“Mbona unajisugua kidole?” Nanaa akamuuliza
kwa sauti ya chini. “Nahisi nilichomwa na mwiba muda mrefu. Pameanza
kuwasha.” “Tuone.” Nanaa akamvuta mkono taratibu. Akaangalia. “Naona
kuna kitu cheusi kwa ndani. Itakuwa mwiba. Upo ndani kidogo. Utavumilia nikutoe?”
“Nitashukuru. Unanikera kweli!” Nanaa akaenda kuchukua pini chumbani
kwake, akarudi kukaa pembeni yake. Akaanza kumtoa ule mwiba
taratibu. “Nikikuumiza uniambie.” Geb akacheka. “Unavyoshika kwa
woga! Sijui kama huo mwimba utatoka.” “Naogopa kukuumiza!” Akaendelea
kumtoa huku wengine wakiendelea kuangalia tv palepale sebuleni. Alijua wazi
wanawasikiliza.
~~~~~~~~~~~
“Nasikia Nanaa leo umepelekwa
Bagamoyo?” Grace alitupia swali, Nanaa akacheka. “Lakini wala
hatukukaa sana. Tulikuta ndio wanamalizia kupakia.” Nanaa
akajibu. “Na mimi nilijaribu kuwa na kwenda kuangalia upakizwaji wa mazao,
lakini nikashindwa.” Nanaa akashangaa kuona wote wanaanza
kucheka. “Kwa nini!?” Nanaa akauliza. “Yaani Nanaa, si unaaga
hapa. Unasema unapokwenda na pengine muda utakao rudi kama watamaliza mapema.
Unakubaliwa vizuri. Unasindikizwa mpaka kwenye gari, hata mkanda unaweza
kufungwa, na maneno mazuri ya kutakiwa safari njema, ‘Mungu akurudishe
salama mke wangu. Tukumbuke mimi na Fili, tunakupenda na tunakuhitaji.’ Na
maneno mengi mazuri, mengi tu. Haya, unafungiwa mlango wa gari vizuri, unawasha
gari unaondoka.” Grace akacheka yeye mwenyewe.
“Nini?” Nanaa akauliza huku na yeye ameanza
kucheka. “Danny nyie! Acheni tu. Yaani wakati unatoka tu hapo getini, unamuona
kwa kutumia vioo vya gari, simu zinaanza. ‘Unarudi saa ngapi?’ Unarudia
tena maelezo yote uliyoyatoa jana yake na muda mfupi wakati mnaagana. Haya.
Ukifika tu kwenye hayo mataa ya kwanza hapo barabarani, simu nyingine. ‘Umefikia
wapi?’ Swali la kwanza na la pili huwa halina shida, ila hayo
yanayofuata kuanzia hapo, lazima ukereke tu. Utasikia, ‘mbona kama hapo
ulipo pako kimya?’ Unajibu labda nimesimama kwenye mataa. Utasikia
tena, ‘mbona hata sisikii mlio wa gari?’ Ujue hapo kazi ndio
imeanza.” Watu walizidi kucheka.
“Yaani hapo nimeondoka nyumbani hata dakika kumi
hazijaisha, tayari kelele zimeanza. Mpaka uje ufike huko, njia nzima ni maneno.
Unafika umenuna, huwezi kuongea na wafanyakazi. Na ukikaa hapo shamba, nusu saa
nyingi, na yeye anakuwa amefika.” Nanaa alikuwa anacheka sana, ila
akatulia na kushangaa. “Haiwezekani Grace! Sasa anatumia njia gani kufika mpaka
Bagamoyo? Kulivyo mbali hivyo!” “Wewe humjui Danny na kichwa chake. Yaani ile
simu ya 3 kuwa mbona hasikii mlio hata wa gari, ujue hapo na yeye anavaa nguo,
ananifuata.” Wote walikuwa wakicheka.
“Sasa na yeye kazini inakuwaje?” Nanaa
akauliza. “Kazi gani tena? Wewe unafanya kazi wakati unaibiwa mkeo? Kazi
itasubiri kwanza.” Danny akajibu. “Huna utakalomwambia Danny kwa
mkewe mkaelewana.” Mama yao akaongeza. “Mimi na Geb tulishajua. Grace
akitoka tu, ujue Danny atafuata nyuma. Yaani umtume mkewe Bagamoyo! Humtakii
mema Danny.” Nanaa alizidi kucheka huku akishangaa.
