Naomi Simulizi |+1 205 767 8163 |naomisimulizi@gmail.com Ni Wangu! - Sehemu Ya 29. - Naomi Simulizi

Ni Wangu! - Sehemu Ya 29.

Nanaa akajua inabidi kuchukua hatua kwa haraka. Akaingia chumbani, akajisafisha na kubadilisha nguo. Alifikiria kidogo, mtu wa kumpigia simu, akajua ni kujidhalilisha tu. Rafiki zake watamcheka zaidi, na kaka yake hakujua kama yeye ni mjamzito. Na Antii hakuwepo. Alipata dharula ikabidi akimbilie Moshi. Mama yake alikuwa mahututi. Ni usiku uliopita tu alitoka kuzungumza naye na kumwambia ilimbidi amkimbize KCMC kwa kuwa alizidiwa. Nanaa akamfariji Antii. Akaagana naye kwa ahadi yakumpigia siku inayofuata kujua hali ya bibi uyo. Kwa hiyo alibakia peke yake.

Akaamua kwenda mwenyewe hospitalini. Alichukua taksii iliyompeleka mpaka hospitalini. Alikutana na muuguzi mcheshi sana. Alimpokea begi la mtoto wake, akampa kitanda. Alipopimwa, akaambiwa njia imeanza kufunguka. “Lazima huyu mtoto azaliwe leo.” Alimwambia yule muuguzi aliyemkuta pale, akacheka. “Kwa nini?” “Nina mtihani siku ya jumatano.” “Si uarishe?” “Hapana. Hii shule haijawahi kusubiri, na haitakaa ikasubiri. Lazima iishe. Nilijua huyu mtoto ndie angesubiri mpaka nimalize, naona anataka tuonane mapema. Amechoka kunisikiliza tu. Anataka kuiona sura ya mama yake. Sasa leo lazima utoke, tuonane.” Nanaa aliongea huku akijipapasa tumbo. Akashauriwa atoke nje ajaribu kutembea tembea ili kusaidia kufunguka kwa njia zaidi. Nanaa akatoka nakuanza kutembea. Alizunguka mpaka alipohisi maumivu makali sana, akarudi tena kuangaliwa njia. Nesi alipoona imefunguka vizuri, akamuingiza chumba cha kujifungulia.

~~~~~~~~~~~~~~

Alisukuma mara kadhaa tena kwa ujasiri bila hata yowe huku akijiambia ni lazima aishi alee mtoto wake. “Lazima nitoke kwenye hichi chumba, nikalee mwanangu mimi mwenyewe. Sitakufa, bali nitaishi.” Nanaa alikuwa akijiambia kila akijitahidi kusukuma mtoto. Kama aliyekuwa kwenye mchezo, akayapita maumivu yote kwa kuwaza uzima wake na mtoto,  akajikaza kwa mara ya mwisho, akasukuma mpaka mtoto wa kike akatoka. Hapo ndipo alianza kulia. Alilia kama amefiwa. “Mtoto wako ametoka na nywele zote na kucha! Mtoto mkubwa kweli!” Nanaa alipata muuguzi mzuri sana. Japokuwa yeye aliisha, lakini alizaa mtoto mwenye afya nzuri. Nywele nyingi kama baba yake, na macho ndio hukuhitaji kuuliza. Geb mtupu. 

Nanaa alipewa mtoto wake huku akilia. Alikuwa mtoto mkubwa sana. Akarudishwa naye wodini, mtoto akaanza kunyonya. Ilipofika mchana muda wakuona wagonjwa, jirani yake alikuja kutembelewa na mume wake, Nanaa akamuomba akamsadie kumnunulia chakula. Yule baba hakukataa, akaenda kumletea chakula kwa ahadi ya jioni atajitahidi kuleta kingi ili ale na mkewe. Na kweli, jioni akaletewa uji kama jirani yake.

Alikula akawa ameshiba, lakini alijikuta akilia usiku kucha. Alijiuliza ni kwa nini yule mtoto amekuja wakati ule. “Si angesubiri tu mpaka nimalize mtihani jamani! Nitafanyaje mitihani na huyu mtoto!?” Nanaa aliendelea kuwaza huku akimwangalia mwanae aliyekuwa amelala vizuri bila hata wasiwasi. Watoto wengine walikuwa wakilia lakini sio mwanae. Yeye ndio alikuwa akilia wakati mtoto wake amelala. Kila mtu alimsifia huyo mtoto. Alichukua rangi ya mama yake, ila nywele ndio zilikuwa nyingi sana. Nyeusi na mviringo kama mtoto wakiarabu. Mkubwa, mrefu kama mtoto aliyekuwa ameshatimiza mwezi. Kila alipokuwa akimwangalia yule mtoto alimkumbuka vile Geb alivyokuwa akipenda kumlalia kifuani kwake ili amchezee nywele zake. Alizipenda sana nywele za Geb, na hakuchoka kuzishika. Alikuwa akitulia wakati Nanaa akichezea nywele zake mpaka analala.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Aliruhusiwa asubuhi wakati madaktari wanapita round mawodini. Akarudi chumbani kwake. Alishukuru Mungu kukuta mwenzake amemuachia ujumbe kuwa amehamia kwa marafiki zake kwa kipindi hicho cha mitihani kwa ajili ya kusoma nao. Yule dada alikuwa mwalimu, alijiunga hapo chuoni ili kuongeza elimu. Alikaa kitandani akamuweka mtoto kwenye ziwa huku anasoma. Alimnyonyesha kwa muda mrefu kwa kuwa maziwa hayakuwa yakitoka mengi. Alipolala, akamuweka kitandani na kuendelea kujisomea huku akiwaza pakumuweka huyo mtoto kesho yake akiwa anaenda kufanya mtihani, ambao ulikuwa mchana.

Mpaka panapambazuka siku ya jumatano, siku ya mtihani, Nanaa hakuwa amepata mtu. Wazo lilimjia la kumtafuta Mama G. Aliangalia saa, akajua atakuwa kwenye biashara yake, dukani kwake. Geb alimfungulia mama yake sehemu kubwa yakuuza mchele kwa bei ya jumla na rejareja. Alikuwa na wafanyakazi wanao msaidia, kwa hiyo alikuwa akienda muda na wakati anaotaka yeye.

Mtaka Cha Mvunguni.

A

