ‘unasoma Oliva?’ Halafu akajijibu yeye nwenyewe baada ya mimi kubaki nikimwangalia. Akasema ‘ndio maana unatafuta kazi kwa kuwa husomi’. Nikamjibu, ‘Exacalty!’ Akazidi kutingisha kichwa. Akaniambia ‘wewe ni mtoto mdogo sana, kwa nini haupo shuleni unatafuta kazi?’ Nikamwambia sipendi kukaa darasani. Naona nitafanya vizuri kazini kuliko darasani. Yaani nikifanya kitu kinachoniingizia pesa ndio naweza kufanya vizuri kuliko kukaa darasani. Akabaki akinitizama kwa muda. Akauliza tena, ‘wazazi wako wako wapi?’ Nikamjibu kwa kifupi tu ‘sijui.’ Akabaki ananiangalia.” “Sasa ulikuwa huogopi?” “Mimi sio muoga Nanaa. Labda mtu aumwe, lakini sio vinginevyo.” Nanaa alitingisha kichwa.

“Kufupisha stori, yule baba akaniajiri, Chalii akanipangishia chumba. Nikaanza maisha. Eti akaja Chalii anadai haki yake. Acha nimbadilikie kama simjui. Hapo nilishamzungusha mpaka basi. Ashanitambulisha kwa mkewe Magesa ambaye ni dada yake sasa. Anajisifia kwa watu eti mimi mkewe. Nikawa namsikiliza tu. Pale kazini nikawa nachapa kazi mpaka Mzee Magesa mwenyewe hakuwa akiamini kama sijasoma. Kazi zikawa zinaenda, ukali akapunguza. Lakini hapo nikawa namchunguza. Nikamjua kila kitu juu ya maisha yake.” Mama G akaendelea.

“Wakati akili zangu zimezama kwa Magesa na kazi zake, Chalii naye akawa ananisumbua. Nikampiga marufuku aache kunifuatilia. Eti akataka kujiua kwa ajili yangu. Eti nimemsaliti. Usiku huo nyumbani kwa dada yake, yaani nyumbani kwa Mzee Magesa eti akajidai amekunywa sumu juu yangu. Akaacha na ujumbe. Akapelekwa hospitalini wakagundua sijui amekunywa dawa mbili, sijui tatu! Dada yake akanifuata asubuhi pale kazini mbele ya mumewe eti kwa nini nimemsaliti mdogo wake! Nikamwambia, ‘Kwanza, usiniletee habari za mtaani kazini kwangu. Pili sikujui na wewe hunijui. Kama ungenijua hata kidogo, ungetambua kuwa mimi sio mwanamke ninayeweza kuwa na mtu kama mdogo wako.’ Akauliza kwa nini. Nikamwambia ‘He is weak.’ Ujue Mzee Magesa hakuamini.  Akaondoka yule baba, mkewe akamfuata nyuma. Nikaendelea kufanya kazi zangu.” “Mama!” Mama G, akacheka.

“Sikuishia hapo. Yule mama alivyoondoka tu nikamfuata mumewe. Nikamuuliza mbona wewe hujaniuliza kama mkeo? Mzee Magesa aliishia kuniita jina langu, ‘Oliva!’ Nikamwambia wewe niulize tu. Akanitizama, kisha akaniuliza, ‘Kwa nini umemsaliti Chalii.’ Nikamsimulia mwanzo wetu mpaka mwisho na nikamwambia nilikuwa namdanganya ili anipe kazi. Kwa hiyo sijamsaliti ila nimemdanganya.’ Yule Mzee alitingisha kichwa. Akauliza tena, ‘Sasa kwa nini unakataa hata wanaume wenye uwezo? Ujue Chalii ni mfanyabiashara mkubwa tu. Anamaduka pale Kibaha kituo cha mabasi.’ Nikamw..” “Kwani kuna wengine walikuwa wakikutongoza?” “Nilikuwa gumzo. Vijana kwa wazee walikuwa wananifuata pale kazini. Wapi useme Oliva usisimuliwe umbo langu! Ilikuwa si mchezo. Oliva nilikuwa natingisha kweli kweli.” Nanaa akacheka sana.

