Akarudi chumbani kwake kuoga. Akawa amekaa tu
kitandani akisubiria. Saa 4 asubuhi kila mtu akawa ameamka. Vilijaa vicheko
pale mezani. Danny akishangilia vitafunio. Akapiga picha kila kitu pale mezani,
akatuma kwenye kundi lao la Whatsapp. Watu wakaanza kutuma jumbe zao kwenye
kundi hilo. ‘Mko hotel gani, kaka?’ ‘Mbona mapema
kaka?’ ‘Sherehe kama hizo huwa hatuachani Danny.’ Grace alikuwa anasoma
zile jumbe huku wanacheka wote, kwani na yeye alikuwa kwenye hilo kundi. ‘Tupo nyumbani kwetu. Nanaa kapageuza hotel. Na hatutaki
wageni.’ ‘Tumetoka mbali sana bwana Danny.’ Danny
akawajibu. ‘Kuleni makwenu jamani! Leo jumamosi
nataka kupumzika na mke wangu. Msitujalie huku kwetu. Tulieni.’ ‘Lazima mama
atatoa exception kwa bwana harusi. Kwanza nina shida naye.’ Malii
aliendelea. ‘Mama hayupo. Nipo mimi na Grace tu.’ Simu
zikaanza kwa mama G. Aliposema tu yupo nyumbani. Kila mtu alitaka kufika hapo nyumbani.
Mama G akawakaribisha.
Geb na yeye alikuwa mmoja kwenye hilo kundi.
Alipoona wote wanakaribishana nyumbani kwake, akamwambia Nanaa waondoke haraka
kabla hawajawakuta pale. Lasivyo hawataweza tena kutoka. Nanaa akachukua pochi
yake. Geb akachukua uji wake wakatoka. Baada ya lisaa limoja, tayari nyumba ya
Geb ikawa imejaa. Kila mmoja ananjaa. Anataka chakula kwa mama G.
~~~~~~~~~~~~~~~~
“Naomba nikupe kazi moja. Lakini kuna
masharti.” Geb alianzisha hayo mazungumzo wakati wanaelekea kazini siku
hiyo ya jumamosi. Nanaa akacheka kidogo akamwangalia. “Mmh!” “Nataka
ufikirie na uandike chini, kitu chochote. Namaanisha kitu chochote, ambacho
unatamani kuwa nacho. Nikimaanisha mahitaji yako binafsi. Kuanzia asubuhi
unapotoka kitandani mpaka unapoenda kulala. Kila kitu. Nataka ufikirie sasa
hivi. Halafu tukifika kazini uandike wakati mimi nafanya kazi za jana. Andika
kila kitu. Iwe mswaki, nguo za ndani, nguo za kuvaa kazini, nguo za kulalia,
pochi, hereni, chochote. Sio lazima ukanionyesha. Labda utake mwenyewe. Lakini
naomba andika kila kitu. Usiache kitu chochote. Mimi nitakuwa dereva wako leo.
Unaweza kuvigawa kwenye mafungu. Ukasema kama leo ni nguo za ndani tu.
Nitakupeleka kwenye hayo maduka. Ukanunue vile utakavyo, mimi nitalipia. Kama muda
hautatosha, kesho tutaenda kwengine. Hivyo hivyo mpaka tumalize.” Nanaa
akainama akifikiria.
Geb akamuona amekosa raha badala
yakufurahia. “Umenielewa lakini?” “Sina kitu ninachotaka uninunulie Geb.”
“Unanidanganya Nanaa. Mimi mwenyewe nina vitu nataka kununua. Sema naona uvivu
kuzunguka madukani au sijipi muda. Na ninakumbuka uliniambia James anakuwa na
majukumu mengi. Wakati mwingine unakuwa na shida, unashindwa hata kumwambia
matatizo yako. Sasa nataka uniambie mimi.” Nanaa akakumbuka ni kweli alimwambia
wakati wa safari ya Bagamoyo.
“Kwa hiyo naomba usinidanganye Nanaa. Labda
uniambie hutaki.” “Sio kuwa sitaki. Ila sitaki tena nigeuke kuwa mzigo kwako.
Yaani uone ni kama una mradi fulani wa kuufanyia kazi. Nakushukuru kwa hilo,
lakini nimechoka kusaidiwa. Acha nitajinunulia tu mwenyewe.” “Kwa hiyo unayo
mahitaji?” Nanaa akanyamaza.