kaweka line yake yazamani, akapata namba ya mama G. Akapiga. Iliita mara moja tu, akapokea. “Hujambo Nanaa, mwanangu?” Nanaa alishindwa kujibu akaanza kulia. Alilia kwa muda, “Vipi mama? Hujambo?” Mama G aliendelea kumbembeleza kwa upendo lakini Nanaa aliendelea kulia. “Umenitupa mama yako!” “Nina shida sana mama yangu. Naomba msaada wako.” “Unataka nini?” “Nahitaji msaada wako kwa masaa kama matatu tu. Lakini usimwambie mtu yeyote kama unakuja kwangu na tumewasiliana.” “Unataka nije wapi?” “Hapa chuoni. Tukutane ofisi za Utawala. Saa sita kamili.” “Nitakuja mama. Usiwe na wasiwasi.” Nanaa akamshukuru na kukata simu. Aliendelea kulia kidogo, akajiambia anapoteza muda.

Nanaa na Mama G.

Ilipotimu saa 5:50 asubuhi, Mama G alikuwa akiegesha gari karibu na ofisi za Utawala hapo chuo kikuu cha Mlimani. Yaani dakika kumi kabla ya muda wa miahadi yao. Alitafuta sehemu yenye kivuli ndipo akaegesha gari yake. Akabaki ndani ya gari akimsubiria Nanaa. Ilipofika saa sita na dakika tano, Mama G akashangaa mtu anagonga kwenye kioo chake cha dirisha. Akashusha kioo, akabaki anamshangaa Nanaa na mtoto. “Nipo kwenye mtihani mama yangu. Naingia saa sita na nusu. Nisaidie kukaa na mwanangu wakati nafanya huu mtihani. Nikitoka nitamchukua mwanangu.” Mama G akiwa na mshangao mkubwa sana, akakubali. “Hamna shida. Utanikuta hapahapa.”

“Nakuomba mama, usimwambie mtu. Ibaki siri yetu tu.” “Wala sitasema.” Nanaa akambusu mwanae, akamfunua kidogo ili amuongeleshe. “Nitarudi muda sio mrefu. Unisubiri. Umesikia eeh? Mama hatachelewa.” Alimuongelesha mwanae kwa upendo. Akambusu tena mtoto wake huku Mama G akimwangalia. Akamkabidhi yule mtoto kwa Mama G, akabaki akimwangalia mwanae. “Nenda usiwe na wasiwasi naye. Atakuwa salama tu.” “Asante mama.” Akashukuru huku machozi yakimtoka. “Nenda kawahi mtihani. Utanikuta hapahapa na mwanao.” Nanaa akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Cha kwanza alichofanya Mama G, ni kuanza kumchunguza huyo mtoto aliyeachiwa. Alibaki akimgeuza asimalize. Alimkumbatia nakushindwa kumuweka chini, akabaki akimwangalia kwa muda wote. Huku machozi yakimtoka. Alianza kuomba. Akamshukuru Mungu kwa karibia nusu saa huku machozi yakimtoka. Alianza kumuombea yule mtoto huku akimbariki bila kuchoka. “Asante Mungu umekumbuka uzazi wangu. Asante Yesu kunipa huyu mtoto.” Akaendelea kushukuru huku amemkumbatia huyo mtoto kwa upendo sana.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Baada ya kumaliza tu mtihani wake, Nanaa akarudi. “Pole mama. Amekusumbua?” Nanaa aliongea akiwa amesimama dirishani upande wa dereva alipokuwa amekaa mama G. “Hata kidogo. Kwanza hajaamka!” Nanaa alikuwa akimwangalia mwanae. “Analala sana. Inabidi niwe namuamsha ili anyonye.” “Naomba uingie ukae hapo kwenye gari, Nanaa.” Nanaa akaingia kiti cha mbele. Nakukaa. 

“Umejifungua lini?” “Juzi.” Nanaa akajibu, na kumuacha yule mama akiwaza. “Mtoto anaitwa nani?” “Sikuwa hata nimefikiria bado. Maana mtoto mwenyewe nimejua jinsia yake siku amezaliwa. Halafu sikumtarajia kama angekuja kipindi hiki ambacho nina mambo mengi. Mitihani inayonilaza macho. Nilijua atasubiri mpaka nimalize mitihani, pengine akili ingekuwa imetulia na kuweza kufikiria. Sikutaka kukurupuka tu na kumpa jina. Nilitaka mpaka nitulie ndio nifikirie vizuri jina la kumpa. Au wewe unajina lolote ungependa nimpe?” Nanaa alimuuliza huku akimwangalia mtoto wake. 

Mama G akacheka. “Labda tumpe langu. Oliva.” “Liv! Zuri sana. Basi hilo hilo ndio atakuwa akiitwa. Nikimaliza chuo nitaenda kumuandikisha hilo la Oliva.” Nanaa alimchukua mtoto wake. “Nakushukuru sana mama.” “Mitihani imeisha?” “Bado mama yangu. Kesho ninao mwingine asubuhi. Nilitaka kukuomba uje tena, kama utaweza.” “Hamna shida. Lakini Nanaa, kwa nini tusiende wote nyumbani? Nitakuleta asubuhi.” “Hapa nipo naishi vizuri tu, nipo kwangu.” “Ulikodi chumba mtaani?” “Hapana mama. Ni hapahapa hosteli. Ila nipo chumbani mimi na Liv tu. Mwenzangu amehama chumba. Anajisomea na wenzake kwa ajili ya mitihani. Ila kama hutaweza hamna shida nitatafuta mtu mwingine.” “Nitaweza Nanaa. Unajua sina kitu chakufanya sasa hivi. Grace na familia yake walishaondoka pale, wanaishi kwao. Nipo mimi na Geb tu. Sina chakufanya. Nitakuja.”

“Asante mama. Lakini naomba usije kumwambia mtu. Nitahitaji msaada wako kwa masaa machache tu, ambayo nitakuwa kwenye mtihani, baada ya hapo unaweza kuondoka tu.” “Basi nitawahi kidogo, nitakuletea uji. Unywe kabla yakuingia kwenye mtihani.” Nanaa akacheka. “Asante mama yangu. Nitakuona kesho.”  Alimuacha Mama G amekaa kwenye gari yake akiwaza. Hakuwa amezima hilo gari tokea afike hapo, akawa amewasha AC kiasi kwa ajili ya mtoto.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Alitoka hapo na kuanza kununua vitu vya mtoto na vyakula vya kumpikia Nanaa. Alipofika tu nyumbani akaingia jikoni. Geb alimkuta mama yake anahangaika jikoni. “Una wageni?” “Hapana? Kwani vipi?” “Naona unamasufuria zaidi ya mawili hapo jikoni. Halafu chupa za chai kubwa, tena mpya na hotpots mpyaa!” Akanyamaza, kitu kilichomtia wasiwasi Geb na kurudi tena pale jikoni. Akafungua mlango akaingia mpaka ndani kwani mwanzoni alisalimia, akawa anaongea naye akiwa anaelekea chumbani kwake.

