Kwa Nanaa!
Wakati yupo hospitalini akiuguza, Nanaa akaanza kupokea jumbe na
picha kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kama Rita. Akafungua. Akamuona Geb akiwa
amevaa vizuri, amekaa mezani na chupa yake ya maji. ‘Naitwa Rita.
Nipo na mpenzi wangu sasa hivi.’ Nanaa akasoma. Moyo ukampasuka kama
unaotaka kutoka. Akaamua asijibu. Akatulia. Baada ya muda zikaanza kuingia zile
picha za Rita akiwa uchi chumbani na Geb hana shati. ‘Hivi ndivyo
tunavyomalizia siku yetu.’ Huo ndio ukawa ujumbe wa mwisho.
Kituo Cha Polisi!
Mama G na familia yake wakaingia pale
polisi wakiwa hawaelewi. Wakaulizia jina la Geb, wakapewa maelezo
yaliyowashangaza. “HAIWEZEKANI!!” Wote
walikataa kwa pamoja. “Hata wahudumu wa pale wanasema yule dada aliondoka pale
mezani akiwa analia. Akimlalamikia Geb kuwa anamsaliti. Mashahidi wanasema yule
dada alijaribu kuondoka lakini Geb alimkimbilia. Ndipo wakachukua chumba. Baada
ya muda, ndipo wakapokea simu ya kuitwa chumbani kwao. Mimi nilikuwepo kwenye
tukio.” Huyo polisi waliyemkuta hapo kituoni alisistiza.
“Tulimkuta huyo binti yupo uchi
kabisa, na kijana wenu hivyo hivyo.” Mama G alitamani akae chini sakafuni.
Walipoomba kumtoa kwa dhamana, walikataliwa. Kwanza waliambiwa siku ile ni ya
jumapili, pili aina ya kesi aliyoshitakiwa na Rita ni kesi ya mauaji. Hawezi
kupata dhamana. Mpaka mahakama iamue.
Mama G na familia yake walitoka pale
wakiwa hawaamini. “Haiwezekani!” Kila mmoja alisema kwa wakati wake. “Danny.
Naomba usimwambie mtu yeyote juu ya hili jambo. Tafadhali sana. Naomba nifichie
aibu yangu mpaka nizungumze na Geb mwenyewe. Bado moyo wangu unasita.” Mamaa G
aliongea kwa uchungu sana wakati wanaingia tu ndani nyumbani. “Siwezi mama.
Sithubutu.” Danny akajibu. “Basi nashukuru.” Mama G akajibu.
Grace alikuwa kama amepigwa na
butwaa. “Sasa unaenda wapi mama?” Danny akamuuliza. “Nakwenda kumuita Mungu
wangu. Yeye baba wa yatima na mume wa wajane. Nitamuita, mpaka aniitike. Hakika
atanitetea.” Yule mama akaingia chumbani kwake akiwa ameshabeba kosa la mwanae na
kuanza kuomba.
~~~~~~~~~~~~~~
Mama G alikesha usiku kucha akiomba
huku akimuuliza Mungu afanye nini. Grace na Danny walimsikia akilia kwa uchungu
sana huku akiomboleza. Hakuna aliyeweza kulala. Yule mama alikuwa akilia
akiomba bila kunyamaza mpaka panapambazuka. Alikuwa akilia kwa uchungu sana
huku akinung’unika. Kuna wakati Grace aliingia akamkuta amelala sakafuni kabisa
analia. Alimmiliki huyo Mungu, usiku kucha kana kwamba ni wake peke yake. Kuna
wakati alimlilia kama baba yake akimkumbusha yeye ni yatima. Alimpokonya ndugu,
ndugu zake ni hao watoto.
Wakati mwingine alimtambua kama mume.
Akimkumbusha alimchukua mumewe. Hana kimbilio ila yeye tu mume wa wajane.
Akamsihi achukue nafasi ya marehemu Magesa, baba yake Geb, ili akamtoe mtoto
wao huko jela. Yule mama alilia na kugaragara mpaka asubuhi.
Mungu
Ajibuye Maombi.
“Mama Magesa! Kuna nini!?” Ndipo Danny akasimulia. Mzee Simba na
mkewe wakaangaliana. “Hebu ingieni ndani. Wala huna haja yakulia. Rita amekuwa
mwehu. Utusamehe sana mama Magesa.” Ndipo wakapewa historia nzima ya Rita. Wote
wakabaki mdomo wazi.
Kisa Cha Wehu
Wa Rita.
Sio kwamba Rita aliolewa na mwanaume
tu wa Canada. Alihakikisha anaolewa na mwanaume mwenye pesa ili anufaike kote. Akabahatika
kupata kijana mwenye pesa na pia alikuwa akitokea kwenye familia ya watu wenye
pesa sana. Kwahiyo maisha yao yalikuwa mazuri huko nchini Canada. Aliishi
kwenye jumba la kifahari na kuendesha magari mazuri.
Baada ya kukamilisha mambo yake ya ‘Permanent Resident’ huko nchini Canada, ndipo alipotoa makucha yake.
Starehe zikaanza kunoga kwa Rita. Hata shule akaacha bila mumewe kujua. Club na
yeye, yeye na club. Starehe mchana na usiku. Anavaa nguo za madizaina na nywele
za aghali kweli. Kwa kuwa mumewe alikuwa mtu wa mshahara tu, akaanza kulemewa
na garama za maisha. Rita akiwa amezama kwenye ulevi wa kumpindukia ndipo
akaanza utapeli.
Kukopa kila mahali kwa kutumia jina
la mumewe na kufuja pesa kwa kutumia Credit Card za mumewe.
Haikuchukua muda mrefu yeye na mumewe kufilisiwa. Isivyo kawaida kwa familia za
wenzetu, ikabidi wahamie ukweni tena wakiwa hawana kitu. Wizi wa vito vya
thamani kwa wakweze ukaanza. Anaiba hapo nyumbani na kutoroka hata siku mbili
tatu, akimaliza pesa, anarudi nyumbani. Walipewa Basement/Sehemu ya chini
kabisa ya nyumba ya gorofa ambako ndiko alipokuwa akiishi na mumewe.
Walipochoshwa naye, wakamtegeshea
kamera, wakapata ushahidi wakutosha, ndipo Rita akapelekwa jela. Mumewe
alimtafutia mwanasheria wakumtetea, baada ya miaka miwili Rita akatolewa na
talaka juu. Akaanza kuzunguka nchini Canada kama chokoraa. Leo kwa mtanzania
huyu, kesho Kanisa hili. Ilimradi shida tu.
