Siku ya jumanne asubuhi sana kama saa
11, Geb akarudi tena pale CRDB kuzungumza tena na yule mlinzi kabla hajatoka
kazini. Akamuomba simu yake. Akakuta alifuta namba zote zilizotoka kwenye simu
yake siku ya jumamosi. Hakukata tamaa. Akamwambia atamlipa pesa, kama atakubali
kuongozana naye mpaka kwenye kampuni ya simu awaombe wampe historia yote ya
simu yake. Namba zilizotoka siku ile, muda wa karibia na muda Geb alipokuta
Missed call, kutoka kwenye simu ile ya yule askari. Yule askari akakubali bila
shida. Wakaongozana mpaka kampuni ya simu. Akaombwa kitambulisho, kuhakikisha
yeye ndio mmiliki wa ile namba.
Akapewa namba mbili tu kwa muda ule
alioonyesha Geb. Muhudumu wa hapo akawaambia ndizo zilizotoka usiku ule.
Akaziandika, akamkabidhi yule askari. Yule askari akachukua kile kikaratasi
akamkabidhi Geb. Ilikuwa namba yake Geb na nyingine hakuwa akiifahamu. Geb
akamlipa yule askari, akamshukuru wakaagana.
Atafutaye Hachoki.
Geb akarudi kwenye gari ili kupiga ile
simu. Iliita mara kadhaa ndipo ikapokelewa na lafudhi nzito ya kichaga. Geb
akasalimia na kumuuliza kama anamfahamu Nanaa. Antii akamwambia kwa wakati huo
yeye ndio ametoka TMJ alipolazwa Nanaa, hali yake sio nzuri. Alisema alikwenda
kumpelekea uji asubuhi hiyo lakini Nanaa alishindwa kabisa kula. Ameacha ndio
wanamuongezea dripu ya maji. Kwani hajawahi kuingiza kitu mdomoni tokea afike
hapo.
Geb alitoa gari pale huku akimpigia
simu James kumtaarifu habari za Nanaa. Akampigia na Danny. Wakati Geb anaingia
TMJ hospital yupo mapokezi, Danny na James nao wanaingia pale hospitalini. Kwa
kuwa Danny na James walikuwa wakifanya ofisi moja, waliongozana. Pale mapokezi
kulikuwa kumejaa sana muda ule wa asubuhi na muhudumu alikuwa mmoja. Walikaa
pale, mwishowe wakaamua kumpigia tena Antii kuuliza alipolazwa Nanaa. Antii
akawaelekeza. Baada ya muda kidogo, akaingia Grace na Mama G.
Wakaongozana mpaka alipo Nanaa.
Wakakuta amelala huku amezungushiwa mashine kila pande. Kila mtu akashituka.
Daktari akaingia wakauliza kulikoni. Akawaambia aliletwa hawezi kupumua kabisa
na anavichomi vikali sana. Aliwekewa oxygen kwa matumaini ya kumsaidia kuhema
kwa muda, huku wakidhani ni pumu, lakini asubuhi yake Nanaa alianza kupandisha
homa. Wakajua ni pneumonia.
Akaendelea kueleza kuwa, Nanaa ameanzishia matibabu ya hiyo Pneumonia siku iliyopita, lakini
hapakuwa na nafuu. Wanamwangalia siku hiyo, kama bado hali itakuwa ni hiyo hiyo
itabidi juhudi za kupasuliwa na kufyonzwa maji yaliyopo kwenye mapafu,
yanayosababisha homa hiyo kali ifanyike. Ili maji hayo yatolewe kabisa.
James alibaki kimya akimwangalia dada
yake akiwa amelala pale kitandani. “Umejaribu kuzungumza naye?” “Hawezi
kupumua. Kwa hiyo tunamwacha apumzike. Ili asitumie nguvu chache alizonazo.
Anaonekana ana maji mengi kwenye mapafu. Hana nguvu.” Geb akamsogelea akamshika
mkono. Ilikuwa ya baridi sana. “Nafikiri anasikia baridi. Naomba afunikwe.”
“Walimpunguzia mashuka sababu ya homa. Ilikuwa juu sana.” Geb akaanza kusugua
viganja vya Nanaa huku akivipulizia ili vipate joto. Akapandisha shuka
lililokuwa kiunoni mpaka shingoni. Wakabaki wote wameduaa. “Mkihitaji kitu
chochote, mtatuambia.” Daktari akaaga. “Asante sana.” James akashukuru.
~~~~~~~~~~~~~~~
“Yaani mimi huwa nasema, kama kuna mkosi humu
duniani, au bahati mbaya, basi dada yangu huyu amepata! Namuona anavyojitoaga
kwa watu. Anajituma, upendo kwa watu, lakini wote wanamtendea unyama! Hajawahi
kupata mtu au watu wakampa kipaumbele. Wakati wote huwa anapewa nafasi ya mwisho.
Sijui ni kwa nini?” James akalalamika. “Nyinyi mpo pale. Watu wazima watatu,
kweli jamani mnashinda kumjali mtu kama Nanaa! Hamkuwahi hata kuhisi kama ni
mgonjwa?” “Nanaa alikuwa mzima kabisa James. Yaani alianza kulalamika baridi
tulipokuwa njiani kuelekea pale Mlimani City. Akasema anasikia baridi kali
mpaka kwenye mifupa.” Mama G, alijibu kinyonge kama kutetea, kumbe ndio
anaharibu.
“Na bado ukamuacha nje!?” James
akauliza kwa kulaumu. “Mmemtoa nyumbani, mkaenda kumtupa pale Mlimani City!
Mnawezaje kumfanyia unyama kama huo?” “Nikupitiwa James. Mambo yalikuwa mengi
pale.” “Usiniudhi zaidi ya hivi, Danny. Kwa hiyo mnachoniambia sasa hivi ni
kuwa, baada ya mambo yenu mengi kuisha ndio anakuja Nanaa!? Nilipowaona pale
ukumbini vile mnavyosherehekea, nikajua mmeamua kumuacha nyumbani! Kumbe
mnakula na kunywa, wakati mmemuacha dada yangu nje! Tena bila kujali!? Nyinyi
ni binadamu wa namna gani jamani?” James alikuwa akitetemeka. Wasijue ni hasira
au hofu. Maana dada yake alikuwa mahututi pale. Taarifa alizopewa ni kuwa
hawezi hata kuhema na ana maji kwenye mapafu.
“Naomba unisamehe James. Nisamehe
mwanangu. Sijui nilipitiwa kivipi baba. Lakini muda wote akili yangu ilikuwa
inaniambia Nanaa yupo ndani ukumbini. Kwani nilishamuaga kuwa mimi nitakaa meza
ya wazazi, yeye akasema atakaa nyuma kabisa. Miguu inauma baba. Hata chakula si
uliona Grace ndiye aliyeniletea? Naomba radhi James mwanangu. Nisamehe baba.
Lakini nampenda sana Nanaa. Na yeye anajua.” James akatoka nje, baada yakuona
machozi yanamtoka.
~~~~~~~~~~~~~~~
Zilipita siku tano bado Nanaa anahema
kwa mashine na bado homa ipo juu. Daktari akamshauri James akubali wajaribu
kumfanyia upasuaji kufyozwa maji. Ilikuwa ni uwamuzi mgumu tena wa hatari,
lakini ilibidi James akubali kusaini makaratasi ya upasuaji kwani hali ya Nanaa
ilizidi kuwa mbaya. Kuachwa bila upasuaji ilionyesha infection itazidi kusambaa na kuziba kabisa njia ya upumuaji.