 “Mama!?” “Sufuria hili la supu ya kuku, hili lina mifupa ya nyama ya ng’ombe ili nipate supu ya kupikia mtori. Na hapa naandaa kupika mtori, pale ni uji wa kawaida.” Geb akakunja uso. “Vyote hivyo!?” “Kwani shida yako wewe nini?” “Basi mama. Mbona mkali?” “Nakuona maswali hayakuishi!” “Ujue nimekuuliza swali moja tu mama.” “Bwana eeh!” Geb akacheka, akatoka, baada ya kuoga akarudi jikoni kwa mama yake.

“Mchana nilipita pale dukani, sikukuona?” “Nilitoka.” Mama G, alijibu kwa kifupi huku akiendelea kupika. “Najua ulitoka mama yangu, ndio nataka kujua ulikwenda wapi wakati uliniita, nikakwambia nitakuja wakati wa chakula cha mchana!” Mama G, akasimama kidogo akiwaza, akajua ameshagonganisha magari. “Kwani leo vipi, mama?” “Kuhusu nini?” “Upo kama una wasiwasi. Uso wako haujatulia kabisa! Au kuna kitu unahangaika kunificha?” “Wewe naona umechoka leo. Hebu nipishe bwana nimalizie kupika.” Geb akaamua kunyamaza.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Mama G aliamka asubuhi na mapema, akamalizia kupika kila kitu na kupasha moto vyakula vya jana yake, akaviweka kwenye zile chupa za chai, na hotpots. Akaanza kuweka kwenye gari yake. Geb aliamka baada ya kukurukakara nyingi za mama yake. “Nikusaidie?” “Hapana. Nishamaliza.” “Kwani una mgonjwa?” “Mbona una maswali mengi wewe Geb? Unashida gani na mimi?” “Mbona mkali hivyo mama yangu? Mbona swali ni dogo tu?” “Ndiyo nina mgonjwa. Na sitaki swali jingine.” Geb akacheka nakurudi chumbani kwake. “Siri hizo Mama G, wewe! Zitakutokea puani.” “Hayakuhusu. Wewe nenda kazini.” “Haya mama yangu.” Geb alijibu akiwa chumbani kwake na Mama G jikoni.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Alifika sehemu ile ile aliyokubaliana na Nanaa, akaegesha gari. Baada ya muda mfupi Nanaa akaja na mtoto wake. “Sijalala mama. Mtoto ameanza kulia.” “Hashibi. Mlete nikae naye hapa, wewe kula. Nimekuletea vyakula. Kula kwa haraka vikiwa vya moto, ili maziwa yatoke.” Bila kujivunga, Nanaa akamimina uji, akaunywa wote. “Nikirudi nitakula tena. Nilikuwa na njaa sana. Asante mama yangu.” “Wewe nenda, niachie wajina wangu.” Nanaa akatoka baada ya kumbusu mwanae mara kadhaa akiwa ameshikwa na mama G. 

Baada ya mtihani akarudi na kukuta yule mtoto ni kama ameogeshwa. “Umemuogesha?” “Nimemfuta tu. Nimenunua kila kitu, nazunguka navyo kwenye gari. Nilichemsha maji kabisa, nikaweka kwenye chupa. Kwahiyo nimemfuta, nikambadilisha nguo kabisa. Vipi mtihani?” “Hivyo hivyo mama, itaisha tu. Nataka nikalale ili baadaye niamke nisome.” “Twende wote nikakae na mtoto ili wewe ulale.” Nanaa akaanza kulia.

Alilia kwa muda mrefu. “Naomba utusamehe Nanaa. Tulishindwa kukuthamini mwanangu. Wote tulijilaumu sana. Zaidi mimi niliyekuacha nje. Nisamehe mwanangu. Nilipitiwa.” “Hamna neno mama. Hata hivi nakushukuru kwa kuja kunisaidia. Ngoja sisi twende.” “Siwezi kurudi na hivi vyakula vyote Nanaa. Nimekupikia wewe mwanangu. Naomba uvichukue.” “Sina pakuviweka mama!” “Basi naomba uniruhusu twende wote mpaka huko unapoishi. Nikusubiri ule, ulale, wakati nakushikia mtoto. Ukiamka ukaoga na kula tena, nitaondoka.” Nanaa alianza kulia tena. 

“Najua tulikuudhi mwanangu. Lakini sasa hivi unahitaji msaada ili umalize salama. Acha nikusaidie ili juhudi zako zote za miaka yote zisiende bure. Umejinyima vingi sana ili umalize. Kubali nikusaidie mtoto, ili wewe uzingatie mambo ya shule tu. Ukimaliza mitihani, ukinifukuza, wala sitakusumbua.” Nanaa akacheka na machozi yakimtiririka. “Haya mama yangu.” Wakaongozana mpaka chumbani kwake. 

Akala tena na kulala wakati Mama G anambadilisha mtoto wake. Aliamka akampa tena chakula, akajaribu kumnyonyesha mtoto wake, maziwa yakaanza kutoka kidogo. “Kazana kula. Yatatoka tu.” “Sasa umemletea nguo zote hizo, nitaziweka wapi?” “Nitakuwa naondoka nazo kwenda kufua, asubuhi narudi nazo.” Nanaa akacheka. “Umeamua kuhamia hapahapa?” “Nakushikia mpaka mitihani iishe.” “Mmh! Kwani unampango wa kuhamia hapa?” “Hapana. Nakuja asubuhi, naondoka usiku.” “Kwa hiyo huondoki sasa hivi?” “Saa mbili au tatu usiku mwisho. Naondoka.” “Kweli umeamua kunisaidia mama yangu.” “Ili usilemewe. Wewe waza mambo ya shule tu. Mtoto kazi yangu. Mnyonyeshe tu, mengine yote ni mimi” Nanaa alimshukuru sana Mungu kwa hilo. “Asante mama.”

Bila kupoteza muda, akaoga, akala, nakurudi kusoma. Siku hiyo alikaa na Mama G, mpaka usiku. Alihakikisha Nanaa ameshiba, akamuachia uji wakunywa usiku kama ataamka nakusikia njaa. Akambadili mtoto nguo, akamlaza vizuri. Ndipo akaondoka. 