Ndipo habari zikamfikia Mzee Simba.
Akatuma nauli na kumtaka arudi nyumbani. Rita alirudi nchini akiwa kama mwehu.
Starehe tu. Na hawezi kulala bila kunywa. Lazima alewe ndipo alale. Mchafu na
yupo tayari kulala na yeyote. Swala la kwenda kuchukuliwa na wazazi wake baa,
walishachoka wakaamua kumuacha. Mara nyingi alikutwa akiwa kama sio vifichoni
akiwa amebakwa, basi amerudishwa mpaka hapo nje akiwa hajitambui na wazi
alionekana amebakwa. Hakusikia la mtu na wala hakuwa akijali. Mzee Simba na
mkewe walishazungumza naye mpaka wakachoka. Tapeli wa mchana na usiku.
Anajulikana kila mahali hapo mtaani. Hata wenye maduka walishakatazwa na Mzee
Simba wasimruhusu kukopa.
~~~~~~~~~~~~~~
“Wewe sio wakwanza kulizwa na Rita.
Hivi umewahi tu. Hodi zote za humu ndani ni mashitaka yake huyo Rita!” Mama
Simba aliongeza. “Basi hayo mliyoyasema. Naombeni mkawaambie polisi ili wamtoe
mwanangu. Tafadhali mama Simba. Nihurumie mwenzio. Ndio mwanangu wa mwisho huyo!
Hajui hata kupiga mtu kofi! Naomba umuokoe. Nitawalipa chochote kile.” Tayari mama G
alikuwa amepiga magoti. “Wala huna haja yakutulipa. Ingekuwa nikulipwa, naona
sasa hivi tungekuwa mamilionea hapa mjini. Vilio kama vyako hivyo haviishi humu
ndani kwetu. Si vijana, si wazee. Vilio ni vya huyo Rita. Mnatofautiana tu
majanga. Ni msalaba wetu huyo! Tunabeba mpaka na sisi Mungu atakavyotusaidia.
Maombi ya kila mtu ni Rita. Twendeni tuwahi wasije muhamishia jela.” Mzee Simba
na mkewe wakavaa na kutoka pale sebuleni.
~~~~~~~~~~~~~~
“Lakini jamani, hatuwezi kufuta kesi
mpaka tuelewane na Rita mwenyewe.” Mama G akakumbuka. “Wala usipate shida.
Ngoja nimuamshe.” Mama Simba akarudi ndani kwenda kumuamsha. “Lakini lazima
mjue atataka pesa. Atadanganya chochote kile ili awatoe pesa.” “Hamna neno Mzee
Simba. Tutampa tu.” Mama G akajibu.
Rita akaja. Akionyesha bado anapombe
kichwani. Baba yake akamwambia lazima waongozane wakafute hiyo kesi. “Lakini
ameniharibia simu yangu na kuniumiza. Lazima anilipe.” “Kiasi gani unataka?” Akaitaja
hiyo pesa bila kuuma maneno. “Bila hivyo sifuti kesi.” Mzee Simba akatingisha
kichwa kwa majonzi. “Unaniona mimi muongo?” Rita akauliza kwa ukali. “Kama
huniamini basi.” Rita akataka kuondoka kurudi ndani. Baba yake akasimama kwa
haraka. “Usiondoke Rita.” Baba yake akamuwahi. “Tutamlipa hiyo pesa Mzee Simba.
Bora hiyo kesi ifutwe.” Mama G na Grace wote wakasimama.
“Rita mwanangu wewe! Hakika Mungu
akusaidie” Baba yake akaongea kwa uchungu akimuhurumia huyo binti yake. “Kwa
hiyo wewe unawatetea wao badala unitetee mimi?” Rita akauliza. “Twende mama.
Wamesema watakupa hiyo pesa. Twende sasa hivi ukawaambie polisi unafuta kesi.
Na ubadili maneno yako kuwa Geb juu ya Geb kutaka kukuua.” “Mimi sikusema
hivyo.” Rita akakataa kabisa kama sio yeye aliyekuwa akijiliza kwa polisi.
“Haya. Twende mama. Twende.” Baba yake hakutaka kesi.
Wakatoka tena pale mpaka polisi.
Kwa Mungu
Wa Yasiyowezekana.
Rita alikana kila kitu. Akawashangaa
wale polisi waliwezaje kuchukua maneno yake. “Kwanza nilikuwa nimeshalewa! Wewe
vipi?” Mama G na kina Danny hawakuamini. Mpaka saa tatu asubuhi, kesi ya Geb
ikawa imefutwa, akatolewa. Geb alitoka nje akilia kama mtoto mdogo. Mama G
alipomuona anatoka, ni kama na yeye alipandwa na kitu. Akapiga magoti palepale
nje ya kituo cha polisi mbele ya mama Simba na mumewe, akaanza kulia, mpaka
Grace naye akaanza kulia. Alilia mama G mpaka Mzee Simba akamnyanyua na
kumsindikiza kwenye gari ya Danny. Wote wakiwa wanalia kasoro tu Danny.
“Sasa ile pesa yangu?” Rita akauliza
bila hofu wala kuonyesha kujali. “Naona mnanisahau wakati mimi ndio nimemtoa
huyo Geb!” Rita akaongeza. “Hatujasahau Rita. Na tunakushukuru sana. Sasa
naomba tuongozane tena mpaka Sea cliff nikachukue gari ya Geb, halafu mimi na
wewe twende benki.” Rita akakubali. Waliongozana magari mawili la Mzee
Simba na gari ya Danny mpaka Sea cliff hotel alipokuwa ameacha Geb gari yake
siku iliyopita. Danny, Mama G, Fili na Geb wakaondoka kurudi nyumbani baada ya
kumuacha Grace hapo ili achukue gari la Geb na kumalizana na Rita. Ndipo Grace
na familia ya Simba wakaelekea benki baada ya Grace kulipia na hapo pia maana
hawakuwa wamelipia hata chumba alichokuwa amechukua Rita na ile Wisky. Ndipo Grace
akatoa hicho kiasi cha pesa alichodai alipwe kutoka kwenye akaunti yake,
akamkabidhi Rita. Wakaachana.
