Yule dalali akafika. Alikuwa na maneno mengii.
Alisimama upande aliokaa Geb. Aliongea kama dakika kumi, Geb na Nanaa
wakimsikiliza. “Kwa hiyo chumba kipo au hakipo?” Nanaa akamkatisha. “Kipo.
Lakini si unajua inabidi unilipe ya kukupeleka?” “Hata kabla sijaona chumba
chenyewe!?” “Hiyo ndio garama ya kukupeleka kwanza.” Akajibu. “Naomba
unisubiri hapo pembeni kwanza.” Nanaa alimwambia na kumuomba Geb apandishe
vioo vya gari wazungumze.
“Nakushukuru sana kwa moyo wakutaka
kunisindikiza. Lakini hivyo wewe ulivyo, na gari lako hili, tukiongozana wote,
sitaweza kulipia chumba hata mwezi mmoja.” Geb akaanza kucheka. “Jamani
Nanaa! Mimi nimefanyaje?” “Kuanzia wewe na gari lako, mnaonekana ni pesa tupu.
Ndio maana ameanza kunidai hapa pesa zisizokuwa kwenye makubaliano. Anajua wewe
ni mtu wangu, unataka kunipangishia chumba. Na kwa kuwa amekuona una pesa,
anajua hata akikutajia pesa kubwa vipi, utalipa tu. Wakati mimi mwenzio pesa
yangu ndogo. Naomba nishuke hapa. Wewe ondoka.” Geb alizidi kucheka.
“Usinifukuze Nanaa.” “Mimi nawafahamu vijana wa
mjini. Wanapenda pesa wasiyoitolea jasho. Watadai pesa nyingi, Geb. Wewe niache
tu, nitakufuata nyumbani.” “Sasa kama nitapeli, akikuchukua halafu akaenda
kukufanyizia na wenzake?” “Acha kuniogopesha bwana Geb! Mbona yule mwingine
hakunitapeli?” “Mimi nakwambia ukweli. Sikuogopeshi. Watu hawafanani. Ni heri
twende wote. Kila pesa atakayokuongezea, mimi nitailipia.” “Hapana bwana
Geb. Hata kodi wanaweza kunitajia kubwa mara mbili ya hapo.” “Nitalipa ile
itakayoongezeka.” “Hapana Geb, bwana! Na ya mwakani nani atalipa?”
“Mimi.” Nanaa akamwangalia.
“Nimekuomba usinidanganye Geb. Nishadanganywa
sana maishani. Usiweke tumaini la uongo moyoni mwangu.” “Kwa nini unafikiri
nakudanganya?” “Sasa mwakani utanionea wapi mimi!?” “Kwa hiyo inamaana wewe
ukiondoka leo, ndio basi!? Mbona ni kama ulisema ukiondoka utanitafuta?
Uliniahidi ukikwama utaniambia, au na wewe ndio unanidanganya?” “Sikudanganyi
Geb.” Nanaa akaishiwa nguvu.
“Sasa mbona unanigeuka tena!? Naomba kuwa makini
na kila unachoniahidi, Nanaa. Huwa naumia sana nikidanganywa. Ni heri uniambie
ukweli, hata kama unajua utaniuma, kuliko kuniwekea ahadi ambayo unajua huna
hata mpango wa kuja kiitimiza.” “Sikuwa na maana mbaya, Geb. Samahani. Ila
sitaki..” Nanaa alikwama akanyamaza. Geb akabaki akimwangalia.
“Nakuahidi sitakudanganya, na wewe nakuomba
usinidanganye. Kitu unachojua hutakitimiza kwangu, naomba usiniahidi. Tafadhali
Nanaa. Huwa naumia vibaya sana.” “Lakini sijakudanganya, Geb.” “Uliponiambia
utakuwa mlinzi wangu. Ulimaanisha ni hapa barabarani tu, tukifika nyumbani
unakuwa unaendelea na maisha yako? Yaani unakuwa umemaliza kazi yako, au
ulimaanisha nini?” Nanaa alianza kutokwa na machozi asijue kama ni hofu ya
kuamini mtu tena au ni hofu hata ya kufikiria kujaribu kurudi kwenye hiyo njia
yakuahidiana na mtu kwenye mapenzi. Kumbukumbu za kutendwa na wanaume gafla
zikamrudia zikiwa ‘so fresh’. Mpaka mwili ukaanza kutetemeka baridi.