~~~~~~~~~~~~~~~~

Kesho yake tena mama G akarudi. “Nakushukuru kwa chakula mama. Maziwa yameanza kutoka. Liv amelala vizuri kwa kushiba.” Nanaa alimuwahi Mama G, mara alipoingia, akacheka. “Basi nipe nimshike, wakati wewe unakula. Kazana kula, yatatoka mengi zaidi.” “Unamizigo mingi! Ni nini tena umeleta?” “Matandiko yake huyo. Vitambaa vyakumshikia na kumsafishia. Mashuka yake, na kichandarua kidogo, ili mchana akilala nimuwekee.” Nanaa akacheka. 

“Naona nimekupa kazi kubwa! Pole mama yangu.” “Ndio nafurahia mwenzio!” “Kwa hiyo huoni kama usumbufu?” “Naona umeniheshimu sana Nanaa. Wewe kula, usome. Mengine tutaongea wakati mwingine.” Alimpisha pale kitandani ili amtandikie mjukuu wake, yeye akahamia mezani kula. 

Alikula, akaoga na kuanza kusoma tena wakati Mama G, akimsafisha mtoto kitomvu. “Kitaanguka mapema kweli!” “Sasa hivyo unavyomsafisha, haumii?” “Angelia. Lazima kumsafisha vizuri ili kisioze.” “Vitu vyote hivyo umekuja navyo!?” Mama G, akacheka. “Shuguli imenipata! Na hivi umempa jina langu, basi ndio na mapenzi yanazidi.” Nanaa akaendelea kucheka akimtizama vile anavyohangaika na huyo mtoto.