“Sasa ukamjibu nini wakati ulimfuata mwenyewe?” “Nikafungua kijitabu changu, nikaanza kumsomea. Nikamwambia, ‘Nina mpenda mwanaume mmoja tu. Lakini, 1. Ni mume wa mtu. 2. Ana watoto wanao lingana na mimi. 3. Ni mcha Mungu sana na ni Mzee wakanisa. Nimeambiwa kuwa hajawahi kumsaliti mkewe. Japo mkewe sio mtu wa mapenzi, anajua kusaka pesa tu. 4. Hata yeye mwenyewe sio mtu wa mambo ya mapenzi, nasikia anapenda sana pesa. 5. Kwa asili hana tamaa ya wanawake. Hata wanawake wakimtongoza, huwa hakubali.’ Yule baba alibaki akinitizama. Nikamwambia, ‘huo ndio uchunguzi nilioufanya juu ya huyo mwanaume ninayempenda mimi na ndiye atakuwa baba wa watoto wangu. Wawili.’ Yule baba alinitizama, akanyanyuka na kuondoka. Hakurudi siku ile. Siku inayofuata, mkewe akaja na kunifukuza kazi.” “Mama!” Nanaa akashangaa.

“Kabisa! Nikamwambia nipe pesa yangu niondoke. Sikutaka hata kujua sababu. Ile nimetoka tu, nikasimamishwa na baba mmoja, alikuwa mteja wa hapo. Na yeye anachukua maziwa hapo kwa Magesa kwa bei ya jumla anayauza kwa kuyasambaza maeneo ya Kibamba mpaka Ubungo. Alikuwa na magari yakusambazia. Basi akaniambia nipande kwenye gari yake. Nikapanda bila woga. Akanitongoza. Nikamwambia simpendi lakini nataka anisaidie. Anipe pesa nianze biashara. Kama utani, yule baba akanipa pesa, akanishusha kwangu.” Mama G akaendelea.

“Sikuamini. Alinipa pesa yote bila shida. Nikatafuta sehemu, nikafungua duka la kuuza ‘yogurt.’ Nikawa nanunua maziwa kwa Magesa, nakuja kutengeneza ‘yogurt’, kisha nauza. Nikaajiri vijana wawili. Ndani ya miezi 6, kitu kimechanganya. Nikaongeza vijana wengine wawili ambao wakawa wananiuzia kwenye kituo cha mabasi pale standi. Pesa ikaanza kuwa nyingi. Nikabuni njia nyingine ya kufunga hizo yogurt kwenye vilailoni kama ice cream. Nikawa nauza kweli. Nikahama Kibaha sababu ya usumbufu wa wanaume, nikahamia Kibamba. Nikakodi kinyumba kidogo. Nikaanza maisha. Hapo hata sijatimiza miaka 20.” “Mama una akili!” “Sana.” Nanaa akacheka kwa sauti.

“Nakumbuka ni kama mwaka ukawa umepita, tokea niache kazi kwa Magesa na mkewe. Siku hiyo ya jumamosi sikwenda kazini, nilikuwa sijisikii vizuri. Niliamka sijisikii vizuri, nikarudi kulala ili kuona kama nitajisikia vizuri hapo nikiamka tena ili niende kazini. Nikaamka mchana mchovu zaidi na homa ipo juu. Nikawapigia simu wafanyakazi wangu kuwa sitakwenda hata jioni kwa kuwa nina homa. Ukifika muda wakufunga, wafunge tu mmoja aniletee funguo na mahesabu. Ilikuwa mchana. Nikarudi kulala tena.”

“Ilipofika jioni nikaamshwa na mtu anagonga. Nikajua nikijana wa dukani analeta funguo. Nikaamka kichwa kinauma kweli, nikafungua mlango. Ana kwa ana na Magesa. Nilisimama pale mlangoni nikimwangalia. Akaniambia, ‘naomba kuingia ndani’. Nikamwambia, ‘nimebadili mawazo, naomba uondoke’. Akaniambia ‘acha ukorofi Oli, nipishe mlangoni niingie.’ Nikajikuta naanza kulia. Sikuwa nimelia sijui zaidi ya miaka hata mitano. Nikalia wee, nikampisha. Akanishika mkono akanivutia ndani. ‘Una homa kali Oli. Umekunywa dawa?’ Nikanyamaza. ‘Oli?’ Nikanyamza.” “Alikuwa anakuita Oli?” Nanaa akauliza.

Mama G akacheka kama anayekumbuka mbali. “Yeye ndio alikuwa akiniita Oli. Na ungependa kumsikia akiniita.” Nanaa akazidi kucheka. “Basi, nikaendelea kulia nikamwambia, ‘ulinifukuza kazi. Umeniacha peke yangu kwa mwaka mzima! Sikutaki tena. Naomba uondoke.’ Akaniambia, ‘Sijawahi kukuacha hata siku moja. Njovu ni kijana wangu. Umemuajiri lakini ni kijana wangu na ninakufuatilia kila kitu. Leo ameniambia unaumwa ndio maana nimekuja kwa haraka. Leo sio siku niliyotaka kuja.’ Akajaribu kunituliza. ‘Sasa lini ulitaka kuja?’ Nikamuuliza. ‘Hivi unajua nina mke na watoto, Oli? Nina maisha niliyojenga kwa muda mrefu sana. Sidhani kama ulitegemea ni kurupuke tu, na wewe bado mdogo na ni binti mzuri unayetakwa na kila mtu! Ilibidi kukuchunguza Oli.’ ‘Kwa hiyo umeonaje sasa?’ Nikamuuliza. ‘Si ndio maana nipo hapa?’ Akanijibu.” Mama G, akatulia.