Ilikuwa lazima apasuliwe asafishwe, japo hali yake ilikuwa dhaifu sana. Kwa
hali yake ilivyokuwa, kuingizwa chumba cha upasuaji kulikuwa na hatari
yakutotoka hai.
“Kwa hiyo mmesema vyote ni hatari?”
James akauliza tena kabla ya kusaini. “Upasuaji ni hatari na kuachwa hivyo pia
ni hatari. Lakini angalau kupasuliwa kunaweza kuokoa maisha yake kama atatoka
salama.” James aliomba tena dakika kumi za kufikiria kabla ya kusaini.
Alizunguka na yale makaratasi huku akijiambia ni kama anaweka saini ya kifo kwa
dada yake. Alikuwa kama amechanganyikiwa.
Alirudi kuuliza tena na tena, huku
rafiki zake wakimwangalia nakushindwa chakufanya. Hakuna aliyeweza kufanya kazi
siku nzima. Walikuwa wakipokezana kwenda kukaa na James pale hospitalini.
Daktari alimlazimisha kutoa maamuzi, kwani alimwambia kadiri wanavyochelewa
kumpasua, ndivyo nafasi ya kumtoa Nanaa hai huko chumba cha upasuaji, zinazidi
kupungua. Ndipo ikabidi James aweke saini kuidhinisha upasuaji huo, akiwa
ameelewa madhara yote.
Taarifa kwa marafiki wa karibu wa James
na wake zao zilishaenea kila mahali. Wakawa wakifika pale hospitalini, watu
mbali mbali kumtizama Nanaa ambaye
alikuwa hajaweza kuzungumza hata kidogo, muda wote alikuwa amelala. Geb
alishindwa hata kufanya kazi. Hakuonekana ofisini kwake, BOT wala kwenye
biashara zake. Muda wote alikuwa hospitalini na James. Angalau James alikuwa
akitoka mchana na kwenda kuchungulia ofisini, lakini sio Geb. Hakuzungumza
chochote kile. Si kumlaumu mama yake wala kuomba msamaha kwa James. Alikuwa
kimya muda wote. Alikuwa akiingia na kukaa akimtizama Nanaa tu huku ameshika
viganja vyake wakati wote.
Nanaa afanyiwa upasuaji.
Siku Nanaa anaingizwa chumba cha
upasuaji marafiki wote waliokuwepo kwenye harusi, mpaka Malii na mkewe
walikuwepo hapo kusubiria kama Nanaa atatoka hai. James alikuwa akizunguka huku
akisikika akivuta pumzi nakuzishusha kwa nguvu mara kwa mara kama kutoa wasiwasi
kifuani. Grace na mama yake walikuwa kimya tu. Hamna aliyemsemesha mwenzake.
Kadiri muda ulivyozidi kwenda, dada yake akiwa chumba cha upasuaji, ndivyo hali
ya James ilivyokuwa ikizidi kuwa mbaya. Mikono ilikuwa kichwani wakati wote
akitembea huku akiliita jina la Yesu amsaidie. Alitia wasiwasi kila mtu
aliyekuwepo pale.
Baada ya muda daktari
akatoka na kumwambia James mambo yamekwenda vizuri. Hapakuwa na madhara mengi.
Na wanaamini kama ataendelea hivyo, Nanaa atapona tu. Ndipo James alipoanza
kulia huku ameweka mikono kichwani. Akainama huku ameshikilia magoti yake. “Uuuuu!
Uwuuuuu!” Alisikika kijana huyo
wa kichaga, James akivuta pumzi huku akilia kwa sauti ya chini. “Asante Mungu wangu. Hata sasa hujatuacha. Asante.” James
aliendelea, akapiga magoti huku machozi yakimtoka.
~~~~~~~~~~~~~~~
Baada ya muda kidogo, Nanaa akatolewa chumba cha
upasuaji akiwa kwenye kitanda chake kurudishwa wodini. Bado alikuwa amelala.
Baada ya muda, akashituka. Akafungua macho. Akataka kujigusa usoni, Geb
akamuwahi mkono. “Unamashine ya kupumulia. Usitoe.” Akamwambia taratibu. “Pole.”
Nanaa akafunga macho. James akamsogelea. “Pole Nanaa.” Nanaa akafungua macho.
Akamuangalia kaka yake kwa macho ya usingizi, wakaona machozi yanamtoka. “Pole
sana. Utapona. Umesikia?” James akamshika na yeye mkono wakushoto. Akafunga
macho na kurudi kulala. Daktari aliwaomba watu wote waondoke ili kumuacha
apumzike, mpaka tena baadaye.
~~~~~~~~~~~~~~~
Walipotoka tu nje, James akawaita Geb, Danny,
Grace na mama yao. Akaomba azungumze nao. “Niliwaomba mnisaidie kuishi na Nanaa
kwa muda wakati nikijiweka sawa, ili nimtafutie sehemu ya kuishi. Nashukuru kwa
kumpokea na kumuhifadhi kwa kipindi hicho. Nitakuja kuchukua vitu vyake
nitakapotulia. Naona niendelee naye mimi mwenyewe tu. Naomba kwa sasa mumuache
kabisa.” Kimya.
James akawatizama kwa zamu, akaona
wanamuangalia kama wasioelewa. “Namaanisha hivi, sitaki kuwaona tena hapa
hospitalini. Kwa kuwa tunaheshimiana, naomba mnielewe na msiniudhi zaidi.” “Naomba
utusamehe James. Tafadhali sana.” Grace alijaribu kabla James hajaondoka.
James
akarudi na kumgeukia Grace. “Unakumbuka niliwaambia nini tulipokuwa Marangu?” Kimya.
“Mmemuona mama yangu mzazi hapa?” Kimya. Hakuna aliyethubutu kujibu. “Mama yupo
hapa Dar, hajarudi Moshi. Lakini hata yeye nimemkataza kufika hapa. Na ninaomba
mnielewe na msirudi tena jamani. Urafiki wenu upo na mimi tu. Hilo mmeliweka
wazi, na mimi ninaliheshimu. Narudia, Nanaa ni jukumu langu. Nitamlinda dada
yangu na kila hatari, hata ikibidi mama yangu mzazi. Mlishindwa kuishi na Nanaa
akiwa mzima, msikae hapa kumkejeli dada yangu na kudanganya uma. Naombeni
muondoke kabla sijakasirika zaidi.” James akarudi chumba alicholazwa Nanaa.
~~~~~~~~~~~~~~~
Alikaa
hospitalini akiwa analala tu kwa muda wa siku tatu mbele baada ya upasuaji,
homa ikashuka. Akaanza kuhema bila mashine. Kwa siku hizo nane tu, tayari Nanaa
alionyesha amedhoofu mpaka usoni. Kwa kuwa mapafu yalikuwa yakimuuma,
akaendelea kupewa chakula kwa mrija. Antii alikuwa akijituma sana. Hakuacha
kumletea vyakula vya kusagwa. Alionyesha yeye ndio muhusika haswa wa Nanaa. Alikaa
siku 15 hospitalini ndipo akaruhusiwa. Antii alionyesha utayari wa kuendelea kuishi
naye nyumbani kwake. Alimuahidi James kujitahidi kumlisha ili arudishe mwili.
Alitoka
pale sauti haitoki kabisa. Mpaka usikilize sana ndipo ungeweza kumsikia.
