Akamuona anacheka. “Nanaa kwa
kupenda kucheka! Sasa unacheka nini?” “Mwenzio sijawahi kuishi haya maisha. Ila
nimeona kwenye movie.” Geb alianza kucheka huku akitingisha
kichwa. “Kweli tena. Sasa wewe unavyofikiria nani angenileta sehemu kama
hii? Au nani aninunulie magauni ya bei hii! Hata mimi mwenyewe najua
nimependeza.” Geb alizidi kucheka. “Kwa mara ya kwanza na mimi
nimevaa vitu vya dukani.” “Acha bwana Nanaa.” “Kweli tena. Hata nilivyojaribu
kulala, usingizi ulikuwa hauji.” “Sababu ya vitu vipya?” “Sasa je? Yaani mimi
mwenyewe ndio nimekuwa wakwanza kutoa lebo zake! Tena vilebo vyenye bei! Acha
utani Geb. Sijui kama usiku nitalala.” Geb alikuwa akicheka huku
akimwangalia Nanaa, haamini.
Walipata wakati mzuri sana wa pamoja.
Ilikuwa siku ya kufahamiana zaidi. Waliambiana siku za birthday zao. Wakaagiza
vinywaji. Wakaanza kunywa huku wakicheka na kuongea mambo yao. Siku hiyo hata
Geb aliagiza chakula. Akala. Nanaa alishaanza kuchoka. Wakaamua waondoke tu.
Yaliyojiri!
K |
wa kuwa walikaa meza ya mwisho kabisa iliwalazimu kupita meza
kadhaa ili kutoka hapo. Wakati wanatoka Geb akiwa ametangulia kidogo, Nanaa
akasikia dada mmoja akiita jina la Geb kwa mshangao na furaha. Akasimama,
akamkumbatia Geb na kumbusu mdomoni huku akionekana amejaa furaha zote.
Alimtambulisha kwa marafiki zake wengine wawili waliokuwa wamekaa nao. Wote wakasimama.
“We heard so much about you!” Mmoja alisema na kumpa mkono
Geb. “Finally! Nice to meet you.” Mwingine akaongeza kwa lugha
hiyo ya kingereza. Na yeye akampa mkono.
Japokuwa Nanaa hakuwa akijua kuongea
kingereza, lakini hakuwa na tatizo la kuelewa hata kidogo! Na aliliona lile
busu la mdomoni na vile yule msichana alivyomkumbatia Geb kwa nguvu. Hakuwa
rafiki wa kawaida kwa hakika, alikuwa mpenzi. Nanaa akabaki amesimama pale
nyuma ya Geb akiangalia wale warembo waliokuwa wamesimama wakimshangilia Geb.
“Umerudi lini?” Geb
akauliza. “Sina muda mrefu hapa nchini. Nilikufuata kule mlikokuwa mkiishi
zamani na mama. Nikaambiwa mlishahama muda mrefu. Sikujua nitakupata vipi!” Yule
msichana aliyemkumbatia Geb akaongeza akionyesha bado yupo na shauku
kubwa. “Naomba namba yako ili kesho nikutafute.” Geb akamtajia bila
shida. “Basi nitakupigia kesho.” “Sawa. Usiku mwema.” “Na wewe pia Geb.
Nimefurahi sana.” Akatoa busu jingine la mdomoni. Wakaagana tena. Wale
wasichana wakarudi kukaa. “OMG! Nimemuona Geb! Yiiiiiii!” Walimsikia
yule dada akishangilia wakati wanaondoka.
Kulikuwa na ukimya mkubwa sana kati
yao. Nanaa alianza kusikia baridi mpaka ndani ya mifupa. Alijawa hofu, wala si
wivu. Geb alimfungulia mlango, akaingia. Na yeye akaingia. Pakawa kimya kabisa
ndani ya gari. Walitoka pale wakiitafuta Morogoro road. Hapakuwa na maongezi
mpaka walipokuwa wakikaribia maeneo ya Fire, simu ya Nanaa ikaanza kuita kutoka
kwenye pochi. Ilikuwa inaelekea saa 4 usiku. Akatoa simu yake, jina lilionyesha
ni Zena. Kwa hali aliyokuwa nayo, ikabidi apokee tu.
~~~~~~~~~~~~~~
“Haloo!” Sauti ya kiume. “Zena!?”
“Hapana. Mimi Yasini. Zena mgonjwa.” “Nini tena!?” Nanaa akauliza. “Ni
habari ndefu. Lakini mpaka nakupigia wewe, ujue nimekwama.” “Yeye yuko wapi?”
“Yupo hapa nyumbani. Ameniomba nikupigie. Ukiweza uje.” “Saa hizi!?” Nanaa akajikuta anashangaa kwa sauti huku akiangalia muda
kwenye simu yake. “Ingekuwa si muhimu hivyo
nisingekusumbua Nanaa. Nimekwama. Naomba msaada.” “Labda niulize, ni msaada wa
namna gani?” “Zena ni mgonjwa Nanaa. Tupo peke yetu. Sina msaada. Nahisi
kuchanganyikiwa.” “Kwa nini msiende hospitalini?” Akaendelea kuhoji.
“Labda ukija utaelewa zaidi.” “Sasa
hivi ni saa 4, Yasini! Hata kama nataka kuja leo, nakujaje?” “Nitakufuata.”
“Mmh! Mbona unaniogopesha?” “Naomba msaada wako.” “Lakini sasa hivi mimi
naelekea Tabata Barakuda. Sipo kwa kaka. Jeff anapafahamu.” “Basi Jeff atakuja
kukuchukua.” “Naomba mwambie basi aje kama baada ya dakika 45 kuanzia
sasa.” “Sawa. Nakushukuru sana Nanaa.” Nanaa hakujua
ajibu nini. Akakata simu.
~~~~~~~~~~~~~~
“Zena ni mgonjwa. Anahitaji
msaada wangu. Inabidi niende.” Nanaa akavunja ukimywa. “Nimesikia
mazungumzo yenu. Kwani wazazi wake wako wapi?” “Hapa hapa Dar. Lakini Zena huwa
anawadanganya anasafiri kikazi, kisha anaishia nyumbani kwa Yasini. Nafikiri
ndio huko alipoanza kuugua. Sijui!” “Kuwa mwangalifu. Chochote kisije
kikatokea, ukaja kujulikana na wazazi wake kuwa na wewe unahusika.” Nanaa
akanyamaza.
“Ningeweza kukupeleka.” “Ni usiku
sana sasa hivi. Acha tu waje wanichukue wao wenyewe. Nisikusumbue zaidi. Leo
inatosha kwa ajili yangu. Kapumzike tu.” Wakanyamaza. Hapakuwa na
mazungumzo mengine mpaka wanafika nyumbani.
~~~~~~~~~~~~~~
Hawakukuta mtu pale sebuleni. Lakini
wakasikia Danny na mkewe wakiongea na Fili chumbani kwao. Wakajua na wao ndio
wamerudi nyumbani. Akawahi chumbani kwa mama G. “Mbona upo
hivyo?” Mama G akamuuliza Nanaa. Nanaa akatabasamu kidogo. “We Nanaa?