‘Umekunywa dawa?’ Akaniuliza tena. Nikamjibu sijanywa dawa na wala sijala. Nikamwambia huwa siumwi. Kwa ufupi ndio ilikuwa mara yangu ya kwanza kuugua. Nikashangaa akanichukua akanipeleka hospitalini. Nikakutwa na UTI. Nikapewa dawa, akanirudisha nyumbani. Akahakikisha nimekula na kunywa dawa, ndipo akaondoka. Hakuna usiku niliolala vizuri kama huo. Nilifurahi sana. Kesho yake asubuhi siku ya jumapili alipotoka kanisani akaja tena. Akaniletea chakula. Nakumbuka alikaa na mimi mpaka usiku ndipo akaondoka. Jumatatu nilirudi kazini nikiwa na nafuu, akaja, akaniletea chakula na kuniambia nijiandae, siku ya jumamosi tunasafiri mimi na yeye tu. Akaniambia nimuachie Njovu maelekezo mazuri yakutosha kwa kipindi ambacho sitakuwepo. Basi.” Uso wa mama G ukajawa furaha mpaka Nanaa akamuona nakucheka.

“Basi, siku ya jumamosi asubuhi akanipitia nyumbani mpaka uwanja wa ndege. Ndio ilikuwa mara yangu ya kwanza kupanda ndege. Tukaenda Arusha. Tulikaa huko hotelini kwa juma zima. Hakuna kutoka, ni mimi na yeye tu. Sijawahi kupata wakati mzuri hivyo maishani. Japo aliniudhi, lakini nilifurahia sana.” Nanaa akacheka.

“Sasa alikuudhi nini tena?” “Yule baba alijua kabisa mimi ni jeuri. Mkorofi wa asili, lakini..” Mama G akaanza kucheka. “Nini?” “Kwanza tulipoingia tu chumbani ujanja wote ukaniishia. Sijui mapenzi wala sijawahi kufanya mapenzi. Sasa sijui natakiwa nifanye nini! Nikaanza kuhangaika sasa. Mara nitoe nguo zote kwenye begi nianze kupanga upya. Kwa mara ya kwanza nikaingiwa hofu. Natetemeka. Mara nikunje mataulo ya bafuni, mara niyatoe. Sasa yule baba kumbe amekaa tu ananiangalia. Akajua. Lakini akataka kunikebehi, akaacha nihangaike mpaka nisalimu amri. Nikawa nimeishiwa sasa vitu vya kufanya, na yeye akajidai anaandika vitu vyake kama hanioni. Nikamuuliza,…” Mama G akaanza kucheka.

“Nini?” “Sasa si sijui! Kusema naona aibu, sababu yakujidai mjuaji eti nikamuuliza, ‘Wewe unapenda kuvuliwa nguo au unavua mwenyewe?’ Akabaki akiniangalia. Nikarudia, lakini safari hii natetemeka mpaka naonyesha. Nikamuuliza, ‘Wewe unapenda kumvua mwanamke nguo au unataka ajivue mwenyewe?’ Yule mzee akaanza kunicheka. Akaniambia, ‘Sikujua kama kuna mazingira huwa yanakufanya ukawa mtoto mzuri hivyo! Njoo kwanza hapa.’ Nikabaki nimesimama. ‘Njoo Oli. Njoo tuzungumze kwanza.’ Nikamuuliza, ‘Kwani nimeharakisha sana?’ Akazidi kunicheka. Nikamwambia, ‘usinicheke bwana! Nielekeze.’ Yule Mzee alicheka mpaka basi.” Hata Nanaa na yeye alikuwa akicheka.