~~~~~~~~~~~~~~
“Mama!” Geb akaita wakati wapo
njiani. “Umewasiliana na Nanaa?” “Alinipigia jana asubuhi kabla sijakwenda
kanisani. Ilibidi kumrudisha Zena hospitalini. Anaonekana ni mgonjwa sana.” Geb
akanyamaza. “Pole baba. Pole sana.” Mama yake alimshika mkono. Alimuona machozi
yakimtoka. “Sijui kama Nanaa atanisamehe!?” Walimsikia akilalamika.
“Naomba pata muda wakupumzika Geb. Mengine utajua baadaye.” “Unajua
muda wote nipo pale rumande nilikuwa nikimuwaza Nanaa, mama! Nilimfanyia kitu
cha ajabu sana. Najua nitakuwa nimemuumiza vibaya sana.” “Mimi
nashauri kama mama, Geb. Umepitia masaa machache magumu sana kwenye maisha
yako. Twende ukalale. Ukiamka, utajua kitu chakufanya.” Danny akashauri tena.
Geb akainama kwa muda. Kisha akainua
kichwa. “Unajua nilishindwa hata kumtambulisha kwa Rita! Sijui nilipatwa na
nini jamani!” Geb akasimulia kuanzia mwanzo wa kukutana na Rita akiwa na Nanaa,
mpaka alipoishia polisi. “Masikini Nanaa wangu!” Geb aliendelea kulalamika
wengine wakiwa kimya. Wasijue ndio yupo kwenye mshituko au la. Aliongea bila
kuulizwa. “Nilimkuta amekaa pale nje ya geti peke yake! Na pia nikashindwa
kuzungumza naye chochote juu ya mabusu na kukumbatiwa na Rita! Sikutegemea kama
na mimi naweza kumfanyia hivi Nanaa, tena kwa mwanamke kama Rita! Kweli
nimeumia sana. Nahisi adhabu ya jela, inanistahili kabisa. Tena baada ya
kumuahidi..” Geb akanyamaza.
“Pole Geb.” Ikabidi mama yake arushie
neno. “Mimi sistahili pole mama. Nanaa ndiye anastahili pole. Sijui niliingiwa
na nini!?” Geb bado alikuwa ameinama anajisugua mikono. “Amekwambia kama
atarudi?” Baada ya muda akamuuliza tena mama yake. “Geb! Lazima atarudi.”
“Lini?” Akauliza tena. “Nafikiri mpaka mgonjwa apone.” “Wapo hospitali gani?”
“Hakunitajia. Amesema Zena hataki mtu yeyote ajue. Hata hivyo amesema wakati
anamnyanyua Zena, simu yake ikaanguka. Anahisi imepata matatizo. Amesema Yasini
amemwambia ataichukua kuipeleka kwa fundi. Inawezekana hana simu kwa sasa.” Geb
akabaki kimywa.
~~~~~~~~~~~~~~
Walirudi nyumbani. Geb akaoga.
Akanywa uji na kujitupa kitandani. Alilala mpaka saa moja usiku akaamka.
Akamkuta mama yake jikoni. “Nanaa amerudi?” “Hawezi kurudi leo Geb. Yule binti
ni mgonjwa sana.” “Amekupigia simu?” “Hapana. Lakini wewe umelala vizuri?”
“Nimelala.” Geb akavuta kiti pale jikoni akakaa. “Mama!” Mama yake akamgeukia.
“Najua uliniombea. Asante.” Mama G akaanza kulia. “Pole mama na samahani.” Geb
akasimama kwenda kumbembeleza mama yake. Alimuona vile alivyokuwa ameumia.
“Pole mama. Pole sana mama yangu.” Geb akaendelea kumbembeleza. Grace akaingia
akawakuta wanabembelezana. Akasimama pale kwa muda mpaka mama yao akatulia.
“Pole mama.” Grace naye akaongeza.
“Pole na wewe Geb.” “Asante.” “Na nyinyi poleni kwa hekaheka.” “Asante. Ulipata
muda wakupumzika?” Grace akauliza. “Nililala.” Geb akajibu kwa upole. Grace
akataka kutoka. “Grace!” Grace akarudi. “Vipi?” Akamuuliza kaka yake. “Nanaa
amekutafuta?” “Alinipigia simu jana asubuhi kuomba ruhusa ya kazini. Alisema
rafiki yake mgonjwa sana. Yupo kwenye matibabu. Daktari amewaambia inaweza
kuchukua siku tatu ndipo akaruhusiwa.” “Okay. Asante.” Geb akanyamaza.
“Jaribu kutulia Geb. Kila kitu
kitakuwa sawa.” “Sidhani. Sidhani tena.” “Kwa nini unakata tamaa Geb!?” “Nahisi
Rita amemtumia picha. Na sijui atakuwa alimwambia nini?” “Amepataje namba ya
Nanaa?” “Aliniomba simu yangu wakati anakula. Alisema hajawahi kushika simu
kama hii. Akawa anaigeuza kulia na kushoto. Nikahisi anasoma kitu, ndipo
nikamuomba anirudishie. Baada ya hapo kila mazungumzo yaliyoendelea akawa
anamlaumu Nanaa. Hata kulia kote kule akitaka niende naye chumbani nikafanye
naye mapenzi, alikuwa akimlaumu Nanaa. Nilihisi ananipiga picha. Wakati
namkimbiza ili nimpokonye simu nione, ndipo akajikwaa na kuanguka. Alikuwa
amelewa sana. Yaani sijui pale Sea Cliff nitakuwa nimeacha deni kiasi gani!?
Maana alichukua chumba Presidential Suite.” “Nimelipia kila kitu, mpaka Whisky!”
Grace akacheka.
“Usicheke G. Nimempoteza Nanaa.”
“Utamuelezea, ataelewa tu.” “Ni heri angesikia kutoka kwangu mimi kwanza.
Kuliko kusikia kutoka kwa yule mwendawazimu kwanza! Maneno yangu yatakuwa
hayana nguvu tena.” “Mungu atakutetea Geb.” Mama yake akamfariji. “Naamini
hivyo mama. Japo nimetenda kila kitu kwa upumbavu, lakini naomba Mungu
anirehemu.” Geb aliongea kwa upole huku akifikiria.
Huko Kwa Nanaa
Na Zena.