Siku hiyo hakuwa na mtihani. Wakashinda hapo chumbani pamoja, Nanaa akila na kusoma huku Mama G, akimlelea mtoto. Ilipofika usiku akaondoka na kumuacha Nanaa ameshiba. Akaondoka na nguo chafu za Nanaa na za mtoto wake. Akarudi nazo nyumbani.

 ~~~~~~~~~~~~~~~~

Alimkuta Geb amekaa sebuleni. “Natamani kukuuliza habari za huko ulikokuwa mpaka unarudi usiku kila siku! Lakini najua hutanijibu.” “Sasa si unyamaze!” Geb alinyanyuka kwenda kumpokea. Alikuwa na mizigo mingi na begi ambalo hakutaka Geb ashike. “Wewe nenda kanioshee hivi vyombo vyote. Chupa za uji na chai, hizo hotpots na hayo mabakuli. Halafu bandika nyama. Nakuja sasa hivi.” Geb hakuongeza neno, akapokea na kwenda jikoni.

“Mama G! Naona mapenzi yako yameisha kabisa kwangu. Natamani kumjua huyo aliyechukua nafasi yangu! Siku hizi hata hunitafuti kwa la kheri wala la shari. Hunipigii kuniuliza kama nimekula au la! Haya, nikikufuata tukale pia sikupati!” Mama yake alikuwa akimsikia mwanae alipokuwa jikoni yeye anafua kwenye mashine, lakini akanyamaza. “Najua unanisikia mama.” Akamsikia mama yake anacheka. 

Akarudi pale jikoni. “Mbona shuguli zimekuzidi Mama G, vipi?” “Mmbea wewe? Unachonifuatilia ni nini?” “Mimi na wewe Mama G?” “Huna lolote. Nipishe nipike bwana wee. Umemsikia Grace?” “Alipita hapa na mwanae, kukuangalia. Anasema hakupati kwenye simu.” “Yaani nyinyi wawili, mtafikiri bado mnanyonya! Kutwa mpo mgongoni kwangu! Niacheni na mimi nipumue.” “Yamekuwa hayo?” “Ndiyo. Niacheni. Kutwa mnataka kunisikia! Na mimi nina maisha yangu.” “Mwenyewe huyo Mama G!” “Ukisikia mwingine ujue kopy. Mjini nipo peke yangu.”  Geb akaanza kucheka akimwangalia mama yake.

“Nikusaidie?” “Sitaki. Mbona umenikazania hivyo?” “Basi mama. Nakaa hapo pembeni nakusubiria. Sikuongeleshi tena.” “Bora.” Mama G, alimaliza kupika haraka. Akaenda kuoga na kulala. Hakuongea sana na Geb, Geb alimuona amechoka.

Hakuna Siri Duniani.

Asubuhi tena akaamka na kaunza upishi wake. Geb alitoka akanywa uji aliokuwa amemtayarishia, akabeba chupa yake ya uji akamuaga mama yake akatoka. Aliondoka akaenda kuegesha gari mbali kidogo na nyumbani kwake. Kama baada ya lisaa akamuona mama yake akitoka, akamfuata nyuma kwa siri. Akashangaa anaelekea chuo kikuu cha Mlimani! Aliendelea kumfuata bila mama yake kujua. Akaona ameegesha gari nje ya moja ya hosteli, akaanza kushusha vile vitu kutoka kwenye gari lake, na kupandisha navyo juu.

Kwa kuwa Geb alishasoma hicho chuo, hakupata shida kuficha gari yake na kumfuatilia mama yake mpaka juu. Alimuona mama yake akimalizia mzigo wa mwisho. Akamfuata taratibu na yeye akipandisha ngazi huku akijificha na gazeti usoni. Akawa kama mtu anayelisoma. Alipanda naye bila mama G, kujua msoma gazeti nyuma yake ni mwane Geb, mpaka akaingia chumbani kwa Nanaa, Geb akapitiliza mbele kidogo, akawa anachungulia. Pakatulia. Geb akaanza kufikiria kama aingie au la. Mara akamuona Nanaa anatoka akiwa na haraka. Akasubiri kidogo tu akagonga.

 Damu Nzito Kuliko Maji.

“Umesahau nini?” Mama yake akafungua mlango huku amebeba mtoto. Alishituka sana baada ya kumuona Geb. “Kumbe huku ndiko unapokuwa unakuja?” Geb aliingia akakaa kwenye kiti. Mama yake akafunga mlango kimya kimya akijua ameshakamatwa.

Akarudi akaanza kumsafisha mtoto vizuri, akambadilisha nguo. Akabaki amempakata mtoto bila hata kumsemesha Geb. Alipomlaza tu kitandani, Geb akaenda kumchukua pale kitandani. Akampakata, akamuangalia kwa muda mrefu huku akimgeuza geuza bila yakusema kitu. Aliporidhika akachukua kitambaa akajifunika kifuani kisha akamlaza yule mtoto kifuani kwake, akanyoosha miguu kwenye kiti kingine, akanyamaza. 

“Nanaa aliniambia nisimwambie mtu.” Mama G akaanza kama kujitetea lakini Geb hakujibu. Aliendelea kumpapasa yule mtoto taratibu mgongoni kama anayembembeleza. “Lakini nilipanga baada ya kumaliza mitihani yake ndio nikwambie. Yupo kwenye mitihani, sikutaka kumkera akashindwa kufanya mitihani yake.” Geb hakumjibu kitu. Akajivuta nyuma akajiegemeza, akafunga macho akiwa amemuweka mwanae kifuani kwake.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Baada ya masaa mawili,  Nanaa akarudi. Alikaribia kuanguka baada ya kumkuta Geb amebeba mtoto wake huku amefunga macho, palepale kwenye kiti. Akamgeukia Mama G. “Pole na mtihani.” Nanaa akabaki kimya. “Kaa chini unywe supu.” “Maziwa yanamwagika. Nataka nikaoge, nije kumnyonyesha.” Nanaa alitoka, baada ya muda akarudi akiwa amejifunga khanga. Akamchukua mwanae kutoka kifuani kwa Geb bila hata kumsemesha Geb, akaanza kumnyonyesha. Liv alinyonya mpaka alipomaliza, Nanaa akamuweka begani ili ateuke lakini Geb akaenda kumchukua, akamuweka yeye begani kwake. Alizunguka naye pale chumbani mpaka akasikia mtoto ameteuka, akarudi kukaa naye palepale,  na mtoto kifuani kwake.

Mama G, alimuwekea supu kwenye bakuli, Nanaa akaanza kunywa. “Nguo inalowa, Nanaa!” “Maziwa yamekuwa mengi. Itabidi kukamua. Ningekuwa na friji ningekuwa nakamua, nakuweka kwenye friza kama nilivyofundishwa kliniki.” Pakazuka ukimya mwingine. “Jilaze mama kidogo.” Nanaa alimuhurumia Mama G aliyekuwa akifika pale asubuhi sana, nakuondoka usiku. Na wazi alionekana anaamka alfajiri ili kupika vyakula vyote vile. Alikuwa amebadilika kama sio yeye mama G. Alirudi kuwa msichana. Mwili ulipungua sana. Nanaa aliona, lakini hakuwa na muda wa mazungumzo ya ziada, zaidi ya kuomba msaada na kupokea kile anachopewa. Alitaka akili zitulie ili amalize mitihani yake, basi. Sio kuanzisha stori za zamani. 

“Wewe ndio unatakiwa kulala Nanaa. Upumzishe huo mgongo.” “Nina mtihani wa mwisho kesho. Lazima nisome. Nitapumzika baadaye. Wewe lala kidogo. Najua umechoka.” Mama G akajilaza kitanda cha mwenzake Nanaa, akalala muda huo huo. Alikuwa na uchovu wa kuamka asubihi asubuhi.

Nanaa aliendelea kusoma bila yakusemeshana chochote na Geb. Liv naye alilala kama masaa manne tena ndipo akaamka. Nanaa alimchukua, akamuangalia diaper yake, akambadilisha na nguo, ndipo akaanza kumnyonyesha tena. Walikaa pale mpaka usiku. Kama kawaida Mama G akachukua vyombo na nguo chafu, akaondoka, akamuacha Geb pale amembemba mtoto wake huku amemfunika ili asing’atwe na mbu. Nanaa alishangaa usiku unazidi kwenda lakini Geb haondoki pale na wala haongei chochote. 

Yeye akapanda kitandani akalala wakati Geb yupo na mtoto. Alimuamsha mara mbili kunyonyesha na kila alipomaliza kumnyonyesha mtoto, yeye Geb alimchukua huyo mtoto na kumrudisha kifuani. Mpaka asubuhi mama yake alipokuja, ndipo na yeye Geb akaondoka.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Nanaa alipumua kwa nguvu. “Kwa nini umenigeuka mama jamani!? Nilikwambia usimwambie mtu!” “Mungu wangu ni shahidi Nanaa, Geb amenifuata bila ya mimi kujua. Nimesikia mlango unagongwa mara tu ulipotoka hapa jana. Nikadhani ni wewe unarudi labda umesahau kitu, kumbe ni yeye. Amenikasirikia hataki kuniongelesha. Nimejaribu kumuelezea kuwa nilikuwa nafuata matakwa yako kuwa nisimwambie mtu, lakini hajanijibu. Amenikasirikia sana.” “Pole na samahani mama. Lakini leo ndio mwisho. Nikitoka kwenye huu mtihani utakuwa huru, nitamlea mwanangu mwenyewe. Kwenye saa kumi nitakuwa nimemaliza na wewe uwahi kurudi nyumbani.” Mama G, akanyamaza.

Nanaa akala nakurudi kujisomea mpaka kwenye saa sita, Geb akarudi na mashine ya kukamulia maziwa, akaweka mezani bila ya kumsemesha mtu. Mama yake akaichukua, aliposoma akamkabidhi Nanaa. Ilikuwa nzuri na ya kisasa yenye chupa zake kabisa ya kuhifadhia maziwa. Ilikuwa na cooler box yake, ya kutunzia hayo maziwa yasiharibike. Nanaa akakamua maziwa yake. Kwa kuwa alikuwa na maziwa mengi, akafanikiwa kujaza hizo chupa zote alizokuwa ameletewa na kuzihifadhi ndani ya hiyo cooler boksi. Muda wakwenda kwenye mtihani wa mwisho ulipofika, akaondoka na kumuacha Geb amembeba mwanae.

Shilingi Yapinduka…

Kumbe Geb alirudi na kiti cha gari chakumuweka mtoto. Car seat. Nanaa alipotoka tu kwenda kwenye mitihani, Geb naye akakusanya vitu vya mtoto wake na maziwa aliyoyaacha Nanaa, akataka kutoka. “Unaenda wapi na mtoto? Naomba usiondoke na huyo mtoto, Geb. Nanaa atachanganyikiwa. Huyo mtoto ni roho yake! Anazungumza naye usiku kucha. Tafadhali usimchukue huyo mtoto.” “Mwambie sasa hivi ni zamu yangu. Alishakaa na mtoto wangu miezi 9 tumboni bila kuniambia. Akamzaa pia hakuniambia. Mwambie sasa hivi na mimi ni zamu yangu. Nitamtafuta baada ya miezi 9, ndipo tutajua hatima ya mtoto.” “Huyo mtoto ni mdogo sana Geb. Bado anamuhitaji mama yake kwa maziwa. Ananyonya. Acha ukorofi kama baba yako.” Geb akatoka bila kuongeza neno.