Mbona umenyongea hivyo?” “Unamfahamu yule rafiki yangu Zena?” “Zena wa Yasini,
Yasini rafiki yake Jeff?” Mama G akajibu nakumfanya Nanaa acheke kidogo.
“Sasa Zena ni mgonjwa sana. Yasini
kanipigia simu wakati tupo njiani.” Nanaa akamuelezea kwa
kifupi. “Kwa hiyo wanakuja kukuchukua sasa hivi!?” “Yasini anaonekana
amekwama.” “Lakini kuwa makini.” “Hata Geb ameniambia hivyo hivyo. Ngoja nifike
huko ndio nitajua chakufanya. Nitakujulisha.” “Sasa utarudi lini?” “Nikifika
huko ndipo nitajua mama. Nitakupigia kesho. Najua sasa hivi ni usiku. Mpaka
nifike kwao, tuzungumze na kama ni wakumpeleka hospitalini tuende, sio leo.
Mpaka kesho. Ngoja nikajiandae.” Nanaa akatoka.
Akarudi chumbani kwake. Akabadili
nguo. Akavaa suruali yake ya jinsi na top ya kawaida tu. Akachukua vitu muhimu
alivyojua angehitaji. Akatoka pale chumbani akaenda kumuaga mama
G. “Nanaa! Kuna nini?” Mama G akauliza tena. “Sijui
mama.” Nanaa akajibu kwa unyonge. Mama G akabaki
akimwangalia. “Naomba niagie na kwa wengine. Ngoja mimi nitoke ili asije
fika, halafu mlinzi akaja kuanza kusumbua. Usiku mwema mama.” Nanaa
akatoka bila kusubiri jibu.
Alipotoka tu, mama G akamuita Geb.
Geb akaja, na yeye akiwa ametulia kabisa. “Kaa hapo.” Geb
akakaa. “Kuna nini?” Mama yake akahoji. “Nimekutana na Rita,
mama.” “Rita! Rita yule aliyekuwa mpenzi wako akaenda masomoni?” Mama G
akashituka sana. “Ndiyo. Amerudi. Anasema alikwenda kunitafuta mpaka pale
tulipokuwa tukiishi mimi na wewe.” “Pale alipotuacha?” “Ndiyo. Anasema
akaambiwa tulihama.” “Sasa?” “Sijui mama yangu. Nahisi akili ilisimama kwa
muda. Unajua nilishindwa hata kumtambulisha Nanaa! Tumeachana pale na Rita, nimeshindwa
hata kujua namwambia nini Nanaa.” Mama G akavuta pumzi kwa nguvu na
kuzishusha.
“Alikuwa wapi na yeye siku zote
hizo!?” “Hata sijui, mama yangu! Amechukua namba yangu. Najua
atanitafuta.” Wakatulia kidogo, wote wakiwa wamepigwa na butwaa. “Lakini
uzuri hujafika mbali na Nanaa. Ni kumwambia ukweli tu, ataelewa.” Geb
akabaki kimya. “Naomba nikapumzike mama yangu.” “Pole. Mimi naelewa
kabisa. Lakini kuwa sana makini na maamuzi yako. Ujue wazi, utakachoamua sasa
hivi, hakuna kurudi tena nyuma.” “Nanaa ameshaondoka?” Geb akauliza
akionekana wazi ameishiwa nguvu. “Ndiyo. Amesema watakuja kumfuata. Hataki
waje halafu mlinzi aje asumbue ndani. Pengine yupo hapo nje ya geti.” Geb
akafikiria kwa muda akatoka.
Alisimama pale sebuleni kwa muda
akifikiria. Mwishowe akaamua kutoka kumfuata Nanaa, angalau ahakikishe yupo
salama pale nje. Akamkuta amekaa nje kabisa, kwenye kipande cha tofali
amejiinamia akichora chini. Geb akamuhurumia. Akamsogelea. Alipomuona akasimama
kwa haraka. “Vipi?” “Bado hajafika. Nafikiri yupo karibu
kufika.” Nanaa akajibu. Akabaki akimwangalia asijue aseme
nini. “Utarudi leo?” “Sijui.” Nanaa akajibu. “Basi nitakaa na
wewe hapa mpaka aje. Ili usiwe peke yako.” “Naona mlinzi anakuja kunichungulia
kila wakati. Hamna neno. Nenda kapumzike tu.” Geb akajivuta mpaka ukutani,
akaegemea. Nanaa akarudi kukaa. Kimya.
Baada ya muda Jeff akafika. “Uwe
na usiku mwema.” Nanaa akamgeukia Geb. “Asante na
wewe.” Hapakuwa na kupeana mkono wala busu. Nanaa akapanda ndani ya gari
ya Jeff akaondoka. Geb akasimama pale kwa muda kama aliyepigwa na bumbuazi.
Asijue chakufanya, mwishoe akaingia ndani.
~~~~~~~~~~~~~~
Nanaa alipelekwa mpaka Sinza
anapoishi Yasini. Mbali na salamu, hawakuzungumza chochote na Jeff. Alimkuta
Zena ni mgonjwa sana. Anatokwa damu nyingi, mpaka ameishiwa nguvu. “Kuna
nini?” Akamuuliza Yasini mara alipoingia chumba alichoelekezwa na
Jeff. “Zena alishika mimba. Imetoka.” “Mlienda hospitalini?” “Tulimpeleka
hapo kwenye hicho kihospitali hapo kama zahanati. Tukamkuta daktari wa hapo,
akampa dawa. Alimwambia kwa kuwa mimba ilikuwa ni changa, atapona tu. Jioni hii
akazidiwa. Nimemrudisha hapo, kamchoma sindano akasema turudi nyumbani. Lakini
analalamika maumivu makali ya tumbo.” Nanaa akavuta pumzi kama na yeye
yupo kwenye mshituko.
“Alimchoma sindano ya nini?”
“Kupunguza maumivu, na kushusha homa.” “Kama ameanza kupatwa na homa ujue
amepata infection. Lazima tumpeleke hospitali kubwa na ya maana. Sio hizi
hospitali za mtaani.” “Zena hataki. Anasema anaweza kukutana na mtu
anayewafahamu wazazi wake.” “Naomba utupishe Yasini.” Yasini akatoka,
akamuacha Zena na Nanaa.
“Pole Zena.” “Nahisi nitakufa Nanaa.” Zena
aliongea kwa sauti ndogo. “Kwa nini hutaki kwenda ukatibiwe? Nashauri
ukatibiwe kwa garama yeyote ile ili uishi kuliko ufie hapa? Hata kama wazazi
wakijua si basi!” “Watamchukia Yasini. Na kunitenga naye maisha.” “Sasa bora
lipi. Ufe umtie Yasini matatizoni, afungwe kwa kukufungia wewe humu ndani mpaka
kifo, au uende hospitalini ukatibiwe? Hata kama sasa hivi wazazi watakasirika,
ukipona si utarudiana na mpenzi wako?” Zena akafikiria, akaona Nanaa
yupo sahihi.
Wakaamua kwenda hospitalini. Yasini
akaendesha mpaka hospitali ya Agakhani. Zena akapokelewa kwa haraka, akaonana
na daktari. Yasini alieleza kila kitu. Daktari akauliza kama Zena alisafishwa
baada ya mimba kutoka. Ikawa hapana. Akasema ni infection na ni lazima
asafishwe kwa kuwa mimba haikuwa ndogo kama walivyoambiwa. Zena akaingizwa
chumba cha upasuaji kusafishwa kwa haraka.