Alijua wazi angeweza kurudi nyumbani
usiku ule. Lakini akaaamua alale tu na siku hiyo palepale hospitalini mpaka
kesho yake. Alikaa pale nje akiwaza. Akakumbuka maneno ya Geb. Akakumbuka picha
alizotumiwa na Rita mpaka wakiwa chumbani. Nanaa akacheka. “Kweli mimi sina
mkosi. Bali mimi mwenyewe ni mkosi. Khaa! Haiwezekani jamani!” Nanaa
alijiwazia akiwa amekaa pale nje peke yake. Wauguzi walishamjua kuwa yupo
kwenye chumba cha Zena akisaidia kuuguza. Kwa hiyo hata walipomuona amekaa pale
kwenye makochi, sehemu ya wageni, hakuna aliyemsumbua.
Alikaa akiwaza, mpaka Yasini
alipomuita. “Zena anakuita.” Nanaa akanyanyuka. “Nakushukuru sana Nanaa.”
“Karibu Zena na pole.” “Asante.” Zena akashukuru tena. “Naombeni niwashauri
mimi kama rafiki tu.” Wote wawili wakamtizama. “Nyinyi wawili mnakitu cha
kipekee sana kati yenu. Sidhani kama utofauti wa dini unaweza kuwatenganisha.
Nashauri hayo mahusiano myafikishe kwa wazazi. Yasini, binafsi namuomba Mungu
nipate mwanaume kama wewe. Unampenda na kumjali sana Zena. Nilidhani
ungemkimbia baada ya mimi kuwa naye hapa hospitalini, lakini nimeona jinsi
ulivyokuwa ukihangaika naye. Kutafuta damu bila kuchoka. Nashauri hofu ya dini
isikunyime mke. Mfikishe Zena kwa wazazi. Muone watawashauri vipi.” “Asante
sana Nanaa. Nitaanza kuzungumza na Mzee wangu kwanza.” Yasini akajibu.
Palipo pambazuka siku hiyo ya
jumatano, Nanaa akaoga hapo hapo hospitalini. Akavaaa haraka. Yasini alipokuja
kuleta uji wa mgonjwa, akaomba lifti. “Nishushe popote nipate daladala za Kariakoo
niwahi ofisini. Najua Zena atatolewa leo kama mambo hayatabadilika. Na ninaomba
yasibadilike.” Wakacheka. “Nitakupigia simu mchana kujua alipo ili jioni nije
kumuona ndio nirudi Tabata. Lakini naaamini atakuwa ametoka.” “Amina.” Yasini
akampeleka mpaka ofisini kwake, akamshusha nje.
Kuliko
Ungua Mpini.
Siku ilikuwa nzito sana kwa Nanaa
kuliko siku nyingine. Alikuwa akisinzia kama mlevi. Ilipofika saa kumi ilibidi
aage tu. “Hali mbaya Grace. Kichwa kizito kama kinaanguka kwa usingizi!” Grace
akacheka taratibu akimwangalia. “Nenda kapumzike.” “Nitakwenda. Lakini nataka
nimpitie kwanza Zena nyumbani kwao, ndipo niende nyumbani.” “Mvua itakuwa
kubwa. Imeshaanza manyunyu.” Grace alimtahadharisha. “Nikiona kubwa sana,
nitalala tu kwao mpaka kesho. Hamna shida.” “Sawa.” Wakati anatoka, akamkuta
Geb mapokezi. Hakujua kama alifika pale muda gani.
“Habari yako?” Nanaa akasalimia.
“Nzuri.” Alipojibu tu, Nanaa akampita. Akarudi ofisini kwake kwenda kuchukua
pochi yake, Geb akamfuata. “Nimesikia unaondoka sasa hivi.” Nanaa akainuka.
Maana alikuwa ameina kuchukua pochi yake, akamgeukia. “Ndiyo.” Akajibu kwa
kifupi tu. “Tunaweza kuongozana?” Geb akauliza. Nanaa akakunja uso kidogo kama
anayemshangaa. “Wapi!?” Geb akaingia akafunga mlango.
“Namaanisha nikusindikize huko
unapokwenda, halafu turudi wote nyumbani.” Safari hii Nanaa akaweka uso wa
mshangao kabisa. “Kwa nini!?” Akamuuliza Geb. “Mvua inaonekana itakuwa kubwa.
Utasumbuka swala la usafiri.” “Hapana. Nitakuwa sawa tu. Nakushukuru.” Nanaa
akataka kutoka, Geb akawa bado amesimama mlangoni. “Samahani, naomba kupita.”
Nanaa akaomba kiustarabu. “Naomba twende wote Nanaa.” “Mbona kama unalazimishia
kitu Geb? Kuna nini!? Mimi naenda kumuona Zena ndipo nirudi nyumbani. Unanizuia
mlangoni!” “Mvua itakunyeshea.”
“Kweli Geb? Ujue unazungumza na Nanaa. Sijui
wala sijazoea maisha ya gari mimi. Kwangu si mvua wala jua ni hatari kwangu
hata kidogo. Sina tatizo la kunyeshewa na mvua. Kama unahofia mimi kuloa, usiwe
na wasiwasi hata kidogo. Na nitahakikisha nakauka, kabla yakuingia nyumbani
kwako ili nisiloweshe chochote kile.” “Simu yako ipo wapi? Nimepiga
haipatikani.” “Yasini alinipelekea kwa fundi. Niliiangusha. Imepasuka. Lakini
nilimpigia simu Grace kumuomba ruhusa yakutokuja kazini, sababu ya kuuguza. Kwa
hiyo anataarifa. Hata mama anajua kama nauguza.” Nanaa alikuwa akiongea kwa
jazba kidogo, na Geb akajua amebeba hasira.
“Mbona mimi hukunipigia?” Hapo Nanaa
akanyamaza na kuinama. “Nanaa!” Kimya. “Mbona mimi hukunipigia?” “Nilijua
unahitaji muda.” Nanaa akajibu kwa upole akiwa ameshajirudi na jazba imeisha.
“Ni kweli nilihitaji muda.” Geb akajibu na yeye kwa upole. “Samahani.” Samahani
ya Geb ikamfanya Nanaa atulie na kumwangalia vizuri. “Mbona
unaonekana umechoka? Upo sawa?” Nanaa akamuuliza kwa kujali huku
akifuta machozi. Geb akavuta pumzi kwa nguvu huku amefunga macho. “Geb!” Nanaa akamuita.
“Upo
sawa?” “Hapana Nanaa.” Nanaa akakausha machozi, kisha akamshika mkono.