Lakini huyu ni Geb Magesa. Mwanaume ambaye hisia
zake zote zimekubali kuwa anampenda, tatizo ni Liz tu. Swali la je na yeye
akimuumiza, ndilo lililokuwa likikubaliana na wazo la kuhama nyumbani kwake
angalau waachane wakiwa na kumbukumbu nzuri. “Naomba uniambie ukweli
Nanaa. Na naomba usinidanganye.” Geb akasisitiza. “Naogopa Geb. Naogopa sana.” Geb akaondoa
gari pale kituo cha Mwenge, akaendesha mpaka Mlimani city, akaenda sehemu ya
kuegesha magari.
Akashuka na kwenda upande alipokuwa amekaa Nanaa,
akafungua mlango, akamfungua mkanda, akamgeuza na kumkumbatia. Alimkumbatia kwa
nguvu huku akimpapasa mgongoni kama kumtuliza. Nanaa aliweka uso wake mwilini
mwa Geb aliyekuwa amesimama. Alipata faraja ambayo aliihitaji kwa wakati ule.
Alipata utulivu wa nafsi, akajikuta anatulia. Alikuwa ameficha uso wake na
viganja vyake huku amemuegemea Geb, akatoa mikono taratibu akapitisha mikono
yake nyuma ya Geb na yeye akamkumbatia.
~~~~~~~~~~~~~~
“Oooooh!
Siamini kama nimemkumbatia Geb Magesa!” Nanaa akawaza. Akashindwa hata kujisogeza
jinsi mwili ulivyokuwa umekufa ganzi. “Uwiii Nanaa! Au ni ndoto?” Hakuwa
akiaamini. Ni vidole vya Geb mgongoni mwake vilivyomsisitizia kuwa ile haikuwa
ndoto. Alitamani dunia isimame, kwa muda. Imuachie ule wakati ambao alitamani
uje utokee, lakini alijua haitakaa ikatokea. Alivuta pumzi taratibu kama
akichukua hisia nzuri ndani yake.
~~~~~~~~~~~~~~
Walikaa vile kwa muda mpaka simu ya dalali
ilipoingia tena. Nanaa akajitoa kwa Geb, akachukua simu yake. “Ni
dalali.” Nanaa alibaki akiingalia ile simu. “Sijui nifanyaje Geb?”
“Naomba tubaki wote Nanaa.” “Mpaka lini!?” Mahusiano ya Geb na Liz
hayakuwa ya siri. Nanaa aliogopa kujidanganya. “Unakumbuka nilikwambia tutafute
chumba hosteli, utakachokitumia pale itakapo lazimu?” Nanaa
akanyamaza. “Naomba tuishi wote, Nanaa. Nitakuwa nikikupeleka chuoni,
nakuja kukuchukua mimi mwenyewe.” “Sasa ni lini na mimi nitaanza kujitegemea?”
“Ndio unaanza kujitegemea sasa hivi.” “Najitegemeaje nyumbani kwako, Geb!?”
“Kwani ulitaka kufanya nini ukiwa kwako?” Nanaa akanyamaza.
“Yale uliyotaka kuyafanya nyumbani kwako, naomba
uyafanye pale kwangu. Kuwa huru. Hesabu kama Mungu amekupa familia nyingine,
tunayokupenda. Acha kukimbilia chumbani. Kaa na sisi pale sebuleni. Zungumza na
kila mtu, sio unaenda kujificha kwa bibi Fili kila wakati.” Nanaa
alicheka, akainama.
“Naomba tuishi wote. Sio kwa sababu nataka
kukusaidia, ni kwa kuwa nataka uwepo kwenye maisha yangu.” Nanaa
akamwangalia kidogo kama kumuuliza kitu kilichoshindwa kutamkika mdomoni,
akainama. “Naomba jipe nafasi nyingine yakumuamini mtu fulani Nanaa. Najua
unaogopa, hutaki kuumizwa tena, lakini ujue ndio unajiumiza zaidi. Kadiri
unavyojifungia milango, ndivyo unavyokaribisha simanzi moyoni. Lazima uje
umuamini mtu fulani na upende tena. Kwanza katika mazungumzo yote
tuliyozungumza, sijakusikia kama ulipenda Nanaa.” Nanaa akacheka kidogo.