Alitolewa huko akiwa analia maumivu.
Mpaka saa 8 usiku, ndipo Zena anatulia, akiwa ameshapewa kitanda chake.
Hapakuwa na jinsi Nanaa angemuacha Zena akiwa kwenye hali hiyo. Akakubaliana na
Yasini yeye abakie na Zena pale hospitalini amuuguze mpaka atakapo ruhusiwa.
Yasini awe anakuja na kuondoka. Matibabu ya Zena yakaendelea, Nanaa akiwa
muuguzaji.
Ilibidi kuanzishiwa antibaiotic kali
ili kutoa ile infection. Zena alikuwa ameshapoteza damu nyingi. Yasini na Jeff
ilibidi kutoa damu ili aongezewe. Nanaa alikuwa akihangaika na Zena, mchana na
usiku. “Kwa nini nisimpigie hata mama simu?” “Ni afadhali uondoke uniache
peke yangu kama umechoka, kuliko kuwaambia wazazi wangu. Wataniua nikiwa
hapahapa hospitalini.” Zena alikataa kabisa.
Geb na
Rita.
Siku inayofuata, Geb aliamshwa na ujumbe mzuri sana kutoka kwa
Rita. ‘I choose you. And I will choose you, over and over and OVER.
Without pause, without a doubt, in a heartbeat. I will keep choosing you’. Geb
alifikicha macho, akarudia ule ujumbe tena. Haukuwa na jina lakini alijua
aliyetuma ni Rita. Msichana waliyekuwa kwenye mahusiano ya muda mfupi, lakini
yalikuwa mapenzi ya moto kweli kweli.
~~~~~~~~~~~~~~
Geb alikutana na Rita wakati
akitafuta kazi, mara aliporudi nchini Tanzania. Alielekezwa ofisini kwa baba
yake Rita, akaangukia mikononi kwa Rita. Alipojitambulisha kwake kuwa
anamtafuta Mzee Simba na anashida ya kazi, akidhani Rita ni secretary wake.
Akamkarimu sana Geb. Alimpa kinywaji wakati akimsubiria baba yake.
Alipofanikiwa kuonana na Mzee Simba, alimwambia ni kweli anatafuta mtu, lakini
yeye Geb ame ‘over qualify’. Vyeti vyake vilikuwa vikubwa sana kwa kazi yake.
Kwa kuwa Geb alikuwa na shida sana ya pesa, akamuomba ajishikize kwa siku
chache, kwa mshahara huo huo mdogo mpaka atakapopata kazi yakueleweka.
Mzee Simba akamkubalia, akampa
majukumu yanayofanana na yeye. Akawa kama msaidizi wake. Ni kweli ofisi ilikuwa
ndogo. Wakawa wao watatu tu wakisaidiana pale ndani. Rita kama muhasibu, na Geb
akifanya kazi zozote atakazopewa kwa siku hiyo. Muda mwingi wakajikuta peke yao
pale ofisini. Geb na Rita.
Rita alikuwa amebakisha kama miezi
mitatu tu arudi chuoni alipokuwa akisoma nchini Canada. Alirudi nchini kwa
mapumziko baada ya chuo kufungwa. Na ndipo alipokuwa akisaidia kazi kwenye
biashara za baba yake aliyekuwa aki supply vitu mashuleni. Mzee huyo alitafuta
tender kwenye mashule mengi ya hapo jijini, akawa akipeleka vitu huko. Kuanzia
vitu vya maofisini mpaka vyakula. Kwa shule za kutwa na bweni. Na Geb akawa
ndio mnunuaji na msambazaji. Hakuwa akilipwa pesa nyingi sana. Lakini
ilimtoshea nauli ya kumtoa na kumrudisha nyumbani. Ikampunguzia yale mawazo
yakukaa tu nyumbani. Na angalau aliweza kuchangia chakula cha nyumbani kwa
wakati ule kabla hajapata kazi BOT.
Mzee Simba alishajua Geb ni kijana
mwenye ndoto kali. Kwa hiyo tangia mwanzoni alionyesha kumuheshimu sana Geb.
Alijua siku Mungu atakapomfungulia milango, hatakuwa mtu wa kawaida. Akamfanya
kuwa ni kijana wake wa karibu sana. Huku akimuuza kwa Rita. Asijue hata Rita
alishaanza kumpigia mahesabu Geb. Mzee Simba akazungumza na mkewe kufanya
juhudi za makusudi kumkaribisha Geb na familia yake nyumbani.
Mahusiano ya karibu yakaanza. Hata
mama G akawafahamu wazazi wa Rita. Wakaheshimiana sana. Ndani ya muda mfupi,
Rita na Geb wakaanza mahusiano. Mzee Simba alipokuwa akitoka na kuwaacha wao
wawili, mapenzi yaliendelea pale ofisini. Penzi likakolea kati yao. Iwe asubuhi
iwe jioni, walitaka kuwa pamoja. Tena si tu kuongea, Rita alitaka penzi la Geb.
Rita Simba
R |
ita akiwa ameshaishi nchini Canada kwa miaka takribani 2, akisomea
shahada yake ya kwanza, na akiwa na malengo ya kusoma mpaka shahada ya 3,
nchini humo. Aliona ni vyema kutafuta uraia wa huko ili kwanza kupunguza ada.
Asome kama raia wa hapo, na sio ‘International student’ ambapo
ilimgarimu sana baba yake. Na yeye ilimbidi kufanya kazi nyingi ili kuweza
kujikimu.
Njia moja wapo aliamua kutafuta raia
wa nchini hapo ili amuoe. Alijua akiolewa na raia wa hapo nchini Canada,
ataweza kubadili uraia kwa haraka. Atapata ‘Permanent Resident’,
itakayompunguzia garama kubwa sana. Kwa hiyo Rita alitafuta kijana wa hapo hapo
nchini Canada. Japokuwa hakuwa akimpenda sana, lakini akaamua aolewe ili
afanikishe mipango yake. Alifanya harusi ya kimya kimya hata wazazi hawakuhudhuria.
Japo alishawashirikisha na kuwaeleza mipango yake. Kwa hiyo wazazi wake walijua
anaolewa ndoa ya kupata uraia nchini Canada, lakini si huyo kijana aliyemuoa
wala wazazi wake huyo kijana wa Canada waliojua ndoa hiyo ina hila.
Ili kuaminisha serikali hiyo ya
Canada kuwa ndoa yao ni ya kweli na si yakutaka uraia tu, Ilimlazimu Rita
kupiga picha kadhaa za harusi hiyo na mumewe huyo mzawa wa nchi hiyo.
Wakatafuta sehemu ya kuishi pamoja. Maisha yakaanza wakiwa wote wanatumia
anuani moja. Kama mke na mume. Akapata uthibitisho wakutosha kuwa anahaki ya
kupata vibali vya kuishi nchini humo kwani ameolewa na raia wa nchini
hapo.