“Pole Geb. Naanimi kila kitu kitakuwa sawa. Pole.” Geb akataka kumkumbatia
lakini akasogea nyuma kidogo kama kumkwepa. Na Geb akajua.
“Nitakuona baadaye kidogo. Naomba
niwahi Sinza nikamuone Zena.” “Naomba nikupeleke Nanaa.” “Hapana Geb. Haya ni
maisha yangu. Nimeshazoea hivi. Naomba niache niishi hivi. Huko bado sijafikia.
Nitakuona nyumbani baadaye.” Alikataa kwa upole, bila jazba. Akampita pembeni
yake, akafungua mlango, akatoka. Alimuacha Geb amesimama palepale ofisini
kwake.
~~~~~~~~~~~~~~
Alitembea mpaka kituo cha Fire,
akapata daladala za Sinza. Alimkuta Yasini anapika, akamwambia Zena amelala
ndani. “Basi nisimwamshe. Mwache apumzike tu. Nitampigia simu hata kesho.”
“Lakini ujue simu yako bado haijawa tayari.” “Mpaka lini?” “Nimepitia jioni
hii, sikumkuta fundi.” “Hamna shida. Nitawatafuta kwa simu ya mtu yeyote yule
atakayekuwa karibu yangu.” “Nashukuru sana Nanaa. Asante kwa kila kitu.” “Karibu.
Muwe na usiku mwema.” Wakaagana, Nanaa akarudi tena kutafuta daladala.
~~~~~~~~~~~~~~
Alipanda daladala nyingine mpaka
kituo kikubwa cha Mwenge ili kupata daladala ya Tabata. Hapo angalau hakupata
shida ya kupata daladala. Lakini alipoingia tu ndani ya daladala, mvua
ikamwagika. Nanaa akacheka moyoni. Akajua hiyo ameikwepa. Yakabaki maombi kuwa
ikatike hapo njiani ili akifika Mwenge asilowe. Lakini ikawa tofauti. Mvua
ilizidi kunyesha. Magari hayaendi. Mpaka anafika kituoni Mwenge, tayari giza
limeshaingia.
Ilimlazimu kushuka hivyo hivyo na
mvua ili kutafuta daladala za Tabata. Sababu ya mvua, daladala zikawa za shida
sana. Nanaa akabaki hapo anasubiri. Ilipokuja, ikabidi tu na yeye agombanie
kuingia ili atoke pale kituoni. Maana ni kama alisikia wakitangaza ndio
daladala ya mwisho kwenda Tabata. Akapata nafasi ya kusimama. Safari ikaanza. Ilichukua
zaidi ya masaa mawili kumfikisha Tabata Barakuda kwenye kituo cha mabasi ya
karibu na nyumbani kwa Geb. Foleni ilikuwa kubwa sana.
Akavuka barabara huku anakimbia mpaka
getini kwa Geb. Akashangaa geti linafunguliwa mara tu alipojitambulisha kuwa yeye
ni Nanaa. “Labda wameanza kulijua jina langu.” Nanaa akawaza wakati
anaingia. Alishakuwa amelowa sana, akaona hamna sababu ya kukimbia tena.
Akaanza kujivuta taratibu mpaka ndani. Kwanza alikuwa amechoka. Wakati anavua
viatu na kuacha pochi yake ili ajikaushe, Geb akatoka na taulo lake. “Pole.”
“Asante.” “Sasa mbona ulikuwa hukimbii?” “Niliona haina haja tena. Nilishaloa.”
Nanaa akajibu. “Jikaushe na taulo.” Nanaa akapokea. “Asante.” “Njoo ndani.”
“Nachuruzika sana maji. Ngoja yapungue kidogo. Nitalowesha nyumba nzima.”
“Utakohoa Nanaa. Ingia ndani. Tutakausha tu.” Nanaa akabaki akifikiria huku
akijikausha taratibu. “Nanaa! Acha ubishi basi.” Akacheka kidogo, kisha
akaingia ndani. Alikuta kila mtu yupo hapo sebuleni wamejifunika na vikombe vya
chai pembeni.
“Shikamoo mama.” Akamsogelea mama G.
“Poleni na kazi.” Akimaanisha Danny na Grace. “Marahaba. Simu bado haijapona?”
“Mimi nahisi huyu fundi ananichezea mama. Kesho naenda kuchukua simu yangu
hivyo hivyo.” Nanaa akaendelea. “Kwani nilipokupigia si tulisikilizana kama
kawaida?” Nanaa akauliza. “Nilikuwa nakusikia vizuri tu.” “Basi naenda
kuichukua simu yangu, asinichezee akili.” “Si umesema imepasuka?” Mama G
akaendelea kuhoji. “Nitaifunga na tape.” Mama G akacheka. “Nanaa wewe!”
“Wanaweza kuniharibia zaidi bure, wanitie hasara ya mwaka. Wakati mimi sina
bajeti ya simu sasa hivi. Ujue naweza kusoma jumbe na kuona kila kitu?” Geb
moyo ukampasuka. “Basi hiyo nzima kabisa.” “Sasa je?” Mama G akacheka.
“Nenda kabadili nguo uje ule.” “Hilo
ni kosa ambalo sitafanya.” Nanaa akajibu huku akielekea chumbani kwake. “Nina
usingizi, nusura nipitishwe kituo mama. Yani nilisimama mpaka kituo kimoja
kabla ya kushuka ndipo nikapata kiti. Ile kukaa tu, usingizi mpaka konda
ilibidi aniamshe kuniuliza. Nikajihisi nililala kizembe labda akaniona.” Mama G
akacheka. “Kweli mama! Sasa kwa nini anifuate mimi?” “Au labda ulikuwa ukikoroma
sana mpaka ukasumbua abiria wengine?” Nanaa akacheka mpaka akasimama huko
koridoni.
“Mama wewe!” “Kumbe! Sasa kwa nini
uamshwe wakati sio mwisho wa daladala?” Nanaa akatulia kidogo akifikiria aliyosema
mama G, kisha wakamsikia akicheka huko koridoni. “Umekubali mwenyewe.” “Bwana
sijakoroma mama! Acha kunitia hofu ukanifanya nishindwe kulala.” “Kula kwanza
ndio utalala vizuri.” “Hapa nipo hoi mama yangu. Hamna jinsi naweza kupitisha chakula
hapo kooni kikapita kwenda huko tumboni. Natamani tu kitanda. Acha tu nilale
mpaka kesho.” Nanaa akaanza kukohoa.