~~~~~~~~~~~~~~

Nanaa alitoka kwenye chumba cha mtihani akiwa anafuraha zote. “Sasa hivi unaweza kwenda mama yangu. Nakushukuru sana kwa msaada wako.” Akashangaa Mama G, ameinamisha kichwa. Nanaa akaangalia kitandani. “Mtoto wangu yuko wapi, mama?” “Geb amemchukua.” “Unamaanisha nini!?” Nanaa alishaanza kulia kweni alielewa lakini alikataliana na alichokielewa. “Anasema ulikaa na mtoto wake miezi 9 tumboni bila kumwambia, ukamzaa pia hukumwambia. Amesema atakutafuta baada ya miezi 9 ya kukaa na huyo mtoto kama wewe.” Nanaa alikaa chini nakuanza kulia. “Namtaka mtoto wangu, mama! Mpigie simu Geb.” “Hapokei.” “Naomba nipeleke nyumbani kwake.” Wakatoka huku Nanaa akilia sana.

Mtakuja!

W

akafika getini mlinzi akawaambia Geb amesema asimfungulie mtu yeyote geti. Mama yake akamwambia aende akamwite Geb, amwambie mama yake yupo getini. Geb akasema geti lifunguliwe. Nanaa na Mama G, wakaingia. Wakamkuta Geb yupo sebuleni. “Namtaka mtoto wangu Geb.” Nana aliendelea kulia. “Mtoto yupo amelala. Na hapa ni nyumbani kwao, amelala. Unakaribishwa kumpa huduma zote unazotaka kumpa mtoto wangu, lakini hapahapa ndani. Unaruhusiwa kutoka na kuingia utakavyo, ila mwisho ni saa kumi na mbili jioni. Ukizidi huo muda haujarudi, ujue utalala nje. Na hutaruhusiwa kutoka na mtoto wangu.” Geb alimbadilikia Nanaa kama sio yeye.

“Huwezi kufanya hivyo Geb!” “Basi subiri baada ya miezi 9, ndipo na mimi nitakutafuta tuzungumzie hatima ya huyu mtoto inakuaje. Sasa hivi na mimi nalipizia muda wote uliokaa na mwanangu bila kuniambia. Ukikubaliana na hayo masharti nakukaribisha uishi hapa ili kumuhudumia mtoto.” Geb akaingia chumbani alikokuwa mtoto na kumuacha Nanaa akilia palepale na mama yake yupo kimya.

Baada ya muda walimsikia mtoto ameamka, Geb anambembeleza. Nanaa akamuomba Mama G khanga. Akamtolea khanga na vitenge, akaingia bafuni kuoga ndipo akaingia chumbani kwa Geb. Alitaka kumchukua yule mtoto atoke naye, Geb akamkataza. “Nimekwambia huyu mtoto hapa ndio amefika.” “Nataka kwenda kumnyonyesha.” “Nimekwambia unakaribishwa kumuhudumia humu humu ndani kama utaweza. Kama huwezi, basi. Lakini hatatoka humu chumbani. Ninayo maziwa yakumtosha mtoto wangu. Na yakiniishia, nitaenda kumnunulia. Kwa hiyo kama unahitaji muda wa kwenda kufikiria, mlango uko wazi. Ila ikifika saa kumi na mbili kamili jioni, ujue hutaruhusiwa kurudi, mpaka tena kesho.” Nana alitamani kuchanganyikiwa. Alikaa kwenye kochi pembeni ya kitanda, akaanza  kumnyonyesha mtoto wake. Mtoto alitulia akaanza kunyonya, lakini Nanaa aliendelea kulia kwa kwikwi.