Alirudi nyumbani kwa Antii, moja kwa moja akaingizwa chumbani, akalala. Alilala
akaamshwa na ndoto ambayo ilikuwa siku ya harusi ya Malii. Kumbukumbu
zilimchukua mpaka vile Geb alivyokuwa anaingia na Liz ukumbini. Akashituka. Akamuona
Geb amekaa pale pale chumbani. Akamtizama kwa muda mrefu kama akijaribu kujua
kama ni ndoto au ni kweli anamuona Geb. Kwanza ilikuwa usiku sana. “Pole
Nanaa.” “Asante.” Nanaa alijibu kwa sauti ya chini sana. Akaanza kutokwa na
machozi. Geb alivuta shuka, akamfunika tena vizuri. “Pole sana.” Nanaa akarudi
kulala asijue kama bado anaota au ni kweli!
Alipoamka,
Geb hakuwepo, akajua ilikuwa ndoto tu. Antii akaingia na chakula akimtaka kula.
Akajitahidi, lakini akashindwa. Zilipita siku nyingine 7, ndipo Nanaa aliweza
kujaribu kukaa na kuweza. Alikondo, akawa kama katoto. Alipokuja James, akamuomba
ampeleke Tabata, nyumbani kwa Geb, akachukue mizigo yake. Chuo kilikuwa kimeshafunguliwa.
Wenzake walishafanya usajili, lakini Nanaa bado alikuwa amedhoofu sana hakuweza
kwenda.
Kulikoungua
Mpini, Kukabaki Shoka.
Baada ya kazi siku hiyo ya ijumaa, James
alimfuata Nanaa na kumrudisha Tabata, nyumbani kwa Geb. Bado sauti haikuwa
ikitoka, na bado mwili ulikuwa unachoka sana. Mpaka wanaingia ndani ya geti
nyumbani kwa Geb, Nanaa hakuwa hata na habari! Alishakuwa amelala muda mrefu
sana tokea hata James hajaondoa gari pale nyumbani kwa Antii. James akaenda
upande wake. Akamuamsha kwa muda mrefu ndipo akaamka.
Akatembea
taratibu mpaka mlango wa kuingilia ndani. Kaka yake akamfungulia, akabaki
ameshikilia ule mlango, ili Nanaa aingie. Akaweza kupanda ngazi kwa shida,
akaingia mpaka ndani. Akaenda kukaa moja kwa moja kwenye kochi.
“Vipi mama?” Mama G, akamuuliza. Kwani aliwakuta
wote wapo sebuleni. James alishawaambia angemleta kuchukua vitu vyake. “Pole.”
“Asante, mama.” Nanaa akajibu kwa sauti iliyosikika kwa mbali sana,
akajiegemeza kichwa kwenye kochi akafunga macho.
“Unakula
vizuri?” Grace akamuuuliza. “Najitahidi lakini mwili hauna nguvu, naona na sauti
imekataa kutoka!” Nanaa akajibu huku amefunga macho na kichwa bado amekilaza
kwenye kona ya kochi. “Pole sana Nanaa. Kazana kula utapata tu nguvu.” Akatingisha
kichwa kukubali, akatulia. “Tukuletee chakula?” Mama G, akauliza kwa upendo. “Hapana.
Nina maji kwenye gari. Ndio hayo nabembelezana nayo niyamalize. Lakini
nimefuata documents zangu. Nimeweka kwenye kabati. Chuo kimefungua,
nataka niwaombe kina Zena, wanisaidie kunifanyia usajili. Nimechelewa, lakini
nataka nijaribu tu.” Nanaa alikuwa akiongea kwa shida sauti ya chini mpaka
wakazima tv kabisa ili kuweza kumsikia. James alikuwa kimya tu.
“Si
ungeahirisha huu mwaka ili upone kabisa?” Mama G, akatoa wazo. “Hii shule
haijawahi kusubiri mama. Lazima nimalize tu. Nitamaliza tu mama yangu.”
“Tunakuombea Nanaa mwanangu.” “Asante.” Nanaa akashukuru akafunga tena macho. “Nanaa!
Jikaze twende nikakusaidie kukukusanyia vitu.” James akamsogelea dada yake. “Ulipotuambia
unakuja leo kuchukua mizigo yake, tuliikusanya vizuri. Ipo yote kwenye mabegi
na masanduku yake. Kasoro hizo documents. Ngoja nikazitafute. Nitaleta
na mizigo yake yote. Mwache apumzike tu.” Grace akanyanyuka. “Asanteni sana.”
Nanaa akashukuru huku akipandisha miguu kwenye lile kochi dogo alilokuwa
amekalia. Akaikunja miguu yake ndani ya sweta alilokuwa amevaa, akaegemea
kwenye kochi, akalala. Alilala pale pale wakimwangalia.
Hakuwa akisikia kitu chochote kinachoendelea.
Wakapandisha vitu vyake vyote kwenye gari, bila hata Nanaa kujigusa. Wazi
alionekana bado ni mchovu. James akarudi
kumchukua. “Nanaa! Nanaa!” James alimwita, lakini hakuitika. Akaamua
kumtingisha kidogo. “Nanaa!” Akafungua macho. “Vipi?” “Nasikia kuchoka kaka!” “Unalala
mchana lakini?” “Nalala. Hapa nimelala siku nzima, lakini bado mwili umechoka
sana.” “Unataka nikubebe?” James akamuuliza Nanaa, akacheka. “Tutaanguka wote!”
James akacheka. “Siwezi kukuangusha bwana! Kwanza umerudi kuwa kama katoto!
Enzi zileee upo la kwanza. Sijui kama unajua hilo?” Nanaa akacheka. Akatoa
miguu kwenye sweta. “Acha tu nitembee, nijipe mazoezi. Ninalala sana.” Akavaa kandambili
zake alizokuwa amevua wakati anapandisha miguu.
“Geb!” Nanaa akaita, Geb akamwangalia. “Nakushukuru
sana kwa kunipokea.” Geb hakujibu alibaki kimya. “Jamani, nikipata nguvu nitarudi
kuwasalimia. Nashukuru sana kwa kuishi na mimi vizuri na kwa upendo. Nashukuru.
Asanteni.” Grace alibaki ameinama. “Uje kutuona tena Nanaa.” “Nitakuja mama.
Lazima nitakuja. Ngoja nipate nguvu, akili iwe shuleni. Mambo yakikaa sawa,
nitakuja angalau niwasalimie.” “Naomba usiache kurudi kuja kutuona, Nanaa.” “Usijali
mama yangu.” Nanaa akatoka na kaka yake.
Alipompandisha kwenye gari na kumfunga mkanda,
James akarudi ndani. Bado akakuta wenyeji wao wamekaa vile vile kama
alivyowaacha kinyonge. James akaingia na kusimama katikati yao. “Naomba kuweka
msisitizo. Kama mlivyomsikia Nanaa. Shule yake haijawahi kusubiri, na amekataa
isisubiri. Kwa hali mliyomsababishia nyinyi, bado ameamua kurudi tena
shule na kuendelea na masomo yake. Tafadhalini.” James akawaangalia mmoja baada
ya mwingine. “Narudia tena, TAFADHALINI jamani. Mwacheni Nanaa amalize hiyo
shule. Kumuingilia kwa namna yeyote ile, ni kutangaza vita vikali sana
na mimi.” James akatoka bila kutaka kujibiwa.
~~~~~~~~~~~~~~
Alirudi kwa Antii, moja kwa moja akapanda
kitandani akalala. James akataka kumuamsha. “Muache tu alale. Mchana alikula
vizuri. Muache alale. Akiamka nitampa maziwa.” James aliingiza vitu vyote
ndani, akakaa kidogo. Kisha akaondoka akimfikiria dada yake na kumuhurumia sana
asijue amsidie nini tena! Alishamaliza dawa zote alizokuwa ameandikiwa.