“Basi, akaniuliza, ‘Ujanja wote huo hujui kabisa maswala ya mapenzi?’ ‘Sasa ningelala na nani?’ Nikamjibu kwa kumuuliza swali. Hapo nimepooza kama sio mimi! ‘Sasa ulipokubali kuja huku, ulikuwa na picha gani?’ Akauliza. ‘Nilijua nikifika tu huku ingekuwa rahisi, ningejifanya najua halafu tungelala, lakini kumbe ni ngumu hivi!’ Alizidi kucheka. ‘Usicheke bwana. Mwenzio sijawahi kuvua nguo mbele ya mtu. Hata wasichana wenzangu huwa sikai uchi mbele yao.’ Nikajitetea. ‘Kweli Oli?’ Akauliza. Na nikweli. Sikuwahi kujiweka uchi mbele ya mtu yeyote. Yaani wale masista walikuwa wakiniambia tokea napata akili zangu, nilikuwa naogopa hata paja langu lisikae nje. Wakati wote nilitaka nguo ndefu.” “Na ulivyo na mguu mzuri mama!?” Nanaa akashangaa.

          “Wakati nipo msichana kila mtu alikuwa akiniambia hivyo! Lakini wapi. Nguo hajafika chini, siivai. Yaani wanaume walikuwa wanahangaika, moyoni nilikuwa najiambia nia yao ni kunivua tu nguo wanichungulie, wajue ndani nikoje. Nikajiambia si thubutu. Tena nikikuona unahangaika sana na mimi ndio nakuchukia kabisa. Nakuona wewe dhaifu. Ndio maana naona nilitulia sana kwenye swala la wanaume.” Nanaa alibaki akimwangalia.

“Basi, yule baba akaja akanichukua pale nilipokaa. Nafikiri akanihurumia, akajisikia vibaya. Akaniambia yeye ni mkubwa sana kwangu, sina sababu yakufanya naye mapenzi. Naweza kuendelea kujitunza tu mpaka nitakapo olewa. Nililia. Nikajua ananikataa kwa kuwa sijui mapenzi. Nikamwambia asinikatie tamaa nitajifunza. Akaniambia anafanya vile kwa ajili yangu sio yeye. Hapo nilikuwa mdogo. Kumbuka niliishia kidato cha pili nikatoroka. Nikafanya kazi kwake muda mfupi, mkewe akanifukuza kazi. Ndio nikaanza biashara zangu. Na walinianzisha shule mapema kwa sababu ya utundu na ukorofi. Masista waliona ni heri waniingize darasani kuliko kuniacha nje. Nilikuwa sisikii kama sina masikio! Kila nilichokuwa nikiambiwa nisifanye ndio nilikuwa nafanya. Jeuri, kweli kweli!” “Sasa ulirudi tena?” Nanaa akauliza.

“Sikuwahi kurudi tena.” “Sasa si watakuwa walikutafuta?” Kidogo akamuona Mama G, amepooza. “Sidhani. Kwa kuwa yule padre aliyetuokota mimi na kaka yangu au pacha wangu akanipa jina la Oliva, alikuwa ni mtu wa kutoka Italy. Alianza kuugua akataka arudi nchini kwao. Lakini akasema hawezi kuondoka bila mimi. Alikuwa akinipenda sana. Nakumbuka tokea nakua alikuwa akinifundisha kusali na kuimba. Sasa katika harakati yakukamilisha utaratibu wakunichukua kutoka hapa nchini kunipeleka nchini kwao kama mtoto wake, akaja kufa gafla kabla hata mambo ya safari yangu hayajakamilika. Jamani walinitesa wale watu. Walinitesa sana. Nikawa sisikilizwi tena. Hakuna mtu ananiangalia. Ndipo nikajua ule uangalizi niliokuwa nikipata wakati ule ni kwa sababu ya yule padre. Nilipoona wanazidi kunionea na mimi siwezi kujishusha ndipo nikaondoka.”

“Nafikiri pia walichangia kuondoka kwangu, au ni mimi tu mwenyewe na jeuri yangu! Sijui. Lakini sikurudi na wala sikutaka kuwatafuta tena mpaka leo. Yule padre akanipa jina lake. Alikuwa akiitwa padre Angelo Romano. Akaandika vyeti vyangu vyote vya kuzaliwa, Oliva Angelo Romano. Niliumia sana alipokufa yule padre. Sana. Lakini nilishindwa hata kulia.” “Kwani wewe mama si mlizi?” “Hata iweje. Aliyekuwa akiweza kuniliza ni baba yake Geb tu. Basi.” “Labda kwa kuwa ulimpenda sana.” “Sana. Mzee nilimpenda yule! Karibia kurukwa na akili.” Nanaa akacheka sana mpaka akajisahau.