Mungu akawa upande wa Rita, vibali
vya kusafiria na kufanya kazi kavikukawia. Ndio kwa mara ya kwanza tokea afike
nchini humo kwa miaka miwili, akawa amerudi nyumbani. Na ndipo akaangukia
mikononi mwa Geb. Akiwa na mume nchini Canada na amekolezwa kimapenzi na Geb
ambaye ndio alikuwa hana kitu, anawafanyia kazi hapo ofisini kwao. Akaadhimia
kuficha siri ya huko nchini Canada. Akajua kwa hakika, baada ya miaka mitatu ya
kumiliki hiyo Permanent Resident Card, ataweza kuachana na mumewe huko
nchini Canada, na kuja kuolewa na Geb.
Hakutaka kufanya kosa kote kote. Rita
akahakikisha hashiki mimba ya Geb wala ya mumewe. Kwa hiyo alilala na Geb kwa
kutumia kondom wakati wote. Mapenzi yakanoga kati yao. Wazazi wakafahamiana.
Hata siku za sikukuu, walialikwa nyumbani kwa Mzee Simba. Kwa hiyo picha za
kina Grace, Danny, Fili akiwa mdogo kabisa, mama G na Geb, zilijaa nyumbani kwa
kina Rita. Kwani kwa muda mfupi sana, wakawa ni familia moja yenye umoja,
wakijua vijana wao siku moja wataoana.
Ugumu ulianza pale Rita alipotakiwa
kurudi chuoni au kwa mumewe. Akaihirisha muhula mmoja. Akaendeleza penzi jijini
na Geb. Lakini siku hazigandi, lazima Rita arudi kwa mumewe. Ilikuwa ngumu
sana. Geb alimuaga kama mchumba wake, kwa makubaliano ya kuwasiliana na Rita
na kurudi kumtembelea hapa nchini mara kwa mara. Kumbe Rita anarudi kwa
mumewe asiyejua kuwa anatumiwa tu.
Hapakuwahi kutokea ugomvi wala tatizo
kati ya Rita na mumewe. Japokuwa aliolewa kwa hila, lakini Rita hakuwa na
mahusiano yeyote nchini Canada. Kwa hiyo alijituliza kwa mumewe. Na alikuwa
mtiifu sana akihakikisha lolote halitokei kabla hajakamilisha mipango yake
yakuwa raia. Alimpa mapenzi mumewe. Yule kaka alijisifia kuoa mwanamke wa
kitanzania anayempenda.
Rita alimpa yale yote aliyojua
wanawake wa kizungu hawawezi kumpa mwanaume. Si kitandani tu, hata kwenye mambo
ya chakula. Ukweli ndoa ya Rita ilikuwa nzuri huko nchini Canada. Na uzuri yule
mwanaume alikuwa mfanyakazi. Kwa hiyo kulikuwa na unafuu mkubwa sana kimaisha.
Ada ilipungua. Tena mlipaji akawa mumewe. Rita aliacha kazi kabisa, akatulia na
shule tu. Matatizo ya ndoa yake yalianza baada ya Rita kurudi kwa mumewe akiwa
ameshachanganywa na penzi la Geb.
~~~~~~~~~~~~~~
Wakati Geb anasoma ule ujumbe, Rita
akampigia. “Nina hamu na wewe Geb. Mpaka nasikia kuchanganyikiwa.” Geb
akacheka kidogo. “Tunaweza kuonana leo?” Rita akauliza. “Ndiyo. Naomba
tukutane palepale Sea Cliff.” Geb akakubali. “Saa ngapi?”
“Wewe tu. Utakapokuwa tayari unijulishe nije.” Rita
akafurahi sana. “Basi tukutane kwa chakula
cha mchana.” “Hamna shida.” Geb
akakubali.
Geb alikwenda kumwambia mama yake
kuwa hatakwenda kanisani siku hiyo, anakwenda kukutana na Rita. Mama yake kama
kawaida hakuchangia neno. Akanyamaza. Grace alikuwa akisikiliza wakati
anamalizia kifungua kinywa chake pale pale jikoni. Akasimama ili kuweka vyombo
alivyokuwa akitumia kwenye sinki. “Naomba nikwambie kitu Geb.” Geb
akamgeukia akitaka kumsikiliza dada yake kwani alikuwa amesimama na mama yao hapo
jikoni. “Mimi nakufahamu Geb. Naomba uwe makini.” Kama kawaida yake, Grace
akawa amemaliza. Na wao wakajua amemaliza, akaondoka. Mama G akageuka pale
alipokuwa jikoni, akaendelea na shuguli zake bila hata kuongeza neno. Geb
akatoka.
Rita Na Geb.
A |
limkuta Rita akimsubiria sehemu ya kuegesha magari. Geb alijua
wazi amechanganywa na gari yake. Alibaki amekodolea macho ile
gari. “Unaonekana mambo yako safi Geb!” Geb akatabasamu. Rita
akamsogelea na kumbusu tena. “Si tutachukua chumba, tukalie chakula
chumbani?” Rita akauliza. “Naomba tukae kule nje kwanza, halafu baada
ya hapo ndio tutajua.” Rita akashangaa kidogo. Geb alikuwa mtu
wakuchangamkia penzi lake. Iweje leo asite? “Au kwa kuwa hatujaonana
muda mrefu anataka kujua nilikuwa wapi, au ananikwepa kwa ajili ya yule
msichana aliyekuwa naye jana usiku!” Rita akawaza.
Wakaongozana mpaka sehemu yakulia
chakula. “Vipi mama, Grace, Danny na Fili? Wanaendeleaje?” Rita akauliza
wakati tu wanakaa. “Hawajambo. Waliniacha tokea asubuhi wakati wao
wanaenda kanisani.” “Nina hamu nao. Itabidi nije kuwaona.” Geb akatabasamu
tu. Muhudumu akasogea. Rita akaagiza red wine, Geb akaomba aletewe chupa ya
maji ya Kilimanjaro.
“Umerudi lini?” Geb
akamuuliza. “Sio muda mrefu sana.” Akakwepesha lile swali, Geb
akajua. “Shule imeisha?” “Bado. Nilipunguza madarasa. Nilikuwa na mambo
mengi. Nikaona nipunguze mzigo wa shule. Si unakumbuka nilikwambia nilikuwa
nachukua madarasa mengi?” “Nakumbuka uliniambia ilikuwa ni moja ya sharti kama International
Student.” “Husahau!” Rita ni kama alisifia. Geb akacheka.
“Sasa nilipobahatisha kupata
ile Permanent Resident, nikaona nisijiue!” “Okay.” Geb
akajibu huku akimwangalia. Rita akacheka. “Kwa hiyo una mpango wa kurudi
lini tena Canada?” Geb akarusha swali jingine. “Sasa hapo inategemeana na wewe
Geb. Tukiamua nibaki, na kama utaweza kunipa support yako, naweza kubaki
nikasomea hapa. Kwanza naona mambo yako sasahivi, safi. Hebu nipe siri ya
mafanikio.” Muhudumu akaleta vinywaji. Rita akaanza kunywa wine yake.
“Niambie Geb, unafanya nini?”
“Nilipata kazi BOT.” “OMG!” Rita akashangaa sana. Akasimama na kwenda
kumpa busu jingine. “Hongera sana. Nilikwambia utafanikiwa tu. Ndio maana
umebadilika Geb! Unaonekana mambo sio mabaya! Nipe tano.” Wakagonga.