“Alivumilia mara ya kwanza na ya pili. Ya tatu,
akamfuata Geb. Eti aache kumvunjia ndoa yake.” Walikuwa wakicheka
sana. “Na usifikiri anatania? Yaani hapo kanifuata amenikasirikia kweli
kweli. Eti kama shida yangu aachwe, yeye ahangaike na mtoto hapa mjini, basi
niendelee kumtuma mkewe mashambani. Nakuwa kama namuuza mkewe kwa watu. Eti
nashindwa kufikiria swala la usalama wa mkewe, namtuma kwa wanaume. Kama ni
pesa, eti basi. Hapo Danny kawaka kweli kweli. Unajua alinitoa kazini akanituma
nikamfuate mkewe nimrudishe nyumbani?” “Haiwezekani! Sasa
ulienda?” Nanaa hakuwa akiamini, akamuuliza Geb kwa mshangao.
“Unacheza na Danny wewe? Hivyo hapo ni kwa kuwa
hakuwa akipafahamu alipo mkewe, lasivyo angeenda mwenyewe. Ikabidi niage
ofisini nimfuate Grace. Kwanza alinipa dakika kumi ya kuondoka pale nikamfuate
mkewe, lasivyo angewasha moto majengo yote yale ya BOT.” “Haiwezekani!” “Humjui
Danny wewe. Hapo kaja na kiberiti, kakishika mkononi.” Danny alikuwa kimya
kama sio yeye.
“Kwanza nilikuwa kwenye kikao, simu nimeacha
ofisini. Nilipokuja kuitwa kwenye kikao kuwa Danny anataka kuniona, nikaanza
kujipapasa mifukoni kuangalia simu yangu. Nikajua atakuwa amenipigia amenikosa
ndio maana yupo pale. Haraka sana nikaanza kujiuliza alipo Grace, nikakumbuka
alisema angeenda Bagamoyo. Basi nikatoka pale nikiwa nimeshajiandaa. Nimefika
tu pale, akanitupia swali, eti ‘hivi wewe Geb, tatizo lako ni kwamba
hujui kutangaza biashara yako au simfikirii yeye na mwanae, Fili?’ Nikatulia
kwanza sikujibu kwa haraka, kwa kuwa alikuwa amekasirika sana. Nikabaki
kimya.” Geb akaendelea.
“Eti akaniambia kuwa najua wazi kuwa mkewe
anavutia. Hakuna mwanaume atakayemuona Grace asimtamani. Eti akiwa amekaa tu
huyo mkewe anavutia usoni, akisimama ndio kabisaa. Hakuna mwanaume atakayeacha
kumtamani mkewe, hata kipofu akisikia sauti ya mkewe atataka kumshika
mkewe.” Wote walikuwa wanacheka.
“Usifikiri maneno hayo Danny anaongea akiwa
amekaa, ni amesimama, anawaka kama moto. Sasa hapo najiuliza moyoni, sijui
Danny kama hapo alipo wakati huo anaponigombesha najiuliza hakuna kweli wazo hata
moja linalopita na kumkumbusha kuwa Grace ni dada yangu, tena pacha!? Sasa zile
sifa anazozisema za mkewe, hajui kuwa anamwambia kaka yake? Huku natamani
kumjibu kuwa labda huo uzuri wa mkewe anauona yeye tu, wanaume wengine
hawauoni, lakini sikuthubutu, nikajua utakuwa ugomvi mkubwa zaidi.” Geb
akaendelea.
“Hapo ananitukana na kunigombesha eti kwa kuwa
nimeshindwa kufanya biashara zangu, ndio nimeona nitumie uzuri wa mkewe
kujipatia wateja. Sasa hapo ni kelele, na amenitoa katikati ya kikao.