Baada ya siku 5 nyingine, aliweza kwenda kwenye
ofisi za utawala kuzungumza nao. Mwezi ulishapita tokea chuo kifungue. Antii
alikuwa amemsindikiza. Akaonyesha vyeti vya hospitalini. Wakaangalia matokeo
yake ya miaka iliyopita, akaruhusiwa aendelee. Yule matron alishamtafutia
chumba hapo hosteli, tokea chuo kinafunguliwa, Nanaa alishakuwa na chumba hapo
hostel. Kwa hiyo hakupata shida. Mbali na yote, alitakiwa pia kuwakilisha
repoti ya field aliyofanya na bado alipambana kusoma kwa kasi ili kufikia
wenzie darasani. Alijitahidi kuchukua notes kutoka kwa wenzake. Mchana
na usiku Nanaa alikuwa busy kusoma. Alishaondoka kwa Antii, akawa anaishi
hosteli.
Nanaa
Arudi Ofisini Kwa Grace
Akatoka siku hiyo mchana, hakuwa na kipindi.
Akaenda ofisini kwa Grace. Alimkuta Grace ofisini kwake. “Nimefurahi kukuona
Nanaa!” “Asante.” “Mwili umegoma kurudi?” Grace alimuuliza, Nanaa akacheka. “Naona
angalau sauti inasikika kidogo.” “Najitahidi.” “Karibu.” “Asante. Nipo kwenye
kutengeneza ripoti yangu ya field. Naomba nisaidie barua ya kuthibitisha kama
nilikuwa hapa na nilimaliza muda wote niliokuwa natakiwa kuwepo hapa.” “Hamna
shida kabisa. Ila na mimi naomba nikuombe kitu kimoja Nanaa.” Nanaa akajiweka
sawa.
“Naomba utusamehe.” Nanaa akajaribu kufikiria. “Tusamehe
kwa chochote kibaya tulichowahi kukutendea.” “Usijali Grace. Mimi nipo tu
sawa.” Nanaa alijibu kiuungwana. “Mbona sasa hujarudi nyumbani? Mama hana raha
Nanaa!” “Ukweli mambo yamekuwa mengi tu. Nimerudi chuoni nimekuta wenzangu wapo
mbali kweli! Imebidi kuanza upya, tena peke yangu. Halafu na vimitihani vya
chuo! Si unaelewa?” “Nakumbuka.” “Lazima nitarudi kuja kuwaona, najitahidi
kupunguza mambo. Nikikaa sawa, nitakuja tu. Naomba mwambie mama asiwe na
wasiwasi hata kidogo. Mimi mwenyewe namkumbuka. Ila akili haijatulia Grace.
Bado napambana na afya yangu na shule. Naomba mtulize mama. Mwambie bado
nampenda tu. Ajiandae nikija nitakuja na mazawadi kibao.” Grace akacheka.
“Nitamwambia.
Naona kidogo atatulia.” “Msalimie na Fili wangu. Na Danny. Wote nawakumbuka.”
“Mnawasiliana na Geb?” Nanaa akatulia kidogo, na kuinama. Uso wake ukabadilika
kabisa, hata Grace akamuona. “Hapana Grace. Hata yeye sijamuona muda mrefu!” “Naomba
na yeye ukiweza umtafute.” “Nakuahidi kufanya hivyo Grace. Acha nijiweke sawa
ili kunusuru hii shule. Ndio mwaka wa mwisho huu. Sitaki chochote kibaya
kitokee nishindwe kumaliza.” “Nimekuelewa Nanaa. Na nitawafikishia nyumbani
salamu zako.” “Hapo umenifurahisha na kunituliza. Mungu atasaidia hili la shule
likiisha, nitakuwa huru.” Baada ya kukamilisha mambo yake yote akaondoka pale
kurudi chuoni.
~~~~~~~~~~~~~~~
Alijitahidi na mambo ya shule, mchana na usiku
akipambana ili kufikia wenzake. Baada ya mwezi mwingine, akajikuta yupo sawa na
wenzie darasani. Tena yeye ndiye alikuwa akifanya vizuri zaidi kwani aliweka
juhudi za ziada ili asipitwe. Kila matokeo ya test na assignments
zake zilipokuwa zikitoka, Nanaa alikuwa na alama za juu sana mpaka akawa
anajishangaa. Hakuwahi kuongoza kwenye darasa lolote. Akabaki akifurahia.
Mambo ya shule yalipokaa sawa, ndipo akili zake
zilipotulia na kuanza hata kujifikiria yeye mwenyewe. Akaenda saluni
kutengeneza nywele na kucha. Kidogo akaanza kurudia hali yake. Miezi miwili na
majuma kadhaa yalishapita tokea apate wakati mzuri na Geb kimapenzi. Kitendo
cha kusahauliwa nje siku ya harusi, kilimuuma sana Nanaa. Hasa akizingatia Geb
alikuwa na Liz! Tena alimshuhudia akiwa amemshika mkono! Nanaa alisema wengine
wote wangeweza kumsahau, lakini si Geb. Zaidi ya masaa 4 hakumuona ukumbini,
asijali na hata alipompigia simu hakupokea!
Nanaa alizidi kuumia na kushindwa kuwatafuta familia ya Geb na Geb mwenyewe.
Hata week ambazo hakuwa na mitihani, aliamua kukaa tu chuoni. Alishindwa kwenda
kuwatembelea kabisa.
Siku zikazidi kwenda, ndipo akagundua hajatumia
pedi kwa muda mrefu. “Mmmh!” Akaguna
baada ya kuwaza. Akajiangalia vizuri
hakuona kitu cha ajabu. Kwa kuwa alikuwa amekonda sana, akajiambia mwili
unarudia hali yake. Akaanza kujiuliza mara ya mwisho kuona siku zake. Akakumbuka
alipata siku zake alipokuwa nyumbani kwa Geb. “Kaaa! Hata kama nimeshika mimba ya Yesu, ingetoka tu. Madawa yote yale
niliyokunywa na operation juu! Hii sio mimba. Mwili umeshituka tu sababu
yakuugua muda mrefu. Ndio maana nimepitisha siku zangu.” Akajifariji huku
moyo wake ukiwa na wasiwasi sana.
Marefu
Yenye Ncha.
Alipoona hofu inazidi, akaona asijitese. Akaenda
duka la madawa kununua kipimo cha kupimia mimba ili kujipunguzia wasiwasi,
ndipo akagundua ni mjamzito. Hofu ilimuingia asijue Geb atapokeaje lile jambo
na yeye ndio alikuwa mwaka wa mwisho. Hakuwahi kuruhusu kitu kiingilie shule
yake. Kama ni mwanaume aliyekuwa akimsumbua na akajua atahatarisha masomo yake,
Nanaa alimuacha bila kufikiria mara mbili. Aliazimia lazima shule yake iwe
mkombozi wake, kwa hiyo hakuruhusu muingiliano wa aina yeyote. Kitendo
chakujigundua ni mjamzito, tena akiwa anamalizia chuo, kilimshitua sana. Zaidi
mimba ya mwanaume ambaye hawajawasilina kwa muda mrefu na alishajua Geb
alirudiana na Liz.
~~~~~~~~~~~~~
Tokea augue, hakutaka kuwasha simu yake. Alipopona
kabisa ndipo alipopata nguvu ya kufungua mizigo yake akiwa hapo hostel.
Akakuta Grace alimfungashia vitu vyote.