“Hicho kipengele ni cha muhimu kwa kila
mwanadamu.” “Nikija kuumizwa?” Nanaa alijikuta akiuliza. “Hayo ni
matokeo. Lakini umeshajiuliza kama usipoumizwa? Ikatokea unapata mtu
anayekupenda kwa dhati. Umeshafikiria hiyo furaha yake?” “Itakuaje nije kupenda nisipopendwa,Geb? Yaani ikatokea
ninayempenda hanipendi mimi anampenda mtu mwingine?” Nanaa aliuliza
huku akilia. “Naogopa hata kuwaza. Naogopa
kufika umbali ambao nitashindwa kurudi. Nimebakisha muda mfupi sana nimalize
chuo. Naogopa kuja kuchanganyikiwa nikiwa nahitajika kutuliza akili
chuoni.” “Unakumbuka niliomba kazi ya kufuta machozi?” Nanaa
akainama. “Pia nitahakikisha hayatoki. Na kama yatatoka, mimi
nitakuwepo.” Nanaa akabaki akifikiria huku akikausha machozi. “Naomba usiwaze
mbali sana Nanaa. Mimi nipo hapa na wewe.” Geb alikuwa akiongea kwa
utulivu sana. Nanaa akavuta pumzi.
“Anamaanisha nini?” Nanaa
akawaza. “Bahati kama hii inaweza isirudie tena! Ni Geb ndio ananiambia
hivi!” Nanaa alikuwa akijikumbusha. “Kwa hiyo umekubali kubaki tuishi
wote?” Geb akamuuliza kwani Nanaa alibaki akiangalia simu yake iliyokuwa
inaonyesha namba ya yule dalali. Alikuwa kwenye wakati mgumu sana. Njia panda
haswa! Achague nini? Geb ameongeza kitu kingine. Amemtupia swali lililozidi
kumfanya afikirie. Alimwambia, ‘Lakini umeshajiuliza kama usipoumizwa? Ikatokea
unapata mtu anayekupenda kwa dhati? Umeshafikiria hiyo
furaha yake?’ Huo ukawa mtego mkubwa kwake.
“Kama utakataa. Nitakuruhusu ushuke hapa, urudi
kwa huyo dalali, ukatafutie chumba. Lakini ukikubali kubaki, nakuahidi hutalala
ukilia tena. Na ikitokea unalia, nitakuwepo kukufuta machozi.” Nanaa
akamwangalia kama haamini huku machozi yakimtoka. Ni kama na yeye Geb
alijiweka kwenye nafasi yakutaka kuchaguliwa. Alitaka mtu anayemchagua yeye
zaidi ya kitu kingine. Lakini zipo siku Geb anakuwa amelala na Liz chumbani
kwake! Atajuaje kama Nanaa analia? Hata kama akijua. Kweli ataweza kumuacha Liz
kitandani na kwenda kumbembeleza yeye Nanaa? Hayo ni maswali ambayo yalikuwa
yakiendelea hata kwenye kichwa kwa Nanaa.
“Najua huamini na una maswali mengi. Lakini
chukua hatua ya imani tu. Jaribisha. Ila sitakulazimisha Nanaa, upo huru
kuchagua na kufanya kile unachotaka.” Geb akampisha mlangoni, akarudi
upande wake, akaingia ndani ya gari, akakaa akabaki akimwangalia. Hata yeye
mwenyewe asiamini nafsini mwake.
~~~~~~~~~~~~~~
Ni msichana wa pekee anayekutana naye katika
kipindi hiki cha mafanikio yake, eti anashindwa kumkubali moja kwa moja!
Anachukua muda kufikiria ombi zito kama lile! Hata Geb alishangaa. Hata kabla
hajafanikiwa sana kimaisha, umbile na macho yake vilimuuza sana kwa wasichana.
Alitongozwa kila aendapo. Alijua wazi ni wengi wanamtamani. Na kumuota awe wao.
Hata hakuwa mtongozaji sana. Walijileta wenyewe na pesa yake iliongea. Lakini
ni Nanaa aliyempenda na ndiye anayemringia. Yupo tayari kuacha nyumba yake, na
kwenda kuanza maisha yake kwengine, hata baada ya ahadi ambazo hakumbuki kumpa
mwanamke mwingine, ila yeye Nanaa.