Muhuhumu wa chakula akawasogelea na Menu.
“Yaani mimi leo nina hamu ya vyakula
vya baharini tu. Sina haja hata yakusoma menu. Niletee chips, shrimps wa
kukaanga na samaki wakuchoma.” Rita akamuwahi muhudumu. Akamgeukia na Geb.
Geb kama kawaida yake akasema akiwa tayari ataagiza. Alishakunywa uji
aliotengenezewa na mama yake, akawa yupo tu sawa. Muhudumu akaondoka.
“Kwa hiyo sasa hivi mnaishi
wapi?” Rita akatupia swali mara baada ya muhudumu kuondoka huku akinywa
wine yake. “Tunaishi Tabata.” “Usiniambie kama ulijenga!” Geb
akatabasamu. “Hongera sana Geb. Am so happy for you! Sasa kina
Grace bado wanaishi kulekule kwenye nyumba ya chumba kimoja na mumewe?”
“Hapana. Tunaishi wote.” “Waw! Kumbe! Safi sana kama uliamua kuwasaidia. Kile
chumba kilikuwa kidogo, na mtoto! Bado mumewe anasoma tu?” Rita akauliza
tena. “Alimaliza shule yake.” Geb akajibu taratibu.
“Afadhali atafute na yeye kazi
asaidie familia yake. Umeona sasa? Karibia unatua mzigo mmoja. Shemeji yako
akipata kazi, anatafuta hata nyumba ya kupanga wakati anajenga kwake. Na mama
naye?” Rita akaongeza swali jingine. “Mama yupo mzima kabisa.”
“Jamani mama yangu! Nina hamu naye kweli. Mama ana roho nzuri yule! Ndio maana
Mungu alimjalia hata umbile zuri. Tena akamrithisha na dada yako.” Rita
akacheka. “Nimefurahi sana kukuona Geb. Jana nilimwambia mama. Akaomba
kama leo tutawahi kutoka hapa, upitie kumsalimia. Maana nilimwambia sijui
nitakuachia saa ngapi! Nina hamu na wewe kweli Geb. Kwa nini tusiende kula
chakula chumbani tu. Najua hutashindwa kuchukua chumba hapa, wewe mfanyakazi wa
BOT!” Rita akagonga.
Chakula nacho hakikukawia. Baada ya
dakika 20 tu, kikaletwa. “Kinaonekana kizuri!” Rita
akasifia. “Unauhakika wewe huna njaa Geb? Mwenzio hata chai
sikunywa.” Rita akaanza kula. “Tena chamotoo. Onja hata
kidogo.” Rita aliendelea wakati anasogelea glasi yake ya
wine. “Onja.” Rita akamsogezea sahani. “Asante. Mimi naona nipo
sawa tu.” “Waw! Yaani! Sikujua kama nitakuona tena Geb! Nimefurahi sana. Kwanza
nimefurahi Mungu amekukumbuka na wewe jamani! Lakini baba alikuwa anakusifia
sana. Alijua utatoka tu.” Rita aliendelea kula huku akiongea bila kujali
kama anajibiwa. Ni kweli alionekana anafurahia kile chakula.
Geb alitoa simu yake mfukoni
akaangalia muda. “Unategemea simu?” Rita akauliza. “Kwanza kabla
hatujaendelea. Yule msichana uliyekuwa naye jana ni nani? Maana hata hatukupata
muda wa kutambulishana! Nilikuwa kama nimechanganyikiwa baada ya kukuona.
Nilikuwa siamini! Hata wale rafiki zangu walijua kama nimefurahi. Nilikufuata
mpaka kule ulipokuwa ukiishi na mama. Sijui nilikwmbia?” Geb akabaki hajui
ajibu swali la kwanza au la pili. “Bwana chips zao tamuu. Halafu hawa
shrimps wamewaweka kilimao kwa mbalii. Basi wee! Mpaka moyoni.” Rita
alisharudisha macho yake kwenye sahani yake.
“Kwa hiyo yule msichana ndio nani?”
“Anaitwa Nanaa!” Ile kutaja tu jina lake, Geb mwenyewe moyo
ukampasuka. “Woowwww! Simu yako nzuri. Hebu tuione.” Rita alihamaki kwa
sauti baada ya kuona simu ya Geb. Akiwa na mikono yenye mafuta ya samaki,
akanyoosha ili aipokee ile simu. “Kweli Geb nimekukubali. Mambo yako sio
mchezo. Kwani huko BOT wanawalipa mshahara kiasi gani? Hebu nipe niione kwa
karibu.” Ilimbidi Geb ampe tu. Akaipokea na kuanza kuiangalia mbele na
nyuma.
~~~~~~~~~~~~~~
“Nanaa!” Geb
akakumbuka. Mpaka usoni akabadilika. Akakumbuka alichomfanyia Nanaa. Akakumbuka
mabusu aliyokuwa akiyapata kutoka kwa Rita usiku ule. Tena ya mdomoni! Vile
Rita alivyokuwa amemkumbatia mbele yake. Kutoka kwenye kumkumbatia na kumuahidi
ahadi ya kumfuta machozi, Geb akajikuta anashindwa hata kumtambulisha mbele ya
Rita. Ikawa kama ufahamu ndio unamrudia.
Akakumbuka vile Nanaa alivyomwambia anaogopa, lakini akamuahidi
asiogope. Tena kwa mabusu mengi. Mazuri. Huku amemkumbatia. Akakumbuka furaha
aliyoiweka moyoni kwa Nanaa, mara baada ya kumbusu mbele ya walinzi wake. Na
hayo wala hayakuwa ni ya muda mrefu. Aliyafanya siku iliyopita tu. Na
aliyaanzisha yeye mwenyewe siku ya ijumaa. Tena kwa Nanaa aliyekuwa muwazi sana
kwake. Akimsimulia vile wanaume walivyomtenda. Na yeye akarudia yaleyale muda
mfupi tu wa kuanza naye.
“Lakini sikujua kama Rita huyu siye
yule wa wakati ule! Rita amebadilika! Hakuwa hivi! Halafu na mimi nilikuwa
kwenye mshituko. Sikujua niseme nini kwa Nanaa. Wakati mwingine ni heri
kunyamaza.” Geb akajitetea nafsini kwake. “Lakini hata kutoa
maelezo baada ya pale!?” Sauti nyingine ikamsuta. Akakumbushwa jinsi
alivyomuona Nanaa amekaa pale nje kwenye tofali. Tena peke yake! Halafu usiku.
Nanaa alipanda kwenye gari akionekana ana huzuni. Alishindwa hata kumpa mkono
wa kwaheri.
~~~~~~~~~~~~~~
Ni kama kitu kilimtoa kwenye mawazo,
akamuona Rita anasoma kitu kwenye simu yake. Akashituka alipomuona Geb
anamwangalia akiwa amerudisha mawazo pale. “Huna hata game!? Wenzio
wenye simu kama hizi, hazikosagi games.” Akamrudishia simu yake. Na
yeye akatoa simu yake. Akaanza kuandika kitu, Geb asijue anaandika
nini. “Sio mchezo Geb. Nimekukubali. Iphone toleo jipyaa!? Wewe wa ukweli.