Kuanzia laptop mpya aliyokuwa amenunuliwa na Geb. Simu yake mpya pia ilikuwepo.
Nguo zote mpya na zazamani zote zilikuwa kwenye masanduku na mabegi mapya.
Mengine alikumbuka alinunuliwa na Geb, lakini mengine akahisi labda
walimnunulia ili kuhifadhi vizuri vitu vyake. Ulishapita mwezi, hata James
hajamuona. Alishamwambia anahitaji kutuliza mawazo chuoni tu. Kwa hiyo James
akamuacha.
Kwa Geb.
Akaichukua ile simu, akaiwasha. Ujumbe wa Geb
ukaingia. ‘Naomba kukuona Nanaa. Tafadhali. Japo kwa
muda mfupi tu. Geb.’ Wakati anasoma ule ujumbe, simu ya Geb ikaingia. “Haloo?” Nanaa aliitika. “Unaendeleaje?”
“Naendelea vizuri.” “Umepata ujumbe wangu?” Geb akauliza. “Ndio nimewasha simu na wenyewe ukaingia. Sikuwa nimeiwasha
muda mrefu. Nilitaka kutulia chuoni. Nilichelewa sana kuanza chuo. Nikakuta
wenzangu wapo mbali. Ilibidi kutulia ili niwafikie.” “Umefanikiwa?” “Kwa
asilimia kubwa. Lakini mambo ni mengi kweli! Nahitaji kutulia kweli ili hii
shule iishe.” “Pole.” “Asante.” Wakatulia.
“Nanaa!” “Bado nipo.” “Ninahamu sana na wewe.” Nanaa
akaanza kulia. “Naomba unisamehe kwa kukusahau.”
“Nilikuona siku ile ya harusi. Ulikuwa na Liz. Tena
umemshika mkono.” “Hapakuwa na kilichoendelea
zaidi ya kule kumshika mkono, Nanaa!” “Ndio
maana ulinisahau Geb. Unajua nilikaa pale nje zaidi ya masaa manne? Nikimuomba
Mungu angalau uhisi mle ndani sipo, ili utoke uje unikute pale mlangoni.” “Nisamehe Nanaa. Ule utaratibu wa kusimamia harusi ulipangwa
zamani sana. Hapakuwa na jinsi ya kubadilisha. Na wala Liz hakuwa sababu ya
kukusahau. Nilizungumza na Mama, akaniambia umekaa kiti cha nyuma.” “Kama kweli unanijali basi ni kwa nini hukunitafuta kama
ulivyoniahidi? Nilikuwa saluni, wakati unanilazimisha kuja! Nilikuja kwa ajili
yako Geb. Ukaniahidi utanitafuta, hutaniacha peke yangu.” Nanaa akazidi
kulia.
“Naomba niambie ulipo ili nije. Nipo
safarini. Kesho ninarudi nyumbani. Nitakufuata ili tuzungumze vizuri.” Geb alibembeleza. “Hapana Geb. Acha nitulie nimalize hii shule. Nakushukuru
kwa kila kitu.” “Nanaa please! Nakuomba kukuona!”
“Hamna cha kuona tena Geb. Mwili bado
umeisha, hamna tena nyama.” “Sijawahi kukupendea
umbile lako Nanaa! Nilikupenda kabla hata sijakuona!” “Mimi najua kupenda kunaambatana na kujali Geb. Mara zote
umekuwa ukimtanguliza Liz, mimi ninafuata. Unakumbuka Marangu? Nilikuacha ukiwa
unamkumbatia. Kwenye harusi ulikuwa umemkumbatia. Ungekuwa unanijali mimi na
hisia zangu, usingefanya uliyofanya Geb. Hujawahi kunipenda kwa mapenzi ya
kweli. Na nina uhakika ingekuwa mimi ni Liz, usingenisahau nje ya ukumbi.
Hujawahi kufikisha thamani yangu kama ulivyomthamani Liz. Alikuwa akiweza
kunitukana mbele yako, lakini hukuwahi hata kunitetea mbele yake!” “Ukisema hivyo unakosea Nanaa! Nimemuacha Liz, ili niwe na
wewe!” “Ni lini umemuacha Liz, Geb? Maana
mpaka mara ya mwisho nimewashuhudia mmeshikana mikono kama wapenzi. Labda
uniambie utakuja kumuacha kwa ajili yangu. Lakini haukuwahi kumuacha Liz.” “Nanaa, nakupenda wewe.” “Asante,
na kwa heri Geb. Uwe na wakati mzuri, na safari njema wakati unarudi nyumbani.”
“Nanaa!” Nanaa akakata simu huku
akiendelea kulia.
~~~~~~~~~~~~~~~
Alikaa pale akilia. Mishowe akajiambia lazima
ampe mwanae haki ya kuwa na baba. Akajiambia hata kama hatakuwa na mahusiano na
Geb, basi mwanae apate haki ya kuwa na baba. Na lazima Geb ajue mapema, ili
ikitokea anakufa chumba cha kujifungulia, kama mama yake, basi mwanae
achukuliwe na baba yake. Akaazimia kesho yake kwenda nyumbani kwa Geb. Akasoma
kidogo, akalala.
Aliamka asubuhi, akakimbilia maktaba kujisomea
tena, kisha akaendelea na vipindi vingine kama kawaida mpaka ilipofika jioni
akaingia kwenye mtihani. Alitoka kama kwenye saa moja na nusu usiku akiwa
amechoka, lakini akakusudia lazima akamuone Geb wazungumze. Alirudi kwenye
chumba chake, akaacha madaftari akachukua pochi yake, akaondoka kwenda nyumbani
kwa Geb.
Hakuna Msiba Usiokuwa Na Mwenzie.
Kwa kuwa walinzi walishamfahamu, hawakuhitaji
kupiga simu ndani kuuliza kama Nanaa aruhisiwe. Akawasalimia pale getini, akaingia.
Alikuta magari mawili tu. Moja analifahamu ni la Geb, jingine hakuwa
akilifahamu. Akaamua kuingia tu ndani. Alipofika sebuleni hakumkuta mtu.
Wasiwasi ukamwingia. Lakini akahisi labda ni la Geb, amenunua gari nyingine.
Akaamua kumfuata Geb chumbani kwake. Haikuwa kawaida ya Nanaa kuingia chumbani
kwa Geb. Mara chache sana, tena ilikuwa kama ametumwa na Mama G, kwenda kuweka
kitu. Hasa nguo safi. Ile kufungua tu mlango akamkuta Liz yupo uchi kitandani kwa Geb.
Akabaki ametoa macho. Kabla hajakaa sawa, Geb naye akawa anatoka bafuni akiwa
uchi na taulo mkononi anajikausha. Nanaa akawaangalia wote kwa zamu, kisha
akatoka pale chumbani.
“Nanaa!” Alimsikia Geb akimwita. “Nanaa!” Nanaa
akaendelea kutembea. “Nanaa! Naomba simama tuzungumze.” Nanaa akaendelea kutembea.
Akataka kufungua mlango wa kutoka nje kabisa. Pale barazani. “Nanaa! Sio kama
inavyoonekana.” Nanaa akasimama, akamgeukia. “Sio kama inavyoonekana. Naomba
usiondoke. Nisikilize.” “Huo mchezo nimeshachezewa tokea nipo sekondari Geb.
Nina uzoefu nao.” “Mchezo gani!?” “Huo unaoufanya sasa hivi.” “Sio kama inavyoonekana!”
Nanaa akacheka akafungua mlango akatoka.
“Nanaa! Naomba usiondoke.” Geb akakimbilia mbele
yake, Nanaa akasimama. “Nakwenda shule Geb. Kitu ninachokifanya bila kuingiliwa
na mtu, na ndio kitu pekee nilicho nauwezo wa kukitawala na kukiongoza.
Namshukuru Mungu pia nina uwezo wa kukilinda. Hakuna mtu anaweza kuniingilia
kwenye shule yangu. Nilazima niisome na nimalize. Haiuhusiani na mwanaume
yeyote wala hisia zangu. Ni moja ya kitu ambacho nilazima nimalize.” “Nanaa!”
“Mbona sikuelewi Geb!? Nini?” Akampita pembeni na kuanza kuondoka akielekea
getini.
“Sio kama inavyoonekana, naomba usiondoke.” Nana
akamgeukia Geb akasimama vizuri. “Katika
kumbukumbu zako, mara ya kwanza kulala na mimi ulinikuta bikra?” Geb kimya. “Basi
walipita wenzako kama wewe, wengine wenye stori kama zako. Wewe sio wa kwanza.
Kwa kusema hivi, namaanisha nina uzoefu wa hizi habari. Najua utaanzia wapi na
kuishia wapi, ili kunidanganya. Usifikiri umeniumiza Geb, hata kidogo. Wewe ni
ukurasa niliousoma, nimeuelewa, nakufunika, naendelea
na maisha yangu.” Ni kama alimfunga Geb mdomo. Akashindwa ajitetee vipi.
Ila akajikaza kuuliza.“Kwa hiyo unatupilia mbali
kila kitu?” Nanaa akakunja uso. “Ni nini chakutunza kati yetu? Eti Geb? Nini
cha kuweka kumbukumbu? Kama ni mapenzi tulifanya na wewe kama nilivyofanya na
wanaume wengine. Uliridhika na mimi nikaridhika. Sasa hivi unaendelea na
mwanamke wako na mimi ipo siku nitapata mwingine, nitaendelea. Tatizo liko
wapi? Hunidai, sikudai. Nakuruhusu endelea na maisha yako kwa amani, na mimi
naendelea na maisha yangu. Nakushukuru kwa kuniweka nyumbani kwako kwa muda niliohitaji
msaada, basi. SITAKI unitafute, na mimi sitakutafuta.” Geb akabaki kimya,
haamini.
“Huna tofauti na matapeli wengine wote
niliokutana nao maishani mwangu. Tofauti yako wewe ni pesa tu basi. Labda na
good sex. But am sure, one day I will find the BEST one.” “Kwa hiyo hutaki
nikutafute tena?” “Kwa nini unitafute!? Na usifikiri naongea kwa hasira Geb.
Nilitoka kwa Jamal kama hivi ninavyotoka kwako. Nilikusanya vitu vyangu,
nikaondoka bila ugomvi wala maneno mengi, maisha yakaendelea. Nilimuacha na
mkewe, na wewe nakuacha na mwanamke wako. Nikarudi chuoni nikatuliza mawazo,
nikasoma na nikamaliza mwaka wa pili. Ndio na wewe hivyo hivyo. Naomba uniache
nikaendelee na maisha yangu. Hutaniumiza kichwa wala roho yangu.” Nanaa akageuka, kama utani akaondoka. Geb
hakuamini.
~~~~~~~~~~~~~
Alitegemea fujo na kelele. Kulia na lawama,
lakini Nanaa alitoka akionyesha amemdharau na kama hakuwa na hisia zozote juu
yake, kitu kilichomuuma sana Geb. “Yaani
Nanaa alikuwa akinitumia tu? Hakuwa na hisia zozote kwangu!?” Geb alibaki
akiwaza kwa kuumia sana utafikiri yeye ndio amemfumania. Alirudi ndani
akajikuta anapitiliza jikoni badala yakurudi chumbani alipomuacha Liz. Asijue
anafuata nini huko. Akavuta kiti na kukaa hukohuko jikoni. Akiwa amezama
mawazoni wala asijue anayeingia na kutoka, akasikia sauti ya Grace. “Naomba
ukavae nguo Liz. Danny yupo hapo nje anaingia sasa hivi na mtoto. Tafadhali
sana.” “Namtafuta Geb.” “Basi kavae nguo ndio utoke. Huwezi kujiacha uchi mbele
ya mume wangu! Hapo tutakosana! Tafadhali sana.” Geb akatoka.
“Naomba
uondoke Liz.” Geb alikuwa amekasirika sana. Hata Grace alimuona usoni. “Wewe
Geb vipi?” Liz akajilalamisha, hakutaka kuondoka. “Geb na Liz, wote mpo uchi.
Fili na Danny wanaingia sasa hivi. Naomba muingie chumbani kwenu. Tafadhali
sana.” “Sio chumbani kwetu. Ni chumbani kwangu.” “Sijali utakavyopaita, naomba
ingia ndani. Fili hawezi kukuta hapo na boxer.” Grace akambadilikia hata kaka
yake. Geb akaondoka kuingia chumbani kwake, Liz akafuata.
Maisha
Ya Nanaa Shule Na Ujauzito.
Ni kweli kwa Jamal aliondoka na maisha yakaendelea,
lakini sio safari hii, alipokuwa na mtoto wa Geb tumboni. Siku zilizidi kwenda,
akijaribu kujiliwaza, lakini yule mtoto naye alizidi kumkumbusha ukurasa
aliotaka kuufunga. Ulikuwa haufungiki. Kila akicheza, alimkumbusha yeye yupo,
na ni mtoto wa Geb. Mwanaume aliyeacha historia kubwa sana ya mapenzi mwili
mwake, tofauti na wanaume wengine wote. Hakuna siku Geb alishika mwili huo
asimridhishe Nanaa visivyo vya kawaida. Iwe ni katikati ya usiku akiwa amelala,
au siku zile alizomwingilia chumbani kabla hata hajalala. Geb aliutendea haki
mwili wake.
Ndiye mwanaume aliyemuonyesha anahitaji mwili
wake visivyo vya kawaida na kuuthamini. Alimuonyesha mwilini mwake ndiko
anapopata starehe aliyokuwa hata hatarajii! Mambo mengi aliyasimamisha ili tu
kwenda kufaidi mwili huo.
Ndoto akiwa amelala na Geb nazo hazikukawia. Mara
nyingi aliota Geb yupo akichezea kifua chake, au akichora mgongo wake, huku
akimbusu mara kadhaa. Mabusu ya shingoni ndiyo yalikuwa yakimsisimua na kumtoa
usingizini. Alikuwa akishituka na kukaa kitandani kwake, nakubaki akiwaza.
~~~~~~~~~~~~~
Hakutaka kuanza kliniki mapema, mpaka alipomsikia
mtoto wake alipoanza kucheza tumboni, ndipo alipojua nilazima aanze kliniki.
Alianza kliniki katika hospitali ya taifa ya Muhimbili na huku akipambana na
masomo. Mimba haikumsumbua sana ila upungufu wa damu ndio likawa tatizo kubwa
la kumsumbua yeye, lakini si mtoto. Mtoto alikuwa akikua salama bila shida. Akashauriwa
na daktari wake huko kliniki kuongeza kula vyakula vyakuongeza damu na kunywa
bila kukosa vidonge vya kuongeza damu.
Hilo
likamtia hofu na kumuongeza umakini. Hakutaka aje afe amuaache mtoto wake kama
yeye alivyoachwa na mama yake. Akaweka juhudi za makusudi kujitunza vizuri bila
kupuuzia dalili yoyote anayoona ni hatarishi kwake.
Akajitahidi kuweka mazoea na huyo daktari
anayemuona kwa kliniki kwa makusudi ili tu awe msaada. Alimuelezea historia ya
maisha yake. Vile alivyozaliwa bila kukutana na mama yake. Maisha ya upweke anayopambana
nayo, akamsihi huyo daktari amsaidie bila kumpuuza. Huruma ikamuingia huyo
daktari, akawa akimfuatilia kwa karibu kama mtu anayemuhusu haswa, ili kuhakikisha
anabeba hiyo mimba na kujifungua salama.
Na yeye akaweka juhudi ya kula vizuri kutokana na
uwezo wake, na kuendelea kufuata ushauri wa huyo daktari. Kila wazo aliloona
litamuharibia mudi yake, au kumchafua moyo, alijitahidi kuliepuka ilimradi tu
kujituliza.
~~~~~~~~~~~~~
Kila James alipomtaka wakutane, alimkwepa. Wakati
mwingine James alitaka kumtoa kwa ajili ya chakula cha mchana au kumpa ofa ya
kutaka kumnunulia gauni au kiatu. Tena wakati mwingine James alimpigia akiwa
amejawa furaha. “Leo nina pesa Nanaa. Pesa ya kufa mtu.
Twende ukapate hata kiatu tu!” Nanaa alikuwa akicheka tu. Akitamania
kukutana na kaka yake lakini hakutaka kabisa amgundue kuwa ni mjamzito. Akazidi
kumkwepa kwa maneno ya busara na kumuaminisha shule ndio kipingamizi. “Ni miezi kama 6 tu imebaki kaka yangu. Naomba nijikaze hii
shule iishe. Ikiisha tutakuwa wote. Mungu ni mwema atajalia.” Hiyo ndio
kauli kwa kaka yake.
Kwa hiyo kila alipokuwa akimpigia simu labda
akitaka kumtoa au amtembelee, alimtajia muda uliobaki. “Imebaki
miezi miwili tu kaka yangu, hii shule iishe. Acha nikazane. Hata mimi nina hamu
ya kutoka. Lakini siku 60 sio nyingi.” Alikuwa akiweka hiyo line
yenye namba ya simu mara moja moja sana akitaka kuzungumza na kaka yake tu, na
kila alipomaliza kuzungumza naye, alitoa hiyo namba na kuweka namba mpya ambayo
hata James hakuwa akiifahamu. James aliendelea kumtunza dada yake. Alimtumia
pesa kila mara, na kwa kuwa Nanaa alifanya kazi ofisini kwa kina Grace, alikuwa
na akiba iliyomfanya aishi maisha ya kawaida tu bila shida yeyote.
Na Walimwengu Hawakosi Yao.
Maisha yakaendelea, tumbo likawa bayana. Kila mtu
aliyemuona alijua ni mjamzito, lakini hakuonyesha wasiwasi hata kidogo. Hata
rafiki zake walipomuuliza baba wa mtoto wake, jibu lake lilikuwa moja tu, “Mama yake ndio mimi.” Wakajua safari
hii kwa hakika Nanaa amepatikana. Ameachwa kama walivyozoea kumuona akiachwa,
ila safari hii ameachwa na mtoto juu.
Kwa kuwa hakuwa akienda popote hata siku za
likizo, kwa hiyo wakawa wakiambiana amefukuzwa hata kwa kaka yake sababu ya ile
mimba. Walio mcheka walimcheka, na kumsema. Alijua lakini hakujali. Alijitahidi
kuweka mawazo yake shuleni tu bila hata kuweka wasiwasi wa kuwaza pakwenda mara
baada yakujifungua. “Kila kitu nitakijua
mbele ya safari.” Nanaa alikuwa akijiambia hivyo.
~~~~~~~~~~~~~
Penzi la Zena na Yasini lilikolea. Yasini alikuwa
akimtunza vizuri sana Zena. Akapendeza. Zena alijawa na furaha. Kila walipokuwa
pamoja, Tia na Nanaa, Zena hakuacha kueleza uzuri wa Yasini. Alipendeza akawa
mtu wa vipya kila wakati. Kama sio nguo mpya basi Zena alirudi na viatu vipya
au pafyumu, chochote kile kizuri ambacho lazima awaambie vile Yasini
anavyomjali yeye. Yale maisha ya Nanaa aliyokuwa akiishi wakati wapo na Jamal,
kuondoka ijumaa na kurudi jumatatu akayaanza kuyaishi Zena. Tena hakuondoka
kimya kimya. Alikuwa akiaga darasani kwenye kipindi cha mwisho. Nanaa alikuwa
akimsikia akisema kwa sauti tu. “Jamani eeeh! Naenda kulea penzi. Naona na mume
anasubiri nje. Hapa tena ni mpaka jumatatuuuu!” Basi hapo Zena atasimama kwa
mikogo na kutoka.
Tia na Evan nao pia penzi likawa lakaribu. Evan
alishamaliza shule yake huko mjini Morogoro akawa yupo jijini. Kwa hiyo kutoana
kwa chakula cha mchana siku za weekend likawa jambo la kawaida kwao.
Kutoka asubuhi siku za jumamosi na kurudi usiku au hata kesho yake wakichukua
chumba nyumba za kulala wageni, likawa jambo la kawaida tu kwao.
Kwa kuwa mashoga hao wote walikuwa na wapenzi,
ikabidi Yasini na Evan wafahamiane. Kwa hiyo wakati mwingine walitoka kama couple.
Nanaa akaachwa na tumbo lake. Hata alipokuwa akikaribishwa, alikuwa akikataa.
Wakajua anajificha sababu ya kupewa mimba. Tia alikuwa akimcheka anapokuwa na
Zena.
“Alivyokuwa akimringia Terry vile! Lazima
ajifiche.” Tia aliongeza kwa Zena. “Wewe hukumuona alivyokuwa akimringia Jeff.
Jeff hakutaka kuzungushana naye, akatafuta mwanamke mwingine. Tulipoenda
Kigamboni kwenye birthday ya Yasini, bwana Jeff mtoto wa mjini alimfanyia shoo
hiyo! Asikwambie mtu Tia. Ilikuwa shoo yakufunga mwaka. Mbona aliaga!” Zena
alimsengenya. Wala asisimulie msaada aliopewa wakati mgonjwa. Ushoga na Tia
ukarudi kunoga zaidi, Nanaa hakumtaka tena. “Ulinisimulia! Acha ajifungie. Sura
ile ataficha wapi? Alitingisha wanaume, sasa hivi kachina!” “Bi dada hata kwa
kaka yake kafukuzwa.” Waliendelea kucheka.
“Unafanya mchezo na wanaume wa mjini?” “Lakini
sasa hivi atakuwa anajuta. Jeff alitaka kumuoa ki ukweli. Akamringia! Sasa ona
yaliyompata. Anazunguka na tumbo lisilo na baba.” Wakacheka. “Ujue hata likizo
haendi mahali?” “Kweli!?” Zena akashangaa. “Kweli tena. Alibaki hapa hapa
chuoni.” Wasijue Nanaa alikuwa katikati ya kundi lililokuwepo pembeni yao
wakijisomea. Na wao walikuwa wamekaa wawili tu chini ya mti huo mkubwa wakipena
habari za weekend iliyopita. Watu wote waliokuwa wakisoma na Nanaa walikuwa
wakisikiliza jinsi Zena na Tia wanavyomsema rafiki yao. Nanaa akacheka tu,
akanyamaza. Walimsengenya mpaka wakachoka. Hawakusoma kitu chochote pale,
wakaondoka wakicheka na kupongezana.
~~~~~~~~~~~~~
Hakuacha kwenda kliniki. Tena bila kukosa.
Alitaka kujua maendeleo yake na ya mtoto wake huyo waliyekuwa wakizungumza kila
wakati. Alimgeuza kuwa ndiye rafiki yake wakaribu. Kucheka na kumuongelesha kwa
kila jambo.
Wasiwasi
ulimwingia pale alipopewa tarehe ambazo anatakiwa ajifungue. Zilikuwa zikiendana
kabisa na tarehe zake zakuanza mitihani yake yakumaliza chuo kikuu. Akabaki
kumuomba Mungu utokee muujiza apitilize siku zake zakujifungua ili ajifungue
akiwa ameshamaliza chuo. “Inabidi upunguze shuguli humo ndani ili ukae mpaka
nimalize mitihani. Umesikia? Ukija sasa hivi, mama atakuwa na mambo mengi
hatutapata muda wa pamoja. Umesikia kipenzi cha Nanaa?” Nanaa alikuwa akiongea
na mwanae kila akimsikia akizunguka tumboni. Alilishika tumbo lake na
kulipapasa kama anampapasa mtoto wake. Jina kubwa alilokuwa akimwita huyo mtoto
ni kipenzi cha Nanaa.
Kila alipoamka, alishika tumbo lake kwa upendo
nakuzungumza na mwanae. “Umeamka salama kipenzi cha Nanaa?” Alimuuliza mwanae. “Amka
umsalimie mama, basi.” Atapiga piga tumbo lake taratibu huku akizungumza na
mtoto wake mpaka mwanae acheze huko tumboni ndipo afurahi. Atamwambia mipango
yake yote ya siku hiyo. Wapi watakwenda na nini watafanya ndipo atoke
kitandani. Hivyo hivyo ikifika usiku wakati analala. Atampa pole ya mahangaiko
ya siku hiyo. Mafanikio yake kwa siku hiyo na changamoto zinazomkabili. Basi
atazungumza na huyo mtoto hapo mpaka wanalala.
Ujauzito huo ukawa faraja tofauti na wenzie
walivyofikiria. Wakati wao wakimcheka, Nanaa alikuwa amepata rafiki mzuri
kuliko wao. Rafiki huyu hawakuwa wakigombana kwa lolote. Alimsikiliza kila
wakati na kuongozana naye kila mahali. Hata akisikia kiu ya maji, basi
atamwambia mwane huko tumboni. Akichoka au akisikia usingizi pia,
atamshirikisha mwanae. Hakukosa kitu cha kuzungumza na huyo mtoto.
Miezi 9 Ya
Mimba Ya Nanaa.
Miezi tisa ikatimia na mitihani ikawa imefika.
Nanaa alikuwa amejiandaa vizuri tu na mitihani yake, hakuwa na wasiwasi. Kwa
kuwa hakuwa na mtu wakumfikiria ila yeye na mtoto aliyekuwepo tumboni, basi
alisoma vizuri bila shida. Msichana aliyekuwa naye chumba kimoja, alikuwa ametulia
sana. Alikuwa ni dada aliyekuwa ameolewa, lakini hakuwahi kupata watoto.
Alimuacha mumewe mkoani Lindi, akaja chuoni hapo kujiendeleza. Alikuwa
akimsaidia sana Nanaa. Alishazoea mazungumzo ya Nanaa na mwanae hapo chumbani.
Si asubuhi si jioni alikuwa akimsikiliza Nanaa akiongea na mwanae nakuishia
kucheka tu.
Alishanunua vitu vyote anavyohitaji siku ya
kujifungua na begi la mtoto wake lilikuwa tayari. Furaha ilimjia pale alipoenda
kliniki akaambiwa mtoto wake yupo salama. Japokuwa siku za kujifungua zilikuwa zimetimia,
lakini walipompima wakakuta njia bado
haijafunguka. Aliambiwa ni kitu cha kawaida kwa kuwa alikuwa ni mtoto wake wa
kwanza. Alimshukuru sana Mungu. “Ukae humo humo ndani mpaka mama amalize
mitihani. Sawa eeh!” Nanaa hakuacha kumsisitiza mtoto wake kila alipomsikia
anazunguka nakumletea vichomi.
“Kwanza huko ndio utakuwa salama. Unakuwa na mama
kila wakati na kila mahali. Hakuna kutengana. Usishawishike kutoka huko.” Nanaa
alikuwa anamsisitiza mwanae kila wakati. “Nitakupenda sana mwanangu. Mimi ndio
nitakuwa rafiki yako wa kwanza hapa duniani. Tulia tumuombe Mungu atujalie sote
maisha marefu. Tuje tuonane, nikulee mimi mwenyewe.” Basi hapo Nanaa huanza
kuomba na mwanae huku ameshika tumbo akilipapasa.
~~~~~~~~~~~~~
Roho ya umama nayo haikukawia. Hakuacha kumuombea
na kumtabiria mambo mengi mazuri. “Uwe na akili kama za dad. Uwe mpole na
hekima kama anti Grace. Usikubali nywele zangu. Nina kipilipili kibaya sana.
Utanilaumu maisha.” Hapo Nanaa ataanza kucheka naye. Na kama ukimkuta, basi
ungedhani anazungumza na mtu. Hata akisoma, atamuelezea anachosoma. Kama
nikigumu atamlalamikia. Kama ni kitu anachokipenda atamuelezea hicho kitu. Na
wakati wote alipotaka kuingiza kitu kichwani kikae, alimshirikisha mwanae. “Lazima
umsaidie mama kukumbuka kwenye mtihani.” Basi hapo atasoma kwa sauti, huku
akimuelezea mwanae. “Umeelewa lakini?” Atamuuliza.
Mara nyingi alitamani kumuona mtoto wake. Alikuwa
na wasiwasi naye. Jinsi atakavyokuwa baada ya yeye kunywa madawa yote yale
makali wakati mgonjwa. “Hata ukiwa vipi, bado utakuwa ni mwanangu tu.
Nitakupenda sana. Unajua sifa yako kubwa?” Nanaa alimuuliza mtoto wake. “Wewe
ni jasiri kama simba. Upo kama mti wa mzeituni. Unamea jangwani. Umeweza
kushinda mauti! Basi wewe huwezi kushindwa na changamoto za haya maisha. Mungu alikutuma
kwangu kwa makusudi. Wewe ni faraja yangu.” Nanaa hakuacha kumsifia mwanae.
~~~~~~~~~~~~~
Week inayofuata Nanaa akaanza mitihani. Aliingia
kwenye mtihani wake wa kwanza, ilikuwa asubuhi akatoka bila shida ila kiuna
kilianza kumuuma. Akajiambia kwa kuwa ni miezi tisa na ametoka kwenye mtihani
mgumu labda ndio sababu. Akaamua kurudi chumbani kwenda kulala. Alikuwa amepata
chumba kilichopo gorofa ya juu kabisa, kwa hiyo mazoezi yake yalikuwa yakupanda
ngazi hizo kila siku kama alivyoshauriwa. Wakati amemaliza ngazi zote anataka
kuingia chumbani kwake, chupa ikapasuka.
~~~~~~~~~~~~~
Karibu Na Ukingoni
Mwa Mkakati wake wa SHULE, Ambao Haukuwahi Kuruhusu Ivunjike Au Ibadilike, Mtoto Anakuja.
Hana Mtu Wa Karibu Wa Kumsaidia Kwa Wakati Huo.
Ni Nini
Atafanya ? Nini Kitaendelea?
Usikose
Muendelezo.
0 Comments:
Post a Comment