Alipomaliza kunyonya Geb akamchukua akamuweka begani ili ateuke. “Unakaribishwa kitandani kulala.” Geb aliendelea kumbembeleza mtoto wake huku akimwambia Nanaa. “Sina shida. Wanawake zako unalala nao hapohapo. Halafu unataka mimi na mtoto wangu pia tuje kulala hapohapo ulipokuwa ukilala na wanawake zako! Uchafu wa namna gani huo? Humthamini hata mtoto!” Nanaa aliendelea kulia. Geb akanyamaza kimya, mtoto alipotoa mlio kama ametoa hewa, akamrudisha mtoto kwa Nanaa, akatoka.

Baada ya muda akarudi. “Usiku wa leo mtalala kule kwenye chumba chako. Nimeshawatayarishia. Kesho nitaenda kununua kitanda kingine, nitakuja kumchukua mtoto.” Nanaa akasimama na mtoto wake akatoka huku akilia.

Alipoingia tu kule chumbani Mama G, naye akaingia. “Naomba utulie Nanaa. Sio vizuri unavyolia huku umebeba mtoto. Unamtia simanzi huyo malaika wa Mungu asiye na hatia. Huyo mtoto anahitaji mapenzi yako sana. Naomba utulie ulee mtoto wako.” “Sio humu ndani, mama.” “Unataka kwenda wapi? Maana pale hosteli chuo kikifungwa mtatakiwa kuondoka, utaenda wapi na mtoto mdogo hivyo?” “Nina pesa ya kukodisha chumba.” “Ulishapata hicho chumba?” Nanaa akashindwa kujibu akaendelea kulia.

“Eti Nanaa?” “Nitapata tu mama.” “Basi mimi naomba utulie mpaka utakapo weka sawa mambo yako ndio ufikirie chakufanya. Lakini sasa hivi naomba utulie na mtoto. Pata muda wakupumzika, jilaze hapo kitandani na mtoto wako.” Nanaa alipanda kitandani na mtoto wake huku akilia kwa uchungu. Akamkumbatia kwa upendo huku akiendelea kulia mpaka akapitiwa na usingizi.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Aliamshwa na Mama G akitaka ale. “Sisikii kula mama.” “Lazima ule. Lasivyo hayo maziwa yatakauka yote, halafu mwanao atateseka. Kwanza umelowa. Kaa uyakamue, tumuamshe na Liv anyonye.” “Mmemuita mwanangu jina gani!?” Kumbe Geb alikuwa amekaa pembeni. “Nanaa alinipa ruhusa kumpa jina lolote ninalotaka, ndio nikampa la kwangu. Olivia. Lakini mama yake analifupisha anamwita Liv. Ila kama hujapenda, unaweza kumpa jingine unalotaka wewe.” “Mimi, mama yake nimelipenda hilo la Olivia. Ataitwa Olivia sitaki jina jingine.” Geb akacheka, akasimama. Akamsogelea mtoto wake akamchukua pale kwa mama yake, akaanza kumuangalia tena.

“Mtoto amefanana na mimi huyu! Mpaka raha.” Geb akajisifia. “Wala hajafanana na wewe kitu chochote! Kwanza nashangaa kwa nini unafikiri ni mtoto wako.” “Haya macho ni alama ya kwanza na ya pekee. Muulize mama, hata baba yetu alishindwa kutukana tulipozaliwa. Fili mwenyewe alizaliwa na haya macho, hayaepukiki na hakuna mwenye haya macho. Utazunguka sana, utagundua ni sisi tu ndio tuna haya macho.  Haya hilo moja, na kubwa na la kwanza. Kingine hii nywele ni yangu kabisaa! Halafu mrefu kama mimi. Sasa kama kuna uliyemdanganya huko, ataandika maumivu. Huyu mtoto hapa amefika kwao. Hataishi kwengine ila humu ndani. Sasa huyo baba mwingine uliyemdanganya umemzalia mtoto, mtafutie stori nyingine.” Nanaa akaanza kulia tena.

“Hivi wewe Geb umechanganyikiwa lakini? Kwa hiyo unaona raha hivyo Nanaa anavyolia huku ananyonyesha?” “Kwani mimi nimesema jambo gani baya? Nimemwambia ukweli unaomuuma. Hapo analia kwa kuwa amedanganya huko nje. Sasa ananikasirikia mimi kwa kumchukua mtoto wangu, hana mtoto mwingine wakwenda kumuuza. Hii ni damu yangu, hakuna mtu wakuifanyia biashara. Hata kama na wewe mama ulishiriki kunificha, lakini damu yangu ilinililia mpaka nikaipata.” Nanaa akaendelea kulia. 

“Sasa atanyonyeshaje mtoto akiwa analia hivyo?” “Mimi sina shida. Akishindwa kunyonyesha, nampa mwanangu maziwa ya kopo. Kwani yeye ndio atakuwa mtoto wa kwanza kukuzwa na maziwa ya kopo? Eti Liv wangu? Twende tukatafute maziwa unywe.” Geb akataka kutoka. Nanaa akasimama kwa haraka akamkimbilia Geb kabla hajatoka mlangoni. “Namuomba mwanangu Geb!” Mama G, akatafuta mahali akakaa vizuri kujiangalizia. “Wala usivunje mguu. Ukitaka kumnyonyesha mnyonyeshe tu, ukishindwa pia hamna shida.” Nanaa akamchukua mtoto akarudi kukaa kitandani na kuanza kunyonyesha.