“Kweli. Na sikuja kuwahi kupenda tena. Na sikuwahi kuwa na mahusiano mengine ya mapenzi. Alikuwa wa kwanza na nikajiambia ndio wa mwisho.” “Kwa nini mama!?” Nanaa akauliza kwa mshangao. “Nilijua wengine watanichafua tu. Sikutaka tena. Yule mzee alinipenda Nanaa! Sijawahi pendwa hivyo. Alijidhalilisha sana kwa ajili yangu. Kwanza alikuwa akifahamika yale maeneo ya Kibaha, huko Picha ya Ndege mpaka kuja huku Kibamba. Alifahamika kama chumvi. Wapi upite usisikie Magesa!”

“Alikuwa anapesa mnooo. Hilo shamba lake la mifugo, lilikuwa gumzo. Lilikuwa kubwa sana na akafanikiwa kufanya ufugaji ule wa kisasa. Walikuja watu kutoka Denmark, wakawa wanatafuta sehemu nzuri yakufanya majaribio ya uwekezaji wakisasa kwa kutumia mashine. Serikali ikamteua yeye kupokea hao wazungu. Kwa kuwa alikuwa na eneo kubwa sana na tayari alikuwa na ng’ombe wengi wakisasa. Wale wazungu wakamuinua zaidi. Kwa hiyo alikuwa na mashine za kumsaidia mambo mengi sana kwa ufugaji. Alikuwa akitangazwa sana kwenye vyombo vya habari kwa ufugaji wa kisasa. Sasa wakakutana na mama wa Kimachame anayejua pesa, basi usiseme. Enzi hizo kuendesha Cruzer ilikuwa sio kitu kidogo. Sasa yeye alikuwa nalo la silver. Akipita mtajua tu ni yeye Magesa amepita. Jeuri kama hivyo unavyomuona Geb. Mkali kama pili pili.” “Sasa ikawaje?” “Mmbea wewe!” Nana akacheka.

“Bwana nisimulie mama!” “Basi, akanikatalia. Akaniambia mimi bado mdogo sana. Hawezi kuwa ndio mwanaume wangu wa kwanza. Nikaanza kuvua nguo zangu zote. Nikamwambia basi ajue yeye ndiye mwanadamu wa kwanza kuniona nipo uchi. Nikamwambia tokea napata akili zangu, nilikuwa naoga mwenyewe ili tu mtu mwingine asinione. Nikamwambia hata kama hataki mahusiano na mimi, basi anisaidie yeye ndio awe mwanaume wangu wa kwanza. Alisadiki kwa sababu alishanijaribu sana.” “Ki vipi?” Nanaa akauliza.

“Kumbe tokea siku ile ofisini nilipomwambia juu ya mwanaume ninayemtaka mimi nikimaanisha yeye, akaondoka, kumbe akaanza kunijaribu. Mkewe ndiye wakati wote alitaka nifukuzwe kazi.” “Kwa nini?” Nanaa aliuliza. “Unakumbuka Chalii alitaka kujiua kwa ajili yangu halafu yule mama akanifuata, nikamjibu mbovu?” “Oooh!” Nanaa akakumbuka nakuanza kucheka. “Basi ndio akanichukia. Lakini yule baba, mumewe, Mzee Magesa alikuwa hataki kuniachisha kazi kwa kuwa nilikuwa nikifanya kazi sana. Kwa asili mimi sio mvivu wala sio mwizi. Alishanitega mpaka akaridhika kuwa mimi sio mwizi. Wafanyakazi wake wengine walikuwa wakimwibia sana. Wanadanganya lita za maziwa wanazopokea kutoka shamba, wanaandika kidogo, halafu zile zinazozidi wanauza. Lakini mimi sikuwa nafanya hivyo. Akajua. Nilipokuwa mimi, aliona mahesabu yake yapo sawa.”

“Haya, akawa akinitumia vijana kuja kunitongoza. Au anawashawishi marafiki zake wanitongoze. Nikawa nawalia pesa zao tu lakini siwapi mapenzi. Wakaanza kujua mimi ni tapeli. Habari zikamfikia Magesa. Kuwa Oliva anatapeli wanaume lakini hataki kufanya nao mapenzi. Ndio kipindi hicho nilipokuwa naye hapo hotelini, akaniambia ni lazima tukirudi niwalipe pesa zao. Nikakataa. Akaniambia, ‘Sio ombi Oli, nilazima. Utamtafuta mmoja mmoja, utaomba msamaha, na kuwarudishia pesa zao.’ Nilihisi kuchanganyikiwa.”

 “Sijui watu wanaombaje msamaha! Nikamwambia. Akasema kama nampenda kama ninavyosema, nitafanya hivyo. Na akaniambia ni lazima kuacha hiyo tabia. Hataki kusikia tena natapeli watu.” Nanaa akacheka sana.