“Labda niulize hivi. Ni lini unampango wa
kuyatimiza hayo mahitaji yako?” “Sijui Geb. Nikipata pesa. Sasa hivi
kipaumbele ni kukusanya pesa kwa kadiri ya uwezo wangu. Ili niweze kujikimu
baadaye. Najua navaa nguo za kawaida sana. Tena nanunua kwenye ile mitumba ya
bei ya chini sana. Sinaga nguo za kulalia. Sio kwamba sijui kama kuna nguo
maalumu za kulalia! Najua zipo. Naweza kuvaa nguo za ndani miaka na miaka. Sio
kwamba sijui natakiwa kubadilisha kila baada ya muda mfupi. Nafahamu Geb. Najua
kama kuna aina nzuri za nguo za ndani. Najua watu wanavaa za ma ‘designer’. Na
ninawafahamu. Lakini mimi sijafika huko. Naogopa hata kuwaza huko kwa sasa.
Sitaki kujiwekea mahitaji yakuja kuniumiza mimi mwenyewe baadaye. Nina mahitaji
ya msingi kuliko kufikiria kununua nguo za kulalia wakati naweza kununua tisheti
ninayoweza kuvaa darasani na pia nikalalia usiku. Sijui umenielewa? Naomba huko
tusiende Geb. Ni papana, na parefu mno. Naogopa hata mimi mwenyewe
kupaangalia.” Geb akamtizama na kunyamaza.
Walifika kazini. Geb akaegesha gari yake.
Wakashuka. Walinzi walikuja kumsalimia. Nanaa akataka kuondoka kama kuwapisha,
Geb akamuwahi kwa kumshika mkono. “Nisubiri twende wote.” Kisha akamvuta
karibu yake na kuanza kumbusu, mbele ya wale walinzi! Nanaa alifurahia sana
japo aliogopa. Geb ni mmiliki wa lile eneo. Na nikijana anayeheshimika sana
pale. Inakuaje leo kumbusu hadharani mbele ya wafanyakazi wake! Hakuwahi hata
kumuona akimbusu Liz kwa muda mrefu vile mbele za watu. Kwanza hakuwahi kumuona
akimfanyia Liz vile mbele ya wafanyakazi wake. Alimuona akipewa busu na Liz,
tena juu ya mdomo tu. Lakini yeye alimshika kiuno na kumvutia karibu yake na
kumbusu bila haraka. Akamuachia, na kumwangalia kidogo. Akaendelea kuzungumza
na wale walinzi. Akaagana nao.
“Twende nikaangalie huko stoo. Nataka kuzungumza
na yule kiongozi wa mambo ya stoo.” “Leo jumamosi Geb.” Nanaa
akamkumbusha. “Nilimwambia aje leo. Kuna uzembe mwingi unafanyika na yeye
akionekana yupo kwenye payroll ya wafanyakazi. Sasa nataka kujua kama huwa
anakuwepo kwenye majukumu yake! Na ni mlalamishi sana. Grace huwa
hamuwezi.” Wakaongozana mpaka stoo ndogo tu waliyokuwa nayo ya hapo hapo
ofisini, akiwa amemshika mkono Nanaa.
Walimkuta akiwasubiri. Alikuwa mtu mzima kidogo.
Mkubwa hata kwa Geb mwenyewe. Alikuwa na kijana mwengine anayefanya kazi hizo
hizo za stoo, wote wawili walikuwa wakimsubiria Geb. Wakakaa naye chini. Yule
kiongozi alikuwa na maneno mengi sana. Wote pale kazini walimjua ni mbishi na
jeuri. Lakini Nanaa alishangaa vile Geb alivyokuwa akizungumza naye kwa
kumuuliza maswali ya papo hapo mpaka akaishiwa maneno. Akakubali kosa.
Kulikuwa na uwizi unaendelea kati yao. Na yeye
ndiye aliyekuwa akituma madereva kudanganya. Anakuwa akikubaliana na madereva
pindi wanaposhusha mzigo kuandikisha hata robo ya lori kuwa mazao hasa matunda
yalifika yameharibika, yeye anayapakia kwenye gari yake aina ya pickup ndogo na
kwenda kuwauzia wateja haohao wa Geb, lakini sehemu nyingine.
Geb aliambiwa na wateja wake kuwa meneja wake
anawauzia mzigo kwa siri. Ndipo akazungumza naye. Baada ya kuzungumza naye kwa
muda mrefu akibisha. Geb alimpigia simu mmoja wa wateja wake, akakiri kuuziwa
naye matikiti jana yake usiku. Nanaa akashangaa sana. “Ni yale ya jana
tuliyoyapakia Bagamoyo!?” Nanaa akauliza kwa mshangao. Geb
akacheka. “Ona hasara mliyoandika tuliyoingia kwenye yale matikiti. Lakini
huyu dereva mpya alinipigia simu jana jioni kuniambia mnaniibia sana. Yeye
hawezi kukubali kosa la kuharibu mzigo njiani wakati anasema alifikisha mzigo
wote salama. Tena aliwaonya na kuwaambia msidanganye kwa kuwa mimi mwenyewe
nilihusika katika upakiaji. Na tukahakikisha yamekaa vizuri hakuna
yatakayoharibika. Mkamwambia yeye anakazi ya kuyafikisha tu hapa. Basi.
Mambo mengine awaachie nyinyi.” Wakanyamaza.
Nanaa aliumia sana. Akamuhurumia Geb. Alimuona
vile alivyoteseka jana yake kule mjini Bagamoyo. Kwanza alimka alfajiri.
Akajinyima usingizi wake. Akaenda kufanya kazi, si kusimamia. Alifanya kazi kwa
makini mpaka mwisho. “Wanawezaje kuiba kirahisi hivyo?” Nanaa
akajiuliza. “Naomba tusifikishane mbali ndugu yangu. Mimi nitakwenda
kukusanya pesa yote huko nilikouza hayo matunda. Nitakurudishia. Tamaa ndiyo
iliniingia. Haitatokea tena.” Yule kiongozi wa stoo akakiri
mwishoni. “Basi, pesa yote naomba mumkabidhi muhasibu.” Geb
akasimama. “Twende Nanaa.” Wakaondoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Geb alikuwa na godown kubwa tu alilokuwa
akikodisha kutoka kwa tajiri mmoja wa kihindi, maeneo ya Temeke,
Kurasini. Hapo hapo jijini. Ndipo alipokuwa akihifadhia bidhaa zake zote.
Lakini ofisi ambazo zilikuwa zikiendesha biashara hizo ambazo Grace ndio
alikuwa akisimamia, zilikuwa maeneo ya Fire kama ukielekea Kariakoo. Walipata
na stoo kubwa tu, iliyokuwa kama na cold room ili kufanya mazao yasiharibike.
Hasa matunda. Waliweka baadhi ya mazao waliyokuwa wakiuza kwa wateja wao wadogo
wadogo pale pale mjini. Kwa kuangalia uwekezaji wake tu, utajua ni kweli ni
kijana mwenye kufikiria. Hakurupuki.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Nanaa hakuamini. Akabaki akimtizama
Geb. “Ndio basi!?” Geb akacheka. “Yaani huwafukuzi kazi!
Unawasamehe!?” “Watu waaminifu ni wachache sana Nanaa. Wengi wakiwa kwenye hizo
nafasi, ni rahisi kushawishika. Ataingia mwaminifu, baada ya muda huwa
wanabadilika. Heri huyu nimeshajua ni mwizi, na nimeshajua jinsi ya
kumdhibiti. Kuliko kuanza na mwingine mpya. Nitampunguzia majukumu. Na kuweka
kamera hapo wanaposhusha mizigo. Screen yake itakuwa ofisini kwa Grace tu. Kila
mzigo utakapokuwa ukishushwa, Grace atapata rikodi yake hata kesho yake.
Kuanzia mazungumzo mpaka picha zenyewe. Nitaweka hapa na kule kwenye godown ya
kurasini. Basi.” Nanaa akamshangaa sana Geb. “Una akili wewe!
Hongera Geb.” Geb akafungua mlango wa ofisini ya muhasibu.
Akamvutia Nanaa ndani. Akamkumbatia kwa nguvu
kabisa. Karibu naye, kisha akaanza kumbusu tena. Alimbusu taratibu kisha
akaacha kumbusu, akamwangalia akiwa bado mikononi mwake, tena karibu yake.
Nanaa akacheka kwa aibu. “Nimefurahi umenibusu pale nje. Mbele ya walinzi!
Nimeona raha.” Geb akacheka.
“Naomba usijifikirie kama wewe ni mzigo kwangu
Nanaa. Najua unahistoria ngumu sana ya maisha. Naomba fungua moyo wako kupokea
vitu vipya. Nilikwambia lazima ufungue moyo wako na ukubali kutambua na kupokea
upendo mpya. Usifananishe watu na matukio ya nyuma. Sikuchukulii na
ninakuahidi, sitakuchukulia wewe kama mradi wangu. Na mimi nitakuwa muwazi
kwako. Nitakapochoka, au nitakapoona jambo litakuwa gumu kwangu, naahidi
kukwambia.” Geb aligusa hisia za Nanaa.
“Kweli?” Nanaa akauliza huku
akilia baada ya kukumbuka masimango kwenye maisha yake. Ni James tu ndiye
aliyembeba bila kuchoka. Lakini sasa hivi mama yake ameanza kumsimangia misaada
anayopewa na James pia. “Nakuahidi hivyo, Nanaa. Chochote nitakachofanya
kwako, ujue kipo ndani ya uwezo wangu. Kwa hiyo usiogope. Sawa?” “Sawa. Nakushukuru Geb.” Geb akambusu tena.
“Basi naomba tuangalie pamoja kule ‘kurefu
na kupana sana’. Kule unakoogopa wewe kupaangalia, ukiwa peke
yako.” Nanaa akaanza kutokwa tena na machozi, akiwa palepale mikononi mwa
Geb. “Naomba uandike kila kitu. Hata kile unachoona ni cha kijinga sana.
Hata kile unachoona ni cha garama sana. Naomba uandike tafadhali.” “Ni vingi Geb!” “Basi naomba uanze sasa
hivi.” “Sawa.” Geb akambusu tena
kwa muda huku amemkumbatia kwa kumvutia kwenye mwili wake. Kisha
akamwachia. “Asante.” Nanaa akashukuru akiwa ameshatulia na tabasamu
usoni. “Karibu” Akamvutia kiti pembeni ya kompyuta ya muhasibu
alipojua atakuwa akifanya kazi. Wakakaa. Nanaa akaanza kuandika.
Akamuona ameinama anaandika huku
anacheka. “Unacheka nini?” “Leo naenda kutupa vitu vingi sana vilivyokuwa
vinanikera.” Geb akacheka. Akakumbuka ni muda mrefu umepita hakuwa
amebadilisha nguo zake za ndani. Sidiria alizokuwa amenunua mtumbani alikuwa
nazo zaidi ya miaka miwili. Tena tatu tu. Na zote zilikuwa nyeusi. Alijitahidi
kuzitunza kwa kadiri ya uwezo wake. Chupi zilikuwa nyingi kidogo. Alizotenga
kwa ajili ya kuvaa kipindi cha hedhi, na siku za kawaida. Alikuwa nazo tatu
alizotenga za kutokea. Nazo zilikuwa ni za muda mrefu sana.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Kwa
asili yake hakuwa akichagua wanaume wenye pesa sana. Na alikuwa muoga kuonyesha
anatanguliza pesa. Alijitahidi kuwaonyesha wanaume wote kuwa yeye ni mwanamke
anayejua kubana matumizi. Na anafaa kuolewa na kuwekwa ndani. Kwa hiyo hata wao
walipata aghueni wakawa hawajisumbui hata kumpa pesa za kujikimu. Zaidi ni pesa
ndogo ndogo kama zakupandia daladala baada ya kulala nae. Hakuna aliyekuwa akimfikiria
yeye kama Nanaa. Walitumia mwili huo mzuri, na kumuacha aende zake. Leo Geb
anataka kubadili historia! Ilikuwa ngeni na mpya kabisa kwa Nanaa.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Akainua macho akamwangalia
Geb. “Vipi?” Geb akamgeukia. “Hata kama nataka kubadili mswaki
niliokaa nao kwa muda mrefu, pia niandike?” Nanaa akauliza akiwa hana
uhakika. “Andika kila kitu unachotaka.” Nanaa akacheka, akaendelea
kuandika. Geb alimtizama kwa kumuhurumia. Akamuona ametulia kama amesita.
Anang’ata kalamu. “Hata hicho unachosita kuandika, pia kiandike.” “Naona
kama nimeandika vitu vingi sana! Inatosha Geb.” Nanaa akaonyesha
wasiwasi. “Naomba andika Nanaa. Andika tu.” Nanaa akavuta pumzi kwa
nguvu. Akabaki akifikiria.
“Unajua body spay?” Akamuuliza Geb. Geb
akacheka. “Lakini haina ulazima.” Nanaa akainama. “Naomba
uandike Nanaa.” “Nahisi ni tamaa tu. Nilimuona rafiki yangu Tia, aliletewa na
Evan mpenzi wake. Nikapenda. Ila nitamaa tu. Nimeshaandika deodorant, inatosha.
” Geb akavuta kile kijitabu alichokuwa akiandika Nanaa, akaanza kuandika
na yeye.
‘Body spry, perfume, nguo za kutokea
usiku, pochi zake na viatu, Accessories, pochi ya kazini, pochi ya kanisani,
pochi ya kawaida, sandals, viatu vya kanisani, nguo za kanisani, nguo za
kushindia, na..” Geb
akamkabidhi tena kile kijitabu kidogo na karatasi. “Vyote
hivi!?” Nanaa akashangaa. “Sasa kwani wewe ulikuwa ukiandika nini
hapo?” Nanaa akacheka. “Unataka nikusomee?” “Nisomee.” “Haya. Mswaki, dawa ya mswaki, sabuni ya kuogea, malapa,..” Akamuona
Geb anaanza kucheka. “Bwana usinicheke Geb!” “Nimekwambia andika Nanaa.
Kwa nini unanipa mahitaji ya vitu unavyoweza kupata dukani kwa Mangi?” “Naona
itakuwa garama sana!” Geb akamgeuza kwenye kile kiti chakuzunguka.
“Niangalie mimi Nanaa na unisikilize kwa makini. Ninafanya
kazi na nina biashara. Kwa sasa sina ndugu wala mtu anayenitegemea isipokuwa
wewe tu. Mama anabiashara zake, zinamwingizia pesa nzuri tu yakumtosha
mwenyewe. Grace na mume wake hivyo hivyo. Mimi sio kama James. Sina majukumu
mazito. Nataka wewe uwe na kila kitu unachokitaka. Kila kitu. Kwa mfano kuna
kipindi nilisoma kwenye kundi letu, James alituma ujumbe akiuliza kama kuna mtu
anayo laptop anayotaka kuuza. Nikasoma majibu na maswali ya watu wengine na
vile James alivyokuwa akijibu kuwa anatafuta laptop kwa bei nafuu, kwa ajili
yako.” Nanaa akainama.
“Aliweza kukupatia laptop?” “Nilimwambia aache,
nikawa natumia ya Zena. Majuzi akaniazima ya kwake ili nianze kuandikia
ripoti.” “Sasa mbona hapo kwenye kidaftari chako sioni?” “Laptop!?” Nanaa
akashangaa kwa sauti. “Ndiyo. Si unahitaji? Unafikiri utapataje sasa?”
“Naona itaku..” Akanyamaza. Akainama na kuandika huku anang’ata
meno. “Nimeandika.” “Naomba uandike kila kitu Nanaa. Acha
woga.” Nanaa akainama nakuendelea kuandika tena mpaka akamaliza.
“Mimi nimeandika kila kitu. Haina maana nilazima
uninunulie au..” “Nanaa! Mimi ndio nimetaka mahitaji yako. Acha mimi ndio
niamue. Sasa unataka kunionyesha au unajua wapi pakuvipata nikusindikize?”
“Naomba nikuonyeshe ili unishauri.” Geb akavuta kile kitabu. Akasoma
mwanzo mpaka mwisho. Akamuona Geb anavigawa kwa makundi mpaka akamaliza.
“Sasa
hapa na mimi nimeshamaliza. Nilikuwa napitia pitia tu kuona kazi za watu
wengine. Kuna maduka maalumu unataka ukanunue hivi vitu?” “Mwezio nguo zangu
mpaka sidiria huwa nanunua mtumbani. Nikitaka nguo nzuri yakutokea ndio naenda
pale Magomeni kuna kaka mmoja namfahamu ndio ananiuzia magauni mazuri ya
mtumba, kwa bei nafuuu.” “Naomba leo tusiende huko.” Geb aliongea
kiustarabu kidogo.
“Wanauza vitu kwa bei ya chini sana.”
“Naelewa. Lakini nitakupeleka sehemu nyingine. Tuanzie kwenye hili duka,
nalifahamu. Linauza nguo za ndani nzuri. Hata kama hufahamu saize yako,
watakusaidia. Nina uhakika mpaka utoke hapo, utakuwa umepata chupi, sidiria na
nguo za kulalia za kutosha. Lakini naomba nikuombe kitu kimoja Nanaa.” “Nini?”
“Tafadhali usiangalie bei. Halafu ukachukua kitu kimoja kimoja sababu ya
uoga wa bei. Wewe chagua vitu vya kutosha na utakavyopenda, halafu muachie yule
muhudumu. Toka nje, mimi nitaingia kulipia. Tafadhali sana. Sitaki tena tuje
turudi huko kila baada ya siku tatu. Mimi ni mvivu sana wa shopping. Nikinunua
vitu huwa nanunua hata vya miezi, ili nisirudi tena madukani. Ukifanya hivyo
itanisaidia sana. Sawa?” “Sawa.” Wakakubaliana na kutoka.
Mpaka inafika jioni wanarudi nyumbani, Nanaa
alikuwa na robo tatu ya mahitaji yake. Wote walirudi wakiwa wamechoka. Lakini
Nanaa alikuwa na furaha yakupitiliza. Alinunuliwa vitu vya thamani vitupu
ambavyo hata hakuwa amevifikiria.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Akaingia chumbani kwake akaviweka vile vitu
kitandani kwake kisha akaenda kumuita mama G akiwa amefurahi sana. “Njoo
nikuonyeshe vitu.” “Ulivyofurahi!” “Njoo haraka.” “Geb yuko wapi?” “Nimemuacha
kwenye gari anaongea na simu. Njoo.” Akakuta amemwaga kila kitu kitandani. “Ona
mavitu yote hayo nimenunuliwa mwenzio.” Mama G akaanza kucheka huku
anasogelea kitanda cha Nanaa.
“Nimepelekwa kwenye maduka ya maana matupu mama.
Ona.” Nanaa akaanza kunyanyua kimoja baada ya kingine.“Ujue mwenzio sijawahi kuvaa vitu kama hivi!” Nanaa
akaanza kulia. “Sijategemea mama!” “Usilie
sasa. Wewe ukoje? Mwenzio amekununulia ufurahi, halafu aje akute unalia tena!?” “Sijawahi pata mtu ananijali hivi mama yangu.” “Kwa
kuwa na wewe unamjali ndio maana. Sasa mbona hizi chupi sizielewi!? Au sio chupi?” Nanaa
akaanza kucheka. “Bwana mama!” “Aaah!
Naona vimikanda tu. Unavaaje sasa!?” Nanaa akazidi kucheka.
“Huku ndiko kutembea uchi huku! Sasa kwa nini
usinunue chupi nzuri, zinazokusitiri vizuri!?” “Angalia huo mfuko
mwingine.” Mama G, akafungua. “Sasa hizi ndio chupi. Nguo za kulalia
nzuri. Kila kitu kizuri.” “Sasa fungua mfuko huo mwingine. Ni wako.” “Wewe
Nanaa vipi bwana!? Umepelekwa wewe, unaanza kununua vitu vya watu wengine!”
“Ukiona zawadi yenyewe utaacha kulalamika.” Alimnunulia Mama G nguo nzuri
mbili za kulalia. “Njoo kwanza nikukumbatie mwanangu. Nimependa kweli.
Kwanza nilikuwa nikiona uvivu tu kwenda madukani. Kila siku Grace
ananizungusha. Mara tutaenda kesho, mara leo jioni. Na mimi kuzunguka mwenyewe
sipendi. Nakushukuru sana.” Nanaa akacheka. “Umeona sasa? Kama
nilijua.” Geb akaingia akakuta Nanaa amekumbatiana na mama yake.
Waliongea watatu hao wakicheka chumbani hapo kwa
Nanaa. “Kina Grace wako wapi?” Geb akauliza. “Wameenda kuangalia
nyumba yao.” “Sasa kwa nini na wewe hukwenda!?” “Danny anataka kututoa kwenda
kuangalia sinema usiku. Kwa hiyo nikamwambia wao waende huko waniache mimi
nipumzike mpaka baadaye wakirudi, ndio nitaongozana nao huko sinema.” Mama
G akamjibu mwanae. “Lakini mimi na Nanaa tuna ratiba nyingine.” Geb
akaongeza. “Mnaenda wapi?” “Namtoa kwa chakula cha usiku.” Nanaa
akacheka. “Muone anavyofurahi.” Mama G akamgeukia Nanaa.
Usiku Wa Nanaa
Na Geb.
Ilikuwa mida ya saa moja usiku wakati Nanaa na
Geb wanatoka. Mpaka Grace akataka kumpiga picha Nanaa. Alipendeza sana. Alikuwa
amenunuliwa na Geb, kigauni cha rangi ya damu ya mzee. Kigauni hicho kilikuwa
kinafika juu ya magoti kisha kimechanua vyakutosha tu kuanzia chini ya kiuno
kilichokuwa kimeshikiliwa na kiungio kama mkanda mweusi kwenye kiuno chembamba
cha Nanaa. Juu kilikuwa hakina mikono, ila kilipita kitambaa kimoja kama kola.
Kikazunguka shingoni na kuja kufunika matiti yake kwa mbele. Alinunuliwa kiatu
cha sandals cha juu kidogo. Rangi nyeusi.
Alivuta nywele zake zote juu kabisa akazizungusha
katikati. Alivaa hereni kubwa kidogo kwa kuwa hakuwa amevaa mkufu wowote.
Akaweka lipstic nzuri nyekundu aliyokuwa amenunuliwa mchana huo. Mkono
wake wa kushoto alivaa bango kubwa sana la dhahabu iliyofanana na hereni. Nanaa
aliwaka. Kila mtu alikuwa akimshangilia pale ndani.
“Kumbe mwanangu na wewe wamo!?” Nanaa
akajificha uso. “Utajitoa sasa urembo. Acha kujishika usoni.
Muone!” Mama G akamuwahi. Geb alimpitisha sehemu akanunu foundation
waliyomjaribisha kwanza. Ikaendana na uso wake. Hakika Nanaa alikuwa amependeza.
Geb akatoka amevaa jinsi nzuri nyeusi na tisheti
ya maruni kama Nanaa. Akavaa na blazer nyeusi. Nzuri sana. Akavaa sneakers za
rangi ya kijivu, zilizoendana na mkanda aliovaa wa hiyo jinsi. Hakuna
aliyemuona Geb huyu. Alikuwa ametulia, lakini usoni alionekana kuna tofauti.
Alijawa furaha ya namna yake. Kitu kidogo alicheka mpaka akatoa sauti. Alikuwa
akinukia pafyum nzuri sana ya kiume aina ya Creed. Ile harufu tu, ilisikika ni
harufu ya pesa nyingi iliyomwagwa pale.
“Yaani mmependeza mpaka raha! Zaidi amani
nafuraha usoni mwenu. Hivyo ndio vimeongeza mvuto.” Grace akasifia.
“Asante.” Nanaa akaitikia. “Lakini Nanaa unapungukiwa
kitu.” Geb akamtizama akaona yupo vizuri. “Nini tena?” Geb
akauliza. “Nyumba zima imejaa harufu nzuri ya Geb, lakini sio wewe.”
“Mwenzio sijuagi pafyumu.” Nanaa akanong’ona. Wote wakacheka.
“Geb amenipeleka leo kwenye maduka ya pafyumu.
Nikasikia kutapika.” “Walimpulizia harufu nyingi sana mpaka akashindwa
kuchagua.” Geb alimtetea. “Basi njoo upulizie ya kwangu. Huwezi
kutoka hivihivi.” Grace akanyanyuka kuelekea chumbani kwao. Nanaa
akamfuata. Geb akabaki akimsindikiza kwa macho. Kile kigauni kilichanua, lakini
hakikuacha kuonyesha umbile la Nanaa. Baaada ya muda wakatoka
chumbani. “Nitakuletea zawadi mama.” “Hapana Nanaa. Naomba ukatulize
mawazo. Usiku wa leo ukajifikirie wewe tu. Usianze kuwaza huku tutakula nini,
au itakuaje! Katulie ufurahie. Na sisi tutatoka sasa hivi. Tunamsubiria Fili
aamke, tuondoke. Tutakula, na tutakuwa na wakati mzuri tu.” Nanaa
akacheka. “Asante mama yangu.”
Mama G,
Amrithisha Mkoba Nanaa, Bila Kujijua.
“Na mimi kuna kitu nataka kukupa. Ulikataa
cha Zinda, mimi mama yako huwezi kunikatalia.” Nanaa akacheka na kuuliza
kwa utani. “Unataka kunipa nyumba?” Wote wakacheka sana. “Nanaa
wewe mtundu sana!” Grace akadakia. “Nina sheni yangu nzuri sana ya
dhahabu. Dhahabu nzuri sana. Nimekaa nayo kwa muda mrefu sana nikiitunza.
Inaweza kuwa ina umri wa huyo Geb au zaidi kidogo. Nilikoitoa, nitakuja
kukwambia siku nyingine. Ila nataka uitunze sana.” Wakaona Nanaa analia.
“Yaani huyu bwana!” Mama G
akadakia. “Usilie sasa Nanaa. Furahia.” Grace akaongeza. “Basi
hapo ataondoa urembo wote. Ushamba tu!” Mama G akamfanya Nanaa acheke huku
akilia. “Ona ulivyotoa wanja machoni! Ukoje bwana Nanaa!?” Mama G
aliendelea kuzungumza naye lakini Nanaa akaendelea kulia. Geb akamsogelea na
kumkumbatia palepale mbele ya watu. “Nipe nimvalishe mimi au haiendani na nguo
aliyovaa?” Geb akauliza. “Mimi nataka
kuvaa sasa hivi. Sijawahi kuvaa dhahabu mwenzio.” Mpaka Danny
akacheka. “Basi itabidi tutafute na hereni zake. Usilie sasa.” Geb
akajaribu kumtuliza.
Mama G akaingia ndani na kwenda kumtolea hiyo
cheni. Ilikuwa imewekwa kwenye kiboksi kizuri sana na cha thamani. Nanaa
akaipokea na kuifungua huku Geb amemsimamia nyuma yake, amemkumbatia kiunoni.
Ilikuwa nzuri na nzito. Pana na imekerezwa maua mazuri yaliyochanganywa na maua
yenye staili ya moyo. Hakika ilikuwa nzuri. Nanaa akainama tena
nakulia. “Ningejua wala nisingekupa sasa hivi!” Mama G
akaongeza.
Geb akaichukua na kuiweka shingoni mwa
Nanaa. “Umependeza sana.” Geb akamsifia. “Asante mama.” Geb
akashukuru mama yake. “Karibu.” Mama yake akajibu. Nanaa akaenda
kumkumbatia. “Nanaa wa dhahabu!” Mama G akamchokoza. “Mbona nitalala nayo! Siivui mpaka mwili wangu uzoee
dhahabu.” Nanaa akafanya wote wacheke. Akabaki anajiangalia.
“Haya nendeni sasa. Mungu awajalie muwe na wakati
mzuri.” Wakatoka. “Umependeza sana Nanaa.” Walimsikia Geb
akimsifia. “Asante. Nakushukuru. Halafu na wewe umependeza. Unaonekana
ulipata muda mzuri wa kupumzika.” “Wewe hukulala?” Geb
akamuuliza. “Nilikuwa nahangaika kujipamba na kujaribisha vitu vyangu.
Sijalala kwa furaha.” Wote wakacheka.
~~~~~~~~~~~~~~~~
Mambo Ya Nanaa Yanazidi
Kunoga. Mama G, Ameonekana Kutoa Baraka Zake Zote Kwake. Hakuna Asiyempenda Nanaa
Pale Ndani. Yale Aliyoyakataa Kwa Zinda, Anaanza Kuyapata Maradufu. Amani Hiyo
Na Furaha Vinadumu Milele?
Usikose Kuwa
Naye Kujua Anakopelekwa.
Na Nini Kitaendelea Huko Kwenye Chakula Cha
Usiku!
0 Comments:
Post a Comment