Natamani simu kama hiyo yako.” Akaita muhudumu amuongezee wine
nyingine. “Utakunywa hayo maji? Nahisi mwiba wa samaki
umenikwama.” Geb akamsogezea ile chupa. Hakuwa hata ameifungua.
Akamfungulia, akamkabidhi. Rita akayanywa kama nusu ya chupa. Akabeuka kwa sauti. “Excuse
me!” Kaongea huku akijipiga piga kifuani.
“Oooh! Afadhali.” Akaonekana
amepata nafuu. “Sasa Geb?” Rita akauliza huku akipokea glasi nyingine
ya wine. “Kuna mahali nataka kwenda.” “Haiwezekani Geb! Leo ni siku yetu.”
“Tunaweza kupanga kukutana wakati mwingine?” “Kabisa. Leo hauwezi ukawa mwisho
wetu wa kukutana. Kwanza namalizia hapa, halafu twende chumbani tukakate kiu.
Huwezi kuniacha hivi nilivyo Geb. Kumbuka mapenzi yetu. Mpaka juu ya meza
tulikuwa tukiridhishana. Sasa Mungu amekujalia pesa, lazima tukafaidi
kitandani.” Rita akamaliza ile wine ya pili kwa haraka sana, kisha
akamwita muhudumu alete nyingine. Akarudi kwenye sahani yake kuendelea kula.
Bila kuchelewa, muhudumu
akaleta wine nyingine. Akainywa nusu ya glasi. Akamwangalia
Geb. “Geb!” Akamwita. “Unakumbuka penzi letu lakini?” Rita
akamuuliza kwa upendo. “Nini kimetokea au ni huyo Nanaa? Maana
sikuelewi mpenzi. Nakuomba penzi, unanikatalia! Nakuomba simu, pia
unanikatalia. Unakumbuka enzi tuko wote? Pesa ndogo niliyokuwa nayo tulikuwa
tukigawana mpenzi. Nilijinyima kwa ajili yako! Nilikukaribisha penzi wakati
nikijua wewe si kitu. Au leo unanionea kinyaa kwa kuwa nimeishiwa?” Rita akaanza
kulia. Geb asijue amelewa au ni janja yake. Aliendelea kulia kwa kulalamika,
huku watu wa meza za pembeni yao wakiwaangalia kujua kinachomliza mrembo huyo
ni nini.
~~~~~~~~~~~~~~
Ukweli Rita alikuwa amependeza haswa.
Alivaa wig ya lace front, yenye mawimbi. Aliachia ikawa imeanguka kila mahali.
Ilifunika mabega yake yaliyokuwa yameachwa wazi. Alivaa kigauni kifupi mpaka
kati kati ya mapaja. Kilimbana vizuri. Kilikuwa cheusi. Akavaa na kiatu
chekundu kirefu. Mapaja yake ya rangi ya maji ya kunde na miguu mizuri vilikuwa
wazi na kung’arishwa na ule weusi wa gauni. Aliweka kucha nzuri za bandia za
rangi nyekundu. Geb aliweza kuona kwani mara kadhaa alijaribu kurudisha nywele
zake kwa ustadi ili zisiingie machoni au kwenye chakula. Akapaka na lipstiki
nyekundu kabisa, kama rangi ya viatu. Alijaliwa macho mazuri na midomo iliyoweza
kuwakilisha hiyo lipstic ipasavyo. Hakika alikuwa amependeza. Kama mwanamitindo
mashuhuri wakutokea Hollywood.
~~~~~~~~~~~~~~
“Naomba niambie ukweli
Geb!” Rita akaendelea kulia. Wakati Geb akijaribu kumtuliza, mmoja wa wafanyakazi
mwenzake akiwa amekuja na familia yake eneo hilo akawasogelea. Alikuwa mkubwa
kidogo kwa Geb. Na waliheshimiana kazini japo walikuwa vitengo
tofauti. “Vipi kaka?” Geb akasimama. “Kwema tu. Nipo na
familia.” “Safi sana.” Geb alijibu akionyesha kutotulia kwani bado Rita
alikuwa akilia. “Nakupenda Geb. Na sitabadilika mpenzi. Nimekuchagua wewe.
Kwamwe sibadiliki hata iweje. Nanaa ametukuta na atatuacha.” Yule
mfanyakazi mwenzake aliposikia hivyo, akaamua kuaga kwa haraka sana.
“Naomba utulie Rita.” “Hapana
Geb. Wewe sio wakunitolea nje.” “Lakini mbona sijakataa kitu hata
kimoja hapa!? Umezungumzia swala la simu, kabla sijajib...” “Unafikiri
nimelewa? Nakumbuka kila kitu.” “Naomba punguza sauti Rita!” “Unanionea
kinyaa kwa kuwa wewe unapesa sasa hivi. Unashindwa kunisaidia wakati mimi
nilikuwa nawewe wakati unashida! Huna kitu.” “Rita! Sijakukatalia
kukununulia simu.” “Kwa hiyo unanipa pesa?” “Hapa nilipo sina pesa. Mpaka
labda kesho.” “Nashukuru Geb. Basi ngoja nikachukue chumba.” Rita
akasimama akiwa halii tena.
“Rita! Rita!” Geb akamkimbilia.
Rita akasimama. Muhudumu naye akamuwahi Geb na bili. Akatoa wallet yake ili
amtolee pesa ya chakula na vinywaji. Rita akaondoka. Geb akaangalia tena ile
bili yao. Akaanza kuhesabu pesa. Akalipia chakula, na kumpa tip
yake. “Nashukuru sana.” Yule muhudumu akashukuru. Geb akarudisha ile
wallet kwa haraka, akamkimbilia Rita ambaye alishatokomea ndani upande wa
vyumba. Nia ya Geb ilikuwa ni kumuwahi kabla hajachukua chumba.
Akakimbia mpaka ndani. Alimkuta
mapokezi ndio anakabidhiwa kadi za chumba. “Rita, naomba tuzungumze
kwanza.” Wakati anamvuta pembeni, muhudumu naye akamsogelea Rita na chupa
nzima ya whisky. “Afadhali kama mna HIBIKI. Yaani hii nilikuwa naipenda
sana wakati nipo Canada. Tena 17 years Old! Waw…” Rita akaipokea kwa
furaha. “Ingiza kwenye bili ya chumba.” Akamwambia yule
muhudumu.
“Twende tukapumzike Geb. Nimefurahi
sana. Hii whisky nilikuwa na hamu nayo, sema bei ndio ilikuwa ikinishinda. Leo
nataka nikate kiu zote. Mzinga mzima niumalize peke yangu wakati na wewe
ukinifaidi utakavyo!” Rita akaanza kuondoka kuelekea vyumbani huku
amejawa furaha sana. Geb akabaki haelewi chakufanya. Rita aliondoka huku
anacheka kwa sauti. Ilikuwa hata shida kuongozana naye. Kila mtu alikuwa
akiwatizama wao.
Rita akafungua ile chupa ya whisky
na kuanza kuinywa huku akitafuta chumba chao. Alikunywa kama maji, wakati
ni whisky. Ikabidi Geb amfuate. “Rita! Rita!” Geb akazidi kumuita
huku akijaribu kumsimamisha. “Yaani hii whiskey, Canada huwezi pata kama
huna dolla 270 na kuendelea. Inategemea unainywea wapi.” Rita aliendelea
kuongea huku akiitwa. “Nimechukua Presidential Suite. Najua
hutashindwa kuilipia mpenzi. Nataka leo tuandike historia. Nakupa huu mwili,
uchezee tani yako!” Rita aliongea huku akiendelea kutafuta chumba.