“Mama wewe! Ulikuwa unawatapeli?” “Sana. Ukija kichwa kichwa, nakulia pesa yako, halafu hupati penzi. Sasa ole wako uniguse. Utajuta.” Nanaa akabaki anamwangalia. “Unashangaa nini sasa?” “Nisimulie bwana.” “Hivi wewe mtoto ujue mimi ni mama yake Geb?” Nanaa akajificha uso. “Yaani unataka kujua habari za mapenzi za baba na mama yake Geb! Shika adabu yako.” Nanaa akacheka sana kwa aibu. “Lakini imenoga mama. Si unimalizie tu? Usiniche katikati mama!” “Sitaki. Ila ujue ndio muda huo nikawa muwazi kwake. Nikamuelezea historia yangu ya maisha. Akaniambia hata yeye ananipenda lakini kuna garama kubwa sana ya kulipa ili tuweze kuwa naye.” “Garama gani tena?” Nanaa akauliza.

“Kwanza alijua itagundulika. Watu watataka kujua umri wangu. Tayari nilikuwa ni mtoto sana kwake. Nafikiri nilikuwa nalingana na mtoto wake wa pili, wakike. Alikuwa na watoto wakike wawili tu. Kingine alijua ndoa yake inaweza kuvunjika, lawama itakuwa kubwa kwenye jamii. Alijua jina lake litaharibika sana. Kwa kujulikana anamahusiano na mtoto anayeweza kumzaa. Akaniambia ndio mambo yaliyomfanya akae mbali na mimi kwa muda wote huo, kuhesabu hasara, na kujua kama ninastahili kulipiwa garama yote hiyo! Kwa kifupi ni kama aliamua kutoa maisha yake kafara, kwa ajili yangu.” “Masikini!” Nanaa akamuhurumia.

“Akanielezea umbali aliotoka na yule mwanamke. Kwa nini alimuoa. Akakiri ni kweli haikuwa mapenzi. Ila akasema mkewe ni mwaminifu sana, na ni mchapakazi. Ndio kitu kikubwa alichompendea mara tu alipofika hapo Kibaha na kukutana naye. Akasema kwa kuwa alikuwa na uchu na pesa, akajua akiwa na yule mwanamke watafika mbali. Akasema hakukuwa na mapenzi makubwa kati yao, lakini haikuwahi kuwa shida kwake, kwa kuwa na yeye hakuwa mtu wa wanawake. Shida yake ilikuwa pesa tu.”

“Alisema ndoa yake haikuwa na matatizo makubwa kwa kuwa hakuna aliyetarajia cha ziada kutoka kwa mwenzake, zaidi ya pesa. ‘Sikuwahi kulalamika juu ya kitu fulani kwa mke wangu na yeye hivyo hivyo. Ilimradi pesa inaingia. Mazungumzo yetu ni juu ya biashara zetu basi. Mfanyakazi huyu anaendeleaje. Biashara hii inaingiza pesa kiasi hiki, na kwa nini? Ni nini tufanye ili tuongeze faida, na nini tuwekee mkazo. Basi. Hayo ndio mazungumzo yetu kwa jumla. Na kwa kuwa wote tunakuwa tunachoka na kazi’ .” Mzee Magesa aliendelea.

“Hata ufanywaji mapenzi sio kipaumbele kwetu. Mara chache sana. Tena ikibidi. Mke wangu sio mtu wakupenda mapenzi. Ni haki yake, kwa kuwa anafanya kazi sana. Akijitupa kitandani ni saa 5 au 6 usiku, na yupo hoi kwa kuwa anaamka mara nyingi saa 11 asubuhi kuwahi kwenye miradi. Hatuna utaratibu wa likizo. Kwa kuwa hatuna mtu tuna mwamini na miradi yetu. Labda ndio maana tumefanikiwa sana katika hilo eneo la pesa lakini si kindoa. Ila narudia tena, hatujawahi kuona tatizo, kwa kuwa hakuna aliyetarajia kitu cha ziada kwa mwenzake.’ ‘Kwa nini hukuwahi kutafuta mwanamke wa nje? Nimesikia wanawake wengi wakisema washakujaribu sana, lakini umekuwa ukikataa. Mpaka wasichana wadogo na wazuri.’ Nikamuuliza.”

“Alisema, ‘Najua watu wengi wananipendea pesa. Kila mtu anajua akiwa na mimi ataneemeka. Kitu ambacho nakipata kwa mke wangu. Hata yeye akiniona, anaona kichwa kitakachofikiria haraka na kumpa ufumbuzi wa matatizo yake ya kipesa. Hajui kufanya kitu bila kuniuliza. Kwa kuwa Mungu alinijalia akili ya haraka ya kufikiria, na hekima katika maamuzi. Ndio maana nategemewa sana katika jumuiya. Iwe kanisani, au kwenye jamii, watu wananitegemea sana.’ Nilimuhurumia. Nikasimama, nikaanza kuvaa nguo zangu. Akaniuliza kwa nini nafanya hivyo? Nikamwambia sitaki kumuharibia maisha. Nimeelewa kwa nini hataki kufanya mapenzi na mimi.’ Mama G aliinama kidogo, akafikiria.