~~~~~~~~~~~~~~
Nanaa bado alikuwa akifuta machozi, huku haelewi
ile ofa ya Geb inaishia wapi. Inamipaka gani! “Na Liz?” Nanaa
alizidi kusita moyoni na mawazoni. Alikuwa akikimbilia kitandani kwa haraka
sana kutoa penzi. Bila kuangalia umbile wala utajiri. Alitumia mwili wake kama
silaha ya kuvutia wanaume. Lakini leo hofu na maumivu ya kusalitiwa na wanaume
wengine, vinamzuia kumpokea mwanaume ambaye moyo wake umempenda. Anasifa ambazo
hata hakuwahi kuzihitaji kutoka kwa mwanaume. Ni zaidi ya matarajio yake.
Akabaki amechanganyikiwa. Hajui afanye nini na Geb asiyeweza kumkatalia kitu,
ameng’ang’aniza ombi lake.
~~~~~~~~~~~~~~
“Naomba usilie Nanaa. Nitakuunga mkono kwa kila
utakachoamua.” “Nimechoka kulia peke yangu,
Geb.” “Basi mwambie huyo dalali tutamtafuta wakati mwingine. Turudi
nyumbani.” Nanaa akafuta machozi, akamtumia ujumbe yule dalali na
kumwambia atamtafuta wakati mwingine.
“Nimeshamtumia ujumbe.” Geb akavuta pumzi
kwa nguvu. “Asante Nanaa. Naomba twende tukapumzike nyumbani.” Geb
akaondoa gari mpaka kwake. Hapakuwa na maongezi mengine yeyote mpaka walipofika
nyumbani kwa Geb. Kila mtu alikuwa akiwaza lake pale ndani ya gari. Ulikuwa
umbali wa kutokea Mlimani City mpaka Tabata Barakuda. Lakini uliwapa nafasi
nzuri na tulivu kila mmoja kutafakari maneno aliyomwambia mwenzake.
Baada Ya
Safari Ya Bagamoyo.
“Leo Nanaa amenibadilikia bwana! Amehakikisha
nimekula chakula cha kwanza nilichoagiza.” Mama yake akacheka. “Kwani
na yeye ashaujua ule mchezo wako wakujidai kama unataka kula, halafu unaagiza
vyakula vya kila aina, ili kupoteza muda halafu huli?” Mama yake akauliza,
wote wakacheka. “Kumbe ndio mtindo wake!?” Nanaa akashangaa.
“Kumbe ulikuwa hujui!? Basi akiona utamkera
kwa kumlazimisha kula, ukiagiza cha kwako, na yeye anaagiza cha kwake. Anaanza
na ugali na nyama choma. Kachumbari inakuwa na masharti mengiii. Vikiletwa
hapo, anaanza kutoa kasoro kimoja baada ya kingine. Halafu ili usimjue kama
hataki kula, anaagiza kitu kingine, wakati wewe unaendelea kula. Kikiletwa
hicho cha pili, basi kimoja wapo lazima kitakuwa na kasoro kubwa na ya msingi
sana, itakayosababisha chakula chote kisiliwe. Basi. Anaendelea kuagiza kingine
tena. Lakini cha tatu, lazima kiwe kigumu na kichukue muda mrefu sana
kutengenezwa huko jikoni. Tena anaweza akaagiza ambacho anajua wazi pale
hakipo. Lakini mwenyewe anaita Special Order.” Nanaa alikuwa
anacheka sana.
“Bahati yake ikiwa nzuri, yule mpeleka oda jikoni
akikataliwa na mpishi, basi mwanangu huyu anakuwa amepata sababu ya kuondoka
pale bila kula. Wakimletea kwa haraka kabla wewe uliyenaye hujamaliza, ule
mchezo wake utaendelea vilevile. Anaagiza na kutoa kasoro, mpaka uliyenaye uwe
umechoka kusubiri. Kama ni Grace basi huwa anaharaka zake. Si unamjua Grace?
Kama hana haraka ya kuwahi kazini, basi anamuwahi mumewe au mtoto. Basi Grace
anaomba afungiwe vyakula vyote, anaondoka naye huyu bila kula. Ujue hapo kapona
kupika usiku. Atakuja kuvipanga hapo mezani, ndio chakula chenu cha usiku huo.