“Nimekusikia unakohoa Nanaa! Kunywa
hata chai upate joto. Mvua hiyo.” “Sidhani. Huko hospitalini walikuwa wanawasha
AC kwenye baridi kali kweli. Ili kushusha homa ya Zena. Nahisi huko ndiko
nimepata hiki kifua. Usijali mama yangu. Nitapona tu.” Wakamsikia amefungua
mlango wa chumbani kwake. Alikuwa akiongea na mama G akiwa nje ya chumba chake.
Hata hakuoga. Alivua tu zile nguo.
Akavaa nguo za kulalia, akajitupa kitandani. Geb akagonga, akaingia na
blangeti. “Hapo utakuwa umenisaidia. Mbona asante!” Geb akacheka. Akamfunika.
“Zito hilo! Mpaka raha.” Nanaa akasifia. “Asante Geb.” Geb akabaki
akimwangalia. “Nasinzia mwenzio.” “Wewe lala tu.” Hapo hapo Nanaa akalala. Geb
akamkusanyia nguo mbichi, akatoka nazo pale chumbani.
Habari Mbaya
Huenea Kwa Haraka.
“Sasa mbona wewe haupo kazini!?”
“Nilitaka kubaki na wewe.” Nanaa akakunja uso huku na tabasamu. “Yaani uache
kwenda kazini, ubaki na mimi!?” “Ndiyo.” Nanaa akatoa kicheko cha sidhani, huku
akifikiria na kumtizama Geb kama hana uhakika na anachozungumza. Akaondoka kurudi
chumbani kwake bila kuongeza neno na kumuacha Geb amesimama palepale.
Akaoga vizuri. Akavaa gauni la
kawaida tu lakini lilimkaa vizuri. Ni moja ya magauni aliyojinunulia mwenyewe.
Akaweka mafuta ya mdomo yenye rangi nyekundu kidogo. Akapulizia body sprey
aliyonunuliwa na Geb. Ilibidi kuachia nywele zake kwa kuwa bado zilikuwa
mbichi. Alikuwa amesukia rasta ndogo ndogo. Kwa hiyo akazifungua ili zikauke na
upepo tu. Akatoka akiwa amependeza.
“Njaa inauma!” Nanaa aliongea huku
akielekea jikoni. “Mama amekuachia kitu cha kula hapo jikoni.” Geb na yeye
akasimama, akamfuata huko jikoni. Akasimama na kumgeukia Geb. “Umependeza.” Geb
akamuwahi kabla hajazungumza kitu. Nanaa akamuona anawasiwasi usoni.
“Ni nini kinaendelea Geb!?” “Tupate
kifungua kinywa kwanza ndipo tuzungumze.” “Kama nikuhusu Rita, usiwe na
wasiwasi. Hata yeye nilimwambia asiwe na wasiwasi na mimi. Wewe endelea tu Geb.
Huna haja yakuacha kwenda kazini kwa ajili hiyo.” “Subiri kwanza Nanaa. Unasema
ulizungumza na Rita!?” “Ndiyo. Si yule mpenzi wako mliyekumbatiana na kupeana
mabusu mbele yangu? Ukanionea haya hata yakunitambulisha jina tu kwake! Ndiye
huyo huyo alinifuata mpaka hospitalini baada ya kunitumia picha zenu, na jumbe
zenu zote mlizokuwa mkitumiana siku ya jumapili asubuhi kabla ya kukutana.”
Nanaa akaendelea akiwa ametulia tu bila jazba.
“Amenitumia picha za familia yake na
yenu. Tokea Fili ni mtoto mchanga. Amenieleza kwa undani na kwa kituo juu ya
mapenzi yenu na mahusiano ya kifamilia mliyokuwa nayo. Urafiki kati ya mama
yenu na mama yake. Picha zao. Akaniomba niachane na wewe. Nimemuhakikishia
mimi si mpenzi wako. Na haitakaa ikatokea nikaja kuwa mpenzi
wako. Nimemuhakikishia hata kama kulikuwa na wazo lolote juu yako,
nikamuahidi Rita, NIMEFUTA. Nimemuomba msamaha na amenielewa. Akaondoka na kuniacha kwa
amani.” Geb alitamani kukaa chini.
“Kwa hiyo kama uliacha kwenda kazini
kwa ajili hiyo, naona mpenzi wako amekupunguzia kazi. Wahi tu kazini.
Maana hata mimi nikimaliza tu kula, naenda kazini. Nashukuru kwa ofa ya
mapumziko ya leo, lakini sina sababu ya kujilaza hapa kama mgonjwa.” Nanaa
akatulia kidogo, akajishika tumbo. “Halafu unajua nini? Nahisi tayari
nimeshiba. Ngoja tu niende kazini.” Nanaa akatoka pale jikoni. Aliingia
chumbani kwake akachukua nauli ya daladala, akatoka bila hata kugeuka nyuma.
Akaenda kazini.
~~~~~~~~~~~~~~
Geb alibaki amesimama palepale
jikoni. Akaamua kumpigia simu mama yake. “Vipi Nanaa? Mmeweza kuzungumza naye?”
“Nimeshindwa kabisa mama yangu. Kumbe Rita alimfuata mpaka hospitalini!
Amemueleza kila kitu. Nanaa anahabari zote juu yangu na Rita. Mahusiano yako na
wazazi wa Rita. Alimtumia picha za wakati ule tunakwenda kwao. Mbaya zaidi
ameambiwa na Rita sio mimi. Najuta mama, natamani kama mimi ndio ningekuwa
nimezungumza na Nanaa kwanza.” Geb alisikika amechoka sana.
“Umekula?” Ndilo
swali mama yake alilomuuliza. “Nilikuwa
namsubiria aamke tule naye. Lakini ameshindwa hata kula! Amesema ameshiba,
ameenda kazini.” “Nisikilize Geb. Wewe unamtaka Nanaa kwa kiasi gani?”
“Nampenda Nanaa, mama yangu. Ndiye mwanamke anayenijali mimi binafsi hata kama
nimemuudhi, ananijali. Anataka kuniona ninafuraha wakati wote. Namtaka Nanaa,
mama yangu. Nikuchanganyikiwa tu. Nilikosa sana.” “Basi nataka ukae chini. Kula
vizuri ushibe. Usichanganyikiwe. Nanaa anahabari ya upande mmoja tu kutoka kwa
Rita. Hajakusikiliza wewe. Ukishamaliza kula, mfuate kazini. Hakikisha unarudi
naye hapo nyumbani akusikilize. Usikubali kushindwa na Rita, ambaye ni mwehu
tu.” Mama yake akasisitiza.