“Nakumbuka alisimama, akanikumbatia na kuniweka kitandani. Akaniambia, ‘Oli! Wewe ni mtu wa thamani sana kwangu. Wakati wote umeonyesha kunijali mimi kuliko pesa yangu.’ Yeye ndio mtu pekee aliyekuwa akiniita Oli. Kila alipokuwa akija kazini, nilihakikisha anakunywa chai.” “Mama! Ulikuwa ukimtengenezea?” “Nilijua hali vizuri Nanaa. Na hasira zile zilikuwa ni njaa. Kwa hiyo nikawa nampikia vitafunio nyumbani, na kaanga mayai au nyama. Naenda navyo ofisini. Akija tu, nampashia maziwa moto, namuwekea Cocoa, namtayarishia namuwekea mezani kwake, ofisini kwake.” “Sasa wenzio walikuwa hawakusemi?” “Mimi huwa sijali Nanaa. Nilimpenda yule baba, kama mwehu. Nilikuwa nikimuona amekasirika, nilikuwa naumia sana. Nilikuwa nahakikisha anakunywa maji kila wakati.” “Sasa wangemwambia mkewe?” “Mimi sinaga hayo maswali na majibu ya kesho. Ninaloliweza kulifanya leo, nafanya. Kesho napambana nayo ikifika.” “Nimekuheshimu mama.” Mama G akacheka kidogo.

“Basi. Akaniambia mimi ndio nilikuwa mtu wa kwanza kumjali na kumthamini kama yeye. Lakini akaniambia umri wake umekwenda. Akaniambia ananihurumia kunianzishia jambo halafu akaniacha nateseka peke yangu. Akili ikanijia kwa haraka. Nikamwambia mimi sitegemei chochote kutoka kwake isipokuwa mapenzi. Nikamwambia naweza kujitunza. Na hata kama nikipata watoto, naweza kulea wanangu bila yeye. Nikamwambia ninachotaka maishani ni yeye tu kuwa mpenzi wangu. Yule baba hakuwa akiamini Nanaa. Alibaki akiniangalia. Nilikuwa mtoto, halafu navutia kwa kila kitu. Akabaki ananiuliza, ‘Kwa nini mimi!?’ ‘Sijui. Lakini najua nakupenda wewe. Na ninataka wewe ndio uwe mwanaume wangu. Nitaacha kukusumbua tu, endapo utaniambia nakuharibia maisha yako. Nitaondoka na sitakusumbua tena.’ Nikamwambia hivyo. Alikuwa akiniangalia na macho yake yale, nazidi kuwa mdogo. Ujeuri wote unaniisha.” “Kama Geb. Anamakusudi kweli. Anayajulia macho yake. Basi akikuangalia hata kama unampango wakusema hapana, unajikuta unasema ndiyo. Halafu unataka akubusu tu.” Mama G akacheka mpaka machozi.

“Kweli mama. Mimi hata sikuwa na mpango wa mwanaume mpaka nimalize chuo. Kwanza nilivyomwambia Zinda, sikuwa nimemdanganya. Sikuwa nataka wanaume kabisa. Nilishakinahiwa. Lakini Geb akitaka jambo lake, hutoki mama.” “Basi na baba yake yupo hivyo hivyo. Na hana papara ya mambo. Mkikaa hapo kitandani, hutataka mtoke.” Nanaa alificha uso. Akawa anacheka. Alimkumbuka Geb. Hakuwahi kupata mwanaume mjuzi wa mapenzi vile. Geb aliweka historia mpya na nzuri kwenye maisha yake.

“Nimalize basi mama.” “Basi. Ndio tukakubaliana. Akaniomba tusubiri kwanza swala la watoto, ili na yeye apumzike kidogo. Aliniambia hajawahi kuishi hayo maisha ya mapenzi. Anataka ayafurahie kidogo kabla watoto hawajaja. Ukweli yeye hakuwa akitaka watoto kabisa. Mimi ndiye nilimuomba. Mapenzi yakaanza. Nikawa kile anachokitaka kwa kuwa yeye ndio alikuwa mwalimu wangu. Akaja kuwa kama mjinga na yeye. Kutwa yupo mlangoni kwangu. Asubuhi na mapema, anakuja kwangu, Kibamba.”