Grace kamaliza.” Geb alikuwa anacheka kama sio yeye.
“Haya, kama ni mimi, basi tena nakua nimechoka
kelele za baa, nataka anirudishe nyumbani au kazini kwangu. Akiwa nawenzake
kina Malii, Danny, Zinda, Gozi na James, wao huwa wanakula chakula chote bila
shida. Na ndio furaha yake, kwa kuwa wao hawamuulizi. Akikataa hiki, wakati
anaagiza kile, wao wanagawana na kula kile alichokataa mwanzo. Kikija cha pili
akikikataa, wakati anaagiza cha tatu, wenzie wanakula kile cha pili. Basi
mchezo unaendelea mpaka waondoke pale. Tena huo mchezo wa kuendelea kuagiza
akiwa na wenzake anaufanya kama na wao wakimkera kwa swali la kwa nini yeye
hali kitu wakati wao wanakula? Sasa ili asieleweke vibaya, kama labda
amepadharau pale ujue ataendelea kuagiza tu. Mpaka waagane na
wenzake.” Geb na Nanaa wote walikuwa wanacheka.
“Sasa leo Nanaa amenitolea uvivu. Hakutaka hata
niagize sahani ya pili. Ile ile ya kwanza, akaniambia nile. Sasa na mimi
ikabidi niwe mstaarabu huku nikitamani pale pale angegeuka akawa wewe.” “Ili
unikaripie, nikuache usile?” “Sikukaripii bwana mama! Sema wewe huwa
nakuweza.” Nanaa alizidi kucheka. “Basi mimi ndio mnyonge wake.
Nikijaribu kumlazimisha kula, anakuwa mkali kweli kweli. Mpaka naona heri
nimuache tu, nije kumpikia huku nyumbani, yaishe.” Geb aliendelea
kucheka.
“Haya, mlifanikiwa huko?” “Sanaaa.” Geb
alijibu harakaharaka huku akimwangalia Nanaa. Mama yake akaguna. “Labda
niulize. Mafanikio haya tunayozungumzia hapa ni ya matunda au kuna jingine?”
“Yote.” Geb akajibu tena, wakacheka. “Haya, nenda kaoge, uje
unisimulie kila kitu.” “Acha kupenda stori, Mama G. Hamna nyongeza.” “Umeanza
kunificha?” “Sasa kama hamna nyongeza, nikwambie nini mama?” Geb alikuwa akicheka
huku akitoka. “Na usirudi hapa. Kalale huko huko chumbani kwako.” “Acha
hizo mama bwana!” “Wewe si unajidai msiri wewe? Sasa hapa kitandani kwangu
nisikuone. Nenda na siri zako.” “Basi nakuja kukusimulia. Mama naye!” Geb
akatoka, wote wakacheka.
“Ukimuona anachekacheka hivyo, ujue kuna
kilichomfurahisha. Mlalamishi kama nini huyo.” Nanaa akacheka. “Na
mimi naenda kuoga, nilale kidogo.” Nanaa
akasimama. “Nanaa!” Akamwita kabla yakufungua mlango. “Nashukuru
kwa kumsindikiza. Naona amerudi na furaha.” Nanaa akacheka asijue ajibu
nini. “Anakuwa mpweke kweli! Anazunguka huko maporini peke yake, hali kitu
na wala hana mtu wakuzungumza naye. Hana mtu anayeweza kumfikia hisia zake
binafsi na kumtuliza, yeye kama Geb. Kule kuwepo tu pembeni yake, kunamsaidia
sana. Huwa nakuwa naye kwenye simu wakati wote, angalau kumfanya asijisikie
yuko peke yake, lakini kama unavyojua mimi ni mama. Siwezi kumliwaza kabisa.
Halafu na magoti yangu yananisumbua mara kwa mara. Siwezi kuwa naye kila
mahali.”
“Grace naye kama unavyoona. Hao wanaume wawili,
Fili na Danny, wanamganda hana hata pakuhemea. Kila wakati Danny anamtaka awepo
alipo yeye. Tena afadhali yeye asiwepo nyumbani kuliko Grace. Danny
anakuwa kama mtoto anayenyonya! Anataka Grace awepo kazini na hapa nyumbani,
basi. Akijua yupo nyumbani halafu aje hapa asimkute, hapatakalika hapa.