Nikamuomba kiustarabu, nikamwambia, naomba tukazungumze nyumbani. Wewewewe,
ndio niliharibu zaidi. Akaniambia, ananipa dakika kumi, niwe nimetoka pale
nikamfuate mkewe popote nilipomtuma. Nimletee mkewe ndipo tutazungumza. Lasivyo
hata ikizidi sekunde, anawasha moto lile jengo lote. Hapo katoa kiberiti. Na
ananiambia nimebakiza dakika 9, niwe nimetoka pale. Haraka sana anamtaka
mkewe.” Walikuwa wanacheka sana. Nanaa ndio alikuwa anafuta machozi.
“Sasa kwa nini usimpigie simu Grace mwenyewe
umwambie arudi?” “Hapo Grace mwenyewe kakasirika kweli kweli. Danny
kashamchemsha kwa maswali kuanzia anaondoka mpaka anafika huko. Mara amesikia
sauti ya mwanaume pembeni yake. Mara kama amesikia sauti kama yupo kwenye
chumba kitulivu, ilimradi tu. Sasa Grace hapo na yeye kashakasirika anawazimia
simu wote au hapokei simu ya mtu. Hataki kurudi mpaka akamilishe kazi yake, na
Danny naye anamtaka mkewe. Basi hapo ni shuguli. Simu zinapigwa kila mahali
mpaka kwa mama.”
“Sasa na mimi huko kazini kwangu shuguli sio
ndogo. Grace anapiga simu analia, Geb naye anakwambia Danny amemwambia
akamfuate mkewe, na alikuwa kwenye mkutano, sasa bado simu ya mwenye mke. Hapo
ndio utachoka. Utasikia ‘mama, si unayajua maumbile ya mke wangu
yanavyotamanisha?’” Watu walizidi kucheka.
“Basi
mimi namjibu taratibu maana hapo anawaka kweli kweli, namwambia ‘Sijui
mwanangu.’ Kidogo ndio anashituka kuwa anaongea na mama yake Grace,
anatulia. Lawama zinahamia kwa Geb. Geb anamuuza mkewe kwa wanaume. Geb sio
muungwana. Geb anashindwa kumfikiria yeye na Fili. Mkewe akiwaacha yeye
ataleaje mtoto peke yake. Yeye ni yatima, hataki maisha aliyoishi yeye ndio
Fili ayaishi. Geb anaweka pesa mbele kuliko utu. Hapo atalalamika
mpaka wafike Bagamoyo amuone mkewe ndio anakata simu.” “Bagamoyo tena!?” Nanaa
akauliza.
“Kwani wewe unafikiri aliponituma
kumfuata mkewe Bagamoyo yeye alibaki? Tuliongozana naye mpaka Bagamoyo
akamuone mkewe.” “Haiwezekani!” Nanaa hakuwa akiamini. “Hujamjua Danny.
Hapo tena wewe adui. Unamuuza mkewe, hawezi kukuamini tena. Kwanza haamini mtu
na mkewe. Hataki umsifie mkewe hata kidogo. Mbona kina James wanajua. Ukitaka
ugomvi na Danny, anza kumsifia mkewe. Hapo utamjua yeye ni nani.Wewe utakuja
kumuona tu. Si Upo hapa? Utamuona, na hana aibu yeyote linapofika swala la
mkewe.”
"Basi huyo Grace anakuwa anarudishwa
nyumbani kutoka Bagamoyo na msafara. Yeye Grace mbele, mumewe anafuata, halafu
mimi nafuata nyuma nikishamalizana na watu huko shamba. Hapo kashanitukana
mbele ya mkewe, kama ni mshahara ninao mlipa mkewe, nisimbambaishe nao. Na yeye
pesa anayo, anauwezo wa kumlipa mkewe, tena kwa dola. Niache dharau. Magari
matatu au watu watatu tumeenda kufanya kazi ya mtu mmoja! Na sio kwamba wengine
hatuna kazi, tumeacha kazi maofisini kwetu, tumemfuata Grace. Ndio mama
akasema niwe naenda mwenyewe, nisimtume tena Grace. Ndio
pakatulia.” Walizidi kucheka.
“Lakini niliona hata tulipokuwa safarini kuelekea
Marangu. Sikuwa nimeelewa. Grace alijidai kama anatuma ujumbe. Kumbe anataka
mumewe ahamie pale alipokaa.” “Ehee! Unakumbuka alivyotaka nisimamishe gari
katikati ya barabara?” Geb akauliza. “Mimi mwenyewe niliogopa mama.
Ilikuwa katikati ya barabara kubwa. Magari makubwa na madogo yanapita kwa kasi
kweli!” Nanaa akaongeza.
“Basi pale nisingesimama hata dakika moja mbele,
ungeshuhudia varangati yake. Ikifika swala la mkewe, Danny ubinadamu
unamuisha.” “Yaani huyu, raha yake anione nimekaa hapa kama mjinga. Sijui
yukoje Danny?” “Mimi nawafahamu wanaume wa mjini bwana. Hawakawii kunipora
halafu maisha yote yakakosa ladha. Mwanangu akakua hana mama.” “Kwa nini uporwe
bwana? Kwani mimi sina akili?” “Shetani yupo kama simba angurumae. Hachoki.”
“Mimi nilijua akishanioa labda tutapumzika. Lakini naona ndio
vinazidi.” Walizidi kucheka.
Kabla Ya Ndoa Yao.
“Danny!” Grace akamuita mumewe na
kuanza kucheka. “Danny! Unakumbuka yule mwanaume wangu wakati tupo
chuoni?” “Yupi?” Grace akazidi kucheka. “Yaani huwa nakaaga mwenyewe,
nikimkumbuka Danny nacheka mwenyewe mpaka machozi. Yaani sijui huwa
anafikiriaga nini huko kichwani mwake.” “Ilikuwaje?” Nanaa akauliza.
“Geb alipoondoka pale chuoni mwaka wa pili,
akaniachia kina James na Danny kama kaka zangu. Danny akaanza taratibu
kunifuata na kuniuliza naendeleaje na mambo mengine. Basi hapo na mimi nikawa
nimepata mwanaume wangu. Alikuwa na kazi nzuri, na usafiri. Anakuja kunichukua
jioni ananipeleka kula, halafu ananirudisha chuoni. Ananinunulia vinguo, na
kunipa vihela vya matumizi, nikawa napendeza kweli. Sijui bwana Danny akatokea
wapi? Sijui akaambiwa na nani!? Akaanza kuniambia niachane na yule mwanaume.
Sasa nikamwambia, ni mpenzi wangu, hata mama anamfahamu.”
“Hapo ndipo nilipo haribu kabisa. Akaanza fujo.
Sina raha. Kila mahali Danny ananifuata, mpaka darasani. Yaani upo kwenye
kipindi, unashangaa Danny huyo. Basi wenzangu walikuwa wakimuona tu
wanaanza kucheka, nikiona wanacheka tu, najua Danny yupo nje. Usipotoka kwenda
kumsikiliza, anaingia yeye. Mbele ya Profeser na mbele ya wanafunzi wote.
Nilikuwa nachukia jamani, natamani kulia. Na yeye hakomi Danny. Akikukosa
kwenye kipindi, anakusaka kila mahali. Unamfukuza asubuhi, jioni
amerudi.” Nanaa alikuwa anacheka mpaka machozi.
“Sasa siku hiyo natoka chumbani, yule mwanaume
kaja kunichukua tunaenda kula. Nimependeza kweli kweli. Kila mtu ananisifia.
Ile nafika kwenye gari tu, Danny naye akaja. Eti anamuuliza yule
mwanaume, ‘unampeleka wapi mke wangu?’ Jamani nilitamani kukaa
chini.” Kila mtu alianza kucheka upya.
“Yaani eti mimi ni mke wake sio hata mchumba,
mkewe! Bwana Danny alifanya fujo hapo. Kina James, Zinda, Malii, Gozi na wale
wenzake wote uliowaona tukiwa safarini kule Marangu, eti wako hapo
wanamsubiria. Mimi nikamwambia yule mwanaume tuingie kwenye gari tuondoke.
Tukaondoka. Njia nzima nina kazi yakujitetea kwa yule mwanaume. Namwambia
simjui Danny, wala sina mahusiano naye. Tukafika hotelini. Tukaagiza chakula
na vinywaji, hatujaanza hata kula, Danny tena huyu hapa.” Walizidi
kucheka, bila kunyamaza.
“Sasa ulifanyaje?” “Nilitamani kuingia chini ya
meza. Hapo amekasirika kweli kweli. Eti anamwambia alishamuonya akae mbali na
mkewe lakini hasikii. Sijakaa sawa, sijui yule kaka alimtukana au alimwambia
nini, Danny akarusha ngumi. Wakaanza kupigana. Danny akafanya fujo zakutosha
huku anamtukana yule jamaa anamwambia yeye sio mwanaume, kama angekuwa ni
mwanaume kweli angekuwa na uwezo wakutafuta mwanamke wake kuliko kung’ang’ania
wake za watu.” “Jamani!” Nanaa akazidi kushangaa huku amejawa cheko.
“We acha tu. Basi, Danny akafanya fujo pale,
tukafukuzwa sisi wote watatu, tukatolewa nje. Sasa mwenzetu akapanda kwenye
gari lake akaondoka, katuacha mimi na Danny. Hapo mimi ninalia kweli kweli.”
“Sasa yeye anasemaje?” “Ananibembeleza! Eti pole, lakini wanaume ndivyo walivyo
ni wadanganyifu. Jamani Danny nyie! Nilikuwa natamani kummeza. Tubebaki
tumesimama nje ya ile hoteli. Pesa hana hata yakunichukulia taksii kunirudisha
chuoni. Ananiambia twende tukapande daladala. Yaani Danny!” Nanaa alizidi
kucheka huku anashangaa.
“Yaani amekutoa kwenye gari, halafu anakupandisha
kwenye daladala!?” Nanaa akauliza. “Tena bila aibu. Huku ananiambia
vumilia mpenzi wangu, Mungu atatujalia magari yetu.” “Haiwezekani!?” “Mimi
nakwambia kichwa chake anakijua mwenyewe Danny. Hapo tupo kwenye daladala
ananirudisha sasa chuoni. Mimi nalia na yeye ananibembeleza mpaka tunafika.
Mchezo ukaendelea hivyo hivyo. Akisikia tu nasoma na mwanaume popote pale,
na yeye anakuja kusoma hapohapo na kina James. Hata kama nichumbani kwa huyo
mwanaume na wao wanakuja kusoma humo humo ndani. Akikataa kuwafungulia mlango,
anaanza kufanya fujo. Ikifika siku za ijumaa narudi kwa mama, na yeye
ananifuata.” “Haiwezekani! Anakufuata
mpaka tena kwa mama?” Nanaa hakuwa anaelewa.
“Hakuna asikofika Danny kama mkewe
yupo.” Mama G akajibu yeye maana Grace aliishia kucheka. “Hivi unajua
atakaa hapo kwa siku zile ambazo na mimi nakaa nyumbani?” “Kweli?” “Muulize mama.
Yaani yeye ndio akawa kama Geb pale ndani. Haitaji kukaribishwa wala nini,
analala kwenye makochi anaamka. Anasaidia usafi, nakuomba kupewa kazi za
kutumwa na mama. Sasa arudi hapo nyumbani asinikute, hapatakalika. Mtaa
mzima walikuwa wanatujua mimi na Danny. Wapangaji wote walikuwa wamemzoea,
wanamwita mtoto wa Mama G.” Grace akaendelea.
“Basi mama ananiambia wewe si umkubali tu yaishe.
Namwambia hana sifa hata moja yakuwa mume wangu. Namwambia namtaka mwanaume
mrefu kama baba, sijui awe na gari, nyumba, basi sifa zote ambazo Danny hana
ndizo namtajia mama ndio aina ya mwanaume ninayemtaka mimi. Akipata hela
siku hiyo, mtamjua. Anaenda kuninunulia chips, kuku, mayai na soda. Anakuja
navyo pale nyumbani ananiletea, kama ni chuoni, atakutafuta huku ameshika
mifuko yake. Anaweza akakununulia losheni, dawa ya mswaki na mswaki mpya. Hebu
niambie mtu ndio anavyohonga hivyo jamani! Yaani nilikuwa namwambia mama,
sitaki kumsikia hata kidogo.” Walizidi kucheka.
“Sasa Geb akarudi likizo. Akanikuta nipo kwenye
heka heka ya Danny. Sina raha. Nikamuelezea matatizo yangu yote na Danny,
nikamuomba azungumze naye.” Watu wote walianza kucheka mpaka Danny
mwenyewe. “Bwana, nilimjia juu Geb, hatakaa akasahau.” Danny alifanya
kila mtu acheke upya. “Yaani nilishindwa hata kujieleza, nikaishia
kumwambia ‘lakini Grace anaomba umpe nafasi, Danny’. Danny alitaka kunipiga.
Nikaamua kumuacha. Huwezi kumwingilia Danny, kwa Grace. Hana undugu wala
urafiki. Hajali kama wewe ni kaka yake au mama yake Grace. Yeye anachotaka
Grace tu. Na hataki ushauri.” Nanaa alihisi ni stori tu.
“Sasa ikawaje mkaona?” “Hiyo fujo ikaendelea
mpaka namaliza chuo. Sina mwanaume yeyote, ni yeye tu yupo mgongoni kwangu.
Mchana na usiku.” “Sasa ulipomaliza chuo si alichanganyikiwa?” Nanaa
akauliza. “Achanganyikiwe kwani nyumbani hapafahamu? Yaani ndio akafurahi.
Na yeye akahamia nyumbani rasmi. Anatoka asubuhi anakwenda chuo, jioni anarudi
na kina James. Wanasomea hapo hapo nyumbani. Hajakaribishwa na mtu yeyote.
Yaani kundi la marafiki wa Geb, likahamia hapo nyumbani. Chumba chenyewe ni
kimoja, na sebule. Mwaka wake ule wa mwisho, alikuwa akiishi hapo hapo
nyumbani. Siku za mwisho za mitihani, wote wakahamia kabisa hapohapo nyumbani
wanasoma.”
“Kila nikijaribu kumshauri Danny, kuwa arudi
chuoni mpaka mitihani iishe, hataki. Anasema yeye anamjua shetani vizuri
sana. Na usemi wake ni huo huo, shetani ni simba angurumaye, anazunguka
kutafuta mtu amrarue. Mama naye akawa na kazi ya kuwapikia. Wamejaa humo ndani,
sina raha.” Kila mtu alikuwa akicheka na kutingisha kichwa.
“Nikapata kijikazi, nako huko ilikuwa shida.
Akaenda kujitambulisha kuwa yeye ndio mume wangu, na tunaishi pamoja.”
“Jamani!” Nanaa akashangaa. “Hapo wala sijamkubalia. Kwa hiyo ofisini
wote wakajua nimeolewa, naishi na mume wangu, Danny. Kukanusha tena huwezi, kwa
kuwa ikifika jioni, giza limeingia hajaniona nyumbani, utamuona mwenyewe huyo
amekuja kunichukua kazini. Utasikia mlinzi getini anatangaza kwenye kipaza
sauti, Grace umekuja kufuatwa. Unaweza kudhani nimefuatwa na
gari.” “Kumbe!?” Nanaa akauliza kwa mshangao.
“Alitoe wapi gari huyo Danny!?
Mnatembea kutafuta daladala. Siku za mvua ndio alikuwa anakuja mapema mwenyewe,
ananisubiri mpaka nitoke naye. Eti nisitembee peke yangu kwenye mvua.” “Kumbe
alikuwa anakujali!” “Sana. Wewe subiri usikie.” Grace alitaka kuendelea.
“Basi, kuna dada mmoja alikuwa sekretari wa
kampuni, akawa ananiunganishia na wanaume. Ananiambi mdogo wangu, kiuno hicho,
na tako hilo, ukichanganya na macho hayo, huyu ameahidi kukupa gari, yule
nyumba. Kila siku anakuja na majina mapya ya wanaume na ahadi mpya.” “Sasa
uliwakubalia?” “Hivi wewe Nanaa hujaelewa. Naanzia wapi? Danny alikuwa
ananikaba mpaka kooni, sina pakuhemea. Si nyumbani, si kazini. Akiona
mwanaume amekusogelea, anamuonya kwa maneno kwanza, kinachofuata ngumi. Mkali
kwa mama, mkali kwa Geb. Anawaambia Grace ni jukumu lake, Mungu amempa.” Mama
G, alikuwa anacheka tu.