Mama G alijua wazi Geb amemkasirikia sana hataki kumsemesha wala kumsikiliza, akaamua kunyamaza. Baada ya kunyonya, Mama G akamchukua Liv, akamteusha. Akambadili nguo akataka kumuweka kitandani alale. “Namuomba mtoto wangu.” “Utamfanya huyo mtoto azoee mikono, Geb! Atakuwa anataka kushikwa muda wote.” “Kuna tatizo gani? Mbona alikaa tumboni kwa mama yake miezi 9 bila shida? Kitakachotushinda kumshika sasa hivi ni nini? Namuomba nimshike mtoto wangu. Tena ndio vizuri azoee mikono yangu.” Mama G akamnyanyua pale kitandani, Geb akampokea, akamuweka kifuani kwake, akajiegemeza vizuri kwenye kochi, akamfunika Liv, akatulia. “Naomba na wewe ukaoge, ule ulale, ili upumzishe huo mgongo.” Mama G, alibaki akiongea na Nanaa.

Nanaa alimaliza kila kitu akapanda kitandani. “Namuomba mtoto nilale naye.” Geb akafungua macho akamtazama Nanaa. “Nimesema namuomba mtoto wangu, ni lale naye.” “Sasa hivi ni zamu yangu na mimi. Ulilala na huyu mtoto miezi 9, tena kwa siri, bila kuniambia baba yake ili uwe huru kufanya unayoyataka. Sijui amezaliwa wapi! Sijui alikuwa akilishwa nini na nani kwa miezi yote hiyo 9! Sijui alikuwa akishikwa au ulikuwa ukilala na nani wakati mtoto wangu alipokuwa tumboni! Uliamua kunificha mtoto wangu, kwa sababu unazozijua wewe. Sasa na mimi ni zamu yangu. Nitafanya kile ninachotaka na mtoto wangu, tena bila mtu yeyote kuniingilia. Unaona huwezi, mlango huo hapo, ondoka.” Mama G, akasimama akaondoka kwenda chumbani kwake kulala. Nanaa akajirudisha kitandani kulala.

~~~~~~~~~~~~~~~~

Kwa kuwa alikuwa amekamua maziwa mengi, ameweka kwenye friji, wakati mwingine alipoamka usiku akitaka kumnyonyesha, Geb alimwambia alishamnywesha maziwa. Nanaa alikuwa anahasira asijue afanyaje. Geb alimuonyesha wazi hamuhitaji yeye mle ndani. Asijue amemkasirikia kwa kutomwambia ni mjamzito au maneno aliyomwambia mara ya mwisho wakati anaondoka huku Geb akimsihi abaki! Nanaa aliondoka humo ndani kwa jeuri sana, akimtamkia wazi Geb ni ukurasa uliopita kwenye maisha yake, na hana shida naye tena, anakwenda kuanza ukurasa mpya na wanaume wengine. Alimuacha Geb amesimama nje na boxer tu, akaondoka huku akimbembeleza.

Mbio Za Sakafuni.

N

anaa aliamka asubuhi ya saa 11, akakuta amewekewa mtoto wake pembeni. Akakaa vizuri kuangaza macho kulia na kushoto, akajikuta yupo peke yake. Akavaa harakaharaka, akamvalisha na mtoto wake vizuri, akamfunika na vitambaa vingi ili asiingiwe na baridi, akatoka pale chumbani huku akinyata. Nyumba ilikuwa imetulia kabisa kuashiria watu wote walikuwa wamelala. Akasogea mpaka sebuleni, hakukuta mtu. Akajaribu kufungua mlango wa ndani kwa kutumia funguo zilizokuwa zimening’inia hapo mlangoni, zikafungua bila shida. Akafungua mlango wa pili wa barazani na geti dogo nje ya mlango wa barazani, na wenyewe ukafunguka bila shida. Nanaa alikuwa akitetemeka kwa hofu. Alivuta pumzi, akaangalia tena ndani akakuta kumetulia. Ndipo akatoka kwa haraka kukimbilia getini.

Alipofika tu getini, alipokelewa na walinzi wawili. “Unaenda wapi?” Nanaa alibabaika kidogo, akajikaza. “Namuwahisha mtoto hospitalini. Naomba utupishe.” “Bosi mwenyewe anafahamu? Maana amesema huyo mtoto akiwa ndani, sisi tutakuwa nje, lakini huyo mtoto akiwa tu nje bila idhini yake, basi sisi tutakuwa ndani. Sasa je, anafahamu kuwa huyo mtoto anatoka?” Nanaa alinyamaza na kuanza kulia. Mmoja akaenda kumgongea Geb dirishani, Geb akatoka. Nanaa alikuwa amekamatwa, amewekwa kwenye kibanda cha walinzi.

Alimsikia yule mlinzi akizungumza na Geb, “Tumemuweka chini ya ulinzi.” Hakusikia Geb akijibu kitu, kumbe alikuwa akimfuata pale getini. Alienda kumchukua mtoto wake pale alipokuwa amekaa Nanaa, akaondoka na kumuacha Nanaa pale chini akilia sana. Aliingia ndani akafunga milango yote kwa ndani. Nanaa alinyanyuka kurudi ndani, akakuta amefungiwa. Alihisi anaota. Alilia kwa sauti kama amechinjwa. “Geb! Namtaka mtoto wangu. Geb fungua mlango.” Nanaa aliendelea kulia, 

~~~~~~~~~~~~~~~~

Haya Tena, Geb & Nanaa. Sasa Hivi Ameongezeka Mtoto Wakiwa Hawapo Kwenye Maelewano. Geb Anadai Mtoto Wake, Nanaa Naye Anamtaka Mtoto Wake. Lakini Mwenye Kisu Kikali….

Nanaa Amefungiwa Nje, Mtoto Ndani. Hatima Yao Ni Nini? Geb Asiyejua Kuzungumza Ila Hasira Tu, Tena Safari Hii Hasira Ya Kukataliwa Penzi Alilokuwa Akilisubiri Tokea Anasoma Sekondari.

  Itakuaje? 

CONVERSATION

0 Comments:

Post a Comment