Atafanya fujo mpaka Grace arudi. Anawivu Danny, wakupitiliza. Kila saa
anahisi ataporwa huyo Grace. Akianza kumtafuta hapa, utafikiri mtoto mchanga
analilia nyonyo.” Nanaa akacheka.
“Nilimuona juzi!” “Ile juzi mbona alijikaza, kwa
kuwa alijua yupo na Fili. Nakwambia inakuwa kelele hapa, mpaka Grace arudi.
Tena wakati mwingine anamfuata huko huko.” Nanaa akacheka sana. “Sasa
wewe huwa unamwambiaje?” “Kimyaa. Nawaangalia tu. Huna utakachomwambia Danny
juu ya Grace, mkaelewana. Tokea anamchumbia mpaka leo. Yupo hivyo hivyo kama
amechanganyikiwa. Kila saa anataka amsikie mkewe. Ajue yupo sehemu anayotaka
yeye, na watu anaowajua. Sio mwanaume asiyemtaka yeye. Akisikia yupo
mahali na mwanaume asiyemjua yeye, anaacha kazi zote anamfuata
mkewe.” Nanaa akashangaa.
“Haiwezekani Mama! Sasa Grace anasemaje?”
“Nakwambia huna utakachomwambia Danny, kwa mkewe. Atakuja kukusimulia yeye
mwenyewe stori za Danny wakati wanachumbiana. Utacheka mpaka ulie. Ngoja siku
wakiwa wamekaa hapo sebuleni, nitawachokoza umsikie Grace mwenyewe. Haishiwi
vituko. Kutwa yupo na mkewe huko chumbani. Akiwa hapo sebuleni, basi Grace
awepo jikoni. Tena asikae sana huko jikoni, atamfuata. Hataki mkewe eti akae
jikoni muda mrefu anampikia yeye! Haiwezekani. Yupo radhi akanunue chakula
sehemu yeyote. Tuje kula, kuliko kumwambia mkewe akae jikoni apike, wakati yeye
yuko sebuleni. Ni heri na yeye ahamie hapo jikoni au mtu mwingine apike. Na
uzuri wake, hachagui chakula. Chochote atakachowekewa na yeyote yule, atakula
tu. Utamuhurumia huyo Danny. Nenda mwaya kapumzike, lakini asante
sana.” Nanaa akatoka akiwa anacheka.
~~~~~~~~~~~~~~
Nanaa alikuwa akiwaza na kujiuliza nafasi
yake kwenye maisha ya Geb itakuwa ipi, lakini mama yake Geb, alimsaidia kumjibu
swali hilo gumu sana lilokuwa limemsumbua sana Nanaa, asijue kwa nini Geb
alimtaka asihame, aishi nae pale. Alienda kujilaza kitandani kwake baada ya
kuoga, akabaki akiwaza. “Labda kweli Geb ananihitaji! Amekuwa
akinifuata kazini siku nne mfululizo! Ametaka niende naye Bagamoyo. Anaonekana
anafurahia nikiwa naye karibu. Anajitahidi kuniongelesha. Marangu alinivalisha
sweta mbele za watu, huku akinituliza! Labda kweli lipo pengo maishani mwake
ambalo naweza kuziba. Liz anaonekana mbinafsi sana. Labda hamjali.” Nanaa
aliendelea kuwaza. “Lakini ngoja nisiharakishe nisije kuwa nimeelewa
vibaya, nikajiingiza kichwa kichwa nikaishia kuumia.” Nanaa alipitiwa
na usingizi.
~~~~~~~~~~~~~~
Nanaa Amesitisha
Ramsi Swala La Kujitafutia Mahali Pa Kuishi Ili Awe Na Geb. Hajui Kwa Wazi Na
Wala Hajatamkiwa Kwa Hakika Nafasi Yake Kwenye Maisha Ya Geb Ni Ipi. Japo Ipo
Ahadi Yakufutwa Machozi Na Kuhakikisha Halii Tena.
-
Ni Nini Geb Atafanya Kuhakikisha Anatunza Furaha Ya Nanaa Na Liz Akiwa
Pichani?
Usikose MUENDELEZO.
0 Comments:
Post a Comment