“Maneno yakaanza kuenea kwa kuwa gari yake ikawa inaonekana mitaa ya Kibamba, nyumbani kwangu. Wakati mwingine mchana ananifuata kazini, ananirudisha nyumbani. Ananiomba niwe naye hata kwa lisaa tu. Mchana, kweupe! Asubuhi anatoka kwake, anakuja kwangu. Wakati mwingine nakuwa hata sijaamka, nashitukia anapanda kitandani kwangu. Maana alichongesha funguo za kwangu. Akawa anaingia na kutoka vile atakavyo. Maneno yalivyozidi, akanihamishia mjini. Akanichukulia nyumba mitaa ya Kinondoni. Akanunua kila kitu. Sikufurahia sana, kwa kuwa kulikuwa mbali na kwake.” “Yeye alikuwa akiishi wapi?” Nanaa akauliza.

“Alijenga bonge ya jumba huko Picha ya ndege, karibu na shamba lake. Kibaha ndio kulikuwa na kiwanda chake cha maziwa. Nikalalamika. Lakini akasema ni kwa usalama wangu. Lakini atajitahidi kila siku lazima tuwe tunaonana.” “Biashara yako sasa?” “Aliifunga. Maneno yalikuwa mengi sana. Na yeye alikuwa hawezi kujizuia. Nakwambia mchana kweupe, anaonekana amekuja kunifuata kazini, ananichukua kwenye gari yake, ananirudisha nyumbani kwangu. Tutakaa hapo kitandani mpaka jioni. Ananirudisha tena kazini kwangu, yeye anaendelea na shuguli zake.” Nanaa akaanza kucheka.

“Watu wakawa wanatufuatilia. Wakawa wananisema kuwa ninakataa vijana wenzangu, halafu nimemkubali yeye Mzee sababu ya pesa. Chalii ndio alizidisha fujo. Analalamika kuwa shemeji yake kampora mwanamke wake. Ndio sasa Magesa akanilazimisha kuhama. Akanifungulia sehemu nyingine ya biashara ileile ya Yogurt, maeneo ya posta. Nilikuwa natengeneza pesa, kama nini sijui! Sasa hapo sina mtoto, sina ndugu. Pesa yangu ni yangu. Na Magesa naye akawa ananipa pesa.”

 “Kwanza tuliporudi kutoka mapumzikoni Arusha, baada ya miezi michache tu, akanizawadia gari akasema ni zawadi ya kujitunza. Ilikuwa Toyota Corola. Enzi hizo waendesha magari wachache sana, tena wanahesabika. Sasa uje kukuta ni mwanamke! Ndio kabisaa. Nilikuwa Oliva kweli kweli. Nikipita mahali utajua nimepita. Sisikii la mtu, ni Magesa tu.” Nana alikuwa akicheka kama sio yeye aliyepokonywa mtoto.

“Nakumbuka siku hiyo akaja nyumbani amepoa.  Kila nikimuuliza kulikoni hasemi, anatoa tabasamu huku ananiambia nisiwe na wasiwasi. Nikamwambia yeye ananijua huwa sina wasiwasi isipokuwa yeye akiwa kwenye matatizo. Nikambembeleza siku hiyo, ndio akaniambia yupo kwenye matatizo na watoto wake. Wamejua kama anamwanamke mwingine. Tena mtoto umri wao. Wanataka kujua ukweli. Kwa kuwa mama yao hana raha. Nikamuuliza aliwajibu nini? Akasema alishindwa kukubali au kukataa. Nikamwambia mimi sitakuwa tayari kumuona yupo kwenye hali ile. Nipo tayari kumuacha aendelee na maisha yake. Au hata akitaka tuachane kwa muda, mpaka aweke mambo yake sawa. Nikamuahidi nitamsubiri tu.” “Maskini mama! Kumbe ulimpenda sana!” Nanaa alimwingilia.

“Yaani Nanaa, nilikuwa nahisi kurukwa na akili nikimuona yule Mzee hana raha. Basi. Nikamwambia namruhusu aondoke. Sitamtafuta wala kumsumbua mpaka atakapoweka amani nyumbani kwake. Nikamwambia lakini kabla ya kuondoka lazima tuagane. Maana alikuja kama mgonjwa. Nikambembeleza mapenzi, akakubali tukiambiana ndio tunaagana kwa muda. Tukajisahau siku ile, tukashitukia pamepambazuka. Akatoka kama amechanganyikiwa. Sikumuona tena mpaka baada ya miezi kama 5 hivi.”

~~~~~~~~~~~~~~

Nini Kiliendelea? Usikose Kufuatilia.

 


CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment