“Huyo ndio Danny. Pale kwenye ile nyumba,
wapangaji wote walikuwa wanatujua. Mpaka mtaani pale uswahilini mimi na Danny
tulikuwa gumzo. Walikuwa wanasema ukimuona Danny yupo nje ya mlango wa bafuni,
ujue Grace anaoga ndani na ukimuona Grace anapita, ujue Danny yupo nyuma au pembeni
yake. Inategemea siku hiyo tunarudije. Akiwa ameniudhi huko nilipotoka,
tunarudi nyumbani kwa Mama G, mimi nalia nipo mbele, yeye ananibembeleza yupo
nyuma ananifuata. Hapo amenitoa kwa mwanaume, kafanya fujo, au kapigana, ndio
tunarudi sasa nyumbani kushitakiana kwa mama.” Wakacheka.
“Basi, siku ya nne Danny hajarudi nyumbani,
nikaanza kuchanganyikiwa. Danny hayupo na hatujui yuko wapi. Yule kijana hata
akija kunisalimia, sitaki tena. Kila nikimfananisha na Danny, ni kama Mungu na
shetani. Hawafanani hata kidogo. Gafla pakawa hamna tena mwanaume kama Danny
hapa duniani. Nahangaika sasa. Si unajua tabia ya mama? Kimya mwenyewe
ananiangalia ninavyohangaika.” Wakacheka kidogo.
“Sijui
pakumpata Danny, chuo kilishaisha, wenzake wote walisharudi makwao. Najaribu
sasa kuvuta kumbukumbu kujua kama Danny alishawahi kuniambia kama ana ndugu
hapa Dar. Kumbukumbu hazinijii hata kama anawazazi au la, sijui. Kwa kuwa
nilikuwa nampuuza. Simchukulii maanani. Hata akiongea tukiwa wawili, mawazo
yalikuwa sio pale na yeye, nawaza mambo yangu. Kwa hiyo nikajikuta simfahamu
Danny, mwanaume aliyekuwa kwenye maisha yangu zaidi ya miaka miwili. Tena kwa
karibu.” Grace akatulia.
“Endelea!” “Nanaa kwa kupenda stori!” Danny
akaingilia. “Ndio kazi yake hiyo. Basi anakazi ya kudodosa tu. Wewe
uongee, yeye acheke au alie. Na hataki umfupishie stori.” Mama G
akaongeza, wote wakacheka. “Basi, hali yangu ikazidi kuwa mbaya. Niliamka
siku hiyo siwezi hata kutoka kitandani, nalia kama ninaumwa. Sitaki tena kwenda
bafuni, Danny wakunibebea maji hayupo. Mama naye anajifanya hajui
kinachoniliza, eti ananiambia nikupeleke hospitali? Nashindwa kujibu, nalia
tu.” Wakacheka tena.
“Kazini siwezi kwenda tena, kitandani siwezi
kutoka. Nilishazoea nikiamka namkuta Danny kwenye makochi ananipeleka kuoga,
halafu ananisindikiza kituoni, anasubiri mpaka nipande daladala ndio anaondoka.
Na jioni siku za mvua, nilizoea nikimaliza kazi namkuta ananisubiri nje na
mwamvuli na koti la mvua, ananivalisha koti, ananishikia mwamvuli nisilowe.
Danny ndiye anajua kama sina dawa ya mswaki. Danny ndiye anajua natakiwa
kubadili mswaki, ananinunulia. Danny ndiye anajua sabuni yangu ya kuogea kama
imeisha anunue nyingine au la. Yaani nikajikuta Danny ndio anajua kila kitu
changu. Vile vitu vidogo vidogo mwanadamu yeyote anavyohitaji, vya msingi
kabisa kwenye maisha, ndio Danny alikuwa ananifanyia.” Grace
akaendelea.
“Si unajua hata kama unamamilioni ya pesa, nyumba
na gari, lakini lazima utahitaji kuoga na maji, sabuni na lazima taulo.
Kusafisha kinywa. Kwa hiyo pia ni lazima utahitaji mswaki na dawa ya mswaki. Na
lazima uwe na malapa kwa sisi tuliokulia uswahilini. Bafu la watu wote. Lazima
kuvaa malapa.” “Usisahau mashuka.” Mama G akaongeza. “Ehee, mama. Na
mashuka. Vyote hivyo Danny ndio alikuwa mnunuaji. Akiona chochote kimekaa muda
mrefu, akipata pesa tu, anaenda kubadilisha. Tena kama ni shuka, akinunua
jipya, anakuja kututandikia kabisa. Hata kama mliamka mkatandika kitanda.
Akinunua shuka lake, mtakuta limetandikwa kitandani. Sasa mtu wa hivyo huwezi
kumlinganisha na mwenye ahadi ya gari hata siku moja. Danny hajui kuahidi kama
vile alivyokuwa akikwambia Zinda. Yeye huwa ananiletea tu. Tena hata sikumbuki
kama nilikuwa nikimwambia asante. Eti Danny?” Grace akauliza.
“Hivi nilikuwa hata nasema asante kweli?” “Mimi
nilikuwa naangalia upande wangu tu. Nilikuwa najiambia lazima nikufanyie hiki.
Nikikitimiza ndio ilikuwa furaha yangu, wala sikuwahi kuzingatia upande wako.”
“Jamani! Lazima ulichanganyikiwa Grace. Huwezi kumpoteza mtu kama huyo hata
iweje.” Nanaa akaongeza.
“Kwani nilichanganyikiwa kidogo? Nilikuwa
nimechanganyikiwa haswa. Kumbukumbu zilikuwa zikinijia kwa kila kitu alichokuwa
akinifanyia. Nikawa ninakazi ya kulia tu. Nakumbuka nilikuwa nimelala pale
kitandani nalia. Sijaoga, sijala, wala mswaki sijapiga. Ilipofika jioni
hali yangu ikazidi kuwa mbaya, ikabidi kumuuliza mama kama katika mazungumzo
yake na Danny, alimwambia kwao ni wapi. Mama akaharibu zaidi aliponiambia Danny
ni yatima. Sijui alilelewa na mapadri, na hakumbuki ni wapi. Nilikaribia kuchanganyikiwa.
Kumbe Danny ni yatima! Mimi nimemfukuza, basi nilizidi kulia.” Grace
akaendelea.
“Siku inayofuata, nikaenda kuchukua likizo
kazini. Nikawaambia naumwa, sitaweza kufanya kazi. Nikarudi nyumbani. Nililala
siku tatu. Sitaki kula wala kunywa maji, nalia nalala, nalia nalala huku
nikitegemea labda Danny atarudi, lakini wapi. Mama alivyo na tabia mbaya, eti
akawa ananiacha kitandani, anaenda zake kwenye shuguli zake, akirudi
anajinyamazia zake kimyaa. Akijitahidi sana, atanishika kichwa, eti anaangalia
homa. Halafu utamsikia ananiambia, ‘lakini huna joto, itakuwa ni
kuchoka tu’.” Wakajikuta wote wanacheka mpaka Mama G, mwenyewe.
“Sasa mama kwa nini hukuwa
unamtuliza?” Nanaa akauliza. “Wewe hukumuona wakati ule namwambia
amkubali Danny, halafu ukayasikia majibu yake. Basi na macho hayo kama ya baba
yake, anasimama ananiambia, ‘niangalie vizuri mama. Nitazame juu mpaka
chini, nilinganishe na Danny. Mimi sio mtu wakuolewa na mtu kama Danny bwana.
Naliliwa na watu wamaana! Danny suruali moja!’ Basi maneno yalikuwa hayamwishi.” Mama
G akaendelea huku wengine wanacheka.
“Nikawa namwambia, mimi nazijua pesa. Zikiwa
mahali hazihitaji zisemewe, zinaongea zenyewe. Tena huwa zinakelele kweli.
Hazihitaji mdomo wa mwanadamu. Haya nikawa namuona vile mwenzie anavyohangaika
naye, namwambia Grace mwanangu, mimi nayajua maisha, wanaume kama Danny hawapo.
Danny anakujali wewe. Basi majibu yake huyo Grace utasikia, ‘Wewe mama
unayajua maisha, lakini hujayaishi bwana. Acha mimi niyaishi maisha.’ Basi
ananitajia mahoteli anayopelekwa. Ahadi anazopewa. Nikasema basi ngoja nimwache
mwenzangu ayaishi hayo maisha. Eti leo Danny kaondoka, anataka anitie
matatizoni! Nikasema nimuache kwanza atie akili. Bwana Grace alikuwa analia
kama kafiwa na mama yake mzazi! Basi mimi nilikuwa najifanya sijui. Naenda,
namshika kichwa najidai nampima homa, huku moyoni namcheka na kumwambia
akome.” Wote walicheka mpaka Danny.
“Lakini tokea mwanzoni, nilijua hatafika mbali.
Nikajua hao wanaume wote wanahangaika naye tu. Wala hatawaweza.” “Kwa nini
mama?” Nanaa akauliza tena. “Grace ni mwanangu. Namjua sana. Anapenda sana
kupendwa na kufuatilizwa kwenye vitu vidogo vidogo. Hana tamaa ya maisha, labda
akutane na mtu, amtie wazimu. Lakini hasumbuliwi na magari au nyumba. Ukimsikia
anaongelea hayo mambo, ujue sio yeye anayeongea, kuna anayeongea huko akilini
mwake. Yeye anataka akumbatiwe, ashikwe shikwe, abembelezwe basi.” Nanaa
akacheka sana.
“Akiumwa na kichwa, asikwambie. Yaani unatakiwa
wewe ujue tu kama kichwa chake kinamuuma. Akikasirika, ujue kilichomuudhi bila
yeye kukwambia. Sasa kazi hiyo niliiona ni Danny peke yake ndiye anayeiweza
kama sio mimi. Maana mimi niliwalea hawa wawili kwa pamoja. Tena kwa karibu
sana ni kama sikusaidiwa hata na msichana wa kazi.” Mama G, akaendelea.
“Geb yeye anataka akuone wakati wote. Anaweza
akawa na shida yake, asikwambie au hata asitake ujue, lakini atataka akitaka
yeye kukuona akuone tu. Huyu dada mtu yeye, umfuatilize. Tena Grace anadeka
kuliko hata Geb. Lakini watu wanasema Geb ndio mdekaji, lakini Grace ndio
amezidi. Nilikuwa namwambia baba yake, sifikirii hata kuongeza mtoto mwingine
sababu ya Grace. Nakuwa kama nina watoto wawili kwa wakati mmoja. Kuongea
hawezi, basi wewe unakuwa na kazi yakumfuatiliza nyuma. Ujue kila kitu
kinachoendelea kwenye maisha yake na umsaidie. Ukiona analia, ujue kuna
ulipompuuza tu. Lakini si Geb.”
“Sasa alipokuja Danny, nikasema asante Mungu
wangu. Nikajua huyu ndiye mume wa Grace. Maana kabla Grace hajalia shida, Danny
ataitimiza. Hata kama hana pesa. Kwa kadiri ya Mungu atakachomjalia, atamsaidia.
Na anamjua mkewe kwa kumwangalia tu. Tokea wapo chuoni. Sasa walipokuwa
wanakuja wanaume hapa wanataka kumuoa Grace, na ahadi za magari na nyumba,
nilikuwa nawajua kabisa hao sio. Nikawa nazidi kuthibitisha kuwa Danny ndio
mumewe. Sasa uzuri mwingine Danny akawa ananisaidia, yeye hajui. Kila
analoliona kwa Grace, anakuja kuniambia. Ikawa ni kama Mungu amenipunguzia
mzigo, akampa hiyo kazi Danny.” Walizidi kucheka.
“Endelea Grace.” Nanaa alitaka Grace
aendelee. Grace akacheka tena kidogo. “Yaani nyie mama ni mchokozi! Eti mwenzie
nalia, yeye ananiuliza, ‘Ni lini sasa tunahamishwa kwenye hiyo nyumba
ya mchumba wako?’ Basi ndio nazidi kulia, sitaki hata mama amtaje.
Kwanza yeye ndio kasababisha Danny wangu aondoke. Sitaki hata kuiona sura yake.” Walizidi
kucheka.
“Nilipoona yananifika shingoni nikamwambia mama
nahisi nisipomuona tena Danny, nitakufa. Eti mama anazidi kunichokoza
ananikumbusha maneno yangu. Ananiambia, ‘Mimi naona uachane na Danny
tu. Kwanza Danny masikini. Danny suruali moja! Achana naye. Twende hospitalini,
ukaangaliwe afya yako, upone tuanze kujiandaa na kuhama hapa. Tufikirie maisha
mapya tukiwa na nyumba na gari.’ Basi ndio ananikera zaidi nazidi
kulia.” Watu wakazidi kucheka.
“Mama wewe!” Nanaa akashangaa huku anacheka.
“Kumbe!” Mama G akajibu. “Na usifikiri anaongea hayo kwa kifupi. Anaongea
mwenyewe huku anafanya shuguli zake hapo ndani wakati mwenzie nimelala, nalia.
Eti ‘huu ndio wakati wa kuyaishi maisha bwana!’ Anajiongelesha
huku anaingia na kutoka. Akaenda kuoga, akala, akapanda pale kitandani
nilipolala. Akanishika tena kichwa, hapo nimeanza kupandisha homa kwa kulia.
Eti ananiambia nimpe namba ya simu ya yule mchumba amuombe alete gari,
anipeleke hospitalini.” Nanaa alizidi kucheka.
“Yaani mama wewe!” Nanaa akaongeza.
“Nilitaka nimwache mpaka akiri ujinga wake. Nikajidai kama sijui kinacho
mliza.” “Ndio nikamwambia mama, mimi siumwi. Namlilia Danny. Namtaka Danny. Eti
mama akajifanya kama gafla hamjui tena Danny. Eti ananiuliza Danny yupi? Eti
yeye anakumbuka jina la yule mchumba niliyemletea haitwi Danny. Tena akaanza
kunishauri, eti niwe makini sana na ninavyowataja majina yao. Nisije
kuwachanganya, nikaachwa. Eti kupata wanaume wanaohonga magari na nyumba ni
shida sana. Mimi nimebahatika, niwe makini, nisije kuishia kama yeye,
nikashindwa kuyaishi maisha.” Walizidi kucheka.
“Nikajua ananikejeli tu. Nikawambia namtaka Danny
huyu tuliyekuwa tukiishi naye. Akaniuliza sasa nyumba na gari? Hapo anazidi
kuniliza. Nalia kweli. Nikamwambia mimi sitaki nyumba wala gari, namtaka Danny
wangu. Mama akazidi kunikera sasa, si nilimwambia hajayaishi maisha? Sasa
akaamua kunikomoa. Eti ananiambia nafanya maamuzi mabaya sana kwa kumchagua
Danny. Sitayaishi maisha. Jamani nikaangua kilio zaidi. Namwambia hamna maisha
bila Danny mama. Namtaka Danny. Lasivyo nitakufa. Nikawa nalia kwa kwikwi
sinyamazi. Hapo ndio akanionea huruma, akashauri niwatafute marafiki
zake. Namba za simu sina. Mama akaongea na Geb, Geb akamtumia namba zote za
marafiki zake Danny.” “Kwani yeye mwenyewe hakuwa na simu?” Nanaa
akauliza.
“Hela ya simu atoe wapi wakati pesa yote anampa
Grace?” Mama G akajibu nakufanya wote wacheke. “Hakuwa na simu. Basi
mama akaanza kazi yakumpigia mmoja baada ya mwingine. Ndio akaambiwa Danny yupo
kwa kina Zinda, Tabora. Anafanya biashara na baba yake Zinda. Anakusanya pesa,
ili aje arudi chuoni asome sasa shahada yake ya pili. Nikaanza kukusanya mizigo
yangu.” “Unaenda wapi sasa?” Nanaa akauliza.
“Tabora kumfuata Danny! Nilikuwa siwezi tena
kusubiri, na sikutaka aambiwe kuwa naenda, asije kunikimbia. Mama akamuomba
Zinda, anisubiri kituo cha mabasi, nakwenda kesho yake. Basi, nikaamka asubuhi,
nikawahi mabasi mpaka Tabora. Zinda akanipokea kituo cha mabasi. Ilishakuwa
jioni, akaniambia Danny huwa anarudi usiku kutoka kwenye biashara zake na baba
yake. Mama yake Zinda akanitayarishia chakula, sikuweza hata kula, nilikuwa
nalia tu. Nikabaki namsuburia Danny. Hapo nalia kama nimefiwa, hakuna aliyekuwa
ananielewa. Ikafika kama saa tatu usiku, ndio Danny akarudi.” Nanaa
akamuhurumia.
“Nakumbuka alikuwa amechoka mwenyewe, halafu
amekondaa gafla. Hakuamini aliponiona pale. Akaniambia nimsubiri aoge, halafu
tuzungumze. Akaoga, akaniambia tuzungumze nje. Nilishindwa hata kuongea
kwa furaha. Nililia mpaka basi. Akanichukua akaenda kunitafutia chumba, kwenye
nyumba ya kulala wageni. Maana pale kwa kina Zinda kulikuwa kumejaa, hakuna
hata pakukanyaga. Zinda akikwambia anakwenda kufuata wadogo zake kwao awalete
mjini, usifikiri anakutania. Ni kweli anampango wakuwahamishia ndugu zake
mjini. Kwa hiyo Nanaa ujiandae.” Nanaa alicheka mpaka machozi.
“Unacheka nini? Ndio ujiandae.” Mama G,
akamchokoza. “Zinda hawezi kuwa mume wangu. Nilishamwambia, tokea tupo
Marangu.” “Ndio maana alikuwa amepooza! Basi kila nikimuuliza Zinda vipi
mwanangu, ananiambia maisha tu mama.” “Alituambia usiku uleule mimi na James.
Kuwa Nanaa amemkataa. Amesema hayupo tayari kuolewa. Nikamuuliza kwa nini
hakuomba hata wawe kwenye mahusiano? Akaniambia alimuomba, lakini
Nanaa amemkataa katakata. Huku akisema mpaka amalize shule, ajiweke sawa kwenye
maisha. Wakati huo bado hajatulia. Ndio James akajaribu kumuelezea wakati mgumu
anaopitia Nanaa wakati huo, akaomba Nanaa aachwe kabisa. Lakini Zinda
akanifuata baadaye akasema anahisi James anamkatalia tu kwa dada yake, kwani
kama angetaka James, angeweza kuzungumza na Nanaa, akamkubalia. Akaniambia hata
siku tuliyokuwa tukimnunulia vitu Nanaa, James hakuonekana
kufurahia.” Danny aliongeza na kumshangaza Nanaa.
“Zinda alininunulia mimi vitu!?” Nanaa
akauliza kwa mshangao sana. Geb akamtizama. Nanaa akajishitukia. Akamtizama
Geb. “Sio kwamba navitaka jamani! Nauliza tu.” Nanaa akajitetea kwa
sauti ya chini, akainama kuendelea kuangalia kidole cha Geb. “Unafikiri
alikuwa akikudanganya alivyosema atakununulia viatu na magauni?” Danny
akauliza, wote wakacheka kasoro Nanaa. “Mwenzio alikuwa hatanii. Sema tu
hajui kutongoza. Pale walikuwa wakiendesha gari yake, kwa kusudi kwa kuwa
ilibeba mizigo yako. Vyote alivyokutajia siku ile alinunua kweli. Ila akaongeza
na maua. Mpaka nguo yakuvaa kwenye ile Sendoff ya mke wa Malii,
alikununulia.” Danny akaongeza.
“Kukimbia kimbia kumekufanya ukose zawadi.”
“Nisingepokea mama. Nisingeweza kumfanyia hivyo wakati nilijua wazi
nisingemkubalia. Na yeye nilimwambia ukweli. Zinda ni mtu mzuri. Sikutaka kuja
kumuumiza baadaye.” “Hukumpenda?” “Mama na wewe! Hayo ni maswali yetu tukiwa
mimi na wewe tu? Mpaka watu wajue siri zetu?” Wakacheka sana.
“Si utuambie tu Nanaa! Na sisi tunataka kujua
bwana. Kwa nini ulimkataa Zinda?” “Bwana Grace achana na mambo hayo. Tuendelee
na stori ya Danny na wewe. Ndio nzuri, kwanza inafundisha.” “Anapenda stori
huyu! Hapo mbona umemfikisha. Na hataki umalize. Ukimuendekeza Nanaa, mtalala
hapa.” “Bwana mama! Usimfanye Grace agairi. Endelea mwaya Grace. Uliishia
alikukodishia chumba.” Watu wote walicheka kwa pamoja.
“Si niliwaambia? Huyo kwa stori hamtamuweza.
Anakumbuka neno kwa neno.” Mama G, akaongeza. “Mimi ndio msikilizaji
mzuri. Si eti Grace? Naonyesha nakusikiliza kwa makini. Mwenzio najifunza.
Endelea.” “Mmmh!” Mama G, akaguna. “Nini mama jamani? Endelea
Grace.” Grace akacheka.
“Basi. Nakumbuka Danny alitaka aondoke,
aniache pale kwenye nyumba za kulala wageni, akaniambia atarudi asubuhi yake,
lakini nilishindwa kumuachia. Nilikuwa nalia sana. Basi akapanda kitandani, tukalala
akawa ananimbembeleza. Ndio kwa mara ya kwanza tokea aondoke, usiku huo
nikalala.” “Si niliwaambia anapenda kubembelezwa? Basi hata umuudhi vipi Grace.
Wewe mbembeleze tu. Tena usichoke. Akikufukuza ukaondoka, ndio umeharibu
kabisa. Wewe hata akikufukuza, wewe endelea kubaki hapo mbembeleze kama Danny
anavyomfanyiaga. Ndio anajua unamjali.” Wote wakacheka.
“Na Danny anajua kubembeleza. Anaweza kukuudhi
mpaka ukasema leo ndio mwisho wetu. Lakini akianza kukubembeleza, mwenyewe
unasamehe.” “Mmmh!” Mama yake akaguna. “Sasa nini mama?” “Wewe endelea na
stori, Nanaa asijekuniona mimi ndio mbaya. Maana usipomaliza, mimi leo
sitalala. Atanifuata mimi mpaka kitandani kwangu nimalizie hiyo
stori.” Wakacheka.
Grace akaendelea. “Basi, asubuhi nikaamka
nikamuona mwenyewe alishaamka kama kawaida yake, ameenda kuniombea maji ya moto
ya kuoga. Ananisubiria niamke nikaoge. Akanipeleka bafuni, nikaoga. Tukarudi
chumbani. Ndio nikamwambia nimemfuata. Nikamwambia sirudi Dar bila yeye. Kwa
hiyo kama hataki kurudi nyumbani, basi atafute sehemu yakuishi na mimi palepale
Tabora. Danny hakuamini. Basi tulikaa pale kama siku nne, akikusanya pesa yake
na kuanza kumfahamu sasa. Kujua yeye ni nani. Kwao ni wapi, kabila gani na
mambo yote, ndio tukarudi Dar. Hatukukaa sana, tukaamua kufunga ndoa kabla hata
hajarudi tena chuoni. Basi, tukafunga ndoa. Harusi ilikuwa ndogo tu, ya pilau
na soda, tena palepale kanisani. Tukarudi zetu nyumbani. Ndio tupo mpaka leo na
Danny wangu tunazungushana.” “Daah! Hongereni sana. Kumbe mmetoka mbali!? Basi
mtu akiwaona, ni kama mmeoana jana. Pale kazini hawaishi kusimulia habari
zenu.” Wote wakacheka.
“Tena pale ndio wametuchoka. Akiamua Danny
kuja kuwasha moto hapo, utafikiri nini sijui! Wateja wote mbona wanatufahamu!
Fujo za Danny kila kukicha. Anaweza kuja pale kazini muda anaotaka yeye,
hakwambii, utasikia mlango umefunguliwa. Sasa akukute unaongea na mteja
mwanaume, umekaa naye peke yenu pale ofisini, mlango umefungwa.
Weeee!” Wote walianza kucheka.
“Ataanza kufanya fujo hapo, utafikiri
amekufumania. Na heri mteja awe mstaarabu. Akifanya fujo, anaanza kurusha
ngumi. Akiwa mstaarabu sio kwamba atamuacha, simu inapigwa kwa Geb, anamuuliza
kama anamfahamu huyo mteja.” “Haiwezekani!” Nanaa akazidi
kushangaa. “Wewe muone Danny katulia hapo hivyo hivyo. Yaani ukimuona
Danny katulia kama hivyo, ujue macho yake yanamuona mkewe alipo. Akinyanyuka tu
pale alipokaa, na yeye akili imeshavurugika. Iwe anaenda chooni au jikoni,
anamuhesabia sekunde. Zikizidi tu sekunde alizomuwekea, na yeye anasimama,
anamfuata mkewe popote alipo.” Mama G, akaongeza.
“Tena anione nimekaa kweli. Sio nimekaa na simu
mkononi, hapana. Anataka nikae kabisa nitulie tukae tunaangaliana hapa. Ndio
anaweza hata kuangalia taarifa ya habari akaelewa au ukamuuliza swali akakujibu
vizuri. La sivyo hii nyumba inakuaga ndogo. Anamtaka mkewe. Na hana yale majina
ya sijui honey, sweet, sijui mpenzi, hana huo muda. Anachojua mkewe tu, tena
tokea zamani hata hatujaoana.” Grace akaongeza.
“Na ikifika swala la mkewe, huyo Grace
anakuwa hana mama wala kaka. Anambadilikia kila mtu. Na anakuwa mkali kweli
kweli. Basi nikiona tu simu yake, hata kama nipo kwenye kikao nilazima niipokee
lasivyo utasikia nina mgeni. Na simu zake hazianzi na salamu, ni swali
moja kwa moja. Utasikia, ‘Unamfahamu mteja fulani?’ Hapo najua
yupo ofisini kwa Grace, na mafaili yote ya huyo mteja yameshaagizwa
aletewe. Kuanzia oda alizowahi kuzitoa, ulipaji wake, yaani kila kitu anataka
kiletwe.” “Sasa aletewe wapi?” Nanaa akamuuliza Geb. “Hapo hapo ofisini kwa
Grace, tena mbele ya huyo mteja. Ili kuthibitisha kama kweli yeye ni mteja, na
kweli anashida na mzigo sio kwamba anamtaka mkewe.” “Sasa mteja anasemaje?”
“Huna utakachosema kwa Danny linapofika swala la mkewe. Hapo anawaka
kama moto. Kazi zote zinasimama hapo ofisini mpaka mafaili yote yaletwe,
yeye mwenyewe ajiridhishe na huyo mteja.” Mama G akajibu yeye.
“Na usifikiri akijiridhisha ndio inaisha. Anapiga
tena simu kwangu. Hapo ananibadilikia, utafikiri hatufahamiani, au hatuishi
nyumba moja au huyo mkewe sio pacha mwenzangu. Anaanza sasa, ‘Nisikilize
vizuri Geb. Kama biashara imekushinda, acha. Tulia kazini. Acha kutumia uzuri
wa mke wangu kukuingizia pesa. Utaniona mbaya kabisa.’ Hapo ataniwakia
kwenye simu, anakutukana, anakutisha, mpaka ajiridhishe ndio anakata
simu.” Nanaa alizidi kucheka wakati Geb anasimulia.
“Sasa Grace anasemaje?” Nanaa akauliza.
“Inategemea na mimi siku hiyo amenikutaje. Nikiwa vibaya, nakusanya vitu vyangu
pale ofisini wakati anafanya fujo zake, naenda kwa mama. Kama yupo nyumbani
narudi nyumbani. Kama yupo kazini kwake, nitaenda. Popote alipo mama ndipo
nitakapokwenda. Basi nitalia weee. Utafikiri ndio mwisho wetu. Basi muda
haupiti na yeye ananifuata. Hapo anakuwa ameniletea zawadi ya kitu chochote
kunituliza.” “Na akiingia hapo Danny, utafikiri wanamsingizia. Anakuwa mpole
kweli kwa mkewe. Atamtuliza wee kwa maneno mengi utafikiri kakosewa na mtu
mwingine. Yale aliyoyafanya kule hatayasema kabisa. Anaweza kumchagua Geb
kuwa ndio mbaya wao, anataka kuwavunjia penzi lao au yeyote yule. Atambembeleza
mkewe hapo, huku anamsema Geb. Utasikia, ‘Geb anataka kutuchonganisha
mke wangu. Anataka kukuuza kwa wanaume wengine sababu ya kujipatia pesa. Geb
anaroho ya wivu, hafurahii kutuona tunavyopendana. Nyamaza mke wangu’ Yaani
Grace anaishia kucheka tu.” Mama G akaongezea nakufanya wote wacheke.
“Lazima ucheke. Eti anakubembeleza hasemi ugomvi
aliouanzisha yeye kule kazini, au aibu aliyokutia mbele za watu, eti lawama
zote anamtupia mtu. Tokea tupo chuo, kazi yake ni hiyo hiyo. Anakutoa hotelini
kwa kupigana kama amekufumania, basi aibu kweli, nalia, hana pesa ya taksii,
mnaishia kupanda daladala tunarudi chuo au kwa mama kusemeana. Umeenda
hotelini na gari, umependeza, unatolewa kwa aibu, kama umefumaniwa! Na hapo
anatangaza mimi ni mkewe, sio hata mchumba, mkewe. Halafu heri akukodishie
taksii kukurudisha nyumbani, mnapanda naye daladala. Kwenye daladala si
ninaendelea kulia, yeye ananiambia, ‘pole mke wangu. Mungu yupo, ipo
siku na sisi tutakuwa na gari yetu. Nitakupeleka kwenye mahoteli makubwa,
tutakuwa tunakula na kulala huko huko.’ Basi nazidi kulia. Aibu mara
mbili. Watu wote kwenye daladala wanajua unalilia kupanda gari, kumbe katoka
kunifanyia fujo.” Nanaa alikuwa anacheka mpaka machozi.
“Basi wakifika hapo nyumbani, Grace akiingia
analia, na Danny anafuata nyuma, najua tayari. Kashamtoa mkewe mahali.” “Sasa
mama ulikuwa unawaambiaje?” “Ndio unaanza kusikiliza tena kesi, lakini Danny
hathubutu kukupa nafasi yakuingilia ugomvi wake. Utafikiri anayesemwa
hapo na Grace ni mtu mwingine sio yeye. Yeye ndio yupo mstari wa mbele
kumtuliza Grace, tena hapo anamwita mkewe. Wataongea wawili hapo Grace analia
huku anagomba, Danny kajishusha kweli kweli. Mpole kama yeye hamna. Kila
anachoongea Grace anaitikia, huku anambembeleza, mpaka Grace anaishia kucheka.
Asubuhi wanaondoka tena kurudi chuoni. Naweza kutulia siku mbili au tatu,
utawasikia tena hao wamerudi, au utasikia mtoto anakuja mlangoni kwako huku
anakimbia, utasikia, ‘Mama G! Mama G! Grace na Danny wanakuja.’ Basi
tena hapo natafuta mahali pazuri, nakaa. Najua kesi inaanza.” “Kwa hiyo mpaka
watoto walikuwa wanawajua!?” Nanaa akauliza.
“Mpaka vitoto vidogo vilikuwa vinatujua.
Wakimuona Danny anapita, wanamuuliza dada Grace yuko wapi, au mimi nikipita,
watamuulizia kaka Danny! Kila mtu alikuwa akitujua pale mtaani. Maji yangu ya
kuoga anayafuata Danny bombani. Na wakati mwingine anafika amechelewa anakuta
watu wapo bombani. Utasikia naombeni mniruhusu nichote ndoo moja tu. Basi watu
wanamuuliza, ‘ya Grace?’” Nanaa akacheka. “Yaani walishatujua.
Kila siku mimi na Danny ni vituko tu.” Waliendelea kucheka.
“Yaani hata hii kazi kama Geb angekuwa sio ndugu
yangu, mbona angeshanifukuza muda mrefu sana! Fujo zikianza pale, kuna wateja
wanafukuzwa, kuna wanaojibiwa vibaya, yaani ni fujo mpaka mama akanishauri
nisiwe nafunga mlango wa ofisi. Kwa hiyo siku hizi mlango wa ofisi yangu
haufungwi. Nikiingia tu naacha mlango wazi kabisa, ili akija awe anaona
ninayezungumza naye huko ndani.” Grace akaendelea.
“Na
akifika tu, hana salamu. Anaenda moja kwa moja kwa mteja, anajitambulisha kuwa
yeye ni mume wangu na tumeshazaa mtoto mmoja. Basi wakati mwingine ni aibu.
Unakuta upo na mteja wa maana, na heshima zake, Danny naye anaingia. Unatamani
kumficha huyo mteja. Mara Geb anapigiwa anaanza kugombeshwa na kuulizwa
majukumu yangu.” “Hilo swali nishalizoea. Kila siku naulizwa kwani kazi za
Grace pale ni zipi. Naelezea. Mama akaniambia nimwandikie Danny nimpe ili ajue
majukumu ya mkewe. Lakini akikasirika hakumbuki. Na usithubutu kumwambia
nilikuandikia. Hapo utajuta. Ni heri akikuuliza wewe umtajie tu. Mkewe anaingia
nakutoka kazini siku na muda anaotaka yeye Danny, na usimuulize. Ukimuuliza
mbona Grace hajafika kazini mpaka sasa hivi, upo naye? Utasikia, ‘kwani
wewe wakati unamwajiri, hukujua kama Grace ameolewa? Grace anamajukumu ya
muhimu sana kuliko hiyo kazi yako’.” Nanaa akazidi kucheka.
“Basi hapo inabidi kumpigia simu mama, utasikia
Grace yupo chumbani analia, mumewe kamkataza kwenda kazini. Labda utaambiwa
siku hiyo alitoka na nguo yakumbana. Kwa hiyo amehisi siku hiyo Grace atakuwa
kuna anapokwenda au kuna mtu atakwenda pale ofisini kwake, kwa hiyo Grace
ameambiwa asitoke humu ndani. Hapo ukute kuna kitu cha muhimu ulitaka Grace
afanye siku hiyo, ila mumewe kasema asiende kazini. Na ukizidi kumuuliza anakwambia
ukizidi kumkera, mkewe anaacha kazi. Basi inabidi siku hiyo ufanye kazi mara
mbili. Nitoke ofisini kwangu, niende tena ofisini kwa Grace kufanya kazi zake.
Ukija hapa nyumbani Grace naye analia amemnunia mumewe, mumewe anakulaumu wewe,
halafu umechoka! Utajuta kumuajiri Grace. Unatamani kumfukuza kazi, lakini
huwezi. Mama anakwambia wavumilie tu.” Waliendelea kuongea hapo huku
wakicheka.
~~~~~~~~~~~~~
Nanaa akarudi kwenye kidole cha
Geb. “Kinauma?” Nanaa akauliza kwa upendo. “Wala sisikii kitu!” Nanaa
akacheka. “Utanifanya nilale hapa hapa kama Fili!” “Mbona natumia nguvu
nyingi!” “Ona mikono yako inavyotetemeka! Inatoa jasho kwa woga.” “Naona kama
nitakuumiza!” “Huniumizi Nanaa. Acha woga.” “Haya. Lakini nikikuumiza, naomba uniambie.” Geb
akacheka. “Usicheke bwana!” “Kila wakati unarudia kusema hivyo hivyo,
lakini hunitoi huo mwiba!” “Sasa hivi nakutoa.” Nanaa akajifuta jasho la
kwenye viganja vyake, Geb akaanza kucheka.
“Nakwambia huyo nesi wa Geb anavyohangaika! Yeye
ndio ana maumivu kuliko mgonjwa!” Wote wakacheka na
kuwageukia. “Naogopa mama!” “Basi hutautoa huo mwiba! Mtakesha hapo.”
“Sasa hivi nautoa.” Akasogea karibu akaendelea kumtoa mwiba huku Geb
akimwangalia.
Mtu Chake.
Sababu yakucheka na stori nyingi pale, hawakusikia
hata geti likifunguliwa. Wakashitukia Liz ameingia. Watu wote wakanyamaza.
Nanaa akaachia mkono wa Geb taratibu, akajisogeza pembeni kwa tahadhari. Liz
akasimama pale kwa muda akishangaa aina ile ya mkao wa Nanaa na Geb. Nanaa
akaingiwa na hofu mpaka Geb akajua.
~~~~~~~~~~~~~
Akiwa na
ahadi ya kulindwa asilie, na kama atalia basi atafutwa machozi. Hata siku
haijaisha, historia inataka kujirudia. Mwenye mali amerudi. Liz aliyeanza
kumtilia mashaka Nanaa, amemkuta amekaa karibu na mpenzi wake. Ilikuwa sweta la
Geb, leo ni mkono wake.
Kipi Chakujitetea
Tena Juu Ya Mkono Wake Mikononi Mwa Nanaa?
Amani na
furaha iliyokuwepo pale, gafla imepotea baada ya mwenye mmpenzi kuingia. Ni
kweli wengine wamemzoea na kumfahamu tabia zake. Lakini anamnyima raha Nanaa
kitu kinachomfanya Nanaa kutaka kuhama pale. Na amekwisha kumwambia Geb jinsi
asivyopenda kumnyima raha mpenzi wake. Ni heri yeye aondoke. Na Geb ameshindwa
kuishi mle ndani bila Nanaa.
Ni Nini Geb Atafanya
Usiku Huo Katikati Ya Wanawake Hao Wawili?
NANI WA
NANI?
Usikose Kufuatilia…...
0 Comments:
Post a Comment