“Rita. Naomba tuzungumze kwanza.”
“Mpaka tuingie ndani.” Akachomeka kadi kwenye chumba chao. Ile kuingia
ndani tu, moyo ukampasuka. Kwa hakika chumba kilikuwa ni kizuri sana.
Akakumbuka na bei aliyotajiwa ya ile whiskey huko nchini Canada, Geb
alijua lazima awe na si chini ya milioni moja ndipo ataweza kutoka pale. Kwa
haraka sana Rita alivua nguo zote akabaki kama alivyozaliwa. Akamrukia Geb na
kumvuta kwa nguvu mpaka akachana shati lake.
“Acha kwanza Rita. Subiri.” “Nina
uchu na wewe Geb. Siwezi kusubiri.” Akamvuta tena kwa nguvu. Akafanikiwa
kulirarua kabisa lile shati likachanika kabisa. Geb alikuwa kwenye mshituko
asijue ni nini kinamtokea. Wakaanza kukimbizana humo chumbani. Rita anataka
kumtoa suruali kwa nguvu, Geb hataki. Ilimbidi Geb kumkwepa palepale chumbani
huku akimtuliza, akijua hatakuwa na jinsi yakutoka pale. Kwanza alishamchania
shati. Akajua akimkamata suruali, basi tena. Atatoka uchi na pesa hana. Geb
akaruka kushoto na kulia huku akijaribu kumtuliza. Lakini Rita ni kama alikuwa amepagawa.
Anamtaka Geb kwa hali na mali. Alikuwa akimlilia kwa sauti ya kujilalamisha
akimtaka kimapenzi.
Kila waliposimama, Rita alimpiga
picha na kujipiga na yeye. Geb akahisi anatuma ujumbe mahali. Akaogopa isije
kuwa anatuma na zile picha anazompiga yeye Geb na kujipiga yeye mwenyewe tena
akiwa uchi. “Unafanya nini Rita? Nani unamtumia hizo picha?” Rita
akawa anacheka sana. Zoezi la kumkimbiza Geb ili amkamate kwa nguvu afanye naye
mapenzi akalisitisha, likawa zaoezi la picha. Geb akaamua kumpokonya ile simu
ili kujua anachofanya. Rita akakimbia.
Ikawa sasa Geb ndiye anayemkimbiza
Rita mle chumbani. Kutoka upande kilichopo kitanda mpaka sehemu ya makochi.
Rita yupo uchi, Geb shati limeraruliwa. Kwa kuwa alikuwa amelewa sana, Geb akaamua
amrukie ili amkamate kwa rahisi kuliko vile wanavyokimbizana. Kwanza Rita
alikuwa akipiga kelele. “Niachie! Niache Geb!” Geb akajua kwa mtu
yeyote atakayekuwa akisikiliza nje, ataelewa yeye ndio anataka kumbaka Rita.
Akaona apunguze ule mchezo wa kukimbizana, amrukie na kumkamata ili ampokonye
simu, ajue anachofanya.
~~~~~~~~~~~~~~
Geb ni kijana mdogo aliyekuwa
amefanikiwa sana kimaisha. Alishawakuta wazee wa mjini wakihangaika kwenye
ulimwengu wa biashara, akawapita. Hapakuwa na ubishi kuwa mkono wa Mungu
ulikuwa juu yake. Alitoka kwa namna yake na kushangaza watu wengi sana.
Waliojaribu kuiga wakaiga lakini hapakuwa na mafanikio kama yake. Walimtafuta
katika kila eneo ili kujua udhaifu wake, wautumie ili kumwangusha lakini
wakakuta ni kijana wa kawaida tu. Maisha yake ni kazini, nyumbani. Tena mtoto
wa mama. Ambaye anaweza kulala na mama yake! Kisha kanisani. Tena hata huko
kanisani utamkuta pembeni ya mama yake.
Huwezi kumkuta baa akinywa, wala kumbi za starehe
akijichanganya na vijana wenzake au na matajiri wenzake kubadilishana mawazo.
Akisafiri ni mashambani kutafuta mzigo. Ila alijulikana kwa aina ya magari
mazuri aliyokuwa akiendesha. Akipita, watu walijua Geb Magesa amepita. Wengine
walisema ndiko anakomalizia pesa zake. Wengine walisema ni utajiri wa kichawi,
una masharti ndio maana anashindwa kutapanya pesa yake. Ilimradi walioweza
kuongea waliongea.
Ukimya wake ndio uliwanyima
watu maneno. Hawakujua anawaza nini juu ya yeyote wala usingeweza kutoa siri
kifuani mwake. Labda kwa kupitia mama yake. Ambaye na yeye ajira yake ya kwanza
na kubwa ni wanae kwanza. Aliyatoa maisha yake yote kwa ajili ya Grace na Geb.
Aliwalinda hao watoto kama mboni ya jicho lake. Hata kuna kipindi wakati
anahangaika na ada ya Geb, alipata mwanaume aliyechanganywa na umbile lake mama
G, alitaka kumuoa, lakini alikataa. Alijua hataweza kuwafikiria wanae kama
akiolewa na mtu mwingine. Ni heri abakie kuwa Magesa kama Geb na Grace.
~~~~~~~~~~~~~~
“Rita! Unafanya nini? Unataka nini
wewe!?” Geb akaamua asimame kwanza. “Nakutaka wewe Geb. Wewe ni
wangu. Hilo halina ubishi. Huwezi kuninyima mapenzi sasa hivi kwa kuwa
umefanikiwa, wakati ulikuwa ukitumia mwili wangu kipindi kile unatembea na jua
kali. Ulikuwa ukiugusa mwili wangu bila shida tena popote na muda wowote,
hatukujali. Nilikuruhusu uniguse hata ukiwa unanuka jasho, wakati umetoka
Kariakoo kununua mzigo. Sikujali jasho lako. Nikakuachia mwili wangu uufanye
utakavyo. Leo tupo kwenye mazingira mazuri. Mungu ametukumbuka,
unanikataa!” Geb akataka kumrukia ili amkamate kirahisi kwa kuwa
alikuwa amesimama, ametulia anazungumza naye, Rita naye akataka kuruka upande
wa pili akajikwaa na kujigonga kwenye meza akachanika kwenye kipanda uso. Damu
zikaanza kumwagika kama maji.
Shetani Kazi Yake Kuharibu,
Kuangamiza Na Kuua.
G |
eb alishituka sana. Akaogopa asije akamfia pale ikawa kesi kwake.
Bila kufikiria, akapiga simu mapokezi kwa haraka kuomba huduma ya kwanza. Baada
ya nusu saa, chumba kikawa kimejaa wahudumu na polisi. Alipoona hali mbaya
anahojiwa na kuonekana alifanya makusudi, ilibidi kumpigia Danny simu. “Uko wapi wewe?
Mbona nasikia mtu analia?” Danny akauliza. Rita alikuwa akilia sana
kuwa Geb amemuumiza kikatili. “Naomba msaada Danny.