“Unamaanisha nikamfuate Nanaa?”
“Ndiyo.” “Namwangaliaje?” “Tena hakikisha anakuangalia machoni. Unanisikia Geb?
Nanaa anakupenda. Sema amekasirika tu. Lakini ukifanikiwa kumtuliza, umempata.
Kula uende.” “Asante mama yangu. Nakwenda sasa hivi.” “Hapana Geb. Nimesema
kula kwanza.” “Siwezi mama.” “Basi ndio umemkosa Nanaa. Mimi nakujua Geb. Ukiwa
na njaa huwezi kuongea kabisa. Kula kwanza. Hata usiku hujala. Ungekuwa
umeshiba wewe, Nanaa asingekuponyoka hapo. Kaa chini kula.” “Sasa nile nini?”
“Vyakula vyote vipo mezani.” Geb akamshukuru mama yake akakata simu.
Akakaa, akala. Tena hakunywa uji.
Akala chakula cha mchana alichokuwa ametayarishiwa na mama yake. Akala matunda,
akaongeza na juisi ndipo akatoka. Hakumaliza hata lisaa tokea Nanaa atoke, na
yeye akatoka.
~~~~~~~~~~~~~~
Grace
akashitukia Nanaa anaingia ofisini kwake. “Uchovu umeisha?” Nanaa akacheka.
Lakini Grace alijua ile sio cheka ya Nanaa. “Ungeniona nilivyoamka nikagundua
ni saa nne asubuhi, ungenihurumia! Nusura nichanganyikiwe. Samahani mwaya.”
“Ungepumzika tu Nanaa.” “Grace wewe! Huko sijafikia mwenzio! Yaani siku ya kazi
kama sasa hivi eti nimekaa nyumbani napumzika! Uwiii! Baada ya kufanya nini?
Acha nifanye kazi tu.” Grace akacheka. “Haya. Funguo za ofisi yako hizi hapa.”
Nanaa akazichukua na kuingia ofisini kwake. Akakaa.
~~~~~~~~~~~~~
Baada ya muda kidogo, akasikia mlango mkubwa
unafunguliwa Geb anamuulizia kwa Grace. “Nanaa amefika hapa?” “Yupo ofisini
kwake.” Akamsikia akielekea kwenye ofisi aliyokuwepo. Akainamia kompyuta kama
aliyetingwa na kazi nyingi. “Na mimi nina haki yakusikilizwa Nanaa.” Geb
aliingia na kuanza kuzungumza bila hata salamu. Nanaa akabaki tu kimya. “Kama
uliweza kumsikiliza Rita, na mimi lazima unisikilize.” Kimya. “Nanaa!” Kimya. “NANAA!” Geb akaongeza
sauti. “Nipo kazini Geb! Naomba tuzungumze baadaye.” “Kwa hiyo umekubali
tuzungumze?” “Si unataka nikusikilize tu?” Nanaa akamuuliza. “Ndiyo.” “Basi
nitakusikiliza baadaye. Naomba niache nifanye kazi.” Geb akavuta kiti pembeni
yake akakaa.
Wakatulia kwa muda, Nanaa akishangaa haondoki. Akamuacha
tu. “Lakini nataka ujue, muda wakati Rita anazungumza na wewe, alikuwa
ameniweka jela.” Hilo likamshitua mpaka akamgeukia. “Rita!?” “Ndiyo. Rita
alinisingizia kosa la mauaji. Nikafungwa siku hiyo ya jumapili nikatolewa
jumatatu. Tena baada ya mama kuwafuata wazazi wake kuwabembeleza. Rita akataka alipwe
pesa. Amelipwa mamilioni ya pesa na Grace ndio mambo yakaisha.”
“Pole Geb. Pole sana.” “Ningefungwa kifungo cha maisha
Nanaa. Huwezi amini muda wote nipo huko rumande, nilikuwa nakuwaza wewe.
Nilikuwa nafikiria vile..” Geb akainama. Akaona machozi yanamtoka. Akamuhurumia
huku na yeye ameingiwa na hofu asijue ni hofu ya nini! Kwa mwanamke kulia ni
jambo la kawaida. Tena wakati mwingine wengine huchukulia kama ni ishara ya unyenyekevu.
Inapendeza. Lakini sio mwanaume, tena wakiafrica! Ukiona chozi lao na hawapo
msibani au mbele za Mungu, basi ujue kuna jambo zito limemsibu.
Akasimama na kumkumbatia. Ikawa zamu ya Geb kupata
faraja mikononi mwa Nanaa. Ni kama aliyekuwa amebeba mzigo mzito kifuani. Geb
kwa mara ya kwanza akajikuta anapoteza uasili wa mtoto wa kiume wa kiafrica.
Akalia bila kujizuia mbele ya mtoto wa kike, tena anayempenda. Nanaa alimsugua
mgongoni mpaka akatulia.
“Nina hamu na wewe Nanaa!” “Sijui nisemeje Geb.” Geb
akasimama. “Naomba niamini hakuna kilichotokea kati yangu mimi na Rita. Na wala
sikuwa nimekusudia kufanya chochote na Rita. Sema nilikutana naye kwa gafla.
Halafu nikashindwa niseme nini wakati sikuwahi hata kumtaja kwako! Wakati mara
ya mwisho kuagana naye, tuliagana naye vizuri sana. Kiukweli alikuwa mpenzi
wangu. Sijui alikwambia nini, lakini tulikuwa na mahusiano mazuri kuliko
uliyonikuta nayo na Liz. Wazazi walijua kwa hakika tutaona. Nilitaka tukutane
naye siku ya jumapili, niwekane naye sawa ndio tuzungumze. Aliiba namba yako kwenye
simu yangu. Baada ya kutaka nifanye naye mapenzi nikakataa, ndipo akaanza
kukulaumu wewe. Alinitia aibu yule msichana, hujawahi ona!” Nanaa akacheka
kidogo. Geb alimsimulia kila kitu akamuacha Nanaa na mshangao.