“Danny! Mimi sijawahi kuona jamani! Na hana aibu
hata. Utamuona anaamka asubuhi, anakuomba nauli ya kwenda chuoni. Namwambia
sasa Danny mwanangu, labda ungekaa tu chuoni kwa muda. Utamuona anavyobadilika.
Hapo hapo anakasirika. Tena nilichompendea Danny, hakuwahi kuniona mimi ni mama
mkwe wake au sijui mama yake Geb. Nakwambia alinimiliki kuliko hata Geb
mwenyewe. Akipata tu pesa, zote anamnunulia vitu Grace. Namkumbusha, namwambia
labda angehifadhi pesa baadhi zimsaidie nauli ya kwenda chuoni. Basi mwenyewe
anakutolea kidaftari chake alichokuwa akiandika vitu vya kuja kumnunulia
Grace.” Mama G akaendelea.
“Akimsikia tu analalamika anataka kitu fulani,
anaandika chini, kila kitu anaandika. Hata kama akimsikia anahamu ya kula kitu
fulani, hutamsikia akiongea kitu, anaandika chini. Sasa akilipwa huko chuoni,
pesa yote itaisha siku hiyo hiyo. Utamuona anaingia humu ndani na mifuko yake.
Atanunua chakula kidogo tu cha kula watu wote humo ndani, lakini pesa nyingine
zote zinaishia kwa Grace. Yeye anasuruali zake mbili tu za jinsi, na tisheti 3.
Namwambia labda ujiongezee tisheti, hapo tena ugomvi, Grace kwanza.” “Jamani!
Kumbe alikuwa anampenda hivyo?” Nanaa akavutiwa. “Mpaka leo Danny
yupo hivyo hivyo. Ni heri akose yeye, mimi nipate kwanza. Hakuna nitakachotaka
kwa Danny asinipe. Mpaka wakati mwingine sipendi kulalamika mbele
yake.” Grace akaongeza.
“Kwa hiyo ndio mkaoana?” “Hapana. Yaani yote hayo
alikuwa ananifanyia nilikuwa wala sijamkubali. Wewe hujakutana na Grace
wawakati huo. Nilikuwa gumzo kila mahali, halafu nije kuolewa na mtu kama
Danny! Hana gari, nguo zake kila mtu anazifahamu! Sithubutu. Kila anayeniona
anataka kunioa! Wanawake wananithaminisha, basi wananiambia yaani wewe Grace,
hongo ya mwanaume anayekutaka wewe ni gari, huyo ni masikini, au Jumba. Ukiwa
makini utapata vyote. Basi hapo kichwa kinazidi kuwa kikubwa, wala sioni
anayonifanyia Danny. Yaani naona anajipotezea muda tu.”Grace akaendelea.
“Sasa yule dada wa ofisini kwetu, sekretari,
alikuwa dada mtu mzima tu, akaniunganishia kwa kijana mmoja mfanyabiashara.
Alikuwa anakujaga pale ofisini. Alikuwa na pesa kweli kweli. Nikaamua kuolewa
naye bila hata kipingamizi, hapo yule dada ananishawishi kila akiniona,
anamsifia huyo kaka. Ananiambia kama ni kuyapatia maisha, basi hapo nimeyapatia.
Basi tukakubaliana na yule kaka, nikaamua kumuwahi kabisa. Nikamuelezea tabia
zote za Danny. Nikamwandaa nakumwambia mambo yote ambayo Danny anaweza
kumfanyia. Akaelewa kwa haraka sana. Maana na yeye alikuwa kama kachangayikiwa.
Kila ninachomwambia anakubali, ilimradi tu anioe.”