Nimejiingiza kwenye matatizo bila kujua ndugu yangu.” Geb alikuwa akitetemeka mpaka kwenye simu alikuwa
akisikika. “Geb! Ni nini?” “Nahisi
ninapelekwa polisi Danny. Naomba uje unisaidie.” “Polisi!?” Danny alikuwa nyumbani, akashitua kila mtu.
Mama G akaruka akampokonya simu
Danny. “Kuna nini Geb?” Geb akaanza kulia. “Geb!” Mama yake
aliita kwa sauti ya juu akionekana ameshapaniki. “Itabidi twende Osterbay
polisi kuandikisha kesi.” Mama G alisikia mtu anazungumza na Geb upande wa pili wa
simu. Akashituka sana. “Geb! Geb!” “Napelekwa polisi mama.” “Wapi?” “Osterbay.” “Nisikilize Geb. Naomba utulie kabisa. Tulia. Mimi nitakukuta
huko.” “Watanifunga mama! Maisha yangu
ndio yameshaharibika.” Kimya. “Mama! Naogopa sana.” “Usiogope Geb. Nakuja.” Mama
G akakata simu. Geb akatolewa pale akiwa na pingu mkononi. Akaingizwa kwenye
gari la polisi, mpaka Osterbay polisi.
Mama G alitoka anakimbia. Grace
akamkimbilia mpaka nje akamshika. “Nisikilize mama. Sasa hivi
kuchanganyikiwa hakuta saidia kitu. Geb anakuhitaji sana sasa hivi. Tena ukiwa
na akili iliyotulia sio hivyo ulivyo sasa hivi. Naomba utulie, Danny
atatupeleka.” Danny akatoka akiwa amembeba mwanae na funguo za gari.
Wakaingia kwenye gari, kuelekea Osterbay polisi.
~~~~~~~~~~~~~~
Njia nzima akiwa kwenye gari ya
polisi kama mtuhumiwa akipelekwa polisi, Geb alikuwa akimuwaza Nanaa. Shutuma
ambazo ataaminishwa na watu na vyombo vya habari. Akakumbuka jinsi anavyowindwa
na matajiri wa mjini na hata rafiki zake. Akajua ni wengi watalipia habari zake
zianikwe mitandaoni. Akajua wengi watamfuata Rita kumuhonga pesa nyingi ili tu
aongee uongo wakumtoa yeye mtaani afungwe, ili awapishe kwenye ulimwengu wa
biashara.
Lakini hilo halikumsumbua Geb kama
vile Nanaa atakavyoweza kusadiki kirahisi kwani hata jana yake alishindwa
kumtambulisha kwa Rita wakaagana bila maelezo yeyote. Na hapo ilikuwa jumapili
jioni, hata hakuwa amemtafuta Nanaa kumjulia hali. Kujua kama alifika salama
huko alikokwenda kumuona mgonjwa? Kwanza alikuja kuchukuliwa na Jeff, mwanaume
aliyekuwa akimuonea wivu wakati wote. Lakini alikuja kumchukua Nanaa, Geb
hakuonyesha hata kujali. Kama aliyeshukuru kuondoka kwake. Hakutaka hata kujua
kama alimfikisha salama. Kama je, alimka salama na anaendeleaje! Yeye aliamshwa
na jumbe za Rita, mpenzi wa ujanani. Waliyejuana kwenye shida. Wakapendana na
kukubaliana kuja kuoana. Bila kufikiria wala kujipanga, akamkimbilia hotelini.
Yote hayo Geb aliyakumbuka akiwa na
pingu zake mkononi, akipelekwa kituoni kama muhalifu. Alikumbuka mabusu
aliyoyapokea na Rita, tena mbele ya Nanaa, bila hata kubisha au kuyatolea
maelezo. “Nanaa wangu jamani!” Geb akawaza akiwa ndani ya hiyo
gari ya polisi, machozi yakimtoka asiamini kuwa juhudi zake zote zinaishia jela!
Mali, majumba na mapesa yake yote aliyoweka benki hatakaa afaidi tena kwa kosa
la jinahi ambalo amebambikiziwa na Rita aliyekuwa akilia kuwa Geb alitaka
kumuua. Rita alitolewa pale akapelekwa hospitalini akivuja damu.
~~~~~~~~~~~~~~
“Kwani mama
wewe amekwambia nini?” Grace akahoji wakiwa njiani. “Hajaniambia kitu
chochote zaidi yakulia tu.” “Na wewe Danny?” “Mimi ameniambia anaomba msaada.
Anahisi watampeleka polisi. Basi.” “Mmh! Sijui nini kimempata! Tutajua huko
huko.” Grace ndiye aliyekuwa akiwahoji.
Walipofika polisi, Geb alifunguliwa
kesi ya ‘Jaribio La Kutaka Kuua’. Kwani Rita alikuwa akilia na
kuwaambia polisi kuwa Geb alimsukuma kwa makusudi. Rita aliwaambia kulitokea
kutoelewana kidogo, Geb akataka kumpiga. Akafanikiwa kukimbia mara ya kwanza,
lakini mara ya pili akamkamata. Ndio purukushani hizo za kumchania mpaka shati
wakati akijitetea. Rita aliendelea kuelezea polisi akiwa tayari amefunikwa
shuka walilolitoa kitandani hapo, palepale chumbani. Polisi aliyekuwa akimuhoji
alijaribu kumtuliza ili kupata maelezo yakutosha kwani Rita alikuwa akilia kwa
uchungu sana. “Geb alipoona namzidi nguvu, ndio akanirukia kwa nguvu na
kunisukuma kikatili.” Rita alihitimisha maelezo yake kabla yakuwahishwa
hospitalini kwani bado alikuwa akivuja damu.
Geb aliwekwa lupango, asiamini kama
ndio maisha yake yanaishia jela. “Sijui nani atamuoa Nanaa wangu!” Geb
aliwaza wakati amekaa chini kwenye chumba hicho kichafu kinachonuka. Asiamini
ni masaa machache tu alikuwa akipuliziwa na Ac ya nyumbani kwake, kwenye gari
na upepo mwanana wa Sea cliff.
~~~~~~~~~~~~~~
-
Kufumba na kufumbua, Historia imembadilikia Geb. Kutoka kuwa kijana
wakuheshimiwa na kutamaniwa mtaani, mambo yamembadilikia kabisa. Rita
amembadili jina. Kutoka kuitwa milionea, gafla ni Mtuhumiwa. Tena kwa kosa la
jaribio la kutaka kuuwa!
-
Kwa shutuma au kesi inayomkabili Geb, adhabu yake ni kifungo cha
maisha tu. Hakuna mjadala. Rita yu hospitalini, akilia kutaka kuuwawa. Hakuna
shahidi, ila Mungu mwenyewe ndiye aliyekuwepo nao tokea mwanzo na Nanaa
aliyewashuhudia wakikumbatiana na kupeana mabusu bila hofu mbele yake.
-
Hakuitwa na mtu, amejiingiza na kujipeleka yeye mwenyewe kwenye
matatizo. Hana wakumlaumu. Hukumu ndio inamtesa kwa yale aliyomfanyia Nanaa.
Kipi
kitaendelea kwa Geb?
0 Comments:
Post a Comment