“Nisamehe Nanaa.” “Naelewa mimi bado mgeni sana kwako
Geb. Una maisha uliyoishi nyuma. Na mimi hivyo hivyo. Hatuwezi kuambiana kila
kitu kwa wakati mmoja. Lakini niliumia uliposhindwa hata kunitambulisha!” “Ni
kweli nilikosa Nanaa. Lakini nilikuwa sijui niseme nini! Nilijua nikianza
utambulisho, hata kwake kwako. Ingebidi niseme ni mpenzi wangu. Wakati
tulitengana zaidi ya miaka mitatu, nafikiri.” Geb akafikiria kidogo. Kisha
akaendelea.
“Mara ya mwisho tuna agana na Rita, yeye akirudi
nchini Canada kwa ahadi akirudi tuoane. Kwa kifupi hakuwa tu kama Liz. Rita
alikuwa mchumba wa kuja kumuoa. Baada ya ukimya wa miaka yote hiyo ndipo na
mimi nikamuona tena siku ile. Nilikuwa kwenye mshituko Nanaa. Nilitaka kwanza
nimsikie ndipo nijue jinsi yakumtambulisha kwako.” Nanaa akanyamaza.
“Sijui umenielewa?” “Nina swali Geb. Na ninaomba uwe
mkweli kwangu.” “Uliza tu.” Geb akajiweka sawa kupokea swali. “Endapo Rita
asingekugeuka kwa kiasi hicho, inamaana mngerudiana. Si ndiyo?” Geb alivuta
pumzi kubwa akaishusha taratibu. “Naomba niwe mkweli kwako. Kidogo
nilishawishika. Lakini kadiri masaa yalivyokuwa yakisogea bila wewe. Huku
nikijiambia ndio nitaachana na wewe niwe naye, ndivyo ugumu ulipoanza Nanaa.
Nimegundua siwezi tena kuishi bila wewe. Nakuhitaji wewe kuliko kitu kingine chochote.
Najua nilikosea tangia mara ya kwanza nilipomuona. Nakiri nimekosa. Nisamehe.”
Nanaa akanyamaza.
Akarudi kukaa alipokuwa amekaa tokea mwanzo. “Nanaa!
Nimeomba msamaha!” “Yameisha Geb.”“Unajua sio ninachokuulizia Nanaa!” “Unataka
kunisikia nikisema nini Geb?” “Nimekuwa muwazi kwako! Usiniadhibu. Unajua wazi
ningeweza kukudanganya. Lakini kwa kuwa nakupenda, sikutaka kukudanganya.
Usiniadhibu kwa hilo.” “Sikuadhibu Geb.” “Ila ni nini?” “Mbona nimesema
yameisha!?” “Nanaa!” Geb akalalamika.
Nanaa akamgeukia. “Nipo kazini Geb. Sina maisha
yakueleweka. Naomba niache ni focus.
Nisaidie shule yangu iishe na pia nisiharibu hapa kazini. Sitaki kujichanganya
sasa hivi.” “Sitakubali uchanganyikiwe Nanaa.” “Unakumbuka hiyo ni moja ya
ahadi ulizonipa ijumaa, jumamosi ukaishia kwenye mikono ya mwanamke mwingine?
Nakuamini vipi tena?” Nanaa alimuuliza bila jazba. Geb akabaki kimya.
“Nimesoma jumbe zako na zake mlizokuwa mkitumiana siku
ya jumapili asubuhi kabla yakukutana. Tena nimesoma kwa kurudia rudia, ili
nisije kukuelewa vibaya. Kilichonishangaza ni vile ulivyoweza kuamka jumapili
asubuhi, ukawasiliana na yeye, sio na mimi tuliyeachana nikiwa sina raha Geb!
Hukujali hisia zangu ila zake. Nimesikiliza mazungumzo yenu asubuhi ya
jumapili. Ulimwambia unamsikiliza yeye. Achague muda na wakati anaotaka yeye
ili mkakutane kwa kuwa alikwambia anahamu sana na wewe. Geb, tuwe wawazi. Mimi
sio mtoto mdogo. Mimi nimekuwa kimbilio pale unapohitaji. Lakini wanapokuwepo
watu wa muhimu kwako, nakosa maana. Hukunipa uthamani wowote kwa Rita.” Nanaa
aliongea kwa upole bila hata hasira. Lakini alijua ujumbe wake unafika.
Akaendelea.
“Sidhani kama ulikosea Geb. Nafikiri hakuna hisia za
penzi la dhati kwangu. Hujali hisia zangu. Na sishangai. Wewe sio wa kwanza.
Wanaume wote wanakuwa hivyohivyo kwangu. Nafikiri sikuwahi kubahatika kupata
mwanaume ambaye ananipa mimi kipaumbele. Ninachoogopa kwako zaidi, ni kwa
sababu nahisi naanza kukupenda. Utaniumiza na kunichanganya zaidi Geb.
Tafadhali naomba niache nitengeneze maisha yangu. Angalau hii shule iishe. Ili
na mimi niwe na kitu mkononi mwangu. Tafadhali Geb. Unajua nilikotoka.” Nanaa
akacheka kwa kujihurumia.
“Unakumbuka mvua ya jana uliyokuwa ukihofia nitalowa?
Tena mvua ya jiji la Dar, kwenye joto! Basi mimi nilikuwa nikilazwa nje. Kilimanjaro!
Kwenye baridi na mvua inaninyeshea usiku kucha ili nimalize kazi zangu. Asubuhi
wakiamka ndipo naruhusiwa kuingia ndani. Sio kulala, ninaingizwa ndani kuanza
kazi za ndani tena. Ujue hapo ni siku ya shule. Sio weekend. Na hapo ilikuwa ni juu yangu mimi. Niamue kurudi
kulala baada ya wao kuondoka au niwahi shule pengine nitakuja kukutana na hicho
kitanda usiku kama nitabahatika. Hakuna wakukulazimisha usome. Lakini
ilinilazimu mimi mwenyewe kwenda shule. Bila kujali kama nililala nikinyeshewa.
Na hapo bado mvua inanyesha nje. Ilinilazimu kujibidisha mwenyewe kwenda shule.
Nimefika hapa kwa shida sana Geb. Acha nisiharibu sasa hivi. Na nina hakika sio
nia yako kuniharibia maisha.” Nanaa aliongea taratibu bila jazba. Geb akatoka
akiwa amenywea kama maji.
~~~~~~~~~~~~~
Nanaa
aamua kuachia ngazi. Mapenzi yameshindikana kwa Geb ampendaye. Nini kitaendelea
akiwa bado anaishi nyumbani kwake?
Usikose
Muendelezo.
0 Comments:
Post a Comment