“Basi wakati huo mama ananiambia nizunguke kila
ninakotaka, lakini kulala na mwanaume mwiko. Hapo mama akawa mkali kweli kweli,
hanichekei. Kila wakati swali ni hilo hilo, sina raha. Hata ukipata mwanaume,
huwezi kulala naye! Sasa yule mwanaume akawa anataka sana tulale naye. Kila
akiniona ananibembelezea mapenzi. Mimi nikamwambia mama yangu ameniambia ni
marufuku kulala na mwanaume asiye mme wangu. Bila kufikiria, akatangaza ndoa.
Akasema nakuoa. Akanipeleka kwao, wakanipokea. Ndugu zake wote wakamsifia
kapata mke mzuri. Sasa na yeye akawa anataka aje amuone mama, wapange siku ya
kulipa mahari.” Grace akatulia kidogo.
“Nakumbuka siku niliyompeleka kwa mama,
Danny alikuwepo. Nikamtambulisha. Alikuwa kijana mtanashati, pesa ipo,
anajielewa, sio kama Danny. Sitasahu sura ya Danny aliyoniangalia siku ile
wakati nimemleta yule kijana. Danny aliumia mpaka mama alimuhurumia. Sasa hapo
mama mapenzi yashakuwa kwa Danny. Anampenda Danny kama mwanae Geb. Huna
utakachomwambia mama tena juu ya Danny akakuelewa. Kamaliza chuo, eti mama
anamwambia aendelee kusoma. Nikaona hapa nikucheleweshana. Mtu hana pesa,
amemaliza chuo, badala atafute kazi, apate pesa kama wenzake kina James, eti
anarudi tena chuo! Nikaamua niolewe, niendelee na maisha yangu.”
“Ehe!” Nanaa alitaka aendelee.
“Basi, mama akamkarimu huyo mchumba mtu. Baada ya
chakula mimi na yule kijana tukaondoka. Nikashangaa siku ile Danny hakuzungumza
neno hata moja wala hakufanya fujo kama nilivyotarajia. Alinyamaza kimya
akisikiliza mipango mizito ya yule kijana ya kulipa mahari. Kijana alijigamba
pale siku ile, si mchezo. Basi kama unavyomuona mama pale, ndio alikuwa
vilevile siku ile katulia kimya anamsikiliza kijana akitoa mikakati yake. Sasa
najiuliza mbona mama mwenyewe hafurahii. Maana tulipewa ahadi chungu mzima,
ikiwemo yakuhamishwa pale kwenye chumba cha kupanga, kupelekwa kwenye nyumba.
Tena akasema kwa haraka kabla ya hiyo siku ya mahari, kwa kuwa siku hiyo
atakuja na marafiki zake wengi sana, magari yatakuwa mengi, hapatakuwa na
sehemu ya kuegesha magari pale uswahilini tulipokuwa tukiishi.”
“Nakwambia kijana ametoa mikakati kibao. Mama,
mtoto wa mjini katulia kimya yeye na Danny wake wanamsikiliza. Basi mimi cheko limenijaa.
Furaha tele. Napewa nyumba na gari! Basi hapo huna utakaloniambia nikaelewa juu
ya kuyapatia maisha. Basi, baada ya kujigamba pale tukaondoka na yule kijana,
hapo alikuwa ameleta vyakula kibao, akamuachia mama pesa za
matumizi.” Grace akatulia.
“Sasa akanirudisha usiku mwenyewe nimejawa
furaha, nimehongwa pesa, nina ahadi ya kuolewa na kwenda kuishi kwenye jumba la
kifahari, akasema ataninunulia gari ili nisipate shida ya usafiri. Nimeingia
pale ndani, Danny hayupo sehemu aliyokuwa akilala. Alikuwa akilala kwenye
makochi sebuleni, mimi na mama chumbani. Mama akasema aliondoka mara tu
tulivyotoka. Usiku ukapita, Danny hajarudi. Usiku wa pili tena, Danny hajarudi.
Nikaanza kukosa raha.”
~~~~~~~~~~~
Usikose Kufuatilia
Mkasa Wa Grace Na Danny. Nini Kilitokea Mara Baada Ya Danny Kuondoka? Ilikuaje Mpaka
Kijana Huyo Asiye Na Kitu, Akaishia Kummiliki Grace, Msichana Aliyesumbua Wengi
Wenye Pesa Zao?
0 Comments:
Post a Comment